Simulizi : Mshumaa
Sehemu Ya Tatu (3)
Rebeka alikuwa akishadadia kuona Shery akihamia hapo. Maana alijua mipango yake mingi itatimia endapo wakiishi na Shery hapo. Akashukuru kimya kimya huku akiombea Shery asije akabadili maamuzi.
* *
Siku iliyofuata. Shery alikuwa akipanga panga nguo zake huku akisaidiwa na Mkasi. Walikuwa wakipanga nguo huku wakiongea hili na lile. Yote ni kuagana maana kila mmoja alikuwa akienda sehemu yake. Nusu saa ilitosha kufanya hicho walichokuwa wakikifanya. Baada ya hapo walikaa kitandani.
“Kwahiyo wewe ndio unaondoka saa hii?” Shery alimuuliza Mkasi. Mkasi akajibu kuwa muda huo ndio amepanga kuondoka. Maana hatotaka kukaa pekeake kwenye nyumba hiyo ilhali yeye alikuwa akienda kwa baba yake mdogo. Shery akainuka pale kitandani na kuuendea mkoba wake mdogo uliokuwa juu ya meza. Akauchukua na kuufuangua. Akatoka na kibunda cha pesa. Akampelekea Mkasi na kumpatia. Mkasi akazipokea pesa zile na kuzihesabu. Zilikuwa ni shilingi laki tano. Akamtumbulia macho Shery ambae muda wote alikuwa akimuangalia yeye.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Zote hizi ni za nini?” Mkasi akahoji kwa mshangao huku akiwa bado amemtumbulia macho Shery. Shery akatabasamu na kumjibu kuwa. Achukue tu kama nauli. Nauli? Yote hii? Mkasi akajiuliza. Akaongezea kuwa. Kama alivyosema kuwa anataka kwenda kuanzisha familia. Basi akiwa tayari asisite kumjulisha ili swala zima la sherehe alisimamie yeye. Mkasi akafurahi zaidi baada ya kuona kumbe alikuwa akijaliwa sana na familia hiyo kuliko hata vile adhaniavyo yeye.
Akainuka na kwenda kumkumbatia Shery. Wakakumbatiana na kujikita wote wakitokwa na machozi. Haikujulikana ni ya furaha ama huzuni. Mwisho wakaachina na Mkasi akawa tayari kwa kuondoka. Akaenda chumbani kwake kwenda kuchukua begi lake la nguo. Sebuleni alimkuta Shery akimsubiri tayari kwa kumsindikiza. Wakatoka wote na kuingia kwenye gari. Safari ya kwenda Stendi ikaanza. Nusu saa ilitosha kuwafikisha mahala hapo na Mkasi akapanda kwenye gari linalokwenda kwao. Wakaagana vya mwisho na Shery akaondoka kurudi nyumbani.
Shery alipofika. Akajiandaa na yeye kuenda kwa Frank baba yake mdogo. Alipomaliza kila kitu. Akatoka yeye kama yeye akiwa na mabegi yake ya nguo mawili tu. Vitu vyote aliviacha. Labda vya kuongezea ni simu yake na ‘laptop’ yake. Akatoka nje na kutafuta usafiri utakaomfikisha huko anapotaka kuenda. Dakika kadhaa akawa ameshafika. Alipokelewa na Rebeka kwa furaha nyingi. Majira hayo Frank hakuwa bado amerudi kutoka kazini.
Wakakaa Sebuleni baada ya kwisha kuwa Rebeka ameshamuonyesha chumba atakachokitumia muda wote atakapokuwa hapo. Hapo wakazungumza wanayoyajua wao hadi pale majira ya saa mbili usiku yalipotimu. Frank alirudi kutoka kazini. Alifurahi sana baada ya kuona Shery amekuja kama alivyoahidi siku iliyopita. Wakaanda chakula na kula pamoja. Baada ya kumaliza kula. Walihamia sebuleni. Na hapo waliendelea na maongezi hadi pale kila mmoja alipoona ipo haja ya kwenda kujipumzisha kutokana na pia muda ulishakwisha.
* * * *
Mwezi mmoja ulipita na mambo yalianza kubadilika taratibu. Ule upendo aliokuwa akionyeshwa wakati anahamia hapo. Ulianza kupungua. Hivi sasa mateso na manyanyaso yalianza kudhihirika kwa Shery kutoka kwa mama yake mdogo, Rebeka. Mwanzo walikuwa wakishirikiana kupika chakula cha usiku, lakini hivi Rebeka alikuwa akimshinikiza kupika pekeake. Kwa madai ya kuwa. Muda wa mchana hakuwa akipika yeye na arudipo kutoka chuoni anakula tu pasi na kujua shida azipatazo wakati wa kupika.
Swala hilo lilimshangaza sana Shery. Lakini akajiambia huenda ikawa kweli mama yake mdogo anachoka kupika. Akalivaa rasmi jukumu la kupika mwenyewe usiku. Rebeka alipoona jaribio lake hilo halikuwa na mantiki. Akaongeza jengine. Ikawa kila arudipo chuo Shery. Hukuta hakuwekewa chakula. Na kila alipohoji alijibiwa kuwa. Hapawezi kupikwa chakula kingi mchana ilhali Shery majira hayo yupo chuo. Na inajulikana dhahiri muda huo atakuwa ameshakula huko huko na arudipo nyumba halafu akila tena. Utakuwa ni uroho maana amekwisha kula huko atokapo.
Alaa! Ni tangu lini mimi nikala chakula cha mchana chuoni ilhali najua nyumbani nimwekewa? Alijiuliza Shery. Akapuuza tena swala hilo ili kuepusha shari akidhani huenda ikawa mama yake mdogo amemdhania vibaya tu kuwa anakula chuoni. Na kuanzia siku hiyo akawa hali tena cha mchana nyumbani. Badala yake alikuwa akila huko huko chuoni. Labda siku za mapumziko tu ndio anakula hapo. Tena hadi iwe amepika yeye ila vinginevyo hatii mkono.
Kwa akili ya haraka haraka Shery alijua hayo ni manyanyaso yanayoanza kidogo kidogo. Ila akikumbuka mwanzo alivyopokelewa na Rebeka na walivyokuwa wakiishi. Akajiambiza kuwa huenda ikawa sio manyanyaso ila dhana mbaya tu aliyokuwa nayo mama yake mdogo. Akapuuza!.
Siku moja majira ya usiku. Rebaka akiwa amelala na Frank chumbani kwao. Rebeka alionekana kama kuna jambo anataka kumuambia Frank ila hakujua amuanze vipi. Akajipa ujasiri na kumuita Frank. Frank akamgeukia bila kuongea chochote ishara ya kuwa yupo tayari kumsikiliza anachotaka kusema. Rebeka alijikohoza kidogo na kusema.
“Mume wangu. Kwani ile nyumba aliyotoka Shery. Kwanini usiiuze tu badala ya kuipangisha na pesa zitakazo patikana tukafanya mambo ya maana” Rebeka aliongea. Frank alimtazama usoni huku akiwa amehamaika kwa ushauri huo.
“Niiuze kivipi? Na hayo mambo ya maana ni yepi tutakayo yafanya?”
“Ina maana umesahau kwamba juzi nilikuomba hela kuna shamba linauzwa huko kijijini kwetu kwahiyo ninataka kulinunua?”
“Kwani hilo shamba linauzwa kiasi gani?”
“Ni milioni moja na nusu...”
“Kwahiyo milioni moja na nusu ndio unataka tuuze nyumba? Mbona unaakili za kipumbavu wewe” Frank alimjia juu kiasi kuonyesha kuchukizwa na jambo hilo. Rebeka akajifanya amenuna. Akageukia pembeni na Frank nae akageuka pembeni. Wakawa wamepeana migongo. Muda huo Rebeka akisubiri kubembelezwa. Dakika tano zikapita. Kumi, kumi na tano hadi ishirini pakwa kimya na pasitokee jambo lile alilolitarajia. Akageuza shingo na kuona Frank akiwa amelala vile vile.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akajiinua pale kitandani na muda huu akitoa sauti za kilio. Akaliendea kabati na kutoa nguo zake. Akavuta begi na kuzipaki humo moja moja. Frank alishtushwa na sauti ya kilio cha Rebeka. Akainuka haraka na kumfuata pale alipo. Akamuuliza kwa utaratibu ni kipi kimlizacho. Rebeka akajifanya kununa zaidi mara hii hakutaka hata kuguswa na Frank. Ikabidi Frank atumie nguvu kidogo kumnyamazisha na Rebeka akatulia lakini kununa kusimuondoke.
Akamuuliza ni kipi kimlizacho hadi kupelekea kupanga nguo zake kwenye begi akitaka kuondoka. Rebeka akadai ni kule kupuuzwa wazo lake. Frank akacheka kidogo na kumuambia kumbe ni hilo tu ndilo ambalo lilikuwa likimliza. Akamuambia kuwa kama ni hiyo hela ya kununua hilo shamba atampatia lakini si kwa kuuza nyumba. Rebeka akalalamika kuwa hitaji lake si shamba tu. Hata anataka kuzikarabati nyumba za wazazi wake waliokuweko huko kijijini nyumba zao ziwe ni za kisasa. Sasa pesa za kufanya hivyo zitapatikana wapi kama si kuuza nyumba?
Frank alikuna kichwa, kisha akimuahidi mke wake kuwa swala hilo atalifanyia kazi. Rebeka akafurahi na kurudi tena kitandani. Nguo zake alizozitoa kabatini akiziacha pale pale. Wakalala huku Rebeka akiwa na furaha tele.
Siku iliyofuata. Frank alimjia taarifa mke wake kuwa. Lile swala lake la kutaka kuuza nyumba ya kina Shery lilikuwa linaenda kukamilika. Wateja wameshapatikana ikiwa ni wale wale waliopangisha nyumba ile. Kinachosubiriwa hapo ni Frank kutumia ujanja wake ambane Shery amuonyeshe hati za nyumba ile zilipo ili biashara ifanyike pasi na shaka. Rebeka alifurahi kupita maelezo na kujikuta akimkumbatia Frank kwa furaha. Frank alitabasamu baada ya kuona mke wake amefurahi kwa taarifa hiyo.
Majira ya jioni. Shery alirudi kutoka chuo. Alimkuta Rebeka akiwa amekaa sebuleni akiangalia Tamthilia iliyokuwa ikionyeshwa kwenye luninga. Shery alimsalimu mama yake mdogo kwa adabu lakini Rebeka pamoja na kuisikia salumu hiyo. Wala hakujishuhulisha kuitikia. Shery na yeye hakujali kutoitikiwa maana alishazoea ila alimsalimu kama ilivyo ada yake.
Akapotelea chumbani kwake. Huko alibadili nguo na kuingia chooni. Na baada ya muda kidogo akatoka akiwa anatiririkwa na maji mwili mwake. Bilashaka alitoka kuoga. Akabadili nguo na kuvaa nyengine. Kisha akajianda kama wajiandaavyo wanawake pindi wawapo na mtoko. Baada ya kumaliza. Alivuta pochi yake ndogo na kutoka nje. Alipofika sebuleni alimuaga Rebeka kuwa kuna pahali anaenda ila hatochelewa kurudi. Rebeka alimtazama kwa dharau huku akibenua midomo yake na kumfanya afananiane na mgonjwa wa kiharusi pindi auguapo. Akageukia pembeni na kuendelea kuikodolea macho luninga.
Shery akatoka bila kusema chochote. Akatafuta usafiri na kuelekea huko alipopanga kwenda. Alifika maeneo ya Toyota na kushuka kwenye usafiri uliomleta hapo. Akafanya malipo na jamaa akaondoka zake akimuacha Shery akivuka barabara na kwenda kuingia kwenye Restaurant iliyokuwa ikiangaliana na jengo la Toyota. Akapiga hatua kuiendea meza moja ambayo kwenye viti vyake kulikaliwa na kijana mmoja.
Yule kijana akasimama kwaajili ya kumpokea mgeni wake. Kisha akamkaribisha kwenye kiti chengine na Shery alipokaa naye akakaa. Wakasalimiana kwa bashasha na salamu ilipoisha. Pakafuata mazungumzo mengine. Wakazungumza kwa dakika kadhaa na kimya kikafuata. Hakuna ambae alimsemeza mwenzake chochote. Muda huo kila mmoja alikuwa bize na kinywaji chake.
Muda kidogo Shery alifungua kinywa cheke akimtaka mtu yule ambae alimtaja kwa jina la Suma aeleze alichomuitia hapo. Suma akatabasamu na kumuangalia binti huyo. Hakika hata macho yake yalikiri kuwa binti aliekuwa mbele yake ni mzuri. Mwenye kila sifa ya kuitwa Mrembo. Akajikohoza kidogo na kusema.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Shery, kwanza nikushukuru kwa hii nafasi ya upendeleo ulionipatia bila kujali hali yangu. Pengine unashauku ya kutaka kumaizi ni kipi hasa kilichonifanya nikakupotezea muda wako na kukutoa kule ambapo makazi yako yapo na kuja hapa ambapo ni sehemu ya kustarehesha macho na kuupa akili mpya ubongo.
Labda nikupongeze na kukupa sifa zako kwa kukuambia kuwa wewe ni mwanamke jasiri sana. Maana hukuwaza wala kuhofia ugeni niliokuwa nao kwako. Hukuwa na hofu labda nitakudhuru na vingine kama hivyo. Ila umeniamini na kuamua kunipa nafasi hii bila kujali lolote. Hahahah kwa haya, acha nikuite Malkia wa Nguvu.
Shery watambua kuwa wewe umzuri sana? Naamini unalitambua hilo kwasababu sina shaka ya kuwa mimi sio wa kwanza kukuambia hilo. Wewe umzuri sana na unang'aa mithili ya wingu lenye rangi ya dhahabu lipatikanalo kila mawio ya siku kwenye anga la muumba. Hakika uzuri wako siwezi ufananisha na chochote hata hilo wingu la dhahabu nahisi pia linauonea wivu.
Hapana. Siwezi sema ati wewe ni umzuri sana kama umejiumba mwenyewe kwasababu kila mmoja anatambua hakuna kilichojiumba chenyewe. Labda niseme muumba alitumia muda mrefu kukupamba.
Shery nayanena haya si kwaajili ya kukupa sifa tu. Bali pia ni kwaajili ya kukifurahisha kinywa changu kitamkacho maneno haya kutokana na msukumo utokao ndani ya moyo wangu.
Nikuambie kitu mpendwa. Ubongo wangu umekuwa mtumwa wa fikra zako kila niikumbukapo taswira yako. Na kila mara niwapo katika hali hiyo. Moyo wangu nao unatamani hata nichukuwe walau japo nafasi kiduchu nikuelezee maumivu yaupatayo. Aaaa hata ukiniuliza ni maumivu yepi yaupatayo moyo wangu naweza nisipate jibu sahihi kwababu si mimi niumiae.
Nashindwa kukiwakilisha kile kilichopo moyoni mwangu kutokana na hofu niliyo nayo. Hata ukiniuliza ni hofu ipi hasa iliyonipata? Pia nitashindwa kukupa jibu yakinifu kwasababu sina hali kila inaponijia taswira yako.
Samaki aliyefumba kinywa chake katu hawezi kutwekwa na ndoano ya mvuvi. Lakini hiyo ni kinyume kwangu. Kwasababu mara nyingi najaribu kufumba macho nikidhani kuwa taswira yako itanitoka fikrani. Lakini ndio kwanza uzuri wako unaniteka na kuniweka kifungoni na isijulikane ni lini nitakuwa huru.
Hakika umeniteka na sijui ni kwanini imekuwa rahisi hivyo ilhali ni siku chache tu tangu mboni zangu zilipotua kwenye taswira yako. Sijui mpaka hapa ushaelewa nini namaanisha. Lakini wewe ni mkubwa, najua ushaelewa nini namaanisha. Labda kama unataka nikutamkie waziwazi kwa kinywa changu”
Suma aliongea msururu wa maneno hayo na mwisho alimalizia kumtamkia Shery ya kuwa anampenda. Alijieleza vya kutosha kiasi ambacho Shery alikosa cha kusema. Akabaki kimya huku akitazama chini. Isijulikane kama anafikiria jibu la kumpa ama analipima ombi la kijana huyo alieonekana mtanashati sana. Akainua kichwa na kumtazama.
“Ismail. Siwezi kukujibu chochote kwa sasa. Sio kwamba sijakuelewa ama laa! Nimekuelewa ila nahitaji muda wa kufikiri hili. Now naomba niende nyumbani nitakucheki siku yoyote” Shery aliongea hayo na kuinuka bila kusubiri jibu lolote kutoka kwa kijana huyo. Akavuta mkoba wake na kupotea eneo hilo kwa mwendo wa maringo. Ebwana ee!.
Kijana Suma mate ya uchu yalimdondoka. Jicho la kuhusudu lilimkodoka kodo-kodo likimsindikiza mnyange huyo hadi pale alipopotea kwenye upeo wa macho yake. Akapepesa macho na kuachia tabasamu. Akaachia cheko dogo na kuinua glasi yenye shurubati na kupiga tafu kubwa. Akaishusha chini na kuitazama. Akasikitika huku akitabasamu.
“Walah Mungu fundi aisee!” Mmmh! Akaguna kisha akainuka pale na kupotelea kusikojulikana.
Shery majira ya saa moja jioni alikuwa akirudi nyumbani kwao. Akafungua mlango na kuzama ndani. Hali aliyokutananayo ilimshangaza sana. Nini kinaendelea? Alijiuliza. Alishuhudia sura ya Frank ikiwa imekunjana kwa hasira. Sura ambaya ilitangaza chuki za waziwazi. Akapeleka jicho lake kumtazama mama yake mdogo. Akamuona akimtazama kwa dharau na kejeli. Ghafla Frank alimuendea kwa ghadhabu hadi pale mlangoni. Kofi kali likatua shavuni mwake. Akiwa bado anatahamaki kwa anayoyaona. Alishtukia akikwidwa nguo yake enoe la shingo. Nini shida? Alijiuliza!.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unatoka wapi malaya mbovu wewe?” Frank alimuuliza kwa hasira. Natoka wapi? Shery alijiuliza huku akimtazama Baba yake kwa wasiwasi. Machozi yalikuwa yakimtoka taratibu kwenye mboni za macho yake. Pamoja na kupigwa kofi kali la shavu. Pia kuitwa malaya kumemuumiza sana. Pengine ni zaidi ya maumivu ya lile kofi. Mara hii alikuwa akilia kwa sauti ya chini na asijue amjibu nini Baba yake.
“Nakuuliza unatoka wapi unanitolea machozi. Umeambiwa na nani kwamba mimi nataka kuona machozi yako. Nenda kawaonyeshe hao hao makahaba wenzako. Nijibu swali langu” Frank aliendelea kufoka huku akiwa bado amemkwida Shery.
Muda wote huo alikuwa bado akiendelea kulia. Frank alipoona Shery anamlilia tu pasi na kumjibu. Akamvuta kwa nguvu mbele na Shery akaenda kujibwaga sakafuni. Frank aliuchomoa mkanda wake uliokuwa umefungwa kiunoni. Kichapo kikaanzia hapo. Adhabu ya kosa ambalo hakulijua mpaka muda huo ikaanzia hapo.
Frank alimchapa mithili ya punda achapwaye na bwana wake asie na huruma juu yake. Shery alilia kwa uchungu kiasi ambacho mpaka akashindwa kufungua kinywa chake kuongea chochote. Maumivu ya kuitwa malaya na kahaba ndio yaliyotawala nafsini kwake kuliko hata yale ya mkanda anao adhibiwa nao. Tangu lini akawa kahaba ilhali hata mwanaume hamjui? Ili muumiza!.
Tangu uzazi wake mpaka kumiliki miongo hiyo aliyonayo sasa. Hakuwahi kupigwa kiasi hicho na wazazi wake sembuse kutukanwa tu. Machozi meupe yanayotiririka kwenye mboni zake, yalidhihirisha uchungu alionao moyoni kwake. Frank alimchapa mpaka akahisi sasa huko anapoelekea anaweza kumjeruhi pakubwa. Akaacha kumpa adhabu na kilichofuata hapo ni kumtukana huku akitweta kwa hasira.
“Tokaa mbele ya macho yangu malaya wewe usije ukanipa kesi ya kuua bure” Frank alimfokea huku akimtazama kwa jicho kali. Jicho ambalo lilitangaza hasira alizonazo. Shery alijiinua kutoka pale chini na kuanza kupiga hatua kuingia chumbani kwake huku akijikokota mdogo mdogo kutokana na maumivu ya mwili aliyonayo.
Aliingia chumbani kwake na kuufunga mlango wake taratibu. Kisha akauegamia na kushuka nao chini taratibu huku machozi yakipamba kilio chake. Alilia sana huku akiwataja wazazi wake. Alinung'unika kiasi ambacho alikuwa akikufuru sana. Sasa ni nani wakusikiliza kilio chake kama si yeye na mungu wake? Alikaa sehemu ile kwa muda mrefu mpaka usingizi ukampitia pale pale kutokana na uchovu uliyouvaa mwili wake ghafla.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata. Shery hakuweza kwenda chuo. Achilia mbali maumivu yaliyotawala kwenye mwili wake. Hata majeraha aliyonayo yalimsababishia kutokwenda chuo siku hiyo. Akabaki ndani chumbani kwake. Muda huu kilio kilikata lakini uchungu haukukoma. Alisha maizi muasisi wa kesi isiyojulikana hadi kupelekea kupokea kipigo namna ile ni Rebeka mama yake mdogo. Alimjua fika Baba yake mdogo hakuwa na ujasiri wa kumpiga namna ile. Sasa ni kisa ama kosa lipi aliloambiwa na mkewe kuwa yeye amelitenda mpaka kumpiga kiasi kile?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment