Simulizi : Upendo Kutoka Sayari Nyingine
Sehemu Ya Nne (4)
Na mara hiyohiyo Seba alishtuka usingizi kisha anasikia kengele ya mlangoni ikilia kuashiria kuwa kuna mtu anabisha hodi. Kwa uchomvu wa usingizi alinyanyuka kivivu kisha aliminya kifufe cha kuondoa lock mlangoni na mgeni huyo baada ya kuona taa ya kijani pale mlangoni alisukuma mlango na kuingia ndani. “Habari za mapumziko bwana Seba pole kwa kukukatishia mapumziko yako rafiki.” Alisema mr. Njoroge ambaye ni rafiki yake na Sebastian na pia walikuwa wanasoma wote chuoni hapo.
“Usijali rafiki yangu mambo vipi una jipya?” alisema Sebastian wakati akijiinua kitandani na kukaa. “Nimekuja kukuomba kuwa tuungane kesho kwenye sherehe ya harusi ya mdogo wangu Chris itakayofanyika kwenye ukumbi wa Rick Rose Hotel.” Alisema Njoroge huku akinyoosha mkono kumpa card ya mwaliko.
“Uliwahi kuniambia wiki kadhaa nyuma kuhusu jambo hilo ila sikujua kuwa ni kesho. Itafanyika kuanzia saa ngapi?” Aliuliza Seba. “ndoa itafungwa kuanzia saa kumi jioni lakini sherehe itafanyika kuanzia saa tatu usiku hadi saa saba. Alisema Njoroge. “Usijali kuhusu hilo tutakuwa pamoja. Ila rafiki yangu umenistua kwenye ndoto nzuri ajabu?” Alisema Seba kwa shauku kubwa. “Ndoto gani hebu nidokeze.” Alisema Njoroge huku akijiweka vizuri kwenye sofa ili kusikia kuhusu ndoto hiyo.
“Nimeota ndoto ambayo imenipa faraja sana nikawa kama niko kwenye uhalisia wa hicho nilichokiota.” Alisema Seba kwa unyonge huku akionekana kama bado ana uchomvu wa usingizi. “Eehee, Nakusikiliza rafiki yangu.” Alisema Njoroge kwa shauku ya kusikia kuhusu ndoto hiyo. “Nilikuwa kwenye mandhari nzuri sana kule kwenye kijito cha maji juu ya lile jabali lililopakana na msitu. Nilikuwa na mchumba wangu Judith tukipanga mambo yetu ya maisha.
“Hekima yake na busara katika mazungumzo yake zilikuwa ni zilezile alizokuwa nazo kabla hajapata tatizo. Wakati mipango ya maisha inaendelea muda huo huo ninashtuka ndio na wewe unapiga alamu mlangoni.” Alisema Seba kwa unyonge kidogo. “Hongera kwa ndoto hiyo na pole kwa kukatisha muendelezo wake.” Alisema Njoroge huku akiinuka na kwenda kwenye jogofu ili achukue kinywaji, alijichagulia malta guiness ya kopo kisha akataka kufunga jokofu “Niletee na mimi kopo la Redbull tafadhali.” Alisema Seba na njoroge alichukuwa hicho kinywaji na kumletea. huku akijifungulia na kupiga funda moja. “Rafiki yangu nimekupongeza kwa ndoto hiyo kwa sababu ina dalili zote za kutimia. Ninajua taabu unayoipata moyoni mwako kwa miaka mingi juu ya mchumba wako.
Nataka nikutie moyo kuwa kila mtihani una mwisho wake. Kumbuka ndoto huletwa na aidha kile mtu anachokiwazia sana kila siku, wakati mwingine ni taarifa ya Mungu juu ya jambo fulani litakalotokea mbele yako. Sasa hii ni taarifa ya jambo hilo na huenda likatokea siku si nyingi kutoka sasa.” Alisema Njoroge huku akimwangalia kwa umakini mkubwa rafiki yake kama maneno hayo yanamwingia akilini. “Nimekuelewa rafiki yangu na nina imani mwisho wa safari hii ndefu ya kumsubiri mchumba wangu twende tukafunge ndoa umefika. Ningetamani sana kesho kwenye sherehe ya ndoa ya mdogo wako ningehudhuria na mchumba wangu Judithi.
Naamini atakuwa mzima tu na ndio dua yangu ya kila siku.” Alisema Seba huku machozi ya huzuni yakimtoka na wakati huo huo akiwa ameangalia mahali pamoja tu kama anayetembelea kihisia kule walikotoka na mchumba wake. Njoroge alipata huzuni pia na kutokwa na machozi. “Tufanye maombi kwa ajili ya mchumba wako rafiki yangu.
Nina imani maombi yetu yatasikiwa na Mungu atatenda jambo tunalolitazamia kwa Judith.”Alisema Njoroge kwa shauku na imani kubwa sana. Mara wote wakapiga magoti na kuomba Mungu kwa ajili ya uponyaji wa Judithi. Baada ya maombi waliinuka na kuagana Njoroge akaondoka na kumwacha rafiki yake akiendelea kutafakari
10
Safari yenye mategemeo.
Urafiki wake na watu wa idara mbalimbali uliweza kumpatia faida nyingi katika maisha yake. Katika faida ambazo amefanikiwa kuzipata ni pamoja na hii ya kupata ufumbuzi juu ya swala ambalo lilimtatiza yeye pamoja na baadhi ya watu nyuma yake. Ilikuwa ni sherehe ya aina yake aliyoifanya moyoni mwake kwa kufaulu kupata fununu ya kile kinachotafutwa kama lulu kote nchini na hata nchi za Afrika.
Kuzima kwa vyombo vya habari katika kutangaza jambo hili nyeti kuliwafanya wanahabari wengi nje ya Tanzania nao kukaa kimya. Hii ilionyesha kuwa watu hao walikuwa wanategemea kupata habari hizo kupitia vyanzo vya habari hizo kutoka ndani ya nchi ya Tanzania. Hii ndio sababu habari hizo zikawa zinashabihiana kwa kila kitu.
Ukimya wa vyombo vya habari nchini kuhusu yule kijana tajiri pamoja na mpenzi wake ambaye ni meneja wa kampuni ya Usafirishaji ulikuwa na mshindo mkuu. Akiwa juu ya ndege Andrew alikuwa akitafakari mambo mengi sana hasa kujaribu kutafakari jinsi atakapoianza kazi yake. Umakini ndio uliokuwa mwongozo wake wa kwanza katika kila jambo maana hakutaka kuharibu katika swala hili nyeti.
Ndege ya shirika la ndege la nchini Kenya ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Jommo Kenyata mnamo saa kumi na nusu jioni. Na wasafiri walitoka taratibu wengine wakiwa wanasubiriwa na wenyeji wao mara tu baada ya ukaguzi, na wengine wakiwa wanasubiriwa na Madreva Taxi kwa ajili ya kuwapeleka mahali wanapotaka. Kenyata View Hotel ni Hoteli ya kitalii iliyopo nje kidogo ya viwanja vya Uhuru Park. Ni hoteli ya nyota tano yenye sifa zinazopendwa na watalii wengi.
Hoteli hii ndiyo aliyoichagua Andrew na alilipa kiasi kikubwa kwa siku. Pamoja na bei yake kuwa kubwa ambayo malipo yake yalifanywa kwa Dola za kimarekani, lakini Andrew alilipa kwa wiki nzima ambapo alijipangia kuwa ndio muda muafaka ambao atakamilisha kazi yake iliyomleta katika nchi hiyo.
Baada ya kupanga vitu katika chumba chake alijipumzisha kidogo kisha akaandaa vifaa vyake vya kazi na muda wa saa moja na nusu jioni alitoka na kutembea mitaani. Huko mitaani alijipatia rafiki aliyempata kwa ofa ya kinywaji katika mgahawa mmoja.
Rafiki huyu naye hakuwa mchoyo wa habari kwani alipoulizwa juu ya Hosptal ya Pyschological Mantal Hospital alitoa maelekezo vizuri na kufanya wepesi wa kazi ya mpelelezi huyo. Baada ya kupata mwanga kuhusu mahali alipopahitaji alirudi hotelini na kupanga mipango kabambe ya jinsi ya kuingia mahali pale na namna atakavyoweza kupata habari husika kuhusu Seba na mwenzi wake Judith Martin.
***
Ni mazingira tofauti sana kwake! Hajawahi kukutana na mazingira ya aina hii ya Hospitali. Ilikuwa ni kama nyumba ya matumizi ya kiofisi kwani kila chumba kilionekana kama sehemu ya ofisi na watu waliopo walikuwa katika hali ya usafi wa hali ya juu na mavazi yenye hadhi ya kiofisi hasa. Tofauti kidogo tu zilizoonekana ni kwa baadhi ya watu walioonekana kama wana matatizo ya akili. Hii ilidhibitishwa na mtu mmoja aliyemjia na kumsimamia huku akimwangalia kwa kumshangaa kisha akamwongelesha kwa lugha isiyojulikana kuwa ni ya kabila gani. Mwanamme huyo mrefu mwenye mwili uliojazia na mweusi kama kipande cha mpingo alimtisha hasa kwa macho yake mekundu.
Wakati Andrew akitafuta namna ya kujitetea iwapo yatatokea matata zaidi alimwona jamaa mwingine akija kwa haraka na kumsogelea yule mtu mwenye macho mekundu akamshika bega kisha akageuka na wote wakaongozana kuondoka katika eneo lile. “I am so sorry brother!” Yule jamaa mwingine aliyekuja kumchukuwa yule wa macho mekundu alimwambia Andrew neno hilo wakati akiondoka na mtu wake. “Don’t worry.” Alijitutumua kujibu huku akiwa hajui ikiwa varangati lingeanguka pale lingetafsiriwaje na watu wakati yeye alikuwa ni mgeni kabisa maeneo yale na ilikuwa bado hajaonana na mkurugenzi wa shirika lile.
Baada ya kuondoka watu wale ndipo akadhibitisha kuhusu Hospital ile ya kipekee ambayo alipata habari yake tangu akingalipo nchini kwake Tanzania. Hii ni hali iliyomshangaza sana Andrew huku akiendelea kuyaangalia mazingira ya mahali pale, kisha akaondoka kwa mwendo wa taratibu kutoka pale alipokuwa, akiliendea jengo lililokuwepo mbele yake.
Mbele kidogo alitokea mama mmoja wa makamo kwenye mlango wa jengo lile akionekana mwenye haraka. “Habari za asubuhi dada?” aliitupia salamu hiyo kwa mashaka kidogo ya kutopata jibu kutokana na haraka ya mwanamke yule. “Habari ni musuri sana kaka yangu karibu.” Alijibu dada yule kwa Kiswahili cha Kikenya lakini kwa uchangamfu sana.
“Asante mimi ni mgeni maeneo haya nina shida ya kuonana na uongozi wa Hospitali hii.” Alisema Andrew. “Unaweza kwenda kwenye jengo hilo kubwa lenye bendera kisha ingia ndani utakutana na katibu Muhtasi anatakuonyesha ofisi ya Mkurugenzi ilipo.” Alisema yule mwanamke na kwa tabasamu pana lililoufanya uso wake mweusi upendeze zaidi pale meno yake meupe yenye mwanya yalipotokeza.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Asante dada.” Alisema Andrew huku akiachana na mwanamke yule mwenye umbo nene na urefu wa wastani akiendelea na safari yake. Ndani ya jengo hili kulikuwa na utulivu wa aina yake uliopambwa na kiyoyozi chepesi kulingana na hali ya hewa kuwa ya joto kiasi katika majira yale yanayoendea mchana. Watu kadhaa walionekana wakiwa katika harakati za shughuli aidha kwa kwenda hapa na pale ilimradi kila mmoja alikuwa na mambo yake ya kutimiza katika siku hiyo. Baada ya kuingia alipokelewa na maandishi yaliyobandikwa kwa ustadi mkuu ukutani yaliyosomeka “MAPOKEZI”
Bila kusita Andrew alielekea mapokezi ambapo alimkuta dada mrembo aliyekuwa ameketi nyuma ya meza kubwa. “Karibu sana kaka yangu.” Alisema dada yule kwa sauti iliyokaribia na ile ya kinanda. “Asante mrembo pole kwa kazi.” Alisema Andrew huku akijisogeza na kuegemea kwenye kaunta alipo yule binti mrembo. “Nashukuru sana naweza kukusaidia tafadhali?”
Alijibu yule dada huku akimwangalia Andrew usoni akiwa hajasahau lile tabasamu lake la awali. “Nahitaji kumwona Mkurugenzi.” Alisema Andrew kwa shauku. “Una miadi ya kuonana naye leo?” Aliuliza dada wa mapokezi. “Kwakweli sina miadi yoyote na Mkurugenzi ila kuna jambo muhimu la kuongea naye leo.” Alisema Andrew. “Nimwambie nani anataka kuonana naye?” Aliuliza yule dada huku akiwa kashikilia simu ya mezani huku akibonyeza namba kadhaa.
“Mwambie Andrew Charles wa shirika la habari la UWARIDI kutoka Tanzania.” Alijibu Andrew kisha akatulia huku akiangalia baadhi ya mapambo yaliyoko ukutani hapo. Yule dada aliongea na mkurugenzi akimjulisha kuwa ana ugeni kutoka Dar es Salaam Tanzania. Kisha baada ya kuongea hivyo alirudisha simu mahali pake. “Nenda kamwone Mkurugenzi utaongozwa na mlinzi yule pale. Nafurahi kukutana na mwandishi wa habari mashuhuri kutoka katika shirika la habari la UWARIDI. Kiufupi ni kwamba mimi ni mpenzi wa habari zenu zinazofanyiwa uchunguzi wa kina, pamoja na makala za kusisimua, bila kusahau hadithi tamu kama vile Mkimbizi iliyoandikwa na Hussein Tuwa na barua kutoka jela ya Ibrahim Gama, Run niger run ya Hussein Kulindwa na The beach Man (Mtu wa Ufukweni) ya mwandishi Andrew Mhina na nyinginezo nyingi.”bila kusahau kazi za Beka mfaume, Sudi Nyang’oro, Husein Wamaywa, Raymond, Mwigizi, Kijogoo na wengine.
Alisema dada yule kwa shauku ya aina yake na kutaja baadhi ya mambo yanayomfurahisha ya Shirika hilo la habari. “Duh! Umekariri majina ya waandishi kama vile unasoma kwenye karatasi!” Alisema Andrew kwa mshangao. “Mmmh! Ni kwa sababu ndio rafiki zangu kila siku ninawasoma kwenye Kona ya Riwaya. Wengine vitabu vyao ninavyo kwenye Library yangu.” “Hongera mrembo nashukuru pia kuona kuwa kazi zetu zinawafikia na mnazifurahia.” Alisema Andrew huku akielekea alipo mlinzi yule na kabla hajamfikia sauti ya dada yule ikasikika nyumba yake: “Huyo ni mgeni wa Mkurugenzi.” Mlinzi yule alitikisa kichwa na kumwongoza Andrew hadi kwenye ofisi ya Mkurugenzi.
Ilikuwa ni ofisi nzuri ya aina yake na yenye ukubwa wa vyumba viwili vya kawaida na safu ya viti ikiwa imepangwa vema ilionekana kama ofisi hiyo ilikuwa ikitumika pia kwa vikao maalumu. Meza kubwa ya kioo ilikuwa imepambwa vilivyo na mafaili mengi pamoja na maua yaliyozungushwa pembezoni mwa meza hiyo kubwa na nzuri ya kifahari.
Kando kidogo ya meza hiyo kulikuwa na jogofu kubwa la wastani na shelfu kubwa lililofungwa kwa kufuli aina ya Solex ilionekana kama ni mahali pa kuhifadhia nyaraka za muhimu au fedha kabla hazijapelekwa Banki. Nyuma ya meza ile nzuri ya kioo aliketi mwanamke mzuri sana wa kizungu, aliyeonekana wa makamo. Utajiri ulisomeka katika sura yake haikuwa na haja ya kuuliza. “Woow! Karibu sana Andrew! Nimeweza kutajiwa jina lako na katibu wangu na kwamba unatoka nchini Tanzania. Karibu kwetu.” Alisema mwanamke yule kwa uchangamfu. Alikuwa ni mwanamke wa kizungu ambaye umri wake haukuzidi miaka arobaini na tano lakini uzuri wake ukiwa wazi kabisa katika sura na umbo lake.
“Nashukuru sana nimefurahi kuwepo katika ofisi yako nzuri ajabu!” Alijibu Andrew huku akinyoosha mkono wake nao wakapeana mikono kisha akasogea kwenye kiti kilichoko mkabala na meza ya mkurugenzi huyo na kukaa. “Naitwa Matilda ni mkurugenzi wa Hospital hii pamoja na chuo cha Udaktari wa watu wenye matatizo ya akili. Ninakukaribisha katika ofisi zetu.”
Alisema Matlda kwa uchangamfu. Naitwa Andrew Charles natokea Nchini Tanzania na pia niko katika shirika la habari la UWARIDI. Kwa mara ya kwanza nimepata habari juu ya kuwepo kwa Hospitali hii ambayo nchi mbalimbali duniani zimefaidika na huduma zake.
Chuo cha Udaktari cha Psychological Mental Universty ni chuo kinachozalisha madaktari bingwa duniani kwa huduma zilizo bora. Baada ya kusikia maneno hayo ikabidi nije kujionea mwenyewe yale niliyoyasikia. Pia sikusahau kalamu yangu na daftari ili niandike yale nitakayoyashuhudia kwa macho yangu.
Pia kamera yangu ikiruhusiwa kuchukuwa baadhi ya mambo muhimu, itasaidia kuwajulisha watanzania na wasomaji wa magazeti yetu juu ya chuo na Hospitali hii.” Alisema Andrew kwa shauku. “Andrew unakaribishwa sana katika Taasisi hii ya afya na utatembezwa kila mahali ili uone kama kuna kitu kinachotosha kuwaambia watu na kuwaonyesha. Wewe utajua mwenyewe utafanyaje. Wanahabari kwetu ni watu muhimu sana kwa sababu hii ni huduma inayowahitaji watu na watu wanaihitaji.
Kujuana kati ya huduma hii na watu ndilo lengo husika kwa faida ya huduma na ya watu wenye mahitaji na huduma hii.” Alisema Mkurugenzi Matlda na wakati huo huo mhudumu aliingia baada ya Matlda kuminya kitufe cha njano kilichoko mezani. Mkononi mwa mhudumu yule kulikuwa na chano kilichokuwa na soda mbalimbali za kopo pamoja na chupa ndogo ya kahawa na kikombe kimoja.
Mhudumu yule aliviweka mezani vitu vile. “Nikuhudumie nini kati ya hivi?” Bila kujibu Andrew alichukuwa soda ya kopo na kuifungua matlda naye alifanya hivyo. Mhudumu aliwawekea glasi kisha akaondoka. “Nasikia pia kuna Mtanzania yupo hapa anasomea Udaktari?” aliuliza kiuzushi Andrew huku moyoni akiwa na shauku ya kujua habari kamili zinazosubiriwa na vyombo vya habari vya Tanzania kwa hamu kubwa. “Ndio yuko Mtanzania ambaye ni wa kwanza kabisa katika chuo chetu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tunamthamini sana kutokana na dira yake ya kusababisha Taasisi yetu kufungua tawi nchini Tanzania kupitia yeye. Bidii yake na uelewa wa hali ya juu sana vimemfanya afahamu mambo mengi ya msingi kwa Elimu hii ya udaktari. Kwa ujumla tunamshukuru Mungu kwa nafasi hii nyingine ya kupata namna ya kulifikia Taifa linalosifika kuwa na hazina ya amani kuliko mataifa mengi sana duniani.” Alisema Matlda huku akijiweka sawa kwenye kiti chake. “Kwakweli itakuwa ni fahari sana kwa Tanzania kuwa na Hospitali hii na chuo kwani watu wetu watapata huduma nzuri pamoja na elimu ya juu kuhusu huduma hii ya afya ya akili. Ninakupongeza sana mkurugenzi kwa kazi njema sana.” Alisema Andrew kwa shauku. “Nashukuru kwa kila jambo linavyoenda kwa kuwa mwasisi wa huduma hii ilikuwa ndio ndoto yake kuufikia ulimwengu kwa huduma hizi.
Hayo yote yanatokana na Ugumu wa historia ya maisha yake. Kwa habari zaidi nitakupa kitabu chake cha historia mara tu wakati utakapomaliza ziara yako ya kuzunguuka katika eneo hili. Kwa sasa nitakukabidhi kwa watu watakaokupeleka katika maeneo mbalimbali. Na la muhimu kwako ni kwamba inabidi urudishe chumba cha Hotel ulikofikia na kuhamia katika Hotel yetu iliyopo hapa kwa gharama ya Taasisi.
Hii itakupa nafasi ya kuwa huru kuzungukia maeneo haya na nadhani itakuchukuwa siku tatu kuweza kuyatembelea maeneo yote. Sawa?” Alisema Matlda. “Asante sana Mkurugenzi kwa ukarimu wako, naamini baada ya ziara yangu kuna mengi nitaandikia gazeti letu ili Watanzania waone ile hazina iliyojificha jirani tu mwa nchi yao.”
Alisema Andrew huku akijiweka katika mkao wa kuondoka. Mkurugenzi alibonyeza moja wapo ya kitufe katika meza yake na muda usiozidi dakika moja aliingia jamaa mmoja mtanashati na kusimama katikati ya ofisi. “Nimekuja bosi.” Alisema jamaa yule kwa unyenyekevu mkubwa. “Nenda na huyu ndugu kwenye Hoteli aliyofikia achukuwe mizigo yake na umpeleke kwenye Hoteli yetu na kumkabidhi kwa meneja.” Alisema Mkurugenzi kisha akanyoosha mkono Na kukutanisha na wa Andrew wakaagana. Andrew aliondoka mahali pale huku akishangaa sana kwa ukarimu ule.
11
Kujifunga kwa ukurasa wa giza
Ulikuwa ni wakati wa chakula cha mchana watu wote walikuwa kwenye harakati za kujipatia chakula. Bwalo kubwa sana la chuo hicho lilikuwa limejaa wasomi wa ngazi zote. Hapa ndipo wanapokutania watu wa chuo hicho kwa ajili ya kujipatia chakula. Mara wakiwa kwenye mstari wa chakula Sebastian na rafiki yake njoroge walisikia sauti ya mmoja wa wahudumu wa Hopitali ilisikika ikiita jina la Dr. Seba.
Sauti ya kuita haikuwa ya kawaida ilimfanya Seba atoke kwenye foleni alikwenda kwa haraka mpaka kwa mhudumu yule ili kujua kuna tatizo gani limetokea. “Unaitwa na mkurugenzi.” Alisema mhudumu yule. “Ni kwema au kuna tatizo?” Aliuliza Seba akiwa ana wasiwasi kidogo. “Hakuna tatizo ila nimeagizwa nikuite haraka.” Alisema Mhudumu yule wakati akiondoka eneo lile.
Sebastian akashika njia kuelekea ofisini kwa Mkurugenzi. Kabla hawajafika ofisini kwa mkurugenzi walimwona kwa mbali akiwa amesimama nje ya jengo la ofisi yake. Seba alichapusha mwendo huku akiwa na shauku ya kujua ninini kilichojiri. “Woow!” Alisema maneno hayo mkurugenzi baada ya Seba kukaribia mahali alipokuwa. Tabasamu lake lilimwondoa wasiwasi Seba ila shauku ilikuwa kubwa kutaka kujua alichoitiwa ninini? Tabasamu la mkurugenzi wakati Seba alipofika mahali aliposimama lilikuwa linaongezeka. “Nina habari njema sana kwako Seba karibu ofisini.” Asante bosi alisema Seba wakati alipokuwa akiingia ofisini huku akishusha pumzi zake kwa nguvu.
***
Kulitokea kelele za aina yake kutoka katika wodi ya Judith kiasi cha kusikika katika eneo lote la ofisi ya mkurugenzi. Wahudumu wawili aliowekewa wamhudumie walimkimbilia na kutaka kujua kuwa kuna nini kimetokea. “Siamini kama mama yangu umeniacha mwenyewe duniani! Kwanini umekufa mama wakati mwanao bado ninakuhitaji?” Ni maneno aliyokuwa akiyasema Judithi huku akiuomboleza sana kwa kifo cha mama yake. Ilikuwa ni jambo la kushangaza kidogo kwa wale Madaktari lakini mkurugenzi alipoingia wodini aliwatoa wasiwasi.
“Huyu naijua historia yake kwa kuhadithiwa na mchumba wake. Huu ni muujiza wake.” Alisema mkurugenzi na kuzua mshangao kwa mmoja wa madaktari wale. Mmoja wa madaktari hakushangaa kwakuwa alikuwa katika shughuli hiyo kwa muda mrefu lakini mmoja alikuwa ni mgeni na ndio alikuwa akipata mafunzo ya udaktari. “Huyu tayari amepona na yale yaliyompata kwa mara ya mwisho na kumsababishia tatizo la akili yake yanajirudia. Kilichosababisha apate shida hii ni kupokea taarifa za kifo cha mama yake mzazi, kwa hiyo kuzinduka kwake katika tatizo lake hilo lazima kunatokea palepale alipopatia tatizo hilo. Umeelewa Fred?” Alisema mkurugenzi. “Ahaa! Kwa hiyo sasa hivi ndio anapewa taarifa za kifo cha mama yake kulingana na maelezo yako?” Aliuliza Fred kuonyesha kama anaelewa sasa somo hilo.
“Hasa! Kwa wakati huu ndio anapata taarifa za msiba na kwa sababu mbele yake ndipo alipopata tatizo la kutokuwa tena na akili ya kujua nini kinaendelea, ataishia katika kumlilia mama yake na baadae atajitambua na kushangaa mazingira aliyopo.” Alisema mkurugenzi, na wakati huo bado Judith alikuwa akilia na kumwombolezea mama yake mzazi.
Muda wa kama robo saa ya kuomboleza mara Judith alinyamaza kimya kabisa kisha akafumba na kufumbua macho yake na kutazama huku na huku akishangaa chumba kile na watu walioko. Alionyesha woga na mshangao. “Kwani hapa niko wapi jamani?” aliuliza kwa utulivu wa hali ya juu sana. Mkurugenzi alimsogelea na kumshika begani. “Hapa uko nchini Kenya umeletwa kwa ajili ya mapumziko baada ya kifo cha mama yako. Mimi ninaitwa MatIlda. Sijui wewe mwenzangu?”
Alisema Dr. Matilda akitaka kuhakikisha kuwa ufahamu wa Judith umerudi sawasawa na hapo hapo kutoa somo la kivitendo kwa mwanafunzi wake Fred. “Naitwa Judith Martin, ni mtoto wa pekee kwa baba na mama yangu. Ninaye mchumba wangu anaitwa Sebastian Changawe, vipi anazo habari za kuwepo kwangu hapa? Nilipopata ajali alikuwa pamoja na mimi aliniuguza na kunijali sana ila baadaye alipoona nimepata nafuu aliondoka kwenda masomoni Marekani. Ningefurahi kuongea naye kwenye simu ili kumjulisha kuwa kwa sasa ninaendelea vizuri ikiwezekana arudi tufunge ndoa.” Alisema Judith katika kujitambulisha.
“Sawa Judith pole sana muda sio mrefu tutakupa uongee na mchumba wako.” Alisema mkurugenzi. Hapa nimeletwa na baba yangu? Na sasa yupo wapi? ningetamani kumwona.”Alisema Judith akihitaji majibu mengi kwa maswali aliyonayo. “Ngoja tukuitie mtu wa muhimu sana kwako ili mzungumze mengi kuhusu yale yote unayotamani kuyajua sawa?” Aliuliza mkurugenzi. Judith hakuwa na cha kusema juu ya hayo aliitikia tu kwa kichwa. Mkurugenzi alimpa ishara Fred akamwite Seba. Na wote walitoka nje ya wodi hiyo na kumwacha Judith akiwa kitandani kwake.
** *
Seba alikaa kwenye kiti ofisini kwa mkurugenzi huku akisikiliza alichoitiwa. “Ninamekuita nikujulishe kuwa Mungu amekujibu sala zako. Mchumba wako ni mwenye akili timamu sasa.” Alisema mkurugenzi huku akitabasamu. “Wooow! Kweli Madam? yuko wapi sasa?!” Aliruka Seba kwa mshangao na furaha. “Nenda kwenye chumba chake utamkuta anakusubiri japo sijamwambia kuwa upo hapa. Mengi mtaongea wenyewe huko.” Alisema mkurugenzi kwa furaha. Seba alitoka mbio kwenda kwenye chumba alichopo Judith.
Hatua zake zilikuwa za kunyata mara tu alipofika karibu na mlango wa chumba cha Judith. Alishika kitasa cha mlango na kuusukuma polepole kisha akainga kwa taratibu sana. Judith aliona mlango ukisukumwa polepole na mtu akiingia kwa kutanguliza mguu na baadaye mtu huyo alijitokeza na kusimama mbele yake huku akiufunga mlango nyuma yake.
Haikuchukuwa sekunde tano Judithi alimkumbuka mtu huyo kuwa ni Sebastian Changawe Mchumba wake. Wakati huo Seba alikuwa amesimama tu mbele ya Judith huku akiwa na tabasamu kubwa sana. “Wooow Seba!” Alisema Judith kwa mshangao wa hali ya juu sana huku akiamka na kukimbilia pale Seba alipokuwa amesimama na kumkumbatia kwa furaha sana.
Judith alikuwa na furaha sana lakini Seba alikuwa na furaha kubwa zaidi iliyosababisha machozi mengi. “Habari my dear pole na safari ndefu umerudi lini kutoka marekani?” Alisema Judith kwa huku akionyesha kushangaa upendo wa Seba ulivyo mkubwa kwake. “Ninashukuru kukuona uko mzima mpenzi wangu. Kuhusu ni lini nimerudi kutoka masomoni ni habari ndefu sana ila kwa ufupi ni kwamba nimerudi miaka mitatu iliyopita kwa ajili ya kukuhudumia. Sikuona kama masomo ni bora kuliko wewe.”
“Whaaat!!! Eti miaka mitatu! Ilikuwaje urudi miaka mitatu wakati miaka mitatu nakumbuka nilikuwa sijaonana na wewe na nilikuwa chuo kikuu nchini Uingereza? Usinitanie Seba nyoosha maelezo yako. Alisema Judith huku akitoa kicheko kama anayefanyiwa utani na mchumba wake huyo. “Judith mpenzi wangu tuna mengi ya kuongea nitataka leo baadaye twende sehemu kwenye bustani nzuri sana huko tutaongea mengi. Mara hiyo kabla hajamaliza alamu ililia ya mlangoni Seba alifungua mlango na Wadada wawili waliingia ndani wakiwa na vyakula vya aina mbalimbali na kuviweka mezani. “Tumetumwa na mkurugenzi tuwaletee chakula.” Alisema mmoja wa wahudumu wale. Asanteni sana alisema Sebastian wakati wahudumu wale wakiishia mlangoni. Judith alichukuwa chakula na kuandaa mezani kisha wakanawa kwenye sinki lililopo chumbani hapo kisha wakaanza kula chakula pamoja.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatua zote hizo za maandalizi ya chakula aliyoyafanya Judith Seba alikuwa anayafuatilia kwa mshangao mkubwa Tayari Judith alikuwa ni mzima kabisa. Moyo wake ulilipuka furaha ya kipekee sana. Seba alijizuia sana kuonyesha mshangao huo kwa wazi ili asije akazua maswali mengi ambayo hawezi kuyajibu yote kwa wakati huo.
Walikaa wote na kuanza kula chakula huku wakikumbushana baadhi ya vitu na Judith alifurahi sana kukumbushwa juu ya kukutana kwao kwa mara ya kwanza katika ofisi yake ya usafirishaji. Natamani ofisi yangu sijui wateja wangu watanielewaje maana huenda hawana taarifa kuwa nimesafiri kuja huku. Alisema Judith. Utarudi tu ofisini kwako siku za kukaa hapa zinahesabika.” Alisema Seba huku akitabasamu.
“Hivi nilipatwa na nini hadi mkanisafirisha bila mimi kujua mpaka huku?” aliuliza Judith swali ambalo Seba alijua akilijibu litaleta mtiririko wa maswali mengi zaidi. Ulipopewa taarifa za msiba wa mama ulizimia ndio tukakuleta huku kwa matibabu ndio leo umezinduka.” Alisema Sebastian kwa kifupi. “baba yuko wapi kwa sasa?” Aliniaga karudi Tanzania ila tukimpigia simu na akasikia sauti yako atakuja haraka sana.” Alijibu Seba huku wakiendelea kula.
***
Ilikuwa ni katika mazingira mageni sana kwake lakini mazingira mazuri ajabu. Bustani ya maua yaliyokatwa kwa ustadi kwa kutumia mashine maalumu yalikuwa kama safu nzuri sana zilizojipanga zenye rangi tofauti za kuvutia. Majani nayo yalikuwa yamekatwa vizuri na kupafanya mahali hapa papendeze na kuwa maalumu sana kwa ajili ya wawili hawa kupatumia kwa mazungumzo yao. Bwawa la kuogelea lilizua mshangao mwingine kwa mmoja wa watu hawa walioonekana kuwa wageni katika eneo hili.
Ni bwawa kubwa sana lililokuwa na madoido mengi yakiwepo maputo ya kuogelea ya kila namna. Yapo yaliyofanana na kitanda na yapo yaliyokuwa kama boti dogo ambayo mtu akiingia ndani yake hujiendesha akielea kupitia katika mikondo mbalimbali iliyopo katiaka maeneo ya bwawa hilo. Haya ni baadhi tu ya mambo mengi yaliyopo hapa. Mshangao wa uzuri wa eneo hilo nao ulikuwa mkubwa sana. “Leo nimeona tuje katika eneo hili zuri na la kuvutia ili tuwe peke yetu kwa mazungumzo muhimu.
Unajua kuwa nimeitamani nafasi hii ya kuongea na wewe ukiwa mzima kabisa kwa siku nyingi sana. Utanisamehe sana kwa sababu ninaona ni vizuri nikueleze ukweli wa kila kitu juu ya maisha yako na yangu pindi ulipopotelewa na fahamu zako. Sina budi kuongea kila kitu ili ujue yote hayo kwani huu ndio msingi hasa wa maisha yetu ya ndoa.”
Alisema Sebastian huku akiwa amemshika mkono mchumba wake wakati walipokuwa wakitembea kuelekea mbele kwenye kijito cha maji. “Na mimi nitafurahi kusikia kutoka kwako maana ninaona kuna mambo mengi yamejifumba katika akili zangu na kila ninapotaka kuyauliza maswali yanakuwa ni mengi na ya kutatanisha.
Mfano nikitaka kujua habari za wewe kuwa umerudi lini kutoka masomoni. Mimi hapa nilifika lini? Kwanini nimefika hapa? Kwa mfano tulipotoka pale kwenye chumba changu watu wote walioniona walinishangaa sana na kila mmoja anaonekana kunijua sana. Umaarufu huu umetoka wapi huku kwenye nchi za watu. Ninahitaji kweli Seba unifafanulie yote ili nipate ukweli wa kila kitu.” Alisema Judith kwa utaratibu na kwa msisitizo huku wakiendelea na safari yao na wakati hii walikifikia kijito cha maji na ng’ambo ya kijito hicho kuna jabali kubwa sana. Walivuka kijito kile kupitia kidaraja kidogo kilichojengewa mahali pale na moja kwa moja walifikia jabali lile.
Seba alimshika mkono na kumvuta mchumba wake ili kuweza kupanda juu ya kilele cha jabali like. Pale juu ya jabali palionekana kuwa na mahali pazuri sana pa kukaa huku wakiona maeneo mbalimbali ya kuvutia ya chuo hicho. Chini bondeni Judith aliweza kuona Bwawa kubwa alivutiwa na bata bukini waliokuwa wakiogelea. Sambamba na bata hao bukini kulikuwa na bata mzinga nao walikuwa kandokando ya maji yale huku wakijitafutia chakula chao. Na kwa upande mwingine kulikuwa na msitu mdogo lakini mnene kiasi ambao juu yake walikuwa anarukaruka tumbili na kima nao walisikika kwa mbali wakitoa milio yao. Mbele ya msitu ule kulikuwa na shamba zuri la migomba. Mahali hapa ni pazuri sana. Waliobuni mazingira haya walifikiri sana aisee!” Alisema Judith huku akijiweka vizuri mahali alipokaa huku akirejesha macho yake kwa mchumba wake.
“Ni kweli Judith, mahali hapa na mpangilio wake vilibuniwa na mtu ambaye alikuwa na maono makubwa sana ya kuwasaidia watu katika matatizo yao magumu. Mipango yake aliitekeleza kwa nguvu zote kupitia akiba yote ya fedha aliyoachiwa na wazazi wake. Huyu mtu ni mwanamke mwenye asili ya kijerumani ambaye alipata majaribu ya kutisha sana katika maisha yake.
Uvumilivu wa majaribu hayo ambayo yalimpiga mfululizo haukuweza kufua dafu mbele ya jaribu la mwisho la kufiwa na mama yake mzazi. Hapa ndipo giza lilipoingia katika akili zake na maisha yake yakawa ya kupapasa huku akiishi na kufanya vitendo vya ajabu bila yeye mwenyewe kujitambua.
Muda wake mwingi aliutumia kwa kuokota makopo na kila chenye kuokoteka na kula chochote alichoona kinafaa huku akilala popote alipopachagua. Kwa ujumla mtu huyu alikuwa kichaa kabisa katika umri wake wa kupambazukia maisha ya dunia hii. Alikuwa bado ni msichana mbichi aliyekuwa bado katika masomo yake. Lakini kwa namna isiyoweza kuelezeka maisha yalimgeukia na kumpiga vibaya.
Mwishowe aliokotwa na aliyekuwa mwalimu wake na kupelekwa katika kituo cha afya ya ubongo iliyokuwa nchini uswisi. Kituo hiki kilikuwa kinamilikiwa na kanisa katoliki hivyo msichana huyu alipata matibabu mahali hapa. Tatizo lake lilikuwa ni mchubuko wa ubongo lililotokana na matatizo yake mengi aliyokutana nayo. Madaktari walimtibu na kuhakikisha hapati bugdha yoyote ile. Kwa zaidi ya miaka mitatu alikuwa katika eneo hilo lakini Mungu si athumani wala John siku moja akiwa na Sista aliyekuwa akimhudumia akili zake zilirejea. Hapo ndipo alipopelekwa kwenye chuo cha udaktari akasomea namna ya kuwasaidia watu wanye matatizo kama aliyokuwa nayo yeye.
Baada ya kuhitimu masomo yake alikwenda kwenye bank iliyokuwa ikitunza akiba ya fedha za baba yake. Baada ya kufaulu kuchukuwa kiasi hicho ambacho hakikuwa haba alikusudia kujenga Hospitali katika nchi yake ya Ujerumani, Uswisi, Ufaransa na kimoja Afrika Mashariki. Hospitali hizo zilijengwa sambamba na vyuo vya mafunzo ya udaktari kama unavyoona hiki hapa.”
Alisema Sebastian kwa kufupisha sana historia hiyo huku akimwangalia mpenzi wake kama anafuatilia kwa umakini habari hiyo. “Ninakufuatilia Seba endelea.” Alisema Judith huku akifurahia kusikia habari hiyo yenye kusisimua. Huu ndio mwanzo wa ndoto za mwanamke huyo wa kihistoria kutimia. Hospitali hii na chuo unachokiona ni matunda ya bidii zake katika kutimiza kile alichojiahidi katika maisha yake. Ni Hospital inayotibu wagonjwa wenye matatizo ya akili kwa njia za kisaikolojia zaidi.
Tiba zake hazitegemei madawa kama hospitali nyingi duniani. Hosptali nyingi madaktari wanawatibu wagonjwa wa aina hiyo kwa kuwasindilia madawa mengi na kuwaweka katika mazingira yasiyoleta heshima. Hata pale wanapokuwa wazima baada ya hapo, japo asilimia ya wanaopona ni ndogo sana. Madaktari wa Hospitali hizi wamepitia mafunzo maalum juu ya saikolojia ya mwanadamu. Mafunzo hayo yanawafanya Madaktari kumaliza matatizo ya wagonjwa wao bila kutegemea madawa, labda kwa asilimia ishirini tu pale inapobidi. Kusudi la kuweka Hospitali pamoja na vyuo ni ili kuwapa watu wanaojiunga na vyuo hivyo kujifunza kwa vitendo zaidi kusudi kujipatia uzoefu usio wa kinadharia tu.
Hivi unavyoona hapa ndivyo ilivyo pia katika hospitali nyingine zilizoko Uswisi Ujerumani na Ufaransa. Hizi ni hospitali za kwanza alizozianzisha mama huyo ambaye jina lake aliitwa Matilyer Ardolph. Baadaye aliwaachia watoto wake wawili ambao ni Matlda na Mark nao waliendelea kufungua vituo maeneo mengi duniani.
Madaktari wanaozalishwa kila mwaka katika vyuo hivyo ndio hupelekwa katika vituo hivyo kokote vinapofunguliwa.” Alisema Seba kisha akafungua kwenye mfuko wake na kuchukuwa kopo la Redbull huku akitoa malta Guiness na kumkabidhi mchumba wake. “Nashukuru kusikia kuhusu Hospitali na vyuo kwa kuanzia historia ya mwasisi kama ulivyonieleza.
Kwa kweli inasisimua sana kuona kuwa mtu anaweza kuuahidi moyo wake jambo na hatimaye kulifanikisha kwa asilimia mia moja, huu ni ushujaa mkubwa. Ila nataka tugeukie kwangu nadhani maelezo yako ndiyo yatakayojibu kila swali nililonalo. Karibu uendelee. “Alisema Judith akimwangalia Seba ambaye alikuwa anamalizia kufungua kopo lake la kinywaji na yeye akafungua la kwake wakati huo huo na kupiga funda moja kisha akatulia kusikiliza. Seba aliweka chini Redbull yake baada ya kupiga funda moja kisha akaendelea:
“Historia ya mwanamke huyu Matlyer Ardoph haikupishana sana na historia yako katika matukio uliyopitia...
Kama unakumbuka nilikwambia kuwa nilirudi kutoka masomoni miaka mitatu iliyopita kwa ajili yako huo haukuwa utani hata kidogo. Leo ni tarehe 24/10/2013. Wakati ninakuaga kuwa naenda marekani ilikuwa ni February mwaka 2010.
Nadhani unalikumbuka hilo. Mwaka uliomalizia masomo yako Uingereza ni mwaka 2008 kutoka hapo mpaka sasa ni miaka mitano na miezi kadhaa imepita. Miaka mitatu kwako ilikuwa ni ukurasa wa giza nene. Nilipokuwa Marland Marekan kwenye chuo kikuu kwa ajili ya masomo ya shahada ya uinjinia wa magari, nilipata mashaka baada ya kukukosa kwa wiki nzima kwa mawasiliano. Kama utakumbuka tuliwasiliana mara tatu tu baada ya mimi kufika marekani.
Hali yako ilionyesha kutengemaa pale nilipokuacha, lakini baada ya kukukosa nikapatwa na wasiwasi mkubwa na majibu ya mfanyakazi wenu hayakutosheleza haja ya kujua kuwa uko wapi na unaendeleaje na hali yako? Kwa ajili ya wasiwasi huo nilichukuwa uamuzi wa kurudi nchini ndipo nilipokutana na wewe ukiwa katika hali mbaya na kwamba ulikuwa hujitambui kile ulichokuwa ukikifanya.” Alisema Hivyo Sebastian kisha akageuza macho yake kwa wizi kisha akayapitisha kuangalia kule chini bwawani akaona ndege wengi wa kiruka usawa wa bwawa lile kubwa la samaki. Judith alikuwa ameduwaa kusikia historia ile huku akiwa ameinamisha kichwa chake chini ikiwa na maana bado alihitaji maelezo ya kutosha kukidhi maswali yake. Kwa namna hiyo niliamua kuacha kazi ofisini kwangu na makampuni yangu niliyaacha mikononi kwa mameneja wangu. Kuanzia hapo sikuwa tena na jukumu lolote jingine zaidi ya kuhakikisha kuwa unapata matibabu. Sina wakati unaotosha kukueleza kila hatua mambo yaliyotokea moja moja. Ila kwa ufupi tulipitia hatua nyingi nikiwa na mzee Martin na shangazi yake adela na baba yako mdogo Allen.
Hospitali walitoa majibu yaliyotoa mwanga kuwa tatizo lako linatokana na mchubuko wa ubongo. Hivyo unahitaji kuwekwa mbali na jambo linalokusumbua akili yako. Nikamwomba Mzee Martin akuache mikononi mwangu na ukawa huru kutembea popote ulipotaka na mimi nikawa sambamba na wewe popote ulipoenda. Nilikuwa bodigadi mzuri nikihakikisha usalama wako kwa zaidi ya miezi sita nikifikiri kwa njia hiyo utapona haraka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipoona unachelewa kupata fahamu zako tukapeleleza tena tuone ni Hospitali gani inayoweza kukupatia tiba nzuri tofauti na hizi ninazozijua. Mwisho tukapata kupitia mtandao wa Internat juu ya Hospitali iitwayo, “Psychological mental Hospital.” Mambo yote kuhusu tiba zake tuliyapata kupitia mtandao huu na kwamba ilianzia Ujerumani hatimaye Uswis na Ufaransa. Tukiwa katika hali ya kutazama zaidi ndipo tukapata kuwa Hospitali hiyo ipo pia hapa kwetu Afrika ya mashariki. Ilikuwa furaha kujua kuwa Hospital hii ya viwango ipo jirani na Tanzania. Ndipo kwa kutaka kuhakikisha zaidi huduma zake tukafunga safari kuja hapa. Siku mbili tulizokuwa hapa zilitosha kutupa uhakika kuwa ni Hospitali ya aina yake na inayokufaa sana. Ndipo tukaja hapa baada ya miezi sita ya kutafuta namna ya kukutibia.
Mpaka sasa ni miaka miwili na miezi minne tupo wote hapa na mimi nimebakiza miezi minne tu kuchukuwa shahada yangu ya udaktari katika chuo hiki.”Alitulia kidogo na kunyanyua kopo la Redbull na kupiga funda moja kisha akaendelea. “Hii kwangu ni furaha ya ajabu ambayo ningetamani kupaaza sauti yangu ili dunia ifahamu ninavyojisikia.” Alisema hivyo huku akimtazama mchumba wake ambaye alikuwa akimwaga machozi kwa kusikia historia yake ya kusikitisha.
“Pole Judith usilie hiyo ni historia tu ambayo imeshapita na sasa uko sawa kama ulivyo. Huhitaji kuumizwa na Historia ila kutokana na historia hiyo kuna mambo mazuri yatazaliwa ili kutoa nafasi ya faraja katika maisha yako. Waswahili husema: “Baada ya dhiki ni faraja.” Wakiwa wamekumbatiana Judith alikuwa akilia kwa kwikwi huku maneno yake yakigoma kutoka pale alipotaka kuzungumza jambo.
“Sipati neno linalofaa kulisema mbele yako kulingana na yote uliyoyafanya kwa ajili yangu. Moyo wangu unanikataza kufikiri kuwa ni upendo tu wa kawaida uliokusukuma kuwa na mimi katika hali niliyokuwa nayo majalalani na kwingineko. Ni vichaa wangapi wanaotembea mitaani peke yao wakiwa hawana watu walio timamu wakuwalinda kama mimi nilivyokuwa nikilindwa? Wachumba wangapi walipatwa na matatizo ya akili ambao wameachwa wakitembea peke yao mitaani na kulala kando ya barabara bila ya kupata msaada wa wale walioonyesha kuwapenda hapo kwanza? Kama sikosei wapo pia wake za watu ambao wamepatwa na matatizo ya akili na waume zao walikata tamaa na kuwaacha wahangaike peke yako huku wakidhalilika mbele za walimwengu.
Ninaushangaa upendo wako kwangu uliopitiliza. Sina neno linalotosha kusema ila kushangaa tu. Labda wewe uliumbwa kwa ajili yangu na ndio maana umevumilia maisha yangu katika karaha za aina zote na matatizo yangu. Vinginevyo asante sana kwa kunijali kwa viwango vikubwa hivi, Mungu akupe maisha marefu na ya heri kwa tendo hili kubwa.”
Hatimaye alijimudu kusema Judith huku akitiririkwa na machozi ya shukrani. “Usijali Judith sijaona kama nimetenda jambo la ajabu kutendwa na mwanadamu wa sayari hii. Ila nataka tu kusema kuwa ninafurahi kwa kupona kwako na ninakupenda sana mpenzi wangu. Mahali hapa nimekuleta ili niirudie ndoto yangu niliyoiota juzi mchana chumbani kwangu.
Niliota tuko hapa tulipokaa tukiongelea mambo yetu ya maisha. Kisha tulipitia kwenye bwawa lile tukaogelea japo leo sitataka tuogelee.” Alisema Sebastian huku akimkumbatia Judith. “Kwanini tusiende kuogelea sasa?” Aliuliza Judith kwa shauku kubwa. “Hapana leo tusiende tutaogelea siku nyingine maana nikiifuatisha hii ndoto moja kwa moja kila kitu cha ndoto kitatimia vingine ni karaha kukutana navyo.” Seba alisema hivyo kwa utulivu. Karaha gani tena kuogelea tu?” Judith aliuliza kwa mshangao. “Wewe hujui. Katika ndoto hiyo niliota wakati tunaogelea walikuja wagonjwa wa akili wa kiume wengi na kuingia bwawani kuchanganyika nasi katika kuogelea na hapo tukatoka na kuwaacha wakipiga makelele. Kwa hiyo nahofia kutokana na kutimia kwa ndoto hii ya wewe kupona na hayo pia yasije kutokea na kutukwaza sawa mpenzi wangu?” Alisema hivyo huku akimshika Judith mkono na kumnyanyua.
“Twende tukajiandae kwa ajili ya kwenda kwenye arusi ya mdogo wa rafiki yangu. Naamini tutakuwa na wakati mzuri sana wa kujifunza namna na sisi tutakavyoandaa Arusi yetu.” Seba aliyasema hayo wakati wakishuka kutoka juu ya jabali lile. Vile utakavyopanga mimi niko tayari.” Judi alisema huku wakimalizia kupita kwenye kile kidaraja kidogo. Wakiwa karibu na kufika chuoni walikutana na kundi la wagonjwa wa akili wakienda maeneo lilipo lile bwawa la kuogelea.
“Nilikuambiaje?” Seba alimkumbusha mpenzi wake. Ndoto zako ni kama ratiba za mambo yaliyopangwa kutokea. Au labda mwenzangu wewe ni nabii?” Alitania Judith wakati huo wakiwa wamesimama kuwaangalia watu wale waliwaona wakiingia bwawani na kuogelea kwa fujo. Seba alitoa simu yake mfukoni mwake na kuupigia uongozi wa Hospitali na kuwaarifu juu ya wagonjwa wale, kisha wakaendelea na safari. Wauguzi walikutana nao wakienda kuwatoa wagonjwa wale kule bwawani, wakati wao wakiingia ndani ya majengo ya hospitali wakielekea kwa mkurugenzi.
***
Simu iliita kwa mara nyingine tena. Nafasi hii ndiyo aliyokuwa anaingoja kwa hamu kubwa. Mara tatu simu hii ilipigwa wakati yeye akiwa bafuni. Alipotoka aliona namba ngeni za simu ya mezani lakini kutoka nje ya nchi yake. Hakujua ninani mpigani ila alisubiri maana alijua kuwa kama mpigaji amedhamiria atapiga tena. Haraka sana aliichukuwa simu yake na kuminya ok kisha akaitikia kwa sauti ya utulivu. “Hallo baba shikamoo.” Alisalimia mpigaji na hapohapo akaitambua sa
uti hiyo kuwa ni ya Sebastian. “Marahaba mwanangu hujambo baba? Tangu juzi sijakupigia kuwajulia hali kutokana na kutingwa kwa shughuli mbalimbali za hapa na pale. Vipi mwenzio anaendeleaje?” alisema Mzee Martin. Kwakweli nashukuru sana baba ni mzima kabisa, hata hapa nilipo tuko pamoja naye anataka kukusalimia.” Alisema Sebastian kwa furaha tele.
“Siamini maskio yangu juu ya hilo! Leo amekubali kuongea na mimi wakati siku zote hataki hata kunisikia?” Alishangaa Mzee martin kwa maneno hayo. “Mzee Leo na jana ni tofauti, mambo yamebadilika naona ni jibu la kilio chetu cha muda mrefu. Seba aliongea maneno hayo kwa namna ya kutaka kumjulisha muujiza uliotokea. “Unataka kuniambia kuwa Binti yangu Judith amepona kabisa?”
Alifoka mzee Martin kwa kutokuamini maneno hayo. Sikuambii kwa maneno matupu baba yangu nataka uzungumze na binti yako mwenyewe hapo ndio mahali penye jibu la swali lako.” Alijibu Seba na kumkabidhi Judith simu lakini Judith alikuwa akilia machozi mengi. Ilibidi mzee Martin ajaribu kumtuliza ili wasalimiane. “Baba shikamoo.” Hatimaye Judith aliweza kutoa sauti na kumsalimia baba yake. Woow! Judith binti yangu umepona kabisa?” Alisema mzee Martin kwa sauti iliyokuwa na kitetemeshi kinachoashiria kilio. “Ndiyo baba yangu. Nashukuru sana kwa ninyi kunishuhulikia hadi kufikia hapa. Niko mzima kabisa na nitafurahi sana kukuona mzazi wangu.” Alisema Judith huku akifuta machozi machoni mwake.” Asante mwanangu lakini mtu aliyesumbuka na wewe kwa kiwango kikubwa ni huyo mchumba wako Seba. Alitelekeza kila kitu cha maisha yake kwa ajili ya kukuhudumia. Ametumia mali zake kwa ajili ya kulipia kila gharama ya matibabu yako. huu ni upendo mkubwa sana ambao sijawahi kuona popote japo nimeishi miaka mingi na kusikia historia nyingi. Kamwe sijawahi kusikia mtu aliyefanya hivyo alivyofanya huyo kijana Sebastian.” Alisema Mzee Martin.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nashukuru baba nimesikia kila kitu juu ya hilo na mimi sina la kufanya zaidi ya kushukuru na kumpa Mungu utukufu kwa ajili ya kuyashikilia maisha yetu na kuharakisha kupona kwangu. Seba ni chaguo langu sahihi na Mungu alimleta kwangu ili awe mwenzangu katika maisha yote. Najua kuwa alilofanya ni wajibu wake kwa ajili ya mke wake mtarajiwa japo si wengi wanaoweza kufanya alivyofanya.” Alisema Judith maneno ambayo yalimhakikishia kuwa amepona asilimia mia moja.
Hekima zake na busara zilikuwa za hali ya juu. “Nashukuru kusikia hivyo binti yangu. Nitakuja huko sio siku nyingi kuanzia leo.” Mzee Martn alihitimisha mazungumzo na binti yake kwa furaha ya aina yake. Judith alirudisha simu kwa Seba. “Mzee panda ndege ya kesho mchana nitapiga simu ofisini kwangu nao watakuchukulia tiketi ya ndege na kukuletea hapo nyumbani. Ningependa usafiri na shangazi Adela pamoja na baba mdogo Alen. Usiku wa kesho tutakuwa na muda mzuri wa kuwa pamoja kwa mazungumzo yetu. Nao nitatuma tiketi zao ili msafiri wote hiyo kesho.” Alisema hivyo Sebastian na hatimaye akakata simu.
***
Jioni hii ilikuwa ni shangwe kubwa mioyoni mwa Seba na mchumba wake pale walipoyatembelea maduka mbalimbali ya nguo ghali sana katika jiji la Nairobi. Waliweza kununua nguo za gharama kubwa wakiwa wote. Seba alihakikisha anamnunulia mchumba wake nguo za gharama kubwa kwa matumizi ya chuoni na zile zilizohusu sherehe ya Arusi ya mdogo wake na Njoroge usiku wa siku hiyo. Baada ya kufanya manunuzi hayo waliingia katika gari na kurudi chuoni kwa maandalizi ya sherehe ya usiku huo. Judith alijisikia malkia hasa katika kipindi chote akichokuwa karibu na Seba.
Hata baada ya Arusi kwisha walirudi chuoni wenye furaha nyingi na kujifunza mengi. “Nimejifunza mengi sana Seba. Naisubiri siku ya arusi yetu itakuwa ni ya kihistoria hasa.” Alijibu Judith wakati gari likisimama kwenye uwanja wa chuo na wao wakaanza kuteremka na kuelekea ndani. Baada ya Seba kumfikisha Judith chumbani kwake alimuaga na yeye akaenda chumbani kwake.
12
Utata ndani ya ofisi ya Chief
Ilikuwa ni mshangao wa aina yake kwa katibu muhtasi wa ofisi ya mkurugenzi wa habari ambaye hakupenda kutajwa jina lake moja kwa moja. Haikujulikana sababu hasa ila jina la Chief ndilo lililozoeleka na watu waliridhika kumwita hivyo. Sambamba na ughali wa kulijua jina lake hata hivyo mtu huyo amekuwa adimu sana kuonekana machoni kwa watu. Huyu alikuwa ndiye Chief wa shirika la uandishi wa habari. Shirika lenye kusimamia haki za waandishi wa Riwaya na miswada mbalimbali, lijulikanalo kama UWARIDI.
Majukumu yake yalikuwa ni makubwa sana kwa ajili ya shirika na pia alikuwa ni Mpelelezi wa kujitegemea akisaidia kukabiliana na ujambazi pamoja na hujuma zinazofanyika nchini. Kazi zake nyingi alikuwa akishirikiana na Serikali lakini alikuwa akizifanya kwa siri sana na mara kwa mara alikuwa akisafiri kwenda katika nchi mbalimbali kwa mujibu wa majukumu yake.
Mambo mengi alikuwa anayafanya kwa umakini sana huku akijigawanya katika kutimiza kila eneo la majukumu yote aliyonayo. Ilikuwa ni aghalabu sana kukaa nyumbani kwake familia yake ilimkosa sana na hata mkewe ambaye alikuwa ni mbunge wa viti maalumu alikuwa hakai na mumewe hata kwa masaa mawili mfululizo kwa ajili ya mazungumzo ya kifamilia. Kila wakati majukumu ya kiserikali na ya shirika lake la uandishi wa habari yalimlemea.
Mara zote alikuwa akiacha maagizo kwa ajili ya kazi na msaidizi wake alikuwa akiyawakilisha kwa watu muhimu.Huu ndio uliokuwa utaratibu hasa wa bosi wa shirika hili, utaratibu ambao umezoeleka kwa watendakazi walioko chini yake. Mkuu huyu wa shirika alikuwa akifika mara kwa mara hasa kunapokuwa na mambo muhimu ya kuyashughulikia yanayohusu habari nyeti, au vikao muhimu. Mara nyingine hupotea na kusahaulika kwani habari zake sio wote wanazipata zaidi ya msaidizi wake ambaye huchukuwa nafasi yake mara nyingi. Mwingine ambaye hubeba siri za bosi wake ni katibu muhtasi. Huyu ni mama wa makamu ambaye umri wake hauzidi miaka arobaini na mbili jina lake aliitwa Selina.
Asubuhi hii alikuwa na mshangao mkubwa baada ya kukuta kwenye meza yake kuna kipande cha karatasi chenye mwandiko wa Bosi wake. Hakujua kama alikuja ofisini saa ngapi na alitoka muda gani. Moyo wake ulienda mbio kidogo kwani bosi wake huyo alimjulisha kuwa yuko safarini nchini Uholanzi. Hakujua kuwa karatasi hiyo yenye mwandiko wa bosi wake ilifikaje ofisini kwake wakati mtu mwenyewe hayupo kabisa nchini. Kabla ya kufungua karatasi ile ili aisome alitoka nje ili aonane na mlinzi. “James hivi mkurugenzi amefika hapa ofisini saa ngapi?” Aliuliza Selina huku akiwa na na wasiwasi.
“Alifika saa mbili usiku Mamy na aliondoka saa nane na robo usiku Inaelekea alikuwa na shughuli nzito sana ofisini.” Alijibu James mlinzi wa jengo hilo la shirika la uandishi. “Ina maana James umeingia zamu ya usiku? Kwani Ricky hajaja kukupokea si jana ulishinda hapa kazini?” Aliuliza Selina Katibu muhtasi wa ofisi ya Chief. “Madamu, Ricky ni mgonjwa jana alinipigia simu kuwa hatoweza kufika ndio maana nikachukuwa na zamu yake. Alisema Jemes.
“Sawa lakini sijapenda huu mtindo. Pamoja na matatizo ya Ricky lakini usisahau kuwa wewe ni mwanadamu ambaye pia unachoka. Ungetoa taarifa ofisi ingefanya mpango kwa ajili ya kuleta watu wanaoweza kushika zamu ya Ricky kwa usalama wa mali za ofisi na kwa usalama wa afya yako pia.”
Alisema Selina Katibu Muhtasi wa Chief kisha akazama ofisini kwa ajili ya kuendelea na kazi zake. Alipofika ofisini kwake alikuta simu ya mezani ikiwa inamalizia mlio wa mwisho ikimaanisha kuwa ililia muda mrefu wakati alipokuwa akiongea na mlinzi. Kwa kuwa hakujua ninani aliyepiga ilimbidi avute subira akijua kuwa mtu huyo anaweza kupiga tena.
Kilichomvuta zaidi kwa wakati huo ilikuwa ni ile karatasi yenye mwandiko wa bosi wake. Aliinyanyua na kuifungua kwa pupa na kuanza kuisoma nayo ilikuwa imeandikwa hivi:
“Habari Selina. Labda utastaajabu sana kuona kipande hiki cha karatasi nilichokiandika kwa mkono wangu. Hizi siyo salamu kutoka Uholanzi bali niko hapa nchini nimeingia kwa kunyata kutokana na jambo nyeti nililoazimia kulifanya. Kilichonirudisha ni kuchunguza tatizo la upotevu wa mabilioni ya Escrow Tegeta. Hivi nimepotea tena lakini nitakapoibuka nitakuwa na mambo mapya ya kuyalisha magazeti yetu kwa faida ya wananchi wa Tanzania.
Ila habari kutoka mahali fulani zinaeleza kuwa Andrew yule mwandishi machachari yuko nchi ya jirani akiwa na habari za kutosha kuhusu Sebastiani Changawe na mpenzi wake. Ila nakutahadharisha kuwa usitoe habari hizi na wala waandishi wetu wasiandike chochote kwa sasa mpaka tutakapopata kitu hasa cha kuandika kuhusu watu hao. Nitakuona kwa wakati mtulivu ambao utakuwa na mengi ya kujaza kwenye mafaili yako ya kazi. Na kutakia kazi njema
Chief!
Salamu hizi zilimduwaza sana Selina na alisisimka kwa habari za kupatikana kwa Seba na Judith Martin. Maswala ya Escrow nayo yalichukuwa nafasi nyingine ya utashi ndani ya kichwa cha Selina na hapo ndipo alipoanza kumfikiria zaidi bosi wake na kutambua baadhi ya mambo ambayo hapo mwanzo alikuwa hayajui.
Akiwa anaendelea kutafakari mara simu ya mezani inaita Selina akanyoosha mkono wake na kuuinua mkonga wa simu kisha akaweka sikioni. “Halo.” aliitika kwa sauti ndogo. “Selina nategemea umepata ujumbe wangu.” Ilikuwa ni sauti ya Chief. “Ndio bosi nimeuona na nitazingatia yote. Alisema Selina.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Okay Selina fanya hivyo na kuanzia sasa angalia watu waelekeze macho na masikio yao kwenye Bunge la Katiba mpya na kuchunguza mambo ya msingi ili kuyatoa kwa jamii. Na hili suala la Upotevu wa mabilioni ya Escrow yachukuliwe uzito. Hakuna kuandika jambo ambalo halijafanyiwa uchunguzi kwa upana. Simamia hayo na kiongozi wa waandishi bwana Wingo nitampigia. Kumbuka bado niko safarini Uholanzi. Waliojua hilo waache waendelee kuamini hivyo kwaheri.
Alisema Chief Kisha simu ikakata. Selina alibaki na tabasamu lake kama kawaida lakini mawazoni akiwa mbali sana katika kuyachukulia mambo hayo kwa uzito wake unaostahili.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment