Search This Blog

Friday, October 28, 2022

ZARI LA NDOA - 4

     





    Simulizi : Zari La Ndoa

    Sehemu Ya Nne (4)





    Saa 6 juu ya alama, Noah nyeupe ambayo walikuwa wakiitumia siku iliopita, leo tena ilipaki nje ya nyumba na kuwachukua kuwapeleka eneo la Ruaha, nje kidogo ya Jiji la Iringa lakini ikiwa ni ndani ya Manispaa hiyohiyo ya Iringa, huko ni eneo la watu wenye pesa zao.

    Kila upande walikuwa wakiziona nyumba nyingi sana ghali tena ni za thamani kubwa. Katika nyumba zile ndio waliingia moja wapo na kukuta ndani ya uwanja wa nyumba ile kila upande ukiwa umepambwa vizuri.

    Ulikuwa ni uwa mdogo tu ukiwa umezungukwa na maua halisi ambayo sasa yaliongezwa na mapambo, hali iliyofanya pavutie zaidi na kusababisha pawe na mvuto wa kipekee.

    Walikuwepo watu wachache mno na meza zisizozidi nne, wao wakakaribishwa kwenye meza moja iliokuwa na viti vinne na vyote vikiwa ni vitupu. Walipoketi tu akaja mtu na kuwaulizia vinywaji.

    Taratibu walipitisha vinywaji vyao baridi kwenye makoo yao huku Zain akiwa na hofu, mapigo yake ya moyo hayakuwa kwenye mwendo wake wa kawaida. Bado pale mezani hawakuwa na mwenyeji yoyote, walikuwa wao wageni watupu.

    Baada ya dakika chache mbele ndio akatokea mama mmoja alievaa kikongo, akiwa ameongozana na kijana mmoja alievaa suti ya bluu ikiwa ni zile style mpya iitwayo 'Dont touch,' yaani suti ambayo iliishia kwenye usawa wa vifundo vya miguu, wengine huita macho ya miguu.

    Walitoka moja kwa moja ndani na kuelekea kwenye ile meza walikuwa wamekaa Zain na wazazi wake. Wazazi wa Zain walimtambua yule kijana kuwa ni Makos ila yule mwanamama hawakumjua ni nani.

    Zain yeye hakumtambua yoyote kati ya wale walikuwa wakiwaelekea pale walipo, lakini walipowakaribia, ile sura ya kiume Zain aliweza kuikumbuka sura ile lakini alishindwa kabisa kuitambua ni wapi aliiona na lini.

    Walifika na kusalimiana wakiwa wote wamesimama, kisha Makos akamuita mmoja wa watu waliokuwepo pale kwa ajili ya kuhudumia, akamtaka aongeze kiti kimoja pale ili waenee, akawaruhusu wageni wao wakae.

    Muitikio wa salamu, ukamfanya Zain ahisi yule ndio Makos kutokana na sauti ile ya kwenye simu, lakini yeye mwenyewe akajipinga hasa baada ya sura ya yule kijana kujirudia na kukumbuka kuwa kuna sehemu aliwahi kumuona.

    Hiyo sehemu aliyowahi kumuona ndio wala haikumbuki ni wapi. Aliamini kabisa kwamba Makos yeye atakuwa hajawahi kabisa kumuona, akaendelea kumtazama kwa jicho pembe hadi wakati kiti kilipoletwa.

    Makos akamuomba mama yake asimame wakati huo hata nae alikuwa hajakaa chini. Akamtambulisha mama yake kwa wageni wao, kisha akawageukia wageni wake na kuwaambia

    "Wazee wangu kwanza samahani sana, leo tukio hili linatokea wakati baba yangu akiwa hayupo, amekwenda safarini Zanzibar kikazi, maana yeye ni mfanya biashara, lakini bahati mzuri yupo mama yangu mzazi hapa, nafikiri hakijaharibika kitu, tunaweza kuendelea tu bila tatizo..." Aliongea na tabasamu usoni huku akiwatazama wote kwa zamu, kama vile anawataka ushauri vile, akawaona kuwa wanatikisa vichwa kukubaliana nae, akaendelea

    "Napenda kumtambulisha kwanza kwenu, mama yangu huyu, karibuni sana!" kisha akamgeukia mama yake na kumwambia

    "Mama hawa ndio wageni wetu tuliokuwa tukiwasubiri kwa hamu, huyu hapa ni Mzee Mapunda na pembeni yake ni mkewe, hawa ndio wazazi wa Zain ambae ni huyu hapa mwisho," aliwatambulisha wote pia kwa ishara kama alivyokuwa akiwataja, ndivyo alivyokuwa akiwaonesha huku akiwa amesimama.

    Wakasalimiana kwa mara nyingine sasa wakiwa wametambuana vema, ajabu Makos hakujitambulisha yeye wala hakumgusia Zain hata kidogo tofauti na jina alilolitaja, chakula kikaletwa na wakaanza kula taratibu wakiwa kimya.

    Hapo ndio Makos akamtazama Zain kwa jicho la wema na kumuuliza kama anamfahamu? Zain akajibu kwamba sura ile si ngeni kwake lakini hakumbuki alimuona wapi, Makos akacheka huku akimtazama mama yake na kusema;

    "Mama nilipokuwa nikikwambia Zain nimeonana nae mara moja tu ulikuwa unakataa, leo umeamini?" Huku uma ikwa mdomoni, mama Makos alitikisa kichwa kukubali.

    Makos akamgeukia tena Zain aliekuwa kashika glasi ya kinywaji, nae Makos mkono wa kushoto alikuwa kashika uma na mkono wa kulia alikuwa na kisu akikata nyama, akasema akiwa na tabasamu pana usoni

    "Zain, mimi nawe tulionana mara moja tu japo najua hukumbuki ni wapi wala ni lini, hahahaa… lakini kama utakumbuka, tulionana mwaka juzi kwenye uwanja wa Bombambili kwenye mechi ya Basketball kati ya Iringa na Songea," Makos akacheka na Zain akacheka huku akitikisa kichwa kwa shauku ya kuongea akasema

    "Ok! Ok... nimekumbuka, dah! Kitambo sana! Uliniambia unaitwa Matwiga kama sikosei."

    "Asee! Safi sana, una kumbukumbu nzuri mno." Wote mezani wakacheka na kuendelea kuongea huku wakipata mlo kidogo kidogo.

    Jioni ndio waliondoka pale wakishindikizwa na Matwiga aliekuwa ni dereva na mama yake ambae alikaa nyuma pamoja na wanawake wenzie wakati Mzee Mapunda alikaa mbele na Makos.

    Kabla ya kuwafikisha walipofikia, waliwatembeza mjini karibu kila sehemu hadi waliporidhika ndio wakaelekea hotelini kwa ajili ya chakula cha usiku, kisha ndio wakarejea nyumbani.

    Mama Matwiga alikuwa ndio kama mwenyeji wao, alikuwa akiwaonesha kila sehemu aliyoiona inafaa kwa wao kuoneshwa, Mzee Mapunda nae mbele aliendelea kula kipupwe huku akioneshwa mandhari ya mji na mkwewe mtarajiwa.

    Siku hiyo muda wote simu ya Zain haikutumika, ilikuwa likizo isiyo rasmi, jambo la kushangaza ni kwamba hata Sungura hakutuma sms wala kupiga simu, kama mtu alimwambia vile.

    Usiku kama kawaida kabla ya kulala, Matwiga sasa ndio akajitambulisha kuwa yeye ndio Makos. Zain akashangaa na kutabasamu, kisha Makos akamwambia ile Makos ni kifupi cha jina lake yeye na jina la ukoo wake.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yeye anaitwa jina la Matwiga na familia yao inatumia jina la Komba. Zain akatoa kicheko kikubwa na kumuuliza Makos kwa nini alikuwa akimsumbua vile kwa muda mrefu kuumiza kichwa.

    Matwiga akamwambia alikuwa akitaka amuache awe huru na chuo bila kuchanganya mapenzi na elimu na wakati huohuo asikate mawasiliano na Sungura kwa ghafla vile. Makos alikuwa na maana yake kulichomeka jina la Sungura kwenye maongezi yale.





    Jina lile la Sungura lilipotajwa na Matwiga, lilimshitua Zainab na kumwambia Matwiga safi kama anatambua uwepo wa Sungura. Nae akamueleza kwamba sasa wakati wa Sungura umekwisha na huu sasa ni muda wake yeye Matwiga.

    Zainab akamjibu kuwa ni vigumu mno kufanya uamuzi kama huo, Makos wala hakumlazimisha kufanya maamuzi yale muda ule, bali akamwambia akae chini na kufikiria, kwani muda bado anao.

    "Unamkumbuka Komba?" alivyoona msimamo wa Zainab ni uleule, akampoteza kwa swali.

    "Komba? Komba gani?" alivuta taswira lakini wala haikuja picha yoyote kichwani mwake, picha iliisha futika kitambo.

    "Komba wa bodi ya mikopo!"

    "Yeah! namkumbuka sana yule jamaa, nawe unamjua?"

    "Ndio, yule ni jamaa yangu, nina muda mrefu sana sijaonana nae!"

    "Duh! jamaa tapeli yule... ni wa kwanza na hata anae mkaribia sijamuona dah!" Huku akicheka, akamuhadithia tangu mwanzo hadi mwisho. Makos alikuwa akimsikiliza akiwa na tabasamu usoni, alipomaliza kuhadithia Zain, yeye akacheka tu. Zainab akamuuliza mbona anacheka? Makos akamwambia

    "Zainab, ile ilikuwa ni plan A, iliposhindikana, ndio ikaingia plan B."

    "Sijakuelewa Matwiga, unamaanisha nini?"

    "Komba yule wa bodi ya mikopo, ndio huyu Matwiga unaeongea nae sasa hapa mbele yako."

    "What!?" Alishangaa sana Zainab karibu amwage juisi yake aliyokuwa nayo mkononi, na kukubali moyoni mwake sasa kuwa Matwiga alimpenda kwa dhati tangu alipomuona kwa mara ya kwanza kule uwanjani.

    Taratibu bila hodi, Matwiga akaanza kujisogeza kwenye moyo wa Zainab ambao ulikuwa umejaa kwa penzi la Sungura, lakini kwa kasi ndogo ndogo akawa akajikuta akimsukuma mwenzie nje polepole.

    Masikini pasina kujua Sungura kuwa anadondoshwa kutoka kwenye moyo wa Zainab, yeye aliendelea tu kuja kwamba penzi lao daima litadumu.

    Lakini pamoja na kuhisi Matwiga kuingia ndani ya moyo wake, bado Zainab alishindwa kuzizuia hisia zake kwa Sungura, hata Makos alipomuhitaji faragha alimgomea na kumwambia kamwe hatokuwa ndani ya mapenzi ya ngono hadi afunge ndoa, lakini hakubainisha kufunga ndoa na nani.

    Hilo wala halikuwa ni tatizo kwa Makos ambae alikuwa amedhamiria kabisa kuwa na Zainab hadi milele, alimtaka kabisa kuwa ni mkewe wa ndoa tena ndoa ya kidini.

    Waliendelea kuongea mambo ya kimaisha pasina kuzungumzia sana mapenzi, Matwiga aliamini fika kabisa kwamba Zain hana jeuri ya kupinga kuwa Mpenzi wake kutokanana mambo anayomfanyia.

    Pia aliamini kwamba hata wazazi wa Zain nao wapo upande wake, hivyo swala la kukwama kwake aliona ni kama ndoto, ndio maana hakutaka kulizungumzia hilo jambo kila mara.

    Upande wa Zain sasa aliona kama anashindwa kufanya maamuzi sahihi, kauli ya mama yake ikawa inamrudia, na hata hapo sasa ilikuja kama mawimbi ya bahari

    “Mwanangu, ukishindwa kufanya maamuzi kwa sasa, utakuwa unajiweka kwenye wakati mgumu zaidi hapo mbeleni…” ndio kauli ya mama myake na sasa aliuona ukweli wa kauli hiyo toka kwa mama yake.

    Walimaliza maongezi yao pale na kuachana kila mmoja akiwa na wazo lake kichwani huku Zain ndio akiwa kwenye wakati mgumu kuliko watu wote wengine.

    **********





    Siku chache mbele kama zilivyo mila zetu za kiafrika, Mshenga toka kwa Matwiga alikwenda hadi kwa wazazi wa Zainab ili kupeleka posa lkama ambavyo alipaswa kufanya.

    Suala la kukataliwa wala hakuna alielipa nafasi, kwani tayari pande zote walikuwa wakitambua uhusiano uliopo baina yao, japo Zainab hata hakua akijua ni upande upi asimame.

    Wazazi wa Matwiga, hasa mama yake Matwiga alikuwa akiwasiliana na wazazi wa Zainab kila mara, lakini hata siku moja wazazi wala mtu yeyote wa upande wa kina Sungura hakuna alie onekana kwa wazazi wa Zainab.

    Hivyo posa ile ikakubaliwa na hatimae siku chache mbele mahari ikalipwa na kubakia siku tu ya kufunga ndoa. Mambo hayo yote yalifanyika kimya kimya kabisa pasina jirani yoyote kujulishwa.

    Pamoja na hayo, habari zikavuja na kumfikia Simba, nae hakutaka kulikalia kimya jambo hilo, tena bila hata ya kufanya uchunguzi, akamfikishia mdogo wake. Sungura wala hakupanic, alijua zile ni figisufigisu tu za mambo ya mjini, akachukua simu na kumuuliza Zainab ili kuhakiki.

    Alijibiwa kama alivyo tegemea yeye, kuwa huo ni uzushi tu, yeye atulie na masomo yake hadi amalize mwakani ndio mambo mengine yataendelea, akamuahidi na kumrushia kiasi cha pesa baada ya maongezi ili kimsukume kidogo.

    Na siku hiyo ndio Zainab akamwambia kuwa amepata kazi ya kujishikiza kwa muda huko Iringa mjini, hivyo baada ya muda atakwenda Iringa kuripoti. Sungura alifurahi mno na aliona hiyo ni kama bahati kwa mpenzi wake.

    Alijua fika ni kiasi gani watu huhangaika kupata kazi mara baada ya kumaliza masomo, kila wanapokwenda huambiwa wanahitajika wazoefu. Mbaya sana hata nae hakuhoji ni vipi yeye Zainab kapata kazi kwa haraka vile.

    Sababu kuu ni kwamba alimuamini Zainab kupita kiasi, kichwani sasa akajua hata zile shida ndogo ndogo sasa zitafikia tamati kama si kikomo, ikiwa mpenzi wake ambae anategemea kuja kuwa ni mkewe atapata kazi yenye maslahi hata kama ni kidogo.

    Mwezi mmoja ulitosheleza kabisa kwa upande wa Matwiga na familia yake kufanya maandalizi kwa ajili ya harusi na maandalizi yote ya ndoa. Siku ikapangwa na kusubiriwa kwa hamu kubwa, kila upande ukiwa upo kwenye maandalizi ila kwa siri hasa upande wa kina Zainab.

    Hadi kipindi hicho bado Zainab hakuwa na maamuzi sahihi, alitamani mno kuongea na Sungura juu ya jambo lile lakini hakujua ni vipi aanze, kibaya zaidi hakuwa anajua ni upi msimamo wa Sungura kuhusu penzi lao.

    Akawa akijipa moyo kwamba siku bado ataongea nae tu hadi zinasalia siku takriban 10 bado hata hajaongea nae chochote, kuficha tena ikawa haiwezekani, ni lazima sasa kiila kitu kiwekwe hadharani, wakapita kina mama kutangaza mambo yao.

    Ilikuwa wanapita nyumba kwa nyumba na wakati huo huo wakiuza Madera ambayo walisema yatatumika kama sare kwa kina mama ambao watakuwepo kwenye shughuli.

    Kwa mara nyingine Simba akapata fununu za ndoa ya Zainab, lakini safari hii akiwa na uhakika kabisa kutokana na mzazi mwenzie yaani Mpenzi wake Simba anae ishi nae nyumbani kwao, kuja kualikwa.





    Lakini hakujua ni nani anaetaka kumuoa shemeji yake Zain. Safari hii hakutaka kumjulisha ndugu yake kinacho endelea bila kuwa na ushahidi wa kujitosheleza, alitaka kujua anaolewa wapi, lini na anaemuoa ni nani? Akapeleleza sana lakini hakufanikiwa kujua lolote.

    Jina la mchumba wa shemeji yake liligeuka kuwa ni lulu, maana halikupatikana, akaamua kumpigia mdogo wake na kumueleza kwa kituo kila kinachoendelea, Sungura akacheka tu kwa kujua kaka yake anamtania.

    Msisitizo aliokuwa akiuonyesha Simba, ikamlazimu Sungura atulie na kuwa makini, Simba akamueleza kile alichokifanya na hatua alioishia na kumtaka yeye sasa aendeleze kutokea pale.

    Sungura akaghadhibika sasa, akakata simu kwa kaka yake na kumpigia mpenzi wake ambae muda ule alikuwa hapatikani hewani. Alikuwa bado na imani nae Akapiga tena kwa kuamini huenda tu ni mtandao umesumbua na kama ikiwa ni kweli asemacho basi simu itakuwa haipatikani.

    Lakini simu ikaita, akahisi habari ile si kweli na kama ni kweli basi simu haitapokelewa, lakini ndani ya dakika 0 tu simu ikapokelewa, na aliepokea simu ile ni Zainab mwenyewe. Kupokea tu kule simu Sungura akaona huu ni uzushi.

    Alihisi kaka yake kadanganywa kwa mara nyingine. Baada ya salamu na kuongea kwa dakika kadhaa, sasa ndio Sungura akaona huu ndio wakati muafaka wa yeye kukata kiu yake kwa kuuliza kile alichoambiwa, alipaswa kutumbua jipu wakati huo.

    “Zain Mpenzi wangu, mara ya kwanza nilipokuuliza kuhusu kutaka kuolewa, ulikataa kabisa na kusema ni uzushi, lakini sasa suala hilo limerejea tena, nimekuwa nikikataa tu huku nipo mbali nawe, hebu nieleze ukweli, ni nini kinaendelea huko Songea?”

    Zainab akasinyaa kutokana na swali la Sungura, ni swali ambalo wala hakulitegemea, alitamani sasa nae awe ni mmoja kati ya watu wa kuuliza lakini si mtu wa kujibu swali gumu kama lile, alikosa jibu.

    Baada ya kujifikiria kwa sana na kuomba radhi mara kadhaa, radhi ambayo wala hata Sungura hakuisikiliza, yeye alichotaka kujua kama habari ile iliyomfikia ina ukweli ama ani uzushi tu?

    “Yaani usihofu chochote Mpenzi wangu, maana kama ningekuwa karibu ungehofu labda nitakupiga, lakini nipo kilometa mia 3 za umbali nawe, unafikiri nitakufanya nini? Zaidi ya kukusikiliza tu na kukubali usemacho kiwe ni cha kweli amam ni uongo? Nieleze tu Zain wangu!”

    Maneno yalikuwa kama mkuki wa moto kwenye nyama ya shingo na misuli laini ya shingoni, iliuma sana, lakini Zain akapata ujasiri wa ajabu na kumwambia Sungura kile alichokisikia ni kitu cha kweli kabisa wala si cha kubuni.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sungura aliishiwa na pumzi, alitaka kuongea maneno milioni lakini alishindwa kutoa hata neno moja, alitamani Mbingu imfunike kwa ukaribu kabisa ili asionekane tena.

    Hilo alilokuwa akiliwaza muda huo la kufunikwa na mbingu lilikuwa haliwezekani kabisa, akamuuliza tena Zainab, je ni kweli asemacho ama anamtania? Ukweli ukabaki hivyo lakini awamu hii huruma na mapenzi ya dhati toka kwa Zainab ikajionesha wazi.

    Akamueleza kwamba anafunga ndoa ambayo hata yeye mwenyewe hajapenda,

    “Mpenzi wangu, tambua kuwa hii ndoa itakuwa na maslahi kwetu…” Sungura hakutaka kuendelea kusikia chochote, akakata simu na kuanza kulia, alitamani hata ile simu nayo aipigize ukutani huko, maana aliona kama inamzidishia machungu tu, alilia mno akiwalaumu wanawake wote duniani.

    Masikini ya Mungu, alisahau kuwa hata mama yake nae ni mwanamke, na pia amekosewa na mwanamke mmoja tu ambae ni Zainab wala si wote walio mkosea. Akiwa ndani ya majonzi ya kuondokewa mikononi na mpenzi aliekuwa akimuamini na kumtegemea, simu yake ikaita tena.

    Aliinyanyua na kumtazama mpigaji, alihisi atakuwa labda ni Simba anataka kujua kama tayari ameongea na Zain, lakini wala hakuwa Simba, alikuwa ni Zainab safari hii akiwa amepiga yeye, Sungura akaikata na kuizima kabisa.

    Mapenzi ni kama upofu, pamoja na kauli zote zile alizo sikia toka kwenye kinywa cha Zain mwenyewe, lakini Sungura hakutaka kuamini kabisa kuwa ni kweli Zainab anaolewa na wala hakutaka kujidanganya kwamba anamtania.

    “Hata kama ni utani, wa aina hii mimi wala siuhitaji hata kwa bahati mbaya, japo ninaomba iwe ni masihara, ila je kama ni kweli Sungura mimi nitafanyeje?” alijiulliza Sungura huku akijifuta machozi, alihisi kama Dunia imemtenga vile.

    Alifikiria mbali sana kwa muda mchache, akaanza na kujuta juu ya ushauri alioutoa kwa Mpenzi wake

    “Dah! Chuo… Ni mimi mwenyewe ndio nilimshauri kwenda chuo, sasa ananiliza, masikini mimi… ndio maana wazee wetu walikuwa hawataki watoto wa kike wasome, sasa nimejua ni kwanini, ahsante sana Zain…” akanyanyuka kuelekea nje.

    **********



    Matwiga aliendelea kupokea ndugu na jamaa kutoka sehemu mbalimbali za Iringa pale na sehemu zingine za mbali. Alijipanga haswa kwa shughuli ambayo alitaka iwe ni ya kupendeza na mfano kwa wengine pale mkoani na mikoa ya jirani.

    Alipanga iwe ni shughuli ya mfano kwa wakazi wote wa Songea na Iringa kwa ujumla, ndio maana hata baadhi ya wageni kutoka sehemu mbalimbali walianza kuwasili.

    Usiku Sungura alimpigia simu kaka yake na kumueleza kuwa ile fununu aliyomueleza, kumbe ni habari ya kweli wala sio uongo. Akamwambia juu ya maongezi yake na Zainab na mwisho akamueleza juu ya kauli alizotoa Zainab kwamba hata yeye hajapenda ile ndoa.

    "Ndio kauli zao hizo ndugu yangu, wewe kwani ulitegemea atasema ndio amependa?"

    "Kaka ujue hapa mimi hata sijielewi, hebu niambie nifanyeje?"

    "Sungura mdogo wangu wewe tulia... fanya kazi zako, mapenzi yapo, wanawake wapo wengi sana, achana na Zainab anaetarajia kuwa mke wa mtu."

    "Sio kwa urahisi kama unavyo tamka kaka, nampenda mno Zainab, ila kuna kitu nimefikiri hapa."

    "Kitu gani hicho?"

    "Kesho ninakuja Songea, kesho ninarudi nyumbani."

    "Kha! Sungura, na kazini je itakuwaje?"

    "Nitaomba kama siku 3 hivi ili nije hukohuko nyumbani."

    "Sawa, sasa unakuja kufanya nini?"

    "Nataka Zainab aniambie mbele ya macho yangu kuwa hanitaki na anataka kuolewa na huyo mwanaume."

    "Achana na habari hizo mdogo wangu, huku maandalizi yamepamba moto, ujaji wako hauwezi kubadili chochote dogo, hebu kaa huko uendeleze maisha yako."





    "Hapana kaka, mimi kesho ni mgeni wako, kwa heri kwa sasa," akakata simu bila hata kumpa nafasi kaka yake ya kuendelea kuongea, alijua kabisa kwa nasaha za kaka yake zilivyo, anaweza kujikuta ameahirisha safari, kitu ambacho alikuwa hataki kitokee hata kwa bahati mbaya.

    Hivyo hata baada ya kukata simu, aliizima kabisa na kupanga kuiwasha akiwa tayari yupo Songea, maana maneno ya Simba ni hatari sana, alikuwa na ushawishi mkubwa lakini pia alimuheshimu mno kaka yake.

    Ngonyani Ndunguru, rafiki mkubwa wa Matwiga kwa pale Songea ambae kwa sasa anaishi kwenye nyumba anayoimiliki Matwiga iliyopo eneo la Mahenge, alimuona Sungura akishuka kwenye basi na kushtuka sana.

    Hakutegemea kumuona mtu yule maeneo yale kwa siku zile chache zilizobakia, maana yeye alikuwa akijua vema uhusiano baina ya Sungura na Zainab, na ndio aliongozana kwa mara ya kwanza na Matwiga hadi ndani ya nyumba ya kina Zain, kwa hiyo kule kumuona Sungura pale ilikuwa ni kama mkosi kwao.

    Akapata shaka na kumpigia simu Matwiga kumueleza juu ya kuonekana kwa Sungura pale mjini.

    Matwiga hata nae akapata hofu, akampigia simu Zainab na kumuuliza kama ana mawasiliano na Sungura. Kwa mara nyingine jina lile likamshitua Zainab na kuhoji kwani vipi hadi anamuulizia.

    Akamueleza juu ya kuonekana kwa Sungura, mshituko alioupata Zainab hata Matwiga japo alikuwa mbali ambapo hakuweza kumuona, lakini aliweza kuugundua. Akamuuliza vipi? Nae akajibu kuwa hakuna kitu.

    Lakini alificha ukweli, aliogopa mno kuwepo kwa Sungura pale mjini, kwani alikuwa bado anampenda sana tofauti na penzi lake alilonalo kwa Matwiga. Kingine alichohofia ni iwapo Sungura atafika kwao na kuonana nae, ni nini atamwambia hadi Sungura amuelewe?

    Hilo ndio lililomtia shaka! Matwiga akakata simu bila ya muafaka, nae sasa hofu ikamuingia bila hata ya kujua ni kipi hasa kilicho sababisha apate hofu na hali akijua dhahiri kwamba Sungura ni mtu mdogo sana kwake.

    Kwa kila hali, Sungura asingeweza kumsumbua Matwiga, kwani alimzidi kila kitu, alimzidi umri, alimzidi kipato naha elimu pia limzidi, lakini kwanini alimuhofu? Hata yeye hakupata jibu.

    Akajiuliza tena ama labda uzito wa penzi kwa Zai umezidi? Mana hata Zain nae alishtuka baada ya kusikia uwepo wa Sungura pale mjini, lakini hata nae akajishangaa kwanini aingie hofu, alijiuliza ni kipi hasa kinachompa mashaka hadi anakuwa na hofu? Akajipa moyo na kuamua kusubiri aone ni nini kitakacho tokea mbeleni.

    Wakati wao wakiwa na hofu na Sungura, nae kichwani mwake alikuwa na wazo moja tu... kumtafuta Zainab na kuongea nae ili amueleze ni kwa nini ameamua kumsaliti, kibaya zaidi akataka waonane uso kwa uso.

    Kitu hicho nacho Zainab hakuwa tayari, alilazimisha tu waongee kwenye simu na Sungura hilo nae pia akawa halitaki, hapo ndio pakawa hapatoshi.

    Zikapita siku 3 bila ya kuonana, sasa ikabidi Sungura aweke silaha chini na kukubaliana na matakwa ya Zainab ya kuongea tu kwenye simu. Ni kweli waliongeqa kwenye simu, lakini bado Zainab hakunyoosha maneno.

    Sungura akamuomba tu amhakikishie neno moja kwa ulimi wake, kuwa hampendi tena.

    "Ni heri Zainab wewe ninae kupenda, uniambie neno moja baya toka kinywani mwako, kuliko kuambiwa maneno elfu moja mazuri kutoka kwa nisiempenda."http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Sungura sina neno lolote ambalo ninaweza kukwambia kwa sasa," alijibu Zainab.

    "Upweke umekuwa ni rafiki yangu, kia wakati nipo nao, lakini tangu sasa natamani kuwa kwenye dunia ya peke yangu, dunia ambayo kila upande ninaotazama, hakuna nionacho zaidi ya nafsi yangu pekee, labda kingine ninachotamani kukiona ni msitu tu mnene wenye miti mizuri mirefu ya kijani hasa, dah! dunia hii..." Aliongea Sungura kwa fumbo lakini kwa hisia kali ambazo zilimgusa Zainab na kumuuliza

    "Sungura kwa nini unasema maneno hayo?"

    "Zainab ninenayo hapa wala si njozi, ni kweli, maana nipo kwenye dunia iliyojaa watu wengi wazuri wa sura na maumbo, nikiamini hata mioyo yao pia itaendana na uzuri wa nje, lakini si hivyo, ninaachwa mpweke, nahisi kutengwa na jamii nzima," maneno ya leo ya Sungura yalikuwa ni kama msumari wa moto kwenye uso wa mtu alietumia madawa makali ili kujichubua ngozi yake.

    "Hujatengwa Sungura, mimi ninakupenda sana Sungura, lakini tu kuna vitu hapa kati..."

    Alijaribu kujitetea Zainab na Sungura akamkatisha kauli yake hata kabla hajamaliza;

    "Huna jipya la kunieleza, ulijitetea hivyo kule awali, nashukuru sana lakini tambua nami nimechoka aina hii ya maisha, lini nami nitakuwa kwenye maisha yenye furaha na amani kama maisha hayo uliyonayo wewe?" Swali hilo lilimzidi uzito Zainab na kukata simu.

    Akaangusha kilio kikubwa sana huko alipo. Ikamlazimu Sungura kuanza kukubali matokeo kuwa Zainab dsi wake tena, nae akaanza kulia kwa ghadhabu hadi alipokuja kaka yake na kumtuliza.

    Wakatoka na kuzunguka huku na kule ili angalau mdogo wake apunguze mawazo. Wakaenda hadi Matarawe shuleni na Simba akaingia uwanjani kufanya mazoezi na wenzake huku Sungura akiwa na jamaa wengine wanapiga soga.

    Mazungumzo yalikuwa matamu sana, yalikuwa yakihusu uchaguzi mkuu ambao ulikuwa ufanyike mwezi ujao, mazungumzo yale yalimpa unafuu mkubwa mno Sungura maana akili yake ilipata nafasi ya kupumzika.

    Ila jinamizi la ndoa ya Zainab halikuacha kumfuata kila mara, lakini kutikana na kuchangia kila wakati mada ile waliyokuwa nayo, ikamsaidia mno kuweza kukaa muda mrefu bila kumtokea.

    Mazoezi yalikwisha nao wakaanz kurejea nyumbani, njiani wakakutana na msafara wa garikama 5 hivi zikiwa zimepambwa kama vile zipo kwenye sherehe fulani hivi, na ni wazi kabisa ilionekana kama ni harusi.

    Mmoja kati ya vijana waliokuwepo pale, akasema kumwambia mwenzie kuwa Zainab anaolewa siku ya Jumamosi na pale ndio wanakwenda kwenye sherehe ya Send off inayofanyika kwenye ukumbi wa Matarawe.

    Moyo wa Sungura ukapiga 'Pah!' japo anajua suala la harusi lakini ile kusikia mambo ya Send off, ndio ikamzindua akili kuwa Zainab anaolewa kweli wala sio utani. Yeye mwenyewe akawa hata hajielewi.

    Akamgeukia kaka yake na kumkuta akimtazama yule kijana aliekuwa akihadithia kwa kujiamini kama katumwa vile, bado alikuwa akimuhadithia mwenzie;





    "Halafu huyo Zainab alikuwa na jamaa fulani nasikia jina lake alikuwa anaitwa Sungura, jamaa yupo chuo, kamtosa na sasa anaolewa na Matwiga, si unamjua huyo jamaa?" wengi wao pale walikuwa wakimjua Sungura na tukio walikuwa wakilijua, lakini walinyamaza, walishindwa kumzuia kijana asiendelee kuongea.

    Swali la yule kijana kwa mwenzie, likafanya wote wamtazame Sungura, nae akajitutumua na kumuuliza yule kijana

    "Huyo Matwiga yupoje? Nae anaishi hapa Songea?"

    "Matwiga anaishi Iringa Mjini, ni jirani yetu kule mtaani, ana mawe huyo? Kama vile yanamfuata yenyewe, achana nae kabisa..." Dogo kwa kuwa alikuwa hamjui Sungura akaendelea tu kufunguka

    "...wewe kama unapenda Basketball, basi ni lazima umjue Matwiga, nasikia kuna siku alikuja hapa na kusumbua sana..." Sio tu Simba aliemjua mtu anaetaka kumuoa Zainab, bali hata Sungura sasa alimtambua mtu huyo ambae anatarajia kumpora mpenzi wake.

    Kwa kweli aliumia mno nafsi yake, roho ilimuuma sana, moyo ukafa ganzi, kwa mara ya kwanza akili yake ikamtuma kufanya jambo. Halikuwa jambo baya, bali kwake aliona ni unafuu mkubwa, alitaka kumrejeshea Zainab kila kitu alichompatia kile ambacho kipo.

    Hiyo ndio aliona ni njia muafaka kwake ili kupunguza machungu, maana alikuwa akihisi pindi ambapo akiviona atakuwa anaumia tu moyo wake na hawezi kugawa wala kuvitupa, maana alipewa.

    Hakumwambia mtu yeyote juu ya wazo lake lile, alisubiri hadi walipofika nyumbani na kuingia chumbani kwake, akachukua mikanda mitatu ya kiuoni iliyo tengenezwa kwa ngozi, saa mbili, simu yake akachomoa sim card na kuiweka pembeni, miwani pia zilikuwa mbili.

    Pia akachukua viatu kama pair 3 hivi na kapelo 1, akavitia kwenye begi dogo aina ya Lasket ambalo nalo alipewa na Zainab, kisha akatazama nje kuangalia usalama, aliporidhika baada ya kuona hakuna mtu, akatoka na begi lake hadi nje.

    Akasimamaisha Bodaboda na kudandia akimtaka dereva amuwahishe Matarawe shuleni haraka iwezekanavyo. Hakufanya ajizi dereva wa bodaboda, alikuwa kazini. Moja kwa moja hadi getini na kumuacha pale baada ya malipo yake kufanyika akaondoka.

    Sungura akiwa na begi lake mkononi, akasogea pale walipo walinzi wa ukumbi na kuwaomba kuingia ndani ukumbini ili akatoe zawadi kwa bibi harusi mtarajiwa. Walimtazama tu na kugeuka upande mwingine hakuna aliemjibu.

    Akawasogelea na kuwaomba kwa mara nyingine, mmoja wa maaskari akamwambia hana haja ya kuomba ruhusa iwapo tu ataonyesha kadi, ataruhusiwa kuingia na iwapo hana kadi wala asijisumbue kuomba, maana hawata mruhusu kuingia.

    Hakuwa na kadi na pia hakuwa tayari kukubali kurejea nyumbani akiwa na begi lake lile pasina kurejesha vitu vile ambavyo yeye aliamini kuendelea kuwa navyo ni kujitesa tu, maana kila muda vitakuwa vinamuweka kwenye wakati mgumu kila anapo vitazama.

    Nao walionyesha ustaarabu kwa kumuomba mara kadhaa arejee nyumbani amsubiri kwao ampe zawadi ile ama lah awaachie wao watampa wakati akitoka, hakuwa akiwaelewa hata kidogo, alishikilia palepale.

    Alisema anataka zawadi ile ampe yeye mwenyewe tena ni palepale ukumbini. Walinzi sasa wakashindwa kumvumilia, uzalendo nao ukatoweka, wakaamua kumfukuza.

    Bado akawagomea na kuonesha kiburi cha hata kutaka kupigana nao, masikini alikuwa ni kama mtu aliechanganyikiwa, hapo sasa akawa kachokoza moto. Ikawa ni kizaazaa, Ngonyani, mpambe mkubwa wa Matwiga alikuwa pale japo alikuwa hatulii lakini alikuwa sambamba na walinzi.

    Alikuwa pale kwa kazi maalum, kazi ya kuangalia chochote kinachojiri pale ambacho si salama kwao na hata pia kutazama iwapo Sungura atafika, ilikuwa ni kama Matwiga ameweka tahadhari tu.

    Sungura aliwapa wasiwasi sana, hawakuwa wakijiamini kabisa, kwa hiyo katika ile hali ya kuonekana pale muda ule, Ngonyani pale pale akamjulisha Matwiga, ambae alishtuka sana kusikia vile, akapanic.

    Fedha daima siku zote huwa na nguvu, dakika kadhaaa mbele ikafika gari ya Polisi ikiwa na askari kama wa5 hivi, walipofika pale ajabu wakamuulizia Sungura ambae moja kwa moja hata kabla hajajitambulisha, wakamjua kutokana na kuwa na aina tofauti ya mavazi na wengine waliopo pale.

    Wemgi walikuwa wametandika suti za nguvu miilini mwao na hata wale ambao hawajavaa suti walikua na mavazi mepesi, hpakuwa najinzi hata moja ila yeye Sungura peke yake ndio alitandika jinsi.

    Muonekano wake huo na wale waliokuwepo pale ulionesha kabisa walikuwa ni tofauti, wakambeba msobe msobe na kumtia garini kisha wakaondoka nae huku akilalamika kuonewa.

    Hakuna aliemsikiliza na ndani ya ukumbi hakuna aliejua kilichokuwa kikiendelea nje ya ukumbi, kwani vinywaji vilikuwa vimewakolea waliopo ndani na ukichanganya na muziki mkubwa uliokuwa ukivuma masikioni mwao, wala hata kuhisi kama kuna vurugu nje hawakuhisi.

    Lakini hata askari wa ulinzi waliokuwepo pale nje, nao hawakujua ni wapi wale askari wametokea, ila wao alifurahi tu kupunguziwa kero.

    Sherehe ikafungwa na kila mtu kurejea kwake wakiwa wameimaliza vizuri siku ile ya jumatano na sasa walikuwa wakirejea majumbani kwao kuisubiri kwa hamu siku ya Ijumaa ambayo ilipangwa kufungwa ndoa baada ya salah ya Ijumaa.

    Hadi usiku wa manane, Simba hakufanikiwa kumuona ndugu yake, aliamini yupo sehemu fulani na kukamia kweli kwamba muda wowote atakaorudi atamsema sana kwa ujinga alioufanya.

    Ujinga wa kuondoka bila kuaga wala kusema anakwenda wapi na tena simu akiwa amezima, ulimkera sana Simba, akafunga mlango na kulala akiamini atarejea na kumgongea.

    Hadi saa nne asubuhi siku ya Alkhamis, Sungura bado akawa hajarudi nyumbani, damu ni nzito kuliko maji, Simba sasa akaanza kupata hofu kwa kutokuonekana ndugu yake, akawaza huenda ndugu yake amekwenda sehemu na kujidhuru.

    Alianza kumtafuta peke yake kimya kimya, kila sehemu hakufanikiwa kumuona, akapiga simu kwa kila ndugu na jamaa kumuulizia, alijibiwa hayupo na hawajamuona.

    Alifika hospitali Kuu ya Songea na zahanati zote pale mjini na zile za nje kidogo, alitembelea chumba cha maiti, lakini wapi... Hakumuona!

    Kituo kikuu cha Polisi Songea mjini napo alifika na kumuulizia, napo hakuwepo na wao wakakana kupokea mtu mwenye jina kama hilo. Hapo tayari ni saa 9 alasiri, Simba akahisi kukata tamaa.

    Akarudi nyumbani kuangalia huenda akawa amerejea, napo hakumkuta. Akawa hana jinsi ila tu kumpigia simu Zainab japo aliakua akiamini hana msaada wowote, lakini akaamua tu kumpigia ili kumjulisha.





    Simba alimuuliza Zainab kama anaweza kujua ni wapi alipo Sungura kama alimuaga. Taarifa ile ilikuwa ni habari mpya kabisa kwake, kwanza alihisi ni utani wa kawaida tu, tena akahisi ule utakuwa ni mchezo wamepanga ili kumshitua.

    Zainab akajibu kwamba yeye hajawasiliana na Sungura tangu siku iliyopita mchana hadi leo hawajaongea wala kuonana. Simba akamjulisha kuwa Sungura haonekani tangu usiku wa jana hadi leo muda huu.

    Alimueleza kuwa kila sehemu kaisha enda kumtafuta na hajafanikiwa kumuona hata kupata fununu tu. Sauti ya Simba sasa ilionesha kabisa kuwa haitanii, ilikuwa ikimaanisha kile ikisemacho.

    Mwenyewe Zainab akilini kwake akajiongeza kwamba hakuna hata siku moja ambayo Simba amemtania, kufikia hapo ndipo nae sasa kichwa kikaanza kumgonga na kujiuliza

    "Hivi kama itakuwa amekwenda kujiua, mimi si ndio nitakuwa chanzo cha kifo chake? Mama yangu... kwanini lakini initokee mie?" Chozi likamdondoka.

    Polepole akaanza kukumbuka muda na wakati waliokuwa pamoja, kilio kikaongezeka. Hakujificha tena, nafsi yake ilimsuta, moyo uliumia, akajuta ni kwa nini hakufanya mamuzi mapema, akakumbuka kauli ya mama yake, akazidi kulia.

    “Mwanangu, ukishindwa kufanya maamuzi yako sasa, ni sawa na kujiweka kwenye wakati mgumu zaidi mbeleni, huenda leo hunielewi ila ipo siku utanielewa tu,” hayo ni maneno yalijirudia kichwani mwake na kumfanya apayuke kwa kilio.

    Alitamani kuzirudisha siku nyuma, lakini ilikuwa haiwezekani kurudisha hata sekunde moja acha na dakika moja.

    Matwiga na familia yao nzima walikuwa Songea Mjini kwenye nyumba yao ambayo alikuwa akiishi Ngonyani, hapo ndio walipanga kila kitu kifanyike pale kwenye siku ile ya Ijumaa na kisha Reception itafanyika siku ya Jumamosi huko Iringa, nyumbani kwao wanapoishi.

    Hivyo kwa siku ile ya Alkhamis, hadi Mzee wake Matwiga, Mzee Komba nae alikuwa pale Songea akiendelea kuratibu mipango yote ya harusi, kwani kule Iringa waliamini kamati ya maandalizi haita waangusha, ilikuwa na watu maarufu na wazoefu wakubwa wa shughuli ile ya harusi na bado kulikuwa na nafasi ya kujipanga zaidi mara baada tu ya kufunga ndoa.

    Zainab nae aliendelea kupiga simu kwa Simba kila baada ya dakika chache, jibu liliendelea kuwa ni lilelile, jibu ambalo likazidi kumuweka Zainab kwenye wakati mgumu zaidi, kila ushauri alioutoa, Simba akamwambia yeye tayari kaisha ufanyia kazi.

    Pozi likamuisha, kilio ndio kikazidi kutawala, tangu alasiri ile hadi usiku ule ambao alikuwa akiongea na Simba.

    Ilipofika saa 2 usiku, Simba nae akawa analia na kumpigia simu Zainab kumuuliza ni kipi walichoongea mara ya mwisho na Sungura. Zainab akamueleza ukweli mtupu tangu mwanzo hadi mwisho.

    Ukweli ambao wala haukusaidia lolote kuweza kujua ni wapi alipo Sungura. Kwa sasa Simba wala hakutaka kuzunguka, alimwaga lawama moja kwa moja kwa Zainab, hadi Zainab akaanza kulia kwa sauti baada ya kukata simu.

    Maongezi yalipokwisha baina ya Zainab na Simba, kilio sasa kilisikika na mama Zainab akaingia chumbani na kumkuta ni mwanae ndio anaelia. Akamuuliza ni kipi kinachomliza? Wala Zainab hakumficha mama yake.

    Akamueleza kila kitu hadi lawama anazo angushiwa na familia ya kina Sungura, hapo sasa hata mama mtu akapata woga. Alikuwa akimjua vizuri mno Sungura na hata uhusiano wao pia alikuwa akiutambua japo haukuwa rasmi.

    Sasa kama itakuwa ni kweli amejidhuru, itakuwaje? Jamii ikielewa kuwa chanzo ni usaliti wa Zain, je watachukuliwaje na waungwana pale mjini?

    Hata nae aliweza kabisa kuona kwamba mwanae hatoweza kuzikwepa lawama zile, wakatazamana na kisha mwana akamuuliza mama wafanyeje?

    Mama akamtoa shaka mwanae kwa kumwambia atulie tu hadi kesho asubuhi akiamini watapata muafaka. Zainab akagoma na kumwambia mama yake kuwa yeye hatofunga ndoa hadi ajue hatma ya Sungura.

    Mama akamshangaa na kumtuliza kuwa asiwe na hofu, huenda ikawa yupo sehemu anasikilizia tu ili kumpima. Zainab akashikilia kuwa anataka kujua hatma ya Sungura, ajue kama yu hai ama amekufa ndio mengine yatafuata.

    Alisisitiza kuwa hapendi kuwa mtuhumiwa kwa kosa ambalo hata hahusiki, na sasa rasmi akamtaka mama yake atangaze hivyo. lilikuwa ni jambo gumu mno kwa mama kulifanya. Alichoweza kukifanya mama ni kumbembeleza sana mwanae asiahirishe tukio lile adhwimu, lakini wapi.

    Mwisho mama akatoka na kuelekea chumbani kwake kumueleza mumewe juu ya jambo lile jipya lililojitokeza. Hata nae taarifa ya kutoweka Sungura ilimshitua, lakini ile habari ya kutaka kuahirisha ndoa, hiyo hakuiafiki kabisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akamuarumu mkewe aende kumuita Zainab ili yeye aongee nae, dakika 3 zilitosha kabisa kumleta pale Zainab. Baba akamwambia mwana kuwa amepata ujumbe wake, lakini yeye haukubali hata chembe.

    Akamjulisha rasmi kwamba hawezi kuahirisha ndoa kwa ajili ya kutokuonekana mtu ambae hata familia yake haimtambui yeye ni nani.

    "Zainab unajua ni gharama kiasi gani ambayo imetumika hadi sasa kwa pande zote mbili? Yaani upande wetu sisi na up[ande wa kina Matwiga?"

    "Samahani baba yangu kwa majibu yangu ya ukweli, lakini tambua hata ingetumika pesa yote iliyopo kwenye Benki kuu ya Dunia, bado haina thamani ya nafsi ya mtu mmoja tu dhalili kabisa. Hiyo pesa ni makaratasi tu ambayo mtu anaweza kutengeneza, lakini ni nani anaweza kutengeneza nafsi ya kiumbe mmoja tu baba yangu?" maneno kuntu mara nyingi hufanya mtu kupandisha jazba, ndio kilicho tokea kwa baba Zain

    "Sasa huyo Sungura ni nani hapa kwangu?" Aliuliza kwa jazba baba Zainab.

    "Sungura si lolote kwako, Mzee wangu hata mimi ninajua hilo, kwako wewe Sungura hana thamani kama tone la maji chumvi baharini, lakini kwa familia yake, Sungura ni kama tone la maji baridi Jangwani baba yangu, hatupaswi kuangalia upande mmoja tu..."

    "Sasa Nasema hivi, kesho ndoa ipo kama ilivyopangwa awali, basi!" Aliamua kufanya udikteta mzee.

    "Mkinilazimisha, basi jiandaeni kwa aibu ambayo haitosahaulika kwenye maisha yenu..." kisha akanyanyuka na kukimbilia chumbani huku akilia.

    Baba nae akasimama na kusonya huku akisema wataona, akatukana na kuelekea chumbani kwake. Mama sasa ndio akawa njia panda, hajui asimamie upande gani, wote wawili ni watu wake, mume na mtoto, akaomba subira kwa Mungu huku akijutia maamuzi yao.





    Baada ya dakika chache akawa akijifikiria awe upande wa mumewe ili kuficha aibu, lakini pia akajiuliza, iwapo atakuwa upande wa mumewe, Zainab si ndio anaweza kuwatia aibu kubwa zaidi ya hiyo ya kuahirisha ndoa?

    Akanyanyuka na kuelekea chumbani kwa mumewe na kuanza kumpoza mumewe kwanza, alipoona mzuka umempungua kidogo, ndio akaanza kuongea nae.

    Alimueleza athari za kumlazimisha kufunga ndoa na hali kaisha toa tahadhari.

    Japo awali alikuwa tayari, lakini sasa aligoma, iwapo watamlazimisha huenda akawatia aibu kubwa zaidi ya hiyo ya awali wanayo iogopa, hivyo ni heri wakae chini na kufikiria njia muafaka.

    Mzee Mapunda nae sasa akakaa na kutafakari, hivi kama Zain atakwenda mbele ya Masheikh na kukataa kuolewa, si itakuwa ni aibu kubwa kwa familia zote mbili kwa wageni waalikwa? tofauti na kuwatangazia kwa kesho kuwa ndoa imeahirishwa?kutangaza ndoa imeahirishwa ni rahic na hakuna gharama ila kuelekea eneo la tukio na kukataliwa mbele ya watu itagharimu mambo mengi ikiwepo la amani ya nafsi.

    Akaona ni vema kuketi kwa pamoja na kulizungumzia jambo lile na kuliweka vizuri mapema kabla ya siku na muda wa kufunga ndoa haujatimu. Akanyanyua shingo na kumuuliza mkewe wafanyeje?

    Mama akamshauri mumewe ni heri wampigie simu mshenga wa Matwiga na kumuita aende muda uleule ili wakajadiliane na kufikia hatma ya jambo lile kabla jogoo hajawika, Mzee Mapunda akaafiki.

    Wakampigia simu Mshenga na bahati mbaya akawa hapatikani, ikabidi wampigie simu Matwiga na kumuomba amtafute Mshenga wake muda uleule wana shida nae muhimu na tena ni yadharula.

    Bahati ilikuwa yao, maana alijibu kuwa wapo nae pale nyumbani wakiwa kwenye maandalizi ya mwisho mwisho. Wakamtaarifu kuwa kuna dharula imejitokeza, hivyo aende muda uleule na iwe ni haraka iwezekanavyo.

    Matwiga alishtuka sana kusikia vile, ikambidi aulize kama kheri ipo? Baba akamwambia kheri ipo tu tena ina amani tele. Matwiga akaitika kishingo upande kukubali lakini hakuridhika kabisa, alihisi kuna jambo limeingia hapo kati.

    Mara baada ya kukata simu akafikisha ujumbe kwa Mshenga wake, ambae muda huo alikuwa akiongea na Mzee Komba huku wakinywa kahawa. Wazee wale wote wawili walishtuka na kutazamana kwa mshangao. ilionekana kama kila mmoja alikuwa anataka kuhoji na lakini sasa atamuhoji nani?

    Kila mmoja aliwaza lake kichwani mwake, lakini mshenga akawa ni wa kwanza kuliweka wazi lile lililopo kichwani mwake. Akamuuliza Matwiga kama Zainab ni mjamzito, Matwiga akamjibu kuwa yeye hajawahi kufanya nae mapenzi hata mara moja.

    Baba nae akauliza swali lake, akamuuliza kama siku ile waliwasiliana na Zainab? Akakiri kuwa waliwasiliana asubuhi muda wa saa 5 na hadi muda ule hawajawasiliana tena.

    "Alikueleza nini hiyo asubuhi?" Alihoji Mzee Komba baba yake Matwiga.

    "Hakuniambia chochote, alikuwa kwenye hali yake ya kawaida kabisa. Tena alionesha furaha tu na hakuwa na hali yoyote ya tatizo la kiafya wala mawazo."alijibu huku bae akiwa kama mtu ambae hajiamini hivi.

    "Sasa hapa cha kufanya hebu twendeni sote watatu, wewe Matwiga utabaki garini, mimi na mzee mwenzangu tutaingia ndani, ili kujua tatizo hasa ni lipi.. naamini wito huu una jambo ambalo ni la maana sana" aliamuru mshenga huku akinyanyuka na kisha wote wengine nao wakanyanyuka kutoka nje kuanza safari.

    Bado Simba aliendelea kumtafuta ndugu yake Sungura kila sehemu, tayari baadhi ya ndugu zake walianza kuungana nae na kumtafuta kila sehemu, aliopo kule chuo walikwenda hadi chuoni kwao kuulizia kama amerejea huko.

    Wakaaambiwa kule bado wanachuo hawajaripoti, karibu asilimia kubwa wapo field hivyo waende wakaulizie kule anapofanya Field. Huko nako wakajibiwa alitoroka kama siku kadhaa zilizopita na hajaonekana tena, hali ilikuwa ni mbaya mno kwa Simba.

    Hakuwa na ndugu mwingine yoyote wa damu zaidi ya Sungura, waliobakia ni ndugu wa mbalimbali tu. Kila akifikiria hapo, amani ilitoweka na ujasiri ulimkimbia kabisa, kilio kikawa kikitawala. alihisi ndugu yake atakuwa amekwenda kujidhuru.Dhahiri moyoni alisema mtu wa kwanza anaebeba zigo la lawana ni Zain kwa hilo wala hakwepi. alihisi kumchukia mno.

    Mzee Komba na Mshenga wakawasili ndani ya nyumba na kukaribishwa na Mzee Mapunda ambae hakuwa akitegemea kupokea wageni wawili, alikuwa akijua anaekuja ni mtu mmoja tu.

    Hakuna alietaka kupoteza muda, kila mmoja likuwa na shauku, Mzee Mapunda alikuwa na shauku ya kutaka kulisema lile lililofanya awaite pale usiku ule na walioitwa nao walikuwa na shauku ya kutaka kujua kile kilichowafanya waitwe kwa pupa vile.

    Alianza Mzee Mapunda kwa kuwataka radhi kwa usumbufu wa wito ule wa ghafla, kisha akawa akimtazama mshenga na kumwambia kuna dharula imejitokeza kama alivyomueleza Matwiga amuambie.

    Kabla hata hajaendelea, mshenga akamwambia hata nao wamepata shaka kubwa mno kutokana na wito wa usiku ule, ndio maana wameamua kuongozana wawili, ili kusikiliza kwa umakini."Siku zote wito wa Mzee huwa una jambo, na jambo la Mzee huwa ni zito iwapo atakutwisha peke yako, ndio maana nikaamua tuje wawili ili kama ukinitwisha na likawa zito basi mwenzangu anituwe ama lah tuligawe ili tuweze kulibeba vizuri," alisema mshenga na kusababisha wote wacheke ila hakikuwa kicheko cha furaha bali ni cheko la kumfanya tu aliesema asione amedharaulika.

    Kisha Mshenga akamtambulisha Mzee komba kwa Mzee Mapunda na vivyo hivyo na Mzee Komba kwa Mzee Mapunda. Walisimama na kushikana mikono wakifurahi kufahamiana kisha wajkaketi tena.

    Kwa kituo sasa, Mzee Mapunda akawaelezea kwa kirefu toka mwanzo hadi mwisho na maamuzi ya Zainab. Walichoka kabisa, nao wakajikuta wakishindwa kuamua chochote, kutokana na kauli ya Zainab, nao wakaingia hofu.

    Baada ya tafakuri ya dakika kadhaa, Mzee Komba yeye akaomba aonane na Zainab ili waongee nae na kujaribu kumshawishi. Mzee Mapunda akmuita mkewe na kumtaka aje na Zainab kule barazani.

    Wao wakaendelea kupiga soga ili kuvuta muda. wakajitokeza mama na mwana wakiwa wameongozana, mama akiwa yupo mbele, na mwanae akiwa anamfuatia kwa nyuma. Wakiwa wameongozana hivyohivyo, wakaanza kusalimia.

    Mama Zainab akaaanza kumsalimia Mshenga huku wakitaniana, maana tayari alikuwa ni kama mwenyeji pale kutokana na kupita mle ndani mara kwa mara. Kisha akamuelekea Mzee Komba.

    Zainab alikuwa tayari amewasalimia wote na kuketi jirani na baba yake. Mama Zainab na Mzee Komba walipo kutanisha macho, kila mmoja akamshangaa mwenzie;

    "Ha! Komba..." Mama Zainab aliita huku akimsogelea Mzee Komba aliekuwa akinyanyuka

    "Mama Matwiga huyo..." Kauli ya mzee komba ikazua mshangao kwa wote waliokuwepo pale barazani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakasalimiana na kuketi wakiwa kimya kabisa hadi Mzee Mapunda alipoamua kuvunja ukimya kwa kuuliza kama wanafahamiana. Mama Zainab ndio akajibu kuwa wanafahamiana kitambo sana.

    Mshenga ambae tayari alihisi jambo, akamuuliza wanafahamiana kivipi? Mama Matwiga akasema akimtazama mumewe

    "Huyu ndio yule mzazi mwenzangu nilie kuambia awali kwamba nilifunga nae ndoa huko Zanzibar na kuachika nikiwa nimezaa nae mtoto mmoja wa kiume, niliemuacha hukohuko kwa baba yake kabla sijarudi huku nyumbani Songea."









    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog