Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KUTI KAVU - 4

 









    Simulizi : Kuti Kavu

    Sehemu Ya Nne (4)





    Ikawa hivyo, mama Domi alijiweka sawa pale kitini alipokaa kisha akasema, “Kama amebahtaisha kamfupa hilo ni jambo la kheri sana, na nimefurahi sana kusikia hivyo. Lakini hili la kwenda sisi wote mpaka Dar es salaam limekuwa la ghafla mno!”

    “Kwa nini unasema ni ghafla mama?” Tina mdogo wake na Domi alirukia.

    “Hah… hapo unakosea Tina, mwache mama yako azungumze kisha nawe utazungumza. Yawezekana majibu ya swali lako yalikuwa kwenye maelezo yanayofuata,” Alisema mzee Masaka na kuungwa mkono na mkewe, “Ni kweli Tina mwanangu, una haraka gani?” Alisema mama Domi halafu akaendelea, “…nasema ni ghfla kwa sababu, hiyo ajira aliyoipata Domi… ameipata hivi karibuni. Si ndiyo? Mama Domi aliwatupia swali na kisha kuwaangalia usoni pao kwa zamu. Wote kwa pamoja, yaani Mzee Masaka na bintiye wakajibu, “Ndiyo”
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Basi kama ndivyo, ni wazi kuwa bado anahitaji muda zaidi wa kujipanga”

    “Kweli kabisa” Mzee Masaka aliunga mkono maelezo ya mkewe huku Tina akiwa ametulia kimya akifuatilia kwa makini.

    “Mi naona ni bora mmoja wetu akatuwakilisha huko mjini ili tumpe muda zaidi wa kujipanga… ili siku moja atupokee wote huko mjini”Alimaliza mama Domi.



    Maelezo ya mama Domi yalionekana kuwaingia wote na wakakubaliana na mawazo yake .

    Walijadiliana ni nani aende, mwisho wote wakakubaliana aende mzee Masaka.



    ***

    Mudi aliendelea kulifuatilia lile gari alilopanda Zai mpaka ameneo ya kona ya Kigogo Fresh ambapo mara baada ya gari kufika Zai alishuka.

    Baada ya Zai kuwa ameshuka, gari lile likaendelea na safari.



    Mudi alikuwa amesimama mita kadhaa nyuma kabla ya ya eneo kilipo kituo. Hivyo kutokea pale alipo aliweza kumuona Zai wakati anashuka kutoka kwenye lile gari na kuvuka barabara.



    Mudi naye alivuka, kwa umakini wa hali ya juu kabisa akaendelea kumfuatilia Zai bila yeye kujua.



    Mara baada ya kuvuka barabar Zai alishika njia ndogo iliyokuwa ikiongoza kuelekea yalipo makazi ya watu. Alivuka mtaa wa kwanza, wa pili kisha akapinda kushoto ambako aliongoza moja kwa moja kwenye nyumba ndogo ambayo ilikuwa haijaisha sawasawa.



    ****

    Mapunda kijana mwenye urefu wa wastani, alikuwa akitoka bafuni. Mkononi alikuwa ameshikilia ndoo ambayo bila shaka ilikuwa ni ya kuogea. Mwilini mwake alikuwa amejisitiri kipande cha suruali ambacho kiliishia magotini.



    Mapunda alijongea taratibu mpaka kwenye msingi wa nyumba katika upande ambao haukuwa na tofali hata moja, isipokuwa msingi ambao Mapunda aliiweka ndoo yake ya kuogea.



    Mapunda alikuwa akiishi kwenye nyumba hiyo, nyumba ambayo alikuwa akiishi kama mlinzi kwa sababu mwenyewe alikuwa mbali na alitaka ahamie hapo baada ya nyumba yake hiyo kuwa imekamilika, hivyo alimuweka Mapunda kwa shughuli mahsusi ya kusimamia mafundi na pia kulinda vifaa vingine vya ujenzi ambavyo vilikuwa hapo hapo kwenye chumba cha pembeni.



    Akiwa anaweka ndoo yake pale kwenye msingi, Mapunda alimuona mgeni wake akija kwa madaha huku akisukumwa na upepo mwanana wa kadiri, upepo ambao uliiwahisha harufu nzuri ya uturi aliojipulizia Zai mpaka kwenye pua zake.



    Baada ya kumuona mgeni wake, Mapunda alitabasamu na Zai naye akajibu mapigo.

    Zai alipiga hatua na hatimaye akawa amefika mpaka alipokuwa Mapunda, wakakumbatiana na kubusiana huku nyuso zao zikiwa zimeshamiri furaha isiyo kifani.

    “Vipi mpenzi,?” Mapunda alisalimia huku akizungusha mkono wake kwenye kiuno cha Zai na kumkokota kuelekea ndani.

    “Safi tu, za hapa?” Zai alijibu wakati anapiga hatua sambamba na Mapunda kuelekea ndani.



    ****

    Baada ya kupinda mtaa wa kwanza , njia ikaanza kuwa finyu na mbovu kiasi cha kutoruhusu pikipiki kupita. Kwa tabu Mudi aliikokota pikpiki yake lakini hakufanikiwa, pikipiki ikagoma kabisa kupita kwenye njia ile finyu na mbovu.



    Mudi alipoona njia inaleta usumbufu, aliizima pikipiki akaiegesha pembeni kwenye upenu wa nyumba. Akaanza kumfuatilia Zai kwa miguu huku kichwa chake kikiendelea kukingwa na ile helmet ili asiweze ktambulika.



    Mudi alijibanza nyuma ya mnazi na kumshuhudia Zai akikumbatiwa, na baadaye kukokotwa kwa kushikwa kiuno kuelekea ndani.

    ‘Ahaa…. Kumbe, hivi kuna kitu gani huyu zai amekikosa kutoka kwangu? Simridhishi kwa lipi, Fedha, mapenzi au kitu gani? Huyu mwana izaya huyu…. Dah.. ngoja,” Alijisemea Mudi wakati akiwashuhudia wezi wake wakiingia ndani.



    Mudi alitembea kwa kunyata mpaka kwenye ile nyumba, akazunguka kwa nyuma mpaka lilipo dirisha akatega sikio.

    Kabla hajasikia lolote Mudi aliamua kujivuta nyuma kwa umakini zaidi ili asiweze kusikika na walio ndani, “Kwani nahitaji kusikia nini tena?” Mudi aliwaza.

    “Haya niliyoyaona yanatosha kunithibitishia kuwa ninasalitiwa. Huyu mpuuzi huyu…. Leo ndiyo amelikalia kuti kavu” Mudi alijisemea wakati anaondoka kutoka pale alipokuwa kwa mtindo wa kunyata, kuelekea kule ulipo mlango wa ile nyumba ambayo wamo wezi wake.

    Mudi alifika mpaka mlangoni pale akiwa mwenye hasira na mawazo tele. “Nifanye fujo?.... aah hapana haina haja” Mudi aliuegemea ukuta wa ile nyumba kimgongomgongo huku akiomba busara itawale maamuzi yake. Aliugeukia tena ule mlango akaugonga, “Ngo…ngo ngoo…”

    “Nani?” Sauti ya kiume kutoka ndani ilisikika ikihoji.

    “Mimi Jafari fungua,” Mudi aliamua kubuni jina akiamini kuwa; ni kawaida, kuwa unapobisha hodi popote pale, na ukaulizwa wewe ni nani, unataja tu jina lolote na mlango utafunguliwa.





    Ikawa ni kama vile alijua. Mlango ulifunguliwa na Mapunda akatoka nje akiwa amelowa jasho. Mapunda alimtazama Mudi huku akijaribu kuvuta kumbukumbu ni wapi amewahi kumuona, lakini hakufanikiwa kukumbuka ni wapi aliwahi kumuona.

    “Oya vipi?” Mapunda aliuliza.

    Mudi alikaa kimya kidogo halafu akanyanyua midomo yake, “Oya mshikaji sikiliza,”

    Mapunda akajiweka vizuri huku akiitazama sura ya Mudi kwa umakini, sura iliyojaa ujasiri na jazba. Wasiwasi ukamwingia Mapunda na mapigo ya moyo yakambadilika ghafla!

    “Sisi wote hapa ni wanaume unasikia man…. Huyo uliye nae ndani ni mke wangu. Hatujafunga nae ndoa lakini nimeishi nae kwa muda mrefu sana. Kwao wananijua na kwetu wanamjua” Mudi alisema na kumsababisha Mapunda aingiwe na hofu kwa kukutwa na mke wa mtu. Kwa woga akauliza, “Huyu Asha ni mkeo?” Mapunda aliuliza kwa mshangao.

    “Haitwi Asha, jina lake ni Zai… Zainabu Mpotoshi. Hapa sikuja kufanya fujo, nakuachia huyo mke simtaki tena…. Ila nakuomba umuite aje … aje ahakikishe kuwa ni mimi na nimezijua nyendo zake” Alimaliza Mudi kisha akajivuta hatua moja nyuma kama vile anajiandaa kufanya chochote.

    Maneno ya Mudi yalimchanganya Mapunda kiasi cha kuifanya akili yake ichoke ghafla, bila kutarajia chuki ikamjia Mapunda dhidi ya Zai aliyekuwa ndani akitetemeka kwa woga.

    Akauachia mlango aliokuwa ameushikilia kuuzuia ili usifunguke wote kwa lengo la kusitiri yaliyomo ndani, alipouachia mlango ulifunguka wote ukawa wazi kama goli na kuacha pazia lililokuwa likining’inia kuyasitiri ya ndani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Karibu ndani kaka… ingia uje tuzungumze” Maneno yalimtoka Mpunda.

    “Hapana kaka… hapa panatosha, muite tu huyo Malaya aje anione niondoke.

    Mapunda aligeuzia shingo yake kule ndani akamuita Zai, “Oya.. hebu simama ue hapa”



    ****

    Wakati Mudi anaanza kuongea Zai, aliitambua fika sauti yake, na maneno yote aliyoyaongea Mudi aliyasikia barabara. Hofu ikamwingia, ubaridi ukamwingia na malaika yakamsimama mwilini na kufanya vipele vidogovidogo vya baridi vionekane juu ya ngozi yake.

    Zai akajiona amelikalia kuti kavu, akajiona hana jinsi katika maisha, Zai hakujua nini kitafuata baaada ya hapo.

    Zai alimdanganya Mapunda kuwa hajolewa na anaishi kwao na wazazi wake, hiyo bado haitoshi.. alimdanganya kuwa anaitwa Asha kumbe jina lake ni Zai.

    Akiwa kwenye lindi la mawazo, Zai aligutuliwa na sauti ya Mapunda ikimuita, “Oyaa… hebu simama uje hapa”

    Zai alipoinyanyua shingo yake aliyokuwa ameiinamisha chini kwa aibu, alimuona Mudi akiwa nje amesimama huku mikono yake akiwa ameifumbata kifuani.

    Zai alihisi kama mkojo unamtoka, akiwa bado anajishauri cha kufanya, Mapunda alimfuata pale kitandani na kumvutia mlangoni!

    Pale mlangoni Zai alisimama akiwa na khanga yake moja tu, iliyokuwa imemfunika kuanzia kifuani mpaka magotini. Zai alihisi kupatwa na aibu.. aibu ya karne, machozi yakamtoka na kuyaharibu mashavu yake mazuri ambayo kwa wakati huo yalikuwa yamepoteza mvuto kwa sababu ya michilizi machozi.

    Zai alitamani akimbie lakini hakuweza, mkono wake mmoja ulikuwa umeshikiliwa na Mapunda, hivyo asingeweza kuchoropoka… na mbele yake alikuwepo Mudi hivyo asingeweza kufika mbali kabla hajakamatwa endapo angejaribu kufanya upuuzi wa kutaka kukimbia.

    Akabaki ameganda kama nyamafu asijue la kufanya!

    “Oya braza demu mwenyewe si ndiye huyu?”

    “Ndiye huyo huyo, Zai…. Zainabu Mpotoshi, mwanamke niliyempenda nikampa kila kitu” Mudi alisema huku akiwa amesonta kidole kuelekea pale mlangoni waliposimama Zai na Mapunda.

    “Yaani hawa wanawake bwana…. mi angeniambia kuwa ni mke wa mtu wala nisingehangaika naye… ona sasa! Powa kaka, yaani akitoka hapa ndiyo mwisho wa mimi na yeye sitaki tena kumuona” Mapunda alisema na maneno yake yalisikika sawia masikioni mwa Zai aliyekuwa pembeni yake. Maneno yale yalimchoma moyo kiasi cha kumfanya aangue kilio cha sauti. Akajiona kama mjinga na mpumbavu wa mwisho chini ya jua, akaliona kuti kavu alilolikalia likidondoka na yeye akiwa juu yake. Alilia sana.

    Mudi aliiweka helmet yake ubavuni, kisha akachapa mwendo.



    *****

    SIKU ya Jumapili Domi aliamka asubuhi, aliamka asubuhi na mapema akafaya maandalizi yake kisha akaelekea kanisani. Siku hiyo alipanga kusali misa ya kwanza ambayo huanza saa 12:30 asubuhi. Alipanga hivyo kwa lengo la kurudi mapema nyumbani ili ajiandae na kazi za kesho ofisini kwao.

    Baada ya ibada Domi aliwasha gari kurejea nyumbani, kabla hajafika nyumbani alipita kwa muuza magazeti kwa lengo la kununua magazeti ili pindi awapo nyumbani ayasome ili kujua yaliyojiri duniani, ilikuwa ni kawaida yake kutopitwa na gazeti. Alipofika tu pale kwa muuza magazeti, yule muuza magazeti alichukua magazeti manne akampelekea kwenye gari, Domi aliyapokea na kuyatupia magazeti yale kwenye kiti cha abira kilichokua pembeni yake. Akatoa pesa akampa yule muuza magazeti akaondoka.

    Domi alifika nyumabani kwake, akaingia ndani, akajitupa kwenye kochi na kuanza kuyapitia magazeti yake moja baada ya jingine.

    Aliposhika gazeti la kwanza, Domi alibaki mdomo wazi baada ya kukutana na kichwa cha habari kilichoandikwa; “MREMBO AKAMATWA NA KILO 6 ZA COCAIN UWANJA WA NDEGE” Domi alizidi kupagawa baada ya kuiona picha ya msichana anayedaiwa kukutwa na madawa hayo hatari ya kulevya ikiwa imeipamba habari. Alipoitazama picha ile kwa makini alibaini kuwa picha ile ilikuwa ni ya Doi, “Ooowh nooo… hapana!” Domi alimaka kwa mshangao.

    Akalitupa gazeti lile pembeni akachukua jingine. Gazeti alilolichukua pia lilikuwa na habari kama ile aliyokutana nayo kwenye gazeti la kwanza, kichwa cha habri kwenye gazeti hili kiliandikwa, “MREMBO AKALIA KUTI KAVU, AKUTWA NA MADAWA YA KULEVYA UWANJA WA NDEGE” kama gazeti la kwanza, hili pia lilikuwa na picha ileile ambayo Domi alijiaminisha kuwa ni ya Doi.

    Akalitupa na hili kando, akashika jingine ambalo pia lilikuwa na kichwa cha habari kisemacho, “MADAWA YA KULEVYA TISHIO, MREMBO MWINGINE AKAMATWA” Domi hakuchoka, akiwa kwenye taharuki alichukua tena gazeti jingine ambalo lilizidi kumtisha zaidi kwa kichwa chake na picha zilizopamba ukurasa wa mbele gazeti lile, lilikuwa na kichwa kisemacho, “MREMBO MATATANI KWA KUSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA” Domi alipoitazama picha iliyopamba habari hiyo alizidi kuthibitisha kuwa ile picha ni ya Doi, Domi alipagawa!

    Ikabidi aanze kuisoma habari yenyewe, na sehemu ya habri hiyo ilisomeka hivi; “……mrembo huyo aliyefahamika kwa jina la Doi Vioja, mwenye umri wa miaka 26 kwa mujibu wa pasi yake ya kusafiria, alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere akiwa na kiasi hicho cha madawa hatari ya kulevya akiyasafirisha kuelekea nchini Ufaransa.

    Taarifa zaidi zinadai kuwa; kuna wimbi kubwa la wasichana wanaotumiwa kusafirisha madawa haya na mengine kwa kuyaingiza ama kuyatoa nchini Tanzania kuelekea nchi za nje.

    Kukamatwa kwa Doi Vioja kumetokana na maboresho ya kiutendaji yaliyofanywa na waziri wa wizara ya usafirishaji na uchukuzi kwa kuwafukuza kazi na kuwabadirisha wengine kutoka idara moja hadi nyingine baada ya mrembo mwingine wa Tanzania kukamatwa katika uwanja wa ndege wa Afrika kusini akiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya aina crystal methamphetamine au maarufu kama blue stones….http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mkuu wa kitengo cha kupambana na kudhibiti madawa ya kulevya katika jeshi la polisi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na amesema kuwa, Doi Vioja amepelekwa mahabusu kusubiri apelekwa mahakani mara baada ya uchunguzi kukamilika….” Domi alichanganyikiwa kabisa na hakujua afanye nini kwa wakati huo. Alisimama kutoka pale kwenye kochi alipokuwa amekaa na kuanza kuzungukazunguka mule sebuleni kama mwendawazimu.

    “Oowh.. noo… it can’t be” Sauti ilimtoka Domi. Akarudi pale mezani yalipo magazeti akaichukua simu yake ya mkononi, akaibonyezabonyeza baadhi ya vitufe katika simu ile kisha akaiweka sikioni, “..namba unayopiga kwa sasa haipatikani….” Sauti kutoka upande wa pili wa simu ikajibu na kuzidi kumuweka Domi kwenye wakati mgumu.

    Akaitupa simu kwenye kochi kisha akawasha luninga iliyokuwa pale sebuleni.

    “….msichana huyo aliyefahamika kwa jina la Doi Vioja, ambaye ni raia wa Tanzania amepelekwa mahabusu kusubiri uchunguzi utakapokamilika ili afikishwe mahakamani kusomewa mashitaka yanayomkabili…” Sauti ya mtangazaji wa kituo cha luninga iliendelea kutangaza huku picha ya Doi ikionekana bayana kwenye kioo cha luninga.

    Domi alijibwaga kivivu kwenye kochi huku maneno yakimtoka, “Ooh… Doi kwa nini… kwa nini lakini?” sauti ilimtoka sambamba na machozi yaliyokuwa yakimchuruzika kwenye mashavu yake.

    “Ina maana.. umeamua kuniacha ili ukafanye biashara haramu na ya kishenzi… yaani wewe uliyekuwa mstari wa mbele kupinga matumizi ya madawa ya kulevya leo umekamatwa na madawa hayo… kilo sita…kilo sita” Domi alizidi kuwaza.

    Domi hakutaka kabisa kusadiki kuwa Doi anaweza kukutwa na madawa ya kulevya. Lakini alipojaribu kulihusisha tukio hilo na zile dola za marekani, Domi alipata tena mkanganyiko.

    “Huyu amerubuniwa huyu …. Hii siyo akili yake… siyo akili yake kabisa ina maana hizi dola ni matokeo ya hii biashara?” akiwa mawazoni, Domi alishituliwa na mlio wa simu yake ya kiganjani iliyokuwa kwenye kochi, “Ngriii…ngriii…” Domi akaipokea simu na kuiweka sikioni, “Hallow baba shikamoo” Saut ilimtoka Domi.

    Bila hata kujibu salamu, sauti ya upande wa pili ilionesha dhahiri kuwa ilikuwa imetwaliwa na hofu, wasiwasi na mashaka tele ikajibu kwa swali, “Una taarifa gani kuhusiana na mwanangu?”

    “Mzee taarifa nilizo nazo kuhusiana na Doi si nzuri,,, magazeti yote ya leo yameandika kuhusu yeye, nimefungua pia luninga habari ni kuhusiana na yeye…Doi amekamatwa na madawa ya kulevya mzee,” Alisema Domi.

    “Ina maana hukuwa na taarifa zozote kuhusiana na safari yake?” Sauti ya upande wa pili ilizidi kuhoji.

    “Kusema ukweli baba mimi sikuwa na taarifa zozote kuhusiana na Doi kwa zaidi ya wiki tatu sasa” Domi alijibu, na safari hii alijibu kwa utulivu zaidi.

    “Yaani huyu mtoto huyu…. Sasa ameleta tabu gani hii,” alisema mzee Vioja na kukata simu “Hallow hallow…” Domi aliita bila mafanikio.

    Aliendelea kushikilia simu yake mkononi, aliitazama kama vile anaiuliza kitu kisha akabonyeza vitufe kadhaa kwenye ile simu kabla hajaiweka sikioni, “Hallow bwana Makeke….aliuliza Dominic na sauti ya upande wa pili ikajibu “Ndiyo bwana Masaka…. habari za weekend?”

    “Za weekend sio njema hata kidogo bwana Makeke…. kuna tatizo… tena tatizo kubwa sana…..” Domi akaweka pumziko kidogo ili ameze walau funda la mate. Wakati anaweka tu pumziko bwana Makeke akamuwahi kwa kuuliza “ Kuna tatizo gani tena ndugu yangu?”

    Dominic akajibu, “Sikuwa nimewahi kukueleza juu ya hili swala ….. ila kwa ufupi nikupe tu dokezo” “Ndiyo bwana Masaka endelea…”

    “Nadhani umeipata taarifa kuhusiana na huyu binti aliyekamatwa uwanja wa ndege akiwa na madawa ya kulevya?”

    “Ndiyo nimeipa na hapa mkononi nina gazeti la leo ambalo lina habari hiyo,”

    “Basi siku chache zilizopita yaani kabla sijaanza kazi KWITALE…. nilikuwa nikiishi na huyo binti kama mke wangu ingawaje hatukuwa tumefunga ndoa. Hata siku niliyosaini mkataba wa kazi KWITALE yeye nilikua nimemuacha nyumbani asubuhi ya siku hiyo… lakini niliporudi nyumbani jioni ya siku hiyo sikumkuta kabisa….. na tangu siku hiyo si mimi wala wazazi wake, hakuna aliyekuwa akijuwa ni wapi alipokuwa Doi mpaka hii leo baada ya kusoma kwenye gazeti na kutazama kwenye luninga,” alimaliza Domi na kuacha uwanja wazi ili asikie au apate neno la bwana Makeke.





    “Kwanza kabisa pole…. Pole sana bwana Masaka nimekusikia na nimekuelewa lakini ni vyema endapo mimi na wewe tukaonana leo kwa mazungumzo ya kina ili tujue nini cha kufanya”

    “Sawa bwana Makeke mi nafikiri tusipoteze muda… hapa nyumbani kwangu kuna utulivu unaoweza kuturuhusu kuzungumza kwa nafasi, lakini pia nisikubane ….. unaweza kupendekeza mahali popote ambapo unaona panafaa kwa mazungumzo”

    “Mi nafikiri uje tu hapa nyumbani kwangu, kuna ofisi ndogo ambayo inaweza kutupa faragha na wakati tunaendelea na mazungumzo shemeji yako atakua anatuandalia chakula cha mchana”

    “Hakuna shida bwana Makeke… nipe kama dakika arobaini na tano hivi nitakua hapo nyumbani,” “Sawa karibu sana bwana Masaka,” wakaagana kwenye simu, na bila kupoteza muda Domi alikusanya magazeti yote aliyoyanunua asubuhi akayaweka kwenye gari tayari kwa safari ya mikocheni mahali alipokuwa akiishi bwana Makeke.

    ****

    Doi alikuwa amejikunyata kwenye kona iliyokuwa katika moja ya vyumba vya mahabusu vilivyopo katika gereza la Keko. Macho ya Doi yalikuwa mekundu na yaliyovimba kwa sababu ya kulia kwa muda mrefu. Doi alikuwa amejitenga kabisa na mahabusu wenzake. Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza yeye kuwa eneo kama lile! Kwani tangu azaliwe Doi hakuwa amewahi hata kukamatwa na polisi wachilia mbali kulazwa lupango.

    Mwanga hafifu, joto kali pamoja na harufu nzito vilizidisha tabu kwa Doi akapakumbuka nyumbani kwake Buza, mahali ambapo alikuwa amepanga pamoja na mchumba wake Dominic. Chumba alichokuwa akiishi na Domi kilikuwa na joto… lakini ni afadhali mara mia moja kuliko joto analokabiliana nalo sasa. Chumba alichokuwa akiishi na Domi kilikuwa na mbu… lakini ni afadhali mara kumi kuliko mbu hawa wa gerezani. Mbu ambao hawakujua mchana wala usiku…. Wao walichojua ni kufyonza damu ya Doi pamoja na wafungwa wengine.

    Hali aliyokuwa akikabiliana nayo ilimfanya Doi ajute kwa uamuzi wake wa kipumbavu, uamuzi ambao umemfungulia milango ya jela ambamo yumo akiwa hajui nani wa kumsaidia!

    “Madawa ya kulevya !” hatimaye sauti ilimtoka Doi na kusababisha mahabusu wenzake wamshangae. Doi alishindwa kuelewa jamii ingemtafsiri vipi, taswira ya Damiani ilipomjia akilini machozi yaliongezeka mashavuni mwake. Alimwona Damiani kama adui yake namba mbili baada ya Zai ambaye mpaka wakati huo alimchukulia kama adui yake namba moja.

    Doi alijua fika kama asingekuwa Zai basi yeye asingemfahamu Damiani ambaye amemkalisha kwenye kuti kavu, kuti lisilo na matumaini ya uhai isipokuwa kifo tu.

    Doi aliendelea kulia mule ndani huku matumaini ya kupona katika kesi ya madawa ya kulevya inayomkabili yakizidi kupungua kadri muda ulivyokwenda. Hakujua nani angekuwa msaada kwake. Alipowafikilia wazazi wake uchungu ulimzidia kabisa, hakujua ni vipi wazazi wake wangeweza kumsaidia kuepukana na balaa ambalo yumo ndani yake. Balaa ambalo kwa jinsi anavyowajua wazazi wake lilikuwa limewazid uwezo mara sabini. Doi alimjua fika baba yake mzee Vioja, mzee aliyeogopa mahakama kuliko njaa! Mtu wa namna hii ni vipi angeweza kumpigania? Alipoyafikilia hayo matumaini yake kuiepa jela yakazidi kupungua nukta baada nukta ****

    Baada ya Mudi kuondoka kutoka katika nyumba ambayo alimfumania mkewe mtarajiwa Zainabu Mpotoshi na kuwaacha Mapunda na Zai wakiwa katika hali ya sintofahamu. Mudi aliondoka akiwa na msongo wa mawazo huku akiwaraani kabisa wanawake wote kwa sababu ya kile alichofanya Zai.

    Aipofika tu nyumbani kwake, kwanza alihakikisha amemwona bi Udaku mtonyaji wake, ambaye kwa msaada wake ameweza kuyagundua madhambi ya Zai akamshukuru. Licha ya kumshukuru bi Udaku kwa hilo, chuki yake kwa wanawake bado haikukoma.

    Mudi alimpa bi Udaku kiasi cha pesa kwa ajili ya kulipia pikipiki aliyotumia kumfuatilia Zai tangu Buza mpaka Jeti Corner. Pia alichukua nguo za gharama za Zai, nguo ambazo alizinunua yeye ili mkewe avae apendeze, nguo hizo zote Mudi alizichua akampa bi Udaku kama shukurani kwa kumfunulia ubaya wa mkewe.

    Hakuishia hapo, aliamua kubadili kitasa ili Zai akija asiweze kabisa kuingia ndani “Jirani,” Mudi aliita.

    “Abee… jirani,”

    “Huyu mpuuzi akija tu hapa uniambie, ili tusije tukagongana naye hapa akanihadaa kwa machozi nikamuonea huruma,”

    “Sawa jirani, akija tu, nitakufahamisha,” **** Haikupita muda mrefu tangu Mudi aondoke, Mapunda aliingia ndani na kumwamulu Zai avae aondoke, “Ondoka hapa nyumbani usije ukaniletea balaa… kumbe wewe ni mke wa mtu”

    “Nisamehe Mapunda, naomba nibaki hapahapa,” alisema Zai huku sauti yake ikitoka kwa tabu kutokana na kwikwi iliyosababishwa na kilio.

    “Usinizingue malaya mkubwa wewe …piga bunda, kama udiliki kunidanganya kuwa hujaolewa unafikili kuwa utashindwa kunidanganya kwa mengine? Fanya haraka utoke usije ukanilea balaa jingine hapa.” Zai alivaa nguo zake akaondoka huku akiendelea kulia. Alilia kwasababu ya upuuzi alioufanya, upuuzi wa kumsaliti mpenzi wake Mudi na kuja kutembea na Mapunda.





    7

    TINA alikuwa amebeba begi dogo aina ya montana ambalo lilikuwa maarufu sana kwa wakati huo. Tina na mama yake walikuwa wakimsindikiza mzee Masaka ambaye alikuwa anasafiri kuelekea Dar es salaam kwa Dominic mtoto wake.

    Wote watatu walikuwa na sura ambazo zilionyesha dhahiri kuna uhaba wa furaha baina yao. Furaha ya Tina na mama yake ilisababishwa na jambo ambalo walilitegemea kutokea ndani ya muda mfupi la kuondoka kwa mzee Masaka kwa safari ya kuelekea Dar es salaam.

    Wote walijua fika kuwa watagubikwa na upweke baada ya mpendwa wao huyo kuwa amepanda gari, gari ambalo lilikuwa tayari kituoni likiwasubili abiria.

    “Baba ukirudi usisahau kuniletea zawadi,” Tina alisema huku akimkabidhi baba yake begi baada ya kuwa wameshafika kituoni. “Nisipokuletea wewe zawadi n’tamletea nani? Usijali nitawaletea wote zawadi.” mzee Masaka alisema kwa sauti ambayo ilizidi kudhihirisha kuwa hana furaha.

    “Tena kabla sijasahau, mama Domi umekumbuka kuniwekea kiko kwenye begi?”

    “Nhu! Sikumbuki vizuri… ila nadhani kila kitu cha msingi nimekiweka. Lakini baba Domi…” alisita kidogo akamtazama Tina mtoto wao kisha akamwambia, “Tina mwanangu naomba unipe nafasi kidogo nizungumze na baba yako”

    Tina alikuwa mwelewa akajisogeza pembeni ili kuwapa nafasi wazazi wake. Baada ya Tina kuwapa nafasi, mama Domi alimgeukia mumewe, akamwambia, “Hivi mume wangu kwani ni lazima kuvuta hayo masigara yako? Hebu tazama unavyoipa sigara kipaumbele…”

    Mzee Masaka alikaa kimya kwa sekunde kadhaa kisha akasema, “Nitajitahidi ili niache mke wangu… nipe muda,” baada ya kusema hayo, gari lilipiga honi wakaagana na Tina aliyekuwa pembeni alisogea wakapeana mikono huku wakimtakia safari njema.

    Baada ya masaa manne ya safari ndefu mzee Masaka alifika Mwanza majira ya saa 12 jioni tangu saa nane, muda ambao alianza safari yake akitokea Nyamuswa.

    Kwa sababu alifika Mwanza kwa kuchelewa, Mzee Masaka aliandaa kwanza utaratibu wa safari kwa kukata tiketi kisha akaenda kulala katika nyumba ya wageni ambayo ilikuwa palepale Nyegezi jirani na kituo cha mabasi yaendayo mikoani.

    Akiwa chumbani kwake Mzee Masaka alijipapasa mifukoni, mwishowe akatoa kipande kidogo cha karatasi kutoka kwenye mfuko wa koti alilovaa, alitambua kuwa hicho ndicho kilikuwa kipande cha mwisho cha karatasi alichonacho ukiachana na tiketi ambayo alitakiwa kuitumia kesho kwa safari.

    Kuishiwa karatasi hakukumshitua sana kwa sababu; alijiaminisha kuwa kuna kiko ndani ya begi, aliamini hivyo kwa sababu alimsisitiza mkewe amuandalie kila kitu chake cha muhimu kwa safari na kiko kikiwemo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzee Masaka alisokota sigara yake kisha akaiwasha na kuivuta kabla hajapitiwa na usingizi mzito uliomfanya asahau kushusha neti kabla ya kulala.

    ****

    Baada ya kuwa gari alilokuwa amepanda mzee Masaka kuondoka, mama Domi na bintiye walirudi nyumbani ili kuendelea na shughuli nyingine.

    Wakiwa nyumbani mama Domi alibaini kuwa hakumuwekea mzee Masaka kiko, hii ilikuwa ni baada ya kuanza kurudisha kabatini baadhi ya vitu ambavyo alivitoa ili kumuandalia mumewe safari. Wakati anamalizia kupanga nguo, mama Domi alikiona kiko cha mumewe na moyo wake ukumpasuka!

    “Hee….. hivi hiki kiko sikikuweka! Basi alivyo baba Domi atagomba wee… anaweza akadhani nimefanya makusudi kwa sababu huwa namkataza kuvuta sigara.

    ****

    Mzee Masaka alishituka usingizini majira ya saa 7:15 usiku, chumbani mote palikuwa giza, alipochungulia nje pia alikumbana na giza totoro. Kwa akili ya haraka mzee Masaka aling’amua kuwa umeme umekatika!

    Kiu ya sigara ikamvaa mzee Masaka ghafla, alichukua simu yake ndogo ya Nokia akawasha tochi kwa lengo la kumulika ili achukuwe kiko kwenye begi ili avute tumbaku yake. Alitafuta kila pembe ya begi bila mafanikio, akaamua kutoa nguo moja moja ili aone kama anaweza kukiona kiko chake. Alitoa nguo zote kisha akalikung’uta begin a bado kiko hakikuonekana! Akajisemea, “Huyu mama Domi… Si nilimwambia aniwekee kiko ina maana hakunisikia au alifanya makusudi?” mzee Masaka alifura kwa hasira akiwa mule chumbani huku kiu ya sigara ikizidi kumkolea.

    Kwa hasira alizokuwa nazo aliamuwa kubonyeza simu yake kwa lengo la kumpigia mkewe angalau apoze hasira zake kwa kumtukana, lakini alipoiweka simu ile sikioni alizidi kuchoka. Sauti kutoka upande wa pili ikamjibu kama inamzomea vile, “Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa… jaribu tena baadae…” baada ya kusikia sauti hiyo mzee Masaka alizidi kufura kwa hasira huku akiachia matusi, “Mpumbavu sana huyu mwanamke…”

    Mwani wa sigara ukazidi kumkolea mzee Masaka, alijisachi mfukoni ili kuona kama ana akiba ya karatasi, lakini hakuna alichoambulia zaidi ya tikiti ya basi ambayo alipaswa kuituma kesho kwa ajili ya safari yake ya Dar es salaam pamoja na noti kadhaa ambazo alikuwa nazo kama akiba na tahadhari njiani.

    Akaamua kufungua mlango ili aende mapokezi akaonane na mhudumu wa gesti kwa lengo la kumuomba muhudumu huyo kipande cha karatasi ili aweze kusokota tumbaku yake avute.

    Alipofika mapokezi aligonga mlango bila mafanikio na matumaini ya kupata kipande cha karatasi yakazidi kufifia. Akarudi chumbani kwake akiwa amefura kwa hasira huku kiu ya tumbaku ikizidi kumkereketa! Alijisachi tena mifukoni lakini majibu hayakubadilika hakuwa na kitu kingine zaidi ya tikiti yake ya safari pamoja na hela za noti, wakati mwani wa sigara ukizidi kumkolea.

    Mwani wa sigara ulimfanya mzee Masaka afanye jambo ambalo lilihitaji kuwehuka kwanza ndipo ulifanye. Angefanyaje ikiwa hakuwa na uchaguzi mwingine wa nafuu isipokuwa huo! Mzee Masaka aliamua kuichana tiketi yake ya safari katika vipande viwili, ambapo kimoja aliamua kusokotea tumbaku ili kuikata kiu yake ya sigara iliyokuwa ikimuweka katika wakati mgumu.

    Baada ya kuwa amefanikiwa kuikata kiu yake ya tumbaku mzee Masaka alipata usingizi mnono saa 8:00 kamili usiku akalala.

    ****

    Domi alifika nyumbani kwa Makeke dakika kumi na tano mbele baada ya muda aliokuwa ameahidi kupita. Alijitahidi kukimbiza gari lakini hakuweza kufika ndani ya muda alioahidi kwa sababu ya msongamano wa magari aliokutana nao maeneo ya Moroco.

    “Karibu bwana Masaka… karibu sana,” alisema Makeke wakati akimkaribisha Domi baada ya kuwa wamesalimiana.

    Domi aliingia ndani na moja kwa moja wakaenda kwenye ofisi ndogo iliyoko nyumbani kwa Makene, ofisi ambayo huitumia mara nyingi awapo nyumbani kwa shughuli zake za kiofisi na za binafsi.

    Ofisini, Domi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuizungumzia maada iliyowakutanisha pamoja katika siku na muda kama ule ambapo alianza kwa kusema, “Bwana Makeke, hili swala kama nilivyokwambia hapo awali kuwa huyu binti aliyekamatwa na madawa ya kulevya ni mchumba wangu ambaye nimeishi naye kwa zaidi ya miaka miwili…” Domi alisema hayo kisha akaweka kituo na kumtazama usoni bwana Makeke.

    Makeke alikuwa akimsikiliza Domi kwa umakini wa hali ya juu. Hivyo baada tu ya Domi kumaliza kuongea, ukimya ulishika hatamu kwa muda wa takribani nusu dakika. Ukimya huo ulishika hatamu kwa sababu Domi alikuwa akitegea Makeke aseme neno baada ya yeye kuwa amekwishaongea, na kwa upande wa pili Makeke alikuwa akitafakali maneno ya Domi pamoja na kujipanga katika namna njema ya kuongea.





    Baada ya ukimya kudumu kwa muda huo Makeke aliuvunja kwa kusema, “Nimekusikia na nimekuelewa vizuri bwana Dominic licha ya uvulivuli ninaoupata kwenye historia yako wewe na huyu binti unajua kesi hii inayomkabili, kesi ya madawa ya kulevya ni nzito sana, na kwa mujibu wa sheria za nchi hii yeyote atakaekutwa na hatia katika kesi ya namna hiyo hana budi kupokea adhabu kali kwa mujibu wa sheria.” Makeke aliweka kituo kwenye maelezo yake kisha akamtazama Domi kwa muda kidogo kabla akaendelea, “…. Mr Dominic, labda nikuombe unipe historia ya maisha yako wewe na huyo binti kabla hatujaenda mbali zaidi…. hapo nikiwa na maana uanzie siku ya kwanza tangu ulipokutana naye mpaka alipotoweka,” alisema Makeke.

    Domi alishusha pumzi ndefu, akajivuta nyuma akiwa palepale kitini alipokaa, kisha akarudi tena katika mkao wake ule wa awali, lakini kwa namna ya pekee. Aliisimika mikono yake yote miwili juu ya mezza iliyokuwa mbele yake kwa kutumia viwiko vya mikono yake, huku kidevu chake akikiacha kiegemee katika viganja vya mikono yake.

    Domi alimtazama Makeke kwa mara nyingne, kisha akaanza kwa kusema, “Yapata miaka miwili na sehemu sasa tangu nimfahamu Doi na kuanza kuishi naye.” Alijiinua kutoka katika mkao wake ule, na safari hii alijiegemeza kwenye mgongo wa kiti halafu akaendelea, “…. Ilikuwa ni wakati ambao nilikuwa mahakama ya mwanzo ya Temeke kwenye mafunzo kwa vitendo. Mara tu baada ya shughuli za mahakama kuisha, nilielekea kwenye kituo cha daladala tayari kuelekea nyumbani kwa mapumziko.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Watu walikuwa ni wengi sana kituoni na kusababisha kila gari lilokuja pale kuonekana lulu machoni pa wasafiri kwa sababu ya mahitaji yao ya huduma ya usafiri. Yalikuja magari kadhaa kituoni, lakini yote yalikuwa yamejaa kiasi cha kutokuwa hata na nafasi ya kusimamisha abiria ndani yake. Nilikaa pale kituoni nikiendelea kusubiri gari lenye nafasi angalau ya kusimama ili niwahi nyumbani nikapumzike. Ikawa kama nilivyotarajia. Lilikuja gari aina ya Toyota Coaster likiwa na abiria wachache, nikajitoma ndani.

    Humo nilielekea mpaka kwenye siti za upande wa kulia, siti ambazo huwa na viti maaalum kwa ajili ya abiria wawili, nikakaaa kwenye siti ya dirishani, siti ambayo ilifuatia baada ya siti ya nyuma, ambayo hukaliwa na abiria wanne na pengine hata watano kutokana na shida ya usafiri iliyopo.

    Nikiwa nimekaa pale kwenye siti, alikuja dada mmoja mrefu wa wastani, ambaye ama hakika alikuwa ni mrembo wa haja! Alikuwa ndani ya gauni refu la rangi ya kijani iliyochanganyika na weusi. Gauni lile aina ya dila lilimfanya mrembo yule avutie, nami nikavutika naye.

    Nilitamani akae kwenye siti niliyopo, ikawa kama vile aliyasoma mawazo yangu. Alikuja tukajumuika naye kwenye siti ile, “Mungu anipe nini tena!” nilijisemea.

    Wakati pua zangu zikipokea burudani ya manukato mazuri aliyojipulizia mrembo yule, mara masikio yangu yakajiwa na sauti yake laini, “Habari yako kaka?”

    “Salama tu, sijui wewe?” nilimjibu na kumtaka hali, lengo likiwa ni kuziteka hisia zake.

    “Njema tu,” alijibu huku akijaribu kujiweka sawa pale kitini tulipokuwa. Wakati huo gari lilikuwa katika mwendo kwa safari ya kuelekea Mbagala na vitongoji vyake na mwiso wake ulitarajiwa kuwa Mbagala Rangi tatu.

    Shauku ya kutaka kuendeleza mazungumzo na mrembo yule ikazidi kuzitwaa fikra zangu, niligeuka na kumtizama kwa mara nyingine.

    Naweza kusema safari hii uzuri wake uliongezeka maradufu. Wakati bado naendelea kumtizama, wasiwasi ambao sijui ulikotokea uliuvamia moyo wangu na kuyabadiri mapigo yake kutoka kwenye mwendo wa kawaida na kuufanya udunde kwa kasi zaidi.

    Alikuwa pilikani huku mkono wake mmoja ukiwa ndani ya mkoba na mwingine uliobaki ulikuwa umeshikilia mkoba aliokuwa nao. Punde mkono uliokuwa ndani ya mkoba uliibuka na ‘Earphone’ ambazo alizichomeka kwenye simu yake ya mkononi aliyokuwa nayo na baadaye aliziweka zile Earphone kwenye Masikio yake kisha akaruhusu muziki ucheze kutokea kwenye simu yake.

    Nadhani haikuwa kama alivyopanga, kwani badala ya muziki kusikika kupitia kwenye zile spika ndogo alizoweka masikioni mwake, ulisikika kupitia spika ya simu! Licha ya sauti kusikika kupitia spika ya simu, sauti ile haikuweza kuvuka mipaka ya eneo tulilopo, kwa maana ya kusikika na watu walio nyuma au mbele yetu isipokuwa mimi na yeye.

    Naam, ulikuwa ni wimbo wa ‘hero’ ulioimbwa na Enrique Egliasis.

    Kitendo kile cha mambo kwenda kinyume na matarajio yake kilimfanya mrembo yule ahisi kupatwa na aibu, mara ghafla akaanza kuhangaika kuusimamisha muziki uliokuwa ukiendelea kusikika kupita spika za simu. Niliushika mkono wake kama ishara ya kumzuia asifanye alichokusudia huku nikifuatisha baadhi ya mashairi ya wimbo ule, “… I can be your hero…. Now I stand by you forever….” Aligeuka kunitazama na mara macho yetu yalipokutana aliachia tabasamu pana lililozidi kuukonga mtima wangu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Who is the lucky guy?” nilimuuliza lakini hakujibu chochote zaidi ya kuchanua tena tabasamu lililozidi kumpamba na kumfanya aonekane mrembo zaidi, hasa kwa vile vijishimo vilivyojiunda mashavui mwake ‘Dimpozi’.

    Sikuishia pale, nilimuuliza tena, lakini safari hii kwa lugha ya Kiswahili, “Ni nani mwenye bahati?”

    “Una maana gani?” aliuliza.

    “Namaanisha kuwa; ni nani huyo mwenye bahati ya kuwa na mrembo kama wewe?”

    Hakujibu kitu, alizidi kutabasamu huku wimbo ule wa ‘hero’ ukiendelea kucheza kwenye simu yake.

    Sikuona sababu ya kumlazia damu, nikaendelea, “Naitwa Dominic Masaka. Ila wengi hulifupisha jina langu kwa kuniita Domi. Je wewe mwenzangu waitwa nani?”

    “Naitwa Doi,” alijibu.

    “Sabasaba wa kushuka, sabasabaa..” sauti ya tandiboi ilisikika kuwakumbusha watu vituo wanavyopaswa kushukia ili wasije wakavushwa kwenye vituo husika.

    Ni sauti hiyo ya konda ndiyo iliyonikumbusha kuwa ndani ya muda mfupi ujao tutatenganishwa na Doi.

    Japo safari yangu ilikuwa bado ni ndefu, sikutaka kujiaminisha kuwa angedumu kwenye gari lile mpaka nitakapokuwa tayari kushuka baada ya kuwa nimefika. “Yawezekana akashuka kituo kinachofuata.” Niliwaza.

    Nikaona ule ndiyo wasaa pekee nilionao, wasaa wa kuandaa mazingira yatakayonifanya nizidi kuonana na Doi. Sikutaka kushuhudia nikipotezana na mrembo yule katika hali ya uzembe namna ile. “Sina budi kufanya jambo....” niliwaza.

    Nilimtazama tena Doi ambaye alikuwa ametulia kimya, sijui kama alikuwa amezama kufuatilia mashairi ya wimbo ule ama lah!

    “Doi,” nilimuita.

    Aliitika na kunitazama, tukawa tunatazamana kwa hisia tofauti. Wakati nafikiria maneno mwafaka ya kuzungumza kwake, yeye alikuwa makini akisubiri nimueleze sababu ya kumuita.

    “Nisingependa kuona kuwa, huu unakuwa mwisho wa mimi na wewe kuonana. Natamani tukutane tena na tena,”

    “Mh!” aliguna na kubetua mabega yake juu kisha akasema, “Unaenda kwenu… sijui kwako, nami naenda kwetu, ni vipi tutaonana tena?”

    “Ipo namna Doi,”

    “Namna ipi hiyo?”

    “Nipe namba yako ya simu na wewe uchukue yangu.” Nilisema.

    “Lakini….” Alisita kidogo kabla hajaniuliza, “kuna nini cha mno?”

    Swali lake lilikuwa gumu kwa mimi kulijibu ghfla. Nilituliza akili yangu, nikafikiri kwa nidhamu kisha nikasema, “Maisha yana namna ya ajabu sana Doi, leo tumekutana kwenye daladala kama wasafiri. Huwezi jua kesho tutakutana wapi tukiwa katika hali gani… tafadhali tubadilishane namba zetu za simu”

    Ombi langu la namba ya simu kwa Doi lilikubaliwa, tukabadilishana namba. Wakati huo gari lilikuwa limekaribia kizuiani, kondakta aliwakumbusha tena abiria wake wanaoshukia kizuiani wajiandae.

    Doi alikuwa ni mmoja wao. Tuliagana huku akijiandaa kushuka na mara gari lilipofika Kizuiani alishuka sanjari na abiria wengine ambao walikuwemo garini.

    Baada ya gari kuwa limewashusha watu kizuiani liliendelea na safari yake na lilipofika Zakhem nilishuka na kuliacha gari likiendelea na safari yake ya kuelekea Rangi tatu. Hiyo ikawa ni siku ya kwanza.

    ****





    ITAENDELEA
    Pseudepigraphas

0 comments:

Post a Comment

Blog