IMEANDIKWA NA : STALLONE JOYFULL
*********************************************************************************
Simulizi : Nenda Na Moyo Wangu
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ninachokumbuka ni mlio wa simu, ambao ulinikumbusha kuivua suruali kisha
viatu; nilivyotaka kulala navyo bila kuvua kutokana na pombe nyingi
nilizokunywa. Ulikuwa ni mlio ulioashiria ujumbe mfupi wa maneno uliingia
katika simu yangu, hata hivyo sikushuhurika nayo nikajitupa kitandani
kivivu. Siku hiyo sikuoga wala kukumbuka chakula.
Mara nikiwa katikati ya usingizi, ghafla simu ikaita kwa sauti ya juu.
Hapana!
Ilikuwa ni sauti ndogo ya kawaida ila kwa kuwa niliilalia kwa sikio langu,
ndio maana niliisikia kuwa ilikuwa ikitoa sauti kali mno. Kwa hasira
sikutazama aliyekuwa akipiga wala aliyenitumia meseji ile, nikaizima.
Usingizi mzito ukanibeba kwenye usiku ule wa manane mpaka nilipoamka
asubuhi majira ya saa 4:25 asubuhi. Niliandaa maji ya moto ya kuoga huku
simu yangu nikiwa nimeiweka chaji. Nikiwa nayasubiri maji yachemke,
nilikihisi kichwa changu kizito kutokana na pombe nilkizokunywa, nikaanza
kuikumbuka siku ya jana nikiwa nimekaa kitandani, kiunoni n'na taulo zito
jeupe kifua wazi tayari kwa kuoga.
....
NIKIIKUMBUKA SIKU YA JANA JINSI ILIVYOKUWA:- Jana ilikuwa ni jumatatu, kama
jumatatu nyingine zenye pilikapilika nyingi tofauti. Hiyo ilikuwa ni
kuanzia asubuhi mpaka ilipotimu majira ya jioni, jumatatu hiyo ikabadilika
kwetu na kuwa sawa na wikiendi. Katikati ya hoteli ya Lamada kwenye bustani
murua yenye ukijani uliokolea, tulijumuika katika tafrija ya tukio maalumu
la kuvishana pete mimi na mpenzi wangu Beatrice.
Tuliwaalika ndugu jamaa na rafiki zetu wa karibu, kushuhudia tukio hilo la
kipekee. Kila mmoja alikuwa na uso wa furaha kwa kushuhudia tukio lile
likitimia. Mimi na Beatrice tulifurahi zaidi kwa kuwa ndoto zetu
ziliendelea kutimia tangu tulipoanza uhusiano wetu tukiwa chuo.
"Nakupenda sana Beatrice"
"Hakuna mwingine zaidi yako Ramon"
Kisha tukapeana papi zetu, huku ndimi zetu zikipigana kwa furaha kwakitendo
cha badilishana lita kadhaa za mate midomoni mwetu. Sherehe iliendelea,
watu wakafurahi wakala wakashiba, walevi wakanywa wakalewa nikiwa mmoja wao
kati yao, huku Beatrice akiwa ameshika chupa yake ya tatu ya soda akinywa
taratibu.
Ilikuwa yapata saa 6:45 usiku, ndio tuliondoka baada ya Beatrice kunifuata
katikati ya meza niliyokaa na Michael pamoja na rafiki zetu wengine, mara
baada ya sherehe kuisha na watu kadhaa kuondoka akiwemo mama yangu, baba
akiwa na wazazi wa Beatrice wakinywa kwa furaha.
"Tunachelewa baby, saa saba kasorobo sa' hivi"
Aliniambia huku akitazama saa kwenye simu yake. Nikawaaga rafiki zangu
kisha tukaenda kuwaaga wazazi waliozama katika vicheko. Nikamsindikiza
Beatrice mpaka nyumbani kwake Mikocheni ambapo alishaacha kuishi na wazazi
wake waliokuwa wakiishi Bunju.
kisha mimi nilirudi nyumbani kwangu kijichi.
....
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mlio wa kitufe kilichofyatuka kutoka katika birika la kuchemshia maji, ndio
ulinitoa katika mawazo hayo ya siku ya jana na kunirudisha tena chumbani
kwangu. Nikazima ukutani na kuyamwaga maji yale ya moto kwenye ndoo ya
kuogea, kisha nikabeba sabuni pamoja na mswaki niliouweka dawa nikaingia
bafuni nikiwa nimeshajaza maji mengine ya baridi ya kuyapooza yale ya moto.
Nilipomaliza kupiga mswaki baada ya kuvua taulo huku nikipiga mluzi
niliokuwa nikiimba wimbo fulani wa "Msondo Ngoma" nikakumbuka jambo. Jana
usiku nilipigiwa simu, na nani? Meseji pia? Atakuwa nani? Nilikumbuka
kutazama kweli? Si kwenda kuangalia mpaka nilipomaliza kuoga na dakika kumi
zilitosha kufanya hivyo.
Nikamaliza kuoga na kutoka bafuni huku nikijifuta maji kwa taulo.
Saa iliyopo juu ya meza ya chumbani kwangu ilionesha kuwa imetimu Saa 5:58
zilibaki dakika mbili itimie saa 6 mchana. Nikaiwasha simu yangu kuangalia
ni nani aliyekuwa akinipigia simu. Nikafungua sehemu ya simu ambazo
hazijapokelewa, alikuwa ni mpenzi wangu Beatrice. Nikaipiga simu yake,
haikupokelewa. Mara ya pili haikupokelewa, ya tatu vivyo hivyo.
Nikakumbuka kuwa jana usiku ilianza kuingia meseji kabla ya simu kupigwa,
nikaenda upande wa meseji, alikuwa ni Betrice pia. Nilipousoma ujumbe wake,
moyo ulinilipuka vuuup!! Kama taa ya kandili inayoanza kuishi mafuta yake,
nikaanza kuhisi joto kali licha ya upepo mkali wa feni ulioendelea kupuliza
ndani ya chumba changu.
Meseji hiyo iliandikwa "KWANINI UMENIUWA RAMON?"...
Nilijaribu tena kuipiga simu ya Beatrice lakini nilichojibiwa, kilikuwa ni
kile kile nilichoambiwa mara ya kwanza na sauti ya mwanamke wa huduma kwa
wateja "simu unayopiga haipokelewi, bonyeza..." Nikaikata na hapo nikahisi
naanza kuchanganyikiwa. Sikujua Beatrice alimaanisha nini mpaka aseme kuwa
ninamuuwa. Nikaamua nimpigie rafiki yangu Michael ambaye alimfahamu vizuri
Beatrice, Michael hakuwa akipatikana.
Nikaamua kwenda mwenyewe hadi Mikocheni anapoishi Beatrice.
Niliwasha gari yangu na kushusha kilima cha kijichi kisha nikaibukia kwa
buruda na kupita misheni nikaitafuta barabara ya kilwa road nije kuibukia
azikiwe niitafute barabara ya mwai kibaki baada ya mwendo wa speed kali
ulionichukua zaidi ya dakika 45 mpaka kukatisha katika mtaa anaoishi
Beatrice.
Nilisimamisha gari mara baada ya kufika getini kwake na kupiga honi nyingi,
lakini sikuona dalili za kufunguliwa. Nikaizima gari yangu na kushuka,
niseme ukweli kuwa nilikuwa n'na hasira kwa kuwa nilijua ni utani wa
Beatrice lakini wasiwasi ulinijia kila nilipowaza itakuwaje kama ni kweli
amepatwa na matatizo?
Nikaitazama kwa dakika kadhaa kamera ya ulinzi pale getini, lakini haikuwa
ikitazama tena getini kama nilivyozoea. kitu cha ajabu na kilichonitia
mashaka niliona kuwa ilinyofolewa kwa makusudi au bahati mbaya na mtu awaye
yeyote, lakini sikutambua. Nikaamua kugonga hodi mara kadhaa na kuona
kimya, nikaamua kulisukuma geti lile likafunguka bila ajizi. Mshangao
mwingine, haikuwa kawaida kwa Beatrice kuacha mlango wazi.
Nilipoingia ndani mara baada ya kuvuka geti lile, nyumba ilikuwa kimya huku
mlinzi Baraka akiwa hayupo eneo lake la lindo.
Nikapiga hatua chache mpaka kwenye nyumba kubwa ya Beatrice, moyo wangu
ukapiga pah! Ukutani mwa nyumba ya Beatrice karibu na ulipo mlango wa
kuingilia, niliona alama ya kiganja kilicholowa damu na kushika eneo hilo
la ukuta.
Miguu yangu ilianza kutetemeka na kuwa kama inayogongana huku kengele ya
hatari ikipiga kichwani mwangu. Ukweli ni kwamba sasa matumaini ya kumkuta
mpenzi wangu akiwa hai yalikuwa madogo kuliko nilivyokuwa nikitoka
nyumbani. Nilianza kuona ukweli wa meseji yake lakini wasiwasi ulisukuma
zaidi mapigo yangu ya moyo, kwanini aandike mimi ndiye ninayemuuwa? Ukimya
ule ulinitisha zaidi kuliko alama ya kiganja cha damu juu ya ukuta wa
nyumbani kwa Beatrice.
Nikaingia ndani ya nyumba hiyo, pale mlangoni nikalakiwa na mburuzo wa mtu
aliyekuwa akivuja damu kutoka mwanzo wa mlango mpaka katika moja ya mlango
wa kuingilia chumba ambacho Beatrice alifanya kama stoo.
Nilipofungua chumba hicho, nilichokikuta hakielezeki. Kichwa
kilitenganishwa na mwili wala kichwa chake hakikuonekana na hadi leo sijuhi
kiko wapi. Tumboni kulikuwa na shimo kubwa lililoacha sehemu kubwa ya
utumbo kutoka nje na kuleta picha iliyotisha zaidi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Baraka!!!" Niliita kwa hofu huku nikiziba sura yangu kwa uoga na machozi
yakanibubujika.
Nilijaribu kutaka kukimbia na kuingia chumbani kwa Beatrice huku nikimuita
Beatrice. Beatrice hakuitika bali nikapokelewa na utelezi ulionifanya
niisalimie sakafu na kuibusu ardhi ya chumbani kwa Beatrice na kunifanya
niilambe damu iliyoganda pembeni ya mwili ulio uchi huku macho yakinitazama
na mdomo kama unaonizomea wa mpenzi wangu Beatrice.
"Mamaa weee!!" Kwa wahka nilipiga kelele za kuchanganyikiwa, nilipomsogelea
Beatrice nikamsukasuka huku nikimuita "Beatrice, Beatrice amka mama. Nini
kimekukuta jamani Beatrice, amka mama"
Bisu kubwa lilizama tumboni kwake huku kwenye sehemu ya koromeo lake ikiwa
imekatwa hivyo kuweka kama mfereji fulani uliotisha kuutazama. Nilikuwa
nikitazama mwili wa Beatrice na si Beatrice mwanamke niliyekuwa naye jana
usiku.
Nikiwa katika kulia huko? Nikasikia mchakato wa nyayo za mtu zikitembea
kuja ndani ya nyumba ya Beatrice.
"Wauwaji!!"
Akili yangu ikaninong'oneza. Nilinyanyuka upesi kuelekea sebuleni,
nikajificha nyuma ya kochi ili niweze kuwaona waliokuwa wakiingia. Tulikuwa
tumepishana sekunde chache kwani mara baada ya kuzama nyuma ya kochi lile,
wale waliokuwa wakija wakawa wamesimama eneo la stoo karibu na kochi
nililojificha mimi. Nilipoinua kichwa changu kuchungulia ni watu wa aina
gani? Nikawa nimefanya kosa, walikuwa ni askari sita, wa kike wakiwa wawili
kila mmoja akiwa amevaa gloves wanne wakiwa na silaha mikononi mwao huku
wawili wakiwa hawajavaa nguo za kipolisi bali mikononi walibeba simu za
upepo.
"Muuwaji!" Alikuwa ni askari mmoja mweusi wa kiume, aliyeshika bastola yake
ndogo kiukakamavu akaropoka huku akinielekezea silaha ile. Mwingine
akaropoka kwa sauti yake thabiti.
"Mikono juu ya kichwa usijiguse popote ukikiuka maagizo haya tunakutoa
ubongo. Usijaribu kufanya ujanja wowote" Ilikuwa ni sauti isiyo na mzaha
hata kidogo
Niliogopa sana kuoneshwa mdomo wa bastola kama mtu mwenye makosa. Ila
kukutwa ndani ya nyumba yalipofanyika mauaji, hakika sikuwa na ujanja.
"Mimi sihusiki!?"
Nilijaribu kujitetea kwa sauti ya kitetemeshi lakini haikusaidia. Mmoja wa
askari wale akaangua kicheko cha fedheha na kunitazama katikati ya miguu
yangu. Nikaushusha uso wangu pia kutazama kilichomfanya askari yule
kucheka, nikaishusha mikono yangu haraka kuiziba sehemu ile. Kumbe ile hali
ya ubaridi uliokuwa ukipenya katikati ya miguu yangu ni mikojo
iliyonichuruzika kutokana na uoga.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mikono juu, pumbavu" askari yule aliyekuwa akicheka akabadilika ghafla na
uso wake ukawa ule wa kuudhi. Mmoja kati yao akawa amenisogelea na
kunifunga pingu kwa nyuma katika mikono yangu. Kisha nikatolewa ndani ya
nyumba ile na kuwekwa katika gari ya polisi kwa mateke huku nikiwa
nimekwidwa kwa nyuma kwa style ya tanganyika jerk(suruali kukamatwa kwa
nyuma ya makalio na kufanya miguu kuelea juu juu) kisha walikaa ndani huku
nikiachwa na askari wengine watatu wenye bunduki aina ya Ak-47 wakinilinda
zaidi ya dakika 40.
Nikiwa nimefungwa pingu zile huku nikitazama askari waliokuwa wakinilinda
huku wale wengine wakitoka na kuingia ndani ya nyumba ya Beatrice na
mwingine akipiga piga picha kiganja kile ukutani na mburuzo ule mimi nikawa
najiuliza. Nilianza kujiuliza meseji niliyoipokea kutoka kwa Beatrice
"kwanini unaniuwa Ramon?" Kisha nakuta maiti mbili katika nyumba yake!
Inawezekana Baraka ndiye aliyemuua? Sasa kwanini aseme mimi ninamuuwa?
Ilianza meseji kisha ikafuata simu, inamaana aliyekuwa akinipigia simu ni
Beatrice au aliyemuuwa? Kwanza aliyemuuwa ni nani? Na hawa polisi, nani
amewataarifu mapema hivi kuwa ndani kuna mauaji yametokea? Hiki ni
kitendawili na huu ni mtihani wa aina yake niliokutana nao. Kwa sababu kama
nitadhani ni Baraka ndiye alimuua Beatrice na je yeye ni nani alimuua? Na
mbwa wako wapi?
Baada ya askari wale kutoka ndani ya nyumba ya Beatrice walinifunga
kitambaa cheusi machoni pangu na hivyo sikuweza kuona chochote mbele yangu.
Wakawasha gari na msafara wa kwenda kusikojulikana ukaanza. Akili yangu
ikawa na hopfu na kule ninakopelekwa. Sasa kama ni askari na ninapelekwa
mahabusu kwanini nizibwe na kitambaa cheusi? Nikaogopa zaidi.
Ulikuwa ni umbali mrefu ambao siwezi kukadiria tulitumia dakika ngapi au
kilometa ngapi mpaka kufika katika jumba hili kubwa lenye giza nene.
Nilitolewa ndani ya gari na kufunguliwa kitambaa na kisha taa zikawashwa,
kumbe tulikuwa tumeingia gereji nikapitishwa katika mlango mdogo wa
kuingilia katika nyumba hiyo. Ilikuwa ni nyumba kubwa sana, nyumba ambayo
haikuonesha dalili ya kuwa ni makazi ya mtu labda ni ofisi fulani. Kama ni
ofisi, kwanini niletwe ofisini na sio nipelekwe mahabusu nizijuazo?
Nikapelekwa katika chumba fulani kidogo chenye meza fulani ndogo na viti
viwili vikitazamana. Nikawekwa katika kiti kimoja huku taa yenye mwanga
mkali ikining'inia. Nikatolewa zile pingu kisha nikaachwa peke yangu.
Nilikitazama kile chumba kile pemnbe na kuziona kamera nne katika kila
pembe ya ukuta. Mbele yangu kulikuwa na kioo kipana ambacho hakikuwa na
tofauti na vile ambavyo huwa naviona kwenye picha za wazungu katika vyumba
vya mahojiano kama hiki.
Sikujua kuna siku na mimi nitakuwa katika mazingira kama haya.
Nilikaa kwa dakika kumi na tano mpaka mlango ulipofunguliwa na kuingia
kijana mrefu mwenye mwili uliokomaa kimazoezi na misuli iliyojazia. Alikuwa
ana kipara kichwani mwake na sauti nadhifu iliyombana.
"Habari yako Ramon?" Alinisalimu mtu yule. Nikajiuliza amenijuaje?
"Salama tu!" Sauti yangu ilitoka kwa shida kutokana na hofu ya hapo nilipo.
Kwanza nilianza kuhisi huenda wauaji waliomuua mpenzi wangu ndio
walionichezea mchezo huu na kujifanya wao ni askari. Sikujua ilikuwaje
walifahamu ndani ya nyumba ile kumetokea mauaji na iweje waje dakika chache
tu mara baada ya mimi kwenda katika nyumba ile na vipi huyu sasa anitaje
jina langu? Nini hiki kinaendelea?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Unavuta sigara?"
Nilimuona yule mtu ambaye bado hakuwa amejitambulisha kwangu, akitoa kasha
la sigara aina ya embassy na kuiwasha moja ya kwake baada ya kuitupia
mdomoni. Aliivuta mikupuo miwili mimi nilipokataa kisha akarudisha kete ya
maongezi mezani.
"Naitwa Jafari Hiza ningependa unifahamu hivyo kwa sasa mpaka hapo baadaye"
akanyamaza kwa tuo, kisha akavuta mkupuo mwingine wa sigara na moshi wake
ukaelea angani kisha akaizima sigara ile. "Nakufahamu wewe ni Ramon na ni
mpenzi wake Beatrice, Sivyo?"
"Ndivyo, Lakini..."
Alininyooshea kiganja chake kilichokomaa na kuinamisha uso wake kama kwamba
hakutaka kunisikiliza nilichotaka kuzungumza.
"Sihitaji uongee kitu ambacho sijakuuliza" alinyamaza kwa muda kama
anayetafakari jambo, kisha akaendelea. "Umefanya kosa kubwa sana mdogo
wangu. Kumuuwa mtoto wa kigogo wa umoja wa mataifa? Unajiamini nini?"
"Mimi...?"
Akanikatisha tena
"Mimi sijauuwa!" nikajitetea bila matumaini
"mimi sijamuuwa" Akaniigiza kwa kubana pua kisha akacheka kwa kebehi. "Na
ile meseji aliyokutumia kuwa kwanini unamuuwa, aliituma saa ngapi? Ulimuuwa
na kuondoka zako kisha wakati anakata roho ndio akapata nafasi ya kukuuliza
swali lililotia simanzi kiasi kile au meseji ile alikutumia wakati gani?"
"Mimi sijauuwa"
"Hujauwa? Jana usiku wa manane haukuwa naye? Mlisimama getini ukiwa na gari
yako aina ya Funcargo ukiwa umevaa shati nyeusi ya polo iliyokubana? Labda
nikuulize, ulirudi saa ngapi tena kufanya mauaji yale?"
Nikapatwa na ubaridi wa unyevunyevu fulani wa uchungu ulionitiririsha
machozi kama chemchem kutoka juu ya maporomoko na kwenda chini ya ardhi.
Nikalia sana kwa kuwa sifahamu chochote kuhusu mauaji ya Beatrice lakini
kila anachozungumza kilikuwa ni kweli na kuweza kunitia hatiani katika
mauaji hayo. Nilimuona akisimama na kuweka cd kwenye deki na kuiwasha tv
iliyopo pembeni yetu. Nikatumbua macho kushuhudia nini alikuwa anaenda
kunionesha.
Cd iliyowekwa ilikuwa ikionesha giza, lakini kwa msaada kidogo wa taa
niliweza kujiona mimi pamoja na Beatrice. Wajihi alioutaja huyu mtu
aliyejitambulisha kwangu kama Jafary Hiza ndio ule niliouona kwenye cd ile.
Hapo nikagundua kuwa waliitazama kwanza kabla hawajanihoji chochote.
Nikajiuliza sana hawa ni watu gani? Kwanini nisipelekwe polisi basi kama
n'natuhumiwa kwa mauaji na niletwe katika chumba hiki ? Hakika niliumia
sana nafsi. Jafary Hiza alinitazama na kuniambia
"Nimekuonesha cd hii kukuambia kuwa vithibitisho vyote vya wewe kuwa umeuwa
tunavyo sasa sielewi utakataa nini? Na pia labda nikuulize swali"
akanyamaza kiasi kisha akaendelea "hivi nyinyi vijana kwanini unapomchoka
mwenzio unamfanyia jambo la kinyama kiasi kile? Na yule mlinzi wa watu
amekukosea nini? Ndio kupoteza ushahidi? Wale mbwa uliowapa sumu je! Ndio
walianza au ni Baraka alianza kufa? Kwanini umeamua kufanya mauaji ya
kutisha kiasi hiki Ramon?"
Nikanyanyua mdomo wangu kwa mshangao wa ajabu baada ya kusikia kuwa mbwa
wale waliokuwa wakimlinda Beatrice kuwa wameuwawa kwa sumu "Mimi sihusiki
na mauaji hayo Jafary sihusiki chochote na sifahamu chochote kuhusu mauaji
hayo"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kabla Jafary Hiza hajazungumza alichotaka kuzungumza, kuna sauti ilitoka
kutoka katika chombo fulani pale mezani.
"Namba 3 kuna mwanasheria anahitaji kuzungumza na mtuhumiwa"
Jafary Hiza akajibu "Sawa nimekuelewa namba 1 mfungulie mlango niwaache
wazungumze"
Kisha niliuona mlango ambao aliingilia Jafary Hiza ukifunguka na kuingia
mwanamke mmoja mrembo sana. Kiukweli mwanamke yule alikuwa ni mrembo
kuanzia alivyovaa hata sura pamoja na umbo lake. Alivaa suruali ya kitambaa
iliyonyooshwa vyema na kutiwa upanga mkali kisha na koti lake la kitambaa
kinachofanana na suruali ile aina ya linen ya kahawia, usoni akiwa
amebandika miwani nyeupe. Hata mwendo wake mwanamke huyu, ulikuwa ni ule wa
kujitupa tupa kama wa walimbwende waoneshao mavazi au kugombania taji la
umisi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment