Search This Blog

Friday, October 28, 2022

KURASA (THE PAGES) - 3

 

     





    Simulizi : Kurasa (The Page)

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Siku moja wafanyakazi wenzie Stellah wakaja nyumbani ili kumpa hongera Stellah ya kujifungua, hapo tayari ilikuwa imeishapita kama mwezi mzima tangu ajifungue na wakati huo mimi hata Sijui Stellah mwenyewe na mtoto wapo wapi.

    Walinikuta nipo kifua wazi nimelewa vibaya, nilipofungua tu mlango na kuwaona ni wao, nikawatimua na zawadi zao bila soni, sikutaka hata kuwakaribisha ndani, niliona kama vile wametumwa tu kuja kunisanifu na hawakurudi tena nikiwa pale.

    Wiki sita zikaisha nikiwa sijafika kazini bila taarifa yoyote, nikafukuzwa kazi, wala sikujali, tayari nilikuwa nimepoteza dira. Stellah alikuwa ndio kila kitu kwangu, nilipompoteza yeye ikawa ni kama nimepoteza kila kitu naweza kusema nikapoteza mwelekeo wote.

    Sikuwa tena na kazi, nikawa mlevi wa kutupwa, ndugu zangu hawakujua lolote huko mkoani, akaunti zangu zikanza kukaukiwa salio, maana pesa zilikuwa zinatoka tu bila kurudi, lakini mimi wala sikushtuka, nilijiona nipo sahihi tu, niliamini lawama zote zinapaswa kumuangukia Stellah.

    Kila nilipolala nilikuwa nipo chakari na nilipoamka tu niliwaza pombe. Siku hiyo asubuhi nipo na VAT 69 kwenye sofa saa 2 mlango ukagongwa, nikatembea kilevi kuufuata mlango, nikauliza ni nani anasumbua watu wakiwa wameji pumzisha? Sikupata jibu lolote

    Nikamwambia aliegonga kama hataki kujitambulisha, basi mie sifungui mlango na ninarudi chumbani kulala. baada ya kama dakika moja naona aliegonga mlango akajiongeza alipoona ni kweli mlango haufunguliwi, akajitambulisha kuwa yeye ni Daud, nikamfungulia na kumkaribisha ndani.

    Hali aliyonikuta nayo nina hakika kabisa ilimuumiza maana alinisogelea na kuniuliza kama ni mie, nikamjibu kihuni tu kuwa kwani anaona mie ni nani? Kisha nikamsukuma, nae akanipisha kidogo tu huku akinitazama kwa masikitiko makubwa, nikaingia sebuleni kwangu.

    Sijui akili yake ilimtuma nini hadi kuniuliza vile? Ila alivyokuja kule sebuleni..,







    Akashika glasi na chupa yangu ya wine na kutoka navyo nje, kisha karudi na kuketi karibu yangu na kuanza kunihoji kulikoni? Nakumbuka kabisa nilimwambia sijui.

    Akanibembeleza nimwambie ni kwanini nipo katika hali ile, mwanzo niligoma na kumwambia kwanza alete pombe yangu, nae akakataa, akadai atanipa baada ya kumaliza maongezi yetu, nikamwambia aapie, Daud akaapia, alifanya hayo ili kuniridhisha tu, name nikaridhika na kuanza kumuhadithia.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikamwambia tatizo ni Stellah, akasema anajua, nikamuuliza kajuaje? Akasema kaambiwa na mkewe tangu akiwa Afghanistan ila hakujua kama ndio nipo katika hali ile, nikamwambia kuwa yale ndio maisha yangu niliyo amua kwa sasa, nimechagua kuishi vile ili kupunguza mawazo.

    Daud alikuwa ni mtu mwenye busara sana, akaniuliza hali ile itakuwa vile hadi lini? Nikamwambia hadi nimuone Stellah ama nife tu. Akasikitika na kuanza kunipa darasa juu ya maisha ya kimapenzi.

    Alinieleza kuwa kuna watu wengi sana wamewahi kupata matatizo makubwa zaidi kuliko hata yale ya kwangu lakini hadi leo wanaishi hapa Duniani wakiwa noi wenye amani na furaha tele. Nilimtazama na kumwambia tatizo lililonikuta mie kama lingemkuta mtu mwingine kama yeye Daud, basi angekufa kabisa.

    Niliamini tatizo langu ni kubwa kuliko matatizo yote hapa duniani, nilimuona hata Daud alinionea huruma, alijitahidi sana kunipa moyo ili niyashinde yale mawazo potofu, hakika alionesha ukomavu sana rafiki yangu Daud.

    “Ukweli hukupa kujiamini na kukufanya uwe huru kifikra, bora uujue ukweli unao uma kuliko kusikiliza uongo unaokuhadaa,” hiyo ni sehemu tu ya maneno yake adhwim aliyonishawishi kukubaliana na kauli zake.

    Hatimae alifanikiwa, hasa baada ya kutoka nae na kwenda kwa daktari wa magonjwa ya Saikolojia, huko nilipewa darasa la kutosha sana, nikawa kama mpya vile, hakika kumbe sikujua kama nimeathirika kiasi kile.

    Tulirejea nyumbani nikiwa ni Ramaah mpya kabisa, nilifika na kufanya usafi, kuanzia nyumba, nguo na hata mazingira yote yalikuwa hayafai, nikalala usiku wa kwanza nikiwa ni Ramaah mpya kabisa baada ya kuikosa amani kwa muda mrefu.

    Asubuhi nilipoamka nikawa ninasumbuliwa na kitu kimoja... kazi! Sikuwa na kazi na nyumbani nilihisi pananichosha, yaani mapema tu niliona nyumbani ni kama Jehanamu, ukiwa na kazi nyumbani hapachoshi, ila ukiwa huna kazi, nyumbani napo hupatamani hata kidogo.

    Niliwaza mengi sana, ila mapenzi sikuyapa nafasi, nilifikiri kuhusu maisha yangu, nilitamani maisha mapya, niliona kama yananielemea bila kazi na kiukweli ni heri jiwe likuegemee kuliko maisha yakuelemee.

    Jioni nilikwenda mwenyewe kuonana na Daud na kuongea nae juu ya suala lile, alifurahi kusikia nimerejea kwenye akili ya kawaida, akili ya kiubinadamu, akaahidi kunisaidia, kwani lile kwake ni jambo dogo sana.

    Ndani ya mwezi mmoja, kwa kutumia nakala ya vyeti vyangu, Daud akafanikiwa kunipatia kazi, ilikuwa ni katika jeshi la wananchi. Kulikuwa na vigezo vingi vilivyohitajika na kwa bahati mzuri nilifnikiwa sana kutokana na kuwa na umri sahihi uliopangwa na wenye Jeshi lao na elimu yangu.

    Nikashinda usaili na kuingia kama daktari, pale nikapewa miezi kadha ya kula shushu kwanza nikionesha kile ambacho kimenifanya nichukuliwe mle jeshini, kisha nikapelekwa Depo huko Makutupora, mkoani Dodoma.

    Nikiwa huko mazoezi yalikuwa ni magumu mno. Mwanzo nilikata tamaa kabisa, lakini kilka nilipoongea na Daud, alinitia moyo na kuniambia sasa ninaanza maisha mapya, na ile ni sehemu yenyewe ya hayo maisha mapya ambayo nimekubali kuwa ndio sehemu ya maisha yangu.

    “Maisha hayabahatishwi, maisha yanapangwa, ndugu yangu panga maisha yako kwa sasa kwa kusisitiza kazi na si mapenzi, kwani kazi inapanga mapenzi na maisha, lakini mapenzi hayapangi kazi wala maisha,” aliniambia akiamini huenda ni mapenzi ndio yananishawishi kuwa vile.

    Hakujua kama ninalia ndani ya moyo wangu, ninalia bila kutoa machozi, nina huzuni kubwa kila ninapofikiria kuhusu penzi langu ambalo limelazimishwa kuvunjwa bila hiari yangu.

    Lakini kifupi maneno yake yalikuwa yakinipa ujasiri wa hali ya juu sana, ikafikia hatua nikaona mazoezi yale ni ya kawaida sana, nikazidisha na kujituma zaidi ya pale kiasi ambacho hata mkuu wa mafunzo yetu akawa akinichukua mie kama mfano.

    Hali ile ya kujituma kimazoezi iliwashangaza wengi sana maana nilitoka Zero hadi kuwa Hero, yaani kutoka muoga hadi kuwa shujaa kukasababisha hata Wakufunzi wa awali, jamaa zangu nilioanza nao na kila mtu alie kuwa karibu yangu alinipongeza japo wao hawakujua ni nini nilikuwa nimelenga kichwani mwangu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tukiwa tunakula kiapo cha utiifu kwa Rais na jeshi letu, zikatokea nafasi 3 za watakaopenda kujitokeza na kusomea mafunzo ya awali ya ukomandoo. Walituweka wazi kabisa kuwa mafunzo ni magumu sana ambayo wakati mwingine hupelekea hata kifo kwa askari waliojitokeza.

    Kundi lote liligwaya, watu wawili tukajitokeza, wenzetu walitushangilia sana na kupelekwa kwenye ofisi ya komandoo wa Kanda, kwanza alitupongeza na kutuasa kuwa mafunzo tutakayo anza kujifunza ni magumu mno, je tumejiandaaje?







    Nikamtazama mwenzangu na kukuta akinitazama mie, nikageuka na kukuta Brigedia nae akituangalia kwa zamu, mimi nikamwambia huku nikimtazama kuwa sisi ni watu wakubwa na wenye akili zetu kamili, tumeamua kwa ridhaa yetu na wala hatujashawishiwa wala kulazimishwa na mtu yeyote.

    Jamaa niliekuwa nae akaongezea kuwa tumeamini tunaweza na ndio maana kama wengine wanavyoweza ndio maana nasi tupo pale, nikawa nikitikisa kichwa kumuunga mkono, Brigedia nae akaitikia sawa na kutupa mikono. Mi nikajua hapa sasa kazi imekwisha.

    Ajabu Brigedia akatuambia anatupa nafasi ya mwisho ya kujifikiria tena na kutuambia tuwasiliane na watu wetu wa karibu ili tushauriane nao bila kuzisahau familia zetu, siku ifuatayo mapema saa 2 tumpelekee majibu, akaturuhusu tuondoke.

    Tuliondoka tukiwa kama hatujiamini vile, kifupi nasi tulianza kuuona ugumu wa kazi yenyewe hata kabla hatujakabidhiwa. Nilijiuliza kichwani iweje hadi Brigedia anatupa nafasi ya kujifikiria mara mbili?

    Usiku ule niliutumia kuongea na jamaa zangu, wapo walionipa moyo na hawakukosekana wa kunitisha na kunikatisha tamaa, nikakumbuka kauli moja ya mwanafalsafa mmoja mbobevu isemayo

    ‘Yanayotukatisha tamaa, kamwe hayawezi kutuvunja moyo’ nami binafsi huwa nina kauli yangu hupenda sana kuitumia ‘What we do, depends on what we feel’ ikimaanisha kile tunachokifanya inategemea na kile tunachofikiri.

    Hivyo msimamo wangu mie ukabaki palepale, nikamjulisha Daud kuhusu msimamo ule, sikuwa naelewa yeye atasimamia upande gani kwenye suala lile, lakini baada ya kumpigia alishangaa na kuniuliza ni wapi nimepata ujasiri ule?

    Nikamwambia kwamba katika kupambana na maisha kuna mengi sana anatokea, mema na mabaya, ugonjwa na kifo, sasa ni bora ufe ukitafuta kuliko kufa kwa kuteseka na njaa na manyanyaso.

    Akaguna na kusema yeye kwa muda ule hatokuwa na jibu la moja kwa moja, bali anataka kuongea na wazazi wangu kwanza kisha ndio atanipigia yeye na kuungana rasmi na jibu la wazazi wangu.

    Nilicheka na kumwambia kuwa hata yeye hajiamini? Nae kule akacheka na kusema ameanza kuniogopa maana huo ujasiri wangu umekuwa ni wa ghafla sana na tena ni wa muda mfupi sana, tukaagana.

    **********



    Kwa kuwa nae alikuwa ni mmoja kati ya wanajeshi wenye vyeo vikubwa, aliweza kunipigia simu wakati wowote na nikaitwa kwenda kuongea nae, hivyo nusu saa baadae, alinipigia na kuniarifu kuwa wazazi wametoa Baraka zao japo hapo awali sikutaka kumwambia kuwa walinikatalia.

    Nilipoongea nao mie mwenyewe hawakuwa radhi kabisa mie kuendelea mbele zaidi ya pale, maana hata ile kazi ya Jeshi tu, wao hawakuwa wakiitaka, walipenda niendelee tu na kazi yangu ile ya udaktari maana wao hawakujua kuwa ni hiyo hiyo ndio kazi yangu hata kule jeshini.

    Wazee wetu wengi hawapendi vijana wao tujiingize kwenye suala la kijeshi wakiamini huko kuna mambo mazito mno na kifo kipo karibu nawe kuliko alie nje ya jeshi. Baada ya kunieleza matokeo ya huko, akanitakia mafunzo mema na kukata simu.

    Furaha yangu ilipita kiasi mara baada ya kujua sasa hata wazazi wapo radhi mi kuingia kwenye mafunzo ya ukomandoo, nikapata shauku kubwa mno ya kuanza mazoezi, hadi nikahisi hata asubuhi haifiki. Usiku ule nikauona ni mrefu sana na vile sikuwa na usingizi, ndio ikawa shida zaidi.

    Muda wote uliobakia kabla ya kufika asubuhi niliutumia kwa mawazo kedekede. Nilipitia mengi hadi kufika kwa Stellah, nikamkumbuka mwanangu, hasira zikanishika hasa nilipokumbuka jinsi nilivyodhalilishwa na Amani mbele ya mke wangu.

    Nikanyanyuka usiku uleule na kuelekea Gym nikiwa na jazba vibaya mno, mwili ulitamani kuchangamshwa, akili nayo ilikuwa tayari kwa hilo, nikaisogelea milango ya chumba cha mazoezi.

    Bahati nzuri askari wa zamu akanizuia na kunitaka nirejee bwenini kwangu kulala, nilimuomba aniruhusu tu akakataa na kuniamuru nirejee ndani, sikumbishia japo nilijua kuwa nimemzidi cheo, lakini itifaki ilizingatiwa.

    Asubuhi baada ya mzazoezi ya awali, niaelekea kwenye ofisi ya Komandoo, nikishangaa kumkuta tayari jamaa yangu ameisha fika, tena inaonekana ni muda mrefu tangu awasili pale. Niliungana nae pale kwenye viti vya kusubiria na kumsalimia

    Haikuchukua muda mrefu sana kabla mtu tuliekuwa tukimsubiri hajawasili na kutuita kuingia ndani ili kuzungumza nae, cha kwanza alichofanya baada ya salamu ni kutuuliza misimamo yetu, msimamo ambao hata kichwani mwake tayari alikuwa ameisha ujua.

    Kile kitendo cha kutukuyta tu pale tayari kilikuwa ni ishara tosha kuonesha msimamo wetu ni upi. Lakini kwa kuwa alitaka kauli kutoka midomoni mwetu, tulimwambia kuwa msimamo wetu ni uleule na katu haubadiliki.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akatuuliza kama hatuogopi kifo. Nilimtazama jamaa yangu nae akatambua ni kipi ninamaanisha, akaweka koo lake vizuri na kusema kumwambia mkuu pale kuwa kila kilicho na uhai ni lazima kife, tatizo ni kupishana tu muda.

    Komandoo akasema huku akitutazama kwa zamu kuwa sisi ni bado wadogo sana kufa, mimi sasa nikanyanyua ulimi wangu na kumwambia, kuishi muda mrefu hakuna maana kama hakuna cha maana ulichokifanya.







    “Unaweza kuishi kidogo lakini ukafanya kitu kitakachokufanya uendelee kuishi milele,” akatikisa kichwa kuikubali kauli yangu na kusema kuwa sasa ameamini tumedhamiria kuingia kwenye mafunzo ya ukomandoo.

    Kwa ruhusa yake tukatoka baada ya kutuambia kuwa kabla ya kuisha wiki hii, atakuwa ametupa maelekezo mengine. Tukaelekea nje tukiwa ni wenye furaha kubwa na mwenzangu huku tukipongezana, kila sehemu tuliyokuwa tunapita, tulikuwa tunanyooshewa vidole.

    Kuna waliotunyooshea vidole kwa kutupongeza wakituona mashujaa, hawa walikuwa ni wachache sana, lakini wengi wao walitunyooshea vidole kwa kutusikitikia na kutuona ni wapumbavu kupita kiasi, ila kwa sababu tulikuwa tumeamua wenyewe, hiyo wala haikutusumbua.

    Sisi tulikuwa tayari kwa lolote, na hasa mie ambae kwa sasa nilihisi kama sina cha kupoteza kwani kama ni mke na mtoto Sijui wapo wapi lakini niliamini kama hata nitakufa huko, mtoto wangu atalelewa vizuri tu na mama yake kwani ana kazi nzuri tu.

    Ikitokea kama nitarudi salama kutoka huko, ndio nitafanya mpango wa kuanza kuwasaka mke wangu na mtoto wangu hadi nitakapowaona, hasa nikilenga kumsaka mtoto.

    **********



    Jioni ya siku hiyohiyo nikiwa na daktari mwenzangu mmoja, nikaja kuitwa nikiambiwa nahitajika kwenye ofisi ya mkuu wa kikosi cha mizinga, kikosi cha mizinga kinatenganishwa na hospitali kwa kilometa kama 6 hivi, na hapa hupaswi kutembea, ni mbio tu.

    Eneo hilo ambalo ni maarufu kama Smart Area, huwa ni eneo matata sana, unaweza kujikuta unapata adhabu bila watu kukutazama machoni, hivyo ili kuepuka adhabu zingine ambazo zinaepukika, nikaona nitii sheria tu.

    Nikaanza kutrokt taratibu, maana mbele kidogo kutoka ilipo hospitali, kuna kama kilometa 2 hivi unakutana na kichaka kidogo. Kufika pale nikasimamishwa na askari mwenzangu Yule ambae nae anakwenda nami kwenye mafundisho ya Ukomandoo aliekuwa akitokea kikosini huko Mizinga.

    Kabla mi nae hatuja salimiana, kutoka usawa wa kile kichaka, likatokea kundi kubwa sana la askari lisilopungua kumi na kidogo na kututeka kiurahisi sana, maana walivyokuwa wakija, tulihisi hawa wapo kwenye mazoezi ama kwenye adhabu, kumbe dah!

    Walitukaribia na kutuzunguka, kisha wakatuvamia na kuanza kwa kunifunga mikono na miguu kwa nyuma, wakanifunga kitambaa usoni na kunivua Tshirt yangu ya jeshi ile yenye mabaka mabaka na kifuani nikabaki na Singland, nayo ilikuwa na pale pale wakaikata suruali yangu kwa juu ya magoti nikiwa ninaona.

    Nikashikwa na jazba na kuwauliza kwa hasira wao ni kina nani na kwanini wananifanyia vile? Hawakunijibu bali walinicheka tu kwa kejeli na wakati huohuo Yule mwenzangu pia alikuwa akitendewa hayohayo kama mimi.

    Wakachukua kitambaa na kunifunga usoni ili nisiweze kuona kinachoendelea, nikasikia sauti ya gari ikisimama, wakanibeba juujuu kama gunia na kunisweka ndani ya ile gari na kuondoka pasina kujua naelekea wapi

    Kwa hasira kubwa nikawauliza ni wapi wananipeleka? Mmoja wao akajibu kwamba sisi si tunajidai tunautaka ukomandoo, mbona tumeshindwa kuziokoa nafsi zetu wenyewe? Kisha wakacheka kwa sauti ya dhihaka tena ile ya juu kabisa.

    Kichwani mwangu nikagundua kuwa hawa ndio katika wale wasiopenda kutuona sisi tukisomea ukomandoo, mimi nikajiuliza tena imekuwaje wakafanikiwa kuniteka kiurahisi hivyo na hali tupo kwenye eneo la ndani la jeshi? Tena ni eneo lenye ulinzi mkubwa muda wote?

    Nikahisi hapa kuna namna tu, kama hawa hawajawaua walinzi pale getini, basi watakuwa wameshirikiana nao. Kichwani suala la kuwaua walinzi bado halikukubali, maana bado wangeweza kuonekana tu, maana kila sekunde watu wanapita pale.

    Wazo la kushirikiana nalo nikalipitisha moja kwa moja hasa pale niliposikia getini mtu akifungua geti huku akiuliza mmewapata. Wakaondoa gari na inaonesha tulikwenda mbali sana, maana gari ilikuwa ikikimbia mno kiasi hata sikujua kama hata ningekuwa macho wazi ningeweza kuruka.

    Nikiwa sijui niwapi, walituteremsha sehemu Fulani lakini niliweza kupata hisia za maji maana walinifungua kamba za miguuni na kunisukuma wakinitaka nitembee huku nikiwa naongozwa na mmoja alienishika mkono wa kulia, nilijitahidi sana kuwa mtata lakini haikusaidia.

    Hatua kama 10 mbele hivi tukiwa kwenye maji, nikanyanyuliwa na kuwekwa ndani ya kitu Fulani na kusikia muungurumo wa injini ikiwashwa. Nikagundua kuwa nimepakiwa kwenye boti ya kienyeji, nikawaomba wanifungue mikono, wakanijibu kwa hasira hadi nikishangaa, nikajiuliza kwani mimi nina ugomvi nao gani watu hawa?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alienijibu aliniamuru kukaa kimya kabisa na kunitaka nisiwasumbue, tena sauti hii ilionekana ni tofauti na zile za walionileta kutoka kambini. Nikataka kuanzisha utata, lakini nikajiona ni bwege, maana nimefungwa na sijui wapo wangapi, nikatulia.

    Hata sasa ilionekana tulikwenda mbali mno, maana miungurumo ilikuwa ni kero lakini hadi nikaizoea. Tulifika sehemu nikaambiwa nisimame, nikatii maamrisho yao, nikasimama na kushushwa hadi ndani ya maji na wakaanza kunikokota watu wawili, mmoja kila upande hadi nchi kavu, hapo ndio nikafunguliwa kitambaa.

    Duh! Ilikuwa ni giza kweli kweli, sikuweza kuona chochote hata miti sikuweza kuiona, nikafikicha macho kwa kuyafumba na kufumbua mfululizo.





    Jamaa kuwatazama wapo kama 6 hivi tena ni tofauti na wale walioniteka kambini. Wakaniuliza pale ni wapi, nikawatazama kwa ghadhabu, maana niliona kama wanachokifanya wao ni kama kunifanyia dhihaka, kitu ambacho sikutaka hata kukisikia.

    Baada ya kuniona kama nimewadharau, basi mmoja wao akanipiga ngumi kali kama mbili hivi za tumbo, kisha nikaulizwa tena swali hilo hilo na mwingine, sasa nikajibu kuwa sipajui, basi mmoja akatoa kamba na kusimama nyuma yangu.

    Nikiwa bado nimefungwa mikono, akaanza kunifunga kamba nyingine kuanzia begani hadi kwenye vitanga vya mikono, yaani kifupi ni kwamba, mikono yangu yote ilifungwa mbavuni, lakini kamba zile za mikononi walizifungua na kunifunga miguuni.

    Sikuwa na ujanja wowote, nikajiuliza kichwani hawa watu wamelenga nini vichwani mwao hadi kunifanyia vile? Maana mimi niliona ni kama ukatili Fulani hivi nafanyiwa.

    Wakaniacha nimesimama na kurejea kwenye boti yao, wakanitupia begi na kuondoka bila kusema chochote, nikabaki nimepigwa na butwaa, yaani sikuwa naweza kufanya chochote, hata kukaa haikuwezekana, nilianza kujuta kwanini niliomba ile nafasi.

    Kama watu waliosahau kitu, wakarudi na kunikuta vilevile nimesimama sijielewi, akanisogelea mmoja akiwa na kisu na kuja kunikata kamba zile za miguuni na kuniambia kwenye lile begi kuna kisu, kiberiti, risasi mbili, pamba na sindano, akageuka na kuondoka.

    Nilikuwa nikimuangalia tu akiondoka huku nikitamani mnimuombe anifungue na ile mikono, lakini aligeuka wakati ameanza kugusa maji na kusema mwenzangu mmoja yupo hapo hapo kisiwani, yeye amebeba chakula nimtafute na sipaswi kuwasha moto mle kisiwani.

    Kidogo nimuulize sasa mmenipa kibiriti cha nini? Nikajizuia maana tayari nimeisha jifunza kuwa jeshi ni nidhamu, ukiwa huna nidhamu jeshi hutaliweza, wakati wanawasha boti yao ya kienyeji, wakaniambia kitu kilichonitia shaka zaidi na kunifanya nianze kuogopa.

    Walichoniambia ni kuwepo kwa wanyama wakali na sitakiwi kuuwa hata mmoja, napaswa pia kuwalinda wasidhurike kwa aina yoyote, kuna Simba, Chui na Nyoka wenye sumu kali.

    Sasa ndio wakaondoka na kuniahidi watarudi baada ya siku 3, ama viumbe wale walikuwa ni makatili sana, hawakuwa na huruma hata kidogo, waliniacha na kamba zangu vilevile japo niliwaomba walifungue hata kiasi.

    Sikuweza kukaa wala kulala na kusimama tayari nilikuwa nimeisha choka, kamba nilizofungwa zilinitesa sana, walizibana mno kiasi kwamba nikahisi hata damu haitembei vizuri kwenye zile sehemu ambazo zimezungushiwa kamba.

    Sikujua hata ni wapi nianzie, nilitamani kulia, nilipokumbuka wazazi wangu na mtoto wangu japo sikuwa nimemuona bado, masikini ya Mungu… Nilijuta kuiomba nafasi ile.

    Nilibaki nikiwa nazunguka zunguka hadi alfajiri ilipoonekana. Kitu cha kwanza kukifikiria ni jinsi gani nijifungue zile kamba ili nirudi kuwa huru tena. Nikapata wazo la kutafuta jiwe, ilinichukua muda sana ambao siwezi kuukadiria maana sikuwa na saa, sikufanikiwa kuona hata kipande cha kokoto.

    Nikapumzika kwenye kipande cha gogo nikiwa kama mtu aliesimama vile kakiegamia. Jua lilipoanza kushika kasi nikaanza kutembea taratibu nikiomba Mungu nisikutane na kiumbe kikali, mbele yangu nikaona kitu kama pango, nikaliendea na kuingia ndani mlangoni niliweza kuona fuvu la mnyama, kama sikosei alikuwa ni Pundamilia.

    Nikapata wazo la kulisogelea na kukuta sehemu ile ya kichwa, meno yalikuwa yametokeza kwa nje na iliobaki ilikuwa imezama kwa ndani ya ardhi, nikaamua nilalie yale meno huku nikienda mbele na nyuma hadi nitakapofanikiwa kuzikata kamba zile.

    Nilijua kuwa nikiisha ikata moja, ina maana zitafunguka zote na hapo nitakuwa huru tena, ilikuwa ni vigumu mno kujilaza ukiwa umefungwa mikono yote, sasa ndio name nikatakiwa nijiangushe chini.

    Nikafaulu kukaa kwa kuanza kupiga magoti na ndio sasa nikajiangusha na kuanza zoezi langu nililolipanga. Wastani wa nusu saa nzima baadae, nikawa nimefanikiwa kukata kamba moja, kumbe kamba zile zilikuwa zimefungwa zikijitegemea.

    Kila ilipozunguka na kuishia, basi ilifungwa fundo, hivyo kwa haraka haraka nilivyo hesabu nikakuta kuna mizunguko 9 iliosalia. Kwa hesabu za haraka haraka zilihitajika nusu saa zingine 9 hapo ni sawa na masaa manne tena kwa mtu mwenye nguvu na sio dhaifu kama mimi kwa wakati ule, maana nilipigwa sana na vitu viwili, kwanza ni njaa na pili mchoko.

    Kutokana na muonekano wa jua ilikuwa inajionesha ni saa 8 ama 9, nikaamua niache na kutafuta njia nyingine mbadala. Kazi ikawa ni jinsi gani nitanyanyuka pale chini. Pale napo palinichukua wastani wa nusu saa nzima nikiwa nimeumia karibu kila sehemu ya mwili wangu.

    Kwa shida na dhiki kubwa nikafanikiwa kunyanyuka na kusimama huku nikiwa hoi bin taaban, nikawa sasa sina muelekeo maalum huku nukijiuliza nifanyeje? Mateso yalikuwa ni makubwa sana kwa upande wangu.

    Naam nikaamua kuelekea ufukweni nikiwa hata sijui ninakwenda kufanya nini japo nililenga kwenda kujipanga upya. Tahadhari ya wanyama wakali ilizidi kujirudia kichwani mwangu huku nikijiuliza iwapo itatokea kwa mimi kukutana nae nikiwa kwenye hali ile, nitafanyaje?

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Nilijiuliza nitawezaje kupambana nae iwapo tu kutembea natembea kwa shida?



    Nikaamua tu sasa liwalo na liwe, acha niende huko mbele huenda nikafanikiwa kuvuka salama ama nikapata njia mbadala kuliko kukaa na kusubiri kitu ambacho sina ahadi nacho…



    Naweza kumshukuru Mungu, bahati ilikuwa upande wangu siku ile, maana sikukutana na aina yoyote ya mnyama mkali zaidi ya kukutana na fisi pekee.



    Nilipofika pale ufukweni na kushindwa kujitambua kilicho nipeleka, kifupi sikujua nifanyeje.



    Kiu kilinishika barabara na kama ujuavyo, maji ya bahari hayanyweki, na hata ukijilazimisha jua dhahiri hayatokukata kiu,



    Nikajiuliza nifanyeje mie Ramaah komandoo mtarajiwa? Nikajiuliza ni kipi kilinishawishi kujiunga na mafunzo haya?



    Sikupata jibu, zaidi ya kuona majuto tu ndani ya nafsi yangu, nikaanza kutembeza tembeza macho yangu kila upande.



    Katika angaza angaza nikaona gamba la samaki wa baharini, nikalisogelea na kuligeuza geuza kwa miguu, nikapata wazo jipya kabisa.



    Kiu ikaniisha palepale, lakini kabla sijalifanyia kazi wazo langu, nikaiona changamoto moja, hakika ilikuwa ni kikwazo kwangu. Viatu...



    Naam Viatu nilivyovaa viligeuka kuwa ni kikwazo kwangu, nitavivuaje na hali mikono yote imefungwa?



    Kama ujuavyo, viatu vya kijeshi ni virefu na vinafungwa kamba hadi mwisho kule juu, nilihisi hasira sana, lakini nilijua kuwa haitanisaidia maana muda nao ulizidi kunikimbia.



    Nikasogelea tawi la mti ulio anguka na kuchomeka sehemu palipofungwa fundo la kamba zile za viatu, huku nikijisaidia na mguu mwingine, nikabana upande mmoja wa kamba na kuruka kwa kurudi nyuma.



    Japo niliumia lakini nilifanikiwa kufungua fundo la juu kabisa la kamba ile ya kiatu kama vile nilivyokuwa nikihitaji.



    Nikaendelea kulegeza kamba kwa kusaidiwa na tawi la mti, kila nilipolitazama jua, likawa linanilazimisha kuongeza kasi, sikutaka giza liingie na kunikuta vile tena.



    Kumbuka hapa nalazimisha haya yote kwa ajili ya kufungua kamba tu za viatu.



    Baada ya kamba za viatu ndio nianze utaratibu wa kamba za mikononi na kisha suala la chakula na kumtafuta jamaa yangu ndio ianze, haikuwa ni shughuli ndogo lakini ililazimika tu ifanyike.



    Jua likiwa ni jekundu sasa, nikafanikiwa kuvua kiatu kimoja, sox haikunisumbua sana, kwa utaratibu uleule wa tawi la mti, nikavua na sox na kusogea kule lilipo lile gamba la samaki.



    Sikutaka kujishughulisha na kiatu cha upande wa pili, nilijua kuwa nikiisha ifungua mikono yangu, basi ina maana nitavua kiatu kwa uzuri zaidi.



    Hivyo kwa kupitia vidole vyangu viwili vya miguuni, nikalinyanyua lile gamba la samaki kwa kulibana kwa kati ya vidole.



    Sasa ndio nikaanza kulifanyia kazi wazo langu nililolipata masaa kadhaa kabla ya kukwamishwa na viatu, muda huu sasa, ndio ilikuwa muafaka kwake kulikamilisha maana kama ni viatu tayari nilikua nimeisha vua.



    Nilienda nalo hadi kwenye gogo la mnazi lililokatwa na kuweka juuyake lile gamba nikitumia mguu wangu ule ule.



    Giza lilikuwa limeanza kuingia, nikainama na kuliuma huku nikilirekebisha kwa midomo na ulimi nikilielekeza kwenye zile kamba na kukata nikilitumia kama kisu.



    Mwanzo lilionyesha uhai, lakini halikuweza kumudu kukata zaidi ya kamba moja, nayo ilichukua kama robo saa nzima ndio nilifanikiwa, maana kamba walizotumia kunifunga ilikuwa ni shida tupu.



    Hakika nikakata tamaa kabisa, maana lilivunjika vunjika lote na kusambaa lile gamba, likasababisha nianze kusikia njaa kwa kasi na kiu ikarudi na nguvu mpya,



    Njaa ilinitesa zaidi maana sikuwa nimetia chochote tumboni kwa zaidi ya masaa 24 sasa.



    Nikaamua acha nipige magoti tu, hiyo ndio ilikuwa ni njia yangu ya kukaa kwa urahisi, nisubiri litakalotokea, kama kuna litakalokuja nikiwa nimekaa pale, basi acha tu lile nitapambana nalo, yaani nilipoteza kabisa matumaini ya kufungua kamba zile.



    Sikuwahi kuuona usiku mrefu katika maisha yangu kama ule, alfajiri ilipojitokeza tu, wazo linguine likajitokeza, lakini tayari nilikuwa ni dhaifu sana kimwili,



    Nikanyanyuka kurejea kule nilipoteremshiwa awali, nilifika lilipo begi nami nikiwa hoi kweli kweli na kuliegamia. Sikuwa na nguvu ya kufanya lolote.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilijibiringisha hadi kwenye maji ili nipate nguvu mpya wakati natoka, nikaliona gamba gumu kama lile la siku iliyopita, nikalibeba kwa meno hadi pale lilipo begi langu.



    Akili yangu hapo tayari ilikuwa imezinduka na kuwa mpya sasa, ila nilihisi kama zile kamba zimeanza kugandisha damu kwenye baadhi ya sehemu ya mwili wangu zilipopita kamba zile.



    Kwa kuwa ndani ya begi niliambiwa kuna kisu, akili ikanituma kulifungua tu begi na kwa kuwa sikuwa na funguo, ndio nikaona lile gamba linafaa kutumia.



    Nikatafuta sehemu zilizo na maungio na kufumua taratibu kwa kutumia lile gamba nikiwa begi nimelikandamiza kwenye mti.



    Ilinichukua kama saa nzima kufumua kama inchi mbili ambayo niliihitaji kwa ajili ya kupenyeza kidole change, kilipopita tu kidole gumba.



    Basi nikaanza kulitatua kwa kusaidiana na mguu mwingine ambao wenyewe ukawa unalizuia kwa kulikandamiza kwenye mti lile begi.







    Mabegi ya kijeshi yametengenezwa kwa ustadi wa hali ya juu, turubali likiwa limezunguka mzunguko wote wa juu huku nyuzi za kushonea viatu zikiwa ndio zilizotumika kwenye kulishikiza, linasababisha liwe ni gumu sana kwenye suala zima la kulifumua.

    Lakini kutokana na shida niliokuwa nayo nikafanikiwa kulitatua nikiwa taaban, ilinichukua zaidi ya saa nzima nyingine hapo hadi kukutana na vilivyomo ndani ya begi.

    Vikamwagika vyote, niliweza kuviona, tena basi kulikuwa na kidumu cha kama lita 1 hivi cha maji, kwa wakati huo hata sikushughulishwa nacho japo nilikitamani hasa.

    Nikajilaza kwanza palepale chini ili kuvuta nguvu mpya, kwani niliishiwa kabisa nguvu hadi pale nilipojiona kama mpya tena ndio nikanyanyuka na kuchukua kisu kwa meno na kuanza kukiseti ili nikate.

    Nikafanikiwa kukiseti vizuri na kuanza kukata, ilikuwa ni rahisi kwa zile kamba za juu ila kadri nilivyozidi kuzipunguza ndio ugumu ukawa unazidi kwa zile za chini. Maana kisu kikawa hakifiki tena, ikawa ni changamoto nyingine tena kwangu.

    Ila baadae nilifanikiwa kuivuta mikono kwa juu na ikasaidia kamba kulegea na kuichomoa, hapo sasa niliweza kujinyoosha na kushukuru Mungu kuwa nimekamilisha zoezi nikiwa hai, niliweza kuhisi muda ule kuwa ni alasiri.

    Tayari nilikuwa nimechoka vibaya sana, kiu ilinisumbua kupita kiasi, njaa kwa sasa haikuwa na nafasi kubwa ila nayo si haba, kitu cha kwanza kukifikiria ni maji, nikanyanyua kile kidumu nikiamini kitakuwa na maji.

    Bahati mbaya nikakikuta kitupu, nilikasirika na kukivugumiza kule, huku nikisonya na kujiuliza walikuwa na maana gani kuniwekea mle ndani ya begi, nikasimama nikiwa sijui ni wapi pa kuanzia.

    Hata mwelekeo sikuwa nao, pembeni nikaona mnazi, nikapanda huku nikijikongoja kutokana na kutokuwa na nguvu mwilini, nilifika juu na kuangusha madafu ma5 nikayafua kwa mawe yaliyochongoka na kunywa maji kisha nikayala. Hapo sasa nikawa mpya kabisa nikanyanyuka kujipima kama nipo sawasawa, nikaridhika.

    Wazo la kumtafuta mwenzangu sasa ndio likaniijia. Nikakusanya vile vyangu vya muhimu na kuviweka mfukoni, maana begi halikunifaa tena kwani lilikuwa lime chanika vibaya.

    Nikaanza kukata mapori, ghafla bila kutegemea. Simba huyu hapa, tena kwenye kisehemu chenye kibwawa kidogo, nikapanda mtini hata kabla hajaniona. Alipoondoka nikashuka na kuendelea na safri yangu nikiwa nachomwa na miba mguu mmoja.

    Uzalendo ukanishinda nikalazimika kurudia kiatu changu kule kwenye kile kijipango nilipokiacha jana. Nilipokaribia kule, nikasikia sauti ya risasi, hapo nikapata matumaini ya maisha eneo lile, ilinionyesha kuwa kuna mtu alie hai ndani ya msitu.

    Nami ili kumjulisha aliefanya kitendo kile kuwa kuna mtu mwingine alie hai kama yeye, nikatoa risasi na kuchuchumaa, nikaiweka kwenye majani makavu na kuwasha majani yale risasi ikiwa kati nimeisimamisha ikiangalia juu, mie nikasogea pembeni.

    Nikanyanyuka na kuendelea na safari mara tu ile ya kwangu ilipoitika, nikaanza kuifuatilia ile ya kwanza ilipotokea. Nikiwa nimepiga hatua chache tu, nikasikia nyingine, sasa niliweza hata kuuona moshi wake, nikatoka mbio kuelekea kule iliposikika bila kujali ni nani aliepiga.

    Nikajitokeza na kukuta ni mwenzangu akiwa amelala yupo hoi bin taaban. Kitu cha kwanza alichosema ni kiu, sikuwa na maji, lakini nilikumbuka kuyaona sehemu, sasa nitayabebaje? Hapo sasa sikupata jibu, ikawa ni kazi nyingine ya kufikiria nitamfikishiaje maji.

    Niliikumbuka ile chupa niliyoitupa kule ufukweni, hapo ndio nilianza kuiona thamani yake na kutambua sasa ni kwanini waliamua kuiweka. Nikagundua kuwa ni kwanini tangu awali wametuambia kwamba Jeshi ni nidhamu.

    Basi nilimsogelea jamaa na kumvua shati lake, hakujua namaanisha nini, nami wala sikutaka kumwambia, bali nikachukua kiatu changu kilichokuwa pembeni yake na kuondoka zangu kasi nikimuacha akiwa hoi.

    Nilifika kwenye kile kibwawa na kulifua kwanza shati lake kiushahidi, ilikuwa ni katika kupunguza tu jasho la mwilini, maana haingewezekana kulisafisha kabisa, kisha nikaliloweka na kutoka nalo mbio hadi pale alipo jamaa.

    Nilifika na kumkamulia mdomoni, alishukuru japo hayakumtosheleza, lakini kiu yake ilipungua sana. Akapata nguvu na kuniambia amefika pale zamani sana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alisema alikuwepo pale tangu usiku uliopita na kuona kiatu changu pale na kuamini nitarudi pale kuijia kiatu. Nikamuuliza kiko wapi chakula chetu, akaniambia kuwa hata nae hana chakula, nikamwambia kuwa niliambiwa yeye ana chakula chetu mie nae.

    Katakata akakanusha nami nikamuamini, wale jamaa waliondoka bila kuacha chochote lakini walijua kuwa sie tutakula tu, basi nikamgeukia na kumtazama. Kumbuka kuwa hadi muda ule tulikuwa hatujatambuana majina, tena huyu sio Yule ambae tulikuwa nae kambi moja.

    Huyu sasa alikuwa ni mwingine tofauti kabisa, Yule nilie toka nae kambi moja sikujua kapelekwa wapi. Nikamuuliza huyu jina lake ni nani, akasema anaitwa James nami nikamwambia jina la kwangu.

    Alikuwa ni muongeaji lakini alionekana kama kwamba ameathirika na mateso ya mafunzo yale ya ukomandoo, maana hata uso wake ulionyesha majuto. Nikamuuliza sasa ilikuwaje tangu jana usiku asinitafute ama kufanya kama vile alivyofanya leo?









    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog