Search This Blog

Friday, October 28, 2022

UPENDO KUTOKA SAYARI NYINGINE - 1

 

     





    IMEANDIKWA NA : ANDREW MHINA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Upendo Kutoka Sayari Nyingine

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Simu ya wito

    Alishtuliwa na mlio wa simu yake ya mkononi, ambayo baada tu ya kuichukua ilikata! Ni hapo alipogundua kuwa mpigaji alipiga mara zaidi ya nne, bila kupokelewa. Usingizi ulikuwa umemzidia kwani alirudi nyumbani kwake mida ya saa kumi alfajiri, kutoka kwenye shughuli zake. Shughuli za kuchukuwa habari toka kona mbalimbali za jiji zilimfanya usiku uliopita autumie robo tatu zote kwa ajili ya kufuatilia habari moja iliyokuwa muhimu, katika kulilisha gazeti mojawapo kati ya matatu anayoandikia.

    Kufichua habari za siri ndio kazi yake inayomweka mjini hapa. Jina lake anaitwa Gadna rafiki zake walipenda kumwita Gady na yeye alipenda kuitwa hivyo. Gady alikuwa ni kijana mcheshi na mwenye muonekano mzuri, wazungu hupenda kuwaita watu wa aina hii HB kwa kifupi ili kuongeza ladha au kwa kirefu “Hand some” Kazi yake hasa ni mwanahabari aliyekuwa anaandikia magazeti matatu tofauti mawili yanatoka mara tatu kwa wiki na moja linatoka kila siku.

    Shughuli zake zilikuwa nyingi sana na alifanya kazi kwa bidii jambo lililomfanya aaminiwe na wamiliki wa magazeti haya.

    Huyu alikuwa mwandishi wa kujitegemea ambaye habari zake alikuwa akiyauzia magazeti haya kwa bei nzuri kutokana na uzito wa habari zenyewe. Sifa yake kuu ni kwamba alikuwa haandiki habari ambayo ameipata juu juu bila kuifanyia utafiti wa kina. Hali hii ilimfanya apate habari zake kwa taabu maana wakati mwingine alikutana na changamoto za kutishiwa maisha yake na wakati mwingine alikutana na kipigo cha mbwa mwizi na kunyang’anywa vitendea kazi.

    Asubuhi hii Gady alipata simu hii ambayo mpigaji alimtambua vema. Hakutaka kuipuuzia maana mpigaji alikuwa ni mchungaji wa kanisa mahali alipokuwa anaabudia. Mara moja aliamua apige yeye ili ajue kile mchungaji wake alichotaka kumwambia. “Nimekupigia mara nyingi kwa sababu kuna jambo la muhimu nataka ulishuhudie likifanyika hapa kanisani mida ya saa tano kasoro.” Sauti ya mchungaji ilisikika upande wa pili wa simu kwa msisitizo.

    “Mchungaji leo nimebanwa sana na ratiba kuna maeneo matatu natakiwa kwenda naomba nisamehe kwa sababu sitaweza kutokea.” Alisema Gady huku akinyanyuka na kuliendea taulo lililoko kwenye msumari ukutani. “Gadna ni muhimu ufike na kamwe huwezi kujutia kufika kwako na kuahirisha miadi yako mingine yote, ninatarajia kukuona mida hiyo, usisahau kuja na vifaa vyako vyote sawa?” Mchungaji alisema hivyo na kabla Gady hajajibu lolote simu ilikuwa tayari imekatwa.

    Gady hakuwa na jinsi ya kukwepa mwaliko huu. Alimfahamu vizuri Mchungaji Willfred Dulanga. Ni mchungaji aliyekuwa na ushirikiano mkubwa sana katika kazi yake kwani mara nyingi amekuwa akimtengenezea habari za kuandika wakati mwingine alikuwa akimpa Michongo ya kuandika makala kwa kumuunganisha na watu waliopitia mikasa ya kila aina. Hatua aliyoichukuwa ilikuwa ni kuahirisha miadi yote mingine na wakati huo huo aliweka simu mezani na kuchukuwa taulo lake na kwenda bafuni kujitayarisha kwa safari ya kanisani.

    ***
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jengo la Ibada lilipo chini ya Huduma ya Evangelism & Prayer Ministry Of Tanzania (EPMT) lilionekana kufurika watu wengi Jumapili hii kuliko siku nyingine. Watu walikuwa wamefurika kanisani mpaka nje ambapo yaliwekwa mahema ili kuwakinga na jua la siku hiyo. Wana kwaya walikuwa wakiimba nyimbo za mwisho kabla ya kupisha kipindi cha sadaka na ushuhuda. Gadna alifika Kanisani na kijana wake aitwaye Chidi, dakika chache kabla ya ushuhuda ambao Mchungaji alimsisitiza kuwa ni muhimu kwake kama mwanahabari. Mara tu alipotokea mlangoni Mchungaji alimtuma shemasi aende kumwita kule madhabahuni. Gadna alifika mbele ya mchungaji, bila kuitikia salamu Mchungaji alimvuta na kumnong’oneza:

    “Andaa haraka vifaa vyako na kama una vijana wa kukusaidia fanya hiyo kazi mara moja kusudi uchukue kila tukio litakalofanyika mara baada ya kutolewa sadaka. Hakikisha hupitwi na kitu chochote wala neno lolote sawa?” Alisema Mchungaji. “Sawa Mchungaji.”

    Gadna aliafiki maagizo ya Mchungaji na kuanza matayarisho haraka ya vifaa vyake akisaidiwa na Chidi kijana wake aliyekuwa alimtumia kwa kazi nyingi kutokana na wepesi wake. Baada ya vifaa vyote kuwekwa mahali pake picha zikaanza kuchukuliwa. Muda haukuwa mrefu mara tu baada ya watu kutoa sadaka walitokea watu watatu baba mmoja na vijana wawili mmoja wa kiume na mwingine ni Binti mrembo sana. Vijana hawa walionekana kupishana umri kati ya miaka miwili ama mitatu wote wakionekana kuwa ndani ya miaka thelasini na na thelasini na mbili.

    “Leo tunao ndugu zetu hapa Mzee Martin na vijana wake Sebastian na Judith, wanalo jambo la kusema nasi kama Ushuhuda. Walisema kuwa sadaka yao itatolewa baada ya kutoa ushuhuda wao.” Mzee wa kanisa alisema. Kisha akamwangalia Mchungaji, Mchungaji wakati anakuja, alisema: “Kabla ya yote ninakabidhi kipaza sauti hiki kwa Mchungaji ana maneno ya kuongea na yeye ndiye atakayewakaribisha watu hawa maalumu kwa siku ya leo.” Alisema Mzee wa kanisa wakati akienda kukaa na Mchungaji akaja akiwa na kipaza sauti mkononi.

    “Leo kuna uwezekano wa mimi kutohubiri kabisa!” Alisema Mchungaji Wilfred Dulanga huku akiwaangalia watu ambao wengi hawakujua kinachoendelea lakini baadhi ya watu walionekana kuwa na shauku na kile kilichokuwa kinaongelewa na Mchungaji. “Leo tuna watu muhimu sana kulingana na ushuhuda walionao. Ushuhuda wao huu utabadilisha maisha ya watu siku ya leo.

    Huenda ukaonekana kama hadithi za kufikirika lakini nakuhakikishia kuwa kila kitakachosemwa na watu hawa ni cha kweli kabisa. Ninachotaka ukiweke akilini na moyoni mwako ni kujaribu kujifunza kwa ushuhuda huu mzuri na wa kusisimua.” Maneno ya Mchungaji yalikuwa ni machache sana yaliyoshangiliwa na watu wote ambao walipata shauku juu ya kile walichogusiwa kuhusu ushuhuda wa watu wale waliokuwa pale mbele ya madhabahu. Baada ya hapo Mchungaji alikwenda kukaa na Msaidizi wake akampa Mzee Martin kipaza sauti.

    * *

    “Inaweza kuwa hadithi ukiichukulia kama hadithi na hata ukitaka iwe sinema inaweza kuwa hivyo na vyote vikaenda sawa na jinsi unavyoweza kuchukulia habari hii. Kwangu ni habari ya kweli sana kuhusu binti yangu mpenzi na kijana huyu japo maelezo mengi binti yangu atakuja kuyaeleza vizuri hapo baadaye na kijana huyu naye atasema kwa upande wake.

    Mimi ni baba mzazi wa judithi Jina langu naitwa Martin Sebwaka. Kwa hiyo jina la jumla la binti yangu ni Judith Martin Sebwaka. Judith ni mtoto wa pekee katika ndoa yangu na mke wangu ambaye kwa sasa ni marehemu. Kama mzazi nilijitahidi sana kumsomesha binti yangu katika shule mbali mbali na vyuo ndani na nje ya nchi hii. Kwa upande wake hakuniangusha kwani alikuwa na bidii sana katika masomo yake na kupata shahada mbalimbali. Mpaka hapa alipo ana shahada ya Daktari wa uchumi na pia ni mwanasheria, wakati huo huo ni meneja wa kampuni ya Kupokea na kusafirisha mizigo. (Clearing and Fowarding) mimi nikiwa ndiye mkurugenzi wa kampuni hiyo, juzi amerudi kutoka nchini Kenya akiwa na shahada nyingine ya Daktari wa magonjwa ya akili aliyoipata chini ya Chuo cha Psychological Mental hospital.” Mzee Martin alikohoa kidogo kisha akaendelea. “Miaka minne iliyopita binti yangu Judith aliniletea kijana huyu nyumbani akieleza kuwa amempenda na angefurahi ikiwa ningetoa ruhusa yangu waweze kufunga ndoa. Kwakweli sikuwa radhi sana juu ya ombi hilo kwani niliona kuwa bado binti yangu anahitaji kuwa karibu na wazazi wake kabla ya kukimbilia ndoa.

    Maneno yangu ya kutokuwa tayari kutoa ruhusa yalimuumiza sana kijana na binti yangu japo kijana huyu hakukata tamaa. Upendo wao ulikuwa wa thati na mimi nililiona jambo hilo, hivyo baadaye nikawaita wote wawili na kuwapa maneno yangu kama mzazi na baada ya hapo nikamwambia akawaite wazazi wake, ili maneno haya yawe wazi kwa pande zote mbili. Hivyo ndivyo ilivyofanyika baada ya siku tatu wazazi wa kijana huyu wakaja tukatambuana na baadaye tukapanga siku ya wao kuleta mahari.

    Lakini mambo hayakuwa kama yalivyopangwa kwani siku mbili kabla ya siku ya kupokea mahari, Mke wangu na binti yangu walipata ajali ya gari. Ajali iliyochukuwa maisha ya mke wangu na binti yangu kujeruhiwa vibaya. Maiti ya mke wangu iliwekwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa muda wa siku kumi. Hii ni kutokana na kumsubiria binti yangu ambaye alikuwa hajarudiwa na fahamu zake tangu siku ya ajali. Mwisho wa yote ndugu zangu na ndugu wa mke wangu waliniomba tumzike tu mke wangu kutokana na kwamba hatuwezi kubadilisha matokeo hayo machungu. Na mimi kwa shingo upande nikakubali mke wangu azikwe bila binti yake kipenzi kuhusika kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo. Maandalizi ya maziko yakafanywa na mke wangu akazikwa.

    Ulikuwa ni uchungu wa aina yake lakini nilikubaliana na kazi hiyo ya Mungu kwani waswahili wanasema, “Kazi ya Mungu haina makosa.” Baada ya mazishi nilirudi tena Hospitali kuendelea kumuuguza binti yangu Judith. Ilipita miezi bila yeye kuzinduka toka alipozimia.”Mzee Martin alisema kisha akanyamaza kidogo na kutupa macho katikati ya umati wa watu ambako kulikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa akitoa sauti ya kilio huku wengine wakigugumia kwa ndani ndani na kufuta machozi kwa vitambaa vyao vya mkononi.





    Madaktari walijitahidi kufanya kazi yao kwa kila mbinu lakini ilikuwa ni kama kazi bure tu. Wakati huo wote Kijana huyu alikuwa bega kwa bega na mimi katika kumuuguza Judithi kwa kuhakikisha kila kilichohitajika na madaktari kilipatikana kwa haraka. Peke yake alikuwa ndiye ndugu wa karibu sana katika kusimamia majukumu ya muhimu katika kipindi hicho kigumu. Baada ya miezi miwili ya kuuguza ilitokea siku kama ndoto Judithi alizinduka na kupiga kelele na kuongea mambo mengi ya ajabu.

    Daktari alisema kuwa ni kawaida kwa watu waliozimia kutokana na matukio ya kutisha wanapozinduka wanaona kana kwamba tukio lile linatokea wakati huo huo. Baada ya muda Daktari alimpiga sindano ya usingizi kusudi asizidi kupiga kelele. Hiyo ilisaidia sana maana baada ya muda wa masaa mawili alishtuka usingizini akiwa hana tatizo la kelele tena. Furaha yangu ilikuwa kubwa sana kuona kuwa binti yangu anaweza kumtambua kila mmoja wetu. Kwa siku mbili mfululizo hali ya binti yangu ilikuwa ni njema sana isipokuwa maumivu ya mwili kidogo pamoja na udhaifu wa mwili.

    Kutokana na hali nzuri aliyoipata binti yangu kijana huyu aliniomba ruhusa kwani alikuwa anatakiwa akaongeze elimu yake ya uinjinia wa majengo nchini marekani kwa muda wa miaka miwili. Baada ya mimi kumruhusu alimwomba mchumba wake pia amruhusu japo walipanga kuwa ataitumia likizo yake ya kwanza kabisa kurudi na kufunga ndoa yao. Makubaliano yao niliyaheshimu sana na kuahidi kuwa nitawajibika kwa upande wangu.

    ***

    Lilikuwa ni swali la kutisha sana kulijibu! Tatizo halikuwa kujibu swali kiusahihi bali namna ya kumjibu muuliza swali ndipo kasheshe ilipokuwa. Waswahili walisema “Ukweli unauma” huo ni usemi wenye busara nyingi ndani yake. Ukweli ni kitu kizuri sana lakini unategemea na matumizi yake ya lipi la kusema na yupi aambiwe na kwa wakati gani ukweli huu uende kwa mlengwa.

    Hiki ndicho kitu nilichogombana nacho kwa zaidi ya siku mbili nzima mbele ya binti yangu. Swali lake kuhusu aliko mama yake lilinisumbua sana kiasi cha kuzunguka katika kulijibu hasa nikizingatia kuwa jibu lake litakuwa na madhara makubwa sana kwa binti yangu. Nisingeweza kusema moja kwa moja ukweli huu japo siku moja ukweli huu huu ninaoukwepa kuusema utakuja kuwa wazi hata kama sikuhusika kuusema mimi. “Mama yangu yuko wapi?!” Alirudia kuuliza mara ya tatu wakati alipogundua kuwa majibu ya kwanza yalikuwa sio sahihi. Kwa kukwepa kumuumiza nilimwambia kuwa mama yake alikuwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi na hakukuwa na ruhusa ya kumwona kabisa. Jibu hilo lilidumu kwa siku mbili kisha lilichuja hivyo lilitakiwa litengenezwe tena ili likidhi haja ya muulizaji hasa ukizingatia kuwa sikuwa nikicheza na mtoto wa chekechea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kukosa namna ilibidi swali la binti yangu Judith lijibiwe kama linavyostahili. Hapo ndipo uchungu wa jibu hilo ulipoleta maumivu kamili yaliyoitesa familia hii kwa muda wa miaka miwili na nusu. Baada ya kumwambia kuwa mama yake amefariki dunia siku ile waliyopata ajali ya gari; alipiga ukelele wa kutisha na kuzimia tena. Hali hii ilichukuwa muda wa wiki moja mpaka kuzinduka. Tatizo lilizidi kwani aliamka akiwa hana akili timamu. Binti yangu na ndugu yangu wa pekee alizinduka akiwa kichaa kabisa. Matibabu hayakufaa kitu wala hakuna ushauri nasaha ulioweza kupenya kwenye akili yake ambayo ilikuwa haipo mahali pake. Moyo wangu uliniuma nilipomwona binti yangu akizurura barabarani huku akipiga watu na kuokota makopo na vitu majalalani.

    Hasira mbaya zilinikamata pale nilipomwona binti yangu akizomewa na watoto wadogo na kutupiwa mawe. Mateso yalizidi pale alipokamatwa kwa amri yangu na kufungwa kamba ili asitoke ndani kabisa. Niliumia kumwona msomi huyu mwenye shahada zake akiumia kwenye kamba huku akipiga kelele na kuongea maneno yasiyoeleweka. Tangu hapo nikawa sifanyi kazi sawa sawa na uwezo wa kusimamia kampuni yangu ya Upokeaji na usafirishaji mizigo ukawa dhaifu sana kiasi cha kusababisha nifunge kampuni yangu hiyo. Mambo haya nitayamalizia mwishoni kwa sasa nampisha Kijana wangu Sebastiani Changawe.” Alisema Mzee Martin Sebwaka huku akikiachia kipaza sauti mikononi mwa kijana aliyeonekana kuwa mpole sana lakini mwenye sura nzuri na umbo la mazoezi.

    2

    Pumbazo la moyo!

    Kwangu ilikuwa ni ndoto ya mchana kweupe! Ndoto ambayo nilijiapiza kuwa ni lazima niishi ndani ya ndoto hiyo siku zote za maisha yangu. Haikuwa rahisi kuisahau na moyoni mwangu ilikuwa ni lazima niitunze ili iendelee kuachilia uzuri wake wa shani katika maisha yangu. Siku hii ilipambazuka vema bila mvua na bila jua, hali ya hewa ilikuwa swari.

    Nilifurahia kuwa barabarani nikiwa ndani ya gari yangu ambayo ilikuwa ndio mara ya kwanza kuiendesha tangu itolewe bandarini. Moja kwa moja niliendesha gari yangu kutoka Mbezi beach kuelekea Mikocheni mahali zilipo ofisi za Usafirishaji na upokeaji mizigo iitwayo Mart & Judika Clearing & Forwding Company. Ofisi hizi nilikuwa sizijui zilipo ila nilipewa ramani na rafiki yangu Sudi, baada ya kumweleza kuwa nina shida ya muhimu inayohusu upokeaji wa mizigo yangu toka bandarini. Hii ilitokana na kufungwa kwa ofisi ya kwanza niliyokuwa ninaitumia kupitishia mizigo yangu binafsi. Uelekezaji wake ulikuwa wa kueleweka kwani sikuweza kupotea baada ya muda nilifika bila tatizo.

    Hapo ndipo nilipokutana na kile nilichokiita ndoto ambacho mpaka sasa kitu hicho ndicho kilichoyafanya maisha yangu kuwa katika sura ya tofauti na hapo mwanzo. Baada ya kuegesha gari yangu katika maegesho ya ofisi zile nilitoka na kuanza kupanda ngazi taratibu kuziendea ofisi hizo ambazo mandhari yake yalikuwa ni mazuri sana. Moja kwa moja nilienda mapokezi na kuuliza kama meneja alikuwepo. Baada ya taratibu za kawaida za kiofisi nilielekezwa ilipo ofisi ya meneja. Niliondoka taratibu na kugonga hatimaye nikasukuma mlango wa Ofisi hiyo.

    Hapo ndipo nilipoona kama niliyeingia katika sayari nyingine. Sio kwamba mimi ni mgeni wa kuingia kwenye Ofisi za viwango kama ile hapana. Nilishatembelea ofisi nyingi sana ndani ya nchi hii na nchi nyingi za ulaya. Mpaka hapo nadhani utakuwa umeelewa nini kilichonipumbaza! mbele yangu alikaa msichana ambaye kwa utashi wangu wa haraka haraka nilidhani kama nimeona malaika.

    Moyo wangu ulipoteza mapigo kama matatu hivi na baadaye ukazidisha mapigo mengine manne kwa haraka. Uzuri wa dada yule sikuweza kuulinganisha na mtu mwingine niliyewahi kumwona. Hata sauti yake ilipotoka na kutamka neno “karibu” mimi nilikuwa kwenye maono mengine yaliyotangaza upendo halisi juu ya kiumbe hiki. Ndani ya moyo kuliimba shairi hili:

    Utashi wanisukuma, kuchunguza ua hili,

    Mapigo yanirindima, tamaa yanikabili,

    Maamuzi yanagoma, yanizunguka akili,

    Ni lulu ama johari, au pumbazo la moyo?



    Naona ni kama ndoto, yanihadaa akili,

    Haikuja kimkato, sio nusu ni kamili,

    Sura yake kama kito, si uongo ni ukweli,

    Ni lulu ama Johari, au pumbazo la moyo?

    Uzuri wanihadaa, nikadhani malaika,

    Kitambo nikaduwaa, upendo ukachipuka,

    Uzuri uso mawaa, wanipa kubabaika,

    Ni lulu ama johari, au pumbazo la moyo?

    Katika taharuki yote hiyo bado nilijaribu kujikaza na kueleza shida yangu kwa sauti ya taratibu na ya kujiamini. Tangu wakati huo nilisukumwa ndani yangu na upendo halisi. Upendo ulionifanya kichaa kwani sikuweza kupitisha siku bila kuchokoza salamu kwa mwanadada huyo. Pole pole niliamua kumweleza vile moyo wangu ulivyo kwake. Ombi langu lilipingwa kwa muda na kunifanya nikose amani kabisa katika maisha yangu.

    Lakini baada ya muda nilipata jibu nililolingojea kwa hamu kubwa. Sharti la kwanza ni kwamba niende nyumbani kwa wazazi wake ili nijitambulishe na taratibu zianze za kuyaendea maisha ya ndoa. Kwakweli furaha yangu ilikuwa ni kubwa sana kusikia hivyo. Nafasi hiyo niliitumia vizuri kwa kuwaendea wazazi wangu na kuwashirikisha. Mipango ilipangwa ya kwenda kujitambulisha kwa familia hii kuwa vijana wao tuna mpango wa kuunga undugu kati yao. mazungumzo yao yalifikia mwafaka mzuri. Naam mwafaka uliopelekea mimi na Judith kuwa wachumba rasmi. Ikabakia siku ya kulipa mahari ikapangwa isiwe mbali sana kusudi kujiandaa siku ya ndoa yetu.

    ***

    Nilihisi kama dunia iliamua kunizomea na kunidhihaki. Taarifa za ajali iliyotokea ili nichanganya sana. Nilitoka ofisini kuwahi eneo la ajali lakini sikuambulia kitu waathirika wa ajali hiyo walikuwa wapo hospitali wakati huo.

    Moyo uliniuma sana nilipofika Wodini na kukuta taarifa za kifo cha mama mkwe wangu na kwamba mchumba wangu alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi. Tatizo la ajali lilitokea ikiwa imebaki siku moja tu kwa wazazi wangu kwenda kutoa mahari kwa wazazi wa Mchumba wangu. Ajali iliyochukuwa maisha ya mama mkwe wangu mtarajiwa na kumwacha mchumba wangu akiwa amezimia kwa muda mrefu sana.





    Hii ilinitesa sana moyoni na kila wakati asubuhi na jioni nikiwa narudi ofisini nilikuwa Hospitali nikisaidiana na baba mkwe wangu. Na baadaye ratiba zilibadilika niliamua kupanga kazi kwa wasaidizi wangu ili niwe ninashinda Hospitali kusudi kumpa nafasi mzee Martin aende naye kusimamia Ofisi yake. Hayo yote yalifanyika pamoja na sala na kuangalia namna ya kupata dawa zilizohitajika na mwishowe kama ndoto Mchumba wangu alizinduka na kukaa japo ilipita miezi miwili.

    Alionekana buheri wa afya baada ya siku tatu tangu azinduke. Ikawa ni wakati wa kuyarudia majukumu ya kazi kwa kila mmoja wetu. Kuona hivyo ndipo nilipoamua niende masomoni Marekani safari ambayo niliiahirisha kwa muda kutokana na tatizo lililotokea. Ofisi yangu ilikuwa imeshagharimia kila kitu, nikisubiriwa mimi tu kwenda kuchukuwa kozi hiyo muhimu.

    Niliagana na familia ya mchumba wangu na kuahidi kurudi wakati wa likizo. Nilipanga kuwa mara tu baada ya kupata likizo yangu ya kwanza ningerudi nchini na kufunga ndoa na mpenzi wangu kisha ningerudi kumalizia masomo yangu kwa amani. Siku ya safari mchumba wangu alinisindikiza, japo ilikuwa ni ngumu sana kuambiana kwaheri, lakini hakukuwa na budi wakati ulipofika. Ndege ilikuwa tayari na mimi nilipaswa kupanda tayari kwa safari. Ni hapo nilipoachiana na mchumba wangu machozi yakiwa yanatutoka kama tulikuwa kwenye msiba. Kabla ya ngazi ya ndege kupandishwa niliwahi kupanda huku nikipunga mkono kwa taabu na ndege ikaanza safari.

    Maisha yangu yalionekana kupwaya hasa pale nilipokuwa mbali na mpenzi wangu. Taarifa za mara kwa mara kuwa anaendelea vizuri zilinifurahisha sana na kunipa nguvu ya kuendelea vema na masomo nikiwa nasubiri likizo ifike upesi niweze kwenda kutimiza ahadi yangu ya kufunga ndoa na mpenzi wangu. Kuna jambo ambalo lilinipa maswali mengi lakini nilijipa moyo siku mbili tatu kuwa huenda lingekaa sawa. Suala hilo lilibaki katika hali yake ileile kwa muda mrefu. Kila ninapopiga simu nilikuwa napokelewa na mtu mwingine! Mchumba wangu hakuwahi kuwa hewani kwa kipindi kirefu pale nilipomtafuta ili tuongee. Maswali yangu yalikuwa yakijibiwa bila utoshelezi wa haja. Kwangu ulikuwa ni utata!

    Hivyo nikafikia hatua ya kuamua kuomba ruksa masomoni ili nirudi nyumbani kwa kusingizio kuwa kuna tatizo kubwa la kifamilia limetokea. Nilikubaliwa ya kuwa ingebidi nirudie masomo yangu pindi nitakaporejea tena. Haraka sana nilianza safari ya kurudi nyumbani Tanzania.

    Mara baada ya kufika nyumbani kwangu nilianza safari kwenda nyumbani kwa mchumba wangu, ili nijue sababu hasa ya kutopatikana kwake hewani. Macho yangu hayakuamini nilichokiona nje ya nyumba ya akina Judith mchumba wangu. Nashindwa kuelezea kutokana na uchungu nilioupata baada ya kumwona mchumba wangu akizomewa na watoto wadogo huku yeye akiokota makopo na kuwafukuza kwa namna ya kiuendawazimu.

    3

    Ukurasa wa giza

    Walikuwa kama mapacha wakizunguka pamoja na kukaa pamoja pale wanapokuwa wamechoka kuzunguka. Mitaa yote waliipitia kama wakaguzi wa mazingira. Mavazi yao yalikuwa yamechakaa na kuchafuka huku wote wakiwa hawajali kutokana na hali yao hiyo. Watu waliowajua sana hawakuamini macho yao juu ya ziara zao za kuzurura hovyo bila mpango. Walionekana wote wawili wamechanyikiwa hasa!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini kwa namna nyingine yalionekana kama maigizo au sinema iliyokuwa inaandaliwa ili ije kuonekana kwenye Television huku wao wakiwa wapo katika majumba ya starehe wakifaidi matunda ya kazi yao hiyo. Hayo yalikuwa ni mawazo ya baadhi ya watu katika upeo mwingine wa ufahamu. Lakini ukweli ukabaki kuwa mmoja wa watu hawa alikuwa na matatizo ya akili na mwingine alikuwa ni mlinzi wake, ambaye alikuwa anamkinga na watu wabaya waliokuwa aidha wakimdhihaki ama watoto waliokuwa wakimtupia mawe. Ilikuwa ni kazi ya hiyari kabisa kwa mlinzi huyu ambayo aliifanya kwa moyo mmoja kama “Jet Lee kwenye sinema yake ya The Boadgurd.”

    Mlinzi huyu ambaye kwa jinsia alikuwa ni mwanamme alikuwa makini sana pale anapoona mwenzake akiingia mahali pabaya, alijitahidi kumrudisha na pale watoto walipotaka kumpiga mawe aliwafukuza na kuwapa onyo kali sana. Hali hii ilifanyika pia pale mwenzake alipotaka kula kitu alichookota jalalani yeye alimkataza na badala yake alimtolea mkate mzuri au tunda kutoka katika mfuko aliokuwa ameubeba.

    Yakikuwa ni mapenzi ya aina yake ambayo hayakuwahi kutokea duniani. Hayakuwa maigizo bali yalikuwa ni kitu halisi kwa watu hawa wa jinsia tofauti. Walionekana kama mke na mume katika maisha halisi yenye utata wa kutisha. Walioshuhudia maisha haya baadhi yao walilia machozi lakini wengine walicheka na kufanyia maigizo ya kuchochea vicheko zaidi kwao na kwa watu wengine. Hii ilionyesha utofauti wa wanadamu katika roho zao. Kuna wengine wanahisia za huruma na upendo, wakati wengine wakiwa sawa na wanyama pori ama mashetani.

    Waandishi wa habari waliweza kuyalisha magazeti na Redio pamoja na Televisheni kwa habari za watu hawa, huku wakieleza kwa undani utafiti wao. Magazeti mengine yaliyokosa kupata habari mbalimbali kwa haraka yaliifanya habari ya watu hawa ichukuwe nafasi kubwa zaidi ya habari nyingine. Wasomaji nao walihitaji kujua zaidi na wengine walitafuta namna ya kufika katika eneo husika ili kuwaona kwa macho yao wenyewe. Yote kwa yote lakini kwa watu hawa wawili maisha yaliendelea katika mfumo wao wa kushangaza. Hakuna aliyeonekana kuchoshwa na maisha haya si mlinzi wala yule mwanamke aliyekuwa akilindwa dhidi ya maadui zake.

    Mlinzi huyu ambaye alionekana pia kuwa halikadhalika na yule aliyekuwa akilindwa alikuwa akionekana kuifurahia kazi yake kwani alitembea sambamba na mwanamke yule na wakati mwingine walikuwa wakizungumza mazungumzo yao na kuonekana kuelewana kwa kila walichoongea.

    Hii ilizidi kuwahakikishia watu waliowaona kuwa walikuwa wakifanya maigizo japo hakukuwa na watu waliokuwa wakiwachukuwa picha za video. Picha nyingine iliyojijenga kwa baadhi ya watu ni kuwa watu wale walikuwa ni wapelelezi kutoka usalama wa Taifa. Mawazo hayo yalipasishwa na baadhi ya watu pale walipojiridhisha nafsi zao kwa utafiti wao uliolingana na viwango vyao kiufahamu.

    ***

    Ilikuwa ni kauli iliyoonekana kama haikutokana na maamuzi sahihi. Kauli ya kuamua kuacha kazi katika shirika kubwa la kimataifa la Uuzaji na ununuzi wa magari yenye ubora wa hali ya juu. Akiwa na cheo cha meneja masoko Sebastian Changawe alikuwa na mafanikio makubwa sana yaliyotokana na mshahara mnono ulioambatana na marupurupu mengi sana japo kando ya hapo alikuwa na kampuni yake mwenyewe.. Haikuingia akilini kwa mkurugenzi wa shirika pale Meneja wake alipoingia asubuhi hiyo na barua mkononi ya kuacha kazi.

    Cha kwanza kilichomshangaza ni siku tatu nyuma kupata habari kuwa Sebastian amerudi kutoka nchini Marekani akidai kuacha masomo kutokana na matatizo ya kifamilia. Pamoja na uchunguzi wake Mkurugenzi huyo hakuona tatizo lolote katika familia ya Seba ila hata hivyo hakuongea lolote mbele yake kuhusu hilo. Uhusiano wao mzuri katika kazi ulimfanya afumbe kinywa chake kwani hakutaka kuingilia maisha binafsi ya meneja wake.

    Kunyamaza kwake wakati wa ripoti ya Seba kuwa amerudi nyumbani toka masomoni kwa ajili ya kutatua matatizo ya kifamilia kulimridhisha yeye mwenyewe kuwa ilikuwa ni njia bora zaidi ya kulinda urafiki kazini na kuheshimu maamuzi ya mtu. Lakini hili la leo kwake lilikuwa ni kubwa sana na la kushangaza hasa pale Meneja wake huyo alipokuja kudai kuwa anahitaji kuacha kazi. Katika barua yake alieleza kuwa anauguliwa na mke wake mtarajiwa ugonjwa ambao yeye asingestahimili kumwacha peke yake.

    Maelezo yake nayo hayakusaliti uamuzi wake aliouainisha kwa maandishi hata pale alipobembelezwa na Mkurugenzi wake. Haikuwa rahisi kubadilisha maamuzi hayo hata kwa ahadi ya mabilioni ya shilingi na hata kwa tisho la kuondolewa kichwa chake. “Kwangu imekuwa habari ngumu sana hii kuisikia bwana Seba. Imekuwa rahisi kusikia kuwa umeacha masomo nchini Marekani kwa matatizo ya kifamilia lakini imekuwa ngumu kwangu kulipokea jambo hili la wewe kuacha kazi.”

    Alisema mkurugenzi mkuu ndugu Gideon Rutashobya kwa masikitiko makubwa. “Ni kweli mkuu wangu wa kazi una haki ya kunishangaa sana na labda utashangaa zaidi kwa mambo yangu, mpaka nitakapoona mchumba wangu amepona ugonjwa wake. Kwa sasa maamuzi yangu yatabaki hivyo hivyo bila kujali kuwa itaniathiri kiuchumi namna gani.” Alisema Seba kwa uchungu.





    “Kwani mchumba wako anaumwa ugonjwa gani? Ningeweza kupitisha kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya matibabu yake hata kama yatafanyika katika nchi yoyote ya Ulaya.” Alisema Mkurugezi huku akimwangalia kwa makini Sebastian akitarajia kupokelewa kwa furaha na shukrani. “Nashukuru sana mkuu kwa kunijali kwa kiwango hicho kikubwa. Ila inabidi tuhakikishe kwanza vipimo katika Hospitali zetu hapa nchini ili wakigundua aina ya ugonjwa watupe rufaa ya kwenda katika nchi yoyote ya nje kama ulivyosema.

    Kwa kweli nashukuru kwa upendo huu mkubwa kwangu.” Alisema Seba na kupatana na Mkurugenzi wake kuwa angempa taarifa ya vipimo kutoka hospitali ya muhimbili na kama watamtibu hapa nchini angetoa taarifa hiyo pia. Kwa hiyo maswala ya kuacha kazi yaliwekwa pembeni ili washughulikie swala la vipimo na matibabu.

    ***

    Serkali ya kichwa chake ndiyo iliyokuwa ikimwamulia kufanya kila alichopanga kufanya. Hakuhitaji mtu yeyote aamue lolote katika mambo yake na wala hakutaka kushirikisha matatizo yake kwa mtu yeyote. Alijua hakuna mtu atakayekubaliana na maamuzi yake kwani yakuwa kama ya kiuendawazimu. Maisha yake yalitawaliwa na utata mara tu baada ya kuingia katika majukumu ya kumuuguza mpenzi wake. Aliyaona mabadiliko hayo kwa uwazi kabisa lakini alikubaliana na kila kilichokuwa kinatokea kama sehemu ya mapenzi ya Mungu kwake.

    Hakuwa mtu wa kumlaumu mtu mwingine na wala hakuwa mtu wa kuogopa kuchukuwa maamuzi yoyote ilimradi uamuzi huo utaleta manufaa kwa mpenzi wake ama nafuu juu ya shida ya maradhi yaliyomkumba. Uvumilivu wake ulikuwa ni mwingi usio na kikomo lakini moyoni akiwa anajua kuwa kila lenye mwanzo lazima lina mwisho wake. Siku hii ilikuwa nzuri sana kwa hali ya hewa lakini katika kichwa cha Sebastian kulikuwa kunawaka jua kali lililoambatana na kipupwe cha kutisha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hii inatokana na majibu aliyopata Hospitalini kuhusu vipimo vya Judith Mchumba wake. “Tatizo la Huyu binti halina matibabu maana limetokana na mchubuko wa ubongo tatizo linalotokea kwa mtu aliyepata mshtuko mkubwa sana ama aliyepata jambo linaloumiza kiasi cha kutumia muda wake mwingi katika kuwazia jambo hilo kwa maumivu makubwa.” Alisema Daktari Gilbert Osward Dr. wa magonjwa wa akili.

    Kwa utafiti uliofanyika katika chuo kikuu cha utabibu cha Mental Human University kilichoko nchini Hispania, jopo la madaktari waligundua kuwa mwanadamu anapokuwa katika kuwango kikubwa cha maumivu ya moyo huufanya ubongo wake kuingia kazini kwa kiwango kikubwa sana. Na katika kiwango kilekile anapopata pigo jingine linalosababisha aingie katika mawazo zaidi huuathiri ubongo na kuufanya aidha uchubuke au mishipa yake ipasuke na kusababisha kifo cha mtu huyo.

    Lakini kama ubongo wake utabakia katika ngazi ya mchubuko mtu huyo atachanganyikiwa kabisa. Tatizo la kuchanganyikiwa kwa kawaida kama limetokana na mchubuko huo wa ubongo halina tiba zaidi ya kumtunza tu mgonjwa na kumpa madawa ya usingizi ambayo hufanya kazi ya kuutuliza ubongo usibughuziwe na kumbukumbu yoyote ile ya mambo yale ya kuumiza.

    Aidha utafiti umegundua kuwa baada ya muda wa kuwepo katika hali hiyo ya kuchanganyikiwa ule mchubuko unaweza kupona jeraha lake na kumfanya mtu huyo kupona kabisa tatizo lake.” Alielezea Daktari kwa ufafanuzi wa kina. “Tunashukuru sana Daktari kwa maelezo yako na jitihada za kumtibu mgonjwa wetu. Ila swali letu ni kwamba inamchukuwa muda gani mgonjwa wa aina hiyo tangu anapoanza kuchanganyikiwa kupona jeraha lake na hatimaye kurudiwa na fahamu zake?.”

    Aliuliza swali hilo Mzee Martin wakati Sebastian akiwa kimya huku ameshika shavu lake kwa mawazo mengi ya uchungu. “Kwakweli utafiti haujasema ni muda gani unatumika lakini kwa maoni yangu ni kwamba uvumilivu wenu kwa mgonjwa na kutokumsumbua kwa lolote ndiyo dawa inayosababisha asiingie katika hali ya kutumia akili zake katika kukumbuka au kukabiliana na matatizo yawayo yoyote yale.

    Kwa mfano hata akivunja kitu jitahidini kumvumilia na kumchukulia kwa upole na upendo badala ya kumfokea na kumwonyesha chuki. Hali hii inaweza kufanywa na madaktari katika Hospitali za watu wenye matatizo ya akili, hawa wamesomea jinsi ya kuchukuliana na wagonjwa na kwakweli wagonjwa wengi wenye matatizo ya namna niliyoielezea hapa walipata kupona na kurudi kwenye majukumu yao ya maisha.” Kimya kifupi kilipita wakati akitafuta kitu fulani kwenye droo ya meza. Kisha akaendelea huku akimwangalia mzee Martin.

    “Kwa vipimo tulivyofanya ni kwamba mgonjwa ana matatizo hayo ya mchubuko wa ubongo. Kwa hiyo hata kama tungemwandikia aende kwenye hospitali yoyote kubwa duniani asingepata matibabu yoyote. Atakachofanyiwa ni kuwekwa sehemu za kuwatunzia wagonjwa wenye matatizo ya akili. Kwangu mimi sioni kama ni muhimu kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa inawezekana hata hapa nchini kwetu akatunzwa vema mpaka hapo akili zake zitakapomrudia.” Alisema Daktari kwa msisitizo.

    “Asante kwa maelezo yako na ushauri wako mzuri. Lakini je kama tutaamua kutokumpeleka kwenye hospitali yoyote na badala yake tukachukuwa jukumu la kumtunza sawasawa na maelekezo uliyotoa si inaweza kusaidia pia? Aliuliza Sebastian huku akimtazama daktari akingojea jibu kwa hamu kubwa.

    “Ndio bwana mdogo inawezekana kwani hata kule wanakotunzia watu kama hawa hakuna matibabu zaidi ya kupewa dawa za kutuliza kasi ya mawazo na wakati mwingine kuwapa vidonge, ama kuwapiga sindano za usingizi wale wanaoonekana wamezidiwa. Ila kwakweli mkizingatia kumtuza wenyewe bila kuchukulia hasira mambo yoyote anayoyafanya na kumpatia dawa za usingizi inawezekana akawa salama zaidi na pia anaweza kurudiwa na ufahamu wake mapema japo haiwezekani kutabiri ni wakati gani.”

    Alisema Daktari wakati akinyanyuka na kuendea kabati lenye madawa ya kila aina. Baada ya kufika alitoa vichupa kadhaa na kutoa dawa za vidonge kisha akarudi pale alipokuwa mwanzoni. “Dawa hizi ni muhimu mumpatie pindi tu anapokuwa anaonyesha kuzidiwa zenyewe ni za usingizi na ndani yake zinatuliza maumivu ya kichwa maana zimechanganywa na paracetamol. Mpaka sasa naweza kuwapa ruhusa muondoke na mgonjwa. Alisema Daktari baada ya kukamilisha maelezo yote na akina Seba kukamilisha taratibu za malipo.

    ***

    Kikao kilishindwa kuamua lolote katika maamuzi yaliyotolewa na Mkurugenzi wa kampuni. Hayakuwa mambo ya kujadili bali yalikuwa ni maamuzi ya mkuu wao wa kazi. Minong’ono ilisikika kwa baadhi ya wajumbe na baadaye katibu wa kampuni George Baro alinyanyua mkono kutaka nafasi ya kuongea jambo. “Enhee sema katibu!” Alisema Mkurugenzi Seba wa kampuni ya Seba & Ellychangawe Enterprisess.

    “Nina wazo mkuu, ambalo ninaona japo niliseme kuliko kuendelea kunyamaza nalo, huenda litakuwa na manufaa kwako na kwetu sote.” Alisema George Lukindo kisha akakohoa ili kusafisha koo lake kwa ajili ya kuendelea kuongea. “Sawa George nasubiri nisikie wazo lako.” Alisisitiza Mkurugenzi. “Kwakweli mimi binafsi bosi siafikiani na maamuzi yako japo inabidi unisamehe kwa kujaribu kuingilia kile ulichoamua na ambacho wewe mwenyewe ulikifikiria kwa muda kabla hujatuita katika kikao hiki. Lakini kwa sababu ni kikao kinachoshirikisha watu wenye mawazo mbalimbali ni vizuri niwakilishe mawazo haya upande wangu.” Akanyamaza kidogo akimwangalia mkurugezi alivyoona anasikilizwa akaendelea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Majukumu unayotaka kutuachia ni magumu iwapo wewe mwenyewe hutakuwepo katika nafasi yako kama mkurugenzi. Kuwepo mahali kwa ajili ya kuuguza mgonjwa tu hakutoshi kukufanya usitokee hapa ofisini kwa muda usiojulikana. Ilimradi utakuwepo hapa hapa mjini tunaomba ututembelee mara moja moja ili kusikiliza shida zetu na kutusaidia. Ni hayo tu mkuu nitashukuru kusikia kuwa nimekubaliwa ombi langu kwa niaba ya wenzangu.”

    Alisema George Lukindo kwa unyenyekevu. “Hilo ombi sio baya bwana George na ni la msingi sana kwa ajili ya manufaa ya kampuni. Ila kwangu kuwaachia nafasi hii ni kuonyesha jinsi gani nimewaamini kwamba mnaweza kusimamia mambo kwa muda huo nitakaokuwepo katika kazi zangu binafsi. Ningejisikia furaha sana kama ningeenda kwa muda huo na siku nikirudi nikaona mambo yameenda vizuri na kampuni ikiwa inaendelea kufanya vema.









    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog