Search This Blog

Friday, October 28, 2022

AHADI YA MAISHA - 4

 

     





    Simulizi : Ahadi Ya Maisha

    Sehemu Ya Nne (4)





    Alipata gari na kuanza kuelekea Ubungo, ilikuwa yapata saa kumi na moja, mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio akiwa anahisi alikuwa anachelewa kufichua ukweli wa uovu wa Frank Joseph. Baada ya dakika arobaini alikuwa amefanikiwa kufika katika eneo la hoteli hiyo iliyokuwa na ghorofa kadhaa na alikuwa akiwaza jinsi ambavyo angeweza kukutana na Winnie. Hakufikiria kama kulikuwa na ulinzi wa aina yeyote dhidi ya msichana huyo hivyo alipanga kueleza alikuwa rafiki yake. Aliongoza mpaka sehemu iliyokuwa ya mapokezi ambako baada ya kujieleza kuwa alifika eneo hilo kumwona bibi harusi mtarajiwa alielezwa aende ghorofa ya kumi na moja ya hoteli hiyo.

    Alitekeleza zoezi hilo lakini alipofika katika eneo la ghorofa hiyo alishtushwa na walinzi wawili wa kampuni moja ya ulinzi aliyoifahamu waliokuwa eneo hilo. Alionekana kama hakujali na alianza kutembea kuelekea katika chumba alichoelezwa Winnie alikuwapo. “we lidada unakwendaga wapi huko” alisikika mlinzi mmoja kwa lafudhi ya kisukuma

    “naenda kumwangalia rafiki yangu Winnie”alijibu Grace katika hali ya kujiamini lakini walinzi hao walimzuia na kumwambia eneo hilo walikuwa wanaingiwa wazazi wa Winnie na wakwe zake tu. Kauli hiyo ilimfanya aanze kuwabembeleza ili wampe nafasi ya kumwona kwa sekunde kadhaa tu lakini alikatazwa. Akiwa ameelezwa pia waliohurusiwa kuingia katika chumba hicho walikuwa wahudumu maalumu walioandaliwa kwa ajili ya kumhudumia. Aliomba kusaidiwa kwa muda wa nusu saa lakini hawakumwelewa wakidai angemwona siku iliyofuata iliyokuwa ya harusi. Aliamua kuondoka baada ya walinzi hao kuonesha dalili zote za kutaka kumpiga.

    Aliwatafuta watu tofauti hotelini hapo akiwaomba wamsaidie katika zoezi la kumwona Winnie lakini alishindwa kupata msaada huo. Mwishoe alipoteza matumaini akiwa nje ya hoteli hiyo huku akiwa hayuko tayari kuondoka akiwa hajaonana na Winnie. Majira ya saa mbili usiku waziri wa nchi mzee Joseph akiwa na mkewe alifika hotelini hapo lakini pia walikuwa na mzee mwingine mwafrika aliyekuwa na mkewe mzungu. Grace alitulia akijifanya hakuwaona lakini aligundua kuwa walikuwapo wazazi wa Winnie mbali na waziri na mkewe waliokuwa wazazi wa Frank. Baada ya saa moja walitoka huku wakiiongelea harusi ya wanao iliyopaswa kufanyika siku iliyofuata. “ harusi hii lazima iwe historia mjini hapa…” alisikika mzee Joseph wakati akipita kando yake kidogo huku yeye akionekana kama alikuwa na mawazo ya mbali sana.

    Baada ya kuondoka kwao ikiwa yapata saa tatu usiku hakuelewa jambo ambalo lingefuata zaidi alianza kusali akimwomba mwenyezi Mungu amsaidie katika harakati zake hizo. Jambo lililokuwa gumu kwake ni vile alivyokuwa ameelezwa kuwa Winnie hakuwa na simu eneo hilo wakihofia angechanganywa na watu. Baada ya kusali kwake kwa zaidi ya nusu saa alitulia akiwaza afanye nini kwa wakati huo. Ghafla liliwasili gari moja muundo wa ‘Jeep’ katika eneo hilo na mtu aliyeshuka alimtambua vizuri na alikumbuka vitu vingi juu yake. Alikuwa mwanamke aliyemtambua kuwa alikuwa mjane ambaye alimfahamu kwa jina la mama James, ambaye pia alikuwa akiabudu naye katika kanisa la ‘Christians Way To Lord’. “mama James, mama James….” Alimuita mama huyo ambaye aligeuka na kumfuata kabla ya kusalimiana kwao. “vipi mbona umekuja hapa” aliuliza Grace mara baada ya salamu. “mmh! hoteli hii ni ya familia yangu, mara baada ya kifo cha mume wangu nafika hapa mida hii kila siku kujua mauzo ya siku nzima” alisikika mama huyo. Grace alifurahishwa na maelezo hayo na kumweleza mama huyo kuwa alikuwa na tatizo ambalo aliamini angesaidiwa nalo. Walianza kutembea kuelekea katika ofisi ya mama huyo iliyokuwapo katika hoteli hiyo.Hakushangazwa sana na umiliki wa hoteli hiyo wa mama huyo kwani aliwahi kuelezwa kuwa alikuwa na uwezo kifedha.

    Mara baada ya kufika katika ofisi hiyo bila kupoteza muda Grace akiwa na uchungu alielezea mkasa mzima ulivyokuwa mwanzo mpaka mwisho na alimalizia na ombi lake la kuhitaji msaada wa kuonana na Winnie usiku huo. Mama James ambaye alisikitishwa na mkasa huo aliungana naye ikimuahidi kuwa lazima Winnie ajue jambo hilo. Alichukua simu yake ya mezani na kumpigia mmoja wa viongozi wa hoteli hiyo, alimuuliza kama kulikuwa na kitu ambacho wahudumu bado walikuwa hawaja mpelekea Winnie.

    “huyu dada hali chakula na alitueleza tusimpelekee usiku huu” alisikika kiongozi huyo. Mara baada ya maelezo hayo mama James alimweleza Grace kuwa ilimpasa aende kama mhudumu katika chumba cha Winnie kupeleka chakula. Alikuwa amemwagiza kiongozi huyo aandae chakula cha usiku cha Winnie na aliondoka na Grace hadi katika chumba kimoja ambacho alibadilisha nguo na kuvaa za wahudumu wa hoteli hiyo.

    Baada ya zoezi hilo tayari chakula hicho kilikuwa kimeandaliwa na aliondoka akielekea katika chumba cha Winnie akiwa na mwonekano tofauti. Alikwa amevaa miwani na kofia vilivyopoteza kabisa mwonekano wake wa sura. Alikuwa amebeba simu kwa ajili ya kumtaarifu mama James juu ya jambo ambalo lingeendelea, mara baada ya kufika katika chumba husika walinzi walimhurusu na aliingia katika chumba hicho cha Winnie. Ilikuwa yapata saa nne na robo usiku, alimshuhudia Winnie akiwa amelala kitandani huku akilia.

    “wewe niliwambia sihitaji chakula usiku huu….. nimechanganyikiwa mwenzenu” alisikika Winnie akiwa kitandani hapo akionekana alikuwa na mawazo sana. “sijaleta chakula nimeleta ukweli juu ya picha za utupu zilizotolewa dhidi ya George…” alisikika Grace akiongea kauli iliyomkurupusha Winnie eneo la kitandani na kumfuata katika sebule ndogo iliyokuwapo katika chumba hicho. “niambie jamani, niambie dada yang…”kabla hajamaliza sentesi hiyo ilisikika sauti nje ya chumba hicho. “halloo we lidada utokage huko haraka….”alikuwa mlinzi mmoja aliyekuwapo nje. Winnie alitembea haraka na kwenda kuwatuliza walinzi hao akiwaambia kuwa alihitaji muda ili aweze kuongea na mhudumu huyo kwa vile alikuwa mpweke siku nzima. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda mbio akiwa na hamu ya kujua kile alichodokezwa na mhudumu aliyefika hotelini hapo. Mara baada ya kufunga chumba hicho alianza kurudi eneo alilokuwa amemwacha mhudumu huyo ambapo alimwona akiwa ametoa miwani aliyovaa na kofia. Kumbukumbu zake zilimbainishia kuwa alikuwa ni msichana aliyetolewa gazetini na George wakiwa katika hali ya utupu.

    Jambo hilo ndilo lilimpa hamasa ya kuutaka ukweli wote, bila kupoteza muda Grace aliomba radhi kabla ya kuanza kueleza kila kitu juu ya tukio zima la picha hizo zilizotolewa magazetini karibu mwaka mmoja uliokuwa umepita. Baada ya robo saa ya kusimuliwa Winnie alikuwa ameishiwa nguvu huku machozi yakimtoka pasipo kujielewa. Alikuwa akisikika kwa sauti ya chini akimwomba msaada Grace wa kuondoka eneo hilo. Bila kupoteza muda Grace aliyemwonea huruma sana, alimpigia simu mama Jamaes na kumweleza juu ya kila kitu kilichoendelea.

    Mama huyo aliahidi kutoa msaada kwani baada ya dakika kadhaa mhudumu mwingine alifika katika chumba hicho na kwa haraka alivua nguo alizovaa kabla ya Grace na mhudumu huyo kusaidiana kumvalisha Winnie nguo hizo. Baada ya kuzivaa, alikuwa akionekana kama mhudumu na imani yao iliwaeleza kuwa walizi wangedhania kuwa Winnie alikuwa mhudumu kwani pia alivaa kofia na miwani kama ilivyokuwa kwa Grace. Alimpa ushauri wa haraka uliomjenga Winnie, akimweleza wajitahidi waokoe uhusiano wake na George uliopoteza dira kwa kiasi kikubwa. Winnie aliyeonekana kupata jambo ambalo alilitafuta kwa muda mrefu, alipata nguvu za ghafla na aliacha kulia kabla ya kumwongoza Grace kutoka eneo la chumba hicho.

    Walifanikisha zoezi hilo na kuondoka hotelini hapo kwa gari la mama James wakiwa wanaelekea Vingunguti ambako Grace alidai alikuwa na picha zaidi za tukio hilo na nyingine alizopiga na Frank wakati wa sherehe ya kupongezana dhidi ya tukio walilolifanya. Njiani Winnie alianza kulia tena kwa sauti akimlaumu Grace kwa kuhusika na suala zima la kuharibu maisha yake zaidi alikuwa akilitaja jina la George na kumwomba kijana huyo msamaha kama walikuwa wote muda huo. “nimekosa nini mimi jamani, nimemtesa George wangu pasipo sababu….” Alikuwa akilalamika Winnie wakati wakielekea nyumbani kwa kina Grace.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipofika huko alithibitisha zaidi kuwa kila kitu kilikuwa ni kweli juu ya mambo aliyoelezwa. Hakuwa na jambo la kuongea zaidi ya kumwomba mama James ampeleke Bunju ili akakutane na familia ya mzee Innocent kwa ajili ya kuiomba msamaha. Zaidi alikuwa akiwaza kwenda katika gereza la Ukonga siku iliyofuata ili kumwomba radhi George pia kwa kila jambo lilokuwa limetokea. Majira ya saa nane usiku gari walilokuwa nalo lilikuwa nje ya geti la mzee Innocent katika maeneo ya Bunju ambako Winnie akiwa analia aliwaomba walinzi aonane na mzee huyo usiku huo. Baada ya kukataliwa ka muda wa saa zima ndipo alipopata nafasi ya kuonana na wazazi hao wa George, aliingia akilia kabla ya kwenda kuwakumbatia na kila mmoja. Walikuwa wametoka usingizini na walikuwa hawaelewi jambo lolote lililoendelea.

    Mama James ndiye aliyechukuwa jukumu la kuuelezea mkasa mzima ulivyokuwa umetokea mpaka kupelekea ujio wao usiku huo. Aliwaeleza kila kitu akianzia picha za utupu ambazo mtoto wao alitolewa nazo magazetini, wakati huo Grace alikuwa mnyonge huku akimfariji Winnie aliyekuwa akilia. Mzee Innocent na mkewe ambao pia walilia kusikia tukio hilo walianza kumfariji Winnie pia. Ingawaje walilia lakini pia walionekana kufarijika kwani waliamini kijana wao angerudi katika ubinadamu wa kawaida baada ya kuchanganyikiwa kwa muda mrefu juu ya kuachana na Winnie. Baada ya muda walikuwa wametulia kwa kiasi kikubwa na walianza kupanga mikakati mbalimbali huku wakiamini mkono wa waziri wa nchi mzee Joseph haungekuwa mbali katika tukio hilo. Siku iliyofuata walipanga kwenda kumweleza George juu ya kila jambo lililokuwa limetokea na baada ya tukio hilo walipanga kwenda kufungua mashtaka dhidi ya Frank, mtoto wa waziri kwa kuhusika na kupigwa kwa picha za utupu dhidi ya George akiwa hana fahamu.

    Hawakupata usingizi,hususani Winnie ambaye macho yake yalikuwa makavu akiwa ametawaliwa na mawazo usiku mzima. Majira ya saa kumi na mbili asubuhi walianza kujiandaa kwa ajili ya ratiba hiyo waliyokuwa wameipanga. Ghafla walisikia mlio wa vin`gora vya magari ya polisi yaliyosikika kama yalikuwa nje ya geti kuu la nyumba ya mzee Innocent. Baada ya muda mfupi magari ya polisi zaidi ya nane yaliingia katika eneo la mbele ya nyumba hiyo. “Mungu wangu tumekosa nini sisi?” alisikika mzee Innocent wakati akifunua pazia la nyumba yake kabla ya kumwona waziri wa nchi mzee Joseph akishuka na mwanaye katika moja ya gari zilizokuwapo nje. Pia kulikuwa na watu wawili mwanaume na mwanamke waliokuwa wameoneshwa bunduki huku mikono yao ikiwa kichwani.





    Wakati huo Winnie alikuwa alilia akiwa amechanhganyikiwa juu ya kila kitu kilichoendelea. Ghafla mlango wa nyumba hiyo uligongwa na mzee Innocent alitii hodi hiyo na kwenda kuufungua mlango. Mtu wa kwanza kuingia eneo hilo alikuwa mzee Gregory akiwa amenyosha mikono yake akifuatiwa na mkewe aliyefanya hivyo pia, wote kwa pamoja walikuwa wakilia. Baada ya kuingia kwao walifuata askari wanne waliokuwa na bunduki huku wakiwa wamewaoneshwa na mwishoe waziri na mwanaye Frank waliingia. Winnie alilia kwa sauti akiwa haamini kuwa wazazi wake pia walikuwa katika hatari iliyowafanya hata wao walie.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “wewe binti ulitoka Ufaransa kuja kuniaibisha na familia yangu….ehh” alisikika waziri huyo wa nchi akiwa amemkazia macho Winnie aliyekuwa akilia. “sasa sikiliza sihitaji kumwaga damu ila nataka ufunge harusi na mwanangu kisha baada ya hapo wazazi wako watakuwa huru…” aliongea tena kauli iliyomchanganya Winnie akili yake kabisa na kubaki kimya kama alikuwa hana akili timamu. Alikuwa akijiuliza jambo lililokuwa bora kati ya kuokoa maisha ya wazazi wake au kujenga upya uhusiano wake na George. Wazazi wake walikuwa wakilia huku wakisisitiza akubali agizo hilo wakati mzee Innocent na mkewe pia walimwoneshea ishara ili akubaliane na waziri huyo.

    Kutokana na upendo aliokuwa nao kwa wazazi wake alitingisha kichwa kuashiria kukubaliana na agizo hilo. Baada ya kufanya hivyo waziri alimpigia makofi ya kumpongeza kwa uamuzi wake, hata nyuso za wazazi wake zilionekana kupata faraja kwa kiasi kidogo. Mwanaye Frank alikuwa kimya akionekana kwa kiasi kikubwa alikuwa hajafurahishwa na tukio hilo lililomweka njia panda juu ya harusi yake na Winnie. Ghafla walishtushwa na mngurumo wa magari ya askari yaliyokuwa zikiondoka eneo hilo la nyumba ya mzee Innocent. Waziri wa nchi mzee Joseph alisogelea pazia la nyumba hiyo kabla ya kuangalia nje na kushuhudia askari hao aliofika nao wakiwa wanaondoka.

    “nani mpuuzi kawahurusu hawa waondoke?” aliongea kwa jazba mzee Joseph kabla ya kuanza kutembea haraka akielekea nje ya nyumba hiyo. Mara baada ya kutoka nje hakumshuhudia mtu zaidi ya gari moja la kifahari aina ya Mercedez Benz ambalo awali halikuwapo eneo hilo la nyumbani kwa mzee Innocent. Lakini pia kulikuwa na gari ambalo alifika nalo akiwa na mwanaye. Tayari watu wote walikuwa wametoka nje ya nyumba hiyo huku mzee Gregory na mkewe wakiwa bado wamenyoosha mikono juu. Askari wanne waliokuwa wamewaoneshea bunduki walikuwa wakisikiliza maelezo kutoka kwa waziri huyo. Punde mlango mmoja wa gari hilo lililokuwapo hapo nje ulifunguliwa na mtu aliyeshuka alikuwa kiongozi mkubwa sana wa jeshi ambaye alijulikana vizuri nchini. “nyie acheni kumtisha balozi kama mateka na mkewe na ondokeni eneo hili haraka iwezekanavyo….” Alitoa amri hiyo kiongozi huyo mkubwa wa jeshi akiwa amewanyoshea mkono askari waliokuwa wakimshikilia balozi wa Ufaransa nchini mzee Gregory na mkewe.

    Amri hiyo waliitii na askari hao waliondoka wakikimbia katika eneo hilo la nyumba ya mzee Innocent kutokana na heshima yao kwa kiongozi huyo wa jeshi. “wewe unajifanya unaijua nchi hii zaidi siyo….eeh” alilalama mzee Joseph kauli ambayo hakujibiwa. Sura ya Winnie na wote waliokuwapo eneo hilo mbali na waziri na mwanaye zilipata faraja kutokana na amri za kiongozi huyo mkubwa wa jeshi. Ghafla wakati kukiwa hakuna jambo jingine aliloongea kiongozi huyo, ziliingia pikipiki tatu kwa kasi ya ajabu ambazo watu waliokuwa wakiendesha walivaa nguo za kijeshi. Pikipiki hizo ziliegeshwa kando yao na zilielekezwa katika geti kuu la nyumba hiyo tayari kwa kuondoka. Mmoja wa watu waliokuwapo katika pikipiki hizo alikuwa na nguo hizo za kijeshi tofauti na wenzake. Watu hao walikuwa wamevaa kofia maalumu za pikipiki kwa ajili ya kujikinga kichwa na ajali kwa hiyo hakuna mtu aliyeweza kuwatambua.

    Kiongozi huyo wa jeshi alimwoneshea ishara Winnie kwa mkono akimtaka apande katika pikipiki ya mwanajeshi aliyekuwa na nguo tofauti na wenzie. Winnie alisita kidogo lakini nyuso za wazazi wake na zile za wazazi wa George zilionesha wazi nia ya kuhitaji akubali ishara hiyo. Bila kupoteza muda aliisogelea pikipiki hiyo na kuvaa kofia maalumu ya pikipiki iliyokuwapo imeshikizwa katika sehemu ya kukaa ya pikipiki hiyo. Mara baada ya zoezi hilo alipanda pikipiki hiyo, Frank alikuwa akiangalia kwa uchungu kila jambo lililokuwa likiendelea na alianza kuamini kuwa harusi yake na Winnie haingekuwapo tena. Hasira alizokuwa nazo alitamani kumzuia mrembo huyo aliyeonekana alikuwa akimchukia ghafla lakini aliwahofia wanajeshi waliokuwa katika pikipiki hizo. Alipopanda pikipiki hiyo, zote tatu ziliondolewa kwa kasi eneo hilo na kumfanya Frank aoneshe dalili ya kuchanganyikiwa wazi wazi.

    “sawa wewe umeshinda lakini elewa mchezo ndio unaanza…tuondoke” alisikika mzee Joseph akimwambia kiongozi huyo mkubwa wa jeshi kabla ya kumwambia mwanaye waondoke eneo hilo. Waziri huyo na mwanaye waliondoka na gari lao huku wakiwa na jazba kupindukia juu ya kuharibiwa kwa mipango yao. Kiongozi huyo wa jeshi alitabasamu kisha akasikika “msihofu Winnie yuko salama….. ninaenda kuendelea na taratibu juu ya tukio hili zaidi” alisikia kiongozi huyo mkubwa wa jeshi kabla ya kuondoka na gari hilo aina ya Mercedez Benz.

    Mzee Innocent na mkewe walisikika wakishangilia hali kadhalika wazazi wa Winnie walifurahia tukio hilo, walionekana wakikumbatiana na kuoneshana upendo. Ni wakati ambao wazazi wa Winnie waliweza kuujua ukweli juu ya picha ambazo George alitolewa akiwa mtupu mwaka mmoja uliokuwa umepita. Mara baada ya maelezo hayo yaliyotoka kwa Grace na mama James, waliweza kugundua sababu iliyokuwa imepelekea wao kutekwa. Waligundua kuwa waziri wa nchi mzee Joseph hakuwa tayari kukumbana na aibu ya mwanaye kukimbiwa siku ya harusi baada ya Winnie kuutambua ukweli dhidi ya hila alizofanyiwa George. Waliondoka eneo hilo la nyumbani kwa mzee Innocent wakiwa na lengo la kwenda kumtazama George katika gereza la Ukonga.

    * * * *

    Winnie alikuwa haelewi sehemu ambayo wanajeshi waliomchukua walikuwa wanampeleka. Pikipiki hizo zikuwa kwenye kasi kubwa wakiwa wameshika barabara iliyoelekea Bagamoyo hakuwa na hofu sana juu ya watu hao. Aliamini kama walikuwa wameweza kumwokoa katika harusi iliyokuwa afunge na Frank, pia hawangemdhuru. Alikuwa katika pikipiki ya mwanajeshi ambaye alionekana kuwa ni mwembamba, lakini pia alikuwa mtulivu kwani hakugeuka wala kutikisika. Muda wote alikuwa amelekeza kichwa chake barabarani akiongoza pikipiki hiyo huku wakifuatwa na wanajeshi wengine nyuma. Pikipiki hizo ziliongozwa mpaka kwenye hoteli moja ya kifahari maeneo ya Bagamoyo, yeye alitoa kofia ya pikipiki aliyokuwa amevaa wakati wanajeshi hao hawakufanya hivyo.

    Walimwoneshea ishara awafuate wakati wakiwa wameanza kuingia katika eneo la ndani la hoteli hiyo, alitekeleza amri hiyo huku akiwa na hofu tele baada ya kuona wanajeshi hao hawakuvua kofia hizo za pikipiki. Hatimaye waliishia kuingia katika chumba kimoja na watu hao walikuwa kimya kwa muda wakimwangalia jambo lililomwongezea hofu zaidi.

    Mmoja wao aliamua kuanza kuvua kofia hiyo ya pikipiki, mara baada ya kutekeleza zoezi hilo Winnie alipatwa na mshtuko zaidi. Alikuwa anamfahamu mtu huyo kwa jina la Tabangu na wakati huo alijua kuwa alikuwapo jela baada ya kusomewa kesi ya mauaji dhidi ya Henry, aliyekuwa baba yake mdogo George. Tayari alitambua kulikuwa na shari dhidi yake hali iliyopelekea aanze kutokwa na jasho kwa woga kwa vile watu hao bado walikuwa hawajaongea jambo lolote.

    Mwingine tena alianza kutoa kofia hiyo mbali na yule aliyekuwa naye kwenye pikipiki, mara baada ya kuitoa alimtambua alikuwa mtoto wa kiongozi mkubwa nchini, ambaye awali alikuwa rafiki wa karibu wa George kabla kwenda masomoni Marekani. Kijana huyo aliyeitwa Sabinus alitabasamu huku akimwangalia pasipo kusema kitu. Jambo hilo bado lilimwogopesha kwani alikumbuka kuwa hata Frank Joseph alikuwa rafiki wa karibu wa George na ndiye aliyeharibu uhusiano wao. Akiwa ametambua kuwa watu hao siyo wanajeshi alianza kumwangalia wa mwisho kati yao aliyekuwa na mavazi tofauti na yao. Mtu huyo alianza kutoa kofia hiyo kabla ya sura yake kuonekana akiwa na makovu kadhaa, Winnie aliruka kwa furaha na kumkumbati baada ya kubaini alikuwa ni George.

    Tabangu na Sabinus walikuwa wakicheka jinsi ambavyo Winnie alikuwa ameingiwa na woga juu yao. Mara baada ya furaha hiyo alitaka kujua jambo lililokuwa limetokea mpaka wakati huyo. George aliyekuwa amekonda akiwa na makovu kadhaa kama alivyokuwa amemwona siku mbili kabla alianza kumwelezea mkasa mzima. Alimweleza juu ya picha za utupu alizokuwa ametolewa ambazo ziliandaliwa na Frank pia alimsimulia juu ya kifo cha baba yake mdogo, Henry ambaye aliuawa na Frank pia. Winnie akiwa analia na kujuta kuwa na uhusiano na Frank, aliambiwa na George kuwa mambo hayo yote alikuwa ameelezwa na Tabangu aliyehusika nayo kabla ya kusingiziwa kuwa yeye ndiye muuaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alielezwa kuwa Sabinus akimtumia baba yake aliyekuwa kiongozi mkubwa nchini ndiye aliyefanikisha kutolewa kwao jela. Alifanikisha hilo baada ya kuelezwa mambo yote yaliyokuwa yanahusiana na Frank Joseph aliyeshirikiana na baba yake. Hapo ndipo Winnie aliyekuwa akilia huku akimwomba msamaha George aliweza kutambua kila kitu juu ya Frank Joseph mtoto wa waziri wa nchi. Alikuwa ameelezwa kuwa taratibu zote zilikuwa zikiendelea ili kijana huo akamatwe na kufunguliwa mashtaka dhidi yake.

    Sabinus alikuwa ameshatoa fedha za malipo kwa ajili ya mapumziko ya Winnie na George katika hoteli hiyo kwa muda wa wiki moja ili wapange mipango ya maisha yao. Hatimaye Tabangu na Sabinus waliwaacha wakiwa na furaha huku wakiamini walikuwa wameokoa ahadi yao iliyokuwa ianataka kupotea. Muda wote Winnie alikuwa hajiamini akifikiri George angemkataa wakati wowote. Furaha hiyo kwake iliambatana na kilio kwani alikuwa akisimuliwa mambo ambayo George alikuwa amekumbana nayo na hivyo alijiona mkosaji.

    Majira ya jioni wazazi wao wakiwa na furaha walifika hotelini hapo baada ya kuelezwa na Sabinus eneo walilokuwapo. Waliwawekea ulinzi wa askari kadhaa lengo haswa lilikuwa kulinda uhusiano wao usivunjike tena kwa mara ya pili. Mzee Gregory alikuwa na wasiwasi wa kuolewa kwa mwanaye na George hivyo alihitaji mipango ya harusi iandaliwe haraka. Jioni ya siku hiyo wakiwa bado wako na wazazi wao vyombo vya habari vilitawaliwa na taarifa ya kukamatwa kwa Frank akishutumiwa kwa kuua lakini pia kuhusika na hila ya kumpiga George picha za utupu akiwa hana fahamu.

    George na Winnie walikuwapo katika hoteli hiyo kwa muda wa wiki moja huku matibabu yakiendelea dhidi ya George ikiwa ni pamoja na kujenga mwili wake. Walikuwa na furaha huku wakiamini ahadi yao ilikuwa inaelekea kutimia, kesi ya Frank ilikuwa imepangwa kusomwa baada ya miezi mitatu. Ni wakati ambao wazazi wao waliamua kuwaandalia safari ili waende nchini Uholanzi kwa mapumziko zaidi kabla ya kurudi Tanzania kwa harusi yao. Lengo lao lilikuwa ni kuona Frank aliyekuwa mtoto wa waziri akipewa hukumu aliyostahili na baada ya hapo waliamini hakuna mtu ambaye angewafuatilia tena George na Winnie. Baada ya maandalizi yote ya safari hiyo waliondoka nchini wakielekea katika nchi hiyo ya Uholanzi, waliondoka pasipo kuwajulisha watu zaidi ya marafiki wa karibu wa familia hizo.

    * * * *





    * * * *

    Vyombo vya habari nchini vilikuwa vimetawaliwa na matukio yaliyohusiana na mtoto wa waziri nchi, kijana Frank Joseph. Jambo mojawapo lilihusiana na aibu aliyoipata na familia yake katika siku ya harusi kwani waalikwa wengi walifika kanisani na kugundua kuvunjika kwa harusi hiyo. Magazeti mengi yaliyowahi kuandika habari tofauti kuhusiana na uovu ambao George alifanyiwa hila, waandishi wake walijitahidi kila wawezalo kukanusha mambo yote yaliyozushwa juu ya kijana huyo. Habari kubwa zilikuwa kwa kijana Frank aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka tofauti huku kubwa likiwa ni la kuua. Waandishi wengi walikuwa wakielezea uwezekano mdogo wa sheria kuchukua nafasi yake hasa kutokana na wadhifa wa mzazi wa kijana huyo katika nchi. Ilikuwa inasusbiriwa kwa hamu siku ya hukumu ili haki itendeke, watanzania wengi walioufuatiliwa mkasa wa George kupitia vyombo vya habari tokea awali walikuwa wakitoa ushauri wao wakihitaji sheria ichukue nafasi yake.

    Waziri wa nchi mzee Joseph alikuwa amechukizwa baada ya kugundua viongozi wengi wa nchi walikuwa upande wa mzee Innocent na balozi wa Ufaransa nchini mzee Gregory ambao walikuwa wazazi wa George na Winnie. Lakini bado hakuwa tayari kushuhudia mwanaye akienda jela ilhali akiwa bado kiongozi mkubwa pia wa nchi. Aliwaza kufanya kila awezalo ili kuhakikisha mwanaye anaukwepa mkono wa sheria. Wakati huo alishindwa kufanya jambo lolote kwani mwanaye alikuwa chini ya ulinzi mkali. Akiwa anaumia dhidi ya tabu alizoendelea kuzipata mwanaye huyo akiwa chini ya jeshi la polisi alitamani siku ya hukumu ifike ili mwanaye aachane na shida hizo. Alikuwa akiamini kuwa siku ya hukumu ya mwanaye ilikuwa ndio siku ya mwisho kwake kuwa chini ya mkono wa sheria.

    Hatimaye miezi mitatu iliisha na Julai mosi majira ya asubuhi, ikiwa ndio siku ya hukumu ya Frank Joseph, watu wengi walifika katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu ili kusikiliza kesi iliyokuwa inamkabili kijana huyo. Watu wengi walikuwa wakimwangalia waziri wa nchi mzee Joseph ambaye hakuonesha hali ya kuhuzunika dhidi ya kesi hiyo ya mwanaye. Akiwa katika tabasamu la wastani lililowachanganya watu waliofika mahakamani hapo, moyoni alikuwa akihuzunika na jinsi mwanaye alivyokuwa amevima usoni kutokana na kipigo alichoamini alikuwa amekipata.

    Kesi hiyo ilianza kuendeshwa huku ikiwa na ushahidi wa kutosha kutoka kwa Tabangu na Grace Stephen waliohusika na matukio ya Frank Joseph. Lakini watu ambao walimuudhi na kumchanganya akili yake mzee Joseph na kupanga kufanikisha jambo dhidi yao walikua askari wanne ambao aliwakuta eneo la tukio la mauaji aliyofanya mwanaye.Aliwapa onyo la kutotoa siri hiyo lakini walikuwa wamekiuka agizo hilo wakiwa tayari kwa ajili ya kutoa ushahidi. Kesi hiyo iliendeshwa huku Frank akikubali kila shtaka alilosomewa, alionekana alikuwa tayari kwa hukumu iliyokuwa mbele yake. Mwishoe hukumu yake iliyopelekea furaha za watu mahakamani hapo ilikuwa adhabu yake ya kifungo cha maisha.

    Mzee Joseph hakuonesha mshtuko wowote zaidi ya kuondoka mahakamani hapo akiacha watu wakifurahia hukumu hiyo lakini aliamini hawakujua jambo lililokuwa linaendelea. Askari wanne walioshuhudia mauaji ya mwanaye dhidi ya Henry walitoa ushahidi wao pasipo kuhusisha uwepo wake katika tukio hilo. Alipanga kufanya zoezi la kumwokoa mwanaye kabla ya kushughulika na watu hao sita waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ya mwanaye. Aliliendesha gari lake kwa kasi na hatimaye alifika nyumbani kwake maeneo ya Masaki, bila kupoteza muda aliongoza chumbani kwake na mara baada ya kuketi kitandani aliichukua simu yake. Alichagua majina kadhaa na mwishoe alipiga katika namba iliyoandikwa `Mkuu wa Gereza`, alisubilia kidogo hatimaye ilipokelewa.

    “haloo mkuu, sasa milioni ishirini unazozihitaji zipo ila namhitaji mwanangu usiku wa leo ili nimtoroshe kabisa katika nchi hii….. naona walimwengu wamechachamaa” alisikika mzee Joseph mara baada ya kusalimiana na mtu huyo

    “usipate taabu hili gereza liko chini yangu.. sasa saa tano usiku nitamleta mwanao nyumbani kwako, ila andaa taratibu zote za kumtorosha nchini kabisa pia usivunje ahadi….” Alisikika mtu huyo aliyeonekana alikuwa mkuu wa gereza. Baada ya mazungumzo hayo ya muda mfupi waliahidiana kukamilisha taratibu zote nyumbani hapo kwa mzee Joseph.

    Alikuwa ameongea na mkuu wa gereza ambalo Frank alipaswa kwenda kufungwa hivyo alikuwa na uhakika wa kumpata mwanaye kupitia fedha alizokuwa ameahidi. Tayari alikuwa amewaandaa vijana wake ili wafanikishe safari ya mwanaye kuelekea visiwa vya Madagascar wakitumia boti. Kulikuwa na gari mbili za vijana wake ambazo zilipaswa zimpeleke maeneo ya bahari ya Hindi ili safari hiyo ianze usiku huo. Majira ya saa tano usiku liliwasili gari moja dogo la mizigo nyumbani kwa waziri wa nchi mzee Joseph ambalo lilikuwa likiendeshwa na Mkuu wa Gereza aliyekuwa peke yake. Kwenye bodi la gari hilo kulikuwa na magunia mahindi, bila kupoteza muda vijana wa mzee Joseph walilisogelea gari hilo na kushusha gunia moja ambalo ndani yake walipolifungua alitoka Frank katika gunia hilo lililokuwa na mahindi kidogo.

    Kijana huyo mtoto wa waziri aliongozwa mpaka kwenye gari zilizopaswa kumpeleka katika maeneo ya bahari ya Hindi tayari kwa kusafiri. Kabla hajaingia mzee Joseph alimsogelea na kuanza kusikika kwa sauti ya chini “inakubidi ukatulie huko mambo yamekaa vibaya nitaangalia uwezekano wa wewe kuondoka tena nchini Madagascar ikibidi” “sawa baba nashukuru..” alijibu Frank kabla ya kuingia kwenye gari kisha kuondoka kwao kwa kasi eneo hilo la nyumba ya mzee Joseph.

    “nashukuru fedha zako hizi hapa…” alisikika mzee Joseph akimkabidhi mkuu wa gereza begi dogo lenye pesa, mara baada ya kuzihakisha fedha hizo mkuu huyo aliingia kwenye gari alilofika nalo na kuliondoa kwa kasi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku iliyofuata vyombo vya habari vilitawaliwa na taarifa za kutoroka kwa mtoto wa waziri akiwa gerezani katika mazingira ya katatanisha. Watu wengi walianza kuhisi tukio hilo lilihusiana na mpango mzima wa waziri wa nchi mzee Joseph. Walikuwa wakiamini kuwa lilikuwa jambo gumu kwa kiongozi huyo kushuhudia mwanaye akihukumiwa hukumu ya kifungo cha maisha na yeye kubaki kimya. Jambo lililokuwa gumu lilihusiana na uthibitisho wa kumhusisha waziri huyo na kutoroka au kutekwa kwa mwanaye akiwa gerezani. Mzee Joseph alitoa tamko kwa uongozi wa gereza husika akidai kuwa alihitaji kuona mwanaye anapatika haraka iwezekanavyo. Aliongea mambo hayo ambayo wananchi wachache walianza kuhisi hakuhusika na kutoroka kwa mwanaye. Alisisitiza kauli ya kumhitaji mwanaye akiwa na uchungu wakati akihojiwa na vyombo tofauti vya habari.

    Mzee Joseph alionekana kama mtu mwenye hasira juu ya kutoonekana kwa mwanaye akiwa katika gereza alilopangiwa. Lakini moyoni alikuwa na furaha juu ya kila jambo alilokuwa amefanikisha tayari alikuwa amelezwa mwanaye alikuwa amefika salama katika jimbo la Antseranana nchini Madagascar. Hakuwa na hofu dhidi ya mwanaye aliyehitaji awe mafichoni katika nchi hiyo kwani alikuwa na ulinzi wa vijana wawili. Wakati huo akiwa anaonekana kama mwenye huzuni juu ya kutoweka kwa mwanaye gerezani aliwatuma vijana kadhaa waliokuwa wakiwafuatilia Grace, Tabangu pamoja na askari wanne waliotoa ushahidi katika kesi ya mwanaye. Jioni ya siku hiyo alipata taarifa kuwa watu hao walikuwa wakilindwa na jeshi la polisi baada ya kuomba msaada huo wakihofia uhai wao kutokana ushahidi waliokuwa wameutoa. Mzee Joseph alikubaliana na maelezo hayo lakini aliamini lazima siku moja wangeipata adhabu aliyokuwa ameipanga dhidi yao.

    Frank Joseph alikuwapo katika hoteli moja ya kifahari iliyokuwapo katika ufukwe wa jiji la Antseranana nchini Madagascar, muda wote alikuwa katika chumba alichofikia akionekana kuwa na mawazo. Alikuwa na vijana wawili walioajiliwa na baba yake kwa kazi kubwa ya kumlinda. Hakupata shida ya pesa kwani alikuwa ametumiwa na baba yake fedha za kutosha. Alikuwa akiendelea kutimiza agizo alililoliona gumu la kutulia katika nchi hiyo alilopewa na baba yake. Akili yake kwa kiasi kikubwa haikuwa sawa na agizo hilo aliona halikuwa rahisi kwake kulitimiza alikuwa akiwaza kufanya jambo ili kupoteza maisha ya George na Winnie kabisa. Alikuwa anaona bora afanye mauaji ya watu hao ndipo ajipeleke kwenye vyombo vya usalama mwenyewe. Hakuwa tayari kuishi huku akisikia watu hao walikuwa katika ndoa. Jambo hilo ndilo lilimfanya muda wote awe akiongea kwenye simu lengo kubwa likiwa kuwapeleleza watu hao.

    “ aaah! sasa mchezo umeisha….” Alisikika kwa sauti ya juu siku moja mara baada ya kukata simu yake. Alikuwa amepata taarifa kutoka kwa rafiki yake wa karibu aliyewahi kumsaidia kutenganisha uhusiano wa George na Winnie ambaye alimweleza kila kitu juu ya watu hao aliodai walikuwapo nchini Uholanzi. Alikuwa amemtajia jimbo walilokuwapo mpaka hoteli ambayo walikuwa nchini humo. Mtu aliyempa taarifa hizo halikuwa katika nchi hiyo jambo lililompa imani Frank Joseph juu ya vitu alivyokuwa ameelezwa. Bila kupoteza muda alichukua hati yake ya kusafiria kabla ya kuchukua fedha zake zote.

    Hakuchukua hata nguo moja kati ya chache alizokuwa nazo katika hoteli hiyo. Alitoka katika chumba chake na kuwaeleza vijana waliomlinda kuwa alihitaji kutembea kidogo baada ya kuwapo katika chumba hicho bila kutoka kwa siku kadhaa. Vijana hao walimhurusu kwa vile waliona hakuwa amebeba kitu chochote ambacho kingewapa shaka kuwa alikuwa akitoroka. Aliondoka katika hoteli hiyo kabla ya kuingia katika mitaa ya jimbo hilo akiwa na lengo kubwa la kuandaa safari yake kuelekea nchini Uholanzi. Siku iliyofuata Frank alifanikiwa kusafiri akielekea Uholanzi kila jambo lilikuwa sawasawa na mipango yake, wakati huo alikuwa akiwaza kuua tu.

    * * * *

    George na Winnie walikuwa katika hoteli moja iliyokuwapo katika jimbo la Tilburg lililokuwa kusini mwa nchi hiyo ya Uholanzi. Katika miezi mitatu walioyokuwapo tayari George alirudiwa na mwonekano wake wa kuvutia zaidi ya vile alivyokuwa wakati akiwa katika chuo kikuu cha Dar es salaam. Ni wakati ambao Winnie pia alihitaji ndoa yao ifungwe haraka akihofia kumkosa kijana huyo mtanashati, hilo lilikuwa wazi kwani walikuwa wakisifiwa kwa mwonekano wao wakiwa nchini humo. Zaidi alikuwa hajiamini kwani warenbo wengi wakizungu walionesha nia ya kumhitaji George, tabia ya wivu aliyojijengea ndio iliyoongeza upendo katika uhusiano wao. Kwani muda wote Winnie alikuwa karibu na George na hakutaka kuwa mbali hata kidogo na kijana huyo. Siku zote hakuhitaji kabisa kusikia yaliyokuwa yamejili mwaka mmoja na nusu uliokuwa umepita. Alipenda kumwangalia George kama mtu waliyekuwa wamekutana naye ndani ya siku kadhaa zilizokuwa zimepita.

    Tayari walikuwa wameshazunguka majimbo kadhaa nchini humo wakifurahia uhusiano wao, walikuwa wamebakiwa na wiki mbili ili warudi Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya harusi yao. Jambo hilo ndilo liliwafanya waandae ziara moja katika hifadhi ya wanyama iliyokuwapo katika jimbo la Breda lililokuwa kaskazini magharibi mwa jimbo hilo la Tilburg walilokuwapo. Ziara hiyo ilikuwa ni ya siku tano kabla ya kurudi kwao nchini Tanzania. Siku hiyo ilipofika waliandaa mizigo yao tayari kwa safari hiyo na walikuwa wakiongozwa na kampuni moja iliyohusika na kutembeza watalii nchini humo. Hatimaye majira ya saa nne waliondoka katika hoteli hiyo waliyokuwapo na gari la shirika hilo lililohusika na wataliii. Nyuma yao lilionekana gari moja lililokuwa la rangi ya bluu ambalo liliwafuata nyuma wakati wakielekea katika jimbo la Breda.





    Baada ya saa tano walifika katika eneo la hifadhi ya taifa ya Steenwijk, walikuwa wakishusha mizigo katika gari walilokuwa wamelitumia. Wakati wakiendelea na zoezi hilo huku wakiwa katika eneo la mbele la ofisi za hifadhi hiyo, George hakuwa na furaha na alionesha hofu ya wazi kama kulikuwa kuna kitu kilikuwa kikiendelea. “Whats the problem George, I don’t understand you……” (“ kuna tatizo gani George sikuelewi….” alisikika Winnie akimuuliza George baada ya kuona alikuwa amebadiliaka ghafla. Kauli hiyo iliwafanya hata waongozaji wa watalii waliokuwa nao wamsikilize George akijibu juu ya hofu aliyokuwa nayo ghafla.

    “Some bastards are here, they wants to ruin our life again” (“kuna wanaharamu wako hapa wanataka kuyahalibu maisha yetu tena”). Alisikika George akisisitiza uwepo wa watu wabaya eneo hilo, aliongea kwa kutetemeka kabla ya kukurupuka na kumrukia Winnie akimkumbatia, Ghafla zilisika sauti za risasi mara mbili ambazo zilishuhudiwa kuwa zilikuwa zimempata George mgongoni sawasawa. George alianguka akiwa amemkumbatia Winnie, wakati waongozaji wa watalii wakishangaa pamoja na askari wa hifadhi hiyo. Walilishuhudia gari moja lililokuwa na rangi ya bluu likitoka kwa kasi eneo hilo huku mtu mmoja waliyembaini alikuwa mwafrika alionekana akizamisha kichwa chake katika gari hilo akiwa na bunduku mkononi. Askari hao waliwasha magari yao na kuyaondoa kwa kasi wakilifuatilia gari hilo, baada ya kulikimbiza kwa umbali wa kilometa mbili walilishuhudia gari hilo aina ya Suzuki likiwa limegongana uso kwa uso na loli la mizigo. Walisogelea zaidi katika eneo hilo la tukio ambalo wao walikuwa watu wa kwanza kufika na kuwasaidia watu waliokuwa wamejeruhiwa vibaya. Hawakumwona mwafrika waliyemshuhudia akiwa na bunduki katika gari dogo aina ya Suzuki, baada ya kuzunguka kwa muda mfupi katika eneo hilo walimshuhudia kijana huyo wa kiafrika akihangaika. Alikuwa umbali wa mita kadhaa kutoka eneo la ajali akiwa ameumia vibaya sana, kichwa chake kilikuwa kimepasuka hata sura yake haikutambulika vizuri na baada ya dakika kadhaa yalitimia, kijana huyo alifariki.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    George alikuwa amepata majeraha makubwa mgongoni mwake jambo lililoanza kuleta hofu juu ya uhai wake, baada ya kupiga kelele kwa muda mfupi tayari alikuwa amepoteza fahamu. Winnie alikuwa akilia kwa sauti kama mtoto mdogo akiwa haamini kama mchumba wake alikuwa katika hatari ya kufariki tena. Viongozi wa hifadhi hiyo ya Steenwijk waliandaa ndege ndogo itumikayo na watalii kuzunguka eneo hilo la hifadhi lengo likiwa kumwahisha George hospitali. Hatimaye alipakizwa katika ndege hiyo ya watu wanne baada ya kupata matibabu ya huduma ya kwanza kutoka kwa madaktari wa hifadhi hiyo. Ndani ya ndege hiyo alikuwapo pia daktari mmoja wa hifadhi hiyo pamoja na Winnie aliyekuwa analia kwa uchungu muda wote. Walikuwa wanaelekea katika jimbo la Rotterdam katika hospitali kuu ya jimbo hilo ili kumwahisha George apate matibabu.

    * * * *

    Mzee Joseph akiwa waziri wa nchi alikuwa amechanganyikiwa juu ya taarifa za kutoroka kwa mwanaye akiwa mafichoni nchini Madagascar. Hakumweleza mtu juu ya taarifa hiyo lakini aliwatumia watu wake kufanya uwezekano wa kumpata mwanaye. Wiki moja ilipita pasipo taarifa yeyote lakini siku moja alipokea simu na kuelezwa mwanaye alikuwa amefariki kwa ajali ya gari baada ya kujaribu kufanya tukio la mauaji. Alielezwa tukio zima hilo lilitokea nchini Uholanzi wakati mwanaye akijaribu kumuua George Innocent. Taarifa hiyo ilikuwa mbaya kwa mzee Joseph aliye changanyikiwa ghafla huku akiwa na hasira. “lazima nilipe kisasi, huyu ni mzee Innocent amemuua mwanangu haiwezekani na mimi lazima niue…” Alisikika mzee Joseph kabla ya kuingia chumbani kwake na kutoka na bastola akiwa tayari kwa kuua. Alitoka nje akiwa ameihifadhi silaha hiyo katika koti lake la suti mwishoe alilitoa gari lake kwa kasi eneo la nyumbani yake akiwa na mpango wa kuelekea Bunju nyumbani kwa mzee Innocent.

    Baada ya dakika kadhaa alikuwa maeneo ya Mwenge akiendesha gari lake kwa kasi ya ajabu jambo lililokuwa limemkaa kichwani lilikuwa ni kuua tu. Aliwaza kuua kila mtu ambaye angemwona nyumbani kwa mzee Innocent. Alikuwa akitokwa jasho kupindukia, hatimaye alifika katika eneo la barabara ya Mwenge liongozwalo na taa. Wakati huo taa hizo hazikuhurusu upande wake kupita, zilikuwa zimehurusu gari zilizotokea upande wa Ubungo. Mzee Joseph hakusimamisha gari lake na alikuwa akimuwaza mzee Innocent tu kichwani mwake ‘lazima na mimi niue lazima…”alikuwa akiirudia sentesi hiyo wakati akiendesha gari lake. Ghafla gari lake liligongana na gari jingine dogo lililokuwa likitokea maeneo ya Ubungo. Mheshimiwa huyo aligundulika amefariki na watu waliosogea kushuhudia ajali hiyo baada ya kuhangaika kwa muda mfupi akiwa amepasuka fuvu la kichwa chake. Siku iliyofuta ilitawaliwa na vilio juu ya kiongozi huyo lakini zaidi tukio la kuchanganya juu ya kifo cha Frank Joseph akiwa nchini Uholanzi. Mwili wa kijana huyo ulirudishwa nchini na alizikwa na baba yake katika kijiji cha Luponde kilichopo wilaya ya Njombe mkoa wa Iringa, mkoa ambao waziri huyo wa nchi alizaliwa. Hakuna mtu aliyebahatika kuuona mwili wa Frank Joseph zaidi ya picha yake iliyowekwa juu ya jeneza wakati wote. Madaktari wa Uholanzi walishauri mwili huo usibughudhiwe kwa vile ulikuwa umehalibika vibaya sana, ikawa hivyo.

    Kama ilivyo kawaida ya ulimwengu huu, mtu yeyote akifariki hufariki na umaarufu wake ndivyo hivyo ilivyokuwa kwa waziri na mwanaye waliokuwapo vinywani mwa watu muda wote. Baada ya wiki tatu tayari wananchi walishaanza kusahau juu ya watu hao ingawaje kuliibuka mambo mengi yaliyowahusu. Kubwa likiwa ni tukio la Frank Joseph kujaribu kumuua George nchini Uholanzi.

    George alikuwa ameumia kwa kiasi kikubwa ingawaje madaktari waliwahakikishia wazazi wake kuwa angerudi katika hali yake ya awali. Jambo hilo mbali ya kuwa faraja kwa mzee Gregory na Innocent wakiwa na wake zao lilikuwa faraja zaidi kwa Winnie ambaye muda wote alikuwa pembeni ya kitanda cha kijana huyo aliyeamini alikuwa pekee wa ndoto zake. Baada ya miezi mitatu George alirudi katika hali yake ya awali na kurejea Tanzania akiwa na familia yake. Walipokelewa na marafiki zao wengi ambao waliufahamu mkasa wake na Winnie tokea mwanzo kwa wakati huo. Wengi walionekana walifurahishwa juu na kurudiana kwake na Winnie. Hatimaye harusi yao iliandaliwa na baada ya miezi mitatu ilifanyika harusi kubwa iliyotikisa jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla, lakini zaidi vyombo vya habari vilivyofuatilia maisha ya wanandoa hao kwa muda mrefu.

    George na Winnie walianza kuishi maisha ya furaha na amani, baada ya mwaka mmoja walibahatika kumpata mtoto mmoja wa kiume waliyempa jina la Henry. Walimpa jina hilo ili kumkumbuka babu wa mtoto huyo aliyeuawa na Frank Joseph miaka ya nyuma. George alikuwa akishirikiana na baba yake katika shughuli za kibiashara wakati huo makampuni ya familia yao yalipata mafanikio kwa kiasi kikubwa na kuifanya familia hiyo kuzidi kuwa tajiri. Baada ya miaka mitano wazazi wake George hawakuweza tena kujishughulisha na maswala ya kibiashara kutokana na umri wao kuwa umesogea kwa kiasi kikubwa. Walikuwa washauri wa biashara kwa kijana wao George ambaye alikuwa kama mrithi tayari wa mali za wazazi wake.

    Siku moja wakati George akiwa katika ofisi yake simu yake ya mkononi iliita na baada ya kuitazama aligundua ilikuwa imepigwa na Winnie bila kupoteza muda aliipokea “baba Henry nakuomba urudi nyumbani ni mhuhimu sana” “sawa…. nakuja” alijibu George ambaye siku zote alimheshimu mkewe na hakupenda tabia ya kuwa mbishi hata kidogo. Aliondoka eneo la ofisini hapo akiwa na dereva wake aliyemweleza ampeleke nyumbani kwake. Mara baada ya kufika nyumbani kwake alishtushwa na mwonekano uliokuwapo eneo la sebuleni. Kulikuwa na maua mengi yaliyoashiria upendo yaliyokuwapo kila eneo la sebule hiyo. Zaidi kulikuwa na taa tofauti zilizowaka zikipendezesha eneo hilo, akiwa anashangaa huku akiwa hajaongea jambo lolote alishtushwa na mkono wa mtu aliyemshika begani baada ya kugeuka aligundua alikuwa ni Winnie. “George unaikumbuka vipi tarehe ya leo?” alisikika Winnie aliyevaa mavazi ya rangi nyekundu, George alitikisa kichwa akiwa hana jibu. “leo tarehe kumi na tano mwezi Desemba ni tarehe ambayo tulipeana `AHADI YA MA…`” Kabla hajaendelea kuongea walishtushwa na sauti ya mlango wa nyumba yao uliofunguliwa kwa nguvu, Tabangu kijana mwenye kifua kipana ambaye alikuwa miongoni mwa walinzi wakuu wa George ndiye aliingia sebuleni hapo. Alikuwa akitokwa jasho kupindukia huku akipumua kwa taabu, kuna jambo lilionekana haliko sawa. Winnie na George walionekana wakimwangalia wakati akiwa ameinama ameshika magoti yake akiendelea kuhema, wanaonekana wakiwa wameshtuka.

    “Tabangu vipi mkubwa wangu kuna nini?” Alisikika George aliyemheshimu sana mlinzi wake huyo. “George, wameuawa, wameuawa wote George wameuawa” Alijibu kwa taabu huku akiendelea kupumua kwa shida, alionekana kama alikuwa amekimbika kwa muda mrefu. “Nani wameuawa Tabangu aah!” aliongea George huku akimsogelea Tabangu taratibu, alionekena kujali huku pembeni yake akiwa amesimama Winnie aliyeonesha dalili za kuchanganyikiwa. “Wazazi wako wameuawa George, wameuawa mchana huu”Alisikika tena Tabangu ambaye alimfanya George aishiwe nguvu na aliishia kukaa chini akiwa ameshika kichwa chake, Winnie aliyeshindwa kujizuia alianza kulia kwa sauti naye aliishia kukaa pembeni ya mume wake ndani ya nyumba yao ya kifahari iliyokuwapo maeneo ya Masaki. Jambo jipya kabisa, nani kawaua wazazi wake? Kwa nini?

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    ITAENDELEA  

0 comments:

Post a Comment

Blog