Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KUTI KAVU - 5

 











    Simulizi : Kuti Kavu

    Sehemu Ya Tano (5)





    Utitiri wa majukumu ulinifanya nitingwe na shughuli kwa muda mwingi. Licha ya kujitahidi kuyapunguza kwa bidii kubwa, majukumu hayo hayakuisha. Wingi huo wa shughuli ulinifanya nikamsahau kabisa Doi. Siku ile iliisha bila kumbukumbu yoyote kuhusu Doi akilini mwangu!

    Siku iliyofuata nayo iliisha, na siku nyingine tena hatimaye wiki ya kwanza, ya pili na ya tatu. Mwezi ukaisha bila kumkumbuka Doi kwa namna yoyote ile.

    Kwa kuwa likizo yangu ilikuwa ikielekea ukingoni, nilianza kufanya maandalizi kwa ajili safari yangu ya kurejea chuoni Iringa ambako nilikuwa nikisoma.

    Siku moja jioni, yapata majira kama ya saa 12 hivi, nilikuwa nimejipumzisha chumbani kwangu huku nikichezea simu yangu kwenye orodha ya majina. Nilianza na majina yanayoanza na herufi ‘A’, yalipoisha niliingia kwenye herufi ‘B’, ‘C’ na baadaye ‘D’ ambapo nilipitia jina moja baada ya jingine, mpaka nilipofika kwenye jina lililonikumbusha siku kadhaa nyuma. Nilikumbuka siku ile nilipokutana na Doi kwa mara ya kwanza kwenye daladala.

    Sura ya Doi ilinirejea akilini. Uzuri wa sura yake pamoja na sauti vilinifanya nipatwe na pumbao pale kitandani nilipokuwa. Shauku ya kutaka kuisikia tena sauti ya Doi ikanijia, hamu ya kutaka kumtia tena machoni pangu ikanivaa, nikaamua kumpigia simu ili kumshawishi tuonane kabla likizo yangu haijasha na kurejea chuoni, Iringa.

    uWakati najiandaa kubonyeza kitufe cha kijani, ambacho ni kitufe cha kupigia simu, mara mtetemo ukasikika kwenye simu yangu ukifuatiwa na mlio ulioashiria kuwa kuna ujumbe mfupi wa maandishi umeingia. Niliupuuza ujumbe ule kwa lengo la kutimiza kwanza jambo nililolikusudia, kumpigia Doi simu.

    Nilibonyeza kitufe cha kijani na mara simu ya Doi ikaanza kuita.

    Mapigo ya moyo wangu yalianza kwenda mbio sambamba na msululu wa maswali ambayo nilihisi ningekumbana nayo baada ya kuwa amepokea simu. Kwanza; niliomba namba yake ya nini, ikiwa sikuwa na umuhimu nayo? Pili; nina lipi la kumueleza, ikiwa ni mwezi sasa tangu niichukue namba yake. Nimekumbuka nini?

    Wakati bado nasumbuliwa na msululu huo wa maswali, mara sauti ikasikika, “Hallow….” hakika ilikuwa ni sauti yake, “Hallow Doi, mambo?” nilijibu na kumjulia hali kwa kumsalimia.

    “Safi tu, za siku?”

    “Salama wangu, wajionaje na hali?”

    “Kwema tu, ina maana nisingekutumia huo ujumbe ndiyo ingekuwa jiii…?” Doi aliuliza kwa sauti iliyojaa mzaha, na hapo ndiyo nikajua kuwa, kumbe ule ujumbe mfupi ulioingia ameutuma yeye! Mara ghafla nikapatwa na hangaiko la akili. Shauku ya kutaka kujua ameandika nini kwenye ujumbe alioutuma ikauvaa moyo wangu. Nikajaribu kubashiri kile alichokiandika bila mafanikio na wakati huohuo sauti yake laini iliendelea kunishitaki. Nikajitetea.

    “Hapana Doi…. Siyo hivyo….” Kabla sijamaliza kauli yangu aliuliza, “kumbe je?”

    Ilinibidi nianze kujitetea, “Nilitingwa na majukumu wangu, na siku zote nimekuwa nikiutafuta wasaa wa kuzungumza na wewe bila mafanikio. Najua huwezi kuniamini nikisema kuwa hata huo ujumbe ulioutuma sijausoma kwa sababu umeingia nikiwa nimekwisha ruhusu simu ije kwako,”

    “Unasema kweli Domi?” Doi aliuliza.

    “Kwa nini nikudanganye?” nikalijibu swali lake kwa kumuuliza swali jingine.

    “Nhuu.. Basi makubwa hayo! Ina maana unataka kuniambia kuwa umenikumbuka wakati ambao mimi nimekukumbuka?” aliuliza.

    Kwa haraka sikujua nimjibu nini. Nilijitahidi niendelee kubaki kwenye mhimili wa staha ili niongee naye kwa uwekevu, lakini haikuwezekana. Nilijikuta nimetamka, “Haswaa…”

    “Kwa nini?” aliuliza tena.

    “Nahisi kuna kitu kati yetu Doi…. Kuna kitu”

    Nilitarajia aseme neno baada ya mimi kusema hayo lakini haikuwa, Doi alikuwa kimya!

    Sikutaka kuruhusu ukimya ule ushike hatamu kati yetu. Hivyo baada ya yeye kuwa kimya niliamua kumuuliza, “Samahani Doi, tunaweza kuonana kabla wiki hii haijaisha?”

    “Tunaweza. Lakini iwe weekend,”

    “Haina shida, nadhani Jumamosi itakuwa ni siku nzuri”

    Tulikubaliana kuwa tuonane siku ya Jumamosi, tukapanga mahali na muda. Hiyo ikawa ni siku ya pili.





    ****

    Siku ya Jumamosi ilifika. Niliamua kuelekea maeneo ya fukwe za Coco saa moja kabla ya muda wa miadi ambao tulikuwa tumekubaliana na Doi haujafika. Lengo la kuwahi eneo lile lilikua ni kwa ajili ya kuandaa sehemu nzuri katika ufukwe ule, ili tuwe na faragha katika mazungumzo yetu. Sababu nyingine ilikuwa ni kuepuka uswahili wa kutokulinda muda, hasa zaidi ukizingatia ile ilikuwa ni siku ya kwanza kuonana na Doi baada ya kuwa tumepanga miadi.

    Niliwasili Coco majira ya saa 6:00 mchana kwa usafiri wa Bhajaji, nilishuka na kumlipa dereva ujira wake. Niliangaza kushoto na kulia katika ufukwe ule, watu walikuwa wamesheheni kila upande… naweza kusema tangu nianze kuhudhuria kwenye ufukwe ule, siku hiyo idadi ya watu ilikuwa ni kubwa kuliko siku nyingine zote nilizowahi kuhudhuria eneo lile.

    Taratibu nilianza kupiga hatua kuelekea upande wa kulia, upande ambao niliamini ninaweza kupata mahali ambapo pangetupa faragha.

    Nikiwa katika hatua ya tatu tangu nilipokata shauri kuelekea upande wa kulia, alikuja mtu nyuma yangu na kuniziba macho kwa viganja vya mikono yake. Sikuweza kujua ni nani kwa sababu; moja, sikutarajia kukutana na mtu ninayefahamiana naye mahali pale kwa sababu, marafiki zangu karibia wote si wapenzi wa maeneo kama haya. Mbili, ni kweli nilikuwa nimeahidiana na Doi kuwa tuonane naye mahali pale, lakini akili yangu haikunituma kuamini kuwa huyo angekuwa ni Doi kwa sababu muda wa miadi yetu ambao ulikuwa saa moja mbele ulikuwa haujafika. Ni nani sasa awezaye kufanya mzaha wa namna hii?

    Shauku ya kutaka kumjua ikanizidi moyoni! Niliunyoosha mkono wangu wa kulia kuelekea nyuma, kule alikosimama aliyeniziba macho kwa viganja vyake. Wakati naunyoosha mkono ule wa kulia yeye alihama na kuelekea kushoto, wakati naunyoosha wa kushoto alihama tena na kurudi upande wa kulia, nikawa sina jinsi.

    Ulaini wa mikono iliyoyaziba macho yangu sanjari na uzuri wa manukato yaliyotuama kwenye pua zangu, vilinifanya kubashiri ni nani aliyeniziba macho baada ya kuwa njia niliyodhani ingenisaidia kumtambua kushindikana. Nilipiga upatu wangu kwa kulitaja jina la Doi huku akili yangu ikijiandaa kukabiliana na aibu ambayo ingenipata endapo jina nililolitaja si la yule niliyedhani kuwa ndiye.

    Mara baada ya kulitaja jina Doi, ile mikono iliyaacha macho yangu huru. Kile kitendo cha viganja vilivyoyaziba macho yangu kuyaacha huru kilifuatiwa na sauti ya kicheko ambacho kilinifanya nitambue fika kuwa aliyeniziba macho yangu alikuwa ni Doi.

    Niligeuka kumtizama, naam, alikuwa ni yeye!

    “Doi!” nilijikuta nimelitaja tena jina hili baada ya kuwa nimemuona Doi akiwa amesimama mbele yangu. Alikuwa amejifunga kikoi kilichouufunika mwili wake tangu kiunoni mpaka sehemu ya juu kidogo ya magoti na juu alikuwa amevaa kijiblauzi cha kubana kilichoyaziba matiti yake tu, na kuiacha sehemu kubwa ya tumbo lake ikiwa nje!
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilijisogeza kidogo kuelekea mahali alipokuwa, kasha nikaitanua mikono yangu naye akajibu mapigo kwa kujaa ndani ya mikono ile, tukawa tumekumbatiana!

    Tukiwa katika hali ile ya kumbato, nilihisi mabadiriko yaliyoufanya mwili wangu kusisimka kwa namna ya pekee, namna ambayo siwezi kuieleza kwa misamiati ya lugha za binadamu, ulikuwa ni msisimko wa ajabu.

    Kwa upande wa Doi, naye pumzi zake zilibadiri mwelekeo na hapo ndipo kikatokea kile ambacho sidhani kama kuna hata mmoja kati yetu alidhani kuwa kitatokea. Kwa pamoja sauti zilisikika zikitamka neno moja, “Nakupenda!”

    Sikutaka kuyaamini masikio yangu kwa kile yalichokisikia, lakini ilinibidi kuamini baada ya kuisikia tene sauti ya Doi ikilirudia neno lile kwa sauti iliyosheheni mahaba, sauti yenye kusisitiza kile kilichotamkwa. Sauti ile laini ilisema, “Nakupenda Domi”

    Sikuwa na la kusema zaidi ya kujibu, “Nakupenda pia Doi… nakupenda sana,”

    Sikujua hasa ni lini na ni wapi ndimi zetu zilipata kufahamiana. Kwani mpaka wakati huo vinywa vyetu vilikuwa vimeumana huku ndimi zetu zikizungumza kwa lugha yao. Ilanza kama mzaha katika siku ile ya tatu.

    ****

    Ukurasa wa kwanza wa mapenzi baina yetu ulifunguliwa katika siku ile ya tatu katika fukwe za Coco beach. Wasaa uliofuata ulikuwa ni wa kufahamiana juu ya taarifa zetu binafsi, ambapo aliniambia kuwa; yeye ni mtoto wa kwanza kwenye familia yao yenye watoto wawili, na mdogo wake anayemfuata ni wa jinsia ya kiume.

    Elimu yake ya kidato cha nne haikumruhusu kuendelea zaidi na masomo baada ya kuwa amefeli vibaya kwenye mitihani yake ya taifa. Hivyo hakuwa na weledi wowote ambao ungemsaidia kupata ajira. Kwa sababu hiyo alilazimika kuwa nyumbani akisaidiana na wazazi wake shughuli za hapa na.

    Likizo yangu ilipoisha nilielekea chuoni kumalizia ngwe ya mwisho ya masomo yangu ya shahada ya kwanza ya sheria. Na wakati wote ambao niliokuwa chuoni, mawasiliano baina yangu na Doi yaliendelea kupitia simu.

    Maneno yake matamu yalinifanya niamini kuwa kuna pendo pevu baina yetu. Kwa sababu Doi alionesha wazi kuwa anayo nia ya dhati ya kuishi nami kama mwenzi wake baada ya kuniahidi kuwa yuko tayari kuishi nami katika hali yoyote ile ya maisha; yawe ya shida ama ya raha! Ni nani wa kuipinga ahadi adhimu kama hiyo?

    Wingu zito la mapenzi likatanda juu yetu huku tukiendelea kuunganishwa kwa mawasiliano ya simu mpaka nilipomaliza masomo yangu na kurudi tena Dar es salaam.

    Niliporudi Dar es salaam, Doi alihamia rasmi nyumbani kwangu licha ya pingamizi kutoka kwa nduguze.

    Hali ya uchumi kwa upande wangu haikuwa njema, lakini hiyo haikutosha kuwa kikwazo cha Doi kunivumilia. Siku zote alinitia moyo… jambo lililonifanya nihisi kuwa na mimi ni miongoni mwa watu wapendwao chini ya jua.

    Hapo niliielewa aina ya upendo wa Doi kwangu, japo sikuwa naelewa nini maana halisi ya mapenzi! Ikiwa tajiri na masikini wote wana nafasi ya kupendwa, nini hasa sababu ya upendo?

    Nililewa kwa penzi Doi, nililewa hasa! Naweza kusema hiyo ni miongoni mwa sababu zilizonifanya niongeze bidii ya kutafuta kazi mara baada ya kuhitimu mafunzo yangu ya uwakili.

    Nilitafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio, hapo likanijia wazo la kutafuta ufadhili wa kuchapisha hadithi zangu katika makampuni mbalimbali yaliyojishughulisha na uchapishaji. Huko pia niliziandika barua nyingi bila kupata majibu huku ugumu wa maisha ukizidi kushika hatamu.

    Katika kuyafanya yote haya, nilikuwa sambamba na Doi ambaye alinitia moyo na kunifariji kuwa nisikate tamaa kwani mafanikio yapo kwa ajili ya wale wayatafutao.

    Maisha yalikuwa magumu, na hata ikafika mahali nikayaona machungu. Mara nyingi sana kula yetu ilikuwa ni ya shida. Usishangae nikikwambia kuwa kuna wakati siku iliisha bila kutia chochote mdomoni isipokuwa maji. Kama ujuavyo jiji hili huwezi kupata chochote kama huna pesa, cha bure ni hewa tu, labda na salamu mara mojamoja.

    Maisha yaliendelea kwa matumaini kuwa; mafanikio yamo mbioni kuja. Niliamini hivyo kwa sababu alikuwepo wa kunifariji, yule ambaye nilimuona kama sehemu ya mwili wangu… kumbe lah! Doi alikuwa na hila.… Doi alikuwa na hilaa…” alisema Domi huku machozi yakimtoka.

    Ilibidi Makeke achukue jukumu jipya, jukumu la kubembeleza Domi ambaye alikuwa hajiwezi kwa kilio.

    “Nyamaza Dominic… wewe ni mwanaume jikaze. Ndivyo maisha yalivyo. Maisha yako katika uwili usiokwepeka. Kuna wakati wa furaha na wakati wa huzuni… jikaze Domi,” alisema Makeke.

    Wakati Makeke na Domi wakiendelea na mazungumzo katika ofisi ile ndogo iliyopo nyumbani kwa Makeke, mke wa Makeke alibisha hodi akakaribishwa.

    Alipoufungua mlango kuingia chumbani mule, sauti ya muziki kutoka sebuleni ilipenya na kuingia mule ofisini amabako kulikuwa kimya. Muziki ule ulisikika barabara masikioni mwa Domi na kumpa wakati mgumu zaidi kwa sababu mashairi ya wimbo uliosikika yaliendana kabisa na kile kilichomtekea. Ulikuwa ni wimbo wa Daz Nundaz, wimbo wa barua ambao ulisikika hivi:

    “…..katika mahaba tulishazama dimbwini,

    Lakini barua niliyopokea nashindwa hata kuamini,

    Ua la moyo wangu halipo tena na mimi,

    Barua hii shika mwenye usome,

    Barua hii….”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yalikuwa ni maneno yaliyouchoma moyo wake kama mkuki.

    Mke wa Makeke aliwakaribisha chakula kisha akaondoka.



    *****

    SIKU ya Jumatatu, majira ya saa tatu asubuhi, Doi alikuwa amejikunyata katika moja ya vyumba vya mahabusu vilivyopo katika gereza la Keko. Alikuwa amejitenga peke yake akijaribu kutafakari hatma yake, kwani tangu afikishwe hapo gerezani hakuna hata mmoja kati ya watu aliowajua na aliyekuja kumjulia hali.

    Akiwa katika lindi la mawazo, Doi alisikia sauti ikiliita jina lake, alinyanyua macho kuangalia kule sauti ilikotokea akamuona askari wa kike akiwa amesimama mlangoni huku akichezesha funguo zilizokuwa mkononi mwake.

    Askari Yule aliyekuwa nadhifu ndani ya sare za jeshi la magereza, shati jeupe na sketi ya rangi ya ugoro alimuita, “Doi Vioja, kuna wageni wako”

    Doi aliisikia vyema sauti ya askari yule, alitii kwa kusimamana kuelekea mlangoni alipokuwa amesimama yule askari huku akili yake ikiwa imetekwa na utitiri wa maswali.

    Alijiuliza juu ya ugeni alioitiwa. Alijiuliza ni wageni gani hao ambao wamekuja kumjulia hali. “Watakuwa ni baba na mama” Doi aliwaza huku akichapua hatua kuelekea mahali alipokuwa amesimama askari ambaye alimpokea kwa kumfunga pingu, kisha akamtanguliza mbele kuelekea kule walipo wageni wake.

    ****

    Koplo Mwalo Mlekwa, alikuwa ni binti wa umri wa miaka 28. Mrefu na mwenye umbo la wastani, mzuri wa sura na hodari katika kazi. Alikuwa ni wakala wa usalama wa taifa katika idara ya magereza, hasa zaidi magereza ya kike kwa sababu ya jinsia yake. Yeye ndiye aliyekuwa amekabidhiwa jukumu la kumlinda Doi, jukumu alilopewa na mkurugenzi wa usalama wa taifa kupitia kwa wakala aliye karibu yake kiutendaji katika idara ya magereza. Mwalo alipewa jukumu hilo kwa sababu ya imani kubwa waliyokuwa nayo waajiri wake hasa katika ufuatiliaji wa mambo nyeti.

    Wakiwa kwenye korido ya gereza la Keko, wakielekea kwenye chumba cha mazungumzo, koplo Mwalo nyuma, na Doi akiwa mbele, koplo Mwalo aliuliza, “Unamfahamu vipi Makeke?”

    Lilikuwa ni swali gumu sana kwa Doi, kwa sababu katika maisha yake hakuwahi kulisikia jina hilo la Makeke. Alijaribu kuvuta kumbukumbu zake ni wapi amewahi kulisikia ama kuliona bila mafanikio.

    “Makeke?” Doi aliuliza baada ya kushindwa kulitambua jina hilo.

    “Ndiyo, Makeke…yule anayefanya kazi KWITALE ADVOCATES & COMPANY, unajifanya humjui?

    “Hapana… simjui”

    “Na Dominic je?”

    Kutajwa kwa jina Dominic kuliyabadiri mapigo ya moyo wa Doi kwa kasi ya aina yake. Moyo wa Doi ulikuwa ukidunda kama moyo utakao kuchomoka kutoka mahali pake! Taswira ya Dominic Masaka ilimjia akilini mwake, mwili ulimuishia nguvu na kasi yake ya kutembea ikaanza kupungua kwa kila hatua aliyopiga.

    Hakudhani kama angeweza kuhimili kumwona Domi baada ya dhuruma kubwa ya pendo aliyomfanyia. Alitamani kukimbia ili arejee kwenye chumba cha mahabusu alikotoka lakini hakuweza, alishindwa kabisa “Hajaja baba wala mama, amekuja Domi!” Doi aliwaza.

    “Samahani afande, naomba unirudishe,” Doi alisema.

    “Inamaana hutaki kuzungumza na mwanasheria wako?”

    Ilimbidi kujikaza kisabuni, Doi aliongoza mpaka chumba cha mazungumzo huku akiwa na wasiwasi na maswali tele. Alipofika mle chumbani Doi, alimtambua Dominic aliyekuwa amekaa akiutazama mlango wa kuingilia ukiwa kama unatokea kwenye kutoka katika vyumba vya mahabusu. Domi alipomuona Doi alitamani kusimama na kumkimbilia lakini Makeke alimzuia.

    Doi alifikishwa pale mezani walipo Domi na Makeke, alipofika tu Makeke akaamuru afunguliwe na koplo Mwalo alitii.

    “Habari yako Doi?” Makeke alisalimia. Doi aliitika huku macho yake akiwa ameyaelekeza chini kwa aibu, alijibu salamu ile kwa sauti iliyotetemeshwa na kilio kilichosindikizwa na michilizi ya machozi iliyoanzia machoni na kutiririka kupitia mashavuni hadi kidevuni mwake. Pale kidevuni machozi yalijikusanya na kutengeneza tone kubwa ambalo taratibu lilikiacha kidevu na kudondoka kuelekea mezani, kabla tone lile la machozi halijafika mezani, Domi aliliwahi likadondokea kiganjani mwake, kisha akatoa leso na kumfuta machozi yaliyosalia kwenye mashavu ya Doi kwa kutumia leso yake huku akisema, “Usilie Doi… ipo namna,”





    Kauli ya Domi ilipenya kwenye masikio ya Doi na kufanya mchomo mkali moyoni akajiona msaliti kwa kijana Domi, kijana aliye na upendo wa kustaajabiwa. Kijana ambaye hakuwa tayari kuliona chozi lake likidondoka chini, ajabu hii!

    Je ni lita ngapi za machozi zimemtoka kijana huyu na kumwagika chini? Tena zikimtoka kwa sababu yake! Doi aliumia sana. Akaikumbuka siku ile ya kwanza alipokutana na Domi kwenye daladala, na namna walivyofahamiana. Kumbukumbu za Doi zilienda mbali zaidi, akakumbuka jinsi Domi alivyokuwa akifuatisha mashairi ya wimbo aliokuwa akiusikiliza siku hiyo kupitia simu yake, “… I can be you hero….now I stand by you for rever…’Sauti ya Domi ikifuatisha mashairi hayo ilijirudia kichwani mwa Doi na kufanya mwangwi uliojirudia mara nyingi, mara zisizo na idadi. Ilikuwa ni sauti yenye kumanisha lakini katika hali ya mzaha.

    “…naweza kuwa shujaa wako… na sasa nasimama upande wako hata milele…” Akili ya Doi ilipata hangaiko la moyo lililomfanya atamke bila kujua, “Naomba unisamehe Domi”

    “Usijali mpenzi wangu nimekusamehe,” alisema Domi huku akijifuta machozi kwa leso ile ile.

    Makeke alishuhudia kila jambo lililokuwa likiendelea baina ya wawili hawa ambao ni dhahiri bado walikuwa wakipendana na kuhitajiana, katika kila hatua, “Doi Vioja, naitwa bwana Makeke. Ni wakili kutoka katika kampuni ya KWITALE ADVOCATES & COMPANY, niko hapa kama wakili wako kwenye kesi unayokabiliana nayo, niko hapa kuhakikisha unapata haki yako kwa mujibu wa sheria. Na huyu hapa ni bwana Dominic Masaka, ni mshirika wangu ambaye nitakua naye bega kwa bega katika swala hili, naye pia anatoka KWITALE ADVOCATES & COMPANY…” Makeke alisita kidogo kisha akayatembeza macho yake kuwatizama Domi na Doi kwa zamu, Domi na Doi wote walikuwa wanalia. Alifikiri kidogo kisha akaendelea… “Bwana Dominic… usiruhusu hisia zikutawale, najua umeumia na kila mtu ameumizwa, hivyo basi, nakuomba uyarudishe mawazo yako kwenye kazi iliyotuleta kwa sababu hatuna muda wa kupoteza.” Mara baada ya kusema hayo alimgeukia Doi, “ok… bibie… kama nilivyosema hapo awali kuwa tupo hapa kuhakikisha unapata haki yako kwa mujibu wa sheria. Uko tayari kutoa ushilikiano?” Makeke aliuliza.

    “Ndiyo niko tayari”

    “Ok… hivyo basi naomba unieleze kwa uelewa wako ulivyoshiriki katika mkasa huu,” Makeke alisema.

    Domi aliyekuwa kimya naye aliongeza, “sheria ina tabia moja Doi, nayo kutenganisha uongo na ukweli ili kuwezesha haki ipatikane, hivyo basi, huna budi kuelezea ukweli ulivyo, ili tujue namna ya kukusaidia.”

    Asikwambie mtu, maisha ya jela si mchezo! Na hakuna mwnye uwezo wa kuyavumilia, wanaotumikia vifungo vyao ndani ya magereza hukesha wakiomba nusra ili waweze kuachiwa. Hivyo Doi hakuwa na namna isipokuwa kutoa ushirikiano uliohitajika ili kama itawezekana aondokane na maisha ya gerezani maisha ambayohayavumiliki hata kidogo, Doi akaanza kwa kusema, “Kusema ukweli kabisa, mimi sihusiki na wala sijui lolote kuhusiana na hayo madawa niliyokutwa nayo.”

    “Ilikuwaje yakakutwa kwenye mizigo yako?” Makeke aliuliza baada ya kuwa ameandika pembeni, mara Doi alipomaliza kutoa maelezo ya kwanza.

    “Sijui ikuwaje kuwaje mpaka yakawa kwenye mizigo yangu.”

    “Iliwezekanaje mizigo yako iwe na vitu usivyovifahamu, kwani kuna mtu mlikuwa mnashea nae begi?” Makeke aliuliza.

    Domi aliandika pembeni, kisha akauliza, “Kwani wakati unapanga mizigo yako, kwa maana ya vitu vilivyokuwa kwenye begi na mkoba ambamo madawa yamekutwa, mlikuwa pamoja na nani?”

    Makeke alitikisa kichwa kama ishara ya kukubaliana na swali alilouliza Domi, akaandika pembeni kisha akatega sikio ili kusikiliza majibu yatakayotolewa na Doi.

    “Mizigo yote ya ndani ya begi na mkoba niliipanga nikiwa pekee yangu,” Domi aliandika, kisha akamgeukia Makeke ambaye bila kuchelewa aliuliza swali linguine kwa Doi, “…. Labda hayo mabegi pamoja na mkoba vilikuwa chini ya miliki ya nani kabla hujaanza kupanga mizigo yako,”

    “Begi na mkoba vilikuwa ni vipya,”

    “Ni nani uliyemtuma akanunue au ulienda mwenyewe? Na vilinunuliwa duka gani?” Domi aliuliza. Maswali yalikuwa ya moto kiasi cha kumchosha Doi kichwa, hali ya kulia ilipungua na hatimaye kuisha kabisa akaielekeza akili yake katika kufikiri zaidi juu ya maswali aliyokuwa akikabiliana nayo kutoka kwa bwana Makeke na Domi.

    “Begi na mkoba vililetwa tu, kwa sababu mimi sikuwa na uchaguzi wa aina wala ukubwa wa begi kwa ajili ya safari, hivyo baada ya kuwa vimeletwa nilichofanya ni kuvipokea tu.”

    “Ni nani aliyeleta?” Makeke aliuliza. Swali la ni nani aliyeleta begi na mkoba lilimuwia gumu Doi katika kulijibu, wakati bado anafikiria namna ya kulijibu, Domi akaongeza, “Labda kabla hujajibu hilo swali, itakuwa vyema kama majibu yake yataambatanishwa na majibu ya swali hili; tiketi yako pamoja na pass vinaonyesha kuwa ulikuwa unaelekea Ufaransa, sio?”

    “Ndiyo,”

    “Vizuri sana, kwa hiyo Ufaransa ndiyo ingekuwa mwisho wa safari yako, au ungeendelea baada ya pale, na lengo la safari yako nchini Ufaransa lilikuwa ni lipi na ulikuwa peke yako au na mtu mwingine?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Swali hili pia lilikuwa kama mwiba akilini na moyoni kwa Doi, alijaribu kufikiri ili apate majibu mwafaka dhidi ya maswali husika. Alikuna kichwa mara kadhaa kabla ya kujibu kisha akasema, “Begi na mkoba vililetwa na Damian, katika safari ya kutoka hapa Tanzania hadi Ufaransa ningekuwa peke yangu. Lakini mara baada ya kufika Ufaransa ningepokelewa na Damiani. Alinieleza kuwa; safari ya Ufaransa ni kwa ajili ya mapumziko tu, na baadae tungerudi nyumbani,”

    “Domi alinieleza kuwa siku ulipoondoka nyumbani ulimwachia barua pamoja na dola za Kimarekani, si sivyo?” kila swali alilokuwa akikabiliana nalo Doi lilikuwa la moto, hili pia kama yalivyo mengine yaliyotangulia lilikuwa kama msumari wa moto kichwani kwa Doi. Licha ya swali lenyewe kutaka jibu jepesi, lakini utoaji wa jibu ulihitaji ujasiri ambao Doi hakuwa nao. Hakuwa na jinsi isipokuwa kujibu maswali yote kwa ufasaha ili aweze kujinasua kutoka katika kuti kavu alilopo, alijibu, “Ndiyo.”

    “Bila shaka pesa hizo ulipewa na Damiani?”

    “Ndiyo,” Doi alijibu.

    “Alishawahi kukueleza kuwa anajishughulisha na nini?”

    Doi alifikiri kidogo, kisha akajaribu kuvuta kumbukumbu kama alishawahi kuambiwa na Damian juu ya shughuli anazofanya. Alijitahidi kukumbuka bila mafanikio. Hatimaye kumbukumbu zake zikamrudisha siku kadhaa nyuma.

    Ilikuwa siku ya Jumanne, siku ambayo Doi alikuwa nyumbani kama kawaida yake baada ya Domi kuondoka kuelekea kwenye mihangaiko yake ya kila siku. Doi alikuwa akijisomea moja ya miswada aliyoiandaa Domi kwa ajili ya kuchapa vitabu endapo angefaikiwa kupata ufadhili. Alikuwa amekolea baada ya kuwa amening’inizwa kwenye uzi wa taharuki iliyojengwa vyema kwa ukufu wa maneno yaliyounganishwa barabara na kufanya hadithi aliyokuwa akiisoma kuukonga moyo wa yeyote ambaye angethubutu kuanza kuisoma. Ilikuwa ni hadithi ile inayoitwa, ‘KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA’ ni hadithi ambayo ilimsahaulisha Doi makali ya njaa yaliyokuwa yakimwandama kwa kutokula tangu asubuhi.

    Akiwa amezama kabisa kwenye ukufu wa maneno yanayosimulia visa vya kusisimua baina ya msichana anayeitwa Wayeka na mpenzi wake Kitiheka, ambao ni wahusika wa hadithi hiyo ya ‘Kwenye siku yangu ya kuzaliwa’ Doi alishituliwa na sauti za mlango uliokuwa ukigongwa.

    “Ngo… ngo… ngo….”

    Hakutaka kabisa kuondolewa kwenye uhondo aliokuwa akiupata kutoka kwenye hadithi hiyo iliyoandikwa na mpenzi wake lakini hakuwa jinsi. Sauti za mlango unaogongwa ziliendelea kumpa kero iliyomsababishia kupatwa na chukizo dhidi ya aliyekuwa anagonga mlango licha ya kutomjua ni nani.

    Hakuwa na budi kusema, “karibu”, huku akijiinua kivivu kutoka kitandani alipokuwa amekaa akisoma kitabu chake, alienda mpaka mlangoni akaufungua mlango. Alikuwa ni Zai… Zainabu Mpotoshi, shoga yake wa siku nyingi ambaye sasa ni jirani yake baada ya kuwa amehamia nyumbani kwa Domi.

    “Karibu shosti… karibu ndani” Doi alikaribisha.

    “Ahsante shosti mwenzio nimegonga kweli…. Mpaka nikahisi labda haupo. Ulikuwa umelala?’

    “Aku, nilikuwa nimemezwa na ufundi wa shemejio hapa,” alisema Doi huku akiushika ule muswada kumuonyesha Zai ambaye hakujishughulisha nao.

    Baada ya salamu na mazungumzo mafupi baina yao hatimaye Zai alimweleza Doi shida yake.

    “Shosti…. Mi sina mengi naomba tu unisindikize Uchumi Supermarket, kuna mtu nataka kukutana naye pale. Naomba unisindikize shoga, jipale nakusubiri.”

    “Jamani Zai… mwenzio nilikuwa nasoma hadithi hapa umenikatisha uhondo wangu, nivumilie basi nijiandae.”

    Saa moja baadaye Zai na Doi walikuwa kwenye viwanja vya ‘Quality Centre’, mahali ambapo lipo duka la Uchumi Supermarket.

    Zai alikwenda pale kwa minajili ya kuonana na hawala yake ambaye alimwambia waonane ili amfanyie shopping ya vitu ambayo Zai aliomba anunuliwe na hawala yake huyo. Hawala yake Zai alijitambulisha kwake kuwa anaitwa Marcus japo jina lake halisi halikuwa hilo, alikuja na swahiba yake ambaye alitambulishwa kuwa anaitwa Damian.

    Damian alipomuona Doi alivutika naye akamtumia Zai kumkuadia baada ya yeye kutopata ushirikiano kutoka kwa Doi kwa namna aliyoitarajia. Hivyo baada ya shughuli ya pale ‘Quality Centre’ Zai na Doi walilejea nyumbani, wakati Zai akielekea kwake alipokuwa akiishi na Mudi, Doi alielekea kwake mahali walipoishi yeye na Domi, siku hiyo ikaisha.

    Siku iliyofuata majira yaleyale kama ya siku iliyopita Zai aliwasiri nyumbani kwa Doi ambako kama ilivyo ada alimkuta akipitisha wakati kwa kufunua kurasa baada ya kurasa za hadithi iliyoukonga moyo wake, hadithi ya, “kwenye siku yangu ya kuzaliwa”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Shoga we nawee…. huchoki? Kila nikija hapa kwako wewe na hicho kitabu… kitabu na wewe utadhani umerogwa!”

    “Mh! Shosti mdomo huo… mdomo huo...”

    “Basi yaishe bibi weee… sikujia hayo…”

    “Haya sasa yaseme yaliyokuleta,”

    “ We ni wangu shosti, lazima nije nikujulie hali. Vipi bukheri?”

    “Mi bukheri shosti”

    “Mi bukheri shosti,” Zai aliigiza sauti ya Doi kwa kubana pua, “Eti bukheri?” alisema Zai. “Tuacchane na hayo” aliendelea, “Mi ni mzuri shosti ila kwako sitii maguu,”

    “Umeanza mambo yako,”

    “Lazima niseme shosti kama umenizidi… umenizidi tu, watu si wanaona wenyewe ila unajichakaza Doi, unajichakaza..”

    “Najichakaza kivipi,” Doi alihoji.

    “Doi…. unadhani wewe ni wa kusuka mabutu na ukifumua tu mabutu, basi unasuka twende kilioni. Unadhani wewe ni wa kufunga kiremba muda wote utadhani bibi wa kinyamwezi aliyeko Tabora wakati uko Dar?” Zai alisema.

    “Yametoka wapi hayo tena shoga?”

    “Hapana Doi wewe ni rafiki yangu wa muda mrefu, nadhani unakumbuka kuwa nilirudia darasa ili nisome darasa moja na wewe, hivyo siwezi kuvumilia kuona unachakaa kiasi hiki! Napenda kuona unasuka sangita na ukifumua tu unaweka relaxer au bonding kabisa!”

    Maneno ya zai yalimchanganya Doi kiasi cha kushindwa kuelewa ni nini hasa alichokimaanisha. Aliyatafakali sana maneno yale lakini jibu halikuwa tayari kuungana naye. Ikambidi kumuuliza shoga yake, “Sijakuelewa Zai”

    “Hivi ni nini kinakufanya ung’ang’anie maisha ya namna hii? Maisha yanayozidi kukuchakaza siku hadi siku… Sikiliza Doi, najua unampenda Domi… ila haina maana kuwa kila unayempenda ni lazima uishi naye….”

    “Zai ishia hapohapo… najua unalotaka kusema, naomba uniache na Domi wangu,” alisema Doi huku akiwa ameunyoosha mkono wake mithili ya askari wa uslama barabarani asimamishaye kuelekea kwa shoga yake.

    “Tatizo lako ni kujifanya mjuzi wa kila jambo, mi sijasema umuache Domi”

    “Kumbe je?”

    “Fanya kitu ambacho kitakusaidia wewe halikadhalika pia Domi, najua Domi ni msomi… tena msomi wa chuo kikuu, lakini kama unavyojua nchi hii bila kutoa kitu hupati kitu… nakusudia kusema kuwa ili Domi apate kazi ni lazima atoe hongo. Hivyo kwa maisha haya hiyo hongo itatoka wapi?”

    “Kwa hiyo afanyeje sasa?”





    “Hilo ni swali zuri sana. Jana wakati tupo na Marcus pale ‘Quality Centre’, alikuwepo pia rafiki yake, si unamkumbuka?”

    Doialitikia kwa kichwa kuwa anakumbuka na Zai akaendelea, “…basi jamaa ana pesa balaa…. mbuzi haruki! Ni mtu na pesa zake anaomba kesho mkutane naye…”

    “Muda umeisha naomba nimrudishe Doi chumbani kwake,” sauti ya afande Mwalo ilimgutua Doi kutoka kwenye lindi hilo la mawazo.

    Domi na Makeke waliagana na Doi huku wakiahidi kurudi tena. Walitoka mpaka nje ya gereza, lakini kabla hawajalifikia gari walilokuwa wamekuja nalo walikutana na Mzee Vioja akiwa sanjari na mkewe, mama Doi.

    Walisalimiana kisha Domi aliwatambulisha kwa bwana makeke, akimuelezea kuwa ndiye wakili watakaye kuwa naye bega kwa bega kwenye kesi ya Doi.

    Baada ya utambulisho huo Domi aliwaomba wakasalimiane na mzee Masaka ambaye aliachwa ndani ya gari akiwasubiri wakati wao wameenda kuzungumza na Doi.

    Mzee Vioja na mkewe hawakuwa na pingamizi, walienda mpaka kwenye gari wakasalimiana na mzee Masaka ambaye pia alifurahi baada ya kutambulishwa kwao. ****

    Mzee Masaka aliamka asubuhi huku akilalamika kuumwa kikohozi pamoja na maumivu makali ya kifua kwa ndani.

    “Koh… koh… koh..” alizidi kukohoa mzee Masaka mbele ya Domi ambaye alikwenda chumbani kwake kumsalimia kabla hajaenda kazini.

    “Nimekohoa usiku kucha na kila nikikohoa nahisi maumivu ndani ya kifua”

    Domi alimuhurumia baba yake,v“Pole sana baba, inabidi twende hospitali upate vipimo ikibidi upate matibabu,” Domi alimrai baba yake.

    Rai ya Domi kwa baba yake ilipokelewa bila pingamizi. Mzee Masaka alijianda na alipokuwa tayari walielekea hospitali.

    Njiani Mzee Masaka aliendelea kukohoa na maumivu ndani ya kifua yalizidi kupamba moto sanjari na maumivu ya koo yaliyokuwa yakimpa wakati mgumu kila alipojaribu kumeza mate.

    Baada ya muda wa takribani saa moja hivi, Dominic na Mzee Masaka waliwasili hospitalini kwa ajili ya kumuona daktari. Mzee Masaka alimweleza Daktari namna anavyojisikia mwilini mwake. Na mara baada ya kutoa maelezo yaliyokuwa yakisikilizwa kwa makini ya hali ya juu na daktari, Daktari alimuuliza, “Unavuta tumbaku?”

    “Ndiyo dokta navuta” Mzee Masaka alijibu swali la daktari bila kuumauma maneno.

    Mara baada ya jibu hilo Daktri alitambua kuwa tatizo la Mzee Masaka limechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya tumbaku. Aliuhisi ugonjwa wa mzee Masaka kupitia maelezo yake lakini hakutaka kumuanzishia matibabu kabla ya kumfanyia uchunguzi wa kina. Hivyo baada ya maelezo mzee Masaka alifanyiwa vipimo ambavyo vilitoa majibu yaliyomshangaza hata Daktari. Mzee Masaka alikuwa mgonjwa, alikutwa na maambukizi ya saratani ya mapafu ambayo kwa mujibu wa Daktari ilisababishwa na matumizi ya tumbaku.

    ****

    Mzee Masaka alianza kutumia tumbaku miaka mingi iliyopita wakati ambao alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya msingi Bukama. Alianza kwa kuokota kipande cha sigara kilichoachwa na mjomba wake ambaye walikuwa wakilala naye chumba kimoja wakati huo. Baada ya kuvuta kipande hicho cha sigara, siku iliyofuata alirudia tena kwa kuvuta kipande alichokiokota nje, bila shaka nacho kilitupwa na mjomba wake.

    Tabia yake ya kuokota vipande vya sigara na kuvivuta ilipamba moto na hata kufikia hatua ya kuanza kuiba sigara za mjomba wake ambaye alikuwa na tabia ya kununua pakiti nzima kwa sababu ya kukubuhu katika uvutaji. Uvutaji wa sigara ulimkolea Masaka kiasi cha kupatwa na tabu isiyoelezeka pindi akosapo sigara. Alivumilia kwa muda na mwani ulipomzidia Masaka alianza udokozi wa vijisenti vya baba yake ili tu akaikate kiu yake.

    Hakuna aliyefahamu kwa wakati huo kama Masaka anavuta sigara, hata baba yake hakuwa na habari licha ya pesa zake zilizoibwa kutumika kugharamia starehe hiyo haramu. Angejuaje wakati muda mwingi alikuwa ‘bwii’? Hivyo kila senti yake iliyopungua aliijumuisha katika matumizi yake ya kilabuni alipokuwa akienda kila baada ya kazi.

    Alipohitimu darasa la saba, mzee Masaka hakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari. Akalazimika kukiacha kijiji akaelekea mjini Bunda ambapo alibahatika kupata kibarua kwenye kampuni inayojishughulisha na ukamuaji wa mafuta ya mbegu za pamba.

    ****

    “Mzee wangu kwa mujibu wa vipimo inaonekanaa kuwa una tatizo la koo pamoja na mapafu” Daktari alifafanua, “Tatizo hili kwa kiasi kikubwa husababishwa na matumizi ya tumbaku ya muda mrefu…” Maelezo ya Daktari yalimchanganya kabisa mzee masaka kiasi cha kumfanya adondoshe chozi. Taswira ya mkewe, mama Domi ilimjia sambamba na sauti iliyokuwa ikimnung’unikia kwa tabia yake ya uvutaji wa tumbaku. Akajilaumu kwa kutokuwa msikivu kwa mkewe na akailaani ile siku ya kwanza alipovuta tumbaku kwa mara ya kwanza. Mzee Masaka alilia!

    Majibu hayo ya Daktari yalipokelewa pia kwa masikitiko makubwa na Domi, ambaye hakuwa na jinsi isipokuwa kumchukua baba yake na kumrudisha nyumbani huku wakisubiri tarehe nyingine ya kurudi tena hospitali kwa ajili ya kliniki kama daktari alivyoshauri.

    ****

    Siku moja Domi akiwa ofisini kwake, aliingia Neema akiwa na bahasha mkononi. Kama kawaida yake alimtania kidogo Domi kisha akamkabidhi barua yake. “Hii ni barua yako… kama itakuwa ni ya nyongeza ya mshahara, usisite kunigawia japo kidogo,” mara baada ya kuyasema hayo aliondoka.

    Domi aliipokea ile barua na kuifungua, hakuamini alichokiona! Ilikuwa ni barua ya majibu ya ombi lake la kudhaminiwa katika uchapaji wa hadithi yake. Barua iliyomtaka afike kwenye ofisi za kampuni ya ‘UBUNIFU WETU’ kwa lengo la kusaini mkataba wa uchapishaji wa kazi zake.



    9

    KESI ya Doi iliunguruma kwa muda wa miezi miwili huku bwana Makeke sambamba na Dominic wakijitahidi kwa kila hali kumtetea kwa mujibu wa sheria. Kisicho riziki hakiliki, kesi iliisha kwa Doi kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatwa na hatia.

    Ilikuwa ni huzuni ya hali ya juu kwa Domi pamoja na wazazi wa Doi ambao walihudhuria mahakamani kila kesi ilipotajwa. Rufaa ilikuwa wazi lakini hata ilipokatwa kesi iliunguruma tena na kuisha bila kubadili hukumu ya awali. Doi alilia sana na Domi alilia naye, lakini ukweli haukubadilika.

    Doi akayaanza maisha mapya akiwa ndani ya sare za magereza, akiwa kama mfungwa mwenye namba P2832.

    Siku hiyo hiyo Domi aliporudi nyumbani, aliufungua mkoba wake na kuitoa ile barua aliyoandikiwa na Doi, barua ambayo alikuwa akitembea nayomuda wote kila mahli alipoenda. Baada ya kuifungua Domi aliisoma ile barua ambayo ni barua chungu katika barua zote alizowahi kuandikiwa;

    “Kwako mpenzi Domi, natambua fika kuwa unajua nakupenda na ndivyo ukweli ulivyo. Ila hali ya maisha imenilazimu kufanya hivi, naomba usinielewe vibaya tafadhali.

    Nafanya hivi kwa ajili yetu sote yaani mimi na wewe na wote wanaotuzunguka, kwa maana ya familia. Si kama sikupendi, ila siyapendi maisha duni, maisha ambayo tumekuwa wafungwa wake kwa muda mrefu sasa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Inaniuma sana kukuandikia haya ila sina budi mpenzi…” hakuendelea kusoma zaidi kwa sababu ya machozi yalyoanza kumtoka. Aliikunjakunja ile barua kisha akaicoma moto ili kuifuta kumbukumbu ya barua hiyo iliyokuwa ikimwumiza.

    Miezi mitatu baadaye Domi alimtembelea Doi gerezani. Uwepo wake gerezani kwa siku hiyo uliibua faraja mpya kwa Doi. Faraja ambayo aliishuhudia ikififia kwenye siku ile ambayo kesi yake ilihitimishwa kwa hakimu kumsomea hukumu yake ya kifungo cha miaka mitano jela kwa mujibu wa sheria.

    Ni kipi alichohitaji tena zaidi ya faraja, hasa katika wakati mgumu kama huu, wakati ambao alikuwa anakitumikia kifungo chake! Ndiyo, alikuwa anahitaji faraja lakini si kutoka kwa Domi. Kwa Doi, Domi ndiye aliyehitaji faraja kuliko yeye.

    Domi alihitaji faraja kwa sababu alisaritiwa na mpenzi katika wakati ambao alihitaji mtu wa karibu kwa ajili ya kumfariji, mtu huyo ni nani kama si yeye?

    Doi alikuwa kimya baada ya kuwa wamesalimiana na Domi. Ukimya huo uliodumu kwa muda wa dakika moja ulivunjwa na Doi mwenyewe, “Hapana,” sauti ilimtoka Doi huku akijaribu kujiinua kutoka pale kwenye kiti alipokuwa. Hakuweza baada ya kuzuiliwa na mikono ya Domi sambamba na sauti yake iliyokuwa ikimsihi asiondoke.

    “Niko hapa kwa ajili yako Doi,”

    “Naelewa Domi , lakini…” kabla hajamalizia kauli yake, Domi alimkatisha kwa kusema, “Usiruhusu fikira zako ziwe mbali na mahali hapa, hasa katika wakati huu ambao niko hapa kwa ajili yako.”

    “Siwezi Domi…. siwezi, nimesha yakosea maisha tayari,” “Hapana Doi hujakosea, maisha ndivyo yalivyo, hakuna aliyewahi kuyapatia… hakuna mkamilifu chini ya jua, kila mtu kuna mahali alipokosea. Ichukulie hali hii kama changamoto, kisha ukubaliane nayo kama changamoto unayopaswa kukabiliana nayo bila kujiuzulu…” Domi alitulia kidogo kisha akaangaza kushoto na kulia. Nadhani alitaka kuhakikisha kama kuna watu wengine tofauti na wao, walikuwepo!

    Aliyarudisha tena macho yake kwa Doi, kwa sauti ya chini zaidi kuliko ilivyokuwa awali akamwambia, “Kama nilivyokwisha kusema Doi, hii ni changamoto katika mfululizo wa changamoto za kimaisha…. hali hii isikufanye ukajihangaisha kutafuta ni nini maana ya maisha, hutoipata! Na pengine utajikuta unakata tamaa ya kuishi kabisa. Kufungwa siyo mwisho wa maisha… bado nayo nafasi Doi,”

    Mazungumzo baina yao yaliendelea, ni katika maongezi hayo, ndiyo Domi alimweleza Doi juu ya kifo cha mzee Masaka. Taarifa za kifo cha mzee Masaka zilimshitua sana Doi, akamhurumia Domi lakini alikuwa amekwisha chelewa, kwani Domi alishakubaliana na hali ya kuondokewa na baba yake kipenzi kwa sababu tamati ya maisha tunayoishi ni kifo.

    Muda uliyoyoma wakiwa pamoja mahali pale, hatimaye ukafika wakati ambao Domi aliaga, lakini kabla hajaondoka alimkabidhi Doi bahasha akaondoka.

    Doi aliifungua ile bahasha akiwa na shauku ya kutaka kujua kilchomo, hakuyaamini macho yake pale alipokishuhudia kitabu kikubwa cha hadithi aliyoipenda, kitabu kiliandikwa kwa maandishi makubwa kabisa juu ya jalada yaliyosomeka hivi, ‘KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA’ aliifahamu vema hadithi hii. Moyoni alijiona msaliti asiyefaa kuigwa, chozi likamtoka.

    Doi aliifungua ile bahasha akiwa na shauku ya kutaka kujua kilchomo, hakuyaamini macho yake pale alipokishuhudia kitabu kikubwa cha hadithi aliyoipenda, kitabu kiliandikwa kwa maandishi makubwa kabisa juu ya jalada yaliyosomeka hivi, ‘KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA’ aliifahamu vema hadithi hii. Moyoni alijiona msaliti asiyefaa kuigwa, chozi likamtoka.



    ****



    VITA dhidi ya madawa ya kulevya ilizidi kupamba moto kila pembe ya dunia, huku idara ya polisi katika kila nchi wakishirikiana bega kwa bega na polisi wa kimataifa ‘INTERPOL’ katika vita hiyo.

    Kwa ushirikiano huu mafaniko makubwa yalipatikana ikiwemo kuwakamata wafanyabiashara wengi waliojihusisha na biashara hii wakubwa kwa wadogo. Ulinzi uliimarishwa maradufu kiasi cha kufanya mianya mingi iliyotumika kiholela hapo awali kuwa migumu katika historia ya biashara hii haramu inayopigwa vita kwa sababu ya uharibifu mkubwa inaousababisha wa kuharibu afya na akili za watumiaji.

    Wale wote waliojifanya kichwa ngumu waliuawa katika makabiliano ya ana kwa na polisi katika jitihada zao za kuingiza mzigo sokoni. Wengi walikufa akiwemo Damian ambaye aliuawa sambamba na gwiji katika biashara hii haramu, aliyefahamika kama Gustavo Maritinez Sucre. Waliuawa mpakani mwa Mexico na Marekani wakiwa katika harakati zao za kuvusha mzigo wa cocain kuingiza nchini Marekani.

    ****

    Miaka mitatu huku Domi akifurahia mapato yaliyotokana na mauzo ya vitabu vyake vya hadithi hasa kile cha ‘KUTI KAVU’ sambamba na kile cha ‘KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA’ ambacho kimekwishachapishwakwenye lugha zaidi ya sita za kimataifa ikiwemo kiingereza na kifaransa.

    Siku moja bwana Makeke alimtembelea Domi nyumbani kwake, ambako alimkuta yuko na mkewe.

    Wakiwa sebuleni kwa Domi, makeke alikuwa amembeba mtoto mdogo ambaye umri wake ulikuwa ni kama miezi mitatu hivi.

    Katika mazungumzo yaliyodhihirisha furaha iliyopo baina yao Makeke alisema, “Jamani mimi napenda kusimulia hadithi,”

    “Basi leo umepata wasikilizaji wa hadithi, anza kutusimulia….” Alisema Domi huku mkewe aliyekuwa nyuma ya kochi amemuinamia akiachia tabasamu sambamba na kumminyaminya mabegani.

    “Haya sasa sikilzeni hadithi yenyewe…”

    “Enhe…!” sauti ya Domi na mkewe zilisikika wakijibu kwa pamoja.

    Makeke alianza, “Hadithi hadithi….”

    “Hadithi njoo.. uongo njoo utamu kolea…” Doi na mkewe walijibu katika namna ya mzaha iliyoongeza furaha baina yao.

    “Hapo zamani za kale… si zamani sana kama zilivyo zama za mawe, hapana. Namaanisha zama hizihizi, yaani kama miaka thelasini na ushei hivi iliyopita. Palitokea kijana mmoja aliyeitwa Dominic Masaka…” alisita kidogo kisha akawatazama hadhira yake ambao bado walikuwa wakielea kwenye tabasamu halafu akaendelea, “….basi Domi huyo alianza shule ya awali, baadaye msingi, sekondari na hata chuo kikuu hatimaye akahitimu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuhitimu, alitafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio, lakini hakuchoka! Ikafika siku ambayo Mungu alimuandikia, Domi akapata kazi. Aliifanya kazi kwa bidii…

    Siku zikapita.. siku zikapita hatimaye Domi akamuoa Neema na sasa wana mtoto wao kipenzi anayeitwa Tumaini.Na hadithi yangu imeishia hapo.”

    Hitimisho la hadithi ya makeke liliwachukua Domi na Neema ambaye ni mkewe mpaka kwenye tabasamu lililozaa kicheko kilichoungwa mkono na mtoto wao mdogo aliyekuwa amepakatwa mikononi mwa Makeke, wote wakacheka!



    ….Mwisho!....



    TOA MAONI YAKO……..

    ASANTENI KWA KUWA NAMI MWANZO HADI MWISHO









0 comments:

Post a Comment

Blog