Simulizi : Kwenye Siku Yangu Ya Kuzaliwa
Sehemu Ya Nne (4)
Baada ya kuwa amegida mafunda kadhaa ya konyagi, mafunda ambayo yalitosha kuanza kuirubuni akili yake, taratibu Cosmas alianza kusahau magumu yanayomsibu. Alishau kuwa; mchana au muda mfupi uliopita alikuwa akikabiliwa na mawazo juu ya mapenzi yake kwa Wayeka, mwanamke ambaye hajui kama duniani kuna mtu anayeitwa Cosmas na Cosmas huyo anampenda kupindukia.
Kuna wakati mawazo hayo yalimrudia na kujikuta anaropoka, “Ni uchizi huu, kumfikiria mtu asiyekufikiria, tena mbaya zaidi hajui kama kuna kiumbe kama wewe duniani…ni uchizi,” alijisemea Cosmas.
Kwa kuwa Stella hakuwa mbali na meza aliyokuwa amekaa Cosmas, maneno aliyoyasema Cosmas yalimfikia barabara kwa sababu spika za redio ya pale bar walipokuwa zilitoa sauti hafifu. Maneno hayo yalimchanganya mno Stella na kumfanya ahisi kuwa labda maneno yale yalielekezwa kwake. Alijikaza kisabuni na kuongeza umakini kwenye windo lake ili kuondoa fikra potofu ambazo zilianza kumzengea.
“Ana mambo yake yanayomchanganya huyu… si mimi,” Stella aliwaza huku akiinua chupa ya maji iliyokuwa mezani kwake na kupiga mafunda kadhaa.
Pombe ilizidi kumkolea Cosmas na kusababisha aanze kuwatazama wahudumu wa pale Bar kwa jicho la matamanio. Kila mhudumu alionekana mrembo mbele ya macho Cosmas.
Kuna mhudumu alipita mbele yake na kuuteka umakini wake, mhudumu yule ambaye alikuwa ndani ya sketi fupi iliyoacha sehemu ya mapaja yake wazi, alisindikizwa na macho ya Cosmas kuelekea kule ilikokuwa meza aliyokaa Stella.
Mara macho ya Cosmas yakaachana na yule mhudumu na kutua kwa Stella. Alipomuona tu, alimpa alama zote na kukiri kuwa huyo ndiye mrembo kuliko wote. Akampa Mungu heko yake kwa kazi nzuri ya uumbaji. Aliyafikicha macho yake ili aweze kumuona vizuri mrembo yule. Alipotupa tena macho kwenye ile meza kwa mara nyingine, Cosmas hakuyaamini macho yake, meza ilikuwa tupu na hakukua na mtu wala kitu juu yake!
Cosmas alitulia na kufikiri huku akiwa haaminiamini, alihisi labda amezidiwa na pombe, “Haiwezekani, nimeona mtu hapo sasa hivi, iweje asiwepo tena? Au ni jini? Hapana nimeshalewa,” aliwaza Cosmas kabla hajamuita mhudumu na kulipa bili yake halafu akaondoka ili akapumzike.
****
Siku iliyofuata, asubuhi na mapema, Stella alikuwa mita chache kutoka ilipo nyumba ya Cosmas. Alikaa pale kwa muda mrefu akimsubiri Cosma atoke ndani. Muda mfupi baadaye Cosmas alitoka tayari kwa kuelekea kwenye shughuli zake za kila siku.
Stella alimtanguliza kwa hatua kadhaa, kisha akaanza kumfuata kwa nyuma, na kwa tahadhali ili asiweze kutiliwa shaka na mtu yeyote.
Cosmas hakupita mahali popote, alikwenda moja kwa moja mpaka dukani kwake ambako aliwakuta baadhi ya wateja wakimsubiri. Alisalimiana nao, kisha akafungua mlango kwa ajili ya kuwahudumia mmoja baada ya mwingine mpaka walipokwisha.
Yote aliyokuwa akiyafanya Cosmas, yalifanyika sanjari na mawazo yaliyokuwa yakiisonga akili yake. Mawazo juu ya nani atakayekuwa mke wake yalizidi kuitesa akili yake. Cosmas alikuwa akiwaza huku akili yake ikiwachambua wasichana aliowahi kutembea nao ili ikibidi amfanye mmoja kati yao kuwa mke ambaye atamlindia heshima yake mbele ya jamii.
Aliwachambua mmoja baada ya mwingine kwa kuangalia madhaifu ya kila mmoja na uimara wake.
Miongoni mwa waliokuwa wakifanyiwa uchambuzi kwenye akili ya Cosmas alikuwemo Stella, ambaye alichambuliwa kwa kila kigezo cha upimaji alichokitumia Cosmas. Katika uchambuzi wake ni Stella tu ndiye aliyeonekana angalau kukaribia vigezo alivyovizingatia. Cosmas aliweka tiki akilini mwake kuwa baada yakumkosa Wayeka sasa nafasi anaitoa kwa Stella.
Swali pekee lililoitesa akili ya Cosmas ni wapi pa kumpata Stella. Cosmas alishindwa kabisa kujua ni wapi atampata msichana huyo ili amuombe msamaha na kumueleza nia yake ya kutaka kumuoa.
Cosmas hakuishughulisha kabisa akili yake kuwaza juu ya mwonekano ambao angeweza kuwa nao Stella, aliamini Stella ni mwanamke mzuri wa umbo na sura endapo tu, atapata matunzo mazuri. Na kwa nafasi yake kiuchumi Cosmas hakuona kitakachoweza kumshinda katika matunzo ya mke. Kama ni pesa, tayari anayo ya kutosha. Nyumba ya kuishi tayari anayo. Ni kipi kilisalia? Hakuna kilichosalia isipokuwa kupatikana kwa huyo mke ambaye ni Stella.
Wazo la kwenda Nyabange, ambako ndiko nyumbani kwao na Stella lilimjia akilini. Alijipa uhakika kuwa hatopotea mahali ilipo nyumba ya akina Stella kwa sababu ameshawahi kwenda mara kadhaa alipokuwa akimtorosha Stella.
Taswira ya Stella akilia baada ya yeye kuwa amemfukuza ilimrudia Cosmas akilini na kumpa wakati mgumu. Alijilaumu kwa kitendo hicho cha kikatili kisichokuwa na hata chembe ya utu. Kuna wakati alikwenda mbali na kufikiri kuwa; yawezekana mateso yote anayoyapata kwenye mapenzi ni laana kutoka kwa Stella. Cosmas akaijutia nafsi yake na kuapa kumtafuta Stella kwa gharama yoyote ili ajitakase kwa kumuoa.
Wakati akifikiria hayo, wazo jingine ambalo lilikuwa ni la kumkatisha tamaa na kumvunja kabisa moyo lilimjia, “Itakuwaje kama atakuwa ameshakufa au kuolewa?” Cosmas aliwaza.
Wazo hilo lilimvuruga kabisa Cosmas na kumchanganya akili, lakini alijikaza na kujipa moyo kuwa ni lazima Stella atakuwa hai na bado hajaolewa. Siku iliyoyoma Cosmas akiwa mawazoni, na muda wa kufunga biashara ulipofika Cosmas alifunga duka lake na kuelekea nyumbani.
Wakati ambao Cosmas alikuwa dukani Stella hakuwa mbali na duka hilo ambalo ni mali ya Cosmas. Hakuganda sehemu moja, kuna wakati aliondoka na kwenda mahali pengine kwa ajili ya kupitisha muda na baadaye alirudi kwa ajili ya kulinda windo lake.
Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya tatu tangu Stella awasili mjini Bunda kwa ajili ya kutimiza azma yake ya kulipa kisasi. Siku hiyo kama ilivyokuwa kwa siku nyingine, Cosmas aliamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli zake kama ilivyo ada. Jioni ilipofika hakusita kuhitimisha shughuli za siku kwa kufunga mlango wa duka lake.
Tofauti na siku nyingine, siku hii Cosmas hakwenda moja kwa moja nyumbani na badala yake alianzia Baani ambako alikwenda kwa lengo la kuyakata maji ili apunguze mawazo yanayomkabili pamoja na kupanga mikakati ili akamuone Stella na kama atamkuta basi amweleze yote atakayoona yanafaa kumueleza ikiwemo nia yake ya kumuoa.
Baa aliyokwenda Cosmas ni ileile aliyozoea kwenda, baa iliyofahamika kwa jina la Tiger Toga.
Akiwa anaendelea kuiteketeza chupa ya pili ya bia yake tangu alipofika, Cosmas alishuhudia chupa nyingine mbili za aina ileile ya bia aliyokuwa akinywa zikiletwa na mhudumu, “Nimeagizwa nikuletee hizi bia, amekununulia yule dada ambaye amekaa pa…” ilikuwa ni sauti ya muhudumu aliyekuwa akijaribu kutoa ufafanuzi kuhusiana na ile ofa bia kwa Cosmas. Wakati anamuonesha Cosmas dada aliyemwagizia bia, yule mhudumu alishangaa kuiona ile meza iliyokuwa imekaliwa na yule dada aliyemwagiza ikiwa tupu!
“Alikuwa pale sasa hivi,” alizidi kusema yule mhudumu kwa mshangao.
“Dada yupi?” Cosmas aliuliza.
“Kuna mdada alikuwa kwenye ile meza… labda ameenda msalani,”
****
“Usizifungue mpaka aje,” Cosmas alishauri na yule mhudumu akaafikiana naye, “Sawa,”
Wakati ambao mazungumzo baina ya Cosmas na mhudumu yanaendelea, yule dada aliyedaiwa kumuagizia Cosmas bia alifika mpaka kwenye meza aliyokaa Cosmas na kuvuta kiti kilichokuwa pembeni akakaa.
Macho ya Cosmas yalimpokea yule mdada kwa namna ya pekee, kama asiyeamini kile anachokiona, mara sauti ilimtoka Cosmas, “Stella!”
****
Katika kuyafuatilia maisha ya Cosmas kabla hajatimiza lengo lake, Stella alifanikiwa kugundua kuwa; Cosmas ni mwenye mawazo mengi, mawazo ambayo kwa namna moja ama nyingine yalimuweka Cosmas kwenye wakati mgumu. Awali hakujua mawazo hayo yalisababishwa na nini kwa sababu; kuna wakati alihisi kuwa ni mawazo yanayohusiana na biashara zake baada ya kuwa zimemwendea kombo. Lakini alipofanya uchunguzi wa kiudadisi aligundua kuwa mawazo ya Cosmas hayahusiani na biashara bali kuna jambo linamchanganya.
Tangu awepo Bunda, Stella hakuwahi kumuona Cosmas akiwa karibu na mwanamke yeyote katika dalili ambazo zingeashiria mapenzi. Si nyumbani wala pale dukani kwake. Hilo ndilo jambo lililomfanya Stella kubadiri hisia zake juu ya jambo linalompa Cosmas wakati mgumu kutoka kwenye biashara hadi kwenye mapenzi. Stella alihisi kuwa mapenzi ndiyo yanayomchanganya Cosmas, Moyoni alijiaminisha kuwa ni upweke wa kimapenzi ndiyo unaompa shida Cosmas.
“Yawezekana ameachwa na mpenzi wake na sasa anajaribu kujisahaulisha.” Stella aliwaza.
Wazo kuwa Cosmas alikuwa na mwanamke liliibua hisia mpya moyoni kwa Stella, hisia za wivu! Hisia hizo za wivu ndizo zilizomfanya Stella adhani kuwa yeye ndiye anayestahili kuwa na Cosmas na si mwanamke mwingine. Taswira ya kuwa yuko na Cosmas wakiyafurahia maisha zikaitwaa akili yake na kumfanya kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili Stella ahisi kumpenda tena Cosmas katika siku aliyopanga kulipa kisasi.
Alijitahidi kuzipinga hisia hizo kwa kulazimisha akili yake iendelee kufikiria juu ya kisasi alichopanga kulipiza kwa Cosmas.
Katika siku hiyo ya tatu, Stella alifika kwenye Bar ya Tiger Toga dakika tatu baada ya Cosmas. Alifika akakaa kwenye meza ambayo haikuwa jirani, ila ambayo ilimruhusu kufuatilia kila kitu ambacho Cosmas alikifanya.
Wakati Cosmas anakunywa kileo, Stella alikuwa anakunywa maji. Aliamua kunywa maji kwa lengo la kutoichanganya akili yake ili aweze kuyafanya yaliyomleta Bunda. Kwa sababu ilikuwa ni siku ya tatu tangu awepo Bunda, siku ambayo alipanga kuikamilisha kazi yake, Stella aliamua kujiweka karibu na windo lake ili iwe rahisi kwake kuifanya kazi yake. Akaamua kujisogeza kwa Cosmas kwa kuanza kumpa ofa ya bia.
Wakati ambao Cosmas alikuwa akihoji ni wapi zilikotoka bia, ndipo Stella akatokea mbele yake.
“Bee Cosmas” Stella aliitika baada ya kuwa Cosmas ameita jina lake.
Kama asiyeamini, Cosmas alipagawa na kusimama ghafla akamkumbatia Stella kimahaba na Stella naye akampokea.
Licha ya kutoa ushirikiano wa kinafiki, polepole Stella alianza kuhisi mguso wa upendo aliouonesha Cosmas katika hali ile ya kukumbatiana. Nyuso zao zilikaribiana na hatimaye papi za midomo yao zikakutana, wakaanza kunyonyana ndimi.
Stella alihisi kupata raha ya ajabu, raha ambayo aliikosa kwa muda mrefu kutoka kwa mwanaume aliyemvunja moyo wake na kumsababishia matatizo yaliyomvurugia maisha.
Waliachana baada ya dakika mbili, wakatazamana kimya katika namna ya kutoamini huku Stella akikumbukia raha aliyoipata muda mfupi uliopita wakati wakibusiana midomo
“Cosmas,” hatimaye Stella aliuvunja ukimya kwa kulitaja tena jiana la Cosmas.
Kabla Cosmas hajaitika Stella alimrukia tena Cosmas, wakakumbatiana na kulirudia tena lile tendo la kubusiana. Midomo yao ilipoachana Cosmas ndiye aliyeanza kuzungumza, “Umekuja katika wakati muafaka Stella, wakati ambao nakuhitaji kuliko pumzi,”
Yule mhudumu aliyekuwa pembeni yao alikuwa ameduwaa muda wote akiwashangaa wateja wake, mara alisikia akiitwa na wateja wengine akaondoka.
“Unadiriki kusema nini Cosmas? Baada ya kunifukuza kama mbwa leo unasema unanihitaji kwa lipi Cosmas kwa lipi..?” alilalama Stella.
Maneno ya Stella yaliuchoma moyo wa Cosmas, hatia ikajiunda ndani yake. Moyoni alikiri kuyafanya aliyosema Stella na akaamua kuitumia nafasi hii ambayo kwake ilionekana ni nafasi ya dhahabu kujisahihisha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tukae mpenzi,” Cosmas alimrai Stella naye akatii.
Ukimya wa dakika kadhaa ulitawala kati yao na baadaye Cosmas aliuvunja kwa kusema, “Nitakuwa mdhambi endapo nitakana kuwa sikukukosea wakati ule. Nakiri wazi kuwa nilikukosea Stella.” Cosmas alisita kidogo, akatazama kushoto na kulia kwa lengo la kumaizi kama kuna mtu anayewasikia.
Alipojiridhisha kuwa hakukuwa na mtu kwenye meza za jirani Cosmas aliendelea, “Yaliyopita si ndwele mpenzi tugange yajayo,”
“Ishia hapo Cosmas… unajua ni kwa jinsi gani uliuvunja moyo wangu?” alisema Stella huku akiwa ameunyoosha mkono wake kama trafiki anayejaribu kuzuia gari lililo katika mwendo.
“Naahidi kukuponya majeraha ya moyo wako Stella..” Cosmas alisema huku akisogeza kiti chake karibu na pale kilipo cha Stella.
Kumbukumbu za nyuma wakati anafukuzwa na Cosmas zilimjia Stella akilini, maumivu ya moyo yakamvaa sambamba na mahitaji ya penzi la Cosmas kwa mara nyingine. Machozi yaliyokuwa yakimlengalenga sasa yalitoka hadharani na kushuhudiwa na Cosmas ambaye alitoa kitambaa mfukoni na kuanza kumfuta.
“Uliniumiza Cosmas… uliniumiza.” Stella alizidi kulalamika kwa sauti ya kwikwi iliyosababishwa na kilio.
Sauti ya Stella akiwa analia iliuchoma moyo wa Cosmas na kumsababishia majuto ambayo sasa yalidhihirika kwa sababu ya machozi yaliyoanza kuonekana machoni pake. Majuto hayo yaliyosababisha maumivu makali moyoni kwa Cosmas yalimfanya Cosmas ajione mwenye hatia, “Naelewa Stella.. naelewa kuwa nilikuumiza sana, naomba unisamehe na unipe nafasi nyingine niyamalize maumivu yako.” Alisema Cosmas katika hali ya kumaanisha kile alichokisema.
Niliwahi kusikia, kama si kusoma mahala kuwa; mapenzi yana nguvu kuliko kifo. Hili lilijidhihirisha pale Stella alipoamua kuondokana na dhamira aliyokuwa nayo, dhamira ya kulipa kisasi kwa kumsamehe Cosmas. Moyoni alijiapiza kuwa huo msamaha ni wa dhati na hatodiriki tena kufikiria kisasi dhidi ya Cosmas. Yote yaliyowahi kutokea baina yao alimuachia Mungu na kufungua moyo wake kwa mara nyingine kwa ajili ya penzi la Cosmas.
Kwa kutambua eneo walimokuwa, eneo ambalo lina mkusanyiko wa watu ambao hufika hapo kwa ajili ya kupata vinywaji kama ilivyokuwa kwake, Cosmas alimsihi Stella waende nyumbani ili wakayamalizie mazungumzo yao badala ya kuendelea kuwepo pale Bar.
Bila hiyana Stella alitii, wote wakaondoka kuelekea nyumbani kwa Cosmas.
9
SIKU iliyokuwa ikisubiriwa na wengi, siku ambayo miaka ishirini na nane iliyopita katika siku kama hiyo Kiti alizaliwa. Siku hiyo haikusubiriwa tu kwa ajili ya kuazimisha siku aliyozaliwa Kiti, bali siku hiyo ilisubiriwa kwa hamu kwa sababu ni siku ambayo penzi la Kiti na Wayeka lingeingia katika hatua mpya ambayo ni muhimu katika mfululizo wa hatua za kuelekea ndoa yao.
Kwa sababu ya umuhimu wa tukio lenyewe, tukio ambalo lingezidi kufungua njia kuelekea katika hatua takatifu, hatua ya watu wawili kuungana na kuwa mwili mmoja kama maandiko matakatifu yasemavyo, mzee Ngomanzito aliamua tukio la Kiti kumvisha pete Wayeka lifanyikie nyumbani.
Eneo la wazi lililokuwa nyumbani kwa mzee Ngomanzito liliandaliwa mahsusi kwa ajili ya shughuli hiyo kwa kadri ilivyotakikana. Mapambo kadha wa kadha ya kuvutia yaliunakshi ukumbi uliokuwa nyumbani kwa mzee Ngomanzito na kuufanya uvutie.
Ukiachana na maandishi yaliyokuwa nyuma ya meza kuu, meza ambayo iliandaliwa mahsusi kwa ajili ya wapendanao, yaani Kitiheka na Wayeka, maandishi ambayo yaliandikwa; ‘Happy Birthday Kitiheka’ pia kulikuwa na maandishi mengine yaliyosomeka; ‘Kila la Kheri Kitiheka’
Sherehe rasmi ilipangwa kuanza majira ya saa kumi jioni, muda ambao wageni wote waalikwa walitarajiwa kuwa wamefika. Hivyo, ilipofika majira ya saa 9 Alasiri, wageni walianza kumiminika ukumbini kwa ajili ya sherehe. Wageni waliofika walielekezwa mahali pa kukaa ambapo walikaa na kupatiwa huduma ya vinywaji ili waendelee kusuuza nyoyo zao. Huku muziki laini ukiendelea kutumbuiza na kukuna nyoyo za wageni waalikwa ambao waliitikia kwa kuchezesha miguu yao na wengine vichwa vyao. Kuna waliooenda mbali zaidi na kuamua kusimama na kucheza vibao ambavyo kwa namna moja au nyingine viliwakuna.
Miongoni mwa wageni waliokuwa kwenye sherehe hiyo ni Boniphace Mayunga na mkewe, Emmy Schzilakta, ambao walifurahishwa na hatua waliyofikia marafiki zao, hatua ambayo ni hatua ya juu katika mapenzi. Hivyo uwepo wao mahali pale ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaunga mkono Kiti na Wayeka na kuwatia moyo katika safari yao ya kuelekea ndoa.
Wageni wengine walikuwa ni marafiki wa mzee Ngomanzito na mama Matobera, ndugu, pamoja na jamaa ambo ni mashahidi katika tukio hilo muhimu na adhimu katika maisha.
****
Saa ya mkononi ya Kiti ilionesha kuwa ni saa 7:10 mchana. Wakati ambao alikuwa chumbani mwake akiikodolea macho kalenda iliyokuwa ukutani huku kidole chake cha pili kutoka kilipo kidole gumba cha mkono wa kulia kikiwa kimegusa ilipo tarehe 10 ya mwezi wa nne, ambayo ilikuwa imezungushiwa wino wa kalamu kuashiria kuwa ilikuwa ni siku yenye tukio maalumu. Tarehe hiyo ndiyo tarehe ambayo miaka kadhaa iliyopita Kiti alizaliwa.
Kiti alikuwa ni kama vile asiyeamini, tarehe aliyoisubiri kwa muda mrefu, tarehe ambayo yeye na Wayeka walipanga kuvishana pete ya uchumba, hatimaye ilikuwa imefika.
“On my birthday!” sauti ilimtoka Kiti alipokuwa akiondoka pale ukutani ilipo kalenda. Alienda moja kwa moja mpaka kitandani akakaa, akaichukua simu yake kutoka kwenye mfuko wa suruali aliyovaa, akaenda mpaka kwenye eneo la ujumbe mfupi wa maandishi akaandika, “Hakuna kitakachonizuia kukupenda, nitakupenda daima kwa sababu moyo wangu umekuchagua Wayeka.” Alipomaliza kuandika, Kiti aliuruhusu ujumbe ule mfupi ukaenda, na punde akajulishwa kuwa umepokelewa.
Haukupita muda mrefu mlio ulioashiria kuwa kuna ujumbe mfupi umeingia kwenye simu yake ulisikika, akaufungua. Kilichoandikwa kilimfanya Kiti achanue tabasamu sambamba na machozi ya furaha ambayo hakuweza kuyazuia. Alikutana na ujumbe uliosomeka; “Siwezi kueleza ni jinsi gani ninafuraha kuwa nawe mpenzi, hata kama itanilazimu kusafiri jangwani kwa miaka kwa ajili yako, nitasafiri… sitakuwa na budi ilimradi tu niwe nawe mpenzi.”
Kamchezo hako ka kuchombezana kwa jumbe fupi za maandishi hakakuishia hapo, Kiti aliandika ujumbe mwingine uliosomeka hivi; “Leo ni siku yangu ya kuzaliwa, tangu nikiwa mtoto nilifahamu hivyo. Lakini siku hii inaongezewa dhima nyingine maishani mwangu baada ya ile ya kwanza, leo ni siku ambayo muda mfupi ujao nitakuvisha pete ya uchumba.”
Mbali na jumbe kutoka kwa Wayeka, Kiti pia alipokea jumbe kutoka kwa marafiki zake ambao walimpongeza kwa kuzaliwa katika siku hiyo.
Muda uliyoyoma kuelekea kwenye ile saa ambayo ilipangwa kuwa ndiyo muda ambao sherehe ilipangwa kuanza rasmi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilipofika saa 9:05, Kiti alichukua simu kwa ajili ya kufanya mawasiliano ya sauti. Alibonyeza namba ya Wayeka na kuiweka simu yake sikioni. Mlio wa kuashiria kuwa simu ya Wayeka inaita ulisikika kupitia spika ya simu yake. Simu ya wayeka iliita na hatimaye ikakata bila kupokelewa!
Hiyo haikumpa shida Kiti, kwa sababu ya kuwa na dhana ambazo alihisi zinaweza kuwa ni majibu. Dhana ya kwanza, Kiti alihisi kuwa yawezekana Wayeka akawa kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya sherehe yao, hivyo ameiacha simu ili amalize kwanza mandalizi halafu atampigia.
Dhana ya pili aliyokuwa nayo Kiti ni; alihisi labda Wayeka alkuwa amekumbatia usukani anaendesha ndiyo maana ameamua kuiacha simu hiyo ili kuepuka kusababisha ajali. Dhana hizo zilimfanya Kiti kuamua kuvuta subira kwa muda kabla hajapiga tena simu kwa mara nyingine.
Dakika tano zilikwisha bila Kiti kupokea simu wala ujumbe wa sauti, hali iliyomsukuma kufanya zoezi lile la kupiga simu kwa mara nyingine. Alipopiga kwa mara ya pili, simu ya Wayeka haikupatikana!
Safari hii Kiti hakuwa na majibu aliyokuwa nayo awali, safari hii Kiti alijiaminisha kuwa, yawezekana Wayeka bado yuko barabarani anaendesha, na yuko kwenye eneo ambalo halina mtandao wa mawasiliano kwa sababu; kuna baadhi ya maeneo ambayo yako katikati ya Nyamuswa na Bunda hayana mawasiliano ya simu. Hili nalo lilimsukuma Kiti katika wasaa mwingine wa subira, ambapo aliamua kusubiri kwa dakika tano nyingine.
Dakika tano hazikukawia kwisha, Kiti alipiga tena simu na safari hii majibu hayakupishana na yale ya muda mfupi uliopita. Simu ya Wayeka ilikuwa haijapatikana! Hali ya kutopatikana kwa simu ya Wayeka ilianza kumpa Kiti wasiwasi ambao ulisababisha kukosekana kwa utulivu moyoni mwake.
Alijaribu tena kuipiga simu ya Wayeka lakini jibu lilikuwa ni lilelile na wasiwasi ukazidi kumwelemea. Wazo kuwa Wayeka amepatwa na tatizo njiani lilimjia Kiti. Aliwaza kuwa, yawezekana Wayeka ameharibikiwa na gari, au kapatwa na ajali ambayo imesababisha mawasiliano yake kutopatikana. Moyoni mwake alimuomba Mungu amuepushe mpenzi wake na jambo lolote baya ili afike salama wakamilishe shughuli ambayo wameisubiri kwa muda mrefu, shughuli ya kuvishana pete ya uchumba.
Muda ulizidi kutokomea bila simu ya Wayeka kupatikana, wasiwasi ulizidi kumtwaa Kiti na kumsababisha achungulie nje kwenye eneo ambalo liliandaliwa maalumu kwa ajili ya shughuli ile muhimu iliyotarajiwa kupevusha safari yao ya kuelekea ndoa.
****
Alipochungulia nje kupitia dirishani, Kiti aliweza kuwaona watu ambao aliwaalika na wale ambao walialikwa na wazazi wake ili wafike kushuhudia tukio lake la kumvisha Wayeka pete kwenye siku yake ya kuzaliwa. Watu waliokuwa ukumbini walikuwa wakiburudishwa na muziki laini uliozikonga nyoyo zao sanjari na vinywaji ambavyo walikuwa wakinywa kila mmoja kwa aina yake na kwa chaguo lake.
Zilikuwa zimebaki dakika kumi natano tu, ili muda ambao sherehe ilipangwa kuanza utimie. Kiti alishangazwa na hali aliyoishuhudia ukumbini. Hakukuwa na na rafiki wala ndugu wa wayeka, watu ambao alidokezwa na Wayeka kuwa ni lazima wawepo ili wawe mashuhuda katika tukio lile.
Hali ya kutokuwepo kwa watu ambao Kiti alitarajia kuwaona kama alivyodokezwa na Wayeka kuwa ni lazima wawepo kwenye tukio hilo ilimchanganya Kiti na kuanza kuhisi kuwa labda Wayeka ameishia mitini. Wazo kuwa kuwa ameachwa solemba liliitawala akili ya Kiti na kusababisha nguvu zianze kumwishia mwilini. Kiti akakaa chini huku akijaribu kufanya mawasiliano kwa mara nyingine. Mara hii pia Kiti alikutana na majibu yaliyozidi kuichosha akili yake, “Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa… tafadhali jaribu tena baadaye,”
Jibu hilo lilimuweka Kiti njia panda na kusababisha kuibuka kwa fikra mpya akilini mwake, “Au anataka kunisuprise?” Kiti aliwaza.
“Lakini suprize gani hii? Oow noo… hapana!”
****
Ilikuwa ni bia ya pili kwa mzee Ngomanzito, bia aliyokuwa anainywa taratibu ili kuvuta muda wakati akisubiri kuanza kwa sherehe. Alipoitazama saa yake, ilimuonesha kuwa zimesalia dakika tano tu ili kutimia kwa muda ambao ulikuwa ukisubiriwa. Mzee Ngomanzito alimuita mkewe ndani ili wazungumze juu ya wasiwasi alionao wa kuchelewa kwa watu waliokuwa wakiwasubiri.
“Kiti yuko wapi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yuko ndani,” Matobera ambaye ni mama yake na Kiti alijibu.
Mzee Ngomanzito alifikiri kidogo kabla ya kusema, akawageukia wageni wake pale ukumbini, aliwaona wakiendelea kupata vinywaji vyao huku wakipiga soga za hapa na pale.
“Nahisi kuna dalili mbaya.. muda unaelekea na hakuna mgeni hata mmoja wa uapande wa wenzetu. Tufanyeje?” mzee Ngomanzito aliuliza.
“Yawezekana kuna tatizo,”
“Sasa mbona hatufahamishwi?”
“Hilo ni swali ambalo hata mimi najiuliza. Nadhani unapaswa kuzungumza na mwanao kujua kama ana taarifa mpya,” Matobera alisema.
“Ni kweli usemayo. Hivi itakuwa ni aibu gani hii endapo mambo yatakwenda ndivyo sivyo?” mzee Ngomanzito alisema huku akiwatazama wageni wao ukumbini, ambao nao macho yao yalikuwa yakitupwa kwenye saa zao.
****
Ilishatimu saa 10:20, yaani dakika ishirini baada ya muda ambao sherehe ilipangwa kuanza. Wazo la kuwa ameachwa solemba lilimkaa sawia Kiti na kumsababishia maumivu makali moyoni. Maumivu yaliyompa wakati mgumu, maumivu ambayo yasingeweza kupoa kwa ganzi au kujikuna pale panapouma, moyoni.
Kiti hakuelewa ni kwa nini Wayeka amfanyie hivyo, tena kwenye siku yake ya kuzaliwa. Mwanamke aliyempenda kwa moyo wake wote, mwanamke ambaye alitarajia kumvisha pete kwenye siku yake ya kuzaliwa, ameamua kumuacha katika siku ambayo ina umuhimu mkubwa kwenye maisha yake.
“Haiwezekani.. haiwezekani Wayeka, huwezi kunifanyia hivi!” Kiti alilalama kwa sauti ilihali akiwa peke yake chumbani. Kwa Kiti huo ulikuwa ni usaliti ambao hakuutarajia. Furaha aliyokuwa akiipata kwa kuwa na Wayeka sasa ikiyeyuka ghafla kama plastiki kwenye moto mkali.
Maisha yakageuka machungu tangu wakati huo, akaiona dunia ni chungu na mahali pasipostahili kukaliwa kabisa na kiumbe kama yeye. Kwake maisha yakakosa maana na hamu ya kuishi hakuiona. Alijiinua ghafla kutoka pale chini alipokuwa amekaa, akaenda mpaka kwenye kabati lililokuwa mule chumbani akalifungua na kuchukua bastola ndogo aina ya revolva, akaifungua kwenye eneo ambalo risasi hukaa kusubiri amri ya mpigaji, akaziona zikiwa zimesheni barabara kwenye eneo lake.
****
Pirikapirika za uokoaji zilikuwa zikiendelea katika eneo la barabara inayoziunganisha barabara ya Mwanza hadi Musoma na ile itokayo Nyamuswa. Magari mawili yalikuwa nyang’anyang’a. Yalikuwa ni magari madogo ambayo kwa mujibu wa wa vibao vya namba za usajiri, magari yale yalikuwa ni kwa ajili ya matumizi binafsi.
Gari la kwanza lilikuwa ni Toyota Rav 4, jeusi, lenye milango mitatu, na jingine lilikuwa ni Toyota, Chaser jeupe.
Hakuna aliyeamini kama wahanga wa ajali hiyo watatoka wakiwa hai. Mungu mkubwa! Dereva kwenye gari jeupe alikuwa bado anapumua licha ya kuumia vibaya kichwani na kwenye mguu wake wa kushoto. Ni yeye pekee ndiye aliyekuwa kwenye gari hilo. Kwenye gari jingine, lile lenye rangi nyeusi, mlikuwa na watu wawili, mmoja mwanamke na mwingine mwanume. Mwanamke hakuwa hai tena na yule mwanaume aliyekuwa dereva wa gari hilo alikuwa hai lakini hali yake ilikuwa ni ya kukatisha tama kwa sbabu ya kuumia vibaya kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.
Majeruhi walikimbizwa hospitalini kwa msaada wa gari la msamalia mwema ambaye naye alikuwa ni miongoni mwa waokoaji waliojitokeza. Mwili wa marehemu ulipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali teule ya wilaya ya Bunda kusubiri taratibu zitakazofuata.
Siku moja kabla ya ajali hiyo kutokea, Cosmas na Stella walipanga kwenda Nyabange, nyumbani kwao na Stella kwa lengo la kumtambulisha Cosmas kama mchumba wa Stella na kupata baraka za wazazi katika uhusiano wao.
Kwa kuwa Cosmas alihitaji faragha katika safari hiyo, hakutaka kabisa kupanda gari la abiria, hivyo akaamua kuazima gari kwa rafiki yake na ambaye alikuwa kama ndugu yake, Boniphace Mayunga. Boniphace hakuwa na hiyana, alimpatia rafiki yake gari aina ya Toyota Rav 4, nyeusi ili alitumie kwa safari yake ya kuelekea ukweni.
Siku iliyofuata, Cosmas na Stella walijiandaa kwa safari ya kuelekea Nyabange, huku Stella akipanga kuitumia safari hiyo kuomba msamaha kwa wazazi wake pamoja na kumtambulisha Cosmas kama mume wake mtarajiwa. Aliamini wazazi wake watamsikiliza na kumsamehe pamoja na kumpatia baraka zao katika maisha mapya aliyoyaanzisha kwa mara ya pili na Cosmas.
Siku hiyo Stella alikuwa ni mwenye furaha kuliko kawaida, alivalia dila lililoshonwa kwa khanga, na kichwani alifunga kilemba cha khanga ileile aliyotumia kushonea dila alilovaa.
“Cosmas,” Stella aliita na Cosmas aliyekuwa kulia kwake aligeukia upande aliokaa Stella akaitika, “Naam mpenzi,”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakupenda,” Stella alisema.
“Nami nakupenda pia mpenzi,”
“Kama nisipokufa kwa ajili yako, basi nitakufa nikiwa nawe..” alisema Stella na kusababisha Cosmas amshangae kwa maneno yake.
Stella alikuwa amekaa kwenye kiti cha mbele, upande wa kushoto, na kulia kwake alikaa Cosmas ambaye ndiye aliyekuwa dereva. Yeye alivaa suruali nyeusi ya kitambaa na shati jekundu la mikono mirefu. Vazi la staha alilolichagua kuendea ukweni.
Gari lao lilikuwa linatoka kwenye kituo cha mafuta kilichopo kwenye kona ya njia iendayo Nyamuswa, mkabala na Silent View. Ghafla likagongwa ubavuni na Chaser nyeupe ililyokuwa ikiendeshwa kwa kasi kutokea Nyamuswa. Kwa kuwa gari hilo lililigonga gari la akina Stella na Cosmas upande aliokuwa amekaa Stella, nguvu ya msukumo iliyotokana na kasi ya gari lile lililowagonga ilimfanya Stella apatwe na mshtuko wa ubongo pamoja na majeraha yaliyosababisha kifo chake palepale. Ilihuzunisha sana.
****
Kiti alikuwa amekaa kitandani, huku macho yake akiyaelekeza juu ya dari ilihali yakiwa yamefumba. Mikononi mwake alikuwa na bastola ambayo mdomo wake uligusishwa kidevuni kwake karibu kabisa na koromeo huku kidole chake kinachofuatana na kidole gumba kikiwa kimewekwa kwenye kitufe cha kufyatulia risasi tayari kwa kufyatua. Akili yake ilikuwa imekwishaghiribiwa kabisa na maisha ya ulimwengu huu, ambayo kwake hayakuwa na maana tena. Taswira za kuzimu ziliutawala ubongo wake na kumwondolea urazini ambao ungemfanya kung’amua ubaya wa dhambi aliyokuwa mbioni kuitenda katika nukta yoyote ya saa iliyofuata.
Ndipo mzee Ngomanzito alipoufungua mlango wa chumba cha Kiti na kumkuta mwanaye akiwa katika hali ile ambayo ilimshtua na kumfanya apaze sauti kwa lengo la kumkemea mwanaye asifanye kitendo kile cha kipuuzi, “Heeeyy…. Stop!”
Lilikuwa kosa. Kwa sababu ukelele alioupiga mzee Ngomanzito ulimshtua Kiti na kumfanya aminye kile kitufe cha kufyatulia risasi bila kujitambua.
Ana bahati siku yake ilikuwa haijafika. Ponapona yake ilisababishwa na hitilafu ndogo iliyokuwa kwenye bastola ile ambayo ilikuwa na muda mrefu bila kusafishwa. Hitilafu hiyo ndiyo iliyosababisha risasi ishindwe kutoka kutokana na mkwamo ulioizuia kutoka kwenye chemba yake.
Mzee Ngomanzito alimuwahi na kuipora ile bastola kutoka mikononi mwa Kiti na kuitupa kando kitambo kidogo kutoka pale walipokuwa. Kiti alikuwa ni kama mtu aliyechanganyikiwa, alikuwa hajitambui. Mzee Ngomanzito alimnasa makofi mawili ya nguvu sambamba na matusi mazito ambayo yalimzindua Kiti kutoka kwenye pumbao alilokuwemo. Mwili wake ulikuwa umelowa jasho lililoyameza machozi yaliyokuwa yakimtoka kwa sababu ya kulia.
“Jinga kabisa…. yaani mapenzi ndiyo yakusababishe ufanye upuuzi wa namna hii!” mzee Ngomanzito alifoka. Huku akimtazama mwanaye kwa jicho kali lisilo dalili ya kukubaliana na kile alichokifanya mwananaye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sura yake na hisi za moyo wake vilikinzana. Japo usoni alionekana ni mkali na mwenye hasira, moyo wake haukuwa hivyo! Moyoni mzee Ngomanzito alimhurumia sana mwanaye, alijua fika maumivu ya moyo yanayomkabili baada ya mambo kwenda kinyume na alivyotarajia ndiyo yamempa msukumo wa kutaka kujaribu kufanya upuuzi ambao ungeyaondoa maisha yake.
Aliamua kuvaa uso wa mbuzi kwa sababu; angeonesha huruma ka mwanaye, angekuwa ni kama anaunga mkono unyonge wa mwanaye pamoja na mambo yote ambayo angeweza kuyafanya kutokana na unyonge wake ikiwemo kujiua.
“Mwanaume unapaswa kuwa imara… kabiliana na hali bila kujiuzulu mpaka dakika ya mwisho, leo wewe unajiua unaacha mwenzako anachukuliwa na bwege mwingine wakati wewe ukiwa umeshakufa.”
“Bora kufa baba.. bora kufa. Haiwezekani Wayeka anifanyie hivi, tena mbaya zaidi kwenye siku yangu ya kuzaliwa?” alisema Kiti huku akilia kwa uchungu.
“Pumbavu mkubwa wewe… ulitaka afanye kwenye siku gani, au unafikiri ukifa ndiyo atakurudia?”
Mzee Ngomanzito alimtazama mwanaye kwa hasira kisha akamtwanga swali jingine, “ Hivi umeshawahi kujiuliza ni kitu gani kinafuata baada ya kifo?” Yalikuwa ni maswali mazito kwa Kiti, hasa hili la mwiso la nini kinafuata baada ya kifo, sina hakika kama alilisikia vema swali hilo na sijui majibu yake yangekuwa ni yapi kama angejibu.
Kweli nimeamini mapenzi yana raha na karaha. Baada ya Kiti kuwa amezifurahia nyakati za raha katika mapenzi yake na Wayeka, sasa ilikuwa ni zamu ya karaha.
10
KWA bahati mbaya sana wapenzi wengi wa leo si wale wenye kujali hisia za mioyo ya wenzi wao. Si wale ambao ukicheka basi watacheka pamoja nawe au ukilia, walie pamoja nawe. Wao ukicheka watakudhihaki ama kukuzomea na ukilia wao watacheka.
Lakini hali hii ilikuwa ni kinyume kabisa kwa Wayeka, yeye alijali hisia za mwenzi wake. Hakuridhika kabisa kumwona Kiti akiwa katika hali ya unyonge wala huzuni, alipomuona au kuhisi Kiti yuko katika hali ya huzuni yeye aliumia zaidi, na pengine alianza kutoa machozi kabla hata ya Kiti. Na alifanyakila aliloweza kumwondolea mwenzi wake huzuni, unyonge au sononeko kwa sababu alitambua kuwa ana moyo wa nyama, moyo ambao ungeweza kuhisi hali ambazo binadamu wenzake wanaweza kuhisi.
Asubuhi ya siku hiyo ya tarehe 10 ya mwezi wa nne, tarehe ambayo Kiti huazimisha siku yake ya kuzaliwa, pia ni siku ambayo yeye na Kiti walipanga kuvishana pete ya uchumba. Siku hiyo Wayeka aliamka mwenye furaha isiyo ya kawaida, kwa sababu siku aliyoisubiri kwa muda mrefu sasa ilikuwa imefika. Aliwatumia ujumbe mfupi ndugu, jamaa na marafiki ambao alikuwa amewaalika waje kushuhudia tukio muhimu katika maisha yake, tukio la kuvishwa pete na mwanamme ambaye ni chaguo la moyo wake, akiwakumbusha kuwa siku ile waliyokuwa wakiisubiri ilikuwa imefika.
Wayeka alifanya maandalizi yote ambayo aliyaona ni ya msingi, na jambo pekee lililokuwa limebaki ni kusubiri tu muda ambao yeye na ujumbe wake walipanga kuianza safari ya kuelekea Bunda kwenye eneo ambalo sherehe ilipangwa kufanyika.
Kwa kuwa alipanga yeye na ujumbe wake waondoke pamoja kama msafara, aliwaarifu wote kuwa; msafara utaanzia nyumbani kwao, kwa mzee Ayuyube.
Nusu saa kabla ya kutimu muda ambao Wayeka na ujumbe wake walipanga kuanza safari yao ya kuelekea Bunda, Wayeka alipokeaa ugeni wa ghafla ambao hakuwa ameutarajia wala kuufikiria. Wayeka alikuwa sebuleni kwao, ndani ya gauni jeupe, vazi ambalo alilivalia rasmi kwa ajili ya sherehe. Hakuwa peke yake sebuleni pale, alikuwa na mashoga zake wawili ambao walimuweka kati kwenye kochi moja walilokalia, huku mbele yao kukiwa na glasi za shurubati ambazo walizinywa kwa tuo, ndipo ukaja ujumbe ulioletwa na mdogo wake wa kike, “Dada kuna mgeni wako,” mtoto wa miaka kama 10 hadi 12 alisema na kusubiri jibu kutoka kwa dada yake.
“Mwambie aingie,” Wayeka alijibu kwa kujiamini, akiamini kuwa labda ni mmoja kati ya wageni aliowaalika.
a kujiamini, akiamini kuwa labda ni mmoja kati ya wageni aliowaalika.
Yule mtoto aliondoka, na dakika moja baadaye mgeni aliingia. Alikuwa ni mwanamke kwa jinsia, na umri wake haukupishana sana na wa Wayeka, naweza kusema umri wao ulikuwa sawa.
Machoni pa Wayeka mgeni yule alikuwa mpya, hakukumbuka kumuona mahali popote na hata miongoni mwa rafiki zake wawili aliokuwa nao pale ndani, hakuna aliyeonesha dalili ya kumfahamu mgeni yule.
“Karibu…” sauti tatu zilisikika kwa pamoja kama waliombizana na yule mgeni akajibu, “Ahsante,”
Alikaribishwa kwenye kochi lililopakana na lile walilokaa Wayeka na mashoga zake, akakaa. Mgeni yule alikuwa na sura ya bashasha ambayo haikusababisha yeyote kati ya Wayeka na mashoga zake kumtilia shaka. Alishamiri tabasamu, na alikuwa na sura isiyo dalili ya hatia.
“Habari yako?” Wayeka alisalimia na yule mgeni akaitikia, “Safi tu, mambo zenu?”
Wayeka na rafiki zake walijibu baada ya kuwa wamejumuishwa wote katika salamu ile.
Ukimya wa sekunde kadhaa ulijiunda kabla ya kuvunjwa tena na yule mgeni, “Vipi za maandalizi?”
“Tunashukuru kwa kweli… kila kitu kiko ok,” alijibu Wayeka akiwa ameachia tabasamu murua usoni pake, tabasamu ambalo lilisababisha kutokea kwa vijishimo mashavuni mwake na kumfanya aonekene mrembo kupindukia.
Yule mgeni naye alitabasamu na kusema, “Inapendeza kwa kweli…” alisita kidogo na kuacha ishara kuwa bado anataka kusema ingawaje hakujua aseme neno gani. Alimeza funda la mate, halafu akaendelea, “Samahani, ni na shida na wewe,”
Wayeka na shoga zake walitazamana kwa zamu kama vile wanamtafuta miongoni mwao mlengwa wa kauli ile.
“Nani… mimi?” hatimaye Wayeka alijitoa kimasomaso na kuuliza, wale shoga zake waliyatega makini yao ili kusikiliza jibu la yule dada mgeni.
“Ndiyo Wayeka… nina shida na wewe,”
Wayeka alishtuka! Alijaribu kubashiri ni shida gani aliyonayo mgeni wake bila mafanikiao. Akawageukia mashoga zake kwa zamu, kisha akawaambia, “Nadhani hamtojali mkinipa wasaa nizungumze na mgeni?”
Hawakubisha. Walitoka ndani kwa lengo kuwapa faragha Wayeka na mgeni wake. Yule mgeni alisimama kutoka kwenye lile kochi alilolikalia awali na kwenda kukaa kwenye kochi alilokaa Wayeka ili waweze kuzungumza kwa karibu zaidi.
“I can feel una furaha kiasi gani katika siku hii,” alisema yule mgeni mara baada ya kuwa amekaa. Wayeka hakusema kitu zaidi ya kutabasamu.
“Na Kiti is a good guy and handsome, ambaye kila mwanamke mzuri angetamani kuwa naye,” yule mgeni aliendelea kusema.
Tabasamu la Wayeka lilizidi kuchanua zaidi, baada ya kusikia mpenzi wake akimwagiwa sifa.
“Do you know the guy?” Wayeka aliuliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Exactly, ni miaka saba sasa tangu nimfahamu,” Yule mgeni alista kidogo, akavuta pumzi kiasi ndani, kisha akasema, “My name is Mina… Minaeli Swai. Sidhani kama unanifahamu?”
“Ofcourse… sikufahamu.” Alisema Wayeka.
“Ni mpenzi wake na Kiti.”
“Whaat?” sauti ilimtoka Wayeka kama asiyeamini kile alichikisikia.
Bila kujali mshtuko alioupata Wayeka, Mina alianza kufafanua ni kwa vipi yeye ni mpenzi wa Kiti. Alianza kwa kumpa historia namna walivyokutana na Kiti tangu siku ile ya kwanza shuleni, mpaka mara ya mwisho alipoachiwa barua na Kiti hotelini, Chang’ombe walipolala siku hiyo.
Kuna jambo moja Mina aliongeza, jambo ambalo lilizidi kuivuruga kabisa akili ya Wayeka.
“Kamwambie Kiti nampenda, na nina ujauzito wake wa wiki sita.”
Haikuwa hiyali yake kulia licha ya kujikaza kisabuni mbele ya mgeni aliyegeuka hasimu wake, uchungu uliomjaa moyoni uliyasukuma machozi ya Wayeka yaliyokuja kutanda kwenye goroli za macho yake, kabla ya kutiririka mashavuni kama maji ya mto Yordani. Hakujua aseme nini, hakuwa na neno mujarabu la kusema. Akili yake ilikwishavurugwa na taarifa aliyoipata. Moyo wake uliwaka moto, kichwa chake kiliwaka moto likawa balaa juu ya balaa mwilini mwake.
Hakuna binadamu mwenye moyo wa chuma, wote tuna mioyo ya nyama iliyoko upande wa kushoto vifuani mwetu. Inaweza kukuwia vigumu kuamini kuwa Mina naye alikuwa analia wakati wote aliokuwa akieleza, mpaka anasimama kuondoka Mina bado alikuwa analia.
Wakati Mina anasimama kuondoka, simu ya Wayeka ilianza kuita. Hakujishughulisha nayo mpaka ilipokata na ilipokata tu, aliizima kabisa.
****
Mina aliwapita watu waliokuwa nje, nymbani kwa kina Wayeka. Wote walishangaa kumwona akiwa analia, alikwenda moja kwa moja mpaka kwenye gari lake akalitia ufunguo, akakikanyaga kibati cha mwendo, gai likaanza kutembea. Aliposhika njia kuu, njia inayoziunganisha Nyamuswa na Bunda, alipanga gia na kuzipangua, gari likachanganyia mwendo na kuwaacha watu wote njiani wakimshangaa kwa namna alivyokimbiza gari kwa kasi.
Alipita salama Kiloleli, Kisangwa na Nyihendo. Ikiwa umebaki umbali wa kama mita elfu moja hivi kuifikia barabara ya lami, barabara inayounganisha miji ya Mwanza na Bunda hadi Musoma, Mina alijaribu kupunguza kasi gari ya gari lakebila mafanikio. Watu waliofanikiwa kuliona gari la Mina na mwendo lililokuwa nao walishika vichwa vyao. Mbele yake kulikuwa na gari lililokuwa likiingia barabarani likitokea kwenye kituo cha mafuta kinachotazamana na jengo la Finca.
Alipoona ameshindwa kabisa kupunguza mwendo huku gari lake likizidi kulikaribia lile gari aina ya Toyota Rav 4, taswira ya jehanamu ilimjia kichwani na kumsababisha apige ukulele mkubwa, “Mamaaa….”
Kilifuatia kishindo kikubwa kilichowashtua watu waliokuwa maeneo ya jirani kiasi cha kuweza kukisikia, “BAAANG..” kishindo kilichotokea baada ya gari la Mina kuligonga gari walilokuwemo Cosmas na Stella.
11
BONY na Emmy na walikuwa na wakati mgumu, wakati ambao Bony alikuwa kwenye wodi ya wanaume, Emmy alikuwa kwenye wodi ya wanawake. Muda wote Emmy alikuwa pembeni ya kitanda alicholala Mina kwa siku ya pili mfululizo bila kufanya mjongeo wa kiungo chochote cha mwili wake tangu alipopoteza fahamu kwenye ajali.
Sehemu kubwa ya mwili wa Mina ilikuwa imefungwa bandeji zilizolowa damu kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata. Pua yake na mdomo vilikuwa ndani ya kifaa maalumu kilichounganishwa na mirija mpaka kwenye mashine kwa lengo la kumsaidia kupumua, au kwa kifupi niseme Mina alikuwa anapumulia mashine.
Macho ya Emmy muda wote yalikuwa kwa Mina, alimuonea huruma na pia alipatwa na uchungu mkubwa kumuona rafiki yake akiwa katika hali ile. Muda wote alitamani arejewe na fahamu, ili aweze kupumua bila msaada wa mashine na baadaye awe mzima kama zamani, hata kama atabakiwa na makovu, bora tu awe mzima.
Kwenye mkono wa kushoto wa Mina, Emmy alikiona kidole kinachofuatana na kidole gumba kikicheza. Awali alidhani ni mawenge yake, lakini alipokiona kikicheza kwa mara nyingine Emmy alitoka mbio na kwenda kumuita mwuguzi.
“Nesii.. nesii… kidole kinacheza,”
“Kidole?” Mwuguzi yule mwenye jinsia ya kike aliuliza baada kutomwelewa vizuri Emmy.
“Ndiyo… kidole,” alisema Emmy akiwa amechanganyikiwa huku akimuonesha nesi ishara iliyomuashiria kuwa amfuate. Yule nesi aliinuka kutoka pale kwenye kiti alipokuwa amekaa, akamfuata Emmy mpaka kwenye kitandaalicholazwa Mina. Walipofika walimkuta Mina akiwa amerejewa na fahamu, ingawaje hakuweza kuzungumza.
Yule nesi alimfuata daktari ambaye naye alikuja kuishuhudia hali ya mgonjwa wake, alipofika na kumuona mgonjwa wake, daktari alifanya ishara ya msalaba huku sauti ikimtoka, “Ahsante Mungu.”
Kauli ya daktari ilifufua matumaini mapya kwa Emmy, naye akafanya ishara ya msalaba kama alivyofanya daktari, sina halika kama alidhamiria au ni kwa sababu alimuona daktari akifanya ndiyo na yeye akaamua kufanya.
Siku hiyo hiyo jioni wazazi wa Mina ambao walikuwa wakisubiriwa kutoka Moshi, ambako ndiyo nyumbani kwao na Mina waliwasili. Walikuja; baba yake mina, mama yake pamoja na mtoto wao mwingine wa kike ambaye alikuwa mdogo kuliko Mina.
Licha ya kumkuta katika hali ambayo waliokuwa nae tangu awali waliiona ni nafuu, ndugu zake Mina, hususan mama yake pamoja na mdogo wake walilia, walimlilia ndugu yao aliyekuwa amelala kitandani akipumua kwa msaada wa mashine.
“Usilie mama… najua inaumiza sana kumuona mpendwa wako katika hali ya namna hii. Yakupasa kushukuru kwa sababu mpendwa wako bado yuko hai na anendelea vizuri.” Alisema yule mwuguzi ambaye ndiye aliyekuwa akimhudumia Mina tangu alipofikishwa hospitalini pale.
“Atapona tu mama, atapona.” Emmy naye aliongeza baada ya kumuona yule mama ambaye kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo machozi yalivyozidi kuongezeka. Daktari aliwaomba wote waongozane naye mpaka ofisini kwake, ofisi ambayo haikuwa mbali na chumba alicholazwa Mina. Waliongozana na kumwacha Emmy peke yake akiwa pembeni ya mgonjwa wao wakifuatana na daktari huku shingo zao zikigeukia alipolala mpendwa wao mpaka walipovuka mlango.
Walipofika ofisini kwa daktari waliketi kwenye viti vilivyokuwa ofisini mule na mara baada tu ya kuketi, daktari alianza kwa kuwafariji na kisha kuwaeleza hali ya mgonjwa kwa kina na maendeleo yake tangu alipofikishwa hospitalini hapo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Majeraha yake si makubwa sana, mingi ni michubuko tu ambayo nadhani haitachukua muda mrefu kabla ya kupona. Ujauzito wake ndiyo imekuwa bahati mbaya kwa sababu umetoka..”
Walishtuka kusikia habari za ujauzito aliokuwa nao Mina, lilikuwa ni jambo ambalo hawakulifahamu. Lakini kabla hawajapata nafasi ya kuuliza swali daktari aliendelea, “… kingine labda ni mshtuko tu ambao ndiyo umemsababishia kupoteza fahamu… ingawaje naamini atarudia hali yake ya kawaida tu, hata kama…” daktari alisita kisha akamtazama mama Mina ambaye bado alikuwa analia pamoja na bintiye.
Alipowadadisi wote kwa undani alibaini kuwa, wawili hao hawatakua na uwezo wa kuhimili yale anayotaka kuyasema. Akayarudisha macho yake kwa mzee Swai kwa namna ya tahadhari, kisha akayarudisha macho yake kwenye picha za X-ray ambazo walimpiga Mina, akashusha pumzi ndefu kiasi, kisha akamgeukia tena mama Mina, “Pole mama… Mina atapona tu usijari,” alisema daktari.
“Ahsante baba, tusaidie Mina apone,” alisema mama Mina kwa sauti yenye kwikwi iliyotokana na kilio.
“Usijari mama, atapona tu, ila naomba mtuache mimi na baba hapa kuna jambo nataka kujadiliana naye,” alisema daktari.
Mama Mina na mwanaye walijiinua kivivu kutoka kwenye viti walivyokuwa wamekalia, wakatoka mule ofisini na kuelekea kule wodini alikolazwa Mina.
Walipoachwa mule ofisini daktari alisubiri mpaka alipohakikisha kuwa mama Mina na bintiye hawako tena karibu na ofisi yake kiasi cha kutoweza kabisa kuyasikia atakayoyasema, alishusha pumzi kisha akasema, “Mzee…” alisita kidogo kabla hajaendelea, nadhani ni kwa sababu ya uzito wa jambo alilotaka kulisema, “… najua ni jinsi gani inavyoumiza kwa mzazi kumshuhudia mwanao akiwa katika hali ya namna hii. Naomba uelewe kuwa kazi yetu sisi madaktari ni kuhakikisha watu wanaohitaji huduma yetu ya kitabibu wanaipata kwa namna inayostahili. Najitahidi kwa weledi na kwa kuzingatia miiko ya kazi kuhakikisha binti yako anarejea katika hali yake ya kawaida kama zamani.” Alimeza funda kubwa la mate, halafu akaendelea, “…ila ipo shida… ipo shida katika hili… tuna wasiwasi kuwa yawezekana akili ya Mina ikawa matatizoni.”
“Oh my God,” mzee Swai alishtuka, kwa mshtuko ambao daktari aliutarajia. Kabla mzee Swai hajapata nafasi ya kusema neno jingine daktari alimuwahi, “Ni tatizo la muda tu, inagawaje litachukua muda mrefu sana kupona,” alisema daktari kwa masikitiko makubwa.
Ni aghalabu sana kuyaona machozi ya mwanaume, tena mtu mzima kabisa kama alivyo mzee Swai, ambaye kwa makadirio, umri wake ni kama miaka hamsini hivi. Mzee Swai alikuwa anatokwa na machozi yaliyounda mfereji mrefu toka kwenye macho yake kuelekea kwenye mashavu yake.
“Nimeona nikuweke wazi wewe, ili uone namna utakavyoweza kuliwasilisha hili kwa mama yake,” aliongezea daktari.
****
Bony alikuwa pembeni ya kitanda alicholazwa Cosmas bila fahamu tangu alipopata ajali. Alikwishawasiliana na ndugu zake kuwajulisha hali ya ndugu yao. Kwa taarifa ya simu, Bony alifahamishwa kuwa mama yake na Cosmas alipoteza fahamu mara tu baada ya kupewa habari za mwanaye kipenzi.
Bony alitarajia muda wowote tangu wakati huo kumuona ndugu yeyote wa Cosmas hospitalini pale baada ya kuambiwa wako njiani wanakuja wakitokea Butuguri ambako ndiko nyumbani kwao na Cosmas.
Bony alikuwa katika lindi la mawazo aliposhtuliwa na sauti hafifu, “Stella… Stella…” ilikuwa ni sauti ya Cosmas ambaye alikuwa akiita huku mkono wake wa kulia ukipigapiga polepole kwenye godoro la kitanda alicholalia, ni sehemu tu ya kiganja cha Cosmas ndiyoiliyokuwa ikipigapiga kwenye godoro.
Bony alitulia tuli ili kushuhudia kinachoendelea pale kitandani alipolala swahiba wake wa siku nyingi. Moyoni, Bony aliumia sana alipomsikia Cosmas akiita jina la Stella, aliumia kwa sababu alijua fika kuwa Cosmas hajui kama Stella hayupo tena duniani. Alimhurumia kwa kuwa alitambua tabu atakayokumbana nayo Cosmas baada ya kupewa taarifa kuwa Stella alikufa palepale ajali ilipotokea. Hakujua ni kiasi gani ataumia.
Akiwa kenye lindi la mawazo huku macho yake akiwa ameyaelekeza kwa Cosmas aliyekuwa kitandani, Bony alishtuliwa na kivuli cha ghafla ambacho kilimfanya ahisi uwepo wa mtu mwingine zaidi yake mahali pale. Aligeuza shingo yake na kutazama mlangoni ambapo macho yake yalimshuhudia muuguzi akiingia mule ndani na pamoja na watu wengine wawili, mmoja mwanaume na mwingine mwanamke. Mwanaume ambaye kichwa chake kilianza kupambwa na mvi alikuwa akishabihiana kabisa kwa sura na Cosmas. Bony akajiaminisha kuwa, ni lazima atakuwa ni baba yake na Cosmas na yule mwanamke ambaye umri wake ulikuwa katika hali ya ubinti, naye alifanana na Cosmas na hivyo kumfanya Bony ajiaminishe kuwa hao ni ndugu zake na Cosmas kwa sababu ya ufanano wa sura na hali ya simanzi waliyokuwanayo.
“Mgonjwa wetu ni huyu hapa, na hali yake siyo mbaya kwa sababu anaendelea vizuri tofauti na alivyoletwa hapa siku ya kwanza.” Alisema yule muuguzi huku akionesha mkono wake pale alipolala Cosmas.
Mara baada ya kuingia mule chumbani, wale ndugu wa Cosmas walisalimiana na Bony na kisha kujitambulisha kwake kuwa wao ni ndugu wa Cosmas, ambapo yule mwanaume alijitambulisha kuwa yeye ndiye baba mzazi wa Cosmas na baadaye kumtambulisha yule binti binti waliyeongozana naye kuwa ni dada wa Cosmas ambaye Cosmas alimuachia ziwa.
“Vipi mgonjwa anaendeleaje?” aliuliza baba yake Cosmas katika hali ya kukata tamaa kwa sababu ya muonekano aliokuwa nao Cosmas pale kitandani alipolala.
“Angalau sasa anaendelea vizuri, kuna muda aliongea, tena muda mfupi uliopita kabla hamjaingia,” alisema Bony.
“Nashukuru sana kwa kuwa karibu na mwanangu katika wakati mgumu kama huu. Mungu akubariki sana mwanangu kwa moyo wako huo,” mzee Manyaki ambaye ni baba yake na Cosmas alisema.
“Usijali baba, Cosmas ni rafiki yangu wa karibu sana na ni kama ndugu yangu, hivyo kila ninalolifanya hapa ninalifanya kwa sababu ni wajibu wangu kama ndugu na rafiki wa Cosmas.” Alisema Bony.
Mzee Manyaki ambaye ni baba yake na Cosmas alipata faraja baada ya kuyasikia maneno yaliyosemwa na Bony. Akamshukuru Mungu kwa kumpa mwanaye rafiki kama Bony ambaye ni rafiki hasa bila kujali hali wala wakati.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakiwa bado mule chumbani wote Bony, mzee Manyaki na dada yake Cosmas walimsikia Cosmas akiita, “Stellaa…Stellaa..” kwa sauti iliyotoka kwa tabu.
Chozi lilimtoka dada yake Cosmas baada ya kumsikia kaka yake akiita jina la mwanamke ambaye hayupo tena duniani, mwanamke ambaye siku chache zilizopita aliwasiliana naye kwenye simu akitambulishwa kuwa yeye ndiye wifi yake na wangeonana siku si nyingi. Hawakujua kuwa Mungu ana mipango yake; wakati ambao binadamu anapanga yeye huwa amekwishapanga tayari.
“Sara mwanangu, acha kulia, hali ya kaka yako ni kama unavyoiona. Nyamaza mwanangu, nyamaza…” alisema mzee Manyaki wakati akimbembeleza binti yake.
“Atakapoamka asiambiwe lolote kuhusu Stella mpaka atakapopona kabisa,” Bony alishauri na wote mzee Manyaki na Sara wakamkubalia kwa kichwa.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment