Search This Blog

Friday, October 28, 2022

BARUA KUTOKA KWA MAREHEMU - 3

 







    Simulizi :Barua Kutoka Kwa Marehemu

    Sehemu Ya Tatu (3)







    Usiku ulikuwa mzito sana kwa Davina, alitumia muda mwingi sana kufikiria uamuzi wake wa kuwa na Gerald, aliona kama anamsaliti Jeff wake waziwazi. Lakini pia, barua ya Jeff ikimwambia kwamba yupo mtu wake wa karibu ambaye alimuua ili aweze kuwa naye, ikarudi akilini mwake upya kabisa.

    “Au yawezekana Gerald ndiyo alimuua nini?” likaja wazo hilo na kuondoka haraka sana.

    Pamoja na hayo, wazo la kuolewa na Gerald lilikuwa linakataa kabisa kukubali kutulia akilini mwake. Baadaye akakata shauri...hakuwa tayari kuolewa na Gerald. Akachukua simu yake na kuandika ujumbe mfupi haraka, kisha akautuma kwenda kwa Gerald.

    Ulikuwa ujumbe mbaya sana. Ulisomeka hivi: “Nimefikiria kwa makini sana juu ya uamuzi wangu, lakini nimegundua nitakuwa nakosea sana. Samahani kwa hili Gerald, lakini ukweli ni kwamba, siwezi kuolewa na wewe tena.”

    Dakika moja haikupita, tayari simu yake ilikuwa imeshaingiza ujumbe mfupi. Alipofungua, akagundua kuwa, ulitoka kwa Gerald. Huku akitetemeka, akaanza kuusoma....

    “Pengine hujui thamani ya mapenzi, hujui jinsi ninavyoumia kwa ajili yako, hufahamu ninavyotesekea penzi lako. Nashukuru kwa uamuzi wako wa kuniua, endelea kuishi kwa amani, kesho ufurahie kifo changu.

    “Ninajiua, lakini kabla sijafanya hivyo, nitaacha ujumbe utakaoeleza sababu za mimi kujiua. Nashukuru sana Davina, NAKUFA NIKIWA NA MZIGO WA MAPENZI YAKO MOYONI MWANGU, nitakupenda milele. Buriani.”

    Davina alirudia kusoma ule ujumbe kwa zaidi ya mara tatu, lakini maneno yalikuwa yale yale!

    Alihisi kuchanganyikiwa!

    Alihisi macho yake yalikuwa hayaoni vizuri, lakini hata alipoyapekecha, bado meseji ile ilibaki kuwa na maneno yale yale. Davina alihisi tatizo, tena tatizo kubwa sana na papo hapo, mapigo ya moyo wake yakabadilisha kasi na kwenda mbio sana.

    Akayafumba macho yake kwa muda, akauacha ubongo wake upate nafasi ya kuchambua mambo peke yake, baadaye akagundua jambo jipya akilini mwake; Alianza kuhisi kumpenda Gerald na kwa hakika hakuwa tayari kabisa kumpoteza mwanaume ambaye alionesha wazi kuwa na penzi la dhati kwake.

    “Hata kama alikuwa rafiki wa marehemu Jeff, tayari Jeff mwenyewe ameshakufa, sidhani kama kutakuwa na tatizo na hata huyo Jeff mwenyewe huko alipo atakuwa anafahamu wazi kwamba mimi sijamsaliti kwa makusudi, maana hayupo tena katika ulimwengu unaoonekana!

    “Sina ujanja, inabidi nikubali kuwa na Gerald, inabidi iwe hivyo maana kwakweli mapenzi yamenielemea sana. Sina jinsi...” aliwaza Davina aliyekuwa ameketi kwenye sofa kubwa macho yake yakiwa yametulia juu ya kioo cha simu.

    Wazo lililokuja kwa haraka ilikuwa ni kumpigia simu Gerald na kumwambia kwamba, hana haja ya kufa tena, maana alikuwa tayari kuolewa naye. Lilikuwa zoezi la haraka kuliko kawaida. Akapiga namba za Gerald haraka sana, majibu aliyopewa yalimtibua!

    “...hakikisha namba unayopiga na upige tena...” ndiyo sauti iliyosikika kupitia kwenye spika ya simu yake.

    Haikuwa rahisi kuamini, namba alizopiga zilikuwa ni zile zile, sasa kwa nini apewe jibu lile? Akarudia tena kupiga zile namba. Majibu yakawa tofauti...

    “...namba unayopiga kwa sasa inatumika, jaribu tena baadaye...” hapa kidogo akapata faraja.

    Akasubiri baada ya muda kisha akapiga tena, majibu yalikuwa yale yale. Zikapita dakika kumi nzima akijaribu kupiga na majibu yakabaki kuwa yale yale. Akachanganyikiwa. Baadaye kidogo alipopiga, alijibiwa jibu lililomkosesha amani ya moyo wake kabisa...

    “...namba unayopiga kwa sasa haipatikani, jaribu tena baadaye!”

    Alirudia zaidi ya mara kumi, lakini simu haikupatikana! Akili yake ikafanya kazi kama umeme, ilikuwa lazima afanye jambo fulani ili kuhakikisha Gerald hapatwi na jambo baya.

    Kichwani alikuwa na vitu viwili kwa wakati mmoja; Kwanza alikuwa na mzigo mkubwa sana wa mapenzi kwa Gerald, mapenzi ambayo yalifumuka ghafla sana, lakini pia alikuwa anaogopa sana kesi ya kusababisha kifo, maana tayari Gerald alishamweleza wazi kwamba angeandika barua ya kueleza sababu za kifo chake kabla hajajiua!

    “Lazima niende kwake, lazima...tena haraka sana...” wakati Davina anasema maneno hayo kwa sauti alikuwa anapiga hatua za haraka sana kwenda nje, sehemu alipoegesha gari lake.

    Mara moja akaingia na kulipiga moto. Hakuwa na muda wa kupoteza, akaondoka kwa kasi.

    ***







    ***

    Kutoka Tandika hadi Mbezi Beach, kulikuwa na umbali sana, lakini kwa sababu ilikuwa usiku na hapakuwa na magari mengi barabarani, Davina alipata mwanya wa kuendesha gari atakavyo.

    Baada ya dakika kumi tu, alikuwa ameshafika Mwenge, kwenye makutano ya Barabara ya Sam Nujoma na Bagamoyo, akashika barabara inayoenda Bagamoyo kasi yake ikiwa ile ile! Alikuwa tayari kupata ajali mbaya na kupoteza maisha yake akiwa anamfuatilia Gerald.

    Akili zake zilikuwa kama zimeruka, aliwaza kumpata Gerald tu, hakuwa na kitu kingine chochote tena akilini mwake. Baada ya muda alikuwa anaegesha gari nje ya nyumba ya Gerald na kugonga mlango kwa nguvu. Mara moja mlinzi akatokea. Alipokutanisha macho yake na Davina, akafungua mlango haraka kwa kuwa alikuwa anamfahamu.

    “Shikamoo mzee,” Davina akamsalimia na kumpita.

    “Marhaba binti yangu, vipi mbona kasi hivyo?”

    “Fanya kazi yako...” Davina akamjibu kwa dharau na kuingia ndani.

    Vyumba vyote Gerald hakuwepo na simu yake bado ilikuwa haipatikani. Alipokagua vizuri chumbani kwa Gerald akaona simu yake ikiwa imezimwa pamoja na ujumbe alioandika kwa mkono. Akachukua haraka na kuanza kusoma...

    ‘Natambua kujitoa uhai ni kosa, tena kosa la jinai. Pia najua vyema kuwa kujiua ni dhambi mbele za Mungu, lakini mimi nalazimika kutokana na kupoteza umuhimu wa kuishi duniani.

    Natamani sana kuendelea kuishi, lakini nashindwa kwa sababu yule mwenye amani ya moyo wangu amenikataa. Nataka jamii nzima itambue kwamba, moyo wangu unampenda sana Davina, lakini yeye ameonesha wazi kwamba hanitaki.

    Nimeshafanya mambo mengi sana ili nimpate, lakini wapi? Imeshindikana.

    Sasa naona ni wakati wangu wa kupumzika kuliko kuendelea kunyanyaswa na mtu ambaye nampenda na siwezi kuishi naye.

    Nawaombeni mnisamehe wote. Najua taarifa hizi zitamuumiza sana mama yangu, lakini sina budi kufanya hivi mama, naomba sana msamaha wako mama’ngu!

    KWAKO DAVINA:

    Nilikupenda sana, huu ukawa wimbo wangu siku zote, lakini hukuupenda na wala haukukuvutia, nimeona ni bora nife nikuache ufurahi na roho yako. Ahsante sana Davina. Kwa heri ya kuonana. Acha nimfuate rafiki yangu Jeff.

    Kuhusu mwili wangu msihangaike sana, nendeni kwenye pori la Makongo, mbele kidogo ya Mlimani City, mtauhifadhi.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nisameheni wote niliowakosea na napenda kuwatangazia kwamba, moyo wangu ni mweupe kwa wote mlionikosea. Buriani nyote.

    Gerald.



    Aliikunja ile barua na kuiweka kwenye mfuko wake wa suruali ya jeans kisha akatoka nje haraka sana.

    “Gerald ameondoka muda mrefu sana mzee?”

    “Hata robo saa hajamaliza, nilijua labda amekufuata na nilivyoona umerudi, nikajua alikuwa nyuma yako.”

    “No! Amekuaga?”

    “Hapana.”

    Davina hakuwa na maswali zaidi ya kuondoka kwa kasi ile ile aliyoenda nayo. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, alikuwa akikatisha eneo la Mlimani City, akiifuata barabara ya vumbi inayoelekea Makongo. Alinyoosha moja kwa moja akiendesha kwa kasi kuliko kawaida kwenye barabara ile ya vumbi.

    Alipoyatupa macho yake kwenye saa iliyokuwa mbele ya gari, aligundua kwamba ilishafika saa 7:36 za usiku. Woga ukazidi kumshika, lakini aliendelea kuendesha gari, akitizama kwa makini kando ya barabara.

    Mbele kidogo, akaona gari limeegeshwa pembeni mwa barabara, akapunguza mwendo na kulisogelea. Hapo akagundua lilikuwa gari la Gerald. Akashuka haraka na kuangalia kila upande kwa hadhari. Akaingia kwenye eneo lenye giza mbele yake, kukiwa na mti mingi sana. Woga alioukuwa nao ulikuwa hauelezeki.

    “Gerald...Gerald...” aliita kwa sauti ya chini huku woga ukiongezeka moyoni mwake.

    Hata hivyo hakuna aliyeitikia. Aliendelea kwa muda mrefu mpaka aliposikia kama mti uliokuwa mbele yake ukitingishika, akatulia na kuyatupa macho yake juu ya mti. Akausogelea ule mti aliokuwa na wasiwasi nao, akaona viatu chini. Hakupata shida sana kujua kwamba vile vilikuwa viatu vya Gerald.

    “Gerald please, naomba usijiue, nipo hapa kwa ajili yako, usife tafadhali, bado nakuhitaji sana, shuka chini mpenzi wangu, nipo tayari kuwa na wewe kwa hali yoyote,” Davina aliongea kwa sauti ya kusihi ingawa hakumuona Gerald lakini alijua wazi lazima angekuwa katika ule mti baada ya kuona viatu pale chini.

    Aliamini alikuwa bado hajakamilisha zoezi la kujinyonga maana kama ingekuwa hivyo, angeuona mwili wake ukiwa unaning’inia.

    “Hapana Davina, UMECHELEWA....lazima nife...” baada ya sauti ile, kishindo kikuu kikasikika ikafuatiwa na sauti ya Gerald akilia!

    Davina alihisi kuzimia!

    Woga tele ukamjaa Davina, alijua kwa vyovyote vile kama Gerald angeanguka chini, angekuwa na hali mbaya sana kama siyo kufa kabisa.

    Kupiga kelel kusingesaidia chochote, kwanza alikuwa mwenyewe, pili ilikuwa ni porini, lakini kubwa zaidi, kama ingegundulika Gerald alikuwa anataka kujiua, angekuwa kwenye hatari ya kukabiliana na mkono wa sheria, jambo ambalo Davina hakutaka litokee kabisa.

    Kitu cha ajabu ni kwamba, Gerald hakutua chini, achilia mbali kutua chini, lakini hata sauti yake ya kilio, ilikuwa ni ya mara moja tu!

    Davina akaogopa sana!

    Mara moja, akili yake ikafanya kazi kama umeme. Akatoa simu yake ya tochi akawasha kisha akamwulika juu ya mti. Kwa macho yake mawili akashuhudia Gerald akiwa amening’inia mikono na miguu kwa pamoja.

    Ilionekana kama wakati anajiachia, alitua katikati ya tawi, hivyo tumbo lake kulala katikati na mikono na miguu kukutana katikati! Davina akazidi kutetemeka kwa woga...

    “Kutetemeka kwangu hakusaidia lolote, lazima nitafute kitu cha kufanya...” akawaza Davina.

    “Geraldiiiiiii....” Davina aliita kwa sauti, lakini Gerald hakuitika.

    Akapata wazo la ghafla; “Acha niende Mwenge mara moja nikachukue vijana waje wamshushe...” akajisemea moyoni mwake huku akipiga hatua za haraka kuelekea barabarani alipoegesha gari lake.

    Alipofika akaingia haraka na kuwasha, kabla ya kuingiza gia, akapata wazo lingine jipta kabisa...

    “Naweza kumpoteza Gerald wangu kama sitakuwa makini hapa...kwani kupanda mti nimeshasahau mara hii? Inabidi nirudi nipande mwenyewe na nimshushe. Mwenge ni mbali sana, naweza kukuta ameshakufa.”

    Wazo lake liliungwa mkono na yeye mwenyewe, akazima gari na kurudi porini. Akavua viatu kisha akaanza kupanda juu ya mti taratibu.

    Kupanda mtini halikuwa jambo geni sana kwa Davina, kwani alipokuwa Kijijini kwao Baura, alikuwa mtaalamu sana wa kupanda miti ya matunda. Alipanda kwa shida kidogo, kutokana na kuwa hajapanda miti kwa miaka mingi sana.

    Kwa taabu alifika juu, akaketi kwenye tawi moja jirani na alipokuwa ameangukia Gerald. Alikuwa anahema kwa kasi sana. Kitu cha kwanza alichokichunguza ni kama Gerald alikuwa anapumua.

    Naam...Gerald alikuwa anapumua...

    “Gerald...” Davina akaita.

    “Niache Davina, niache nataka kufa!”

    “Sikia Gerald, najua unataka kufa kwasababu yangu!”

    “Ndiyo hivyo, niache ondoka zako,” Gerald akazungumza kwa taabu sana.

    “Nimeshaamua kuwa na wewe mpenzi wangu, huna sababu ya kufa tena Gerald, naomba uniamini!”

    “Nimesema nataka kufa, mbona hunielewi? Acha nimfuate rafiki yangu Jeff!”

    “Hapana baby, nipo kwa ajili yako baba. Unadhani kama ningekuwa sikupendi ningekufuata mpaka huku?”

    “Hata kama, wewe ni mwongo, naomba ondoka uniache nife peke yangu.”

    “Huwezi kufa nikiona, huwezi Gerald.”

    “Ondoka tafadhali.”

    “Nakupenda Gerald, naomba uniamini mpenzi wangu, nipe nafasi...sasa nimekuja mzima-mzima, nipe nafasi mpenzi wangu.”

    “Hapana nataka kufa!”

    “Naona kama hatuelewani Gerald, umesema unataka kufa?”

    “Ndiyo!”

    “Sababu ni mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Ok! Sasa acha kwanza nikutoe hapo, tuzungumze halafu utaamua kama bado utataka kufa au kuendelea kuishi.”

    Gerald hakujibu.

    Davina hakuwa na haja ya kusubiri kauli yake, akasogea taratibu, kisha akamshika mkono, huku mkono wake mwingine ukiwa umekamata tawi lingine bara-bara. Akamvuta taratibu na Gerald akajitahidi kujisogeza hadi kwenye tawi lingine.

    Akaketi.

    “Pole.”

    “Ahsante.”

    “Usife Gerald, nimeshajua kwamba unanipenda kwa dhati, naahidi nitakuwa na wewe!”

    “Kweli?”

    “Nakuahidi mpenzi wangu!”

    “Haya tushuke tuondoke, hapa si mahali salama kwetu, isitoshe ni usiku mwingi sana saa hizi!”

    “Sawa, lakini unatakiwa kupumzika kwanza, subiri kwanza mpenzi wangu.”

    “Sawa.”

    Baada ya kama robo saa kupita, Davina na Gerald wakaanza kushuka kwa mtindo wa Davina kutangulia chini na Gerald kumfuata nyuma yake. Wakafanikiwa kushuka hadi chini salama.

    Davina akamshika mkono na kumwongoza kwenye gari. Akamfungulia mlango na kuingia.

    “Utaweza kuendesha?”

    “Ndiyo, usijali.”

    “Nikupeleke hospitalini?”

    “Hapana labda tupitie Phamramcy tukuchukue Diclopar kwa ajili ya kupunguza maumivu.”

    “Sawa, twende. Wapi sasa?”

    “Sinza ya Palestina, huwa hawafungi wale.”

    “Ok!”

    Wakaondoka kwa mwendo wa taratibu sana hadi Sinza, wakachukua dawa na kwenda zao Mbezi Beach. Davina hakwenda nyumbani kwake siku hiyo. Alilala kwa Gerald. Kwa mara ya kwanza wakapeana mapenzi motomoto.

    *****

    Taarifa za uhusiano wa Gerald na Davina zilipokelewa kwa furaha sana na wazazi wa pande zote mbili. Hakuna sehemu waliyoweka kipingamizi.

    Kwanza kabisa, Gerald alimpeleka Davina nyumbani kwao Marangu, Kilimanjaro kumtambulisha kabla ya kwenda kijijini kwa akina Davina, Baura, Kondoa mkoani Dodoma.

    Taratibu zote zikafanyika haraka, mahari ikatolewa na hatimaye ndoa ikatangazwa kanisani. Kama kawaida, baada ya kutangazwa mara tatu mfululizo bila kuwepo kwa kipingamizi, wiki iliyofuata ilikuwa ya ndoa.

    Maandalizi yote yakakamilika!

    ****

    Kanisa lilikuwa limejaa watu wengi sana, ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wa pande zote mbili walikuwa wamefurika kanisani. Nyuso zilizojaa tabasamu ndizo zilizoonekana kila upande wa kanisa hilo.

    Mbele ya madhabahu, walikuwa wamesimama Davina akiwa amevalia shela, Gerald ambaye alikuwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na wapambe wao.

    Tayari Mchungaji alikuwa ameshawauliza Davina na Gerald kama wapo tayari kufunga ndoa. Wote walikubali. Kabla ya tendo muhimu la kuunganishwa katika ndoa takatifu, Mchungaji aliwageukia waumini na kuwauliza kama kuna yeyote mwenye pingamizi.

    “Kabla ya kuwaunganishwa wapendwa hawa, ambao kwa hiyari yao wamekubali kuwa mwili mmoja katika ndoa takatifu. Je, kuna yeyote mwenye pingamizi?” Mchungaji aliuliza.

    Hakuna aliyejitokeza.

    Alirudia kuuliza swali hilo kwa mara ua pili mfululizo, kabla ya kuuliza kwa mara ya tatu na mwisho...

    “Noooo....nooo Pastor...nina pingamizi...” ilikuwa sauti ya kijana kutoka lango kuu akiingia kanisani pale akikimbia.

    Waumini wote wakageuka na kumwangalia. Davina na Gerald wakashtuka sana.

    Alikuwa ni Jeff aliyevalia suti nyeupe na viatu vyeupe!

    Marehemu Jeff!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    KANISA zima lilipigwa na butwaa, wote wakageuka kumuangalia kijana huyo mtanashati wa kuvutia, akiingia kanisani akitembea kwa mwendo wa haraka. Mchungaji hakuamini macho yake.

    Akavua miwani ili aweze kuona kama alichokuwa anakiona na kusikia kilikuwa sahihi. Gerald aliishiwa nguvu, lakini alijipa faraja kwamba inawezekana kabisa ulikuwa mzimu wa Jeff na si Jeff mwenyewe.

    Jeff alipokaribia madhabahuni kabisa, kabla hajapanda akazuiwa na Wazee wa Kanisa.

    “Tulia kwanza kijana, tulia,” Mzee mmoja akamwambia.

    “Acheni nikazungumze na Mchungaji.”

    “Hujazuiwa, lakini zipo taratibu za kufuata.”

    “Mwache aje,” Mchungaji akadakia haraka.

    Akaongeza: “Njoo kijana.”

    Jeff akapanda madhabahuni.

    “Unaitwa nani?”

    “Jeff!”

    “Nani?”

    “Sebastian.”

    Hapo si Davina wala Gerald, walihisi kuchanganyikiwa, maana sauti ilikuwa ya Jeff kabisa na hata umbo lake lilikuwa ni Jeff mwenyewe, lakini hofu tele iliyokuwa mioyoni mwao ni kwamba; Jeff ametokea wapi wakati alikufa?

    Alizikwa?

    “Kwanini unaweka pingamizi?”

    “Davina ni mchumba wangu na tulikuwa katika hatua za mwisho kabisa kabla ya kuoana, lakini yakatokea matatizo.”

    “Matatizo gani?”

    “Ni habari ndefu Mchungaji, lakini nitaisimulia baadaye kidogo, watu wote wasikie.”

    Mchungaji alipigwa na butwaa, tangu ameanza kazi ya utumishi, hakuwahi kukutana na tukio kama hilo, siku zote alikuwa akisikia mambo hayo kwa Wachungaji wenzake, lakini siku hiyo ilitokea kwake mwenyewe.

    Akaduwaa.

    Akamwangalia Gerald na kumwuliza: “Unamfahamu huyu kijana?”

    “Huyo?” Gerald akauliza akitetemeka kwa hofu.

    “Ndiyo.”

    “Anafanana na marehemu Jeff.”

    “Sikiliza Gerald, mimi si marehemu na sijawahi kuwa marehemu hata siku moja. Siku yangu ya kufa ikifika nitakufa...kifo ni ahadi Gerald, ahadi ambayo kwangu bado. Sema ukweli unanifahamu au hunifahamu?” Jeff alizungumza kwa ukali sana, hali ambayo iliwashangaza waumini waliokuwa pale kanisani.

    Gerald akaogopa sana, ni Jeff huyu huyu ambaye siku zote amekuwa mkarimu kwa mambo mema, lakini hakusita kuwa mkali kwenye mambo ya kipuuzi. Kwa sauti ile, alijirudhisha kabisa kwamba aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Jeff mwenyewe.

    Hilo alikubaliana nalo kwa asilimia mia moja.

    “Unamfahamu au humfahamu?” Mchungaji akarudia swali lile.

    “Alikufa!”

    “Lakini unamjua?”

    “Ndiyo!”

    “Anaitwa nani na una uhusiano gani naye?”

    “Ni Jeff kama alivyosema, kabla ya kifo chake alikuwa rafiki yangu,” Gerald akasema akitetemeka kwa hofu.





    Ombi lake kubwa lilikuwa ni ule uwe mzimu wa Jeff na si Jeff mwenyewe, maana kama atakuwa ni Jeff basi kitanzi kilikuwa kinamsubiri.

    “Davina, unamfahamu huyu kijana?”

    “Ndiyo Mchungaji.”

    “Ni nani?”

    “Anaitwa Jeff, alikuwa mchumba wangu!” Kanisa zima likashtuka.

    “Sasa?”

    “Alikufa!”

    Watu wakazidi kuchanganyikiwa. Inawezekana vipi mtu aliyekufa, aonekane tena mara ya pili? Lilikuwa jambo la kushangaza sana ambalo liliwaacha watu wote hoi. Haikuwa rahisi kuamini kuwa aliyekuwa mbele yao alikuwa ni marehemu Jeff.

    Mchungaji akamgeukia tena Jeff: “Enheee...hebu tupe habari kijana. Kwanini hutaki hawa wafunge ndoa?”

    “Hawawezi kufunga ndoa, Gerald ni muuaji mkubwa, yeye ndiye alipanga kifo changu ili amuoe mpenzi wangu, lakini hilo halitawezekana, nilishamuahidi mara nyingi katika barua ninazomuandikia yeye na Davina,” Jeff akasema akilengwalengwa na machozi machoni.

    “Kwahiyo ukweli ni upi, uliwahi kufa?”

    “Hapana, sijawahi kufa Mchungaji.”

    “Mwongo huyu naona anafanana tu na Jeff, anataka kutuharibia ndoa yetu...Jeff alikufa, sijui huyu ametokea wapi? Lakini nahisi anaweza kuwa pepo, kwanini asiombewe kwanza baba Mchungaji?”

    “Tulia kijana, penye ukweli uongo hujitenga. Kumbuka hii ni nyumba ya Bwana, mahala Patakatifu, hakuna lolote baya litakalofanyika chini ya dari la Bwana. Kuwa na amani...yaache haya mambo yaende taratibu, bila shaka yataisha kwa utaratibu pia.”

    Mchungaji alipomaliza kusema maneno hayo, akamgeukia tena Jeff na kumwambia: “Ulikuwa wapi muda wote?”

    “Ni habari ndefu Mchungaji, lakini nataka kukuambia kwamba dunia yote inafahamu mimi nimekufa, hata ndugu na wazazi wangu wote wanafahamu hivyo. Hawana habari kama nipo hapa leo muda huu.

    “Jeff aliyezikwa miaka miwili iliyopita hakuwa mimi. Siku zote hizo nilikuwa naishi Mwanza. Nikifanya mambo yangu kimya kimya na hakuna aliyekuwa anajua, lakini nilipanga kumfundisha adabu Gerald.

    “Huyu ni binadamu hatari sana, hafai kabisa katika hii jamii, ni yeye ndiye aliyepanga kifo changu, nikagundua na kukwepa, nataka kuanika ukweli huu leo.”

    “Enheee....”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yaani inaniuma sana, tulikuwa marafiki wakubwa, lakini kumbe mwenzangu alikuwa anamtamani mchumba wangu, ndiyo chanzo cha kuamua kupanga njama za kuniua...

    “Kabla sijaanza kusimulia, nainua mikono yangu juu, nikimuomba Mungu wangu anisaidie kumaliza salama habari hii ya kusikitisha. Lakini naapa mbele ya Mungu wangu na Kanisa, kwamba haya nitakayoyaongea ni ya kweli na hakuna lolote ambalo nitaongea la uongo. Eee Mungu wangu naomba unisaidie...” Jeff alivyomaliza kusema maneno hayo, akaanza kusimulia huku akizidi kulia...

    “Gerald ana tamaa sana, hakuona thamani yangu...thamani ya damu yangu ya uhai ambao nimepewa na Mungu bure, yeye akaona aimwage tena bila hatia yoyote.....” Ndivyo Jeff alivyoanza kusimulia.

    Watu wote walikuwa makini kumsikiliza.



    KUKUTANA KWA GERALD NA DAVINA

    “Lakini kwanini umekataa kunishusha nyumbani kwangu Jeff?”

    “Kwani nimukuteka? Tulia kijana, mbona una kitete?”

    “Ok! Ngoja tuone.”

    “Na utaona kweli.”

    “Na kwanini leo unaning’ang’aniza niende kwako?”

    “Utajua ukifika, lakini nimeshakuambia rafiki yangu Gerald, kuna kitu special, si usubiri uone?”

    “Special?”

    “Ndiyo!”

    “Haya tutaona.”

    Hawa ni marafiki wawili wakubwa, Gerald na Jeff, wapo kwenye gari wakitokea kazini. Jeff hamwambii Gerald ni kwanini anampeleka nyumbani kwake. Tena imekuwa bahati siku hiyo gari la Gerald lilikuwa bovu, safari yao ikaenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Jeff.

    “Surprise...surprise...” Jeff akasema kwa sauti kubwa wakati wakiingia sebuleni.

    “Kuna nini?”

    “Ingia ndani bwana.”

    Gerald akaingia na kwenda kuketi kwenye sofa kubwa. Jeff akaingia chumbani kwake, akimwacha rafiki yake sebuleni. Ghafla akarudi tena.

    “Leo huna ruhusa ya kufungua friji, subiri kwanza, kama ni kiu isubirishe kidogo!” Jeff akasema.

    Gerald akatabasamu!

    Dakika tano baadaye, Jeff akarudi sebuleni akiwa ameongozana na mwanamke mrembo sana. Mzuri. Mwenye kila aina ya sifa anazotakiwa kuwa nazo mwanamke!

    Gerald akatabasamu!

    Akatetemeka kwa kiwewe!

    “Sijawahi kukutana na mwanamke mrembo kama huyu. Sijawahi. Jeff ni rafiki yangu kipenzi, lakini kwa mwanamke huyu, urafiki na uishe tu. Nitafanya kila ninachoweza huyu mwanamke awe wangu...kila ninachoweza...” Gerald akawaza huku akimtiza mwanamke huyo kwa jicho la mahaba.

    Alionekana kukolea kwelikweli.

    Mwanamke huyo hakuwa mwingine, ni mtoto mrembo wa Kirangi. Mtoto kutoka Baura, Kondoa. DAVINA!!!



    Kwa dakika tatu nzima Gerald alishindwa kuzungumza kitu chochote, uzuri wa Davina ukamchanganya sana, alitumia muda huo kumwangalia Davina kuanzia chini hadi juu na kwa hakika alihisi mapigo yake ya moyo kubadilika.

    “Kaka, upo hapa kweli?” Jeff akamwuliza Gerald.

    “Yeah, I’m here brother!”

    “Kimwili tu, lakini kimawazo, hata kidogo haupo hapa.”

    “Unakaribia kupata tuzo ya utabiri sasa Jeff...ni kweli nilikuwa nawaza kuhusu wale jamaa wa Canada walionipigia mchana!” Gerald akasema akicheka.

    Uongo mtupu!!!

    “Ah! Achana nao, lazima watakubali tu kaka, halafu kumbuka wameshasoma kila kitu kwenye mtandao; sehemu ambayo huwa hatufanyi makosa...tunayo lugha ya ushawishi kaka.”

    “Ni kweli kabisa.”

    “Sasa Gerald, kutana na Davina....my wife to be, my angel, my love, lahazizi na kila jina zuri unalolifahamu. Huyu mwanamke nampenda sana, yeye ndiye ameushikilia moyo wangu!” Jeff akasema akitabasamu.

    “Nakubali kaka...nashukuru sana,” Gerald akasema, mate ya tamaa ya mahaba yakimjaa.

    “Davina, huyu ni Gerald, rafiki yangu kipenzi, lakini kama nilivyokuambia, ni bosi wangu pia.”

    “Nimefurahi kukufahamu Gerald. Karibu sana.”

    “Ahsante shem wangu, ahsante sana.”

    Stori mbili tatu zikaendelea, lakini kichwani mwa Gerald alijihisi amebeba mzigo mzito sana, mzigo wa mapenzi. Mapenzi ya usaliti.

    “Sijui lakini...ninachoweza kusema, nitatumia kila aina ya njia, hata kama ni pesa, lakini huyu mwanamke atakuwa wangu. Potelea mbali kama nitagombana na Jeff, lakini huyu mwanamke nimpate,” Gerald akawaza akiendelea kupata kinywaji.

    Usiku Jeff akampeleka Gerald nyumbani kwake Mbezi Beach.

    “Kaka kile kifaa ni noma, umebahatika kupata mwanamke mzuri sana,” Gerald akasifia.

    “Hakuna kaka, wa kawaida tu yule, najua unababaika na umbo lake. Nakujua vizuri sana wewe ni mtoto wa mawowowo!”

    Wote wakacheka.

    Jeff akageuza gari na kurudi Sinza.

    ******

    Pamoja na umrimdogo wa miaka 29 aliokuwa nao Gerald, alikuwa na mafanikio makubwa sana; alikuwa na pesa, cheo kikubwa na vitu vingi vya thamani. Gerald ndiye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KSQ ambayo Jeff alikuwa akifanya kazi.

    Jeff na Gerald walitokea kuwa marafiki wakubwa kutokana na umri wao kuwa sawa, kupenda mambo ya aina moja wote, lakini kubwa zaidi utendaji kazi wao ulikuwa mzuri na wa kushirikiana.

    Kabla ya kifo cha baba yake Gerald, yeye alikuwa ndiye Afisa Uhusiano wa Kampuni, wakati Jeff akiwa Afisa Masoko. Baada ya kifo cha baba yake, kwakuwa alikuwa ndiye mtoto wa kwanza wa kiume, alirithishwa kampuni hiyo na kuanzia hapo akawa ndiye Mkiurugenzi.

    Alipohamia katika cheo hicho kipya, akamteua swahiba wake Jeff kuwa Afisa Uhusiano, nafasi ambayo alikuwa nayo awali. Uhamishwaji huo wa nafasi, ulikwenda sambambamba na uboreshwaji wa masilahi yake!

    Urafiki wao ukaongezeka maradufu!

    *****

    “Huyu ndiye Mkurugenzi wenu?” Lilikuwa swali la kwanza Davina kumuuliza Jeff aliporudi Mbezi Beach.

    “Ndiyo...”

    “Samahani kwa hili mpenzi wangu, lakini naona ni bora nikueleze mapema.”

    “Nini?”

    “Kwa muda mfupi niliomuona rafiki yako, anaonekana hajatulia!”

    “Kwanini?”

    “Angalia yake ilikuwa inanipa mashaka sana, kwanza alikuwa akiniangalia kwa kuibia, lakini pia kwa macho fulani hivi ya kimapenzi!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hawezi kufanya hivyo bwana, yule ni rafiki yangu wa damu...labda umemuhisi vibaya, ile ndiyo angalia yake.”

    “Nimekuambia kama tahadhari, sasa kama unataka kufuga matatizo, endelea lakini kuwa naye makini.”

    Davina hakuongea kitu kingine chochote tena baada ya pale. Kwa mbali maneno ya Davina yalianza kumingia Jeff, lakini hakutaka kufanya haraka, aliamua kujipa muda zaidi wa kufanya uchunguzi wa madai ya mpenzi wake. Hakuwa hayawahi wa kukurupuka hovyo...ilikuwa lazima atafute ukweli kwanza!

    “Nimekuelewa mpenzi wangu, twende chumbani tukalale.”

    “Sawa mpenzi wangu.”

    “Enhee, utakaa hadi lini?”

    “Wewe unataka hadi lini?”

    “Miezi sita.”

    Davina akacheka sana.

    “Ndiyo unioe sasa ukae na mimi moja kwa moja, nikupikie na kukupakulia hadi uchoke mwenyewe!” Davina akazungumza kwa sauti laini sana.

    “Hayo tutapanga mpenzi wangu, usiwe na wasiwasi. Kuna mambo fulani nayahangaikia, yakikaa sawa tu, tunamaliza.”

    “Haya baba miahadi, tukalale bwana, nimechoka.”

    Wakaingia chumbani kulala.

    ******

    Usiku ulikuwa mrefu sana kwa Gerald, alihangaika akiwaza njia za kumnasa Davina. Hakupata. Lakini baada ya kutulia kwa muda mrefu, akaona njia pekee ni kukutana na Kundi la Kimafia la Nyamangumu Camp, kwa ajili ya kupanga mipango ya kuwaachanisha Jeff na Davina.

    Hapo angemchukua kiulaaniiii!

    “Umepanga kutumia njia gani?” Gerald akamwuliza Master Fikiri ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Kundi lile.

    “Tukutane kwanza.”

    “Sawa.”

    Siku iliyofuata, saa mbili kamili za usiku walikutana katika kikao cha dharula, katika Hoteli moja katikati ya jiji. Kilikuwa kikao cha watu wawili tu; cha kupanga mikakati ya kuwaachanisha Jeff na Davina.

    “Anatakiwa apatikane mtu wa kumlaghai Davina, kisha wapange kukutana hotelini ambapo kamera zitakuwa zimetegeshwa, baada ya hapo Jeff anapelekewa video na picha, hawezi kuvumilia, ataachana naye.

    “Baada ya hapo namuandalia zengwe kisha namfukuza kazi, kila kitu kitakuwa kimeishia hapo...kumbuka kwanza atakuwa na stress za kusalitiwa na mpenzi wake, halafu namwekea mitego, anaharibu kazi na kumtimua...halafu namchukua Davina bila matatizo yoyote. Unaonaje hapo?” Gerald akamwambia Master aliyekuwa kimya muda wote.

    “Umejaribu kuwaza, lakini fikra zako ni za kizamani sana, rahisi kugundulika.”

    “Sasa tufanyeje?”

    “Kipo kitu, lakini nina maswali machache kwanza.”

    “Uliza.”

    “Unampenda Davina?”

    “Ndiyo!”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Kitu kimoja tu, kinatakiwa kufanyika; JEFF ANATAKIWA KUFA!”

    “ Haitajulikana?”

    “Mimi ndiye Master...kama upo tayari sema nikupe maelekezo...” Master Fikiri akasema akichukua sigara moja na kuitupia kinywani, kisha akawasha na kuanza kuvuta kwa mbwembwe!

    “Nipo tayari.”

    “Good. Haya ndiyo maamuzi ya kiume. Kitu cha kwanza, utatakiwa kumuajiri mtu wetu mmoja kwenye kampuni yako, halafu huyo mtu atamaliza kitu mwenyewe. Kifupi utapanga safari ya kikazi na huyo mtu ambaye ataongozana naye mkoani, njiani kutakuwa na vijana wangu wa kazi, watawateka na kumuua Jeff, stori inabaki walitekwa na huyo kijana wangu atajulikana kwamba alinusurika. We unaonaje?”

    “Wazo zuri, lakini kwanini tusipange ajali?”

    “Vyovyote iwavyo, lakini kikubwa kinachohitajika hapa ni Jeff afe, wewe ubaki na Davina.”

    Gerald akatabasamu, wakasimama na kukumbatiana, kisha wakaketi.

    “Mwagize huyo mtu kesho ofisini kwangu, vipi kuhusu bei?”

    “Wewe ni ndugu yangu, utanipa milioni hamsini tu kwa kazi nzima!”

    "Fanya thelathini kaka!”

    “Tufupishe maneno, utanipa arobaini!”

    “Poa.”

    *****



    *****

    Jeff alivyofika tu ofisini asubuhi hiyo, alikuta ujumbe kwa Katibu Muhtasi ukimwambia kuwa anahitajika ofisini kwa bosi mara tu baada ya kufika kazini. Akatii.

    Alimkuta Gerald akiwa ameketi kwenye kiti chake kikubwa, mbele yake kukiwa na kijana mmoja mtanashati ambaye alionekana mgeni. Jeff alisimama kwa muda, akimwangalia yule mtu kisha akamwangalia na Gerald, ambaye alimwonesha ishara ya kumtaka akae.

    “Morning!” Jeff akasalimia.

    “Morning to you Jeff...nimekuita hapa kwa kitu kimoja, kutana na Roy Maketo, huyu ni staff wetu mpya, ambaye atashikilia nafasi ya Afisa Masoko uliyokuwa nayo awali, Lugendo nimemsimamsha kazi leo kutokana na utendaji wake usio na tija.

    “Huyu atakuwa chini yako, tafadhali mpe kila aina ya ushirikiano na umwoneshe jinsi anavyotakiwa kufanya kazi yake vizuri. Kwa kifupi msimamie,“ Gerald alisema bila kupepesa macho.

    Akatulia kidogo kama anafikiria kitu, kisha akamgeukia Roy na kumwambia: “Roy, huyu ndiye Jeff Sebastian, ndiye mkuu wako wa kazi, utakuwa chini yake. Nawatakieni kazi njema,” Gerald akasema kisha akageukia kompyuta yake, akaendelea na kazi.

    Wote wakatawanyika!

    “Kwisha habari yake...” Gerald akasema kwa sauti kubwa, muda mfupi baada ya Roy na Jeff kuondoka.



    *****



    Gerald akazidi kufurahi, aliona kabisa jinsi kazi iliyobaki itakavyokuwa ndogo. Mara moja akayanya simu yake na kumpigia Master.

    “Vipi kuna tatizo?” Master akauliza mara baada ya kupokea simu.

    “Tatizo? Tatizo la nini? Hapa shwari tu na hakushtukia mchezo!”

    “Najua hawezi kushtuka.”

    “Halafu nikaamua kumuweka chini yake kabisa, hapo hawezi kujua hata kama atatumia mizimu ya kwao!”

    Wote wakacheka.

    “Tukutane jioni kwa ajili ya mipango zaidi,” Master akasema.

    “Sawa, saa ngapi?”

    “Saa mbili ndiyo muda mzuri zaidi, kitakuwa kikao cha watu watatu tu; mimi, wewe na Roy!”

    “Sawa kaka.”

    ******

    Kikao kilikuwa tulivu sana, wote walikuwa kimya. Kilikuwa kikao cha watu watatu tu, ambao walikuwa wameizunguka meza ya duara iliyotengenezwa kwa vioo tupu.

    Gerald akawatizama kwa zamu, alianzia kwa Roy kisha akamalizia kumwangalia Fikiri-Master. Midomo yake ikatingishika, akionekana kuwa na jambo la kutaka kuzungumza...

    “Ndiyo kaka, naamini huu ni mwanzo mzuri, sasa sijui kazi itafanyika vipi?” Gerald akaanza kumwambia Master.

    “Mipango yote ipo tayari, hata Roy mwenyewe anajua cha kufanya, ni wewe na muda wako. Sijui unataka hii kazi ikamilike lini?”

    “Nataka ikamilike haraka sana.”

    “Muda gani?”

    “Ndani ya wiki mbili tu, nataka Jeff awe kashahama katika ulimwengu huu.”

    “Niachie hiyo kazi, lakini wewe cha kufanya, simamia ukaribu wao hawa vijana, halafu utawapangia safari siku nitakayokutaarifu, ndani ya wiki hizo mbili, halafu kiulaiiini kazi inamalizika huku ulimwengu wote ukijua ni ajali.”

    “Utafanyaje?”

    “Niachie mimi. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba, Jeff na Roy watasafiri pamoja, halafu Jeff atakufa kwenye ajali feki.”

    “Sawa.”

    Kikao kikafungwa!

    Wakatawanyika.

    Siku zote Roy amekuwa akifanya kazi katika kundi hilo la Kimafia, ameua watu wengi sana, tena kwa mikono yake mwenyewe. Alishawahi kunyonga mama na watoto wake wawili wadogo, kwa mikono yake mweyewe na hajawahi kujisikia huruma.

    Kifo cha Jeff hakikumfurahisha hata kidogo, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kumuua Jeff, lakini moyo wake ulikataa kabisa kufanya hilo. Hata yeye mwenyewe alijishangaa, maana ilikuwa kazi yake ya kila siku. Sehemu ya maisha yake.

    Usiku mzima alikuwa akiweweseka, Jeff alikuwa rafiki mzuri sana kwake, kwa siku moja aliyofanya naye kazi, aligundua alikuwa kijana muungwana sana na hakutakiwa kufa hasa kutokana na upole na ukarimu aliouonesha.

    “Hapana, siwezi kumuacha Jeff afe,” akawaza.

    “Lakini sijui nitatumia njia gani, maana mimi ndiye ninayetakiwa kuhakikisha anakufa, asipokufa ni wazi kwamba nitakuwa nimejisababishia matatizo! Sasa nitafanyaje? Maana moyo wangu hautaki kabisa kushuhudia Jeff akifa, ingawa najua kabisa kwamba kama nisipomuua na ikajulikana ni mimi ndiye niliyemtorosha, nitapata matatizo makubwa sana. Acha nilale, kesho nitajua la kufanya,” aliwaza hayo kisha akajifunika shuka na kulala.

    *****

    Siku iliyofuata, Roy alilazimisha uchangamfu na kumaliza siku salama akiwa hana jibu ya namna gani angemsaidia Jeff. Ndani ya nafsi yake, hakutaka kabisa kuona Jeff anakufa, lakini tatizo lilikuwa ni kwa jinsi gani angeweza kumsaidia. Hapo ndipo palipokuwa na maswali yasiyo na majibu.

    Kwa wiki nzima alikuwa bado anafikiria, huku safari yao ikiwa imebaki wiki moja tu huku Jeff akiwa hafahamu chochote juu ya safari hiyo. Akiwa amejiinamia ofisini kwake, akapata wazo, lakini ilikuwa lazima apate muda wa kuzungumza na Jeff kwanza ili amweleze hali halisi ilivyokuwa. Akanyanyua simu iliyokuwa mezani kwake na kumpigia Jeff.

    “Sema Roy, kuna tatizo?” Ilikuwa sauti ya Jeff kwenye simu.

    “Hapana boss, nina mazungumzo kidogo na wewe.”

    “Njoo ofisini kwangu.”

    “Hapana, hayahitaji mimi kuja ofisini kwako, tunaweza kuongea tu, kwenye simu.”

    “Sawa.”

    “Nataka kukutoa jioni, baada ya kazi.”

    “Kunitoa?” Jeff akahamaki.

    Alikuwa na kila sababu ya kuhamaki, maana alikuwa hana mazoea kabisa na Roy, isitoshe alikuwa mgeni na yeye alikuwa bosi wake. Mazoea yametokea wapi?

    “Ndiyo...kwanini unashtuka? Nataka kukupa ofa.”

    “Ofa?” Jeff akazidi kushtuka, ilikuwa maajabu sana kwa Roy kutaka kumpa yeye ofa.

    “Ndiyo, kwani vipi?”

    “Ahsante sana Roy, tufanye siku nyingine, leo nina ratiba nyingine.”

    “Hizo ratiba zako hazina umuhimu mkubwa kama mwaliko wangu, naomba ukubali maana nina habari muhimu kwa ajili yako, tena unatakiwa kuzipata leo.”

    “Mbona unanitisha?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sikutishi, nakuambia ukweli, tafadhali sana, naomba tukutane jioni.”

    “Wapi na muda gani?”

    “Kuhusu muda ni saa tatu kamili usiku, sehemu nitakujulisha muda huo ukikaribia.”

    “Poa.”

    “Kazi njema bosi wangu.”

    “Nawe pia, ingawa lazima niseme ukweli kuwa umeniacha na maswali mengi sana.”

    “Ni lazima ujiulize maswali, lakini ni bora ujiulize maswali ambayo muda mfupi ujao utapata majibu yake, kuliko kujiuliza maswali ambayo hujui sehemu utakayopata majibu. Nakuhakikishia, jioni nitakuwa majibu ya maswali yako.”

    “Sawa.”

    Wakakata simu zao.

    *****



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog