Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KURASA (THE PAGES) - 5

 

     





    Simulizi : Kurasa (The Page)

    Sehemu Ya Tano (5)





    Akili ikaniagiza kutoa kila kitu mle ndani kinacho muhusu Stellah. nikaanza na picha, nikachana kila picha niliyo iona pale ndani, nikavunja vunja kila fremu yenye picha yake iliyokuwepo mle ndani, sikutamani kabisa kumuona kwani ile ilikuwa ni mara ya pili ananiumiza.

    Kazi ya picha ikaisha, nikaingia kwenye nguo, nikafungua kabati na kuzitoa nguo zake zote na kuanza kuzikagua baadhi. Niliporidhika kuwa hakuna chochote, nikazitoa hadi uwani na kuzimwagia mafuta ya taa ili kuzichoma.

    Nikakumbuka pia kuwepo kwa begi la nguo zake nyingine za gharama ambazo hupenda kuziweka kwenye begi, nikazifuata na kutaka kulichoma begi zima kama lilivyo, lakini nikakumbuka uwepo wa karatasi zangu nyeti, nikalifungua kwanza na kulikagua.

    nilianza kutoa nguo moja moja na kuzitupia kwenye moto, niliona raha na amani ilinijia pale zilipokuwa zile nguo zikiungua. mwishoni wakati nalitupia begi baada ya kukosa kitu chochote cha msingi, nikaona kitu kama kina uzito fulani, nikalitatua begi, nikakuta Diary.

    Sikuwahi kuiona ile Diary hata siku moja, ikanishawishi kuifunua ili niione, kurasa nyingi zilikuwa zipo blank (Tupu - hazijaandikwa), nikaitupa chini, ilipokuwa ikianguka nikaona kuna kurasa zina maandishi, nikaiokota haraka kabla haija shika moto na kuifunua.

    Hapa ndio nahisi palipo nifanya nifute kumbukumbu, ukurasa nilio ufunua ulikuwa ukielezea tukio fulani la mke wangu.

    Nikaona si sahihi kusoma nikiwa nimesimama, nikatoka pale hadi ndani na kuketi sofani, sikujali tena zile nguo kama zinaweza kuleta madhara mengine.

    Nikaanza kufunua kurasa moja moja, kurasa za awali zilihusu sana mambo yetu mi nae, zilikuwa na mambo mengi sana ya kufurahisha, lakini hakuna hata moja ambalo kwa siku ile lilinipa tabasamu hadi nilipofikia kurasa mabazo naamini sitakuja kuzisahau hadi siku naiacha Dunia, naam siku ya mwisho wa maisha yangu huenda ikawa ndio siku ya kusahau.

    Moja ya paragraf ya kurasa ile iliandikwa kwa kalamu ya bluu

    Nimekutanishwa na mfanyakazi mpya aitwae Amani kutoka Zanzibar, ameletwa kuja kuniongezea nguvu kwenye idara yangu ya Upelelezi, anaonekana ni shupavu, huenda ikawa ni kheri kwangu, nachoka sana

    hivyo ndio ilikuwa imeandikwa ile kurasa, niliikumbuka vema siku ile, kumbukumbu ikanirejesha hadi siku yenyewe ya tukio, siku hiyo alirudi mapema sana kunieleza swala lile, nakumbuka nilipata faraja sana na kuamini huenda itakuwa kuna unafuu kwa mpenzi wangu.

    Sikujali baada ya kusoma ujumbe ule nikaendelea kufunua kurasa zingine na hapo nikakutana na ujumbe uliokuwa ni mrefu, sikutegemea kuona kile nilichokiona pale, maandishi yalisomeka;

    Usiku uliopita, Amani kanipigia simu na kuniambia napaswa kuwahi eneo la tukio maeneo ya Mwenge, nifike haraka japo ni usiku mnene. sikujua lengo lake, japo nilikuwa nikijua kuwa nanipenda na mara kadhaa amewahi kunitongoza nikamkataa kwa kumwambia mie ni mke wa mtu.

    Hivyo niliamini itakuwa ni jambo la kikazi tu na si vingine. nikatoka nyumbaniusiku ule ule hali ya kuw mume wangu kipenzi hajaridhika masikini mume wangu..

    hapa tena kumbukumbu iliniijia, nikafunga diary kwa kuitenganisha na vidole na kuikumbuka vema siku ile ambayo alichomoka usiku bila ridhaa yangu, nikafunua na kuendelea kusoma

    Nilifika pale aliponielekeza na kukuta ni shwari, nilipomuuliza kilicho endelea, akaniamuru nisubiri, akaniagizia kinywaji huku akiongea na simu mara kadhaa na akinyanyuka, hiyo ilinifanya hata mimi sasa kuwa makini, ilifanya niamini kuwepo kwa tukio eneo lile.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa ni usiku mnene, akanyanyuka na kuja kuninong'oneza niwe makini kumlinda toka pale nilipo, nikazidisha umakini nae akaondoka na kwenda meza za mwishoni kule kama unaelekea vyooni pale bar, akawa akizungumza na watu fulani.

    Kisha akarudi na kuniambia kwa taratibu pita kwa wale jamaa, angalia kwa umakini kinacho endelea kisha urudi.Nikafanya hivyo, kwani kwa utaratibu wa kazi yangu, sikupaswa kubisha, nilikwenda na kufanya kama alivyo niambia.

    Sikuona chochote, kumbe lile lilikuwa ni kosa kubwa sana, nilihisi atakuwa alinichanganyia madawa ya kulevya kwenye kinywaji changu, nami sikuwa makini kwani nilimuamini, nilipofika nikaendelea kunywa kama kawaida, sikuwa na hofu.

    Tangu hapo, sikujielewa tena hadi siku ya pili alfajiri ndio nilirejewa na fahamu. Amani hakuwepo, lakini mara tu nilipotoka pale nikiwa garini akanipigia simu akiniomba nimsamehe, sikuwa tayari kumsamehe, nilimtukana sana.

    Nililia sana kwa kitendo kile, hasa nikimkumbuka mume wangu kipenzi, sikuwa na nguvu ya kurejea nyumbani, lakini ilikuwa ni lazima nirudi, nikajilazimisha na kurudi, mlangoni nikakutana na mume wangu akitoka kuelekea kazini, hakuwa mwenye furaha kabisa, roho yangu iliumia sana

    Hivyo ndivyo ilivyosomeka ile kurasa, nikaikumbuka pia siku ile, roho ikaniuma sana, nikataka kufunga Diary lakini nafsi ikani lazimisha tu niendelee kusoma ili kuujua ukweli.

    Siku kadhaa mbele akawa ameandika kuwa kipindi chake cha siku za hatari zimepita kimya kimya, akaandika siku iliyofuatia kuwa anahisi ni mjamzito, namnukuu;

    Nimeongea na Amani juu ya suala hilo la mimba na kuitoa, ajabu nae akaja juu na kuniambia kuwa iwapo nitajaribu kutoa ile mimba atamwambia mume wangu, nami sipo tayari kukosana na mume wangu, nampenda sana

    Hapo ndio mwisho wa kunukuu.





    Scholler hukuwepo, nilitamani kuruka na kupaa ili kuwafuata kule walipo niwanyonge kabisa wapotee humu duniani, lakini bado moyo iliniambia niwe na subira, nikaendelea kufunua kurasa.

    Sasa niliamua kuisoma kila kurasa iliokuwa mbele yangu, karibu matukio mengi tu yakiwa yanajirudia, name nilishawishika tu kuyasoma hivyo hivyo nikiamini kipo kitu ambacho nitaambulia.

    **********



    Diary ilikuwa na mambo mengi, ikiwa mimba imetimiza miezi 9, mke wangu akaandika kwamba muda wowote toka sasa atajifungua na mtoto huyu hamuhusu Ramaah kwa nywele wala kucha ila ni yeye ndie alie mtunza kwa kila kitu, akajiuliza ni vipi aniambie kuwa mimi si baba wa mtoto?

    Akaweka na alama nyingi za kuuliza kama vile ameshindwa kupata jibu, name hapo nikaifunika ile Diary na kutamani kulia, hakika nilihisi chozi linakaribia kunitoka.

    Roho iliniuma sana Scholler, kulikuwa na kurasa moja iliyo kuwa imebaki na maandishi, sikutamani kuisoma hata kidogo, maana tayari ukweli nilikuwa nimeisha ujua, sasa hiyo ina kipi kipya? Nikadhamiria kuachana nayo, nikasimama ili nitoke nje kule uwani kwenye moto.

    Akili ilirejea miaka kadhaa ambayo tulikutana na Stellah kwa mara ya kwanza, picha ya awali ile niliyomuona akiwa anaendesha gari kwenye barabara ya Nyerere, nikavutiwa nae.

    Nikakumbuka mizunguko niliofanya na muda ambao nilio upoteza kwa ajili ya kumtia mikononi mwangu, sikusahau wakati wetu wote tulio utumia kwa starehe na hata usumbufu tuliowapa wazazi wangu, niliumia sana Scholler.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakika Sikuwa na uchaguzi mwingine zaidi ya kushikilia tu kuwa nikubali matokeo kwani nikizidi kusoma nitakuwa najiumiza zaidi. mengi ambayo niliyaona mbele nilihisi yatanikwaza.

    Lakini moyo una nguvu ya ziada kuliko akili, uliishawishi akili kwa kuieleza kuwa bila kusoma karatasi ile ukweli halisi utaujuaje? Na hata baada ya akili yenyewe kupima uzito wa wazo lile, nikashusha pumzi kwa nguvu.

    Hapo sasa moyo ukaweza kuisha wishi akili na kufanikiwa kuifungua ili kuisoma na ile ya mwisho, hakika hapo hata ile sehemu ndogo niliyotaka kuitumia kulazimisha kuwa yule ni mtoto wangu, kwani niliamini kitanda hakizai haramu, lakini matumaini yale yakafutika palepale.

    Chini ya tarehe kwenye kurasa ile paliandikwa kwa maandishi ya rangi ya wino mweusi

    ‘Mapenzi kwa mume wangu Mpenzi Ramaah, yanazidi kupungua kila siku, nahisi kumpenda zaidi baba watoto wangu mtarajiwa Mr Amani, kwanza nipo nae muda mrefu kazini kuliko Mume wangu, hapa sasa nina uchaguzi mwenyewe kati ya mume halali na baba halali wa mtoto,’

    Presha ikazidi kunipanda, hasa baada ya kujua kuwa tayari Amani amependekeza jina la mtoto na Stellah nae ametoa lake, kwa mujibu wa ile Diary iliandikwa mkataba, akizaliwa mtoto wa kike atapewa jina na Stellah, ataitwa Maajab.

    Hilo lilikuwa ni jina la Shangazi yangu mimi, sijui ni kwanini yule mwanamke alilipendekeza. Pendekezo la Amani likawa ni kwamba akizaliwa mtoto wa kiume ataitwa Salum bin Amani na ataishi na baba yake kipindi chote cha uhai wake.

    Roho iliumia sana, nikapandwa na jazba, nikaingia chumbani na kuchukua Bastola yangu aina ya Revolver 12/09 na kuikagua kama ina risasi za kutosha, bastola hiyo yenye uwezo wa kuhifadhi risasi 12, ilikuwa imejaa risasi.

    Basi nami niliporidhika tu nikatoka nje na kuingia garini, sikukumbuka hata kufunga mlango wa nyumba, nikaondoka. Hasira zilikuwa zimevuka kiwango, sasa nilikuwa nipo tayari kuuwa, sikuhofia kabisa mkono wa sheria hasa baada ya kujua mtoto aliezaliwa ni wa kiume, hivyo atakuwa ni mtoto wa Amani, nikaamua ngoja nikawaue wote watatu, yaani baba, mama na mwana ili tukose wote.

    Kasi niliyo ondoka nayo pale nyumbani, ilitisha wengi, majirani zangu wakashtuka, mmoja akawa akinifuatilia, nilimuona lakini wala sikumjali, lakini unafikiri Scholler nilifika kwa Stellah? kasi ilikuwa ni kubwa sana na akili haikuwa na mwili, hivyo nilishindwa kuiongoza gari.

    Ajali mbaya ilinitokea huku nikishuhudia kabla sijapoteza fahamu, hadi sasa ndio nimekumbuka yaliyopita, baada ya hapo sifahamu kingine chochote kilicho endelea

    "Hiyo ndio historia yangu dada Scholler"

    "Dah! Pole sana Ramaah, inasikitisha sana historia yako"

    "Nashukuru sana dada yangu, ila..." akanyamaza ghafla Ramaah na kumtazama Scholler

    "Ila nini?" Aliuliza Scholler kwa sauti ya kuonyesha anajali na mwenye hurujma tele

    "Maisha yangu mie" huku akitikisa kichwa

    "Yapoje maisha yako kaka yangu? yatakaa sawa tu Ramaah wala usihofu!"

    "Sawa dada yangu, acha niende nje nikakae kidogo" akatoka akiwa ni mnyonge na kumuacha Scholler akimtazama kwa jicho la huruma.

    Siku 3 baadae, uzalendo ukamshinda Scholler na kumwambia kuwa Stellah ni ndugu yake, Ramaah akamwambia yeye binafsi hataki hata kumsikia licha ya kumuona.

    "Ni kweli Ramaah, una haki ya kusema hivyo, alicho kutendea si kitu kizuri, bali mie kuna kitu napenda kukwambia..." akionekana mwenye aibu usoni ama woga fulani hivi

    "Ni kitu gani hicho dada yangu?"

    "Ramaah nakupenda..!"

    **********







    Mambo yakaeleweka, Scholler na Ramaah wakawa tayari ni wapenzi, tena mapenzi yenyewe yalionekana kama yanakuwa moto sana, lakini yalizamia kwa upande mmoja, kwa Scholler zaidi.



    Scholler alijua ni nini Ramaah anataka, pasina kuchelewa akambebea ujauzito ambao Ramaah alikataa kabisa kuwa anauzungumzia, bado alikuwa na athari za Stellah kwenye akili yake.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakuwa bado anamuamini mwanamke yeyote chini ya jua, labda kidogo kwa huyu aliweza kuwa na imani nae kwani alikuwa anafanya kazi huku akimuona na akitoka kazini wanakuwa wote hadi aingiapo tena kazini siku ifuatayo.

    **********



    Ilipotimia miezi mitatu tangu aanze kukaa kwa Scholler, hali yake sasa ikawa ni mujarrab kabisa kiasi ambacho hata daktari alipomtazama akamwambia kuwa anastahili sasa kurudi nyumbani.



    Rasmi akawa ameruhusiwa kabisa kuondoka eneo lile la hospitali, Scholler hakumruhusu kuondoka peke yake akaaga kazini kwa kuomba likizo ya dharula ya bila malipo ili aende akapafahamu ni wapi anaishi Ramaah.



    Kwa kuwa ilikuwa ni likizo ya bila malipo, akaruhusiwa kwa kupewa siku tatu tu wakiamini zitamtosha, nae kwa kuwa alikuwa amelenga siku mbili mbele za mapumziko, hivyo akapata idadi ya siku tano.



    Kazi ikawa kwa Ramaah, ni wapi sasa aende? Nyumba yake ana muda mrefu sana hajajua hata ipo kwenye hali gani, nani anaishi kwa sasa na pia mazingira yakoje kwenda na mgeni, akakuna kichwa na kufanya maamuzi.



    Serikali ina jukumu la kumsafirisha raia wake aliekwama eneo ambalo si la makazi yake, na hicho ndio kilichpotokea kwa Ramaah, kwa msaada wa Hospitali, alipewa tiketi ya kumrejesha Jijini Dar es Salaam.



    Hivyo ikamlazimu Scholler ajilipie nae nauli yake, kitu ambacho wala hakikuwa kizito, maana alikuwa ameisha ingia ndani ya pendo, alifurahi tu kukubaliwa kwenda pamoja na Ramaah hadi nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam.



    Safari yao moja kwa moja iliishia Mbagala kwa Daud, Daud na mkewe walifurahi sana kumuona Ramaah pale lakini walishangaa kumuona akiwa na Stellah, mtu ambae wao tu hawakutamani kumuona, iweje yeye leo awe nae?



    Hawakuwa na subira, hasa mke wa Daud, hakutaka kusubiri, pale pale akamuuliza imekuwaje awe na Stellah na amemtoa wapi? Ramaah akamuangalia Scholler na kutabasamu kisha kamwambia atulie atawahadithia baadae.



    Hakuna ambae alikuwa yupo tayari kuendelea kusubiri kusikiliza baadae, lakini ndio hivyo, anaejua ndio amekataa kwa muda huo, wao watafanyeje? Wakawa wapole tu wakisubiri huo muda atakao yeye ufike.



    Walikula baada ya kuoga na kisha wakakaa wakitazama TV ndio muda huo Ramaah akautumia kuwaambia kwamba Yule aliekuja nae pale si Stellah, bali yule ni Scholler.



    Daud na mkewe walitazamana na kushangaa sana waliposikia kuwa yule sio Stellah, hawakuwa na tofauti kubwa kwa sura na hata maumbo.



    Sema huyu alionekana kama ni mnene wakati Stellah alikuwa ni mwembamba, hivyo walidhani huenda amenenepa hapo kati walipo potezana nae.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa ndio wakamtaka radhi Scholler kwa kutoa maneno makali mbele yake nae akawaomba wala wasijali, hivyo rasmi wakawakaribisha kwa mara ya pili kwa mikono miwili.



    Walikaa pale kwa siku chache wakari Ramaah akifanya marekebisho madogo madogo kwenye nyumba yake ya Ilala kwani ilikuwa ina muda mrefu haijatumika ilikuwa imefungwa tu.



    Aliifanyia usafi wa kiujumla, kuanzia rangi za ukutani hadi maua bustanini. Mwisho ndio akamfuata Scholler kule Mbagala kwa Daud na kuhamia Ilala.



    Siku tano za mapumziko ziliisha hata bado Scholler hakuwa ameridhia kuondoka.



    Haikuchukua muda mrefu akawa tayari kurejea kazini, wala hakukuwa na longolongo, maana alikuwa kwenye likizo ya dharula, likizo ya ugonjwa ambayo huwa inatokea tu mara moja kwa ghafla na haiahitaji maandalizi.



    Baada ya kuwasili ofisini alimuulizia Imma lakini akaambiwa hayupo, ameenda Congo DR kuongoza mapambano dhidi ya waasi, alimuombea mema tu.



    Kwa wale waliokuwepo pale walimwambia kilichosababisha yeye apelekwe huko ni ubora wa kazi yake.



    “Kwenye ile kazi uliyofanya nae, ile ‘Operation okoa mtoto’ ndio ilisababisha apewe nafasi hiyo, maana aliifanya vizuri sana wakamuona anafaa kwenda Kongo ambapo yupo huko hadi sasa,” Sajenti mmoja wa Jeshi alimwambia na Kanali mmoja akadakia



    “Hata nae siku wanaapishwa kwa ajili ya safari, alikuwa akisikitika sana na kusema angeona fahari sana kama nawe ungekuwepo…” Ramaah akatikisa tu kichwa na kusikitika.



    Scholler nae kwa upande wake kazi ikawa ndio basi tena, akawa ni mama wa nyumbani akisubiri siku tu ya kujifungua, kila kitu sasa kikawa juu ya Ramaah ambae kwa awamu hii alijitahidi kutokuonesha mapenzi sana, tayari alikuwa ameumizwa moyo…

    **********



    Miezi 9 ikatimia, Scholler akajifungua mtoto mzuri wa kike, wakamuita Aggy, mtoto alie ongeza furaha kwenye familia ile na Amani ikazidi kutawala.



    Likizo yake ya kwanza Ramaah akaitumia kwenda kwao kumtambulisha Scholler.



    Wazazi na ndugu pia jamaa wa Ramaah walipomuona Scholler walijawa na hasira na hawakumpa mapokezi mazuri kwa kudhania yule ni Stellah.







    Ramaah alikuwa tayari alikuwa amelitambua hilo mapema na tayari pia alikuwa amempa tahadhari Scholler juu ya suala hilo, hivyo kwa kuwa tayari walikuwa wamejiandaa kisaikolojia, wala haikuwaathiri kwa njia yoyote.

    Walichofanya ni kuwaambia na kuwaeleza kuwa yule pale mbele yao sio Stellah, yule ni Scholler, ilikuwa ni vigumu lakini mwisho wakaelewa. Pamoja na kuelewa kwao, hawakumpa asilimia 100 Scholler kuwa ni chaguo sahihi kwa Ramaah.

    Siku 5 ziliwatosha kukaa Tabora na kutoka kuelekea Kilimanjaro nyumbani kwao Scholler, walipokelewa vizuri sana, wao hawakumtambua Ramaah zaidi ya kumuona kwenye picha tu, walikaribishwa kwa vigelegele na kina mama wa kichagga.

    Scholler alionekana kuwa ni mtu mwenye furaha sana kuliko wote pale nyumbani, akamuulizia dada yake, akajibiwa kuwa ametoka kwenda mjini ila iliahidi kurejea jioni ile, Ramaah hakujua ni nani aliekuwa akiuliziwa, hivyo hata hakushughulika nao alikuwa akitazama mandhari nzuri ya kijiji kile na kilimvutia sana, akatamani pale ndio angekuwa anaishi yeye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    **********



    Jioni saa 12, Scholler na familia yao nzima ilikuwa imekaa ikiongea na kubadilishana mawazo, Ramaah alikuwa amembeba mtoto wake akiwa amekaa pembeni ya Scholler akaingia Stellah! Mshangao alio upata Ramaah na Stellah, kila mtu aliuona.

    Scholler hakushangaa, lakini wazazi wa Scholler walishangaa na kujiuliza kulikoni? Stellah akahoji

    "Ramaah unafanya nini hapa?" Swali lile likawahiwa na Scholler, sio kulijibu, bali kulipoteza

    "Dada si ukae kwanza chini jamani? haraka ya nini? kaa upumzike dada yangu" jibu lile likamfanya Stellah akae chini akiwa ni mwenye mawazo lukuki

    Baba yaoa akauliza kama Stella na Ramaah wana fahamiana? Stellah akajibu ndio, akaulizwa na mama yake anamfahamu kivipi? akawa anashindwa kufunguka, lakini hatimae aliweza kuwaeleza na kuomba msamaha

    Suala lile lilikuwa ni geni kwenye masikio ya wazazi, waliwahi kumsikia Ramaah kwenye simu lakini hawakuweza kumjua kama Ramaah mwenyewe ndio huyu ambae pale ameletwa na mtu mwingine ambae ni Scholler.

    Wakiwa hawajapata jibu sahihi la kipi cha kufanya, Stellah akasimama na kumsogelea Ramaah na kumuomba msamaha.wazazi wakawa wakitazama tu ni hatua gani atakayo chukua Ramaah. kibaya zaidi hata nae hakujua ni ninin cha kufanya hadi Scholler alipo nyanyuka na kwenda kumnyanyua dada yake na kumketisha huku akilia.

    Scholler sasa baada ya kumketisha na kumnyamazisha, ndio akaanza kumpa ukweli wake, Stellah alitamani Ardhi ipasuke imfunike, aliona aibu sana, akabaki akilia tu, huruma ikawa ingia wote, kwa kuzuga tu, Ramaah akamuuliza Stellah yu wapi mtoto?

    Kilio kikaongezeka, kilipo pungua ndio akawaeleza kwamba mara ya mwisho Ramaah kuwaacha kule Kigamboni, walirejea Jijini na kuendelea na maisha kama kawaida wakiishi na mtoto wao bila kujua kama Amani ana mke kule Zanzibar.

    Siku moja jioni wakiwa wamekaa nje ya nyumba yao, ghafla mke wa Amani akavamia na kuanzisha vurugu kubwa, akamshambulia sana Stellah na kuondoka na Aman baada ya kumuonyesha Stellah cheti cha ndoa iliyo fungwa kiislamu huko Zanzibar.

    Wakaondoka na kuniacha nyumbani nikiwa na mwanangu tu, hapo tayari mie nae tulikuwa tumetenganishwa ofisi, mie nikawa nimepelekwa Ilala na Amani akawa yupo Kibaha, hatukuweza kuonana na ajabu hata mawasilianao yakawa hakuna kabisa.

    Siku moja nikiwa ndani na mwanangu tunatazama katuni, mwanangu alikuwa na furaha tele, tukasikia mlango umegongwa, mtoto akaenda kufungua, nikamsikia akimpokea baba yake, nikishangaa leo imekuwaje tena. nikasimama kumpokea.

    kumbe hakuwa maekuja peke yake, siku hiyo alikuwa kaja na mama yake, na hata kabla ya kueleza kilicho waleta, tayari niliona kabisa kuwa wlaikuja kishari, maana walionesha kuwa ni wakali mno, nilijitahidi kupambana, lakini wapi! wakanizidia na kuondoka nae.

    "Nilichanganyikiwa ila sikuwa na cha kufanya, nikawaomba tu niwe nawasiliana nao, mwanzoni iliwezekana ila baadae wakanikatia mawasiliano. maisha upande wangu yakaanza kuwa mabaya, sikuwa nimezoea kuwa mbali na mtoto wangu wala Amani"

    Alieleza kwa kirefu kuwa mwenendo wa kazi ukawa ni mbaya, ikamlazimu kuomba likizo fupi kazini na ndio sababu yupo pale nyumbani akijaribu kupoteza mawazo.

    Kwa kuwa nae alikuwa nyuma ya habari zilizo mtokea Ramaah, Scholler akamueleza kiufupi tu. Habari zile zilimliza zaidi Stellah na kumuomba Ramaah msamaha wa Dhati. hakuwa na kinyongo tena, Ramaah akamwambia Stellah ameisha msamehe na akautumia muda ule kumtambulisha Scholler kama ndie mchumba wake na mkewe mtarajiwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Roho ilimuuma sana Stellah ikiwa yeye ndio alie anza kuipata ile nafasi na kuchezea, alijiuliza mwenyewe, nani amlaumu? akakosa mtu wa kumtwisha mzigo wa lawama. ikamlazimu tu sasa atoe baraka zake hasa ukizingatia tayari walikuwa wmeisha zaa.

    Alichomsisitizia mdogo wake ni kutokuja kuichezea ndoa, na kumtaka aje kuwa ni mke bora na mfano kwa watu wengine, kitu ambacho Scholler aliona kama Stellah anajichanganya tu, maana kama ni somo yeye tayari ameisha lipata kupitia yeye.

    Siku mbili mbele ikafungwa ndoa ya kimila na baada ya siku 3 wakaondoka wote kurejea Dar wakiwa ni wenye baraka tele za wazazi, hadi sasa familia yao imekuwa ni ya mfano mwema kwa wakazi wa Ilala na mapenzi makubwa, ikiwa sasa ni familia ya watu watano.



    Mwisho

    *********







0 comments:

Post a Comment

Blog