IMEANDIKWA NA : CHANGAS MWANGALELA
*********************************************************************************
Simulizi : Kuti Kavu
Sehemu Ya Kwanza (1)
MGUU wa kushoto ulipiga hatua ukifuatiwa na ule wa kulia, hatua kwa hatua lengo likiwa ni kufika kule alikokusudia. Bila kujali amechoka kiasi gani, aliendelea kusonga mbele licha ya utitiri wa mawazo uliofurika kichwani mwake.
Viatu vyake aina ya mokasini nyeusi vilivyoanza kuchakaa, suruali yake nyeusi iliyopauka kiasi, na shati jeupe alilovaa, kwa pamoja vilitosha kabisa kudhihirisha hali ngumu ya uchumi aliyonayo kijana Dominic Masaka, au Domi kama wengi walivyolifupisha jina lake.
Domi alikuwa amechomekea vema, na kuonekana maridadi kwa mavazi yake licha ya mpauko uliodhihiri waziwazi kwenye mavazi aliyovaa.
Njaa iliyokuwa ikimfukuta tumboni mwake haikutosha kumkatisha tamaa na badala yake ilimuongezea hasira na kiu ya mafanikio ambayo ilikuwa ikijipambanua wazi wazi usoni pake.
Kijana huyu mrefu wa wastani, mwenye sura jamali alikuwa akikatisha katika mtaa wa Azikiwe maeneo ya Posta mpya, eneo ambalo liko katikati kabisa ya jiji la Dar es salaam.
Dominic alikuwa na mawazo mengi kichwani mwake ila mawili katika hayo ndiyo yaliyoonekana kumchanganya zaidi. Kwanza; ni aina ya maisha anayoishi, maisha ambayo aliona hayaendani kabisa na kiwango cha elimu aliyonayo!
Kwa msomi kama yeye kuishi maisha anayoyaishi kwa sasa, ni aina ya maisha ambayo hayakumuingia kabisa akilini kijana Domi. “Maisha gani haya!” Domi alilalama.
Kila alipojaribu kutafuta unasaba uliopo baina ya elimu yake na aina ya maisha anayoyaishi, Domi alizidi kuchanganyikiwa kabisa!
Domi hakutaka kabisa kuamini kama kuna wasomi wa kiwango cha elimu yake, ambao wanaishi aina ya maisha anayoishi yeye. Kama wapo na wameiridhia aina hii ya maisha, basi yeye alikuwa kinyume kabisa na fikra zao.
Kwa Dominic, msomi wa kiwango cha elimu yake hakustahili katu kuishi maisha kama anayoyaishi yeye, ndiyo maana kila mahali na kila nukta ya saa Dominic amekuwa akihangaika kutafuta suluhisho la matatizo ya kiuchumi yanayomakabili.
Swala jingine lililoitesa akili ya Domi, ni juu ya mpenzi wake aitwaye Doi. Domi alikuwa akiustaajabia upendo wa Doi kwake, upendo ambao ni wa kupindukia licha ya ugumu wa maisha alio nao!
Doi alikuwa ni mwanamke mwenye mapenzi ya ajabu kwa Domi. Kwa sababu ya mapenzi hayo mazito kwa Domi, Doi aliridhia na kuvumilia kila hali aliyo nayo Domi! Domi aliutafakari sana upendo wa Doi kwake, lakini mfanowe hakuupata.
Ni siku ya tatu sasa, hawali chochote isipokuwa uji wa sembe usiokuwa na hata chembe ya sukari! “Baby, najua unanipenda kama mimi ninavyokupenda, nap engine hata zaid. Lakini hali ya maisha ni kama unavyoiona mpenzi. Unaonaje kama utarudi nyumbani kwanza, halafu nikishaweka mambo sawa nitakuja kukuchua.” Hiyo ilikuwa ni sauti ya Domi akijaribu kumrai mpenzi wake japo kwa shingo upande. Ndiyo ni kwa shingo upande kwa sababu, kwanza yeye kama mwanaume hakustahili kuonesha kuwa amekata tamaa kwenye kuihimili mikikimikiki ya maisha.
Pili, alihofu kauli hiyo isije kutafsiriwa na Doi kuwa ana mpango wa kumtema kijanja, na anautumia ugumu wa maisha kama kigezo ili iwe rahisi kwa Doi kumuelewa.
Kinyume na matarajio yake, Domi alishangazwa na majibu yaliyotolewa na Doi, “Nakupenda Domi, na kwa sababu nimekupenda kwa hiyari yangu toka moyoni, sina budi kuvumilia kila kitu. Usiwe na wasi wasi mpenzi… shida yako ni shida yangu, kwa nini niondoke, eti kwa sababu maisha yamekuwa magumu? Yana mwisho haya mpenzi wangu, cha msingi ni kutokata tamaa...”
Domi hakujua aseme nini na badala yake akawa anatokwa na machozi!
Kwa moyo wa kiume Domi akasema, “Siyo kama nakufukuza mpenzi, usinielewe vibaya… kwa nini uteseke na maisha haya wakati kwenu ungeweza kukipata kila unachokitaka, tofauti na hapa ambapo tunaishi maisha ya kubahatisha….”
“Ni kweli usemayo Domi, ningeweza kupata kila kitu ninachokitaka, lakini wewe siwezi kukupata nikiwa nyumbani kwetu. Niko hapa kwa ajili yako na si kitu kingine…” Alisema Doi na kumkumbatia Domi, “Nakupenda Domi….nakupenda sana” Doi alizidi kusisitiza huku akimtazama Domi kwa macho yaliyojaa huba. Domi alikuwa akiyakumbuka haya wakati yuko barabarani katika mitaa ya katikati kabisa mwa jiji la Dar es salaam.
Njaa ilikuwa ikimwuma lakini alijikaza kwa sababu hakuwa na jinsi. Alitembea mpaka pembeni ya jengo la ATC (Air Tanzania Cooperation) akalitazama lile jengo kwa jicho la matamanio, kisha akaelekea kwa fundi wa kung’arisha viatu aliyekuwa nje ya ya uzio wa jengo lile na kujipumzisha kwenye benchi la huyo mng’arisha viatu.
“Habari kaka” Domi alisalimia na kuitikiwa na yule mngarisha viatu ambaye tayari walikuwa wamekwishazoeana.
“Salama braza, karibu.”
“Ahsante braza, naomba nijipumzishe hapa ofisini kwako kidogo,”
“Hakuna shida, uko huru braza,” Alijibu yule mngarisha viatu huku akiachia tabasamu pana usoni pake.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Domi alikaa pale kimwili tu, na akili yake akaiacha iende safari, iendelee kutafakari juu ya aina
ya maisha anayoishi na mpenzi wake ili kuona ni jinsi gani atayapatia suluisho.
Akiwa kwenye lindi la mawazo, Domi alishtuliwa na mlio wa simu yake ya mkononi. Kwa haraka aliitoa simu mfukoni ili aipokee, lakini kabala hajaipokea aliona ni vema kama atasoma kwenye kioo cha simu ili amjue mpigaji wa simu hiyo. Macho ya Domi yalipotua kwenye kioo cha simu yake ya mkononi moyo wake ukaanza kumwenda mbio! Kwenye kioo hicho cha simu Domi aliliona jina alilolitarajia. Kwa moyo wa matumaini alibonyeza kitufe cha kijani ili kuruhusu mazungumzo na mpigaji wa ile simu, kabla hajafanikiwa kusema “Haloo..” simu yake ikazimika baada ya kuwa imeishiwa nguvu ya betri! Domi alichanganyikiwa baada ya kushuhudia simu yake ikiishiwa nguvu ya betri na kuzimika wakati ambao simu ya muhimu ilikuwa ikiingia.
Kwa haraka Domi hakujua afanye nini! Aliinuka pale kwenye benchi na kusimama wima.
“Vipi braza?” Yule mng’arisha viatu aliuliza.
“Simu yangu kaka!” Domi alijibu na kumuacha yule mng’arisha viatu njia panda kwa kutoa kauli inayoelea, ikabidi aulize tena, “Simu yako imekuwaje kaka?”
“Imeishiwa chaji wakati simu ya muhimu ilikuwa inaingia.”
“Oh… pole sana braza, kama simu yenyewe ni ya muhimu sana kama unavyosema, weka kadi ya simu yako kwenye simu yangu ili ufanye mawasiliano braza.” Alisema yule mng’arisha viatu huku akimpatia Domi simu ili abadilishe kadi ya simu aweze kufanya mawasiliano.
Domi hakujua ashukuru vipi kwa msaada huo! Aliipokea ile simu na kubadiri kadi ya simu kutoka kwenye simu yake kwenda kwenye simu ya mng’arisha viatu.
Wakati ambao Domi alikuwa akibadiri kadi ya simu, akili yake ilikuwa ikikabiliana na wakati mgumu sana. Alijua wazi kuwa simu yake haikuwa na pesa za kutosha kupiga simu! Nini kupiga? Simu yake haikuwa hata na pesa ya kushtua ili apigiwe, na mfukoni hakuwa na hata senti ambayo angeweza kuitumia kununua salio na kupiga simu. Hivyo wakati anafanya mabadiriko hayo, moyoni alikuwa kiomba yule mpigaji apige tena kwa mara nyingine ili aweze kuwasiliana nae.
Mungu si Athumani, kwani mara tu baada ya simu kuwaka, ile namba iliyompigia awali ikawa inapiga tena. Domi akashukuru kwa Mungu wake, akabonyeza kitufe cha kijani ili kuruhusu mawasiliano, “Haloo.. habari za leo?” sauti kutoka upande wa pili ilisikika.
“Salama, habari yako?” Domi alijibu ile salamu na kusalimiana na yule mtu wa upande wa pili ambaye pia alijbu na kuuliza swali, “Samahani ndugu…naongea na Dominic Masaka?”
“Bila shaka, ni mimi hapa ninaeongea” Alijibu Domi kwa utulivu wa hali ya juu kabisa.
“Sawa.. napiga simu kutoka KWITALE ADVOCATES & COMPANY, unaombwa kufika hapa kwenye ofisi zetu zilizoko hapa mitaa ya Posta kwenye jengo la ATC kuanzia saa 7:00 mchana, mpaka saa 9:30(saa tisa na nusu alasiri) na kama hutofanikiwa kufika leo, kampuni inakukaribisha tena kesho kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 9:30 alasiri.”
“Ahsante sana mkuu nimekuelewa” Domi alijibu.
“Ahsante kwa kunielewa, nakutakia mchana mwema.” Ile sauti ya upande wa pili ilihitimisha na kukata simu.
Maelezo yaliyotolewa kwenye simu yalifufua matumaini kwa Dominic, hakujua tena amshukuru vipi yule mngarisha viatu aliyempa simu yake afanyie mawasiliano.
Wakati huo saa yake ya mkononi ilisema ni saa 6:30 mchana. Kwa kuwa muda ulikuwa unaruhusu Domi hakuona sababu ya kusubiri mpaka kesho, wakati hakuna kinachomzuia kwenda leo.
Domi akageuka na kuliangalia lile jengo la ATC ambalo alikaa kwenye benchi kwa kulipa mgongo, kisha akaanza kurekebisha mavazi yake mwilini kwa kulichomeka vizuri shati lake ndani ya suruali, halafu akachukua brashi ya viatu na kuanza kufuta vumbi lilotapakaa kwenye viatu vyake. Na mara baada ya kumaliza alimrudishia yule mng’arisha viatu simu yake huku akishukuru kwa kumwambia, “Ahsante braza, ubarikiwe sana..”
Wakati Domi anaaga kuondoka yule mngarisha viatu akamwambia, “Kila la kheri kaka” Domi akampungia mkono na kuondoka kuelekea kwenye geti lililokuwa hatua chache kutoka alipokuwa huku moyo wake ukimdunda.
****
Sauti ya redio iliendelea kusikika na kukienea chumba kizima! Wimbo uliokuwa ukisikika kutoka kwenye spika za redio ulimfanya Doi atokwe na machozi.
Akiwa ameketi kitandani, mkononi ameshikilia kalamu, na karatasi ikiwa mapajani mwake Doi aliendelea kuandika licha ya machozi yaliyoendelea kumbubujika.
Baada ya kumaliza kuandika Doi aliipitia tena ile barua yake kwa umakini wa hali ya juu, ilhali machozi yakiendelea kusheheni mashavuni mwake. Aliisoma tena na tena huku wimbo wa ‘barua’ ulioimbwa na kikundi cha muziki wa kizazi kipya cha ‘Daz Nundaz’ ukimalizikia katika spika za redio yake.
Kila aliporudia kuisoma barua yake, Doi alishindwa kabisa kuyatofautisha maudhui ya wimbo ule na kile alichokuwa akikifanya kwa wakati huo!
Baada ya kujiridhisha, aliikunja ile barua na kuiweka chini ya mto mahali ambapo alijua fika kuwa ni lazima Domi ataiona. Mara baada ya kufanya hivyo Doi aligeuka nyuma akiwa chumbani mule, na hapo ndipo alipoiona picha waliyopiga na Domi ikiwa ukutani. Ni wazi kuwa picha ile ilikuwa kama inamsuta kwa kile anachokifanya!
Doi akapiga moyo konde na kuishika simu yake ya mkononi, alipotupia macho kwenye kioo cha simu hiyo kwa lengo la kujua muda, Doi alibaini kuwa muda ulikuwa ukielekea ukingoni. Akauendea mkoba wake na kutoa bulungutu la noti la dola za kimarekani na kuliweka pale chini ya mto sambamba na ile barua kisha akaichukua picha ya Domi ambayo aliipiga siku ya mahafali yake ya kuhitimu shahada yake ya kwanza, picha ambayo huwekwa kwenye meza iliyoko chumbani mule. Kwenye ile picha Domi alionekana akiwa mwenye furaha kupindukia kwa sababu ya tabasamu mwanana alilokuwa nalo kwenye picha ile.
Doi aliishika ile picha kwa mapenzi mazito, kisha wazi wazi akaia nafsi yake ikimsuta! Machozi yakaongezeka zaidi, akaibusu ile picha na kuitazama tena kwa mara nyingine kisha akairudisha pale ilipokuwa awali. Akaufungua mkoba wake na kutoa leso kwa ajili ya kufutia machozi yaliyoenea mashavuni mwake.
Doi akatoka nje na kuufunga mlango akiwa na mkoba wake begani. Akaanza kupiga hatua za kuondoka, hatua chache kutoka mlangoni Doi aligeuka nyuma na kuutizama tena ule mlango akiwa hana uhakika kama atauona tena kwa siku za karibuni. Doi akageuka na kuendelea na safari yake wakati huo saa ya kwenye simu yake ilionesha saa 6:56 mchana.
****
Gari aina ya marcedes Benzi yenye rangi nyeusi ilikuwa imeegeshwa kando ya barabara ya vumbi, huku muziki mkubwa ukisikika kutoka ndani yake. Damian aliyekuwa ndani ya gari hiyo aliinua mkono wake na kuitazama saa yake ya mkononi, alifanya hivyo mara kadhaa huku akionesha hali ya kuanza kuingiwa na wasiwasi.
Damiana alipunguza sauti ya redio na kubonyeza bonyeza simu yake kisha akaiweka sikioni, “Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa, tafadhali… jaribu tena baadaye.” hiyo ilikuwa ni sauti iliyosikika kutoka kwenye spika ya simu yake, sauti ambayo ilizidi kumchanganya kabisa Damian! Akaiona simu hiyo kuwa haina tena msaada kwake, akaitupa kwenye kiti cha abiria kilichokuwa kushoto kwake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Damian akaitazama tena saa yake katika hali ya kuhamanika zaidi!
Kupitia kwenye kioo cha pembeni cha gari, kioo cha mkono wake wa kulia, Damian aliona kitu a
mbacho kiliuteka umakini wake! Akayagandisha macho yake kwenye kile kioo na mara pole pole akaanza kuruhusu tabasamu lichukue nafasi usoni pake!
Ni wazi kuwa Damian alikiona kile alichokua akikisubiri kwa muda wote! Alikuwa ni msichana mrefu kiasi, mwenye wembamba wa kawaida, akiwa amevaa miwani myeusi, sambamba na gauni refu lililoyasitiri sawia maungo yake. kifua chake hakikuwa kikubwa sana, kilikuwa ni cha wastani. Kiufupi ni kwamba umbo la mwanamke huyo lilifutuka kwenye mapaja yake kuelekea pembeni kila upande na kumfanya afanane na ile namba iliyo katikati ya saba na tisa, yaani namba nane. Muonekano wake huo ulimfanya aonekane mrembo kupindukia na kuwa kivutio kwa wenye macho yanayoona!
Damian alikuwa akiitambua tabu inayoachwa nyuma na mrembo yule kwa kila aliyemtazama baada ya kuwa amemuachia mgongo. Kwani makalio yake yalikuwa yametuna mithili ya kichuguu. Hili Damian alilijua fika!
Mrembo yule alizidi kusogea kule ilipo gari ambayo Damian alikuwa ndani yake. Tabasam la Damian likazidi kujipambanua zaidi! Na punde si punde mrembo yule akafika! Damian akamfungulia mlango yule mrembo akaingia garini.
“Pole kwa kukuweka, kuna mambo kidogo yalinichukulia muda ndiyo maana nimechelewa. Halikuwa lengo langu..” alijaribu kujitetea yule msichana
“Usijali mpenzi hujachelewa sana” Damian alisema huku akimkumbatia yule mrembo na kuyakatisha maneno yake kwa mabusu motomoto, kisha akasema “Doi mpenzi…..” Damian alisita kidogo huku akimuangalia Doi usoni bila ya kujua aongee nini! Mara ghafla sauti ikamtoka Damian, “Nakupenda Doi..” Damian hakutaka kusubiri jibu kutoka kwa Doi. Aliitekenya gari ambayo nayo ilicheka bila ubishi, akamgeukia Doi akamtizama bila kusema neno kisha akajiweka sawia na kutazama mbele. Polepole akaanza kuipeleka gari ilipo barabara ya lami!
Walipofika kwenye barabara ya Lami, Damian akaipa gari mwendo wakatokomea kuelekea mjini, wakitokea Yombo Buza maeneo ya kiwanja cha Tanesco. Wakati huo ikiwa ni saa 7:12 mchana.
***
Saa 7:00 mchana Dominic alikuwa akimalizia kupanda ngazi za jengo la ATC, jengo ambalo ndani yake kulikuwa na ofisi za kampuni ya mawakili ya KWITALE ADVOCATES & COMPANY.
Dominic aliongoza moja kwa moja mpaka mapokezi ambako alimkuta dada wa mapokezi. Yule dada wa mapokezi alimchangamkia sana Dominic!
Baada ya salamu Dominic alijitambulisha, “Samahani dada, mimi naitwa Bwana Dominic Masaka ni…” kabla hajamaliza kauli yake yule dada alidakia akamkatisha kwa kusema, “Ninakukumbuka vizuri sana Bwana Masaka, huna haja ya kujitambulisha, nilikuona hapa siku ile mlipokuja kwenye ya usaili.”
“Ok…. Vizuri sana dada, niko hapa kwa…..”
“Kwa ajili ya kumuona Bwana Makeke” Yule dada alidakia tena na kumuacha hoi Dominic!
Yule dada wa mapokezi alionekana kuwa ni muongeaji sana, na hata kazi yake ya mapokezi ilionekana kumfaa haswa!
“Nenda moja kwa moja mpaka ofisi ya katibu, tayari ana taarifa zako.” Alisema yule dada huku akimuonesha Domi ofisi ya katibu ilipo.
Wakati Domi anaondoka kuelekea ofisi ya katibu, aliisikia sauti ya yule dada akimuita, “Mr Dominic…” Domi akasimama ili kumsikiliza. “My name is Neema” alisema yule dada huku akiachia tabasamu murua!
Dominic aliitikia kwa kichwa huku akiwa na yeye anatabasam, kisha akampungia mkono kuashiria kuwa amemuelewa.
Dominic alienda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya katibu, alipofika walisalimiana na baadaye Dominic alielekezwa kukaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza kubwa ya kiofisi iliyokuwa ofisini mule.
“Mimi naitwa Mr Makeke Cosmas, ndiye katibu wa KWITALE ADVOCATES & COMPANY sijui mwenzangu unaitwa nani?” alisema Makeke ambaye kwa muonekano alikuwa ni mtu wa makamo, ambaye umri wake ni kati ya miaka thelasini na saba mpaka arobaini hivi. Alikuwa amevaa suti nadhifu nyeusi sambamba na tai nyekundu kifuani pake. Alikata nywele zake kwa mtindo wa low cut na kuzifanya zionekane fupi na zenye mvuto.
“Mimi naitwa Dominic Masaka, muda mfupi uliopita nilipigiwa simu kuwa ninahitajika hapa ofisini”
“Ok, vizuri sana. Nashukuru kukufahamu Bwana Masaka, karibu sana KWITALE.” Alisema Makeke huku akifunua baadhi ya mafaili yaliyokuwa mezani kwake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ahsante sana Bwana Makeke” Alijibu Dominic.
Baada ya muda mfupi, bwana Makeke alikuwa ameshikilia faili moja mkononi mwake, likiwa limeandikwa ‘Dominic Masaka’ akasimama na kumwambia Dominic amfuate.
Dominic alitii, wakatoka pale na kuingia ndani zaidi ambako walimkuta mtu mwingine.
Ndani ya ofisi walimoingia mlikuwa na vitabu vingi vilivyopangwa kwenye ngazi kwa utaratibu maalum uliovifanya vivutie zaidi.
“Habari za saizi tena bwana Kwitale” Makeke alisalimia na kufanya utambulisho mfupi, “Ninayo furaha kubwa kumtambulisha kwako ndugu Dominic Masaka, na bwana Masaka, huyu ndiye bwana Kwitale mkurugenzi mtendaji wa hii kampuni yetu ya KWITALE ADVOCATES & COMPANY.” Alisema Makeke huku akiwaangalia wote Masaka na Kwitale kwa zamu kila mmoja.
Walipeana mikono na bwana Kwitale akamkaribisha Dominic, “Karibu sana ndugu Dominic, jisikie huru kuwa ndani ya KWITALE ADVOCATES & COMPANY.”
“Ahsante sana bwana Kwitale” Alijibu Dominic kwa utulivu na uwekevu wa hali ya juu.
Makeke na Dominic walikaa kwenye viti vilivyokuwa mbele ya meza kubwa ya kiofisi iliyowatenganisha na bwana Kwitale.
“Bwana Dominic Masaka!” bwana Kwitale ambaye alionekana kuwa amekula chumvi si haba alimuita Dominic kwa ukamilifu wa jina lake.
“Naam, bwana Kwitale.” Dominic aliyekuwa ametulia kimya na kwa umakini aliitika na bwana Kwitale akaendelea, “Tumepitia taarifa zako na tumeridhika nazo, na tukaona ni vema kama tutakuajiri ili uzibe pengo la wakili mmoja ambalo limekuwa wazi kwa muda mrefu. Hivyo nitakuomba uupitie mkataba wetu na kama utaridhika nao uanze kazi mara moja.” Taarifa hii ilipotua masikioni mwa Dominic ilimshtua na kuyabadili mapigo yake ya moyo. Dominic alikuwa kama asiyeamini kile alichokisikia muda mfupi uliopita, akajiona mwenye bahati kwani ametafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio! Na leo hii, muda huu anapata taarifa, tena taarifa kutoka kwa mkurugenzi kuwa anahitajika kuziba nafasi iliyo wazi kwa muda mrefu na tayari amepewa mkataba kwa ajili ya kupitia vipengele vya mkataba huo ili kujiridhisha kabla hajamwaga wino na kuwa mtumishi rasmi wa KWITALE ADVOCATES & COMPANY.
Dominic alikuwa akipitisha macho kwenye ule mkataba huku mawazo yake yakiwa kwa Doi mpenzi wake, ambaye wamekuwa naye bega kwa bega katika shida na raha bila kujali umasikini alio nao. Domi aliona kuwa muda wa kumvika Doi taji la ushindi ndiyo huu umefika na furaha iliyokuwa imeugubika moyo wa Domi, hakika sijawahi kuimithilisha!
Dominic akaweka sahihi yake kwenye mkataba ule wa ajira na kuwa mwajiriwa rasmi wa kampuni ya wanasheria ya KWITALE ADVOCATES & COMPANY. Akiwa ameajiriwa kama mwanasheria, taaluma aliyoipenda kuliko zote.
“Eee Mungu ninakushukuru kwa hili kama nilivyokuwa nikikushukuru kwa mengine yote. Naomba Baraka zako na ulinzi wako katika maisha yangu. Amina!” Dominic alikuwa akisali kimya kimya bila kutoa sauti.
Mara baada ya kuwa amemwaga wino kwenye mkataba, Bwana Kwitale alivuta mtoto wa meza na kutoa burungutu la noti za kitanzania zenye thamani ya shilingi laki moja, sambamba na pesa hizo pia Dominic alikabidhiwa hundi ya shilingi milioni mbili, pamoja na funguo za gari. Vitu ambavyo hupewa wafanya kazi wa KWITALE mara tu waajiliwapo ili kuboresha utendaji na ufanisi wao kazini.
“Baada ya wiki moja utapaswa kuhamia kwenye nyumba ambayo kampuni imekupangia. Nakutakia utendaji mwema na unapokuwa KWITALE jisikie uko nyumbani.” Alisema Bwana Kwitale wakati anamkabidhi Dominic vitu hivyo.
Kwa Dominic kila kitu kilikuwa ni kama ndoto! Aliona ameuaga umasikini ghafla mno.
Akawaza sana juu ya kila kinachotokea, alihisi ni kama ndoto na hakutaka kabisa kuishuhudia ndoto hiyo ikiisha na yeye kuurudia umasikini wake uliomtesa kwa muda mrefu!
“Muda wa kutembea kwa miguu kwa kukosa nauli leo umefika kikomo. Mateso ya kushinda na kulala njaa kwa kukosa chakula leo yamefika mwisho. Na ile purukushani na mende kwenye kile kijichumba kibovu leo inahitimishwa, oooh… ahsante Mungu” Dominic aliwaza.
Baadya kukamilisha kila kitu pale ofisni Dominic aliondoka akiwa mwenye furaha sana. Alitamani akifumba macho na kuyafumbua awe tayari ameshafika nyumbani, ili amueleze na kumuonesha kila kitu mpenzi wake.
Dominic aliyetoka nyumbani kwa miguu sasa alikuwa amekumbatia uskani wa gari akiendesha kueleka nyumbani ili kumuwahi mpenzi wake, ambaye alimuacha asubuhi nyumbani bila chakula, zaidi ya unga wa sembe ambao alitakiwa kukoroga uji na kuunywa ili kupunguza makali ya njaa.
Njiani Dominic aliendesha gari kwa kasi, kwa nia na madhumuni ya kuwahi nyumbani na kumpasha mapenzi wake kuwa; matatizo yote yaliyokuwa yakisababishwa na ukosefu wa pesa sasa yametamatishwa, baada ya yeye, yaani Dominic kupata kazi katika kampuni ya mawakili ya KWITALE ADVOCATES & COMPANY.
Punde si punde Dominic alikuwa nyumbani, Domi alishuka kwenye gari kwa haraka akaanza kukimbia kuueleka mlango wa nyumba, huku moyoni akiwaza namna Doi atakavyofurahi baada ya kuwa amempasha juu ya habari hizi njema.
Kinyume na matajio yake Domi alikutana na kufuli kubwa lililokuwa likining’inia mlangoni. Mapigo ya moyo wake yakabadirika ghafla na furaha yake ikatumbukiwa nyongo. Mambo yamekwenda kinyume kabisa na jinsi alivyotarajia!
Dominic alitarajia kumkuta Doi nyumbani kama ilivyo kawaida yake, lakini hakumkuta! “Doi huwa haondoki bila kuaga leo imekuwaje?” Dominic alijiuliza bila kupata majibu. Kwa upole na unyonge wa hali ya juu, aliingiza mkono mfukoni na kutoa funguo, akafungua mlango na kuingia ndani ili kumsubiri mpenzi wake. Alipoingia ndani akaitupia kitandani ile bahasha aliyokuwa nayo mkononi mwake, kisha akaingiza mkono mfukoni na kutoa lile burungutu la noti na kuzitandaza kitandani ili Doi akija, aje azione.
Dominic akakaa kitandani, akaishika ile bahasha aliyoitupia kitanadani na kuitoa ile hundi aliyopewa kazini na baada kufanya hivyo akaitoa nakala ya mkataba wa ajira ambayo alipaswa kubaki nayo kama kumbukumbu yake na yenyewe pia akaiweka kitandani sambamba na ile hundi na pesa taslimu alizo nazo ili mpenzi wake akija avione vizuri.
Domi alijiaminisha kuwa, yawezekana Doi akawa amemsindikiza mgeni, na kama ni hivyo basi atakuwa maeneo ya jirani na asingekawia kurudi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati huo saa ya ukutani ilionesha kuwa ni saa 11:06 jioni, muda mfupi baada ya saa 10:40 muda ambao aliwasili nyumbani hapo, ambapo wanaishi yeye na Doi.
Muda uliyoyoma Domi akimsubiri Doi bila mafanikio. Aliendelea kusubiri huku akipanga kutekeleza mipango yake mingi iliyokwama kwa ukosefu wa pesa ambayo sasa imepatikana. Domi aliwaza kuwatumia pesa wazazi wake ambao wako kijijini Nyamuswa. Aliwaza pia namna ya kutekeleza mipango ya ndoa yake na Doi ili waishi kihalali kama mke na mume. Domi aliyawaza yote haya wakati akimsubiri mpenzi wake ambaye mpaka muda huo alikuwa bado hajarudi.
Licha ya kutokula tangu asubuhi, Domi hakuwa anahisi njaa hata kidogo, na hakuna alichohitaji kwa wakati huo zaidi ya mpenzi wake ambaye alimwacha nyumbani asubuhi.
Muda ulizidi kuyoyoma bila Doi kuonekana! Wasiwasi ukaanza kumwingia Domi, “Amekwenda wapi huyu?” Domi alizidi kujiuliza maswali bila kupata majibu. Domi akasimama kutoka pale kitandani alipokuwa amekaa na kuanza kutembeatembea mule chumbani kama mwehu, mara aende, mara arudi, hatimaye akachoka na kurudi tena pale kitandani alipokuwa amekaa awali akakaa tena, mpaka wakati huu ilikuwa imeshatimu saa 12:37 jioni.
Domi alijiegesha pale kitandani akapitiwa na usingizi bila kujijua. Giza likaenea mule chumbani, na baadaye mbu wakaanza kusikika kwa milio iliyojiunda kwa kuzigonganisha mbawa zao. Mbu wale wenye kiu ya damu walimtafuna Domi akiwa usingizini, na walipozidi kujibidiisha walimwamsha Domi kutoka usingizini. Alipoamka alikuta giza limeenea chumba kizima. Mpaka wakati huo Doi alikuwa hajarejea!
Domi aliwasha taa ya kandiri na mwanga ukashika hatamu mule chumbani.
Wasiwasi ukazidi kumwingia Domi, “Au ameenda nyumbani kwao?” maswali juu ya maswali yalizidi kumpa wakati mgumu.
“Doi ni mtu mzima. Kwa nini afanye jambo la kitoto kama hili?” alikusanya noti zake akaziweka kwenye bahasha ile kubwa pamoja na ile hundi na nakala yake ya mkataba wa ajira.
Wakati huo ilikuwa imeshatimu saa 3:30 usiku kwa mujibu wa saa ya ukutani ambayo iliendelea kuzunguka.
Domi alipoona mbu wanazidisha kero akaamua kushusha chandarua ili kujisitiri dhidi ya mbu wale ambao walikua kero kwake. Kabla hajafanya hivyo alianza kwa kuhamisha vitu vilivyokuwa kitandani ili akung’ute pale juu ya kitanda kwa minajili ya kupunguza vumbi na kuondoa mchanga.
Alianza kwa kutoa shuka iliyokuwa imekunjwa akaiweka juu ya kiti kilichokuwa mule chumbani. Baadaye akaushika mto ili kuutoa auweke pale kwenye kochi alipoiweka shuka. Alipounyanyua mto macho yake yalikutana uso kwa uso na kitu kilichomshitua. Macho ya Domi yalikuwa yakikabiliana na bulungutu la noti za kimarekani, sanjari na kipande cha karatasi kilichokua pembeni ya zile noti. Domi alipigwa na butwaa baada ya kuviona vitu hivyo, akahisi yuko ndotoni lakini akaibishia nafsi yake kwa kujiaminisha kuwa yuko timamu. Moyo wa Domi ukakosa utulivu kifuani mwake kwa kudundadunda kama spika!
Akili ya Domi ilikuwa ikiwaza na kuwazua juu ya kile anachokiona pale kitandani. Wasiwasi ukamzidia tena, akaanza kuhisi anapagawa huku anajiona. Alivitumbulia macho vitu vilivyokuwa pale kitandani kwa muda wa dakika zipatazo kama tano hivi, uvumilivu ukamshinda, akanyoosha mkono wake wa kuume na kulishika lile bulungutu la dola za kimarekani, akalisaili kwa muda halafu akakili kuwa yuko sahihi, kuwa; anachokiona ni bulungutu la dola za kimarekani. Akalihamishia lile bulungutu mkono wake wa kushoto ili ule wa kuume autumie kuchukua ile karatasi ambayo imekunjwa na kuonekana kama kipande. Domi akaichukua ile karatasi kisha polepole akaikunjua na kuanza kuisoma.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati anaisoma ile barua, Domi alihisi kurukwa na akili. Mapigo ya moyo wake yaliongezeka zaidi na miguu ikaanza kumtetemeka, alikosa kabisa uvumilivu akakaa kitandani huku mtiririko wa machozi ukiyapamba mashavu yake. Ilisikitisha sana!
Domi mtoto wa kiume alikua analia! Maumivu aliyoyapata moyoni yalitosha kumfanya atokwe na machozi kwa kile kilichoandikwa kwenye ile barua ambayo ilikuwa mikononi mwake akiisoma.
******
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment