Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KUTI KAVU - 3

 









    Simulizi : Kuti Kavu

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Wakati Domi akiwa anayatafakari yale mapokezi. Baba na mama Doi nao walikuwa wakiwaza yao. Ukimya ukaendelea kushika hatamu kwa muda kidogo.



    “Mwanangu Domi…” hatimaye mzee Vioja aliuvunja ukimya ule. “Mwanetu Dominic,” Mzee Vioja aliita tena kwa sauti ambayo ilikuwa imebeba mamlaka ya baba mwenye hekima.

    “Naam baba,” Dominic aliitikia kwa heshima ya hali ya juu.

    “Kwanza kabisa tunashukuru kwa pesa ulizotutumia, mimi na mama yako tunassema ahsante sana mwanetu” Dominic aliyasikia barabara maneno ya mzee Vioja, lakini hakujua aseme nini kwa wakati huo. Akilini mwake alikuwa akiwaza bila mafanikio. “Pesa…Pesa nilizotuma?” Dominic alijua wazi kuwa yeye hakuwa amewatumia pesa wazazi wa Doi. Na hapo ndiyo akagundua kuwa ; yawezekana Doi alikuja kwao kuleta pesa, na katika ujio wake huo hakuwa ameweka wazi kuwa alishaondoka nyumbani kwake, yaani kwa Domi. Akiwa kwenye lindi hilo la mawazo, Domi alishtuliwa na sauti ya Mzee Vioja, “Dominic” mzee Vioja aliita
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naam baba” Domi aliitika

    “Unaonekana mwenye mawazo sana, vipi Doi yuko salama, au kuna tatizo gani huko nyumbani?” Mzee Vioja aliuliza na kumfanya Domi atambue kuwa fikra zake ziko sahihi kuwa, wazazi wa Doi hawajui kama binti yao hayuko nyumbani kwake. Ikambidi ajiweke sawa kabla hajaanza kuongea.

    “Baba na mama,” Domi aliita kwa heshima kama ishara ya kutaka kuwaweka sawa ili wasikie kwa makini kile anachotaka kuwaambia, “Ukweli ni kwamba, mimi sijatuma pesa, na mpaka sasa tunavyoongea leo ni siku ya tano tangu Doi atoweke nyumbani”



    “Unasemaje?” sauti ziliwatoka baba na mama Doi kwa pamoja hali iliyomfanya Domi ashtuke.

    “Ina maana hizi dola hujatuma wewe?” Mzee Vioja aliuliza.

    “Mimi sijatuma dola zozote wazazi wangu”

    “Na mbona Doi amesema ni zawadi kutoka kwa mkwe wetu, ina maana kuna mkwe zaidi yako?” Mama doi alimtupia swali Dominic, swali ambalo lilizidi kumchanganya kabisa Domi.

    Wakati huo mzee Vioja alikuwa ametumbukwa na jicho la mshangao na fadhaa.

    “Ni kweli, mimi sijatuma pesa” alisema Domi kwa sauti iliyojaa masikitiko makubwa.

    Mzee Vioja alimtazama Dominic kwa umakini halafu akamuita, “Dominic,”

    “Naam baba,”

    “Hebu nieleze kila kitu bila kuficha mwanangu…” Mzee Vioja alisita kidogo na kuruhusu fundo kubwa la mate lipite kooni mwake kuelekea tumboni, halafu akaendelea. “Kulikuwa na mgogoro wowote baina yako na na Doi?”

    “Hapana, hatukuwa na mgogoro wowote,”

    Mzee Vioja alitulia kidogo akawaangazia macho kwa zamu, wote Dominic na mama Doi aliyekuwa ubavuni kwake upande wa kushoto, halafu akamalizia kwa Dominic aliyekuwa amekaa kinyonge mbele yao, akaendelea, “Labda…kuna tofauti yoyote uliyokuwa umeibaini kwa mwenzako kwa siku za hivi karibuni, nikiwa na maana kabla hajaondoka?”



    “Hapana baba, sikuwa nimeibaini tofauti yoyote mpaka siku niliyofika na kutomkuta kabisa Doi” alipokuwa anayasema haya, Domi alipatwa na uchungu usioelezeka, lakini alijikaza kiume.



    “Mama Doi, hebu tupe nafasi kidogo,” Alisema mzee Vioja na Mkewe akaondoka pale sebuleni na kuwaacha Dominic na mzee Vioja ambaye ni baba yake na Doi.



    Baada ya mama Doi kuondoka Mzee Vioja alimgeukia Dominic na kusema, “Mwanangu, hebu nieleze vizuri kwa sababu hapa tumebaki wanaume tu”



    Domi alimueleza kila mzee Vioja, alimueleza juu ya barua na pesa amabazo alizikuta chini ya mto.

    Baada ya kuelezwa Mzee Vioja alisikitika sana kwa jinsi binti yake alivyomtia aibu.hata hivyo baada ya maongezi hayo Dominic aliaga na kuondoka.



    ***

    Doi alikuwa akiustaajabia mkoba ambao Damian amemnunulia, pamoja na begi kwa ajili ya safari yake ya Parris nchini Ufaransa. Ulikuwa ni mkoba safi wa ngozi uliovutia kutazamwa na kila jicho lenye uono! Mkoba wa rangi nyeusi, wenye mishikio ya iliyotengenezwa kwa bati la shaba nyeupe na kurembwa kwa rangi ya dhahabu. Hakika mkoba huu mzito uliipendeza nafsi ya Doi.



    Ukiachilia mbali mkoba, begi ambalo Damian alimnunulia kwa ajili ya safari hiyohiyo ni begi la bei mbaya, lilikuwa ni begi zito la ngozi lililotengenezwa nchini italia. Doi alivitazama vitu hivyo kwa macho ya kustaajabia. Akiwa bado anashangaa begi la safari na mkoba wake, Damian akamkabidhi tikiti ya ndege, “Hii ni tikiti yako kwa ajili ya safari” Alisema Damian wakati akimkabidhi tikiti ya ndege ya shirika la ndege la Emirates.



    Doi aliipokea ile tikiti akiwa anatetemeka, hakuamini kama kweli safari yake ya Parris ilikuwa imeiva!

    Aliisoma ile tikiti ili kujiridhisha zaidi. Ni katika kusoma huko ndiyo akagundua kuwa ile tikiti ilikuwa yake peke yake.



    “Vipi, mbona tiketi ipo yangu tu, kwani wewe husafiri?” Doi aliuliza.

    “Kwa nini nisisafiri? Mimi pia nitasafiri ila hatutaongozana. Mimi nitasafiri kesho kuelekea Michigan, Marekani. Kuna mambo naenda kuyaweka sawa halafu ndiyo niende parris next week kwa ajili ya kukupokea wewe jumamosi kama tiketi yako inavyoonesha.” Maelezo ya Damian yalimshtua kidogo Doi, kwani alitarajia kuona wanasafiri pamoja, kinyume na fikra zake, kila mtu atasafiri kwa wakati wake kama alivyofafanua Damian.



    “Lakini mbona hukuwa umesema mapema?” Doi alimtupia Damian swali.



    Damian alifikiri kidogo halafu akauliza swali badala ya kujibu swali aliloulizwa na Doi, “Kwani kuna tatizo?”

    “Hapana, ila…” kabla hajamalizia kauli yake Damian alimuwahi, “Ni kweli nimefanya kosa kwa kutokueleza mapema juu ya jambo hili. Ila naomba unilewe kuwa sina nia mbaya, nataka niwahi mapema nikafanye kazi zilizo mbele yangu ili tuwe na muda mwingi wa kuyafurahia maisha tukiwa Parris, au waonaje?”

    “Kama ni hivyo basi sawa, ila utaniacha mpweke sana”

    “Najua ila usijali, nitakuachia pesa ya kutosha ili ikupunguzie upweke kwa kufanya ulipendalo”

    Mazungumzo yao yaliisha kwa kuwatupa kwenye dimbwi la kicheko!



    Siku iliyofuata Damian, alipanda ndege na kumuacha Doi akiwa na ukwasi wa pesa kwa ajili ya kufanya lolote la kumuondolea upweke kama alivyoraiwa na Damian.



    Ndege ilipoiacha ardhi, Doi alirudi hotelini ambako aliendelea kukaa mpaka siku ya siku ilipofika. Siku hiyo Doi aliandaa kila kitu chake cha safari ikiwemo pasi ya kusafiria, kibali cha kukaa Ufaransa pamoja na mizigo yake yote aliyokuwa ameiandaa kwa ajili ya safari.



    Jambo lililomtesa Doi ni kusafiri bila ndugu yake yeyote kujua juu ya safari yake. Doi alishindwa kujua ataagaje nyumbani kwao. Pia alijua kuwa; Domi asingeweza kuvumilia kukaa muda wote huo bila kwenda kwao, yaani kwa mzee Vioja. Alijua kama Domi alienda kwao na yeye akaenda ataivuruga safari yake, kwa kuhofia kuhojiwa juuu ya anakokwenda na ilikuwaje akaondoka kwa Domi.



    ***

    Baada ya kuwa amepigiwa simu na Udaku jirani yake, kuhusiana na simu zinazopigwa na mkewe hasa nyakati za jioni, Mudi alipuuza kwa kuamini kuwa ni umbea na hakujishughulisha na suala hilo kabisa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja akiwa kibaruani kwake, Mudi aliwaza juu ya taarifa ile ya Udaku. Aliona si vema kupuuzia kabisa ujumbe ule na pia si vema kuchukua maamuzi ya haraka. “Inabidi kufanya uchunguzi kwanza, isije ikawa ni mbinu ya kutugombanisha na Zai” Mudi aliwaza yote haya wakati yuko barabarni anaendesha.



    Ikatokea siku akiwa kituoni anasubiri abiri abiria, majira kama ya saa 10:15 jioni, Mudi alichukua simu na kumpigia Zai, simu iliita mara moja na mara sauti ya Zai ikasikika kutokea upande wa pili, “Hallow,”

    “Halioo bibie” Mudi alijibu baada ya kusikia sauti ya Zai upande wa pili.

    “Nakusikia mme wngu, habari za kazi?”

    “Za kazi njema tu, nimekukumbuka sana mke wangu”Mudi alisema





    “Usijali mme wangu, mi nipo kwa ajili yako”

    “Ok basi hakuna shida tutaonana baadaye nikirudi” Alisema Mudi na kukata simu.



    Saa moja baadaye Mudi alipiga tena simu kwa Zai ili kuona kama ataweza kugundua lolote lenye kuhusiana na kile alichokisema bi Udaku, kama ilivyokuwa awali, Zai hakuchelewa kupokea simu aliipokea mara tu ilipoanza kuita wakongea.



    Kwa mujibu wa taarifa ya Bi Udaku, Mudi alitarajia kukuta simu ya Zai inatumika kwa muda huo, lakini kinyume na matarajio yake simu haikuwa inatumika kama alivyotarajia. Siku hiyo ikapita Mdi akiwa kwenye mninginio wa taharuki!



    Siku iliyofuta ilikuwa ni siku ya alhamis, siku hiyo Mudi aliamua kukabidhi gari kwa mtu mwingine kwa muda. Mtindo huo ulikuwa ni kawaida kwa madereva wengi wanapokuwa wamechoka au kupatwa na dharula, mtindo huo ulikuwa maarufu kama deiwaka. Mudi alikabidhi gari kwa dereva mwingine ‘Deiwaka’ ili aendeshe mpaka yeye atakaporudi.



    Majira ya kama saa 10:30, Mudi alifika nyumbani kwake alikopanga maeneo ya Yombo Buza. Kwa kunyata alizunguka nyuma ya nyumba na kwenda mpaka lilipo dirisha la chumba chake ambacho wanaishi yeye na mpenzi wake, Zainabu Mpotoshi.



    Alipofika pale dirishani Mudi alitulia tuli ili aweze kusikia yanayojiri ndani. Mudi alitega sikio na kusikiliza kama kuna atakaloweza kulisikia kutoka ndani.



    Kama ilivyoeleza taarifa ya Bi Udaku ni kweli Zai alikuwa bize akionega na simu!



    Mudi alikuwa akiyasikia barabara maneno yote aliyokuwa akiongea Zai na simu ya upande wa pili. Mudi alihisi kuchanganyikiwa kwa maneno aliyokuwa akiyasikia, “Usijali, hiyo jumamosi nikija utafurahi….mimi ndiye Zai binti Mpotoshi” Zai aliendelea kujinadi kwenye simu.



    Mudi alishindwa kabisa kuvumilia akatoa simu yake mfukoni akampigia Zai, akasikia simu inaita ikifuatiwa na suti ya Zai, “Subiri kidogo mpenzi wangu, n’takutafuta baada ya muda ya mfupi,” Mudi alizidi kuchanganyikiwa alipoyasikia maneno hayo.



    Mara akagutushwa na sauti ya mkewe, “Hallow,” sauti ambayo ilisikikia mara baada ya mlio wa muito wa simu kukoma. “Hallow.., niambie mpenzi?” alisemaMudi huku donge la uchungu likiwa limemkaba kooni.

    “Ninalo basi..” Sauti ya Zai ikasikika kupitia spika ya simu ya Mudi na kwenye matundu ya nyavu za dirishani alipokuwa amejibanza.

    Mudi alijitahidi ili aendelee kuongea na simu licha ya uchungu aliokuwa nao, “Nimekukumbuka mke wangu…”

    “Usijali mme wangu nipo kwa ajili yako” hiyo ilikuwa ni sauti ya Zai, sauti iliyojaa unafiki ambao Mudi ameshaubaini.

    “Powa basi, baadaye” Alijibu Mudi na kukata simu.



    Baada ya kukata simu Mudi aliendelea kukaa dirishani, haikupita muda akamsikia tena Zai anaongea na simu, “Enhe nambie mpenzi wangu”



    Hasira zikampanda Mudi, lakini akamuomba Mungu aendelee kumpa ujasiri na subira ili aendelee kuusikiliza upuuzi wa Zai, mwanamke aliye mwamini na kumuweka ndani kama mke. Akamthamini kwa kila kitu, mahaba motomoto, fedha na mavazi! Zai atake nini kwa Mudi asipewe?



    Mudi akazunguka kutoka kule nyuma ya nyumba alipokuwa, akaenda mpaka mlangoni kwake, akausukuma mlango akakuta umefungwa kwa ndani! Akaamua kubisha hodi na mara baada ya muda mfupi Zai akafungua.

    “Vipi, mbona umejifungia saizi?” Mudi alimtupia swali la kizushi. Bila aibu wala woga Zai akajibu, “Nilikuwa nimelala mme wangu,” Alijibu Zai huku akiachia mwayo wa kinafiki.



    Hapo akili ya Mudi ikazidi kupambanua mambo, akajikaza kiume bila kuonesha tofauti yoyote kwa Zai, akaingia ndani. Alipoingia ndani Mudi alivua fulana aliyokuwa amevaa akaitupa kwenye kochi lililokuwa mule chumbani, kisha yeye mwnyewe akajitupa kitandani kama mzigo!

    “Pole mme wngu, umechokaje,” alisema Zai huku akikaa kitandani na kuruhusu mkono wake uchezee manywele yaliyotapakaa kifuani kwa Mudi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Nimechoka sana Zai wangu, na hizi kazi zetu za kuamka usiku usiku hizi we acha tu,”

    “Ngoja nikuwekeee maji ya kuoga” alisema Zai na kunyanyuka kutoka pale kitandani alipokuwa amekaa na na kuelekea nje.



    Hiyo ilikuwa ni bahati kubwa sana kwa Mudi, moyoni alikuwa akiomba itokee nafasi kama hiyo ya kuachwa chumbani peke yake, nafasi amabyo kweli imetokea.



    Zai alipotoka tu nje Mudi aliamka pale kitandani kama ninja, kwa kasi ya ajabu alikisaili chumba kizima na mara macho yake yakatua kwenye kabati la vyombo. Moja kwa moja akaielekea hotpot iliyokua kabatini akaifunua. Mudi hakuamini macho yake baada ya kuishuhudia simu aina ya Nokia ya tochi ikiwa imezimwa na kufunikwa ndani ya ile hotpot!



    Mudi alifunika lile hotpot na kurudi kitandani, akilini alipiga mahesabu makali ya kutega mtego siku ya jumamosi.



    Punde si punde Zai alirejea, akafungua kabati la nguo na kumtolea Mudi taulo. Mudi alivua nguo, akajifunga lile taulo, akaelekea bafuni huku akiongozwa na Zai aliyem’bebea sabuni na mswaki.



    ***

    Dominic alirudi kutoka kazini akiwa amechoka. Baada ya kuegesha kwenye maegesho yake, akaanza kupanda ngazi kuelekea kwenye Apartment yake ambayo ilikuwa ghorofa ya kwanza. Apartment ambayo amepangishiwa na kampuni anayoifanyia kazi kama mkataba wa ajira unavyoeleza.

    Kwenye makazi hayo mapya, yaliyokuwa maeneo ya ilala, Domi aliona angalau sasa ameanza kuishi kama ambavyo siku zote alitarajia kuishi; kazi nzuri, nyumba nzuri na kadhalika.



    Kutokana na uchovu uliosababishwa na kazi nyingi za kutwa nzima, Domi alipitiwa na usingizi muda mfupi baada ya kuwa amejiegesha kwenye kochi!



    ***

    Mnamo majira ya saa 9 alasiri, Doi alikuwa ndani ya Tax akielekea uwanja wa ndege tayari kwa safari ya Parris. Njiani aliwaza mambo mengi sana. Aliwaza jinsi atakavyokuwa akishafika Ufaransa. Alipoyafikira maisha ndani ya Parris, aliiona saa yake kama vile haisogei!



    Doi alitamani kufumba na kufumbua awe tayari ameshafika ndani ya jiji la Parris, nchini Ufaransa. Aliwaza pia jinsi atakavyowamiss ndugu zake hasa baba yake na mama yake. Moyoni aliwaza kuwa, atakaporudi awanunulie angalau gari, ili na wao wafaidi matunda ya kuzaa.



    Katika kuwaza kwake, Doi hakumsahau Dominic, mwanaume aliyempenda Doi kuliko kitu chochote. Aliwaza jinsi Domi anavyopata tabu kwa kumkosa. Doi aliumia sana na kumuonea Domi huruma, katika lindi hilo la mawazo machozi yakaanza kumtoka. Akajipangusa kwa kutumia leso yake, alipotupa macho nje ya gari alibaini kuwa yuko maeneo ya JET CORNER, eneo lililo mita chache kabla ya kufika uwanjani, eneo ambalo kuna njia inayochepuka kwenda Yombo Buza, eneo ambalo yeye na Domi walikuwa wanaishi.



    Kona hiyo ilimkumbusha mengi ya nyuma, alikumbuka kuwa; kwa mara ya kwanza aliipita njia hiyo kuelekea Buza kwa ajili ya Dominic. Na inawezekana asingeipita kama asingekua kwenye uhusianao na Dominic.



    Akiwa kwenye lindi hilo la mawazo, hatimaye sauti ikamtoka, “Kwa heri Domi wangu” alisema Doi huku machozi yakimtoka. Akachukua leso yake akajipangusa tena.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dada tayari tumefika,” sauti ya dereva ilisikika na kumgutua Doi kutoka mawazoni.

    Akashuka, wakasidiana na dereva kubeba mizigo mpaka eneo ambalo abiria hukaaa kusubiri ukaguzi. Baada ya kumfikisha pale, dereva alirudi garini na kuondoka. Doi alibeba mizigo yake kuelekea chumba cha ukaguzi kilichopo pale uwanjani.



    Kama ilivyo kawaida ya viwanja vingine, uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK NYERERE pia kuna utaratibu wa kukagua mizigo ya wasafiri kwa sababu za kiusalama. Askari waliokuwa pale uwanjani kwa ajili ya ukaguzi walikuwa makini sana, hii ni baada ya uwanja huo kukumbwa na kashfa ya kupitisha kilo 150 za madawa ya kulevya aina ya ‘CRYSTAL METHAMPHETAMINE.’ Hivyo ili kulinda kazi yao na heshima ya nchi, iliwabidi wafanye kazi yao kwa umakini mkubwa sana.



    Abiria aliyekuwa mbele ya Doi alikaguliwa, na alipomaliza kukaguliwa ikafuata zamu ya Doi kwa ajili ya kukaguliwa.



    Walianza na mkoba na baadaye begi. Mizigo ya Doi ikawekwa pembeni na Doi akaamuliwa kukaa pembeni sanjari na mizigo yake.



    Kitendo cha kuambiwa kae pembeni yeye pamoja na mizigo yake kilimshtua sana, kilimshtua kwa sababu abiria aliyekaguliwa kabla yake alipita moja kwa moja baada ya ukaguzi, hivyo ikambidi Doi aulize, “Vipi jamani mbona mimi nawekwa pembeni?” kabla hajajibiwa alishtushwa na kundi la askari walioingia mule ndani.

    “Uko chini ya ulinzi, wewe pamoja na mizigo yako,”

    Doi alipigwa na butwaa, askari wale walimchukua msobemsobe na kumpeleka ndani zaidi, “Nimefanya nini jamani, mbona sielewi?”



    Huko ndani mizigo yake ilitawanywatawanywa kwa ajili ya kunya kufanya uchunguzi wa kina. Doi alichanganyikiwa hakujua ni kwa nini anafanyiwa vile!

    Mara unga mweupe ukawa unatolewa kwenye mishikio ya mkoba wake na kwenye mishikio ya begi lake na wale askari waliokuwa wakifanya upekuzi.

    “Leo umepatikana,” sauti ya askari ilisikika ikisema na kuzidi kumchanganya zaidi Doi, “Jamani mimi sijui lolote,” alilalama Doi lakini hakuna aliyemjali.

    “Mmezoea hapa madawa yenu, mnatuharibia kazi na kulitia doa taifa. Sasa kimefika kiama chenu” Alisema akari ambaye alikua anamalizi kuyakusanya yale madawa na kuyaweka pamoja.

    Doi alilia sana!



    Dakika chache baadaye alichukuliwa maelezo na kufungulikiwa jalada, halafu akatolewa na kupakizwa kwenye gari la polisi chini ya ulinzi mkali wa askari wenye bunduki huku waandishi wa habari wakipiga picha.



    Mpaka wakati huo, Doi alikuwa amechanganyikiwa kabisa, safari yake ya Ufaransa ikawa imeota mbawa na uelekeo ukawa ni kituo cha polisi cha kati





    KAMA Kuna kitu Mudi alikiamini maishani, basi ni kujitambua. Aliamini ili uweze kufanikiwa ni lazima ujitambue kwanza; wewe ni nani, unatoka wapi, uko wapi, unaelekea wapi na mtu sahihi kwako ni nani, ili uweze kufanikisha yote unayoyahitaji.



    Siku hiyo ya jumamosi, Mudi aliaga na kuelekea zake kibaruani kama ilivyo ada. Huku akiendelea kuwasiliana na bi Udaku kwa siri kubwa. Kwa pamoja walipanga kufanya mawasilano ili Udaku afuatilie nyendo za Zai kwa siku hiyo. “Ukimuona anatoka tu, we mfuatilie kimya kimya ikibidi kodi hata pikipiki mimi nikija nitalipa” ilikuwa ni sehemu ya maelekezo aliyoyatoa Mudi kwa Udaku.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huku nyuma Zai alijipamba isivyo kawaida! Alikuwa amependeza ndani ya vazi lake la baibui, kilemba aghali kichwani, na mwili wake ukiwa umepulizwa uturi wenye kunukia haswa!



    Baada ya kujitazama kwenye kioo kwa mara kadhaa, Zai arliridhika na muonekano wake, akautwaa mkoba wake akautupia begani tayari kwa kuondoka. Akafunga mlango wa chumba chake kisha taratibu akawa anaiacha nyumba.



    ***

    Wakati Zai anajiandaa, Bi Udaku naye alikuwa akijiweka tayari kuanza kufuatilia nyendo zake. Hivyo wakati anaondoka, bi Udaku alimtanguliza kwa hatua kadhaa mbele huku akichukua tahadhali kubwa ili asiweze kuonekana na macho ya Zai.

    “Hallow… kaka Mudi,” Bi Udaku aliongea kupitia simu yake, na sauti ya upande wa pili ikajibu, “Hallow.. jirani nakupata..”

    “Aisee.. huku mkeo amejipamba haielezeki! Yaani amejipamba ile balaa…” Alisema Bi Udaku kwa mbwembwe nyingi na kumuweka Mudi kwenye wakati mgumu.

    “Enhe, amevaaje?”

    “Amevaa baibui moja matata sana na kichwani ametupia kilemba cha hatari chenye rangi ya dhambarau…. Hayo marashi sasa… yaani mkeo ananukia njia nzima.” Alizidi kuongea bi Udaku kwa kumpamba na kumnanga Zai kwenye simu.



    Huku Mudi alipagawa… alipagawa kiasi cha kuhisi kuchanganyikiwa. “Sasa naomba ule naye sahani moja… hakikisha hakupotei machoni, mfuate hatua kwa hatua na uwe unanijulisha kupitia simu.” Mudi alitoa maelekezo kwa bi Udaku, maelekezo yaliyoonekana kumfurahisha sana bi Udaku.



    ***

    Zai alivuka barabara na kusimama upande wa kushoto, akaipiga bajaji mkono, ikasimama akajitoma ndani, ikaondoka!



    Baada ya Bajaji kuanza mwendo, Bi Udaku naye kwa haraka alivuka barabara, akaiendea pikipiki iliyokuwa upande wa pili, “Ifuate ile Bajaji nyekundu, ifuate kwa umakini ili asiweze kujua kama wanafuatwa”



    “Wameshakuliza au? maana watoto wa mjini hawakawiagi” alisema yule dereva wa pikipiki wakati anaiondoa pikpiki yake tayari kwa kuifuata ile Bajaji.

    “Haya hayakuhusu, jali biashara yako” alisema bi Udaku na yule dereva wa pikpiki akasema, “Utalipa zaidi ya kawaida, hapa ni sawa na kuiweka roho yangu mkononi kwa kutibua michongo ya watu,”

    “kaza mikono motto wa kiume, pesa ndiyo imekuleta kazini,” alizema Udaku na Yule dereva akakaa kimya. Wakawa wanaifuatilia ile Bajaji ambayo ilikuwa mita chache mbele yao.

    “Hallow..”

    “Yeah.. nambie..”

    “Ameshuka hapa Mwisho wa Lami”

    “Kama nilivyosema… hakikisha hakupotei machoni.” Mudi alizidi kusisitiza na bi Udaku akaongeza umakini zaidi kwa Zai ambaye baada ya kushuka alienda moja kwa moja akapanda daladala inayoishia JET CORNER.

    Isingekuwa rahisi kwa Zai kumtambua Bi udaku kwa sababu alikuwa amevaa ‘helmet’ iliyomfanya asitambulike na yeyote ambaye angemwona.



    “Ngriii… ngriiii” Simu ya bi Udaku iliita, “Hallow Mudi” bi Udaku aliongea na sauti ya upande wa pili ikajibu, “Kuna mpya..?”

    “Hapana.. gari bado halijaondoka” Bi Udaku alisema.

    “Ok, usiruhusu akupotee machoni” Mudi alisisitiza na Bi Udaku akajibu, “Sawa”



    ****

    Mudi alikabidhi gari kwa rafiki yake ambaye alifahamika kama Deiwaka. Akachukua pikipiki ambayo alikuja nayo Deiwaka, akaipiga moto na kwa kasi ya ajabu akaendesha mpaka JET CORNER, ambapo alifika na kusimama kando ya barabara mbele kidogo ya geti la CTM-TILES

    “Gari limeanza kuondoka,” bi Udaku aliongea kupitia simu yake ya mkononi.

    “Tayari nimeshafika JET CORNER, we lifuatilie hilo gari kwa nyuma na kama atashuka kabla ya JET nifahamishe..”

    “Powa..” Alijibu bi Udaku.

    Gari lilitembea mpaka LUMO, bi Udaku akiwa analifuatilia kwa nyuma, pale LUMO lilisimama lakini hakuna abiria aliyeshuka, ila kuna abiria wawili waliingia kwenye gari hilo, likaondoka huku bi Udaku akilifuatilia kwa nyuma kwa pikipiki aliyokodi. Baada ya LUMO lile gari halikusimam tena mpaka lilipofika JET CORNER, abiria wote wakashuka akiwemo Zai.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    Akiwa pale pale pembeni ya barabara mbele kidogo na lilipo geti la CTM-TILES, Mudi alimshuhudia Zai akishuka kutoka kwenye gari aina ya TOYOTA HIACE iliyotoka Machimbo. Alikuwa amependeza ndani ya mavazi yake nadhifu aliyovalia. Kwa madaha kabisa Zai alitembea kuelekea kule zinakopaki gari ziendazo, Banana, Gongo la mboto, Chanika na Pugu.



    Wakati bado Mudi amemkodolea macho Zai wake, simu yake iliita. “Hallow Jirani, bibie ameshuka hapa JET CORNER, na hivi tunavyoongea yupo kwenye kituo cha magari yaendayo Gongo la mboto. Nafikiri safari yake iko uelekeo huo.” Alisema bi Udaku.

    “Nimeshamuona, sasa unawezza kurudi nyumbani niachie sehemu iliyobaki… nitaimaliza mwenyewe.” Alisema Mudi kwa sauti iliyojaa gadhabu, licha ya kujitahidi kuificha hali hiyo lakini iliweza kutambulika sawia masikioni mwa bi Udaku..



    Gari la kwanza liliondoka Zai akiwa bado yupo kituoni, likaja pili likaondoka zai akiwa bado yuko palepale kituoni. Gari la Gongo la mboto likaja pale kituoni, Zai akajitoma ndani kwa madaha na kwa kujiamini, gari likaondoka.



    Mudi kwenye pikipiki yake akaanza kulifuata kwa nyuma lile gari alilopanda Zai, huku akiwa ameacha umbali wa mita kadhaa zilizowatenganisha baina yao.



    Gari lilisaga Lami mpaka Uwanja wa ndege bila Zai kushuka, likatembea mpaka Posta.. hapo pia lilisimama lakini Zai hakuonekana kushuka . Lilipita Njia panda segerea, Banana, Mombasa bila Zai kushuka huku Mudi akilifuata kwa nyuma gari hilo aina ya TOYOTA –DCM.



    Gari alilopanda zai lilipofika Gongo la Mboto lilisimama na Zai akashuka huku Mudi akimshuhudia kwa uangalifu ndani ya helmet iliyomfanya asiweze kutambulika na yeyote.



    Aliposhuka tu kwenye gari lile la Gongo la mboto ambalo lilikuwa limefika ukomo wa safari yake, zai alishuka akajisogeza kwenye gari zinazoenda Chanika akajitoma ndani.



    “Anaenda wapi huyu? Hajawahi kuniambia kama ana ndugu maeneo haya, sasa huku anaenda kwa nani?” Wakati Mudi anaendelea kujiuliza maswali hayo, gari alilopanda Zai likaanza kuchapa mwendo huku Mudi akilifuatilia kwa nyuma kwa umakini wa hali ya juu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    Huku Nyamuswa, mama na baba Domi walikuwa wamekaa na binti yao anayeitwa Tina. Walikaa kwa mazungumzo ya kifamilia mara tu baada ya chakula cha mchana. Hii haikuwa mara yao ya kwanza, walizoea kukaa pamoja na kuzungumza kuhusiana na familia yao, juu ya nini kifanywe au kipi kisifanywe kwa manufaa ya familia yao na jamii kwa ujumla.

    Hiki kilikuwa ni kikao cha sita kufanyika bila uwepo wa Domi, kwa sababu tu hakuwepo nyumbani. Tofauti na vikao vingine vyote, kikao cha siku hii kilimuhusu zaidi Domi.



    “Kama nilivyosema jamani, Domi amefanikiwa kupata ajira, na amesema twende wote Dar es salaam tukajue anapoishi, pamoja na kusalimiana kwa sababu hatujaonana naye siku nyingi” Hiyo ilikuwa ni sauti ya kavu ya mzee Masaka, ambaye baada ya kuongea aliweka pumziko na kisha kumuangalia mama Domi na baadaye binti yao Tina kwa zamu kama vile kuna kitu anataka kusikia kutoka kwao kabla hajaendelea.







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog