Simulizi : Kurasa (The Page)
Sehemu Ya Pili (2)
Miezi mitatu baadae, bado penzi letu lilikuwa kwenye kilele cha upendo, nilimchukua Mpenzi wangu Stellah hadi nyumbani kwetu Tabora, tukaenda kuwaona wazazi na pia nilitaka atambulike rasmi,
Jioni tukiwa mie nae pekee, nikamtoa hadi kwenye hoteli moja maarufu pale kwenye Jiji lile la Millenium, hotel ile inaitwa Orion Tabora Hotel. Pale kuna jamaa yangu ambae ni Meneja kwenye hotel ile, nilikuwa tayari nimempanga kuwa nitakwenda pale kufanya tukio.
Tukio ambalo sikutaka hata nae alijue, nikamwambia ninachoomba kwake aniandalie bendi yao ya music ipigayo live, inaitwa ‘One Temi Band’ ili itutumbuize.
Nae hakuniangusha, aliniambia suala lile kwake ni dogo sana, lakini pia alinitaka nimdokeze kidogo juu ya kile nilichopanga kufanya, ili aweze nae kujipanga na kuiandaa vizuri bendi yake.
Nilifikiria kwa sekunde kadhaa na kukubaliana na kile alichokitaka, nikamueleza kifupi tu huku nikimtaka kutokuvujisha kile nilichomueleza kwani Sikuwa tayari mtu mwingine yeyote ajue, akasema sawa na kuondoka.
Magharibi, hapo mkoani huchelewa sana jua kuzama, hivyo hadi kwenye muda wa saa mbili kasoro ndio tuliwasili pale na kuketi Stellah akiwa haelewi chochote kinachoendelea. Alichokiona na kumvutia pale ni mandhari nzuri.
Alisema pamemvutia na hakujua kama kuna hotel nzuri kama ile huko mikoani, akaongezea na kwa hayo mapambo yamezidi kupapendezesha sana, bila kujua kama mapambo yale yanamuhusu yeye.
Nilicheka na kunyanyuka kama ninakwenda msalani, kule nikakutana na MC wa hotel ile aitwae Kagize na kumueleza mchezo mzima ulivyo, yeye sasa ndio nilimueleza kwa kirefu, maana ndio alikuwa anapaswa kuuandaa mchezo huo.
Akanielewa na nikamkumbusha kuwa mchakato ule ufuatie ndani ya dakika 5 zijazo na isichukue zaidi ya robo saa uwe umeisha, akaridhia na kuniambia hiyo kazi nimuachie yeye mwenyewe, akanihakikishia kwamba nitaipenda.
Nikarejea kuketi, Mc nae akajitokeza na muda huo One Temi Band wanapiga muziki laini wa vyombo vitupu, maarufu kama muziki wa ala, akawakaribisha watu wote waliokuwepo pale na kuwaomba washuhudie kuna tukio linataka kufanyika pale, kwa kuwa hakuna mwalikwa, wote wakaombwa wawe ndio wageni.
Sio utaratibu wa kawaida ila akasema lile ni ombi maalum toka kwa mteja wao mpendwa, aliomba afanye tukio pale kwao nao wakaona si vema kumuangusha, hivyo wamemkubalia, kisha akaomba dakika 3 za kumsubiri, akaruhusu muziki uendelee.
Dakika ziliisha, aliekuwa akisubiriwa hakutokea, bali RM Classic Decoration ndio ilifika na kuweka keki mezani, zilikuwa ni keki 7 zilizopambwa barabara na kupendeza kweli kweli.
Mc alionekana akiongea na simu mara kwa mara na kuonekana kusikitika, kitu ambacho kikawa kinazidi kuwapa watu hamu ya kutaka kujua ni kipi ambacho kinatarajiwa kujiri dakika chache zijazo.
Kila mtu alijawa na tashwishi, mimi ili kupima umakini wa Stellah, nikamwambia anyanyuke twende nyumbani. Stellah aliniomba tukae tuone tukio lifuatalo, mie nikamkatalia kabisa kuwa nimechoka, alinibembeleza sana hadi nikamwambia tukae kwa dakika 5 tu kisha tuondoke, akafurahi na kunibusu kwenye kidevu.
Nilitabasamu na kujua kumbe hata nae amependa maandalizi haya japo hajui lolote lakini inaonekana imemvutia, name nikafurahi kuona namfurahisha nimpendae bila kumuandaa kufurahi japo nimemuandalia furaha yenyewe.
Mc alisogea kwenye keki zile na kunyamazisha Muziki kisha akasema kuwa
“Kuna maharusi walifunga ndoa asubuhi ya siku ile na kuandaliwa sherehe fupi jioni ile nyumbani kwao, lakini kwa kuwa waliomba wafanyiwe sherehe fupi hapa kwetu, hivyo kwa kushirikiana na uongozi wa hotel yetu, tukamuandalia sherehe hii fupi, ila kwa bahati mbaya wamepata dharula, ina maana hawatafika,” alisema kwa huzuni huku akigeuka huku na kule kuwatazama watapokeaje, watu karibu wote walisikitika sana ila MC akawaambia kuwa hakijaharibika kitu.
“Ngoja nitafute Couple iliyopendeza zaidi iwawakilishe, maelezo na maelekezo zaidi, tutayapatia hapahapa, nani yupo tayari?” kila mtu hakuwa tayari.
Stellah akaniambia mimi nanyoosha mkono, nikamwambia utakwenda peke yako lakini? Akakataa na kughairi baadhi ya watu wakanyoosha mikono, Mc akatazama na kuona kati yetu hakuna alie nyoosha, akaamuru watu wote washushe mikono yao chini na atachagua mwenyewe.
Akatanguliza ombi kwamba anaweza kuchagua watu ambao wamependeza na kuwapata kama Couple iliyopendeza zaidi, lakini wasiwe wapenzi, hivyo wale watakao kuwa wamekuja nao, wasijisikie vibaya, kwani ule ni kama mchezo tu, akatuuliza kama tumeridhika.
Sote ukumbini tulijibu ndio, watu wote sasa walikuwa na shauku ya kutaka kujua huo mchezo. Nikamwambia Stellah muda tuliokubaliana umeisha huku nikinyanyuka, akanizuia na kuniambia nimuongeze dakika 3 awaone watu waliopendeza sana ndio tuondoke, nikakubali kwa shingo upande.
MC akaanza kuzunguka ukumbini akitafuta watu waliopendeza zaidi ukumbini, bahati ikamuangukia Stellah kwa upande wa wanawake. Akaendelea Mc kutafuta upande wa wanaume.
Alizunguka ukumbi mzima akiangalia kila upande, akimtazama kila mwanaume aliepo mle ndani huku wengine akiwaomba wasimame na kisha alikuwa akiwaomba samahani na kuwataka wakae.
Baada ya zoezi hilo kulikamilisha akarudi mbele ya ukumbi na kudai eti haoni mtu mwenye sifa za kufanana na Stellah wangu,
Nilicheka sana na kutikisa kichwa, akasema yule ambae anajihisi ana sifa ya kufanana na Stellah asimame palepale alipo. Wanaume kadhaa walisimama, ila mie sikusimama. Mc kama vile kashtuliwa, akauliza yule aliekuja na mrembo yule yupo wapi?
Macho yote yakaelekea pale nilipokaa mimi, hapo sasa mie Sikuwa na jinsi, ndio nikasimama, MC nae akaniita huku watu wote wakinitazama nilipojitokeza mbela yao. Akaanza kunisifu akipitiliza, akisemahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umependeza sana kidume, mbona sikukuona wakati natafuta mtanashati wa kufuatana na mrembo huyu?” Nilibaki nikitabasamu tu maana niliona mchezo umepangwa na kupangika na zaidi umepata wachezaji tena na muongozaji hasa.
Akawashukuru wale waliosimama na kuwaruhusu waketi kwenye viti vyao kisha nasi akatuonesha viti viwili vilivyokuwepo pembeni kidogo ya bendi, vilikuwa vimepambwa vema, tukaketi kusubiri utaratibu mwingine.
Muda mrefu sikuwa nimemuona jamaa yangu ambae ni Meneja wa hotel ile, lakini sikuwa na hofu nilikuwa nikijua huenda atakuwa na majukumu yake ya kikazi, sherehe ikaanza kwa matukio mbalimbali na muziki tofauti ikirindima ukumbini.
Katika tukio ambalo watu wengi hawakuliamini ni pale MC alipowaambia watu kuwa sherehe ile fupi iliandaliwa na Meneja wa hotel ile kwa ajili yangu, hakika watu pale walitazamana na hawakuamini hadi pale Mc aliponipa nafasi ya kumvisha pete ya uchumba Mpenzi wangu Stellah.
Hata Stellah mwenyewe hakuamini, almanusura azimie pale alipoiona ile pete aliyoitafuta kwa sonara na kuikosa, leo tena inahifadhiwa kwenye kidole chake, alitoa mshangao mkubwa sana tena ulio endana na kilio. Alionesha kabisa kuwa yeye hakuwa amejiandaa kwa tukio lolote la mfano huo.
Kilio chake mie binafsi nilishindwa kukielewa ni cha furaha ya kuwa mchumba wangu ama ni cha huzuni ya kutokumshirikisha tangu awali. Nikasema vyovyote itakavyokuwa ni sawa tu, ilimradi likamilike na ninaamini baadae atafurahi tu.
Tukiwa bado tumesimama Stellah alikuwa akigeuza geuza pete yake kidoleni, nikashika mkono wake na kuibusu ile pete, kitendo kile hakikuwepo kwenye Program yetu.
Ajabu nae pale pale akanibusu kwenye shingo, kitendo kilicho sababisha ukumbi mzima ushangilie, wakapiga mbinja na kusababisha mimi na Stellah wote tutabasamu.
Mc ambae ni msemaji sana, akasema ama leo amekutana na watu wanaojua mapenzi ni nini! Akatusifia sana na kutuelekeza ilipo meza ya keki, pale mezani hapakuwa na kisu bali jagi zuri la kioo na bakuli kubwa kiasi, vyote navyo vimepambwa vizuri.
Akatuasa tusishike chochote hadi atakapo turuhusu, akachekesha chekesha watu pale na kumuita muandaaji wa keki zile na kumtaka atunawishe. Ulikuwa ni utaratibu tofauti kabisa, tulinawa na kusogelea meza. Keki zilikuwa 7 lakini moja ya kati ilipambwa zaidi na kuvutia kweli.
Hiyo ndio Mc akasema ndio tunayopaswa kuila, akaniamuru nikate kipande kinachomtosha mpenzi wangu kwa mkono wa kulia na kumlisha. Nilihofu kukata kipande kikubwa sana maana kukadiria ni mtihani, kumbe nilikosea, keki ile tayari ilikuwa imekatwa vipande vya wastani ambavyo bado vilikuwa vimeshikiliwa na Icing Sugar.
Nilichukua kimoja na kumgeukia Stellah nikamshika shingoni kwa nyuma, nikamlisha na wakati akianza kutafuna, nikampelekea na ulimi. Sikuhofu chochote kwani wazazi hawakuwepo, ni hao tu ndio niliwaonea aibu.
Ukumbi mzima ukapiga mbinja, wengine vigelegele na wengine miluzi, ilmradi tu kelele zilsikika. Nikatulia kusubiri zamu ya Stellah. Nilihisi hatoweza kufanya manjonjo yoyote, maana tayari niliisha muumiza kisaikolojia.
Kitendo cha kuja na kukuta sherehe yake bila kumuandaa kilimuumiza hivyo nae alinilisha keki kawaida na kunibusu mdomoni, na hicho ndio nilichotegemea, hakuwa na uwezo wa kwenda zaidi ya hapo.
Mc akaturuhusu kukaa na kutuambia Meneja wa hotel ile anataka kuongea nasi maharusi watarajiwa, maana sasa sisi ni wachumba, akamkaribisha. Jamaa yangu hakuwa msemaji sana, akasema mambo mawili tu.
Jambo la kwanza alisema amefurahi sana kuona mie nimepata mchumba tena ni kama yule niliekuwa nikimuota kila siku, maana mie nae tulisoma pamoja hivyo ndoto nyingi mie nae tuliziota pamoja.
Kwa kuwa nimetimiza ndoto zangu, ananipa ofa ya kulala pale hotelini kwa siku 3 nikihudumiwa kwa kila kitu kwenye chumba chenye hadhi ya Suit. Jambo lile lilishangiliwa vibaya sana, hapo Stellah alikuwa kaniegamia begani, bega la kushoto na mikono yake yote kaizungusha kwenye mkono wangu wa kushoto.
Ulikuwa ni muda wa starehe sana starehe ambayo sikujua kama ninaweza kuipata kule mkoani ambako mie sikuwa na umaarufu mkubwa, nilivyo ondoka ningali mdogo, nilihisi pindi nitakaporudi, basi ni lazima nitakuwa kama mgeni.
Jambo la pili hakulisema alidai ni Surprise, akarejesha Mic kwa Mc na kumwambia utaratibu uendelee kama ulivyopangwa. Hapa sasa hata mie sikuelewa jamaa yangu anamaanisha nini, kusema utaratibu uendelee kama ulivyopangwa? Ni kipi tena kingine kilichopangwa? Nikajiuliza tena, ni nani amepanga?
Maana hata hii kitu ya Surprise nyingine haikuwepo kwenye ratiba, Stellah alionekana kushangaa tu, yeye ndio alikuwa mbali zaidi ya mimi, kwake sasa kila kitu kilikuwa kipo sawa tu.
Basi Mc akasema kwa kuwa waliopo ukumbini hawakuandaliwa kwa sherehe, ina maana hawakuja na zawadi yoyote, sasa sisi kama wahusika tutawapa wao zawadi gani kwa kukubali kujumuika nasi kwenye sherehe yetu? Mc alituuliza sisi.
Nami nikanong’ona sikioni kwa Stellah nikamwambia ‘Keki’ Mc akamfuata Stellah na kumuuliza kama na jibu lolote. Jibu lake lilifanya ukumbi mzima urindime, akaongezea Mc kuwa keki zipo 7 je tunapenda tuzigawe vipi?
Swali hili sasa alikuwa amenilenga mie, nikamwambia ninaomnba ile keki ndogo kabisa ya kwanza, ninaomba apewe Meneja wa hotel kama shukran, Muhudumu mmoja aliekuwa hapo jirani, akafanya hivyo.
Mc akampelekea Mic Stellah na kumuuliza ya pili je? Akasema wapewe wafanyakazi wa Orion kama shukran ya kujitolea muda wao kwa ajili ya shughuli yetu iliotokea kama dharula, waungwana wakapiga makofi huku keki zikienda kwa wahusika waliotajwa.
Ya 3 nayo inaelekea wapi? Aliuliza Mc akiniwekea Mic usawa wa mdomo, nikajibu ile itabidi tuwapelekee wazazi, akatuuliza kama wapo? Nikamwambia hawapo pale, akasema basi itabidi tuiache pale pale mezani.
Iliyofuatia ilikuwa ni keki ya 4 ambayo tayari tulikuwa tumeanza kuila sisi wenyewe, Mc akasema ile atapanga yeye ni nani wa kumpa. Akajidai anatafuta mtu, alipoonekana kukosa mtu, akasema tutakula sie wenyewe. Watu wakapiga makofi.
Stellah akaitoa keki ya 5 kwa watu wa bendi akiwepo na Mc mwenyewe, wakashukuru, kisha nikamwambia Mc kuwa keki ya 6 na ya 7 ambazo I kubwa zaidi, tunazitoa kwa wageni wetu waliojitolea muda wao kwa ajili yetu.
Zilkuwa ni keki mbili lakini jinsi wahudumu walivyokuwa faster, kwa muda mchache tu tukaona wapo ukumbini wakiwagaia watu ambao walikuwa ni wastaarabu mno wakiwa na furaha kwa tukio lile ambalo lilikuwa likielekea ukingoni.
Mc akaniambia nichukue keki ya 3 iliyokuwa ni ya wazazi na kumkabidhi Stellah kisha akaniambia mie nibebe yetu, Mc akamuuliza Stellah kama anawajua wazazi wangu, yaani wakwe zake? Akatikisa kichwa kuwa anawajua.
Akaulizwa kama wapo? Akasema hawapo pale, Mc akamuomba yeye apewe aipeleke kwa wazazi wa Ramaah, Stellah akampa bila kujiuliza, lakini Mc akakataa kuipokea na kusema hawezi kuipokea bila kuwa na shahidi.
Watu wote wakashangaa na kuguna, lakini yeye hakujali hivyo akamuita Meneja na kumwambia anataka ushahidi kabla hajapokea keki ile ya wazazi, na ushahidi unatakiwa utoke kwa wageni wetu pale ukumbini, hivyo Mc akamuomba Meneja amshindikize Stellah wazungushe keki ile ukumbi mzima wageni waione kabla yeye hajakabidhiwa rasmi.
Meneja akasema amemuelewa, akamuuliza shemeji yake kama yupo tayari kuzunguka pale ukumbini? Sterllah wala hakujifikiria mara mbili, akamwambia yupo tayari.
Stellah akaanza kuondoka na keki yake mkononi, Meneja akiwa mbele nae nyuma, hatua kama 3 hivi, Mc akaniruhusu nami niwafuatie kwa nyuma, akidai kila abiria anapaswa kuchunga kilicho chake, nikatabasamu na kuwasogelea.
Kama ni Surprise, basi hii ilikuwa ni kubwa kuliko zote, meza 3 kutoka mwisho, tuliwakuta mama, baba na kaka yangu wakinywa soda, nilitikisa kichwa na kushindwa cha kufanya, kama vile Mc aliona, akatuita wote mbele.
Nilimuona dhahiri Stellah akitetemeka, ilikuwa ni hofu na sikujua ni kwanini alikuwa vile, nikahisi hata ile keki anaweza kuiangusha, kwa kuwa Sikuwa mbali, nikamuomba meneja ampokee, akafanya hivyo.
Mie Stellah na familia nzima tukiongozwa na Meneja tukaelekea kule mbele, Mc akampa nafasi kaka yangu aitambulishe familia yetu, kaka kawatambulisha wazee wetu na yeye mwenyewe na kusema ile ilikuwa ni Surprise toka kwa Meneja wa Orion.
Alinichosha pale aliposema wazee wameingia pale tangu wakati wa mchakato wa kutafuta mtu wa kukaa pale mbele, moyo wangu ukapiga Pah! Ina maana matukio yote wameyaona? Kama watu tuliokuwa tunawaza kitu kimoja, Stellah akanitazama kwa jicho la kuuliza... Umeona sasa?
Nikampiga kope, kitu ambacho wengi walikiona na kupiga mbinja, Mc hakuona, akahisi kama wanapiga tu kelele, akaomba utulivu tuwasikilize wazazi kwani wana neno wanataka kulisema.
Baba ndio aliongea, alituasa kufunga ndoa mapema iwezekanavyo na kutupongeza kwa uamuzi mzuri wa kwenda kujitambulisha nyumbani ambapo wengi wa vijana hawafanyi hivyo, kwani hudharau makwao.
Mwisho akasema kuwa kuna zawadi wanayotoa kama wazazi na tutakabidhiwa na mama. Mama aliposhika Mic kwanza alipiga vigelegele na kuonyesha furaha yake kwa kucheza kidogo kisha akatoa bahasha ya kaki na kumpa Mc aifungue na kuisoma.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alitekeleza alicho ambiwa, ilikuwa ni hati ya nyumba iliyokuwa na jina la Mzaham & Sons iliyo kuwepo maeneo ya Kigamboni Jijini Dar Es Salaam, nilikuwa nikiifahamu vema, ilikuwa ni nyumba ya Ghorofa moja na ina bustani kubwa sana kuizunguka nyumba yenyewe.
Mama akasema tangu muda ule nyumba ile si ya familia tena, bali ni nyumba yangu na mpenzi wangu Stellah. Tuliwashukuru wazee, Stellah akapiga magoti wakati akiipokea bahasha ile kutoka kwa mama.
Sherehe ikafungwa kwa muziki ulioanzishwa na mhudhuriaji mmoja aliekuwa na mpenziwe.
Wakati muziki ukiendelea mie na Stellah wangu tukapotelea chumbani, chumba tulichopewa na rafiki yangu kipenzi, aliefanikisha sherehe yangu ya uchumba kwa asilimia 100
Usiku haukuwa mrefu kabisa, ningeweza kusema haukuwepo, lakini naamini siwezi kueleweka maana watu waliuona na hata kuutumia. Ulikuwa ni mfupi kutokana na Stellah kulaumu kwa muda mrefu kwa kutokumshirikisha na muda mwingine mrefu akuiutumia kwa kunisifu kwa ubunifu nilio ufanya na kuniamini kuwa ninampenda , tena kupita kiasi.
Nilimuhakikishia kuwa sitaacha kumpenda, alishukuru na kusema ameniamini, zaidi akasema amevutiwa kwa kiasi kikubwa sana na upendo uliopo kwenye familia yetu, nikamkaribisha, akatabasamu na kutaka kujua kuhusu pete.
Nikamwambia kuwa baada ya yeye kushindwa kuinunua niliichukua mien a kuihifadhi nikiamini kama sio yeye basi ipo siku nitapata wa kumvalisha, lakini leo bahati imeingia kwenye vidole vyake mwenyewe.
Kilicho endelea si muhimu kwako kukijua lakini iilikuwa tayari muda huo ni alfajiri. Tuliamka saa mbili asubuhi na kwenda kuoga na kufungua kinywa na kisha kurudi kulala. Sasa ndio tulilala usingizi mzuri.
Hatukushtuka hadi wakati wa chakula cha mchana, tukala na kutazama TV hadi saa 11 jioni ndio tukatoka kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa tukitumia gari ya Meneja wa Orion. Wale ambao tulijua hatutaonana nao siku ifuatayo kwa sababu tutakuwa safarini, tuliwaaga kabisa.
Safari na mizunguko yetu ilitufikisha nyumbani kwa wazazi saa2 usiku na tuliikuta familia nzima ikitusubiri, tulikula nao chakula cha usiku na kisha tuliwashukuru kwa kila walichotufanyia kwa siku zile chache na kuwaaga
Ilikuwa ni rahisi kwa wao kuelewa kwamba kuna siku moja tu imebakia kabla ya sisi kuwepo makazini. Walituaga vizuri huku wakitutakia safari njema. Walisisitiza sana suala la kufunga ndoa haraka iwezekanavyo, nasi tukaahidi kulitekeleza suala hilo mapema iwezekanavyo.
Maisha ya uchumba ni mazuri sana hasa mkiwa mnapendana, tatizo lililo onekana kwetu lilikuwa ni moja tu... Mtoto! Kila nilipo mueleza suala hilo Stellah aliniambia nisubiri. Siku zilikatika, na sikujua hasa tunachokisubiri ni nini
Siku hiyo nikamuweka kikaangoni, akaniambia kuna kesi moja ambayo ndio ilsababisha mi nae tuwe karibu, inamsumbua sana, ila haina miezi mi3 mbele atakuwa amekamilisha upelelezi na kuikabidhi mbele ya sheria, nikakubali na kusisistiza kuwa nahitaji mtoto kuliko kila kitu.
Sasa Stellah akazidi kubanwa na kazi zake, ikawa wakati mwingine anarejea hadi saa 4 usiku. Karibu kila siku aliyorudi amechelewa, alikuwa anatia huruma sana, maana alikuwa amechoka sana, nikawa namuandalia karibu kila kitu Stellah wangu, sikupenda apate tabu name nikiwa ningali nipo jirani nae.
Kama wiki 3 baada ya maongezi yetu, siku hiyo mie nilirudi kazini saa 9 alasiri, yeye nae akawahi mno kurudi na kuniambia ameongezewa nguvu kwenye kazi yake. Sikumuelewa ni nini amemaanisha, akaniambia kifupi tu kuwa kuna mpelezi kaletwa toka Visiwani kumsaidia, anaitwa Amani.
Nilishukuru kwa kuhisi jambo lile kwa sasa huenda likaisha mapema zaidi ya ule muda alio ukadiria yeye, tukaendelea kula maisha tukiwa na amani na furaha tele, hakuna alietamani kumkosa mwenzie ila tu pale tu ilipobidi.
**********
Maisha yetu yalikuwa ni matamu mithili ya mtu mwenye usingizi kisha akakabidhiwa godoro na chumba chenye ndoto kama zake, ndio ilivyokuwa kwetu, kla kilichokuwa ni sahihi kwetu, hatukujiuliza.
Siku moja katikati ya usiku, simu ya Stellah ikaita, ilinishtua mno! Kilichonishtua si muito wa simu bali ni kauli ya Stellah kusema nakuja, nikitazama saa ya ukutani ni saa 8 usiku, halafu mke wangu bila hata kunishirikisha mimi mumewe, anamuahidi mtu anae ongea nae kwenye simu kuwa anaenda!
Nilishtushwa sana na hilo, nikasema ngoja nimsikilizie ni kipi atakisema baada ya kumaliza mazungumzo yake. Nayo hayakuwa marefu, akakata na kuniambia ameitwa kazini haraka, bila hata kusubiri jibu, akanyanyuka na kuvaa haraka haraka, nikamzuia asitoke lakini alikataa na kusema amekula kiapo juu ya kulitumikia Taifa wakati wowote na mahali popote.
Akanikumbusha makubaliano yetu wakati nina mtongoza, nikatepeta na kumuacha aende. Akachukua funguo za gari lake na kuja kunibusu kisha akatokomea nje. Sikumuona hadi siku iliyofuata asubuhi nikiwa natoka kuelekea kazini, yalikuwa ni masaa machache tu ya yeye kuondoka, lakini niliona kama vile ameniacha kwa mwezi mzima peke yangu.
Nilirudi jioni na kumkuta hayupo katika hali yake ya kawaida, ajabu mie ndio nikaanza kujiuliza kama nimemuudhi mpendwa wangu? Sikukumbuka kumkosea chochote kwa siku ile ama ya nyuma yake, nikajiuliza tena, huenda sijampigia simu leo zaidi ya mara 1 ile ya mchana.
Nikamsogelea na kumlalia mapajani kisha nikamuuliza ana tatizo gani mbona hayupo sawa? Akaniambia anasumbuliwa na kichwa, najua dawa za maumivu anazozitumia, nikamletea, akanikatalia na kuniambia kwamba kaisha kunywa.
Nikamchukua hadi kwenye TV na kuanza kucheza cheza mbele yake na kumfanyia vituko vingi vingi, taratibu akaanza kurejea katika hali yake ya kawaida na hapo nikamuwekea tamthilia ya…
Na hapo nikamuwekea tamthilia ya kiswahili… ‘SIRI ZA FAMILIA’ ambayo yeye huipenda sana.
Siku hiyo akaikataa na kusema nimuwekee nyingine, nikajiuliza leo vipi? Basi nikachukua moja ya kizungu iitwayo ‘Arrows’ na kuiweka tukaanza kuitazama kwa pamoja huku nikijitahidi kumtoa kule alipo na aje nilipo mimi kwa fikra, nikafanikiwa kumrudisha katika hali yake ya kawaida.
Kwani niliamini iwapo yeye hatokuwa sawa ina maana hata name siku ifuatayo siwezi kufanya kazi vizuri.
Hadi usiku unaingia, hali yake ikawa vile nitakavyo mie, nikatoka nae na kuelekea hotelini kwenda kula chakula cha usiku na tulirejea usiku mzito tukiwa tumepitia kuonja mafanikio…
**********
Maisha yakawa yanaendelea kusonga mbele taratibu, kumbuka mie ni daktari, siku moja nipo nae nikaona kuna utofauti, nilichoweza kukiona kutoka kwa mke wangu ni mabadiliko, nikahisi mke wangu ni mjamzito.
Nilipo muuliza tu si akaanza kulia? Nikamwambia kulikoni? Anieleze kwanza kinachomliza ni kipi? Akasema ni heri aache kazi, nikishangaa, mimba na kazi vina uhusiano gani? Tena yeye akiwa ni mchumba wa mtu?
Akanijibu kuwa mie sijui uzito wa kazi yake. Nikamkatalia na kumtaka aendelee tu na kazi yake, muda utatueleza cha kufanya. Hapo sasa si akanitolea mpya? Eti atoe mimba...
Nikanyanyuka mapajani mwake na kumwambia nitakupasua kichwa na kukuchoma choma kila sehemu mwilini ukifanya kitendo hicho, hakika aliniudhi, na jinsi nilivyo badilika, hata nae akishangaa na kuogopa, akaniomba radhi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Uungwana ni vitendo, na kwa jinsi nimpendavyo, hata asingeniomba msamaha, ningemsamehe tu, hapo nilikuwa nimesimama, akanyanyuka na kuja kulala kifuani kwangu akilia taratibu kwa kuomboleza, nikamnyamazisha na kumuuliza kinachomliza hasa ni nini?
Akaniambia amevunja makubaliano yetu ya awali, nikamuuliza ni yapi? Akajibu tulielewana baada ya miezi mitatu ndio tutapanga juu ya suala la mimba, sasa hata kabla ya kutimia miezi mitatu tayari yeye ni mjamzito, nikamtoa shaka kabisa na kumwambia ni kiasi gani nimefurahi kuona hali ile, maana niliitamani sana.
Nikampangia kabisa ajue ni kiasi gani nimejipanga kuwa baba, nikasema baada ya yeye kujifungua, ndio tutabadili jina la ile nyumba yetu ya Kigamboni na kuandika jina la huyo mtoto atakae zaliwa.
Hadi wakati huo tulikuwa bado hatujabadili jina la umiliki wa ile nyumba kule, hii ilitokana na ushauri wa mpenzi wangu Stellah kuwa tusubiri, nasi hapo bado tupo kwenye nyumba ya kupanga pale Ilala na ile yetu kule tumeipangisha.
**********
Siku zikakatika mara miezi 6 ikatimia, niliona kama mimba inampeleka peleka hivi, japo alikuwa hataki, lakini mimi nikaajiri msaidizi ambae alikuwa ni mama wa makamo hivi na ndio kazi zote sasa akawa anazifanya yeye na kuna baaadhi nikawa nazifanya mie.
Nilikuwa najitahidi sana kuwahi nyumbani, na karibu mara zote ikawa ni ugomvi tu. Mwanzo nami nilikuwa ni mkali sana kwake kila alipoanza ukorofi, lakini kutokana na kuwa na mama Yule wa makamo ndani ya nyumba yetu, ametuzidi sote umri akanishauri kuwa mpole, aliniambia nimzoee tu ile ni mimba ndio inampeleka peleka.
Kweli nikamchukulia hivyo hivyo tu ila kitu kimoja kilinichanganya sana, mapenzi yale ya Stella kwangu yalizidi kupungua kadri siku zinavyo kwenda, bado niliamini ni mimba ina maana mara baada ya kujifungua, yote yatakwisha na kubaki kuwa ni historia.
Niliendelea tu kumvumilia siku moja mimba ikiwa na kama miezi 7 hivi nilimkuta kajipumzisha kwenye sofa anaongea na simu, nilifika na kusimama mlangoni nikitabasamu huku nikimtazama. Yeye wala hakuniona.
Alifanya kituko kimoja kilicho nishangaza mno, alichukua simu na kuiweka kwenye kitovu chake kwa sekunde kadhaa kisha akarudisha sikioni mwake na kuuliza umemsikia? Kisha akaaga hapo ndio mie nikamsogelea na kumbusu.
Alishtuka, niligundua kuwa hakuwa akiongea na mtu ambae ni maharim wake, hivyo name nikatumia wasaa ule kwa kumuuliza alikuwa akiongea na nani? Akanijibu alikuwa anaomgea na daktari wa ofisini kwao.
Sikujali, niliamini vyovyote itakavyo kuwa, mie nitabaki tu kuwa baba, hata huyo daktari niliona anapoteza tu muda wake, maana nilijua kwamba katika hali yoyote ile mimi ndio muhusika na pia fani yangu ni daktari.
Lakini sikumuacha hivihivi tu, nikamwambia anapaswa awaambie kuwa hata aliempa mimba ile ni daktari, akatikisa kichwa kuafikiana nami. Tukaongea maneno mawili matatu kuvutia muda wa chakula cha usiku kisha tukaenda kulala.
*********
Miezi 9 ikatimia, sasa tukawa tunategemea siku yoyote anaweza kujifungua, ikawa inanilazimu kuwepo nyumbani muda mrefu kama sio muda wote, ikinilazimu kutoka, basi ujue ni kwa dharula kubwa hasa na sichelewi kurudi.
Siku moja asubuhi, Sikuwa kabisa na ratiba ya kutoka kwa siku hiyo, bahati mbaya nilipigiwa simu kuitwa ofisini kulikuwa kuna ajali mbaya ilioyotokea ambayo iliyosababisha majeruhi wengi, hivyo ilihitajika huduma ya dharula.
Nikamuaga Stellah ambae alikubali kwa shingo upande, nikambusu na kumwambia kuwa nipo hewani muda wote, tatizo lolote ani beep, nikatoka kasi kuwahi hospitalini.
Kila mmoja alionekana kuijali kazi yake kwa nafasi yake, ila kizuri na mwenzie alithamini sana kila hitajio la mwenzi wake. Hiyo ilinipa faraja na kuamua kutoka huku nikijihimu kuwahi kurejea mara tu nitakapomaliza kazi iliyonipeleka.
Nilifika na kuungana na wenzangu, tulifanya kazi kama watumwa na kufanikiwa kuokoa maisha ya wananchi kadhaa, hadi kufikia alasiri, tukafunga kazi na kurejea nyumbani nikiwa nimepanga nikifika nimchuke Stellah twende tukanunue Ice cream katikati ya Jiji.
Nilifika na kuacha gari nje ya geti na kuingia ndani. Kugusa mlango mkubwa wa nje ukawa upo wazi, kusogelea wa Sitting room nao haujafungwa ila bado sikumuona Stellah. Nikaelekea chumbani kwa kuhisi atakuwa labda kajipumzisha, napo sikumkuta pia.
Jikoni napo hakukuwa na mtu yeyote, nikapata wasiwasi, vyoo vyote yaani kile cha pale Sitting room yaani Public toilet hakuwepo, nikaenda cha chumbani pia sikumkuta. Nikajishika kiuno na kushusha pumzi kwa nguvu, nikajiuliza kaelekea wapi kiumbe huyu?
Uamuzi ukawa ni kumtazama bustanini, nikatoka huku napiga simu. Kabla sijafungua mlango, nikamuona kwa uwani Stellah akiwa na mtu nisiemtambua.
Mtu huyo alikuwa ni mwanaume nami nikasimama kwa umakini nikiwatazama wanacho kifanya, roho iliniuma sana na kujuta kwanini nimeona, nilitamani hata nisingeona.
Nikiwa bado naangalia pasina kusikia kinacho zungumzwa, nikakumbuka kauli za wazee kuwa kama unampenda Mpenzi wako na huna uwezo wa kumuacha, basi usitengeneze fumanizi wala usimchunge wala kumchunguza, utaumia bure.
Sasa hicho ndio ambacho leo name nahisi kabisa kunitokea, maana niliona dhahiri kuwa kuna jambo ambalo linaendelea, japo limenitokea kwa dharula lakini nilitamani nisingeliona.
Stellah alikuwa amesimama na jamaa alikuwa amepiga magoti na kuweka sikio la kulia kwenye kitovu cha Stellah kisha akasema kwa sauti sasa, sauti ambayo iliyonifikia hata mimi kule nilipokuwepo, unajua alisemaje? Alisema
“Nasikia sauti ya mwanangu akicheka!”
Hapo ndipo uvumilivu uliponishinda, yaani mimba yangu mimi ambae hata siku moja sijadiriki kusema hivyo, huku nikiomba usiku na mchana mke wangu kipenzi azae salama, mtu mwingine kutoka huko kusikojulikana anakuja kwangu kujitangazia ufalme?
Sikufikiria mara mbili, nikachomoka pale kwa kasi ya ajabu na kuelekea pale walipo wao nikiwa na nia ya kumvamia Yule jamaa, Stella ndio alianza kuniona na kutaharuki na kumsukuma Yule jamaa yake. Akiwa bado kashangaa, nikamvamia na kumuuliza yeye ni nani na anafanya nini pale?
Akanijibu kwa kujiamini kabisa kuwa yeye ni rafiki wa Stellah na amekuja kumuona, nikamuuliza kama ni rafiki iweje ampime mtoto wangu bila ruhusa yangu na kudai ni wake? Jamaa akamtazama Stellah ambae muda huo alikuwa akitetemeka, hakujibu lolote.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikuwa nipo kishari zaidi, nikamvaa mzima mzima nikitanguliza bega la kushoto, nikakuta tayari amejiandaa, akanikwepa na nikaanguka. Upesi nikanyanyuka haraka na kumtupia ngumi iliyompata shingoni na kumtia hasira, akanirushia teke nami likanipata ubavuni.
Ugomvi ukawa mkubwa, Stellah akawa anapiga makelele na hajui la kufanya, mara aniite jina langu ili kuniamua au wakati mwingine anaita jina la Amani, hapo ndio nikalijua jina la Yule jamaa kuwa naitwa Amani, hapohapo nikalikumbuka na jina hilo aliwahi kunitajia siku za nyuma.
Sikuwa vizuri kwenye mapigano, nilihisi kuzidiwa, nikanyanyua kopo la Maua na kumtupia Amani, akaliona na kulikwepa.
Wakati akilikwepa mkono wake mmoja ukamsukuma Stellah aliekuwa akituamua na kuanguka chini, pale alipoangukia ni kwenye kingo za maua ambazo zilitengenezwa kwa tofali za kuchoma, Stella akapigiza kichwa na kupiga kelele mara moja tu, akazimia.
Hatukuamuliwa tena, tulijiamua wenyewe. Tukaacha kupigana na kumsogelea Stellah, nilimnyanyua kichwa na kumtikisa, hakuzinduka. Ila kupitia taaluma yangu ya udaktari.
Nilijua kuwa hatochukua muda mrefu atakuwa amezinduka,kwani alijipiga sehemu ya mshipa wa fahamu ambao ulikata mawasiliano ghafla kutokana na kubanwa, ukashindwa kufikisha hewa safi ndani ya ubongo na kufanya kushindwa kufanya kazi yake inavyostahili.
Nikamwambia Amani ambebe miguuni tumpakie garini ili tumuwahishe hospitali.
Haraka haraka tukampakia garini, wakati mi namuweka vizuri, tayari Amani aliisha shika Sterling.
Akanitazama na bila kuomba, mimi mwenyewe nililielewa lile jicho lina maana gani, nikatoa funguo mfukoni, nikampa, akaondoa gari kama vile yupo kwenye mashindano ya Formula 1, mwendo ulikuwa ni wa kasi sana kiasi nikahisi sio tu kufika salama, bali hatutafika kabisa hospitali ya Muhimbili.
Mungu alitusaidia na kufika salama Muhimbili na kupokelewa na manesi waliomuwahisha kwa daktari akiwa tayari na fahamu zake lakini akilalamika kuwa anahisi uchungu. Alionyesha kabisa wakati wake wa kujifungua tayari umefika.
Tukiwa tunasubiri nje ya chumba cha wazazi, niligeuka na kukutanisha macho na Amani, nikafyonza huku nikijipongeza kwa kuona damu kwenye shati lake, nikajua tayari nimeisha mmwaga damu yake. Yaani hata pale nilitamani tu niendelee kupigana nae.
Chuki ilikuwa ni kubwa sana. Ghafla akatokea Dr Kareem anaenifahamu, akishangaa kuniona pale na jinsi nilivyo, akanitaka niongozane nae ofisini kwake mara moja.
Nikaenda na kumueleza kuwa nipo pale kumsubiria mke wangu anaetarajia kujifungua muda ule, alitikisa kichwa na kuniuliza kwanini hatukwenda Amana na kuamua kuja Rufaa?
“Kareem ni kama kuchanganyikiwa vile, halafu si unajua kuna wakati inabidi mazoea yabadilike? Ningeenda amana kazi zote ningefanya mwenyewe, ni heri hapa mpo nyie,” nikacheka na Dr. Kareem akatabasamu.
Hapo sasa akanishtua baada ya kuniuliza mbona nimepasuka juu ya jicho la kushoto? Sikuwa na jibu la kumpa, nikasogelea kioo na kujitazama. Dah! Tayari damu ilikuwa na dalili za kuganda, nikataka kunawa, Dr Kareem akanizuia na kuniuliza mbona ninafanya mambo kama si daktari?
Kweli hata nami nikaona aibu, akanishauri nishonwe, sikupinga, nikakaa ili kuwapa nafasi wao wafanye kazi yao. Wakaanza kunisafisha na kunishona, wakati wakinishona ndio nikatafakari kwamba Amani amenimwaga damu na si mimi nilie mmwaga yeye, akanizidishia hasira zaidi.
Waliendelea na kazi ya kunisafisha na kunishona, kazi iliyochukua wastani wa kama saa zima, kisha nikashukuru na kutoka kuelekea Maternity kumuona mama wa mtoto wangu.
Niliamini kwa muda huo itakuwa yupo vizuri tayari kiafya japo sikutegemea kumkuta akiwa amejifungua.
Kufika kule nikaambiwa tayari Stella kaisha pelekwa wodini kwani alijifungua salama muda uleule alio fikishwa pale. Nikaruka juu kwa furaha, japo sikuwa nimemuona wala kujua ni mtoto gani aliezaliwa, ila ile hali tu ya kujifungua salama, ilitosha kabisa kunipa faraja.
Nikatoka haraka kuelekea ilipo wadi ya wazazi na kuulizia Stellah, Nesi aliuliza ni muda gani kaletwa? Nikamjibu ni kama saa moja iliyopita. Ama kweli siku ya aibu ni aibu tu hata ufanyeje, siku hiyo suruali hata ukiifunga kamba badala ya mkanda, ni lazima itaanguka.
Jibu la Nesi sikuliafiki kabisa, eti ananiambia Stellah tayari ameruhusiwa na ameisha chukuliwa na mumewe. Nilitazama pembeni nikitabasamu kwa kebehi, kisha nikamgeukia na kumuuliza, “Eti unasemaje wewe?” akanukuu jibu lilelile la awali na kuuliza kwani vipi?
Nami nikamwambia kuwa Stellah ni mke wangu mimi hapa na imekuwaje wamruhusu mapema vile? Swali nililouliza halikuwa la msingi hata kidogo tena kwa daktari ambae jambo kama hilo alilitambua kama nilivyo mie, sikupaswa kuuliza vile.
Lakini kwa kuwa Nesi nae hakutambua kazi yangu, alinijibu kwamba mara baada ya Stellah kufikishwa Maternity, hakuchukua muda mrefu alkajifungua salama u salimin, na walipofikishwa wodini akiwa na mwanae, mumewe akaomba tu waruhusiwe.
“Nasi kwa sababu tuna uhaba wa vitanda, ukizingatia na hali zao wote hazikuwa mbaya, nilipomkagua nikakuta anahudhuria kliniki kila mwezi, anapata matunzo anayostahili mama mjamzito, basi tukamruhusu mumewe amchukue huku nikimpongeza kwa kazi nzuri ya malezi ya ujauzito huku nukimuasa aendelee hata baada ya mtoto kuzaliwa, wakashukuru na wakaondoka...”
Maneno yale yalikuwa ni makali mno moyoni mwangu, nikashindwa kuvumilia, huwezi amini nilimkatiza Yule Nesi na kumwambia mume wa Stellah ni mimi na ndio nastahili kumchukua Stellah pale hospitali.
Akajibu kijeuri kuwa hilo yeye wala halimuhusu, kama vipi niende nyumbani kumuangalia. Nikatoka hadi nje na kulikuta gari langu lipo pale pale kwenye Parking. Nililisogelea na kukuta hata funguo ipo mle ndani ya gari, nikaingia na kujiuliza Stellah kaondoka na nani?
Wakati huo nilikuwa ninalo jibu, ila sikutaka kuliamini, nilichotaka ni kuupindisha ukweli uwe uongo, kitu ambacho isingewezekana, maana ni dhahiri Amani ndio kamchukua Stellah na kuondoka nae. Hadi muda huo simu ya Stellah ilikuwa inaita tu bila kupokelewa.
Nikapiga tena, ikakatwa, kitu kama hicho hakijawahi kunitokea hata siku moja katika maisha yetu, tangu kabla sijampata hadi leo katoka kujifungua ndio ananikatia simu kwa mara ya kwanza, na tangu hapo, simu yake haikupatikana tena. Nikapiga ngumi kwenye Sterling.
Nikawasha gari na kuelekea moja kwa moja nyumbani nikitegemea huenda watakuwa wamerejea, nilikuwa nikijipa moyo tu kutokana na mapenzi makubwa niliyokuwa nayo kwa Stellah.
Lakini akili tayari iliisha kata suala la Stellah kuwepo nyumbani kwetu.
Nyumbani nilifika na kukuta hata taa hazijawashwa, hiyo ndio ilinikatisha tamaa, nikaingia na kuwasha taa zote na kujitupa sofani, nikajaribu kumpigia tena lakini sikufanikiwa kumpata. Nikajiuliza nifanye nini ili nijue ni wapi alipo Stellah?
Nikatoka na kuanza kumtafuta Stellah nikiwa hata sijui ni wapi pa kuanzia, nikaenda kila sehemu ninayoijua, sikumpata. Niliwapigia simu mashoga zake wote kuwaulizia hata kama wana fununu ni wapi alipo, sikufanikiwa. Nikavunjika moyo.
Nikarejea nyumbani na kusubiri muujiza, muda wa kazi ulipofika mie nilikwenda kazini na kukaa tu, nilishindwa kabisa kufanya kazi, kuna muda nilijilazimisha kufanya kazi, lakini mtu alieingia kumtibu nikatoa kali ya karne, kasema jino lina muuma, mimi nikampa cheti akapime Malaria badala ya kumuandikia kwenda kung’oa hilo jino bovu.
Sikushtuka hadi Nesi alipokuja nae ili apate ufafanuzi. Nilisikitika na kumuomba msamaha mgonjwa wetu kisha nikarekebisha. Nikaona leo si siku njema, nikaondoka mapema kabla sijaharibu kabisa.
Niliendelea kumtafuta wiki mzima pasina mafanikio, nilidhoofu na utendaji wangu wa kazi ukashuka, watu wote sasa wakajua kuwa nina tatizo japo niliwaficha. Kipindi chote nikiwa na Stellah sikuwa na rafiki wala mtu yoyote wa karibu zaidi ya Stellah, kifupi alikuwa ni kila kitu kwangu.
Kwenye familia yao niliwajua kwa kuwaona mara moja tu walipokuja kutoka sehemu mbalimbali na hata kwenye simu niliongea nao mara chache mno, Hapa najaribu kukuonyesha umuhimu wa Stella katika maisha yangu ya kila siku, nikaanza kujaribu kumtoa kichwani mwangu, bado nilionekana kushindwa.
**********
Siku moja nilipotoka kazini nikaenda kumtembelea jamaa yangu mmoja niliesoma nae Urusi huko, Yeye akiwa upande wa jeshi mie kwenye udaktari, Jamaa huyu aliitwa Daud, nae nilipofika kwake nikamkosa, mkewe akaniambia amekwenda Afghanistan ila amebakiza wiki 7 kabla ya kurejea Bongo, nilishukuru na kuaga ili niende.
Shemeji yangu akanipa pole kwa yaliyonikuta, nilitoa shukran japo sikujua ana maanisha nini, lakini kama aliejua kuwa ninajiuliza, akaniambia moja kwa moja kuwa amepata taarifa juu ya mke wangu kutoweka nyumbani.
Nilishangaa habari za kutoonekana mke wangu zilivyosambaa, ilinichanganya sana ile. Nikaondoka. Simu ya Stella haikupatikana tena hadi siku moja nikafunga safari hadi zilipo ofisi zake.
Ama kweli wa kukosa ni wa kukosa tu, hata apate kitakua hakifai. Nilifika na kumuulizia Stellah, nikaambiwa ana mapumziko ya uzazi kwa muda wa wiki 10. Nikauliza nitampataje? Wakasema hata wao hawajui, maana hapatikani kwake wala hewani
Palikuwa na mabinti wawili waliokuwa pale mapokezi, nikawauliza ni wapi alipo Eva? Wakasema Eva ana kazi moja ya Interpool, hivyo kwa sasa hayupo kabisa Tanzania. Mabinti wale hawakunijua mie ni nani, nikawauliza tena yu wapi Amani?
Wakasema ana zaidi ya wiki hajakanyaga ofisini, mara nyingi huwa anafanya kazi zake nje ya ofisi, hadi awe na shida maalum ndio hufika pale, kwani vipi? Alinieleza binti mmoja wapo na mwingine akani twanga swali, maana aliona nimezidi maswali.
Nikawajibu kwa kujitambulisha kuwa mie ni mume wa Stellah, walishangaa na kunipa hongera ya Stellah kujifungua, ila kilicho washangaza ni mimi kwenda kumuulizia Stellah ofisini badala ya kujua alipo. Nikawaonea huruma kwa kujua kuwa hawaelewi lolote linalo endelea.
Nikawaaga na kutoka lakini ikionesha dhahiri kuwa wao walinionea mie huruma zaidi, maana niliwasikia wakisema Masikini ya Mungu, sijui Stellah yupo wapi? Sikujali nikatoka nje na kurudi nyumbani, ikawa ni kazi moja tu...http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pombe za kila namna, Ikiisha Whisky navuta Wine, toka jua linachomoza hadi linazama, tangu nyota zinatoka hadi zinapotea, mie mwanaume ni kazi hiyo hiyo, nyumba yangu ikageuka kuwa ni ‘Home of Wine and Spirit’
Ulevi ukasababisha nikawa ni mtoro kazini, nikawa sili vizuri na kibaya zaidi sikuwa na mawasiliano na mtu yeyote, achana na ndugu, si jamaa wala rafiki, niliona ni kama wananipigia kelele tu.
Niliamua kuianza dunia yangu mpya, Dunia ambayo niliona kama kwamba inanifaa kuishi peke yangu, ilikuwa ni sayari mpya, sayari ya vinywaji vikali, vinywaji ambavyo niliamini vyenyewe haviwezi kunisaliti…
**********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment