Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KWENYE SIKU YANGU YA KUZALIWA - 3

 

     





    Simulizi : Kwenye Siku Yangu Ya Kuzaliwa

    Sehemu Ya Tatu (3)





    ****

    Majira ya saa 7:15 usiku Kiti na Wayeka walirejea chumban kwao wakiwa wamechoka kwa sababu ya kucheza muziki kwa muda mrefu. Licha ya uchovu waliokuwa nao, walijikuta tena katika tendo lile ambalo kila walipomaliza ngwe moja walijiona kama waliozaliwa upya. Hawakuishiwa hamu, walirudia tena na tena bila kukata kiu yao. Mwisho walichoka hoi wakapitiwa na usingizi.

    Walikurupuswa na mlio wa simu iliyokuwa ikipigwa. Ilikuwa ni simu ya Wayeka. Kiti aliyekuwa karibu na simu hiyo aliichukua na kuikabidhi kwa muhusika bila hata ya kuona ni nani mpigaji. Alifanya hivyo kwa sababu, aliamini kuwa simu ya mkononi ni kwa ajili ya mawasiliano ya faragha ya mtu, kinyume na hapo labda kuwe na makubaliano maalum baina ya mtu na mtu juu ya simu fulani. Yaweza kuwa juu ya simu ya mtu mmoja au zaidi ya hapo lakini ni kwa makubaliano maalum.

    Wayeka aliipokea ile simu kutoka mikononi mwa Kiti, alitazama kwenye kioo kisha akatabasamu peke yake na kumfanya Kiti naye atabasamu licha ya kutojua sababu ya tabasamu la Wayeka.

    Simu iliendelea kuita mpaka ikakatika bila kupokelewa.

    Wakiwa ndani ya shuka kubwa jeupe la hotelini pale, shuka ililofunika sehemu kubwa ya miili yao isipokuwa sehemu ya mwili iliyoanzia mabegani mpaka kichwani, Kiti alimtazama Wayeka kisha akauliza, “Mbona unacheka bebi?”

    “Nimefurahi tu mpenzi… asubuhi yote hii sijui huyu mchawi wa Kiholanzi anasemaje?”

    “Ili kujua anasemaje ungepokea umsikilize, yawezekana ana shida ya muhimu,” alisema Kiti.

    Kiti alipoimaliza tu kauli yake simu ikaanza kuita tena.

    “Sasa ngoja nimfanyie bonge la surprise, chukua upokee msalimiane nae…” alisema Wayeka huku akimkabidhi Kiti simu.

    Kabla Kiti hajaichukua alisihi, “Mpokelee bwana, yawezekana ana shida ya muhimu”

    “Hana lolote, najua ni umbea wake tu asubuhi hii. Chukua msalimiane nae,” Kiti aliichukua ile simu huku akiuliza, “Ni nani kwani?”

    “Mchawi gani wa kiholanzi zaidi y Emmy?” alijibu Wayeka kwa namna ya kuuliza swali mwangwi.

    “Hallow.. mrembo, mambo? Kiti alisalimia.

    Sauti nzito ya Kiti iliyapenya masikio ya Emmy na kumfanya apigwe na butwaa, huku maswali kadhaa yakipishana akilini mwake. Hakutarajia simu ya Wayeka ipokelewe na mwanaume, tena asubuhi na mapema ya saa 12 kama ile. Emmy akaanza kupatwa na wasiwasi kabla hajajibu, “Powa tu, habari?”

    “Safi,” Kiti alijibu na kabla hajaendelea zaidi, wayeka aliipora ile simu kimahaba na kuendelea, “Haya we mwanga asubuhi yote hii unataka nini?”

    “Mh! Shosti una mambo weye, na hicho kidume hapo pembeni yako ni nani?” Emmy aliuliza.

    “Otea… ukipatia tu, nakuapa zawadi,”

    “Ni shemeji, haya nipe zawadi yangu,” alisema Emmy.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nyooo… unadhani zawadi zinatokaga kirahisi namna hiyo? Hilo jibu ulilotoa ni nusu, kamilisha nikupe zawadi yako,”

    “Haya basi nimeshindwa mimi, niambie basi ni nani,”

    “Ni Kitiheka,” Wayeka alisema.

    Emmy alishtuka, hakuamini masikio yake ikabidi aulize tena, “Eti nani?”

    “Kitiheka Ngomanzito” alijibu Wayeka kwa msisitizo uliokuwa na hali zote za umaanisho.

    “Wacha wee..”

    “Habari ndo hiyo, haya nambie shost..”

    “Mi nilikuwa nakusalimia tu mpenzi, ila kwa hali hii wewe ndiyo una mengi ya kuniambia,” Emmy alisema.

    “Umeanza upaparazi wako, labda nimpe simu akwambie yeye unachotaka kukisikia”

    “Nyie waikizu mna mambo! Haya mpe simu nimpashe,”

    “Powa, huyu hapa” alisema Wayeka huku akimpatia Kiti simu.

    Waliongea mengi huku maongezi yao yakitawaliwa na utani wa hapa na pale kabla Emmy hajakata simu.

    ****

    Emmy aliitazama ile simu kwa namna ya kutoamini, ikawa kama vile ana maswali mengi ambayo alitamani kuiuliza simu ile. Alitabasamu huku akiwa ameikodolea macho simu iliyokuwa mikononi mwake.

    Bony aliyekuwa pembeni yake, kwenye kitanda walicholala alikuwa na shauku ya kutaka kujua ni kipi kilichomfurahisha na kumshangaza mkewe. Licha ya kuwa katika taharuki hiyo Bony akijikaza na kujifanya asiye na haraka juu ya jamo hilo.

    Mara Emmy alimgeukia na kumwambia huku akiwa katika hali ileile ya tabasamu, “Meza namba kumi imezua jambo”

    “Una maana kuwa Wayeka yuko na Kitiheka?” Bony aliuliza.

    “Ndiyo hivyo… nimezungumza nao, tena wanaongea kwa sauti ambazo bado zinaonesha kuwa ndiyo kwanza wanatoka kuamka.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Meza namba kumi imezua jambo” alisema Bony kwa kuirudia kauli ambayo awali ilisemwa na mkewe ambaye bado alikuwa ametekwa na tabasamu la furaha isiyo kifani.

    Bony alikumbuka ujio wa Cosmas usiku wa jana hapo nyumbani kwao pamoja na shida yake ya kutaka kumuoa Wayeka, akaona dhahiri kuwa haitawezekana!



    6

    PENZI baina ya Kiti na Wayeka liliota mizizi na hatimaye kuchanua kabisa. Furaha isiyo kifani ikazigubika nyoyo zao, na nia ya kutaka kuliweka wazi penzi lao bayana ikadhihiri waziwazi.

    Walitambulishana kwa marafiki wa pande zote mbili, yaani, Wayeka alimtambulisha Kiti kwa marafiki zake wote; wa kike na wa kiume, wakamwita shemeji. Kiti naye alimtambulisha Wayeka kwa marafiki zake wa jinsia zote, wakampa heshima yake kwa kumuita shemeji, hii ilikuwa ni kwa upande wa marafiki wa kiume huku wale wa kike wakimwita wifi.

    Hatua ya pili ikawa ni kutambulishana kwa wazazi wa pande zote mbili ambao nao walitoa baraka zao kama wazazi wakiwatakia heri na fanaka watoto wao.

    Baada ya kuwa wametambulishana kwa wazazi wa pande zote mbili wakawa huru kutembeleana makwao kila walipojisikia. Kuna wakati Kiti alikwenda nyumbani kwa kina Wayeka bila wasiwasi wowote kwa sababu tayari alikwishatambulishwa kama mchumba na Wayeka naye akawa anafanya hivyohivyo.

    Uchumba wa Kiti na Wayeka ukafufua tena urafiki wa mzee Ngomanzito na mzee Ayuyube ambao waliwahi kuwa marafiki miaka kadhaa nyuma walipokuwa wanasoma shule ya msingi, tena katika darasa moja.

    Licha ya kila mmoja kumpenda mwenzi wake katika kiwango ambacho tunaweza kusema ni sawa, lakini Kiti ndiye aliyeonekana kuwa na haraka zaidi na ndoa. Alitaka waoane haraka kwa sababu maisha ya ukapela yalichamchosha. Hakuwa ameridhika kabisa na aina ya maisha waliyoishi yeye na Wayeka, alitaka kuoa kabisa. Alitaka iwe hivyo mapema kwa sababu aliamini kila nyuma ya mwanamme aliyefanikiwa kuna mwanamke.

    Alimsihi Wayeka wafunge ndoa mapema, Wayeka alimuelewa, akamkubalia na furaha ya Kiti ikaongezeka maradufu. Wakapanga kuwa baada ya safari ya Kiti ya Dar es salaam ambako alipanga kwenda kusajiri kampuni yake, atakaporudi tu wapange mipango ya kuvalishana pete ya uchumba na baadaye wafunge ndoa ambayo itawaweka huru duniani na mbinguni.

    Siku moja wakati Kiti yuko chumbani kwake akiandaa nyaraka muhimu ambazo alidhani ni lazima awe nazo ili kufanikisha zoezi lake la usajiri wa kampuni. Kiti alifungua moja kati ya droo ndogo ya kabati lake la nyaraka, akakutana na picha zake za muda mrefu alizopiga kipindi akiwa sekondari. Alizitama picha zile moja baada ya nyingine, mwishowe akavutiwa na moja kati ya picha zile. Ilikuwa ni picha ambayo alipiga akiwa amekumbatiana na Mina.

    Picha ile ilivuta umakini wa Kiti na kumfanya asimame kutoka pale chini alipokuwa amechuchumaa, akajivuta kinyumenyume mpaka alipofika kitandani akakaa na picha yake ikiwa mkononi ameitumbulia macho. Aliitazama picha ile mpaka ilipomchukua mpaka kwenye bahari ya kumbukumbu, akakumbuka siku ya kwanza walipokutana na Mina; walikutana katika siku ya kwanza walipowasili shuleni pale kwa ajili ya kujiunga na kidato cha tano.

    Walikuwa wamekaa kwenche benchi lililokuwa nje ya ofisi ya mkuu wa shule, kila mmoja akisubiri zamu yake ya kuingia ofisini mule ifike. Katika mkao waliokuwa wamekaa, Mina ndiye aliyepaswa kuingia baada ya mtu aliyeko ndani kuwa ametoka halafu ndiyo zamu ya Kiti ifuate.

    Aliyekuwa akisubiriwa atoke ndani alikawia kutoka na kusababisha Kiti na Mina waanzishe mazungumzo ya kupitisha muda wakati wakisubiri zamu zao. Mazungumzo hayo ndiyo yaliyowafanya wakafungua ukurasa wa urafiki baina yao, urafiki ambao ulifuatiwa na uhusiano wa kimapenzi siku chache baadaye.

    Kumbukumbu hizo ziliyeyuka polepole na hatimaye macho ya Kiti yaliirejea taswira ya picha ambayo ilikuwa mikononi mwake.

    Aliyatafakari mapenzi yake na Mina enzi hizo na mara sauti ikamtoka, “Mina,” akairejesha picha ile mahali zilipo nyingine akazirudisha kwenye droo sambamba na nyaraka nyingine alizokuwa amezitoa.

    Siku mbili baadaye Kiti alikuwa katika jiji la Dar es salaam ambako alikwenda kwa ajili ya kusajili kampuni.

    Baada ya kukamilisha taratibu zote kwenye ofisi za BRELA ambazo ziko katika jengo la Vyama vya ushirika, ghrofa ya nne, Kiti aliamua kuchukua lifti ili ashuke chini.

    Lifti ilifika Kiti akajitoma ndani. Ilipofika tu Ground Floor, milango ya lifti ilifunguka na Kiti akatoka. Alipotoka tu ndani ya lifti alimuona Mina akiwa pale Ground Floor miongoni mwa watu waliokuwa wakisubiri lifti iwapandishe ghorofani.

    Kama ilivyokuwa kwa Kiti, Mina naye hakuamini kwa kile alichokuwa akikiona. Akabadili uamuzi wake, badala ya kuingia kwenye lifti aliyokuwa akiisubiri, Mina alibaki pale alipokuwa kwa lengo la kumsubiri Kiti.

    Kiti alitoka kwenye lifti na kwenda mpaka alipokuwa Mina, wakasalimiana huku kila mmoja akimtazama mwenzie kwa jicho lililojaa maswali.

    Ni Kiti ndiye aliyeanza kumsemesha Mina baada ya kuwa wamejivuta kando, “Habari za siku Mina?”

    “Salama Kiti, za miaka?”

    “Ni miaka au miezi. Si ni juzi tu tulikutana kwenye sherehe ya Bony na Emmy?”

    “Ni kweli Kiti, lakini…” kabla hajamalizia kauli yake Kiti alimkatisha kwa kuuliza, “Lakini nini tena?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mina hakulijibu swali lile kwa haraka, aliangaza kushoto na baadaye kulia, akabaini uwepo wa watu wengine eneo lile, kisha akamtazama tena Kiti akamwambia, “Kiti..” alisita kidogo kabla hajaendelea, aliiremba sauti yake na kuifanya iwe ya deko, halafu akaendelea, “Naomba tutafute sehemu tukae tuzungumze Kiti, nina mengi ya kuongea na wewe,” Mina alisema.

    “Ni sawa Mina, lakini nahisi kama nitakuawa nimeivuruga ratiba yako. Nasema hivi kwa sababu ulikuwa unasubiri lifti kabla hatujaonana. Unaonaje kama utamaliza kwanza shughuli ulizokusudia kuzifanya humo ndani halafu ndiyo tutafute mahala kama ulivyosema.”

    Wakati Kiti anayasema hayo, Mina alikuwa akimtazama barabara tangu alipoanza kuongea mpaka alipohitimisha.

    “Na kama nilikuwa nakufuata wewe je?” Mina aliuliza kwa mzaha huku akiachia tabasamu murua lililoutekenya ubongo wa Kiti ambaye alimtazama Mina kwa mshangao kama vile asiyeamini kila alichokisikia. Sura ya Kiti ilionesha dhahiri kuwa kuna neno anataka kusema lakini hakujua ni neno gani aseme hali iliyomfanya abaki mdomo wazi kwa muda wa sekunde kadhaa kabla hajasema, “Huwezi kuwa serious Mina! Ulijuaje kuwa niko mji huu?”

    “Kiti you know what…” aliweka tuo kwa lengo lakumeza mate, kisha akasema, “Ukweli kuna issue nilikuja kuishughulikia humo ndani, lakini sidhani kama nitamudu kufanya lolote kama bado sijazungumza na wewe. Niwie radhi tafadhali.”

    “Ok, tufanye kama ulivyosema, sijui ungependelea tukae maeneo gani?” Kiti alisema huku akiushika mkono wa Mina tayari kwa kuondoka.

    Mina aliupokea mkono wa Kiti, wakashikana na kuelekea zilipo Taxi baada ya kuwa wamevuka barabara wakitokea kwenye jengo la vyama vya ushirika.

    Dakika kumi baadaye walikuwa Chang’ombe Village Hotel, maeneo ya Keko. Waliweza kufika hotelini hapo mapema kwa sababu tu, hakukuwa na foleni muda huo. Naweza kusema kuwa bahati ilikuwa yao kwa sababu; ni aghalabu sana nyakati za mchana kwa barabara za Nyerere na Chang’ombe kuokuwa na foleni.

    Mina alipendekeza waende hotelini hapo kwa sababu, ndipo alipochukua chumba kwa siku ya pili tangu alipowasili Dar es salaam akitokea Mwanza kwa ndenge ya shirika la ndege la Communty Air Line ambalo lilikuwa likitoa huduma ya usafiri wa anga kwa gharama nafuu.

    Walichagua sehemu tulivu iliyokuwa kwenye mgahawa wa chakula wa hotelini pale na bila kupoteza muda mazungumzo yao yalianza.

    “Kwanza nikupongeze kwa kuhitimu masomo yako, nasikia uliamua kuunga?” Mina aliuliza.

    “Nashukuru, niliamua kuunga kwa sababu sikuwa na namna, hasa zaidi ukizingatia idadi kubwa ya wasomi wenye shahada ya kwanza ambao wamerundikana hapa nchini”

    “Ni wazo zuri, mi nashukuru tu umerudi Kiti… tena nshukuru tumekutana leo labda unaweza kuniokoa, nateketea Kiti.”

    “Unateketea! Unateketea kivipi?” Kiti alihoji.

    Ilimchukua Mina dakika nzima bila ya kulijibu swali la Kiti, alikuwa aiktafakari namna ya kulijibu swali aliloulizwa, majibu alikuwa nayo lakini alihofu juu ya mapokezi ya jibu lake kabla hajalitoa. Hakuweza kujua kwa haraka ni kwa vipi litapokelewa.

    Mina alijikaza na kuamua lolote liwe, “Maji ukishayavulia nguo huna budi kuyaoga” aliwaza kabla hajasema, “Ni penzi lako Kiti, nimelikosa kwa muda mrefu sasa.. na huu ndiyo wakati ambao nalihitaji kuliko kitu chochote”

    Kiti alitrajia kusikia taarifa ya namna hiyo baada ya kuwa ameziona dalili tangu wakiwa pale Vyama vya Ushirika, lakini katu hakutarajia taarifa hiyo kuwasilishwa kwa namna aliyoiwasilisha Mina. Akilini alijiwa na maswali ambayo majibu yake hayakumjia kwa haraka kama ambavyo maswali hayo yalikuja.

    Wakati bado anatafakari cha kujibu, sauti ya Mina iliyarudia tena masikio yake kwa namna ya pekee.

    “Ni miaka sita tngu tufarakane Kiti… nakumbuka nyakati za raha tulizokuwa nazo wakati ule. Japo ni miaka sita tu, lakini kwangu naona kama ni kama mamilioni ya miaka… natamani tuzirudie zama zile Kiti. Nakiri kuwa ni mimi ndiye niliyekuwa na makosa, lakini yote ni kwa sababu ya utoto na wivu wa kijinga, tusahau mabaya yaliyopita ili tuzirudie zama, Kiti nakuhitaji, nakuhitaji kwa sbabu nakupenda” Mina aliyasema maneno hayo huku machozi yakimlengalenga machoni pake na kumfanya Kiti awe katika wakati mgumu zaidi.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitambua fika kuwa ni kweli walikuwa na nyakati za raha baina yake na Mina, na akakiri kuwa, ni kweli Mina ndiye aliyekuwa mkorofi kwa sababu ya kutokuwa mwelewa. Yawezekana ni kweli hali hiyo ya Mina kutokuwa mwelewa ilisababishwa na wivu pamoja na akili ya utoto aliyokuwa nayo Mina wakati ule. Lakini hii nia yake ya kutaka kurudiana ilimpa Kiti wakati mgumu. Ilimpa wakati mgumu kwa sababu; hakujua udhati uliomo kwenye nia hiyo. Ni kweli kuwa Mina ana penzi la dhati kwake au ana jambo lingine?

    Hili halikumpa shida sana kwa sababu alijiaminisha kuwa si rahisi Mina kuwa na hila dhidi yake, na hata kama ana hila, Kiti aliamini kuwa hakuna mahali ambapo Mina atajificha baada ya kuwa amediriki kumfanyia ubaya wowote, labda aihame sayari. Lakini kama ataendelea kuweka makazi yake ndani ya sayari hii basi ni wazi kuwa atampata kwa sababu yeye ni mtoto wa mjini.

    Sababu nyingine iliyompa Kiti wakati mgumu ni Wayeka ambaye ndiye mpenzi wake wa sasa na yeye mwenyewe anakiri kumpenda kwa dhati, mbali na kumpenda kwa dhati tayari amekwisha muahidi ndoa, ni kwa vipi aahirishe?

    Kiti aliyatafakari hayo huku machozi ya Mina ambayo yalikuwa yameshaunda mifereji juu ya mashavu yake mazuri yakimfanya apate maumivu makali kwa sababu yeye ndiye chanzo. Kiti hakuvumilia kuyaona machozi hayo, aliingiza mkono mfukoni na kutoa leso akaanza kumfuta Mina machozi huku akisema, “Nyamaza Mina, please nyamaza,”

    “Naumia Kiti.. naumia..” Mina alizidi kulalama.

    “Yote yataisha Mina… nyamaza mpenzi,”

    Kwa namna hali ilivyokuwa, Kiti hakuweza kuvumilia. Alimsihi Mina wakaongelee chumbani. Mina alikubali, wakaelekea kwenye chumba alichofikia Mina.

    Chumba kilikuwa na kitanda kimoja kikubwa, kabati dogo la wastani, meza moja na kochi dogo.

    Walipofika chumbani, Kiti alimkalisha Mina Kitandani kisha naye akakaa kwa lengo la kumbembeleza.

    Kwa bahati mbaya sana binadamu tumenyimwa uwezo wa kuyatambua matukio ya mbele. Laiti Kiti angejua kuwa kuwemo chumbani mule ni mwanzo wa kuyahatarisha maisha yake, kamwe asingethubutu kuingia.



    *****

    NIA ya kuwa na Wayeka kama mke wake ilizidi kuuzonga moyo wa Cosmas. Alipanga kumuoa Wayeka endapo watakubaliana licha ya kutokumjua kiundani. Aliamini kuwa binadamu hufundwa akafundika, na kwa kuwa Wayeka ni binadam basi anaweza kubadirishwa endapo atakua na mwenendo ambao kwa namna moja au nyingine unaweza kumfanya apungukiwe sifa ambayo inaweza kumfanya asiolewe.

    Ni nia hiyo ndiyo iliyompeleka tena Cosmas nyumbani kwa Bony kwa nia na madhumuni ya kupata majibu ya kile kilichofanywa na Bony na Emmy kama jitihada za kumuunganisha na Wayeka.

    Alifika nyumbani kwa Bony majira ya saa 2:00 usiku, muda ambao chakula cha jioni kilikuwa mezani tayari kwa kuliwa.

    Kwa kuwa Cosmas alifika katika muda huo, hakuwa na jinsi, isipokuwa kujumuika na wenyeji wake katika mlo huo wa jioni. Nidhamu ya chakula ilishika hatamu yake na kuwafanya wote wawe kimya mpaka baada ya zoezi hilo la kupata chakula kukamilika.

    Mara tu baada ya zoezi hilo kukamilika, Bony, Emmy pamoja na mgeni wao walielekea sebuleni kwa ajili ya mazungumzo.

    Mpaka wakati huo kila mmoja yaani, Bony na Emmy walikuwa wameshamiri tabasamu, hali iliyosababisha pia Cosmas kutabasamu kwa imani kuwa, yamkini wenyeji wake wameifanya shughuli aliyowatuma na imefana kwa namna aliyoitaka.

    Cosmas ndiye aliyefungua dimba kwa kuuliza, “Vipi bro, ule mpango wetu umekwendaje?”

    Swali la Cosmas lilikuwa kama shoti ya umeme iliyowapata Bony na mkewe na kuwafanya watazamane huku tabasamu likififia kwenye kila sura ya mmoja wao.

    Hali waliyoionesha Bony na mkewe ilimshtua Cosmas na kumfanya ahisi kuwa yawezekana walisahau kuifanya shughuli yake na wamekumbuka mara baada ya yeye kuuliza.

    Mpaka wakti huo hakuwa amejibiwa na wenyeji wake walikuwa katika hali ileile ya kutazamana, na kumfanya Cosmas aulize tena, “Vipi shem, mlisahau au?”

    “Hapana shem,” Emmy alijibu.

    “Kazi ilifanyika kaka,” Bony aliongeza.

    Kauli hizo zilimpa matumaini Cosmas na kumfanya ajiweke sawa pale kwenye kochi alipoketi ili aweze kusikiliza vizuri.

    “Enhe.. ilikuwaje bro?”

    Kimya cha dakika kadhaa kilifuatia baada ya swali la Cosmas na kumfanya atwaliwe upya na wasiwasi ulioigubika nafsi yake kwa namna ya ajabu kabla hajasikia tena sauti ya Bony ikiita, “Cosmas..”

    Kabla hata hajaitika sauti ya Bony ilisikika tena lakini safari kwa namna iliyodhihirisha unyonge alionao.

    “Kazi ilifanyika braza… lakini bahati haikuwa kwako,”

    Kauli ya Bony ilimchanganya Cosmas na kumfanya apoteze mhimili wa ustahimilivu na kuuliza swali lenye mantiki licha kulitoa swali hilo katika namna ya kuropoka, “Una maana gani?” Cosmas aliuliza.

    Lilikuwa ni swali jepesi, lakini majibu yake yalikuwa magumu kwa Bony ambaye alikwisha itambua hali ya kiasikolojia aliyomo rafiki yake. Alikohoa kidogo kwa namna ya kusafisha koo lake ili aseme neno, lakini badala ya kuzungumza alimtazama mkewe na kumpa ishara kuwa achukue jukumu la kufafanua,

    Bila kupoteza muda wala kumung’unya maneno, Emmy alisema, “Wayeka amewahiwa shemu, na hilo tulilifahamu katika siku tuliyompigia simu, yaani siku ile ile tulioachana hapa baada ya wewe kuondoka,”

    Maneno hayo yalitua barabara kwenye masikio ya Cosmas, yalikuwa ni kama jiwe la moto ambalo amelazimishwa kulimeza. Yaliutekenya ubongo wake na kumfanya awe kama aliyechanganyikiwa kabla sauti ya Bony ambayo ilimrudisha kwenye utimamu licha ya maumivu makali aliyokuwa akikabiliana nayo.

    “Hilo lisikuvunje moyo bro, kwa sababu yeye si mwanamke pekee… isitoshe hatujui mwitikio wake ungekuwaje baada ya kuwa tumekuunganisha naye,”

    “Ni kweli shem… hakuna sababu ya kuumiza moyo kwa sababu ya mtu ambaye tayari ana mtu,” Emmy aliongeza.

    Yote yaliyosemwa na wenyeji wake yalimkaa vema akilini licha ya kuwa kwa namna ambayo kimtazamo ni tofauti na rai aliyopewa.

    Haikumchukua muda mrefu Cosmas aliaga na kuondoka huku akisindikizwa na Bony mpaka nje ya geti huku wakiendelea na maongezi ya hapa na pale.

    ****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wayeka alikuwa chumbani mwake akiwa mwenye lundo la mawazo baada ya kupiga simu kwa mara kadhaa bila kupokelewa. Alikuwa ameshatuma jumbe zaidi ya tatu za maandishi ambazo nazo hazikujibiwa licha ya kuonesha kuwa zimefika kwenye simu ya mlegwa.

    Alikuwa akiwaza ni nini hasa kimempata Kiti mpaka ashindwe kupokea simu na kujibu jumbe anazomtumia. Kichwani mwake alikuwa na majibu juu ya maswali yake, majibu ambayo yalikuwa ni ya kinadharia kwa sababu hakuwa na uhakika nayo. Kwanza; alihisi kuwa yawezekana Kiti akawa amekunywa kiasi kikubwa cha pombe na hivyo kumfanya alale bila kujitambua na kumsababisha ashindwe kusikia simu wakati inaita. Sababu iliyomsukuma kufikiri hivyo ni ni kutokana na kumfahamu Kiti kuwa, mara anywapo pombe, hususan pombe kali ambazo ndizo huzipendelea sana, mara nyingi hulala bila kujitambua na yawezeka ikawa ndiyo sababu inayomfanya ashindwe kupokea simu kwa sababu hasikii.

    Pili, alihisi kuwa yawezekana Kiti anamwanamke mwingine huko alipo na hiyo ndiyo sababu inayomfanya ashindwe kupokea simu na kujibu jumbe zake za maandishi. Licha ya kutoitilia maanani sababu hiyo, bado hisia kuwa Kiti ana kimada mwingine huko aliko zilimrejea akilini mara kwa mara na kumfanya apatwe na wivu ambao ulizidi kumuweka katika wakati mgumu.

    Ni wivu huo ndiyo ulimfanya Wayeka ashindwe kulala kwa sababu ya kujenga imani kuwa anasalitiwa na mpenzi wake.

    Wakati yote hayo yakiizunguka akili yake, mara hisia kuwa yawezekana kuwa Kiti yuko hatarini zikaivamia akili yake na kumfanya ajilaumu kwa kuruhusu akili yake kumshutumu Kiti. Hisia hizo ndizo zilizomfanya aandike ujumbe mfupi wa maaandishi na kumtumia Kiti, ujumbe huo ulisomeka hivi: Nimejaribu kukupigia kwa mara kadhaa bila mafanikio. Ni matumaini yangu kuwa uko salama na mara upatapo ujumbe huu tafadhali nipigie, kumbuka kuwa nakupenda… usiku mwema.

    Mara baada ya kuandika ujumbe huo aliutuma kwa Kiti na majibu yakarudi kuwa ujumbe umepokelewa.

    ****

    Kiti alijtahidi kumbembeleza Mina ambaye alikuwa akilia huku kichwa chake akiwa amekilaza kifuani kwa Kiti na kumfanya Kiti akumbuke mambo yaliyowahi kutokea baina yao ikiwemo uvunjaji wa amri ya sita. Alikumbuka ufundi wa Mina kwenye uwanda huo, kumbukumbu hizo zilimfanya Kiti apate matamanio mapya ya kimapenzi kwa Mina na bila kutarajia mikono yake ilianza kuyapapasa maungo ya Mina ambaye naye alijibu mapigo. Muda mfupi baadaye hakuna aliyekuwa na nguo kati yao.

    Simu ya Kiti ilikuwa ikiita lakini hakushughulika nayo. Iliita mpaka ikakata, iliita tena mpaka ikakata na mara jumbe za maandishi zikaanza kufululiza moja baada ya nyingine, nazo kama ilivyokuwa kwa simu ya sauti, Kiti hakushughulika nazo.

    Walipomaliza ngwe ya pili, kila mmoja alimtazama mwenzie kwa namna ya pekee. Haikuwa rahisi kwa kila mmoja kubaini hisia alizonazo mwenzake.

    Mina alikuwa akisherehekea ushindi ambao kwake ulikuwa ni mkubwa kupindukia. Kulirejea tena penzi la Kiti kilikuwa ni kitu kilichoitesa nafsi yake kwa muda mrefu. Leo yuko nae kitandani, wakiwa watupu kama walivyozaliwa, tena baada kushiriki tendo ambalo kwa imani yake aliamini lilikuwa kama kilele cha ushindi.

    Alimtazama Kiti bila kuishiwa hamu ya kuendelea kumwona huku moyoni mwake akiamini kuwa pendo lililokuwa limepoa na kusinyaa sasa limechipua upya.

    Aliendelea kumtazama mwenzie huku akijenga taswira akilini mwake kuwa; yuko na Kiti mbele ya madhabahu wakimsubiri kasisi ili aje kuwaidhinisha kuwa wao ni mke na mume halali.

    Wakati Mina akiwaza hayo katika namna ambayo ilimpa faraja na matumaini, mambo yalikuwa tofauti kabisa kwa Kiti ambaye alikwa akijutia kila lililotokea baina yake na Mina. Alikuwa akiilaumu nafsi yake kwa usaliti alioufanya. Kufanya mapenzi na mwanamke mwingine tofauti na Wayeka ilikuwa ni hatia iliyoanza kuutafuna moyo wake na kumfanya ajutie kabisa juu ya kila kilichotokea baina yake na Mina.

    “Siwezi kuwa na wapenzi wawili kwa wakati mmoja.” Kiti alijilaumu.

    Kiti alitambua fika kuwa Mina anampenda, lakini hatoweza kuwa naye kwa sababu tayari ana Wayeka na tayari amekwishapanga naye mambo mengi kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Mapenzi yake na Wayeka yamefikia hatua ya juu ambayo si rahisi kwa yeyote kati yao kurudi nyuma.

    Akiwa katika lindi hilo la mawazo Kiti alizinduliwa na sauti ya Mina, “Ahsante Kiti… ahsante mpenzi wangu.”

    Kutokana na hali aliyokuwanayo Mina, ilimbidi Kiti kutoonesha kuwa yuko kinyume na fikra zake kwa wakati huo.

    “Mina…” Kiti aliita, kisha kama aliyetaka kusema jambo, alibaki mdomo wazi kwa sababu ya kutokujua aseme neno gani.

    Mina aliyekuwa akitarajia kusikia neno kutoka kwa Kiti, alitega sikio kwa muda wa takribani dakika moja hivi bila kusikia lolote, hali iliyomlazimu kuchokoza mada kama lengo la kumkumbusha Kiti ili aseme jambo alilotaka kusema.

    “Nakusikiliza mpenzi, ongea...” alisema Mina.

    “Ni usiku sa’ivi, tulale.” Kiti alisema huku akiivuta shuka na kujifunika yeye na Mina.

    Mawazo yaliendelea kutafuna fikra zao huku kila mmoja akiwaza lake mpaka usingizi ulipowachukua.

    ****

    Asubuhi Mina aliamka, akaunyoosha mko wake kupapasa mahali alipolala Kiti, palikuwa patupu! Ikambidi kunyanyua shingo ili kuangaza mule chumbani ambamo palitawaliwa na mwanga wa jua ulioingia kupitia dirishani. Aliangaza kushoto na kulia, hakuona mtu.

    Ikamlazimu kuinuka ili akae akae kitako na hapo ndipo alipoiona karatasi iliyokuwa juu ya meza ikiwa imegandamizwa na bilauli ya udongo ili isiweze kupeperuka.

    Moyo ulimlipuka Mina na wasiwasi ukautwaa moyo wake. Shauku ya kutaka kujua karatasi hiyo ina ujumbe gani ilimpa msukumo wa kuinuka pale kitandani alipokuwa ili ailekee meza na kuchukua ile karatasi. Alifika mezani akaichukua karatasi na bila kupoteza muda aliifungua ili kuisoma huku mapigo ya moyo wake yakimwenda mbio.

    Kumbuka hakuwa na nguo yoyote zaidi ya shuka jeupe alilojifunga kabla hajaifikia meza. Macho ya Mina yalikutana na maandishi machache yenye kukatisha tamaa na kuvunja moyo, na kusababisha furaha yake iyeyuke sambamba na kupotea kwa matumaini yaliyokuwa yamejijenga moyoni mwake kabla hajakutatana na barua hiyo.

    Barua hiyo yenye kuumiza na kuuchoma moyo ilikuwa imeandikwa hivi:

    Hallow Mina,

    Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama. Naomba usinielewe vibaya na wala usiitafsiri hali hii kama kisasi. Sikukusudia na wala sikupenda iwe hivi lakini imenibidi.

    Sina budi kukueleza kuwa tayari nina mtu mwingine ambaye nimekwishamuahidi ndoa, na hivi karibubuni nitamvika pete ya uchumba. Hivyo haitakuwa rahisi mimi kuwa na wewe tena kwa sababu hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nimeamua kuliweka hili wazi kwa sababu ni ukweli tu, ndiyo utakaoniweka huru.

    Nisamehe kwa kila jambo.

    Kiti.

    Mpaka anamalizia neno la mwisho tayari Mina alikuwa amekaa chini huku mifereji ya machozi ikiondoa uzuri wa mashavu yake, sambamba na kwikwi zilizokuwa zikidhihirisha maumivu makali aliyokuwa nayo moyoni. Mina alilia barua ile ikiwa mikononi mwake, hakujua ni nini hatma ya maisha yake endapo mwanamme aliyempenda ndiye huyo kamuandikia barua yenye maneno makali kama hayo ambayo yalikuwa yakiuchoma moyo wake.

    ****





    ****

    Kiti aliwasili Nyamuswa majira ya saa 7:00 mchana siku iliyofuata baada ya kuwa ameondoka Dar es salaam katika siku ambayo alimwandikia Mina barua na kumwachia pale hotelini. Aliondoka kwa ndege ya Community Air Line. Siku hiyohiyo aliingia Bunda japo kwa kuchelewa na siku iliyofuata alielekea Nyamuswa kwa lengo la kuonana na Wayeka.

    Alipofika alijitetea kwa kutunga uongo uliofanana na ukweli, ikiwa ni baada ya yeye kutopokea simu na kutojibu jumbe fupi za maandishi alizokuwa akitumiwa na Wayeka.

    Utetezi wake ulipokelewa huku akipewa hadhari kuwa; asirudie jambo hilo kwa sababu, ulevi wa kupindukia si mzuri kiafya na huweza kusababisha hatari zaidi.

    “Punguza pombe Kiti, pombe si nzuri,” alisema Wayeka.

    “Nimekuelewa mpenzi, sitorudia na nakuahidi haitotokea tena kulewa kiasi hicho,” Kiti alisema kabla hajaongezea, “Bebi…” alisita kidogo halafu akaendelea, “Tarehe 10 mwezi ujao ni siku yangu ya kuzaliwa,”

    “Waooh..” alidakia Wayeka.

    “Nataka siku hiyo ndiyo iwe siku ya kukuvisha pete mpenzi, au unasemaje?”

    “Niseme nini tena wakati mwamuzi ni wewe,” alisema Wayeka.

    Nia ya kiti ilikuwa ni kumwoa kabisa Wayeka kama alivyokusudia tangu awali. Walikubaliana kuwa kwenye siku hiyo ya kuzaliwa kwa Kiti ndiyo lifanyike tukio la kuvishana pete ya uchumba.

    Taratibu zote za awali zilifanywa, ikiwa ni pamoja na kuwataarifu watu wao wa karibu, ambao ndiyo watakuwa mashahidi katika tukio hilo la muhimu kwao.

    Walikubaliana kuwa; hafla hiyo iafanyike nyumbani badala ya hotelini na wakakubaliana kuwa iwe ni nyumbani kwa mzee Ngomanzito ambapo ndiyo kwao na Kiti.

    Licha ya siku kwenda kwa kasi ileile ya kawaida, kwa wawili hawa waliona kama kasi ya kujongea kwa siku kuielekea tarehe husika kuwa ni ya kusuasua sana. Kwao siku zilikuwa kama haziendi kwa sababu ya kuisubiri siku hiyo kwa hamu.

    ****

    Ukiachana na nyumba ya Nyasura, nyumba ambayo Kiti aliishi pamoja na wazazi wake, mzee Ngomanzito pia alikuwa na nyumba nyingine ndogo ambayo ilikuwa maeneo ya jirani na kituo kikubwa cha polisi kilichopo Bunda. Nyumba hiyo iliyokuwa ndani ya uzio pamoja na geti jeusi lililokuwa mbele kabisa, ilikuwa na vyumba viwili vya kulala ambavyo vyote vilikuwa ni self contained, pamoja na hayo nyumba hiyo pia haikukosa kuwa na sebule pamoja na ukumbi wa chakula wenye ukubwa wa wastani.

    Hivyo ili kumfanya mwanaye awe huru, mzee Ngomanzito alimkabidhi Kiti nyumba hiyo lakini kwa sharti moja, nalo ni; kuhamia kwenye nyumaba hiyo mara baada ya kumvisha pete mchumba wake.

    Taarifa hiyo ilipokelewa kwa shangwe na Kiti, na hakutaka kumwambia mtu yeyote juu ya hilo, lengo likiwa nikum-suprise Wayeka ambaye angelijua hilo mara baada ya kuwa wameshafika kwenye nyumba hiyo ambayo ilisheheni samani za thamani.



    *****



    STELLA KAMUGISHA alikuwa ndani ya vazi la baibui, na usoni alivalia nikabu iliyomfanya aonekane kama ninja. Isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kumtambua kwa sababu ya muonekano aliokuwa nao. Alipanga iwe hivyo, yaani kutotambulika kwa mtu yeyote ili aweze kuifanya kazi yake kwa ufanisi.

    Ilikuwa ni siku ya tatu tangu alipofika mjini Bunda ambako alikwenda kwa lengo la kulipa kisasi kwa Cosmas, mwanamme aliyemuharibia maisha yake na kumfanya atangetange bila muelekeo.

    Katika kuwepo kwake Bunda, Stella alikuwa ameshakusanya taarifa zote muhimu ambazo alizihitaji ikiwa ni pamoja na; kufahamu mahali anapoishi Cosmas, , anaishi na nani, shughuli anazozifanya, hutoka na kurudi nyumbani saa ngapi na anapotoka huelekea wapi.

    Haikuwa ngumu kwa Stella kuzipata taarifa hizo. Mambo yalikuwa rahisi sana tofauti na alivyotarajia, kwani: alipoingia tu Bunda, majira ya saa nne asubuhi siku mbili zilizopita, Stella alifanikiwa kumuona Cosmas akiwa ni mwingi wa pirika kwenye duka lake la vipuri vya magari na pikipiki.

    Cosmas akiwa ndani ya suruali yenye rangi nyeusi na fulana ya bluu, alikuwa akiwahudumia washtiri wake waliofika dukani pale lengo la kupatiwa huduma. Licha ya kutoa huduma kwa washtiri wake, Cosmas alionekana mwenye mawazo ambayo kwa kiasi Fulani yalipunguza umakini wake kwenye shughuli aliyokuwa akiifanya. Hii ilidhihirika baada ya mteja mmoja kulalamika kuwa amepewa bidhaa ambayo hakuihitaji, na mwingine ambaye bila shaka ana tunu ya uaminifu kurudisha pesa kwa Cosmas baada ya kuwa Cosmas amempa chenchi ambayo ni zaidi ya stahiki yake.

    Stella aliyagundua haya kutokea kwenye mgahawa uliokuwa ukitazamana na duka alilokuwemo Cosmas. Alikuwa nyuma ya meza ambayo juu yake kulikuwa na bilauli ambayo ndani yake mlikuwa na shurubati ya maembe aliyokuwa akiinywa taratibu huku akifuatilia kila jambo alilokuwa akilifanya Cosmas.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Majira ya saa 9 Alasiri, Cosmas aliondoka kuelekea nyumbani huku akifuatwa na Stella bila yeye kujua. Alipofika alijitoma ndani bila hofu wala mashaka, na majira ya saa1 jioni, Cosmas alitoka tena na kuelekea kwenye Bar iliyaokuwa jirani na nyumbani kwake.

    Akiwa pale Bar Cosmas aliagiza pombe kali aina ya Konyagi chupa kubwa na kuanza kuinywa kwa tuo huku sura yake ikionesha dhahiri ana mawazo.

    Wakati ambao Cosma alikuwa pale Bar ambayo inafahamika kwa jina la ‘Tiger Toga’ Stella naye alikuwa kwenye Bar hiyohiyo, lakini safari hii akiwa ndani ya vazi tofauti na lile alilokuwa nalo mchana. Alikuwa ndani ya suruali ya dengrizi na fulana ya kike iliyom’bana kiasi na kuyafanya maungo yake yajichore juu ya nguo hizo alizovaa. Macho yake aliyafunika kwa miwani maridadi, na kichwani alijifunga kiremba kwa ustadi wa aina yake na kumfanya avutie kwa kila aliyemwona.

    Stella alikuwa amekaa umbali wa meza kadhaa kutoka kwenye meza aliyokuwa amekaa Cosmas. Kutokea kwenye meza hiyo aliyokaa, Stella aliweza kufuatilia kwa karibu nyendo zote za Cosmas.

    * ***





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog