Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KUTI KAVU - 2

 









    Simulizi : Kuti Kavu

    Sehemu Ya Pili (2)





    MZEE wa makamo, mzee ambaye umri wake unaweza kufikia miaka 60 alikuwa akikokota baiskeli yake aina ya ‘Avon.’ Mzee yule aliendelea kuikokota baiskeli yake mpaka kwenye mti uliokuwa mbele ya nyumba yenye ukubwa wa wastani, nyumba ambayo ilikuwa imeezekwa kwa bati ambazo zimetawaliwa na mabaka yaliyosababishwa na kutu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzee yule aliegesha baiskeli yake kwenye ule mti wenye kivuli, ambao ulikuwa kwenye eneo la mbele la nyumba ile.



    Alipojiridhisha kuwa baiskeli yake iko salama alishusha pumzi ndefu kama ishara ya kutua mzigo wa safari ndefu. Akanyoosha kidole chake ambacho kinafuatana na kidole gumba, akakikunja kile kidole kikawa kama ndoano kisha akakomba jasho usoni pake na kulikung’utia pembeni. Yule mzee alirudia lile zoezi mpaka alipoona kuwa inatosha akakoma.

    “Mama Domii” yule mzee aliita na sauti kutoka ndani ikasikika, “Abee,”

    “Dume la mbegu nimesharudi, niletee maji ya kunywa tafadhali” alisema yule mzee huku karuhusu macho yake yaendelee kutalii mazingira ya nyumbani kwake. Nyumba ambayo ilitazamana na barabara iendayo Bunda. Kwa uapande wa kushoto ukiwa kama unatazama barabarani, nyumba yake ilipakana na nyumba nyingine yenye miti mingi ya miembe na kwa upande wa kulia , ilipakana na nyumba nyingine kubwa iliyokuwa na mti wa ukwaju pembeni yake. Hapo ndiyo kwa mzee Masaka, baba yake na Dominic Masaka. Mahali ambapo ni urefu wa viwanja vitatu vya mpira kutoka kwenye mti mkubwa wa Mong’we ukiwa kama unaelekea Bunda.

    “kililililiiiii…..” sauti ya mama Domi ilisikika akipiga vigelegele huku mkononi akiwa ameshika kombe kubwa la bati lenye maji ndani yake.

    “Pole na safari baba Domi” alisema kwa rafudhi ya kiikizu huku akipiga magoti kumpatia mumewe maji.

    “Uanamme mapambano, nashukuru nimeenda na kurudi salama” kwa mbwembwe kama ilivyo kawaida yake Mzee Masaka alisema wakati akiyapokea maji aliyoletewa na mkewe.

    Alikunywa fundo moja kubwa la maji bila kuyameza, akayatembeza mdomoni kwa mtindo wa kusukutua kisha akayatema pembeni. Akalinyanyua tena lile kombe kubwa na kuliweka mdomoni, aliposhusha lilikuwa tupu!

    “Nikuongeze?” mama Domi aliuliza.

    “Yanatosha mke wangu, tukae unipe habari za hapa.”

    “Hapa ni kama ulivyotuacha, tuko salama salmin. Kama wasemavyo waswahili, ila Tina ndiye hayupo, amekwenda kufanya usafi kanisani, wiki hii ni zamu ya jumuia yetu”

    “Aliondoka hapa nyumbani saa ngapi?” Mzee Masaka aliuliza.

    Mama Doi akajibu “Aliondoka hapa tangu saa tatu asubuhi.”

    “Tangu saa tatu mpaka sasa hivi? Usafi huo usafi gani, au ndiyo tuseme ameachiwa kanisa zima asafishe peke yake?” aling’aka mzee Masaka, mzee asiye na masikhara hata kidogo katika suala la malezi na makuzi ya watoto.

    “Siyo hivyo baba Domi” Mama Domi alijibu kwa sauti iliyojawa na wasiwasi.

    “Kumbe je?” Mzee Masaka alizidi kuuliza.



    Safari hii mama Domi hakujibu kitu na badala yake alibaki akimtazama mumewe kwa woga.

    “Mama Domi…Mama Domi.. angalia usiniharibie mtoto” Mzee Masaka alisema huku akiingiza mkono kwenye mfuko wa koti lake na kutoa kijimfuko cha nailoni ambamo ndani yake mlikuwa na tumbaku. Mzee Masaka akachukua tumbaku kiasi na kuiweka mkononi halafu akakifunga kile kijimfuko cha nailoni, akakirudisha tena kwenye mfuko wa koti lake kilimokuwa awali.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aliifikicha ile tumbaku kiasi iliyokuwa mkononi mwake, kisha akachukua kipande cha karatasi, akakinyoosha vema akaiweka tumbaku yake kwenye kipande hicho cha karatasi alichokiandaa, kisha akaisokota katika umbo la sigara. Alipomaliza akamgeukia mkewe ambaye muda wote alikuwa kimya akimtazama. “Naomba unilee moto mke wangu.”

    “Jamani baba Domi, si ungekula kwanza halafu ndiyo uvute hayo masigara yako?”

    “Hii ndiyo inanipa hamu ya chakula mke wangu, we niletee moto kwanza halafu nikishavuta utaleta chakula” Mzee Masaka alisema kwa sauti ya kubembeleza.

    Mama domi aliinuka huku maneno yakimtoka, “Hayo masigara yako unayong’ang’ania ndiyo maana huponi kifua. Kila siku kukohoa tu, kwa sababu ya hayo masigara yako.”



    Mzee Masaka aliyasikia maneno yote yaliyokuwa yakisemwa na mkewe. Yalikuwa ni maneno yaliyosemwa kila siku na mama Domi, lakini katika hali ya kutojali, mzee Masaka aliendela kuvuta tumbaku siku hadi siku, “Ntaaccha tu mke wangu, mbona ugimbi niliacha.” Alisema mzee Masaka kwa lengo la kujitetea baada ya kubaini ukweli wa wazi uliofumbatwa kwenye kauli ya Mama Domi.



    Haukupita muda mrefu mama Domi alirejea akiwa na kijinga cha moto mkononi, akamkabidhi mumewe ambaye moja kwa moja aliiwasha tumbaku yake akaanza kuvuta. Alivuta mikupuo ya haraka haraka halafu akaruhusu moshi mwingi utoke nje kupitia tundu za pua yake.



    Kwa jinsi moshi ulivyokua ukitokea puani kwa mzee Masaka, nilizifananisha pua zake na bomba la kutolea moshi kwenye pikipiki au trekta.



    Baada ya kuwa amepiga mikupuo kadhaa, mzee Masaka alimgeukia tena mkewe, “Mbona hujaniuliza yaliyojiri huko nilikokuwa nimeenda?”

    “Nilikuwa nasubiri upumzike kwanza baba Domi, enhe mmefikia wapi?”

    “Huyu Mzee Tungu anazidi kunichokoza, si unakumbuka sehemu ya shamba letu aliyokkuwa ameimega?”

    “Ndiyo nakumbuka.” Mama Domi alijibu huku akijiweka tayari kusikiliza mumewe anachomwambia.

    “Basi amemega tena, na safari hii ameingia kwa hatua mbili zaidi. Nimejaribu kumuelewesha lakini anajifanya mgumu kuelewa.” Mzee Masaka alisema huku akiweka msokoto wake wa tumbaku mdomoni tayari kwa kuvuta tena.

    “kwa hiyo umeamuaje?” mama Domi aliuliza.

    “Mimi ni kama unavyonijua, sitaki matatizo na mtu, nimeamua hili suala nilipeleke mbele ya sheria. Likiwa huko, sheria itachukuwa mkondo wake.”

    “Kweli baba Domi, ni bora haya mambo yakazungumziwe mahakamani. Isije ikawa kama ya Mzee Keelo na watoto wa mama Sabela, si unakumbuka walivyokatana mapanga ?”

    “Nakumbuka sana, huyu mzee Tungu anafikiri anaweza kunidhulumu mimi shamba langu kama alivyomdhulumu mzee Kisilo! Hapa ameula wa chuya, mimi ndiye mzee Masaka, nitaisaka haki yangu kwa udi na uvumba mpaka nihakikishe inapatikana” mzee Masaka alisema huku akijipigapiga kifuani.



    Mama Domi alimtazama mumewe kwa jicho la umakini halafu akatikisa kichwa chake juu chini, chini juu kama ishara ya kukubaliana na mumewe halafu akaondoka, na mara baada ya muda mfupi alirudi akiwa na sinia kubwa lililojaa maboga, karanga za kuchemsha, mahindi ya kuchemsha, maharage na njugu za kuchemsha. Vyote vikiwa vimechemshwa kabla ya kukauka. Mchanganyiko huu wa chakula huitwa ‘Imisumo’ katika jamii ya waikizu, chakula ambacho hupendelewa sana hasa wakati wa mavuno.

    “Hewaaa..” mzee Masaka alisema wakati ananawa kwa lengo la kula, “Hapa ndipo nipokupendea mke wangu, hii ‘imisumo’ ndiyo mahala pake hapa. Watu wananiita Mzee kijana, yote hii ni kwa sababu unanijali mke wangu.” mzee Masaka aliyasema haya akiwa ameshamiri tabasamu usoni pake. Wakatazamana na mkewe, kisha kwa pamoja wakaangua kicheko cha furaha.



    *****

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KUPITIA dirishani, dirisha la kioo, juu kabisa kwenye ghorofa ya 18, Doi alikuwa akilisawiri vema jiji la Dar es salaam. Aliliona jinsi jiji hili linavyopendeza hasa nyakati za usiku.



    Akiwa pale dirishani, Doi alikuwa akiwaza mambo mengi sana. Aliwaza jinsi Domi atakavyokuwa anapata tabu baada ya kuondoka kwake, aliwaza pia jinsi Domi atakavyoumizwa na barua aliyomwandikia na kumwachia pale chini ya mto muda mfupi kabla hajaondoka. Hata ilifika wakati akajuta ni kwa nini aliiandika ile barua.



    Doi aliumia sana, alijua fika kuwa; kwa jinsi Domi anavyompenda, na kwa jinsi maneno ya kwenye barua yatakavyomwumiza, Domi hatokuwa na nguvu ya kujishughulisha na zile dola alizomwachia!



    Mawazo yalizidi kumtafuna Doi, akawa kama vile anamuona jinsi anavyopata tabu. Moyoni Doi akajiona ni mwenye hatia, kwa unyama alioutenda. Akatamani aondoke pale hotelini ili aende nyumbani akamwone Domi na kumwomba msamaha. Lakini angewezaje kufanya hivyo baada ya yote aliyoyaandika kwenye barua?



    Doi alijua fika kuwa Domi anapata tabu, na anapata tabu kwa sababu ya kumpenda yeye. Doi akajiona msaliti asiyestahili kuigwa, “Nisamehe Domi” Doi alijisemea moyoni huku machozi yakimtoka.



    Akiwa katika lindi hilo la mawazo, Doi alihisi kuguswa na kitu maungoni mwake, akashtuka!



    ***

    Wakati Doi akiwa dirishani, juu kabisa kwenye ghorofa ya 18 ndani ya chumba cha hotel ya ‘JB BELMONT HOTEL. Ni katika wakati huohuo, Domi alikuwa nyumbani kwake amekaa kwa kujikunyata huku akiwa amejiegemeza mlangaoni, mlango wa chumba chake ambao ulikuwa haujafunguliwa kwa siku ya pili mfululizo.



    Akiwa pale mlangoni, Domi aliweza kuyatalii barabara mandhari ya humo chumbani kwake.

    Ni kweli Domi alikubali yeye ni masikini wa kipato, kwa kuangalia hadhi ya nyumba anayoishi, na thamani ya samani zilizomo. Domi aliumia sana!



    Haikuwa mara ya kwanza kwa Domi kuumizwa na hali ya maisha yake, ameumizwa mara nyingi, lakini hii ya kukimbiwa na mpenzi wake, mwanamke ambaye alimwona ndiye kila kitu kwake ilimuumiza sana.



    Domi aliyazungusha macho yake chumba kizima, yalipotua kwenye picha aliyopiga wakiwa pamoja na Doi, Domi alijikuta akiita, “Doi.. Doi...” Kwa sauti hafifu yenye kukwamakwama. Alipoona hajibiwi Domi alisimama na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye ile picha akaishika, akainyanyua kutoka pale ilipokuwa kwa mkono mmoja, akaisogeza karibu kisha kwa kutumia kidole gumba, na kwa taratibu sana Domi aliigusa ile picha upande aliokuwa Doi, machozi yakamtoka sambamba na maneno aliyoyatamka kwa uchungu, “Umasikini ndiyo umekufanya unikimbie? Ina maana hukuamini kuwa ni kweli nilikuwa nazitafuta pesa kwa ajili yetu? Au ulidhani nimeridhika na hali hii ya maisha? Tumepitia shida ngapi Doi? Nilikwambia mama…nilikwambia haya yote yana mwisho na mwisho wake ndiyo huu umefika. Kama pesa tayari imeanza kuja, rudi mpenzi wangu Doi.. ruuudi” maneno haya yalikuwa yakimtoka Doi sambamba na machozi.



    Akiwa bado ameshikilia ile picha, Domi alipepesa macho na kuziona zile dola za kimarekani zikiwa pale kitandani. Alipoziona zile pesa hasira zikamvamia ghafla, hapohapo nguvu ya ajabu ikamjia, akaivugumisha ile picha akaitupa ukutani, kioo kikavunjika vipandevipande na kuzagaa mule ndani. Domi akajihisi hali isiyo ya kawaida tumboni mwake, hapo ndiyo akakumbuka kuwa hajala kwa siku ya pili mfululizo. Njaa iliyokuwa imetulia sasa ikaanza kuchachamaa tumboni mwake, hitaji la kupata chakula likamjia!



    Domi alichukua funguo za gari akatoka nje na kwenda mpaka alipoiegesha gari yake aliyopewa kazini, alipofika aliufungua mlango akaingia garini, akaiondoa gari kwenda kutafuta chakula.



    ***





    Doi alishtuka baada ya kuwa ameguswa maungoni mwake, alipogeuka alikutana na busu zito kutoka kwa Damian, “Hi baby” Damian alisalimia.

    “Hi” Doi aliitikia lakini kwa sauti ya unyonge.



    Miongoni mwa watu ambao wako makini na wayafanyayo, Damian ni mmoja wao. Damian alikuwa ameshaigundua hali aliyo nayo Doi, kwa utundu wa hali ya juu Damian alianza kujariu kuirejesha furaha ya Doi, “Relax baby” Damian alisema huku akiwa amemkumbatia Doi.

    “Halafu kabla sijasahau mpenzi, nina bonge la zawadi. Na hii ni kukuonesha kuwa mimi siyo mtu wa ahadi hewa” Damian alisema kabla hajamshushia tena Doi mvua ya mabusu ambayo yalizidi kumchanganya kabisa.

    “Fumba macho mpenzi” Damian alisema tena kwa sauti iliyojaa mahaba.

    “Nhu! Jamani Damian, kwani vipi?” hatimaye Doi alifungua kinywa na kuzungumza.

    “Fumba macho, kuna kitu nataka nikuoneshe mpenzi”

    “We nawe una mambo” Doi alisema huku akiruhusu macho yake yafumbe kama alivyoraiwa na Damian.



    Baada ya Doi kufumba macho Damian aliisogelea ile bahasha aliyokuwa ameiweka kitandani wakati anaingia mule chumbani, akaifungua na kutoa kilichomo kisha akamkamshikisha Doi ambaye bado alikuwa ameyafumba macho yake. Kwa mikono miwili Doi akashikilia alichoshikishwa na Damian.



    “Haya sasa fumbua macho yako mpenzi” Damian alisema.



    Doi alifumbua macho yake na kujikuta ameshikilia sanamu ya plastiki, aliitazama ile sanamu bila kujua ni sanamu ya nini na ina maana gani. Alijiuliza maswali mengi bila kupata majibu, Uzalendo ukamshinda, ikabidi aulize, “Hiki ni nini Damian?”



    Damian akamtazama Doi kwa jicho la kisanii halafu akacheka kidogo kabla ya kusema, “That is Parris….hiyo ndiyo Parris mpenzi” Damian alisema.

    Kinyume na matarajio yake Damiana alimshuhudia Doi akiwa katika hali ya mashangao.

    Damian akajua bado hajaeleweka na kabla hajajua cha kusema alimsikia Doi akisema, “Parris… una maana gani kusema hii ndiyo Parris?”



    Kwa umakini wa hali ya juu ikabidi Damian afungue Darasa kwa Doi ambaye alionekana kutoielewa suprise ya Damian, “Sikiliza baby, hiyo sanamu ni sanamu ambayo husimama kama ishara ya jiji la Parris, yaani kama vile hapa Dar es salaam, kuna mnara wa askari na huo mnara wa askari ndiyo kama nembo ya utambulisho wa jiji hili la Dar, hivyo basi nimekuletea hiyo sanamu ya mnara wa ‘EIFEL’ ambao uko jijini Parris, kukujulisha kuwa nitakupeleka Parris, Ufaransa ukapumzike kama ishara ya mapenzi yangu kwako.” Damian alijitahidi kueleza kadiri alivyoweza kumwelewesha Doi.



    Angalau sasa Doi alianza kuelewa Damian anamaanisha nini kwa kumletea sanamu ile.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Doi alibaki mdomo wazi baada ya kusikia maelezo ya Damian. Hakuyaamini masikio yake ikabidi aulize tena, “Damian, tafadhali…naomba unifafanulie vizuri.” Damiana bila hiyana wala kuuma uma maneno akamwambia, “Nitakupeleka Parris ukatembee, ukatembee ili uione dunia. Uone jinsi watu wanavyoponda raha ndani ya jiji la maraha duniani, Parris!”



    Masikio ya Doi sasa yalisikia sawia kile alichokuwa akikisema Damian.



    Ujumbe huo ulizibadiri kabisa fikira za Doi, Doi akaanza kuwaza jinsi atakavyokuwa mara atakapokuwa jijini Parris, Ufaransa.

    Mara nyingi amewasikia watu mabalinbali wakiongea na kusimuliana juu ya maisha ya Parris, jiji ambalo huaminika kuwa ni kivutio cha wapenda starehe duniani, jiji la waponda raha! Amekuwa akisoma na kusikia kuwa mtu fulani maarufu yuko kwenye fukwe za Parris akiponda raha.



    Kwa shauku ya kutaka kujua mengi Doi alishindwa kuvumilia ikabidi aulize tena, “Tunaenda lini Damian?”



    Swali hilo ndilo alilolitarajia Damian, “Muda wowote kuanzia sasa” Damian alijibu.



    Doi alikuwa bado hajayaamini masikio yake, mawazo juu ya Parris yakakipamba kichwa chake.



    ***

    Majira kama ya saa 3:30 usiku Domi alikuwa katikati kabisa ya jiji la Dar es salaam. Ikiwa ni siku ya pili tangu Doi atoweke nyumbani, aliamua kutoka kwa ajili ya kutafuta chakula baada ya kutokula kwa siku mbili mfululizo.



    Domi alikuwa akilipandisha gari lake ghorofa ya pili, mahali yalipo maegesho ya magari ndani ya jengo la ‘MAFUTA HOUSE’



    Haikuwa kawaida yake kuonekana maeneo hayo, iwe mchana au usiku kwa sababu ya kutokuwa na pesa. Kwa mara ya kwanza alifika hapo miaka mitatu nyuma akiwa mwaka wa tatu wa masomo yake. Alifika hapo kwa kupelekwana rafiki yake ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wake ambaye kwake yeyeilikuwa ni kawaida yake kuhudhuria kwa lengo la kucheza muziki hasa nyakati za mwisho wa juma.



    Siku hiyo alikuwa na pesa kiasi mfukoni mwake, akaamua kuja kupata chakula katika mgahawa wa SAVANA LOUNGE. Ni katika jengo hilohilo ndiyo Damian na Doi walichukua chumba tangu siku iliyopita.



    Domi aliingia katika mgahwa huo wa SAVANAH ambao uko ghorofa ya tatu, na Damian na Doi walichukua chumba ghorofa 18 katika jengo hilohilo.

    Baada ya kuegesha gari lake Domi aliingia mgahawani na kukaa kwenye meza ya pembeni, meza ambayo ilimpa uhuru wa kuona karibu kila pembe ya ukumbi wa mgahawa ule wa SAVANAH, meza ambayo Domi aliiona kuwa inamfaa zaidi.



    Domi aliagiza chakula na kutulia kwenye meza hiyo huku akila polepole.



    ***

    “Damian..” Sauti ya Doi ilisikika ikiita.

    Damian aliyekuwa anatazamana uso kwa uso na Doi aliitika, “Naam mpenzi...”

    “Ni kweli tunaenda Ufaransa?” Doi aliuliza.

    “Ndiyo mpenzi…inabidi twende Ufaransa kwa mapumziko ya mwezi mmoja kabla hatujarudi na kufunga ndoa yetu” Alisema Damian kwa ushawishi wa hali ya juu.



    Doi alimtazama tena Damian kwa macho ya kutoamini, Damian akawa ameligundua hilo. Ili kuumaliza utata akauliza, “Kwani we hutaki kwenda ufaransa?”

    “Hapana, siyo kama sitaki…”

    “Kumbe je?” Damian alimtupia Doi swali la udadisi.



    Doi alifikiri kidogo, halafu akajibu, “Unajua nyumbani wanaelewa kuwa mimi niko kwa Domi…na mpaka sasa sijui kama Domi ameshakwenda nyumbani kuniulizia au bado, na pia….”



    Kabla hajaendelea Damian alimkatisha, “Usiwe na wasiwasi na hilo hata kidogo, ngoja kwanza niandae utaratibu wa safari, mipango ya safari ikikamilika wewe utapeleka zawadi kidogo nyumbani, na ukiwa huko nyumbani ndiyo utajua kama wazazi wanajua lolote kuhusu wewe kutokuwepo kwa Domi au la, baada ya hapo ndiyo tutajua cha kufanya au wewe unaonaje mpenzi?” Damian alimlainisha Doi kwa maneno, na ili kumfunga kabisa Damian alihitimisha maelezo yake kwa swali la mtego kwa Doi.



    Bila hiyana Doi alijibu, “Sawa” Baada ya kusema hayo, Damian alimuomba Doi waelekee ghorofa ya tatu kwa lengo la kupata chakula cha usiku kwenye mgahawa wa SAVANAH LOUNGE. Saa 4:15 Damian na Doi waliingia kwenye lifti kwa ajili ya kwenda kupata chakula kwenye mgahawa uliokuwa ghorofa ya tatu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ***



    Chakula kilipita kwa tabu sana kwenye koo la Domi. Alijilazimisha kula lakini alishindwa kabisa. Mawazo juu ya Doi yalizidi kumtesa. Alishindwa kuelewa kama aliyefanya hivi ni Doi yule anayemjua au ni Doi gani? Dominic alizidi kujiuliza ni lini Doi alianza kumsaliti? Alitamani amuone ili amuangalie vizuri na kumfananisha ili aone kama anafanana na kile alichokifanya.



    Katika watu ambao Domi aliwaamini, Doi ni mtu pekee. Domi hakumwamini mtu yeyote isipokuwa Doi, na ndiyo maana mpaka muda huo Domi hajataka kuamini kama Doi ndiye aliyemfanyia hivi.



    Mawazo yalipozidi kumtinga Domi, alishindwa kabisa kula. Aliisogeza sahani ya chakula pembeni kisha akatoa noti mbili za elfu kumikumi akaziweka mezani kwa malipo ya chakula alichokula akaondoka. Wakati huo ikiwa ni saa 4:12 usiku.





    ******



    USIKU wa manane bwana alishtuka usingizini akamwamsha bibi kwa kumpapasa. Bibi alipoamka alimkumbatia bwana ambaye pia alimkumbatia bibi, kwa pamoja wakakumbushana dhamira ya wao kuwa pamoja usiku ule.



    Baada ya kufanya tendo hilo takatifu bila Baraka za watakatifu, wote wakapitiwa na usingizi. Masaa machache baadaye, “Ngriii..ngriii..ngriii….” Sauti ya kengele ya kutegeshwa kwenye simu ilisikika, wote wakaisikia wakanyanyua vichwa vyao juu.



    Zai aliwasha taa halafu akamsalimu bwana wake, “Wajisikiaje mpenzi?”

    “Mi niko salama, hofu ni kwako mahabuba”

    “Nami pia niko salama” Zai alijibu kisha akashuka kitandani, akajifunga khanga iliyofunika mwili wake kuanzia kifuani mpaka magotini, akaenda kumwandalia mume wake maji ya kuoga ili aoge kabla hajaenda kazini.



    Baada ya Mudi kutoka kuoga, alikuta Zai amekwishamuandalia nguo za kuvaa. Mudi alipomaliza kujiandaa alimuaga mpenzi wake kama ilivyo kawaida yao. Akaondoka huku nyuma akimuacha mkewe ambaye aliendelea na usafi wa nyumba.



    Uwepo wa Zai nyumbani kwa Mudi ulimfanya Mudi ayafurahie maisha tofauti na hapo mwanzo kabla hajaanza kuishi na Zai. Kwa kazi yake ya udereva wa daladala, Mudi alijitahidi kuhakikisha mahitaji yote ya muhimu hayakosekani nyumbani. Kila aliporudi usiku kutoka kazini alimpatia Zai kiasi cha pesa ili akitunze kama akiba yao ya baadaye. Akamjali kama mpenzi wa roho yake, kwa mavazi na kila kilicho cha muhimu kwa mwanamke.



    Mara kwa mara gari lake linapokwenda mpaka ‘Yombo Machimbo’ Mudi alimpigia Zai simu ili akachukue mboga, matunda na bidhaa kadha wa kadha kwa mahitaji ya nyumbani. Licha ya kumpatia kila siku kiasi cha pesa kwa ajili ya matumizi hayo ya nyumbani.



    Akiwa amepaki gari lake kituoni maeneo ya Buguruni kwa lengo la kusubiri abiria, mara ghafla simu yake ya mkononi iliita, “Hallow Mudi hapa. Nani mwenzangu?”



    Sauti kutoka upande wa pili ikamjibu, “Ni mimi Udaku, jirani yako, chumba cha pili hapa nyumbani tunapoishi”

    “Ahaa , jirani habari yako?” Mudi alisema kuashiria kuwa ameshamtambua.

    “Safi jirani, hapo ulipo tunaweza kuongea?” Sauti ya Udaku jirani yake na Mudi ilisikika.

    “Ongea tu jirani, nakupata”

    “Samahani jirani, unaweza kuniona mmbeya lakini hili inabidi ulifanyie kazi”

    “Lipi hilo jirani?” Mudi aliuliza ili kupata ufafanuzi zaidi.

    “Mida kama hii, yaani kuanzia saa 10 mpaka sa 12 jioni kila siku, mkeo huwa anaongea sana na simu mpaka ananitia mashaka juu usalama wa hizo simu anazopiga. Sikiliza kaka Mudi, naomba usinielewe vibaya,” alisema Udaku.



    Mudi alishangazwa sana na ile taarifa aliyopewa na jirani yake. Akilini mwake aliona kuwa ni taarifa ya kipuuzi na isiyo na mantiki yoyote. Na kwa Mudi, Udaku hakuwa na jina jipya zaidi ya mmbeya.

    Mudi alijibu, “Ahsante” halafu akakata simu.



    Baada ya kukata simu, Mudi aliingia kwenye tafakuri nzito, “Yaani huyu Udaku anaacha kufanya mambo yake anaanza kuchunguza mambo ya watu, hizi ndiyo tabu za uswahilini”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akiwa kwenye lindi hilo la mawazo, Mudi alishtuliwa na sauti ya kondakta wake, “wawahishe baba… wawahishe, gari limeshapendeza,”

    Mudi akondoa gari, baada ya kuamriwa na kondakta wake.



    ***

    Dominic alikuwa amejinyoosha kwenye kiti cha mbele cha gari lake alilopewa na kampuni, alikilaza kile kiti ili ajinyooshe kwa kujinafasi zaidi. Akiwa kwenye kiti hicho, Domini alikuwa anawaza mambo mengi juu ya Doi. Ni wazi kabisa kuwa Domi hakutaka kukubaliana na kile alichokifanya Doi, “Au ametekwa?” Domi aliwaza.

    “Isije ikawa ametekwa halafu akalazimishwa kuandika ile barua. Oooh no… hapana hajatekwa huyu. Kama ametekwa, watekaji wake wanataka nini? Ningeweza kusema wanataka pesa… lakini siyo rahisi kwa sababu nimekuta pesa ndani,” mawazo juu ya mawzo yalimzonga Dominic.



    Jambo moja lilimuia gumu Domi, nalo ni kupiga simu nyumbani kwa kina Doi ili kuuliza kama anaweza kupata taarifa yoyote yenye kuhusiana na Doi. Jambo hili lilikuwa gumu kwa sababu, ndugu wote wa Doi hawakuwa wameridhia Doi kuishi na Dominic kwa sababu ya umasikini aliokuwa nao. Walijitahidi sana kumzuia Doi lakini pingamizi zao hazikufua dafu, Doi akaenda kuishi kwa Dominic bila kujali umasikini wake.



    Pamoja kuyatambua yote hayo Dominic alipiga moyo konde, akawasha gari na kuondoka kuelekea Mbagala Kibonde Maji ambako ndiyo nyumbani kwao na Doi.



    Mita chache kabla hajafika nyumbani kwa kina Doi, Domi aliegesha gari lake na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea nyumbani kwa kina Doi. Alipofika alibisha hodi akaitikiwa. Kinyume na matarajio yake, Domi alipewa mapokezi ambayo hata yeye yalimshangaza.

    “Karibu…karibu baba ukae…” ilikuwa ni sauti ya mzee Vioja baba yake na Doi, mzee ambaye alikuwa mwiba kwenye uhusianao wa Doi na Dominic.



    Mapokezi aliyopewa Domi yalimtia wasiwasi, kwani hata mama na baadhi ya ndugu wa Doi walionekana kumchangamkia sana.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Karibu baba,” Sauti ya mama Doi ilisikika akikmkaribisha.

    “Ahsante, Shikamoo baba… shikamoo mama” Domi aliwasilimia wote kwa heshima na taadhima.

    “Habari za siku mwanetu?” Sauti ziliwatoka wote kwa pamoja, baba na mama na Doi. Hali hii ya kutoa sauti kwa pamoja iliwafanya watazamane usoni kabala ya kugutushwa na suti ya Domi, “Nzuri tu, za hapa?”

    “Za hapa pia ni nzuri, karibu sana baba..”

    Bada ya salamu na maongezi ya hapa na plale, baadhi ya ndugu wa Doi waliokuja kumsalimia Domi waliondoka na kuwaacha baba na mama Doi wakiwa na Domi sebuleni. Ukimya ukatawala baina yao!







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog