Search This Blog

Friday, October 28, 2022

BARUA KUTOKA KWA MAREHEMU - 1

 







    IMEANDIKWA NA : JOSEPH SHALUWA



    *********************************************************************************



    Simulizi :Barua Kutoka Kwa Marehemu

    Sehemu Ya Kwanza (1)







    YUPO peke yake barabarani, kwenye barabara hiyo ndefu iliyonyooka ya vumbi! Hapakuwa na gari, pikipiki wala baiskeli. Njia nzima alikuwa mwenyewe! Haikuwa barabara kubwa bali nyembamba yenye makorongo mengi ajabu.

    Alikuwa na pesa za kutosha kukodisha gari, lakini kwa hali ya barabara ilivyokuwa, isingekuwa rahisi kupitika! Mvua zilizokuwa zinamalizikia kunyesha ziliharibu kila kitu. Barabara ilikuwa haitamaniki!

    Anakwenda Baura nje kidogo ya mji wa Kondoa, nyumbani kwa wazazi wake. Hii ni baada ya kukaa Dar es Salaam kwa miaka mitatu bila kwenda kwao, lakini sasa analazimika kwenda kutokana na matatizo makubwa aliyokuwa nayo.

    Matatizo mazito!

    Mzimu unamsumbua na kumtesa. Unamnyanyasa. Unamnyima raha, amani aliyokuwa nayo imetoweka. Amekuwa kama mtumwa, tena mtumwa ambaye yupo katika kifungo cha nje. Machozi kwake yamekuwa kitu cha kawaida.

    Sasa anahitaji pumziko la kweli, sehemu pekee ambayo angeweza kupata pumziko hilo ni nyumbani kwao, nyumbani kwa wazazi wake ambapo lazima wangekuwa na wazo la kumsaidia. Kwa umri wake mdogo, asingejua mambo mazito yanayofanyika katika ulimwengu wa giza!

    Pengine watu wazima katika ukoo wao wangeweza kumpa msaada mkubwa na hatimaye furaha yake kurejea. Anatembea kwa uchovu, anapokwenda bado ni mbali, lakini hajakata tamaa. Anazidi kutembea akiwa na simanzi tele moyoni.

    Huyu ni Davina, msichana mrembo mwenye mvuto wa kutosha, ambaye mwanaume yeyote aliyekamilika anaweza kushawishika kuwa naye. Matatizo aliyokuwa nayo yalikuwa makubwa kuliko umri wake, kwa kumwangalia tu, utagundua hajafikisha miaka 27! Ni binti mdogo sana, lakini yupo kwenye mateso makali.

    Baada ya mwendo mrefu sana, akaanza kuona nyumba kwa mbali katika kijiji kilichokuwa mbele yake. Kwa bahati nzuri, akapita kijana mmoja aliyekuwa akiendesha baiskeli. Akamsimamisha.

    “Habari yako?” Davina akasalimia.

    “Salama, vipi hali yako?”

    “Njema...samahani kaka...”

    “Usijali dada yangu, unasemaje?”

    “Unakwenda Baura unipe lifti?”

    “Hapana, naishia Kisewi.”

    “Hata hapo patanitosha, utakuwa umenisogeza kidogo.”

    “Twende.”

    Davina akaketi kwenye kiti cha baiskeli kisha akaweka begi lake kichwani, baiskeli ikaondoka taratibu. Moyoni alitamani sana yule kijana amfikishe nyumbani kwao lakini kwa sababu alikuwa haelekei huko alishindwa kuelewa atamshawishi vipi ili amkubalie.

    “Mimi naitwa Mathayo, sijui wewe mwenzangu?”

    “Davina.”

    “Davina? Jina zuri sana.”

    “Nashukuru hata wewe pia.”

    “Umesema unaishia Kisewi, huwezi kunisaidia kuniwahisha nyumbani jamani, maana nimechoka sana!”

    “Hapana...kama nilivyokuambia awali, halafu isitoshe nimeagizwa vitu muhimu na wazee.”

    “Basi nitakupa soda!”

    “Shilingi ngapi?”

    “We’ unataka ngapi?”

    “Elfu mbili!”
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitakupa tano!”

    “Sawa.”

    Kilikuwa kiasi kikubwa sana cha pesa kwa Mathayo, kwa Davina halikuwa jambo la kufikiria mara mbili, alichohitaji ilikuwa ni kufikishwa nyumbani kwao haraka. Kwanza alikuwa amechoka, lakini mbaya zaidi alikuwa katika matatizo makubwa sana ambayo ufumbuzi wake ulikuwa nyumbani kwao.

    Baada ya mwendo kidogo, baiskeli ilifunga breki nje ya boma la akina Davina. Akashuka na kumlipa yule kijana pesa yake, akamshukuru na kuagana naye. Akaingia ndani akianza kulia. Sauti ya kilio chake ndiyo iliyowachanganya watu waliokuwa ndani. Wa kwanza kutoka alikuwa ni mama yake.

    Akampokea, naye bila kuuliza sababu za kilio cha mwanaye, akaanza kulia. Baba yake Davina akatoka haraka na kuwapokea, akawakaribisha kwenye jamvi chini ya mnyaa.

    “Vilio havitasaidia kitu, kama hamtasema kwanza kinachowaliza!” akasema.

    Hakuna aliyejibu.

    “Mama Davina, kuna nini?”

    “Sijui...nimempokea mtoto akilia, nashindwa kuelewa amepatwa na tatizo gani?”

    “Sasa kama hujui tatizo, kwa nini unalia?”

    “Ningefanyaje kama mwanangu mwenyewe analia? Namjua vizuri sana Davina, asingemwaga machozi yake kama hana matatizo!”

    “Hata hivyo siyo suluhisho, vipi mwanangu? Hebu tuliza kwanza moyo, unieleze vizuri ni nini tatizo?” mzee Ngamseni akasema kwa sauti ya kusihi.

    “Nateseka baba, kila siku nimekuwa wa kulia, nitaishi hivi hadi lini?”

    “Lakini kuteseka kuna chanzo mwanangu, hebu niambie kwanza, tatizo ni nini?”

    Davina hakuzungumza neno, akafungua zipu ya pembeni ya begi lake kubwa, akatoa pochi yake ya mkononi. Akafungua akiwa anaanza kulia kilio cha kwikwi, akatoa bahasha moja ya khaki kisha akaifungua na kutoa barua. Akampa baba yake.

    Mzee Ngamseni akaikunjua, bila kuuliza chochote, akaanza kuisoma. Hakuwa na haja ya kusoma ilipotokea, alikwenda moja kwa moja kwenye barua yenyewe! Akaanza kuisoma kimya kimya.

    Ilisomeka hivi;

    Kwako Davina.

    Nilikupenda sana na bado ninakupenda. Wewe na ulimwengu wote unatakiwa kuendelea kufahamu kwamba, bado nakupenda. Nimekufa na penzi lako na ninatesekea penzi lako. Naumia kukupoteza mpenzi wangu, lakini nasikitika kwamba, kifo changu hakikuwa cha kawaida.

    Kilipangwa! Tena kimepangwa na binadamu ambaye siku moja atakufa kama mimi, ameamua kufanya hivyo kwa masilahi yake, lakini nakuhakikishia, hawezi kufahanikiwa kamwe. Nafikiri unakumbuka kuwa mimi siyo wa kukubali kushindwa kirahisi!

    Unakumbuka jinsi nilivyokupata kwa shida, halafu leo hii anakuja mtu kujaribu kuniingilia. Jambo hili haliwezekani na wala sitaliruhusu liwezekane. Naomba kukuahidi jambo moja; kuliko huyo mpuuzi awe na wewe, ni bora nikuchukue uje kuishi na mimi huku kuzimu.

    Hili nitalitekeleza, muda mfupi ujao.

    Kumbuka kwamba mimi ni mtu wa kusimamia mambo yangu vizuri. Hili pia nitalisimamia! Nakutakia maisha mema, yenye maandalizi mema ya kuja huku kuzimu nilipo. Nakupenda na sitakuacha.

    Wako akupendaye,

    Jeff.



    Mzee Ngamseni akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu sana. Akawatizama Davina na mkewe kwa zamu, kisha akaangalia chini. Kimya cha dakika kadhaa kikapita, hakuna aliyezungumza, ingawa mzee Ngamseni alionekana dhahiri kuwa na kitu anataka kuzungumza, lakini hakufanya hivyo.

    Wakabaki wanatizamana kwa muda mrefu sana. Mama anamtazama mwana, mtoto anatizama baba na baba anamtizama mkewe!

    Wanatizamana.

    Mpaka wakati huo, mama yake na Davina alikuwa hafahamu chochote juu ya kilichokuwa kikiendelea.

    Ni Davina na baba yake tu, ambaye aliisoma barua ile ndiyo waliokuwa wakifahamu. Woga tele ukatanda. Baada ya kufikiria kwa muda mrefu sana, mzee Ngamseni akamgeukia mwanaye na kumwambia...

    “Mbona sielewi-elewi?”

    “Ndiyo hivyo baba!”

    “Inaonekana aliyeandika hii barua ni marehemu siyo?”

    “Ndiyo!”

    “Enhee ni nani?”

    “Jeff!”

    “Jeff...!!!”

    “...ndiyo baba ni Jeff, yule kijana niliyewapa taarifa kwamba anataka kunioa.”

    “Si alikufa?”

    “Ndiyo baba, lakini nashangaa pamoja na kwamba amekufa, ameniandikia barua!”

    “Haiwezekani...kuwa na akili mwanangu, tangu lini mtu aliyekufa akaandika barua? Aliyekufa, amekufa...hana uwezo wa kufanya lolote, hana nguvu ya uhai, sasa amekuandikia vipi? Usijichanganye kwa mambo madogo yasiyo na maana.”

    “Yana maana baba, naujua vizuri sana mwandiko wa marehemu Jeff, ndiyo huu. Haya mambo siyo ya mzaha baba, mwenyewe naogopa sana.”

    “Huna haja ya kuogopa mwanangu, mtu ambaye anataka kukutisha, hashindwi kukuandikia barua na kujifanya ndiye Jeff... lazima kuna mtu anajaribu kukuchezea.”

    “Basi na awepo, lakini hata saini yake ni ile ni ile! Nani anaweza kuandika barua kwa kuiga mwandiko wa mtu pamoja na saini yake? Mimi sina imani na hilo kabisa wazazi wangu.”

    “Lakini bado anaweza kughushi tu mwanangu, watu wanaghushi vitu vingapi, ije kuwa sahihi? Kumbuka kuwa unaishi Dar es Salaam mama, sehemu ambayo ina kila kitu na kila aina ya watu, watu wa mjini wajanja sana mama.

    “Mh! Baba...mbona naona kama huchukulii uzito hili suala? Sikiliza baba, hebu ona hii barua, ona muhuri wa mahali ipotokea, angalia na anwani zake. Zimeandikwaje?” Davina akasema kwa ukali akiwa anatetemeka.

    Mzee Ngamseni akaikunjua ile barua kwa mara nyingine, taratibu akasoma anwani za mwandishi wa barua ile. Ilisomeka hivi;



    JEFF SEBASTIAN,

    PRIVATE BAG,

    KUZIMU MJINI.



    Mzee Ngamseni akashtuka sana!

    Davina hakuzungumza neno, akatoa bahasha aliyokuwa ameirudisha kwenye begi. Akampatia baba yake, mzee Ngamseni alielewa kabisa alichokuwa akimaamisha mwanaye. Alitakiwa kusoma muhuri wa Kituo cha Posta ilipotokea barua hiyo.

    Yaliandikwa maneno kwa herufi kubwa yenye rangi nyeusi, yaliyosomeka;



    MAKAO MAKUU YA POSTA,

    PRIVATE BAG,

    KUZIMU.



    Mzee Ngamseni akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu. Akaonekana kuwaza jambo fulani, ambalo hakutaka kulizungumza. Akameza funda moja kubwa la mate, kisha akaanza kuzungumza.

    “Lakini si ulisema Jeff alikufa?”

    “Ndiyo baba!”

    “Unajua maana ya kufa?”

    “Ndiyo...nafahamu...!!!”

    “Ni nini?”

    “Ni ile hali ya kupoteza pumzi ya uhai, roho kuachana na mwili!”

    “Kwa hiyo roho ya Jeff imeachana na mwili wake siyo?”

    “Ndiyo baba!”

    “Amekufa si ndiyo?”

    “Hata kwenye mazishi yake nilikuwepo, nilishuhudia akifukiwa mbele ya macho yangu. Kifupi naamini Jeff amekufa!”

    “Kama hayo yote uliyoyasema ni sawa, basi tambua kwamba hakuna marehemu anayeweza kuandika barua, acha ujinga,” Mzee Ngamseni akasema akisimama na kuondoka zake.

    “Lakini baba...”

    “Lakini nini? Usiwe na akili pungufu kiasi hicho binti yangu, rudi zako mjini, ukaendelee na kazi, acha kupoteza muda wako. Wajanja wanataka kucheza na akili yako!” mzee Ngamseni hakuzungumza kitu, mguu wa kwanza, mguu wa pili anaondoka zake.

    Alikuwa anakwenda kilabuni.

    Huku nyuma akaacha kilio cha mama na mwana!

    ***

    Siku hiyo ilikuwa ngumu sana kwa Gerald, ofisi haikukalika! Kila alichokifanya alihisi kama anakosea. Alikuwa mchovu kuliko kawaida. Siku nzima hakuna alichokifanya zaidi ya kuchukua faili na kupekua-peua kisha kulirudisha mahali pake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa amechoka kupindukia! Saa 9:30 mchana aliamua kuondoka zake, kwanza hakuwa na cha maana cha kufanya. Akatoka na kwenda kwenye gari lake, akaingia. Mara akajishangaa anakosa mahali pa kwenda!

    “Nakwenda wapi?” akajiuliza mwenyewe bila kupata majibu.

    Akabaki anapiga-piga usukani wa gari lake bila kupata muelekeo.

    “Yeah! Nimekumbuka, acha nipitie kwanza Posta nikacheki barua,” akajisemea mwenyewe moyoni mwake.

    Ni wiki ya tatu sasa alikuwa hajapita Posta kuangalia barua. Akawasha gari na kuondoka kwa mwendo wa kasi sana. Muda mfupi baadaye alikuwa Posta, akafungua sanduku lake na kutoa barua, hakuwa na haraka ya kuziangalia, akaingia kwenye gari na kwenda zake nyumbani.

    Alipofika tu, alifikia sebuleni ambapo alianza kutizama barua moja baada ya nyingine. Alipofikia bahasha hii ya khaki, iliyoandikwa kwa kalamu ya rangi nyekundu, akashtuka sana.

    Hakushtushwa na bahasha wala rangi ya wino uliotumika. Alishtushwa na muhuri wa mahali ilipotoka. Barua ile ilikuwa na muhuri wa kuzimu! Akaifungua haraka, anwani ya mwandishi nayo ikamchanganya!

    Ile barua ilitoka kwa Jeff, rafiki yake wa siku nyingi, ambaye alifariki miezi kadhaa iliyopita. Jeff yule yule anayemsumbua Davina kwa barua yake yenye maneno makali ya kutisha.

    Gerald akaanza kuisoma barua ile kimya kimya. Kila neno alilolisoma, alihisi kuchanganyikiwa. Akajikuta anapiga kelele...

    “MZIMUUUUUU....”

    Gerald alizidi kutetemeka. Woga ukamtanda. Ghafla akaamua kunyamaza. Akawaza inakuwaje Jeff rafiki yake ambaye alifariki, tena alishuka mpaka kaburini na kupokea jeneza lake, aandike barua?

    Lilikuwa swali zito sana, ambalo kwa akili zake mwenyewe asingeweza kujijibu. Moyo wake ukazidi kwenda mbio, akapoteza furaha yake kabisa.

    “Lakini haiwezekani bwana, siwezi kuchanganyikiwa na kitu kidogo kama hiki, yaani mtu aliyekufa anaandika barua? Haya yatakuwa maajabu ya mwaka...acha ninywe zangu pombe, nipumzike...” Gerald akawaza akienda kwenye jokofu na kutoa chupa mbili za bia.

    Akaanza kunywa kwa fujo!

    Alikunywa sana siku hiyo akiamini alikuwa anapoteza mawazo. Alipofika bia ya kumi alijikuta akipitiwa na usingizi pale pale sebuleni. Aliposhtuka ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri! Amevimba mwili mzima kwa kung’atwa na mbu!

    Hakuwa na kumbukumbu yoyote ile, lakini alipotupa macho yake mezani, akaona ile barua. Akakumbuka kila kitu. Akaivuta na kuanza kurudia kuisoma. Machozi kama maji yakaanza kutiririka machoni mwake.

    Ile barua ilimuumiza sana, kama ni kweli ilikuwa imetokea kwa Jeff, ilikuwa na hatari sana kwake, lakini hata kama siyo kweli, kwa nini atishiwe kiasi kile? Kwa mara ya tatu sasa, anarudia kusoma ile barua. safari hii akaisoma kwa sauti ya chini.

    Ilikuwa barua yenye maneno makali sana. Maneno ya kuumiza na kuchoma moyo. Maneno ya kukatisha tamaa ya maisha. Barua yenyewe ilisomeka hivi;



    Kwako mpendwa Gerald.

    Salaam!

    Nilikupenda sana rafiki yangu Gerald, lakini sasa nakuchukia sana! Naomba ufahamu kuwa, kuanzia unaposoma barua hii, ujue kwamba wewe ni adui yangu namba moja! Nakuchukia kwa sababu mbili; Mosi, kusababisha kifo changu na pili, kwa sababu unanichukia.

    Labda nikukumbushe kidogo, unajua vizuri sana jinsi ninavyompenda Davina, unajua sana! Tuachane na hilo, najua unafahamu kwamba Davina ni mwanamke mzuri mno, lakini mwanzoni hakuwa hivyo, nilimkuta akiwa hana matunzo, na ni mimi ndiye niliyehakikisha Davina anakuwa kama alivyo leo!

    Mimi ndiyo nimempendezesha hadi ukajikuta umeshawishika kunisaliti. Usivyo na roho ya kibinadamu, ukaona unitoe duniani kabisa, umefanikiwa rafiki, lakini damu yangu haitapotea bure brother. Nitafanya kitu kama kisasi kwa uliyonifanyia. Fahamu kuwa umeniua nikiwa na malengo mengi sana na Davina wangu, nilikuwa nakaribia kumuoa, lakini wewe umekatisha ndoa yetu. Ukaniua.

    Kwa barua hii, nakutaka uachane kabisa na mpango wako wa kumuoa Davina. Nina ushahidi wa asilimia mia moja, kuwa wewe ndiye uliyepanga kifo changu, umefanikiwa! Kufanikisha kwako unyama huo, hakumaanishi kwamba nia yako ya kumuoa Davina imetimia...

    Hujafanikiwa!

    Na hutafanikiwa!

    Davina ni mwanamke ambaye nampenda kwa moyo wangu wote. Hawezi kufunga ndoa na mtu mwingine yeyote zaidi yangu! Kwa taarifa yako, ahadi hiyo lazima itimie.

    Hivi karibuni, nitamchukua Davina na kumleta huku kuzimu ambapo nitafunga naye ndoa na kuishi naye milele huku, kama tulivyoahidiana mwanzoni. Kwa kifupi, acha kumfuatilia, ukikaidi na wewe pia nitakuchukua uje huku kuzimu ili tupambane vizuri.

    Kaka, ni bora nilipize kisasi ukiwa huko huko duniani ambapo sikuoni, kuliko nikuchukue uje huku ambako nitakuwa nakuona! Lakini adhabu yako inaweza kupungua kama utaacha kumfuatilia Davina.

    Najua bado hujamwambia kama unampenda, na sasa hivi amesafiri, amekwenda Kondoa. Nakushauri usifanye hivyo. Mwache mpenzi wangu tafadhali. Kumbuka kwamba, naandika barua hii, kwa baraka zote za mizimu ya babu zangu ambao nimekutana nao huku. Hawa wameahidi kunisaidia, iwapo wataona nashindwa kukudhibiti. Unaweza kuona ni jinsi gani vita ilivyo kubwa na hatari.

    Gerald wewe si mgeni kwangu, unanijua vizuri sana hasa ninapokuwa nimeamua kusimamia mambo! Hili pia nitalisimamia mpaka mwisho. Usije ukajidanganya kwamba huu ni mzimu wangu!

    Hapana rafiki.

    It’s me,

    Jeff.

    Gerald alirudia kusoma ile barua zaidi ya mara tano, maneno hayakubadilika. Yalikuwa yale yale. Akatizama na anwani ya mwandishi kwa mara nyingine.

    Ilikuwa ile ile!

    Akageuza bahasha na kuangalia muhuri wa ilipotokea, ulikuwa ule ule!

    Akahisi kuchanganyikiwa!

    Kilichomchanganya zaidi ni jinsi anavyoandika, mwandiko na sahihi. Kila kitu ilikuwa ni Jeff. Kwa vyovyote vile, barua ilikuwa imetoka kwa Jeff, lakini swali la msingi ambalo lilizidi kuutibua ubongo wake lilikuwa ni; Marehemu anaweza kuandika barua?

    “Shiiiiiit...nitajua la kufanya...mtu mzima hatishiwi nyau bwana. Iwe ni kweli Jeff kaandika, isiwe kweli, nitajua la kufanya. Kubwa zaidi, siwezi kuacha kumfuatilia Davina, mwanamke anayeutesa moyo wangu.

    “Mimi ni Gerald, mwanaume wa shoka, najiamini na nasema wazi kwamba, Davina ndiye mke wangu. Aliyekufa amekufa, lake halipo tena,” maneno haya yalizunguka kichwani mwa Gerald akijipa-piga kifua.

    Akaingia chumbani kulala.

    ***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kilabuni, mzee Ngamseni alijaribu kushauriana na wazee wenzake juu ya tatizo la mwanaye. Ukaibuka mjadala! Wapo walioona ni tatizo, wengine waliona kama anafanyiwa mchezo.

    “Hakuna mzimu wa hivyo Ngamseni rafiki yangu, tena umesema tukio lenyewe limetokea Dar es Salaam, kwa wajanja? Mwambie binti yako atulie, asiwe na wasiwasi, kuna mtu anamchezea tu,” mzee Mbwingira, rafiki wa karibu na mzee Ngamseni akamwambia.

    “Lakini inawezekana ikawa kweli, hili siyo suala la kufanyia mchezo, kama inawezekana ufanyike mtambiko haraka, tuongee na mizimu mtoto arudi mjini kwa amani,” mzee Biso akadakia.

    “Achana na mambo hayo mzee Biso, hakuna mtama na uwele wa kuchezea na hata kondoo na mbuzi pia, kifupi kuna watu wanataka kumchezea binti yetu. Sikiliza mzee mwenzangu, mshauri mtoto atulie, arudi mjini,” mzee Mbwingira alizidi kushikilia msimamo wake.

    “Hata mimi naona hivyo,” mzee Ngamseni akaunga mkono.

    Siku zote aliheshimu sana mawazo ya wazee wenzake, ni hao ndiyo walikuwa msaada kwake katika mashauri mbalimbali. Kwa kupitia mawazo yao, alifanikisha mambo mengi. Hata katika suala la Davina, aliamua kufanyia kazi mawazo yao.

    Alifika nyumbani na kuwakuta mama na bintiye wapo katika hali ya majonzi makubwa, binti aking’ang’ania mtambiko! Busara ya mzee Ngamseni ilihitajika sana, akaitumia vizuri. Baadaye wakamwelewa. Safari ya kurudi mjini ikapangwa!

    Siku tatu baadaye Davina alikuwa kwenye basi anarudi Dar es Salaam.

    Hawazi barua!

    Wala Jeff.

    ***

    “Hivi Halima ulikuwa unakumbuka kwenda Posta kweli mdogo wangu, tangu nimekwenda Kondoa?” hili lilikuwa swali la kwanza kabisa, Davina kumuuliza housegirl wake mara baada ya kufika nyumbani kwake Tandika anapoishi.

    “Ndiyo dada, tena kila siku...”

    “Umepata barua?”

    “Ndiyo!” Halima akajibu huku akifungua droo moja katika kabati maalum la vitabu na kutoa barua tisa na kumkabidhi.

    Haraka, Davina akaanza kufungua moja baada ya nyingine akiangalia majina ya watumaji. Kati ya barua zile tisa, tatu zilikuwa za Jeff. Akaanza kuisoma barua ya kwanza...

    Iliandikwa hivi; Mpenzi wangu wa moyo Davina.

    Nilikupenda, nakupenda na bado nitaendelea kukupenda daima.

    Pole na safari mpenzi. Najua kwa nini ulifunga safari kwenda Kondoa. Usiendelee kusumbuka mpenzi, huu siyo mzimu wangu, ni mimi mwenyewe Jeff.

    Kama nilivyokuambia awali, ahadi yangu ya ndoa iko pale pale! Ila kutakuwa na mabadiliko kidogo, ndoa yetu ifafungwa huku kuzimu badala ya duniani kama tulivyopanga.

    Mimi pia sikupenda hili litokee, lakini mtu mmoja mwenye roho ya kinyama amesababisha haya. Sitakutajia leo wala kesho, siku ukija huku ndiyo nitakuambia ni nani mtu huyo.

    Endelea kujiandaa mpenzi, siku si nyingi nitakuja kukuchukua.

    Nikupendaye kwa dhati,

    Jeff Sebastian.



    Davina akabaki ameduwaa! Akaanza kutetemeka. Akajikuta anapiga kelele...

    “JEFF MPENZI WANGU, KWA NINI UNANITESA?”

    Machozi ndicho kitu pekee ambacho kingeweza kumpunguzia machungu Davina. Alilia sana. Akili yake haikukaa sawa. Barua za vitisho kutoka kwa marehemu Jeff zilizidi kumchanganya!

    Marehemu kuandika barua siyo jambo jepesi, ambalo linaweza kuchukuliwa ki-wepesi kiasi kile! Lilikuwa jambo zito ambalo ufumbuzi wake pengine ungehitaji wanajimu!

    Kwa binti mdogo kama Davina, hakika asingeweza kujua mambo hayo, asingeweza kufanya chochote kile bila ya uangalizi ulio sahihi na makini. Uangalizi huo usingeweza kupatikana mahali popote zaidi ya kwa wazazi wake!

    Baba yake!

    Ni baba, kwa sababu mwanaume wa Kiafrika ndiye kichwa cha nyumba. Maamuzi yake huwa ya mwisho na hakuna ambaye anaweza kuyayumbisha!

    Alipofika hapo, akazidisha kilio zaidi, alifanya hivyo kwa sababu baba yake, ambaye ndiye agetakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha jambo lile linaisha, ndiye ambaye anapingana naye kwa asilimia mia moja!

    Haamini mizimu!

    Haamini uchawi!

    Davina anazidi kuchanganyikiwa!

    “Nikimbilie wapi mimi jamani? Kama baba yangu mwenyewe ambaye ndiye mwenye uwezo wa kunisaidia anakataa na anasema wazi kuwa haamini mizimu? Lakini siyo haamini, bali haamini kabisa juu ya hili jambo...

    “Anaweza kuwa sahihi kidogo, lakini kwa nini hataki kuishughulisha akili yake zaidi ya hapo? Kweli kuna marehemu ambaye anaweza kuandika barua kweli? Kwa nini hawezi kuona hili tatizo?!!” Davina anajisemea maneno haya akizidisha kilio.

    Halima, msichana wake wa kazi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu akisikiliza kilio cha bosi wake, sasa ameshindwa kuvumilia. Anajisogeza kichovu hadi kwenye mlango wa chumba cha Davina.

    Hakuwa na haja ya kugonga, akaingia moja kwa moja hadi chumbani. Akamkuta Davina akizidi kulia, akiwa amekumbatia bahasha ya khaki. Kwa haraka, Halima akajua ilikuwa ni taarifa za msiba.

    “Kuna nini dada?” Halima akamwuliza dada yake, akiwa ameketi chini akimtizama kwa huruma.

    “Niache tu, Halima mdogo wangu, niache...”

    “Kwa nini nikuache? Kuna nini kwani dada’ngu?”

    “Jeff!”

    “Jeff kafanyaje tena?”

    “Kaandika barua zingine, tena tatu...nimeshasoma moja, anaendelea kusisitiza atakuja kunichukua hivi karibuni!”

    “...sikiliza dada, hebu kwanza nyamaza kulia. Tuliza moyo kwanza...unajua sasa naanza kuingiwa na wasiwasi juu ya hili jambo. Nadhani tunatakiwa kufanya kitu fulani kwanza.

    “Nahisi kuna kamchezo kanachezwa, utakuwa unalia na kujiumiza kumbe kuna watu wanafanya mambo yao...lakini naona kabisa njia ya kupata ukweli,” Halima akasema kwa utulivu sana.

    “...anaonekana anajua jambo fulani huyu, acha nimsikilize...” akawaza Davina na kusema: “Kwani mdogo wangu, we’ ulikuwa unafikiri kuna nini?”

    “Siyo rahisi kusema moja kwa moja nafikiri nini, lakini naweza kushauri kitu kwa ajili ya kuutafuta ukweli. Nenda Posta, uonane na uongozi, waeleze juu ya jambo hili, halafu waombe barua zote zitakazotumwa, zisiingizwe kwenye sanduku letu moja kwa moja, zihifadhiwe mahali maalum, ambapo tutakuwa tunazifuata hapo...” Halima akashauri.”

    “Halafu?”

    “Wakati huo tutakuwa tunaendelea kufungua sanduku letu kama kawaida, ikiwa zile barua ni za miujiza, zitaendelea kuingia lakini kama ni mchezo, basi hapo mchezaji atakuwa amenasa, maana hakutakuwa na barua kwenye sanduku letu, isitoshe hata Uongozi wa Posta utakuwa na taarifa kuwa barua zote zinafikia sehemu maalum na siyo kwenye sanduku. Naona huu unaweza kuwa mwanzo wa kuelekea kwenye kuupata ukweli,” alisema Halima kwa utulivu sana akionekana kupangilia vyema hoja yake.

    Davina alimwangalia yule binti akiwa haamini kabisa kuwa maneno yale yalikuwa yanatokea kwenye kinywa chake. Hakuamini kama Halima angeweza kuwa na maneno yenye akili kama yake. Akasimama kisha akamkumbatia kwa furaha.

    “Ushauri wako umenipa nguvu, unaweza kusaidia kuujua ukweli. Nitafanya hili zoezi kesho asubuhi, halafu kesho hiyo hiyo narudi Kondoa, lakini nikirudi nitafaya kitu kwa ajili yako...” Davina alimwambia Halima.

    “Nitashukuru sana dada...nitafurahi sana.”

    “Anza kufurahi mapema, amini kwamba umenifungua. Ahsante sana Halima, nashukuru sana.”

    “Usijali dada, ni wajibu wangu, sehemu ya kazi yangu. Wewe ni dada yangu, inanipasa kukusaidia ushauri pale inapobidi, hasa katika mambo mazito kama haya,” Halima akamwambia Davina.

    Davina akaingia bafuni, baadaye akarudi chumbani kubadili nguo, kisha akajongea sebuleni na kuanza kuangalia filamu. Aliisubiria kesho kwa hamu kubwa sana.





    ***

    Gerald aliamka asubuhi akiwa na nguvu mpya, hata akili yake ilikuwa mpya. Hakuwa amelewa kama jana yake, Gerald huyu ni mpya na mzima wa afya njema. Barua ya Jeff ikarudia upya kichwani mwake.

    Ikafunguka ubongoni mwake na kuanza kuisoma. Alipofikia sehemu iliyoandikwa kuwa Davina alikwenda Kondoa, akachanganyikiwa kidogo. Kwake ilikuwa nafasi ya kuweza kuanza kutafuta ukweli wa ile barua.

    “Yap! Hapa hapa nitaujua ukweli, nampigia Davina sasa hivi,” akawaza Gerald huku akibonyeza namba za Davina na kupeleka simu sikioni.

    Muda mfupi tu, baadaye Davina akapokea...

    “Vipi shem Gerald, za siku mwanya?” sauti laini ya Davina ikasikika.

    “Salama, enhee hebu niambie, uko wapi?”

    “Town, naelekea Posta!”

    “Posta? Kufanya nini jamani wakati una msichana wako wa kazi?”

    “Ni special case Gerald, lazima niende mimi!”

    “Special case? Sipaswi kujua?”

    “Ni habari ndefu shemeji yangu, lakini fahamu kwamba Jeff ananisumbua sana...nafikiri tukionana nitakueleza vizuri zaidi!”

    “Jeff anakusumbua kivipi? Shemeji yangu unaanza kuzeeka vibaya! Jeff si tumemzika?” Gerald alitamka maneno hayo kwa ujasiri, lakini moyoni mwake akiwa na wasiwasi mwingi sana na hamu ya kutaka kujua kitakachofuata.

    Alianza kuhisi kuwa Davina naye aliandikiwa barua. Alihitaji sana kuujua ukweli zaidi.

    “Ndiyo maana nimekuambia tukikutana tutaonana.”

    “Lini sasa, maana umenishtua sana!”

    “Wiki ijayo.”

    “Kwa nini isiwe leo?”

    “Nina safari asubuhi hii baada ya kutoka Posta, nakwenda Kondoa...nimetoka huko jana tu, lakini nalazimika kurudi tena leo, sababu ni hiyo ya Jeff kuniandikia barua, nachanganyikiwa sana shemeji yangu,” Davina alisema kwa sauti iliyojaa majonzi.

    Gerald alihisi kuchanganyikiwa. Hapo akajua kwamba ni marehemu Jeff alikuwa akiandika barua. Akakata simu.

    Kitendo cha Davina kumthibitishia kwamba ni kweli alikwenda Kondoa siku za karibuni na siku hiyo pia alikuwa njiani kwenda huko baada ya kutoka Posta alipokwenda kwa mambo yake binafsi, kilimchanganya sana Gerald!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alibaki ameishikilia ile simu asijue la kufanya. Moyo wake ukaingiwa na ubaridi mkali, akahisi kama kizungu-zungu kikali. Akajitupa kitandani. Barua ya Jeff ilimchanganya sana, lakini kubwa zaidi ambalo lilimtisha ni kwamba, kifo cha Jeff kilikuwa cha siri kubwa sana. Ni kweli yeye ndiye chanzo.

    Muuaji!

    Ni yeye ndiye aliyepanga njama zote za kifo cha Jeff na ni kweli kwamba alifanya hivyo ili aweze kumpata Davina kirahisi! Alishawishika kufanya hivyo kutokana na penzi lao kuwa motomoto na lisilo na dalili za kuvunjika kirahisi.

    Njia pekee ambayo ingemsaidia kumpata Davina ilikuwa ni kumuondoa Jeff duniani! Jambo lilo likapangwa katika vikao vya siri na wakafanikisha kwa asilimia mia moja!

    Hakuna mtu aliyegundua jambo hilo, lakini kuandikiwa barua na Jeff, tena kwa mwandiko wake mwenyewe na kuelezea tukio zima lilivyokuwa, kulimpa mashaka sana.

    Akili ikachemka...

    “Natakiwa kufanya jambo lingine zaidi. Sitakiwa kuwa mjinga wa kiwango kikubwa kiasi hiki, kuna mtu aidha ananisaliti au alinisaliti...yes I think so! I have to do something to prove it. I’m Gerald...” Gerald akajikuta akitamka kwa sauti ya juu akipiga-piga kifua chake.

    Akachukua simu yake, akitaka kupiga namba fulani, lakini kabla hajafanya hivyo, simu yake ikaita. Macho yakaganda kwenye kioo baada ya kuona jina la Davina. Akajishauri sana, lakini mwisho wake akaamua kupokea.

    “Yes shem...” Gerald akasema.

    “Vipi ulikata simu au ilikatika?”

    “Bwana wangu! Mitandao yenyewe hii ya mjini...ilikatika. enhee niambie!”

    “Ndiyo kama nilivyokuambia shemeji yangu, yaani nimechanganyikiwa sana, nafikiri nitakuwa na mambo mengi ya kuzungumza na wewe nikirudi Kondoa,” Davina akasema kwa sauti ya upole sana.

    Gerald akashtuka.

    Mambo mengi?

    Moja kwa moja Gerald akafikiri inawezekana katika barua alizotumiwa na Jeff, amemtaja!

    “Ni juu ya hii issue ya barua za Jeff?”

    “Ndiyo!”

    “Mbona maajabu lakini? Enhee, hivi ameandika nini hasa kwenye hizo barua zake?” Gerald akauliza kimitego, akihitaji kujua kitu zaidi.

    “Vitisho tu...sijui eti anataka kuja kunichukua...ah, nimechoka sasa, lakini nikirudi Kondoa nitakutafuta. Sitegemei kukaa muda mrefu sana.”

    “Sawa, safari njema.”

    “Ok! Ahsante sana.”

    Wakakata simu zao.

    Jeff alibaki ameishikilia ile simu kwa muda mrefu sana, baadaye akakumbuka kufanya mambo mawili muhimu. Kwanza kabisa alitakiwa kukaa kikao na wale jamaa wote waliokuwa wanashughulikia mauaji ya Jeff, pili, alitakiwa kumtaarifu meneja wake kwamba hatafika ofisini siku hiyo, ili akaimu nafasi yake. Kwanza, akampigia meneja.

    “Nina dharura, sitafika ofisini leo, pengine na hata kesho. Endelea na majukumu yako kama kawaida na viporo vyangu vilivyopo ofisini kwangu, lakini kumbuka usiruhusu malipo yoyote wiki hii, kazi njema Edward,” Gerald aliongea kwa sauti tulivu, iliyoonyesha kuwa ana jambo zito lakini lisilohitaji ushauri wa mtu yeyote.

    “Nimekuelewa bosi.”

    Gerald akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha kwa mkupuo huku akitembeza macho yake kila kona ya chumba chake nadhifu. Akabonyeza namba za Fikiri, Mkuu wa Kikundi cha Kigaidi cha Nyamangumu, lakini alizoeleka zaidi kwa jina la Master. Huyu ndiye aliyeongoza zoezi zima la mauaji ya Jeff.

    “Master unanifahamu vizuri nilivyo makini na mambo yangu, lakini kama kuna mambo ambayo nayachukia zaidi duniani, basi ni USALITI!” Hivi ndivyo Gerald alivyoanza kuzungumza, baada ya Master kupokea simu.

    “Unamaanisha nini mkubwa?”

    “Saa 2:00 usiku wa leo, nahitaji kukutana na wewe pamoja na jopo zima lililoshughulikia kifo cha Jeff. Ni muhimu sana, zingatia tafadhali!”

    “Wapi?”

    “Pale pa siku zote!”

    “Shwari!”

    ***

    “Kwa nini umeamua kufanya hivi?” Meneja Mkuu wa Posta akamwuliza Davina, baada ya kumweleza nia yake ya kuzuia barua zisiende moja kwa moja kwenye sanduku lake.

    “...ni habari ndefu sana bosi, unaweza kustaajabu kidogo. Iko hivi....” Davina akamsimulia kila kitu.

    Meneja akachanganyikiwa!

    “Unahisi kuna mtu wetu labda anatumiwa kukuchezea?”

    “I’m not sure, lakini nafikiri tujaribu kufanya hivi kwanza, tunaweza kugundua kitu fulani. Nina safari asubuhi hii, baada ya wiki moja nitakuwa nimerudi, hapo ndipo tutakapojua kitu fulani,” Davina akasema.

    “Ok! Hakuna tabu katika hili, ukirudi tuwasiliane.”

    “Ahsante sana.”

    Davina akatoka nje ya Posta, akachukua taxi iliyompeleka Kariakoo, mtaa wa Kamata, zilizopo ofisi za basi la Scandinavia.

    ***

    Saa 12:00 za jioni, basi la Scandnavia liliingia mjini Dodoma, ikiwa ni safari ya saa sita kutokea Dar es Salaam. Davina alishuka akiwa mchovu sana. Kwa muda huo haikuwa rahisi kupata usafiri wa Kondoa, hata kama angepata isingekuwa rahisi kufika Baura kwa miguu, akipita kwenye mapori peke yake, tena mwanamke!

    Akaamua kulala pale Dodoma.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akatafuta hoteli nzuri, akapumzika kwa maandalizi ya kwenda Baura, Kondoa, asubuhi inayofuata.

    Saa 7 na dakika zake za usiku, akiwa katika usingizi mzito, akasikia simu yake ikiita, akapuuza akidhani huenda alikuwa ndotoni. Simu ikaita hadi ikakatika. Baada ya muda ikaanza kuita tena, akaamka na kutizama kwenye kioo cha simu.

    Hapakuwa na namba!

    Ilikuwa ni private!

    Akapokea...

    “Haloo...” Davina akaongea kwa uchovu sana.

    “Yes mpenzi wangu Davina...pole kwa uchovu wa safari, lakini nakushangaa sana ni kwa nini hutaki kusikiliza maagizo yangu?” ilikuwa sauti ya taratibu sana, ambayo hakuifahamu mapema, lakini kila muda ulivyozidi kusogea, ndivyo alivyozidi kuikumbuka vizuri ile sauti.

    Ilikuwa sauti ya Jeff.

    “Nani mwenzangu?” Davina aliuliza kwa sauti ya juu, iliyojaa woga na kavu, macho akiwa ameyatoa kuliko kawaida.

    “Usiniambie umeshaisahau hii sauti mpenzi, Jeff hapa nazungumza kutoka kuzimu...”

    “What?”

    “Jeff...narudia tena kukuonya, fuata maagizo yangu tafadhali, acha ubishi usio na maana. Kwa nini unakuwa mgumu kuelewa? Sasa Kondoa unakwenda kufanya nini? Unapaswa kusubiri hadi nitakapokuja kukuchukua na siyo vinginevyo. Nitafurahi kama asubuhi utapanda gari la kurudi Dar na siyo kujisumbua kwenda Kondoa. Usiku mwema.”

    Davina alihisi kuzimia!

    ***

    Uso wa Gerald ulionekana wazi kuwa na hasira, hapakuwa na dalili zozote za kuwa na jambo jema mbele yao. Kikundi kizima cha Kigaidi cha Nyamangumu, kilikuwa kimya kabisa wakisubiri kusikiliza kauli ya Gerald.

    Jumla ya watu watano walikuwa wamezunguka meza ya duara iliyokuwa na mvinyo mezani. Ukimya ulitawala. Kilikuwa kikao cha siri kubwa, kilichofanyika katika ghorofa ya chini, kwenye jengo moja kubwa na maarufu katikati ya jiji la Dar es Salaam.

    Gerald akawaangalia kwa zamu, kwanza aliyagandisha macho yake kwa Master, akarudi kwa Kijeba, Kisisii na kumalizia kwa Roy ambaye alikuwa amevaa miwani myeusi. Gerald akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu.

    “Sitakuwa na mengi sana ya kuzungumza na nanyi, ni machache, lakini yanayotaka ukweli. Hakuna asifahamu kwamba Jeff amekufa, sivyo?”

    Wote wakatingisha vichwa kuashiria kukubaliana na kauli yake.

    “Na wote tunafahamu kwamba alizikwa?”

    “Ndiyo maana yake...” Master akajibu kwa kujiamini.

    “...na ninyi ndiyo mliomuua...” akasema.

    “Hilo ndiyo jibu sahihi!”

    “Sasa inawezekana vipi marahemu aandike barua?” Gerald akauliza kwa ukali.

    “Barua?” Roy akang’aka.

    “Ndiyo, Jeff ananiandikia barua za vitisho, mbaya zaidi anaonekana kama anafahamu kila kitu, sidhani kama alikufa, ingawa nashindwa kuelewa ilikuwaje wakati tulimzika na mimi nilishuhudia maziko yake.

    “Isitoshe anamwandikia mpaka Davina, tena yeye ndiye anamwandikia nyingi. Sijajua anaandika nini, lakini Davina amechanganyikiwa, kiasi kwamba, mara ya pili sasa anasafiri kwenda kwao Kondoa kuomba msaada wa wazee wake! ”

    “Unahisi nini bwana Gerald?” Master akauliza.

    “Hujuma, kuna kaujanja fulani hivi kanachezwa...kuna mchezo tu...yupo mtu ametusaliti,” Gerald akasisitiza.

    “Hivi Gerald una kichaa? Jeff alikufa hakufa?” Master akamwuliza kwa hasira.

    “Alikufa!”

    “Alizikwa, hajazikwa?”

    “Alizikwa?”

    “Sasa huu ujanja unaosema ni upi? Inamaana hauna imani na sisi? Mbona kazi yako ilifanyika kwa uaminifu mkubwa na wewe umeshuhudia mpaka maziko yake au unataka kutuchoma?”

    “Siyo hivyo Master!”

    “Bali?”

    “Lakini mbona anaandika barua sasa?” Gerald akasema akifungua bahasha yake ya khaki na kutoa barua na kuwapa ili waisome.

    Wote walipigwa na butwaa.

    “Lakini mimi siamini kama ni Jeff mwenyewe ndiye aliyeandika hii barua!”

    “Kwa kwanini?”

    “Mtu aliyekufa hawezi kuandika barua, kwanza hana uhusiano wala mawasiliano yoyote na dunia, si ameshakufa jamani?”

    “Lakini huo ni mwandiko wake niliouzoea na hata sahihi ni yake pia!”

    “Hata kama...kuna mtu anaghushi, amini usiamini. Sasa ukiendekeza hisia hizo, tunaweza kuharibu uhusiano wetu mzuri kikazi kwa sababu ya mtu anayekuchezea akili, siamini kama kuna kijana wangu anaweza kunisaliti, siamini hata kidogo!” Master akasema kwa kujiamini.

    “Kweli Master?” Gerald akauliza.

    “Bila shaka unaniamini.”

    “Poa...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kikao kikaahirishwa, Gerald akiwa hana matumani kabisa. Akaondoka akiendelea kuwaza njia za kuutafuta ukweli zaidi, lakini kwa sasa alikuwa na hamu sana ya kuzungumza na Davina, ambaye alionekana kuwa na siri nzito moyoni mwake.

    ***

    Anaamka kitandani, anajisogeza kwenye swich ya taa, anawasha. Anahema kwa kasi na kuzidi kuchanganyikiwa! Anafungua simu yake kwenye ‘Call register’ kisha anabonyeza ‘Received calls’ halafu anaangalia namba ya mwisho kupigwa.

    Haionekani!

    Ilikuwa private number!





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog