IMEANDIKWA NA : BULIBA MAGAMBO
*********************************************************************************
Simulizi : Chunga Saana Laazizi Wangu
*********************************************************************************
Simulizi : Chunga Saana Laazizi Wangu
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ni msichana mzuri siyo mwembamba siyo mnene,siyo mweupe na wala siyo mweusi.Mwenye kila sifa ya kuitwa mrembo.Alionekana akiwa na haraka kuelekea kituoni kupanda gari.Baada ya dakika chache aliwasiri kituoni.Akiwa kituoni anapepesa huku na kule kuangalia gari lenye kumfaa katika safari yake,ghafla alipigwa kikumbo na na kudondokea kwenye mtaro uliokuwa pembeni.Aliloa kwa maji machafu ya mtaroni.Watu walimzunguka kuangalia kulikoni.
Alijiangalia huku na kule katika mwili wake,ndipo aligundua amekwishachafuka kuanzia miguuni mpaka kiunoni kutokana na maji taka yaliyopita kwenye mtaro huo.Akiwa amekunja sura huku mdomo kauchongoa,alimtupia jicho yule aliyempiga kikumbo.Alitoka ndani yam taro kwa kushikwa mkono na wasamalia wema walioshuhudia tukio.Baada ya kutolewa mdani ya mtaro kwa kasi ya ajabu alimfuata kijana huyo aliyempiga kikumbo.
Kwa muda wote huo kijana huyo hakuwa na lakfanya.Alibaki akiangalia tukio zima. “Alipe faini huyo! Haiwezekani akuchafue !”Ni sauti za fujo kutoka kwa madereva wa Bodaboda waliokuwa wameegesha pikipiki zao kusubiri wateja.Kijana mdomo ulikuwa mzito kama uliobugia nyama kila mbili,miguu ilimuisha nguvu huku fikra zikiwa mbali kwani haikuwa dhamira yake kumkumba msichana huyo.Alibaki amesimama akisubiri kumuomba msamaha.
Kabla hajanyanyua kinywa chake kuomba radhi, alipigwa kibao shavu la kulia na msichana huyo. “Uwaa huyo!Piga tenaa..!Tenaa..!” Ni sauti za fujokutoka kwa watazamaji walioangalia filamu ya bure.Aliongezwa kibao kingine shavu la kushoto kiasi cha sauti kali kusikika “Paaa!”.Kijana alisimama imara pasi na kukwepa huku akimuangalia msichana huyo bila ya kupepesa macho kwa takribani sekunde kumi.Alijishika shavu la kulia na kujipapasa kwa takribani sekunde tano kisha aliondoka bila ya kusema chochote. “Yaani wewe fala umeniharibia siku yangu leo..!”Maneno ya kashfa yalimtoka msichana huyo huku akifyonya kila baada ya sekunde mbili.Alitukana kila tusi linalokuja mdomoni ilimradi kupunguza jazba yake.Kijana hakujibu chochote zaidi ya kuendelea na safari yake.
Watu walimpa pole msichana huyo huku wengine wakijaribu kumfuta tope lililomjaa kuanzia miguuni mpaka kounoni.”Jamani pole mwaya! Yaani huyo mkaka inabidi apigwe sana sema basi tu.”Ni maneno yaliyotoka kwa baadhi ya akinamama waliokuwa wanampa faraja.Alilazimika kurudi alikotoka kwani akili yake haikmuwezesha kupambambanua mambo kwa wakati huo.Alirudi mpaka chumbani kwake mtaa wa Madafu maeneo ya Mtongani. “Huyu mjinga anabahati hajanikuta na kichaa changu angekoma.Daah….!Ningemchafua na yeye” Aliongea kwa hasira huku akizivua nguo zake zilizoloa kwa maji taka.Baada ya kubadili mavazi,aliziloweka nguo zile zilizochakaa kwenye maji yaliyokuwa kwenye beseni kisha alichukua ndoo ya maji na kwenda kujimwagia.
Chumbani mwake alikuwa amejitosheleza kwa kila kitu cha muhimu kilichohitajika.Meza kubwa ya kujisomea,viti viwili vya plastiki,Kitanda cha tano kwa sita kilichotandikwa kwa shuka la kijivu lenye maua sehemu mbalimbali huku uwa kubwa lenye kupendeza likiwa katikati pamoja na mito miwili ya rangi ya pinki.Pembeni kulikuwa na ndoo tatu za maji,jiko la gesi,friji,gunia la unga wa ngano na sembe,sufuria na sahani zilizopangwa vizuri.Baada ya kutoka kuoga,alijilaza chali kitandani.Alivuta pumzi na kupumua kwa nguvu kasha baada ya muda kidogo aliinuka na kulisogelea friji.Alifungua na kuchukua chupa lililojaa maji baridi na hapo aliishika vyema glasi ya kioo safi na kumimina maji kasha alikunywa kama glasi mbili na kurudi kitandani.
Alichukua simu yake ya mkononi na kupiga. “Ndio bwana kuna jitu limeniharibia ratiba zangu! Yaaah!....Siwezi kuja tena mpaka kesho shosti wangu…Aaa! Usijali nitakuelezea nikija. Haya!...Sawa…!” Alisikika akiongea baada ya kupokelewa simu hiyo.Aliwapigia rafiki zake mbalimbali kuwajuza kuwa asingeweza kufika kutokana na dharura iliyomkumba.
Kesho yake asubuhi na mapema mida ya saa mbili asubihi,msichana huyo alionekana akishuka dalala kituoni kisha alivuka na kuelekea upande wa pili na kulisogelea geti kubwa lililoandikwa kwa maandishi yalisomeka “DAR ES SALAAM UNIVERSITY COLLEGE OF EDUCATION{DUCE}.Baada ya kuingia ndani ya geti hilo,alikutana na rafiki yake kipenzi Sakina.Sakina alikuwa mrefu wa wastani,mwemba kidogo na mwenye mwanya uliokaa vyema kwenye meno yake ya mbele.Sakina alikuwa mchangamfu na mwenye kuongea sana kiasi cha kuonhea maneno hamsini ndani ya dakika tatu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alikuwa anasoma mwaka wapili chuo hapo akichukua shahada ya ualimu wa masomo ya Hisabati na Fizikia. “Heee! Salma vipi hali shosti wangu?”Sakina aliongea kwa tabasamu pana huku akimkumbatia msichana huyo alijulikana kwa jina la Salma. “Hali yangu nzuri shosti nimekumisi tu” Salma alikibu.Urafiki kati ya Sakina na Salma ulianza siku tatu zilizopita tangu Salma alipowasili chuoni hapo akiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza akichukua shahada ya ualimu wa masomo ya Hisabati na Fizikia hivyo Sakina alimsaidia baadhi ya maelekezo ya usajili na ndiyo hapo urafiki wao ukaanza.
Baada ya kusalimiana,walielekea kwenye vimbweta vya kujisomea na kukaa kwa ajili ya kusubiri muda wa vipindi vyao maana ratiba yao iliwaonesha saa tatu asubuhi.Waliongea mambo mbalimbali kiasi cha Salma kumeleza mkasa uliomkuta siku ya jana. “Pole sana shosti wangu”.Sakina aliutumia muda huo kumpa ushari rafiki yake juu ya maisha ya chuo kutokana na uzoefu wa zaidi ya mwaka mmoja aliokuwa nao.
“Vijana wengi wa hapa hususani wa mwaka wa pili wasikupotezee muda,ni wahuni tu watakuchezea.Ila nakushauri uwe pamoja na kijana mmoja tu...”. “Nani huyo..!?” Salma aliuliza kwa shauku kubwa kiasi cha kumkatikiza kauli. “Vuta Subira bado sijamaliza,shosti viipi?Kuna kijana mmoja mstaarabu sana,ananidhamu,mpole,mkarimu na mwenye hekima.Isitoshe tu kwa sifa hizo bali ni mzuri sana.Naamini ukimuona utaamini ninayokuambia.” Sakina alimaliza kueleza.Alimuangalia Salma usoni kuona ameitikia vipi taarifa hizo;alikutana na tabasamu zito lililojaa usoni mwa Salma.
“Mmmh!.Shosti natamani nimuone huyo mkaka maana ulivyompambia,kama tangazo la biashara!” Aliongea kwa utani na wote waliangua kicheko cha furaha.Salma alipandwa na Shauku ya kumjua kijana huyo mwenye sifa kemkem.”Anaitwa nani shosti?” Alizidi kudadisi. “Anaitwa Tuntu.Kila mmoja hapa chuoni anamfahamu.Ni rafiki wa kila mtu.Jana alikuwepo ila leo hayupo nadhani kesho atakuwepo.”Sakina alizidi kumwagia sifa mbalimbali kijana huyo. “Sawa kesho usisahau kunionesha”Salma aliongea huku akichukua vitu vyake kuelekea darasani.
***********
Kesho yake ilikuwa siku ya ijumaa,Tuntu hakuonekana chuoni.Sakina aliamua kumuulizia kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma na Tuntu mwaka wa tatu,alikutana na jibu moja tu hata wao hawakufahamu kwanini haonekani chuoni na walimtafuta kwenye simu na kumkosa.Walijawa na wasiwasi kwanini Tuntu hakuonekana chuoni kwa takribani siku mbili.Walijipa moyo huenda jumatatu angewasili kujumuika nao.
Tuntu alikuwa kijana mrefu.Mweupe kidogo na mwenye misuli iliyotuna na kuufanya mwili wake kujengeka vyema.Muda wote alikuwa ni mtu wa kutabasamu kiasi kwamba huwezi kujua muda gani huwa anakasirika.Kila umuonapo lazima atakuwa amezungukwa na wanafunzi siyo chini ya watano akiongea nao mambo mbalimbali.Alikuwa mtu wa watu.Usijaribu kumsema vibaya maeneo ya chuoni utashambuliwa na kila mmoja kabla ya kukutana naye.Kutokuwepo shuleni kwa siku mbili mfululizo kulitokana na hali ngumu ya maisha yake iliyomlizimu kwenda kufanya kazi ndogondogo za kumuingizia kipato cha kujikimu.
Jumatatu mida ya saa nne asubuhi,Salma na Sakina wakiwa wamekaa chini ya mti maeneo ya chuoni hapo wakiongea mambo mbalimbali,ghafla waliliona kundi la wanafunzi takribani kumi na tano wakiwa wanashangiria kwa furaha huku wamemnyanyua kijana mmoja wakisema kwa sauti. “Tuntu..! Tuntu…! Tuntu amekuja….! Tuntu amekuja….!”Sakina baada ya kuzisikia sauti za vijana hao zikilitaja jina la Tuntu,alimuambia Salma wasogee. “Twende..Twende…!Tuntu ndio yule,sinilikuambia! Unaona anavyopendwa!?”Sakina aliongea huku akimshika mkono rafiki yake na kuelekea lilipokuwa kundi la vijana hao.
Baada ya kulifikia kundi hilo,Sakini alimuonesha Salma Tuntu ni yupi kati ya wale vijana kwa kumnyoshea kidole.Salma alimsogelea Tuntu na kuuliza kwa hasira “Huyu ndiyo Tuntu…!? Ndio yeye…!?”Vijana wote walikaa kimya wakimuangalia Salma aliyekuwa mgeni machoni mwao.Wakiwa katika hali hiyo ya sitofahamu,Salma alimpiga kibao shavu la kulia.Watu walishangaa sana kuona kitendo hicho akifanyiwa Tuntu aliyeheshimika na asilimia kubwa ya wanafunzi chuoni hapo.Salma alitaka kumuongeza kingine,mara hii Tuntu aliudaka mkono wake.
“Uliandikiwa kunipiga mara tatu tu katika maisha yako,hutanipiga tena.” Tuntu aliongea kwa sauti ya utulivu isiyo na uoga wowote kisha aliushusha mkono wa Salma taratibu.Baada ya kuushusha,aliondoka kuelekea darasani na kundi lote la wale vijana lilimfuata nyuma......
Salma alibaki mdomo wazi;alimuangalia Tuntu bila ya kummaliza.Sakina alimsogela na kumuuliza kulikoni mpaka kufikia hatua ya kumpiga Tuntu mbele ya watu.Salma alimueleza kuwa Tuntu ndiye aliyemkumba na kuangukia mtaroni siku hivyo aliapa kutomsamehe. “Uliniambia kuwa alimpiga vibao viwili,bado hujatosheka tu?” Sakina alimlaumu sana Salma kwa kitendo alichofanya siku hiyo.Salma alijiona ni mwenye makosa kiasi cha kuhitaji kumuomba radhi Tuntu ila alijiuliza ataanzaje.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naona ameingia darasani akitoka tumfuate umuombe samahani.”Sakina alimpa ushauri rafiki yake. “Hivi atanisikiliza kweli?” Salma alionesha wasiwasi wake wa kuhisi kutosamehewa. “Tuntu ni kijana wa tofauti sana lazima akusamehe.”Sakina alimpa moyo rafiki yake.
Walimsubiri mpaka mida ya saa sita mchana.Wakiwa wanaendelea na majadiliano mbalimbali,Sakina aliaangalia saa yake ambayo ilimwambia ni saa sita na dakika arubaini na tano hivyo walijongea kumuangalia Tuntu kama alikwishatoka darasani.Wakati huo Tuntu alikuwa amekwishaondoka nyumbani kwake.Alipitia geti la upande wa Mgulani karibu na JKT,hivyo hawakubahatika kumuona tena.Sakina aliomba namba ya Tuntu kwa wanafunzi wenzake na alipatiwa.Sakina na Salma waliagana na kila mmoja aliondoka nyumbani kwake.
Salma baada ya kufika nyumbani kwake,aliingia bafuni kuoga ili kupunguza joto mwilini.Baada ya kutoka kuoga,aliandaa chakula cha mchana.Muda wote wa maandalizi ya chakula alikuwa akimuwaza Tuntu tangu siku ya kwanza ya kuonana naye. “Huyu ni mtu wa aina gani !?.Anatukanwa,anapigwa lakini hafanyi chochote zaidi ya kukaa kimya?Mmhh!......” Aliwaza na kuwazua hakumpatia jibu.Baada ya kumaliza kula,alichukua kalamu na karatasi kisha aliandika ujumbe mzito sana wa kumuomba radhi Tuntu kisha aliikunja vizuri karatasi.
Kesho yake mida ya saa tano asubuhi baada ya kutoka darasani alionana na Sakina.Hakuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kuelekea alipokuwa Tuntu kumuomba msamaha.Kama ilivyokuwa kawaida yake,wakati huo Tuntu alikuwa amezungukwa na kundi la watu akiongea nao mambo mbalimbali.Sakina aliawapa mkono wa salamu kila mmoja aliyekuwepo mpaka kwa Tuntu.Ilipofika zamu ya Salma kuwapa mkono,kila mmoja alikataa kumpa mkono mpaka ilipofikia zamu ya Tuntu;watu wote walikuwa wakiangalia Tuntu atalifanyaje.Tuntu alimpa mkono huku akitabasamu kana kwamba hakijatokea chochote kati yao.Walipoona Tuntu kampa mkono nao waliinuka na kumfuata Salma kumpa mkono.Salma alistaajabu sana kwa heshima aliyopewa Tuntu na wanafunzi wa chuoni hapo.
“Kama asingekupa mkono na sisi tusingekusalimia.”Alisema kijana mmoja kumuambia Salma.Salma alimkabidhi Tuntu ile karatasi.Tuntu hakuipokea ila aliashilia apewe kijana mmoja kati ya wale ndio ampe Tuntu na sio Salma.Salma alitaka kuongea kitu lakini Tuntu alimkatikiza kwa kusema.”Najua unachotaka kuongea.Nimeshakusamehe tangu siku ile ya kwanza hivyo kuwa huru.” Aliinuka na kuondoka bila ya kuaga.
“Naomba namba yako.”Salma aliongea kwa sauti kubwa kwani Tuntu alikuwa mbali kidogo.”Kaangalie kwenye ubao wa matangazo” Tuntu aliongea bila ya kuangalia nyuma.Watu walibaki wakimlaumu Salma kwa kitendo cha kukatikiza maongezi yao kwani Tuntu alikuwa kama mtandao wa “Google” .Alikuwa akiulizwa maswali ya kila aina na aliyajibu kwa ufasaha.Ndiyo maana alikuwa akizungukwa na kundi la watu muda wote.Walimuliza masuala ya maisha,siasa,afya,mahusiano,uchumi na kadhalika yote aliwajibu.
Salma alibaki ameduwaa kwa jibu alilopewa na Tuntu.”Usijali namba yake ninayo.”Sakina alimwambia Salma kwa sauti ya upole. “Naomba unipatie sasa hivi.”Salma hakutaka kuchelewesha muda,alichukua simu yake na kuandika namba ya Tuntu.Baada ya kuandika,hawakuwa na muda wa kupoteza bali walielekea kituoni kupanda gari la kuelekea nyumbani kwa Salma Mtoni mtongani.
Walitumia takribani dakika kumi na tano kutoka DUCE Chang’ombe mpaka Mtongani,kisha waliingia uchochoroni alikopanga Salma.Salma hakuwa na hamu ya kupika,aliamua kununua sahani mbili za chipsi na kuingia nazo ndani kwa ajili ya chakula cha mchana wa siku hiyo yeye na rafiki yake Sakina.
“Shosti Tuntu ni Mzuri sana,ni Handsome!”Salma aliongea kwa furaha huku akiendelea kula.”Umeamini maneno yangu niliyokuambia?Kila binti chuoni lazima amkubali.”Sakina alinogesha maongezi. “Lazima leo nimpigie usiku kumuomba radhi zaidi.”Alikunywa fundo moja la soda kisha aliendelea na maongezi.”Girlfriend wake amepata mwanaume maana siyo uzuri ni kufuru”Salma alizidi kumsifu Tuntu.Waliongea mengi kuhusu Tuntu na ilipofika saa kumi jioni,Sakina aliaga na kuondoka kwao maeneo ya Vingunguti.
Usiku ulipofika Salma alijiunga kifurushi cha chuo rasmi kwa ajili ya kuongea na Tuntu.Ilikuwa mida ya saa nne usiku,Salma alimpigia Tuntu kwa mara ya kwanza simu iliita kwa muda haikupokelewa,mara ya pili haikupatikana.Alitulia kwa muda wa dakika mbili akapiga tena aliambiwa inatumika.Alitulia tena kwa dakika tano akapiga haikupokelewa kwa mara ya pili.Akapiga tena akaambiwa haipatikani.Aliendelea kupiga kwa takribani mara tatu aliambiwa haipatikani. “Inamaana Tuntu kanizimia simu!?” Aliongea kwa hasira kidogo. “Mbona tabia mbaya,kama amelala si alikuwa anatumika muda mfupi tu kwanini hakupokea simu yangu?”Salma ilimuuma Sana hakupendezwa na tabia hiyo.Aliizima simu yake na kujilaza kitandani.
********
Kesho yake Salma alionana na Tuntu.”Kwanini Jana hujapokea simu yangu?” Ni swali la kwanza baada ya kusalimiana naye.”Majukumu!”Tuntu alimjibu kwa ufupi. “Hee! Tuntu mbona unajibu kwa ukali inamaana haujanisamehe?” Salma aliuliza. “Baadaye.”Tuntu hakumjibu zaidi ya neno hilo kisha aliondoka.Salma alibaki anamkodolea macho.Hakuelewa kwanini Tuntu anamfanyia hivyo wakati ameshamsamehe.Salma alihitaji kuongea na Tuntu lakini Tuntu hakuwa na muda wa kupoteza kutokana na majukumu ya kimaisha aliyokuwa nayo.
Salma aliondoka nyumbani kwake mida ya saa kumi na mbili jioni.Alifanya shughuli zake kama ilivyokawaida na baadaye usiku alimpigia tena simu Tuntu.Mara ya kwanza iliita haikupokelawa.Mara ya pili iliita kwa mud asana kiasi cha Salma kukata tamaa hatiaye Tuntu alipokea.”Poa Vipi hali yako?”Salma aliongea kwa sauti ya falagha. “Unajua unaongea nani?”Salma aliuliza.
“Ongea shida yako nimeshakufahamu kitambo.”Tuntu alijibu kwa sauti nzito.Wakati wakiwa wanaongea,kuna mtu alikuwa anampigia Salma alikuta inatumika. “Mmmh! Hata sijakuambia jina langu umenijuaje?” Salma hakuamini kama Tuntu alimfahamu. “Haina haja ya jina niambie shida yako maana unadakika mbili tu zilizobaki za kuongea na mimi usiku huu.” Tuntu aliongea kwa ukali kidogo. “Jamani hata hatujaongea vizuri?”Salma aliongea kwa kujidekeza akihisi itamfanya Tuntu abadili mawazo yake na kuongea naye usiku kucha.Baada ya dakika mbili,Tuntu alikata simu.Salma hakuamini kama kweli Tuntu angelikata simu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda mfupi simu ya Salma iliita.Kuangalia jina alikuwa ni Shedrack mpenzi wake.Alibetua mdomo ishara ya kwamba hakuhitaji kuongea naye siku hiyo.Simu iliita mpaka ikakata yenyewe.Alimuandikia meseji “Nipigie kesho kwa sasa najisomea”Kisha alifunga simu yake.Shedrack alipiga simu haikupatikana.Alichanganyikiwa,alipiga ngumi ukuta kwa hasira. “Hawezi kunifanyia hivi!Nampigia anatumika halafu mimi ananiambia anajisomea!?”Alifyonya kisha muda kidogo baadaye alijilaza kitandani.
Kwa upande wa Salma mawazo yake yalikuwa kwa Tuntu.Baada ya muda mrefu kupita,alifungua simu yake akijua Shedrack atakuwa amechoka kumtafuta.Alimpigia simu Tuntu haikupatikana kwani kwa wakati huo Tuntu aliizima simu na kufanya mambo yake.
Muda mfupi meseji iliingia kwenye simu ya Salma.Aliifungua na kukuta ni Shedrack aliyemtumia meseji hiyo.Ulikuwa ni ujumbe mzito na mrefu kiasi cha kutumia dakika kumi kuusoma.”Mpenzi wangu Salma!Naelewa kama unajua nakupenda sana kuliko kitu chochote katika hii dunia ndiyo maana unanifanyia hivi.Mateso,manyanyaso pamoja na vitimbi unavyonifanyia mimi sijali kwani moyo wangu umekwishaamua kuyabeba yote hayo kwa ajili yako.Hatakama hautaki kuongea nami siku ya leo nakuomba kesho tuonane.Salma huenda ukanikosa muda si mrefu kwani sioni haja ya kuishi kwenye dunia hii kama sina thamani mbele yako.Nakupenda sana.”Ulisema ujumbe huo.
Salma alipata wakati mgumu sana baada ya kuusoma ujumbe huo.Aliijua nafasi ya Shedrack kwenye maisha yake ila kwa wakati huo moyo wake uliaanza kuguswa na Tuntu.Tuntu alikwisha penya taratibu kwenye mishipa ya damu ya Salma. “Aaaah! Nitajua la kufanya.”Salma alisema kwa kupuuzia kisha alijilaza kitandani.
Kesho yake Shedrack alimpigia simu Salma mida ya asubuhi mapema.Alimuomba nafasi ya kuonana naye,lakini Salma alikataa kwa kutoa udhuru kemkem.Shedrack hakupenda kumkera,alimuomba kesho yake kama atakuwa na nafasi,Salma alimjibu “Nitaangalia ratiba yangu ikoje kisha nitakuambia.”
Baada ya kuongea na Shedrack,Salma alimtumia meseji Tuntu kumuomba waongee kwa kupitia meseji.Tuntu alimjibu kuwa hana muda na kumuomba amtafute baadaye mida ya saa tano kamili akichelewa hata dakika moja hatopata nafasi ya kuongea naye.Salma alikubaliana naye.Wakati wote akijibizana meseji na Tuntu,Shedrack alikuwa akituma meseji bila ya kujibiwa.Alituma meseji ya mwisho iliyosema “Umebadilika sana mpenzi wangu lakini naamini utarudi kuwa kama zamani,nakutakia kila la heri.”Baada ya kuisoma meseji hiyo,Salma alifyonya na kuifita meseji hiyo.
Usiku ulipofika mida ya saa nne na dakika hamsini na saba,Salma alikuwa makini kwa ajili ya kuisubiri saa tano kamili kwani alimjua Tuntu ni mtu wa misimamo mikali akisema hapana huwa anamaanisha kweli.Ilipofika na dakika hamsini na tisa simu yake iliita,kuangalia aliikuwa ni Shedrack aliyepiga.Salma alikasirika sana kiasi cha kutoa matusi mazito kwa Shedrack “Huyu mjinga angejua kuwa ananichefua asingepiga muda huu.”Yalimtoka maneno hayo kutokana na kubakia dakika moja ya kuimpigia Tuntu.Kutokana na muda kuwadia,Salima aliikata simu ya Shedrack na kwa haraka isiyo ya kawaida alimpigia Tuntu.
Waliongea takribani dakika kumi na tano.Kwa muda wote huo Shedrack alikuwa akimpigia Salma simu na kukuta ikitumika. Shedrack Alipiga ukuta,alitokwa machozi ya uchungu kwani mapenzi aliyonayo juu ya Salma anayajua yeye tu.Alikuwa tayari hata kuua mtu kwa ajili ya Salma.
Kwa upande wa Salma wakati huo hakuwa na mpago na Shedrack.Mpango uliokuwepo kichwani mwake alitamani sana kumfahamu kwa undani zaidi Tuntu.Simu baada ya kupokelewa,waliongea mengi huku Salma akimuuliza maswali mengi juu ya maisha yake binafi na familia. “Tuntu umeshawahi kuwa na mpenzi? Salma aliuliza.”Sipendi uniulize swali hilo tena nakata simu sasa hivi !”Tuntu hakupenda kuulizwa swali hilo hata siku moja.Ukitaka mkorofishane muulize masuala ya mahusiani ya mapenzi huwa anabadirika haraka na kuwa kama mbogo.
“Naomba unisamehe”Salma aliomba radhi. “Basi umeshaniharibia “mood” yangu leo hivyo nitafute kesho”.Tuntu alikata simu.Salma alibaki ameduwaa baada ya simu kukatwa.Alishindwa kumtafsiri Tuntu kwani alikuwa na misimamo ya ajabu kuliko vijana wengi.Aliingalia simu yake na kukuta “miss calls” kama saba kutoka kwa Shedrack.Hakuwa na hamu ya kumtafuta kwani hisia zake zilianza kuhamia kwa Tuntu.Salma alivutiwa sana na misimamo na vijitabia vya Tuntu.Alikumbuka siku ya kwanza alipomkumba na kuangukia mtaroni,alikumbuka siku ya pili alipomwambia kuwa alipangiwa kumpiga mara tatu katika maisha yake.Pia alikumbuka kauli na misimamo mbalimba ya Tuntu.
Shedrack alipiga simu tena kwa mara ya nane.Salma alipokea baada ya kukereka. “Nataka uniambie ulikuwa ukiongea nani!?”Shedrack aliongea kwa hasira ya hali ya juu. “Salma fikiria tulikotoka,ni mangapi nimekufanyia kwa moyo wangu wa dhati kabisa.Nimejitole kila kitu kwa ajili yako hivi kweli malipo yako ndio hayo!? Salma uchungu unaonipatia ni sawa na kunichoma msumari bila ya ganzi.Tumeishi kwa furaha na amani kwa muda mrefu lakini kwa sasa kunamabadiliko makubwa sana kipi kimekusibu mpenzi wangu?Nakupenda Salma!”Shedrack aliongea kwa uchungu na hisia kali sana huku machozi yakimtoka.Salma aliguswa kidogo na maneno ya Shedrack.Huruma ilimjia taratibu lakini iliondoka kila alipomkumbuka Tuntu.
Alishindwa atoe jibu gani.Alibaki kimya tu akisikiliza malalamiko ya Shedrack.”Salma….naku…nakuomba….ke..ke.. kesho.. tuonane naamini kuna jambo linalokusibu.Sio Salma yule nayemjua mimi.”Shedrack alikuwa akiongea kwa shida kutokana na uchungu aliokuwanao.”Tuonane saa ngapi?”Salma aliuliza.”Muda wowote utaokuwa na nafasi. “Shedrack alijibu. “Labda mida ya saa tisa njoo nyumbani nitakuwa nimesharudi. “Walikubaliana kukutana muda huo.Baada ya maongezi hayo Salma aliifunga simu yake na kujilaza kitandani.Aliutafuta usingizi kwa muda mrefu bila ya mafanikio na hatimae aliubahatisha baada ya dakika therathini.
Kesho yake asubuhi na mapema Salma alikutana na rafiki yake kipenzi Sakina.Waliongea mengi kiasi cha Salma kumshirikisha juu ya mawazo akiyokuwanayo. “Shosti kiukweli moyo wangu unanielekeza kwa Tuntu,nimetokea kumpenda sana nina mpango wa kumwambia,sijui unanishauri vipi.”Aliongea kwa kumaanisha alichokisema.”He heee! Wewe huyoo…! Na Shedrack umuweke wapi?Tangu lini jiwe moja likauwa ndege wawili kwa wakati mmoja..?Shosti sikushauri ila kama unanisikia…baki njia kuu mama!”Sakina alimshangaa rafiki yake na hakuwa radhi Salma amsaliti Shedrack.
“Unamaanisha nini nibaki njia kuu?”Salma alihitaji ufafanuzi zaidi.”Shosti kila king’aacho siyo dhahabu.Umekosa nini kwa Shedrack…? Sioni unachokifuata kwa Tuntu.Hana pesa,hana mbele wala nyuma maisha yake kulenga kwa manati.Halafu isitoshe umemfahamu juzi tu leo unampenda,kweli kabisaa!Usitupe mbachao kwa msala upitao.”Sakina alizidi kumpa ushauri rafiki yake.Salma alihisi dunia inamgeukia kwani aliamini Sakina angelimuunga mkono lakini sivyo alivyotegemea.Alikubaliana naye kishingo upande kisha waliendelea kuzungumza mambo mengine.
Salma alifika nyumbani kwake mida ya saa nane kamili mchana.Alibadilisha nguo zake na kuandaa chakula cha mchana.Aliandaa ndizi na nyama maarufu mtori kwasababu alijua Shedrack anapendelea chakula hicho.Mida ya saa tisa kamili Shedrack alimpigia simu na kumueleza kuwa atachelewa kidogo kwasababu ya foleni iliyokuwepo maeneo ya uhasibu kuelekea kwa Azizi Ally.Ilipofika mida ya saa tisa na nusu,Shedrack aliwasili nyumbani kwa Salma.Alishuka ndani ya gari lake aina ya HARRIER 240 ya rangi nyeusi.Alifunga vioo na kuhakikisha usalama kisha alielekea chumbani kwa Salma.Alibisha hodi na Salma alimfungulia.
Walikumbatiana kwa furaha na upendo.Baada ya kukaribishwa Shedrack alikaa kitandani.Salma alimpatia glass ya maji ya baridi ili atulize koo.Muda kidogo aliandaa chakula na kumkaribisha kwa upendo wa dhati.
Baada ya kumaliza kula walianza mazungumzo yaliyowakutanisha siku hiyo. “Naomba usinifiche mpenzi wangu hivi ni nani huwa unaongea nae usiku?”Shedrack aliuliza. “Huwa naongea na rafiki zangu tu”Salma alijibu kwa mkato.Shedrack hakulidhika na majibu ya Salma.Alimuomba simu yake na Salma alimpatia.Shedrack alifungua kwenye sehemu ya kumbukumbu ya watu waliompigia jana usiku na kuikuta namba iliyoandikwa kwa herufi kubwa “MY..”.Wivu ulianza kuitawala nafsi yake.Alichukua simu yake na kuichukua ile namba kisha alimkabidhi Salma simu yake.Salma hakujua Shedrack alifanya nini baada ya kuichukua simu yake.
“Nilijua unalala kumbe unaondoka.” Salma alijiulizisha kinafiki baada ya Shedrack kusema alihitaji kuondoka. “Yaaah! Kuna ishu bado naifuatilia ikikaa vizuri nitakuja kulala weekend.”Shedrack alijibu huku akichomoa noti za shilingi laki mbili na kumkabidhi.”Asante mpenzi wangu.”Salma alishukuru kisha alimsindikiza mpaka alipoegesha gari lake.Waliagana kwa furaha na Salma alirudi chumbani kwake akiwa na furaha ya pesa alizopewa siku hiyo.
********
“Unaongea na Shedrack hapa…!Yaaah…!”Alitulia kidogo kisha aliendelea kuongea “Brother kuna jambo naomba tuongee kama wanaume.Kuna binti mmoja anaitwa Salma…..!”Alikuwa ni Shedrack akiongea na Tuntu kwenye simu.Tuntu aliposikia jina la Salma alishtuka sana.Aliuliza ni Salma yupi anayezungumziwa na Shedrack.Alipewa maelezo ya kutosha ambapo alimfahamu Salma aliyezungumziwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nadhani umeshamfahamu..yule pale ni mchumba wangu wa muda mrefu sana.Tumepanga kuoana mwakani…ila tangu amekutana na wewe kuna mabadiliko makubwa sana kiasi cha mahusiano yetu kupungua.Kila nikimpigia nakuta anaongea na wewe hivyo nakuomba umuache maana nimeshapoteza gharama nyingi sana.Kama umeshaenda nyumbani kwake kila kilichomo mle ndani nimemnunulia mimi na isitoshe kila mwezi lazima nimtumie matumizi.Nakuomba broo..! Nisitiri kama mwanaume mwenzako.”Shedrack aliongea kwa uchungu.
“Usijali brother nimekuelewa ila toa hiyo fikra kuwa Salma anamahusiano yoyote ya kimapenzi na mimi.Nakuahidi kukusaidia ili uhusiano wenu uende vyema ila kuwa makini na jina hilo.”Tuntu alikata simu baada ya kuongea maneno hayo.Shedrack alishtushwa na kauli hiyo.Alimpigia tena Tuntu aliambiwa haipatikani kwani aliizima simu yake....
Kwa upande mwingine Shedrack alipata faraja ya moyo kutokana na maneno aliyoambiwa na Tuntu.Alitamani kuonana na Tuntu ili kumjua ni mwanaume wa aina gani mwenye moyo wa upendo kiasi cha kumuahidi ushiriakiano.Aliandika meseji ya kumshukuru kwa kumtia moyo kisha alijilaza kitandani kwake.
Nyumba ya Shedrack ilikuwa kubwa sana na yenye mvuto wa ajabu.Aliinunua kwa gharama ya shilingi milioni mia sita kwa muhindi mmoja maeneo ya Msasani kwa .Baba yake alikuwa ni mfanyabiashara wa madini huko Merelani Arusha hivyo pesa kwao haikuwa kitu.Shedrack alinunuliwa nyumba nyumba hiyo akiwa mwaka wa pili chuoni akichukua shahada ya uhasibu katika chuo cha Tanzania Institute of Accountancy{TIA} kilichopo maeneo ya Temeke karibu na uwanja wa mpira wa taifa.
Shedrack baada ya kuhitimu,aliajiliwa na kampuni ya Wachu Investment akiwa kama muhasimu msaidizi.Alimfahamu Salma miaka kadhaa walipokutana katika ukumbi wa Karimjee,Posta kwenye sherehe za maazimisho ya siku ya watoto duniani.Shedrack alikuwa kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Shaaban Robert na Salma alikuwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Kibasila iliyopo Temeke.Siku hiyo kulikuwa na viongozi mbalimbali akiwemo waziri wa Afya maendeleo ya jamii jinsia na watoto Profesa Zabron Kayuguyugu.
Salma alikuwa miongoni mwa watumbuizaji wa siku hiyo.Akiwa anatumbuiza kwa mashairi mazuri,aliinua macho yake kuiangalia hadhira.Katika pitapita ya macho yake,alikutana na sura iliyojaa tabasamu kutoka kwa Shedrack.Lilikuwa siyo tabasamu la kawaida,ilibeba ujumbe mzito ulioashiria upendo.Baaada ya Salma kushuka jukwaani,Shedrack alijongea mpaka alipokuwa amekaa Salma na rafiki zake.Hakuwa na wasiwasi ya kujihisi vibaya kutokana na sare yake kumtofautisha na wanafunzi wa kibasila,bali alikomaa na lengo lake la kuhitaji kuongea na msichana huyo aliyeushitua moyo wake kwa kipindi cha dakika chache alizomuona.
Baada ya kuwasalimia Salma na rafiki zake huku hakuna aliyemshitukia kutokana na watu kushughulishwa na furaha kutoka kwa watumbuizaji,Shedrack alimnong’oneza Salma.Kwanza alimuuliza jina lake ambapo jina lake kamili aliitwa Salma Jabu kisha naye alijitambulisha na bila kupoteza muda alimuomba namba yake ya simu.Salma alimuandikia harakaharaka na kumkabidhi.Shedrack alirudi kwenye nafasi yake na kuendelea na kilichowaleta eneo hilo.
Wakati wote wa sherehe,Salma alikuwa akigeuka nyuma kumuangalia Shedrack.Walikuwa wakitabasamu kila macho yao yalipokutana.Hii ilikuwa ishara ya ushindi kwa Shedrack kwani kama Salma asingekuwa na furaha na jambo hilo wala asinge tabasamu.Jioni yake Shedrack alimpigia simu na kuongea naye mambo mbalimbali na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa ukaribu kati ya Salma na Shedrack.
********
Ilikuwa mida ya jioni.Tuntu alikuwa uwanjani akifanya mazoezi ya kujiandaa na rigi ya chuoni iliyojulikana kama Inter-courses competition ambayo hufanyika kila mwaka chuoni hapo.Kutwa nzima hakuonana na Salma.Akiwawanamalizia mazoezi na wenzake,Salma alikuwa amekwisha wadia maeneo hayo akitokea darasani. Alimfuata Tuntu kwa furaha akihitaji kuongea naye.Siku hiyo ilikuwa tofauti kidogo na Salma alivyozoe kila akikutana na Tuntu.Siku hiyo Tuntu baada ya kumuona Salma,alikunja sura huku akigeukia upande mwengine na kuendelea na mazungumzo.
Salma alifika karibu yake na kumsalimia.Shedrack aliitika kwa sauti ya chini kama aliyelazimishwa kuongea. “Leo mbana uko hibyo unaumwa?”Salma aliongea kwa sauti ya upole.Tuntu alimuangalia kwa jicho la ukali kwa takribani sekunde kumi.Salma alishikwa na hofu kidogo kwani hakuwa kumuona Tuntu katika hali hiyo.
“Salmaa…! Salma…!Salma ni jina ninalolichukia sana katika dunia hii.Ni jina la watu wasaliti,waongo,walaghai na wenye kila sifa mbaya.Kwanini unamtesa Shedrack?” Salma alishtuka baada ya kusikia jina la Shedrack.Alianza kujiuliza Tuntu alilijuaje jina hilo hakupata jibu. “Umemjuaje Shedrack”Alikosa subira akaamua kuuliza. “Haina haja ya kujua wapi nimelipata jina hilo ila tambua kuanzia leo ninakuchukia!Sitaki uwe karibu yangu maana jina la Slama sitaki kulisikiaaa!!”Tuntu alisema kwa sauti kali kisha alisogea pembeni.Salma alimfuata na kumuuliza “kwanini unalichukia jina la Salma”?Tuntu alivuta pumzi kwa nguvu na kuitoa nje kisha alianza kumuelezea kwanini alilichukia jina la salma “Miaka sita iliyopita……”.Alianza kuhadithia.
******
Miaka kadhaa iliyopita Tuntu alikuwa akitokea maeneo ya “fire” akielekea shuleni kwao Azania karibu na hospitali ya Muhimbili.Akiwa anakaribia karibu na geti la sekondari ya Jangwani,kamba ya kiatu ilifunguka.Aliinama na kuanza kuifunga.Akiwa anamalizia kuifunga vizuri,alipamiwa na mtu asiyemjua.Alijikaza kiume ili asidondoke;kisha aliinua kichwa chake ili kumuangalia aliyempamia,alikutana na sura nzuri ya msichana ambaye alikuwa na macho ya unyonge.Aliisikia sauti tamu ya msicha huyo ikimuomba samahani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Samahani kaka nimejisahau kwa kugeuka nyuma.Haikuwa kusudio langu kukupamia,naomba unisamehe.”Aliongea msichana huyo kwa unyonge sana. “Unaenda wapi muda huu mbona mapema?”Tuntu aliuliza kwani ilikuwa mida ya saa mbili asubuhi.Muda huo Tuntu alichelewa kuingia shuleni kutokana na majukumu ya hapa na pale nyumbani kwao kiasi cha baba yake kutokwenda kazini hivyo alikosa lifti hivyo ilimbidi apande daladala.
“Nimefika shuleni hali yangu ikawa mbaya zaidi inabidi nirudi nyumbani.”Alimjibiwa na msichana huyo.
“Una nauli?” Tuntu alimuuliza.
”Ninayo”Alijibu msichana huyo.
“Chukua hii itaongezea kwenye dawa.”Tuntu alimkabidhi shilingi elfu mbili kisha aliondoka kuelekea shuleni kwao Azania.
Kutokana na haraka aliyokuwa nayo,Tuntu hakuwa na muda wa kuuliza jina la msichana huyo.Baada ya kukabidhiwa kiasi hichi,alibaki akimuangalia bila ya kummaliza.Maswali mengi yalimjaa kichwani kiasi cha kukosa majibu na hatimaye aliondoka kuelekea kituoni.
Tuntu alikuwa anasoma kidato cha nne mchepuo wa biashara katika shule ya sekondari Azania.Japo alikuwa anasoma mchepuo wa biashara,lakini alikuwa anayapenda sana masomo ya mchepuo wa sanaa.Ndoto yake ilikuwa kuja kuwa mwalimu kutokana na kipaji cha ushawishi alichokuwa nacho.Wazazi wake walimtaka asomo masomo ya biashara ili aje kuwa mweledi wa biashara na kuzisimamia biashara za baba yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baba yake alikuwa mfanyabiashara wa vifaa vya umeme,compyuta,redio aina za sabufa pamoja na friji.Alikuwa akiagiza mzigo kutoka china na kuuza kwa jumla nchini Tanzania,hivyo alihitaji kijana wake wa kwanza asomee biashara ili amsaidie kuendesha biashara kisomi.Hivyo alikubaliana nao kishingo upande.
Tuntu alikuwa mtaalamu wa masomo ya sanaa hususani historia,kiingereza,jiografia pamoja na civics.Katika masomo hayo hakuwahi kushuka chini ya asilimia 60 tangu aanze kidoto cha kwanza.Kwa upande wa masomo ya bishara,book-keeping hakuwahi kuvuka alama 40 huku commerce akiwa anaishia asilimia 50.Aliendelea kupambana na kujitahidi Zaidi katika masomo mengine huku yale ya Sanaa akiyashikilia barabara.
******
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment