Simulizi : The Holy Sin (Dhambi Takatifu)
Sehemu Ya Tano (5)
Kauli hiyo ya Kamanda Mdimu ilimfanya abaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa, macho yakiwa yamemtoka pima. Alishindwa kuelewa atoe jibu gani kwani ni kweli mumewe alikuwa amemfanyia kosa kubwa la kumdhalilisha lakini suala alilolizungumzia mkuu huyo wa kituo lilimfanya azidi kuchanganyikiwa.
“Niamini, nitakusaidia kuhakikisha unapewa talaka yako, si unakumbuka uliniahidi kuwa utakuwa tayari kwa chochote ilimradi nimsaidie mumeo awe huru na kesi ile tuimalize?” alihoji Kamanda Mdimu.
“Ndi...yo nilisema nitakuwa tayari kwa lolote lakini siyo hili,” alisema mama Aidan kwa kubabaika.
“Tafadhali nionee huruma mwenzio, nipo chini ya miguu yako, nakuhitaji kwenye maisha yangu, nimechoshwa na huu upweke,” alisema Mdimu kwa hisia huku akilengwalengwa na machozi kwa mbali.
“Basi naomba unipe muda wa kufikiria kwa kina, nitakupa majibu tutakapoonana tena.”
“Kwa hiyo tutaonana tena lini?”
“Nipe muda nitakwambia.”
“Jitahidi basi usichelewe sana, yaani ukinikubalia tu hata wiki haitaisha utakuwa umeshapewa talaka yako kisha tutaoana na kuishi kama mume na mke, nimekuandalia vitu vingi sana vizuri,” alisema Kamanda Mdimu na kuinuka, akamuinamia mama Aidan pale alipokuwa amekaa na kumbusu.
Japokuwa mwenyewe hakupendezewa na tukio hilo, alishindwa kufanya chochote kulizuia, akakusanya vitu vyake tayari kwa kuondoka, Mdimu akataka kumsaidia kubeba pochi lakini mwenyewe akakataa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakaongozana mpaka kwenye gari walilokuja nalo, akamfungulia mlango mama Aidan kisha akarudi upande wake na kukaa nyuma ya usukani, safari ya kuondoka kwenye hoteli hiyo ikaanza huku kila mmoja akiwa kimya ndani ya gari.
“Naomba nikupeleke hadi nyumbani.”
“Hapana usinifikishe nyumbani, twende ukaniache kituoni halafu nitajua mwenyewe namna ya kufika nyumbani,” alisema mama Aidan lakini bado mkuu huyo wa kituo akawa king’ang’anizi. Mwisho walikubaliana kuwa akamuache karibu na nyumbani kwake.
Baada ya dakika kadhaa, walikuwa wameshafika jirani na nyumbani kwa akina Aidan, akapunguza mwendo na kusimama pembeni ya barabara. Kabla mama Aidan hajateremka, alifungua ‘dashboard’ ya gari na kutoa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi.
“Hizi zitakusaidia matumizi madogomadogo,” alisema Kamanda Mdimu kisha akambusu tena mama Aidan shavuni. Akamfungulia mlango na kuagana naye. Kila kilichokuwa kinatokea kwenye maisha ya mama Aidan alikifananisha na njozi za mchana.
Alitamani awe ndotoni lakini haikuwa hivyo, tukio la mumewe kumbaka Caro lilikuwa limefungua mlango kwa mambo mengi ambayo hakuwahi kudhani kwamba yanaweza kutokea kwenye maisha yake hata mara moja.
Hakuwahi kushikwa mwili wake kimahaba na mwanaume mwingine tofauti na mumewe lakini sasa Kamanda Mdimu alifikia hatua ya kumbusu, tena mara mbili bila ridhaa yake mwenyewe.
Pia suala la fedha halikuwa tatizo kwenye maisha yake na mumewe hajawahi kupata matatizo yoyote ya kifedha kiasi cha kufikia hatua ya kuhongwa na mtu yeyote lakini sasa Kamanda Mdimu alikuwa amempa fedha nyingi ambazo wala hakuwa na shida nazo ila alishindwa kuzikataa.
“Eeeh Mungu wangu, ninusuru na hii mitego iliyopo mbele yangu, nipe busara ya kuamua ninachokitaka bila kutetereka,” aliwaza huku akitembea, machozi yakawa yanamtoka bila mwenyewe kugundua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alienda moja kwa moja mpaka nyumbani kwake, akapokelewa na mwanaye Aidan aliyekuwa amekaa sebuleni akijisomea.
“Mbona unalia mama? Unaumwa?” alihoji Aidan wakati akimpokea mama yake mkoba, akatingisha kichwa kumkatalia kisha akajifuta machozi harakaharaka, akaongoza mpaka chumbani ambako alimkuta mumewe akiwa amelala.
“Mbona umechelewa sana?”
“Kuna mambo ya kisheria tulikuwa tunakamilisha na mkuu wa kituo,” alijibu mama Aidan huku akikwepa kutazamana na mumewe usoni.
“Ooh! Sawa, pole kwa usumbufu ninaokusababishia,” alisema mzee Kenan huku akikaa kitako kwa lengo la kuendelea kumbembeleza mkewe abatilishe uamuzi wake wa kudai talaka.
“Naomba unisamehe mke wangu, na mimi ni binadamu wala siyo malaika, kukosea tumeumbiwa. Naomba usiniache,” alisema baba Aidan kwa sauti ya kubembeleza lakini mkewe hakujibu kitu chochote zaidi ya kujiinamia.
“Kumbuka wapi tulikotoka mke wangu, wewe ni shahidi kwamba sijawahi hata mara moja kukusaliti tangu tuoane, ni shetani tu alinipitia mke wangu, nipo chini ya miguu yako,” alisema mzee Kenan huku akiteremka kitandani na kumpigia mkewe magoti.
Akiwa bado anaendelea kumbembeleza, simu ya mkewe ilianza kuita mfululizo, mama Aidan aliyekuwa amejiinamia aliinua uso wake na kuichukua, akawa anaangalia namba ya mpigaji.
Mapigo ya moyo wake yalilipuka na kuanza kwenda mbio baada ya kugundua kuwa Kamanda Mdimu ndiye aliyekuwa akimpigia. Hakujua kama apokee au asipokee simu hiyo, akabaki kubabaika, jambo ambalo mumewe aliligundua.
“Nani anakupigia?” aliuliza mzee Kenan huku akisimama.
“NI mkuu wa kituo, kuna maelekezo alisema anataka kunipa kuhusu kesi yako.”
“Ooh! Basi hakuna tatizo, ongea naye tu,” alisema mzee Kenan bila kuelewa chochote kilichokuwa kinaendelea. Mkewe akapokea simu ambapo jambo la kwanza ilikuwa ni kumtaarifu Mdimu kama yupo na mumewe kwa kujihami.
“Haloo! Eeh za kazi afande, nipo na mume wangu hapa tunajadili kuhusu kile ulichoniambia,” alisema mama Aidan kisha akabonyeza kitufe cha kukatia simu.
“Vipi anasemaje?” mzee Kenan alimuuliza mkewe huku akiwa na shauku ya kutaka kujua ni maelekezo gani amepewa. Kwa kuwa hakuwa na maelekezo yoyote, ilibidi atunge uongo kwamba kuna fedha zinatakiwa ili kutuliza kabisa kesi yake ya ubakaji.
“Amesema shilingi ngapi?”
“Hajasema ila amesema tujiandae, atatupa taarifa muda wowote akishakuwa na jibu kamili,” mama Aidan alizidi kudanganya, mumewe akamjibu kuwa asiwe na wasiwasi kwani fedha siyo tatizo kubwa kwao. Akashusha pumzi ndefu baada ya kufanikiwa kumdanganya mumewe.
Japokuwa mumewe aliendelea kuzungumza naye, akili za mama Aidan zilihama kabisa, akawa anawaza namna ya kuutatua mtihani mkubwa uliokuwa mbele yake. Ni kweli mumewe alimsaliti na hakuwa akitaka kuendelea kuishi naye lakini hakutaka mtu mwingine atumie udhaifu huo kwa manufaa yake binafsi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimtazama mumewe kwa muda, akajiinamia na kuendelea kutafakari nini cha kufanya, alijikuta akimuonea huruma kwani kwa jinsi Kamanda Mdimu alivyokuwa na hamu ya kuishi naye, alikuwa tayari kufanya chochote ili mradi atimize malengo yake.
“Mbona bado unaonekana una mawazo mke wangu? Tafadhali, nipo chini ya miguu yako, naomba usiniache,” alisema mzee Kenan kwa upole, akaendelea kumbembeleza mkewe kwa muda mrefu lakini muda wote alikuwa kimya.
Siku ya kwanza ilipita, kesho yake Kamanda Mdimu akampigia simu mama Aidan na kumuuliza kuhusu jibu lake.
“Mbona una haraka? Nimekwambia subiri nifikiri, nitakupa majibu usijali,” alisema mama Aidan.
Baada ya siku tatu kupita huku akiwa bado hana maelewano na mumewe, aliamua kuchukua uamuzi mgumu wa kumkatalia Afande Mdimu. Alimpigia simu nakumtaarifu wakutane palepale walipokutania mara ya kwanza.
“Japokuwa mume wangu amenikosea sana, nimeamua kumsamehe na sitadai tena talaka kwa hiyo ombi lako limeshindikana,” alisema mama Aidan kwa sauti ya utulivu akiwa na Mdimu, kwenye hoteli ileile waliyokutania mwanzo.
“Lakini uliniahidi kuwa upo tayari kufanya chochote ili mradi nikusaidie, sasa shida yako imeisha unaniona sina maana tena, unafikiri ni sawa?”
“Siyo sawa Mdimu lakini tambua mimi ni mke wa mtu na nimeshakwambia kwamba nimeamua kumsamehe mume wangu.”
“Huyo mumeo angekuwa anakupenda kweli angekutia aibu kwa kumbaka mtoto ambaye ni sawa na binti yenu?”
“Sawa lakini nimeamua kumsamehe.”
“Kwa hiyo vipi kuhusu mimi?”
“Sasa nitakusaidiaje Mdimu?”
“Hata kama mmeamua kusameheana na mumeo, na mimi nataka uwe mpenzi wangu lakini tutafanya siri mtu yeyote asijue.”
“Haa! Hilo haliwezekani kabisa, siwezi kuwatumikia wanaume wawili kwa wakati mmoja, sikulelewa hivyo mimi.”
“Kwa hiyo shukrani ya punda imekuwa mateke si ndiyo? Yaani msaada wangu wote niliokufanyia leo unashindwa kulipa fadhila kwa kitu chepesi kama hicho?”
“Nipo tayari kulipa fadhila lakini siyo mwili wangu, we sema chochote unachotaka nitajitahidi kukupa lakini siyo mwili wangu.”
“Sasa sikia, nakupa muda nenda kajifikirie tena, nataka uwe mpenzi wangu wa siri kama nilivyokwambia na kama utaendelea kushikilia msimamo wako, naifufua upya kesi ya mumeo akafungwe miaka thelathini. Nimemaliza,” alisema Mdimu kwa hasira, akasimama na kuanza kuondoka, mama Aidan akiwa amepigwa na bumbuwazi.
“Basi usiondoke kwanza,” alisema mama Aidan kwa sauti iliyoonyesha dhahiri kutishwa na kauli iliyotolewa na Kamanda Mdimu.
“Mimi nimeshamaliza, naondoka zangu,” alisema Kamanda Mdimu huku akionyesha kutokuwa na hata chembe ya masihara. Mama Aidan akazidi kumbembeleza, hali iliyomfanya alegeze msimamo wake, akarudi na kukaa palepale alipokuwa amekaa awali. Mama Aidan akawa anang’ata kucha zake kwa aibu huku akishindwa hata pa kuanzia.
“Nakusikiliza!”
“Basi sawa nipe muda nikafikirie upya ila nakuomba usiwe na hasira na wala usiifufue kesi ya mume wangu, nakuomba nipo chini ya miguu yako,” alisema mama Aidan huku akilengwalengwa na machozi.
“Mimi nakushangaa, mbona jambo jepesi unataka kulifanya liwe gumu?”
“Naogopa mume wangu atajua, hakuna siri kwenye mapenzi.”
“Atajua kwani utamwambia wewe?”
“Hapana lakini najua ipo siku atajua tu, isitoshe mimi sijazoea kumsaliti mume wangu. Tangu anioe sijawahi kutoka nje hata mara moja,” alisema mama Aidan huku akitetemeka kwa hofu.
“Wala usijali, hawezi kujua chochote na hata kama akijua, mimi nitakulinda,” alisema Kamanda Mdimu na kusogeza kiti chake jirani na mama Aidan, akapitisha mkono wake shingoni na kumkumbatia kisha akambusu shavuni. Japokuwa mama Aidan hakufurahishwa na kitendo hicho, hakuwa na cha kufanya.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nikubalie uyafaidi maisha, achana na yule bwege wako anayekutia aibu mbele ya jamii, njoo kwangu nikuonyeshe maana ya mapenzi na heshima ya mwanamke,” alisema Kamanda Mdimu huku mkono wake mwingine ukivinjari taratibu kwenye mwili wa mama Aidan.
“Ha…ha…pa…na,” mama Aidan alijaribu kujitoa kwenye mikono ya Mdimu lakini haikuwezekana, akaendelea kumfanyia uchokozi wa makusudi huku akimtolea maneno matamu ya kumlainisha.
Mdimu aliendelea kumfanyia vituko vya kimahaba mama Aidan ambaye aliendelea kupambana naye kwani hakuwa tayari kwa wakati ule kufanya kile Mdimu alichokusudia.
Baada ya kusumbuana kwa muda mrefu, hatimaye mama Aidan alifanikiwa kujitoa kwenye mikono ya Mdimu ambaye alionyesha kuwa hoi kutokana na kuelemewa na uchu wa penzi haramu.
“Sawa nimekuelewa, nipe muda nikajifikirie tena,” alisema mama Aidan huku akichukua mkoba wake na kuanza kuondoka. Kutokana na hali aliyokuwa nayo, Mdimu alishindwa kusimama na kumsindikiza, akamuacha aondoke mwenyewe mpaka nje ya hoteli hiyo ambapo alisimamisha teksi na kumuelekeza dereva sehemu ya kumpeleka.
Akiwa ndani ya teksi, mama Aidan alikuwa akitetemeka mwili mzima kutokana na kilichotokea. Hakuwahi kufikiria hata mara moja kama ipo siku anaweza kuingia kwenye mtego mkali kama huo wa kumsaliti mumewe.
Japokuwa ni kweli alikuwa amemkosea lakini mwenyewe alikuwa tayari kumsamehe na hakutaka kumlipizia kwa kumsaliti kama Mdimu alivyokuwa akimshawishi. Njia nzima alikuwa amejiinamia, machozi yakimtoka kutokana na ugumu uliokuwa mbele yake.
Kitisho alichokitoa Mdimu kwamba endapo atakataa kuwa na uhusiano naye wa siri basi ataifufua kesi iliyokuwa inamkabili mumewe ya kumbaka Caro, kilimkosesha amani kabisa, akabaki njia panda akiwa hajui kama akubali au akatae.
“Mama tumefika,” sauti ya dereva teksi ndiyo iliyomzindua kutoka kwenye lindi la mawazo, kwa kupitia vioo vya teksi aliyokuwa amepanda aliangalia pembeni na kugundua kuwa kumbe ni kweli tayari walikuwa wameshafika sehemu aliyomuelekeza dereva teksi.
Harakaharaka alifungua mkoba wake na kumlipa fedha zake kisha akashuka huku akijifuta machozi yaliyokuwa yameulowanisha uso wake. Taratibu akaanza kutembea kuelekea nyumbani kwake huku mawazo machungu yakiendelea kukisumbua kichwa chake.
Siku hiyo ilipita huku akiwa amekosa raha kabisa, mumewe na mwanaye Aidan walipomuuliza kilichomfanya akawa kwenye hali hiyo, aliwadanganya kwamba anaumwa sana kichwa. Akawaomba wamuache apumzike, ombi ambalo wote walikubaliana nalo.
Kamanda Mdimu aliendelea na kazi yake ya kumshawishi mama Aidan akubaliane na alichokuwa anakitaka, kila siku alikuwa akimpigia simu zaidi ya mara nne, asubuhi, mchana na jioni akimuulizia kuhusu majibu yake. Kila siku jibu la mama Aidan lilikuwa ni kumtaka aendelee kuwa na subira mpaka siku atakayokuwa anampeleka mwanaye Aidan shule.
Wiki moja ilipita, hatimaye tarehe ya kufunguliwa kwa shule aliyokuwa anasoma Aidan na Caro iliwadia, kama ilivyokuwa kawaida, wazazi wake walianza kumuandaa kwa ajili ya kwenda shule lakini uchangamfu wao haukuwa kama siku za nyuma. Kila mtu alikuwa akiwaza lake.
Kwa kipindi chote hicho, bado Aidan aliendelea kubaki gizani akiwa haelewi ni kitu gani kilichokuwa kinaendelea. Ule utaratibu ambao familia hizo mbili zilikuwa zimejiwekea wa kuwaandaa Caro na Aidan pamoja, safari hii haukuwepo tena, jambo lililozidi kumuumiza mvulana huyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lakini mama, kwa nini hamtaki kunieleza ukweli wa kile kilichotokea kati ya familia yetu na ya akina Caro? Siku hizi hataki kuonana na mimi, wazazi wake wamenikataza nisimfuate nyumbani kwao na sasa hata maandalizi ya kwenda shuleni kila mmoja anafanyiwa peke yake, kwani kuna nini?”
“Aidan, ipo siku utaufahamu ukweli lakini kwa sasa elekeza nguvu na akili zako kwenye masomo, haya mambo mengine achana nayo mwanangu,” alisema mama yake Aidan akionesha dhahiri kuficha siri kubwa ndani ya moyo wake.
Hatimaye siku ya kuondoka kwenda shuleni iliwadia, safari hii hakupelekwa na baba yake ambaye mara kwa mara ndiye aliyekuwa akiwapeleka na Caro na kuwafuata pindi shule zinapofungwa bali alipelekwa na mama yake.
Hata hivyo, ndani ya moyo wake alifurahi shule kufunguliwa kwani aliamini atapata muda wa kuwa jirani na Caro na pengine kuufahamu ukweli uliokuwa unamsumbua msichana huyo aliyetokea kumpenda tangu akiwa mdogo.
“Najua nikimbembeleza atakubali kuniambia ukweli wa kinachomsumbua na kwa nini wazazi wake wamenibadilikia ghafla wakati hakuna baya lolote nililolifanya,” aliwaza Aidan akiwa njiani kuelekea shuleni pamoja na mama yake.
Walipofika kwenye shule yao, mama yake alimpeleka mpaka kwenye jengo la utawala ambapo alimlipia michango yote muhimu iliyokuwa inatakiwa, akampa na fedha za matumizi kama ilivyokuwa kawaida kisha wakaagana.
“Zingatia niliyokwambia mwanangu, elekeza nguvu zako zote kwenye masomo, hayo mambo mengine tuachie tutayamaliza sisi wenyewe,” alisema mama yake Aidan, akamkumbatia mwanaye huyo kipenzi kisha wakaagana, akatoa siku yake na kuanza kuzungumza na mtu ambaye Aidan hakumjua.
Taratibu Aidan akawa anavuta begi lake kuelekea bwenini kwake huku akiwa na shauku kubwa ya kuonana na Caro kwani aliamini na yeye atawasili shuleni hapo siku hiyohiyo. Alipogeuka nyuma, alimuona mama yake akiishia kwenye geti huku akiendelea kuzungumza na simu.
Baada ya kufikisha mizigo yake bwenini, hakukaa sana, akarudi kwenye jengo la utawala kwa lengo la kumsubiri Caro ili akifika, ampokee kwa uchangamfu. Moyo wake bado ulikuwa na simanzi kubwa kwani tangu alipomtamkia Caro kuwa anampenda, mambo yalikuwa yakienda ndivyo sivyo huku akiwa hajui kosa lake ni nini.
Alikaa eneo la utawala kwa muda mrefu lakini hakumuona Caro zaidi ya wanafunzi wengine ambao walikuwa wakiletwa na wazazi wao. Aliendelea kusubiri kwa muda mrefu lakini mpaka giza linaingia, Caro hakuwa ametokea.
“Inawezekana leo wamechelewa labda kesho atakuja,” Aidan aalijifariji wakati akisimama pale alipokuwa amekaa kwa muda mrefu akimgoja Caro. Alirudi bwenini kwake ambapo siku hiyo hakupata usingizi akimfikiria Caro mpaka usiku wa manane.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kesho yake aliwahi kuamka na kwenda tena eneo la utawala kumsubiria Caro. Aliamini lazima siku hiyo atamuona kwani kesho yake ilikuwa ni Jumatatu, siku ambayo masomo yangeanza rasmi. Alikaa kwa muda mrefu eneo hilo lakini kama ilivyokuwa jana yake, aliendelea kuwaona wanafunzi wengine wakiwasili lakini miongoni mwao, Caro hakuwepo.
Alisubiri kwa muda mrefu lakini mpaka giza linaanza kuingia hakumuona Caro wala kivuli chake, jambo lililozidisha huzuni ndani ya moyo wake. Akapoteza hamu ya kufanya kila kitu. Hakutamani kula wala kujiandaa kwa ajili ya kuingia darasani siku iliyokuwa inafuatia, akawa ni mtu wa mawazo muda wote mpaka wenzake wakawa wanamshangaa kwani haikuwa kawaida yake.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment