Simulizi :Barua Kutoka Kwa Marehemu
Sehemu Ya Nne (4)
Bado Jeff hajayabandua macho yake usoni mwa Roy ambaye hazungumzi kitu. Zimeshakatika dakika kumi tangu Jeff amefika katika hoteli hiyo, Sinza jijini Dar es Salaam. Wamebaki wanaangaliana.
“Nakusikiliza kaka...” Jeff akasema.
“Acha presha mkubwa, lakini nataka kukuambia kwamba, haya mazungumzo yetu ni siri kubwa sana. Gerald hatakiwi kujua kama niikutana na wewe.”
“Mbona sikuelewi?”
“Utanielewa tu, kaka tulia kwanza.”
“Ok! Nakusikiliza.”
“Kwanza nakuomba sana, usipaniki kwa haya nitakayokuambia, wewe ni mwanaume na ni vyema kuyachukua kama yalivyo. Kikubwa unachotakiwa kufahamu ni kwamba, nimeamua kwa moyo mmoja kukusaidia.
“Sikiliza Jeff, najua unaamini kwamba nimekuja pale kwa ajili ya kufanya kazi ya Afisa Masoko, sivyo?”
“Ndiyo!”
“Sasa ukweli sio huo, nimekuja kwa kazi nyingine kabisa, ambayo sitaki kuifanya.”
“Ni nini?”
“Una mchumba anaitwa Davina?”
“We’ umemjuaje?”
“Unaye au huna?”
“Ninaye.”
“Gerald anamfahamu?”
“Ndiyo!”
“Ok! Sidhani kama nina haja ya kuzunguka kiasi hicho, lakini ukweli ni kwamba, Gerald anamtaka mchumba’ko!”
“Unasema?”
“Acha papara, hilo ni dogo sana, tulia kwanza, kuna kubwa zaidi.”
“Lipi?”
“Ili aweze kumpata, amepanga kukua!”
“What?”
“Ndiyo...na mimi nipo pale kazini kwa ajili ya kukuua wewe!”
Jeff akayatoa macho yake kwa mshangao mkubwa, hakuamini kama maneno yale yalitokea kinywani mwa Roy.
Afisa Masoko!
*****
KWA muda mrefu sasa, Jeff alikuwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Roy kwa mshangao mkubwa! Haikuwa rahisi kuamini kwamba Roy alikuwa akizungumza maneno yale kwa kumaanisha. Akayatembeza macho yake katika mwili mzima wa Roy!
Bado hakutaka kuamini!
Alihisi kama anaota, tena ndoto ndani ya ndoto hiyo anayoiota. Yaani Gerald anataka kumuua ili aweze kuwa na Davina? Mbona ni jambo jipya na la ajabu sana?!
“Sikiliza Roy, tunafanya kazi pamoja siyo?” Hatimaye Jeff akasema kwa sauti ya unyonge sana.
“Ndiyo!”
“Wewe unafanya kazi chini yangu siyo?”
“Ndiyo!”
“Mimi ni bosi wako...nadanganya?!”
“Uko sahihi kabisa.”
“Sasa ni vizuri ukatambua na kuheshimu mamlaka yangu, siamini kama tunapaswa kutaniana kiasi hiki, tena utani mkubwa kama huu, ambao unahusu maisha yangu. Hata kama unatania, lakini nadhani ni bora kama utabadilisha utani wako!”
“Sikiliza Jeff, kwanza nazidi kukusisitiza kwamba jambo hili ni siri, hutakiwi kuvujisha hii siri. Halafu kaa ukijua mimi ni Mafia, sitakuwa tayari kukuacha hai kama nikijua hii siri imevuja.
“Hii ni kwa faida yako, kazi yangu ilikuwa ni kukuua, lakini kwa moyo wangu wa upendo, umeamua kukusaidia, lakini sasa naona huamini mpaka haya mambo yatakapokukuta,” alisema Roy akiwa amemkazia macho Jeff.
Jeff alikuwa kimya kama anayefikiria jambo zito sana kichwani mwake, jambo linalomchanganya na kumkosesha kabisa furaha. Kwa muda akauacha ubongo wake uchanganue mambo wenyewe. Akajiuliza maswali mengi sana. Kwamba inawezekana vipi Roy amfahamu Davina wakati alikuwa mgeni ofisini kwao, tena hawakuwa na mazoea kabisa?
Hapo sasa akaanza kuhisi kwamba yawezekana kuna ukweli fulani katika jambo lile.
“Umesema unamfahamu Davina.”
“Namsikia.”
“Kutoka kwa?”
“Gerald.”
“Gerald?”
“Sikiza, acha maswali yasiyo na maana, tunatakiwa kupanga jinsi ya kukuokoa, wewe unatakiwa kufa, tenda imekuja ofisini kwetu, cha msingi ni kuangalia kilicho mbele yetu siyo mambo yaliyopita.”
“Kwahiyo tutafanyaje?”
“Hilo ndiyo swali sasa...kila kitu nimeshapanga, wiki mbili baadaye tutapangiwa safari ya kikazi kwenda Dodoma, katika safari hiyo wewe unatakiwa kufa njiani katika ajali ya kutengeneza...” Roy akasema, Jeff akimsikiliza kwa makini.
“Mungu wangu!”
“Ndiyo hivyo, sasa wewe unatakiwa kutulia. Fuata maagizo yangu.”
“Sawa.”
“Kwanza lazima ujue mimi nafanya hii kazi kwa malipo makubwa, lakini nimeamua kusaliti kwa ajili yako. Unatakiwa kunipa kifuta machozi kidogo.”
“Kiasi gani?”
“Sitaki pesa nyingi sana, niandalie milioni tano tu!”
“Nitakupa usijali, kwahiyo tutafanyaje?”
“Usiwe na shaka na hilo. Kipo kitu cha kufanya, wewe utaonekana umekufa na jamii nzima itaamini hivyo.”
“Kivipi?”
“Tutakwenda pamoja katika hiyo safari, lakini wewe fanya maandalizi yako ya jumla, tukiondoka tutafika mahali tutaachana, utavua nguo ulizovaa na kunipatia, pamoja na kitambulisho chako, halafu wewe utaondoka zako, uende katika mkoa mwingine kabisa.
“Huko utaishi maisha mapya, ukiwa tofauti na ulivyo hapa Dar. Lazima ubadilishe staili yako ya maisha. Kwa kifupi uwe mwingine!”
“Hapo nimekuelewa, lakini sasa nitajulikana vipi nimekufa wakati nitakuwa nimeondoka?”
“Ndiyo maana nikakuambia utaacha nguo zako pamoja na kitambulisho!”
“Ni kwa ajili ya nini?”
“Nitatafuta maiti ambayo nitaivisha nguo zako na kuweka kitambulisho chako, kila mtu atajua ni maiti yako!”
“Sasa huoni kwamba sura zitakuwa tofauti?”
“Ataharibiwa sura, haitatambulika kabisa, alama itakuwa ni nguo na kitambulisho chako.”
“Mh! Kweli kazi ipo.”
“Ndiyo hivyo...enhee sema unapenda kwenda mkoa gani?”
“Nitaenda Mwanza, kule ni pazuri zaidi kwa kujificha, nitaanza maisha yangu kule.”
“Sawa, nadhani tumemaliza, lakini naendelea kukusisitiza kwamba haya ni mazungumzo ya siri. Usijaribu kumwambia mtu yeyote yule. Fanya maandalizi yako taratibu na kimya kimya. Chukua fedha zako kwenye akaunti mapema, safari ni muda wowote kutoka sasa.”
“Poa kaka, nimekuelewa vizuri sana.”
Kilichoendelea hapo ilikuwa ni kunywa pombe kwa kasi ya ajabu.
*****
*****
SIKU KUMI BAADAYE
Kilikuwa kipindi kigumu sana kwa Jeff, akiwaza namna ya kuishi maisha mapya. Tayari alikuwa ameshaanza kuweka mipango yake ya safari vizuri. Akatoa fedha kwenye akaunti zake karibu zote, akawa tayari kwa lolote.
