Search This Blog

Friday, October 28, 2022

AHADI YA MAISHA - 3

 

     





    Simulizi : Ahadi Ya Maisha

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Baada ya kumteka Frank waliongaza gari lao hadi eneo lililokuwa na miti mingi pamoja na vichaka katika barabara iliyoelekea wilaya ya Mkuranga. Jambazi aliyeendesha gari hilo alilipeleka mpaka kwenye vichaka vilivyokuwa umbali wa nusu kilometa kutoka katika barabara hiyo kuu. Hatimaye alisimamisha gari na Henry alionekana akiwa na hasira kupindukia dhidi ya Frank kwani baada ya kumshusha alianza kwa kumshushia kipigo kwa mateke mfululizo. Kijana huyo alipiga kelele za maumivu hasa kutokana na majeraha aliyopigwa na George kwa nondo ambayo yalikuwa yamepona siku chache zilizokuwa zimepita.

    Jambazi aliyekuwa ameongozana na Henry alikuwa eneo la mbele la gari hilo na alionekana kama vile alikuwa akivuta msokoto uliokuwa kama vile wa bangi. Wakati huo alikuwa akijiandaa tayari kwa kutimiza zoezi zima aliloajiriwa na mteja wake bwana Henry. Tayari alikuwa amemhakikishia kuwa ni lazima Frank angetoa siri zote ambazo Henry alikuwa akizihitaji. Muda wote wakati akiendelea na zoezi lake hilo la kuvuta msokoto huo, Henry bado alikuwa akiendeleza kipigo dhidi ya Frank. Baada ya dakika kadhaa jambazi huo alimaliza zoezi lake la kuvuta msokoto huo na macho yake yaligeuka ghafla na kuwa na rangi nyekundu kwa kiasi kikubwa. Alitembea mpaka eneo ambalo Henry alikuwa akiendelea kumpiga Frank mara baada ya kufika, alimweleza akae kando akihitaji kutimiza zoezi hilo.

    Alimshushia kipigo cha nguvu kwa dakika kama tatu kabla ya kutulia kidogo, alionekana aligundua kitu toka kwa mtu huyo aliyempiga ambaye alitoa kelele za yowe kupindukia. “Henry nipe hiyo Bastola….” alisikika jambazi huyo aliyekuwa amejaa kifua akimwomba Henry bastola aliyokuwa nayo. Alitekeleza kwa kumpa silaha hiyo wakati huo bado alikuwa na hasira kali dhidi ya Frank. Baada ya kuipokea jambazi huyo alianza kwa kuikoki akiiweka tayari kwa kuua, mara baada ya zoezi hilo aliinyanyua na kuielekeza katika paji la uso wa Henry. Jambo hilo lilimshtua kijana huyo kwani lilikuwa tofauti na makubaliano yao na jambazi huyo. Frank alikuwa bado akipiga kelele za kilio baada ya kupigwa kwa muda mrefu lakini naye ghafla alituulia akionekana kugundua jambo.

    “kijana ulitaka nimdhuru bosi wangu, sikutambua kama ni yeye nisinge kubali kazi hii” alisikika jambazi huyo kwa msisitizo wa hali ya juu na alionesha tayari alikuwa upande wa Frank. “wewe huna nidhamu kabisa umesababisha tumemteka mtoto wa waziri eeh!” alisisitiza jambazi huyo ambaye alitokwa na kijasho chembamba kwenye paji lake la uso.

    Frank alikurupuka na kumvamia Henry kabla ya kuanguaka wote chini na alianza kumpiga ngumi mfululizo usoni. Alipata msaada wa ghafla toka kwa mtu aliyeongozana na adui yake. Alimtambua jambazi huyo kwani alimsaidia katika zoezi alilokuwa amelifanya miezi ya nyuma la kumpiga picha za utupu George akiwa hana fahamu pamoja na mwanamke ambaye pia alipewa kazi hiyo kwa malipo. Baada ya kumpiga kwa muda mfupi Frank alihitaji kumtambua zaidi Henry, aliamini alikuwa na undugu wa karibu na George jambo lililopelekea amteke. Hata hivyo sura yake alihisi aliwahi kuiona sehemu lakini kumbukumbu zake zilikuwa mbali kutambua mahali walipowahi kukutana.

    “wewe mshenzi umetumwa na familia ya mzee Innocent si ndio?” aliuliza Frank kwa ukali wakati mishipa ya hasira ikiwa imetawala paji la uso wake.

    Swali hilo hakujibiwa na Henry ambaye alikuwa akitetemeka kwa hofu huku jambazi aliyempa kazi akiwa pembeni na bastola aliyokuwa amemwonyeshea. Hakuna jambo jingine ambalo liliweza kuongelewa wakati huo kutokana na mwonekano mzima wa eneo hilo zaidi ya shari. Frank aliiomba bastola aliyokuwa ameishika yule jambazi kabla ya kuanza kusikika “hata usipojibu najua umetumwa na mzee Innocent, Hamtuwezi mtandao mkubwa huu, huwezi kujua jambo mshenzi wewe! Hivi unaelewa hata jambo dogo tulilofanya kumdhalilisha George magazetini?” aliongea Frank kwa madaha kauli iliyompandisha hasira Henry ambaye alikurupuka pasipo kujali bastola aliyokuwa nayo mkononi akiwa amemwonyeshea. Alimvamia Frank akiwa amempiga kichwa usawa wa tumboni na wote waliangaka chini kabla ya mlio wa risasi uliosikika wakiwa wote chini huku Henry akiwa juu ya Frank. Damu iliruka na kutoka kwa kasi mgongoni mwa Henry aliyepigwa na risasi hiyo pasipo na ridhaa ya Frank

    Baada ya sekunde kadhaa Frank alikuwa amelowa damu iliyomtoka kwa kasi Henry, hakuamini jambo ambalo tayari lilikuwa limetokea alianza kumuinua taratibu kijana huyo akimtoa kifuani kwake alipokuwa amemlalia. Mara baada ya kumaliza zoezi hilo alishtushwa na gari la askari lililokuwa likielekea eneo lile kwa kasi ambalo liliishia kuegeshwa kando na lile la awali walilofika nalo wakina Henry. Jambo lililomshangaza Frank lilihusiana na jambazi aliyekuwepo eneo hilo la tukio ambaye hakumwona tena eneo hilo. Alikuwapo peke yake na Henry aliyerusha mikono na miguu kuonesha alikuwa katika hatua za mwisho ili afariki. Mara baada ya askari hao kushuka kwenye gari lao walimshuhudia Frank akiwa ameua kwani hata bastola aliyoitumia alikuwa nayo mkononi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa akitetemeka na wakati huo kijana Henry alikuwa ametulia katika hali iliyoashiria alikuwa amekata roho tayari. Askari hao hawakuonesha hali yoyote ya kumweka chini ya ulinzi kwani walimtambua kuwa alikuwa mtoto wa waziri na wakati huo walikuwa katika zoezi la kumtafuta baada ya kutekwa kwake. Askari mmoja kati ya wanne waliokuwapo aliusogelea mwili wa Henry akiwa na lengo la kuhakikisha kama kweli alikuwa amekufa, aliweka mkono kifuani kwake kwa sekunde kadhaa. Askari hao pamoja na Frank mwenyewe walikuwa kimya wakisubiri angewajibu nini. Mara baada ya kunyanyuka askari huyo alitikisa kichwa akiashiria kijana huyo alikuwa amefariki.

    Frank alilia akiwa haamini kama alikuwa amefanikisha zoezi la kuua. Siku zote alikuwa na mipango ya kufanya mambo tofauti lakini siyo kuua kama ilivyokuwa imetokea. Hasira zake siku zote zilikuwa juu ya George ambaye ilikuwa ni rahisi kwake kumuua kutokana na ugomvi waliokuwa nao kwa wakati huo. Askari mmoja kati yao hao wanne aliyeonekana alikuwa kiongozi wao alimwambia anyamaze kulia haraka iwezekanavyo, jambo alilolitekeleza. Askari huyo alichukua simu yake na kuonekana alitaka kumpigia mtu. Wakati huo Frank alitetemeka akiamini kundi la askari liliitwa eneo hilo na baada muda mfupi aliamini angekuwa chini ya ulinzi mkali.

    “haloo mheshimiwa waziri mtoto wao tumemwona ila amefanya jambo moja hatari sana kwa maisha yake,sasa naomba uje maeneo ya wilaya ya Mkulanga ili tuone tutafanya nini…! Tafadhali uje peke yako” alisikika askari huyo mara baada ya simu ya waziri wa nchi mzee Joseph kupokelewa. Kiongozi huyo aliyeonekana kuchanganyikiwa aliahidi kufika eneo la tukio ndani ya muda mfupi. Askari hao walibaki eneo la tukio wakiwa kimya wakimsubiri waziri aje kuamua juu ya tukio hilo, wakiwa na vyeo vidogo katika jeshi la polisi walihofia usalama wao endapo wangeitoa siri hiyo kwa raia pasipo waziri kuamua. Waliamini jambo hilo lingekuwa hatari sana kwa maisha yao huku wakielewa waziri huyo asingekuwa tayari mwanaye afikishwe katika vyombo vya sheria.

    Hatimaye waziri huyo aliwasili akiwa peke yake kama alivyokuwa ameagizwa ikiwa ni nyakati za saa mbili usiku. Bila kupoteza muda alijongea eneo la tukio na kuelezwa mwanaye alikuwa ameua, mzee Joseph hakuamini jambo hilo mpaka walipofunua maiti ya Henry iliyokuwa imefunikwa na turubai la askari hao. Baada ya zoezi hilo waziri aliamini kuwa ni kweli mwanaye Frank alikuwa ameua. Akiwa amechanganyikiwa kwa kiasi fulani, mwanaye alikuwa akimwomba msamaha huku akiamini yeye pekee angemsaidia. “usijali jambo dogo hilo, nimekutana na mambo haya mara nyingi katika maisha yangu ya siasa, hakuna atakaye tugusa” alisikika waziri huyo kwa ujasiri.

    Jambo alilolitaka toka kwa askari hao lilihusiana na siri juu ya tukio hilo aliwaahidi kiasi cha shilingi milioni nane kila mmoja. Kitu kikubwa alichohitaji ni kutunzwa kwa siri hiyo, akionesha kuwajali askari hao ambao kwa vyovyote walikuwa tayari kumsikiliza mkubwa huyo wa nchi aliwaeleza kuwa angehakikisha wanapandishwa vyeo ndani ya wiki mbili. Askari hao wote walitii na kuapa kutotoa siri hiyo kwa mtu yeyote, baada ya zoezi hilo mzee Joseph alihitaji kujua juu ya tukio zima lililopelekea kifo cha Henry. Wakati huo tayari walikuwa wameingiwa na hisia kuwa kijana huyo alikuwa ni ndugu yake mzee Innocent.







    Ghafla mlio wa simu ya mkononi ulianza kuita eneo hilo na baada ya kutulia kwao vizuri waligundua sauti hiyo ilitoka eneo alilolazwa Henry akiwa amefariki. Mzee Joseph aliusogelea mwili huo na kuitoa simu hiyo ya mkononi iliyokuwa ikiita katika mfuko wa suruali wa maiti hiyo. Aliona jina la mzee Innocent kama mpigaji bila kupoteza muda aliikata simu hiyo kabla ya kuizima kabisa. Tayari aliamini mtu huyo aliyekuwa amefariki alikuwa ni ndugu yake na mzee Innocent lakini bado aliona jambo hilo lilikuwa dogo. Hakushangazwa na kifo hicho kwa vile aliamini mtu huyo alikuwa ametumwa na mzee Innocent na alihisi wakati huo alikuwa akihitaji kujua mafanikio aliyoyapata baada ya kumteka Frank.

    Frank alianza kuelezea tukio hilo lilivyokuwa kama alivyohitajika kufanya. Baada ya kupata maelezo ya tukio zima waziri huyo aliwaeleza kuwa mtu ambaye awali alikuwapo eneo la tukio na Henry ambaye pia alikimbia ilikuwa ni lazima akamatwe. Waziri huyo alidai mtu huyo ndiye aliyepaswa kuchukua adhabu ya kuhusika na mauaji dhidi ya Henry, askari hao walielezwa siku iliyofuata mtu huyo akamatwe. Hiyo iliwezeakana kwa vile Frank aliyemtaja mtu huyo kuwa ni jambazi pia, alidai alikuwa anafahamu eneo alilokuwa anaishi. Baada ya kuelewana vizuri dhidi ya mipango yao waliondoa magari yao kwa kasi wakiliacha eneo hilo. Walikuwa wameliacha pia gari la Henry aina ya Land Cruiser ambalo alilitumia kumteka Frank akiwa na jambazi lake kabla kifo chake kilichotokea porini hapo. Waliendesha magari yao kwa kasi huku askari waliokuwapo eneo la tukio wakiwa kimya pasipo kuzungumza kitu, waliamini kila jambo lililoelezwa na waziri lilikuwa lazima litekelezwe kutokana na heshima na uwezo aliokuwa nao katika nchi.

    * * * *

    Tabangu lilikuwa jina la jambazi aliyetoroka eneo la tukio la mauaji dhidi ya Henry, mara baada ya kugundua alifahamiana zaidi na Frank aliyekuwa mtoto wa waziri aliamua kumsaliti mteja wake Henry. Lakini sekunde kadhaa kabla ya tukio la kifo cha Henry kutokea alikuwa amelishuhudia gari la polisi lililoelekea kwa kasi eneo walilokuwapo. Alijaribu kumwita Frank lakini alikuwa wakikurupushana na Henry jambo lililomfanya aamue kuanza kukimbia peke yake akitokomea vichakani. Baada ya sekunde kadhaa wakati akiendelea kukimbia alisikia sauti ya risasi ikitoka eneo walilokuwapo Frank na Henry. Hakuwaza hata kidogo kurudi eneo hilo zaidi ya kuongeza kasi ya kukimbia. Akilini alikuwa ameingiwa na hisia kuwa mmoja wao kati ya Henry na Frank alikuwa amedhuriwa na risasi hiyo.

    Tabangu alikimbia akipita vichakani umbali wa kilometa kadhaa kabla ya kuelekea barabara kuu akiwa na lengo la kupata msaada wa kusafiri na gari lililotoka katika wilaya hiyo ya Mkuranga na hatimaye kurudi Dar es salaam. Hakuwa na hofu hata kidogo kwani aliamini hakuhusika na jambo lolote ambalo lingetokea eneo la tukio alilowaacha Frank na Henry. Bado aliamini Frank hangeweza kumsaliti kwani alikuwa amemwokoa na kifo baada ya Henry kuwa na hasira za wazi za kufanikisha jambo hilo. Hakutumia muda kuwapo barabarani hapo kwani alipata msaada wa gari moja la mizigo lililokuwa likirudi jijini Dar es salaam.

    Majira ya saa mbili usiku alikuwa amepumzika katika kitanda ndani ya chumba chake alichopanga maeneo ya Tabata huku akiwa na mawazo ya kuendelea na shughuli zake siku iliyofuata. Jambo ambalo bado kidogo lilimpa shaka lilihusiana na mlio wa risasi aliousikia wakati akikimbia eneo alilokuwapo Henry na Frank. Alikuwa na hisia akiamini huenda risasi hiyo alimdhuru mmoja wao na hatimaye kufariki, alijikuta akipuuza mawazo yake hayo ya kifo kupitia Bastola hiyo iliyokuwa yake. Hatimaye majira ya saa tatu usiku alikuwa katika usingizi mzito kabla ya kushtuka majira ya saa kumi na moja alfajiri baada ya kusikia mlango wa chumba chake ukigongwa. “nani wewe muda huu?” aliuliza Tabangu wakati akiendelea kuvaa suruali yake ili ajongee kuufungua mlango huo. “mimi Frank, mtoto wa mkubwa……” ilisikika sauti hiyo kutoka nje. Tabangu alitabasamu kidogo baada ya kugunndua mtu huyo alikuwa Frank Joseph, mtoto wa waziri na walikuwa na mazoea ya kumwita mtoto wa mkubwa. Tabasamu lake lilitokana na ukweli aliotaka kujua juu ya mlio wa risasi uliosikika wakati akikimbia akiwa amemwacha na Henry.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “dah! Bora umekuja mtu wangu, naamini nita….” Tabangu alikuwa akiongea sentensi hiyo huku akifungua mlango lakini hakuimalizia baada ya kuona taswira ya kutisha nje ya chumba chake. Kulikuwa na askari wanne waliokuwa wameongozana na Frank, kwa haraka akili yake ilimtuma na kuamini tayari kulikuwa na hatari. Kabla hajaongea jambo lolote alisikia sauti ya askari mmoja iliyotoka kwa mkwaruzo ambayo ilimdhihilishia hatari hiyo.

    “kijana ulidhani kuua ni jambo rahisi siyo, sasa tumekupata eti Frank huyu ndiye muuaji?” alongea askari huyo na kumuuliza swali Frank aliyejibu kwa kutikisa kichwa akiashiria Tabangu alikuwa muuaji. “sasa kijana uko chini ya ulinzi na mikono juu” alisikika askari mwingine na kumfanya Tabangu achanganyikiwe ghafla. Alipiga kelele akipinga mambo aliyoelezwa kuwa alikuwa ameuwa lakini hakuna askari kati yao aliyemsikiliza. Alijaribu kumkalipia Frank afute maelezo yake ya yeye kuhusika na mauaji lakini hakufanya hivyo. Mara baada ya kufungwa pingu aliondoka na gari la askari hao wakiwa wanaelekea kituo cha polisi huku njiani akiendelea kulalamika akidai hakuhusika na mauaji hayo.

    * * * *

    Mzee Innocent ambaye muda wote alikuwa ni mtu mwenye mawazo kufuatia adhabu ya mwanaye George, alishtushwa na kuitwa kwake kituo cha polisi ambako alielezwa alihisiwa kuhusika na kutekwa kwa mtoto wa waziri. Mzee huyo alitoa utetezi wake dhidi ya jambo hilo na kukana maelezo hayo yaliyotolewa na askari hao. Baada ya kuhojiwa kwa muda mrefu alielezwa afike tena kituo cha polisi siku iliyofuata kwa ajili ya kuhojiwa tena. Aliondoka kituoni hapo akiwa ametii agizo hilo lakini akiwa amechukizwa na mwenendo mzima wa tabia za waziri wa nchi mzee Joseph. Alikuwa akimchukia mzee huyo huku akiamini alichangia kuharibu maisha ya mwanaye aliyekuwapo gereza la Ukonga akitumukia kifungo cha miezi sita.

    Siku hiyo wakati wa usiku akiwa nyumbani kwake aliamua kumpigia simu mdogo wake Henry, lengo kubwa lilikuwa ni kumweleza asimamie kazi kadhaa alizopaswa kusimamia siku iliyofuata. Hiyo yote ilitokana na agizo alilopewa na askari la kurudi kituo cha polisi siku iliyofuata hivyo aliamini hangeweza kusimamia kazi hizo. Alimpigia kwa mara ya kwanza simu yake iliita kwa muda mfupi kabla ya kukatwa, aliamua kumpigia kwa mara ya pili ilikuwa haipatikani. Baada ya kujaribu kwa mara kadhaa bila mafanikio aliamua kusubiri kumweleza jambo hilo siku iliyofuata akiamini huenda alikuwa eneo baya na kushindwa kuwasiliana naye.

    Siku iliyofuata mzee Innocent baada ya kuamka alijaribu kumpigia Henry lakini bado simu yake ilikuwa haipatikani. Jambo hilo lilianza kumpa hofu kiasi fulani, hatimaye aliondoka nyumbani kwake akielekea kituo cha polisi kama alivyokuwa ameelezwa. Mara baada ya kufika kituoni hapo askari hao walimweleza aendelee na shughuli zake wakidai Frank alikuwa amepatikana. Walionekana wakimwomba radhi dhidi ya imani zao za kumhusisha na kutekwa kwa Frank lakini walihitaji atambue kuwa lilikuwa jukumu lao kufanya hivyo. Mzee Innocent hakuwa na makuu aliondoka kituoni hapo akiwa amewaelewa askari waliokuwapo. Aliamua kuelekea maeneo ya Posta ambako kulikuwapo na ofisi yake, alipofika ofisini hapo akiwa anatarajia kumwona Henry haikuwa hivyo jambo lililoanza kumpa hofu zaidi kwani hata wafanyakazi wake hawakuwa na taarifa yeyote dhidi yake.

    Majira ya saa nne asubuhi wakati akiwa anaendelea na shughuli zake za kiofisi simu yake iliita kwa namba ambayo ilikuwa ya meneja wa kampuni yake iliyohusika na usafirishaji. Bila kupoteza muda alipokea simu na kuelezwa taarifa zilizomchanganya, aliambiwa aelekee hospitali kuu ya taifa ya Muhimbili kwani kulikuwa na tatizo lililomhusu. Akiwa na mashaka na mwanaye aliyekuwa jela akiamini huenda alikuwa amefariki aliondoka eneo hilo la ofisini akiwa na dereva wake. Kichwani alitawaliwa na mawazo ya George, ingawaje mara nyingi alimtembelea katika gereza la Ukonga alihisi lolote liliwezekana kumtokea. Zaidi alimkumbuka kwa jinsi alivyokuwa amedhoofu kiafya na kuamini iliwezekana akawa hospitalini hapo.

    Mara baada ya kufika hospitalini hapo ambapo alipokelewa na marafiki zake kadhaa sambamba na meneja aliyempigia simu alielezwa ajikaze wakati walivyoanza kuelekea eneo la mochuari. Miguu yake ilitetemeka nakumfanya asitembee vizuri aliwaza vitu vingi kwa muda mfupi pasipo kuchagua kilichokuwa sahihi. Mara baada ya kuingia katika chumba hicho na kuwa na utulivu wa muda mfupi, mzee huyo alianza kulia baada ya kumwona mdogo wake Henry akiwa amefariki. Miguu yake iliishiwa nguvu na kumfanya aanguke kabla ya kuondolewa eneo hilo, hakuamini macho yake juu ya tukio hilo alilokuwa amelishuhudia hata kidogo. Bado alihisi mdogo wake huyo alikuwa hai lakini haikuwa hivyo kwani kila dakika iliyoenda iliendelea kuthibitisha ukweli wa kifo hicho.

    Baada ya wiki moja tayari Henry alikuwa amezikwa wilayani Bagamoyo ambako Henry alikulia akiwa na kaka yake mzee Innocent. Walikuwa na makazi ya familia yao ingawaje wazazi wao walikuwa wameshafariki. Mzee Innocent aliyekuwa na uchungu juu ya kifo cha mdogo wake huyo alishangazwa na kushiriki kwa Waziri wa nchi mzee Joseph akiwa na mwanaye katika msiba huo. Hakutambua jambo haswa lililopelekea kuhudhulia kwao msiba huo kwa vile alitambua walikuwa maadui wake. Mara baada ya msiba huo alihakikishiwa na waziri huyo kuwa mtu aliyekuwa anahusishwa na mauaji hayo angechukuliwa hatua za kisheria.

    Hatimaye kesi dhidi ya kijana huyo aliyejulikana kwa jina la Tabangu ilianza huku ikiendeshwa kwa ubabe mbali na nia ya kijana huyo ya kutaka kujitetea, hakupewa nafasi hiyo. Hatma yake ilipatikana ndani ya wiki moja baada ya kusomewa kifungo cha maisha, Tabangu alilia kwa uchungu akikana kuhusika na mauaji hayo lakini hakusikilizwa hata kidogo. Kuna wakati mara baada ya hukumu alionekana alitaka kulitaja jina la mtu aliyefanya mauaji dhidi ya Henry lakini alipigwa mpaka akapoteza fahamu kabla ya kufanya hivyo.Alizinduka tayari akiwa katika gereza la Ukonga akiwa katika kuitumikia adhabu yake ya kifungo cha maisha. Tabangu aliia kwa uchungu huku akijilaumu dhidi la zoezi lake la kufahamiana na Frank aliyekuwa mtoto wa waziri. Alikuwa haelewi hatma ya maisha yake baada ya kusomewa kesi akiwa anahusishwa na mauaji ambayo hakuyafanya.

    Mzee Innocent alimshukuru waziri wa nchi mzee Joseph kwa ushirikiano wake katika kesi ya mtu aliyehusishwa na mauaji ya Henry kwani kiongozi huyo alikuwapo mahakamani siku ya kesi. Jambo alilolishangaa lilihusiana na upendo wa ghafla na msaada alioupokea kutoka kwa kiongozi huyo. Kuna wakati alihisi kuna jambo liliendelea lakini alikuwa hana uthibitisho juu ya hisia zake hizo. Aliamua kujifanya mtulivu akiamini huenda kijana Tabangu alihusika na mauaji hayo. Mbali na uchungu aliokuwa nao dhidi ya kifo cha mdogo wake aliamini huenda waziri huyo alikuwa amerudiwa na huruma kuhusiana na familia yake. Jambo hilo lilimfanya aamini kuwa angeweza kupata msaada kutoka kwa waziri huyo ili mwanaye apunguziwe adhabu ya miezi sita ya kuwapo jela aliyosomewa

    Winnie na Frank walikuwapo katika maandalizi ya mwisho kabisa tayari kwa harusi yao iliyobakiwa na siku sita. Jambo lililomshangaza msichana huyo alikuwa akihisi harusi hiyo haingefungwa, muda wote alikuwa mnyonge na alionekana kuwa ni mtu aliyejutia uamuzi wa kuingia katika ndoa na Frank. Hakufikiria kuikana harusi hiyo lakini alikuwa akihisi alikuwa akiingia katika mtihani mgumu. Moyoni alikuwa akiumia dhidi ya adhabu ya kuwapo jela kwa muda ya miezi sita aliyoipata mchumba wake wa zamani. Alijikuta akiingiwa na huruma juu ya George na kuona ni bora angekuwa huru akifanya mambo yake.

    Winnie alikuwa akitatizwa na ndoto alizokuwa akiziota usiku kwani mara kadhaa akiwa ndotoni aliaswa na George kutoingia katika ndoa aliyotarajia kuifunga na Frank. Mara nyingine aliota George akimwambia kuwa mume wake mtarajiwa alikuwa muuaji

    na asijaribu kumkubali. Alikuwa akipuuzia ndoto hizo akiamini zilitokana na uadui uliokwisha jengeka kati ya George na Frank. Kadri siku zilivyosogea ndivyo ndoto hizo zilivyomzidia jambo lililomfanya asielewe maana yake. Hatimaye akiwa amebakiwa na siku tatu ili harusi yake ifungwe aliamua kuchukua uamuzi wa kumtembelea George katika gereza la Ukonga kabla ya harusi hiyo.

    * * * *

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    * * * *

    George alikuwa amekonda kwa kiasi kikubwa kutokana na hali nzima ya ugumu alioupata akiwa gerezani. Alikuwa akipigwa kila siku nyakati za usiku na watu waliomvamia eneo alilolala ambao walifanya hivyo wakati kukiwa na giza. Kwa ujumla hakuelewa hatma ya maisha yake, watu hao walikuwa wakimpiga siku zote walikuwa wakiondoka kwa kumwambia kuwa lazima afie gerezani hapo. Jambo hilo lilimchanganya sana na kumpa hofu kila ilipofika nyakati za jioni akiamini lazima angepigwa. Watu hao waliompiga ambao hakuwatambua vizuri walikuwa wanadai walipewa kazi hiyo na bosi wao. Alikuwa akiamini kuwa walikuwa wametumwa na Frank pamoja na Winnie, kwa muda mfupi tu alikuwa na makovu kila eneo la mwili wake jambo lililowatoa machozi wazazi wake pindi walivyomtembelea.

    Kutokana na kukonda kwake kwa kiasi kikubwa sura yake nayo ilionekana kama vile alikuwa mzee huku akikumbana na adhabu nyingi toka kwa manyapara kadhaa wa gereza hilo. Wafungwa wenzie kadhaa walipenda kumwonea kwa vile walimtambua alikuwa mtoto wa tajiri. Siku zote akiwa gerezani hapo watu walimcheka kwa kumshangaa baba yake kwa kushindwa kumtoa gerezani hapo hata kwa rushwa kutokana na uwezo wake wa kifedha aliokuwa nao. Wapo waliokuwa wakimtania kuwa alikuwapo gerezani hapo kutokana na masharti ya kibiashara ya baba yake yaliyohitaji afie gerezani hapo. Alikuwa hajali kwa vile hata saikolojia yake ilikuwa imeathirika kwa kiasi kikubwa akiwa ni mtu ambaye hakuwa na rafiki gerezani hapo. Alikuwa akiongea zaidi na wazazi wake na ndugu kadhaa waliofika kumtazama gerezani hapo.

    Baada ya mwezi mmoja wa kuwapo gerezani hapo tayari akilini alitambua kuwa Frank na Winnie walikuwa wamefunga harusi. Hiyo yote ilitokana na kumbukumbu zake kwani alivyompiga Frank na nondo ulikuwa ni wakati ambao watu hao walikuwa katika mafundisho ya ndoa. Jambo la harusi hiyo lililomkaa kichwani lilimuumiza sana ila alijitahidi kuifanya nafsi yake ikubali kuwa Winnie alikuwa ameolewa. Hakuthubutu kuwauliza wazazi wake mara kadhaa walivyomtembelea juu ya harusi hiyo akiamini angeumia zaidi moyoni. Ikiwa siku hiyo ya Ijumaa akiwa ametimiza mwezi huo mmoja wa kutumikia adhabu yake alianza kuingiwa na hofu baada ya kugundua kuwa kulikuwa na mfungwa aliyemfuatilia na kumchunguza sana.

    Mfungwa huyo aliyejengeka kimwili kwa kuwa na misuli iliyoashiria alikuwa mbabe alimtisha sana George. Hiyo yote ilitokana na zoezi la kupigwa ambalo bado lilikuwa likiendelea dhidi yake. Alihisi mtu huyo ambaye awali hakuwahi kumwona gerezani hapo alikuwa na lengo la kumpiga pia. Zaidi alizidi kuchanganyikiwa baada ya kugundua alikuwa amepangiwa kulala karibu na chumba chake alicholala na wenzie ambao siku zote walikuwa hawamsaidii wakati akipigwa. George alikuwa ameigiwa na hofu juu ya mtu huyo baada ya kuelewa suala zima la watu kutopenda kumsaidia wakati akipigwa wakihofia kujiingiza katika matatizo.

    Majira ya saa nane usiku kundi la wafungwa kadhaa walifika eneo alilolala na kuanza kumpiga kama ilivyokuwa kawaida yao, George alipiga kelele juu ya kipigo alikichopata lakini hakuna hata mfungwa mmoja aliyethubutu kumsaidia kama ilivyokuwa kawaida yao. Wafungwa hao waliokuwa wengi siku hiyo walimfanya alie akipiga kelele kuyataja majina ya Frank na Winnie akiamini watu hao ndio waliwatuma. “nyie mbwa mwachieni huyo haraka kabla sijawaangamiza” ghafla ilisikika sauti hiyo kwa nguvu ikionekana ilikuwa ya mtu aliyekuwa mbabe. Hawakuweza kumwona kwani ilisikika kutoka gizani katika eneo hilo ambalo halikuwa na mwanga hata kidogo. Sauti hiyo iliwafanya wafungwa waliokuwa wakimpiga watulie wakimhofia mtu huyo aliyewaamru.

    “we nani? unatuzingua… eeh ,unadhani sisi watoto wa mama” mmoja wao alitoa kauli hiyo ya kejeli baada ya sekunde kadhaa, wakati akipaza sauti hiyo ya juu alikuwa akitembea kuelekea eneo ambalo kauli ya kuwataka waache kumpiga George ilisikika. Ghafla alishtushwa na ngumi yenye uzito wa ajabu iliyotua usoni mwake wakati akiwa amekaribia eneo hilo lenye giza, ngumi ambayo ilipelekea aanguke mpaka chini. “mama weeee! nakufa uwiii…”alipiga kelele mfungwa huyo ambaye kabla ya kutulia kwake vizuri aliongezewa teke zito kifuani. Mtu huyo ambaye hakumwona vizuri kutokana na giza aliendeleza kumpiga kwa mateke eneo alilokuwa ameanguka.

    Jambo hilo liliwafanya wafungwa wengine waliokuwa wakimpiga George watoke wakikimbia kwa kasi eneo hilo wakihofia usalama wao. Hiyo yote ilitokana na kelele ambazo mfungwa mwenzao alikuwa akizipiga kufuatia kipigo alichoendelea kukipata.

    Baada ya dakika kadhaa mfungwa aliyekuwa akipigwa na mtu ambaye hakumtambua kama alikuwa askari au mfugwa mwenzie, alikuwa anavuja damu sehemu kadhaa za mwili wake. Alikuwa akitokwa na damu kwa kasi katika paji lake la uso ambao alipigwa ngumi na mtu huyo. “sasa we mshenzi, potea kabla sijakumaliza kabisa” alisikika tena mtu huyo kauli ambayo mfungwa aliyekuwa akipigwa alionekana hakuielewa kutokana na kipigo alichokuwa amepata kwani hakuondoka. Mtu huyo alirudia tena kauli hiyo na mfungwa huyo alitoka akikimbia huku akiendelea kulia kwa maumivu aliyoyapata.

    George naye alikuwa akilia kwa sauti ya chini baada ya kuwa amepigwa na wafungwa ambao wakati huo walikuwa wameshaondoka kufuatia msaada wa mtu ambaye hakumwona kutokana na giza. Hata baada ya wafungwa hao kuondoka mtu huyo alikuwa kimya na hakusema kitu, jambo lililoanza kumpa hisia kuwa huenda mtu huyo alipanga kumuua usiku huo. “George Innocent……” ilisikika sauti ya mtu huyo baada ya takribani dakika moja. “naaam!... naaam! nakusikia…. .” alijibu George huku sauti yake ikikatika katika na alionekana alikuwa na hofu dhidi ya mtu huyo. Alisikia sauti ya kishindo cha mtu huyo akitembea na alienda kukaa pembeni na eneo alilokaa George na mara baada ya kuhakikisha alikuwa eneo husika alimshika bega. “usihofu mtu wangu, naitwa Tabangu nina kifungo cha maisha hapa nitakusaidia, hawatakuonea tena” aliskika mtu huyo.

    Hapo ndipo George alipata rafiki na siku iliyofuata akiwa karibu na Tabangu aliweza kuongea naye mambo tofauti akiwa amemwambia alikuwa amemuua mtu. Hakupata maelezo zaidi juu ya mkasa huo lakini aliamini angeupata kwa vile Tabangu alikuwapo. Wafungwa kadhaa walikuwa wakimwangalia na walionekana kugundua jambo kutokana na vile Tabangu alivyoonekana mbabe. Siku hiyo George alilala kwa amani pasipo kusumbuliwa hata Tabangu alihamia katika chumba hicho alichokuwa akilala George gerezani hapo. Katika siku mbili tu alizokuwa na Tabangu alikuwa akiishi kwa amani kwani kwa muda mfupi wafungwa waligundua kuwa hakuwa mtu wa kuchezewa. George alihisi Tabangu alikuwa na mambo makubwa aliyokutana nayo ila hakuwa tayari kumweleza wakati huo akimwambia muda ungefika angeyafahamu.

    Tabangu kama alivyokuwa amesomewa kesi ya kwenda jela kifungo cha maisha kwa kesi aliyogandamizwa kwani ilimhusu mtoto wa waziri, Frank Joseph alimwonea huruma sana George gerezani hapo. Wakati akiamini lazima angefia akiwa eneo hilo kutokana na mkono wa waziri bado alikuwa na siri kadhaa zilizohusu uovu wa Frank. Kwani alihusika katika tukio ambalo George alipigwa picha za utupu baada ya kupoteza fahamu. Zaidi alikuwapo eneo la tukio ambapo Henry, baba yake mdogo George aliuawa na Frank Joseph. Katika matukio yote hayo alihusika katika mchango wa kuiumiza familia ya mzee Innocent, jambo lililomfanya aogope kutoa siri alizoshiriki kumsaidia Frank. Kikubwa zaidi George alikuwa hajui juu ya kifo cha Henry kwa vile alimshuhudia akilalamika kuwa baba yake mdogo huyo aliacha kumtembelea. Aliamini wazazi wake hawakumweleza wakihofia kumchanganya zaidi akiwa gerezani hapo. Hivyo Tabangu aliamua kutulia akiwaza kuutoa ukweli huo siku moja ikimbidi kufanya hivyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku mbili kabla ya harusi yake, Frank alionekana akiwa maeneo ya gereza la Ukonga. Lengo lake lilikuwa kwenda kuwaulizia wafungwa kadhaa waliokuwapo gerezani hapo kwani alikuwa amewapa kazi ya kufanikisha mauaji dhidi ya mfungwa mwenzao, George. Jambo lililomuudhi kadri siku zilivyoenda hakusikia kifo cha kijana huyo aliyemchukia sana. Kitu kilichoanza kumwumiza sana kichwa ni vile Tabangu aliyekuwa ameadhibiwa kwa kesi ya mauaji aliyofanya yeye dhidi ya Henry alikuwapo katika gereza hilo. Alikuwa akihofia siri zake kuvuja kwani Tabangu alihusika na matukio yote aliyokuwa ameyafanya.

    “sasa nyinyi mbona huyo George sipati habari za mauaji dhidi yake?” alisikika Frank kwa sauti ya chini sana akiongea na mfungwa mmoja kati ya wale aliowapa kazi ya kuhakikisha kifo dhidi ya George. Alifanya hivyo kwa vile kulikuwa na askari magareza mmoja pembeni ambaye alisimamia maongezi hayo. “tutajitahidi ila jamaa siku hizi kuna mtu anamlinda ndio maana tunashidwa……” alisikika mfungwa huyo kwa sauti ya chini pia kabla ya sauti ya askari magareza iliyokemea jinsi walivyokuwa wakiongea kwa sauti ya chini. Askari huyo alionekana kutomfahamu kijana aliyeongea na mfungwa huyo, Frank Joseph mtoto wa waziri wa nchi kwani angelitambua hilo angeweza kuhofia kazi yake. Frank na mfungwa huyo walianza kuongea kwa sauti mambo mengine tofauti na lile lililompeleka gerezani hapo. Alikuwa anaelewa kuwa agizo alilotoa lingefanyiwa kazi kwa vile mfungwa huyo alikuwa amemjibu. Hakuelewa mtu aliyekuwa anamlinda George alikuwa ni mfungwa gani ila aliamua kupuuzia.

    Mara baada ya maongezi na mfungwa huyo aliondoka eneo hilo kabla ya kutoka nje na kuelekea eneo aliloegesha gari lake na hatimaye aliingia. “Frank!, Frank!......” iliita sauti ya kike toka kwenye gari lililokuwa limeegeshwa sekunde kadhaa kabla ya kutoka kwake katika eneo hilo la maegesho. Frank hakusikia sauti hiyo na aliondoa gari lake kwa kasi gerezani hapo. Sauti hiyo ya kike iliyomuita haikuwa ya mtu mwingine zaidi ya Winnie aliyefika kumtazama George kama alivyokuwa amepanga. “eeeh! afadhali ameenda, nimekurupuka kumuita angeniuliza nimekuja kufanya nini lakini na yeye alikuja kufanya nini?” Alisikika Winnie kwa sauti ya chini akiongea peke yake.

    Hakupoteza muda kujiuliza juu ya suala hilo akiamini angepata jibu jioni ya siku hiyo kwani lazima angekutana na Frank. Alianza kutembea kurudi kwenye gari lake alilokuwa amefika nalo lengo likiwa kwenda kuchukua chakula alichokuwa amempelekea George. Mara baada ya kuchukua usoni alibadilika ghafla na kuonekana mwenye huzuni wakati akielekea katika eneo la mapokezi. Alikuwa akijiuliza maswali mengi kichwani pasipo kupata majibu, alihisi George angekataa kukutana naye. Zaidi alikuwa akiwaza ni jinsi gani mchumba wake huyo wa zamani alikuwavyo wakati huo akiwa jela. Alikuwa akiumia moyoni na ndoto alizoota ndizo zilizompa kiulizo juu ya harusi yake iliyobakiwa na siku mbili.

    Mara baada ya kufika eneo hilo hakupoteza muda, alijitambulisha na kueleza alimhitaji George Innocent. Alipelekwa mpaka eneo ambalo lilikuwa maalumu kwa ajili ya wageni waliofika kuwaona wafungwa gerezani hapo, alikaa akimsubiri George ambaye alikuwa amefuatwa na askari magereza.

    Alibaki kimya akimsubiri huku akiendelea kuwa katika hali ileile aliyokuwa nayo awali, baada ya dakika kumi alimshuhudia mfungwa aliyemfananisha na George akiwa ametangulia wakati askari magereza alikuwa akimfuata nyuma. Mtu huyo alishtuka na kuonesha dalili za kutaka kurudi, ila alijikaza kabla kuendelea kuelekea eneo ambalo Winnie alikuwapo. Mara baada ya kufika eneo hilo alikaa upande wa pili akiwa anatazamana uso kwa uso na Winnie. Wakati akiwa amekaa kimya alimshtua Winnie aliyegundua kuwa mtu huyo aliyekuwa amekonda kupindukia akiwa na majeraha mengi alikuwa George. Sura yake ilikuwa imebadilika kwa kiasi kikubwa na ilikuwa vigumu kwa mtu wa kawaida kukubali kuwa alikuwa ni George. Akiwa amebaki mdomo wazi huku akimshangaa pasipo salamu yeyote George alisikika akiongea kabla yake

    “Winnie hongera naamini unafuraha katika ndoa yako” aliongea George katika hali ya tabasamu lililojaa majonzi. “tuachane na ndoa mimi sijaolewa bado, hivi imekuwaje uko katika hali hii?” alisikika Winnie akitaka kujua kuhusu majeraha aliyokuwa nayo pamoja na jinsi alivyokuwa amekonda. “unauliza nini wakati kila kinachoendelea ni mpango wako na mumeo” alijibu George akiwa hana nia ya kuelezea jambo lolote.



    o wako na mumeo” alijibu George akiwa hana nia ya kuelezea jambo lolote.

    “mmh! haiwezekani mimi ni binadamu hata Frank yuko hivyo, hatuwezi kukufanyia kitu kibaya binadamu mwenzetu halafu usimuite mume wangu sijaolewa bado na sijisikii kuongelea harusi yangu…” aliongea Winnie katika sauti ya upole akijaribu kumweleza George. “sawa kama hujaolewa, bado naamini kama ulikuwa mchumba wangu na mke mtarajiwa uliyepangwa na mwenyezi Mungu tukiwa chuo kikuu Dar es salaam basi itakuwa, kama haikupangwa hivyo harusi yako iko palepale hata kama kesho…” alisikika George akiongea katika hali ya kujiamini, maneno hayo yalimuumiza sana Winnie na akajikuta akitibua nywele zake alizosuka kwa mikono kama mtu aliyechanganyikiwa. Wakati huo George alikuwa akisimama kumwacha mrembo huyo aliyekuwa na mchanganyiko wa damu ya baba mwafrika na mama mzungu. “George vipi sasa mbona unaondoka? subiri basi nikupe chakula nimekuletea” alisikika Winnie kutoka kwenye mawazo ya ghafla baada ya kumwona George akiwa amesimama tayari kwa kuondoka. “aaah! nile chakula ulicholeta wewe, siko tayari hata kidogo si umetumwa na mumeo”

    “nimekwambia sijaolewa halafu inamaana hata mimi huniamini” alisikika Winnie kwa jazba kidogo “kiukweli si kuamini kama ambavyo huku niamini nilivyokwambia sielewi na sihusiki na picha za utupu nilizotolewa magazetini nakutakia harusi njema…” aliongea George kabla ya kuondoka eneo hilo akimwacha Winnie akitokwa na machozi pasipo kujitambua. Alikuwa amekutana na mambo mengi kwa muda mfupi. Alianza kuingiwa na hisia za hali ya juu kuwa Frank hakuwa mtu mzuri lakini jibu likibaki kuwa palepale kuwa hakuwa na uthibitisho wa mawazo hayo.

    Alikuwa ameingiwa pia na hisia za kuwa tena na George ambazo alijaribu kuzipinga zisichukue nafasi moyoni mwake. Alianza kuhisi kuwa huenda George alikuwa mtu mwema lakini alijipinga mwenyewe akikumbuka picha za utupu zilizotolewa magazetini miezi kadhaa iliyokuwa imepita. Alikuwa amechanganyikiwa zaidi juu ya masaa arobaini na nane yaliyokuwa yamebakia ili aingie katika kifungo cha ndoa na Frank. Alitamani kama kungekuwa na uwezekano wa kusogeza mbele harusi hiyo ili aweze kuwachunguza George na Frank wote kwa mapana lakini hilo halikuwezekana. “…..kama ulikuwa mchumba wangu na mke mtarajiwa uliyepangwa na mwenyezi Mungu tukiwa chuo kikuu Dar es salaam basi itakuwa……” “…si kuamini kama ambavyo huku niamini nilivyokwambia sielewi na sihusiki na picha za utupu zilizotolewa magazetini….”aliongea Winnie peke yake baadhi ya maneno aliyoya kumbuka ambayo George alikuwa ameyazungumza yaliyozidi kumchanganya. Wakati huo alikuwa akitoka gerezani hapo baada ya kumkabidhi askari magereza jukumu la kumpa chakula alichompelekea George mfungwa yeyote gerezani hapo. Aliondoka na gari lake huku akiwa mnyonge lakini ilimpasa akajiandae kwa ajili ya sherehe iliyoandaliwa jioni ya siku hiyo na waziri wa nchi mzee Joseph akiwa na lengo la kuwapongeza kwa kukaribia kufunga harusi. Tayari alikuwa ameshafanyiwa sherehe ya kuagwa na familia yake na jambo pekee lililosubiliwa lilikuwa harusi hiyo.

    Sherehe hiyo ilifanyika kama ilivyokuwa imepangwa, Winnie alipata nafasi ya kumuuliza Frank juu ya kwenda kwake katika gereza la Ukonga akidai kuna mtu alimweleza hivyo. Mchumba wake huyo alimjibu kwa ufupi akidai alikuwa na ndugu yake katika gereza hilo. Siku iliyofuata iliyokuwa ya Jumamosi Winnie alipangiwa chumba katika hoteli moja iliyokuwa maeneo ya Ubungo wakati Frank alikuwapo maeneo Kariakoo. Walipaswa kuondaka katika hateli hizo siku iliyofuata na kwenda kukutana katika kanisa la kikistro walilotarajia kufunga harusi lililokuwapo maeneo ya Posta. Katika hoteli hizo kulikuwa kumeandaliwa taratibu zote za maandalizi ikiwapo kupambwa kwa maharusi hao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Winnie alikuwa peke yake katika chumba cha hoteli hiyo ya kifahari iliyokuwapo maeneo ya Ubungo. Huku akiwa ametawaliwa na mawazo ya kutoamini tukio ambalo lingetokea katika masaa kadhaa yaliyokuwa yamesalia. Aliachwa katika chumba hicho peke yake ili apate muda wa kupumzika kabla ya kuingia katika ndoa rasmi. Kulikuwa na wahudumu zaidi ya sita waliokuwapo hotelini hapo waliokuwa maalumu kwa ajili ya kumhudumia kitu chochete alichohitaji. Hata simu yake ilifungwa, akiwa ameshauriwa kutoiwasha kwani angeweza kupokea taarifa mbaya ambazo zingemfanya ashindwe kushiriki harusi hiyo. Hakuna mtu aliyehurusiwa kuingia katika chumba hicho zaidi ya wazazi wake na wa Frank ambao walimtembelea kwa nyakati tofauti.

    Alikuwa akiumia katika hali ambayo hakutambua maana yake kwani muda wote alijiona mkosaji kwa kushindwa kufuatilia kwa undani ukweli juu ya tukio lililotenganisha uhusiano wake na George.Alitamani litokee jambo ambalo lingepelekea harusi hiyo isogezwe mbele au ifutwe kabisa, aliona ni bora angeishi peke yake baada ya kuachana na George. ‘nakupenda sana Winnie na naahidi nitakuoa mara baada ya masomo yetu’ mawazoni alikumbuka maneno hayo ya George aliyoahidiwa, siku waliyokuwa katika kivuli cha miti iliyokuwapo chuoni. Swali kubwa lililomtawala kichwani lilihusu uaminifu ambao George aliuonyesha kabla ya tukio lililopelekea kuvunjika uhusiano wao, hakuwa na jibu wakati akisubiri miujiza itokee ili harusi hiyo isifungwe.

    * * * *

    Grace Stephen alikuwa amepita mambo mengi ya uovu katika ujana wake, jambo lililopelekea akane uovu huo na kuokoka katika kanisa la kikristo la ‘Christians Way to Lord’. Akiwa na miaka kumi na nane alitumia uzuri wake kwa kufanya biashara ya kuuza mwili wake, haikuwa taabu kwake kuzunguka katika hoteli na baa tofauti jijini Dar es salaam akifanya biashara hiyo. Hakuamini jambo lolote kuhusu mwenyezi Mungu zaidi alifanya kejeli juu ya watu waliongelea uweza wake. Siku moja katika harakati zake hizo za biashara hiyo haramu, alikuwa maeneo ya Hoteli moja Sinza ambako baada ya kuona siku hiyo alielekea kukosa mteja aliamua kujisogeza kwa kijana mmoja aliyevaa suti na zaidi alikuwa mtanashati. Kijana huyo alidhania Grace alikuwa na njaa jambo lililopelekea amnunulie chakula bila kupoteza muda alishukuru kabla ya kuanza kula. Baada ya kula Grace alimwomba kijana huyo aliyekuwa anakunywa soda amnunulie bia. Kijana huyo alikataa ombi hilo ila alikuwa tayari kumnunulia soda jambo ambalo Grace aliamua kukubali.

    Mara baada ya fadhila zote hizo kijana huyo wakati akiondoka, Grace alimn`gan`gania waondoke wote. Alimkatalia lakini alikuwa mgumu kuelewa kwani alishakunywa bia kadhaa kabla ya kukutana na kijana huyo, kwa hiyo kwa kiasi fulani alikuwa amelewa. Hatimaye kijana huyo aliondoka huku akifuatwa nyuma na Grace aliyekuwa mgumu kuelewa, mwishoe wakati kijana huyo akiingia katika chumba chake alichopanga katika hoteli hiyo na yeye aliingia. Huko ndiko alikoenda kutambua kwamba kweli Mungu yupo kwani alikuwa akimlilia mtu huyo afanikishe biashara yake wakati alikuwa Mchungaji.

    Alikemewa kwa nguvu na mchungaji huyo mara baada ya kuingia katika chumba hicho na kusababisha aanguke kabla ya mapepo kuanza kulia yakiomba msamaha. Wakati huo alikuwa akitupa mikono na miguu eneo alilokuwapo na mchungaji huyo alikuwa akiendelea kumwombea. Baada ya muda wa dakika kumi alirudiwa katika hali ya kawaida na alionekana kuutambua uwepo wa mwenyezi Mungu kwani aliomba kuokoka wakati huohuo.

    Hivyo ndivyo Grace Stephen alivyoachana na uovu na kuwa muumini mwema wa kanisa la mchungaji huyo la ‘Christians Way to Lord’. Ni wakati huu ambao aliona ni vema alekebishe makosa ambayo aliyatenda ambayo iliwezekana kusahihishwa, aliwafuata wazazi wake waliomtoa kabisa akilini nakuwaomba msamaha. Baada ya zoezi hilo aliwaomba msamaha pia watu kadhaa ambao alikorofishana nao wakati akiwa katika biashara yake ya kujiuza. Wakati akiendelea na zoezi hilo alikumbuka tukio kubwa alilowahi kufanya ambalo lilikuwa gumzo nchini ila alifanya hivyo kutokana na hitaji la pesa lililokuwa kila kitu kwake. Alikuwa amehusika na tukio zima la kutenganisha uhusiano wa mtoto wa tajiri mkubwa nchini mzee Innocent na yule wa balozi wa Ufaransa nchini.

    Alikuwa ni msichana aliyepiga picha za utupu na George wakati akiwa anafanya kazi yake katika hoteli ya Kenniville maeneo ya Mwenge. Alishiriki tukio hilo haramu wakati kijana huyo mtoto wa tajiri akiwa hana fahamu baada ya kupigwa na chuma kizito kichwani. Picha hizo walizisambaza katika ofisi mbalimbali za magazeti kwa njia ya anuani ya barua pepe lengo likiwa kutenganisha uhusiano wa George na Winnie. Alifanikisha hayo yote baada ya kupewa kazi hiyo na mtoto wa waziri wa nchi Frank Joseph aliyekuwa akimhitaji Winnie. Baada ya miezi kadhaa ya tukio hilo lililokuwa gumzo nchini aliweza kusikia mtoto huyo wa waziri alifanikiwa kumpata Winnie. Hakufuatilia zaidi mwenendo wa uhusiano wao zaidi kwani aliendelea na shughuli zake.

    Mawazo yaliyompata yalikuwa ni kuutoa ukweli wa jambo hilo haraka sana kwani vielelezo vingine juu ya suala hilo alikuwa navyo. Bila kupoteza muda alimpigia simu rafiki yake mmoja akitaka kuelezwa juu ya uhusiano huo wa Frank na Winnie. “he! huna habari bibie, wamebakiza masaa tu ili wafunge harusi yao” alisikika rafiki yake huyo katika maongezi hayo ya simu akimweleza kuwa watu hao walibakiwa na masaa machache ili wafunge harusi yao katika kanisa la kikistro lililokuwapo maeneo ya Posta. Grace alihisi kuchanganyikiwa wakati akielewa yeye pekee ndiye alipaswa kuharibu harusi hiyo haramu isifungwe katika masaa machache yaliyokuwa yamebakia. Aliondoka nyumbani kwao maeneo ya Vingunguti akiwa na lengo la kwenda kupata maelezo ya harusi hiyo katika kanisa hilo lililokuwapo maeneo ya Posta.

    Hatimaye alifika katika kanisa hilo ambako alipata maelezo juu ya harusi hiyo iliyofungwa siku iliyoifuata. Alijaribu kuwaeleza watumishi kadhaa kuwa harusi hiyo ilikuwa haramu na isifungwe lakini walionekana kumwona kama ni mtu mwenye wivu. “We siku zote harusi hii inatangazwa ulikuwa wapi halafu unakuja leo” alisikika mtumishi mmoja ambaye hakutaka hata kujua jambo ambalo Grace alitaka kuwaeleza. Mwishoe aligundua uwezekano mdogo wa kuweza kuzuia harusi hiyo kanisani hapo hivyo aliamua kuanza kuondoka ili ajaribu njia nyingine. Wakati akiendelea kuondoka alilishuhudia gari la kifahari liingia katika eneo hilo la kanisa. Alitutulia kidogo kabla ya gari hilo kusimama kando yake kidogo na alimshuhudia waziri wa nchi mzee Joseph akishuka katika gari hilo nakufuatiwa na mtu aliyehisi alikuwa kiongozi mkubwa wa kanisa hilo kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “sasa itakuwa saa nne….eeh tutakuwa tumefika tayari kwa misa, kwa heri” ilikuwa ni sentensi ya mwisho aliyoisikia kutoka kwa waziri ambaye pia alimsikia kuwa Winnie alikuwapo katika moja ya hoteli iliyokuwapo Ubungo wakati Frank alikuwapo maeneo ya Kariakoo. Alipata furaha ya ghafla ambayo hakuionesha wazi akiwa anawaza kuhakikisha anafanikisha kuitoa siri hiyo kwa Winnie kwa vile aliitambua hoteli ambayo waziri huyo aliitaja. Bila kupoteza muda alianza kuondoka eneo hilo la kanisa wakati waziri huyo naye alikuwa akiondoka.









    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog