Search This Blog

Friday, October 28, 2022

AHADI YA MAISHA - 1

 

     





    IMEANDIKWA NA : RAYMOND MWALONGO



    *********************************************************************************



    Simulizi : Ahadi Ya Maisha

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    “Nakupenda sana Winnie na naahidi nitakuoa mara baada ya masomo yetu” Ilikuwa sauti ya George Innocent ambaye alikuwa mtoto wa tajiri mkubwa hapa nchini Tanzania. Wakati huo George na Winnie Gregory aliyekuwa mtoto wa balozi wa Ufaransa nchini, walikuwa chini ya kivuli cha miti iliyokuwapo katika chuo kikuu cha Dar es salaam. Wote walikuwa katika mwaka wa mwisho wa masomo yao, George alisomea biashara wakati Winnie alikuwa akisomea sheria chuoni hapo. Uhusiano wao hakuna mtu ambaye hakuutambua kutokana na umaarufu wa wazazi wao waliokuwa na uwezo kifedha. Watu walivutiwa na ukaribu wao zaidi kwa jinsi walivyoendana kwani walikuwa warefu wastani, wakati George akiwa mtanashati aliyewavutia wanafunzi wa kike chuoni hapo. Wanafunzi wa kiume nao hawakuwa mbali siku zote walikuwa wakiwaza jinsi watakavyo weza kumpata Winnie aliyekuwa na kila kigezo cha kushiriki mashindano ya urembo. Uzuri wake uliongezeka zaidi kwa vile alizaliwa kwa mama mwenye asili ya kizungu na baba yake aliyekuwa mfaransa mwenye asili ya kiafrika.

    Ndoto za walimwengu kutenganisha uhusiano huo zilionekana kugonga mwamba kwani uhusiano wao ulionekana kuendelea kudumu kadri siku zilivyozidi kuisha ili waondoke chuoni hapo. George na Winnie walikuwa wakisikia mambo mengi ambayo yalikuwa na lengo la kutenganisha uhusiano wao lakini walijitahidi kuyakabili ili yasipate nafasi. Siku zote George alitamani wamalize masomo chuoni hapo kwa vile alikuwa akihisi jambo baya lingetokea. Aliamini kama angemaliza masomo hakuna mtu ambaye angeweza kutenganisha uhusiano wao, jambo hilo ndilo lilimfanya ajitahidi kulinda uhusiano wake na Winnie.

    Frank Joseph akiwa mtoto wa waziri mkubwa nchini alikuwa mmoja wa watu ambao hawakuwa tayari kushuhudia harusi ya George na Winnie ikitokea siku moja. Alikuwa akimpenda sana Winnie na alipanga kuhakikisha kwa gharama yeyote anampata. Alikuwa amevutiwa naye toka akiwa mwaka wa kwanza wa masomo chuoni hapo lakini kulikuwa na kikwazo kwani kwa mara ya kwanza alivyomfuata Winnie hakumpa nafasi na alimtaja George kama mchumba wake. Frank aliendelea kujipa matumaini ya kufanikiwa kumpata Winnie, hakujali urafiki aliokuwa nao na George kwa muda mrefu. Urafiki uliotokana na uwezo wa kifedha wa familia zao, alipanga kutumia muda mfupi wa masomo uliokuwa umebaki ili kuvuruga uhusiano huo.

    Aliwatafuta rafiki zake kadhaa na kuwaomba ushauri juu ya nini cha kufanya katika zoezi kama hilo lililokuwa gumu. Baada ya kushauriana nao kwa kipindi kirefu hatimaye walipata jibu juu ya kitu cha kufanya na waliandaa njia zote za kutenganisha uhusiano huo. Walihitaji kuipata simu ya Winnie ili kufanikisha zoezi lao, jambo lililowaumiza vichwa ingawaje Frank alikuwa na namba ya simu ya mrembo huyo lakini hakuwa na mazoea ya kumpigia na namba waliona haina mchango katika zoezi hilo. Mwishoe Frank aliamua kumtumia rafiki wa karibu wa Winnie ili afanikishe zoezi hilo kwa vile msichana huyo walikuwa karibu kwa kila kitu ikiwa ni pamoja na kulala chumba kimoja.

    Alikuwa amemuahidi malipo endapo angefanikisha zoezi hilo, siku ya Jumamosi majira ya saa tano usiku wakati Winnie akiwa amelala, tayari Frank Joseph na rafiki zake walikuwapo nje ya eneo hilo. Ni wakati ambao rafiki yake Winnie alifanikiwa kuichukua simu iliyokuwa kando kidogo na eneo alilokuwa amelala. Aliondoka taratibu pasipo kugundulika na Winnie na hatimaye aliipeleka simu hiyo kwa Frank na rafiki zake waliokuwa nje ambao walimweleza awali wangeitumia kwa dakika kumi tu.

    Mara baada ya kuichukua Frank alielekea eneo la ujumbe mfupi wa maneno na kuandika mistari kadhaa kabla ya kuutuma ujumbe huo kwenye namba aliyoamini ilikuwa ya George. Baada ya sekunde kadhaa ujumbe huo ulipokelewa na Frank aliamua kuizima simu hiyo na kumpa rafiki yake huyo wa Winnie.

    “umefanya kazi nzuri, sasa simu hii usiiwashe kairudishe na zawadi yako hii hapa” Aliongea Frank akiongeza kwa kumpa msichana huyo fungu la pesa ambazo kwa haraka zilionekana kufikia kama laki tatu hivi. Msichana huyo alipiga kelele kabla ya kumkumbatia kwa kutimiza ahadi yake. Frank na rafiki zake waliingia kwenye gari tofauti kati ya mbili walizofika nazo na kuziwasha kabla ya kuziondoa kwa kasi wakionekana walielekea sehemu. Msichana huyo akitembea taratibu alifanikiwa kuirudisha tena simu ya Winnie mahali pake pasipo kugundulika, alikuwa na furaha kupindukia mara baada ya kuhesabu fedha alizopewa na kubaini zilikuwa laki tatu.

    George Innocent hakuwapo chuo siku ya Jumamosi kwa vile alikuwa na mazoea ya kujumuika na familia yake kila mwisho wa wiki iliyoishi maeneo ya Bunju. Siku hiyo alikuwa amechoka sana kutokana na masomo ya wiki nzima jambo lililomfanya ampigie simu Winnie majira ya saa mbili usiku akiwa kitandani tayari kwa kulala. Alimtakia usiku mwema kama ilivyokuwa kawaida yake na mwishoe alilala. Majira ya saa tano simu yake ilimshtua kwa mlio wa ujumbe mfupi ulioingia alivyotazama kwenye simu yake aligundua ujumbe huo ulikuwa umetoka kwa Winnie na alianza kuusoma. Baada ya sekunde chache za kuusoma alijikuta akitabasamu, ujumbe huo ulikuwa ukimtaka aende ‘Kennivile Hotel’ iliyokuwapo maeneo ya Mwenge.

    Hakujiuliza mara mbili aliamka na kuanza kujiandaa akiamini Winnie alikuwa na zawadi aliyotaka ampe. Kilichompa matumaini zaidi ni tabia aliyokuwa nayo mchumba wake huyo ya kufanya mambo kwa kushtukiza. Mara baada ya kujiandaa alitoka nje na funguo za gari la familia alilopenda sana kulitumia lililokuwa aina ya ‘Range Rover’, hakuwa na hofu juu ya wazazi wake ambao walikuwa wanamuamini. Aliingia kwenye gari hilo na kuliwasha kabla ya kuanza kuliendesha kuelekea katika geti la nyumba yao.

    “ebwana sijui kama nitarudi, mzee akiniulizia mwambie nimeenda chuo kujiandaa kuna mtu kaniambia tuna mtihani kesho” alisikika George akimweleza mlinzi wa getini kwao kwani alielewa hangerudi siku hiyo na zaidi alikuwa hajawaaga wazazi wake waliokuwa wamelala.

    Mara baada ya kufunguliwa geti alianza kuendesha gari kuiacha nyumba yao kabla ya kuingia barabara kuu akieleka Mwenge katika hoteli aliyokuwa ameelezwa. Njiani alijaribu kumpigia simu Winnie lakini alikuwa hapatikani, hakuumiza kichwa kwa vile alimtambua vizuri akiamini aliizima simu akihofia kujibiwa kuwa hangeweza kufika katika hoteli ya Kenniville. Baada ya muda mfupi alikuwa ameegesha gari lake mbele ya hoteli hiyo na alianza kutembea taratibu kuelekea eneo la mapokezi. Kichwani alitawaliwa na mawazo ya kukutana na zawadi toka kwa mchumba wake kwani jambo hilo lilikuwa la kawaida kutokea.

    “samahani, kuna mgeni yeyote anayeitwa Winnie?” alimuuliza mhudumu aliyekuwapo mara baada ya kufika eneo la mapokezi. “aah! wewe ndo George?.... amesema ukifika uende chumba namba ishirini na tano” alimujibu mhudumu huyo. George alianza kutembea kuelekea chumba husika kilichokuwa ghorofa ya kwanza, baada ya dakika mbili alikuwa nje ya chumba hicho na kuanza kugonga.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Baada ya sekunde kadhaa mlango huo ulifunguliwa na mfunguaji alionekana kama vile alijificha nyuma ya mlango huo, George alijikuta akicheka akiamini Winnie alifanya utani alianza kuingia ndani ya chumba hicho. Mara baada ya kuingia alianza kuufunga mlango akiamini angemuona Winnie baada ya kuufunga, akiwa anaendelea na zoezi hilo alishtushwa na sura ya mwanamme aliyekuwa ameshika chuma kilichokuwa kama bomba mkononi na kabla hajafanya kitu mtu huyo alimpiga na chuma hicho kichwani na kumfanya aanguke chini kabla ya kupoteza fahamu.

    George alishtuka majira ya saa moja asubuhi akiwa hajielewi lakini pia alikuwa na maumivu makali ya kichwa, alikuwa ufukweni mwa bahari na baada kuzungusha kichwa huku na kule aligundua eneo hilo lilikuwa la wavuvi maeneo ya Bagamoyo. Gari alilokuwa nalo aina ya ‘Range Rover’ lilikuwa kando kidogo na eneo alilokuwapo, alipojipapasa mifuko ya suruali zake aliziona funguo za gari hilo. Alikuwa haelewi jambo ambalo lilikuwa limetokea usiku wa siku iliyopita, alikuwa akikumbuka alielekea hoteli ya Kenniville ambako katika chumba alichoelekezwa na Winnie alimuona mwanamme.

    Aliyakumbuka hayo ingawaje kichwa kilimuuma, alinyanyuka na kujitahidi kujongea katika gari lake kabla ya kuliwasha na kuanza kuliendesha akiwa na lengo la kuelekea katika hospitali kuu ya wilaya hiyo.

    Maumivu hayo yaliongezeka kila muda ulivyozidi kwenda lakini alijitahidi kuendesha gari, akiwa anaendelea na zoezi hilo aliwaza jambo na kuhitaji kumpigia simu Winnie lakini aligunduwa hakuwa na simu katika suruali yake. Tayari hisia za hila juu ya uhusiano wake na Winnie zilianza kumuingia akiwaza watu waliompiga walikuwa na lengo la kumuua. Baada ya muda alikuwa ameegesha gari lake katika hospitali ya wilaya ya Bagamoyo alishuka na kuanza kutembea kwa taabu, wakati huo maumivu yalizidi kupindukia jambo lililopelekea aanguke na kupoteza fahamu tena akiwa mbele ya mlango wa hospitali hiyo. Wauguzi kadhaa walifika eneo hilo na kumchukua wakiwa na lengo la kumsaidia, walianza kumchunguza kila eneo la mwili wake kama alikuwa na jeraha lakini hawakubahatika kuliona. Jambo hilo lilianza kuwapa hofu kwa vile walishindwa waanzie wapi kumtibu mtu huyo, mmoja wao aligundua uvimbe kichwani mwa mtu huyo pamoja na alama ya kitu kizito kilichoonekana kutumika kumdhuru.

    Walimpa huduma husika na baada ya dakika arobaini na tano alikuwapo katika wodi la wagonjwa akiwa bado hana fahamu. Watu kadhaa walikuwa wakimwangalia baada ya taarifa za madaktari kuwa mtu huyo alikuwa hatambuliki. Majira ya saa nne asubuhi kijana mmoja alimtambua mtu huyo na kumtaja kwa jina la George Innocent akiwa mtoto wa tajiri mkubwa nchini ambaye alikuwa mfanya biashara. Baada ya utambuzi huo watu kadhaa waligundua ukweli huo lakini hawakuelewa jambo lililokuwa limemtokea kijana huyo. Madaktari walitafuta namba za simu zilizotumiwa katika kampuni tofauti za tajiri huyo na namba moja iliyokuwa ya kampuni yake ya nguo ndiyo ilipatikana bila kupoteza muda waliwaeleza juu ya tukio zima la George.

    Majira ya saa saba gari nne za kifahari ziliwasili hospitalini hapo na mara baada ya kushuka mzee Innocent alionekana kuchanganyikiwa juu ya tukio hilo dhidi ya mwanaye pekee. Alipewa maelezo na madaktari na mwishoe aliamua kuondoka na mwanaye akiwa na lengo la kumhamishia hospitali kuu ya taifa ya Muhimbili. Jambo hilo lilitokana na kupoteza fahamu kwa George mpaka wakati huo, baada ya masaa kadhaa alikuwapo hospitali ya Muhimbili akiendelea na matibabu. Mzee Innocent na mkewe walikuwapo kando ya kitanda cha mtoto wao wakiwa na lengo la kusubiri azinduke na kuwaeleza jambo lililokuwa limemtokea. Mzee huyo alipanga kuhakikisha sheria inachukua nafasi dhidi ya mtu ambaye angetajwa kuhusika.

    Majira ya saa mbili usiku alizinduka na kwa kiasi kikubwa maumivu ya kichwa yalikuwa yamepungua, jambo hilo liliwapa faraja wazazi wake ambao walihitaji kujua juu ya tukio lililompata mtoto wao. George aliwasimulia tukio zima lilivyokuwa na zaidi aliwaeleza kuwa hamkumbuki mtu aliyemdhuru hata kwa sura jambo lililompa hasira mzee Innocent ambaye hata hivyo alishindwa jambo la kufanya. Siku iliyofuata asubuhi George alirudishwa kwao ili akaendelee na matibabu kwa vile familia yao ilikuwa na daktari aliyehusika matatizo tofauti katika familia yao. Mara baada ya kufika nyumbani kwao George alielezwa na wafanyakazi wa ndani kuwa siku iliyopita Winnie alifika nyumbani kwao hapo na kumuulizia lakini hata wao hawakujua sehemu aliyokuwapo. Alilitambua suala hilo akiwa na lengo la kumtafuta Winnie mchana wa siku hiyo kwa vile muda huo alikuwa chini ya uangalizi wa karibu wa wazazi wake. Jambo ambalo bado lilikuwa likimuumiza kichwa lilihusiana na kutumika kwa simu ya Winnie kuelezwa aende hoteli ya Kenniville. Hakuwa na hofu sana akiamini siri iliyohusika na suala hilo ingejulikana muda wowote.

    Majira ya saa nne mlinzi wao alipiga simu na kueleza kuwa kulikuwa na wageni wa George, mama yake ambaye alikuwa akiongea na mlinzi huyo alimweleza awahurusu wageni hao. Alielekea dirishani kisha akafungua pazia na alishuhudia gari aina ya ‘Mercedez Benz’ likiegeshwa mbele ya nyumba yao na Winnie alishuka akiwa ameshika magazeti kadhaa akiwa ameongozana na rafiki yake. Mama yake George alimtambua msichana huyo ambaye alikuwa mtoto wa balozi wa Ufaransa nchini kuwa alikuwa na uhusiano na mwanaye George. Mama huyo alimwonyeshea ishara mmewe mzee Innocent iliyoashiria kumwachia nafasi George na mchumba wake Winnie. Mzee huyo alinyanyuka eneo alilokuwa amekaa na kuanza kutembea akimfuata mkewe aliyekuwa akielekea chumbani kwao katika ghorofa ya kwanza ya nyumba hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    George alitabasamu akiamini mgeni aliyekuwa amefika alikuwa ni Winnie, alikuwa amekaa kwenye sofa dogo huku akiwa na pamba za hospitali zilizozungushwa kichwani mwake.Punde baada ya kuingia kwa Winnie na rafiki yake ambaye alimfahamu alishtushwa na kelele za kulia alizozitoa mchumba wake huyo. Kwa haraka alihisi labda alikuwa amesikia tukio alilokuwa amefanyiwa jambo lililompa hamasa ya kusubiri nini kingefuata. “umenidhalilisha George, ungesema mapema kama hunitaki” alilia akipiga kelele Winnie huku akimsogelea George eneo alilokuwa amekaa. “kwani vipi! mbona sikuelewi…..” aliuliza huku akiwa na mshangao. “picha! George picha! Picha za utupu ulizopiga na mwanamke wako” alijibu Winnie jambo lililompa mshtuko George.

    “ za utupu? Picha gani hizo Winnie sijawahi kuwa na mahusiano na mtu yeyote zaidi ya…” “huyu nani George usinifanye mtoto” alimdakia Winnie akiwa hajamaliza sentesi yake huku akimwonyesha George moja ya picha zilizokuwapo kwenye gazeti moja alilokuwa amelishika. “huuuwiii mama weeee nakufa, wamenimaliza watu hawa nakufa” alipiga kelele George baada ya kuiona picha ambayo alikuwa na mwanamke ambaye hakumtambua wakiwa katika mwonekano usio wa kawaida na zaidi nje ya maadili ya kitanzania. Picha hiyo ilikuwa imefichwa sehemu kadhaa na visanduku vyeusi vilivyotengenezwa.

    “unakufa nini George! magazeti yote ya leo yanakuhusu wewe” aliendelea kusisitiza Winnie huku akilia wakati akimsogezea George gazeti jingine lililokuwa na picha nyingine tofauti. Akiwa ameishiwa nguvu na kushindwa jambo la kufanya Winnie alimalizia magazeti mengine mawili kati ya manne aliyokuwa nayo. “nilikupenda, nakupenda lakini tunaishia hapa endelea na mwanamke wako” alisisitiza Winnie kwa hasira kabla ya kuanza kuondoka akimuacha George na magazeti hayo ambaye alitulia akiwa ametoa macho na mwishoe aliishia kupoteza fahamu. Mzee Innocent na mkewe walisikia kelele za vilio zilizotokea eneo la sebule yao jambo lililowafanya wajongee eneo hilo na kumshuhudia Winnie akiondoka na rafiki yake eneo hilo hata walipojaribu kumwita hakutii.

    Mzee Innocent na mkewe walionekana kutoelewa kilichoendelea kwa mbali walimuona mtoto wao kama kalala jambo lililowafanya wamfuate katika sofa alilokuwa amekaa. Mama yake George alianza kumwangalia wakati mzee Innocent aliyaona magazeti sakafuni na kuyachukua, gazeti la kwanza lilikuwa na kichwa kilichoandikwa ‘Uozo Wa Mtoto Wa Tajiri’ zaidi alichanganyikiwa na picha za mwanaye akiwa na mwanamke katika mwonekano ulio nje ya maadili. Alichukua gazeti jingine ambalo lilikuwa na picha nyingine za mwanaye na mwanamke huyo ambalo liliandikwa ‘Tajiri Innocent Adhalilishwa Na Mwanaye’ alitupa magazeti hayo bila kumalizia mengine na alisikika akipiga kelele “nooo! haiwezekani George hawezi kufanya hivyo haiwezekani” Aliongea na kuanza kuondoka sebuleni hapo akitembea kwa haraka akielekea nje ya nyumba yake.

    Mara baada ya kutoka alimwita dereva wake aliyekuwa karibu na kumtaka ampeleke ofisini kwake maeneo ya Posta. Dereva huyo alitoa gari kwa kasi akifuata maelezo aliyokuwa amepewa, kichwani mzee Innocent aligundua kuna jambo baya lilikuwa likiendelea dhidi ya mwanaye. Alipanga kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha anatetea heshima ya mwanaye. Wakati huo alikuwa na mawazo ya kwenda kukutana na washauri wake ili kujua atafanya nini ili kulinda heshima yake na ya mwanaye. Hisia zake zilimtuma na kuamini picha hizo zilipigwa wakati mwanaye akiwa amepoteza fahamu na alipanga kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kisheria. Mama yake George aligundua mwanaye alikuwa amepoteza fahamu hivyo alimpigia simu daktari wa familia ambaye alifika nyumbani hapo na kuanza kumtibu.

    Baada ya muda mzee Innocent alikuwa katika ofisi zake na kikao cha ghafla kilikuwa kimeitishwa kikihusisha wanasheria wake na washauri wa kampuni zake tofauti. Aliwaagiza wanasheria wake kufungua kesi dhidi ya magazeti yaliyotoa habari hizo alizoamini ni za uongo dhidi ya mwanaye. Washauri wake walimpa wazo la kununua magazeti hayo katika vituo tofauti vya kuuzia ili fitina hiyo isiendelee kusambaa. Bila kuchelewa mzee Innocent alikubaliana na wazo hilo na kuamua kuandika hundi ya shilingi milioni kumi na tano kwa ajili ya zoezi hilo. Magari yake nane ya mizigo yaliyokuwa ya makampuni tofauti, ikiwa yapata saa saba mchana yaliingia mitaani na zoezi la kununua magazeti yaliyoandika habari juu ya mwanaye lilianza. Kila kituo walichopita walikuwa wakinunua magazeti hayo yote pasipo kuacha hata moja.

    “chalii yangu leo zali yani tumeuziwa magazeti tena yananunua yote, saa tisa nimemaliza kazi?” alisikika kijana mmoja aliyekuwa akiuza magazeti maeneo ya Kimara Mwisho. Wakati huo magari ya mzee Innocent yalikuwa yakielekea maeneo ya Kibaha baada ya zoezi lao kufanikiwa kwa kiasi kikubwa jijini Dar es salaam. Zoezi hilo walienda kulimalizia maeneo ya Kibaha na mzee Innocent alifurahi kwa kiasi fulani akiamini alikuwa amepunguza aibu iliyojengwa na fitina.

    Tayari kesi dhidi ya magazeti yaliyoandika habari kuhusu mwanaye ilikuwa imefunguliwa na ilipangwa kusoma kwa mara ya kwanza baada ya wiki mbili. Zoezi alilolifanya mzee Innocent lilikuwa limefanikiwa kwa kiasi kidogo sana kwani hata vituo vya televisheni kadhaa vililitangaza jambo hilo ikiwa ni pamoja na vituo vya redio. Suala hilo lilikuwa vichwani mwa watu nchi nzima kwa vile walimtambua mzee Innocent kwa utajiri wake. Mambo yalikuwa makubwa katika maeneo tofauti ya chuo kikuuu cha Dar es salaam ambapo wanafunzi walitawaliwa na jina la George vinywani mwao. Wengine walimshangaa kwa tabia chafu alizoonekana kuwa nazo wakati wachache walionekana kutoamini walichoshuhudia. Jambo hilo ndilo lilipelekea Winnie apange kuondoka chuoni hapo baada kuona watu wakimshangaa na wengine walikuwa wakimzomea. Majira ya saa kumi alichukua begi lake akiwa mnyonge na alisindikizwa na rafiki yake mpaka eneo la nje kulikokuwa na gari lililotumwa na baba yake kwenda kumchukua.

    “Winnie njoo umwone George kwenye gazeti” ilikuwa sauti ya juu ya mwanafunzi mmoja wa chuoni hapo akimwita Winnie katika hali ya kumkejeli, alijikuta akitokwa na machozi pasipo kujielewa. Wakati huo hata sauti ilimkatika kwani alikuwa amelia siku nzima juu ya tukio hilo, aliongoza mpaka kwenye gari hilo lililofika chuoni hapo kumchukua mara baada kuagana na rafiki yake alipanda na kuondoka na gari hilo.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jioni siku hiyo George alirudiwa fahamu na mzee Innocent aliwapeleka wataalamu watatu wa kisaikolojia ili wamweke sawa mwanaye. Jambo hilo walianza kulifanya muda mfupi tu baada ya George kuzinduka lakini alikuwa akilia muda wote juu ya jambo lililokuwa limetokea. Kwa kiasi kikubwa aliamini alikuwa ameharibu maisha yake. Aibu aliyoipata kwake aliona ni jambo dogo lakini kuvunjika kwa uhusiano wake na Winnie kulimfanya ashindwe hata kula chakula. Bado hakuelewa mtu aliyehusika na zoezi hilo lakini alitambua wazi lengo lilikuwa ni kutenganisha uhusiano wake na Winnie. Siku iliyofuata gazeti jiigine lilikuwa na picha ya mzee Innocent pamoja na kichwa kilichoandika ‘Mzee Innocent Ahangaika Kuuficha Ukweli’ ndani ya habari hiyo ilielezwa jinsi alivyonunua magazeti yenye picha za utupu za mwanaye na mwanamke ambaye hakufahamika jina lake.

    Gazeti hilo lilimfikia mzee Innocent ambaye wakati huu alitulia akisubira kesi ianze dhidi ya magazeti yaliyotoa picha za utupu na habari zilizohusu mwanaye. Aliamini watu hao wangeeleza mtu ambaye alizipeleka na mkono wa sheria alihitaji uchukue hatua juu ya zoezi hilo la fitina. George hali yake haikuwa nzuri kwani ndani ya siku mbili unyonge wake ulimwonyesha kama alikuwa matatizoni kwa miezi kadhaa. Bado hakuwa tayari kushuhudia uhusiano wake na Winnie ukivunjika, kwa vile namba yake aliishika kichwani aliamua kumpigia na alivyotaja jina lake alimkatia. Alizidi kuchanganyikiwa zaidi na baada ya siku kadhaa namba hiyo ilikuwa haipatikani kabisa. George hakuwa na mpango wa kurudi tena chuo ingawaje alikuwa ameshapona kichwa aliamini akifanya hivyo angezidi kuchanganyikiwa. Alikuwa akisubiri kesi iliyofungiliwa dhidi ya magazeti akiamini ingetoa ufumbuzi juu wahusika wa tukio hilo na mwishoe aliamini angerudiana na Winnie.

    Hatimaye wiki mbili zilipita na kesi ya mzee Innocent dhidi ya magazeti manne aliyodai yalimdhalilisha mwanaye ilianza. Kesi hiyo ilifikia muafaka siku hiyo ya kwanza ya kusikilizwa kwake kwani wanasheria wa vyombo hivyo vya habari waliwasilisha vielelezo vyao vya utetezi. Magazeti yote yalikuwa yamepokea picha hizo kutoka kwenye mtandao kupitia anuani ya barua pepe iliyosomeka kwa ‘uovu@yahoo……..’ ambayo mtumaji alitambulika kwa jina hilo la Uovu. Mtu huyo aliyetuma picha hizo alikuwa ameandika maelezo juu ya picha hizo akidai picha hizo za ridhaa zilipigwa na George akiwa na mchumba wake. Mtu huyo aliendelea kueleza kuwa yeye ndiye aliyehusika katika kuzipiga picha hizo lakini hakukamilishiwa malipo yake jambo lililomfanya aanike uovu huo.

    Utetezi huo ulimfanya mzee Innocent achanganyikiwe zaidi akiwa haelewi jambo la kufanya wakati kesi hiyo ikiwa imekosa mwendelezo. Alipanga kwenda kujiandaa ili kuhakikisha anapata njia nyingine ya kumtambua mtu aliyehusika na zoezi hilo. Majira hayo ya saa saba mchana aliamua kurudi nyumbani kwake maeneo ya Bunju baada ya kuona kichwa chake kilikuwa hakijatulia. Hiyo yote ilitokana na utetezi uliotolewa na magazeti ambayo aliamini yalimdhalilisha mwanaye, punde tu alipofika nyumbani kwake alimweleza George juu ya suala hilo la kesi iliyosikilizwa. George alizidi kuchanganyikiwa akiamini alikuwa amepoteza mwelekeo wa ndoto zake na Winnie.

    Frank Joseph akiwa mtoto wa waziri mwenye dhamana kubwa nchini alikuwa amefurahia kufanikiwa kwa mipango yake. Wakati wote alikuwa kimya akisubiri maamuzi ya kesi ya mzee Innocent dhidi ya magazeti yaliyomtoa mwanaye akiwa mtupu.

    Mara baada ya kesi hiyo kukosa mwelekeo aliamua kusherekea na watu wake waliohusika katika zoezi zima, walikuwa katika hoteli moja ya kitalii iliyokuwa pembezoni mwa bahari ya Hindi. “ kaka yule mtoto wako tena hakuna ubishi”alisikika rafiki yake mmoja wakati hafla yao ya ushindi ikiendelea. Frank alikuwa amekamilisha zoezi kubwa kwani siku ya tukio la picha hizo alifanikiwa kumlaghai George akitumia simu ya Winnie kuwa afike katika hoteli ya Kenniville. Huko akiwa na rafiki zake mara baada ya kumpiga na kuzimia kwake walimtumia mwanamke mmoja ambaye alilipwa kupiga picha hizo. Hawakutaka kuzipeleka picha hizo katika vituo vya magazeti na waliamua kuzituma wakitumia anuani yao ya barua pepe ambayo hakuna mtu ambaye angeweza kuwatambua.

    Mpaka wakati huo alikuwa na uhakika wa kuhakikisha anampata Winnie, alielewa wazi suala la kurudiana na George halikuwapo tena. Hafla yake hiyo akiwa na rafiki zake iliisha salama majira ya saa nane usiku na waliamua kulala katika hoteli hiyo. Siku iliyofuata aliipanga kwa ajili ya kwenda kumtembelea George na sababu kubwa ilikuwa ni kuendeleza furaha za ushindi wake. Alifika nyumbani kwao majira ya mchana akionekana alikuwa na huzuni juu ya tukio zima lililompata George. Aliongea mambo ya kumfariji akimtaka asikate tamaa lakini moyoni alikuwa na furaha juu ya kila kitu kilichoendelea. Alikuwa akijisikia raha jinsi George alivyokuwa akilia huku akimwelezea Winnie walivyoachana naye na zaidi kitendo chake cha kubadilisha namba ya simu. Hatimaye Frank aliamua kuondoka akiwa amemwambia kuwa Winnie alikuwa amerudi chuo akiendelea na masomo.

    George bado aliendelea kukosa raha jambo lililomfanya aondoke nyumbani kwao siku iliyofuata nyakati za asubuhi lengo likiwa kwenda kumwona Winnie. Alikuwa ameondoka kwa kutoroka na hakuchukuwa gari kama ilivyokuwa kawaida yake, kwa kipindi kifupi alionekana alikuwa amedhoofu kiafya. Alielekea mpaka kwenye kituo cha daladala na kupanda gari lililokuwa likielekea Mwenge, wakati safari hiyo ikiendelea waliomfahamu walikuwa wakimshangaa kwa jinsi alivyokuwa. Alivaa vizuri lakini alidhoofu kiafya zaidi mishipa yake ya fahamu ilionekana kama haifanyi kazi kwani kamasi zilimtoka pasipo kujitambua. Aliegesha kichwa upande mmoja muda wote gari hilo likiendelea kuendeshwa na wakati wakikaribia kituo cha Mwenge aliwashtua abiria “Winnie!, Winnie! Winnie!” alilitaja jina hilo kwa sauti ya juu na kuwafanya watu waanze kumcheka. Alikuwa kama mtu ambaye hakutambua jambo hilo kwani alitulia tena kama awali. Hatimaye gari hilo lilifika Mwenge na alikuwa wa mwisho kushuka kwani alikuwa hajitambui vizuri, alishuka baada ya kuambiawa na konda kuwa kituo hicho kilikuwa mwisho wa gari.

    George alipanda gari jingine lililopitia chuoni kwao likielekea Ubungo na akilini alikuwa ametawaliwa na Winnie, hakuna jambo aliloliwaza zaidi ya mrembo huyo. Baada ya dakika ishirini alikuwa ameshuka eneo la chuo na wanafunzi kadhaa waliomfahamu walionekana wakimshangaa na wengine walimcheka. Wakati akitafakari jambo la kufanya alishtushwa na sauti ya kike ikimwita, aligeuka na kukutana na sura ya mmoja wa rafiki yake Winnie. “George afadhari nimekuona, mimi siamini hivi ni kweli?” aliuliza dada huyo baada ya salamu. “mwenyewe siamini na zaidi sielewi lakini naomba unisaidie jambo moja Winnie yuko wapi wakati huu” Alijibu George kwa unyonge na kuuliza swali, hali yake ya kuchanganyikiwa aliigundua dada huyo na hakutaka majibizano naye. Bila kuchelewa alimwonyesha ukumbi ambao Winnie alikuwa akiendelea na kipindi chake cha asubuhi na wanafunzi wenzie waliosoma sheria. Baada ya maelezo hayo George alianza kutembea kuelekea katika ukumbi huo kabla hajaufikia wanafunzi hao walianza kutoka.

    Kwa umbali alimuona Winnie akiwa miongoni mwao “Winnie! Winnie!……” alipiga kelele George wakati akimkimbilia mrembo huyo aliyeshtuka kuona jina lake likiitwa. Wanafunzi hao waliokuwa wengi eneo hilo walitulia wakiwa na nia ya kuona nini kingefuata, George alikimbia akimfuata Winnie akiwa na lengo la kumkumbatia lakini kabla hajamfikia alisukumwa na msichana huyo na kuanguka chini.Tukio hilo liliwafanya wanafunzi hao waanze kucheka wakimshangaa George ambaye hakukata tamaa kwani alinyanyuka na kuhitaji kuongea na Winnie. “kwa nini hivi Winnie? Sina kosa nipe nafasi tuzungumze” alisikika George akimwambia “Sina mpango na wewe, sikutaki! nasema sikutaki! na sihitaji uendelee kunifuatilia” aliongea Winnie kabla ya kumsukuma tena George aliyekuwa amesimama mbele yake na alianza kutembea akiondoka eneo hilo.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “amehalibu mzushi hampati tena” “chalii yangu kama vipi kajinyonge yani kamba zipo” “ubishoo hawa watoto wa kishua wanajifanyaga wanapesa sasa uozo wao hadharani wanadatadata nini?” walisikika watu tofauti kati ya wale walioshangilia tukio hilo. Frank alikuwapo eneo hilo kwani yeye pia alisomea sheria tukio hilo la kudhalilishwa na Winnie alilofanyiwa George lilimfurahisha sana ingawaje hakuonyesha furaha hiyo. Alimsogelea George na kumnyanyua toka eneo aliloanguka baada ya kusukumwa kwa mara ya pili na alijifanya akimfariji alimtaka aondoke eneo hilo ili kuepuka karaha alimsaidia kumfikisha barabarani na alihakikisha amepanda gari. Alimweleza arudi nyumbani kwao akatulize akili, George alihuzunika juu ya aibu aliyokuwa ameipata, akiwa kwenye gari akielekea Mwenge muda wote alikuwa akilia.

    Mara baada ya kufika maeneo ya Mwenge alianza kuelekea eneo lililokuwa na magari ya Bunju, akili yake haikuwa sawa kwani alianza kuvuka barabara pasipo kuangalia magari yaliyopita. Akiwa katikati ya barabara kuna gari aina ya ‘Toyota Hilux’ lilikuwa katika kasi likielekea usawa wake tayari kwa kumgonga, dereva wa gari hilo alipiga honi lakini George hakujali hata kidogo kutokana na mawazo ambayo yalimpeleka mbali. Hatimaye gari hilo lilishia kumgonga na alibuluzwa nalo kwa urefu wa mita kadhaa kabla ya kutulia. Ndani ya sekunde chache watu kadhaa walifika wakimshuhudia jinsi damu ilivyomtoka kwa kasi sambamba na majeraha mengi aliyoyapata, alikuwa ameumia vibaya. Gari lililomgoga lilibonyea sana jambo lililoashiria kuumia kwake kwa kiasi kikubwa. Walimsaidia kwa kumfunga na vitenge vya akina mama waliokuwa wapitaji kabla ya kumpakia kwenye gari moja ‘Toyota Surf’ ambalo mmiliki wake alijitolea na safari ilianza kuelekea hospitali kuu ya taifa ya Muhimbili.

    Watu waliokuwapo eneo la tukio waliamini mtu huyo aliyegongwa ilikuwa ni vigumu kupona kwake kwa vile alikuwa ameumia kwa kiasi kikubwa. Walielewa walikuwa wametimiza wajibu wao wa kusaidia kuokoa maisha ya mtu huyo aliyekuwa amegongwa. Dereva na mmiliki wa gari lililomchukua George alijitahidi kukimbiza gari hilo ili amuwahishe hospitali akiwa mzima. Alikuwa ameongozana na watu kadhaa waliokuwapo eneo la tukio ambao walijitolea ili kusaidia kuokoa maisha ya George. Walifanikiwa kufika hospitali kuu ya taifa ya Muhimbili ndani ya muda mfupi kwa vile barabara haikuwa na foleni ya magari wakati huo. Bila kupoteza muda wauguzi walisogeza machela katika gari hilo na George alichukuliwa na kuwahishwa mapema katika chumba kilichokuwa cha upasuaji.

    Madaktari walianza kumfanyia matibabu huku wakiwa hawana imani kama mgonjwa huyo angepona. Alikuwa amevunjika mguu wa kushoto pamoja na majeraha mengi aliyokuwa nayo lakini pia alionekana alipata madhara zaidi katika kichwa chake. Mmoja wa madaktari aliyekuwa katika chumba hicho alimtambua George kuwa alikuwa mtoto wa mzee Innocent kwa vile alihusika katika matibabu yake ya kichwa wiki tatu kabla. Hakutambua jambo lililokuwa linamsumbua kijana huyo lililopelekea agongwe na gari kutokana na uzembe wake kama maelezo ya awali yalivyotolewa. Daktari huyo aliyeitwa Mutayoba alipanga kuhakikisha anaokoa maisha ya kijana huyo pekee wa mzee Innocent. Aliamini kuna jambo ambalo lilikuwa linaendelea dhidi ya kijana huyo lililopelekea achanganyikiwe.

    Baada ya saa moja na nusu la kukamilisha matibabu ya awali walimpeleka George katika chumba maalumu ili kumpiga picha zaidi wakiwa na lengo la kugundua kama alikuwa na tatizo jingine. Picha hizo ziliwakatisha tamaa zaidi madakari baada ya kugundua ubongo wa George ulikuwa umetikisika kwa kiasi kikubwa na kuacha nafasi yake. Hawakuwa na jinsi zaidi na walimwachia mwenyezi Mungu, walimpeleka katika chumba maalum akiwa na vifaa tofauti kichwani mwake ili kujalibu kurudisha ubongo wake sehemu husika. Mara baada ya zoezi hilo Mutayoba ambaye pia alihusika na matibabu hayo ya George aliamua kumpigia simu mzee Innocent na kumweleza ajali iliyompata mwanaye. Mzee huyo ambaye alieleza wakati huo alikuwa akimtafuta mwanaye aliahidi kufika hospitalini hapo baada ya muda mfupi.

    Baada ya nusu saa mzee Innocent akiwa na mkewe walifika hospitalini hapo na waliongozwa na daktari Mutayoba mpaka chumba ambacho George alikuwapo akiendelea na matibabu. Wazazi hao walichanganyikiwa na kujikuta kila mmoja wao akianza kulia kutokana na hali halisi aliyokuwa nayo George. Alikuwa akipumua kwa kutumia mpira maalum pia kulikuwa na mpira mwingine ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya chakula. Maelezo waliyopewa na daktari Mutayoba waliyeongozana naye ndiyo yaliwakatisha tamaa na walianza kuamini wangempoteza mtoto wao huyo pekee. Alikuwa katika hali mbaya lakini pia alikuwa hana fahamu, mzee Innocent hasira zake bado zilikuwa kwa mtu ambaye alihusika katika kupoteza ndoto za mwanaye. Aliamini yote yaliyoendelea kutokea yalikuwa matokeo ya picha za utupu ambazo mtoto wao alitolewa gazetini.Mutayoba aliwaahidi kujitahidi kadiri awezavyo ili kuokoa maisha ya George na alionyesha kuumia juu ya tatizo hilo la familia ya mzee Innocent.

    Hali ya matumaini dhidi ya afya ya George ilionekana kuzidi kupoteza mwelekeo kwani wiki mbili zilikatika pasipo dalili zozote za kuanza kupona. Jambo hilo lilimchanganya mzee Innocent na mkewe ambao walilala na kushinda hospitalini hapo, wakati huo shughuli za mzee huyo ziliendelea chini ya usimamizi wa mdogo wake aliyeitwa Henry. Hakuwa tayari kumpoteza mwanaye huyo, kwa gharama yeyote aliwaza kuitumia ili kuokoa maisha yake. Alipewa ushauri wa kuendeleza matibabu ya mwanaye hospitalini hapo baada ya mawazo yake ya kutaka kumpeleka nchini Uingereza kwa matibabu zaidi. Mzee huyo hakuonekana kama tajiri kwani siku zote alikuwa akizunguka hospitalini hapo na zaidi karibu na chumba alicholazwa mwanaye. Muda wote alikuwa akisubiri na kutarajia angeambiwa mwanaye alikuwa amerudiwa na fahamu.

    Wanafunzi wachache waliosoma pamoja na George walikuwa wakifika hospitalini hapo kumtaza na walikuwa wakitokwa na machozi kwa jinsi alivyokuwa katika hali mbaya. Mama yake George hakufurahishwa na tabia ya Winnie ambaye alikuwa mchumba wa mwanaye siku za nyuma kwani hakuwahi kufika hospitalini hapo. Aliamini angefika siku moja ili kumtazama George ingawaje walikuwa wameachana, aliwaza kumweleza ukweli juu ya vile alivyoamini kuwa mwanaye hakuwa na makosa. Siku zilipita hata mwezi ukaisha lakini Winnie hakufika hospitalini hapo kumtazama George jambo lililomuumiza sana mama yake. Hatimaye aliamua kumtoa akilini kama angefika hospitalini hapo kumwangalia mwanaye ambaye hali yake bado ilikuwa mbaya.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja wakati mama huyo akiwa kando ya kitanda cha George kama ilivyokuwa kawaida yake aliingia dada mmoja akiwa na maua kadhaa ambaye mama huyo hakumtambua. Mara baada ya salamu dada huyo alimwangalia George kwa huruma kabla ya kutokwa machozi lakini alionekana hakuwa na jambo la kufanya. Aliketi na kuanza kumweleza mama huyo, alikuwa ametumwa kufikisha maua hayo na Winnie ambaye hakuwa tayari kufika eneo hilo. Alikuwa ameambatanisha na ujumbe mfupi uliokuwa kwenye bahasha, mama yake George alipokea na kuweka kwenye meza iliyokuwapo karibu. Baada ya maongezi ya muda mfupi dada huyo aliaga na kuondoka akimwacha mama huyo.

    Aliamua kuchukuwa bahasha ambayo iliambatanishwa na maua hayo na kuifungua akiwa na lengo la kusoma ujumbe uliokuwapo. ‘George pole nasikia unaumwa, pole sana nakuombea upone ili uendelee na maisha yako, kiukweli uliniumiza sana lakini kwa sasa nimepata faraja kwani nimempata mtu anayenijali, Sijaweza kufika kwani sipendi kukumbuka jinsi ulivyonitenda. Siku njema’ alimaliza kusoma ujumbe huo uliopelekea atokwe na machozi. Aliona ni bora ulimfikia yeye na si mwanaye ambaye bado hakuwa na fahamu kwa vile aliamini angechanganyikiwa zaidi. Jambo ambalo lilianza kumuumiza kichwa lilikuwa juu ya mahusiano mapya ambayo Winnie alionekana kuyaanza. Aliamini jambo hilo lilikuwa hatari kama George angepona na kuligundua kutokana na upendo alioufahamu wa mwanaye kwa mrembo huyo.

    Tayari Winnie alikuwa amemaliza masomo yake ya chuo na zaidi alikuwa na uhusiano na Frank Joseph aliyekuwa mtoto wa waziri. Waliaanza uhusiano huo mwezi mmoja baada ya kuachana na George, hiyo yote ilitokana na faraja aliyoipata toka kwa kijana huyo. Frank alikuwa mtu wa karibu baada ya mkasa huo na alionekana kumshauri mambo mengi yaliyompa faraja jambo lililopelekea waanze uhusiano wao. Siku zote Winnie hakupenda kusikia jina la George hata wakati huo alikuwa haelewi kwa kiasi gani alikuwa akiumwa. Watu kadhaa waliojaribu kumsimulia juu ya matatizo ya mchumba wake huyo wa zamani alikuwa akiwakatisha kabla hawajamaliza.

    Alimtuma rafiki yake akampe George ujumbe mfupi aliouandika akiwa anaamini alikuwa na matatizo ya kawaida. Jambo lililompa taabu lilihusiana na ugumu wa kumsahau George kichwani mwake, alikuwa akimpenda Frank lakini kumbukumbu juu ya kijana huyo zilikuwa hazimtoki kichwani. Hakuwa tayari hata kidogo kurudiana na George jambo lililomfanya apende kuwa karibu na Frank ili amsahau kabisa. Zoezi hilo lilionekana kuwa gumu kwani alikuwa akipokea simu za rafiki zake waliokuwa wakiongelea suala la yeye kumtembelea George. Hivyo aliamua kuandaa safari na Frank kwenda kupumzika Ufaransa, lengo lake lilikuwa kujenga uhusiano wao lakini pia alikuwa na lengo la kumsahau George. Jambo hilo la kuandaliwa safari halikuwa gumu kwa vile balozi wa Ufaransa nchini mr. Gregory na Waziri wa nchi mr. Joseph walikuwa wakiutambua vyema uhusiano wa wanao ulioendelea. Hatimaye Winnie na Frank waliondoka nchini wakielekea jijini Paris, Ufaransa ambako mr. Gregory alikuwa na nyumba yake katika jiji hilo.

    Tayari miezi kadhaa ilikuwa imepita pasipo dalili zozote za kupona kwa George hata mzee Innocent na mkewe walishaanza kukata tamaa. Siku moja wakiwa wanaendelea na uangalizi huo dhidi ya mtoto wao majira ya asubuhi walichanganyikiwa na mshtuko alioutoa baada ya kuanza kujitupa mikono na miguu eneo hilo alilokuwapo. “daktari! daktari!....” ilikuwa sauti ya mzee Innocent akipiga kelele kuwaita madaktari. Sauti yake ilisikika vizuri na kumfanya Mutayoba awe daktari wa kwanza kufika katika chumba hicho kilichokuwa maalum kwa ajili ya George. Alimwomba mzee Innocent wasaidiane kumshika George ambaye alikuwa bado akirusha mikono na miguu, jambo ambalo walifanikiwa na baada ya muda alitulia kabisa. Baada ya dakika kumi madaktari wanne waliongezeka katika chumba hicho na walimtaka mzee Innocent na mkewe waondoke.

    Walikuwa wamechukua vifaa tofauti vilivyohusika kuchukua vipimo mbalimbali na lengo lilikuwa kumfanyia uchunguzi George. Mzee Innocent alikuwa nje ya chumba hicho akiwa amemkumbatia mkewe aliyekuwa analia, kulikuwapo na rafiki zake kadhaa waliofika kumwangalia mwanaye asubuhi hiyo ambao walikuwa wakiwafariji. Tukio alilolifanya George lilikuwa limewapa picha ya kuwa alikuwa ameshapoteza maisha.Mzee Innocent alikuwa akisali kimyakimya sala ambazo hakuzimaliza kutokana na hofu ya majibu kuhusu mwanaye ambayo aliamini angeyapata baada ya muda mfupi. Baada ya nusu saa mlango wa chumba hicho ulifunguliwa na daktari mmoja alitoka akiwa hana furaha, alipokelewa na swali toka kwa mzee Innocent. “niambie daktari mwanangu anaendeleaje?” “subiri utaambiwa lakini naamini hatma ya siku zote imepatikana” aliongea daktari huyo akiwa anaondoka eneo hilo katika mwonekano wa kushidwa kuokoa maisha ya George. Maelezo hayo yenye utata aliyowaachia yalimkatisha tamaa mzee Innocent na mkewe ambao wote kwa pamoja walianza kulia wakiamini tayari walikuwa wamempoteza mtoto wao.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/







    ITAENDELEA  

0 comments:

Post a Comment

Blog