Pamoja na kujiandaa kwa safari ya maisha mapya, bado hakumuamini Roy kwa asilimia mia moja, alihisi kama alikuwa na nia ya kumtapeli fedha zake, hivyo hakumpatia zile fedha mpaka siku ya safari itakapofika. Roy hakuwa na tatizo na hilo, maana maelezo yake siku zote yalikuwa kwamba anamsaidia kwa nia njema na zile fedha ni kama maji ya kunywa tu!
Lakini asubuhi hii, ndipo alipoanza kuamini kwamba yale yote aliyoambiwa na Roy yalikuwa ya ukweli. Alipoingia tu ofisini, Sekretari akamwambia bosi Gerald alikuwa akimuhitaji ofisini kwake. Mara moja akaenda hadi ofisini kwa Gerald, akamkuta Roy akiwa amekaa mbele ya Gerald wakimsubiri yeye.
“Habari za asubuhi bosi!” Jeff akamsalimia Gerald.
“Nzuri kaka, za nyumbani?”
“Salama tu.”
“Kaka vipi?” Roy akamsalia Jeff.
“Njema kaka, za kwako.”
“Namshukuru Mungu!”
“Yes! Wakubwa. Nimewaita hapa kwa agizo moja muhimu,” Gerald akasema kisha akameza fundo moja la mate.
Jeff akakaa sawasawa kwenye kiti chake, alishajua kitakachosemwa na Gerald.
“Kifupi mnatakiwa kwenda Dodoma keshokutwa jioni, mnatakiwa mkafanye ukaguzi wa Tawi letu la huko, pia mtatoa Semina Elekezi kwa watumishi wetu. Kwa muda mrefu sasa, siridhishwi na ripoti za Dodoma, nahisi kuna kitu. Sasa mnatakiwa muende kule, mtakuwa huko kwa wiki moja.
“Taratibu nyingine zinaendelea vizuri, gari lipo lakini kwasababu tuna uhaba wa madereva, mtaendesha wenyewe mkipokezana. Naamini wote ni madereva wazuri kwahiyo mtabadilishana kwenda na kurudi.”
Wote wakatingisha vichwa, kuashiria kukubaliana na alichokiongea.
Wakatawanyika!
Jeff alihisi moyo kutaka kutoka, hapo aliamini kweli Gerald alikuwa na roho ya kinyama sana. Hakuamini kabisa alichokisikia, lakini pia ilikuwa vigumu sana kwake kuamini kuwa Roy alikuwa muuaji! Hapo aliamini.
Jeff alipofika ofisini kwake, mara moja akamwandikia Roy meseji: “Kaka nimeamini, inabidi nifanye maandalizi mazuri na kwa siri sana.”
“Ni kweli, hata Davina hatakiwi kujua kabisa kuhusu hili. Tuachane na mambo ya simu, tukutane jioni pale pa siku ile, tujadiliane vizuri. Uje na mzigo wangu kabisa.”
“Sawa.”
*****
Kitu cha kwanza Jeff kufanya baada ya kukutana na Roy jioni hiyo ilikuwa ni kutoa fedha kiasi cha milioni tano na kumpatia. Mipango ikaanza...
“Nadhani sasa umeniamini, hatuna muda wa kukaa sana hapa, kama tulivyozungumza, wewe andaa mambo yako na mimi naandaa mambo yangu, lakini itabidi uniongeze milioni moja!”
“Za nini tena?”
“Tunatakiwa kupata maiti, suala la maiti si tatizo, ninao vijana wa kazi ambao watahangaikia hili ndani ya siku tatu, lakini natakiwa kuwalipa.”
“Kesho asubuhi nitakuja nazo ofisini.”
“Sawa.”
Kikao kikafungwa.
*****
Usiku mzima Jeff alikuwa na Davina wake wakipeana mahaba mazito, alijitahidi sana kuhakikisha anamuacha mpenzi wake akiwa ameridhika vya kutosha. Pamoja na yote, hakuonesha dalili hata moja, kwamba safari yake ya siku inayofuata ilikuwa ya moja kwa moja!
Hiyo ilibaki kuwa siri yake mwenyewe ndani ya moyo wake, hakuruhusu kabisa jambo hilo lijulikane na mpenzi wake Davina. Asubuhi Jeff alimuaga mpenzi wake, lakini Davina alionekana kukosa furaha.
“Vipi mbona unakuwa hivyo?” Jeff akamwuliza Davina.
“Unaniacha peke yangu!”
“Kwani nakwenda kufa, ni safari ya wiki moja tu mpenzi wangu.”
“Haya bwana, lakini sijui kwanini moyo wangu hauna amani na safari yako....sijui kuna nini?!!” Davina alisema kwa sauti ya taratibu sana akimaanisha alichokiongea.
Jeff alishtushwa sana na kauli ile, kichwani mwake kukagonga kengele ya hatari.
*****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jeff alihisi kupoteza furaha ghafla, hakuweza kuelewa ni kwanini Davina alisema hana imani na safari yake. Ndani ya moyo wake alijua kila kitu kinachoendelea, lakini hakutakiwa kueleza chochote kwanza, ilikuwa mapema sana kwake kufanya hivyo!
Mapema sana...
“Kwani unahisi nini?”
“Hata mimi sijui.”
“Hujui?”
“Ndiyo sifahamu kabisa.”
“Sijakuelewa bado.”
“Baby sifahamu kwanini sina amani na safari yako, lakini kikubwa moyo wangu una mashaka sana. Umeingiwa na baridi ya ghafla, nahisi kutakuwa na tatizo.”
“Hapana usiwaze hivyo mpenzi wangu, amini kwamba nakwenda Dodoma kikazi na nitarudi salama, kikubwa unatakiwa kuniombea kwa Mungu niende na kurudi salama.”
“Sawa mpenzi wangu, nitafanya hivyo.”
“Hilo ndiyo la msingi.”
“Tulale basi mpenzi wangu.”
“Haya...sogea basi huku...”
Jeff akamsogelea mpenzi wake, wakakumbatiana kimahaba. Taa ikazimwa, wakalala.
*****
Bado Davina anaendelea kumng’ang’ania Jeff huku akilia kwa uchungu, katika maisha yao ya kimapenzi, hakuwahi kuwa na uchungu na safari yoyote ya Jeff ya kikazi kama siku hiyo. Moyo wake ulikuwa mzito kuliko kawaida, hata yeye mwenyewe alishindwa kuelewa ni kwanini alijihisi mzito kiasi kile.
Amejilaza kifuani mwa Jeff, akilia kwa uchungu bila kukoma, hana dalili za kunyamaza kabisa.
“Davina nachelewa...” Jeff akamwambia.
“Kwani ni lazima uende?”
“Ingekuwa nakwenda kutembea, isingekuwa lazima sana kwenda, lakini kwasababu nakwenda kikazi ni lazima...”
“Baby....”
“Unasemaje?”
“Bado nakuhitaji sana Jeff wangu.”
“Hata mimi pia nakupenda na ninakuhitaji sana mpenzi wangu, wewe mwenyewe ni shahidi wa hilo.”
“Sawa bwana, safiri salama mpenzi wangu, fahamu kwamba nakupenda sana, moyoni mwangu kuna mzigo mzito wa mapenzi juu yako, siwezi kuishi bila wewe mpenzi wangu.”
“Siku zote nimekuwa nikilitambua na kuliheshimu sana hilo, itaendelea kuwa hivyo siku zote za maisha yangu.”
“Ahsante sana,” Davina akajibu akitabasamu.
“Sasa unaniruhusu, siyo mpenzi wangu?”
“Moyo wangu mweupe.”
“Ahsante sana.”
“Lakini bado sijafanya kitu kimoja.”
“Nini?”
“Sijakubusu mpenzi wangu.”
“Hilo tu, mbona rahisi sana, midomo hiyo hapo...mashavu hayo hapo....paji la uso hilo hapo....nibusu popote upendapo...” Jeff akasema akiachia tabasamu mwanana sana usoni mwake.
Davina naye akatabasamu.
Akamsogelea Jeff kisha akaanza kumwangushia mvua ya mabusu motomoto. Wakaagana kwa furaha.
*******
Ndani ya ofisi ya Gerald mchana huo, walikuwa wamekaa Gerald, Jeff na Roy wakijadiliana juu ya mipango ya safari. Kila kitu kilikuwa tayari, kilichokuwa kinasubiriwa ni muda wa safari tu.
“Nadhani mpo tayari kwa safari sasa,” Gerald akawauliza.
“Ndiyo boss,” Roy akajibu haraka-haraka.
“Gari linamaliziwa kufanyiwa service ya mwisho, endeleeni na kazi kwanza, mpaka saa kumi, gari litakuwa limeshaletwa. Si vibaya kama mtaanza safari yenu saa kumi na moja jioni!”
“Tena ni muda mzuri sana, barabara inakuwa imetulia na lami imepoa!” Roy akasema.
“Sawa, endeleeni na majukumu mengine, baadaye.”
“Ok!”
Wakatawanyika.
Saa kumi na moja kamili, kama walivyokubaliana walikuwa wanaanza safari yao ya kwenda Dodoma. Wakaagana na Gerald ambaye alikuwa ana furaha sana, alifurahia safari hiyo maana alijua ilikuwa safari ya mwisho ya Jeff. Safari ambayo ingempa uhuru wa kuwa na Davina, mwanamke ambaye aliufanya mateka moyo wake.
Safari ya Dodoma ikaanza. Waliingia Chalinze saa 12:15 za jioni, Roy akaegesha gari nje ya baa moja maarufu iliyochangamka pale Chalinze. Waliamua kupumzika kwa muda kwa ajili ya kulanisha makoo yao kwanza.
“Sasa kaka, kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kufanya ni kubadilisha nguo zako.”
“Ok!”
“Halafu unipatie kitambulisho chako pamoja na vitu vingine muhimu, ifupi uache pochi yako, pesa ondoa ila acha vitu vya muhimu ambavyo vitaweza kutumika kama alama yako.”
“Nimekuelewa kaka.”
“Hata simu yako, inabidi uiache.”
“Hapo tutakuwa tumecheza, kila mtu atajua nimekufa.”
“Sasa hili zoezi litafanyika wapi?”
“Hapa hapa!”
“Wapi sasa?”
“Chooni, hakuna pengine. Acha niende mara moja na begi langu.”
“Poa kaka, fasta.”
“Usijali.”
Dakika tano baadaye, Roy alirudi akiwa amevaa nguo zingine, kofia ya pama na miwani ya jua. Akaketi kitini na kumalizia bia yake haraka.
“Kaka hapatufai tena hapa, tuondoke...” Roy akamwambia Jeff.
“Poa, twende.”
Wakasimama na kurudi zao kwenye gari, wakaondoka kwa kasi. Njia nzima walikuwa wakizungumza na kuweka mipango yao sawa. Mara simu ya Roy ikaita, alipotizama kwenye kioo cha simu yake, akakutana na jina la Kijasho. Akatabasamu na kupokea mara moja.
“Niambie kaka...” Roy akatamka maneno hayo, mara baada ya kupokea simu.
“Poa, mambo shwari kabisa.”
“Uko wapi?”
“Nimeshapita Chalinze nakuja, mzigo umepatikana?”
“Ndiyo, ninao hapa!”
“Tayari mmeshauharibu sura?”
“Kaka mwenyewe utapenda, hajulikani kabisa.”
“Poa, tutakutana mbele kidogo ya Mikese.”
“Haya, utanijulisha ukikaribia.”
“Poa.”
Roy alipokata simu, akasimamisha gari pembeni.
“Kaka mambo yanataka kuanza, naona hapa panakutosha, shukia hapa subiri basi la Morogoro, nenda ukalale hapo, asubuhi na mapema fanya mipango ya safari ya kwenda Mwanza.”
“Poa.”
“Hakikisha huonekani sura hovyo, sawa?”
“Poa mkubwa, nimekuelewa vizuri sana.”
Roy hakuondoa gari haraka, akasubiri mpaka Jeff alipopanda basi ndipo naye akaondoka polepole. Aliendelea kuendesha polepole, akitaka giza liingie. Kuna wakati aliamua kuegesha kabisa njiani kwa muda, akijifanya anakagua gari, lakini nia yake ilikuwa ni giza.
Mwanga haukuwa na kazi na yeye kabisa, ilipotimu saa 1:16 za usiku, akaingia garini na kuanza tena safari. Akiwa kilometa tano kabla ya kufika Mikese, akaegesha gari pembeni kwenye pori dogo kando ya barabara kisha akampigia simu Kijasho.
“Uko wapi Kijasho?”
“Mikese, hapa kwenye mizani.”
“Njoo mbele kama unakuja Chalinze, soma kilometa tano, utaona gari langu.”
“Poa.” Baada ya muda Kijasho alikuwa ameshafika sehemu aliyoagizwa.
“Kaka hapa noma, tuingize magari ndani kidogo.”
“Haina shida.”
Zoezi hilo likafanyika haraka, halafu kilichofuata hapo ikawa ni kuivalisha ile maiti nguo za Jeff, ikawekewa pochi yenye kila kitu muhimu pamoja na simu. Baada ya hapo, wakaibeba na kuiingiza kwenye gari la Roy. Malipo yakafanyika chapchap na kuagana.
“Kaka ahsante sana, waweza kwenda.”
“Poa, kazi njema, ni dili gani lakini?”
“Najua mwenyewe.”
“Poa kaka.”
“Lakini nikutahadharishe kwamba, ikiliki tu mimi na wewe!”
“Hatuaminiani kiasi hicho?”
“Tunawekana sawa tu.”
“Usijali.”
Kila mmoja akaondoka na njia yake, Kijasho akaenda na barabara inayoelekea Chalinze, Roy akashika barabara inayoenda Morogoro. Akili yake ikiwa sehemu ya kuliingiza gari. Akakanyaga mafuta kisawasawa, alipofika eneo lenye mteremko mkali, pembeni kukiwa na mti mingi, akalipeleka gari usawa wa ile maiti na kuligongesha upande mmoja!
Kilichosikika baadaye ilikuwa ni mshindo mkuu!
Ilikuwa ajali mbaya sana.
****
KWANZA ulisikika mlio mkali wa kupasuka matairi halafu kukawa kimya. Hakuna sauti ya binadamu iliyosikika baada ya mlio ule. Roy alikuwa katika hali mbaya sana na hakujitambua! Alipoteza fahamu pale pale!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda mfupi baadaye, magari mengine yaliyokuwa yakipita eneo lile yalisimama na kushudia ajali ile mbaya. Haraka simu ikapigwa Polisi na muda mfupi baadaye, gari lenye maasakari kutoka Kituo cha Polisi Mikese likafika. Roy akatolewa na kupakiwa kwenye gari pamoja na ile maiti.
Kilichofuata hapo ilikuwa ni kuwapeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu, hawakugundua kwamba moja ilikuwa maiti tayari. Baada ya kufika hospitalini na uchunguzi kufanyika, ile maiti ikagundulika tayari ilikufa! Lakini kwa bahati mbaya sana, iliharibika sana sehemu ya usoni. Kama walivyofikiria ndivyo ilivyokuwa, wakaikagua mifukoni na kuona kitambulisho pamoja na pochi yake ambayo ilikuwa na vitu vyake mbalimbali.
Kitambulisho kile kiliandikwa jina la Jeff Sebastian. Taarifa zikapelekwa Makao Makuu na usiku huo huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro akatoa taarifa kupitia redio Abood na Ukweli za mjini humo.
******
Hadi saa 7:30 za usiku, Master alikuwa na Gerald ofisini kwake, wakinywa sana pombe usiku huo. Hamu yao kubwa ilikuwa ni kusikia Jeff ameshafariki. Hilo halikutokea. Mbaya zaidi, simu ya Roy ilikuwa haipatikani mpaka muda huo.
Master akaona njia pekee pale ni kuwapigia vijana wake ambao walikuwa njiani wakimsubiri Roy. Akaweka glasi ya wine mezani, akanyanyua simu na kubonyeza namba za mmoja wao, akapeleka dole gumba katika kitufe cha kupiga.
Akapeleka simu sikioni.
“Hallow!”
“Ndiyo boss!”
“Mbona kimya?”
“Tumepoteza mawasiliano mkubwa.”
“Mmepoteza mawasiliano, kivipi?”
“Roy hapatikani!”
“Hata sisi pia hatumpati, tukajua kwamba yawezekana kazi yenu mmeshaimaliza....”
“Hapana mkuu...”
“Kwahiyo hamjakutana mpaka muda huu?”
“Ndiyo, lakini sisi tupo kamili tunasubiri kazi tu.”
“Anyway, endeleeni na kazi, nitawapigia baadaye.”
“Sawa mkuu.”
Simu zikakatwa.
Gerald na Master wakaangaliana.
“Sasa...” wakati Gerald akitaka kuzungumza jambo, mara simu yake ikaita.
Alipotizama kwenye kioo akakutana na jina la Jerome; huyu ni mfanyabishara mkubwa mjini Morogoro ambaye ni rafiki yake mkubwa.
“Samahani kaka niongee na huyu mtu, sijui ana nini hadi ananipigia simu usiku huu, inawezekana ana ishu muhimu.”
“Poa ongea naye kaka.”
“Hallow...”
“Kaka!”
“Nipe ripoti mkubwa.”
“Aisee pole sana....” Jerome akasema kwenye simu kwa sauti ya taratibu sana.
“Ya nini tena, mbona unanitisha? Au ile zabuni niliyoomba nimezidiwa na wajanja wa mji kasoro bahari nini kaka?”
“Hapana.”
“Ni nini hasa? Niambie, roho yangu ipo juu juu!”
“Gari yako imepata ajali huku Morogoro na vijana wako wawili walikuwa ndani ya hilo gari. Mmoja amefariki, mwingine ana hali mbaya, hajazinduka mpaka sasa hivi.”
“Ni kweli nina vijana wangu wawili walikuwa safarini usiku huu kuelekea Dodoma, wamepata ajali?’
“Tena mbaya sana, mi nimesikia redioni kwenye gari, nikiwa natokea zangu Kilakala nilipokuwa nakunywa na rafiki zangu, nikaamua kuja moja kwa moja mpaka hapa hospitalini.”
“Mungu wangu, ni nani huyo aliyekufa?” Gerald akauliza akiwa na shauku sana ya kutaka kujua aliyekufa ni nani.
“Ameharibika vibaya sura, siyo rahisi kumtambua, lakini kwa kupitia simu, kitambulisho na vitu vingine alivyokuwa nayo, imegundulika kwamba anaitwa Jeff Sebastian na huyu mgonjwa ni Roy Maketo!”
“Ndiyo hao hao...sasa mi nakuja usiku huu huu, nikifika nitakujulisha ndugu yangu.”
“Sawa kaka, pole sana ndiyo maisha.”
“Ahsante.”
Alipokata simu akamgeukia Master akiwa anatabasamu.
“Vipi kaka?”
“Tayari!!!”
“Niambie....”
“Kashakufa nyang’au yule, lakini inaonekana ni kwa ajali ya bahati mbaya, maana taarifa zinasema hata Roy hana hali nzuri.”
“Hana hali nzuri?”
“Ndiyo!”
“Duh! Hapo sasa lazima tuwe makini....nimesikia ukiambiwa kitu kama hajarejewa na fahamu siyo?”
“Ndiyo!”
“Ni hatari, anaweza kuzinduka na kujikuta akianza kutoa siri yetu, lazima tuwe wajanja hapa kaka.”
“Tufanyeje sasa?”
“Anatakiwa kuhamishwa hospitali usiku huu huu.”
“Wataturuhusu kweli?”
“Pesa itaongea....”
Gari mbili aina ya Land Cruiser usiku huo huo zilitoka kuelekea Morogoro. Moja ikiwa imewabeba Gerald na Master wakiwa wanaendeshwa na dereva wao na lingine likiwa limebeba vijana wa Master. Kwa mwendo wao mkali, saa mbili tu baadaye walikuwa wameshafika mjini Morogoro.
Wakafikia katika Hoteli ya Mount Uluguru, wakafanya malipo kisha wakarudi kwenye magari. Safari yao ikaishia Kahumba Night Club, wakatafuta kona nzuri wakakaa na kuanza kutunga sheria.
“Mzee mzima tunafanyaje hapa?” Gerald akamwuliza Master.
“Hili zoezi ni jepesi, anayehusika zaidi hapa ni wewe, mpigie rafiki yako kisha muende hospitalini, muone daktari wa zamu, halafu mweleze shida yako...uzungumze vizuri, naamini atakusaidia...hakikisha Roy anatoka hospitalini usiku huu.”
“Poa poa, baadaye...” Gerald akaamka na kuacha bia yake mezani, akaliendea gari na kuingia.
Dakika mbili badaye, alikuwa kwenye kona ya kuelekea kwenye geti la hospitali ya mkoa, eneo la Posta. Hapo akachukua simu yake na kumpigia Jerome...
“Nimeshaingia mjini kaka.”
“Kweli unaendesha, upo wapi?”
“Nakaribia getini.”
“Getini kwangu au hospitalini?”
“Hospitalini!”
“Ok! Nakuja, sipo mbali sana na hapo... nipo Bwalo, baada ya dakika mbili tu nitakuwa hapo!”
“Sawa mkuu wangu!”
Muda huo haukupita Jerome alikuwa ameshafika, wakaongozana hadi ndani ya hospitali. Wakashuka na kwenda hadi wodini. Wakaomba kuonana na daktari wa zamu. Huko kazi kubwa iliyofanyika ilikuwa kumuomba awaandikie charge ya kuwaruhusu waondoke na mgonjwa wao.
“Kwanini mnataka kufanya hivyo lakini?”
“Tunataka kumwamishia kwenye hospitali kubwa zaidi.”
“Lakini hali yake siyo nzuri, hajazinduka bado, kwanini msisubiri kwanza?”
“Yote hayo tunayafahamu dokta, lakini tunaomba sana msaada wako....” Gerald akasema.
“Hapana…siyo taratibu za hospitali yetu, mgonjwa bado anahitajika kuwa na uangalizi mkubwa.”
“Najua, lakini lengo ni kuhakikisha anapata huduma bora zaidi.”
Baada ya mazungumzo marefu, huku Jerome akitumia umaarufu wake mjini, walikubaliwa kuondoka na mgonjwa wao usiku ule ule, akiwa hajarejewa na fahamu. Jerome hakufahamu kitu chochote kilichokuwa kikiendelea, baada ya kupewa mgonjwa wao, Jerome akaenda zake nyumbani na kumwacha Gerald akiendelea na safari yake.
“Nimefanikiwa mkubwa,” alikuwa ni Gerald akimwambia Master.
“Safi sana, sasa atakuwa chini ya uangalizi wetu.”
“Kweli kabisa.”
Wakamhamishia katika hospitali moja ya binafsi mjini humo. Gerald na Master wakarudi Dar usiku huo huo, vijana wa Master wakalala Mount Uluguru.
******
Davina akiwa kwenye foleni akielekea kazini asubuhi hiyo, muuza magazeti alipita na kumwita. Kama kawaida yake, alinunua magazeti yote ya siku hiyo. Magazeti karibu yote yalikuwa na habari ya ajali iliyotokea usiku wa kuamkia siku hiyo, jirani na Mikese nje kidogo ya Morogoro.
Alipokazia macho gazeti moja, alishtushwa kuona picha ya maiti ambayo ilikuwa imevaa nguo kama alizokuwa amevaa Jeff mara ya mwisho wakati wakiagana kwa safari ya kwenda Dodoma. Alipoamua kuisoma vizuri habari ile, alishindwa kuamini, kwani aligundua kwamba mpenzi wake Jeff, alifariki dunia!
“Noooooooooo.....” alitoa sauti hiyo kali, kisha akaangukia usukanu.
Akapoteza fahamu!
Kilichofuata baada ya taa kuruhusu, ilikuwa ni honi mfululizo! Hakuna aliyejua kwamba Davina alikuwa amezimia!
Jeff alishuka kwenye basi akiwa mchovu sana usiku huo, si wa mwili bali wa mawazo yanayomtatiza na kumnyima raha kabisa. Alikuwa akiumizwa na jinsi alivyotakiwa kuanza kuishi maisha mapya yenye kifungo cha kila aina.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kushuka kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Msamvu mjini Morogoro, alivuka barabara hadi ng’ambo ya pili kwenye keep-left cha Msamvu.
Hapo akaingia kwenye taxi iliyokuwa imeegesha barabarani, ikionekana kuelekea mjini.
“Mia tano bro ingia, wakifika abiria watatu tunaondoka,” alisema dereva wa taxi akimkaribisha Jeff.
“Nataka kukodisha mwenyewe, itawezekana?” Jeff akasema kwa sauti tulivu sana.
“Pochi lako tu kaka, sema unakwenda wapi?”
“Nahitaji Gesti yoyote ya bei poa, lakini isiwe nje ya hapa Msamvu na Mji Mpya!”
“Sawa, ipo ninayoifahamu Mji Mpya...bei poa na imetulia, inaitwa Marangu Guest House, naamini patakufaa sana.”
“Kiasi gani hadi hapo?”
“Elfu na mia tano!”
“Twende.”
Dereva akawasha gari na kuliondoa kwa kasi, dakika moja na sekunde chache baadaye, alikuwa anakatisha kushoto kwake, jirani na Kituo cha Polisi Mji Mpya, akiifuata barabara ya vumbi. Dakika moja mbele, alikuwa anaegesha mbele ya baa hiyo yenye Gesti. Akashuka haraka na kumpatia yule dereva kiasi cha shilingi elfu mbili, alipotaka kumrudishia chenji yake, Jeff akakataa.
“Utakunywa soda kaka.”
“Ahsante.”
Mguu wa kwanza, mguu wa pili hadi Mapokezi alipochukua chumba na kuingia ndani kisha kufunga mlango. Bado alikuwa na mawazo lukuki kichwani mwake, alitakiwa kuwaza jinsi atakavyoanza kuishi maisha mapya ambayo hakuyazoea kabisa. Alijifungia ndani hadi saa nne na nusu alipotoka nje na kuagiza chips na nyama choma, akala.
Akaomba kupewa pombe kali na kuingia nayo chumbani. Hiyo ndiyo ikawa dawa yake ya usingizi!
*****
Pamoja na pombe aliyokunywa, aliweza kudamka alfariji sana siku iliyofuata. Akakimbia bafuni kujimwagia maji, kisha akarudi chumbani kuvaa. Hapo sasa alitakiwa kuvaa nguo zake za kazi! Alivaa suruali nyeusi ya jeans, kisha akavaa t.shirt nyeupe na juu yake akavaa jaketi kubwa, kichwani akiwa na kofia aina ya pama!
Baada ya kukamilisha zoezi hilo, akakusanya nguo zake na vitu vingine vyote kisha akatoka tayari kwa safari ya kwenda kituoni kutafuta usafiri. Ikiwa ni saa 12:00 za asubuhi, alitembea mwenyewe hadi barabara kubwa, ndipo kulipoanza kupambazuka kidogo na kupishana na magari ya abiria.
Akaamua kutembea taratibu kwa miguu hadi kituoni, akakata tiketi ya kwenda Mwanza. Tiketi yake ilionesha wazi kwamba gari lingeingia Morogoro saa 2:30, hivyo muda huo akautumia kupata kifungua kinywa kisha kusubiri gari. Kama alivyopata maelekezo, muda huo ulipofika, basi liliingia kituoni, mara moja Jeff akapanda na kuketi kwenye siti yake.
Dakika chache sana kabla basi halijaondoka kituoni, Jeff aliamua kununua magazeti ya siku hiyo, huo ulikuwa utaratibu wake siku zote. Wakati gari linaanza kuondoka Morogoro, Jeff alikuwa amekazia macho gazeti moja lililoandika kuhusu ajali iliyotokea hapo Morogoro.
Alipotizama picha ya maiti juu ya gazeti, ilikuwa imevaa nguo zake alizokuwa amevaa jana. Akaamua kuisoma habari nzima! Akashtuka sana...habari ilikuwa kwamba yeye amefariki dunia!
Haikuwa habari mpya sana, maana aliitarajia, lakini kidogo ilimshtua. Ilimpa mshtuko kwa sababu kubwa mbili; kwanza ajali iliyotokea inaonekana si ile iliyopangwa awali na habari iliandikwa wazi kwamba Roy alikuwa na hali mbaya Hospitali ya Mkoa. Pili, alishindwa kuelewa jinsi mpenzi wake Davina atakavyopokea habari za kifo chake.
Anamjua vizuri sana Davina...
Akarudisha kumbukumbu zake, jinsi Davina wake anavyompenda, anavyomthamini, asivyoweza kuishi bila yeye, akakumbuka jinsi ilivyokuwa imebaki muda mfupi kabla ya ndoa yao. Bila hiyari yake, machozi yakaanza kumiminika machoni mwake!
Ghafla akachanachana magazeti yote na kuyatupa nje kupitia dirishani. Kila mtu alimshangaa sana, wapo waliomuuliza, lakini hakuwa tayari kuwajibu. Faraja yake ilikuwa machozi. Njia nzima alilia...
Hakuna aliyejua sababu!
******
Wafanyakazi wote wa Kampuni ya KSQ walikuwa kimya asubuhi hiyo, huzuni ilikuwa imetanda, wengi wao hasa wanawake walionekana wakilia karibu muda wote. Wapo kimya wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Gerald ambaye uso wake unasoma simanzi tele aliyonayo moyoni mwake.
Ofisi nzima ilikuwa imeshapata taarifa za kifo cha Jeff, Gerald akiwa na magazeti mkononi mwake, alijikohoza kidogo kisha akachukua kitambaa chake na kujifuta machozi usoni. Hakuna mtu hata mmoja aliyegundua kwamba Gerald alikuwa akifanya maigizo na wakati huo alikuwa katika onesho gumu la kuonesha majonzi na uchungu.
“Naamini kila mmoja anajua kinachoendelea...tumepatwa na msiba mkubwa katika kampuni yetu. Kila mmoja anafahamu kwamba jana Jeff na mwenzake Roy walikwenda Dodoma kwa ajili ya kutoa Elimu Elekezi kwa vijana wetu wa Tawi la Dodoma, lakini wakiwa njiani, wakapata ajali.
“Jeff amefariki na Roy ana hali mbaya sana hospitalini, amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Wengi tunafahamu na tumesoma kwenye magazeti. Huu ni wakati wetu wa kutulia katika tukio hili kubwa lenye kutia simanzi.
“Tunayo kazi ya kuwapa faraja ndugu wa marehemu, lakini pia tuna wajibu wa kumsaidia Roy katika kipindi hiki kigumu. Hiki ni kipindi ambacho anahitaji sana faraja kutoka kwetu. Najua mnafahamu jinsi ya kujipanga na kuhakikisha mambo haya yanafanyika vizuri.
“Mimi kwasasa nafanya mawasiliano na ndugu wa marehemu Jeff kisha nakwenda Morogoro kwa ajili ya kushughulikia kuusafirisha mwili wa Jeff na kuangalia hali ya Roy. Tuweni wavumilivu katika kipindi hiki kigumu...lakini niwatie moyo kwamba, tumeambiwa tushukuru kwa kila jambo...” Gerald akamaliza kuongea na wafanyakazi wote wakaondoka ndani ya chumba cha mkutano.
Siri ya mauaji hayo alikuwa nayo Gerald mwenyewe, hakuna mtu mwingine aliyejua. Gerald aliongea maneno mazito sana, kwa sauti iliyojaa huruma na simanzi tele. Akarudi ofisini mwake akiwa na furaha sana moyoni. Kitu cha kwanza ilikuwa ni kusaka mawasiliano kwa rafiki wa karibu na Jeff, hao ndiyo waliofikisha taarifa kwa wazazi wake. Mtu wa mwisho kumtafuta alikuwa ni Davina, lakini kitu cha ajabu, simu yake ilipokelewa na mtu mwingine, tena mwanaume!
Gerald akashtuka sana!
Asubuhi yote hii?!
“Nani mwenzangu? Siwezi kuongea na mweye simu?” Gerald aliongea maneno hayo haraka-haraka.
“Samahani ndugu, ni Hospitali ya Taifa Muhimbili hapa...mimi ni Daktari.”
“Muhimbili Hospital?”
“Yeah!”
“Kuna nini tena?”
“Huyu binti ni mgonjwa, ameletwa hapa asubuhi hii baada ya kupoteza fahamu akiwa anaendesha gari. Hali yake kwasasa si mbaya sana, unaweza kuja kumwona.”
“Ok!”
Gerald akakata simu akiwa amechanganyikiwa sana.
Bila kumweleza mtu yeyote taarifa za Davina, Gerald aliingia garini haraka na kuondoka kwa kasi kwenda Muhimbili, akamkuta Davina akiendelea kupatiwa matibabu. Kilichofanyika ilikuwa ni kuacha fedha za kutosha na kuomba Davina aendelee kuhudumiwa vyema.
Taarifa zikaenea kwa kasi sana, mchana wa siku hiyo Gerald alikuwa njiani akielekea Morogoro, akaenda Polisi na kukamilisha taratibu zote, gari lake lilikuwa limeharibika vibaya, lakini kwake yeye halikuwa tatizo kubwa, alichotaka kwa wakati huo ilikuwa ni Davina tu.
Baada ya hapo akaenda Hospitalini kushughulikia taratibu nyingine, saa kumi alasiri, ndugu wa Jeff wakaingia hospitalini, kwakuwa walikuwa wameshawasiliana, zikafanyika taratibu zote kisha mwili wa Jeff ukachukuliwa na kupelekwa Dar es Salaam katika chumba cha kuhifadhia maiti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Msiba ukawekwa nyumbani kwa wazazi wake na Jeff Kimara. Kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo, ilipangwa azikwe alasiri ya siku inayofuata. Gerald hakutulia kabisa, akarudi hospitalini usiku, kwa bahati nzuri alimkuta Davina akiwa amerejewa na fahamu!
Davina alilia sana!
“Shem, mpenzi wangu amekufa shem...sitamuona tena Jeff wangu jamani....kwanini lakini? Kwanini imekuwa hivi?” Davina alilia sana akiwa amemkumbatia Gerald.
“Tuliza moyo shem, jikaze ili uruhusiwe asubuhi angalau ushiriki maziko yake, maana anazikwa kesho, jipe moyo....haya ni marajibu ambayo lazima ukubaliane nayo. Tulia shemeji yangu,” Gerald akasema akiwa amezidi kumkumbatia Davina.
Kila mmoja alikuwa akihisi tofauti moyoni mwake, Davina alikuwa akilia kwa hisia na alimkumbatia Gerald kwa hisia za majonzi, lakini kwa Gerald ilikuwa tofauti, joto la Davina lilimburudisha kimahaba, alikuwa anasubiria mambo yaishe ili aweze kutimiza ahadi yake, kumnasa Davina!
Siri iliyokuwa nyuma ya kifo cha Jeff hakuijua! Yeye aliamini amemuua Jeff kwa siri, lakini Jeff mwenyewe alikuwa na siri ya kifo chake.
Siri ndani ya siri!
Siri sirini!
Kama Davina angeweza kujua kilichokuwa ndani ya Gerald, bila shaka angepata nguvu za ajabu na kumsukuma pembeni. Gerald hakuwa mtu mzuri kabisa kwake, alikuwa muuaji wa mchumba wake. Siri hii hakuijua kabisa.
Gerald aliendelea kumng’ang’ania Davina ambaye hakuweza kujua kama mwenzake alikuwa akijisikia faraja kukumbatiwa na mwanamke mrembo kama yeye. Akilini mwake alijua alikuwa anapewa pole kutokana na matatizo yaliyomkuta, lakini ukweli haukuwa huo, Gerald alikuwa na kitu tofauti kabisa moyoni mwake.
“Jikaze shem, ndiyo maisha.”
“Lakini Gerald imekuwa mapema sana, mapema sana kwa Jeff wangu kufa!”
“Usiseme hivyo, kazi ya Mungu haina makosa.”
“Najua, lakini angeniachia basi angalau nifunge naye kwanza ndoa halafu ndiyo amchukue, imekuwa haraka sana.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ukisema hivyo Davina utakuwa unakufuru, kazi ya Mungu haina makosa Davina. Kumbuka kwamba, sote tunaelekea huko huko, kinachoonekana hapa ni nani anatangulia na nani anafuata, lakini wote njia yetu ni moja.”
“Usijali, nashukuru kwa kunipa moyo, ingawa lazima ufahamu kwamba kifo cha mpenzi wangu kinaninyima raha sana, yaani nakosa amani ya moyoni kabisa...” Davina alisema huku akionesha simanzi tele.
“Haya ni majaribu ya maisha Davina. Kila chenye uhai lazima kionje mauti, isitoshe, kila kinachozaliwa lazima kitakufa. Jipe moyo, ujitulize katika kipindi hiki kigumu, maana hata kama utahangaika na kulia wakati wote, haitasaidia kitu, maana utakuwa unajiumiza mwenyewe.”
“Nashukuru sana kwa kunipa moyo...ahsante sana.”
“Jitahidi ili kesho nawe, upate nafasi ya kutupia udongo kwenye mwili wa mpenzi wako!”
“Nitajitahidi.”
Waliendelea kuzungumza mengi ya kupeana moyo, hadi muda wa kuwasabahi wagonjwa ulipoisha, Gerald akaondoka zake.
******
Saa 5:30 za usiku, basi liliingia jijini Mwanza, wasafiri wakiwa wachovu sana baada ya mwendo wa saa takribani kumi na sita wakitokea Dar es Salaam hadi Mwanza. Jeff alishuka akiwa mchovu sana, mwenye koti lake kama kawaida na kofia yake ya pama.
Hakuwa mgeni sana Mwanza, aliwahi kuishi miaka ya nyuma wakati akisoma elimu yake ya Seekondari, hivyo hakuwa mgeni sana katika mitaa ya Mwanza. Alichokifanya baada ya kushuka kwenye basi ni kuingia kwenye taxi moja kwa moja.
“Mwanza Hotel!” Akasema mara moja kisha akatulia akiwa mwenye mawazo tele.
“Sawa brother...karibu Mwanza,” dereva yule akasema.
Jeff hakuitika!
“Bro!” Akaita tena.
“Unasema?” Jeff akajibu kwa kugutuka kidogo.
“Karibu jijini Mwanza.”
“Mimi si mgeni hapa.”
“Samahani kama sikukufurahisha na swali langu!”
“Usijali.”
“Lakini maana yangu ilikuwa kwamba, hata kama wewe ni mwenyeji wa hapa, sasa umerudi safari una haki ya kukaribishwa!”
“Oyaa wewe ni dereva au dalali, mbona unaongea sana? Nipeleke Mwaza Hotel baasi, sina kitu kingine ninachohitaji kutoka kwako.”
“Ok! Samahani, sikujua kama hupendi kuzungumza.”
“Fahamu hivyo na kuanzia sasa usinisemeshe kwa chochote mpaka nifike hotelini!”
Dereva hajibu!
Inaonekana alielewa alichoambiwa. Siku zote Jeff amekuwa mtu mwema na mwenye kuzungumza sana na watu, lakini kwa muda huu ambao ana matatizo na mawazo tele kichwani, alikuwa hana hamu ya kuzungumza na mtu yeyote. Alipenda kupata muda wake peke yake.
Muda wa kuwaza mambo yake akiwa mwenyewe.
Baasi!
Walikuwa kimya mpaka walivyofika hotelini, Jeff akashuka na kutoa noti ya elfu tano, hakutaka kujua kama pesa aliyotoa inatosha au alitakiwa kurudishiwa chenji. Akaondoka zake na kwenda Mapokezi. Hapo akapokelewa na tabasamu mwanana lililoshiba. Msichana mrembo mwenye macho ya mviringo, alimpokea kwa shangwe!
“Habari za kazi.”
“Nzuri tu anko, za kwako!”
“Salama.”
“Karibu sana.”
“Ahsante. Nahitaji malazi.”
“Umepata, lakini tunavyo vya bei tofauti,” akasema msichana huyo akifafanua aina ya vyumba walivyonavyo.
“Ok! Nipatie hicho cha elfu ishirini na tano!”
“Sawa!” Msichana yule akajibu kisha akachukua maelezo ya Jeff na kuyaandika kwenye kitabu cha wageni.
Jeff alitoa maelezo ya uongo kwa kila kitu. Kwanza alijitambulisha kwa jina la Christopher Mkumbo, akasema ametokea Singida, akadanganya kabila kwamba yeye ni Mnyiramba na kila kitu! Hakutaka kueleza ukweli kabisa. Baada ya kukamilisha usajili katika kitabu cha wageni, binti yule ambaye baadaye alijitambulisha kwa jina la Queen alimpeleka chumbani kwake, ghorofa ya 4 katika hoteli hiyo.
“Karibu sana Chris, lala unono...” Queen akamwambia akitabasamu.
“Nawe pia ulale salama.”
“Chris, silali mimi, bado nipo kazini.”
“Poa, kazi njema.”
“Ahsante.”
Queen akaondoka na kumwacha Jeff peke yake chumbani. Kwanza alivua nguo zote, akachukua taulo na kujifunga kiunoni, akaingia bafuni kuoga. Aliporudi akaiendea simu na kubonyeza namba za Restaurant, akaomba kupelekewa mbuzi na ndizi choma, alipokata simu hiyo, akapiga tena baa, alipoomba mzinga mzima wa konyagi!
Akajilaza kitandani mawazo tele kichwani. Pombe ndiyo ilikuwa ya kwanza kuletwa chumbani, akaanza kunywa taratibu, imani yake ilikuwa anapunguza mawazo. Muda mfupi baadaye, chakula kikapelekwa. Akala na kushiba kisha akaendelea na pombe yake.
Akalewa sana!
Akalala!
Asubuhi alipoamka, aliondoka hotelini pale, lengo lake likiwa ni kutafuta Gesti ya bei nafuu mitaani. Alitakiwa kutumia akili, kwani kama angeendelea na matumizi mabaya ya fedha, basi angeishiwa fedha na maisha yake yangekuwa magumu jijini Mwanza.
Akiwa mitaani, alienda kwenye meza moja ya magazeti na kuanza kupitia vichwa vya habari katika magazeti ya siku hiyo. Gazeti moja likauchoma moyo wake, likamwumiza na kumnyong’onyesha.
*****
*****
Umati wa watu ulikuwa umejaa nyumbani kwa wazazi wa Jeff Kimara, katikati kukiwa na jeneza lenye mwili wa marehemu Jeff. Ibada ya mazishi ilikuwa ikiendelea. Ndugu wa Jeff walikuwa wanalia sana, baba yake mzazi, mama yake, wadogo zake na ndugu wengine walikuwa na sura iliyojaa majonzi tele.
Davina muda wote alikuwa amekaa sehemu moja na Gerald, ambaye alionekana kumfariji sana. Wafanyakazi wa KSQ walikuwa wanalia muda wote, kifo cha Jeff kiliwahuzunisha wengi sana. Kiliwachoma wengi na kuwaachia simanzi nzito.
Watu wote wakiwa kimya kabisa, mshereheshaji wa maziko hayo, akasogea mbele akionekana kuwa na tangazo muhimu sana. Akasogeza kipaza sauti karibu yake, kisha akaanza kuzungumza...
“Ndugu zangu wafiwa, majirani na wote ambao mnahusika kwa namna moja ama nyingine na msiba huu wa mpedwa wetu Jeff Sebastian. Tunasikitika kwamba, wakati tukitoa heshima zetu za mwisho, hatutaweza kumuona, kwasababu ameharibika vibaya sana usoni na kichwa kizima kwa ujumla. Utaratibu utaotumika ni kufika mbele ya jeneza lenye mwili wa mpendwa wetu, kisha kuligusa na kupita kabla ya safari ya kwenda makaburini,” Mshereheshaji huyo alisema kwa sauti ya taratibu sana.
Kilio kikaibuka upya!
Watu wakapita mbele ya jeneza kama utaratibu ulivyotangazwa kisha baadaye jeneza linabebwa na kupelekwa makabuni. Jeneza lenye mwili wa marehemu Jeff likashushwa kaburini, waombolezaji wakapita mbele ya kaburi na kutupia mchanga!
Simanzi tele!
Davina naye akapita akiwa ameshikwa na Gerald, wakatupia mchanga na kuondoka! Watu wakalia sana. Jeff alikuwa bado kijana mdogo, kifo kilimchukua akiwa na ndoto nyingi sana maishani mwake. Watu walilia sana!
Kila mtu akaamini huo ulikuwa mwisho wa maisha ya Jeff!
Siri iliyokuwa nyuma ya pazia, hakuna aliyeijua. Si Nyamangumu Camp wala Gerald. Walijua watu watatu tu; Roy, Kijasho na Jeff mwenyewe.
Jeff si marehemu!
Yupo Mwanza!
*****
Jeff aliyatuliza macho yake juu ya gazeti hilo huku akihisi machozi kuanza kudondoka! Alitakiwa kutulia sana na kujikaza ili machozi yasidondoke maana kwa hali aliyokuwa nayo ilikuwa vigumu sana kuyazuia machozi yake. Habari ile ilimchoma moyo!
Ilikuwa imeandikwa gazeti la Uwazi, ikiwa na maandishi makubwa kwa wino uliokolezwa MSHTUKO! Chini ya maneno hayo, kulikuwa na mandishi mengine madogo yaliyosomeka; Mchumba wa marehemu Jeff wa KSQ azimia kwenye foleni, nusura asababishe ajali nyingine, Marehemu Jeff kuzikwa leo Kimara!
Ilikuwa habari mbaya sana kwake, haikuwa mbaya kwa maana ya mpya, lakini alijaribu kuchukua taswira nzima ya wazazi wake, wadogo zake, ndugu zake wengine na Davina wake, akachanganyikiwa!
Alishindwa kuelewa ni kiasi gani wangekuwa na huzuni muda wote. Hakuweza kuitafsiri kwa haraka jinsi nyumbani kwao kutakavyokuwa! Akatoa pesa mfukoni na kununua gazeti hilo kisha akaondoka zake.
Akatafuta sehemu iliyotulia na kuanza kusoma habari ile kwa makini, kila aliposoma mstari mmoja ndivyo alivyozidi kulia. Jeff akagundua kitu kingine tofauti kabisa, aligundua kwamba Davina wake alikuwa akimpenda sana. Moyo wake ukazidi kuumia na kuugua kwa maumvu makali yasiyopona kwa urahisi.
“Kwahiyo mama yangu, atakuwa analia akijua nimekufa kumbe nipo hai...baba naye atakuwa analia...Davina wangu hadi amezimia akijua nimekufa kumbe nipo. Kwanini inakuwa hivi lakini? Kwanini jambo hili linatokea kwangu?” Jeff alijisemea moyoni mwake akizidi kulia.
Hapo sasa akajua kwamba Gerald alikuwa mtu mbaya tena asiyefaa kabisa katika jamii ya watu wastaarabu. Gerald ni muuaji tena asiye na huruma. Alimchukia sana na hakuwa na hamu naye kwa namna yoyote ile.
“Lakini lazima siku moja nitafanya kitu...siwezi kumuacha Gerald. Mawili, nimuue kwa mkono wangu mwenyewe au aozee jela! Yote haya yanawezekana, lakini nitatulia na kuangalia lipi ni bora zaidi ili nianze nalo. Geraaaaaldiiiiiiiiiii....” akajikuta amepayuka na kujipiga-piga kifuani.
Ghafla mvua ya machozi ikaanza kumiminika machoni mwake. Machozi kwake, sasa ikawa ndiyo faraja yake!
*****
“Nakufaaaaaaa...” ndiyo neno la kwanza Roy kutamka siku nne baada ya ajali ile kutokea.
Ilikuwa ni siku mbili baada ya Jeff kuzikwa. Kwa bahati nzuri, alizunduka mbele ya vijana wa Nyamangumu Camp, kwa hiyo haraka wakajitahidi kumpa taarifa za kila kitu kilichotokea na kumbukumbu zake kurejea vyema.
“Kwahiyo tulia, Jeff alikufa!” Alex, mmoja wa vijana wa Nyamangumu akamwambia.
“Alikufa?”
“Ndiyo, shaka ondoa.”
“Kama ndivyo basi poa.”
Ilikuwa kazi kubwa kidogo kwa Roy kurejewa na kumbukumbu zake haraka, lakini alijitahidi kuzirudisha polepole, akakumbuka picha nzima. Kabla hajarejewa na kumbukumbu zake vyema, alikuwa hataki kuzungumza kitu chochote, alipokumbuka kila kitu, akaelewa mchezo mzima!
Kubwa alililoshukuru ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyetilia mashaka ajali ile, walijua ilikuwa ajali ya kawaida, ya bahati mbaya, maana walipanga kumuua Jeff njiani wakiwa wanakaribia kabisa kufika Dodoma, lakini hakuna aliyelaumu, kwasababu kama ni suala la Jeff kufa, tayari alikuwa marehemu tena amelala kaburini!
*****
Siku kumi baadaye Roy alikuwa ameshapona kabisa, akarudishwa Dar es Salaam, kwenye Makao Makuu ya Nyamangumu Camp. Kiongozi wao Master alikuwa aamekaa mezani akimwangalia Roy huku akitabasamu.
“Hongera Kamanda, kazi yako nimeikubali, lakini pole kwa matatizo yaliyokupata, naamini ile ajali haikuwa ile tiliyopanga, lakini tushukuru kwamba wewe ni mzima.
“Unatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa Gerald mpaka hali ya hewa itulie. Endelea kuwa mchapakazi na usioneshe dalili zozote za kujua ukweli wa kifo chake, kwanza hakuna boya yeyote aliyeshtukia mchezo. Sawa?!”
“Sawa Mkuu!”
“Kuhusu pesa usijali, mchana nikitoa benki utafurahi, ila kesho nenda karipoti kazini.”
“Nimekuelewa Mkuu.”
Wakatawanyika.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
******
Vilio vikaibuka upya ofisini kwa Gerald, asubuhi hiyo Roy alipowasili kazini, alisababisha watu walie sana. Kila walipomwangalia walimkumbuka marehemu Jeff. Kila mtu alimpa pole. Baadaye wafanyakazi wakatulia na kutawanyika.
Siku zikazidi kwenda, Gerald akizidi kumpongeza Roy kila siku kwa kazi aliyoifanya, lakini moyoni mwa Roy alikuwa hana amani kabisa. Alihisi kufanya makosa makubwa sana. Ile haikuwa siri tena, tayari alishaanza kumhisi Kijasho tofauti!
“Kijasho akinisaliti tu, hapa NAUAWA! Na mimi sipo tayari kufa....so what to do now?! I have to kill him....stooop!” Roy akasema akionekana kuwa na mawazo sana.
“Ndiyo lazima Kijasho afe, ataniharibia....” Roy akawaza huku kichwa chake kikianza kupanga mauaji yake.
****
Roy anaendelea kuwaza jinsi atakavyoweza kuondoka kikwazo kilichopo mbele yake, Kijasho! Ni kweli Kijasho naye alikuwa muuaji mzoefu, mwenye kutunza siri, lakini si hii ya Nyamangumu ambayo hata mkuu wake wa kazi Master alikuwa haifahamu.
Ilikuwa lazima ahakikishe uhai wake unakatishwa. Lazima. Kama angeacha kufanya hivyo, basi kulikuwa na hatari ya siri hiyo kuvuja, jambo ambalo kwa hakika hakutaka kabisa kuliruhusu litokee. Ilikuwa ni hatari kubwa sana kwake.
“Kijasho anatakiwa kufa, lazima afe!” Akawaza akiwa bado hajapata mbinu za kufanya mauaji yake.
“Lakini mimi najiamini, lazima niwe mjanja, mbinu za mauaji nazifaha vizuri sana. Kijasho anatakiwa kufa kama wengine wanavyokufa, tofauti hapa ni moja tu; Kijasho atakufa kwa siri, wakati vifo vingine Camp ilikuwa inajua baaasi...” aliendelea kuwaza huku ubongo wake ukigoma kabisa kufungua njia ya kumaliza tatizo lile.
“Njia itapatikana tu, acha niende zangu nyumbani, najua itapatikana tu. Mimi ndiyo Roy Maketo!” Akawaza akisimama na kwenda ofisini kwa Mkurugenzi Gerald.
“Sema Maketo,” Gerald akasema baada ya Roy kuingia ofisini kwake bila hodi!
Roy hakujibu!
Akaketi!
“Kamanda wangu...niambie kaka, shwari?”
Bado Roy alikuwa kimya.
“Najua unataka kuchomoka, sasa acha tugawane hivi visenti kwanza, halafu mambo mengine tutajua mambo mengine baadaye,” Gerald akasema akiatoa bahasha ya khaki kwenye mfuko wa ndani wa koti.
Akaanza kuchambua noti za elfu kumi-kumi!
Akachomoa noti thelathini na kuziweka mezani.
Roy akatengeneza tabasamu!
“Mimi naondoka, tutaonana kesho,” Roy akasema akichukua zile fedha pale mezani.
Akasimama.
Akaondoka zake!
Gerald akabaki kumsindikiza kwa macho hadi alipofunga mlango na kuubamiza tena. Ukjalia puuuuu! Gerald akatingisha kichwa, kwa mbali alihisi Roy alikuwa na matatizo yanayomchanganya.
Kuwa na matatizo si jambo geni katika maisha, lakini alipata wakati mgumu sana kuwaza kwamba alikuwa na tatizo gani. Wazo la kwamba kifo cha Jeff kilikuwa kikimchanganya hakuwa nalo, maana kama ni suala la kuua, kazi iliyomuweka mjini ilikuwa hiyo! Kuondoa uhai wa watu ili yeye atajirike.
Anasumbuliwa na nini sasa? Likabaki kuwa swali lisilo na majibu. Mwenye majibu alikuwa mmoja tu, Roy! Akabonyeza jina la Roy kwenye simu yake. Sauti ya upande wa pili ikasikika...
“Kaka vipi?”
“Shwari!”
“Nahisi kama haupo sawa, una tatizo lolote?”
“Nipo poa.”
“Sisi wamoja kaka, if there’s something wrong, just tell me nikusaidie, usibaki kimya na tatizo ndugu yangu!”
“Worry out men, I’m okay!”
“Basi sawa, tutaonana kesho ofisini.”
“Sawa boss!”
Simu ikakatika.
******
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment