Simulizi : Zari La Ndoa
Sehemu Ya Tano (5)
"Ooh! Mungu wangu wee... Hakuna ndoa tena hapa," akadakia Mshenga huku akijishika kichwa na kuwafanya baba na mwanae watazamane, wakati baba Matwiga na mama Zainab nao wakitazamana.
Mama Zainab akatoa macho na kumuuliza Mzee Komba kama Matwiga ndio mwanae, Mzee Komba akavua kofia yake kichwani na kuiweka chini, akajikuna kichwa na kujibu
"Ndio mama Zainab, Matwiga ndio mwanao uliemuacha Zanzibar, akiwa ni mdogo" mama akaanza kulia, Zainab nae akaanza kulia pia huku akikimbilia chumbani kwake, Mshenga akaanza kumbembeleza mama Zainab anyamaze.
Mzee Mapunda akawa hajielewi, akanyanyuka na kumfuata mwanae chumbani kwake alipokwenda huku akilia. Akajaribu kumtuliza, ilikuwa ni kazi kweli kweli, lakini alifanikiwa na kutoka nae barazani huku akiwa amemkumbatia kwa mapenzi makubwa.
Suala la ndoa likawa halipo tena, swali likawa watumie njia gani kumueleza Matwiga na jamii pia ambayo ipo tayari kwa ajili ya sherehe hiyo ambayo itafanyika siku ifuatayo? Hakika wote walionekana kuishiwa mbinu.
Dhahiri walionekana wamekosa cha kusema hadi Mzee Mapunda aliposhauri apigiwe simu Mapunda na kuitwa nae afike pale nyumbani usiku uleule. Mshenga akasema wala Matwiga hayupo mbali, yupo jirani tu akitakiwa anafika.
Baba Matwiga akamwambia Mshenga amfuate, akanyanyuka na kumfuata akiwa amewaacha watu wote mle ndani wakiwa kimya kila mtu akiwa na wazo lake. Hakuchukua muda mrefu akawa ameongozana na Matwiga. Hali aliyo wakuta nayo watu mle ndani, hasa wale wanawake wawili, ilimshitua sana.
Ajabu alipoingia akashangaa kuona mama mkwe wake akilia na alipokutanisha nae macho, kilio kikaongezeka. Alipomuangalia Zainab nae alionekana macho mekundu na walipo kutanisha nae akakwepesha macho yake na kuangalia pembeni.
Akabaki kashangaa tu hajui hata ni wapi pa kukaa, baba yake akamuita na kumwambia aketi pale kwenye sofa aliloketi yeye. Matwiga alisogea na kuketi karibu yake akiwa na tamaa ya kutaka kujua.
Wote walikuwa kimya ikisikika sauti ya Mama Zainab ikilia kwa mbali, Matwiga akaamua kuuvunja ukimya kwa kuuliza kwa mshenga wake pale kuna nini? Mshenga akamtazama Mzee Komba kwa jicho la kuuliza, 'nimwambie?'
Mzee komba akatazama chini bila kujua kuwa Matwiga anafuatilia kwa umakini mkubwa ishara zao, alikwenda sambamba na kila tukio lililokuwa likitokea pale. Akamgeukia baba yake na kumuuliza tatizo nini?
“Baba inaonekana kama kuna tatizo, mkao huu si shwari hata kidogo?” hapo ndio akakumbuka kuwa waliopo mle ndani bado hajawasalimia. Akawasalimia na wote waliitikia kila mtu kwa sauti ambayo mwenzie wala hakuisikia, akhoji tena swali lilelile, kuna nini?
Baba yake akashindwa kumjibu, hadi ikamlazimu mshenga kuingilia kati na kumueleza kiufupi tu ili kuokoa muda. Matwiga hakuamini masikio yake, kuwa yule anaemuona pale mbele ya macho yake ndio mama yake mzazi.
Akanyanyuka kwa huzuni huku machozi yakimtoka, haieleweki kama yalikuwa ni ya furaha ya kuonana na mama yake ama ni ya huzuni kwa ndoa yake kuruka. Akamsogelea na kumkumbatia mama yake ambae nae wakati huo alikuwa akilia kwa sauti kubwa sasa, haikuwa na kificho tena.
Huzuni ikatawala ndani ya nyumba ile ambayo ilikuwa inategemea furaha kwa siku zote hizi za kuelekea kwenye ndoa ya Zainab, Matwiga alionekana kama vile ana dukuduku kubwa mno moyoni, akataka kulisema lakini alijizuia tu, roho ilimuuma sana.
"Kwa hiyo Matwiga hakuna ndoa tena mwanangu, maana Zainab ni ndugu yako kabisa tena wala sio wa kupapasa," aliongea mshenga na kumfanya Matwiga ainame chini, akashusha pumzi kwa nguvu huku akisemahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ni kweli, hatuna budi kukubali matokeo, hilo limeisha tokea na tunapaswa kumshukuru Mola kuwa hakuna chochote kilichopita kati yetu…” alizungumza kwa huzuni akijizuia kutoa sauti ya kilio chake cha ndani, huku akijiweka vizuri na kuendelea
“Jambo jema zaidi ni mimi kumuona mama yangu, mama mzazi ambae nimekuwa nikimtafuta sana kipindi cha nyuma." Alisema Matwiga na kulia kiume akiwa kafunika uso wake kwa viganja vyake.
Mshenga alinyanyuka na kwenda kumtuliza Matwiga kisha wakaanza kuongea baada ya hali kurejea kwenye hali yake. Alifungua pazia la maongezi Mzee Mapunda ambae ndio alikuwa ni mwenyeji
"Jamani sasa inakaribia kuwa ni saa 8 usiku, ndoa ilipangwa kuwa mchana wa siku hii ya leo, ndoa ambayo kwa sasa haipo tena, kilichotokea kinapaswa kuwa ni siri yetu, lakini sasa tunafanyeje ili jamii ibaki na uelewa tofauti na kilichojiri hapa ndani? Kwani muda unakwenda na tunapaswa kufikia muafaka."
"Mimi ninaona tuwaambie tu kuwa tunaahirisha harusi hii kwa muda, kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, na itakapokuwa tayari tutawajulisha!" Alishauri mshenga na baada ya mazungumzo marefu kidogo, wakaamua alfajiri ya siku hiyo watangazie hivyo.
Wakiwa wanaagana, Matwiga akawaomba warudi kukaa kwani nae ana habari moja ambayo wao hawaijui. Wote wakaketi na kumtazama kwa shauku, akapeleka macho yake kwa Zainab ambae alikuwa amekaa na baba yake.
Awamu hii Matwiga alikuwa ameketi na mama yake na sofa lingine waliketi mshenga na baba Matwiga. Wakati Zainab na baba yake walikuwa kwenye sofa moja.
Matwiga akamuuliza Zainab kama anamjua Sungura. Zainab kama mtu aliegutuka kutoka kwenye usingizi mzito, huku akimtazama Matwiga akajibu ndio.
Matwiga, akamtazama Zainab ambae dakika chache zilizopita alikuwa ni mchumba wake, sasa alikuwa ni dada yake, akamuuliza tena kama anajua alipo? Zainab akawa mnyonge na kujibu hajui alipo.
Kabla hawajaongea zaidi, Mzee Mapunda ndio akawaeleza kisa kamili cha kuwaitia pale hadi kutokea lile lililotokea, lakini chanzo hasa kikiwa ni huyo Sungura.
Walimuelewa vizuri, Matwiga akamuuliza dada yake kama anampenda Sungura, swali ambalo wote waliosikia kile alichokieleza baba Zainab, dakika chache zilizopita, walijua jibu litakua ni ndio.
Na ndivyo ilivyokuwa, akajibu kwa jicho kavu kuwa anampenda sana ila hajui kama yu hai ama amekufa. Akaanza kulia, wote wakawa wakimtuliza.
"Upo tayari kuolewa nae iwapo atapatikana?" Swali lile likamvuruga mdogo wake
"Kaka kwanini unaniuliza kitu ambacho hakipo?" badala ya kujibu akauliza tena.
"Hakipo kivipi Zainab?" Wote walikuwa kimya wakiwasikiliza ndugu wakiulizana.
"Leo ni siku ya pili familia yao imekuwa ikimtafuta kila sehemu bila mafanikio, wewe unazungumzia suala la kumpata, utampatia wapi ikiwa wao kila sehemu unayoijua wamefika na kumkosa?" Alijibu kiurefu Zainab na kumalizia kwa swali.
Matwiga hakujibu, alinyanyuka na kwenda hadi pale alipoketi Zainab, dada yake na kupiga magoti mbele yake, maana sasa alitambua ni kiasi gani dada yake anampenda Sungura na kipimo alichokuwa nacho alijua ni kiasi gani pia Sungura atakuwa anampenda Zainab.
"Zainab mdogo wangu, Zainab dada yangu wa pekee, ni mimi pekee ndio nijuae ni wapi alipo Sungura," aliongea kwa kujiamini huku akitazama pembeni kwa huzuni.
"Nini? Unasemaje?" Aliuliza kwa mshangao mkuu huku akimtazama kaka yake, mama yao nae alipatwa na mshangao nae akaelekeza jicho kwa baba Zain.
"Yupo salama kabisa, tena sehemu ni nzuri kuliko kwao, japo alipo huko ni sehemu nzuri, lakini sasa nimetambua haikuwa ni sehemu muafaka kwake kuwepo,"
"Yupo wapi kwani?" Huku akinyanyuka, Zainab alionekana kama kapagawa vile.
Wazee wakamtuliza Zainab na kumnyanyua Matwiga pia pale chini na kumtaka aketi, mazungumzo yakaanza upya, muda huu Zainab alikuwa akilia. Matwiga akawaomba radhi na kuwaeleza sababu ya yeye kufanya vile.
Ilikuwa ni mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa Zainab ambae hakujua kama ni dada yake na kuhofia usumbufu wa Sungura kwenye sherehe walizo ziandaa. Walimuelewa na kuhoji ana wazo gani?
Matwiga akamtazama dada yake na kumuomba akuballi kubeba aibu ya familia kwa kukubali kufunga ndoa na Sungura. Wakamtazama Zainab ambae alikuwa akilia, Mzee Komba akasema lile ni wazo zuri.
Mzee mapunda akasema kabla ya kumuomba Zai akubali kufunga ndoa, akauliza huyo Sungura atakubali kufunga ndoa na Zain hali hajajiandaa kwa jambo hilo na pia ametendewa ndivyo sivyo na Matwiga?
Hapo sasa ikawa ni shida, kila mmoja aliona ugumu hapo, mshenga akashauri aulizwe Sungura, maana ndio mwamuzi wa uwepo wa ndoa ile na tayari hapo ikiwa ni alfajiri, ina maana usiku mzima uliisha wakiwa bado hawajapata muafaka na muda sio mrefu wageni wataanza kuwasili kutoka sehemu mbalimbali.
Matwiga akapiga simu na kumtaka aliekuwa akiongea nae kwenye simu amlete Sungura haraka nyumbani kina Zainab muda uleule tena haraka na bila kuchelewa, mtu yule alikubali, kwani hakuwa na uwezo wa kupinga amri ya Matwiga.
Dakika 10 baadae Sungura aliingizwa pale ndani huku kashikiliwa na Ngonyani, Zainab akamkimbilia na kumkumbatia huku akilia. Sungura hakuonesha ushirikiano wowote bali alisimama tu kama sanamu.
Wazee wakamuomba aketi kwenye sofa lilikuwepo pembeni la mtu mmoja, akagoma na kuwashukuru huku akimtazama Matwiga kwa jicho la hasira sana, Matwiga aliliona hilo na kumwambia Sungura kwamba ni haki yake kukasirika na hata kununa kwa kilicho tokea.
"Lakini hatuwezi kufikia muafaka iwapo nawe hutakubali kukaa chini na kuongea."
"Hivi mimi na wewe Pundamilia unahisi tutaongea nini? Labda uniambie tu usimame tupigane tu, ndio neno pekee ninaloweza kukusikiliza na kulikubali, hakuna neon linguine lolote kwani nakuchukia sana!" Aliongea Sungura bila kuogopa chochote.
"Kijana hata sisi suala hilo sasa tumelitambua, basi tunaomba uketi chini hapo tuongee ili liishe," Aliingilia kati Mzee Komba na Mshenga akadakiahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tupo wazee hapa na hakitoharibika kitu kijana."
"Mimi siwezi kukaa hapa na hali najua fika kuwa kuna ndugu zangu wananitafuta na hawajui ni wapi nilipo, suala la msingi ni nyie kuniacha tu mimi niende nyumbani kwetu." Alichokiongea ni ukweli, lakini suala la kumuacha aende lilikuwa ni gumu kuliko jambo lolote.
Maana kikao kile kilimuhitaji yeye kuliko yeye alivyo kihitaji, ikamlazimu Mzee Mapunda aingilie kati kumuomba Sungura akubali kukaa angalau kwa nusu saa kisha wakimaliza yeye atatoka na kwenda huko kwao.
"Baba yangu Mzee Mapunda, nakuheshimu sana na ndio maana hata nimeingia humu ndani nikiamini ni sehemu salama kwangu, lakini siwezi kukaa labda nami ningekuwa na angalau mtu wangu mmoja, hivi mnajua kuwa huyu Paka amenipa siku mbili za dhiki sana?" Aliongea Sungura kwa kwa uchungu huku akimnyooshea kidole Matwiga.
Matwiga alitikisa kichwa na kutoa tabasamu la majuto
"Sawa Sungura, ndio maana sisi tupo hapa, labda ni nani mtu wako wa karibu ambae ungependa aungane nawe kwenye kikao chetu hiki?" Aliuliza Mshenga kupunguza kelele.
"Aje kaka yangu hapa."
Matwiga akatoa simu yake na kumpa Sungura, akaikataa na kusema yeye hana shida, kama wao ndio wana shida basi wao ndio wampigie na kumuita aje. Zainab akampigia kwenye simu yake na kumuomba Simba achukue bodaboda na afike kwao haraka iwezekanavyo.
Akahoji kuna nini? Zainab akamwambia akifika tu kule atajua ni kwa nini kaitwa ila afanye haraka. Akiwa ni mwenye hofu tele, akakurupuka kitandani bila kuoga wala kupiga mswaki, akaita bodaboda iliyo mpeleka kwa Mzee Mapunda.
Alifika na kuingia ndani moja kwa moja, aliwaona watu wamekaa kama kuna kikao vile, mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni Zainab na kuwaona wengine pia. Lakini baada ya kugeuka akamuona mdogo wake akiwa salama bin Salimini.
Wakasogea na kukumbatiana wakiwa na sura za huzuni, hata waliokuwepo pale wakajua ndugu hawa wanapendana sana, siku mbili tu za kutokuonana inakuwa vile, je wanapotengana miezi wakati Sungura anapokuwa chuo inakuwaje?
Mawazo yao yalikatishwa na sauti ya Simba alliemuuliza ndugu yake ni wapi alikuwepo kwa zile siku mbili? Sungura akamtazama Matwiga kisha akamwambia kaka yake kuwa
“Kuna bwege mmoja alijiona yeye ni kila kitu kaka yangu, akasahau kuwa chini ya jua anaejua kila kitu ni mmoja tu, sasa we subiri, mimi nawe tutaongea nyumbani.”
Akamtaka nduguye awasikilize kile walichomuitia pale, Simba ndio akaketi kwenye sofa lile la mtu mmoja na Sungura akalazimisha kukaa chini kwenye miguu ya kaka yake ili kusikiliza kile kilichofanya wawepo pale.
Ni wao tu pekee ndio walikuwa hawaelewi kilichotokea, Mzee Mapunda ndio akawaeleza kila kitu tangu kuanza kwa uhusianao wa Matwiga hadi kutambulika kwa udugu wao. Walishangaa na kutazamana wale ndugu.
Kisha Mzee Mapunda akawaeleza tukio la kutoweka kwa Sungura na uhusika wa Matwiga huku akimuonesha Matwiga ambae akawaomba radhi. Akamtazama Simba na kumueleza kuwa ile ilikuwa ni katika kulitetea tu penzi lake kwa Zainab ambalo Sungura alikuwa amelitia shakani.
Sungura akauliza kwa jazba kwamba
“Angalia watu wengine walivyokuwa ni wapumbavu? hiyo ni aina gani ya utetezi kwa kuwaweka wengine shakani na kuwasababishia maumivu?” Simba akaongeza swali kwa kuuliza kwani ni nani alietangulia kuwa mpenzi wa Zainab kati ya wao wawili?
Swali lile likampa nguvu kidogo Matwiga kwa kujibu kuwa Sungura alitangulia kuwa mpenzi wa Zainab, lakini hakuwa akitambulika pale nyumbani kwa wazazi, Sungura akataka kusema kitu, lakini Mshenga akamuwahi kumzuia.
Ilimlazimu kufanya hivyo, maana lah sivyo mle ndani pange geuka kuwa ni kama mahakamani, kila mtu angetaka kuongea lake. Hivyo akawataka waongee na kumaliza tofauti zao ili watimize lengo la kuwepo kwao pale.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lengo la kuwa hapa ni kulimaliza tatizo hili kwa njia muafaka na sio ugomvi, siku zote alie uchi anahitaji nguo zaidi kuliko viatu japo anatembea kwenye miba, Matwiga anahitaji sana msamaha ndio maana amekubali kukiri kosa,” mshenga aliongea mambo ya nahau.
Simba sasa ndio alikuwa akiangaliwa na watu wote pale kama ndio mtu pekee anaeweza kumtuliza Sungura, wakatumia muda ule kumueleza kuwa lengo la kuwaita pale ni kutaka kumueleza nia ya kuwafungisha ndoa Sungura na Zainab.
Kauli ile ilimshangaza mno Simba, hakuwa na jibu la moja kwa moja Simba, alimtazama mdogo wake kwa ishara ya kuwa ndio mtu pekee ambae ana uamuzi wa kusema ndio ama hapana.
Tayari wageni walikuwa wameanza kuwasili pale nyumbani kwa ajili ya kuanza maandalizi ya shughuli. Sungura nae wala hakupepesa macho wala kutikisa masikio, palepale akakataa wazo lao.
Wazo lile lilipowekwa mezani, hakusuasua kwenye maamuzi, aliwaambia wanataka aibu yao yeye ndio aibebe na kisha yeye ndio aaibike? Hakuwa tayari kwa hilo.
Jibu hilo lilimtoa machozi Zainab ambae alikuwa katulia kwa muda sasa. Zain akanyanyuka na kukimbilia chumbani kwake huku akilia, wazee wakaona pale si sehemu salama tena kuzungumzia jambo lile, maana tayari wageni wameisha anza kuwasili, Mzee Komba akashauri waende kuzungumzia sehemu nyingine ili kuficha aibu yao.
Simba akawaambia waende kuzungumzia nyumbani kwao kama hawatajali, wazo ambalo Matwiga alilipinga kwa hoja yenye nguvu, aliwaambia ni heri wakakae kule nyumbani kwao kwa sababu kuna watu wengi wanakuja kwa ajili ya shughuli ile, hivyo watakapokuwa wanaonekana, hakuna hofu itakayo kuwepo.
Sungura akagoma kuendelea na mazungumzo mengine ya aina yoyote, kwa kusema yeye hayupo tayari kufunga ndoa, kisha akamwambia kaka yake anyanyuke waondoke, Simba akakataa na kumtaka mdogo wake asubiri.
Hakutaka hata kumsikiliza kaka yake, akaondoka na kumuacha Simba ambae alionyesha busara kubwa kwa kuwaambia wamuache tu aende, yeye atabakia na kufanya maamuzi kwa niaba yake.
Hekima ya Simba iliwafurahisha wazee na na wakaelekea nje kwenye gari tayari kwa ajili ya kuelekea nyumbani kwa kina Matwiga ambapo waliamua kikao kihamie huko. Waliongea vizuri na Simba na kufikia muafaka.
Akawaambia mipango yote iendelee kama ilivyopangwa na kuhusu suala la Sungura wamuachie yeye, lakini alitaka kujua kuhusu maisha ya Sungura baada ya kukubali kufunga ndoa?
Mzee Komba nae akasema jambo hilo aachiwe yeye kwani analimudu. Bado Simba alikuwa na swali lingine, swali lilihusu mambo ya ndoa, aliwajulisha kuwa wao hawana uwezo wowote wa kujiandaa kwa masaa matano yaliyo bakia.
Akahoji wanafanyaje sasa ili kujua ni kipi kitafanyika? Matwiga aliekuwa amekaa jirani yake akamshika bega na kumwambia
"Kila kitu kimeisha andaliwa na kipo tayari, kuhusu mavazi yapo nyumbani hapahapa, mavazi yale niliyokuwa niyatumie mimi kwenye sherehe zote, nitamuachia Sungura..." Akanyamaza kidogo, kisha akaendelea
"Pia sherehe zote zilizokuwa zimepangwa kwa ajili yangu, zitafanyika kama zilivyo pangwa, atabadilika mtu pekee, toka kwa Matwiga na kuwa ni Sungura," alimaliza Matwiga.
Wazee wakatikisa kichwa kumpongeza Matwiga kwa busara alio ionyesha, hasa ukizingatia hata kimaumbile ya nje na muonekano, hawakuwa na tofauti kubwa sana kati ya Sungura na Matwiga.
Zainab bado alikuwa akilia chumbani kwake akiwa amejifungia kwa ndani peke yake. Mama yake alijitahidi mno kumgongea mlango lakini hakufungua, hata nae akaanza kupata hofu kuwa huenda huyu nae sasa atajidhuru.
Hakuna aliekuwa na hakika ni wapi alipoelekea Sungura bali wote walihisi atakuwa amekwenda nyumbani kwao tu, hawakuwa na shaka yoyote kwani uwepo waSimba ulithibitisha tu kuwa kila kitu kitaenda sawa.
Nyumbani kwa kina Matwiga kikao kilikamilika na sasa kusubiri juhudi binafsi za Simba juu ya kumshawishi ndugu yake kuhusu ndoa ile. Akiwa pale hajaondoka Simba, wakajaribu kumpigia simu Sungura.
Hakuwa akipatikana kila walipojaribu kumpigia hadi Matwiga alipokumbuka kuwa yeye ndio ana simu yake. Akatoa hiyo simu na kumpa Simba kisha akamuita Ngonyani na kumtaka akatoe gari nyingine iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili yake kama bwana harusi.
Ilikuja mbele yao gari mpya kabisa ya kisasa aina ya Toyota Bravis ya rangi ya Chocolate, akamuamuru Ngonyani aende na Simba na kukaa huko hadi atakapo pewa taarifa nyingine kwani watakuwa wakiwasiliana mara kwa mara.
Ngonyani alitii amri ya bosi wake na kumfikisha nyumbani Simba ili aweze kuongea na mdogo wake wakiahidi kuwasiliana nae kila mara. Simba aliingia ndani na kuanza kumtafuta mdogo wake na kumkosa.
Alitoka nje na kumuulizia kila sehemu, lakini hakufanikiwa kujua ni wapi alipo, ni mtu mmoja tu ndio aliesema alimuona dakika chache zilizopita. Baada ya kama nusu saa hivi, walikuja baadhi ya watu kutoka kwa kina Matwiga ili kujua kinacho endelea.
Hawakuridhishwa na maongezi ya kwenye simu, walikuwa na hamu mno ya kujua msimamo wa Sungura, walipo ambiwa kuwa Sungura hayupo, hawakuamini, walihisi tu kuwa yupo lakini tayari kagoma, hivyo Matwiga akalazimika kwenda huko.
Zainab bado aligoma kufungua mlango, watu wa mapambo tayari walikuwa nje ya chumba wakisubiri afungue mlango ili waanze kufanya kazi iliyo wapeleka pale. Kazi ya kumpamba yeye pamoja na eneo la makazi yake wakati washughuli nzima ya harusi, Zainab aibu ilimtawala mno na aliiogopa aibu hiyo kuliko hata kifo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hivyo alipanga iwapo Sungura atashikia msimamo wake wa kumkataa na kukataa kufunga nae ndoa siku hiyo, ni heri yeye atoweke duniani kuliko kuivaa aibu ile.
Bravis ilikuwa imepaki nje na sasa ikaongezeka Murano aliyokuja nayo Matwiga, nje ya nyumba ya watu masikini pale mtaani, siku hiyo yalipaki magari ya kitajiri na kuzua mwaswali yasio kuwa na majibu kwa wakazi wa eneo lile.
Watu wawili walikuwa wamesimama nje ya gari ile iliyo pangwa kubeba harusi. Ndani ya gari ile palikuwa pamesheheni vitu vizuri vitupu.
Kulikuwa na mavazi ya kisasa na mapambo ya kiume ghali, Perfume na viatu vipya kabisa, lakini mvaaji wala hakuonekana, karibu watu wote walianza kukata tamaa, simu hadi muda huo sasa ziligeuka kero kwa waliopo kwa kina Simba wakimsubiri Sungura.
Wote waliona ugumu wa kile wakitakacho, maana ilikuwa imesalia saa 1 tu muda ambao ulipangwa kufanyika tukio la ndoa, kuwa umewadia. Simba bado hakuwa akitulia, alikuwa akizunguka huku na huku akijuta kuwaahidi jambo lile kuwezekana, ambalo kwake aliamini akirudi nyumbani na kumkuta Sungura mdogo wake, basi ataongea nae na kuliweka sawa.
Lakini sasa ndio Sungura haonekani, anaona kabisa sasa ile aibu anaivaa yeye wakati huko tayari nae alikua ameisha anza kukata tamaa.
Ghafla kama miujiza pasina kutegemea, Matwiga alikuwa kasimama na kuegamia Roof ya gari lake, Ngonyani akiwa amefungua mlango wa gari kwa nia ya kuingia ili akae, Simba nae alikuwa kasimama kwenye mlango wake, simu ikaita.
Ilikuwa ni simu ya Ngonyani. Ajabu watu wote watatu waliacha walichokuwa wakifanya na kuanza kuiangalia simu ya Ngonyani alipoitoa mfukoni mwake. Namba ilikuwa ni ngeni kwake, akaipokea na kuongea na sauti iliyokuwa ikilia.
Aliepiga alijitambulisha kuwa ni mama Zainab, akasema anataka kuongea na Sungura, Ngonyani hata bila kumjibu mama Matwiga kuwa Sungura hayupo, akachukua simu na kumpa Simba.
Mama Zainab akamsalimia, sauti alipoisikia tu akajua kuwa yule si Sungura, akamwambia Simba kwamba yeye anataka kuzungumza na Sungura, Simba akakosa cha kumjibu, lakini akajikakamua na kumjibu kuwa hajaonekana hadi muda huu.
Kama mtu ambae amechanganyikiwa, mama akamwambia Simba kwamba Zainab ametishia kujiua iwapo tu Sungura hatokubali kufunga nae ndoa ama hatokwenda kuongea nae muda huu.
Simba akawa haelewi ajibu nini, maana Sungura haonekani, na simu ikakatika muda huohuo. Wakati hata hakuna aliewahi kufumbua mdomo, simu ya Matwiga nayo ikaita, akaitoa kiuvivu mfukoni na kuitazama, kisha akaipokea.
Lakini kila aliepiga simu alikuwa na nia ya kutaka kujua ni hatua gani wamefikia huko, kabla hata hajajibu, Sungura akatokea akiwa na jama kama watatu hivi ambao walionekana kama ni askari.
Askari wawili wakiwa wamevaa nguo za kiraia na mmoja alikuwa amevaa sare zake za kijeshi. Mmoja kati ya wale waliovaa nguo za kiraia, akamgeukia Sungura na kumuuliza kama kuna mmoja wao kati ya wale?
Sungura akamnyooshea kidole Matwiga aliekuwa bado kapigwa na butwaa akiwa na simu yake mkononi. Yule askari alievaa sare za kazi, akamsogelea Matwiga na kumuweka chini ya Ulinzi.
Matwiga wala hakubisha wala kuleta usumbufu wowote, bali alimsogelea Sungura na kumwambia yeye anakwenda kituoni, lakini gari ile aionayo pale ina kila kitu ndani, kuanzia mavazi hadi pesa kiasi cha akiba kwa ajili ya matumizi yake ya kwenye ndoa ile.
Akamueleza kuwa hata dereva aliepo kwenye gari ile ni kwa ajili yake, suala la msingi, aende kufunga ndoa na Zainab, kwani amebaki anasubiriwa yeye tu, kisha akageuka na kumpa nafasi askari ya kuondoka nae.
Simba akaingilia kati na kuzuia kitu kile kisitokee, palizuka mtifuano kidogo kati ya Simba na mdogo wake, Simu ya Matwiga ambayo ilikuwa hewani, ikakatwa na kupigwa tena. Akaipokea na kuongea kwa sekunde kadhaa.
Akamsogelea Sungura kwa hatua kama mbili na kumpa simu akimwambia aongee, Sungura akasonya na kugeuka, Simba akaichukua simu ile na kuongea na mpigaji. Alikuwa ni mama Zainab.
Alikuwa akimuomba Simba awaokoe na aibu kubwa ambayo dakika chache zijazo itawakuta na pengine hata kuhatarisha maisha ya mtoto wao wa pekee.
"Kwani upo karibu na Zainab hapo?" Aliuliza Simba, kisha akaomba kuongea nae, askari walipotaka kuondoka na Matwiga, Simba akawaomba wasubiri kwa dakika 3 tu kisha watachukua maamuzi yao.
"Zainab, usilie, mimi ni Simba na nipo nao wote wawili hapa, nipo na Sungura hapa pia pembeni yangu yupo Matwiga, nikupe nani uongee nae kwanza?" Alitumia busara kubwa mno Simba ili kumtuliza Zainab aliekuwa akilia.
Akamjibu kwamba anataka kuongea nao wote wawili kwa wakati mmoja, hivyo akamuomba aweke Loud Speaker, Simba akafanya kama livyo ambiwa na kusema
"Haya tayari sote tunakusikiliza!"
Matwiga kaka yangu, natambua fika ulichokifanya hakikua sahihi lakini siwezi kukulaumu, kwani kilisababishwa na mapenzi makubwa uliyo nayo kwangu, na ndio maana hadi sasa umeyaweka rehani maisha yako kwa ajili yangu, umenionesha moyo wa ujasiri sana, nakupenda sana kaka yangu..." Alimaliza Zainab, ambae alikuwa akiongea kwa kwikwi.
Maneno hayo yalisikika vizuri mno na wote wakiwepo askari wale. Wakatazamana na kisha Zainab akaendelea
"Mpenzi wangu Sungura, najua unafahamu kwamba sijawahi kupenda kama kiasi ambacho nimekupenda wewe, lakini naomba usitumie udhaifu huo kuninyanyasa, ninapenda kukueleza sasa, iwapo haupo tayari kuonyesha upendo wako kwangu kwa muda huu ambao ninauhitaji zaidi faraja toka kwako, ili kuficha aibu yangu..," akanyamaza kidogo kupunguza kilio chake na kuendelea;
"Basi tambua sitahitaji tena kuona upendo wako, ambao utakuwa hauna maana, nitakao uita ni upendo wa kinafiki, kwani wakati kaka yangu anapelekwa gerezani, nami nitakuwa napelekwa kaburini..." Akaaangua kilio kikubwa na simu ikakatika hapohapo.
Sungura akashusha pumzi kwa nguvu na kukaa chini kwenye ardhi huku akimtazama Matwiga, Matwiga akamfuata na kuchuchuma ili aweze kuwa sawa nae pale alipoketi, kisha akasema;
"Huna haja ya kuhofia kile alichokisema Zain, uamuzi uliouchukua ni sahihi japo kuna kosa umelifanya, kosa lako ni kupita kule nyumbani kwa kina Zainab hadi kila mtu atajua ulichokifanya, lakini pamoja na hivyo, ninaomba wakati mimi nikielekea Polisi..." Simba akasogea karibu yao.
"...wewe nenda nyumbani kwangu, tayari watu kule nyumbani ni wengi wanakusubiri wewe tu ili kufunga ndoa ambayo imebaki dakika zisizozidi 20, ninaomba unikubalie hili na watu wasijue nilipo hadi baada ya ndoa kufungwa, naomba Sungura!"
Aliongea Matwiga kwa dhati na kunyanyuka akianza mwenyewe kuelekea ilipo gari ya Polisi, ambao walikuwa na gari aina ya Land Rover 110 Defender, akaingia mwenyewe na kuketi chini bila hata ya kuambiwa na yeyote wala kupewa maelekezo.
Hata wale askari nao waliingiwa huruma kutokana na kulisikia tukio zima pale, walitamani wamuachie, lakini haikuwezekana, wakaingia na kuwasha gari lao kisha wakaondoka kuelekea kituoni.
Simba, Sungura na Ngonyani hata hawakujua ni nini cha kufanya. Baada ya gari kuondoka tu, Simba akaanza kumlaumu mdogo wake kwa uamuzi wa kijinga alio ufanya, lakini hakujua tu moyoni mwake Sungura kwa wakati ule.
Hata nae huruma ilimuingia na kujuta kwa kile alichokifanya, wakiwa bado hawana maamuzi ya kufanya, gari nyingine aina ya Prado ya Mzee Komba nayo ikafika, wakashuka Mzee Komba mwenyewe, Mshenga na Mzee Mapunda.
Wote walionekana kuwashangaa kutokana na hali waliyo wakuta nayo pale. Simba akawapa ishara wenzie kuwa wasiongee chochote bali wamuache yeye ndio awe msemaji, wakakubali nao pia kwa ishara.
Mzee Komba aliposhuka tu akamsalimia Sungura kwanza na kisha akamgeukia Simba na kumuuliza kulikoni? Simba akamwambia wanamsubiri Matwiga ametoka kidogo. Mzee akaanza kutukana kweli, kuwa Matwiga Yule hajielewi na kumtaka Sungura ajiandae kabisa ili waondoke.
Sungura akamtazama kaka yake aliempa ishara ya kwamba akajiandae. Mshenga akaongeza;
"Simba mwanangu, kule watu wote tumeisha wapeleka msikitini, tumewaambia bwana harusi yupo Saloon, hivyo tunasubiriwa sisi tu na hapa tuna kama robo saa tu, msaidie ajiandae haraka haraka ili tuondoke..."http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Samba alithaminika kuliko hata Sungura mwenyewe, leo alionesha thamani kubwa mno, walijuwa wakimuudhi tu yeye basi huyo Sungura ndio ataingia shimoni na milele hawatamuona, ikawalazimu sasa wanyenyekee.
Simba akachukua vifaatoka ndani ya gari ile Bravis na kuingia navyo ndani na baada ya kama dakika 7 na 9 hivi, wakatoka Sungura akiwa amebadilika kabisa, sasa alionekana ni mtu tofauti kabisa.
Baadhi ya ndugu ambao walikuja kwa nia ya kusaidiana kumtafuta Sungura, walikuwa hata hawajielewi na hawakutambua ni kipi kinacho fanyika. Sasa ndio Simba akwaambia kwamba leo ni siku ya Sungura kuoa.
Karibu wote walipatwa na mshangao. Akawaambia wazee kuwa pale kuna ndugu zo kadhaa ambao walikuja kwa nia ya kumtafuta Sungura, sasa nao wanapaswa kujumuika nao, Mzee Mapunda akasema itakuwa vizuri zaidi.
Ikaamuliwa kuwa waingie kwenye Prado ya Mzee Komba, na ile gari ya Matwiga aiendeshe Mzee Mapunda wakati Simba yeye ataingia kwenye gari pamoja na bwana harusi mtarajiwa. Suala ikabaki kwa Matwiga.
"Hebu sisi tutangulie, Matwiga atatufuata kwa sababu anapajua hadi msikitini ambapo ndoa inafanyika, jana tulienda kwa sheikh pale kufanya utaratibu wa ndoa hii, hivyo tumuacheni, akipenda atakuja!" Alisema Mzee Komba huku akiingia kwenye Prado yake na kusababisha Mzee Mapunda achomekee
"Huenda nae kaenda kujidhuru, maana hawa vijana mie kwa kweli sijawaelewa kabisa," wote wakacheka lakini Ngonyani, Simba na Sungura wao wakatazamana tu na kuingia garini kimya kimya, walijua ni wapi alipo mtu anae angushiwa lawama, msafara ukaanza.
Kutokana na jina kubwa la Matwiga na wingi wa majamaa alionao, umati ulikuwa ni mkubwa mno na hata kumshangaza Sungura na kufikia hatua ya kuingia woga ukizingatia hakuwa amejiandaa kwa tukio kama lile la ghafla, maana kichwani mwake hakuwahi kuota kuwa atakuja kufunga ndoa ambayo itahudhuriwa na watu wengi kiasi kile.
Lakini wakati yeye akiwa anaushangaa ule umma uliopo pale, karibu umma wote nao ulikuwa ukimshangaa yeye pia ambae kutokana na mavazi yake, alivyovaa alionekana kama yeye ndio bwana harusi wakati kwenye kadi za mwaliko kukiwa na jina jingine na tena la mtu wanae mfahamu karibu wote pale.
Kadi zilionyesha bwana harusi ni Matwiga Komba lakini sasa wanamuona kijana wa mtaani ambae hana uwezo wa ndoa kama ile, Sungura Katembo ndio kavaa kama bwana harusi.
Sheikh wala hakuwa na lingine zaidi ya kufungisha ndoa na hali ilikuwa ni tulivu kweli kweli watu wakisikilizia huenda anafungishwa kwa niaba. Lakini mwisho wa siku majina yakatajwa kuwa Sungura Katembo anamuoa Zainab Mapunda.
Mshangao ulijitokeza mkubwa mno, watu wakashindwa kuelewa ni kwa nini wamefanya vile, maswali yalikuwa ni mengi mno, lakini huyo wa kujibu ndio alikuwa hayupo, maana hata Matwiga hakuonekana pale msikitini.
Ngonyani na Simba wakati mishemishe za ndoa zikiendelea, wao mioyo yao ilikuwa haijatulia kabisa, wakachukua bodaboda na kuchomoka kuelekea kituo kikuu cha Polisi Songea ili kumdhamini Matwiga.
Walifanikiwa kwa sababu kesi yenyewe ilikuwa ni ndogo na wao walikuwepo wakati suluhu ikitafutwa. Wakarejea nae lakini akawaambia wao waende tu moja kwa moja msikitini nae anaelekea nyumbani kwanza kubadili nguo.
Jambo la kwanza aliuliza tu iwapo Sungura amekubaliana na ombi lao, walimjibu kuwa kila kitu kimekwenda vizuri, nae aliwaambia amefurahi sana kusikia Sungura amekubali kufunga ndoa na Zainab, alirejea nyumbani na kuingia maliwatoni na kujiswafi haraka haraka, kisha akaondoka kwa kasi na boda boda ili awahi msikitini.
Bahati nzuri akawakuta nao ndio wanatoka ndani ya msikiti kuelekea nyumbani kwa Mzee Mapunda alipo Bi harusi. Akaunganisha akiwa amedhamiria wamkute kule, na ndio hicho kilicho tokea.
Alifika na kwenda kwa mama yake aliempokea kwa kilio na kisha wakajituliza wenyewe hasa baada ya Matwiga kumwambia waoaji wapo njiani. Waliwasili na kumkuta Matwiga ambae aliwapokea na kuongoza kazi za pale nyumbani.
Sungura hakuamini pale alipomuona Matwiga pale, maana wale walio kwenda kumtoa wala hawakumuambia, akamkimbilia na kumkumbatia akiwa na tabasamu kubwa usoni, Matwiga nae akampokea kwa bashasha.
Akampa hongera kwa kufunga ndoa tena na mtu ampendae, wakakumbatiana tena na walipoachiana wakaongozana kuingia ndani na kwenda kumuona bibi harusi, Zainab Mapunda ambae aliangua kilio baada ya kumuona mumewe, Sungura bin Katembo.
Zainab hakunyanyuka wakati Sungura akiingia kutokana na kulia na mshituko alioupata, lakini alivyoingia Matwiga, Zainab akawa analia zaidi lakini akasimama kumpokea kaka yake ambae ndio alimtuliza kilio chake.
Matwiga akamuita Sungura na akasogea pale ana wapambe wake ambao aliwapatia msikitini kulekule, maana hakuwa na maandalizi kabisa ya aina yeyote hata kwa rafiki zake.
Furaha ikarejea na shughuli ikaendelea kama zilivyo pangwa. Sungura na Matwiga sasa walikaa pamoja na kubadilishana mawazo wakiwa ni wenye furaha kama vile hawajawahi kukwaruzana.
Jioni pakawa na sherehe fupi iliyo andaliwa kwa ajili ya kuwapongeza maharusi, ilikuwa ni fupi sana lakini ilifana mno, kila idara ikiwa imekamilika vema, Simba alisimama kwa upande wa bwana Harusi ili kutoa somo kidogo kwa maharusi.
Hakuwa ni mzungumzaji sana kwa kuwa hakuwa amejiandaa kwa tukio lile bali aliwashukuru sana wote waliofanikisha tukio lile. Upande wa mke alisimama Matwiga ambae alitumia muda mwingi mno kumsifu Sungura kwa uvumilivu alio uonyesha.
Mwisho wa nasaha zake akawaambia wao kama familia, wanatoa zawadi ya kuwafungulia kampuni ya kuagiza vipuri vya magari vilivyo tumika huko Japan na kuwakabidhi bahasha iliyokuwa na makabrasha yote.
Hivyo ndivyo ilivyo kamilika sherehe ya ndoa ya Sungura Katembo na Zainab Mapunda, wakati wakiwa wanatoka, Sungura akamuita shemeji yake na kumshika bega kwa upande wa kushoto huku upande wa kulia akiwa amesimama Zainab mkewe.
Wote walikuwa na sura zenye tabasamu pana na bashasha tele, akamwambia
"Matwiga shemeji yangu, nafikiri hakuna kinacho tufaa sisi kwa sasa zaidi ya kusameheana, na ninapenda mno kukushukuru kwa ndoa hii ambayo mimi sikuitegemea, hivyo ninaweza kuiita kuwa ni...http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
NDOA YA ZARI!"
Wazee walikuwa wamesimama pembeni kidogo wakiwatazama, tabasamu zikiwa kwenye nyuso zao, macho karibu zaid ya mia na ushei, yakawaona vijana wale
Wakicheka wote watatu kwa sauti ya juu na kukumbatiana, kisha wakaagana.
Maharusi ndani ya Bravis aliyokuwa akiiendesha Ngonyani, Matwiga nae akiwa dereva wa Prado akaiendesha familia yao hadi kwao.
MWISHO.
* * * * *
0 comments:
Post a Comment