Simulizi : The Love You Had Before (Penzi Ulilokuwa Nalo Kabla)
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Laurence hakutaka kusikia, japokuwa aliambiwa kwamba hakutakiwa kwenda nyumbani kwa kina Evadia lakini kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo, kesho yake tu akajikuta akiwa huko.
Mapenzi yalimsumbua, hakutaka kuona akimuacha msichana huyo kiwepesi kama ilivyotakiwa kuwa. Alipofika nyumbani hapo, hakuingia ndani, alibaki nje na kuanza kugonga.
Katika kipindi hiki hali ilikuwa tofauti, kulikuwa na mlinzi getini ambaye aliambiwa wazi kwamba hakutakiwa kumruhusu mtu aliyeitwa Laurence kuingia ndani ya nyumba hiyo.
Kitendo cha Laurence kugonga geti, likafunguliwa na mlinzi, kwanza alishtuka, hakutegemea kumuona mlinzi mahali hapo kwani kitu alichojua ni kwamba mama Evadia angekuja kufungua kama zamani.
“Karibu kaka,” alimkaribisha mlinzi yule.
“Asante. Nimewakuta wenyewe?”
“Ndiyo! Unaitwa nani?”
“Naitwa Laurence. Nimekuja kumsalimia Evadia,” alijibu Laurence.
“Kumbe wewe ndiye Laurence?”
“Ndiyo kaka!”
“Hautakiwi kuingia humu.”
“Kwa nini?”
“Hayo ni maagizo, hautakiwi kuingia humu,” alisema mlinzi huku akimwangalia Laurence usoni.
Alichokisikia, hakukiamini, alimwangalia mlinzi yule mara mbili mbili, alihisi kama hakusikia vizuri, akamwambia arudie, mlinzi akarudia kwamba hakutakiwa kuingia ndani ya nyumba ile, hilo halikuwa ombi bali agizo.
Laurence hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo huku akiwa na huzuni kubwa. Bilionea yeye, kisa tu kujiweka katika hali ya umasikini, leo hii aliambiwa kwamba hakutakiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo.
Hilo likamfanya kumpigia simu Matilda na kumwambia kila kitu kilichotokea huko. Alihuzunika sana, wakati mwingine alipokuwa akizungumza naye, alikuwa akitokwa na machozi.
“Pole sana Laurence, ila naomba nikazungumze nao,” alisema Matilda.
“Kuhusu nini?”
“Wewe hapo!”
“Hapana bwana, achana nao. Nimeamia sana lakini sina jinsi, ngoja nipumzike, nahisi mapenzi yataniumiza zaidi kama nitalazimisha penzi kwa Evadia,” alisema Laurence.
“Basi sawa.”
“Ok! Kesho naondoka kuelekea Marekani kupumzika, sidhani kama nitaonana tena na Evadia, nitatafuta msichana mwingine wa kumuoa,” alisema Laurence.
“Kwa hiyo nikamwambie ukweli kuhusu wewe?”
“Haina tatizo. Kwa kuwa sitomhitaji tena, hakuna tatizo,” alisema Laurence.
Upande wa pili, Matilda hakuridhika, kitendo cha bosi wake kukataliwa kilimuumiza mno, alichokifanya mara baada ya kumaliza kuzungumza naye ni kuondoka na kuelekea Mabibo, alitaka kuzungumza na wote wawili, alitaka kujua sababu iliyomfanya Evadia kumkataa Laurence.
Kutokana na kutokuwa na foleni barabarani, alitumia dakika chache mpaka kufika Mabibo. Alichokifanya ni kuingia katika mtaa aliokuwa akiishi Evadia, baada ya dakika kadhaa akafika nje ya geti la nyumba hiyo, akaanza kupiga honi.
“Nikusaidie nini dada?” aliuliza mlinzi.
“Nahitaji kuwaona wenyewe.”
“Unaitwa nani?”
“Matilda.”
Mlinzi akalifungua geti na kuingia ndani. Moyo wa Matilda ulikuwa kwenye maumivu makali, kila alipofikiria jinsi Evadia alivyomkataa Laurence, moyo wake uliumia mno, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea kwani huyo Laurence aliyekataliwa alikuwa miongoni mwa mabilionea wakubwa nchini Tanzania.
Alipoliingiza gari ndani, Matilda akateremka na kisha kuelekea ndani ya nyumba hiyo, mlango wa sebuleni ukafunguliwa na mfanyakazi na kukaa katika makochi makubwa.
Wala hazikupita sekunde nyingi, Evadia na mama yake wakatokea sebuleni hapo ambapo wakasalimiana kwa kukumbatiana kisha kukaa kochini.
“Evadia, hebu nieleze tatizo nini,” alisema Matilda.
“Tatizo kuhusu nini?”
“Umefikia wapi na Laurence?”
“Tumefikia sehemu nzuri tu.”
“Ndoa ipo?”
“Ndoa?”
“Ndiyo!”
“Bado tunalizungumzia hilo,” alisema Evadia.
Matilda akamwangalia Evadia usoni, alitamani kumwambia ukweli kuhusu Laurence lakini kila alipotaka kufanya hivyo, akasita kabisa. Moyo wake ulijawa huruma mno, alimuona Evadia kuwa msichana mpumbavu ambaye bahati ilimjia mpaka mlangoni ila pasipo kujua, akaipiga teke.
“Evadia….”
“Abee dada.”
“Hivi kweli umemkataa Laurence?” aliuliza Matilda, wote wakashtuka, wakajua kwamba Laurence alimwambia msichana huyo. Akabaki akiangaliana na mama yake.
“Kweli umemkataa Laurence?” alilirudia swali lake.
“Dada…”
“Niambie ukweli!”
“Sina cha kuongea.”
“Au kwa sababu ya umasikini wake?”
“Hapana!”
“Kumbe kwa ajili gani? Haukumbuki kwamba alikusaidia figo yake ili mradi uweze kupona?”
“Nakumbuka dada.”
“Niambie tatizo nini?”
“Hakuna kitu”
“Ila umemkataa?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kimyaa.
Matilda alionyesha chuki za waziwazi kiasi kwamba wote wawili wakaogopa. Matilda alionyesha kuchukizwa kwa kile kilichotokea, kitendo cha bosi wake kukataliwa kisa tu alionekana kuwa masikini ilimuumiza mno moyoni mwake, akabaki akimwangalia Evadia kwa hasira kubwa.
“Evadia, wewe ni msichana mpumbavu,” alisema Matilda huku akionekana kuchukizwa.
“Wewe ni mpumbavu kwa sababu humfahamu Laurence ni nani, amekuja kwako kwa lengo gani, yaani kisa masikini unamkataa Laurence, kweli una akili wewe? Hivi unamjua Laurence wewe?” aliuliza Matilda huku akimwangalia msichana huyo usoni.
“Nisamehe dada…”
“Evadia, kumsikiliza mama yako umekosa bahati, Laurence amekuja kwako, amejifanya masikini, amekusaidia kwa kutoa figo yake, mwisho wa siku unamwambia haumtaki. Evadia, hakuna mwanamke yeyote ambaye angekuwa na uwezo wa kumkataa Laurence,” alisema Matilda maneno ambayo yaliwafanya wote kubaki kimya.
“Unatumia mtandao gani wa simu?”
“Tritelcom.”
“Unamjua mmiliki wa mtandao huo?”
“Hapana.”
“Evadia, sikutaka kukwambia hili, hata Laurence hakutaka ulifahamu hili ila kwa kuwa umemuacha na yeye ameamua kuondoka na kutorudi tena, ngoja nikwambie tu,” alisema Matilda.
“Kuna nini dada.”
“Huyu Laurence unayemsikia kwamba ni bilionea, mwenye fedha nyingi, kampuni za simu na mafuta, ndiye huyuhuyu aliyekufuata wewe na kujifanya masikini, fedha zote nilizokuwa nikiwapa, ni zake, zile milioni thelathini za hospitalini, ni zake, japokuwa aliniambia kwamba unamkataa, nikamwambia hata fedha asitoe kuwasaidia, ila yeye akasema fedha ziendelee kutoka kwani alikupenda sana, mwisho wa siku, kwa kutokujua kwako, kwa kupenda wanaume wenye pesa, umeamua kumuacha Laurence, ni aibu iliyoje,” alisema Matilda kwa uchungu mno.
“Unasemaje?” aliuliza mama Evadia huku akionekana kutokuamini.
“Mmechezea bahati. Laurence ameumia mno, amezungumza nami huku akilia, hivi anajiandaa kwenda Marekani kupumzika, umeuumiza mno moyo wake,” alisema Matilda, hapohapo akasimama.
Wawili hao wakabaki wakimwangalia Matilda, hawakuamini kile walichokisikia, walitamani msichana huyo arudie tena kuwaambia juu ya Laurence kwani walihisi kwamba walisikia vibaya.
Hapohapo Evadia akaanza kulia sana, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kilichokuwa kimetokea, hakuamini kama mwanaume aliyekuwa amemuacha ndiye yule ambaye kila siku alisikia kwamba alikuwa bilionea.
Pamoja na biashara walizokuwa wakizifanya, lakini bado fedha walizopewa na Matilda ndizo zilezile ambazo ziliwasaidia kuyafanya maisha yao kuwa juu.
Machozi yalimmwagika machoni mwake lakini hilo halikuweza kubadilisha matokeo, bado ukweli ukabaki palepale kwamba alichezea bahati ya kumkataa mwanaume bilionea, tena kwa dharau kubwa.
“Dada…naomba ukaniombee msamaha kwa Laurence….” alisema Evadia huku akilia, hapohapo akapiga magoti mbele ya Matilda, si yeye tu aliyefanya hivyo, bali hata mama yake.
Moyo wa Dickson ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile alichokisikia kwamba mpenzi wake hakutaka aingie ndani ya nyumba hiyo kwa sababu tu alikuwa na mwanaume mwingine ndani ya nyumba hiyo.
Dickson angeweza kujifanya kiburi, kuleta vurugu mahali hapo na kuingia kinguvu lakini kila alipomwangalia mlinzi yule, alikuwa na mwili uliojazia mno, tena mkononi alishika bunduki, hivyo akaogopa.
Akanyong’onyea, kila alipomfikiria msichana huyo moyo wake ulimuuma sana, hakujua nyumbani angesema nini, hakujua ni kwa jinsi gani angewaambia wazazi wake juu ya kile kilichotokea nchini Rwanda.
Hakuwa na jinsi, hakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, alichokifanya ni kupiga hatua kurudi nyuma, kwa sababu dereva taksi hakuwa ameondoka mahali hapo, wakarudi garini na kurudi walipotoka.
Akashindwa kuvumilia, kile kilichotokea kilikuwa aibu kubwa kwake, alishindwa kuyazuia machozi kububujika mashavuni mwake, japokuwa Buka alimbembeleza sana lakini Dickson hakutaka kunyamaza.
“Nyamaza Dickson….”
“Hivi kweli Luciana ananifanyia hivi!”
“Pole sana, achana naye.”
“Inaniuma sana, unajua tumeanza mbali sana na Luciana,” alisema Dickson.
Machozi yake hayakubadilisha kitu chochote kile, alichokikuta nchini Rwanda ndicho kilichokuwa kimetokea, mpenzi wake alichukuliwa na mwanaume mwingine.
Hakutaka kubaki nchini Rwanda, kwa kuwa alikata tiketi ya kuja na kuondoka, siku iliyofuatia alikuwa ndani ya ndege akirtudi nchini Tanzania. Bado maumivu ya mapenzi hayakupungua moyoni mwake, muda mwingi alibubujikwa na machozi tu.
Alikosa tumaini, wakati anamfikiria Luciana hapo ndipo jina la Evadia likaanza kujirudia kichwani mwake. Akaanza kumkumbuka msichana huyo ambaye aliachana naye kipindi cha mwaka mzima uliopita kisa tu alimpata Luciana ambaye aliamua kuumiza moyo wake.
Hakukuwa na kitu alichokifikiria kwa wakati huo kama kurudi kwa Evadia na kumuomba msamaha juu ya kile kilichokuwa kimetokea, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, alikuwa tayari kwa kila kitu, kumfuata msichana huyo na hata kama lingekuwa suala la kumpigia magoti, kwake angekubaliana nalo.
Baada ya saa kadhaa akafika nchini Tanzania na ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akateremka na kisha kuchukua taksi na kurudi nyumbani.
Mawazo hayakuisha, kila wakati aliendelea kumfikiria msichana Evadia, alijua fika kwamba alimuacha katika kipindi muhimu sana, ila katika kipindi hicho, alihitaji msamaha.
“Nitahitaji anisamehe, dunia imenifunza, na mapenzi ya kukurupuka yamenifunza pia,” alisema Dickson wakati gari likiingia katika Barabara ya Kawawa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipofika nyumbani, hakuwakuta wazazi wake, hivyo akaingia moja kwa moja chumbani na kujilaza. Moyo wake uliendelea kuwa kwenye maumivu makali mno, macho yake yalikuwa mekundu mno sababu ya kulia sana njiani.
Ilipofika saa kumi na moja jioni, wazazi wake wakarudi nyumbani hapo na kumkuta. Walishangaa sana kwani ni jana yake ndiyo alikuwa ameondoka na kuelekea nchini Rwanda, sasa ilikuwaje mpaka arudi tena ikiwa ghafla mno? Kila walipojiuliza, wakakosa jibu.
“Kuna nini?” aliuliza mama yake.
“Mapenzi yamenishinda,” alisema Dickson huku akijaribu kuyafuta machozi yake.
“Nini kimetokea?” aliuliza baba yake.
Dickson hakutaka kuficha kitu chochote kile, alichokifanya ni kuwahadithia wazazi wake kile kilichotokea nchini Rwanda. Katika kipindi chote alichokuwa akisimulia, machozi yalimbubujika, alionekana kuumizwa na kile kilichokuwa kimetokea.
“Pole sana, kwa hiyo umeamua nini?” aliuliza baba yake.
“Kumuomba msamaha Evadia na nimrudie, tena nimuoe kabisa,” alisema Dickson.
“Umrudie Evadia?”
“Ndiyo! Haina jinsi baba. Kama kuumia nimeshaumia sana, sina jinsi, ni lazima nimrudie Evadia,” alijibu Dickson.
“Atakubali kweli?”
“Sijui! Ila ni lazima nimrudie.”
Wote wawili walichanganyikiwa, maneno waliyoambiwa na Matilda yaliwachanganya mno, wakabaki wakiwa wamempigia magoti kana kwamba yeye ndiye alikuwa Laurence.
Walijilaumu na kujuta kwa kile walichomfanyia mwanaume huyo ambaye kila siku walijua kwamba alikuwa kijana masikini. Evadia alilia huku mama yake akimbembeleza Matilda akawaombee msamaha lakini msichana huyo aliendelea kuwalaumu.
Alimfahamu Laurence, alikuwa mwanaume mwenye msimamo, alipoamua kufanya jambo fulani, hakuwa akiangalia, alichokijua ni kufanya na kuendelea na mambo yake.
Kitendo cha kukataliwa na msichana huyo kilimpa uhakika Matilda kwamba Laurence asingeweza kuwa naye, ila kwa sababu waliomba sana, hakuwa na jinsi, akawaambia wajiandae ili waweze kwenda nyumbani kwa Laurence, kwani kama wasingefanya hivyo siku hiyo, wasingeonana naye kutokana na safari ya kwenda nchini Marekani ambayo alikuwa nayo.
“Fanyeni haraka,” aliwaambia.
Hakukuwa na mtu aliyekwenda bafuni kuoga, kila mtu akabadilisha nguo na kuanza safari ya kuelekea Mbezi beach alipokuwa akiishi Laurence. Njiani, hawakuacha kumbembeleza Matilda awaombee msamaha kwa mwanaume huyo, yeye mwenyewe hakuwa na uhakika kama angekubali kuwasamehe kwani kama kulia kwa ajili ya mapenzi, alilia sana lakini mwisho wa siku hakuna aliyefahamu thamani ya kilio chake.
Walichukua dakika kadhaa ndipo wakafika huko. Gari likasimama nje ya jumba moja kubwa na la kifahari, geti likajifungua na kisha Matilda kuanza kuliingiza gari.
Hawakuamini kama jumba la namna hiyo lingekuwepo nchini Tanzania. Lilikuwa na eneo kubwa, bwa la kuogelea, mbuga ndogo ya wanyama, sehemu kubwa ya kufugia samaki huku kukiwa na sanamu kubwa ya Laurence ikiwa imesimamishwa, tena huku ikimuonyesha akiwa ameshika cheti mkononi.
Evadia hakuamini kama jumba hilo la kifahari ndiylo alilokuwa akiishi mwanaume aliyemchukia, alishindwa kuyazuia machozi yake, yakaanza kumbubujika kwa uchungu.
“Tumefika,” alisema Matilda na kuteremka.
Katika sehemu ya kuegesha magari hakukuwa na gari lililokuwa chini ya shilingi milioni mia moja, yote yalikuwa juu mpaka Ferrari Spider ambalo dukani lilikuwa na gharama zaidi ya milioni mia tano.
Evadia akahisi kuchanganyikiwa, alitamani kurudisha muda nyuma ili aweze kurekebisha mambo yake, awe na Laurence ili kila kitu alichokiona kiwe chake lakini hakuwa na uwezo huo tena, muda haukurudi nyuma.
Kwa kuwa Matilda alikuwa mwenyeji, wakaanza kuelekea ulipokuwa mlango wa kuingilia sebuleni na kuingia ndani. Kila mmoja alikodoa macho, jumba lile lilikuwa na vitu vya thamani mno, kwa muonekano wake halikustahili kabisa kujengwa nchini Tanzania.
“Hapa ndipo anapoishi Laurence?” aliuliza mama Evadia.
“Ndiyo hapa. Subiri, atakuja tu,” alijibu Matilda.
Mfanyakazi mmoja aliyevalia nadhifu akafika sebuleni hapo na kuwakaribisha kwa kuwaletea vinywaji. Hakukuwa na mtu aliyehisi radha yoyote ile kwani hali waliyokuwa nayo katika kipindi hicho ilikuwa tofauti kabisa.
Hawakukaa muda mrefu, Laurence akatokea sebuleni hapo. Siku hiyo ndiyo walimuona jinsi alivyokuwa, mwanaume msafi aliyevalia mavazi mazuri na ya thamani, hata Evadia mwenyewe alivyomuona, alijuta moyoni kumpoteza mwanaume kama huyo.
Hapohapo, kabla hawajazungumza naye neno lolote lile, wakampigia magoti na kuanza kumuomba msamaha.
Laurence alibaki akiwaangalia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, kila alipomwangalia Evadia na mama yake, alikumbuka saa chache zilizopita kwamba alitimuliwa kama mbwa na kuambiwa asirudi tena nyumbani kwao.
Moyo wake uliumia sana kwa kuwa alikuwa na mapenzi ya dhati kwa msichana huyo. Alimwangalia sebuleni hapo, jinsi alivyopiga magoti na mama yake na kuanza kuomba msamaha, moyo wake ulimchukia, mapenzi yote aliyokuwa nayo kabla, yalipotea kabisa.
“Naomba unisamehe Laurence,” alisema Evadia huku akilia kama mtoto.
“Nikusamehe?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo! Naomba unisamehe kwa upumbavu nilioufanya,” alisema msichana huyo.
“Upumbavu gani tena?”
“Kukukataa na wakati ulikuwa ukinipenda kwa penzi la dhati,” alisema msichana huyo.
“Evadia, kunikataa mimi si upumbavu, ni haki yako, kila mtu ana haki ya kumpenda mtu fulani na kumchukia mtu fulani, ulichokifanya si upumbavu bali ni uamuzi,” alisema Laurence kwa sauti ya upole kabisa.
“Naomba utusamehe Laurence,” alisema mama Evadia.
“Mama! Hakuna kosa mliolifanya.”
“Tulikufukuza nyumbani.”
“Pia hilo si kosa, ni uamuzi tu, unaweza kumkaribisha mtu fulani na kumfukuza mtu fulani, huwezi kufungwa kisa umemfukuza mtu fulani,” alisema Laurence huku akiwaangalia usoni.
“Laurence, tunaomba utusamehe,”
“Evadia, hamkunifanyia ubaya wowote, hakuna kosa mlilonifanyia, sasa niwasamehe kwa lipi? Kama kungekuwa na kitu kibaya mmenifanyia, sawa, ila hakuna lolote baya,” alisema Laurence huku akiwaangalia wa zamu.
Walilia na kujuta, walitamani masaa yarudi tena ili wasifanye makosa tena lakini hilo halikuwezekana. Laurence aliumia kumuona msichana aliyekuwa akimpenda akipiga magoti mbele yake na kuomboleza lakini hakuwa na cha kufanya, alimpa nafasi ambayo aliichezea na kuona si kitu chochote katika maisha yake.
Hakutaka kukaa sana nyumbani hapo, alichokifanya ni kuaga, siku hiyo hakutaka kulala nyumbani, alitaka kwenda kulala hotelini kwani kichwa chake hakikuwa sawa kwa wakati huo.
“Matilda,” aliita.
“Abee bosi.”
“Utawasaidia kiasi fulani cha fedha. Nafikiri msaada wangu umeishia hapa,” alisema Laurence, hakutaka kuendelea kubaki hapo, alichokifanya ni kuondoka huku akiacha vilio vikali nyuma yake.
Dickson na wazazi wake wakafika katika nyumba aliyokuwa akiishi Evadia na mama yake, walifika hapo kwa lengo moja la kumuomba msamaha ili waweze kuishi pamoja kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Hakujua kama angekubaliwa au kukataliwa, alifika hapo kwa ajili ya kuomba msamaha tu. Moyoni mwake alijisikia kuwa na huzuni tele, alihisi kwamba mapenzi yake kwa Evadia yalirudi kama zamani.
Baada ya kufika karibu na eneo la nyumba ile, walichokishangaa ni kwamba nyumba hiyo haikuwepo bali kulikuwa na nyumba nyingine, tena iliyoonekana kuwa ya kifahari ikiwa kwenye ujenzi.
Walishangaa, hawakuamini kile walichokiona, maswali mengi yakaanza kumiminika vichwani mwao kwamba watu waliokuwa wakiishi humo walikwenda wapi? Walikuwa masikini wa kutupwa, je nyumba ile walikuwa wameiuza kwa tajiri mmoja, kila walipojiuliza, walikosa jibu.
Alichokifanya Dickson ni kusogea katika nyumba ile kwa lengo la kuwauliza mafundi juu ya wale waliokuwa wakiishi katika nyumba ile, walitaka kufahamu mahali walipokuwa.
“Mbona walihama kitambo,” alisema fundi mmoja.
“Walihamia wapi?”
“Nasikia Mabibo.”
“Kwani hii nyumba mnayoijenga ni ya nani?”
“Ya hao waliohama hapa.”
“Mmmh!”
“Ndiyo! Mbona maswali mengi mwana, wewe polisi nini?” aliuliza fundi huyo, alionekana kuwa bize na hakutaka kusumbuliwa zaidi.
“Hapana! Ila asante.”
Alichokifanya Dickson ni kwenda kwa majirani waliokuwa karibu na nyumba hiyo kwa lengo la kuuliza juu ya mahali alipohamia Evadia na mama yake. Alipowauliza majirani hao, walimwambia kwamba walihamia Mabibo kipindi cha miezi miwili iliyopita.
“Walipata wapi hela?”
“Mmh! Hata sisi hatujui.”
“Ila walipohamia mnapajua?”
“Sana tu.”
“Naomba mtupeleke.”
“Hakuna tatizo. Ngoja niwaitieni kijana wangu awapeleke.”
Aliyesimama mbele yake hakuwa mwingine bali Dickson, mwanaume ambaye kipindi cha nyuma alimwambia kwamba angemuoa lakini mwisho wa siku akamkataa kwa kuwa tu alimpata mwanamke mwingine ambaye alidai kwamba alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Kumuona Dickson mahali hapo kulimkumbusha mambo mengi, alizikumbuka vilivyo siku alizokuwa akijifungia chumbani na kulia kisa tu mapenzi, hakuwa na hamu naye lakini kwa sababu sehemu ya moyo wake ilikuwa kwa mwanaume huyo, hakuwa na jinsi, aliamua kumsamehe.
“Nashukuru sana Evadia, naomba unipende kwa penzi ulilokuwa nalo kabla, naomba unipende namna hiyo, nakuahidi kwamba sitokuumiza tena,” alisema Dickson huku akilia kama mtoto.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari yao nyingine ya mapenzi, pamoja na kuwa na mwanaume Dickson lakini haikuwa sababu ya kuisahau bahati ambayo aliichezea ya kutokumpenda Laurence kwa kuwa tu alikuwa masikini.
Kitu hicho kilimuumiza sana, japokuwa Laurence alimwambia kwamba halikuwa kosa lakini kila siku alikuwa akilia na alikosa amani kabisa.
“Ninataka nikuoe mpenzi, sina muda wa kupoteza,” alisema Dickson.
“Kweli?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo! Sitaki kukupoteza tena,” alisema mwanaume huyo.
“Sawa. Hakuna tatizo, ninafurahi kusikia hivyo,” alisema Evadia huku akiachia tabasamu pana, alichokihitaji kwa wakati huo ni kufunga ndoa na Dickson kwa kuamini kwamba angesahau kila kitu kilichotokea kati yake na Dickson.
“Niambie vizuri bosi,” ilisikika sauti ya Matilda kwenye simu.
“Nikwambie nini?”
“Kwa hiyo unaishi na figo moja?”
“Kwa nini?”
“Si moja uliitoa kwa Evadia!”
“Hahaha!”
“Mbona unacheka sasa?”
“Kiukweli sikutoa figo.”
“Mmmh!”
“Iliwezekana vipi na wakati kila mtu aliona kwamba ulitoa figo?” aliuliza Matilda.
“Kawaida tu, ila amini kwamba sikutoa figo kwa kuwa nahisi hata yangu haikuwa na vinasaba vinavyoendana na vyake,” alisema Laurence.
“Hebu niambie nini kilitokea,” alisema Matilda.
“Nilitoa kiasi cha fedha kwa ajili ya Evadia kupatiwa matibabu lakini kitu cha kushangaza, hakukuwa na mtu aliyefika ambaye alikuwa na vinasaba vilivyofanana na vyake.
“Nilichoamua ni kupotea, sikumwambia mtu yeyote, nilichukua ripoti ya majibu ya Evadia na kuondoka nayo kuelekea nchini Nigeria. Kule, niliwapa watu wa matangazo watangaze kama kulikuwa na mtu anayetaka kutoa figo yake kwa malipo makubwa, huwezi kuamini, walikuja wengi, na mwisho wa siku tukampata mtu ambaye vinasaba vyake viliendana na Evadia, nikaamua kumchukua na kumleta Tanzania huku nikiwa nimemlipa zaidi ya milioni hamsini,” alisema Laurence.
“Mmmh!”
“Ndiyo hivyo! Kilichofuata ni kufanya mchezo na madaktari mpaka kukamilisha kazi, ila kiukweli, sikutoa figo,” alimalizia Laurence na Matilda kushusha pumzi nzito.
Kipindi hicho Laurence alikuwa nchini Marekani, kila siku ilikuwa ni lazima kuwasiliana na Matilda na kumwambia afuatilie kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika kampuni zake, alimwamini kwa kuwa kwa kipindi cha miaka mitano aliyofanya naye kazi, msichana huyo alimuonyeshea uaminifu mkubwa.
Baada ya kukaa nchini Marekani kwa kipindi cha mwezi mzima ndipo akarudi nchini Tanzania. Haikuwa rahisi kumgundua Laurence, alijifanya mtu wa kawaida mno, alipanda ndege za kawaida na abiria wengine, alitaka kuishi huru, hakutaka kuzungukwa na watu au kuchukuliwa mtu wa tofauti.
Hayo ndiyo maisha aliyoyazoea. Ndege ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Laurence akateremka na kuanza kutoka nje ya ndege hiyo kisha kuelekea katika jumba la uwanja huo ambapo baada ya kuchukua mizgo yake, akatoka nje.
“Karibu sana bosi,” alisema Matilda ambaye alifika uwanjani hapo kumpokea.
“Asante sana.”
Wakaingia ndani ya gari na safari ya kuelekea nyumbani kuanza. Njiani, walikuwa wakizungumza mengi, kila mmoja alionekana kuwa mwenye furaha mno, hakukuwa na mtu aliyemkumbuka Evadia, kila kitu kilichopita waliamua kuachana nacho.
“Nataka nikutoe mtoko wa usiku,” alisema Laurece.
“Mimi?”
“Kwani nazungumza na nani humu garini?”
“Hahaha!”
“Au kuna shemeji naye ana ratiba ya kutoka nawe?”
“Shemeji? Kwa mapenzi haya ya kina Evadia?”
“Ndiyo! Labda kuna mtu nyuma,” alisema Laurence.
“Hakuna mtu bosi.”
“Kwa hiyo itawezekana?”
“Itawezekana, wala usijali.”
Usiku Matilda alionekana kuwa na mawazo, moyo wake uliwaza mambo mengi ila kubwa zaidi ni kuhusu hicho alichotaka kuzungumza Laurence.
Hakukuwa na alichojifikiria zaidi ya mapenzi, hakuamini masikio yake kwamba bosi wake ambaye kila siku alimfanyia kazi kwa kujitolea leo hii alitaka kuzungumza naye, tena katika sehemu ambayo wangekuwa wawili tu.
Mara baada ya kujiandaa, Matilda akatoka chumbani kwake na kwenda katika sehemu ya maegesho ya magari na kuchukua gari lake kisha kuanza safari ya kuelekea huko alipopanga kuonana na Laurence kwani tayari muda ulitimia.
Njiani, mawazo hayakumtoka, alijua fika kwamba kile ambacho kingekwenda kutokea huko kilikuwa ni mapenzi tu. Kama ingekuwa hivyo, kwake ilikuwa ni bahati kubwa, kuwa na mwanaume kama Laurence, mwanaume mwenye sura nzuri na fedha nyingi, kwake ilitosha kumkubalia.
Mbali na hivyo, moyo wake kwa kipindi kirefu ulikuwa kwenye mapenzi juu ya mwanaume huyo ila kitu ambacho hakutaka kukiweka wazi ni juu ya jinsi alivyompenda.
Kitendo cha Laurence kumng’ang’ania Evadia kipindi cha nyuma ilimuuma sana lakini hakuwa na jinsi, alikubali kuumia kwani hakutaka kumwambia ukweli bosi huyo kwa kisingizio cha kuogopa ila mwisho wa siku, leo hii aliambiwa kwamba walitakiwa kuonana sehemu wawili na kuzungumza.
“Karibu sana mrembo,” alisema Laurence, alikuwa akimkaribisha Matilda mara baada ya kuwasili, hakuamini kama yeye ndiye aliyeitwa mrembo na Laurence.
“Asante sana.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Laurence akabaki akimwangalia Matilda, siku hiyo, msichana huyo alipendeza mno, kila alipomwangalia, hakuisha hamu. Kichwa chake kikaanza kujifikiria juu ya msichana huyo kama ilikuwa sahihi kuwa naye au la, jibu pekee lililokuja kichwani mwake ni kwamba alistahili kuwa mke wake.
Hakujua mapokeo ya maneno yake yangekuwa vipi, hakujua kama angekubaliwa na msichana huyo au angekataliwa. Hakutaka kuangalia fedha zake, hakutaka kuzipa nafasi, kwake, aliamini kwamba msichana angeweza kumkataa hata kama alikuwa na fedha.
Kabla ya kuanza mazungumzo akamuita mhudumu na kuagiza vinywaji. Hakuwa mnywaji wa pombe, hivyo akaagiza juisi ambapo baada ya dakika chache mhudumu huyo akawaletea.
“Matilda, kuna haja ya kuanza kukudanganyadanganya?” aliuliza Laurence huku akichia tabasamu pana.
“Kunidanganyadanganya?”
“Kuna haja hiyo?”
“Kivipi?”
“Najua unajua nimekuitia nini mahali hapa, sidhani kama nitatakiwa kuzungumza sana mpaka kutoka nje ya kile nilichopanga kukwambia usiku wa leo,” alisema Laurence, alionekana kutokuwa na wasiwasi kabisa. Kila alipoongea, alishushia na juisi.
“Sijajua umeniitia nini?”
“Matilda. Nimejikuta nikiwa kwenye hali ambayo sikuitarajia kabla, sikupanga kukwambia hili katika maisha yangu lakini nimejikuta sina jinsi ni lazima nikwambie ili niwe na amani,” alisema Laurence kwa sauti ya chini yenye kumaanisha alichokuwa akikisema.
“Unataka kuniambia nini?”
“Jinsi ninavyokupenda na jinsi ninavyotaka wewe uwe mke wangu wa ndoa,” alisema Laurence.
“Niwe mke wako wa ndoa?” aliuliza Matilda huku akijifanya kushtuka.
“Ndiyo!” alijibu Laurence kwa kujiamini.
“Mimi?”
“Ndiyo! Wewe!”
“Hapana! Haiwezekani,” alisema Matilda.
“Kwa nini?”
“Sitaki tu.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Sijisikii kuwa na mwanaume, na sidhani kama nitataka kuolewa, siwezi kuwa nawe bosi,” alisema Matilda, kwa kumwangalia usoni alionekana kumaanisha lakini ukweli kutoka moyoni mwake, alitingisha kiberiti.
Kazi kubwa ikawa kwa Laurence, hakuamini kile alichokisikia kwamba msichana huyo aliyekuwa akimpenda hakuwa akitaka kuwa naye. Moyo wake ukaanza kupatwa na maumivu kama yale aliyoyapata kipindi alichokataliwa na Evadia.
Alijiona akiwa na mkosi mkubwa. Alijaribu kumwangalia Matilda kwa macho ya kuonewa huruma lakini msimamo wa msichana yule ulikuwa huohuo kwamba hakutaka kuwa na Laurence, yaani hakutaka kuwa mkewe.
Fedha hazikusaidia, Matilda alionekana kuwa msichana mwenye msimamo mkubwa, alijua fika kwamba mwanaume aliyekuwa mbele yake alikuwa na fedha lakini hiyo haikuwa sababu ya kujirahisisha namna hiyo.
Alichokifanya ili kumuonyesha Laurence kwamba hakufurahishwa na kile alichoambiwa, hapohapo akasimama na kuanza kuondoka bila kuaga. Laurence hakukubali, alitokea kumpenda Matilda, alichokifanya ni kusimama na kuanza kumfuata, alipomkaribia akamshika mkono na kumwangalia usoni.
“Matilda, pleaseee…nakupenda,” alisema Laurence huku akimwangalia msichana huyo usoni.
“Laurence, naomba uniachie…”
“Tatizo nini Matilda?”
“Sikupendi!”
“Umesema?”
“Sikupendi…sikupendi….” alisema Matilda, hapohapo akaendelea na safari yake mpaka garini.
Laurence alichanganyikiwa, hakuamini kile alichoambiwa, akamfuata Matilda mpaka lilipokuwa gari lake na kusimama mbele, hakutaka Matilda aondoke, pale mbele, akapiga magoti na kumuomba msichana huyo ateremke na kuzungumza naye lakini Matilda hakuteremka zaidi ya kupiga honi akitaka apishwe ili aondoke. Watu waliokuwa pembeni wakabaki wakiwaangalia tu.
Laurence alikuwa tayari kwa kila kitu, kama kugongwa na gari hilo, alikuwa tayari lakini si kutaka kumuona Matilda akiondoka mahali hapo. Watu wengine waliokuwa katika mgahawa ule wakatoka nje na kumwangalia vizuri Laurence, -hawakumfahamu, wao walimuona mwanaume fulani ambaye alipiga magoti mbele ya gari ambalo ndani yake alikuwepo mwanamke kisha kumuomba kuteremka kutoka garini.
Matilda hakuacha kupiga honi, aliendelea kumsisitizia Laurence atoke mahali pale ili aondoke lakini mwanaume huyo hakuweza kuondoka pale alipokuwa amepiga magoti.
“Kuna nini dada?” aliuliza mwanaume mmoja, hakuwa akijua kinachoendelea.
“Nataka huyo mwanaume aondoke hapo mbele,” alijibu Matilda.
“Nani? Huyu?”
“Ndiyo!”
“Una mawe?”
“Shilingi ngapi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hata buku tano, naweza kumtoa peke yangu,” alisema jamaa huyo, hapohapo Matilda akachukua pochi yake na kutoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi huku akitaka abaki na chenji.
Jamaa huyo, ili kuonekana kwamba alikuwa na nguvu, akaelekea mbele ya gari na kusimama mbele ya Laurence, hakuwa akijua kwamba huyo ndiye alikuwa yule bilionea mkubwa nchini Tanzania, alichokifanya ni kumnyanyua mzobemzobe kumpeleka pembeni kabisa.
“Tulia hapa wewe…” alisema jamaa yule, Matilda akawasha gari na kuondoka mahali hapo.
Moyo wa Laurence uliumia mno, hakuamini kile kilichotokea, kipindi cha nyuma alifikiri kazi ingekuwa nyepesi sana lakini baada ya kuianza, akagundua kwamba ilikuwa ngumu mno.
Hakuzungumza kitu chochote kile, alichokifanya ni kuondoka kulifuata gari lake huku kila mtu akimwangalia, wengi walimuonea huruma. Alipolifikia gari lake, kila mtu akashtuka, akashangaa ni kwa jinsi gani msichana yule alimkataa mwanaume huyo aliyekuwa na gari la kifahari ambalo lilionyesha ni jinsi gani alikuwa na fedha.
Hakuliwasha gari hilo, alipandisha kioo, akaegemea usukani kisha kuanza kufikiria kwa kina, machozi yalimtoka, yaani kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, wakati mwingine alihisi kwamba alikuwa ndotoni.
“Matilda, why are you doing this to me?” (Matilda, kwa nini unanifanyia hivi?) aliuliza.
“I want nobody than you,” (Simhitaji yeyote zaidi yako) alisema Laurence na kisha kuondoka mahali hapo.
Njia nzima alikuwa mtu wa kulia tu, bado hakuamini kilichokuwa kikiendelea, aliendesha gari kwa umakini mkubwa kwani pasipo kufanya hivyo angeweza kupata ajali kutokana na kichwa chake kuwa na mawazo lukuki.
Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani kwake, akateremka na kisha kuingia ndani. Safari yake ikaishia kitandani, alijilaza, usingizi haukumjia, alibaki macho huku akiendelea kuwa kwenye mawazo lukuki.
Kwa kipindi kifupi, penzi la Matilda likaanza kumburuza, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake, Matilda yuleyule, msichana aliyekuwa akimchukulia kawaida, leo hii ndiye huyohuyo ambaye alimfanya kuteseka moyoni mwake.
Aliendelea kuwa macho mpaka ilipofika majira ya saa saba usiku, hakutaka kukubali, alichokifanya ni kumpigia simu msichana huyo, simu ikaanza kuita, iliita na kuita lakini haikupokelewa.
Moyoni aliumia ila hakuwa na jinsi, aliendelea kupiga zaidi, matokeo yalikuwa yaleyale kwamba simu haikupokelewa. Moyo wake ukachoka, alichokifanya ni kujaribu kwa mara ya mwisho, hakutaka kujiuliza, akapiga tena, majibu yakawa tofauti na mwanzo, mara hii, simu haikupatikana kabisa, ilikuwa imezimwa. Maumivu aliyoyasikia moyoni hayakuelezeka.
Hakutaka kujirahisisha, alichokuwa akitaka kumuonyeshea Laurence kipindi hicho ni kwa jinsi gani alikuwa msichana asiyebabaikia fedha, alimpenda sana mwanaume huyo lakini hiyo haikuwa sababu ya kumkubali kwa haraka sana.
Alipoondoka kwenye ule mgahawa, alijifanya kuchukia lakini ukweli wa moyo wake ulikuwa na faraja tele, hakuamini kilichokuwa kikiendelea kwamba bilionea yule aliyekuwa akifanya kazi kwake, leo hii alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.
Alipofika nyumbani, Matilda akaelekea chumbani kwake na kukifuata kioo alichokibandika ukutani na kuanza kujitazama. Alijitazama kuanzia chini mpaka juu kisha akarudia kujitazama tena, alitaka kuona kama alibadilika na kuwa mzuri zaidi ya kipindi kilichopita, alipojiangalia na kujichunguza, akagundua kwamba alikuwa vilevile.
“Sasa kanipendea nini?” alijiuliza.
“Au hakuwa anamaanisha alichoniambia? Mmmh! Kweli Laurence anipende mimi? Au ananitega?” alijiuliza lakini akakosa jibu.
Akaelekea kitandani na kutulia, mawazo yake juu ya Laurence hayakumtoka, aliendelea kumfikiria mwanaume huyo. Kila kilichoendelea katika maisha yake juu ya Laurence hakuwa akimaanisha, wakati mwingine alikuwa akijiuliza kama mwanaume huyo angechukulia kila kitu kuwa kweli, asingeamua kuachana naye?
Hilo lilimuogopesha lakini hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kupiga moyo konde, ilikuwa ni lazima kumuonyeshea Laurence kwamba alikuwa miongoni mwa wanawake wasiompenda mtu kwa kuwa tu alikuwa na fedha.
Baada ya kupita saa mbili, Matilda akasikia simu yake ikianza kuita, alijua fika kwamba mtu aliyekuwa akipiga muda huo alikuwa Laurence kwani hakukuwa na mazoea ya kupigiwa simu katika usiku mkali kama ilivyokuwa.
Alichokifanya ni kuichukua na kuangalia kioo cha simu yake, jina la ‘Boss’ lilionekana vilivyo kwenye simu ile. Akaanza kujifikiria kama alitakiwa kupokea au la, alikaa huku akiiangalia simu ile ilivyokuwa ikiita, hakupokea, akaamua kuachana naye kwa kuitupa pembeni.
Hiyo haikuwa mwisho, mpigaji ambaye alikuwa Laurence akapiga tena lakini Matilda alifanya vilevile, hakuipokea simu ile. Simu ilipokata kwa mara ya pili, alichokifanya ni kuizima kabisa kisha kujilaza huku akiwa na mawazo tele juu ya mwanaume huyo. Alichojua ni kwamba ilikuwa ni lazima Laurence amtafute siku inayofuata.
Dickson alimaanisha aliposema kwamba alihitaji ndoa tu kwa msichana Evadia. Hakutaka kumuona msichana huyo akiondoka mikononi mwake kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Alimrudia na kumuomba msamaha, kweli alisamehewa na hivyo mapenzi kurudi kama zamani. Muda mwingi msichana huyo alionekana kuwa na mawazo, hakuwa na furaha kama kipindi cha nyuma kitu kilichomfanya Dickson kuhisi kwamba bado Evadia alikuwa na wasiwasi naye.
Huo haukuwa ukweli wenyewe, msichana huyo alikuwa na mawazo tele kwa kuwa tu bado alimfikiria Laurence na utajiri mkubwa aliokuwa nao ambao aliamini kwamba endapo angekuwa wake, basi ule utajiri wote naye angekuwa anahusika nao.
Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali lakini hicho hakikuwa kipindi cha kujuta tena, kama ni bahati aliichezea hivyo kuendelea mbele na maisha yake kama kawaida.
Siku zikakatika, wazazi wa pande zote mbili wakakubaliana kwamba harusi ifanyike baada ya mwezi mmoja, maandalizi yakaanza kufanyika huku ndugu, jamaa na marafiki wakiambiwa wajiandae kusherehekea harusi hiyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ukaribu wao ukaongezeka zaidi, mapenzi yao yakapamba moto zaidi. Maandalizi kabambe yaliendelea na michango kuanza kukusanywa kutoka kwa watu mbalimbali.
“Nitamshukuru Mungu utakapoolewa binti yangu, ni faraja kwa mzazi kuona harusi ya mtoto wake,” alisema mama Evadia, alikuwa akimwambia binti yake.
“Ninamshukuru Mungu kwa kila kitu.”
“Ila mbona unaonekana hauna furaha, tatizo nini?” aliuliza mama Evadia.
“Laurence mama!”
“Binti yangu, kilichotokea achana nacho na usonge mbele na mambo mengine, kama ni bahati, si wewe tu bali hata mimi niliichezea, Mungu anapoamua kufunga mlango mmoja, jua kuna mwingine unafunguka. Huwezi jua, inawezekana Mungu hajataka uolewe na Laurence kwa kuwa kuna siku ungepanda ndege kwenda Marekani, ndege ingepata ajali na kufariki,” alisema mama Evadia.
“Inawezekana mama?”
“Ndiyo binti yangu! Mshukuru Mungu kwa kila kitu.”
Walifarijiana usiku kucha, mioyo yao iliumia sana, kila waliposoma kwenye magazeti juu ya utajiri aliokuwa nao Laurence maumivu yakaongezeka mioyoni mwao.
Baada ya siku tatu, Evadia akapokea bahasha iliyokuwa na karatasi ndani. Ililetwa na mwanaume mmoja aliyevalia nadhifu sana, alipofika nyumbani hapo akaomba kuonana na msichana huyo, akatoka nje.
“Karibu,” alimkaribisha.
“Asante sana. Mimi si mkaaji, nimekuletea mzigo wako huu,” alisema mwanaume huyo huku akimkabidhi bahasha ile.
“Kutoka wapi?”
“Imeandikwa hapo juu,” alijibu. Evadia alipoisoma, alikuta imeandikwa jina la Laurence.
Moyo wake ukapiga paaa. Akataka kuifungua lakini yule mwanaume alimwambia kwamba alitakiwa kusaini karatasi maalum ili aondoke zake, Evadia akapewa karatasi ambayo alisaini na kisha kuingia ndani.
Moyo wake ulikuwa kwenye presha kubwa, alitaka kuona mule ndani kulikuwa na kitu gani, wakati mwingine alifikiri kwamba ilikuwa barua ambayo ilimtaka kuweka mambo sawa ili warudiane na kuwa kama zamani.
Breki ya kwanza ikawa chumbani kwake, alikuwa kwenye presha kubwa, akaifungua, alichokutana nacho humo ni cheki ya shilingi milioni hamsini iliyosainiwa huku ikiwa imeambatanishwa na maneno machache yaliyosomeka ‘Uwe na harusi njema, huo ni mchango wetu, mimi na mchumba wangu, Matilda. Tutakuwa nanyi bega kwa bega kwa kila kitu’
Evadia akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumbubujika machoni mwake, hakuamini kile alichokisoma, mwanaume yule aliyekuwa amemfanyia mambo mabaya, leo hii alitoa mchango wa kiasi kikubwa kwenye harusi yake.
Hakuamini, pamoja na mchango huo, kitu kilichomshtua ni kwamba Laurence na Matilda walikuwa wachumba, yaani msichana yuleyule ambaye kila siku alitumiwa na Laurence ndiye hatimaye alibahatika kuwa mchumba wa Laurence.
Moyo wake ukawaka moto mkali wa wivu, aliumia kupita kawaida. Akajilaza kitandani, majuto moyoni mwake kamwe hayakupungua, yaliendelea kuwa vilevile mpaka mama yake aliporudi na kumuhadithia kilichokuwa kimetokea.
Asubuhi ilipofika, mtu wa kwanza kabisa kupiga simu yake alikuwa Laurence, kama kawaida yake akaipuuzia simu ile, iliita mpaka pale ilipokata. Moyo wake ulimuuma na kujuta alichokuwa akikifanya lakini hakuwa na jinsi, alitaka kuonyesha msimamo wake kwa Laurence kwamba hakuwa mtu wa kubabaikia fedha.
Muda ulizidi kwenda mbele, kwa sababu ilikuwa ni katikati ya wiki, akainuka na kwenda bafuni kuoga kisha kujiandaa kwa ajili ya kuelekea kazini. Kwa kumwangalia tu Evadia alionyesha kutokuwa na furaha kabisa, alionekana kuwa na mawazo tele mpaka baadhi ya wafanyakazi wenzake kumshangaa.
Ilipofika saa sita, muda ambao wafanyakazi wote katika ofisi ya Laurence walikuwemo, tena wakiwa bize ile mbaya, Laurence akaagiza wafanyakazi wabaki ofisini humo kwani kulikuwa na kitu cha muhimu alichotaka kukifanya.
Kila mmoja akatulia, minong’ono ikaanza kusikika kila kona, kila mmoja alianza kuhoji ni kitu gani ambacho bosi wao alitaka kukifanya siku hiyo. Wengi wakahisi kwamba kungekuwa na wafanyakazi ambao wangefukuzwa kazi lakini kila walipokumbuka namna ambavyo Laurence alivyokuwa mpole na kuwajali wafanyakazi wake, wazo hilo likaondoka vichwani mwao.
Evadia alionekana kuwa na wasiwasi zaidi, alichoamini ni kwamba Laurence alikasirika na hivyo angeweka wazi uamuzi wa kumfukuza kazi au kumpumzisha kwa sababu tu alimkataa.
Alipofikiria hivyo, Evadia akaanza kujuta, akatamani usiku wa jana urudi nyuma ili arekebishe kila kitu, amkubalie Laurence na mambo mengine kuendelea.
Ilipofika saa sita mchana, saa moja kabla ya kupata chakula cha mchana, watu kutoka katika kampuni ya kuandaa vyakula ya Mama G Delicious Food wakafika ofisini hapo, wakapanga meza zao na kuwafanya wafanyakazi wote kushangaa kilichokuwa kikiendelea.
“Vipi tena?” aliuliza jamaa mmoja, kila mtu humo ofisini alikuwa nadhifu, kuchomekea na kufunga tai ilionekana kama sheria.
“Hata mimi nashangaa….kwani leo sikukuu?”
“Hapana!”
“Sasa mbona msosi? Au bosi ameshinda bingo?” aliuliza jamaa huyo.
“Mmmh! Sijui.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya dakika chache, Laurence akatokea mahali hapo. Wafanyakazi wote wakaanza kupiga makofi kwa furaha, kila wakati bosi huyo alionekana mtu mwenye furaha ila kwa siku hiyo, alionekana kuwa na furaha zaidi ya siku zote.
“Nimefurahi sana kuwa nanyi katika kampuni hii, mmekuwa watu wa tofauti ambao kila siku mmekuwa mkinisapoti katika kila hatua na ili kuonyesha malipo yangu kwenu, nimefanya vile ambavyo ilikuwa ni lazima niwafanyie kama kuwanunulia magari na hata kuanza ujenzi wa nyumba zenu,” alisema Laurence, kila mmoja alikuwa kimya. Akaendelea:
Utajiri wangu umeongezeka, nimefungua kampuni nyingi, nina wafanyakazi wengi ila katika kila hatua, ninarudia kusema kwamba ninawashukuru sana kwa yote mlionifanyia na leo hii kuwa Laurence huyu mnayemuona,” alisema na kuendelea.
“Ninataka kuoa….” alisema.
Aliposema maneno hayo tu, minong’ono ikaanza kusikika ofisini humo, kila mmoja alishtuka kwani hilo lilikuwa jambo geni ambalo wala halikuwa na tetesi zozote zile hapo kabla kitu kilichowafanya wafanyakazi kushangaa, ilikuwaje tetesi za bosi wao kutaka kuoa zisijulikane kabla, maswali yakawajaa.
Kwa Matilda, alionekana kuwa na presha kubwa, hakuamini kile alichokisikia kwamba Laurence alitaka kuoa. Alichohisi ni kwamba baada ya kumkatalia, mwanaume huyo aliamua kutafuta mwanamke mwingine kwa ajili ya kumuoa na kuachana naye, hivyo akajuta zaidi.
“Ninayetaka kumuoa ni mmoja wa watu miongoni mwenu,” alisema Laurence, kilichofuata si minong’ono bali wanaume kuanza kuuliza alikuwa nani.
“Au Magreth….Au Frida…..Au Amanda….” kila mmoja alisikika akilisema lake.
Alichokifanya Laurence ni kurudi ofisini kwake, huku nyuma aliacha minong’ono mingi, aliporudi tena, mkononi alikuwa na maua kadhaa, alipiga hatua taratibu na kusogea kule alipokuwa Matilda, hakutaka kuzungumza lolote, watu wote ofisini walikuwa kimya wakimwangalia tu. Laurence alipomkaribia, akapiga magoti mbele ya Matilda na kuwafanya watu wote kushtuka.
“Matilda, wewe ni msichana wa tofauti sana kwangu, nilijaribu kukwambia ukweli kwamba ninakupenda lakini haukunielewa. Leo, nipo tayari kusema hivyo mbele ya watu wengi, ili wawe mashahidi wa kile ninachokizungumza, wawe mashahidi wazuri wa moyo wangu, ninakupenda. Will you marry me?” alisema Laurence huku akimwangalia Matilda usoni, maua yaliwekwa chini, mkononi alikuwa na pete.
Matilda akaanza kububujikwa na machozi, hakuamini alichokuwa akikiona.
“Will you?” aliuliza.
Watu wote wakataka kusikia jibu kutoka kwa Matilda, wote wakabaki kimya wakimwangalia msichana huyo aliyekuwa akibubujikwa na machozi. Hakujibu kitu zaidi ya kumsogelea Laurence, akamuinua na kumkumbatia, watu wote wakapiga makofi na vigelegele vya shangwe, hatimaye msichana Matilda akakubali kuolewa na Laurence.
“Nitakupenda milele,” alisema Laurence.
“Nitakupenda pia,” alisema Matilda, kilichofuata ni kumwagiana mabusu mfululizo.
Watu walikusanyika ndani ya Kanisa la Ukombozi lililokuwa Mbezi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushuhudia harusi kati ya kijana Dickson na Evadia ambao walitarajiwa kufunga ndoa dakika chache zijazo.
Kila mtu aliyekuwa kanisa humo alikuwa na furaha mno, watu hao ambao walikuwa pamoja kwa kipindi kirefu, leo hii walikuwa wamefikia hatua ya kufunga ndoa na kuishi pamoja kama mke na mume.
Miongoni mwa wahudhuriaji katika harusi hiyo alikuwepo Laurence na mchumba wake, Matilda. Muda wote nyuso zao zilikuwa na furaha tele, walimpenda Evadia, walikumbuka maisha aliyopitia na mama yake, yalikuwa na umasikini mkubwa na ndiyo maana waliamua kwa moyo mmoja kumsaidia yeyey na mama yake.
Mara baada ya maharusi kuingia kanisani, hatimaye Dickson na Evadia wakawa mume na mke huku kukifuatiwa na sherehe kubwa usiku katika Ukumbi wa Hoteli ya Traveltine iliyokuwa Magomeni jijini Dar.
“Hongereni sana,” alisema Matilda huku akimpa mkono Evadia na mumewe, Dickson.
“Asanteni pia, asanteni kwa kuwa pamoja nasi,” alisema Evadia huku akiwakumbatia Laurence na mchumba wake.
Hiyo ilikuwa harusi ya kwanza, baada ya miezi miwili, hatimaye Laurence na Matilda wakafunga ndoa katika Kanisa la Roman Catholic lililopo Mwenge jijini Dar.
Watu wengi walihudhuria harusi hiyo, mabilionea wakubwa, waandishi wa habari, makamu rais na wengine wengi. Baada ya harusi hiyo kufungwa, sherehe kubwa ikafanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena na baada ya hapo fungate kwenda kufanyika nchini Marekani katika Visiwa vya Hawaii.
“Hatimaye nimekuoa,” alisema Laurence.
“Siamini kama miaka yote hiyo nilikuwa nafanya kazi kwa mume wangu!” alisema Matilda huku akimwangalia mume wake usoni.
“Kumbe na mimi niliajiri mwanamke ambaye baadaye angekuja na kuwa mke wangu! Ni bahati iliytoje!” alisema Laurence.
Walikaa nchini Marekani kwa muda wa mwezi mzima huku mchakato kamili wa kutafuta mtoto ukianzia nchini humo. Maisha yalibadilika, kila mtu akaonekana kuwa na furaha, hakukuwa na ugomvi, waliishi kwa amani, magazeti na vyombo mbalimbali vya habari vilimtangaza sana Laurence hasa mara baada ya kufanikiwa kuwa Bilionea Kijana ndani ya mwaka mmoja.
Huo ukawa na muendelezo wa mafanikio yake. Katika kila hatua aliyokuwa akipiga, mkewe alikuwa pamoja naye.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**MWISHO WA HADITHI**
Toa Maoni yako Kuhusu Hadithi hii.
Stori hii inatufundisha usimdharau mtu usiyemjua,hata kama ni maskini wa kutupa inatupasa tuwe na upendo wa dhati kwao.Lakin pia tusiwe ni wepesi wa kuvunja ahadi tunazoziweka kwa watu wetu wa karibu
ReplyDelete