Simulizi : Ahadi Ya Maisha
Sehemu Ya Pili (2)
Baada ya dakika kadhaa madaktari wengine watatu wakiwa na mmoja wao aliyeonekana kuwa mkubwa walitoka, mzee Innocent alinyanyuka toka kwenye kiti alichokuwa amekaa na kuhitaji kujua jambo liloendelea “Mzee Innocent wewe ni mwanamme, naamini uko tayari kwa mapokeo ya kila kitu…..” “unamaana mwanangu ameshakufa daktari” alidakia mzee Innocent kwa sauti iliyojaa mikwaruzo ya kulia.
“nahitaji utulivu, kiukweli mwanao ameshafariki na hivi naenda kuongea na mtu wa Mochuari aje kuchukua mwili wake hivyo jikaze wakati ukiangalia taratibu nyingine” alimalizia daktari huyo na kumfanya mzee Innocent na mkewe waishiwe nguvu na kukaa chini kabisa.
Walikuwa wakilia huku wakifarijiwa na watu waliofika hospitalini hapo asubuhi hiyo, bado walikuwa hawaamini kama ni kweli George alikuwa amekufa. Walianza kusaidiwa na watu hao kunyanyuliwa wakiwa na lengo la kuwaondoa hospitalini hapo. Wakati zoezi hilo likiendelea daktari Mutayoba alitoka katika chumba hicho alicholazwa George na alianza kukimbia kwa kasi kama alielekea sehemu. Mzee Innocent na mkewe hawakumtambua daktari huyo, akili zao zilikuwa kwenye maelezo ya mwisho kuwa mtoto wao alikuwa amefariki. Walisaidiwa na watu hao ambao wengi walikuwa marafiki wa mzee Innocent hadi nje na kupakizwa kwenye gari na safari ilianza kuelekea maeneo ya Bunju kwa ajili ya maandalizi ya mengine ya msiba huyo. Henry, mdogo wake mzee Innocent ambaye alikuwapo hospitalini hapo alipiga simu akiwaeleza mameneja wa viwanda vya mzee huyo kusimamisha shughuli zote za kibiashara zilizoendelea.
Daktari Mutayoba ndiye pekee alikuwa haamini kama kweli George alikuwa amefariki, alikuwa amebishana na madaktari wenzie ambao waliamua kumwacha kwani walimfahamu alikuwa na tabia ya ubishi. Ikiwa tayari taarifa ya kifo cha George imetolewa na daktari mkuu aliyefika eneo alilolazwa alitoka mbio katika chumba hicho akiwa na lengo la kwenda kuchukua vifaa vyake vingine vya kazi katika ofisi yake. Baada ya dakika kumi alikuwa anafungua mlango ambao ulikuwa wa chumba alicholazwa George, mkononi tayari alikuwa na vifaa alivyoeenda kuvifuata. Mara baada ya kufungua alishuhudia kitanda alichokuwa amelazwa kikiwa tupu jambo lililomfanya aamini tayari George alichukuliwa kupelekwa Mochuari. Hakukata tamaa kwani bado aliamini iliwezekana kuokoa maisha ya George, alitoka mbio akifuata upande uliokuwa na Mochuari akiamini mtu aliyemchukua bado alikuwa hajafika naye eneo husika.
“wewe vipi mrudishe huyo nani amekwambia umchukue?” alisikika Mutayoba baada ya kumuona muuguzi mmoja akisukuma kitanda alichobebwa George akiwa karibu na mlango wa Mochuari. “ebwana dokta Mutayoba tumeanza utani lini” alijibu muuguzi huyo akionesha kutotii. “ahh! nakwambia mrudishe huyu hajafa…..” aliongeza Mutayoba, kwa kasi alikivamia kitanda hicho na kuanza kukisukuma akirudi tena wodini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alikikimbiza kama vile George alikuwa mgonjwa aliyekuwa anawasili muda huo, jambo hilo lilimuacha muuguzi huyo katika mshangao akiamini daktari Mutayoba alikuwa amechanganyikiwa. Alimfuata nyuma kabla ya kumshuhudia akimrudisha George katika chumba ambacho awali alikuwa amelazwa. Muuguzi huyo alikuwa hajafurahishwa na zoezi hilo lililofanywa na daktari Mutayoba, aliamua kuelekea ofisi ya daktari mkuu ambaye alimpa agizo la kuutoa mwili wa George akiwa amekufa. Katika ofisi hiyo alikuta foleni ya watu kadhaa waliokuwa na nia ya kukutana na daktari huyo, aliamua kusubiri kwa robo saa kabla ya kupata nafasi yake. Bila kupoteza muda aliamua kuingia huku akimwona daktari huyo akiongea na simu.Mara baada ya kuketi aliendelea kumsubiri daktari huyo aliyegundua alikuwa akitoa taarifa ya kifo cha George kwa mtu fulani. “eeh ni hivyo George Innocent amefariki elewa hivyo basi….” Alimaliza daktari huyo kabla ya kukata simu yake. Muuguzi huyo aliamua kuanza kumueleza daktari huyo juu ya tukio zima alilokuwa amelifanya daktari Mutayoba.
“Mtayoba ameanza lini ubishi wa kiasi hiki yaani bado anabisha, mwenyewe nimehakikisha yule kijana kafariki anataka nini tena hata vyombo vya habari tumesha vitaarifu juu ya kifo hiki” alisikika daktari huyo akionekana kupandwa na hasira juu ya tukio hilo lililokuwa linaendelea. Aliwapigia simu madaktari wengine watano akiwa na lengo la kumjadili daktari Mutayoba na baada ya dakika kadhaa madaktari hao walifika ofisini hapo. “kazidi huyu huenda kachanganyikiwa, tumfuate” alishauri mmoja wao baada ya kuelezwa jambo lililokuwa limefanywa na daktari mwenzao. Walitoka ofisini hapo na kuanza kutembea wakielekea chumba ambacho awali George alikuwa amelazwa. Walitembea kwa haraka na hatimaye walifika katika mlango wa chumba hicho bila kupoteza muda daktari huyo mkuu aliyekuwa ameongozana nao alifungua mlango huo. Mara baada ya mlango huo kufunguliwa walimshuhudia Mutayoba akiwa anatokwa jasho kama kanyeshewa na mvua lakini vifaa alivyokuwa amefungwa George vilionesha alikuwa akipumua.
Madaktari hao walishtuka kushuhudia tukio hilo na hawakuamini kama ni kweli mtu aliyekufa alikuwa akipumua, bila kupoteza muda waliungana na Daktari Mutayoba katika harakati za kuokoa maisha ya George. Baada ya nusu saa walikuwa wametulia wakishuhudia mafanikio ya zoezi lao la kurudisha matumaini ya kupona kwa George. Daktari mkuu alionekana kuanza kujilaumu juu ya taarifa alizozitoa kwa wazazi wa George kuwa tayari mtoto wao alikuwa amefariki alitoka nje na kumpigia simu mzee Innocent. Simu ya mzee huyo iliita pasipo kupokelewa, alipiga kwa mara ya pili bado haikupokelewa akajaribu kwa mara ya tatu ikapokelewa na mtu mwingine.
“ Haloo! samahani George hajafa, tumemrudisha tena katika chumba chake aendelee na matibabu” alisikika daktari huyo akiongea huku akitetemeka. “wewe unauhakika na unachokiongea” iliuliza sauti ya mtu aliyeongea naye upande wa pili. “ndiyo nina uhakika mimi ni daktari”. “ebwana kweli? maana mzee Innocent na mkewe hawana fahamu hivi ninavyoongea” alisisitiza mtu huyo ambaye alionekana kutoamini aliyoelezwa.
“nakuhakikishia anapumua muda huu….” Aliongeza daktari huyo kabla ya kukata simu.
Madaktari walionekana kumpongeza mwenzao Mutayoba kwa kazi aliyokuwa ameifanya, walionekana wakijilaumu kwa zoezi lao la kukata tamaa dhidi ya kuokoa maisha ya George. Wakuu kadhaa wa makampuni ya mzee Innocent wakiongozwa na Henry walikuwa wa kwanza kufika hospitalini hapo wakiwa hawaamini kama George alikuwa hai. Mara baada ya kushuhudia ukweli wa maelezo hayo, walihitaji kupiga simu katika kituo kimoja cha redio kilichoweka kipindi maalum na cha ghafla kikielezea kifo cha George. Waliyasikia maelezo yote yaliyotolewa na watangazaji wa kituo hicho lakini simu yao ilikuwa imefungwa. Watangazaji wa redio hiyo walikuwa wakihusianisha kifo cha George walichokisikia na picha alizotolewa akiwa mtupu miezi kadhaa iliyokuwa imepita. Walidai George alichanganyikiwa na suala zima la picha hizo na zaidi kuachana kwake na mchumba wake wa zamani Winnie aliyekuwa na uhusiano mpya na mtoto wa waziri.
Baada ya maelezo mafupi ya watangazaji hao walihurusu simu za wasikilizaji wakihitaji mchango wao kuhusiana na kifo cha George. Henry akiwa na jazba juu ya kituo hicho kufuatilia maisha ya familia yao alifanikiwa kuwa mtu wa pili kutoa mchango katika kituo hicho cha redio. “eeh! Kaka una mchango gani juu ya kifo cha George Innocent?” Henry alipokelewa na swali hilo kutoka kwa mtangazaji wa kike wa kituo hicho cha redio.
“wewe dada huyo mtu mnaye mjadili hajafa, familia ya mzee Innocent haijatoa maelezo yeyote mnakurupuka, yupo hai na fungeni rasmi kipindi chenu”alisikika Henry kwa jazba na kukata simu, baada ya sekunde kadhaa watangazaji wa kituo hicho walisitisha kipindi hicho na kuendelea na ratiba yao wakidai wanautafuta ukweli zaidi wa tukio hilo.
Tayari watu kadhaa sehemu tofauti za Tanzania walikuwa wamepata taarifa za kifo cha mtoto wa tajiri George Innocent. Hiyo yote ilitokana na watu kupigiana simu mara baada ya kuelezwa George alikuwa amekufa zaidi ni taarifa aliyoitoa daktari mkuu katika redio moja juu ya kifo hicho. Baada ya nusu saa mzee Innocent akiwa na mkewe baada ya kurudiwa na fahamu walikuwa katika chumba alichokuwa amelazwa George, wote walikuwa hawaamini kama mtoto wao bado alikuwa hai. Walionekana wakimshukuru Mungu huku wakilia juu ya tukio hilo, kulikuwa na waandishi wengi wa habari waliokuwa wakihitaji kujua maendeleo ya George. Hiyo yote ilitokana na taarifa walizopewa awali kuwa alikuwa amefariki lakini ghafla walipata taarifa nyingine kuwa kijana huyo alikuwa mzima. Muda wote wakati mzee Innocent akilia alikuwa akivuta shati lake kwa hasira akiamini kila jambo lililoendelea kutokea dhidi ya mwanaye lilitokana na fitina alizofanyiwa magazetini.
Hatimaye waandishi wa habari walipata maelezo kamili juu ya suala hilo kwamba George hakufa na bado alikuwa hai. Walibakia ndugu na marafiki kadhaa wa George na wa familia hiyo kwa ujumla ambao nao walikuwapo hospitali hapo wakimfariji mzee Innocent na mkewe. Mzee huyo alikuwa amefurahishwa sana na kazi aliyokuwa ameifanya daktari Mutayoba na alimuahidi zawadi mara baada ya matibabu ya mwanaye. Baada ya wiki tatu katika hali iliyoonekana kuwa ni miujiza madakari walieleza kuwa ubongo wa George ulikuwa umerudi sehemu yake husika. Taarifa hizo zilianza kuwapa amani wazazi wake waliokuwapo hospitali hapo muda wote. Majeraha kadhaa aliyokuwa nayo yalikuwa yamepona kutokana na muda mrefu wa kuwepo hospitali hapo ingawaje alikuwa na fahamu kwa kiasi kidogo. George alikuwa amekonda kwa kiasi kikubwa na sehemu yake kubwa ya mwili ilikuwa imetawaliwa na mifupa hata sura yake ilionekana alikuwa kama mzee.
Siku moja wakati wa mchana muda ambao mzee Innocent alikuwa nje na chumba alicholazwa mwanaye akiwa na watu kadhaa alisikia kelele toka katika chumba hicho zilizompa hofu na kumfanya aende haraka. Mara baada ya kufungua mlango wa chumba hicho hakuamini macho yake mara baada ya kumwona George akiwa amekaa kitandani “Baba, baba aaah! Kwani vipi? tuko wapi na mama je? Kwa nini niko hivi?” yalikuwa maswali mfululizo yaliyotoka kwa George akimuuliza baba yake. Alikuwa ametoa mpira kadhaa aliyokuwa amefungwa huku akijishangaa, mzee Innocent alimkimbilia na kumkumbatia akipiga kelele za juu kwa furaha. Kelele hizo ndizo zilizowaongeza watu katika chumba hicho wakiwamo madaktari waliohitaji kujua afya ya George. Miongoni mwao alikuwapo mama yake George aliyepiga magoti chini akimshukuru mwenyezi Mungu kumuokoa mwanaye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Madaktari walifurahia ushindi wa kuokoa maisha ya George na baada ya wiki moja walimhurusu kurudi nyumbani kuendelea na matibabu wakiwa wamelidhia afya yake.
Furaha ya madaktari iliongezeka baada ya kuandikiwa hundi ya shilingi milioni kumi na mzee Innocent kama zawadi kwa kuokoa maisha ya mwanaye. Daktari Mutayoba ndiye aliyefurahi zaidi kwani alipewa zawadi ya gari la kutembelea aina ya ‘Mitsubish’. Mzee Innocent aliamini bila daktari huyo mwanaye angefia mochuari baada ya kuaminika kuwa alikuwa amekufa. Masaa machache baada ya kufika nyumbani walikuwa wakiamini kumbukumbu za George zilipotea kwani alikuwa hajamuulizia Winnie, msichana aliyempenda hata mara moja toka arudiwe na fahamu. Jambo hilo liliwapa faraja wazazi wake wakiamini angeanza maisha mapya pasipo msichana huyo baada ya miezi mitano ya kuumwa kwake.
Baada ya ukimya huo wa muda mrefu pasipo kumwongelea Winnie, George alivunja imani zao kuwa alikuwa amepoteza kumbukumbu “hivi mama Winnie ameshawahi kuja kuniaangalia, halafu yuko wapi maana sijamwona hospitali toka nirudiwe na fahamu” aliuliza George akionesha kujali jambo hilo “eeh! ameshawahi mara nyingi, usihofu kwa sasa yupo Ufaransa na familia yake lakini sina mawasiliano naye” Alijibu mama yake kwa ujasiri akihofia kuchanganyikiwa kwa George. Hakuwa tayari kumweleza mwanaye kuwa mtu aliyempenda alikuwa Ufaransa na mchumba wake mpya Frank Joseph aliyekuwa mtoto wa waziri. Aliamini mwanaye angeanza kuumwa tena juu ya taarifa hiyo, George alicheka kicheko cha furaha baada ya kuelezwa na mama yake kuwa Winnie alikuwa akifika kumtazama hospitali. Bado alikuwa na imani ya kurudiana na msichana huyo kwa vile aliona hakuwa na kosa juu mambo yote yaliyokuwa yametokea. Alikuwa anamsikiliza mama yake aliyemfariji siku zote akimwambia angeonana na Winnie, bado alikuwa na maumivu katika mguu wake wa kushoto aliokuwa amevunjika jambo lililopelekea atembee kwa kuchechemea.
Baada ya miezi kadhaa ya kuwapo jijini Paris, Ufaransa hatimaye Frank na Winnie waliamua kurudi nchini. Walionekana wakiwa na furaha na kwa kiasi kikubwa uhusiano wao ulionekana kuboreka, mara baada ya kufika waziri wa nchi mzee Joseph alikuwepo uwanja wa ndege na balozi wa Ufaransa nchini mzee Gregory. Wote kwa pamoja walikuwa wameenda kuwapokea watoto wao hao waliokuwa na uhusiano. Msafara huo wa mapokezi uliosindikizwa na magari kadhaa ulielekea nyumbani kwa waziri huyo maeneo ya Masaki kulikoandaliwa hafla fupi dhidi ya watu hao. Hafla hiyo ilifanyika na kufurahiwa na ndugu wa familia zote hizo mbili na wote walihitaji kushuhudia harusi ikifungwa. Frank na Winnie walikubaliana na mawazo hayo na kuongeza kuwa walirudi nchini kwa shughuli moja ya kufunga harusi.
Moyoni Winnie alikuwa na furaha katika uhusiano huo alikokuwa nao na Frank lakini haikuwa furaha ya aslimia zote. Bado kulikuwa na jambo gumu ambalo alishindwa kulisahau katika maisha yake, alikuwapo nchini Ufaransa kwa miezi kadhaa ili kusahau jambo hilo lakini alishindwa. George alikuwapo moyoni mwake ingawaje hakuwa tayari hata kidogo kuwa na kijana huyo, alishindwa kufuta upendo aliokuwa ameshaujenga. Alikuwa akiona ni bora aolewe na mtu mwingine lakini siyo George hiyo yote ilitokana na picha za utupu alizopiga ambazo zilitolewa magazetini miezi kadhaa iliyokuwa imepita. Jambo hilo ndilo lililopelekea apate hisia za kuolewa na Frank ili aendeleze zoezi la kumsahau George. Tayari kulikuwa na hafla ya kuvalishwa pete ya uchumba na Frank iliyokuwa imepangwa siku chache zilizofuata na taratibu za harusi ya kikristo zilishaanza kuchukua nafasi.
Baada ya wiki kadhaa George alikuwa amepona kabisa na muda wote alikuwa akishinda nyumbani kwao kama wazazi wake walivyomtaka afanye. Kulikuwa na watu wanne waliokuwa wameandaliwa kuhakikisha haondoki nyumbani kwao hapo lakini pia hakuna rafiki wa George aliyehurusiwa kuonana naye. Mara nyingi alikuwa na maswali kadhaa kwa mama yake juu ya Winnie na alipewa majibu ya kilidhisha yaliyomfanya aamini angerudiana na mrembo huyo. Alikuwa ameelezwa na mama yake kuwa Winnie bado alikuwa Ufaransa na alihitaji maongezi na George juu ya tukio lililotokea mara baada ya kurudi nchini. Akiwa nyumbani hapo alikuwa akitazama picha za Winnie na zawadi kadhaa alizopewa wakati wakiwa katika uhusiano wao. Alikuwa amejiandaa kwa kiasi kikubwa kumsimulia Winnie kila jambo alilolifahamu ambalo lilihusiana na picha zilizotolewa magazetini.
Siku moja wakati wa taarifa ya habari ya jioni katika kituo kimoja cha televisheni alisikia mtangazaji akielezea tukio la mtoto wa waziri kumvalisha pete mtoto wa balozi wa Ufaransa nchini katika maandalizi ya harusi yao. Taarifa hiyo ilimfanya George mapigo yake ya moyo yaanze kwenda mbio kabla ya kuisogelea luninga yao ili kushuhudia hafla hiyo. Hakuamini macho yake baada ya kuona mtu aliyekuwa akiamini ni mwanamke wa ndoto zake akivalishwa pete na rafiki yake mkubwa, mtoto wa waziri mzee Joseph. “Hapana! haiwezekani, haiwezekani Winnie aolewe mbele ya macho yangu” alisikika George kwa sauti ya juu akiwa haamini tukio zima alilokuwa amelishuhudia tayari machozi yalianza kumtoka na mishipa kadhaa ya hasira. Alitoka mbio kuondoka sebuleni hapo akionekana alikuwa na lengo la kufanya jambo aliongoza mpaka kwenye gari aina ya ‘Land Rover’ lililokuwapo eneo la maegesho ya nyumbani akiwa na lengo la kuondoka. Kabla hajaliwasha gari hilo vijana wanne walioandaliwa kumlinda walimzuia na kumtoa kwenye gari hilo wakati akilia kwa sauti kama mtoto mdogo. Alijitahidi kutumia nguvu kujitoa kwa vijana hao alishindwa na mwishoe walimfungia kwenye chumba chake cha kulala. Vijana hao waliomkamata walikuwa karibu na chumba hicho ili kuhakikisha hali ya usalama ya George na tayari walikuwa wamempigia simu mzee Innocent na mkewe wakiwaeleza juu ya tukio hilo.
“Frank! Frank rafiki yangu wa karibu anamwoa mchumba wangu, haiwezekani hata kama itagharimu damu nitajitoa, Winnie hawezi kuolewa” alisikika George akiongea peke yake huku akilia.
Baada ya muda mfupi mzee Innocent na mkewe walifika nyumbani kwao wakiwa na hofu tena juu ya afya ya mtoto wao. Mkewe mzee Innocent tayari alitambua uwezekano wa George kuutambua ukweli juu ya Winnie kwani siku zote hakumweleza mwanaye uhusiano wa msichana huyo na Frank aliyekuwa mtoto wa waziri. Walijitahidi kumshauri George kupunguza hasira na kusahau uhusiano aliokuwa nao awali na Winnie lakini ushauri huo haukusaidia. Hakuwa tayari kusahau na kuanza maisha mapya bado ndoto zake zilikuwa kwa Winnie. Jambo lililowapa hofu ni juu ya kauli yake aliyodai kuwa tayari kumuua Frank ili harusi yake isifungwe. Alimtaja kijana huyo kama msaliti wa kwanza kwani alikuwa na uhusiano na msichana ambaye alielewa jinsi alivyompenda.
Zoezi hilo la ushauri lilionekana kushindikana na George aliwaomba wamwache peke yake akionekana kutokuwa tayari kupokea ushauri wao. Hisia za kuua zilanza kumkaa kichwani, aliwaza kumuua Frank na mwishoe kujiua ili wote wamkose Winnie. Alipanga kufanikisha zoezi hilo siku iliyofuata, tayari aliandaa nondo moja ya kuitumia katika zoezi hilo. Siku iliyofuata majira ya saa kumi na mbili asubuhi aliamka na taratibu alianza kutoka nje ya nyumba yao akiwa amechukua kadi yake ya kuchukulia fedha benki na nondo mkononi aliyokuwa ameiandaa . Aliamini angefanikiwa kuondoka kwa vile vijana waliokuwa wakimlinda hawakuwapo nyumbani kwao wakati huo. Walikuwa wakifika kila siku asubuhi nakuondoka majira ya usiku nyumbani kwao hapo. Aliwaza kutumia gari la baba yake ili kumchanganya mlinzi wa getini adhanie baba yake ndiye alikuwa akiondoka. Mara baada ya kufika sebuleni alichukua ufunguo wa gari la baba yake katika sehemu ambayo funguo za magari ya familia yao zilikaa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alitembea taratibu akijongea mlango wa nyumba yao kabla ya kuufungua na kuelekea kwenye gari hilo la baba yake aina ya ‘Mercedez Benz’ akiwa na nondo yake. Mlinzi hakumwona kwa vile wakati huo alikuwa katika chumba chake kilichokuwa pembeni ya geti lao kuu. Aliwasha gari na kuliondoa kwa kasi akielekea geti kuu, “fungua mlango wewe, mlinzi gani unalala” alisikika George akiigiza sauti ya baba yake aliyoifahamu vizuri. Mlinzi huyo ambaye wakati huo alikuwa amelala alishtushwa na mlio wa gari hilo na mara baada ya kugundua lilikuwa la mzee Innocent alifungua geti haraka akihofia kugombezwa na mzee huyo.
Mara baada ya kufunguliwa kwa geti hisia za kuua ndizo zilikuwa zimemtawala kichwani kwani alilitoa gari hilo kwa kasi huku mawazo yakiwa yametawaliwa na sura ya Frank Joseph mtoto wa waziri. Aliendesha gari lake akiwa na lengo la kwenda nyumbani kwa waziri mzee Joseph lengo hasa lilikuwa kwenda kuanza kumfuatilia Frank ili mwishoe amfanyie mauaji. Alikuwa na hasira kupindukia akiwa amechukizwa na tabia ya rafiki yake huyo aliyeonekana kufurahia kuachana kwake na Winnie. Baada ya dakika kadhaa alikuwapo maeneo ya Mwenge ambapo aliongoza gari lake katika kituo kimoja cha kutoa fedha kilichokuwa cha benki yake. Hakutumia muda mrefu eneo hilo kwani hakukuwa na foleni yeyote asubuhi hiyo. Baada ya kuchukua fedha hizo aliwasha gari lake na kuliondoa kwa kasi akielekea maeneo ya Masaki eneo ambalo waziri wa nchi mzee Joseph alikuwa akiishi.
Hatimaye alifika katika nyumba ya kiongozi huyo ikiwa tayari saa moja asubuhi, aliliegesha gari lake eneo la mbali kidogo na geti la nyumba hiyo. Alikuwa akitafakari jambo la kufanya ili kuhakikisha anampata Frank, wakati akiendelea na mikakati hiyo alilishuhudia gari moja aina ya ‘Land Cruiser’ likitoka katika nyumba hiyo ya waziri. Gari hilo lililotoka likiendeshwa kwa kasi lilisimamishwa kando kidogo na geti hilo na George alimshuhudia Frank akishuka na kuanza kurudi nyumbani kwao kama alikuwa amesahau kitu. Hasira zilimpanda huku jasho likimtoka alishuka haraka akiwa na nondo mkononi lakini kabla hajamfuata, Frank alizamia kwenye geti lao.
George alitulia kidogo na kujaribu kupunguza hasira zake, aligundua zoezi lake lilihitaji utulivu wa kutosha hivyo kwa haraka alirudi tena kwenye gari lake. Alipanga kumsubiri Frank arudi kwenye gari lake ili amfuate eneo alilokuwa akielekea.Baada ya dakika kadhaa Frank alitoka nyumbani kwao na kuelekea moja kwa moja kwenye gari alilotoka nalo awali, aliliwasha na kuliondoa eneo hilo. Bila kupoteza muda George naye aliwasha gari lake na kuanza kumfuatilia Frank, alijitahidi kuwa mbali naye kidogo ili asigundulike. Tayari aliingiwa na hisia juu ya kijana huyo akiamini alikuwa anaelekea nyumbani kwa kina Winnie. Jambo hilo ndilo lilitokea baada ya muda mrefu wa kumfuatilia Frank aliishia eneo la ubalozi wa Ufaransa.
Hakufanya jambo zaidi ya kumsubiri atoke ili zoezi lake alilolipanga liweze kufanikiwa siku hiyo, alianza kuhisi uwezekano wa Frank kutoka na Winnie eneo hilo. Kifua chake kilikuwa kikimbana mara kadhaa kutokana na hasira alizokuwa nazo juu ya Frank. Alikaa eneo hilo kwa zaidi ya saa bila Frank kutoka na alianza kuhisi mambo mengine tofauti yaliyomwongezea hasira zaidi. Baada ya muda mrefu hatimaye gari la Frank lilitoka ubalozini hapo na kushika barabara iliyoelekea Posta. Alisubiri liondoke na mwishoe alianza kuendeleza zoezi lake la kumfuatilia Frank. Gari la Frank lilienda kuegeshwa katika kanisa moja kubwa la kikistro maeneo ya Posta eneo ambalo George naye aliegesha gari lake na kubaki ndani ili asigundulike. Ilikuwa tayari yapata saa nne asubuhi, alimshuhudia Frank akishuka katika gari lake kabla ya kuzunguka upande wa pili na kufungua mlango. George alishuhudia mguu wa kike ukitoka hatimaye mwingine na mwishoe alimwona Winnie aliyepokelewa kwa kukumbatiwa na Frank kabla ya kupigwa busu.
Akiwa ameshika nondo mkononi mwake bado alijihisi alikuwa akiota kwani mambo ambayo aliyaona kwenye televisheni yalikuwa yakiendelea. Alibaki ametoa macho wakati Frank na Winnie walikuwa wakitembea taratibu wakiwa wameshikana mikono na mwishoe waliingia katika kanisa hilo. George alianza kulia huku akiwa na hasira zilizoambatana na kwikwi, hakuwa tayari kushuhudia harusi hiyo ikifanyika hata kidogo. Tayari aligundua walifika kanisani hapo kwa ajili ya mafundisho ya ndoa, alibaki katika gari lake akiwa na hamu ya kutimiza lengo lake la kuua ndani ya masaa machache yaliyokuwa yamesalia. Baada ya muda walitoka na kuondoa gari lao, bila kucheklewa George naye alianza kuwafuata, waliongoza gari lao hadi katika hoteli moja iliyokuwapo maeneo ya Kunduchi. Wakati huu ndio George alijiapiza kuhakikisha anafanikisha mauaji aliyokuwa ameyapanga.
Alikaa nje ya hoteli hiyo kwa dakika kadhaa akijiandaa kwa lolote, mwishoe alishuka kwenye gari akiwa ameificha nondo aliyokuwa nayo katika shati alilokuwa amevaa. Alianza kutembea akizunguka katika hoteli hiyo baada ya muda alimwona Winnie akiwa anaogelea wakati Frank alikuwa kando na eneo hilo la kuogelea akimwongelesha. Alianza kujongea eneo alililokuwapo Frank taratibu kabla ya kumfikia na kumgusa bega katika hali ya kumwita wakati tayari akiwa ameiandaa nondo yake. Mara baada ya kugeuka kwake alipokelewa na nondo hiyo iliyompata sawasawa kwenye paji lake la uso. Frank alipiga kelele kwa maumivu juu ya tukio hilo akiwa haelewi jambo lililoendelea, akiwa bado hajatulia kwa kasi ya ajabu George aliendeza kumpiga kila eneo la mwili wake. Hakujali kelele zilizotolewa, na tayari Frank damu ilianza kumtoka sehemu tofauti za mwili wake akiwa ameanguka chini eneo alilokuwapo.
Winnie wakati akiwa anaendelea kuogelea alishtushwa na tukio hilo lililokuwa likiendelea dhidi ya mchumba wake, haikuchukua muda kumtambua George aliyekuwa akimpiga. Alianza kupiga kelele za kuomba msaada, wakati huo akiwa anahofia usalama wake pia alikuwa katika eneo alilokuwa anaogelea. Kelele zake na za mchumba wake Frank ziliwafikia watu waliokuwapo hotelini hapo ambao walikuwa wakijongea eneo husika. Kabla hawajafika George aliacha zoezi hilo na kuondoka kwa kasi akielekea eneo alillokuwa ameegesha gari lake ambalo aliliwasha na kuondoka eneo hilo. Watu waliofika eneo alilokuwapo Frank hawakuelewa chanzo kilichosababisha apigwe. Wachahe walimsaidia kwa kuondoka naye eneo hilo wakiwa na Winnie lengo likiwa ni kumwahisha kupata matibabu kutokana na majeraha aliyokuwa ameyapata baada ya kupigwa.
Frank alipelekwa katika zahanati moja iliyokuwapo maeneo ya Mbezi Beach ambako alipatiwa matibabu ya awali, alikuwa na hasira dhidi ya George akiamini alidhamiria kumuua. Alikuwa amefungwa na pamba majeraha kadhaa aliyokuwa nayo na aliingiwa na hisia za kuhakikisha George anaenda Jela na zaidi aliwaza kupanga kifo chake akiwa huko. Usoni alikuwa havutii kwa vile alikuwa na uvimbe kwenye paji lake la uso baada ya kupigwa na nondo. Alikuwa amewekwa kamba iliyopita shingoni mwake iliyoshikilia mkono wake usicheze cheze baada ya kuteguka. Wakati huo Winnie alikuwa akilia huku akionekana kumchukiahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/ George kwa kila jambo alilofanya, moyoni aliamini hakuwa na nafasi ya mwanaume huyo. Frank alichukua simu yake na kumpigia baba yake Mzee Joseph aliyekuwa waziri nchini, alimweleza juu ya kila jambo lililokuwa limetokea. Wakati akiendelea na mazungumzo hayo alianza kutembea kuelekea kando kidogo na eneo alilokuwapo Winnie, aliendelea kuongea kwa kumsisitiza baba yake kuhakikisha George anafia Jela.
Mzee Joseph ambaye alikuwa na historia ya uovu katika siasa nchini, alimwahidi mwanaye kuwa angehakikisha George anafia Jela. Kuthibitsha hilo alimweleza angetoa agizo ili George akamatwe mara moja. Alionyesha kuumia juu ya tukio hilo la mwanaye kupigwa na alihitaji mhusika ambaye alikuwa mtoto wa tajiri aadhibiwe ipasavyo. Hakuonyesha hofu dhidi ya mzee Innocent ambaye alikuwa tajiri mkubwa nchini akiwa baba mzazi wa George. Hatimaye waliondoka katika zahanati hiyo huku Winnie akitoa msisitizo kwa Frank kuhakikisha George anachukuliwa hatua kisheria. Walikuwa wanaamini kuwa harusi yao isingefungika kama mtu huyo angekuwapo huru kuishuhudia. Kuna wakati Frank alihisi siri ya uovu alioufanya dhidi ya George ilikuwa imevuja lakini alijipa matumaini akiamini mtu wa kwanza kuelezwa siri hiyo angekuwa Winnie.
* * * *
Baada ya kuondoka na gari lake eneo la tukio George hakuwa na furaha na zaidi hakujali juu ya tukio zima alilokuwa amelifanya. Bado alijiona hakufanya zoezi hilo ipasavyo, lengo lake lilikuwa kumuua Frank lakini mazingira aliyomvamia ndiyo yaliyofanya zoezi hilo kuwa gumu. Alikuwa akiwaza kufanya maandalizi zaidi ili kuhakikisha anatimiza lengo lake wakati huo alikuwa amepanga kuondoka nyumbani kwao baada ya kuamini lazima angetafutwa. Alihitaji kwenda kuchukua vitu vyake muhimu nyumbani kwao na hatimaye aliwaza kwenda sehemu yeyote kwa ajili ya kufichama ili kujiandaa na zoezi la kukatisha uhai wa Frank.
Mara baada ya kufika nyumbani kwao alipiga honi ya gari lake mara mbili na geti lao lilifunguliwa aliongoza gari alililokuwa nalo mpaka sehemu ya maegesho. Kabla hajashuka kwenye gari hilo alishtushwa na gari la askari lililokuwa limeegeshwa pembeni kidogo na lake alilokuwa nalo. Tayari hisia za shari zilimwingia kichwani na kuamua kuwasha tena gari alilokuwa nalo lengo likiwa kuondoka eneo hilo la nyumba yao. Kabla hajaliondoa gari hilo, ghafla alimshuhudia askari mmoja akiwa mbele ya gari lake na bunduki aliyokuwa ameielekeza kwake sawasawa. Baada ya sekunde chache askari wengine wanne waliongezeka na kumtaka ashuke kwenye gari. Bila kupoteza muda George alishuka kwenye gari kabla ya kunyosha mikono juu kuashiria kukubaliana na agizo alilopewa.
Mzee Innocent na mkewe walitoka ndani ya nyumba yao ambako pia askari hao walikuwapo, mkewe alianza kulia baada ya kushuhudia mtoto wao akifungwa pingu na askari hao waliofika kumkamata. Baada ya kufungwa pingu George alipakizwa kwenye gari ambalo walikuwa wamefika nalo askari hao na safari iliaanza kuelekea kituo cha polisi. Mzee Innocent alionekana kusononeka kwani tayari alikuwa amepewa taarifa za kupigwa kwa mtoto wa waziri na mwanaye na aliamini ilikuwa vigumu kwa George kukwepa hukumu ya zoezi hilo. Hiyo ilitokana na imani yake kuwa waziri huyo angefanya kila awezalo ili mwanaye aende jela. Mbali na utajiri wake alielewa hakuwa na uwezo wa kuishawishi mahakama kumsamehe mwanaye kama waziri mzee Joseph alivyoweza kumgandamiza mwanaye. Aliamua kumfariji mkewe na kumpa imani ya kufanikiwa dhidi ya tatizo hilo walilokuwa wamekumbana nalo. Aliwapigia simu wanasheria wake kadhaa akiwataka wahakikishe mwanaye anapewa dhamana siku hiyo.
Baada ya kuwapigia simu mzee Innocent aliondoka eneo hilo nyumbani kwake akiamini alihitajika kufanya jambo. Akiwa anaendeshwa na dereva wake alimweleza ampeleke nyumbani kwa waziri wa nchi mzee Joseph akiwa na nia kubwa ya kuongea naye na zaidi kumwomba msamaha juu ya tukio alilofanya mwanaye. Aliamini iliwezekana kukutana na waziri huyo kwani alishafanya hivyo mara kadhaa zaidi utajiri wake ulikuwa kigezo mara nyingi kukutana na viongozi tofauti wa serikali. Baada ya muda mzee Innocent na dereva wake walikuwa nje ya geti kuu la nyumba ya waziri huyo iliyokuwa maeneo ya Masaki. Hawakuhurusiwa kuingia katika nyumba ya kiongozi huyo kwa vile hakuna taarifa iliyokuwa imetolewa dhidi ya ujio wao. Bila kupoteza muda mzee Innocent alichukua simu yake na kumpigia kiongozi huyo katika namba yake ya simu ya mkononi. Simu hiyo iliita lakini ilikuwa haipokelewi, alipiga kwa mara ya pili haikupokelewa pia, alipojaribu kwa mara ya tatu akiwa amekata tamaa simu hiyo ilipokelewa. “halloo mheshimiwa Joseph niko nje ya geti lako nahitaji kuongea na wewe…”alisikika mzee Innocent mara baada ya simu hiyo kupokelewa. “jambo unalotaka kuliongelea mimi nimeshalifahamu kwa hiyo usijisumbue,tuiachie mahakama ndio itatoa hukumua..” aliongea waziri huyo kabla ya kukata simu.
Mzee Innocent alibaki kimya huku akionyesha kutofurahishwa na jibu alilopewa, tayari aligundua kulikuwa na mipango kadhaa dhidi ya mwanaye. Alimshangaa mzee Joseph kwa kukosa utu na kukataa waongee juu ya tatizo lililokuwa limejitokeza kwa watoto wao. Alibaki kimya akiwa hajamweleza kitu dereva wake, ghafla simu yake ya mkononi iliita alipoitazama aligundua mpigaji alikuwa mwanasheria aliyehusika na kampuni yake. Aliipokea simu hiyo akiamini ilikuwa inahusu dhamana aliyowahurusu wamchukulie mwanaye, baada ya dakika mbili za mazungumzo mzee Innocent alionekana kuchanganyikiwa zaidi kwani dhamana dhidi ya mwanaye ilikuwa imezuiliwa. Alielezwa kesi dhidi ya mwanaye ilikuwa imepangwa kufanyika ndani ya siku tano zilizofuata.
Alimhurusu dereva aliyekuwa naye kuondoa gari eneo hilo la nyumba ya waziri wa nchi mzee Joseph. Mzee Innocent wakati huu alianza kuhisi mambo mengi tofauti hasa kubwa lililohusiana na kuwahishwa kwa kesi ya mwanaye, aliamini kulikuwa na hali ya ugandamizajia ambayo ingejitokeza. Kesi nyingi nchini zilikuwa zikicheleweshwa hadi miezi sita lakini ya mwanaye ilitajwa mapema jambo lililoashiria kuingia kwake jela ndani ya wiki moja. Wakati huo hakuwa na jambo aliloliwaza zaidi alikuwa anaongozwa na dereva wake kurudi nyumbani, alihitaji kwenda kutuliza kichwa chake kabla ya kuwaza jambo jipya la kufanya. Zaidi aliwaza kuwashirikisha rafiki zake kadhaa ili wamsaidie kumshauri dhidi ya tatizo hilo lililompata mwanaye.
Jioni ya siku hiyo akiwa nyumbani kwake walifika marafiki zake kadhaa ambao kwa pamoja walikuwa wakishauriana mambo tofauti juu ya kukamatwa kwa George. Wengi wao wakiwa na uwezo kifedha kama yeye walitoa wazo la kuhitaji kukutana na Waziri wa nchi mheshimiwa Joseph siku iliyofuata. Mzee Innocent alishukuru sana kwa msaada wao akiamini wangemsaidia kwa kiasi kikubwa, siku iliyofuata rafiki zake hao nyakati za asubuhi walienda kwa waziri huyo. Mzee Innocent alikuwa akisubiri kwa hamu na mkewe akiamini wangepokea taarifa nzuri iliyohusiana na mazungumzo hayo lakini muda wa mchana walipigiwa simu wakielezwa waziri huyo alikataa maongezi yeyote yaliyomhusu George.
Mzee Innocent alichanganyikiwa kabisa akionekana kusubiri siku ya kesi ya mwanaye ifike ili hatma ipatikane. Hakuwa na imani juu usalama wa mwanaye hata kidogo, kwani fitina za wazi zilionekana ikiwa ni pamoja na kukatazwa kwao kumtembelea mtoto wao. Bado waliamini kuwa chanzo cha mambo hayo kilikuwa ni picha ambazo mtoto wao alifanyiwa hila akiwa katika mwonekano usio na maadili akiwa chuo kikuu. Siku ya kesi hiyo iliyopangwa kuanza kusikilizwa katika mahakama ya hakimu mkazi iliyokuwapo maeneo ya Kinondoni ilifika, mzee Innocent na mkewe pamoja na wafanyakazi wake wengi waliwahi kufika mahakamani hapo. Alikuwa pia ameongozana na wanasheria wake kadhaa, mahakamani hapo kulikuwa na vijana kadhaa ambao walifahamiana na George, pia kulikuwa na waandishi kadhaa wa magazeti ambao ziku zote walifuatilia maisha ya George.
Majira ya saa tatu na nusu gari la watuhumiwa ambao kesi zao zilipaswa kusomwa liliwasili mahakamani hapo. Hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyehurusiwa kushuka wakati kulikuwa na ulinzi mkali wa askari waliokuwapo, baada ya dakika kadhaa ziliwasili gari mbili za kifahari. Gari la kwanza alishuka waziri wa nchi mheshimiwa Joseph akiwa na watu wawili waliovaa suti nyeusi za kufanana ambao bila shaka kila mtu aliwatambua kuwa walikuwa walinzi wake. Gari jingine alishuka mwanaye waziri huyo yani Frank akiwa amefungwa majeraha kadhaa, aliongozana na mchumba wake Winnie pamoja na watu wengine watatu ambao hawakujulikana. Mzee Innocent wakati mapigo ya moyo yakimwenda mbio huku akishuhudia tukio hilo, ilisikika sauti ya askari mmoja aliyeeleza kuwa muda wa kusikilizwa kesi ya kwanza ambayo mtuhumiwa wake alikuwa George Innocent ulikuwa umefika.
Walianza kuingia katika eneo husika ambalo kesi hiyo ilipaswa isikilizwe, baada ya zoezi hilo kukamilika aliingia George katika chumba hicho kujibu mashtaka akiwa ameongozana na askari mmoja. Watu walionekana wakimshangaa kwa jinsi alivyokuwa mchafu, zaidi alikuwa na majeraha ya wazi wazi yaliyoonekana mwilini. Nguo zake zikiwa zimechanika ovyo zilikuwa na damu kama vile alipokea kipigo muda mfupi kabla ya kufikishwa kizimbani hapo. Alikuwa amedhoofu kama vile alikuwapo jela kwa miezi kadhaa. Jambo hilo ndilo lililomfanya mzee Innocent na mkewe wahuzunike kwa kiasi kikubwa. Kesi hiyo ilianza kuendeshwa wakati waziri huyo naye akiwa anaisikiliza, watu waliofika mahakamani hapo na Frank walikuwa mashahidi na walitoa ushahidi wao ulioonyesha George kuhusika kwa aslimia zote na tuhuma alizosomewa.
Jambo lililowashangaza watu waliohudhulia kesi hiyo lilitoka kwa George, hakuongea jambo lolote tangu kuanza kusomewa kwake kwa mashtaka hayo zaidi ya kulia. Jambo hilo lionyesha kumuudhi jaji aliyeendesha kesi hiyo ambaye toka mwanzo wa kesi hiyo alikuwa na haraka ya kutaka kutoa hukumu dhidi ya George. Hatimaye mwisho wa kesi hiyo ambayo waziri wa nchi mzee Joseph alionekana kuhusika ulifika na George alisomewa kifungo cha miezi sita Jela kwa kosa alilokuwa amelifanya. Watu kadhaa walisikitishwa na hukumu hiyo jambo lililowafanya wainamishe vichwa vyao kwa huzuni, mzee Innocent na mkewe walikuwa wakitokwa na machozi ingawaje walijizuia wasilie kwa sauti.
George alikamatwa na askari husika wa magereza ambaye aliondoka naye toka chumba hicho ambacho hukumu yake ilitolewa na alipaswa kuelekea gereza la Ukonga kutumikia adhabu yake hiyo. Waziri wa nchi mze Joseph alisimama na kuanza kutembea kutoka nje ya eneo hilo, alikuwa na uso uliotawaliwa na tabasamu juu ya maamuzi ya kesi hiyo alikuwa akifuatwa na mwanaye ambaye pia alikuwa katika furaha hiyo. Winnie ndiye alikuwa wa mwisho akiwafuata nyuma, alionesha hali ya huzuni iliyoambatana na aibu wakati akipita mbele ya mzee Innocent na mkewe. Hakuwa na furaha kama ilivyokuwa kwa wenzie aliongozana nao, hata muda wote wakati kesi hiyo ikiendeshwa alikuwa mtulivu akionekana kama alilazimishwa kufika eneo hilo.
Hata wakati akiwa nje kabla ya kuondoka eneo hilo la mahakama rafiki zake kadhaa waliokuwapo walimwita lakini aliwapuuzia akionesha kutokuwa na furaha. Mzee Innocent akiwa na wafanyakazi wake waliondoka na magari yao mara baada ya kumshuhudia George akiwa ameondoka na gari la magereza. Mzee huyo alijipa moyo huku akionesha ujasiri baada ya kuamini kwa muda mrefu kuwa kesi hiyo ingegandamizwa na waziri. Safari yao ilielekea nyumbani kwake maeneo ya Bunju na hakuwa na jinsi huku akiwaza njia nyingine ya kujaribu kumsaidia mwanaye.
* * * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya wiki mbili hakuna jitihada zozote ziliofanyika ili kumwokoa George akiwa Jela. Tayari mzee Innocent na mkewe walionekana kukubaliana na hukumu iliyotolewa huku wakisubiri mtoto wao atoke Jela. Henry akiwa baba yake mdogo wa George ambaye alikuwa ameishi naye kwa miaka mingi hakuwa tayari hata kidogo juu ya tukio lililokuwa limempata mwanaye. Alipanga kufanya jambo kama malipizi dhidi ya kijana Frank aliyeamini alihusika katika kuharibu maisha ya mtoto wao George. Kufanikisha malipizi ya kifungo alichokuwa amekipata George alianza kwa kutafuta namba ya simu ya kijana huyo. Halikuwa zoezi gumu, hiyo ilitokana na uwezo wa kifedha na umaarufu wa kaka yake mzee Innocent jambo lililopelekea aipate namba hiyo kirahisi. Wazo lake kubwa lilikuwa ni kuhakikisha anamteka kijana huyo na mwishoe kufuatilia kwa undani siri alizokuwa nazo. Kufanikisha hilo alimpigia simu akijieleza kuwa alikuwa rafiki yake waliyemaliza wote chuo kikuu cha Dar es salaam katika kitivo cha sheria. Frank alionesha kutokumfahamu kabisa Henry, hakukubaliana naye hata katika ombi lake alilotaka wakutane.
Alimweleza Henry kuwa alikuwa amebakiwa na kipindi cha mwezi mmoja ili harusi yake ifungwe na mchumba wake Winnie. Hivyo alidai muda mwingi alikuwa katika mafundisho ya ndoa na zaidi katika maandalizi ya harusi hiyo. Henry alilidhishwa na maelezo hayo aliyopewa na aliamini alikuwa amepata njia ya kumnasa Frank. Aliwaza kumteka akiwa katika kanisa hilo la kikistro lililokuwapo maeneo ya Posta, kufanikisha hilo alimtafuta jambazi mmoja aliyekuwa maarufu jijini akiwa na lengo la kusaidiana naye. Siku ya Jumatatu majira ya asubuhi walifika katika kanisa hilo wakifuata ratiba waliyopewa ya mafundisho hayo ya ndoa. Walikuwa wamechelewa kwa dakika kadhaa na wanandoa watarajiwa walikuwapo tayari kanisani kwa mafundisho hayo. Tayari zoezi lilionekana kuanza kuwa gumu kwani jambazi huyo aliyekuwa ameongozana naye ndiye alipaswa kufanya kazi ya kumteka Frank baada ya kuonyeshwa na Henry ambaye alimfahamu.
Henry alitatua hofu hiyo na kumtaka jambazi huyo aliyejengeka mwili wake kwa misuli aandae gari lao sawasawa na yeye alidai angefanikisha zoezi hilo la kumteka. Aliondoka akitembea kuelekea ndani ya kanisa hilo, alikuwa ameweka bastola aliyopewa na jambazi aliyeongozana naye katika koti lake la suti. Aliwaza kuitumia bastola hiyo katika zoezi zima la kumteka Frank, akiwa ametembea umbali mfupi ndani ya kanisa hilo hakuona dalili zozote za kuwapo kwa watu waliopewa mafundisho hayo. Jambo lililomfanya amwulize mtumishi mmoja aliyekuwapo kanisani hapo “huwa hawafanyii humu kuna chumba maalumu kwa ajili ya mafundisho hayo njoo nikuonyeshe….” Alisikika mtumishi huyo kabla kuanza kutembea wakitoka nje tena mara baada ya kutoka alioneshwa eneo ambalo mafunzo hayo yalikuwa wakitolewa.
Henry alimwonyeshea ishara jambazi aliyekuwa naye eneo hilo, alimwelekeza asogeze gari upande huo ambao kulikuwa na chumba hicho cha mafundisho hayo ya ndoa. Baada ya kuona zoezi hilo lilikuwa likitekelezwa na jambazi huyo alianza kutembea kuelekea kwenye chumba hicho huku akijiamini. Alisikia sauti za mtu aliyeonekana alikuwa akitoa mafundisho hayo, alijongea mlango husika na kuufungua taratibu pasipo kelele zozote. Alimshuhudia mtu aliyevaa kitumishi akiwa mbele ya wanandoa hao akiendelea kutoa mafundisho hayo. Mtumishi huyo alimwona Henry lakini wanandoa hao watarajiwa walikuwa kimya huku wakiwa wanamtazama mbele.
Alianza kuzungusha macho kwa haraka akimtafuta Frank huku kwa aslimia kubwa alikuwa akiangalia vichwa kwa nyuma na migongo ya wanandoa hao watarajiwa. Baada ya sekunde kadhaa alimwona Frank aliyekuwa mstari wa viti vya nyuma kabisa katika chumba hicho. Alikuwa amekaa huku akifuatana na Winnie katika mstari huo. Akiwa hajashtukiwa na mtumishi aliyekuwapo alianza kutembea taratibu pasipo kelele za vishindo vyake. Alitembea mpaka alipokuwa pembeni kidogo na eneo alilokuwapo Frank na Winnie. Kwa makusudi alikohoa kwa nguvu na kuwashtua wanandoa hao watarajiwa ambao hawakuwa wakiutambua uwepo wake. Wote waligeuka wakimwangalia, kwa haraka aliingiza mkono wake kwenye koti lake la suti na kutoa Bastola. “wote laleni chini kwa usalama wa maisha yenu……” aliongea kauli ambayo bado akili za watu zilikuwa hazijatulia ingawaje tayari kuna wanawake walioanza kupiga kelele za yowe.
“sihitaji kelele za aina yeyote kwani sijafika hapa kuua wasio na hatia” alimalizia kauli yake kwa mara ya pili ambayo ilieleweka vizuri kwani tayari akili za watu zilitambua kulikuwa na shari eneo hilo. Watu wote walikuwa wamelala sakafuni wakihofia kuuawa kama walivyokuwa wameelezwa.
Henry aliendelea kusisitiza kauli yake huku watu kadhaa waliotetemeka kwa hofu wakiwa tayari wamejisaidia haja ndogo. Bila kupoteza muda alimsogelea Frank na kumnyanyua alikuwa anatetemeka kupindukia lakini hali hiyo ilizidi kwa Winnie aliyekuwa anashindwa kuinua hata mkono huku naye akitetemeka kwa hofu. Akiwa ametoa macho na kushindwa kuinua hata mdomo alimshuhudia mtu aliyefika eneo hilo akimvuta Frank taratibu na walikuwa wakitoka eneo hilo kuelekea nje. “atakaye thubutu kunyanyuka nampasua kichwa kwa risasi…” alisisitiza Henry akiwa amempiga roba ya nguvu Frank kwa mkono wake wa kushoto wakati mwingine alimgusa na bastola aliyokuwa nayo katika mbavu zake akimsihi atulie.
Mara baada ya kutoka nje jambazi aliyekuwa naye alisogeza gari na kwa kasi ya ajabu Frank alipakizwa kwenye gari hilo aina ya Land Cruiser katika siti za nyuma ambako Henry naye aliingia akiwa bado amemwonyeshea Frank Bastola aliyokuwa nayo. Bila kupoteza muda gari hilo liliondolewa kwa kasi eneo hilo la kanisa likiendeshwa na jambazi aliyeongozana na Henry. Walipanga kuelekea wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ambako Henry lengo lake kubwa lilikuwa hasa kwenda kumpeleleza kwa undani Frank akiamini mtoto huyo wa waziri alihusika na kila kitu dhidi ya George. Muda wote wakati gari hilo likiendeshwa na jambazi huyo, Frank alikuwa amekaa huku akiwa ameinana kama alivyoamriwa na Henry. Alikuwa haelewi sehemu waliyoelekea na zaidi hofu ndiyo iliyomzidia alikuwa akihisi alikuwa na muda mfupi wa kuishi duniani.
Baada ya kumteka Frank katika eneo hilo la kanisa watu wote waliokuwamo humo walibaki wamelala sakafuni huku wakiamini mtu aliyewaamru kufanya hivyo alikuwa yupo eneo hilo. Mtumishi mmoja wa kanisa hilo alipokuwa akipita alishtushwa na mwonekano mzima wa chumba hicho jambo lililopelekea aingie. Alianza kwa kuwauliza jambo lililowafanya wawe katika mwonekano huo, baada ya dakika kadhaa watu hao waligundua mtu aliyewapa amri hiyo hakuwapo eneo hilo. Kelele za vilio zilianza kutoka kwa wanawake waliokuwapo eneo hilo juu ya tukio zima lililotishia uhai wao katika dakika kadhaa zilizokuwa zimepita. Winnie ndiye aliyelia kwa sauti kupindukia akieleza kuwa mchumba wake alikuwa ametekwa katika tukio hilo, baada ya muda wakati mjadala wa jambo hilo ukiendelea kanisani hapo askari walifika baada ya kupewa taarifa.
Askari hao walipewa maelezo kuhusiana na tukio hilo na waliahidi kuanza msako dhidi ya watu waliohusika na zoezi hilo hasa baada ya kugundua mtu aliyetekwa alikuwa mtoto wa waziri. Baada ya muda mrefu wa kulia hatimaye Winnie alitulia na aliamua kutoa taarifa za tukio hilo kwa waziri mhesimiwa Joseph lakini alifanya hivyo pia kwa familia yake. Moyoni alikuwa anaumia kwa nini baba yake mzee Gregory alipangwa kuwa balozi nchini kwani jambo hilo aliamini lilipelekea akutane na watu waliozidi kuharibu maisha yake. Hata wazo lake la kuolewa ili amsahau George alianza kuhisi halikuwa la busara kwa vile moyoni aliumia kwa kila jambo lililoendelea kwa kijana huyo.
Winnie alielewa jinsi kesi ya George ilivyoendeshwa huku nia kubwa ikiwa ni kumgandamiza, kuna wakati alianza kuhisi endapo George angefia gerezani basi na yeye alihusika. Akilini alianza kuamini jambo pekee ambalo awali alipaswa kufanya baada ya kudhalilishwa na George lilikuwa ni kukaa peke yake pasipo mahusiano. Hakuwa na jinsi kwa wakati huo kwani tayari harusi yao ilikuwa katika hatua za mwisho. Siku zote hakuelewa kwa nini kumbukumbu zake dhidi ya George mbali na uovu wake zilikuwa hazifutiki. Mpaka jioni ya siku hiyo hakukuwa na taarifa yeyote iliyokuwa imetolewa dhidi ya kutekwa kwa Frank jambo lililoanza kutoa hofu kwa familia yake. Tayari mzee Innocent alikuwa akishikiliwa na jeshi la polisi baada ya maelezo ya waziri kuonesha alikuwa akimhisi vibaya tajiri huyo.
* * * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment