Search This Blog

Friday, October 28, 2022

UPENDO KUTOKA SAYARI NYINGINE - 2

 

     





    Simulizi : Upendo Kutoka Sayari Nyingine

    Sehemu Ya Pili (2)







    Suala la kuagiza vipuli vya magari pamoja na mashine za viwandani haliwagharimu nyinyi kwenda nje ya nchi wala kuhangaika kwenye meli bandarini. Ninyi kazi yenu ni kujaza tu makaratasi ya kudhibitisha kuwa mzigo ulioko bandarini ni wa Kampuni hii na baada ya hapo mzigo ungeletwa na kuingizwa stoo kwa malipo tu ya uchukuzi ambayo yanajulikana vizuri kwenu.

    Safari yangu kwakweli haitaniruhusu kujakuja hapa ila ninawaamini sana kuwa mtasimamia vema kazi hii mpaka hapo nitakaporudi.” Alisema Mkurugenzi na baadaye alifunga kikao. Watenda kazi wachache tu wa ngazi za juu katika kampuni hiyo ndio walioitwa katika ofisi hiyo kuongelea swala hilo. Hali kadhalika baada ya kutoka hapo Sebastian alienda kuonana na wasimamizi wa majengo yake ya biashara Kariakoo na kumalizia kwa Mkandarasi wa nyumba yake iliyoko Masaki na kuacha kila kitu kimekaa vizuri baada ya hapo alipotea.

    Hakuna aliyejua aliko kwa zaidi ya miezi sita. Wachache sana walibahatika kupigiwa simu na kupewa maagizo ya nini kifanyike katika usimamizi wa kazi zake. Wachache hao ni kati ya watenda kazi katika kampuni yake. Baada ya kupiga simu alikuwa akipotea tena katika mawasiliano kwa muda mrefu mpaka pale alipoona umuhimu wa kuwasiliana na mmoja wa watendakazi wake muhimu. Tabia yake hiyo mpya iliwashangaza wengi lakini walimwachia mwenyewe japo hawakujua nini maana ya mambo yale. Kwao ulikuwa ni ukurasa usioeleweka japo kwa Seba ulikuwa ni ukurasa wa giza nene.

    4

    Maamuzi magumu

    Haikuwa ikipendeza kuendelea kumdhibiti kwa kamba maana zimemtoa alama katika mikono yake na kumpa jeraha usoni kwa kujipiga ukutani pindi tu anapofungwa. Huzuni ilizidi kuongezeka katika familia hiyo mwishowe uamuzi mgumu ukatolewa kuwa Judith aachiwe huru na afanye apendavyo huenda kwa kufanya hivyo anaweza kurudia hali yake nzuri. Walikumbuka maneno ya Daktari alivyosema: “Maoni yangu ni kwamba uvumilivu wenu kwa mgonjwa na kutokumsumbua kwa lolote ndiyo dawa itakayoyosababisha asiingie katika hali ya kutumia akili zake katika kukumbuka au kukabiliana na matatizo yawayo yoyote yale.

    Kwa mfano hata akiharibu kitu jitahidini kumvumilia na kumchukulia kwa upole na upendo badala ya kumfokea na kumwonyesha chuki. Hali hii inaweza kufanywa na madaktari katika Hospitali za watu wenye matatizo ya akili, hawa wamesomea jinsi ya kuchukuliana na wagonjwa na kwakweli wagonjwa wengi wenye matatizo ya namna niliyoielezea hapo walipata kupona na kurudi kwenye majukumu yao ya maisha.

    Kwa vipimo tulivyofanya ni kwamba mgonjwa wenu ana matatizo ya mchubuko ubongo wake. Kwa hiyo hata kama tungemwandikia aende kwenye hospitali yoyote duniani asingepata matibabu yoyote zaidi ya kuwekwa kwenye Sehemu za kuwatunzia wagonjwa wenye matatizo ya akili. Kwangu mimi sioni kama ni muhimu kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa inawezekana hata hapa nchini kwetu akatunzwa vema mpaka hapo akili zake zitakapomrudia.”

    Maneno haya yaliwaonyesha makosa yao waliyofanya kwa kumsumbua mgonjwa pale walipomfunga kamba. “Uhuru wake ndio jibu la kupona kwake. Tumpe uhuru wa kutembea popote na kufanya lolote.” Alisema Seba katika kikao cha dharura kilichokaliwa na watu wanne. Mzee Martin Adella shangazi yake Judith Alen baba mdogo wa Judithi pamoja na Seba.

    Hilo naliona kuwa ni gumu sana tena litakaloleta fedheha kwa watu kujua kuwa Judithi ni mwenda wazimu. Sikutaka mambo yajulikane angebaki tu hapa nyumbani.” Alisema Mzee Martin na kuungwa mkono na Adella. “Hilo ni sawa kama mnavyosema lakini uponyaji wake tunaoutarajia utatokea wakati gani ikiwa atafungwa kamba hizi? Kumbukeni kuwa anapofungwa kamba ndipo anapozidi kucharuka kwa kutaka kujiweka huru.

    Anapofanya hivyo akili yake inazidi kuwa kwenye shida maana anazitumia kwa kiwango kikubwa ili ajiweke mbali na ufungwa, kwa jinsi hiyo kuna kupona haraka kweli?” alisema Seba kisha akatulia kidogo ili kuona kama maneno yale yanapokelewa sawasawa. Kisha akaendelea: “Kumpeleka

    Hospitali tumeona kuwa ni ngumu kutokana na hali ya kule na kwamba hawezi kuwa huru. Wakati mwingine itamjengea hali mbaya kichwani hasa kama akipata fahamu zake na kujikuta yupo maeneo yale. Kumbukumbu zake zisingeweza kufuta tukio hilo la kujiona kuwa kumbe alikuwa kichaa.

    Lakini hali yake ya fahamu ikimrudia akiwa hapa nyumbani hawezi kuhisi chochote kibaya kuliko akiwa Hospitali ya vichaa. Sasa kama hatawekwa katika mazingira ya kuwa huru basi kwake itakuwa ni vigumu kurudi mapema kwenye akili zake.” Alisema Seba kisha akakohoa baadaye akaendelea: Kwangu mimi haitoshi tu kwamba nimeachana na kazi zote na niko hapa kumwuguza mchumba wangu.

    Lakini ninataka kuchukuwa hatua nyingine zaidi. Kwa kuwa huyu ni mwenzangu maisha yake ni kama maisha yangu mimi pia nimejitolea kuishi kama yeye. Nitatembea naye mahali popote anapoenda. Nitamlinda na kila tatizo linalotaka kumpata. Hakuna atakayeweza kumgusa labda aanze na mimi kwanza. Hali hiyo itaambatana na kumbebea chakula na kumlinda asile kitu kibaya.

