Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA - 2

 

     





    Simulizi : Kwenye Siku Yangu Ya Kuzaliwa

    Sehemu Ya Pili (2)





    Kiti alikuwa mita zipatazo sita kutoka walipo mama na bibi yake simu yake ya mkononi ilipoita. Aliitoa mfukoni ilimokuwa, alipotazama kwenye kioo cha simu hiyo ilisomeka namba ngeni, aliitazama ile namba, akajaribu kuikumbuka bila mafanikio. Akabashiri kuwa; yawezekana ni Mina ndiye anayempigia. Sababu ya kubashiri hivyo, ilikuwa ni hali aliyoigundua kwa Mina mara macho yao yalipokutana kwa mara ya kwanza kwenye sherehe ya Boniphace Mayunga na Emmy Schzilakta, ikiwa ni miaka mingi tangu walipoachana. Wote walishtuka, lakini Mina ndiye aliyeshtuka zaidi. Macho ya Mina yalionesha matamanio mapya ya kimapenzi, jambo ambalo Kiti alilitambua kwa msaada wa elimu kidogo ya saikolojia aliyokuwanayo.

    Kwa sababu hawakupata wasaa wa kukutana tena baada ya pale, Kiti aliamini kwa vyovyote vile, ni lazima Mina atafanya juu chini ili apate mawasilainao yake. Kama hataenda nyumbani kwao, basi atamfuata mmoja kati ya Bony au Emmy ili ampe namba zake za simu.

    Kiti aliipokea ile simu huku imani yake ikimtuma kuamini ubashiri wake kwa sababu alizozidhania. Aliiweka simu sikioni bila kuongea, alipanga hivyo kwa lengo la kutegea ili aisikie sauti ya mpigaji.

    “Hallow,” sauti kutoka upande wa pili ilisikika. Ilikuwa ni sauti nyororo ya kike iliyopenya sawia kwenye ngoma ya sikio lake la kushoto, sikio ambalo Kiti hulitumia kusikilizia simu.

    Kusikika kwa sauti hiyo kulimfanya Kiti afifishe imani kwenye ubashiri wake ambao awali ulimfanya aamini kuwa yuko sahihi kwa zaidi ya asilimia sabini. Unyororo wa sauti hiyo ndiyo ulififisha imani yake kuwa; yawezekana huyo si Mina kwa sababu, sauti ya Mina si nyororo na hiyo ndiyo ilikuwa nduni kuu ya sauti ya Mina.

    “Ni nani sasa?” Kiti aliwaza kabla hajasema, “Hallow,” ili kuruhusu mazungumzo.

    “Habari yako Mr Kitiheka?” sauti kutoka upande wa pili iliuliza ili kumjulia hali.

    Tafakuri juu ya sauti hiyo bado iliendelea kumtesa Kiti, hakuwa ametambua ni nani anayeongea. Baada ya kuwa amejihakikishia kuwa huyo si Mina, Kiti alibadiri ubashiri wake na safari hii alielekeza upatu wake kwa Wayeka, akajibu, “Salama Wayeka, mambo?”

    “Powa jamani, umejuaje kuwa ni mimi?” Wayeka aliuliza na kusababisha tabasamu la Kiti liwe peupe.

    “Masaa matatu tuliyokuwa pamoja usiku wa jana yalitosha kabisa kuiweka akilini sauti yako, pamoja na namna yako ya uongeaji,” Kiti alidanganya ili kuziteka zaidi hisia za Wayeka.

    “Mh... haya. Mi niko home tayari, nimefika kama saa moja lililopita,”

    “Home wapi, Nyamuswa?”

    “Ndiyo, niko Nyamuswa,” Wayeka alisisitiza.

    Taarifa za Wayeka kuwa Nyamuswa ziliibua hisia mpya kwa Kiti. Alitamani akutane naye katika muda huohuo. Hakujua ni kwa nini alipatwa na hisia hizo, yeye alichotaka ni kumuona tu.

    “Nami niko Nyamuswa Wayeka, naweza kukuona?” Kiti aliuliza.

    Wayeka hakuamini moja kwa moja kama kisemwacho na Kiti kina ukweli ndani yake, “Acha utani bhana... unafanya nini huku kijijini kwetu?”

    “Siyo kwenu tu, hata mimi hapa Nyamuswa ni kwetu pia. Wazazi wangu walizaliwa hapahapa Nyamuswa,”

    “Kama kweli uko Nyamuswa naomba nikuone,” alisema Wayeka.

    “Hakuna shida, niambie tuonane wapi,” Kiti alisema katika hali ya kujiamini.

    “Njoo moja kwa moja mpaka nyumbani, ni hapa karibu na Kanisa Katoliki. Muulize mtu yeyote kwa mzee Ayuyube atakuonesha,”

    “Ok, nipe dakika kadhaa nitakuwa hapo,” alisema Kiti na kukata simu tayari kwa kwenda nyumbani kwa kina Wayeka.

    Kabla hajaondoka, Kiti aliona ni vyema endapo atamjulisha mama yake kuwa anatoka kidogo ili asije akapata tabu kumtafuta. Kiti alipofika kwa mama yake mambo yalikwenda ndivyo sivyo. Alikutana na taarifa iliyomnyong’onyesha, “Hatuna muda wa kupoteza Kiti, baba yako amerudi na hali yake siyo si nzuri... anaumwa,” alisema mama yake na Kiti huku akisimama kuelekea kwenye gari.

    Kiti hakuwa na namna. Ilimbidi kukubaliana na maneno ya mama yake akaenda kwenye gari tayari kwa kuondoka kwa sababu; asingeweza kujenga hoja kwa mama yake ili avute subira kwanza akaonane na Wayeka halafu ndiyo waondoke, angeanzia wapi?
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aidha taarifa ya ujio wa baba yake ambaye amefika huku hali yake ikiwa si nzuri kiafya ilimsukuma Kiti kuingia kwenye gari tayari kwa kuondoka. Ni miaka sita sasa tangu waonane na baba yake kwa mara ya mwisho kabla hajaenda Marekani kwa masomo, na jana aliporudi hakumkuta kwa sababu alikuwa Nairobi, Kenya kwa safari ya kibiashara. Kiti hakuwa na jinsi ilimlazimu kuondoka.

    Kiti aliingia kwenye gari huku akili yake ikiwaza ni namna gani atamueleza Wayeka amuamini kuwa kweli alikuwa Nyamuswa, ikiwa ni mara ya kwanza kupanga naye miadi ambayo haikutimia. Hakutaka kabisa kuonekana mswahili kwa mrembo huyo. Aliwaza na kuwazua, mwisho akaamua amtumie ujumbe mfupi wa maandishi uliosomeka hivi, “Sory wangu, unaweza kudhani mimi ni muongo kwa sababu unayo kila sababu ya kudhani hivyo. Ni kweli nilikuwa hapa Nyamuswa, lakini sa’ivi niko kwenye gari naondoka, kuna dharura nyumbani, baba ni mgonjwa sina budi kuondoka. Ukipata wasaa pita hapa kwa bibi yangu, anaitwa Koyonga, pita umjulie hali…” alihitimisha Kiti na kubonyeza kitufe ilichoruhusu ujumbe wake uende kwa Wayeka, ukaenda.

    Punde simu yake ilitoa mlio ulioashiria kuwa kuna ujumbe mfupi umeingia. Aliichukua simu yake, akaufungua ujumbe ule na kuanza kuusoma, “Niljua tu, unanidanganya,”

    Ujumbe huo kutoka kwa Wayeka uliuchoma moyo wa Kiti na kumfanya ajihisi mwenye hatia licha ya kutokuwa na hatia. Alichokifikiria ndiyo hicho kilikuwa kinatokea.



    4

    COSMAS alikuwa chumbani kwake amejilaza kitandani chali, huku mkono wake wa kuume ukiwa umeshikilia simu yake ya mkononi. Alikuwa akiitumbulia macho picha ya Wayeka ambayo alimpiga siku tatu zilizopita walipokuwa kwenye sherehe ya kuazimisha siku ya kuzaliwa kwa Bony na Emmy.

    Licha ya picha hiyo kutoonekana sawasawa, bado ilimridhisha Cosmas. Picha hiyo ilimfanya mara kadhaa avute taswira akilini mwake, taswira ya jinsi Wayeka alivyoumbwa, pamoja na sauti yake nyororo aliyojaaliwa, sauti ya kumtoa nyoka pangoni.

    Alitarajia kupokea simu kutoka kwa mrembo huyo muda wowote tangu siku ya pili baada ya siku ile ya sherehe. Alikuwa na matarajio hayo kwa sababu aliibana business card yake kwenye kadi ya mwaliko ya Wayeka, kadi ambayo iliwekwa kwenye mkoba wa Wayeka sambamba na kadi hiyo ya mwaliko.

    Cosmas alifanya hivyo kwa sababu; aliamini kuwa, endapo kadi yake ingekutwa kwenye mkoba wa Wayeka, ni wazi kuwa ingeibua maswali ambayo yangemsumbua kiasi cha kumpa shauku ya kutaka kujua ni kwa vipi kadi hiyo ilifika kwenye mkoba wake, na huyo Cosmas ni nani. Jambo ambalo lingemsukuma mrembo huyo katika uamuzi wa kupiga simu ili apate majibu ya maswali yake. Na huo ndio ungekuwa wasaa wa kufungua ukurasa mpya ambao ungemsababishia Cosmas kutimiza lengo lake. Hilo ndilo alilolitarajia Cosmas.

    Ilipita siku ya kwanza, ya pili na sasa ya tatu ilikuwa ikielekea ukingoni bila dalili zozote za simu ya Wayeka. Cosmas alikuwa akiwaza ni vipi atampata tena Wayeka ikiwa mbinu yake ya kwanza haikuzaa matunda.

    Alijilaumu ni kwa nini hakuutumia wasaa ule kumsaili Wayeka kiundani, “Ule ndiyo ulikuwa muda mzuri wa kuchukua hata namba yake...” Cosmas aliwaza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Siku nyingine sitarudia tena kosa kama hili… ona sasa imani yangu imeniponza!” sauti ilimtoka Cosmas huku akiiweka simu yake pembeni ili ausake usingizi.

    Alilala kiubavu, akiulalia ubavu wa kulia kisha akafumba macho kwa kusudi la kuupata usingizi kwa haraka zaidi. Alijidanganaya!

    Usingizi haukumjia mapema Cosmas na badala yake alijiwa na taswira ambzo ziliupeleka usingizi wake mbali zaidi na kumfanya auone usiku ule kuwa ni usiku mrefu kuwahi kutokea maishani mwake.

    Taswira hizo zilimchukua Cosmas mpaka kwenye lindi la mawazo yaliyomfanya aingie katika tafakuri nzito juu ya maisha yake, “Nitaishi hivi mpaka lini?” Cosmas aliwaza.

    Mawazo hayo ndiyo yaliyomfanya aanze kuyafikiria upya maisha yake, maisha ya kubadilibadili wanawake kila kukicha aliyaona ni kama vile yanaudhihaki umri wake, “Inabidi nioe... inabidi nioe ili niepukane na maisha haya ya kishenzi...” aliendelea kuwaza Cosmas.

    Mawazo yaliendelea kumtafuna zaidi kabla hajapitiwa na usingizi ambao ulimpeleka kwenye ulimwengu wa ndoto. Cosmas aliota kuwa:

    Stella ambaye aliwahi kuwa mpenzi wake alimfuata nyumbani kwake huku akiwa analia na kumwambia, “Cosmas… Cosmass… uliniharibia maisha yangu Cosmas. Ulinilaghai nikaacha shule kwa ahadi kuwa utanioa….

    Nikagombana na wazazi wangu kisa wewe Cosmas… ona sasa nalandalanda mitaani kama mtu mwenye laana ya ulimwengu mzima, hakuna anayetaka kuniona wala kunisikia… yote hii ni kwa ajili yako. Nakuapia Cosmas… nakuapia… kama si wewe uliyeniharibia maisha yangu basi na uishi kwa furaha daima.” Alipomaliza kusema maneno hayo tu, akaanza kubadilika polepole mwisho akawa Simba aliyeunguruma, “Ngrrri…ngrrr…” aliunguruma huku akimsogelea Cosmas.

    Ghafla Cosmas alishtuka usingizini akiwa anahema kwa kasi isiyoelezeka na kukuta simu yake inatoa sauti ya mlio wa kutegesha, alarm!

    Cosmas aliinyanyua simu yake kwa lengo la kuangalia saa, ilikuwa tayari ni saa 12:30 asbuhi, muda ambao alistahili kuamka ili ajiandae kwenda kazini. Alifanya maandalizi yake, kisha akaenda kazini ambako mambo hayakumwendea vyema kwa sababu ya ndoto aliyoiota, ndoto ya Stella.

    ****

    Stella Kamugisha ndilo jina alilojitambulisha baada ya kuwa ameitwa na Cosmas. Ni jina lake halisi. Wakati huo Cosmas alikuwa ni dereva wa lori ambalo lilikuwa ni mali ya Lake Fish Company, kampuni ambayo ilijishughulisha na usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara mjini Musoma, na wakati huo Stella alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya wasichana ya Songe.

    Alipoitwa na Cosmas hakuwa mkaidi, aliitika wito na baadaye akapewa maneno ambayo pia hakuyapinga. Wakafungua ukurasa mpya wa mapenzi baina yao, ingawaje katika mizania isiyolingana! Wakati ambao Stella alihesabu amepata mpenzi ambaye siku ikifika atakua mume wake na ikibidi wawe na familia, kwa Cosmas ilikuwa ni tofauti kabisa. Cosmas alimchukulia Stella kama msichana tu wa kupitisha naye wakati, yaani ‘demu’ kama walivyo mademu wengine ambao amewapanga karibia kila mahali ambapo gari lake lilipita. Alikuwa nao wahudumu wa Bar, mama n’tilie ambao wengine ni wake za watu na wanafunzi kama Stella ambao idadi yao kamili hakuwa nayo.

    Alipokutana naye kwa mara ya kwanza, Stella alikuwa mbichi, kinda kabisa, yaani mgeni katika ulimwengu huo wa mahaba. Japo aliumizwa katika harakati za kuvuliwa usichana wake, Stella alijikuta akitamani tena kulirudia tendo lile ambalo lilikuja kumtia uchizi na hatimaye kuacha shule kabisa ili aolewe!

    Hakuna hata mmoja kati ya wazazi wake aliyemuelewa kwa uamuzi wake huo. Walipomshauri ikawa ndiyo tikiti ya kuhama nyumbani. Akaenda kwa Cosmas ambaye alisafiri naye kila mahali, mara; Kisorya, Kibara, na sehemu nyingine nyingi ambako Cosmas alitumwa na mwajiri wake kukusanya samaki.

    Wazazi wake walimtafuta bila mafanikio, mpaka alipotemwa na Cosmas kama kapi la muwa ndiyo Stella akarejea nyumbani ambako pia alifukuzwa. Akayaanza maisha mapya, maisha yasiyo na hata chembe ya furaha kwa sababu hakuna aliyemthamini…

    Alijaribu kila mbinu ya kutafuta pesa kwa ajili ya kujikimu kimaisha. Alitafuta kazi ya kuuza Bar, hakuna aliyempatia! Na kuna wakati alijaribu kujiuza kama changudoa ili tu aweze kuyaendesha maisha yake, lakini huko nako hakupata vuno lililoyakidhi mahitaji yake. Akajiunga na kundi la wahalifu waliojishughulisha na uvunjaji wa nyumba za watu kwa nia ya kuiba. Ikawa kama ule msemo wa waswahili usemao: asiye bahati habahatishi. Stella alikamatwa katika siku ileile ya kwanza alipojiingiza kwenye shughuli hiyo haramu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa mujibu wa sheria, Stella alihukumia kwenda jela miaka miwili baada ya kuwa amepatikana na hatia. Alikaa jela kwa miaka miwili akitumikia kifungo chake, huku akiomba usiku na mchana amalize muda wake salama salimini ili amtafute Cosmas kwa lengo la kulipa kisasi, kwani ndiye chanzo cha maisha yake kwenda mrama.

    ****





    ****

    Ilikuwa ni siku ya nne tangu Kiti atoke Nyamuswa alikokwenda na mama yake kwa lengo la kumsalimia bibi yake. Siku nne baada ya ahadi yake ya kwanza kwa Wayeka kutotimia.

    Tangu alipoondoka Nyamuswa siku ile, Kiti aliendelea kuwasiliana na Wayeka kwa njia ya ujumbe mfupi wa mandishi na simu za sauti. Katika mawasiliano yao, Kiti aliendelea kuomba msamaha kwa Wayeka. Alijaribu kumuelewesha kuwa; dharula iliyojitokeza ndiyo ilipangua ahadi yao ghafla.

    Haikuwa rahisi kueleweka kwa Wayeka, lakini Kiti naye hakukoma kumuelewesha huku akimuweka wazi kuwa hiyo si tabia yake.

    Watu husema, “Hata mnyororo mgumu una eneo lake la udhaifu”. Au kama waswahili wasemavyo: kamba hukatikia pembamba. Ndivyo ilivyokuwa kwa Wayeka. Jitihada za Kiti zilimlainisha Wayeka hatimaye akalainika na wakapanga tena miadi mingine, miadi ambayo ilimtaka Wayeka kusafiri hadi Bunda mjini kwa ajili ya kukutana na Kiti.

    Mawasilianao yao ya mara kwa mara katika muda huo wa siku nne, yalisababisha kuibuka kwa hisia za kimapenzi baina yao. Licha ya kutotamkiana bayana kwa sababu ya utegezi wa midomo yao, lakini ukweli unabaki palepale kuwa Kiti alianza kumpenda Wayeka halikadhalika Wayeka pia alianza kumpenda Kiti, walipendana.

    Hatimaye siku ya siku ilifika.

    Wayeka ndiye aliyeanza kumpigia simu Kiti. Ilikuwa ni mita chache kabla hajafika kenye barabara ya lami ambayo inaunganisha mji wa Mwanza na ule wa Musoma. Wakati huo yeye alikuwa bado yuko kwenye barabara ya vumbi itokayo Nyamuswa, ndipo akaichukua simu yake na kumpigia Kiti.

    “Hallow Kiti…” Wayeka alilitaja jina la Kitiheka kwa ufupi, namna ambayo aliichagua yeye katika kumuita.

    “Yes... Wayeka, nambie…” Kiti alijibu.

    “Nimeshaingia Bunda tayari… uko wapi?

    Kiti alikuwa ni kama asiyeamini baada ya kusikia hivyo, “Oooh! My dear, very good… niko hapa NMB, wewe uko wapi?”

    “Nami niko hapa usawa wa NMB”

    “Ok, nipe dakika sifuri nije hapo nje,” alisema Kiti huku akiianza safari ya kutoka nje baada ya kuwa amemaliza shughuli iliyompeleka hapo benki. Alitoka huku simu yake ikiwa sikioni akiendelea na mazungumzo.

    “Uko na gari gani?” Kiti aliuliza.

    “Ukitoka tu utaiona Starlet nyeusi, ndiyo gari pekee yenye rangi nyeusi iliyoko hapa nje”

    “Ok, nimeshaiona,” alisema Kiti na kukata simu.

    Kiti aliifuata ile gari aliyoelekezwa na Wayeka, alipofika alifungua mlango na kujitoma ndani ambako walitazamana kwa muda kama wa nusu dakika bila kusema neno lolote huku tabasamu zikishamiri kwenye nyuso zao, kisha Wayeka akaanza kwa kusalimia, “Mambo jamani?”

    “Ilimchukua tena Kiti muda wa nusu dakika mpaka kujibu ile salamu ya mwenzi wake. “Powa tu, shwari?” alisema Kiti akiwa amekaa kwenye kiti cha abiria na Wayeka aliyekuwa ameenea barabara kwenye kiti cha dereva alijibu, “Shwari.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tabasamu liliendelea kushika hatamu huku wakitazamana kama mazezeta mpaka Wayeka alipouliza, “Uelekeo ni wapi?”

    “Twende pale tulipokutana kwa mara ya kwanza,”

    “CN?” Wayeka aliuliza ili kupata uhakika.

    “Yeah, hapo hapo.” Kiti alijibu na mara gari likapindishwa kulia, likaingia kwenye barabara ya lami na safari ya kuelekea CN ikaanza.

    Kutoka mahali ilipo benki ya NMB, tawi la Bunda kuelekea CN Hotel hapakuwa na umbali mrefu. Kiasi kwamba hawakusema hata neno, tayari walikuwa kwenye maegesho ya magari yaliyokuwa kwenye hoteli hiyo ya CN. Wakati huo saa ya kwenye gari ilionesha kuwa ni saa 9:00 Alasiri.

    Waliteremka kutoka kwenye gari, wakaongozana hadi ulipo ukumbi wa hoteli hiyo. Wakakaa kwenye meza ambayo waliichagua baada ya kuona kuwa hiyo ndiyo itakayowapa faragha kwa sababu ilikuwa mbali na meza nyingine, wakakaa.

    Kabla hata dakika haijaisha, alikuja mhudumu ambaye aliwasalimu kisha akawapa orodha ya vyakula vinavyopatina hotelini hapo. Walifanya uchaguzi wao, walipomaliza yule mhudumu aliondoka na mazungumzo baina yao yakaanza tena, “Enhe za kunidanganya?” Wayeka alianzisha mazungumzo kwa swali.

    “Najua inaweza ikawa ngumu sana kuniamini…laiti ungeenda kwa bibi kama nilivyokuambia siku ile, angekueleza hali ilivyokuwa. Labda hapo ndiyo ungeweza kuniamini kirahisi,” alisema Kiti kwa kutoa maelezo yaliyodhihirisha kuwa alikuwa anajitetea.

    “Nakutania mwaya... nilienda kwa bibi yako, akanieleza kuwa ni kweli ulikuwepo siku hiyo na mliondoka ghafla baada ya mama yako kuwa amepigiwa simu.” Alisema Wayeka na kufufua furaha ya Kiti ambayo ilikuwa imeanza kupotea baada ya swali la awali la Wayeka ambalo ni kama lilikuwa likimshitaki.

    Kabla Kiti hajapata kusema neno lolote, Wayeka alisema tena, “Mnh, halafu bibi yako ana maswali kwelikweli… mpaka nilijuta kwenda”

    “Maswali gani tena?”

    “Kwanza nilipofika siku hiyo nilimsalimia... alikuwa ameshanisahau, nilipomkumbusha kuwa mimi ni mtoto wa mzee Ayuyube ndiyo akakumbuka. Hapo ndipo aliponitwanga swali,”

    “Aliulizaje?” Kiti alihoji.

    “Mh! Ana masikhara sana yule bibi, aliuliza kama mimi ndiye mwenga mwenyewe,” Wayeka alisema na kumalizia kwa kucheka, Kiti naye akacheka, wote wakawa wanacheka.

    Haukupita muda mrefu, mvinyo aina ya Saint Anna uliletwa na mhudumu, ambaye aliufungua na kumimina kiasi kwenye glasi mbili alizokuja nazo.

    Wakati mhudumu anaendelea na zoezi lile la kumimina mvinyo kwenye glasi, alikuja mhudumu mwingine ambaye alileta samaki wa kuchoma aina ya sato sambamba na ugali wenye rangi nyekundu, ugali ambao ni mchanganyiko wa unga wa muhogo na mtama.

    Waliendelea kula huku mazungumzo ya hapa na pale yakiendelea baina yao.

    “Nakumbuka siku ile kwenye sherehe uliniambia kuwa una mpango wa kuanzisha biashara yako ambayo tayari soko la bidhaa linakusubiri wewe tu upeleke mzigo sokoni, vipi umefikia wapi?” Wayeka aliuliza.

    “Yeah, ni kweli, suala hilo lipo kwenye mchakato kwa kuandaa eneo la ofisi na pindi litakapokamilika tu, nitaanza kufuatilia vibali serikalini,” alijibu Kiti kabla hajachukua karatasi laini kwa ajili ya kufutia midomo yake baada yakuwa amemaliza kula.

    “Na eneo la kiwanda, umepanga liwe wapi?”

    “Kiwanda kitakuwa Nyamuswa, baba amependekeza iwe hivyo kwa sababu; anataka pia tutengeneze biskuti ambazo zitatokana na viazi vitamu ambavyo huku vinapatika kwa wingi”

    “Biskuti za viazi vitamu! Ndiyo zikoje hizo?” Wayeka aliuliza huku macho akiwa kayatoa pima kwa mshangao.

    “Utaziona tu mara uzalishaji utakapoanza,”

    “Makubwa hayo,” Alisema Wayeka kisha akaielekea glasi yake ya mvinyo. Alipiga mafunda kadhaa kabla hajairudisha tena mezani. Akamtazama Kiti vizuri kwa zaidi ya mara moja, huku akitamani asikie kile ambacho muda wote alitamani atamkiwe na Kiti.

    Kuna wakati alitamani aseme yeye, lakini hakuwa na ujasiri huo kwa hofu kuwa ataonekana ni Malaya. Mwisho akapiga moyo konde, “Liwalo na liwe mimi namwambia,” Wayeka aliwaza.

    Alijikohoza kidogo kwa lengo la kusafisha koo kabla hajaongea huku akimtazama Kiti kwa jicho ambalo liliashiria jambo zito alilokuwa nalo moyoni. Lakini kabla hajapata kuinua midomo yake kulumba sauti nzito ya Kiti ikasikika, “Wayeka..” Kiti aliita.

    Wayeka akaitika, “Bee..” kisha akatega sikio kwa umakini ili kusikia ambacho Kiti anataka kusema huku mapigo ya moyo wake yakiwa na kasi isiyoelezeka.

    Kama ilivyokuwa kwa Wayeka, Kiti naye alijikohoza kwa lengo la kusafisha koo lake, lakini tofauti na Wayeka yeye alifanikiwa kulumba, “Nakumbuka uliniambia kuwa uko single, siyo?”

    “Ndiyo,” Wayeka alijibu.

    Kimya cha sekunde kadhaa kikajiunda baina yao kisha Kiti akaongea tena, “Kama ilivyo kwangu, nami pia niko single…” Kiti alisita kidogo, akamtizama Wayeka ili kumsaili umakini wake, naam, Wayeka alikuwa makini akimsikiliza.

    Usikivu wa Wayeka lilikuwa ni jambo lililomtia matumaini Kiti, akaendelea, “… maisha ya ukapela yananiwia magumu Wayeka, unaonaje kama tutakuwa wachumba?” alisema Kiti huku macho akiwa ameyaelekeza kwa Wayeka.

    Wayeka alishusha pumzi ndefu kisha akamtizama Kiti huku macho yake yakiwa yametawaliwa na aibu ambayo ilimnyima kabisa ujasiri kiasi cha kumfanya ashindwe kukabiliana na macho ya Kiti ambayo yalikuwa yamesheheni ujasiri.

    Wayeka alitaka kusema neno lakini alishindwa.

    Ni kweli alihisi kumpenda Kiti kabla hata hajafunga safari ya kuja Bunda, na alipofika Bunda, hapo hotelini, tena muda mfupi uliopita alikata shauri la kutaka kusema yanayomsibu, kwa maana ya kuzieleza hisia zake kwa Kiti. Lakini kabla hajasema, Kiti akawa amemuwahi kwa kusema jambo lenye dhima ileile lakini kwa darajia tofauti kabisa na ambayo hakuitarajia kuwa inaweza kuwa ghafla kiasi hicho.

    Wayeka alitarajia kusikia tu neno ‘nakupenda’ kutoka kwa Kiti, huku akifafanua aina ya upendo alionao dhidi yake.

    “Unaonaje kama tutakuwa wachumba” kauli hiyo ya Kiti ilifanya mwangwi uliojirudiarudia kwa mara kadhaa kichwani kwa Wayeka. Katika hali ambayo haikutarajiwa, Wayeka alijikuta akiyarudia kwa sauti yale maneno yaliyosemwa na Kiti kama asiyeamini. “Tutakuwa wachumba?” ikawa kama ameuliza swali.

    “Ndiyo Wayeka… tena uchumba ambao utadumu kwa muda mfupi kabla hatujafunga ndoa,” Kiti alisisitiza kwa kufafanua.

    Ufafanuzi wa Kiti ulizidisha hali ya mtanziko kwa Wayeka. Akaona kama vile mambo yanakwenda ghafla mno! Alitaka kusema neno, lakini hakujua aseme neno gani, akabaki mdomo wazi.

    Wakati ambao Wayeka alikuwa kwenye hangaiko la moyo lililomfanya aonekane kama punguani kwa sababu ya maneno ambayo ametoka kuyasikia kwa Kiti muda mfupi uliopita. Alikaa kimya kwa muda kabla sauti haijamtoka, “Kitiheka..” ikawa ni kwa mara ya kwanza tangu walipoonana pale benki Wayeka kulitaja jina la Kitiheka kwa ukamilifu wake. Alizoea kumuita ‘Kiti’ ambacho ni kifupi cha jina lake. Wayeka aliita kisha kama ilivyokuwa awali alishusha pumzi ndefu kisha akasema, “Imekuwa ghafla sana Kiti, kwa nini…” kabla hajamalizia kauli yake Kiti alimkatisha , “Najua kuwa kwako imekuwa ghafla, lakini mimi nililifikiria hili mapema zaidi… mapema kabla hata hatujapanga uje Bunda,”

    “Naelewa Kiti, lakini….” Kauli ya Wayeka ilibaki ikielea na kuzusha maswali ambayo Kiti alijaribu kubashiri majibu yake.

    “Najua kuwa unataka muda zaidi wa kufikiri juu ya hili, ila ukweli ni huo.. nakupenda Wayeka.. nakupenda,” Kiti alihitimisha kisha akanyanyua glasi yake ya mvinyo, taratibu akaipeleka mdomoni huku macho yake kayaelekeza kwa Wayeka ambaye alikuwa hoi kwa mawazo.

    Ilishatimu majira ya saa 12:45 jioni, yaani saa moja kasarobo walipouacha ukumbi wa CN HOTEL. Waliongozana mpaka kwenye gari ambalo liliachwa kwenye maegesho, wakaingia kila mmoja kwenye nafasi yake kama walivyokuja.

    Walitazamana mule garini kwa muda kabla Wayeka hajasema, “Kiti..” alisita kidogo huku akiendelea kumtazama, halafu akaendelea, “….naomba nikuru-rush home halafu niwahi nyumbani kabla usiku haujawa mkubwa zaidi.”

    “Kwa nini usilale Bunda leo?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana, leo haiwezekani kwa sababu; niliwaahidi wazazi kuwa nitarudi, bado haitoshi, kesho natakiwa kuwasilisha mzigo kwenye halmashauri ya Butiama.”

    “Ok, siyo mbaya… ila tafadhali nakuomba uyafanyie kazi yote niliyokueleza,” alisema Kiti na wakati huo tayari Wayeka alishairuhusu gari.

    “Ulisema ni maeneo ya Nyasura?” Wayeka aliuliza ili kupata uhakika wa mahali wanapoelekea.

    “Ndiyo, nyumbani ni Nyasura”

    Gari likasaga lami kuelekea Nyasura, haikuchukua muda mrefu wakawa wameshafika mbele ya geti jeusi la nyumba ya mzee Ngomanzito, kwao na Kiti.

    Kabla Kiti hajashuka, alimsihi Wayeka japo aingie ndani lakini hakufanikiwa, “Siku nyingine Kiti… usijari,” alisema Wayeka kwa sauti iliyojaa deko la mahaba huku macho yake yakiwa yanatazamana na ya Kiti. Kutizamana huko kuliibua hisia ambazo zilibadili mapigo ya nyoyo zao na kusababisha kila mmoja aelemee upande ambao yuko mwenzake, walipokutana waliumana papi za midomo yao, wakaanza kunyonyana ndimi!

    Tendo la kunyonyana ndimi lilidumu kwa takribani dakika nzima na walipoachana walikuwa wanatazamana huku kila mmoja akiwa haamini kilichotokea.

    “Nakupenda Kiti,” sauti nyororo ya Wayeka ilipasua ngoma za masikio ya Kiti ambaye bila hiyana alijbu, “Nakupenda Wayeka… nakupenda sana,”







    ZILIPITA siku mbili tangu walipoachana mbele ya geti la nyumba ya kina Kiti ambako Wayeka alimsindikiza Kiti baada ya kuwa wametoka CN HOTEL walipokuwa.Licha ya mawasilianao ya simu yaliyokuwa yakiendelea baina yao, mawasiliano ambayo yalifanyika takribani kwenye kila saa la siku, hamu ya kila mmoja kuataka kuonana na mwenzie haikukoma. Si Kiti wala Wayeka wote walikuwa na hamu ileile ya kuonana tena.Jumbe nyingi walizokuwa wakitumiana zilikuwa ni za kimapenzi, kila mmoja akijaribu kueleza hisia zake kwa mwenzie, na ni kwa jinsi gani anapata tabu kwa kuwa mabali naye. Ni jumbe hizo ndizo zilizosababisha wapange tena miadi ya kuaonana.Walipanga kuonana lakini safari hii mahali pa kukutania hapakuwa Bunda wala Nyamuswa, walipanga kuonana Musoma mjini katika Hoteli ya MALT VILLA, na safari hii Wayeka akiwa wa kwanza kuwasili hotelini hapo ambapo alichukua chumba namba118 kilichokuwa ghorofa pili.

    Kiti aliwasili nusu saa badaye majira ya saa 11 jioni na kumkuta Wayeka akiwa kwenye restaurant ya hotelini pale akinywa shurubati iliyotokana na mchanganyiko wa embe na passion.Licha ya familia yake kumiliki magari ya kifahari zaidi ya matatu ambayo Kiti alikuwa na uhuru wa kwenda nayo mahali popote alipotaka, Kiti alienda Musoma kwa usafiri wa kawaida kabisa akichanganyikana na abiria wengine katika gari la kampuni ya BATCO.Alipofika alipokelewa na Wayeka ambaye mara tu alipomwona alisimama na kumkumbatia, akampiga mabusu mawili mazito yaliyoashiria upendo wake wa dhati kwa Kiti, Kiti naye hakuwa mzembe, aliyajibu mabusu huku akimminyaminya kimahaba baadhi ya sehemu za mwili wake na kumchanganya zaidi Wayeka.Walikaa kwenye viti wakitazamana katika hali ya matamanio, huku macho ya kila mmoja yakionesha kiu aliyonayo dhidi ya mwenzake.Mhudumu alileta shurubati nyingine kwa ajili ya Kiti, pamoja na chakula sahani mbili, moja ya Kiti na nyingine ilikuwa ni ya Wayeka, lakini chakula kilikuwa ni cha aina moja. Walikula huku mazungumzo ya hapa na pale yakiendelea baina yao. Kuna wakati walilishana, Kiti alimlisha Wayeka, Wayeka naye akamlisha Kiti. Walifanya hivi na vile ilimradi kuoneshana upendo. Kila aliyewatazama alijua moja kwa moja kuwa watu hao ni wapenzi wanopendana kwa dhati.Saa moja baadaye iliwakuta chumbani, kulekule namba 118 wakioneshana utundu, kila mmoja kwa kadiri alivyojaaliwa na muumba. Walipoona yatosha kwa muda huo walielekea bafuni ambako walioga na kuogeshana. Kuogeshana huko kuliwafanya waziamshe tena ashki zao na kujikuta wakiikata kiu yao wakiwa hukohuko bafuni.

    ****



    Wayeka alikuwa mbele ya kioo kikubwa kilichokuwemo chumbani mule. Alikuwa amevaa gauni fupi jekundu, gauni lililomkaa vyema na kumfanya aonekane mrembo zaidi. Alikuwa ameshika mkufu wa dhahabu tayari kwa kuuvaa. Alipoinyoosha mikono yake kwa lengo la kuuvaa mkufu ule, Kiti aliishika mikono laini ya Wayeka, akachukua mkufu ule na kumvalisha Wayeka huku akisema, “Huwezi kupata tabu wakati mimi nipo,”“Asante darling,” alisema Wayeka huku akimgeukia Kiti na kumkumbatia kimahaba.Kiti alikuwa ndani ya suruali nyeusi aina ya jeanz, na fulana nyekundu. Waliongozana na Wayeka kuelekea kwenye ukumbi wa disco uliokuwa hotelini pale kwa lengo la kwenda kuitakasa siku hiyo kwa muziki.

    ****



    Cosmas na Boniphace walifahamiana miaka miwili iliyopita. Walifahamiana katika mazingira ya kazi, ambapo, Cosmas alifika ofisini kwa Boniphace kwa ajili ya usaili baada ya kuwa ameona tangazo la kazi, kuwa kampuni ya MITI GENERAL TRADERS wanahitaji madereva.Cosmas alifika kwenye usaili akiwa ni miongoni mwa madereva walioitwa kwenye usaili huo. Mwisho wa usaili alikuwa amebahatika kuwa miongoni mwa madereva wawili wa kampuni ya MITI GENERAL TRADERS, kampuni uliyojishughulisha na ugavi wa vifaa vya hospitalini katika sehemu mbalimbali za nchi.Kwa sababu muda mwingi Bony walikuwa na Cosmas pamoja katika safari zote ambazo Bony alisafiri kikazi na binafsi, wawili hawa wakajenga mazoea yaliyopelekea kuzaliwa urafiki ambao baadaye ulikuja kuwa kama undugu. Ukaribu baina yao uliendelea hata baada ya Cosmas kuwa ameamua kuacha kazi ili asimamie biashara yake ya vipuri vya magari na pikipiki aliyoianzisha.Mara kwa mara Cosmas alikwenda nyumabani kwa Bony kuwatembelea, halikadhalika pia Bony hakusita kwenda nyumbani kwa Cosmas alipojisikia. Ikawa si jambo la ajabu Bony kumtumia Cosmas kama dereva alipohitaji kusafiri licha ya kuwa, Cosmas hakuwa tena mwajiriwa wa kampuni ya MITI GENERAL TRADERS.

    Mnamo majira ya saa 2:00 usiku, Cosmas alifika nyumabani kwa Bony. Hakuwa na miadi na yeyote kati yao, wala hakuwa amefanya mawasiliano kuwataarifu juu ya kwenda kwake pale.Kwa bahati nzuri aliwakuta wapo wote, yaani Bony na mkewe, Emmy.

    Alibisha hodi akafunguliwa na Emmy, “Karibu shem.. karibu,” alisema Emmy huku akiachia nafasi kuruhusu Cosmas aingie ndani.“Ahsante shem, za hapa?”

    “Za hapa ni njema, za huko kwako?”

    “Shwari shemu wangu,” alijibu Cosmas huku akiingia ndani.“Umetususa mpaka naogopa!” alisema Emmy.Emmy na Cosmas waliongozana mpaka sebuleni ambako Bony alikuwa amekaa kwenye kochi, na miguuni mwake aliipakata komyuta ndogo ya mpakato, laptop.Walisalimiana kisha Cosmas akaenda kukaa kwenye kochi ambalo lilikuwa mkabala na kochi ambalo Bony na Emmy walikaa.Uwepo wa Cosmas nyumbani pale ulikuwa ni kwa ajili ya jambo moja tu, ambalo limeihangaisha akili yake kwa muda mrefu bila mafanikio. Alijaribu kuwa na subira, lakini subira yake haikuvuta heri, ndiyo maana akaamua kwenda kwa Bony ili amsaidie kwa namna atakavyomsaidia.Jambo lililompeleka Cosmas kwa Bony ni juu ya kumpata Wayeka ambaye alikutana naye kwenye sherehe, ambako yeye alihudumu kama mapokezi kwenye sherehe hiyo.Cosmas alifikiri juu ya namna atakavyowasilisha ujumbe wake kwa Bony, mara wasiwasi ukaanza kumwingia na kupunguza matumaini ambayo awali yalituama sawia moyoni mwake.Sababu iliyomfanya aingiwe na wasiwasi ni juu ya mtazamo wa Bony kwenye tabia yake. Cosmas alielewa ni kwa jinsi gani Bony alivyo kinyume na tabia yake ya kupenda wanawake kupindukia.Maji ukishayavulia nguo huna budi kuyaoga, ndivyo alivyoamini Cosmas. Alidhamiria kuieleza shida yake kwa Bony huku akipanga mikakati ya kukabiliana na pingamizi zote zitakazowekwa na Bony.

    “Mkuu huu ni mguu wako mkuu,” Cosmas alianza kwa kusema na kusababisha Bony atege sikio ili kusikiliza kwa makini.

    “Nakusikiliza Cos wa watoto,” Bony alisema kwa mzaha, kama ilivyo kawaida yao mara kwa mara wanapokutana.“Nina jambo nyeti sana linanitatiza mkuu, na jambo hili ndilo litakaloya-define maisha yangu yote yaliyobaki.”“Jambo gani tena mkuu, na je utajiskia huru endapo utalisema mbele ya wife, au atupishe?” alisema Bony wakati Cosmas alikuwa kimya akitafakari.Ukimya wake ulimfanya Emmy ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu azungumze, “Basi ngoja mi niwapishe ili…” kabla hajamalizia kauli yake, Cosmas alimuwahi kwa kusema, “Hapana shem usiondoke… wewe pia unaweza kushiriki,” alisema Cosmas na Emmy akabaki pale kwenye kochi. Emmy na Bony walikuwa kimya wakimsubiri Cosmas aanze kuzungumza.“Ni kuhusu ndoa ndugu zangu,” Cosmas alisita. Akafikiri kidogo kisha akaendelea, “Siku ile kwenye sherehe, kuna binti nilimuona, alivaa gauni refu jekundu na kadi yake ya mwaliko ilikuwa ni kadi namba kumi, namba ya meza aliyokuwa amekaa yule rafiki yako aliyekuwa Marekani..” kabla Cosmas hajamliza kutoa maelezo ambayo moja kwa moja aliamini kuwa yangetosha kuwakumbusha ni nani anayemwongelea, Bony na Emmy walitazamana wakacheka, kisha kama walioambizana wakasema, “Wayeka”

    “Hewaa… hilo ndilo jina alilonitajia siku ile, basi bandugu hicho kifaa kimenikaa mtimani. Kwanza niulize ameolewa au kuchumbiwa?”Bony alimtazama Emmy kama vile anamwambia ni wewe unayepaswa kujibu maswali hayo, kama vile haitoshi lugha yake ya macho ilifuatiwa na sauti, “Ni wewe unayepaswa kujibu swali hilo,”“Hapana hajaolewa, pia hajawahi kuniamba kama ana mchumba,” alisema Emmy.“Cosmas…” Bony aliita.“Naam mkuu,”

    “Ninavyomfahamu Wayeka, na ninavykufahamu wewe naona kama unataka kumchezea mtoto wa watu na kumpa msongo wa mawazo usio wa lazima. Labda kama utabadirika,” alisema Bony.“Sikia broo… kwenye hili suala niko serious kabisa, niko tayari kubadirika,” alisita kidogo akameza funda la mate, halafu akaendelea, “… kama unavyoona mkuu, kila jua linapozama linaashiria mwisho wa siku. Na linapochomoza tena huashiria mwanzo wa siku mpya. Hiyo ni ishara kuwa ujana ndiyo tunauaga hivyo. Na kama hali iko hivyo, basi sina budi kujitayarisha kwa uzee kwa kubadiri mfumo wa maisha. Ndiyo maana nimesema nataka kuoa na nataka nimuoe huyo Wayeka.” Cosmas alihitimisha.Maneno ya Cosmas yalimwingia barabara Bony, alipima busara iliyotumika kuyatoa na busara iliyomo katika maneno hayo, akakiri moyoni mwake kuwa maneno anayosema rafiki yake yana ukweli usiopingika ndani yake. Wasiwasi aliokuwa nao Bony ni kuhusu tabia aliyonayo Cosmas, tabia ya kubadiri wanawake ambayo amekuwa nayo tangu alipomfahamu. Alifikiri kwa kina kisha akamgeukia mkewe, “Umeyasikia maneno ya shemeji yako?”

    “Nimeyasikia,” Emmy alijibu.Baada ya jibu la Emmy, Bony alimgeukia Cosmas, “Kwanza mkuu, naomba uniahidi kuwa ni kweli una nia ya dhati na Wayeka na pia uniahidi kuwa unayoyasema kuhusu kubadirika kitabia unayamaanisha.”

    “Nakupa maneno yangu mkuu, niamini nisemacho. Sitaki nizeeke nikiwa kapela… sitaki nizeeke nikiwa na matendo yanayodhihaki umri wangu, nataka nizeeke nikiwa na mke na watoto ili niwe na heshima yangu… nakuahidi Bony tangu sasa nimebadirika.”“Ni vyema Cosmas. Tumeishi kama marafiki kwa muda mrefu na sasa nakuchukulia kama ndugu yangu bila kujali kuwa mimi na wewe hatukushiriki kunyonya titi moja. Sasa niambie ni msaada gani unaoutaka kutoka kwangu ili kutimiza malengo yako.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mi naomba uniweke karibu na huyu binti ili nimueleze nia yangu. Nakiri kumtamani katika siku ile ya sherehe, lakini kadri muda unavyozidi kwenda naona si tamaa tena, bali ni upendo wa dhati nilio nao juu yake.” Cosmas alieleza namna anavyohisi juu ya Wayeka lakini hakuweka wazi kuwa alithubutu kuweka kadi yake ya mawasiliano kwenye kadi ya mwaliko ya Wayeka.

    “Siwezi nikakupa uhakika kuwa nitamfanya awe wako, la hasha! Nipe muda nifikiri juu ya nini kifanyike halafu tutafahamishana.” Alisema Bony.Haukupita muda mrefu waliagana na Cosmas akaondoka kuelekea kwake.



    ****









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog