Simulizi : Kurasa (The Page)
Sehemu Ya Nne (4)
Jibu lake lilionekana kabisa kuwa tayari amechoka. Alijibu kuwa wazo lile la kutumia risasi ndio kwanza alilipata siku ile na muda uleule, pia akanionyesha jeraha la mguuni alilipata mara tu alipokua akikimbizwa na Simba. Ajabu ni kuwa mie nilitupwa huku nikafungwa kamba, yeye akaachwa huru lakini akatupwa kwa wanyama wakali, bado sikuona nafuu.
Nilimnyanyua na kuanza kutembea yeye mwenyewe tukiwa tunaelekea kule kwenye mnazi. Pale nikamuangushia madafu kama manne hivi, akala kwa pupa sana kuonyesha kuwa alikuwa na njaa sana.
Tukamaliza siku 3 ndani ya pori la kisiwani pasina kuona mtu yeyote, si mvuvi wala mkazi.
Siku iliyofuata mida ya alasiri tukaona helicopter ya jeshi ikipita angani, tulipiga sana kelele lakini hawakutusikia, walikuwa wapo juu sana, ikatokomea tukiitazama tu. Wakati inarudi nilimuona James akikaribia kulia.
Mikono yake ilikuwa ikijisachi mfukoni na kutoa kiberiti huku bado akionesha kuendelea kutafuta kitu kingine.
Nilimuuliza anatafuta nini? Akaniambia risasi, nikampa risasi yangu moja iliyokuwa imebakia, akachana nguo yake iliyokuwa imechakaa na kuiwekka risasi kati kisha akaiwasha ile nguo.
Akahakikisha imeanza kuwaka na kusogea karibu kusimama huku tukiitazama ile nguo wakati huo ile Helicopter ya jeshi ilikuwa ikiranda angani. Mlio ule wa risasi ukaendana na mikono yetu ambayo ilikuwa hewani tukiipunga kwa nguvu.
Safari hii walituona na kutusogelea kisha wakatutupia kamba, nikamsogezea James kwanza katangulia, kisha nami nikashika kamba na kupanda tukikiacha kisiwa peke yake na tukiwa hatuna hamu hata kidogo ya kuendelea kuwepo pale hata kwa dakika 0.
Ndani ya Helicopter walitufunga tena vitambaa usoni, nafikiri hawakutaka tujue tulikuwa wapi, tukapelekwa sehemu nyingine tofauti. Kufika kule tuliowakuta walikuwa ni watu wageni kabisa machoni mwetu lakini wakatupongeza kwa kuweza kumaliza ile sehemu ya kwanza salama.
Huku sasa yalikuwa ni mazoezi ambayo ni mazito kweli kweli na magumu mno. Mazoezi yalikuwa ni kama vile kupanda milima na kuvuka eneo moja kwenda lingine kwa kutumia kamba, jinsi ya kutumia bunduki na jinsi ya kutegua mabomu. Hakikubaki kitu kule, tulifundishwa hadi urubani wa awali ili tuweze tu kuongoza ndege inapobidi, tuliendesha hadi Excavotor, tulipewa pikipiki na kuambiwa tuziendeshe kwenye korongo huku juu pakiwa na helikopta iliyokuwa ikitupa risasi chini, hakika ni majanga matupu.
Haikuwa ni rahisi, ilichukua takriban mwaka mzima hadi kufaulu na kumaliza masomo yale, hali tukiwa wachache tuliofika mwisho, wengi wetu wakiwa wameshindiwa njiani na wengine kupoteza maisha.
Mwisho wa siku tuliofanikiwa tuliagwa kwa sherehe iliohudhuriwa na viongozi kadhaa wa nchi huku tukipewa nishani maalum ya kijeshi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kama motisha kwetu.
Tulirudishwa Dar Es Salaam na kusubiri kupangiwa vituo vya kazi lakini kwanza wakati tukisubiri kupelekwa maeneo husika, tukapewa likizo ya siku 21, yaani wiki tatu za mapumziko. Nikapanga siku hizo nimtafute mwanangu, maana sasa nilimuhitaji kuliko hata mshahara.
Nikaelekea zilipo ofisi za upelelezi mkoa na kumuulizia Stellah, nikaambiwa kahamishiwa Mtwara. Nikavuta kumbukumbu ni yupi rafiki yake wa karibu? Nikakumbuka ni Eva, nikarejea kumuulizia, nikaambiwa yeye yupo kitengo cha Inter Pol, kwa hiyo haji mara kwa mara sana ofisini, ila nilipoomba namba yake ya simu walinipatia baada ya kujitambulisha kuwa ni shemeji yake kwa Stellah.
Usiku nikiwa na Daud nikampigia simu Eva na kujitambulisha kwa jina la uongo, nikatunga hadithi ya uongo na kweli nae akaingia mzima mzima na kuniamini. Nikamuuliza kama Stellah karudi kutoka Mtwara, akanijibu kuwa hajarudi, hadithi ya uongo ikaendelea.
Nikamwambia nimepoteza namba ya Stellah iliyokuwa kwenye simu yangu niliyopoteza siku chache zilizopita, hivyo nikamuomba yeye kama anayo anitumie. Kwa kuwa tayari niliisha mdanganya awali, akaja na kunitumia. Nilishangilia na hata Daud akanishangaa.
Hata nae nilikuwa bado sijamwambia malengo yangu ni yapi, ila nikamjulisha kuwa siku ifuatayo, asubuhi nitakuwa na safari ya kuelekea Mtwara, hakupinga, maana tayari alikuwa akijua mie ni nani, tukaagana akinitakia safari njema.
Niliwasili Mtwara jioni na kutafuta Guest ili kujibanza, kama kawaida sikutaka kumsumbua akiwa amelala, asubuhi na mapema nikampigia, akaitikia kama mtu aliekuwa akilia, nikiwa nimebadilisha sauti nikampigia na kumuuliza alipo.
Hakunijibu bali aliniuliza ni nani mie? Nikamwambia mie ni mpelelezi binafsi toka Dar Es Salaam na kumdanganya jina. Akaniuliza shida, nikamwambia nataka kuonana nae, akaniambia hana muda, leo ana safari ya dharula kuelekea Dar Es Salaam kuna tatizo la kifamilia, akakata simu na kuniacha sijielewi.
Nikajua kwa vyovyote vile kama kweli ana tatizo la kifamilia ambalo linamlazimu kusafiri, basi ni lazima ataenda ofisini kwao kuripoti kabla hajaondoka. Nikaongoza hadi kituoni na kumuulizia, nikajibiwa bado hajafika, ila muda si mrefu atakuwa pale, nikatoka nje kumsubiri.
Kweli haikuchukua muda mrefu, Stellah akawasili na gari ndogo, akaingia ndani na hakukawia kutoka akiwa ameongozana na kijana nadhifu wa kiume
Walisimama usawa wa gari ile aliyokuja nayo Stellah kwa takriban kama dakika mbili tatu hivi kisha wakaagana, kijana akarejea ofisini na Stellah akaingia garini na kuanza kuondoka taratibu.
Mie nikaita Taxi na kumfuatilia, safari yake iliishia maeneo ya mikindani kwenye nyumba moja nzuri sana, ilionekana kabisa kuwa ni moja kati ya nyumba za maofisa wakubwa wa Jeshi.
Nilimuacha akatangulia kuingia ndani kisha nami nikamfuatia kuingia kwa kutumia utaalamu wangu mwenyewe, sikutaka anione tukiwa nje ama hata mle ndani, kwa sababu maalum ambayo inanifanya nisite kuielezea kwa sasa. Nikazama ndani na kumkuta akiongea na simu akiwa amezamisha kabisa mawazo yake kwenye simu ile na kunipa nafasi mzuri kwa mimi kuweza kuingia bila kushtukiwa nae, nilifanikiwa kwa hilo, pasina kuniona bado mi nikatoa Mask na kuivaa. Alikuwa akimwambia mtu wa upande wa pili kuwa yeye anaondoka muda sio mrefu kuelekea hukohuko Dar kwa gari lake, lakini haamini kama atamkuta mtoto akiwa salama, aliongea huku akilia. Hapo nilihisi kuchanganyikiwa.
Nilijiuliza ni mtoto yupi ambae ametekwa? Ni mtoto wangu mie ama kuna kazi alipewa ya kumlinda mtoto wa mtu mwingine ndio ametekwa? Wazo hilo la mtoto wa mtu mwingine, hapohapo nililifuta kutokana na kulia, niliamini mtoto wa mtu mwingine hawezi kumtoa chozi, huyo alietekwa atakuwa ni mtoto wetu tu huyo.
Nikatoa big G na kuila na maganda yake na kuingia ndani kupitia mlango wa uwani, nikamkuta amekaa sitting room akiwa anaweka nguo kwenye begi. Nikamsogelea, aliogopa sana, niliona kabisa mshtuko alioupata ni mkubwa mno, maana hakutegemea kuona mtu muda ule tena ndani.
Hata kabla sijamsogelea zaidi huku nikitembea kama mtu mwenye ulemavu wa mguu, nikidhamiria kumchanganya kabisa, nilianza kumtuliza huku nikikaa kwenye sofa mbele yake kwa kumwambia kuwa mie ni rafiki yake na nimekuja kwa jambo jema tu wala sikuja kiugomvi, ila nikamuonya kama atajidai yeye anajua sana, basi nami nitambadilikia muda uleule.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kabla sijaendelea kusema chochote, Stellah akasema kwa utaratibu huku akiomboleza akiniomba tusimuue mwanae. Nikamwambia kwa kujiamini hali ya kuwa sijui lolote na tena nami nina wasiwasi na mwanangu, nikasema, mtoto yupo kwenye kamba muda huu.
Dhahiri nilimuona kapoteza ujasiri na chozi likaanza kumdondoka, nikatoa bastola ndogo aina ya Revolver na kumuelekezea huku nikisimama na kumwambia anasadikiwa kuwa yeye anashirikiana na majambazi, nikamlazimisha aniambie mtoto yupo wapi na kwanini ametekwa.
Kwanza alikanusha yeye kujihusisha na majambazi kisha akaniambia mtoto katekwa huko Dar na nilipomuuliza ni kina nani wamemteka mtoto, akajibu kuwa ni majambazi yanataka mtu wao waliomshikilia kituoni Dar Es Salaam ndio watamuachia mtoto wake.
Sasa ndio nikapata picha na ili kuikamilisha picha yangu iliyokuja kichwani, nikamuuliza huyo Jambazi walie mshikilia wamemuhifadhi wapi, alisita kunijibu swali lile hadi nilipomkaribia na kumtaka asimame, nikamkumbusha onyo langu la awali kuwa nitambadilikia.
Hapo ndio akaniambia kuwa wamemuweka kwenye selo ndogo ya pale kwenye idara yao, nikamuita anisogelee nikiwa namtazama kwa umakini wa hali ya juu, nilikumbuka mengi sana wakati Stella akipiga hatua za kiunyonge kunifuata hali bastola imemuelekea.
Bado alikuwa na hofu, aliponikaribia nikamwambia ageuke ukutani, akatii amri, nikamsachi na kutoa bastola ndogo kwenye paja lake la kushoto, nikaitoa Risasi na kuiridisha alipokuwa ameiweka, risasi nikaziweka kwenye koti langu kisha nikafunga mlango wa Sitting room yake.
Na kuweka zile risasi chini na kumpitishia funguo kwa chini ya mlango wake ili afungue kwa ndani aweze kutoka mie nikiwa tayari nimepotea, nilifanya hivyo kwa ajili ya usalama wangu, kisha nikamuwaga na kumwambia tutaonana siku ifuatayo jijini Dar Es Salaam.
Nilitoka haraka haraka na kusimamisha bodaboda iliokuwa ikipita eneo lile na kuelekea hotelini kuchukua vitu vyangu kabla ya kuenda uwanja wa ndege wa Mtwara, nilielekea moja kwa moja kwenye ofisi za mawakala wa ndege na kutafuta nafasi ya usafiri.
Kwa bahati mzuri ndege Mtwara zipo kila wakati, nikapata ndege ya mchana na kuondoka, niliwasili mapema jijini Dar na kwenda nyumbani kwangu moja kwa moja nikiwa na imani ya kumpata mtoto wangu hivi karibuni, nilivyofika nikaanza kujipanga nini nifanye kuanzia siku ifuatayo.
Kichwa kiligoma kunipa msaada nilioutaka, kila nilivyokilazimisha kichwa change kiendane na vile niwazavyo mie, ilinikataa, basi sasa nikalazimika tu kukiachia kichwa nafasi ya kufikiri ili baadae nisije kujilaumu kwa maamuzi ambayo si sahihi.
Hapo ikanilazimu nitoke kwenda nyumbani kwa jamaa yangu Daud, bahati ilikuwa upande wangu, nilimkuta akiwa na mkewe wakitazama Bongo Flavour walifurahi kuniona. Nilikuwa na tabasamu usoni kwa kuwaunga mkono furaha yao walio ionesha mara tu mimi nilipoingia mle ndani, lakini sikuwa na raha moyoni.
Niliwaambia kila kilichotokea kule Mtwara na kutaka ushauri wao. Daud akanishauri niende Polisi,
Nikakataa na kumwambia wazo langu ni kulishughulikia suala lile mie mwenyewe, sitapenda kabisa kulihusisha jeshi la Polisi kwenye suala langu hilo. Daud alishangaa na kuniuliza nitaanzaje kulishughulikia jambo lile bila Polisi kujua na hali linashughulikiwa na hao Polisi.
Sikuwa na jibu la moja kwa moja na kumwambia anipe muda zaidi wa kufikiria, maana akili yangu ilikuwa imechoka sana na ilikuwa ikihitaji kupumzishwa. Nikala chakula cha usiku pale na kuaga nikielekea kwangu nikiwa natembea kwa miguu tu maana sikuwa na haraka japo ni mbali.
Siku ya pili sikuwa nimejua ni nini cha kufanya wala hata wazo kichwani la kuniambia tu nianzeje shughuli ile sikulipata, ilinifanya niwe mnyonge kwa kufikiria hali ya mtoto. Nikapanga nimfuate Stellah moja kwa moja na kuongea nae, lakini akili ikakataa, nikapotezea wazo hilo haraka.
Alfajiri ya siku ya pili lilinijia wazo ambalo skuamini kama litanisaidia, lakini nilioga haraka haraka na kwenda nyumbani kwa Daud na kumtaka ushauri. Nilimwambia nataka kutumia nafasi yangu niliyonayo jeshini ili niweze kumuokoa mwanangu.
Bado hakuwa amenielewa ni nini ninamaanisha, nikamwambia ninaomba anifanyie msaada wa kupata kibali cha kijeshi cha kufanya upelelezi wa upotevu wa mtoto wangu. Sasa alinielewa na kuniahidi kunisaidia tena kwa mara nyingine.
Daud alikuwa ni mkubwa wangu kijeshi, nami nilikuwa nikimuegamia yeye kama ngao yangu, kila nilipokwama nilimuelekea yeye. Kutokana na kufuzu vizuri kwa mafunzo yangu, kikaitishwa kikao cha dharula nami nikaitwa pia.
Wakaniambia wamepata ujumbe wangu kupitia Kanali Daud, sasa nahitaji msaada gani? Nikawaambia naomba kibali cha kufanya kazi ile kama mpelelezi toka jeshini.
Likazungumzwa jambo lile huku nikihojiwa maswali mengi mno yakiwemo ya kwa sababu gani nimeamua mimi ndio nilishughulikie mwenyewe na badala ya kuwaachia watu walio na jukumu hilo?
Niliwajibu kuwa alietekwa ni mtoto wangu, na mimi pia nina uwezo wa kufanya uchunguzi na kumjua huku nikiwa na msaada wa kiusalama toka kwa watu wa usalama pindi utakapohitajika, wakanielewa na hatimae nikapewa kibali na kuulizwa kama kuna kingine?
Nikaomba msaada wa mtu mwingine mmoja tu mwenye uwezo mkubwa wa kupambana ili aniongezee nguvu, wakaniuliza tena naweza kuwaambia mtu huyo ni nani kama nimemuona? Nikasema naam! kabla hata ya kikao hicho tayari kuna kijana nilikuwa nimemuona alikuwa akiitwa Imma.
Ilinyanyuliwa simu na kuitwa Imma, akaambiwa kuwa aende name tukaongee, kuna kazi napaswa kuifanya ikishirikiana nae, kisha Brigedia akatuambia hadi siku ifuatayo, vibali vyote vitakuwa vimekamilika, nikashukuru na kunyanyuka, tukapiga saluti na kuondoka.
Nilimchukua kijana wangu hadi nyumbani na kumueleza hali halisi bila kumficha kitu tukiwa tumekaa Sitting room, muda mwingine nilisimama na wakati mwingine nilikaa, nae alikuwa akinisikiliza kwa umakini wa hali ya juu.
Alinielewa hasa! Alionyesha kuwa na ufahamu wa hali ya juu pia ni mtundu kupita kiasi na alikuwa na maswali ya papo kwa hapo. Tukio langu lilimgusa mno na kukiri kuwa amenielewa na kusema yupo nami kama mtu tuliekuwa nae pamoja Mtwara.
Akasimama na kuja kunipa mkono pale nilipo na kuniambia tusubiri vibali ili anionyeshe kazi, akaniahidi kuwa nitamkubali, nami nilimwambia asijali kwani mwisho wa siku atafurahi sana kama tutafanikiwa kumpata mtoto wangu akiwa salama.
**********
Asubuhi ya siku ya Pili akaja Imma akiwa na vibali mkononi akiwa na shauku kubwa ya kuanza kazi na kunitaka tuanze kazi yetu muda ule ule. Nikamwambia tunatakiwa tujipange kwanza ili tujue ni wapi tunaanzia, tukaketi chini mimi nikiwa nina glasi ya maziwa baridi nae akiwa ameniomba maji ya kawaida, yaani yasiyo ya baridi.
Kikao chetu cha pale kilikuwa ni cha kujipanga, tuanzie wapi na tunaanza na nini. Imma alikuwa vizuri kuanzia kiakili, akanishauri tuanzie ofisini kwa Stellah, ili kujua ni hatua ipi wamefikia.
Tukawasha gari yangu na kunza safari iliyotupeleka katikati ya Jiji la Dar Es Salaam kituo cha Msimbazi, kisha tukaelekea ofisi ya upelelezi ya Jiji la Dar, tukaonana na Mkuu wa Upelelezi wa Jiji (Regional Crime Officer) maarufu kama ni RCO na kumpa vibali vyetu na vitambulisho vya kazi mara baada tu ya kujitambulisha.
Aliviangalia na kutikisa kichwa kichwa kisha akaniuliza mie ni nini nahitaji kutoka kwake, kifupi alitoa ushirikiano mkubwa hasa pale nilipomwambia nataka kujua ni nani anasimamia kesi ile ilio andikwa kwenye kibali kile, hakunijibu, sio kama alidharu, bali hakuwa na hakika, alinyanyua simu na kupiga namba Fulani na kusema neno moja tu ‘Njoo’ kisha akarudisha mkono wa simu mahala pake.
Dakika takribani mbili akafika msichana mmoja na kukakamaa mbele yake na kusalimia, afande alitikisa kichwa na kumwambia atupeleke sie ofisi ya upelelezi kanda maalum na awaambie watusikilize na watupe msaada wowote tunao uhitaji, tukanyanyuka na kumuaga tukipeana mikono na kuondoka.
Sikujua nitakutana na nani kule ofisi ile ninayopelekwa, lakini hamu ya kumuona mwanangu ilinifanya nitamani sana kumuona askari anaesimamia kesi ile iliyofanya mwanangu kipenzi atekwe.
Tulifika ofisini na kuingia akiwa binti ametangulia mbele. Mlango ulipofunguliwa tu, ana kwa ana nikamuona Stellah mke wangu akiwa amesimama kavaa suruali iliombana sana akiwa ameegamia meza, mkononi alikuwa na jalada analisoma kwa umakini.
Nguo za aina hiyo kwa kazi yake ndio zilikuwa ni muafaka maana wakati wowote angeweza kukutana na mapambano ambayo yasinge endana na mavazi ya kujiachia kama sketi.
Unajua mshtuko alioupata? Kwa kweli alishtuka vibaya sana, sijui alikuwa na mawazo gani kwangu mie, sijui alidhani nimekufa? Ama sijui aliwaza nini. Maana mshituko ulionekana dhahiri kabisa hata Imma aliuona na bila hata kumwambia naamini alimtambua Stellah mke wangu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Stellah alikuwa ni mtu wa kwanza kuniona kati ya watu wawili waliokuwepo mle ndani, akasimama vema akiwa usoni anaonekana mwenye majonzi tele, nilijua yale majonzi yametoka wapi, nilikuwa nikitambua fika kwamba ni kutokana na kutekwa kwa mtoto, mtoto ambae ni wangu na nikahisi anaogopa kuniambia.
Mie wala jambo hilo halikuniumiza kichwa hata chembe. Kwa kuwa tulikuwa tumeingia kimya kimya, kuna mtu mmoja likuwa ametupa mgongo akifungua mafaili, niliweza kumtambua kuwa ni Inspektor Amani, nikapandwa sana na jazba, lakini nikajizuia. Nikamsalimia Stellah kwa salamu ya kawaida kabisa isio na bashasha hata kidogo.
Amani nae akageuka baada ya kusikia salamu, aligeuka kwa dharau na alishtuka baada ya kuniona na kuuliza kwa kejeli ni kwa nini tunaingia mle ndani bila rukhsa? Binti alietuleta akataka kuongea, mie nikamzuia, nikampa ishara Imma ndio aongee yeye.
Imma hakusema kitu, akatoa kitambulisho chake na kibali chetu na kumuonyesha Amani, Amani akapoa, yaani alikuwa ni kama bwege Fulani hivi kwa ghafla sana, Imma akanigeukia na kuniita Mkuu kifuatacho? Kauli ile niliona kabisa inawachanganya vibaya Stellah na Amani pia
Nikamtazama Amani na kumwambia tunataka file lile la kesi ile wanayo ishughulikia hakuwa mbishi tena, ajabu hata hakuuliza ni kesi ipi, maana nina hakika kabisa kwamba walikuwa na kesi zaidi ya moja ambayo wanashughulikia.
Nikahisi tayari ameingiwa na woga hasa akikumbuka juu ya kile walichonifanyia na mpelelezi mwenzie na pia hakujiandaa kwa tukio kama lile la kuvamiwa ghafla ofisini.
Akanikabidhi mkononi na nami nikalifungua na kulipitia kidogo wakati huo Imma alikuwa akinitazama mie, sikutaka kumuangusha kijana wangu, nilitaka ajue ni kiasi gani ninamthamini na ndio maana nimemchagua yeye kati ya vijana lukuki waliopo pale kambini.
Kuonesha hilo, nikamsogelea pale alipo japo nilikuwa nina uwezo wa kumuita na akasogea, lakini nilimfuata na kumpa lile jalada nae alipitie na kuona kama kuna chochote ambacho kinachotufaa.
Aliliangalia kwa dakika chache na kulifununua funua kidogo kisha akalifunga baada ya kupata kile alichoona kinatufaa, lakini wakati akilifunga alikuwa analiweka mezani na kuponda kuwa hakuna chochote cha maana ambacho sisi tunaweza kuchukua mle ndani ya file ile.
“Wanachokifanya hawa watu ni kupoteza tu muda wa kazi bure tu,” aliongea huku akiwa tayari ameliweka jalada lile mezani, name nilikuwa nikimtazama kijana wangu na kujivunia kwa kiburi chake ambacho alikuwa akikionyesha pale mie nikiwa nimeweka mikono yangu kifuani nimeikunja, kisha akawageukia na kuwauliza kama wamekula mlungula ama wamepokea takrima?
“Haiwezekani kesi ndogo kama ile ya kuchukua mwezi mmoja, wao watumie muda mrefu zaidi ya ule ambao wameutumia” Imma akawatazama kwa zamu Amani na Stellah waliokuwa kimya, akalinyanyua file lile na kumlazimisha Stellah kulipokea kwa kumuwekea mapajani mwake akiwa amesimama vilevile.
Imam alionekana dhahiri kuguswa sana na tatizo langu, maana niliweza kuona kabisa kwenye macho yake alikuwa akimtamani sana Amani, alitamani kama apewe nafasi ya kuchapana nae makonde, kwa kuwa mie tayari nilikuwa nimeliona, nikalazimika kuliepusha kwa kumuita Imma.
Aliitika na kuongeza kwa kusema kuniambia mie kuwa boss, hawa hawana jipya, wanakula bure tu pesa ya walipa kodi, maana wamejawa na uvivu tu, hawana lolote. Niliona Stellah na Amani wakiangaliana kwa jicho la wizi, nikamwambia Amani wamlete Yule mtuhumiwa wanae mshikilia
Inspekta Amani akasema wanae palepale, akasogea pembeni kidogo na kufungua geti la chuma na kisha kufungua mlango mdogo wa mbao uliokuwepo pale kwenye kile chumba kilichotumika kama selo ndogo kisha akamwita na kumtaka atoke kule chumbani.
NikamuangaliaStellah na kumwambia amfungue, ili tuondoke nae, Amani kwa mara ya kwanza akaonyesha kutaka kuleta upinzani, nikapiga hatua mbili kumsogelea na kujikuta tayari nipo mbele yake. Nikamtolea kitambulisho, alipokitazama, akakutana na bawa la ndege, akakauka Saloot na kunyamaza.
Stellah kama mtu asiejiamini vile, akamfungua pingu huku Imma akiwacheka kwa kejeli
“Yaani mtuhumiwa mmemfungia mlango, mkaweka geti, mkaongeza na kufuli, lakini nae tena kule ndani mkamtia pingu... Daah! Huo si unyanyasaji wa haki za binadamu?” Baada ya kauli hiyo, akiwa na tabasamu usoni akanigeukia na kuniambia…
“Mkuu hawa watu wanapaswa kabisa kupelekwa The Hague, haiwezekani wamnyanyase mwenzao kiasi hicho, duh!” kisha akacheka kwa dharau name nikatabasamu kwa mara ya kwanza huku nikirejesha kitambulisho changu mfukoni na kuanza kutoka bila ya kuaga nikiwaacha wala hawajui ni nini cha kufanya.
Kuna kitu nilikiona machoni mwao, na hicho kilionekana kama kwamba walikitegemea na mimi wala sikukigusia, nilipotezea kimya kabisa, kitu chenyewe kilikuwa ni kuhusu motto.
Niliamini kabisa kuwa hapo walitegemea nitahoji, lakini mimi sikutaka kabisa kujichanganya kupitia mtoto, nilitaka kumpata mtoto kupitia Yule kijana ambae wao walikuwa wamemshikilia.
Imma alinifuatia kwa nyuma akiwa amemdhibiti Yule mtuhumiwa na kuingia nae garini mimi nikiwa tayari nimeingia upande wa dereva, Imma na mtuhumiwa wetu wakawa wameingia sehemu ya nyuma ya gari ile. Wala hatukuwa na subira, bali tulijitambulisha sisi kama marafiki zake tumekuja kumuokoa pale.
“Sisi tutakuweka huru, lakini ili tukuachie, unapaswa kutueleza ukweli kwa kila tutakacho kuuliza. Ukikwepa ukweli wowote, utapata madhara makubwa mno mdogo wangu,” Nilimwambia nikiwa namtazama machoni, kwa sauti ya kijamaa sana, Imma akaongezea
“Najua humo ndani umeteseka sana, lakini hayo mateso uliyo yapata humo ni sehemu ndogo sana ya yale ambayo sisi tutakupa iwapo hutokubali kuwa nasi,” kijana Yule ambae alionekana kama hajatimiza miaka hata 20, aliahidi kuwa pamoja nasi.
Mahojiano yakaanza mle mle ndani ya gari huku Imma akiandika baadhi aliyoyaona ni muhimu, kiukweli alitujibu kila swali tulilomuuliza kutokana na kile alichokuwa amekiona mle ndani.
Tulimuuliza kuhusu bosi wa kazi yake akatutajia na kisha akatuelekezaa yalipo makazi yao na hata namba ya simu ya bosi wake, Imma akanishauri niongee nae.
Kitu cha kwanza kumwambia ni kuwa mtu wake ninae pale na wala yeye hapaswi kujua nimempata vipi, suala la msingi ni kucheza ‘deal’ mtu kwa mtu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaniuliza namaanisha nini? Nikamwambia, mie ni baba wa mtoto alienate, nataka mtoto wangu nimpe mtu wake. Akaridhia na kutaka kuongea na mtu wake.
Sikumfanyia hiyana, nikampa simu tena bila kitisho chochote, akamuhakikishia kwamba yeye yupo sehemu salama na akasisitiza kuwa tufanye makubaliano haraka ili aweze kuwa huru, maana mateso aliyoyapata kule kituoni ni kama kachungulia kifo.
Jamaa akanirudishia simu na kuanza kuongea na bosi wake, tukafikia muafaka kuwa biashara yetu ifanyike siku ifuatayo, maeneo ya Kigamboni saa 12 jioni tena bila askari kuwepo, makubaliano yakaishia hivyo na nikamuona Imma anamvua Tisheti yake, sikujua bado alilenga kufanya nini, lakini akamfunga machoni.
Safari ikaanza kuelekea nyumbani, lakini kichwani mwangu akili ikaniijia tofauti, nikababili mwelekeo na kuanza kuelekea kambini, Imma akaniuliza ni wapi tunaelekea na wakati awali tulielewana tunampeleka nyumbani kwangu? Nikamwambia wazo limebadilika ghafla na hivi karibuni atajua ni kwa nini.
Hakukuwa na swali tena wala mtu yeyote alie ongea. Tulipokaribia kambini nikatazama kwenye kioo cha ubavuni (Sight mirrow) nikaweza kuhisi kuna mtu anatufuatilia, nikamwambia Imma kama ameona. Akageuka nyuma na kutikisa kichwa, kisha akasema ameelewa ni kwanini nilibadili mwelekeo.
Nikamwambia karibu tena, akatabasamu. Kwa kuwa sikuwa na nia mbaya na Yule anae nifuatilia, nikajua ni wapi nitamuacha, nilimzungusha sana kwanza mjini ili kujiridhisha ni kweli anatufuatilia sisi ama nae ana yake, maana hapa ni mjini, nikapata hakika kuwa natufuatilia sisi, hakuwa mtaalamu sana.
Nilipoona nimechoka kuzunguka, nikanyoosha gari hadi getini, nikafunguliwa geti na kuingia ndani kisha nikaelekea hadi zilipo ofisi za Polisi wa Jeshi (MP Military Police) na lkumkabidhi nikiwaahidi kumfuata siku ifuatayo muda wa mchana. Wakamchukua na kumrundika Selo. Imma akaniaga kwa ahadi ya kuonana nae kesho kazini kisha akaelekea kwake.
Yeye alikuwa akiishi mlemle ndani, mie nikaona pia napaswa kwenda kupumzika kutokana na kazi itakayo kuwepo kesho. Sikutaka tena kutumia gari yangu ili kuepusha kuzidi kufuatiliwa, bali nikamuita dereva wangu na kumwambia anirudishe nyumbani kupitia gari ya ofisi.
Tulitoka na kila nilipojaribu kuangalia kama tunafuatiliwa, sikuweza kuona chochote, nikajiridhisha kuwa hatufuatiliwi, tukanyoosha hadi hotelini nikapitia chakula na kubeba kwa nia ya kwenda kula nyumbani.
**********
Saa 8 mchana tayari tulikuwa tunatoka kambini kuelekea Kigamboni eneo ambalo tulilopanga kukutana na wale majambazi, kutokana na Jam za barabarani na kuwa kwenye mwendo wa kawaida, tuliwasili Kigamboni saa 10. Imam alimfunga pingu Yule mtuhumiwa wetu kwenye kiti na kisha akasema anakwenda kuangalia usalama kwanza.
Nilitikisa kichwa kukubali nami pia nikashuka na kuzunguka hapa na pale. Imma alirudi baada ya muda na kusema kote kupo salama lakini mie nikiwa naongea nae nikamwambia usalama haupo, ninahisi kuna kitu kinaendelea. Mi nae wote tulikuwa tumesimama mbele ya gari tukiangalia bahari.
Upande wa kulia wa gari yetu, niliweza kuona kama kuna mtu amekaa na hakuwepo kabla ya sisi kuwepo pale, ina maana mtu huyo amezuka tu muda huu pia eneo lile huwa haliwekewi meza, imekuwaje leo liwe na meza?
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Imma nae akawa ameshtuka, alinielewa vema, kwenye fukwe ile palipowekwa meza, ilionesha kuwa pana msichana ameketi akinywa kinywaji chake huku ameshika kitabu.
Akanyanyuka kama vile anaendea vinywaji, nikarejea garini na kujifungia mlango.
Dakika mbili zilikuwa nyingi nikamuona Imma akiwa amerudi na mrembo akiwa amemuweka chini ya ulinzi, nilipomtazama ni nani, nikamgundua kuwa ni Eva, huyu ni mfanyakazi mwenzie na Stellah ambae tayari nilisha muelezea habari zake huko nyuma.
Tukaanza kumuhoji imekuwaje akawa pale, akatujibu kuwa amekuwepo pale tangu asubuhi akitufuatilia sisi, nikamtazama Imma kisha nikamuuliza amejuaje kama sisi tutakuwepo pale?
Akasema mazungumzo yetu ya Jana na Yule Jambazi ndio yamewajulisha kuwa sie tutakuwa pale, maana namba yake ile imeunganishwa na makao makuu ya Polisi.
“Ok! Nimekuelewa, chochote anachoongea na watu wake, nyie mnakisikia, si ndio?” nilihoji
“Haswaa” akajibu Eva akiwa anajiamini, Imma nae akamuuliza
“Inakuwaje sasa siku zote hamjamtia nguvuni na hali mawasiliano yake yote mnayo na mnayafuatilia?”
“Hajawahi kutoa maelezo ya maana kama jana, kila siku amekuwa akiruka ruka tu, ila yale ya jana ndio yamenyooka, karibu kila wakati wamekuwa wakiongea lugha ambayo inatupa wakati mgumu kuitambua,” jibu lilikuwa haliridhishi, lakini ikalazimika tu kulikubali, nikamwambia Imma amuache aende zake.
“Mkuu, unasema nimuache aende huyu?” aliuliza Imma kwa mshangao ambao ukanifanya nitabasamu, kwani sikutegemea kama atashangaa kiasi hicho kwa jambo hilo dogo tu.
Nikamsisitiza kwamba amuache aende, Imma akamfungulia mlango atoke na wakati alipokuwa akiondoka nikamuuliza tena wapo wangapi. Akaniambia pale kiujumla wapo 7 na muda wote wamekuwa wakiwasiliana na wenzao ambao wapo kituoni hivyo wakihitaji msaada wakati wowote wameambiwa wawajulishe. Akaenda zake, tukaona kazi imekuwa ni nyepesi zaidi kwetu. Muda tulio kubaliana ukafika na tukaanza kusogea eneo husika, garini nilikuwepo mie na Yule mtuhumiwa tu, Imma alikuwa amebaki nyuma yetu akiwa na pikipiki ambayo tulikuwa tumeikodi kwa ajili hiyo na tayari alikuwa ameitanguliza kule tangu asubuhi, maana hivyo ndivyo tulikuwa tumejipanga ili kufanikisha lengo letu.
Nikafika eneo husika na kusimama, nikachukua Big G kwenye dash board ya gari yangu na kuanza kumenya huku nikitoka nje, nikasimama usawa wa mlango wangu nikiangalia huko na kule. Nikamwambia Yule kijana atakaposikia nimegonga dirisha mara mbili atoke nje.
Saa yangu ilinishawishi kuamini kuwa wale jamaa watachelewa kuja, maana tayari ilibaki dakika moja tu kufikia muda tulio kuwa tumeelewana na hakukuwa na dalili yoyote.
Kama hatua 15 mbele yangu, ikasimama gari moja nzuri aina ya Altezza ya rangi ya bluu ya bahari na simu yangu ikaita. Sikujisumbua kuiangalia, bali nilipo ipokea tu nikauliza kama wapo tayari, nae hakujibu bali alisema wanataka kumuona mtu wao.
Nikagonga dirishani kama nilivyomueleza nae akajitokeza, nikamfungua kitambaa machoni na kumwambia hatua kwa hatua, ujanja wowote utagharimu maisha ya watu wengi zaidi, kisha nikamruhusu jamaa aondoke, kule napo wakamuachia mwanangu akianza kuja huku nilipo.
Mwendo wake ulikuwa ni wa taratibu mno, nilitamani afike haraka, nilitamani kumshika na kumkumbatia, lakini mwendo wake wa kitoto, ulinifanya mimi niweke mawazo yangu yote mikononi mwa mtoto wangu ambae leo namuona kwa mara ya kwanza.
Walipishana huku wakitazamana, sote silaha zilikuwa mkononi, ilikuwa ni kama pata potea, wale jamaa sikuwa nikiwaamini sana ila nao ilionekana hata nami pia hawakuwa wakiniamini, hatua 3 kabla hajanifikia mwanangu, nikachuchumaa na kumpokea mwanangu kwa furaha kubwa sana, nafikiri sijawahi kuwa na furaha ya aina ile kwa zaidi ya miaka mitano hivi.
Nilimkumbatia huku nikimpapasa kichwani, chozi la furaha likinitoka, kichwani mwangu nilipanga sitampa tena Stella huyu mtoto wangu. Nikaamua nitamlea mwenyewe.
Nikamgeuza kichwa na kumwambia aniamkie, akaniamkia. nikamuuliza huku nimemshika shingoni, ananijua mie ni nani? akatikisa mabega kukataa, nikafurahi sana hata sijui kwanini.
Nikamwambia kuwa mie ndio baba yake, akakataa na kusema baba yake hayupo, nikamwambia ndio tayari nimeisha kuja. Ghafla nikakatishwa maongezi yangu na kelele za gari iliyokuwa ikiondoka kwa kasi, nami kama umeme nikamkwapua mwanangu na kumuingiza garini na kuanza kuifuatilia ile gari ya majambazi nikiwa na mwendo wa kasi sana.
Nilianza kuwasiliana na Imma akaniambia yeye tayari yupo kule mbele anawasubiri, na kuna timu nyingine inayo ongozwa na Eva ipo upande wa pili. kweli hawakufika mbali, wakakutana na Imma aliekuwa kapaki pikipiki pembeni ya barabara na kusimama katikati ya njia akiwaelekezea bunduki. alimaanisha wasimame.
Dereva hakuonyesha nia ya kusimama, bali aliongeza mwendo na hatimae Imma kwa mbali akaona kuna mtu anajitokeza upande wa pili wa dereva akiwa na short gun. hakutaka tena kujiuliza, aliruka pembeni na kumlenga yule jamaa kisha akapeleka risasi kwenye tairi la mbele.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tairi likakubali sheria, gari likapoteza mwelekeo na kuelekea porini kabla ya kugota kwenye gema, pasina kutegema tukaiona Helikopta ya Polisi ikiranda randa angani na kututaka watu wote tusalimu amri na kuwa watulivu.
Daud nae muda ule ule akanipigia simu na kuniambia amejulishwa na ofisi ya Upelelezi makao makuu kuwa tupo Kigamboni, nae amefika lakini hajui tupo wapi. Nikamuelekeza ili afike pale tulipo, kisha nikashuka garini kusogea eneo la tukio.
Majambazi matano yalikuwa garini, mmoja alikufa kwa risasi, wawili waliumia kwa ajali na wengine wawili wakatoka wakiwa wazima kabisa, lakini wote walijisalimisha kwenye mikono ya askari hasa pale walipoona idadi ya watu ikiongezeka.
Nikamsogelea Imma na kumpa hongera kwa kazi nzuri aliyoifanya na kumwambia turejee hotelini kwetu, kabla ya kuingia garini nikawaona Stellah na Amani wakinisogelea, nilipandwa na jazba vibaya, awamu hii sikuweza kujizuia tena.
Nilimfuata Amani na kumuomba tuongee pembeni kidogo, hakusita kukubali, nikaanza kuelekea ufukweni nae akinifuata bila hofu yoyote tena akiwa na tabasamu usoni, hakujua yaliyopo moyoni mwangu.
Tulienda umbali kidogo na kumwambia kuwa leo ndio leo, nikamtazama na kumwambia kama anakumbuka alivyo niadhibu mbele ya mke wangu akiwa ni mjamzito, nikamwambia kuwa sasa nami leo ninamuadhibu vilevile mbele ya wafanyakazi wenzie.
Aliniona nikimsogelea, hakuamini kama nilikuwa nina maanisha kile nikisemacho hadi nilipompa ngumi ya shingo na teke la kifuani, karibu wengi wao walikuwa wakitazama tukio la gari ile kuanguka, lakini Stellah aliona kilicho jiri na kupiga kelele.
Umbali uliokuwepo kati yetu na wao, ulinipa nafasi ya kumuadhibu zaidi, kwa mafunzo niliokuwa nayo niliamini itawachukua karibu dakika moja nzima kutufikia, na kwa muda huo niliona utanitosha kabisa kumuadhibu Amani ambae niliona ni kama mkosi kwangu.
Daud ndio aliweza kunituliza mara alipofika pale lakini hapo tayari Amani alikuwa kwenye hali mbaya na bado mie nilikuwa na hasira kwelikweli, badala ya kushughulika na majambazi ambayo muda huo yalikuwa ndani ya pingu kwenye magari ya Polisi, wao walihangaishwa na ugomvi wetu.
Stellah alikuwa akilia huku kamshika mtoto wangu, nikamfuata nikiwa na hasira kwelikweli na kumwambia nipe mwanangu, jinsi aliyoniona, hakujiuliza mara mbili, alimuachia bila hiyari, nikasikia sauti ya Amani ikisema nimuachie mtoto wake.
Niligeuka kwa ghadhabu huku nikimtazama kwa hasira, nilitamani nimfuate tena nikaendelee kumchakaza, niliamini huyu ndio chanzo cha matatizo yote yale, Daud aliliona hilo, akanizuia huku akinitaka nipunguze ghadhabu, Imma akamchukua mtoto wangu na kuingia nae garini.
Mtoto wangu alikuwa akilia huku akiita baba na kutaka kutoka nje, niliamini ananiita mimi, nikamwambia Imma amuachie aje, lakini mtoto alipotoka akakimbilia kwa mama yake wakati huo bado Amani yupo chini akiugulia maumivu.
Nikamfuata Stellah anipe mwanangu niondoke eneo lile, mtoto nae hakuwa tayari, nikambeba nikijua tatizo ni mazoea, hakuwahi kuniona hata siku moja hivyo nikaamini akiishi name atanizoea.
Hatua kadhaa mbele, Stellah akanza kuja akilia na kunishika magoti akisema nimuachie mtoto wake. Jibu nililompa lilikuwa yule si mtoto wake pekee, bali ni mtoto wetu sote, yeye amemtunza kwa muda mrefu na sasa ni zamu yangu nami kumtunza.
Amani akajitutumua na kusema yule si mtoto wangu bali ni mtoto wa kwake yeye.
Nikamshusha chini mtoto na kumuuliza Stellah yule mtoto ni wa nani? Akajiuma uma na hatimae akasema yule ni mtoto wa Amani, nikamuachia kwa kuamini kuwa kuna watoto wawili tofauti, hivyo yule sio wa kwangu, sasa mtoto wangu mimi yupo wapi?
Swali lie lilimlenga Stellah moja kwa moja, nikamuona akiwa kimya tu, nilipomuuliza kama mara mbili 3, nikahisi tayari niliisha ibiwa kitambo, nilipatwa na jazba kuliko hata siku ile nilio achwa porini peke yangu.
Nilipiga hatua mbili ndefu, nilipomkaribia nikampiga kibao kimoja cha nguvu sana Stellah na teke la mbavu, akaenda chini moja kwa moja na kabla mwili haujagusa ardhi nikamshindikiza na kifuti cha tumbo, nilidhamiria kumuua kabisa.
Kipigo kile kilimfanya apoteza fahamu palepale, name bado nilikuwa na shauku ya kuendelea kuwaadhibu wote, kifupi nilikuwa nimechanganyikiwa, wakiwa watu wote bado wana tahayari, nikamrukia tumboni na kumkanyaga vilevile akiwa amezimika.
Imma ndio akapata akili ya haraka na kuja kunisukuma pembeni na kuwahi kumnyanyua Stellah, ambae wakati huo alikuwa akivuja damu mdomoni.
Nilitamani angekuwa yupo vizuri, ili nimfinyangefinyange lakini bahati mbaya kwa upande wangu ni kuwa Stellah alikuwa bado kapoteza fahamu na damu ilikuwa ikimtoka mdomoni, ambapo kwa upande wake ilikuwa ni bahati mzuri.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaingia garini na kuondoka kwa kasi hadi Ferry na bahati ilikuwa ni yangu, nikakuta Pantoni ipo nikafanikiwa kuingia na kuvuka kisha nikaelekea hadi kwangu nikiwa hata sijielewi.
Niliingia ndani na kwenda kufungua friji na kuchukua maji ya baridi sana na kuyanywa kwa mfululizo.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment