Simulizi : Kwenye Siku Yangu Ya Kuzaliwa
Sehemu Ya Tano (5)
Chako ni chako tu hata kama kina kasoro. Mzee Kamugisha na mkewe walipopata taarifa ya kifo cha binti yao walipagawa! Hawakutaka kuamini kama kweli binti yao ambaye hawajamtia machoni kwa siku nenda rudi amefariki dunia kwa ajali ya gari, tena amefariki akiwa njiani kuelekea kwao kumtambulisha mchumba wake ambaye yuko mahututi hospitalini. Wangefanya nini wakati Mungu aliye mwamuzi wa kila jambo ameshapanga. Hawakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na ukweli kuwa binti yao Stella amefariki.
Maiti ya Stella yalifikishwa nyumbani kwao, kwa mzee Kamugisha na siku mbili baadaye akazikwa kwa heshima zote alizostahili kupewa kama mwana kwa wazazi wake. Mazishi yake yalihudhuliwa na mamia ya watu. Walikuwepo; ndugu, jamaa na marafiki, kadhalika pia majirani wa karibu na wa mbali walifika kumsindikiza kwenye makazi yake ya kudumu.
Ndugu wa Cosmas pia walifika kushudia safari ya mwisho ya mwenzi wa ndugu yao, ambaye mazishi ya kipenzi chake yalifanyika akiwa mahututi hospitalini. Kaburi la Stella likawekwa kibao kilichoandikwa; ‘Kwa kumbukumbu ya upendo ya Stella Kamugisha, tangu 1994 mpaka 2013.
Pindi moyo uliapo kwa kile ulichpoteza, roho hushangilia kwa kupata mwanzo mpya. Pumzika kwa amni; mwana, mchumba, ndugu na rafiki yetu mpendwa. Amina’
Miezi mitatu baadaye Cosmas alipona kabisa, licha ya kubaki na ulemavu uliomlazimisha kuchechemea pindi atembeapo.
Alipopona, Cosmas alijulishwa kuwa, Stella hayupo tena duniani. Alilia sana na mbingu zikalia pamoja naye kwa kunyeshea mvua kwenye uso wa dunia. Akaomba apelekwe mahali alipozikwa mpenzi wake, alipofika na kuliona kaburi la Stella, machozi yakaanza upya, akapiga magoti chini pembeni ya kaburi na kusema, “Hakika wewe ndiye uliyestahili kuwa mke wangu, kwa kuwa haikuwa kama tulivyopanga, basi nasema leo mbele ya kaburi lako; nafasi yako naibaki wazi daima moyoni mwangu mpaka tutakapounganishwa tena.” Alisema Cosmas kwa sauti na kuwaacha watu wote waliomsindikiza pale kaburini midomo wazi kwa kile alichokisema.
****
KUCHANGANYIKIWA huwa ni jambo linalotarajiwa hasa pale mtu anapoelemewa na msongo wa mawazo. Wakati ambao hamu ya chakula hupotea, ufanisi kazini hupotea kwa sababu ya mawazo yanayoweza kupelekea mtu kukata tama, na kuona hakuna tena sababu ya kuendelea. Jitihada za dhati zisipofanyika, basi jamii ihesabu kuwa haina chake tena.
Nywele ndefu zisizo matunzo, tena ambazo zimetimkatimka kana kwamba mwenye nazo hajui kama kuna chanuo duniani kwa ajili ya kuchania nywele ndefu, au wembe na hata mkasi kwa ajili ya kunyolea. Nywele hizo pamoja na ndevu na masharafa yaliyokaribia kuzoba mdomo yalimfanya Kiti aonekane kama kichaa!
Chupa kubwa ya Whisky aina ya ‘Jack Daniel’ ilikuwa pembeni yake. Ndani yake mlikuwa na pombe shinda, baada ya kuwa amekwishakunywa nyingine iliyokuwa katika chupa hiyo. Mkononi alikuwa ameshikilia picha ya mwanamke aliyempenda huku picha nyingine za mwanamke huyo zikiwa zimebandikwa ukutani. Karibu kila sehemu ya ukuta wa chumba chake kulikuwa na picha za Wayeka.
Lilikuwa ni jambo la kawaida sana kwake kupitisha siku bila kuzungumza neno lolote, huku macho yake akiwa ameyaelekeza kwenye moja ya picha za wayeka zilizokuwa chumbani mwake. Ndugu zake walijaribu kuziondoa picha hizo kwa kudhani kuwa labda kwa kufanya hivyo wangeweza kumrejesha ndugu yao katika hali yake ya kawaida aliyokuwa nayo awali. Walipojaribu tu kugusa moja kati ya picha hizo Kiti aligeuka mbogo!
Matobera ambaye ni mama yake alikwishakata tamaa kabisa, alijua mwanye ndiyo amekwishachanganyikiwa na hakuna tena jinsi, isipokuwa kumwachia Mungu tu, kwani ndiye hupanga kila kitu. Sina hakika kama alifahamu kuwa, Mungu kupitia manabii wake alisema; abishae kwa dhati atafunguliwa.
Wakati ambao Matobera alikuwa amekata tamaa, mzee Ngomanzito hakutaka kabisa kukubali kuwa ameshindwa kumuokoa mwanaye. Alishawatafuta wanasaikolojia mbalimbali na hata kuwapeleka chumbani kwa Kiti ili angalau wamsaidie kumrejesha mwanaye katika hali ya kawaida, lakini waligonga mwamba! Alishawapeleka wachungaji mashuhuri ili nao waende wakamwombee mwanaye, nao wakaishia kugonga mwamba.
Jambo moja tu, ambalo hakuthubutu kufanya, nalo ni kwenda kwa waganga wa kienyeji. Hakuthubutu kuwafikiria kwa sababu imani yake haiwapi nafasi watu hao na kazi zao. Licha ya kujifunza kwenye falsafa ya kiafrika kuwa; waafrika wana nguvu uhai ambayo ikitumika kudhuru huitwa uchawi lakini ikitumika kutibu huitwa uganga. Hakuthubutu kuwapa nafasi kwa sababu; kwake uchawi na uganga ni ushirikina, na ushirikina kwake haukua nafasi.
Mzee Ngomanzito akaanza kukesha kwenye chumba chake cha kujisomea kilichopo nyumbani kwake akijaribu kusoma maandishi mbalimbali yahusuyo saikolojia na ushauri. Huko akakutana na wananadharia mbalimbali wakiwemo: Sigmund Freud na nadharia yake ya ‘Udodosi Nafsi’, akakutana pia na wakina; Victor Frank na nadharia yao ya ‘Kuwako’. Katika kuzisoma nadharia hizi, mzee Ngomanzito alikuwa kama vile anazungumza na wananadharia hao ana kwa ana!
Kwenye nadharia ya ‘Udodosi Nafsi’ alipata kujua kuwa Sigmund anasema: binadamu ana nafsi tatu ambazo hana utambuzi nazo. Nafsi hizo ambazo humkamilisha mtu ni; Idi ambayo ni nafsi ya kibaiolojia, inayotawaliwa na na tabia za ubinafsi na hamasa ya kupunguza au kuondoa maumivu. Katika nafsi hii huwa hakuna mjadala wala nafasi ya kufikiri. Hapa mtu hutenda anayotenda kwa sababu ya msukumo wa ubinafsi uliomo ndani yake. Nafsi hii ndiyo humsukuma mtu kutenda matendo ya ajabu kama vile kubaka, kuua na kadharika.
Nafsi ya pili ni Ego, ambayo ni nafsi ya kisaikolojia inayojaribu kuhusianisha Idi na uhalisia. Katika nafsi hii angalau kuna chembechembe za fikra na mjadala. Hivyo mtu anapoamua kutenda jambo hujaribu kufikiri kabla ya kutenda.
Nafsi ya tatu ni Super-ego, hii ni nafsi ya kijamii ambayo ni nfsi amuzi. Huamua kati ya Idi na Ego kwa kuzingatia maadili, utamaduni na misingi ya jamii. Nafsi hii ndiyo humfanya mtu kuwa na aibu au kutofanya jambo fulani kwa sababu ni kinyume na kanuni na taratibu za jamii fulani.
Nafsi hizi tatu hufanya kazi ndani ya mtu bila ya mtu mwenyewe kujitambua, ila mtazamaji, yaani yule anayemwona mtendaji ndiye hujua ni nafsi ipi inamsukuma mtu kufanya afanyayo.
Katika nadharia ya ‘Kuwako’ bwana Victor Frank na Rollo May wanasema: kila binadamu anao uwezo wa kujitambua binafsi, hivyo mtu anakuwa kwenye matatizo kwa sababu ameshindwa kujitambua binafsi.
Wakaenda mbali na kusema kuwa; kila binadamu anapambana ili kutambulika na wakati huo huo kuhusiana ama kushirikiana na wenzake. Pia wakaongeza kwa kusema: kila binadamu anapambana katika maisha ili kupata umuhimu na maana ya uwepo wake. Hivyo watu hukumbana na matatizo kwa sababu wamepoteza maana ya maisha yao.
Mzee Ngomanzito alisoma barabara nadharia hizo, akaelewa namna zinavyofanya kazi katika kushauri na hatua anazopaswa kuzifuata katika kutoa ushauri, hasa pale atakaohitaji kuzitumia nadharia hizi.
Kwa kuhusianisha hali ya Kiti na nadharia alizosoma, mzee Ngomanzito alihisi kuwa, yawezekana Kiti hajui alitendalo kwa sababu nafsi inayomwongoza ni Idi, na amepoteza maana ya maisha yake ndiyo maana yuko jinsi alivyo.
Siku moja aliingia chumbani kwa Kiti majira ya saa nane mchana. Alimkuta Kiti akiwa amekaa chini kwa kuegemea ukuta kwa mgongo huku miguu yake akiwa amekunja kwa kuelekeza magoti juu darini, na kama ilivyo kawaida yake, mkononi alikuwa na picha ya Wayeka ameilekezea macho kama vile anazungumza nayo.
Mzee Ngomanzito alikua amevaa suruali ya kaki ya kitambaa chepesi na fulana nyeupe nyepesi. Alipiga hatua za taratibu mpaka pale alipokaa mwanae, akatoa picha mfukoni kisha naye akakaa katika mkao uleule aliokaa mwanae, wakawa wameuelekea mlango. Alimtazama mwanaye kwa jicho la udadisi, mwanaye naye akamtazama, wakawa wanatazamana kabla mzee Ngomanzito hajafungua kinywa na kusema, “Utapendelea kunywa chochote kwa sasa?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo, whisky yoyote itafaa,” alisema Kiti kwa sauti dhaifu kabisa.
Mzee Ngomanzito hakushtushwa na kauli ya ya Kiti kwa sababu aliitarajia, alimtazama kwa muda kidogo kisha akaigeukia picha iliyokuwa mkononi akasema, “Vipi kama itaanza glasi ya maji halafu ndiyo ije whisky uipendayo?”
Safari hii Kiti hakujibu kitu, alikaa kimya huku akiitazama picha yake kana kwamba hakusikia kilichosemwa na baba yake.
“Mi’ nafikiri mama alete kwanza maji halafu baadaye whisky, tena nafikiri badala ya whisky angetuletea Konyagi ambayo ni pombe ya Kitanzania au vipi?” mzee Ngomanzito alisema.
“Mi nadhani konyagi ni nzuri zaidi,” aliongeza.
“Sawa, ije na kipande cha limao,” Kiti alisema na kumfanya baba yake atabasamu. Aliichukua simu yake kutoka mfukoni akaibonyezabonyeza kisha akaiweka kando.
Punde tu, mama Kiti aliiingia na jagi la maji pamoja na glasi mbili, alipolifikisha walipokaa Ngomanzito na Kiti alimimina maji kwenye bilauli alizokuja nazo kisha akaondoka. Mara tu baada ya mama Kiti kuondoka mule ndani, mzee Ngomanzito alimgeukia mwanaye, “Umemuona huyo mama aliyetoka humu ndani…” alisita kidogo akachukua bilauli ya maji akapiga funda moja kubwa kisha akirudisha bilauli yake chini akaeendelea, “kuna wakati maishani aliwahi kuwa binti. wakati huo mimi ni kijana hasa, tena mtanashati kweli…” alinyamaza akamtazama mwanaye ambaye alikuwa kimya akimsikiliza akamwambia, “Drink some water please..”
Kiti hakufanya kama alivyoambiwa na baba yake.
“Any way, tuendelee..” alisema Ngomanzito halafu akaisogeza ile picha karibu na uso wa Kiti huku akisema, “Huyu ni mama yako enzi zake. Kwanza baba yake alikuwa alikuwa mchungu… akikuona nyumbani kwake anawaita mbwa wake, alikuwa nao kama sita hivi. Babu yako alikuwa mkorofi sana enzi hizo,” alisema mzee Ngomanzito huku akirudisha mkono wake wenye picha.
“Hebu niambie… huyu ukutani ndiye mama watoto wako siku zijazo?”
Kiti alitazama ukutani zilipo picha kisha akasema, “Ndiyo,”
“Anastahili. Lakini naona kama humaanishi kile ukisemacho”
“Namaanisha baba, ni yeye.” Kiti alijitetea.
Mzee Ngomanzito aliichukua bilauli ya maji akanywa kiasi kabla hajasema, “Hapana, hauko serious,”
“Niko serious baba,”
“Mtu ambaye yuko serious hupambana kuhakikisha anakitia himayani chochote anachokitaka, tena kwa gharama yoyote ile. Sasa kwa kukaa tu ndani unadhani utampataje huyo mama watoto wako?”
Kiti alikaa kimya kwa muda kiasi huku akitafakari, kabla hajajua nini cha kusema alimsikia tena baba yake, “Ni kweli unamhitaji?” Mzee Ngomanzito aliuliza.
“Ndiyo baba namhitaji,” Kiti alijibu.
“Kama kweli unamhitaji, hebu kunywa hayo maji,”
Kiti aliinyanyua bilauli ya maji akainywa harakaharaka, yalipoisha aliongeza tena mengine. Wakati anamalizia bilauli ya pili ya maji aliisikia tena sauti ya baba yake, “Haya sasa fumba macho yako halafu uniambie unaona nini,”
Bila hiyana wala ubishi Kiti alifumba macho kwa muda wa takribani dakika tano. Alipoyafumbua tu, Kiti alishangazwa na hali aliyoikuta mule chumbani mara baada ya kuyafumbua macho yake, baba yake, mzee Ngomanzito hakuwemo chumbani mule. Pembeni yake kulikuwa na lile jagi la maji pamoja na bilauli mbili ambazo, moja ilitumiwa na baba yake na nyingine alikuwa akitumia yeye.
Kiti alinyanyuka kutoka pale chini alipokuwa, akauelekea mlango na kuufungua kwa lengo la kwenda sebuleni kumtafuta baba yake ili amweleze alichokiona. Alipofika sebuleni, Kiti hakumkuta baba yake. Ikambidi aende mpaka nje ambako alimkuta baba yake akiwa ndani ya gari tayari kwa kuondoka.
“Babaa babaa..” Kiti alipaza sauti ambayo ilimfikia baba yake aliyekuwa akimtazama kupitia kioo cha pembeni cha gari ‘Side mirror’
“Yes son,” aliitika mzee Ngomanzito na wakati huo Kiti alikuwa tayari ameshafika mahali ilipokuwa gari alimokuwemo baba yake.
“I saw my future with her,” Kiti alisema huku akihema kwa kasi.
Baba yake alimtazama mwanaye kwa muda kidogo, kisha akashusha pumzi ndefu kutoka kifuani mwake halafu akasema, “Unafikiri hiyo future itakukuta ukiwa chumbani umekaa?”
Lilikuwa ni swali ambalo Kiti hakulitegemea katika wakati huo. Swali hilo likawa kama vile limemzindua Kiti kutoka kwenye usingizi mzito, kabla hajajua nini cha kujibu, sauti ya baba yake ilipasua tena ngoma za masikio yake kwa mara nyingine, “Hebu jitazame kwenye kioo uone kama kweli wewe ndiye Kiti, mtoto mkubwa wa kiume wa familia hii. Mtoto ambaye mara tu baada ya kuzaliwa tulijawa na matumaini juu yako, kwamba; kesho na keshokutwa uwasimamie wadogo zako pindi tutakapokuwa hatupo,” alisita kidogo na kumtizama Kiti ambaye bado alikuwa amekodoa macho yake kuelekea kwenye kioo cha pembeni cha gari alimokuwa baba yake.
Kiti aliishuhudia taswira yake pale kwenye kioo ikiwa katika hali ya kutisha, nywele ndefu zilizo timtimu pamoja na ndevu na masharafa yaliyokaribia kuufunika mdomo wake. Akainyanyua mikono yake na kuishika ile midevu huku akiwa kama asiyeamini kwa kile anachokiona kupitia kioo cha pembeni cha gari.
“Ni wewe wa kuchanganyikiwa kwa sababu ya mapenzi? Unaihangaisha akili yako kufikiri juu ya mtu ambaye hujui kama umo akilini mwake!” alilalamika mzee Ngomanzito kwa sauti iliyojaa uchungu uliodhihirika kwa machozi yaliyokuwa yakimtoka. Alimtazama mwanaye ambaye sasa alikuwa analia baada ya kuchomwa na ukali wa maneno ya baba yake. Mzee Ngomanzito alipangusa machozi mashavuni mwake huku maneno mazito yakiendelea kumtoka, “Siku uliyozaliwa nilifurahi sana, nilijua nimepata mtoto wa kiume wa kujivunia, ambaye ataendeleza jina langu hata baada ya siku za uwepo wangu duniani, kumbe nilijidanganya kwa kuweka matumaini yangu kwa mtumwa wa mapenzi. Mapenzi yamekuchanganya Kiti… kwani wanawake wapo wangapi dunia hii mpaka uchanganyikiwe na huyo Wayeka?” mzee Ngomanzito aliendelea kusema kwa uchungu.
“Nisamehe baba, nisamehe...” Kiti alilia baada ya kubaini ukweli uliowazi kwenye maneno ya baba yake.
****
Baada ya kuona amesalitiwa hakuiona tena raha ya mapenzi, kwake mapenzi yaligeuka shubiri yenye uchungu wa kuukarahisha moyo. Angependaje tena ikiwa dunia imejaa wasaliti wasiojali thamani ya upendo wanaotunukiwa? Wayeka akaapa kutopenda tena maishani, akawachukia wanaume kwa kuwaona wote ni walaghai isipokuwa mmoja tu, naye ni baba yake, mzee Ayuyube. Kwake yeye mwanamke mwenye bahati alikua ni mama yake, kwa sababu yuko na baba yake ambaye si laghai.
Wayeka akayasahau mambo ya mapenzi na kuelekeza akili yake kwenye kazi, akachapa kazi kwa bidii na maarifa yote. Hatimaye akayaona matunda ya bidii yake kupitia mafanikio aliyoyapata.
Kwa sababu uzuri wake haukupotea, wanaume wakware hawakusita kumzengea. Walimfuata na kumpa maneno kwa lengo la kumshawishi wawe naye, lakini hawakufua dafu. Kwake wote hawakuwa tofauti na Kitiheka, mwanaume fedhuri ambaye alimfananisha na vinyesi vya watu wote wa dunia hii.
Wayeka aliichuma pesa kupitia biashara zake kama mzabuni wa wilaya za; Butiama, Musoma mjini na vijijini na hata Rorya. Japo haikuwa pesa ya kumfanya ajiite mwenye pesa miongoni mwa wenye pesa, lakini pesa aliyoipata ilitosha kumtia kiburi dhidi ya wanaume waliomfuata kumtongoza.
Alisahau jambo moja ambalo alipaswa kulikumbuka wakati wote, Wayeka alipaswa kukumbuka kwamba: jua huzama na kuchomoza tena siku inayofuata, na kila linapochomoza huashiria mwanzo wa siku mpya. Na katika siku mpya mambo mapya hutarajiwa.
13http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
EMMY alinyanyua bilauli iliyokuwa na shurubati ndani yake, huku macho yake akiwa ameyaelekeza kwa Wayeka. Baada ya kuridhika na kiwango cha shurubati alichokunywa, Emmy alisema, “Najua inaweza isiwe rahisi kuniamini ila naomba tu uelewe kuwa mazingira yalimlazimisha,”
“Hapana Emmy, Kiti ni muhuni. Labda tu wewe huwajui wanaume. Mnaweza mkapangwa hata wanawake sita bila kujua.. ila ukweli huwa haufichwi daima.” Alisema Wayeka.
“Siyo kama namtetea ili wewe na yeye mrudiane, hapana, mimi najaribu kuweka mambo sawa ili uelewe kuwa; Kiti anakupenda na ndiyo maana hata baada ya hali ile kutokea alichanganyikiwa kabisa.”
“Kwani ni nani asiyejua kuwa nilimpenda
Kiti na kujikabidhi kwake ili anifanye atakavyo? Yeye akaona kunichanganya na Mina ndiyo jambo lililonifaa zaidi. Kwa ufupi shosti moyo wangu hauko tayari kupenda tena,”
Emmy aliyasikia vema maneno ya Wayeka, akayachekecha na kuyapima. Lakini hakuwa ameridhishwa na msimamo wa shoga yake. Alifikiria juu ya mpango wake na Bony, mpango wa kuwakutanisha Kiti na Wayeka mahali hapo ili wazungumze na kuzimaliza kabisa tofauti zao. Emmy alipoyarejea tena maneno ya Wayeka, matumaini ya kufanikisha kile walichokipanga na mumewe yalizidi kupungua kadiri muda ulivyozidi kwenda. Alimgeukia Wayeka ambaye alikuwa anamalizia kuweka bilauli yake ya shurubati juu ya meza baada ya kuwa amekunywa mafunda kadhaa ya shurubati kutoka kwenye bilauli ile.
“Kwa hiyo hutaki hata kukutana naye?” Emmy aliuliza.
Wayeka alishikwa na kigugumizi cha ghafla, “Hapana, Si kama sitaki kukutana naye, ila siyo kwa sasa,”
Kauli ya Wayeka ilimpa wakati mgumu Emmy ambaye alizidi kuchanganyikiwa kwa sababu alijua kuwa Kiti na Bony wako njiani kuelekea mahali walipo wao, yaani yeye na Wayeka. Emmy alishindwa kuendelea kulihifadhi jambo hilo kifuani kwake, pasipo kutarajia alijikuta akisema, “Kiti na Bony wako njiani wanakuja.”
“Eee..” sauti ilimtoka Wayeka kwa mshangao wa hali ya juu. Ghafla Wayeka alisimama na kuchukua mkoba wake uliokuwa juu ya meza na kuanza kuondoka huku akisema, “I’m sory Emmy, siwezi kukutana na huyo mwanaharamu,”
“Unakosea Wayeka,” alisema Emmy.
Kama vile hakujali au kusikia alichosema Emmy, Wayeka alizidi kupiga hatua kulielekea gari lake ambalo lilikuwa mita chache kutoka mahali walipokuwa. Wayeka alifika kwenye gari lake aina ya Jeep Cherokee, lenye rangi nyeusi na kuuinamia mlango ili afungue.
Emmy aliyekuwa hatua chache nyuma yake, akimfuata kujaribu kumsihi asiondoke, alimshuhudia Wayeka akiinama chini huku mkono wake wa kulia ukiwa umeshikilia tumboni, na ule wa kushoto ukijaribu kugusa bodi ya gari bila mafanikio. Ni kama alikuwa akijaribu kuiokoa ili asinguke kwa kujaribu kushika kwenye gari.
Emmy alijikuta akikimbia kuelekea mahali alipoanguka Wayeka huku akipaza sauti kuomba msaada, “Nisaidiee..”
****
Ilibaki umbali wa kilomita kama mbili hivi kufika eneo ambalo Emmy akiwa na Wayeka alikuwa akiwasubiri Bony na Kiti. Kama ilivyokuwa kwa Wayeka, Kiti naye hakuwa na utambuzi juu ya ajenda ya siri iliyokuwa imepangwa na Bony na Emmy, ajenda ya kuwakutanisha kwa lengo la kuwasuluhisha na kulimaliza tatizo lililopo baina yao.
Walikuwa kwenye gari ambalo Bony aliendesha kwa sababu yeye ndiye aliyejua mahali walipokuwa wanaelekea. Wakiwa hawana hili wala lile, wakisikiliza kibao cha ‘Mwanayumba’ kilichoimbwa na mwanamuziki anayefahamika kwa jina la Chege, simu ya Bony ikaita.
Bony aliichukua simu kwa mkono wake wa kushoto na kuiweka sikioni huku ule wa kulia ukiwa umekumbatia uskani. Kwa macho alimuashria Kiti kupunguza sauti ya redio ili aweze kuongea na simu. Simu aliyopokea ilimbadilisha Bony ghafla, mabadiriko ambayo hata Kiti aliweza kuyabaini, lakini kabla hata hajapata nafasi ya kumwuliza kuna tatizo gani, ghala Kiti alimshuhudia Bony akibadili uelekeo wa gari kutoka kule walikokuwa wanaelekea na kurudi walikokuwa wanatoka.
“Is every thing alright man?” hatimaye Kiti aliuliza.
“Hapana bro.. kuna shida,” Bony alijibu huku akizidi kuichochea gari moto.
Dakika tano baaadaye walikuwa kwenye hospitali ya Manyamanyama ambayo ndiyo hospitali teule ya wilaya ya Bunda. Hospitalini walilakiwa na Emmy ambaye alikuwa ni kama amechanganyikiwa. Miguuni Emmy alikuwa peku, hakuwa na viatu huku machozi yaliyokuwa yakimtiririka yakiharibu vipodozi ambavyo awali viliunakshi uso wake.
“Ilikuwaje?” lilikuwa ni swali ambalo Bony alimuuliza Emmy mara baada ya kuwa wanefika hospitalini pale.
“Mi sijui nilimuona tu anaanguka,” alisema Emmy huku akitangulia kuongoza njia kuelekea kwenye chumba alimoingizwa Wayeka.
“Wayeka!” sauti ilimtoka Bony na kusababisha mshtuko kwa Kiti.
“Wayeka amekuwaje?” Kiti aliuliza lakini hakuna aliyemjibu.
Kabla hawajafika kwenye mlango wa chumba alimoingizwa Wayeka, mlango ulifunguliwa, akatoka daktari akiwa ameshikilia jalada mkononi.
Yule daktari alimtambua Emmy kuwa ndiye aliyemleta mgonjwa, hakupoteza muda, aliwaita pembeni na kuwaeleza, “Mgonjwa wako ana tatizo ambalo linahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo. Utumbo wake umejikunja, na tatizo hilo kitaalamu tunaliita ‘Intestinal obstruction’ tunahitaji damu haraka ili tumfanyie upasuaji kuyaokoa maisha yake.
Wote walipigwa na butwaa baada ya kuyasikia maelezo ya daktari, hawakutarajia wala kudhani kuwa tatizo linaweza kuwa kubwa kiasi hiyo, tatizo ambalo linahitaji upasuaji.
“Kwenye benki yetu ya damu tumeishiwa kabisa. Hivyo kama inawezekana apatikane mtu mwenye damu ya kundi ‘O’ ambalo ndilo kundi lake tumfanyie upasuaji haraka.
“Mimi nina group ‘O’,” Kiti alisema, na kwa haraka daktari akasema, “Kama una group ‘O’ tafadhali naomba unifuate,” alisema daktari na kuanza kuondoka huku Kiti akimfuata.
****
****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jopo la madaktari walio katika sare za kazi zenye rangi ya kijani tangu; kofia, kitambaa maalum kilichofunika midomo yao, pamoja na makoti walikuwa wamezunguka kitanda alicholazwa Wayeka akifanyiwa upasuaji. Punde mmoja wao, ambaye bila shaka alikuwa ndiye kiongozi wao na ndiye yuleyule aliyeondoka na Kiti na kuwaacha Bony na Emmy nje alishusha chini, kuelekea shingoni kile kitambaa ambacho kilikuwa kimefunika mdomo wake na kusema, “No deterioration occurred.”
Ghafla wale madktari waliokuwa wamekizunguka kitanda cha upasuaji alicholazwa Wayeka, walinyanyua mikono yao juu na kupiga makofi kwa furaha huku wakipongezana kwa kukumbatiana na kushikana mikono. Dakika chache baadaye, mlango wa chumba cha upasuaji ulifunguliwa na kufuatiwa na muuguzi aliyekuwa akisukuma kitanda kuelekea wodini.
Walipoona kitanda kinasukumwa kutoka kwenye chumba cha upasuaji, wote walisimama, Bony, Kiti, Emmy, mzee Ayuyube na mkewe, walisimama kwa lengo la kujua hali ya mgonjwa wao aliyekuwa akisukumwa kwenye kitanda huku akiwa amefunikwa mashuka meupe yaliyoandikwa ‘Afya’.
Kwa muonekano wote walionekana kuwa na hamu ya kutaka kujua maendeleo ya mgonjwa wao ambaye hawakuwa na taarifa zake tangu alipoingizwa mule chumbani kwa lengo la kufanyiwa upasuaji, kurekebisha utumbo ambao ulikuwa umejikunja.
Wasiwasi zaidi uliugubika moyo wa mama yake na Wayeka ambaye alikuwa akitokwa na machozi muda wote tangu alipofika hospitalini pale baada ya kuwa amejulishwa na Emmy juu ya hali ya mwanaye. Walipotaka kumfuata yule muuguzi aliyekuwa akisukuma kitanda alicholazwa Wayeka, alikuja muuguzi mwingine ambaye alitokea chumbani mule alimotolewa Wayeka na kuwaambia, “Hali ya ndugu yenu inaendelea vizuri baada ya kuwa tumefanikiwa kumfanyia uapasuaji bila shida yoyote,”
Tarifa hiyo ya muuguzi ilifufua matumaini yao. Angalau sasa walishusha jakamoyo ambalo lilikuwa limewaweka kwenye taharuki ya hali ya juu. Wakiwa bado wanashukuru kwa muumba wao kwa kuwezesha ndugu yao kutoka kwenye chumba cha upasuaji akiwa salama salmini, sauti ya muuguzi yule ilisikika tena ikipasua anga, “Naomba mmoja kati yenu ambaye atakuwa karibu na mgonjwa kwa wakati wote atakaokuwa hapa akisubiri kupata fahamu na kuruhusiwa, anifuate.”
Walitazamana kwa zamu usoni kabla mama yake Wayeka hajapiga hatua moja mbele kuashiria kuwa yeye ndiye atakayekuwa karibu na bintiye kwa wakati wote atakaokuwa hapo hospitalini.
“Wengine naomba mtusubiri hapa, tutawajulisha kila kitakachokuwa kinaendelea na mtakuwa huru kumuona ndugu yenu kwenye muda ambao mtaruhusiwa,” aliongeza muuguzi kisha akaondoka na mama Wayeka.
****
Muda mfupi baadaye, Kiti alikuwa nyumbani kwao sebuleni, alikuwa amekaa kwenye kochi lililokuwa sebuleni pale kwa kuegemea huku akionekana dhahiri kuwa yupo kwenye lindi la mawazo.
Mara baada ya kurejea kwenye hali yake ya kawaida kutoka kwenye msongo wa mawazo ambao almanusra umsababishie uchizi kwa sababu ya sintofahamu iliyotokea baina yake na Wayeka. Kiti aliamua kuachana kabisa na Wayeka, japo halikuwa jambo rahisi, aliamua kuyaanza maisha mapya bila Wayeka kwa lengo la kuendeleza mipango yake ya kimaisha ambayo ilikuwa imesimama kwa sababu ya matatizo ya kiakili yaliyokuwa yakimkabili.
Miongoni mwa mambo aliyokuwa akiyashughurikia, ilikuwa ni biashara yake ya kimataifa ambayo alikuwa akiiota tangu akiwa masomoni. Biashara yake hiyo ilikuwa mbioni kuingia katika utekelezaji kwa sababu; miundombinu yote ya uendeshaji wa biashara hiyo ilikuwa imekamilika. Jambo pekee lililokuwa likisubiriwa ni tarehe ya kuanza biashara ifike.
Kwenye kochi pale Kiti alikuwa akiwaza juu ya Wayeka, kwanza; alimhurumia kwa sababu ya matatizo yanayomkabili, matatizo ambayo yamesababisha afanyiwe upasuaji na hatimaye kulazwa. Huruma aliyokuwa nayo Kiti kwa Wayeka ilisababisha kuibuka kwa jambo la pili, jambo ambalo siku chache zilizopita lilimuweka ndani akiwa kama mwehu, mapenzi! Kwa mara nyingine tena Kiti alihisi kuhitaji kuwa karibu na Wayeka, alihitaji kuwa karibu naye ili kumfariji katika kipindi chote ambacho atakuwa anaumwa.
Hakuna jingine lililomsukuma Kiti kufikiri hivyo isipokuwa hisia kali za mapenzi kwa Wayeka, hisia ambazo zilianza kujiunda upya akilini mwake na kutuama kwenye vilindi vya moyo wake. Wayeka ambaye alianza kusahaulika akilini mwa kiti, sasa alianza kurejea taratibu!
Akiwa mawazoni, Kiti alishtuliwa na sauti ya mtu aliyeingia sebuleni, “Habari za hapa?” mzee Ngomanzito alisalimia mara baada ya kuwa ameingia sebuleni mule akitokea kwenye mizunguko yake ya kawaida ya kila siku.
“Salama baba, shikamoo?” Kiti alisalimia.
“Marahaba,” alijibu Ngomanzito huku akichapua hatua kuelekea ndani zaidi.
“Anaumwa na nimemtolea damu,”
Mzee Ngomanzito alisimama ghafla mara baada ya kumsikia Kiti akisema maneno hayo.
“Nani anaumwa?” aliuliza Ngomanzito.
“Wayeka, ilihitajika damu ili afanyiwe operation,”
“Oh my God, anaumwa nini?”
“Wanasema utumbo ulijikunja,”
Mzee Ngomanzito alishtuka na kusababisha koti alilokuwa amening’iniza mkononi mwake kudondoka.
“Utumbo ulijikunja?” mzee Ngomanziti alizidi kuuliza kwa mshangao.
“Ndiyo, ila cha kushukuru ni kuwa operation ilifanyika salama.”
“Kwa hiyo anaendeleaje?”
“Daktari amesema anaendelea vizuri tu,”
Kimya cha sekunde kadhaa kilijiunda na baadaye kuvunjwa na mzee Ngomanzito ambaye tayari alikwishakaa kwenye kochi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umefanya jambo jema sana kutoa damu, umeoka maisha,” alisema Ngomanzito.
Zilipita siku mbili tangu Wayeka afanyiwe upasuaji. Ukiitoa siku ambayo Kiti alikuwepo hospitalini na kutolewa damu ili kufanikisha zoezi la upasuaji, Kiti hakuwa amekwenda tena hospitali. Hakupiga hata simu kuulizia hali ya mgonjwa. Siku hiyo Kiti alikuwa amekaa kwenye bustani ndogo iliyopo nyumbani kwao akisoma riwaya ya ‘Wivu’ iliyoandikwa na mzee Beka Mfaume.
Kiti alishtushwa ghafla na ugeni uliofika nyumbani kwao siku hiyo, ulikuwa ni ugeni ambao hakuutarajia kabisa. Kwenye ugeni huo alikuwepo Emmy, uwepo wa Emmy nyumbani kwao haukumpa shida hata kidogo, kwa sababu; halikuwa jambo la ajabu kwa yeye kwenda kwao na Kiti. Alishawahi kwenda kwa kina Kiti mara zisizo idadi. Kuna wakati alikwenda akiwa na Bony na mara nyingine alifika akiwa peke yake.
Kilichomshtua kiti ni mgeni ambaye alikuja na Emmy, mgeni ambaye alisababisha umakini wa Kiti upotee kwa sekunde kadhaa kabla haujarejea tena. Mgeni huyo alikuwa ni mama yake na Wayeka ambaye macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba. Hapana shaka hali hiyo ilisababishwa na kulia kwa muda mrefu.
Ni nini kilimfanya alie huku upasuaji wa mwanaye ulifanikiwa bila shida? au mwanaye amepatwa na shida gani tena? Hali aliyokuwa nayo mama yake na Wayeka ilimfanya Kiti apatwe na wasiwasi, “Wayeka amekufa?” Kiti aliwaza.
Kabla hajajua sababu ya ugeni ule wa ghafla na hali aliyokuwa nayo mama yake na Wayeka, Kiti alishtuliwa na sauti ya Emmy.
“Anakuhitaji,” Emmy alisema huku machozi yakianza kumlengalenga.
“Anaendeleaje lakini?” Kiti aliuliza.
Angalau sasa wasiwasi aliokuwa nao kiti ukaanzakupungua, japo utitiri wa maswali uliendelea kumzidia kichwani.
“Kama Wayeka anaendelea vizuri kwa nini wanalia?”
“Tafadhali mwanangu, mwenzio anakuhitaji. Amegoma kula mpaka atakapokutia machoni, hataki kula wala kunywa dawa mpaka atakapokuona. Tafadhali naomba twende hospitali ukamuone mwenzio,”
14
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MARA baada ya kuwa ameruhusiwa kutoka hospitalini, Wayeka alirudi nyumbani ambako alikaa mpaka alipopona kabisa. Nyumabni alitembelewa na marafiki wa kila aina, ambao walifika kumjulia hali. Kwake yeye, hata kama wasingekuja wote ila akaja Kiti tu, moyo wake ungefarijika. Lakini tangu alipotoka hospitalini Wayeka hakuwahi kumtia Kiti machoni. Mara ya mwisho kumuona Kiti ilikuwa ni siku ambayo, Kiti alifuatwa nyumbani kwao na Emmy pamoja na mama yake.
Alitamani aonane naye ili amshukuru kwa kukoa maisha yake kwa kumtolea damu ambayo ilihitajika ili afanyiwe upasuaji. Alimtafuta Kiti kwa simu yake ya mkononi, lakini Kiti hakupatikana kwa mara zote alizothubutu kumpigia. Akaamua ampigie Bony ili amuulize kama Kiti amebadili namba yake ya simu ya mkononi au bado anatumia ileile ya zamani ambayo yeye ameshaipiga kwa mara zisizo idadi bila kumpata.
Alipompigia Bony, Bony alimueleza kuwa Kiti alibadili namba ya simu tangu alipopona matatizo yake ya akili ambayo yalimhangaisha kwa muda mrefu. Hisia kuwa Kiti amebadili namba yake ya simu kwa sababu yake zikaanza kuivuruga akili ya Wayeka. Akaanza kufikiri kuwa yawezekana kiti hataki kabisa mawasiliano naye, ndiyo maana ameamua kubadili namba ya simu. Na kama hataki mawasiliano naye sasa itakuwaje? Ina maana ndiyo hataki hata kumuona?
Wayeka akaomba namba mpya ambayo Kiti alikuwa akiitumia kwa wakati huo. Bila hiyana na kwa moyo mkunjufu Bony alimpatia Wayeka namba mpya ya simu ya Kiti.
Wayeka aliipiga simu hiyo, ikawa inaita tu bila kupokelewa, na mara nyingine alipoipiga aliambiwa inatumika. Alilirudia zoeizi hilo kwa zaidi ya siku moja lakini bado simu ya Kiti haikupokelewa. Mawazo juu ya mawazo yakaendelea kuitesa akili ya Wayeka.
Tangu atoke hospitalini Wayeka hakuwahi kwenda kazini licha ya kuambiwa na daktari kuwa amepona kabisa na anaweza kufanya kazi yoyote isipokuwa zile za suluba.
Wayeka akawa hatoki nje, akawa ni mtu wa kushinda ndani muda wote akimlilia Kiti. Ulaji wake pia ukawa wa shida kwa sababu ya mawazo na kilio kwa sababu ya Kiti. Afya yake ikaanza kudhoofika kwa sababu kukonda, hata uzuri wake ukaanza kutoweka kabisa na kuzua hofu kwa ndugu zake kuwa yawezekana ikafikia hatua ya ndugu yao kujiua kwa sababu ya mawazo yanayomsibu. Mawazo juu ya mtu ambaye kwa mujibu wa fikra zao, mtu huyo hakuwa kabisa na habari na Wayeka.
Ili kumnusuru na balaa lililokuwa mbele yake, marafiki wa Wayeka wakaitwa kwa lengo la kumshauri ili angalau wamrudishe kwenye hali yake ya kawaida. Miongoni mwa marafiki ambao walitarajiwa kuwa msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya Wayeka ni pamoja na Bony na mkewe, Emmy ambao baada ya ushauri wao kwa Wayeka kutozaa matunda waliamua kuugeukia upande wa pili wa shilingi.
Siku moja asubuhi na mapema, yapata majira ya saa 10:05, Bony na Emmy walifika nyumbani kwa Kiti, kwenye nyumba yake ndogo aliyopewa na baba yake ili pindi atakapomvisha mchumba wake pete ahamie humo, awe huru kwa jinsi atakavyo yeye na mchumba wake.
Licha ya zoezi la Kiti kumvisha pete Wayeka kutofanikiwa, alihamia hapo nyumbani kwake wiki tatu baada ya wazazi wake kuridhika kuwa matatizo ya akili yaliyokuwa yanamsumbua yameisha kabisa.
Ilibaki kidogo tu wapishane, kwa sababu Kiti naye alikuwa mbioni kutoka ili aelekee kwenye mizunguko yake ya kila siku.
“Karibuni,” Kiti aliwakaribisha wageni wake ndani baada ya kuwa wamesalimiana.
“Ahsante,” Bony na Emmy walijibu na kuketi kwenye moja ya makochi yaliyokuwa pale sebuleni.
Haikumshangaza kabisa Kiti kufikwa na wageni asubuhi ile, kwa sababu walikuwa ni wageni ambao ni nusu ya wenyeji kwa sababu ya uwepo wao wa mara kwa mara nyumbani pale. Kilichomshangaza Kiti ni ujio wa bila miadi ambao kwa namna moja ama nyingine ulianza kumjengea hofu.
“Kwema lakini?” aliuliza Kiti.
Swali lake halikujibibiwa mapema kwa sababu ya ukimya wa sekunde kadhaa kupita, ukimya ambao baadaye ulivunjwa na Bony pale alipojibu, “Kwema si kwema, ilimradi siku zinasogea kaka.”
“Una maana gani?”
“She is dying brother, siyo siri anakufa kwa ajili yako,”
“Usiniambie kuwa bado una drama za Wayeka!”
Bony alishangazwa na jibu la Kiti, hakutegemea Kiti aliyemjua kujibu kwa namna alivyojibu.
“Kaka.. hizi kwako zimeshakuwa drama! Kwa nini unaniweka lawamani kiasi hiki?”
“Siyo kama nakuweka lawamani bro.. ila habari za Wayeka ni drama ambazo sitaki kuzisikia. Nilimtolea damu kwa roho safi kama ambavyo ningemtolea mtu mwingine yeyote, kwa sababu ni swala lililokuwa ndani ya uwezo wangu.” Alisema Kiti na kuzidi kuwaacha Emmy na Bony midomo wazi.
“Shem Kiti,” Emmy alimuita Kiti kabla hajasema, “Wayeka hakuhitaji kwa sababu ya damu uliyompatia, anakuhitaji kwa sababu anakupenda.”
“Come on.. Emmy! Ananipenda baada ya kunidhalilisha na kunifedhehesha kwenye siku yangu ya kuzaliwa?”
“Mazingira yalimlazimu, kwa hilo naomba niendelee kumtetea kwa sababu nina uhakika hakudhamiria.” Alisema Bony.
“Shem… mambo mengi yametokea ndani ya kipindi hiki kifupi, na chimbuko lake ni kwenye siku yetu ya kuzaliwa,”
“Kweli bro.. ayasemayo shemeji yako ni sahihi kabisa. Na kabla sijaenda mbali zaidi naomba niseme ukweli kuwa wewe na Wayeka mnapendana, ndiyo maana kila mmoja anaweweseka anapomkosa mwenziye. Nikuombe jambo moja tu kaka, naomba utusaidie kupata amani ya maisha kwa kututoa lawamani. Kuna mtu amepoteza maisha, mwingine amebakiwa na ulemavu wa kudumu na hali ya Mina ndiyo kama unavyojua.. amechanganyikiwa kabisa na hatujui nini hatma yake. Yote haya chimbuko lake ni kwenye siku yetu ya kuzaliwa ambayo ndiyo siku mliyokutana na Wayeka na ndiyo siku ambayo Mina alikuona baada ya miaka mingi ya kupotezana.
Nakuomba ututakase kaka kwa kwenda kumuona Wayeka ambaye bila wewe tunaweza kumpoteza muda wowote…” alisema Bony kwa masikitiko makubwa na kumfanya Kiti ayatafakari maneno ya rafiki yake kwa namna ya pekee. Alikiri moyoni mwake kuwa; ni kweli, chimbuko la mambo yote ni hafla iliyoandaliwa na rafiki yake, hafla ambayo iliwakutanisha yeye na Wayeka kwa mara ya kwanza na pia ilimkutanisha yeye na Mina kwa mara nyingine na hatimaye yakaja kutokea yaliyotokea kwenye siku yake ya kuzaliwa.
Alimtazama rafiki yake kwa jicho la huruma na baadaye akahamishia macho kwa Emmy ambaye ni shemeji yake, alitamani aseme neno lakini alisita kwa kuhofu juu ya mapokezi ya neno alilotaka kusema. Hakujua litapokelewaje, ndiyo maana akaamua kukaa nalo moyoni mpaka walipoagana huku akiwaacha wenziye njia panda kwa sababu hawakujua msimamo wake ni upi.
****
****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku zilikatika bila Wayeka kumuona Kiti wala kupata jibu la kuridhisha kutoka kwa watu aliowategemea, yaani Bony na Emmy ambao aliwategemea kama kiungo cha kuurudisha uhusiano wake na Kiti. Hakujua kuwa wao pia wako njia panda kwa sababu ya kutojua msimamo wa Kiti juu ya jambo hilo ambalo na wao liliwatesa pia.
Wayeka alisubiri Kiti aje, lakini Kiti hakuja. Alisubiri hadi akachoka, Wayeka alikata kabisa tamaa na kuamua liwalo naliwe.
Akapanga kumfuata Kiti nyumbani kwake ili akaseme naye mwenyewe licha ya kuwa Kiti hapokei simu zake. Aliapa kuwa endapo hatomkuta atamsubiri mpaka atakaporudi.. haijalishi ingemgharimu kiasi gani cha muda.Siku moja kabla ya siku ambayo Wayeka alipanga kwenda nyumbani kwa Kiti, Wayeka alikuwa chumbani kwake ambamo alipageuza kuwa selo yake ya hiyari kwa kujifungia kutwa nzima akimlilia Kiti, mahali ambapo sasa palianza kumchosha na kuamua kukata shauri la kupakacha.Ilikuwa majira ya kama saa moja jioni hivi, muda ambao giza la usiku lilianza kuyatoa makucha yake licha kudhibitiwa vikali na umeme uliotoa mwanga kupitia taa zilizofungwa majumbani nje na ndani kwa lengo ka kukabiliana na giza hilo.
Wayeka alikuwa chumbani kwake akimalizia kupanga vitu ambavyo alivihitaji kwa ajiri ya safari yake ya kuelekea kwa Kiti ambaye hakuwa na uhakika kama angempokea au la.
Miongoni mwa vitu ambavyo Wayeka alipanga kusafiri navyo ni pamoja na: kisu kidogo chenye ncha kali, ambacho alikichukua jikoni pasipo kuonekana na mtu yeyote, vingine vilikuwa ni dawa ya kuulia kunguni, shajara yake na kalamu ya wino ambayo aliletewa na Kiti kama zawadi.
Akiwa bado anaendelea kupanga vitu vyake, ghafla Wayeka alishangaa kuliona giza ambalo lilikivamia chumba chake na kukifanya kiwe cheusi tii.
Awali alihisi labda taa ya chumbani kwake imeungua, lakini alipingana na wazo hilo baada ya kushuhudia giza nene mpaka kibarazani kwao ambako alitarajia kuiona taa ya hapo kibarzani ikiwaka.
Hapo akajiaminisha kuwa umeme utakuwa umekatika, lakini kwa mbali aliziona taa za kanisani zikiwaka na zile za kwenye nyumba zilizo jirani na hapo kwao.
“Luku imeisha?” lilikuwa ni swali lililomjia Wayeka kabla hajasikia mlango wa chumbani kwake ukigongwa, “ Ngongo ngo…”Licha ya asili ya woga aliyokuwa nayo, wayeka hakupata wasiwasi wa aina yoyote baada ya kusikia mlango wa chumbani kwake ukigongwa kwa sababu chumba chake kilipakana na chumba cha wazazi wake ambacho kilikuwa karibu kabisa na sebule.
Hivyo alijua moja kwa moja kuwa ni lazima atakuwa ni mtu wa hapohapo nyumbani kwao ndiyo maana hakuona sababu ya kumfanya awe nawasiwasi.Aliuendea mlango uliokuwa ukigongwa kwa msaada wa mwanga wa simu iliyokuwa mikononi mwake.
Alipoufikia tu mlango, Wayeka alikishika kitasa na kukizungusha kwa lengo la kuufungua mlango ambao ulifunguka sambamba na mwanga wa umeme kwenye taa zote za nyumba ile ambazo zilimulika kila mahali na kila kitu kilichokuwa karibu. Hapo macho ya Wayeka yakakishuhudia kitu ambacho hakukitarajia mahali pale na kumfanya atokwe na sauti ya mshango kama vile asiyeamini kile alichokiona, “Kiti…”Hakika alikuwa ni yeye, Kitiheka Ngomanzito, mwanaume ambaye Wayeka alimuhitaji kuliko uhai wake alikuwa amesimama mbele ya Wayeka. alikuwa amenyoa nywele zake katika mtindo alioupenda zaidi, upara. Kiti alikuwa ndani ya shati jekundu la mikono mirefu ambalo lilikuwa limechomekwa vyema kwenye suruali nyeusi aliyovaa na kumfanya aonekane mtanashati, muonekano aliokuwa nao wakati anarejea kutoka Marekani.
“Wayeka wangu,” sauti ilimtoka Kiti, sauti ambayo ilisikika sawia masikioni mwa Wayeka.
Ilikuwa kama ndoto!Wayeka alikuwa ni kama asiyeamini, kabla hajajua nini cha kusema, alimshuhudia Kiti akiingiza mkono wake wa kulia mfukoni, huku ule wa kushoto akiushika mkono wake wa kushoto.
“Fumba macho yako tafadhali…” alisema Kiti na kumshangaza Wayeka kwa kauli yake hiyo, lakini kwa kuwa alimpenda, hakuwa na jinsi ilibidi kutii kile alichoambiwa na mwanamme ammpendaye. Sekunde chache baadaye Kiti alimwambia tena Wayeka afumbue macho, hapo ndipo mapigo ya moyo wake yaliongeza kasi ya mwendo. Wayeka aliyafumbua macho yake na kukuta pete ya uchumba ikiwa kidoleni kwake, akiwa bado analishangaa tukio lile ambalo kwake lilikuwa kama ndoto ambayo hakuitegemea, sauti za zikasikika kutoka kwa watu waliokuwa nyuma ya Kiti, “Happy birthday to you… happy birthday to you... happy birthday dear Wayeka… happy birthday to you..”Ni wimbo huo ndiyo uliomkumbusha kuwa siku hiyo ilikuwa ni tarehe 04/01/ ya mwaka, 2014, siku ambayo alipaswa kuazimisha siku yake ya kuzaliwa kwa sababu alizaliwa siku kama hiyo miaka kadhaa iliyopita.
Ajabu ilioje! Machozi yalimtoka Wayeka, machozi ya furaha ambayo yalimfanya amtazame Kiti usoni kabla sauti haijamtoka, “On my birthday?” lilikuwa ni swali kutoka kwa Wayeka, ambaye licha ya kumuuliza Kiti swali hilo, bado alikuwa na maswali mengine kichwani; kwanini iwe kwenye siku yake ya kuzaliwa? Na siyo kwenye siku ambayo Kiti huazimisha siku yake ya kuzaliwa, siku ambayo walipanga kuvishana pete lakini kwa sababu ambazo hazikuweza kuzuilika tukio la kuvishana pete halikukamilika.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yeah my dear, it is on your birthday” alijibu Kiti na kisha kumkumbatia Wayeka kwa huba. Sauti za vigelegele ambazo zilisindikiza kumbato hilo zilisikika kutoka kwa mashuhuda waliokuwepo. Wote waliokuwepo walifurahi, Bony na mkewe walikumbatiana huku machozi ya furaha yakiwatoka. Hawakuwa peke yao, walikuwepo pia; wazazi wote wa pande mbili na marafiki ambao walifika kushuhudia.
“Nisamehe kwa kuuvunja moyo wako kwenye siku yako ya kuzaliwa” alisema Wayeka huku machozi yakimtoka na kulowanisha mabega ya Kiti.
“Usijali, nimeirudisha furaha yako kwenye siku yako ya kuzaliwa” alijibu Kiti, wakiwa katika hali ile ile ya kukumbatiana.Ama kweli, mapenzi yana nguvu kama mauti.
MWISHO......
Toa maoni yako msomaji... Usipite bila kutoa neno lako...
0 comments:
Post a Comment