Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA - 1

 

     





    IMEANDIKWA NA : CHANGAS MWANGALELA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Kwenye Siku Yangu Ya Kuzaliwa

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    ANGA lilikwishaanza kuivaa rangi ya kahawia kuashiria kuwa siku inaelekea ukingoni. Utulivu wa hali ya hewa ulikuwa ni wa kuridhisha katika siku ile ya alhamisi, siku ambayo ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya watu mahususi ambao walikuwa wakijiandaa mahususi kwa tukio mahususi katika ukumbi mahususi.

    Naam, ulikuwa ni ukumbi wa ‘CN HOTEL’, ukumbi ambao uko kandoni mwa barabara ya Mwanza-Tarime katika mji mdogo wa Bunda. Ukumbi huu ambao ulikuwa tayari kuwalaki wageni wake katika muda wowote ambao wao wangeona yafaa, ulikuwa umepambwa kwa namna ya pekee, namna ambayo ingemvutia yeyote ambaye angefanikiwa kutupa jicho lake ndani na kuyasawiri yaliyomo.

    Ukumbi ulipambwa kwa mapambo ya kuvutia. Ukiachilia mbali rangi ya vitambaa vilivyotumika, vitambaa vilivyokuwa na rangi ya kukosha kila jicho. Kwa mchanganyiko huu wa rangi ya zambarau na nyeupe, sambamba na maua ya rangi ya pinki yenye kuvutia, utaungana nami kukubaliana na mchanganyiko sawia wa rangi hizi.

    Ndani ya ukumbi mlikuwa na meza zipatazo kumi na sita, cha kushangaza katika meza hizi zilikuwa ni namba. Namba ambazo ziliandikwa kila upande kwenye makaratasi maalum yaliyoumbwa katika umbo la pembe tatu!

    Mbele kabisa ya ukumbi huu, kulikuwa na meza yenye namba sifuri, na sehemu nyingine za ukumbi kulipangwa meza katika mpangilio wa kuvutia, hizi zilianzia namba moja hadi kumi na tano na hivyo kuifanya idadi ya meza katika ukumbi huu kuwa kumi na sita, huku kila meza ikiwa na viti viwili vilivyowekwa kwa mtindo wa kutizamana, na kila meza ikiweka mpaka wa utengano baina ya viti hivyo.

    Kwenye mlango wa ukumbi huu palikuwepo na watu wawili, mmoja wa jinsia ya kike aliyevaa gauni fupi jekundu lililoshuka kidogo hadi chini ya magoti, na mwingine alikuwa ni wa jinsia ya kiume. Yeye alivalia suruali nyeusi, shati jeupe la mikono mirefu, lililofuatiwa na kizibao juu yake huku ile tai ndogo yenye umbo la kipepeo ikiwa shingoni mwake.

    Wote walining’iniza vitambulisho maalum vifuani mwao, vyenye maandishi ya kufanana yaliyosomeka, ‘MAPOKEZI’ kuashiria majukumu yao ukumbini pale. Walikuwa makini wakiangalia saa zao kwa zamu, nadhani walitaka kujua muda uliobakia ili wawalaki wageni wao waliokuwa wakiwatarajia punde.

    ****

    Kitiheka alikuwa amesimama mbele ya kioo cha kujipambia kilichokuwemo mule chumbani alimokuwa. Aliiweka sawia tai yake, na aliporidhika na mkao wa tai, alichukua chupa ya uturi akajipulizia na kukifanya chumba kizima kitawaliwe na manukato yale ya bei mbaya.

    Kitiheka Ngomanzito, kijana wa miaka 28, mrefu na mwenye umbo la wastani ambaye rangi yake ya ngozi ilikuwa ni nyeusi yenye kung’aa. Kichwani alizinyoa nywele zake zote katika mtindo wa kipara, mtindo ambao aliuzoea hata kabla hajaenda Marekani kwa ajili ya masomo yake ya elimu ya juu.

    Elimu yake ilikuwa ni shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara, elimu aliyoipata katika chuo kikuu cha ‘Wisconsin Madison’ kilichopo nchini Marekani ambapo alikwenda kwa ajili ya kusoma shahada ya kwanza katika fani hiyo hiyo. Alipohitimu shahada yake ya kwanza, aliona ni vyema endapo ataendelea na shahada ya pili akiwa huko huko, jambo hilo liliungwa mkono na baba yake ambaye ndiye aliyemgharamia kila senti katika masomo yake kwa kushirikiana bega kwa bega na mkewe.

    Baada ya kuhitimu masomo yake, Kitiheka alidhamiria kuanzisha biashara ya kimataifa, biashara ambayo bidhaa zingezalishwa hapahapa Tanzania na kisha kusafirishwa katika nchi za Marekani na Canada ambako alibaini kuwa zingeweza kuwa na uhitaji mkubwa kutokana na utafiti alioufanya, utafiti ambao ameujumuisha kwenye tasnifu yake ya shahada ya uzamili.

    Ilikuwa ni siku ya pili tangu alipoikanyaga ardhi ya Tanzania akitokea Marekani alipokuwa. Alifika Dar es salaam siku ya jumatano, ambapo alilala kwa siku moja kabla hajachukua ndege nyingine iliyomleta mpaka Mwanza ambako pia hakupoteza muda akapanda basi mpaka Bunda kwa lengo la kuwahi sherehe aliyoalikwa na rafiki yake kipenzi, rafiki ambaye sasa alimchukulia kama ndugu kutokana na urafiki wao kudumu kwa muda mrefu.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kujipulizia uturi ule, kitiheka aliichukua kadi yake ya mwaliko, kadi yenye namba kumi akaiweka kwenye mfuko mdogo wa ndani ya koti la suti aliyovaa.

    Wakati anatoka, alimkuta mama yake sebuleni akimsubiri kwa hamu na shauku kuu. Mama yake hakuwa ameridhika kuzungumza naye kwa saa moja tu tangu alipofika, ikiwa ni baada ya miaka mingi ya utengano uliodumu kwa miaka mitano tangu Kitiheka aende Marekani kwa masomo.

    “Mwanangu Kiti, usichelewe kurudi… bado nina hamu na wewe. Si unajua ni muda mrefu umepita sijakuona mwanangu,” alisema Matobera, mama yake na Kitiheka ambaye alipenda kulifupisha jina la mwanae kwa kumuita Kiti tangu akiwa mtoto mdogo.

    “Naelewa mama, sitachelewa kurudi, naenda kumpa kampani Bony kwenye sherehe yake, sitaki kumuangusha ilhali nilimuahidi tangu nikiwa Marekani.”

    “Sawa baba’ angu, nawatakieni kila la kheri kwenye sherehe yenu,”

    “Ok mama, ahsante,” alisema Kiti akiwa amemkumbatia mama yake.

    ****



    Siku ishirini kabla….



    Emmy alikuwa amekaa kwenye kochi huku kichwa chake akiwa amekiegemeza kifuani kwa Bony mpenzi wake. Walikuwa sebuleni kwao wakifuatilia tamthiliya iliyokuwa ikiendelea kwenye Luninga.

    Bony alikuwa akizichezea nywele za Emmy ambaye kutokana na kitendo hicho, mara kadhaa alipoteza umakini katika kufuatilia tamthiliya ambayo hakupenda kupitwa na hata sehemu moja ya tamthiliya hiyo.

    Ilikuwa ni majira ya saa 4:30 usiku tamthiliya ilipoisha. Emmy alimkumbusha Bony kuwa mwezi ujao ndiyo kuna tarehe ambayo walizaliwa miaka kadhaa iliyopita.

    Wote walizaliwa terehe moja, lakini katika miaka tofauti, ambapo Bony ndiye aliyetangulia halafu miaka mitatu baadaye ndiyo akazaliwa Emmy.

    Emmy msichana mrembo ambaye ni chotara aliyezaliwa kwa mama msukuma na baba yake alikuwa ni raia wa Uholanzi aliyewahi kuishi hapa nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya themanini. Alikuja kama mwambata wa shirika la afya ulimwenguni, ‘WHO’akiwa kama daktari, wakati ule ambao UKIMWI ulianza kugundulika nchini kwa mara ya kwanza.

    Mzee Schzlakta, tamka Shizilakta aliishi hapa nchini kwa mwaka mmoja. Ni katika mwaka huohuo alikutana na Kesego, mama yake na Emmy ambaye alikuwa ni mhudumu katika hoteli aliyofikia Schzlakta. Penzi baina yao likachipua, na hatimaye ujauzito ambao Emmy alizaliwa kwao ukapatikana.

    Muda wake wa kuishi nchini ulipoisha Schzilakta alirudi kwao huku akimuachia Kesego jukumu la kumlea Emmy bila msaada wowote, hakukua na mawasiliano baina yao.

    Kesego alipigana kufa na kupona ili kuhakikisha mwanaye kipenzi anapata kila hitaji la msingi kama mtoto, akampatia chakula, mavazi, mahali pazuri pa kuishi na elimu ya msingi hadi chuo kikuu kwa ujasiriamali aliouvaa baada ya kuwa amebakiwa na vijidola kiasi alivyoachiwa na Schzilakta.

    Wakiwa pale sebuleni Emmy alikumbushia Bony kwa kusema, “Baby, hivi unakumbuka kuwa mwezi ujao ndiyo birthday yetu?”

    “Yeah…. nakumbuka mpenzi,”

    “Vipi, tutaandaa sherehe?” Emmy aliuliza.

    “Mh… sikuwa nimelifikiria hilo, kwani vipi, unataka tuandae sherehe?”

    “Ndiyo, ila kwa namna ya tofauti,” Alisema Emmy huku akimgeukia Bony na kumtizama kwa namna ya kudeka zaidi.

    Bony alimfahamu fika mkewe, alikuwa ni mtu wa kupenda tafrija kila mara. Kwa sababu alipenda siku zote alishuhudie tabasamu la mkewe, Bony aliamua kumpa uhuru wa kufanya kila atakacho, ili tu, moyo wake ufurahi.

    “Unataka iwe ya namna gani?” Bony alihoji.

    “Unakumbuka uliwahi kuniambia kuwa una mpango wa kuwakutanisha marafiki zangu na wako katika mpango wa pamoja wa kibiashara?”

    “Ndiyo, nakumbuka,”

    “Sasa unaonaje huo mpango wako ukafanyika katika siku hiyo, ili tupige ndege wawili kwa jiwe moja?”

    Bony alitabasamu baada ya kuwa amesikia wazo hilo la mkewe, alimkubalia, na kwa pamoja wakaanza kujadiliana namna ambavyo wataifanya sherehe hiyo kuwa ya kipekee.

    “Waalike marafiki zako kumi na tano wa jinsia ya kike, nami nitawaalika wangu kumi na tano wa jinsi ya kuime...” Bony alisema.

    “Mh... Bony jamani, sasa hapo itakuwa ni love networking au business networking?” aliuza Emmy kwa namna ya mzaha.

    Bony alitabasamu kidogo kabla ya kulijibu swali la Emmy, “Hapana… si hivyo, yeyote angeweza kufikiri kama unavyofikiria. Lengo ni kuwakutanisha wafanyabiashara na wanaotarajia kufanya biashara pamoja. Nimesema hivyo kwa lengo la kuweka uwiano sawa wa kijinsia, ingawaje ulichokisema pia kinaweza kutokea… huwezi kuzuia hisia za watu.”

    Emmy alikubaliana na wazo la mumewe halafu akasema, “Na ili kuepuka kuwaweka watu waliozoeana pamoja, inabidi tuwe na namna itakayo wachanganya,”

    “Namna ipi hiyo?” Bony aliuliza.

    “Kwenye kadi za watu wako weka namba…”

    “Halafu?”

    “Nami pia nitaweka namba kwenye zangu, namba ambazo zitakuwa sawa na zile za kwenye kadi zako, na waalikwa wote watapangwa kwa kufuata namba, yaani tutakuwa na meza zenye namba… namba ambazo zitashabihiana na zile za kwenye kadi, hivyo basi, tutawaelekeza mapokezi wawapange wageni kwa kufuata namba. Kwa mfano; wageni wenye kadi namba sita watakaa kwenye meza namba sita.” Alifafanua Emmy.

    “Hapo ni sawa, lakini pia iwe ni siri katika upangaji. Kwa maana, wewe utapanga bila kunishirikisha nami halikadhalika nitapanga bila kukushirikisha. Tukishapanga ndiyo tutafahamishana lakini bila kufanya mabadiliko.”

    “Ni sawa mpenzi wangu,” alisema Emmy huku akimbusu Bony ambaye pia alijibu mapigo, ikawa piga nikupige sambamba na kutomasana kulikoamsha hisia za miili yao.

    Ni Bony aliyeanza kuutoa ulimi wake na kuzilamba papi za midomo ya Emmy ambaye alipagawa kwa kitendo kile. Ukafuatia uchokozi ambao uliwachukua na kuwatupa kwenye dunia nyingine, dunia ya mahaba.



    __________



    ANGA lilikuwa tulivu katika usiku ule maalum. Mbalamwezi iliyozungukwa na mamilioni ya nyota ilimulika kuangazia uso wa dunia na vyote vilivyomo. Naweza kusema mwanga huu ulitosha kabisa, hivyo hata taa za umeme zilizokuwa zimewashwa nje ya majumba zilikuwa ni kama urembo tu.

    Upepo mwanana wa ziwa ulivuma na kupuliza mpaka kule ulipokuwa ukumbi wa CN HOTEL, ukumbi ambao ulitumiwa kwa ajili ya sherehe ile maalum, sherehe ambayo iliandaliwa kwa namna ya pekee na familia ya bwana na bibi Boniphace Mayunga ambao waliwaalika wapendwa wao ili kujumuika nao kwa pamoja katika kuiadhimisha siku yao ya kuzaliwa.

    Takribani wageni wote waalikwa walikuwa wameshawasili ukumbini, isipokuwa mmoja tu, naye ni Wayeka Ayuyube, ambaye yawezekana alichelewa kwa sababu; ni yeye pekee aliyekuwa akitokea mbali siku hiyo. Wengine wote asubuhi ya siku hiyo iliwakuta wakiwa Bunda wakiisubiri sherehe.

    Wayeka, msichana mrembo ambaye uzuri wake ulitosha kudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye sanaa ya uumbaji. Alikuwa mrefu na mnene wa wastani, mwenye kifua chenye ukubwa wa kati, tumbo dogo na nyonga zilizotanuka. Kwa nyuma Wayeka alisusiwa mzigo wa makalio yenye ukubwa wa kuvutia, alijaliwa rangi ya maji ya kunde iliyowatesa wengi kila walipomwona. Ni kama vile alitamkiwa: nenda duniani ukawatese wakware!

    Wayeka aliwasili ukumbini pale majira ya saa 1:45 jioni akitokea Nyamuswa, kijiji ambacho ni kijiji miongoni mwa vijiji vya Wilaya ya Bunda. Huko ndiko nyumbani kwao alikozaliwa na kusomea shule ya msingi hadi sekondari, kabla hajajiunga na chuo kikuu cha Mzumbe, Morogoro kwa masomo ya shahada ya kwanza katika fani ya uhasibu.

    Umbali wa kutoka Nyamuswa hadi Bunda mjini ni kama kilomita ishirini na nne hivi, lakini ilimchukua Wayeka saa nzima kutoka Nyamuswa hadi kufika Bunda kwa sababu ya ubovu wa barabara.

    Alipofika ukumbini, alilakiwa na Cosmas ambaye alikuwa idara ya mapokezi katika sherehe hiyo. Kama ilivyo kwa marijali wengine, Cosmas naye alipapalishwa na uzuri wa Wayeka.

    “Cleopatra?” aliwaza Cosmas mara tu alipomwona Wayeka. Cosmas alimfananisha Wayeka na yule malkia wa Misri aliyewahi kuitikisa dunia kwa uzuri wake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alimfuata pale kwenye gari alipokuwa, akamsalimu, kisha akamshika mkono kumuongoza kuelekea ndani.

    “Samahani bibie, kwanza kabisa mimi naitwa Cosmas Manyaki. Kama uonavyo, leo niko kwenye idara hii nyeti, idara ya mapokezi. Sijui mwenzangu unaitwa nani?”

    “Naitwa Wayeka Ayuyube, ni miongoni mwa wageni waalikwa katika sherehe hii,” alijibu Wayeka kwa sauti ya madaha aliyoikoleza kwa mikogo ya kike. Huo ukawa ni uchawi mwingine uliotumika kumroga Cosmas ambaye alihisi msisimko wa ajabu kila sauti ya Wayeka ilipoyapenya masikio yake.

    “Nikuombe tena samahani bibie…. Niwie radhi, nipatie kadi yako tafadhali,”

    Wayeka aliufungua mkoba wake, akatoa kadi yake ya mwaliko akampatia Cosmas ambaye aliisoma, “Ok, ni namba kumi. Nifuate,” alisema Cosmas huku akimrudishia Wayeka kadi yake ambayo aliiambatanisha na kadi yake ya mawasiliano, yaani ‘Business Card’.

    Wayeka aliitwaa kadi yake, akairudisha tena kwenye mkoba, kisha akachapua hatua kumfuata Cosmas ambaye alimpeleka mpaka kwenye meza namba kumi, meza ambayo kwa wakati huo ilikuwa imekaliwa na Kitiheka ambaye pia alikuwa na kadi namba kumi.

    Kizuri chajiuza, macho ya Kiti nayo yalimwona Wayeka. Akahisi yuko ndotoni, alikuwa kama asiyeamini kile anachokiona, imani ikamjia mara baada ya Wayeka kufika pale mezani. Kabla ya kukaa, Wayeka alinyoosha mkono wake kwa lengo la kusalimiana na Kiti, “Habari yako?” alisalimia Wayeka.

    Sauti ya Wayeka ilimsababishia Kiti ugonjwa uleule kama uliompata Cosmas, lakini hali ya Kiti ilionekana kuwa taabani kuliko Cosmas!

    “Salama, mambo?” Kiti aliitikia salamu ile ya Wayeka.

    “Poa,”

    Kiti alibaki ameushikilia mkono wa Wayeka kwa muda wa takribani dakika nzima. Wayeka aliyekuwa ameshikwa mkono na Kiti, alihisi mabadiliko ya ajabu mwilini mwake, mabadiliko ambayo yalimfanya apoteze ujasiri aliokuwa nao na kutwaliwa na aibu.

    Macho yao yalikuwa yakitazamana, lakini Wayeka alikuwa wa kwanza kuyakwepesha, waliachiana mikono wakaketi.

    ****

    Muziki laini uliokuwa katika mahadhi ya taratibu ulisikika kupitia spika maridadi za ukumbi ule wa ‘CN HOTEL’. Muziki huu ulikuwa ukitoa adhabu pendwa, adhabu ambayo ilikonga nyoyo za wasikilizaji ambao walikuwa makini kabisa wakisubiri sherehe iliyowakutanisha pamoja ianze rasmi. Adhabu ya burudani, ni nani awezaye kuweka pingamizi wakati ambapo moyo wake umeridhia kwa hiyari kupokea adhabu hii adimu?

    Katikati ya burudani mara muziki ule ulikatishwa kwa ghafla, na kuwafanya wote waliokuwa ukumbini mule kushtuka. Wakayatega makini yao ili kujua ni kitu gani kinaendelea.

    Mara ikasikika sauti ambayo bila shaka ilikuwa ni ya mshereheshaji aliyejitambulisha kwa mbwembwe nyingi, “Haya… haya sasa mabibi na mabwana… ambao ni wageni waalikwa katika sherehe hii, ninayezungumza sasa ni MC Mikogo, ambaye nitakuwa nanyi tangu wakati huu kwa ajili ya kuwaendeshea sherehe hii ambayo ni maalum kwa ajili yenu…. Nipigieni makofi tafadhali…”

    Makofi yalisikika sambamba na vigelegele kutoka kwa kina mama.

    “Ahsanteni… ahsanteni sana. Sasa umefika wakati ambao wenyeji wetu wataingia ukumbini ili tuanze rasmi shughuli yetu. DJ tupe muziki...”

    Sauti ya muziki wa shangwe ikashika hatamu. Na wakati huohuo bwana na bibi Boniphace Mayunga waliingia ukumbini kwa kupitia mlango uliokuwa nyuma ya ukumbi. Walikuwa wamependeza ndani ya mavazi yao nadhifu yaliyowafanya waonekane wa pekee sana usiku ule.

    Sauti za hoihoi na nderemo zikasikika ukumbini sambamba na muziki uliokuwa ukisikika kupitia spika safi za mule ukumbini. Katikati ya shangwe hiyo lilitokea jambo ambalo bila shaka hakuna aliyelitarajia, jambo ambalo liliwashangaza wengi na kuwaacha watu midomo wazi huku wakitoa sauti za mfadhaiko.

    Umeme ulizimwa ghafla na ulipowashwa sauti ya MC Mikogo ikasikika ikiimbisha, “Happy birthday to you… happy birthday to you…”

    Wote ukumbini waliitika wito, wakajumuika kuimba wimbo huo kwa pamoja huku wakitaja majina ya Bony na Emmy ambao ndiyo walikuwa walengwa wa wimbo huo katika tukio lile!

    Mara umeme ukazimika tena!

    Kama ilivyokuwa awali hakuna aliyetarajia jambo hili. Watu waliokuwa wakiimba walisitisha ghafla mara tu umeme ulipozimwa huku ukumbi ukitawaliwa na sauti za manung’uniko, kwani hakuna aliyetarajia kitu kama hicho kutokea.

    Umeme ukawashwa tena.

    Umeme ulipowashwa tu, Bony na Emmy walipokea mashambulizi ya ghafla yaliyosababisha kulipuka tena kwa hoihoi na nderemo kutoka kwa watu waliokuwa ukumbini mule, huku wimbo wa ‘Happy birthday to you…’ ukianzishwa upya sambamba na vicheko vilivyodhihirisha furaha ya watu ukumbini mule.

    Nyuso za Bony na Emmy zilikuwa hazionekani baada ya kuwa zimefunikwa kwa sahani zilizokuwa na keki.

    Ilifurahisha sana!

    Kitendo kile cha ghafla na ambacho hakikutarajiwa kilifanywa na Kiti ambaye alimfunika Bony, na aliyemfunika Emmy alikuwa ni Minael Swai, rafiki kipenzi wa Bony tangu walipokuwa kidato cha tano katika shule ya sekondari ya ‘Ikizu High School’ na ni huyuhuyu aliyekuwa msindikizaji, kwa maana ya ‘best bridegroom’ kwenye harusi ya Bony na Emmy.

    Sina hakika kama ilikuwa imepangwa au lah! Kwa sababu; yamkini tukio la kuwafunika Bony na Emmy kwa sahani zilizokuwa na keki lilifanyika katika wakati mmoja. Na mara baada ya taa kuwashwa Kiti na Minael walionekana kupigwa na butwaa huku kila mmoja akilitaja jina la mwezie. Wakati Minaeli akiita “Kiti...” Kiti nae aliita, “Mina!”

    Naam, wanafahamiana!

    Kiti na Minael wana historia ndefu ya pamoja, historia ambayo ilianzia shuleni ‘Ikizu High School’. Walikuwa ni wapenzi waliosoma darasa moja. Ingawa wakati wanaelekea kufanya mtihani wa kidato cha sita walijikuta katika mgogoro uliotia doa sugu katika uhusiano wao. Mgogoro huo ulisababisha kukatika kwa mawasiliano baina yao. Tangu wakati huo mpaka sasa ni miaka sita na ushei.

    Leo wamekutana tena kwenye sherehe iliyoandaliwa na Bony na Emmy ambao walikuwa ni daraja katika mapenzi yao wakati huo!

    Walikumbatiana katika hali hiyohiyo ya kutoamini, kisha kila mmoja akarudi kwenye sehemu yake. Wakati Mina akielekea kwenye meza namba nne, namba iliyokuwa sawa na namba ya kadi yake. Kiti naye alirudi kwenye meza yake.

    ****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    ****

    Baada ya tukio lile la kushangaza Bony na Emmy walirejea tena ukumbini baada ya kuwa wametoka kidogo kwa lengo la kwenda kusafisha nyuso zao.

    MC Mikogo alizungumza tena maneno machache, kisha akakabidhi rasmi kipaza sauti kwa Bony ambaye alianza kwa kusema, “Naomba nianze kwa kuwasalimu; habari za jioni..?”

    Salamu ilijibiwa na wote kisha akaendelea, “… napenda kuwashukuru wote kwa kuitikia wito, kwani mmevunja ratiba zenu kwa lengo tu, la kuja kujumuika nasi katika kuadhimisha siku yetu ya kuzaliwa. Nawashukuru sana.

    Aidha ningependa kuweka wazi kuwa; lengo la kukusanyika hapa pamoja katika jioni hii ya leo, si tu kuadhimisha siku yetu ya kuzaliwa, bali ni kujumuika pamoja kwa lengo la kuboresha maisha yetu na ya wote watakaotufuatia kupitia biashara.

    Wote tulioko ukumbini humu ni marafiki ambao tulikutana shuleni, kwa maana; wapo tuliosoma nao pamoja shule ya msingi, wapo tuliosoma nao shule ya sekondari na hata vyuo.

    Wapo pia ambao wamesoma na mke wangu, bibie hapa Emmy katika mlolongo wa elimu nilioutaja…” alisema Bony huku akimgeukia Emmy ambaye alikuwa kushoto kwake, halafu akaendelea, “…wote leo tumejumuika pamoja kwa lengo la kuuunganisha mawazo yetu ili tuweze kuinuka kibiashara, kwa manufaa yetu na ya watoto tuliowazaa au tutakaowazaa.

    Nitaomba mtuwie radhi kwa namna tulivyowapanga leo, kwa sababu; wapo ambao wametoka nyumbani wakiwa pamoja, kwa maana ya mke na mume, wachumba au wapenzi walio katika safari ya kuelekea ndoa. Tumewatenganisha kwa lengo la kuunda mitandao mipya ya kibiashara, mitandao ambayo itatufanya tuinuke kiuchumi.

    Hivyo basi, huyo uliye naye mezani hapo, ndiye atakayekuwa mshirika wako kibiashara au ndiye atakayekuwa daraja baina yako na watakaokuwa washirika wako kibiashara. Ahsanteni sana.” Bony alihitimisha na kufuatiwa na sauti za makofi na vigelegele kutoka kwa wageni ambao walikuwa wakimshangilia kwa hotuba yake nzuri na ya kuvutia. Alikabidhi kipaza sauti kwa mshereheshaji amabye aliitumia nafasi hiyo kuwahimiza wahudumu wa sherehe katika suala la vinywaji, hata hivyo, wahudumu nao hawakuwa nyuma, kwani walikuwa makini sana kwenye kazi yao.

    Mazungumzo baina ya wageni waalikwa yaliendelea tangu meza hadi meza. Watu walibadilishana mawazo mbalimbali ya kibiashara pamoja na mawasiliano yao kwa maana ya; namba za simu, anuani za barua pepe na wavuti.

    Miongoni mwa watu walionufaika na mpango huo alikuwa ni Kiti. Kiti aliitumia vyema nafasi hiyo kwa kumfahamu barabara Wayeka.

    Mazungumzo ya hapa na pale yalishika hatamu huku wakijimiminia mafundo kadhaa ya vinywaji vya kila aina, kila mmoja kwa chaguo lake. Kiti na Wayeka wao walishiriki chupa moja ya mvinyo aina ya Saint Anna.



    _________

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    SHEREHE ilihitimishwa mnamo saa 6 usiku. kila mmoja alielekea mahali alipokuwa amepaandaa kwa ajili ya malazi. Kwa wale ambao walikuwa ni wakaazi wa vitongoji vya mji mdogo wa Bunda walirejea majumbani mwao. Na wale ambao walikuja wakitokea sehemu mbalimbali walilazimika kuchukua vyumba katika hoteli tofauti tofauti zilizokuwa jirani.

    Minaeli alifika kwenye sherehe akitokea Shinyanga alikofanyia kazi kama mwajiriwa wa benki binafsi iliyopo mjini humo. Hivyo baada ya sherehe, alikuwa ni miongoni mwa waliokodi vyumba kwenye hoteli mbalimbali kwa ajili ya kulala. Alichukua chumba kwenye hoteli iliyofahamika kama MLIMANI PARK HOTEL.

    Akiwa chumabni kwake usingizi haukumjia Mina. Alikuwa na mawazo!

    Mawazo ya Mina yaliasisiwa kwenye kumbukumbu juu ya matukio yaliyowahi kutokea miaka kadhaa nyuma baina yake na Kiti.

    Ni wazi Mina alikiri kumpenda Kiti kwa dhati ya moyo. Alikumbuka wakati wa raha pindi alipokuwa na Kiti, akakumbuka pia wakati wa shida zilizozua mgogoro uliopelekea kufarakana kwao. Mina akazipima nyakati hizo katika mizania kwa lengo la kutafuta uwiano. Raha zilizidi shida kwa uzito usio na hata chembe ya mnuso!

    Kwa matokeo hayo Mina akajiaminisha kuwa; huyo ndiye mwanaume wa masiha yake, “Sasa ilikuwaje tukafarakana?” Mina aliwaza.

    Alizivuta kumbukumbu zake nyuma zaidi kwa lengo la kutafuta chanzo cha mgogoro baina yao, akakumbuka kuwa, ni yeye ndiye aliyeanza chokochoko baada ya kumkuta Kiti akiwa darasani na msichana ambaye kwa mkao waliokuwa wamekaa, Mina alihisi kuwa kuna jambo lisilo la kawaida baina yao.

    Walipomwona walishtuka na kumfanya Mina aziamini moja kwa moja hisia zake, akawatuhumu kama wezi wake. Mina alijiona amesalitiwa kabisa, na hata Kiti alipomjia kwa lengo la kumuelewesha kuwa, hisia zake ni kinyume na ukweli, Mina hakumuelewa.

    Ukazuka ugomvi mkubwa baina yake na yule msichana, ugomvi ulioishia katika kutupiana vijembe na kejeli huku chuki isiyo kifani ikipamba moto dhidi ya Kiti. Bony alipoingilia kati kwa lengo la kutafuta suluhu, Mina hakumuelewa.

    Mawasiliano baina yake na Kiti yalivurugika, kiasi cha kufikia hatua ya kukatika kabisa, huo ukawa ni mwisho wa uhusiano wao wakati ule.

    Sasa Mina amemuona tena Kiti na bado anahisi kumpenda, “Ulikuwa ni wivu wa kitoto,” Mina alijisemea.

    Akiwa pale kitandani Mina alijigeuza; mara kushoto, mara kulia, alilala chali na kuna wakati alilala kifudifudi lakini bado usingizi haukumjia. Akainuka, akakaa kitako akiwa palepale kitandani, “Kitiheka…” sauti ilimtoka Mina kisha taratibu akarudi kulala.

    Alitamani japo awe na namba yake ya simu ili ampigie amweleze kuwa bado anamuhitaji, hakuwa nayo! Akaitwaa simu yake iliyokuwa chini ya mto, akaibonyeza kwenye orodha ya majina, na moja kwa moja akabonyeza kwenye jina la Boniphace Mayunga kwa lengo la kumpigia ili amwombe namba ya Kiti.

    Bahati haikuwa yake, “Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa, tafadhali… jaribu tena baadaye,” ilisikika sauti kutoka upande wa pili wa simu.

    Hakuchoka!

    Alilitafuta jina la Emmy akampigia, simu iliita lakini haikupokelewa. Mina alipoitazama saa kwenye simu yake, ilionesha kuwa ni saa 9:05 usiku.

    “Mungu wangu…” sauti ilimtoka Mina huku akiachia simu yake katika hali ya kukata tamaa. Taratibu usingizi ulimjia akalala.

    ****

    Kiti aliamka asubuhi na mapema siku iliyofuata. Lakini haikuwa mapema kama ilivyokuwa kwa mama yake, ambaye tayari alikwisha jiandaa kwa safari ya Nyamuswa ambako alitarajia kwenda pamoja na Kiti kwa lengo la kumpeleka akamwone bibi yake ambaye alitamani kuonana na mjukuu wake baada ya miaka mingi ya utengano.

    Kiti alipomaliza kujiandaa alienda sebuleni kujumuika na mama yake kwa ajili ya kifungua kinywa kabla hawajaianza safari yao ya kuelekea Nyamuswa.

    Walichukua gari aina ya Nissan short chasis, na Kiti ndiye aliyeendesha.

    “Njia inaonekana kuwa ni mbovu sana?” Kiti aliamua kuvunja ukimya kwa kumuuliza mama yake.

    “Njia ni mbovu haswa… na hii nchi yetu hii…, hapa ni mpaka uchaguzi ndiyo utaona barabara zinajengwa, tena ujenzi wenyewe ni wa kulipua tu.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hali ni mbaya sana, sasa kama wanajenga kwa kulipua… wenye dhamana wanasemaje?”

    “Waseme nini tena wakati wameshazibwa midomo kwa ten percent. Hata zabuni zenyewe wanapeana kwa kujuana tu,” alisema Matobera mama yake na Kiti.

    “Tutamkumbuka sana Nyerere na wimbo wake wa rushwa adui wa haki...” alisema Kiti kabla mama yake hajamkatisha kwa kusema, “Labda nyie wasomi ndiyo mtusaidie… tukikumbuka tu wimbo bila jitihada za kuondoa tatizo haitakuwa na maana. Cha msingi hapa ni kuziba tundu ili kuokoa meli isizame.”

    “Ni kweli usemayo mama, lakini hii vita si ya wasomi tu, ni vita ya watu wote… tuungane,” alisema Kiti.

    Mazungumzo ya mama na mwana yaliendelea ili kuifanya safari yao isiwe ya kuchusha. Walipofika Kiloleli, kijiji kilicho jirani na Nyamuswa Kiti alibadili mada ya mazungumzo.

    “Hivi pale Nyamuswa wazee maarufu si watakuwa wameisha?”

    “Hawajaisha, ila ndiyo kama wanaishia hivyo…”

    “Huyu mzee Ayuyube unaweza kuwa unamfahamu?” Kiti aliuliza.

    “Namfahamu… ila siyo mzee sana, ni rika la baba yako. Na kama sikosei walisoma darasa moja.”

    “Ahaa… na watoto wake je, unawafahamu wote?”

    “Ayuyube hana watoto, ana mtoto mmoja tu, naye anaitwa Wayeka. Labda kama ana wengine aliowazaa huko. Mi namfahamu huyo tu,”

    Kiti aliridhika na maelezo ya mama yake, hivyo akaona ni vema endapo ataitumia nafasi hiyo kuuliza swali la ziada.

    “Unamfahamu kiundani?” Kiti aliuliza.

    “Nani sasa… Ayuyube mwenyewe au binti yake?”

    “Binti yake,” Kiti alijibu bila kusita.

    “Mh! Mwanangu unataka kuwa mkwelima wa Ayuyube?” Mtobera ambaye ni mama yake Kiti alimuuliza mwanaye kwa mzaha huku akimwangalia usoni. Macho yao yalipokutana walicheka.

    Walifika Nyamuswa saa moja baadaye tangu walipoianza safari, walilakiwa na Koyonga mama yake na Matobera ambaye alifurahi kumuona mjukuu wake.

    Walisalimiana, wakapiga soga za hapa na pale huku muda ukiyoyoma.

    ****

    Kama ilivyokuwa kwa Kiti, Mina naye aliamka asubuhi na mapema akajiandaa. Kichwani alikuwa na wazo moja tu, nalo ni kwenda moja kwa moja nyumbani kwa kina Kiti kwa lengo la kuzungumza naye.

    Licha ya kuwa ulikuwa umepita muda mrefu, bado Mina aliamini kuwa kumbukumbu ya nyumbani kwao na Kiti ilikuwa haijapotea kichwani mwake. Alishawahi kwenda mara kadhaa alipokuwa akitoka shule wakati wa kufunga, na alipokuwa akienda shule wakati wa kufungua.

    Aliamini kuwa; ni lazima atafika tu, kwani hata kama kuna mabadiliko yasingeweza kuwa makubwa kiasi cha kubadilisha sura nzima ya mtaa wa Nyasura, nyumba hiyo ilipo.

    “Siwezi kupotea,” Mina aliwaza.

    Aliliendea gari lake jeupe, aina ya Toyota chaser. Akalitia ufunguo na kulitekenya gari lake hilo, likacheka. Aliendesha kuelekea ilipo lami, akalitia mafuta kwa safari ya kuelekea Nyasura, nyumbani kwao na Kiti umbali wa kama kilomita mbili hivi kutoka MLIMANI PARK alipokuwa kwa usiku mzima.

    Dakika tano baadaye alitoka kwenye barabara ya lami, akaishika barabara ya vumbi upande wa kushoto ukiwa kama unaelekea Musoma kutokea Bunda. Ni huko ilipo nyumba ya kina Kiti.

    Alienda moja kwa moja mpaka nyumbani bila kupotea. Alipofika aliegesha gari pembeni ya geti jeusi la nyumba hiyo, kisha akashuka kuiendea kengele.

    Mina alijishauri mara kadhaa kabla hajabonyeza kengele. Alipiga moyo konde akaibonyeza kengele halafu akajivuta nyuma kidogo ili kusubiri mwitikio.

    Geti dogo lilifunguliwa, kikafuatia kichwa na hatimaye kiwiliwili cha msichana mdogo ambaye kwa makadirio anaweza kuwa na umri kati ya miaka kumi hadi kumi na tano hivi. “Shikamoo?” yule mtoto alisalimia.

    “Marahaba, hujambo mtoto mzuri?”

    “Sijambo karibu,” alisema yule mtoto huku akiachia nafasi ili Mina aweze kuingia.

    Mina aliingia kwa kuanza na mguu mmoja uliofuatiwa na mwingine. Aliingia huku akiyaruhusu macho yake kutalii mazingira ya nje ya nyumba ile. Alikiri kuwepo mabadiliko, ingawaje hayakuwa makubwa sana. Waliingia mpaka ndani, sebuleni, ambako pia macho ya Mina hayakukoma kutalii.

    Utalii wa Mina ulikuwa sambamba na wasiwasi uliokuwa ukizitwaa fikra zake katika kila nukta ya saa. Alikuwa akiwaza; ni nini kitajiri mara atakapoonana na Kiti, na atamweleza nini mara baada ya kuwa wameonana. Mina aliwaza yote haya bila kupata majibu.

    Akiwa katikati ya mawazo hayo, mara sauti ya yule msichana aliyempokea ikamzindua Mina kutoka mawazoni, “Karibu… karibu ndani,” alisema yule msichana huku akimuelekeza pa kukaa baada ya kuwa wamefika sebuleni.

    “Asante,” Mina alijibu na kuketi kwenye kochi lililokuwa karibu yake. Mara baada ya kukaa, Mina alianza kwa kuuliza, “Nani yupo, yaani mtu mwingine tofauti na wewe?”

    “Nipo mimi tu na Amanda, yeye yuko bafuni anaoga,” alijibu yule msichana.

    “Na Kiti pia hayupo?” aliuliza Mina kana kwamba hakumsikia vyema yule msichana wakati akimtajia waliopo.

    “Naye pia hayupo,”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Labda alikwambia kuwa anaenda wapi?”

    “Wameenda Nyamuswa kwa Bibi,” jibu hilo lilimkata maini Mina. Alipajua fika Nyamuswa, alipajua tangu wakati ule alipokuwa anasoma Ikizu High School. Kwani kwa mara kadhaa aliwahi kupitisha muda na hata siku akiwa pamoja na Kiti katika kijiji hicho ambacho kiko kilomita nne au tano kabla ya kufika shuleni Ikizu waliposoma yeye na Kiti enzi hizo. Alijua kuwa haitakuwa rahisi wakawahi kurudi, zaidi watachelewa tu. Watachelewa mpaka saa ngapi? Lilikuwa ni swali ambalo jibu lake hakulijua. “Yawezekana wakalala hukohuko” Mina aliwaza kabla hajauliza, “Wamekwenda na nani?”

    “Wamekwenda na mama,”

    “Walisema kuwa watarudi muda gani?” lilikuwa ni swali jingine alilouliza Mina, aliliuliza huku akiwa hana matumaini ya kupata jibu ambalo lingeyapunguza mashaka yake.

    “Sijui kwakweli, kwa sababu hawakusema muda watakaourudi.”

    “Ok sawa, kama sikosei wewe ni Nyakenda, siyo?” Mina aliuliza baada ya kukumbuka kuwa miaka kadhaa nyuma, wakati ambao alikuwa akija na Kiti kwenye nyumba hiyo kulikuwa na mdogo wake na Kiti ambaye alikuwa na Umri kati ya miaka saba mpaka tisa wakati ule, hivyo alijiaminisha kuwa ni lazima huyu atakuwa mtoto yuleyule aliyemfahamu kwa jina la Nyakenda.

    Yue msichana alichanua tabasamu usoni pake kisha akajibu, “Ndiye mimi,”

    Baada ya jibu hilo kutoka kwa Nyakenda, Mina naye aliunda tabasamu ili kuiteka zaidi imani ya Nyakenda ili aamini kuwa Mina si mtu mbaya, kwa sababu alianza kujiaminisha kuwa; yawezekana majibu anayopewa siyo ya kweli kwa sababu ya kutofahamika kwa mtoto yule.

    “Sasa Nyakenda jamani, ina maana umemsahau wifi Mina? Nilikuwa nakuja hapa na Kiti wakati ule tunasoma Ikizu Sekondari”

    Huku akitabasamu na macho yake akiwa ameyaelekeza chini, Nyakenda alijibu, “Namkumbuka,”

    “Mina ndiye mimi… au nimebadilika sana wifi yangu?” njoo tukae hapa unieleze vizuri,” alisema Mina na Nyakenda akaenda kwenye kochi alilokaa Mina, kisha Mina akaendelea, “Hebu niambie ukweli wifi yangu… Kiti ameenda wapi?”

    “Ameenda Nyamuswa… wameenda na mama kwa bibi,” Nyakenda alirudia jibu lilelile la awali na kumfanya Mina aanze kuamini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Una namba yake ya simu?”

    “Hapana, namba yake ya sasa sina. Tangu arudi hajanipa namba yake, labda nikupe ya mama... kwa sababu wako naye huko.” Alisema Nyakenda.

    Mina alilifikiria jibu la Nyakenda, akaafikiana naye kuwa; yawezekana ni kweli Nyakenda hana namba za simu za kaka yake, lakini la kuchukua namba za mama yake na Kiti kidogo lilimtatiza. Atamueleza nini mama Kiti mara baada ya kuwa amempigia simu?

    Mina akapiga moyo konde, akaichukua namba ya simu ya mama Kiti, wakati huohuo akifikiria namna nyingine ambayo ingekuwa mbadala wa kumpigia simu mama Kiti.

    Kabla hajaondoka alimpatia Nyakenda business card yake ili Kiti atakapokuja apewe.





    ****





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog