Search This Blog

Friday, October 28, 2022

ZARI LA NDOA - 2

 

     





    Simulizi : Zari La Ndoa

    Sehemu Ya Pili (2)





    Asubuhi na mapema Sungura akampigia simu na kumueleza kuwa kutokana na vigezo vya elimu yake, tayari amepata vyuo mikoani na kumtaka achague kimoja ambacho atapendezwa nacho.



    Zainab hakuwa na makuu, akamwambia Sungura yeye amalize kila kitu, akakubali na kisha akakata simu na kuelekea Internet Cafe ili kwenda kuchukua fomu kwa njia ya mtandao, akiwa amemchagulia chuo kimoja huko mkoani Iringa.



    Baadaya kudownload fomu ya maombi na kuprint, alirudi nyumbani na kumjulisha mpenzi wake kuwa zoezi alilokuwa amempa, yeye amelikamilisha kwa asilimia 100, kilichobaki sasa ni yeye kumalizia sehemu yake.



    Jioni Zainab akaenda kwa mpenzi wake na kwa kushirikiana nae, wakajaza fomu zile na walipomaliza wakapiga soga hadi usiku, Sungura akamshindikiza kwao akiwa na fomu zile ili kumuonyesha baba yake.



    Baba mtu wala hakuwa na pingamizi, aliipenda sana elimu hivyo alikuwa tayari kabisa mwanae asome, alimpa ushirikiano wa kutosha, kila alichohitaji akamwambia akiandike na ampe mahitaji yote tofauti na yale yaliyo orodheshwa ndani ya fomu ile ya chuo.



    Mapema sana siku iliyofuata, Zainab alifika kwa Sungura na kumpitia waende ofisi za Posta kwa ajili ya kutuma fomu zile kama ambavyo maelekezo yalisema, kisha wakarejea nyumbani baada ya kumaliza zoezi lile.



    Nyumbani napo walikuwa na kazi maalum, Zai alitaka kujua mahitaji ya nje yanayo hitajika tofauti na yale yaliyo orodheshwa kwenye fomu ili ampe baba yake bajeti yake kwa ajili ya maandalizi.



    Ikafika siku ambayo watu wote pale Songea walikuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa mno, ilikuwa ni siku ambayo kulikuwa na mechi kubwa sana ya mpira wa kikapu kati ya vijana wa palepale Songea mjini ambao walitambulika kama wenyeji.



    Vijana walikusanyika na kuunda timu moja kutoka kwenye kata za Bombambili, Lizaboni, Matarawe, Majengo, Ndilimali Tembo hadi Mahenge na kata zingine zote, hivyo kukawa nahamasa kubwa.



    Wageni nao waliwasili mapema mno kutoka Iringa wakiwa na shauku kubwa mno ya kuja kushinda. Waliwasili wakiwa na gari mbili aina ya Nissan Civilian ambazo zilibeba watu wasio pungua mia na kuelekea uwanjani moja kwa moja.



    Huko uwanjani tayari watu walikuwa ni wengi mno wameisha fika na kusubiri mtanange. Mashabiki wa mpira wa kikapu walijitokeza kwa wingi na hata wapenzi wa soka nao siku hiyo walijitokeza kwenda kutazama burudani ile adhwiim ambayo ni adimu.



    Kati ya wapenzi wa soka aliekuwepo uwanjani, alikuwa ni Simba, kaka yake Sungura, alikaa karibu sana na shemejie Zainab akiwa ametenganishwa na watu watatu tu. Timu zote ziliwasili na kusubiriwa muda tu ufike.



    Mpira ulianza kwa kasi ya ajabu, watu walikuwa na munkari ya ushangiliaji, Sungura alikuwa yupo vizuri sana kiwanjani, aliwasumbua sana wapinzani wao, kwenye robo ya kwanza tu pekee alikuwa tayari ameisha tupia michomo ya pointi 3 mara tatu.



    Kitu hicho kiliwauma sana wachezaji na viongozi pia na mashabiki wa Iringa waliokuwa wakijiita Ruaha. Pia upande wao kulikuwa na kijana aliekuwa akiitwa Matwiga, huyu nae alikuwa akisumbua sana kwa upande wa Songea, walinzi walipata tabu mno.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuwa amesumbua sana, walinzi wawili wakapanga na kumfanyia faulo iliyo sababisha atoke nje ikiwa ni robo ya pili tu akaenda kupumzika kwanza. Watu wengi walikwenda kumpongeza.



    Wakati mechi ikiendelea, akanyanyuka na kuanza kutembea tembea kuzunguka maeneo yale ya uwanja. Alizunguuka karibu uwanja mzima. Alipomkaribia Zainab, alimuona na moyo wake ukapiga mshindo mkuu.



    Aliondokea kumpenda ghafla mara tu baada ya jicho la kwanza, bahati ni kuwa walikutanisha macho, Matwiga akatabasamu, Zainab akacheka, basi Matwiga akamsogelea na kumsalimia, hakuleta mapozi, akamsalimia kama ambavyo anasalimiana na watu wengine.



    Baada ya salamu ile kila mmoja akashika hamsini zake, lakini tayari Matwiga alikuwa ameisha pata marafiki kutokana na aina ya uchezaji wake wa mpira na ubora alio uonyesha. Kiwango kikasababisha apate marafiki wa palepale Songea.



    Hao ndio akapanga kuwageuza ngazi ya kupanda kufika kileleni, yaani akapanga kuwatumia ili kumpata Zainab, hivyo akawauliza binti yule mrembo ni nani, kwao wapi na anashughulika na nini?



    Ni rahisi sana mtu kukunyima chakula, lakini sio neno. Wakamueleza jina, wakamuelekeza anapoishi, wakakwama kwenye kile anachofanya, maana walimwambia kwamba Zainab yupoyupo tu hana shughuli yoyote.



    Kumbe walikuwa wamempoteza Matwiga, akawauliza kama wanamjua mpenzi wake, maana aliwaambia msichana mrembo kama yule na kwa umri alionao hawezi kuwa hana mpenzi, hivyo akawaomba kama wanamjua wamuoneshe.



    Jamaa wala hawakumbania, wakamuonesha Sungura aliekuwa akiwajibika uwanjani na kusumbua. Akatikisa kichwa na kumtazama kwa umakini sana Sungura. Matwiga alikuwa ni mdadisi sana.



    Akaendelea kuhoji kwamba Sungura anafanya kazi gani kwa sasa? Wakamjibu kuwa kwa kipindi kile amekuwa akifundisha fundisha tution kwenye shule za sekondari pale Songea wakati akisubiri majibu ya mtihani wa kidato cha sita.



    Matwiga akawashukuru jamaa wale kwa msaada mkubwa waliompatia, kisha akawaaga kuwa anarudi kwenye benchi. Akawaacha wakiwa bado wana hamu ya kuongea nae wakati nae moyoni mwake akijiapiza kumpata Zainab kwa gharama yoyote.



    Mechi ikiwa kwenye robo ya mwisho, Sungura aliendelea kusumbua sana, Matwiga akamfuata dada mmoja aitwae Zawadi ambae wamekuja nae kutoka Iringa na kumueleza kuhusu Zainab.



    Zawadi akawa bado hajamuelewa ni kipi Matwiga anataka, ikambidi afunguke na kumwambia anataka Zawadi aende akamchomoe Zainab pale alipokaa na kumpeleka pembeni ili aongee nae pembeni.





    "Mimi nitakuwa pale chini ya mti nawasubiri, uje nae hapo," aliongea akimuonesha kwa kidole mti ambao ulikuwa mbali kidogo na eneo lile.



    "Changu ngapi? Mjini hapa," Zawadi mtoto wa mjini alimuuliza huku akinyoosha mkono.



    "Shuka la Mmasai, umenisoma? Utabeba tembo wala usiwaze," alimaanisha amemuandalia shilingi Elfu kumi.



    Zawadi akaonyesha poa na kuondoka eneo lile waliopo na Matwiga kuelekea alipokaa Zainab, Matwiga nae akaondoka pale na kusogea kule alipomuelekeza Zawadi, ambae alifanikiwa kumchomoa Zainab kwa njia anazojua mwenyewe.



    Aliondoka nae akiwa amemshika mkono pasina kumwambia ni wapi wanaelekea, Zainab nae hata kabla hajajua ni wapi wanaelekea na kabla akili ya kuhoji haijaja, tayari akawa amejikuta kasimama mbele ya Matwiga.



    Salamu ikahusika kwa mara ya pili, kisha mambo mengine ndio yakafuatia. Zainab alishangaa sana kwa muda mchache mno Matwiga alimpa historia yake kifupi kama kwamba ni mtu wanae juana vema.



    Alimueleza kuhusu maisha binafsi, yakiwepo majina yake yote mawili na anapoishi, pia akamuelezea Sungura. Zainab akatabasamu baada ya kujua Matwiga anatambua uhusiano baina yake na Sungura.



    "Nafurahi sana kusikia unatambua kuwa nipo kwenye mahusiano."



    "Lakini haizuii kwa mimi kuwa ni mpenzi wako Zainab."



    "Huenda ukawa upo sahihi kwa upande wako, maana kuna watu kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja kwao wala sio tatizo."

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Zainab, tatizo lipo wapi hapo wangu? Nipe nafasi, napenda nikutoe kwenye aina hii ya maisha unayoishi."



    "Unipeleke kwenye aina gani ya maisha?" Aliuliza Zainab kwa kebehi.



    "Maisha halisi ambayo wewe unapaswa kuishi, maisha ya kufanya kazi ama kwenda shule, vile utakavyo wewe mie nitatekeleza," alibembeleza Matwiga.



    "Pole sana! Waliokwambia ninaishi maisha ya kuigiza, hao ndio waliokudanganya kaka, wazazi wangu wana uwezo wa kunifanyia hayo usemayo, na kwa taarifa yako, mpenzi wangu amenitafutia chuo na wiki ijayo ninaanza, kifupi sihitaji chochote kutoka kwako." Alionekana Zainab kama amekwazika kutokana nakauli ya Matwiga, ambae alitambua hilo na kujirudi



    "Zainab naomba unisamehe kama nimekukwaza."



    "Na umenikwaza kweli kweli, kwanini unajikweza na hali hunijui kiundani?"



    "Naomba msamaha, nimekukosea Zainab," aliomboleza Matwiga mikono ikiwa kifuani.



    "Poa, tumeambiwa tusamehe saba mara sabini, mimi nimekusamehe maana hujui ulisemalo, kama vipi tutaonana siku nyingine," huku akiondoka, Matwiga akamuita akiwa amemzuia mkono.



    "Samahani Zainab, ninaomba namba yako ya simu."



    "Sina simu, tafadhali niache niende," kisha akaondoka akiwa ameonesha kabisa kukasirika.



    Matwiga nae akapiga ngumi mkononi kujilaumu kwa kuongea pumba na kujikuta kapoteza nafasi yake alioipata ambayo alijua kabisa haitojirudia, hakuwa na budi ila kurejea kiwanjani kushuhudia timu yake ikipoteza mechi.



    Mechi ilikwisha, Zainab akaingia hadi kiwanjani akiwa na washabiki wengine ambao waliingia kuwapongeza wachezaji wao ambao walijitahidi na kuubakisha ushindi nyumbani. Zainab alikimbia na kumkumbatia Sungura ambae baadae watu walimbeba juu juu.



    Matwiga alikuwa akiwatazama tu, alitamani yeye ndio angekuwa ni Sungura, lakini haikuwezekana. Baadhi ya wachezaji wenzie wakamuona kuwa hayupo sawa, walipomuuliza akawajibu kwa sababu wamefungwa.



    Ukweli ulikuwa ni hivyo kuwa wamefungwa na hawakuwa na cha kufanya tena, lakini ndani ya moyo wake hilo sio lililomfanya awe mpole na kunyong'onyea kiasi kile, lakini hakutaka wajue.



    Kipigo cha pale uwanjani hakikumuumiza hata kidogo, alijua wanaweza tu kuomba mechi nyingine na kurekebisha matokeo, kilicho muumiza ni kupoteza nafasi ile adhimu aliyoipata na kuitumia vibaya, maana alijua hii haitojirudia tena, maana leo amelazimisha tu itokee.



    Wenzie baada ya kubadili mavazi kutoka yale rasmi ya kimichezo na kuvaa mavazi mengine, wakawa sasa wapo tayari kuondoka na kurejea kwao, hivyo wakamuambia Matwiga kwamba muda wa kuondoka umewadia.



    Akawaambia wao waende tu, yeye atakuja siku ifuatayo. Walimbembeleza sana akagoma. Muda wote alikuwa akiwatazama wapenzi wale wawili, Sungura na Zainab ambao sasa walikuwa wamekaa chini Zainab akimfungua mpenzi wake raba zake za michezo.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sungura na Zainab walikaa kwa muda mrefu zaidi, muda wote Matwiga alikuwa akiwatazama tu hadi walipoanza kuondoka, ndio nae akamuita mmoja kati ya wale jamaa ambao pale awali walimpa maelezo juu ya Zainab.



    Jamaa huyo ambae tayari alikuwa amejitambulisha kwa jina la Ngonyani, safari hii alimuulizia kuhusu nyumba ya wageni yenye hadhi ya kati ambayo anaweza yeye kulala kwa usiku ule,



    “Lakini pia iwe karibu na nyumbani kwa kina Zainab, si uliniambia unapajua kwao?” Jamaa akakiri kuwa anapajua ila akamueleza



    “Jirani na kina Zainab hakuna guest, itakuwaje?”



    “Basi hata guest ambayo haipo mbali sana na kwao,” hivyo akamuelekeza, lakini Matwiga akamuomba ampeleke, basi jamaa akamuahidi kuwa atampeleka wala asijali.



    Kwa kuwa yeye alikuwa na gari yake binafsi, akaingia ndani ya gari yake na kuwaaga wenzie ambao walikuwa tayari kwa safari, wakamlaumu sana kwa kumwambia idadi yao ni wengi sana na wataendaje ikiwa yeye anabaki huku na gari lake.



    Akaona isiwe tabu, akamuita mmoja kati ya viongozi wake na kumkabidhi gari yake akimuomba kuifikisha nyumbani kwao usiku uleule wakiwasili Iringa. akateremka na kuwatakia safari njema na kuwatazama wakiondoka.



    Sasa ndio akaanza kuondoka na jamaa yule ambae alijitambulisha kama Ngonyani kuelekea hotelini ambapo alitegemea kulala kwa usiku ule. Walielekea Guest wakiwa wapo kimyakimya.



    Waliwasili na kisha Matwiga akamwambia Ngonyani amsubiri kidogo ili amtembeze pale mjini. Matwiga akachukua chumba na wakati akiwa anaandikisha majina akamuuliza Mhudumu wa pale kama anamjua Zainab.



    Alikuwa ni kama mtu alie changanyikiwa vile, mhudumu akamwambia hamjui Zainab. Kumbe wakati Sungura na Zainab walipokuwa wamekaa chini, Matwiga alitoa simu na kumpiga Zainab.



    Akazama mfukoni na kutoa simu na kumuonyesha picha ya Zainab, mhudumu alipomtazama tu, akamtambua lakini akasema hajui ni wapi anapoishi, lakini mara nyigi sana hupita pale nje ya guest, inaonyesha hakai mbali na pale.



    Ngonyani alipoona wanaonyeshana kitu fulani kwenye simu na huku wakiongea, akasogea ili nae ajue. Matwiga akamuuliza tena kama anapafahamu kwa kina Zainab, Ngonyani akamwambia anapafahamu vema.



    Kwa mara nyingine Ngonyani akamuahidi kumpeleka hadi nyumbani kwa kina Zainab huko Bombambili, Matwiga akaingia chumbani kwake na kujiswafi kisha akabadili nguo zile alizokuja kavaa na kuvaa zingine.





    Safari ya kuelekea nyumbani kwa kina Zainab ikaanza, moja kwa moja hadi nyumba ya jirani, kukawa na tofauti ya nyumba mbili tu kati yao, suala likawa ni vipi watampata ikiwa atakuwepo ndani, maana pale nje hakuonekana.



    Akili zao sasa zikaganda, lakini Matwiga akamwambia wasogee hadi mlangoni kabisa watajua wakifika hukohuko ni nini cha kufanya wakiwa hata ndani. Lakini wakiwa nyumba ya pili wakaona duka, sasa ndio akili ya Matwiga ikapata mwanga.



    Wakasimama dukani na kununua daftari na kalamu, kisha akamwambia Ngonyani aandike majina mengi ya kike likiwepo la Zainab.



    Japo hakuelewa ni kipi alichokuwa akimaanisha Matwiga, akafanya kama alivyotaka.



    Majina yalikuwa kama 10 hivi yaliyo muijia kichwani mwake, Matwiga akasema yametosha, akachukua daftari na kumwambia Ngonyani waende sasa, wapo kamili na wakifika ndani, amuache yeye ndio aongee.



    Iwapo atakosea, hapo ndio amrekebishe na pale atakapokwama napo amuongoze, wakapeana mikono ishara ya kukubaliana. Wakagonga mlango. Mama Zainab akatoka na kuwafungulia.



    Aliwakaribisha ndani, nao bila kusita wakaingia na kukaribishwa sofani, wakaketi. Kisha wakasalimiana na mama na baada ya salamu, ikaanza hadithi ya uongo iliyo tungwa na kutungika.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Samahani bi mkubwa, mimi ninaitwa Komba, na huyo mwenzangu jina lake ni Ngonyani, sisi ni maafisa wa bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Makao Makuu Dar Es Salaam, Kama hatujakosea namba ya nyumba, hapa itakua ni kwa Mzee Mapunda?" Aliuliza huku akijidai kufunua funua daftari kama vile anaangalia jina, mama akajaa mwenyewe.



    "Ndio wanangu na mimi ni mkewe, vipi kuna tatizo?" Alihoji akiwa hajiamini kabisa.



    "Hapana mama, tuna maongezi nanyi kidogo, sijui Mzee yupo?" kwanza Matwiga alidanganya jina kwa sababu ambazo mimi na wewe hatuzijui. Mama nae akajibu kuwa Mzee katoka lakini wanaweza tu kuongea kile kilicho wapeleka.



    "Mama sisi tumefika hapa leo tukitokea Mbinga na tunataraji kuondoka kesho asubuhi, tumekua na kazi ndefu ndio maana hata hapa kwako tumeingia usiku." Alianza kutengeneza mazingira ya kuaminika kwanza.



    "Naam hata nami nimeshangaa, mbona usiku tena," mama akamuunga mkono.



    "Ndio hivyo mama yangu,kifupi ni kuwa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, imefanya utafiti na kugundua hapa Songea mabinti wengi sana hawapendi kuendelea na masomo ya juu, unahisi ni kwa nini mama?" lilikuwa ni swali gumu mno kwa mama Zainab



    "Mh! Kwa kweli wanangu hata sifahamu ni kwa nini, ila ninafikiri ni wenyewe tu hawapendi."



    "Mama upo sahihi kabisa," akadakia Ngonyani huku akitikisa kichwa.



    "Sawa mama, sasa leo sisi tupo hapa kwa ajili ya mwanao Zainab Mapunda."



    "Enhe, kafanyeje tena?" Aliuliza huku akinyanyuka na kukaa vizuri kwenye sofa.



    "Hapana, usiogope. Hajafanya lolote baya, lakini nae ni mmoja wao kati ya wale wliokuwa na nafasi ya kuendelea na masomo lakini hadi leo hajaonekana kwenye shule ama chuo chochote Tanzania," akameza mate na kisha akaendelea



    "Watafiti wa elimu hapa Wilayani wametuletea jina lake pamoja na wenzie kadhaa ambao tayari tumewahoji, hawajaendelea na masomo, unafikiri ni kwa nini?" Swali lilimtoa jasho mama Zainab na kutamani hata angekuwepo Zainab ama mumewe.



    "Kwa kweli mimi binafsi jibu sina, labda angekuwepo yeye mwenyewe ndio angeweza kutoa jibu la uhakika, tofauti na mimi mzee hapa nisiejua lolote."



    "Sawa, ina maana hayupo kwa sasa?" Aliuliza Matwiga kwa sauti ya kukata tamaa.



    "Ndio ametoka, alielekea kwa rafiki yake."



    "Ok! Je unaweza kumpigia simu na kumuita mara moj aikiwa huko alipo si mbali? Ama ukatupa namba yake ya simu tukamuita akaja mara moja tumalize hili?" Aliomba Matwiga.



    "Hapana baba, simu yake hiyo hapo aliiacha," mama aliwaonyesha simu iliyokuwa juu ya TV, wakatazamana na kuishiwa pozi.



    Mwisho wakaamua wao kuacha namba ya simu na kumwambia mama kwamba amsisitize Zainab kuwasiliana nao kesho asubuhi kabla ya saa mbili, maana baada ya hapo wanatarajia kuondoka kuelekea ilaya ya ..................



    Mama akaitikia sawa, Matwiga akaandika namba yake kwenye kikaratasi na kumpa mama Zainab ambae hata kabla hawajaondoka akaiweka kwenye sidiria yake nao wakiona. Safari ya kurejea hotelini ikaanza huku Ngonyani akiwa amenyoosha mikono.



    Ngonyani alimwambia Matwiga kuwa hana swali kwa mbinu ile aliyoitumia pale. Matwiga akatabasamu na kumwambia Ngonyani kwamba ilikuwa ni lazima akili ya ziada itumike na kwa kuwa ilishindikana plan A, basi ile plan B ni lazima itafanya kazi.



    Alimuhakikishia kuwa ni lazima Zainab apige simu usiku uleule. Wakiwa wanatembea taratibu, njiani wakakutana wakiwa na umbali wa zaidi ya mita 10 kati yao. Mtu wa kwanza kuwaona alikuwa ni Matwiga.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akamshitua Ngonyani na kumtaka atazame upande wa pili. Ngonyani akawaona na kutaka kuelekea kule walipo, Matwiga akamzuia na kumuuliza anataka kufanya nini? Ngonyani akasema anawafuata ili kumtaka Zai kuongea nae faragha dakika sumni tu, Matwiga akamwambia atulie na kuwatazama tu.



    Sungura na Zainab walikuwa wanaongozana wakiwa wameshikana mikono, walionesha kuwepo ndani ya penzi zito, wakabaki wakiwatazama hadi walipo potea mbele ya macho yao, ndio nao akaendelea na safari yao.



    Kichwani mwake Matwiga alikuwa hajielewi kabisa ni nini afanye, Ngonyani akamshauri ni vema warejee tu hotelini bila kupita popote. Walikuwa wamepanga wazunguke mitaani, ila ile hali ikaonesha ni bora Matwiga aende akatulie tu hotelini.



    Uamuzi ukawa ni huo, akifika ale na kupumzika akisubiri simu kutoka kwa Zainab kama atapiga. Matwiga akamtazama Ngonyani na kumuuliza je asipopiga? Ngonyani akaona tayri jamaa kaisha anza kukata tamaa ya kumpata Zainab.



    "Matwiga naona sasa umesahau kwamba ni wewe ndio ilinihakikishia kuwa ni lazima Zainab apige, inakuwaje sasa unapoteza matumaini ndugu yangu?"



    "Kaka vitendo vinaongea kuliko maneno, umewaona wale watu walivyo?"



    "Naona wanaonesha mapenzi mazito mno."



    "Na hapo ndipo shaka yangu inapoingia," aliongea kwa sauti ya kupoteza matumaini



    "Usikate tamaa, pambana kidume, kwanini ushindwe wakati umeanza vizuri?" Ngonyani alimpa moyo huku yeye mwenyewe akiwa hajiamini.



    Zainab na Sungura walifika nyumbani kwa kina Zainab na kuagana wakiwa nje kwa mabusu motomoto kisha Zainab akaingia ndani na Sungura taratibu akaanza kurejea kwao huku akipiga mluzi akiwa na furaha tele.





    Kila sehemu aliyopita alikuwa akipata pongezi kutokana na matokeo waliyopata siku ile ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa nae. Alifurahi sana na kujiona ni shujaa, akaazimia kuzidisha juhudi zaidi.



    Nao Ngonyani na Matwiga waliwasili guest, Ngonyani hakuingia ndani, wakaagana Matwiga akiingia ndani na Ngonyani akielekea kwake huku kichwani ikijirejea taswira ya penzi la Zainab na Sungura… akabaki anatikisa kichwa tu kumsikitikia Matwiga.



    Kitendo tu cha kuingia ndani, Zainab kakutana na mashambulizi kutoka kwa mama yake akimlaumu kwa kuchelewa kurudi toka huko alipokuwa.



    "Siku zingine mtapishana na bahati kisha mlazimishe kwenda kwa waganga, mkiamini mmerogwa kumbe uchawi mwingine ni uzembe tu," Zainab akashangaa.



    "Mama hayo yote yanatoka wapi?"



    "Hebu shika hii karatasi," akampa karatasi aliyoitua kifuani kwake na kumpa maelekezo kuwa namba ile ni ya watu kutoka bodi ya mikopo ya Elimu ya juu, wanataka kuongea nae.



    Alimueleza kuwa wamefika pale na kumkosa, sasa ni zamu yake kuwapigia. Zainab hakuamini kama watu wa bodi wamekuja na kumkosa, haraka haraka nae akawasha simu na kupiga namba ile.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Simu iliita mara moja tu na kupokelewa, walisalimiana na kisha Zainab akajitambulisha kwamba yeye ni Zainab. Matwiga akajitambulisha nae kwa jina la Komba, kisha akamlaumu kidogo kwa kutokuwepo nyumbani wakati wao walipokuwa hapo kwao.



    Zainab alikiri ni kweli na kumuomba Msamaha kwa kumuambia ndio maana amepiga muda ule ili waongee. Simu ikakatika wakati hata maongezi yao bado hayaja pamba moto, kumbe ni Matwiga mwenyewe ndie aliekata maksudi.



    Sasa akapiga yeye na kumueleza sababu ya kwenda pale huku akiwa ameuficha ukweli bado, akamuuliza kama bado ana mpango wa kuendelea na masomo. Zainab akamwambia ukweli, kuwa wiki inayo fuata anatarajia kwenda Iringa kuendelea na masomo.



    Alimueleza kiurefu tu kuwa na mpango wa kwenda Iringa kuchukua masomo ya PR (Public Relation) ambayo anatarajia kuchukua kwa miaka mitatu. Basi Matwiga akampongeza na kumtaka wawasiliane siku ifuatayo asubuhi, ili wapange sehemu waonane kwa maongezi zaidi.



    Haikuwa ngumu kwa Zainab ambae sasa alikuwa na nia ya dhati ya kutaka kusoma, lakini akaomba waonane mchana, Matwiga akamwambia, asubuhi ya kesho, wao wanapaswa kuwa wameondoka kwenda wilaya nyingine kuendelea na kazi yao.



    Kifupi akamuelewa na kumaliza maongezi yao ambayo hayakuonesha dalili yoyote ya mapenzi kati yao, wala Matwiga hakujitambulisha kiukweli jina lake. Moyo wa Matwiga sasa ulikuwa na furaha akiamini siku ifuatayo, mambo yatakaa vizuri wakikutana.



    Faraja ilikuwa nyingi moyoni, mwamzo ulionekana ni mwema mno, hisia zake zilimtuma kuwa hadi pale kuongea nae bila kuonesha chochote, tayari ilikuwa ni hatua kubwa mno katika mbio zake za kumtia mikononi.



    Mwisho wasimu ile, ikawa ni mwanzo wa simu zingine, wa kwanza kupiga alikuwa ni Matwiga alieamua kumpigia Ngonyani na kumueleza kila alichoongea na Zamza na kumueleza mipango ya kukutana siku ifuatayo asubuhi.



    Ngonyani akamtakia mafanikio na kumsihi asifanye makosa hiyo siku ikifika na kumsisitiza tukuitumia vizuri ile nafasi. Matwiga akamwambia kiukweli hatomuangusha na majibu atayapata siku hiyohiyo, Ngonyani akamuaga kwa kumtakia usiku mwema.



    Wakati wao huko wakiongea yao, nae Zainab alikuwa akiongea na na Sungura na kumueleza juu ya suala la kutembelewa na watu wa bodi ya mikopo ya Elimu ya juu ambao kwa bahati mbaya hawakuonana uso kwa uso.



    Sungura akamuuliza watu wa bodi ya mikopo walikwenda kumtembelea wapi? Zainab kwa kujiamini kabsa akamjibu kuwa walienda nyumbani kwao wakati yeye akiwa nae huko kwao, Sungura alishtuka na kushangaa, akamuuliza



    "We Zainab umechanganyikiwa?"



    "He! Kwanini unaniuliza hivyo?"



    "Tangu lini bodi ya mikopo ikapita mitaani kutafuta wanafunzi na kuwakopesha?"



    "Jamani si ndio wamepita kwetu leo? Huwezi kujua huenda ndio wameanza sasa."



    "Nyie angalieni nyinyi msitapeliwe, jiulize ni kwanini iwe ni wasichana watupu?"



    "Wasichana ndio wengi wao hatuendelei na masomo na ndio maana wameanza nasisi, we unafikiri wale ni matapeli?"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mi ninaamini hivyo, ingekuwa ni hicho usemacho, lazima vyombo vya habari vingetangaza."



    "Ah! Baby mie sijui bwana, hebu tuachane nao hao..." Zainab akakubali yaishe, Sungura sasa



    "Hapana mi ninataka unitumie namba za huyo ulie ongea nae," aliamuru Sungura.



    "Tukimaliza kuongea nitakutumia mpenzi wangu, wala usihofu." Zainab alimtoa shaka.



    Mazungumzo yao ya kimapenzi yakachukua nafasi na baada ya kumaliza, akamtumia namba na kuagana kwa njia ya ujumbe mfupi na kisha wakalala.







    ITAENDELEA
    Pseudepigraphas

0 comments:

Post a Comment

Blog