    Haya yatafanyika kwa muda wote mpaka pale atakaporudiwa na fahamu zake. Kwa upande wenu ninaomba mkafanye ibada na kumwombea kila mara kusudi apone ili turudi kwenye majukumu yetu.” Alisema Seba na kuacha watu wote pale ndani midomo wazi. Lilikuwa ni jambo la nne kubwa la kushangaza kwao. Hakuwahi kuona upendo mkubwa kama huu wala kuusikia.

    Jambo la kwanza la kushangaza ni pale alipoacha kuendelea na masomo yake nchini Marekani na kurudi kwa sababu tu ya kutompata Judith kwenye simu. La pili ni kuacha kazi yake kwenye shirika alilokuwa akifanyia kazi. Kazi iliyokuwa ikimpa kipato kikubwa sana. La tatu ni kuweka watu kwenye kazi zake zote ikiwepo kampuni yake na shughuli za kibiashara na ujenzi wa nyumba zake ili tu aje kukaa na Judith akimuuguza. Jambo la nne ndio kubwa zaidi la kuamua kujivika uwendawazimu usio wake ili tu apate kumlinda mpenzi wake kila aendapo. Huyu ni mtu wa namna gani? Kila mmoja katika kikao kile alikuwa akitathmini mambo yote aliyoyafanya Seba lakini hakuna aliyepata picha kuwa ni aina gani ya upendo aliyonayo.

    “Kijana kusema kweli upendo ulionao hata mimi sina! Sijawahi hata kufikiria kufanya hata kimoja cha vitu ulivyofanya kwa ajili ya mchumba au mke.” Alisema Alen baba mdogo wa Judith. Kisha akatulia kwa sekunde chache kisha akaendelea: “Hakuna mwenye upendo huu duniani hapa? Labda utueleze kuwa unatoka sayari gani kijana. Alen Alimwangalia kwa makini kabla ya kuendelea.

    “Nina watu ninaowajua kabisa ambao wamewakimbia wenzi wao kwa sababu tu hazai au kuwafukuza pale walipogundua kuwa aidha ana kifafa nakadhalika. Hayo ninayoyasema yametokea kabisa sio habari ya kutunga. Na hao ni watu ambao walifunga ndoa kabisa na pengine kuwa na watoto kadhaa. Sisemi hivyo ili kukukataza usiendelee na hayo unayotaka kuyafanya ila ninaongea haya kukushangaa kwa namna ulivyo na upendo wa hali ya juu kwa mchumba wako.” Alimaliza kuongea Alen kisha akanyanyuka na kutoka nje ili kusikiliza simu yake ambayo ilikuwa ikiita.

    “Alichosema bwana mdogo Alen ni kweli kabisa ila ninakushukuru sana kijana kwa uvumilivu wako na upendo wako wa ajabu na nashukuru kwa mchango wako mkubwa wa malipo kwa ajili ya matibabu yaliyotolewa Hospitalini. Kila ulichofanya kinastahili shukrani za kipekee. Ila ombi langu kwako kwa niaba ya wenzangu ni kwamba urudi kazini kwako, inatosha kuja kumwona kila wakati na kumhudumia pale inapolazimu.

    Kumjali mwenzako sio lazima na wewe ujiingize katika hali ya kuishusha heshima yako ambayo ni kubwa sana. Mwenzako huu ni ugonjwa ambao tunajua sote kuwa iko siku atarudia hali yake ya zamani. Lakini kwako nenda ukatulie ila kabla ya yote tuangalie kwa pamoja njia nyingine inayofaa ya kumtunza mwenzako ambayo haitakugharimu wewe kufanya jambo gumu kama hilo.” Alisema Mzee Martin kisha akanyamaza akisubiri jibu ama kama kuna mtu mwingine kati yao mwenye neno la kuongea.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Baba nimekusikia na ninashukuru kwamba kumbe hata haya madogo niliyoyafanya yameonekana kuwa ni mambo ya ajabu. Kiukweli nataka niwaambie kuwa upendo wangu kwa Judith sio wa kimaigizo. Namwona Judith kama mimi mwenyewe na wakati mwingine natamani mambo yanayompata kama kungekuwa na uwezekano niyabebe mimi ili yeye apumzike.

    Lakini kwa sababu haiwezekani lazima nitumie gharama iwayo yoyote ili niweze kumsaidia mpaka pale atakaporudiwa na akili zake kama mwanzo. Haya ninayotaka kuyafanya sisitahili kukatazwa maana ni majukumu yangu kwa Mchumba wangu. Sitajali kama heshima inashuka kiasi gani lakini la muhimu kwangu nimwone Judithi akiwa salama wakati tukisubiri mkono wa Mungu ili apate kupona kabisa.” Alisema Seba kisha akanyamaza kimya kama alikuwa sio yeye aliyekuwa akiongea muda mfupi uliopita.

    “Nakutakia heri mwanangu uko huru kumhudumia mchumba wakio kwa njia yoyote moyo wako unavyokusukuma.” Asante sana kwa yote haya Mungu akubariki maana hufanyi haya kwa ajili ya Judith tu wala kwetu sisi wazazi wake ila unafanya hayo kwa Mungu pia.” Alisema Adella shangazi yake Judith huku akiwa haamini kile anachokisikia.

    “Jamani ninashukuru sana kwa kuitikia wito wa kikao hiki labda sasa niseme kuwa kikao hiki kimefungwa. Maamuzi tuliyokubaliana ni kwamba Judith awekwe huru ili tuangalie maendeleo yake kutoka hapa. Vyovyote ilivyo Seba yupo atamwangalia mchumba wake kwa kila jambo; Tulitaka tuweke mtu wa kumsaidia lakini hakutaka kusikia swala hilo kwa hiyo ninamwachia aweze kumsaidia mwenzake huku sisi tukiomba dua kwa Mungu ili aharakishe uponyaji kwake. Mpaka hapa kikao kimefungwa.” Alisema Maneno hayo Mzee Mrtin na wote wakanyanyuka kwa ajili ya kuendelea na majukumu yao. Seba yeye alienda kwenye sebule ya chini ya ghorofa waliyokuwepo kwenye kikao kwa ajili ya kuangalia usalama wa Judith.

    Alikuwa amefungwa kwa mikanda maalumu katika sofa la kukaa mtu mmoja ili asiweze kutoroka. Alipomwona Seba anakuja alikuwa akipiga kelele: “Wanataka kuniua! Hao haoo! Wanakuja na mapanga wanataka kuniua!” Alisema kwa sauti huku akiwa katoa macho kwa woga. Hawawezi kukuua nimekuja mwenyewe. Si unanijua zangu zilee? Nakwambia watakoma na mimi wako wapi?”

    Alisema Seba kwa mkwara mzito mbele ya mchumba wake. Na Judith alicheka sana, baada ya hapo wakawa wanaongea maneno yao japo hawakuwa wakielewana sana lakini Seba alijitahidi kuenda sawa na Judithi mchumba wake. Seba alikuwa amehama kutoka kwenye nyumba yake na kuwa hapo nyumbani kwa akina Judith kwa ajili ya kusimamia huduma zote zinazohusu matibabu na usalama wa mchumba wake.



    5

    Wapendanao ndani ya vyombo vya habari

    Ilidhaniwa kuwa ni sinema iliyokuwa inachezwa na wawili hawa wapendanao. Hayo ni maoni ya baadhi ya watu waliokuwa wakiwaona Seba na Judith Mitaani wakizurura bila sababu ya maana. Wakati mwingine walitembea na jua kali huku wakiingia maeneo ambayo hawakustahili kufika hususani majalalani. Kwa umakini wa hali ya juu waliona vile Judith alivyokuwa akiokota vyakula jalalani na kutaka kula, lakini ghafla waliona Seba akimnyang’anya vyakula vile na kumtolea chakula kizuri kutoka kwenye mfuko wa nailoni na kumpa ale.

    Mara nyingine walimshuhudia Seba akigombana na watoto waliokuwa wakirusha mawe kwa Judith. Kwa ujumla watu hawa walionekana ni waigizaji wa zoefu wa sinema za wapendanao. Hakuna mtu aliyetaka kukubali kuwa ule ulikuwa ni ukweli wa maisha ya watu makini walioingia katika matatizo ya kidunia.

    Historia za kila mmoja zilikuwa wazi kabisa kwa watu waliokuwa wanawaona kila siku katika mizunguko yao ile. Seba alijulikana vizuri kuwa ni mkurugenzi wa Kampuni ya Seba & Ellychangawe Interprisess na pia ni meneja masoko kwenye kampuni ya uingizwaji wa magari yenye ubora wa hali ya juu pamoja na mashine za viwandani.

    Na wengi walimfahamu Seba kama tajiri mwenye Mahoteli na mfanya biashara mkuu jijini Dar es Salaam. Baba yake Mzee Changawe alijulikana kama Mbunge wa jimbo la kiwikoni na Naibu waziri wa Utalii na utunzaji wa mazingira. Hizi ndio sifa za kijana Sebastiani Changawe. Watu walimfahamu Seba kuwa alichukulia Elimu yake katika nchi ya Marekani na Norway. Sifa hizi hazikumruhusu hata chembe awe katika hali aliyokuwa nayo. Miongoni mwa watu waliomjua Seba ni pamoja na wafanya kazi wake waliopewa majukumu ya kusimamia biashara zake na kampuni.

    Watu hawa hawakuweza kustahimili kuona hali ile. Wenye machozi ya karibu walilia na wenye ujasiri walimsogelea Seba na kumsalimia wakitaka ufafanuzi wa yale yaliyokuwa yakifanyika. Mmoja wao ambaye kwa majukumu ni katibu wa kampuni ya Seba alithubutu kumuuliza baada ya kusogea karibu yake wakiwa katikati ya jiji kwenye magari ya mataka. “Bosi unaweza kuniambia maana ya mambo yanayoendelea kwa wewe kuwa katika hali hii?”

    Aliuliza swali ambalo hakuwa na uhakika kuwa lilikuwa lina kiwango cha nidhamu kwa bosi wake ama la. “Rudi kwenye majukumu yako ya kazi na usijiingize kwenye mambo yangu binafsi. Kama bado una shida na kazi yako nenda kazini na uwaambie wenzako wafanye hivyo sawa?” Alisema Maneno hayo ya ukali huku akimkodolea mfanyakazi wake huyo macho ya hasira. “Sawa bosi samahani kwa maswali yangu.” Alisema katibu wake huyo aitwaye Phily huku akiondoka eneo lile kimya kimya. Sebastian alifuatana na Judith popote mchumba wake huyo alipoenda. Alionekana kama mgeni aongozwaye njia na mwenyeji wake. Mahali walipopita magari yalijazana na kufunga njia na wakati huo wengine walichukuwa picha za mnato na hata zile za video kwa jinsi hii watu wengine walioangalia juu juu walifikiri kweli kuwa Seba na Mwanamke yule walikuwa wakiigiza sinema.

    Kwa upande wa Judith alikuwa akijulikana sana katika mitaa ile kwani ndipo alipokulia. Baba yake alijulikana kama mfanya biashara mwenye kampuni ya kupokea na kusafirisha mizigo iitwayo. Mart & JudikaClearring and Forwarding. Vilevile alikuwa anamiliki magari kadhaa ya mizigo pamoja na magari mawili ya abiria yaliyokuwa yakienda mikoani.

    Judith alikuwa ni msichana msomi aliyechukulia elimu yake jijini London nchini Uingereza elimu ambayo imemtunukia Digrii tatu na kuwa Doktor kwa mambo ya uchumi. Lakini aliyeishia kuwa Meneja wa kampuni ya baba yake. Hali ile iliwababaisha sana wasijue ni sababu gani iliyowafanya vijana hawa maarufu kuingia katika hali ya kuwa vituko mitaani.

    Ni wachache sana kati ya hawa waliofahamu ukweli wote kuhusu yale yanayofanyika japo nao pia hawakuwahi kukutana na upendo wa aina ile. Watu hao ambao walikuwa wakijua mambo yote waziwazi ni pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Seba na mkurugenzi wa kampuni ya uingizwaji wa magari na mashine za viwandani alipokuwa anafanyia kazi Seba. Na wengine ni Daktari aliyekuwa akimtibu Judith pamoja na wazazi wa Seba pamoja na familia ndogo ya Mzee Martin Sebwaka. Wakati watu wengi sana katika jiji la Dare s Salaam wakijua negative, watu hawa niliowataja walikuwa na mambo Positivu ya watu hawa wawili. Vyombo vya habari vilijaa habari siku moja tu mara baada ya Seba na Mchumba wake kuonekana mitaani.

    Kwa uvivu wa kufuatilia habari kwa baadhi ya waandishi wa habari walibeba mambo juu juu na kuandika habari tofauti na ukweli wenyewe. Vichwa vya habari viliuza magazeti mengi kutokana na umaarufu wa vijana hawa. Seba na Judith Martin waamua kucheza sinema ya ajabu sana mitaani. Liliandika Gazeti moja linalotoka kwa wiki mara mbili huku jingine likisema: “Vijana wawili maarufu mjini wawa vikatuni mitaani.”

    Na mengine mengi ambayo ndani kwenye maelezo yenyewe hakukuwa na la maana zaidi ya habari za kudhania tu. Katika habari hizi hakuna habari iliyokuwa sahihi kitu kilichowapa nafasi watu makini kuyachukia baadhi ya magazeti kutokana na uwezo mdogo wa kukusanya habari. Wakati wakiandika maneno haya Seba na mchumba wake walikuwa katika ulimwengu wa kizamani sana. Ulimwengu wa wasiojua kusoma wala kuandika. Ulimwengu wa watu wasio na haja ya kujua kuwa kuna tatizo gani kutembea barabarani na kuokota chochote njiani au jalalani.

    Ndio! Ulimwengu wa watu kuwa huru kupiga kelele wakati wowote hata ikibidi kuvua nguo na kuzitundika kwenye mti na mkukatiza mitaani ukiwa uchi wa nyani. Huu ndio ulimwengu aliokuwa nao mmoja wa vijana hawa na mwingine alikuwa anamwakisi mwenzake akiwa na nia ya kumlinda ila watu waliwaona wote ni hali kadhalika. Ilionekana picha ya ajabu sana kwa watazamaji hivyo kuwa gumzo mitaani magazetini na katika mitandao ya kijamii.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waandishi wa habari wengi walijaribu kila mtu kwa nafasi yake kupata kisa kamili cha hali inayoendelea kati ya Judith na kijana Sebastian Changawe. Ilikuwa ni vigumu sana kuwapata watu hawa na kuwahoji kuhusu mambo yao binafsi lakini waandishi wachache ambao walikuwa jasiri waliamua liwalo na liwe. Walitafuta namna ya kupenya katika ulinzi mkali sana ulioko Nyumbani kwa mzee Martin.

    Ulinzi uliowekwa na Sebastian kwa gharama kubwa kusudi kuepuka bughudha za watu waliokuwa wanakuja na maswali yao waliyoyaona kuwa ya kibiashara zaidi kuliko kuleta ufumbuzi wa tatizo lao. Kwa kuzingatia hayo Bwana Sebastian alikodisha walinzi maalumu kutoka kampuni ya ulinzi ya Group Four Security Guard, kampuni ambayo ina walinzi makini sana wanaotokana na wanajeshi waliostaafu Serikalini na wale waliopitia mafunzo ya kijeshi kwa gharama ya kampuni hiyo ili kujipatia ajira.

    Ziara za Seba na Judith za kutembea mitaani na wakati mwingine kando ya fukwe za bahari zilipata pia ulinzi japo kwa namna ya siri sana ili kuwalinda wasikutane na shida yoyote ile. Mbali na hayo waliokuwa wakilinda kwa usiri pia wapo askari waliokuwa wakifanya ulinzi wao katika nyumba ya Mzee Martin na katika nyumba moja ya Seba iliyoko bahari beach mahali ambapo Seba na Judith walipokuwa wakipendelea kufika mara kwa mara. Nyumba hii ilikuwa na bustani kubwa sana na nzuri ya maua iliyopambwa na mabembea kila mahali katika bustani hiyo. Mandhari ya nyumba hii ni nzuri sana yenye aina mbili za bustani moja ikiwa ni bustani ya maua aina mbalimbali yenye ukubwa wa kutosha na pia kulikuwa na bustani ya miti ya matunda iliyochanganyika na miti ya kimvuli.

    Karibu na bustani hii ya miti ya matunda na kimvuli iliyopakana na bustani ya maua kulikuwa na uwanja mpana kiasi wenye majani yaliyokatwa kiustadi na mashine maalumu. Katikati ya kiwanja hiki kulikuwa na bwawa la kuogelea (Swimming pool) ambalo lilikuwa na ukubwa wa kadiri na nje ya bwawa hili kulikuwa na vihema viwili vizuri vya kupumzikia baada ya kuogelea.

    Mbele ya bwawa hili kulikuwa na nyumba ya kifahari sana yenye ghorofa moja. nyumba ambayo ilikuwa ikitumika kwa Seba na mchumba wake katika ziara zao za kuzunguka kulingana na matatizo aliyokuwa nayo Judith. Mahali hapa napo uliwekwa ulinzi mkali sana na hakukuwa na namna ya kumwona Seba wala Judith kwa ajili ya hoja iwayo yoyote. Simu ya Seba ilikuwa ikifunguliwa usiku kuazia saa nne za usiku na kuzimwa kabla ya mapapambazuko.

    Namba za simu alizokuwa akitumia zilikuwa kwa watu maalumu sana ambao alikuwa anawasiliana nao kwa ajili ya miradi yake. Katika biashara zake na miradi yake ya kampuni na ile ya ufugaji alikuwa akiiendesha kwa njia ya simu. Hakuwa na nafasi ya kufika katika ofisi yoyote ile. Maisha yake yalibadilika kwa namna ya ajabu sana. Kwake kuzurura akiwa na mpenzi wake Judith yalikuwa ndio maisha aliyohiyari kuyaishi tangu siku aliyoamua katika kikao kuwa anataka afanye njia hiyo ili mchumba wake apate kupona haraka kutokana na matatizo aliyokuwa nayo.

    Pamoja na ulinzi huu wote waandishi wachache waliweza kupenya na kumwona Sebastian kwa mahojiano maalumu. Waandishi mashuhuri wa gazeti la UWARIDI wakiwepo Kadabra, Marijani, mwalongo, Kulindwa pamoja na mzee Beka. Hawa ni baadhi ya waandishi wengi jasiri kutoka shirika la utangazaji la UWARIDI. Waliweza kumfikia japo ilibidi kuingia gharama kubwa sana kabla ya kupata nafasi hiyo. Nafasi hiyo ilipatikana kutokana na uzoefu wa kutafuta habari ambao walikuwa nao kwa muda mrefu sana.

    Hata hivyo baada ya kupata habari kamili ya chanzo cha maisha yale ya ajabu kati ya Seba na Judith waliamua kuipeleka habari hiyo katika gazeti lao. Gazeti la UWARIDI likawa la kwanza kabisa kuandika habari hiyo kwa ukamilifu jambo lililosababisha gazeti hili lipewe tuzo wakiwepo waandishi wake machachari. Na Mwandishi mmoja wao alikwenda mbali zaidi kwa kuandika kitabu alichokipa jina la “Upendo kutoka sayari nyingine.” Kitabu kinachoelezea matukio na maisha pamoja na historia ya Seba na Judith. Kitabu kitakachosomwa na vizazi vingi vya baadaye kikiendelea kufundisha vizazi hivyo kuhusu upendo wa kweli wa watu hawa mashuhuri.

    6

    Matlyer Ardolph

    Mawazo yalimzidia usiku mzima na hakupata nafuu yoyote iliyompa usingizi. Moyo wake ulikuwa ukimwuma sana hasa alipokuwa akifikiria namna ya kupata utatuzi wa matatizo yale yaliyokuwepo. Yalikuwa mawazo mchanganyiko yaliyokuwa yakipishana kichwani kila moja likihitaji utatuzi yakinifu. Hakuona kuwa kukaa tu bila kujaribu njia nyingine ni busara. Binafsi hakuridhika na shida iliyokuwepo kwa vijana wake hasa binti yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni kweli kabisa kuwa mtaalamu wa tiba alisema kile alichoona katika vipimo vyake na ushauri alioutoa walikubaliana nao wauchukulie hatua ili waone matokeo yake. Lakini ilipita miezi sita bado hakukuwa na unafuu wowote katika taitizo hilo. Afya ya mgonjwa na muuguzi wake zimeendelea kuzorota kila siku. Heshima yao inazidi kushuka kila iitwapo leo kutokana na kuhangaika huko na huko kama kuku wa kienyeji. Furaha halisi umekuwa ni mtihani mkubwa kwao kuipata kwa maisha yale.

    Hakuna mtu aliyekuwa na jibu la haraka kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa lipi lifanyike. Maswala ya kujaribu kwa wataalamu wa jadi yalikataliwa tangu kwenye kikao chao cha pili katika miezi mitatu ya kwanza ya kutafuta njia ya kutoka katika shida ile.

    Mzee Martin alikumbuka kikao kile kilichohudhuriwa na ndugu wengi kwa upande wake na kwa upande wa akina Seba ukiwakilishwa na ndugu wanne. Mada za kikao zilikuwa mbili ya kwanza ilikuwa kujadili namna ya kukubaliana Judith akatunzwe katika Hospitali IItwayo, Psychological Mantal Hosptal ambayo ilielezewa kuwa ni nzuri sana iliyopo Nairobi nchini Kenya.

    Sifa za Hospitali hiyo zilitofautiana kwa umbali mkubwa na Hospitali nyingine za watu wenye matatizo hayo ya akili na mada nyingine ilikuwa kutafuta mtaalamu wa tiba za jadi ili ajaribu kumtibu. Wazo hilo lilitolewa na mmoja wa ndugu akiwa na imani kuwa Judith alikuwa amerogwa. Wazo hilo la pili lilipingwa vikali na Mzee Martin kutokana na imani yake, hivyo wazo likawa limebakia moja tu kumpeleka nchini Kenya.

    Inasemekana katika Hospitali hiyo kulikuwa na wataalamu wazuri wa Saikolojia ambao wamesomea jinsi ya kuwachukulia watu wa aina hiyo kwa upole sana huku wakiendana na matakwa yao na kama ni maamuzi mabaya na ya hatari waliwarejesha kwa upole na kwa kiwango kikubwa sana cha hila kwa namna ambayo mwenye matatizo ya ufahamu hawezi kujua kama anazuiliwa kufanya kile anachokitaka.

    Hospitali hii iko nje kidogo ya jiji la Nairobi karibu na njia panda ya kuelekea Meru na mji wa Ngong Kikuyu. Ni Hospitali kubwa sana iliyojengwa na Mjerumani mmoja kabla ya uhuru wa nchi hiyo. Ndani ya Hospitali hiyo pia kuna chuo cha mafunzo kinachochukuwa mamia ya wanafunzi kutoka ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo. Matlyer Ardolf ndiye Mwasisi wa Hospitali hiyo kubwa iliyochukuwa zaidi ya hekari kumi kulizunguka eneo la Hospitali hiyo.

    Hata baada ya uhuru bado mzungu huyo aliachiwa aendeleze hospitali yake kutokana na ukweli kuwa alikuwa msaada mkubwa sana kwa Wakenya wengi. Kama ilivyokuwa kabla ya uhuru ndivyo Hospitali hiyo ilivyoendelea na huduma zake kwa kiwango cha juu zaidi kila mara. Wataalamu kutoka Ulaya walikuwa wakiwafundisha waafrika wengi na watu kutoka katika mabara mengine walikuja kupata mafunzo katika chuo hicho. Inasadikika kuwa nchi nyingi zimekuwa na vituo vyenye kutoa huduma kama inavyotolewa katika eneo hili na hii imetokana na ukweli kuwa waasisi wa vituo hivyo wametoka katika chuo hicho.

    ***

    Matlyer Ardolph alikuwa ni mwanamke aliyepitia mambo mengi sana magumu katika maisha yake. Yeye alizaliwa mnamo mwaka 1924 katika mji wa Dormagen St. Michael uliopakana na wa Rhine. Matlyer Ardoph alikulia katika mji huu wa Dormagen St.Michael na kusoma katika shule maarufu ya Enkerniforde Internatinal School Iliyoko katika mji wa Rhine. Maisha yake yalikuwa yenye furaha ya aina yake pale alipokuwa akiona upendo wa mama na baba yake kwake. Hata shule aliyopelekwa na wazazi wake ilikuwa na utaratibu mzuri sana wa malezi ya watoto hivyo kumfanya Matlyer ayafurahie maisha katika pande zote mbili shuleni na nyumbani. Kwa upande wa masomo binti huyu alifanya vizuri sana na kushikia namba moja darasani kila wakati. Hali hiyo iliwafanya wazazi wake wafurahi na kumnunulia zawadi nzuri kila baada ya kupokea matokeo yake shuleni.





    Zawadi aliyoipenda zaidi kuliko zote ni mbwa wake mdogo mwenye manyoya mengi aliyepewa na mwalimu mkuu wa shule yake mara baada ya kuhitimu shule ya awali na kufanya vizuri kuliko watoto wote shuleni pale. Hii iliongeza ari yake ya kufanya vizuri zaidi hata katika masomo yake ya shule ya msingi na sekondari.

    Bidii yake ilimfanya apendwe zaidi na Walimu na baadhi ya wanafunzi walijitahidi kuwa karibu naye ili wapate kujifunza siri ya mafanikio yake. Maisha yalienda hata alipomaliza shule ya msingi na kujiunga na sekondari alikuwa tayari ni binti mwenye mvuto aliyekuwa anapendeza. Kuchanua kwake kuliandamana na matatizo makubwa maana ilikuwa ni katika mwaka 1939 akiwa na miaka kumi na tano baba yake alikuwa ni miongoni mwa watu waliotakiwa kwenda vitani huo ulikuwa ni mwanzo wa vita kuu ya pili iliyoongozwa na Adolph Hitler.

    Habari hiyo ilimsikitisha sana Matlyer wakati alipohadithiwa na mama yake siku alipokuwa akirudi nyumbani kwa likizo fupi. Machozi yalikuwa yanamtiririka kwa uchungu akimlilia baba yake. Kamwe hakupenda kazi ya uanajeshi aliyokuwa akiifanya baba yake. Alijua wakati wowote ni wakati wa hatari kwa mwanajeshi yeyote na hivyo hakupenda kumwona baba yake akiingiia katika matatizo.

    Mama yake alimbembeleza na kumtia moyo kuwa baba yake angerudi mzima na kuungana nao tena. Pamoja na hayo bado maisha yalienda vibaya kwa Matlyer kutokana na kumkosa baba yake. Baada ya wiki mbili katika mji wa Rhine kuliangushwa bomu lililoharibu eneo kubwa ikiwepo Shule ya Eckernforde Internatinaol School. Wanajeshi wa Kiingereza waliingia katika mji huu wakichanganyika na Wanajeshi wa majeshi kutoka katika nchi ya Hispania na Urusi.

    Majeshi ya Ujerumani chini ya chama tawala cha NAZI chini ya mtawala Dikteta Adolph Hitler yalikuwa yameufunika mji kwa wingi wake wakienda huku na huko kupambana na maadui zao. Ujerumani yote ilikuwa imechafuka lakini baada ya wiki chache walifaulu kuvirudisha nyuma vikosi vya wanajeshi kutoka mataifa mbalimbali hadi kuwatoa katika mipaka ya ujerumani. Pamoja na bidii hiyo lakini katikati ya vita ile wanajeshi wengi wa Kijerumani waliuawa sambamba na wananchi wengi pamoja na nyumba na mali zao kusambaratishwa kwa mabomu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Watu waliishi kwa mashaka makubwa sana katika nchi hiyo japo hotuba za Adolph Hitler zilikuwa za kuwatia moyo na kuwafanya wajione kuwa wao ni Taifa lenye uwezo mkubwa duniani. Taarifa za habari zilizokuwa zikitoa habari sahihi za matokeo ya vita ya kila siku kwa wananchi ziligeuzwa mara moja na kutoa habari za uongo. Vyombo vya habari vilitangaza kwamba Majeshi ya Ujerumani yalikuwa katika harakati za kusafisha miji kwa kuwaondolea mbali wanajeshi kutoka katika nchi maadui. Habari za mauaji yaliyokuwa yakitangazwa zilikoma mara moja na badala yake amani na ushindi ndizo zilizotawala katika vinywa vya watangazaji na waandishi wa habari. Habari hizi ziliwafanya watu wapate faraja kwa muda lakini wengi wa wananchi walipata wasiwasi kuhusu ndugu zao waliokwenda vitani na sababu iliyowafanya wasirudi hata baada ya vita kutulia kwa muda. Baadhi ya wanajeshi walirudi nyumbani japo ilikuwa kwa muda mfupi na hii iliwapa wasiwasi familia ambazo hazikuwaona wapendwa wao na ndugu zao wakirudi.

    Wasiwasi ulitanda kwa Matlyer na mama yake kwa kutokumwona baba yao. Hata pale walipoambiwa kuwa wanajeshi wengine walikuwa katika Operation ya kuwasafirisha Wayahudi kwenda Mpakani mwa Ujerumani na Urusi maeneo ya Sobibo bado hawakutulia. Habari ile ya wanajeshi wa Kijerumani kuwasimamia Wayahudi kwenda kwenye matanuru ya Gesi huko Shokoa zilikuwa za kweli lakini hazikuwapa familia ya akina Matlyer nafuu ya kutokumuwazia baba yao.

    Wanajeshi wengi wa ujerumani walipitia katika maeneo matatu walipokuwa wakielekea vitani. Maeneo hayo ni pamoja na Msitu mweusi ambapo kuna mlima mrefu sana uliofunikwa na msitu huo. Bonde la mlima huu kwa upande mmoja wa ujerumani lilikuwa katika mji wa Rhine, na kwa upande mwingine Ulipakana na Uswisi na ufaransa kwa upande wa kasikazini mwa mlima. Katika mlima huu wenye jina la msitu mweusi vilikuwepo vikosi zaidi ya vinne vya majeshi ya Kijerumani. Lakini kwa bahati mbaya ni kwamba majeshi ya maadui wa ujerumani nayo yalijibana kando ya msitu huu kwa ujumla vita ya msituni ililipuka katika eneo hili kutokana na kukutana kwa mahasimu hao wa kivita.

    Kwa upande mwingine majeshi ya Ujerumani yaliyosifika kwa kuwa mengi sana kuliko majeshi yoyote katika ulaya yalipiitia katika mto Rhine. Mto huu ndio mkubwa katika ulaya na ulipita katikati ya msitu mkubwa uliopakana na msitu mweusi kwa upande wa kusini. Mto huu una kina kirefu na maji yanayoenda kasi. Wanajeshi wa majini walipitia katika mto huu na wakati mwingine majeshi ya maadui hupitia hapa na mashua zao ndogo wakiingia kinyemela mjini kupitia msitu uliouzunguka mto huu.

    Lakini kutokana na kushtukiwa majeshi hayo ya maadui mara nyingi hutekwa na kupatiwa mateso makali na baadaye walikufa kwa mateso makubwa. Ulinzi uliimarishwa na kuufanya mto huu kuwa kama sehemu maalum iliyotumiwa na jeshi la kujenga nchi ya ujerumani. Kwa namna ya kipekee baada ya kuanza vugu vugu la vita vya pili vya Dunia majeshi mengi ya Kijerumani yalipitia katika mto huu na katika msitu mweusi ili kuwakabili maadui zao kirahisi.

    Mto Rhine unaosifika kuwa mto mkubwa katika Ulaya. Mto huu uko Nchini Ujerumani.

    Hata baba yake na Matlyer aliyekuwa askari wa majini alipitia katika mto huu akiwa kamanda mmojawapo ya kikosi hatari cha jeshi la Ujerumani. Kwa ujumla vikosi hivyo vya askari wa majini huutumia mto huu kusafiria mpaka kwenye ziwa Konstanz ambamo huingia kwenye manowari zao ndogo kwa ajili ya kuwapeleka katika mipaka yote ya Ziwa hilo lenye ukubwa wa eneo la km.564 lenye kina cha mita 254. Jina la ziwa lilichukuwa jina la mji unaopakana nalo ambao ni Konstanz. Mto Rhine hupeleka maji yake katika ziwa hili ambapo mito mingine miwili mikuu ya Ujerumani pia humwaga maji yake katika ziwa hili kubwa.

    Hili ndilo Ziwa Konstanz Lililoko nchini Ujerumani linalopakana na uswisi pamoja na ufaransa.

    Taarifa zilizopatikana muda mfupi kabla ya wanajeshi waliorudi nyumbani kwa muda mfupi zilizua huzuni kubwa sana kwa familia ya Matlyer Ardoph. Ni taarifa ambazo familia hii ilitamani kuzibadilisha zisiwe kweli lakini ilikuwa haikuwezekana kabisa. Ukweli wa taarifa zile ulihusu kifo cha askari kiongozi wa kikosi cha majini Ardolph. Kifo hiki kilichotokana na kupigwa risasi ya tumbo na mmoja wa Askari kutoka Bulgaria.

    Baada ya kifo cha kiongozi huyu shujaa kikosi chake kilisambaratishwa na baadhi yao kutoroka akiwepo rafiki mpendwa wa Ardolph aitwaye Chelliphy. Huyu ndiye hasa aliyeleta taarifa hizo za kusikitisha kwa mke wa Ardolph na mtoto wao wa pekee Matlyer. Baada ya kupata taarifa hizi Matlyer alizimia na kusababisha mama yake mzazi aingie katika kazi ya ziada huku akiwa na mzigo mkubwa wa huzuni moyoni mwake kwa ajili ya mumewe mpenzi.

    ***

    Pigo alilolipata baada ya kupata habari za kifo cha mumewe mpenzi lilikuwa kubwa sana! Moyo wake ulipoteza mapigo kadhaa na kusababisha presha ya kushuka kushika nafasi katika mwili wake. Tatizo hili lilizidishwa na hali ya binti yake Matlyer kuwa kitandani kwa zaidi ya wiki bila kushtuka. Uchungu usioelezeka ulikuwa katika moyo wa mama huyu akiwa hajui mahali pa kumpeleka binti yake.

    Tangu vita ianze kumekuwa na tatizo la kupata huduma ya hospitali kutokana na vituo vya afya kubomolewa na mabomu wakati wa vita. Hospitali yao kubwa iliyokuwa katika mji wa jirani wa Rhine ilikuwa karibu sana na Shule ya Eckerniforde International School.

    Wakati Shule hiyo ilipatupiwa bomu Hospitali hiyo nayo ilishika moto kwani nyaya za umeme zilizokuwa katika shule ile ziliunganika na hospitali ile. Baada ya kulipuliwa zilikwenda kuwasha transfoma lililokuwa nje ya Hospitali ile kubwa nayo iliwaka moto kutokana na mlipuko wa trasfoma hilo. Habari hiyo hakuikumbuka mapema mama yule ilikuwa hadi alipombeba binti yake na kumwingiza kwenye gari na kuzunguka naye kutoka Dormagen mpaka mji wa Rhine kutafuta Hospitali au Zahanati ili bintiye apate matibabu.





    Hali ilikuwa tofauti sana ila alipata zahanati ya mtu binafsi ambayo haitoi nafasi ya kulaza wagonjwa daktari alimpa dawa na maelekezo ya jinsi ya kumtundikia binti yake drip la Glucose baada ya hapo amtundikie Dripu jingine la kumwongezea maji. Maombi yake kwa ajili ya kupatiwa daktari anayejua kufanya mambo hayo yote yalipata majibu kwa kupewa nesi ambaye walikwenda wote hadi nyumbani kwake. Huko nesi yule alifanya yale yote katika siku nzima. Ambapo baada ya maasaa manne alikuwa tayari amemwondolea dripu la Glucose na kumwekea la kumwongezea maji mwilini kisha akaondoka.

    Usiku wa manane Matlyer alishtuka na kuamka. Hali yake ilikuwa ni dhaifu sana lakini alifurahi kumwona mama yake akitabasamu. “Mwanangu nafurahi sana kukuona umeamka. Pole kwa yote ila usijiumize kwa sababu yote haya Mungu ndiye amepanga. Hatuwezi kuvuka hapa kwa kulalamika kutokana na tatizo hili lililotokea.

    Kumbuka maisha leo yapo katika dunia hii lakini baada ya hapo kila mtu hufa. Hakuna cha ajabu kwa baba yako kufa maana hata sisi tutakufa tu. Ila uchungu unabaki kuwa ametuacha wapendwa wake wakati bado tunahitaji uwepo wake.”

    Alisema mama Matlyer kwa utulivu sana uliochanganyika na uchungu. Alijitahidi kuwa na uvumilivu wa ziada kusudi kumfanya binti yake asijisikie vibaya lakini moyoni mwake alikuwa ameumia kwa namna isiyoelezeka. Maisha ghafla yalibadilika na kuwa maisha ya kutokuwa na uhakika wa baadhi ya mambo. Kwa upande wa fedha zilikuwa hazitoshi, japo kwenye Fixd account kulikuwa na mali ya thamani kubwa iliyowekwa na baba yake Matlyer, mali aliyoipata akiwa safarini nchini Tanzania. Vilikuwa ni vipande vitatu vya madini aina ya Tanzanite vilivyokuwa na thamani kubwa sana, alivyoviokota nje kidogo ya jiji la Arusha vikiwa vimefungwa katika kitambaa kichafu. Safari yao ya kiutalii ilipokamilika walirudi nchini ujerumani. Ikiwa ni siri yake baada ya kuokota vipande hivyo vya madini ya thamani sana aliyaweka kwenye Bank ili yatunzwe, kabla ya kuyauza. Kifo chake kiliweka utata wa namna ya kuyatoa madini yale na kuyauza. Fedha zilikuwa zinaisha kwenye akiba yao na hali ya sintofahamu ilikuwa imegubika familia hii ya watu wawili.

    Kwa Matlyer alifikiria sana masomo na jinsi ambayo ndoto zake zilivyokatizwa kikatili. Moyo wake uliuma sana kwa mawazo ila naye alijaribu kujikaza ili asimtie mama yake simanzi. Kila mmoja kati yao alijua namna mwenziye alivyobeba uchungu moyoni hivyo walijitahidi kila mtu kutolalamikia hali ile japo uchungu na kilio chao vilikuwa ndani kwa ndani.

    Kupata nafuu kwa Matlyer kulikuwa kama kulikotoa nafasi kwa mama yake kuibua ugonjwa wa moyo na kukakamaa mwili. Hali hii ilifuatiwa na kifo baada tu ya siku tano tangu apate ugonjwa huo. Pigo hili la pili lilikuwa kubwa sana kiasi cha kumfanya asijue la kufanya. Taarifa za kifo cha mama yake alizitoa kwa kuzunguka mitaani huku akilia na kupaaza sauti yake kuwa mama yake amefariki dunia.

    Watu walikusanyika wachache walioguswa na taarifa hiyo na taarifa za msiba zilifanywa baada ya kusambaza matangazo kwa njia ya simu, kwenda kwa ndugu zao waliokuwa nchini Uswisi na Ufaransa. Lakini hakuna aliyetokea japo walisema wangefika siku ya pili yake. Siku ya tatu mwili wa marehemu ulikuwa umeshaanza kuoza ilibidi wamzike bila kuwepo kwa ndugu zake. Wakati hayo yanafanyika Matlyer alikuwa yupo hapo kama sanamu tu maana mambo aliyokuwa akiyafanya hayakuwa ya mtu mwenye ufahamu sahihi. Baada ya kukamilisha taratibu za mazishi Matlyer alikuwa haonekani tena. Alikuwa amewatoroka watu na kwenda kusikojulikana.

    ***

    Alishtuka na kujiona yupo mbele ya Sister wa kikatoliki. Chumba alichokuwa kilikuwa kipana chenye vitanda vitatu na baadhi ya vyombo vya matumizi ya chakula vikiwa kwenye meza kubwa pia. Yule Sister alikuwa akimuuliza maswali mengi lakini yanayofanana na yale wanayoulizwa watu wasio na akili timamu. Kitu kilicho mshtua yule Sister ni pale yule aliyekuwa akimuuliza kumwangalia kwa kumshangaa na badala yake kumjibu kiusahihi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hali ile ikamfanya aone kuwa yule aliyekuwa anaongea naye yuko sahihi na alihitajika kuchukuliwa vipimo ili kudhibitisha hilo. “Sister Kwani hapa ni wapi? Na nimefikaje huku?” Aliuliza msichana yule ambaye tangu afikishwe hapo alikuwa hajui hata jina lake. “Kabla sijakujibu ulifikaje hapa naomba niambie jina lako unaitwa nani?”

    Aliuliza yule sister huku akiwa makini zaidi katika maneno yake kwa kujua kuwa fahamu za msichana yule zilikuwa zimerudi. “Jina langu ninaitwa Matlyer Ardorph ni binti pekee wa baba yangu na mama yangu. Lakini baba yangu alikufa kwenye vita na siku si nyingi kutoka pale mama yangu naye alikufa akiwa mikononi mwangu na kuniacha peke yangu.” Alisema hivyo Matlyer huku machozi yakimdondoka.

    Baada ya kusikia maneno hayo sister yule alinyanyuka na kumkubatia Matlyer na kumsihi anyamaze kulia kwani alikuwa kwenye mikono salama kabisa. Baada ya kumwambia hivyo alimtayarishia chai na kumtaka akaoge kisha wajiandae kuondoka katika kituo hicho. Wakati alipokwenda kuoga Matlyer yule Sister alifanya utaratibu wa kuondoka kwenye kituo kile na baadaye walipitia kwa daktari.

    Daktari alimhakikisha Matlyer akadhibitisha kuwa ni mzima na kumpa ruhsa kuondoka na Sisetr yule. Huko ndipo alipopewa historia kamili ya mahali alipokutwa kabla ya kuletwa pale kwenye Hospitali. Ulipatikana kando ya mto Rhine ukiwa unaongea peke yako kama uliyechanganyikiwa. Aliyekuwa mwalimu wako alipelekewa taarifa na wanafuzi waliokuona.

    Mwalimu Marlerune Luther ndiye aliyekuleta hapa baada ya kukaa na wewe kwa wiki nzima nyumbani kwake. Tangu akulete hapa umepita mwaka mmoja na nusu. Sote tunashukuru mimi na wewe kuwa umekuwa mzima sasa. Alisema hivyo Sister akiwa kwenye chumba chake mahali alipopanga kufanya mazungumzo ya kina na Matlyer. “Mwalimu wangu yupo wapi sasa?” aliuliza Matlyer kwa shauku. “Nimempigia simu na kumtaka aje amesema anaanza safari kutoka Rhine na atafika hapa mchana wa saa saba.” Alijibu Sister yule aliyejitambulisha kwa jina la Sister Ruthrene Martias.

    ***

    Matlyer alianza masomo yake nchini ufaransa katika mji mkuu wa Paris kwa gharama za kanisa Katholic. Hapa alikazania masomo yake ya Sekondari na baada ya hapo alijiunga katika chuo cha udaktari. Alisomea maswala ya tiba kwa ajili ya watu vichaa na jinsi ya kuwasaidia mpaka wapone. Mguso wa kufanya hivyo ulitokana na matatizo aliyoyapitia katika maisha yake. Majibu ya Sister kuwa alipata mchubuko wa ubongo baada ya kupata matatizo makubwa mfululizo katika maisha yake vilimfanya awaone vichaa wengi kuwa shida yao inawezekana ikawa inatokana na matatizo kama aliyoyapitia yeye.

    Katika maisha yake alikusudia kuwahudumia wagonjwa wa aina hiyo katika maisha yake yote yaliyobakia. Baada ya kuhitimu masomo yake alijipanga kuanza kituo cha kuhudumia wagonjwa katika ufaransa. Kiasi cha fedha kilichopatikana baada ya kupata thamani ya madini yaliyowekwa Fixid account katika bank ya Internatinal Busness Bank kilitosha. Bank hii iliyopo mjini kwao Dormagen huko Ujerumani iliamua kununua madini yale yenye thamani kubwa. Matlyer aliamua kuanzisha Vituo zaidi ya vinne vya kuhudumia watu wenye matatizo ya akili. Baada ya miaka mitatu Vituo hivi vilitambuliwa na Serikali kiasi cha kupasishwa kuwa Hospitali kamili.

    Hali ya ustawi wa hospitali hizi iliendelea baadae akaamua kujenga vyuo ili aweze kuwapa watu mafunzo ya namna ya kuwahudumia wenye matatizo ya akili. Alikusudia kufungua Hospitali hizo katika nchi nne. Uswisi, Ujerumani, Ufaransa na nchi mojawapo katika Afrika. Mwisho wa mikakati yake hiyo alikuja kuanzisha Hospitali katika nchi ya Kenya iliyokuwa ikiwahudumia wagonjwa kwa namna ambayo ni tofauti kabisa na mahali popote duniani. Kila mgonjwa alikuwa na chumba chake na Daktari wa kumhudumia kwa karibu sana huku akimjali pamoja na kuongea naye kama rafiki. Zaidi ya hapo alikaribisha watumishi wa Mungu ambao walikuwa wanapewa nafasi ya kuwaombea wagonjwa wale.

    Utaratibu ulikuwa unatolewa kwa watumishi wanaohitaji kuwafanyia huduma wagonjwa wawe kutoka katika dini yoyote walipewa masharti na njia nzuri sana ya kuwachukulia wagonjwa wale. Hii ilikuwa ni nzuri sana inayomfanya mgonjwa baada ya kurudiwa na fahamu zake asijihisi kudhalilika kwa kuona kuwa alikuwa kwenye Hospitali ya watu wenye matatizo ya akili. Sifa za Hospitali hizi zilikwenda mbali sana katika Nchi nyingi Duniani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Matlyer alikusudia kuwafundisha madaktari wengi kote duniani. Maono yake yalikuwa kufungua matawi kote duniani kupitia wanafunzi waliotoka katika vyuo vyake. Kila Hospitali ilikuwa na chuo kilichokuwa kinachukuwa mamia ya wanafunzi. Baada ya miaka mitatu kilitoa madaktari na kupokea tena wanafunzi. Mpaka kufika 21/04/2012. Daktari maarufu duniani kwa magonjwa ya akili Matlyer na mumewe Martin walifariki dunia kwa ajali ya ndege wakitokea kwenye ziara ya kikazi nchini Greece.

    Dr. Matlyer Ardolph amefariki akiwa na miaka mingi lakini akiwa ameacha historia kubwa sana katika dunia hii. Hospitali zake zilikuwa zinaendelea huku wanawe wawili Mark Martin na Matlida Martin. Walikuwa makini sana katika kusimamia kazi hiyo kwa utaratibu uliowekwa tangu mwanzo na mama yao.







    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog