Search This Blog

Friday, October 28, 2022

HOLLY SIN (DHAMBI TAKATIFU) - 4

 

     





    Simulizi : The Holy Sin (Dhambi Takatifu)

    Sehemu Ya Nne (4)





    “Nitauficha wapi uso wangu mimi? Mwanaume umenitia aibu wewe sina hamu. Lazima utatoa talaka yangu,” alisema mama Aidan wakati mumewe akitokomea kusikojulikana. Hakutaka hata kuondoka na gari, akatembea kwa miguu mpaka barabarani alikosimamisha teksi.

    “Unaelekea wapi mzee?”

    “Nipeleke Cross Bar,” alisema baba yake Aidan kwa sauti iliyoonyesha wazi kwamba ameamka na pombe kichwani.

    “Cross Bar asubuhi huwa hawafungui!”



    “Kijana, nipeleke Cross Bar, sitaki maelezo wala hadithi za sungura na fisi,” aling’aka mzee Kenan huku akiyumbayumba, akapanda kwenye bodaboda na safari ya kuelekea Cross Bar ikaanza.

    Baada ya muda, tayari mzee Kenan alikuwa amefika Cross Bar, japokuwa baa hiyo aliyozoea kunywa pombe ilikuwa imefungwa kwani bado ilikuwa ni asubuhi sana, aliwagongea wahudumu waliokuwa wakilala vyumba vya uani ambapo waliamka na kumsikiliza.

    “Nataka bia tatu za baridi na mzinga mkubwa wa pombe kali.”

    “Mh! Leo mbona mapema mzee Kenan, kuna usalama kweli huko utokako?”



    “We leta pombe, hayo mengine hayakuhusu,” aling’aka mzee huyo, bila hiyana mhudumu akamletea chupa tatu za bia alizoanza kuzigida kwa fujo. Nusu saa tu baadaye, chupa zote tatu zilikuwa tupu.

    “Niongeze nyingine kama hizi,” alisema mzee Kenan kwa sauti iliyoonyesha wazi kwamba pombe zilikuwa zimemkolea. Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, aliendelea kunywa pombe kwa fujo, ilipofika saa nne za asubuhi, tayari alikuwa tilalila mithili ya mtu aliyeamka na pombe kichwani tangu jana yake.

    “Una nini leo mzee Kenan, siyo kawaida yao kupiga mitungi asubuhi yote hii, ina maana leo huendi kazini?”

    “Hivi kwa nini hamnielewi nyie vijana? Nimesema sitaki maswali ya aina yoyote,” alifoka mzee Kenan kwa sauti ya kilevi, wahudumu ambao ndiyo kwanza walikuwa wakitoa viti kwa ajili ya kuanza kufungua baa hiyo, ilibidi wafyate mkia, wakaendelea kumhudumia mzee Kenan ambaye ndani ya muda mfupi tu, alikuwa amelewa chakari.



    Licha ya kulewa, bado kumbukumbu za tukio alilolifanya usiku uliopita, ziliendelea kukisumbua kichwa chake, mara kwa mara akawa anaweweseka na kutamka maneno yasiyoeleweka.

    Akiwa katika hali hiyo, alishtuka baada ya kuona gari la polisi likija na kupaki mbele ya baa hiyo, askari wanne wenye silaha wakateremka na kuanza kuangaza macho huku na kule.

    “Yule pale,” askari mmoja alisema, kufumba na kufumbua askari hao wakamvamia mzee Kenan ambaye tayari alikuwa amelewa sana, wakamkamata na kumfunga pingu, wakawa wanamkokota kama kondoo anayepelekwa machinjioni.

    “Kwani nimefanya nini jamani?”
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Utaenda kujua ukifika kituoni, mbakaji mkubwa wewe,” alisema askari mmoja, kauli iliyompa picha mzee Kenan, akaelewa kilichokuwa kinaendelea.



    “Mtu mzima naumbuka leo, yaani mimi ni wa kukamatwa na polisi kwa kesi ya ubakaji,” alisema chinichini mzee Kenan wakati akipakizwa kwenye difenda, safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza huku mikononi akiwa na pingu.



    Alipofikishwa kituoni, alishangaa kumkuta mkewe akiwa chini ya ulinzi wa polisi huku baba na mama Caro pamoja na binti yao nao wakiwa wamekaa pembeni, nje kidogo ya kituo hicho.

    Kwa jinsi alivyojisikia aibu kuwakuta wazazi wa Caro wakiwa na binti yao, nje ya kituo hicho, mzee Kenan alitamani ardhi ipasuke na kummeza, akashushwa msobemsobe kwenye gari la polisi na kuingizwa ndani ya kituo hicho. Wakati akiingizwa mahabusu, mkewe alifunguliwa na kuachiwa huru, wakakutana uso kwa uso kwenye korido ya kituo cha polisi.



    “Ukifanikiwa kutoka, nataka talaka yangu, siwezi kuvumilia upuuzi huu, nini ulichokosa kwangu mpaka ukaamua kwenda kubaka, hunifai tena,” alisema mama Aidan huku akilengwalengwa na machozi.

    Mzee Kenan alishindwa cha kujibu, akaingizwa mahabusu na geti la chuma likabamizwa kwa nguvu kisha likafungwa kwa kufuli kubwa. Huo ukawa mwanzo wa maisha mapya ya mzee Kenan.

    ***

    Aidan akiwa bado ameduwaa baada ya kukuta nguo ya ndani ya kike kwenye gari la baba yake, alijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Kitu kingine kilichozidi kumshangaza ni baada ya kukuta hakuna mtu nyumbani kwa akina Caro. Maswali yalikuwa mengi kuliko majibu.



    Akiwa amezama kwenye dimbwi la mawazo, alishtuliwa na sauti ya mama yake aliyeingia ndani ya nyumba yao huku akiangua kilio. Harakaharaka aliacha kila alichokuwa anakifanya, akaelekea sebuleni kutaka kujua ni kitu gani kilikuwa kimemsibu mama yake kwani hakuwahi kumsikia akilia hata mara moja tangu apate akili zake.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama! Mama kuna nini? Mbona unalia,” alihoji Aidan huku akimsogelea mama yake lakini badala ya kumjibu, alipitiliza moja kwa moja mpaka chumbani kwao alikoanza kufungasha kila kitu chake kwenye mabegi makubwa mawili.

    “Mama kwani kuna nini? Mbona sielewi? Polisi walikuja kukukamata, sasa hivi unafungasha vitu vyako vyote, mbona sielewi?”



    “Aidan, baba yako amenitia aibu sana, siwezi kuendelea kuishi naye, najua atakayeteseka ni wewe lakini sina namna, ni lazima niondoke,” alisema mama yake Aidan huku akiendelea kulia kwa uchungu.

    Aidan akiwa amebaki njia panda, alisikia muungurumo wa gari la akina Caro, harakaharaka akatoka na kukimbilia nyumbani kwa akina Caro lakini hali aliyokutana nayo, ilimfanya abaki ameduwaa, akiwa ni kama haamini. Wazazi wa Caro walimfukuza kama mbwa na kumpiga marufuku asikanyage tena kwenye nyumba hiyo.





    “MAAAMA! Tafadhali niambie kinachoendelea, mbona sielewi?”

    “Siwezi kusema chochote kwa sasa Aidan, mimi naondoka tutaonana Mungu akipenda.”

    “Hapana mama usiondoke, nakuomba mama, shule zinaelekea kufunguliwa na hapa nyumbani ndiyo hivyo sielewi kinachoendelea, nyumbani kwa akina Caro nimefukuzwa kama mbwa, nitakuwa mgeni wa nani mimi? Nitakwenda popote na wewe,” alisema Aidan huku akilia kwa uchungu, hali iliyomtia simanzi hata mama yake. Akarudisha mabegi yake ndani na kurudi pale alipokuwa amemuacha mwanaye, akamuinua na kumkumbatia.



    “Basi mwanangu, siondoki kwa sababu yako mpaka baba yako atakaporudi uraiani.”

    “Atakaporudi uraiani? Kwani sasa hivi yuko wapi?”

    “Amekamatwa, yupo lupango.”

    “Niniii! Baba amekamatwa? Kwani wewe na baba mmefanya nini?”

    “Mimi sina kosa, polisi walikuja kunikamata ili iwe rahisi kumpata baba yako.”

    “Kwani yeye baba amefanya nini?”



    “Mwanangu, we elewa tu kwamba baba yako amekamatwa, hayo mengine msubiri akija kutoka lupango ndiyo utakuja kumuuliza,” alisema mama yake Aidan huku akionyesha dhahiri kwamba kuna jambo alikuwa anamficha mwanaye huyo.



    Muda mfupi baadaye, wote walisikia mlango wa nyumba yao ukigongwa, Aidan akatoka haraka kwenda kufungua, akakutana uso kwa uso na mchungaji wao, mzee Katavi ambaye mara kwa mara alikuwa akiwatembelea nyumbani hapo.



    Mama Aidan alipomuona tu Mchungaji Katavi ambaye alikuwa amevaa mavazi maalum kama wavaayo watumishi wa Mungu, mkononi akiwa na Biblia, alianza kuangua kilio kwa uchungu, hali iliyomshangaza mchungaji huyo.



    Akaanza kumtuliza na kumuomba Aidan awapishe kidogo ili aweze kumueleza kilichokuwa kikimsumbua. Mama Aidan alitulia na kukaa kwenye kiti, pembeni ya mchungaji huyo. Ili kuhakikisha kwamba Aidan hasikii chochote, alimuita na kumtuma kwenda kununua soda dukani.

    Alipoondoka, alianza kumueleza kila kitu kilichomsibu. Mchungaji Katavi alibaki ameduwaa kwani hakuwahi kufikiria kwamba mtu aliyekuwa akimheshimu kama mzee Kenan anaweza kufanya tukio kubwa la aibu kama hilo.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nataka kurudi kwetu mchungaji, siwezi kuishi na mwanaume huyu, ameuumiza sana mtima wangu,” alisema mama Aidan huku akiendelea kulia. Mchungaji akawa anambembeleza na kumkumbusha juu ya kiapo cha ndoa alichokula siku walipokuwa wakioana.

    “Uliahidi utakuwa naye katika shida na raha, utakuwa unafanya dhambi kumkimbia mwenzako wakati ana matatizo.”



    “Sasa nitafanya nini mchungaji katika hali kama hii? Nahisi nimeibeba dunia nzima kichwani kwangu, sina namna zaidi ya kuondoka,” alisema mama Aidan lakini mchungaji akawa anambembeleza huku akimpa ushauri wa namna ya kumsaidia mumewe.



    Kwa pamoja wakakubaliana kwamba waende kwa wazazi wa Caro na kujaribu kuzungumza nao ili kama inawezekana wayamalize mambo hayo nje ya mahakama.

    “Akishatoka lupango hapo ndiyo utakuwa na uamuzi wa nini cha kufanya kwa sababu utakuwa umetimiza kiapo chako kwa kuwa naye hata katika wakati wa shida,” alisema mchungaji huyo, kidogo mama Aidan akajihisi ahueni kwenye moyo wake.



    Hawakutaka kupoteza muda, wakatoka na kuelekea nyumbani kwa akina Caro, wakapishana na Aidan mlangoni akirudi kutoka dukani. Mchungaji akatumia busara kumueleza kuwa awasubiri ndani watarudi baada ya muda mfupi. Alifanya hivyo kwa makusudi kwani mama yake alishamueleza kuwa hakuwa akijua chochote.



    Tofauti na walivyotegemea, walipofika nyumbani kwa akina Caro, walipokelewa kishari mno huku baba wa msichana huyo akitishia kufanya kitu kibaya endapo mtu yeyote kutoka familia ya mzee Kenan ataingia ndani ya nyumba yake.



    Ilibidi busara zitumike, mchungaji akamuomba mama Aidan arudi nyumbani kwake kwanza wakati yeye akiendelea kuwabembeleza wazazi wa Caro warudishe nyuma mioyo yao.

    Kazi haikuwa nyepesi kwa jinsi wazazi wa Caro walivyokuwa mbogo kutokana na mtoto wao kuharibiwa na mtu waliyekuwa wakimuamini na kumchukulia kama ndugu yao.

    “Tumefundishwa kusamehe saba mara sabini, katika Biblia takatifu, Warumi 12:19, neno la Mungu linasema: Msijilipizie kisasi bali ipisheni ghadhabu ya Mungu maana imeandikwa kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa.



    “Pia Mithali 20:22, neno la Mungu linasema: Usiseme mimi nitalipa mabaya mngojee Bwana naye atakuokoa,” alisema mchungaji huyo, akaendelea kukemea roho ya kisasi kwa muda mrefu mpaka baba na mama Caro wakaanza kuelewa kwamba walikuwa wakimkosea Mungu wao.

    Baada ya kuelewa neno la Mungu kutoka kwa Mchungaji Katavi, walikubali kuongozwa katika sala maalum, wote wakapiga magoti, mchungaji akawawekea mikono kwenye vichwa vyao na akaanza kusali kwa nguvu.



    Baadaye alipomaliza, wote walikubali mama yake Aidan akaitwe ili kwa pamoja wajadiliane nini cha kufanya kwani hata wangeamua kumfunga mzee Kenan, hiyo isingebadilisha maana kwamba binti yao ameshaharibiwa.



    Mama Aidan alifurahi sana kusikia familia hiyo imekubali wakae mezani na kujadiliana nini cha kufanya. Kilichomfurahisha ni kwamba muda mfupi baadaye angeweza kuikwepa aibu iliyokuwa mbele yake kwani alishapanga kwamba mumewe akitoka tu gerezani, cha kwanza ni kudai talaka yake na kuondoka kabisa kwenye mtaa huo kukwepa aibu nzito.

    Kikao kilikuwa kirefu mno, pande zote mbili zikitoa hoja nzitonzito, Mchungaji Katavi alikuwa makini kuwatuliza kila walipoonekana kupandwa na jazba. Mwisho wakafikia muafaka kwamba wakaifute kesi hiyo na mambo yote yamalizwe nje ya mahakama. Wakakubaliana kuwa asubuhi ya siku ya pili, wote waongozane hadi kituo cha kati cha polisi kwa ajili ya kwenda kufuta kesi hiyo, mama Aidan akiwa tayari kutoa gharama zote za kufuta kesi hiyo.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kesho yake kulipopambazuka, wazazi wa Caro pamoja na mama yake Aidan waliongozana mpaka kwenye kituo kikuu cha polisi ambapo walipofika, waliomba kuonana na mkuu wa kituo ambaye walimweleza shida yao.

    Mkuu huyo wa kituo aliwaeleza wazi kwamba kosa alilokuwa amelifanya mzee Kenan halikuwa la kumalizana kienyeji kwani kwa mtu aliyebaka, huwa anashtakiwa na jamhuri kwa hiyo lazima kesi hiyo ifikishwe mahakamani.

    “Tusaidie baba, mtuhumiwa ni mume wangu na familia nzima tunamtegemea yeye, nipo chini ya miguu yako, naomba msaada wako afande,” alisema mama Aidan lakini mkuu wa kituo alitingisha kichwa kuonesha kutokubaliana na ombi hilo.

    “Mimi nikisema nimuachie, nitajibu nini kwa viongozi wangu? Ishu kama hii siyo ya kumalizwa kiholela, samahani sana siwezi kuwasaidia,” alisema mkuu wa kituo huku akisimama kuashiria kwamba hataki tena kuendelea kuwasikiliza.

    Mama Aidan aliangua kilio cha uchungu ndani ya ofisi ya mkuu wa kituo lakini haikusaidia chochote.

    Mama Caro na mumewe wakamwambia kwamba wao wapo tayari kulimaliza suala hilo kwa hiyo kazi ni kwake kumshawishi mkuu huyo wa kituo kama atakubali. Mama na baba Caro walitoka nje na kwenda kukaa kwenye benchi nje ya kituo hicho, wakamuacha mama Aidan akiendelea kumwaga machozi.

    “Afande nipo tayari kufanya chochote ilimradi tu hili suala liishe, niambie chochote unachotaka nitakuwa tayari,” alisema mama Aidan huku macho yake yakiwa mekundu kutokana na kulia kwa muda mrefu. Baada ya kauli hiyo, mkuu wa kituo ambaye alikuwa ameshasimama, alirudi kwenye kiti chake na kukaa, akawa anamtazama mama Aidan usoni.

    “Unajua hili suala limekaa vibaya sana, naogopa kuharibu kazi yangu,” alisema mkuu huyo kwa sauti ya upole tofauti na awali huku akimtazama mama Aidan. Akashusha pumzi ndefu na kunyoosha mkono wake, akawa anampigapiga kama ishara ya kumbembeleza.

    “Kwani unampenda sana mumeo?”

    “Nampenda sana, nipo tayari kufanya chochote ilimradi atoke.”

    “Sasa unampendaje mtu ambaye haziheshimu hisia zako? Yaani mtu ana mke mzuri kama wewe anashindwa kutulia matokeo yake anaenda kukutia aibu? Yaani mimi ningekuwa na mke mzuri kama wewe mbona ningeringa sana,” alisema mkuu huyo wa kituo huku akiwa amemkazia macho mama Aidan.

    Akaendelea kumbembeleza mama Aidan huku mkono wake ukiwa kwenye bega lake la mkono wa kushoto, akamwambia yupo tayari kumsaidia lakini kwa sharti moja tu.

    “Sharti gani afande?”

    “Usijali, ngoja kwanza nishughulikie suala la mumeo halafu akishatoka nitaomba kuonana na wewe jioni ya leo kwa maelekezo zaidi,” alisema mkuu huyo wa kituo, kauli iliyomshtua mno mama Aidan lakini kwa kuwa alikuwa na shida, hakuwa na ujanja zaidi ya kukubali.

    “Hebu niandikie namba yako ya simu,” alisema mkuu huyo wa kituo huku akitoa simu yake ya mfukoni na kumpa mama Aidan, akaipokea huku akitetemeka na kuandika namba yake, akamrudishia simu yake.

    Baada ya hapo, mkuu wa kituo alisimama na kutoka, akamuacha mama Aidan ndani ya ofisi yake, akaenda mpaka kwenye ofisi ya wapelelezi ambapo alimuita Inspekta Kiiza, mpelelezi aliyekuwa akishikilia jalada la kesi hiyo. Akazungumza naye na kumpa maagizo ya kulifunga jalada la kesi iliyokuwa ikimkabili mzee Kenan kisha kumtoa nyuma ya nondo. Akarudi ofisini kwake.

    Baada ya dakika kadhaa, mlango wa ofisi ya mkuu huyo wa kituo uligongwa, akaingia Inspekta Kiiza akiwa na faili mkononi mwake, nyuma yake akiwa ameongozana na mzee Kenan. Muda mfupi tu aliokaa nyuma ya nondo, ulitosha kumbadilisha mno.

    Alionekana kuchakaa utafikiri amekaa mwezi mzima gerezani, macho yake yakagongana na ya mkewe, akashindwa kujizuia, machozi yakawa yanamtoka kama chemchemi ya maji.

    “Umshukuru sana mkeo kwa kukuhangaikia lakini hata hivyo bado mambo hayajaisha, hutakiwi kutoka nje ya mji kwa kipindi chote mpaka utakapoambiwa vinginevyo, mke wako atakuwa anakuja mara kwa mara hapa kituoni kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kisheria,” alisema mkuu wa gereza huku akilipitia faili la kesi yake.

    Mzee Kenan alimshukuru sana mkuu wa kituo, akamshukuru pia na mke wake ambapo mkuu wa kituo aliwaruhusu kuondoka, wakaenda mpaka kaunta ambapo mzee Kenan alirudishiwa vitu vyake kama mkanda, viatu na vitu vingine alivyovuliwa wakati akiingizwa mahabusu.

    Wakatoka hadi nje walikowakuta wazazi wa Caro wakiwa wamekaa, nyuso zao zikionesha kuwa na majonzi. Hakuna aliyeweza kumsemesha mwenzake, wakatazamana kwa sekunde chache kisha kila mtu akatazama pembeni.

    ***

    Baada ya mama yake kuondoka asubuhi akiwa ameongozana na wazazi wa Caro, Aidan aliona huo ndiyo muda muafaka wa kwenda kuzungumza na Caro. Akasubiri wazazi wao walipoondoka kabisa, harakaharaka akatoka nyumbani kwao na kukimbilia nyumbani kwa akina Caro.

    Akagonga mlango lakini hakuitikiwa, alipousukuma aligundua kuwa haukuwa umefungwa kwa funguo, akaufungua na kuingia mpaka ndani. Kwa kuwa alikuwa akikifahamu chumba alichokuwa analala Caro, alienda moja kwa moja mpaka mlangoni, alipojaribu kuufungua aligundua kuwa ulikuwa umefungwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Caro! Caro! Ni mimi Aidan, naomba ufungue mlango,” alisema kwa sauti ya kubembeleza. Caro ambaye alikuwa amejilaza kitandani akiendelea kutafakari juu ya kitendo alichofanyiwa na baba yake Aidan, alishtuka mno kusikia sauti ya Aidan.

    Tangu alipotokewa na tukio la kubakwa na mzee Kenan, hakuwa akitaka kumuona Aidan kwenye macho yake kutokana na jinsi alivyokuwa akijisikia vibaya ndani ya moyo wake. Harakaharaka aliamka na kuvaa nguo, akaenda kuufunga mlango kwa funguo akiwa hataki kabisa kukutana na Aidan.

    Aidan aliendelea kubembeleza pale mlangoni lakini Caro hakukubali kumfungulia zaidi ya kuendelea kulia kwa uchungu. Japokuwa alikuwa akimpenda mno Aidan, kitendo alichofanyiwa na baba yake kilimfanya atamani kwenda kuishi kwenye dunia ya peke yake, mahali ambapo hatakutana tena na mtu yeyote.

    “Siwezi kukufungulia Aidan, we ondoka tu,” alisema Caro huku akilia kwa uchungu, Aidan akazidi kumbembeleza huku akimkumbusha mambo mbalimbali waliyofanya pamoja. Baada ya kutumia ushawishi wa hali ya juu, hatimaye Caro alikubali kumfungulia lakini moyoni akajiapiza kuwa kamwe hatamwambia kitu chochote, ni bora aufahamu mwenyewe ukweli.





    “CARO, unaumwa?”

    “Hapana siumwi.”

    “Kwani kuna nini kinachoendelea? Mbona sielewi? Hebu nifumbue macho Caro,” alisema Aidan lakini badala ya kumjibu, Caro alianza kuangua kilio, hali iliyozidi kumchanganya Aidan, akamsogelea na kumkumbatia huku akimfuta machozi.

    “Tafadhali niambie Caro, kwani kuna nini kimetokea?” Aidan alizidi kumbana Caro lakini bado hakutaka kumweleza chochote zaidi ya kuendelea kulia. Walikaa pamoja kwa muda mrefu lakini bado hakuwa tayari kufungua mdomo wake na kumweleza ukweli Aidan.

    Walikuja kushtuka baada ya kusikia muungurumo wa gari kwa mbali, harakaharaka Aidan akatoka na kukimbilia kwao akikwepa kukutwa na wazazi wa Caro ambao walishampiga marufuku kukanyaga kwenye nyumba hiyo. Hata hivyo, aliondoka akiwa bado na shauku kubwa ndani ya moyo wake ya kuujua ukweli.

    Muda mfupi baadaye, wazazi wake nao waliwasili wakiwa kwenye Bajaj, akatoka kuwapokea huku akiwa na hamu kubwa ya kujua nini kilisababisha baba yake akamatwe na polisi.

    “Pole baba,” alisema Aidan, baba yake akatingisha kichwa na kujiinamia kutokana na aibu aliyokuwa anaihisi.

    “Kwani ulifanya nini mpaka polisi wakakukamata,” alihoji Aidan lakini hakujibiwa swali hilo, mama yake akamshushua na kumwambia aende akajisomee badala ya kujishughulisha na mambo yasiyomhusu. Akaelekea chumbani kwake huku mawazo mengi yakiendelea kukisumbua kichwa chake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya mzee Kenan kuoga na kuchoma moto nguo alizokuwa nazo lupango, mkewe alimuweka kitimoto na mjadala mkali ukaanza chumbani kwao.

    “Nilikuwa nakusubiri utoke na kutulia ndiyo nikwambie langu la rohoni,” alisema mama Aidan na kuanza kueleza masikitiko yake kutokana na kitendo cha aibu kilichofanywa na mumewe na mwisho akaeleza alichokuwa anakitaka.

    “Nataka talaka yangu, nimekusaidia umetoka salama, baki na mwanao na hata ukitaka kuoa mke mwingine ruksa lakini mimi siwezi kuishi na wewe, najihisi aibu kubwa kwa hiyo uamuzi niliofikia ndiyo huo.

    Kauli hiyo ilikuwa kama mkuki kwenye moyo wa mzee Kenan, tamaa ya muda mfupi iligeuka shubiri kwenye maisha yake. Ilibidi apige magoti na kuanza kumsihi mke wake amsamehe, akaahidi kuwa tayari kumfanyia chochote atakachokitaka ilimradi amsamehe.

    Hata hivyo, bado mama Aidan alishikilia msimamo wake, mpaka wanamaliza maongezi yao yaliyochukua zaidi ya saa tatu, hawakuwa wamefikia muafaka. Jioni ilipofika, kama mama Aidan alivyokuwa amekubaliana na mkuu wa kituo, alijiandaa na kumuaga mumewe ambaye alimruhusu kwa moyo mkunjufu.

    Akatoka na safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza. Alipofika, alipokelewa kwa bashasha na mkuu huyo wa kituo ambaye baadaye alijitambulisha kwamba anaitwa Ibrahim Mdimu.

    “Kuna mahali nataka tuende pamoja, hapa hapafai kwa mazungumzo,” alisema Kamanda Mdimu, kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa cha mama Aidan. Awali alihisi kuwa mkuu huyo wa kituo alimuita ili wajadiliane kuhusu kesi ya mumewe lakini kwa maelezo mafupi tu aliyompa, ilionyesha kuna jambo lingine la ziada.

    Hata hivyo, hakutaka kuonyesha wasiwasi wake mapema, akatoka na mkuu huyo wa kituo mpaka mahali alipokuwa amepaki gari lake, akamfungulia mlango mama Aidan kisha na yeye akapanda, wakaondoka kituoni hapo.

    “Samahani, huwa unakunywa pombe?”

    “Hapana situmii, labda waini kidogo ambayo huwa nakunywa nikitaka kulala,” alijibu mama Aidan, safari ikaendelea na baada ya muda, Kamanda Mdimu alipaki gari kwenye maegesho ya hoteli nzuri ya Eastern Beach iliyokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi.

    “Nimepachagua hapa kwa sababu ya utulivu wake na mandhari nzuri,” alisema Kamanda Mdimu wakati akimuongoza mama Aidan sehemu ya kwenda kukaa. Wakakaa kwenye meza iliyokuwa imejitenga na kuagiza vinywaji, wakawa wanapunga upepo mwanana wa baharini.

    “Vipi mmefikia wapi na mumeo?” Kamanda Mdimu alimuuliza mama Aidan, akashusha pumzi ndefu na kumtazama.

    “Bado hatujafikia muafaka lakini siwezi kuendelea kuishi naye.”

    “Unamaanisha nini?”

    “Nataka anipe talaka yangu, siwezi kuishi na mtu asiye na hata chembe ya ubinadamu.”

    “Safi sana, nakupongeza kwa uamuzi uliouchukua, usirudi nyuma kwani amekutia aibu sana,” alisema mkuu huyo wa kituo na kuahidi kumsaidia endapo atahitaji msaada wake. Alionekana kufurahishwa mno na uamuzi huo, jambo lililomshangaza mama Aidan.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mke wangu alikufa miaka saba iliyopita kwa ajali ya gari, tangu kipindi hicho sijawahi kuoa, wanangu wameshakuwa wakubwa lakini nahisi kuna kitu nakikosa kwenye maisha yangu.”

    “Pole kwa yaliyokukuta, unahisi unakosa nini?”

    “Furaha ya moyo wangu, nimeishi mpweke kwa kipindi kirefu sana, sasa nahitaji kubadilisha maisha yangu,” alisema Kamanda Mdimu na kusogeza mkono wake, akamshika mama Aidan mkono na kumtazama usoni.

    “Siwezi kuficha hisia zangu, tangu mara ya kwanza nilipokuona nimetokea kukupenda sana na ndiyo maana nikakusaidia, naomba wewe ndiyo uzibe pengo la mke wangu, nitakusaidia kumshinikiza mumeo akupe talaka haraka iwezekanavyo,” alisema Kamanda Mdimu huku akiendelea kumtazama mama Aidan kwa macho yaliyobeba ujumbe.





    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog