Simulizi : Yamenikuta Salma Mie
Sehemu Ya Pili (2)
“Si nimekwambia ufanye subira. Mambo yakiwa mazuri utapata pikipiki, hata gari”
“Yako ni hayo tu kila siku. Wanaume wengine hawapendi hata kuwapendezesha wake zao!”
“Salma usiige mambo ya watu. Kwa vile umemuona jirani yako ana gari na wewe unataka ununuliwe gari. Wewe unajua mume wake anafanya kazi gani?”
“Wala sio hivyo. Mimi nina akili zangu na naangalia maisha yangu. Siigi mtu mimi. Kama ninataka pikipiki ninaitaka kwa shida yangu. Tatizo ni kuwa kila ninachokwambia mume wangu lazima ukipinge”
Ibrahim akajidai kucheka.
“Si kweli. Mbona vitu vingi nakununulia. Nguo nakununulia pamoja na kukutimizia mahitaji mengine. Sema wewe sasa unataka makubwa”
“Haya basi nayaishe. Naona labda kuna mwenzangu wa pembeni maana siku hizi umebadilika sana”
Siku ile nilijaribu tu kumpima mume wangu ili nione atanijibu nini. Lakini jibu lake lilikuwa ni la kukatisha tamaa. Sikamini kabisa kuwa kwa kipato cha mume wangu angeshindwa kuninunulia pikipiki.
Pia sikuamini kuwa mwaname huyo angeshindwa kunitimizia mahitaji yangu mengine ninayotaka kama anavyofanyiwa shoga yangu na mume wake.
Pegine ulikuwa ni ugumu au roho mbaya inayotokana na mila zilizopitwa na wakati zinazowadharaulisha wanawake kwa wanaume.
Baada ya siku ile sikumuuliza kitu tena Ibrahim lakini ndani ya moyo wangu nilishaamua kama tabia ya Ibrahim itaendelea kuwa ile nisingeweza kupata maendeleo kama wanawake wenzangu.
Nilikaa kama siku tatu hivi nikiwaza, siku ya nne yake nikaenda kwa yule rafiki yangu. Nilimkuta amekaa sebukeni akitizama filamu kwenye televisheni yake.
“Vipi shoga?” akaniuliza.
“Ah mambo ya mume wangu yananichokesha!” nikamwambia huku nikiketi kwenye kochi.
Shoga yangu Rita akanicheka.
“Yamekuchokesha vipi shoga?”
“Ugumu shoga! Mume wangu ni mgumu sana. Juzi nilijaribu tu kumuomba aninunulie pikipiki, eti anajidai kuniuliza pikipiki ya nini…gari si hili tunalo”
“Labda hana pesa”
“Sio kutokuwa na pesa, sema ni mgumu. Pesa anazo lakini ana dharau, hataki maendeleo yangu. Nimeshamuona yule si mume ni gume gume”
Shoga yangu akacheka tena lakini mimi sikucheka nilijifanya nimekasirika.
“Kweli nakwambia shoga…yule si mume ni gume gume”
“Siku ile nilikwambia mwendee kwa songoma ukaleta gozi gozi. Si unamuona huyu mume wangu nimemnyoosha, haoni wala hasikii, nikikohoa tu ananiuliza wataka nini mke wangu?”
“Na hilo la songoma ndilo lililonileta, nataka unipeleke na mimi nikamtengeneze, awe kama mume wako. Nikimuona amekaa sawa, namwambia anijengeee nyumba”
Mimi na shoga yangu tukacheka pamoja.
“Na huyo songoma mwenyewe akikufanyia dawa zake utakuja kuniambia. Lazima mumeo atakujengea nyumba” Rita akaniambia na kuzidi kunipa moyo.
“Sasa utanipeleka lini shoga?”
“Siku yoyote utakayotaka, mimi niko tayari”
“Nataka unipeleke kwa huyo huyo aliyekufanyia wewe”
“Na ndiko huko huko nitakakokupeleka”
“Na itachukua siku ngapi hadi matokeo yaonekane?”
“Si siku nyingi. utamuona akibadilika kidogo kidogo”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilinyamaza kidogo kufikiri kisha nikamuuliza.
“Tunaweza kwenda kesho?”
“Tunaweza lakini iwe asubuhi, mpaka saa sita twe tumerudi”
“Na mimi pia muda wangu mzuri ni wa asubuhi, yule bwana akienda kazini. Najua akiondoka harudi mpaka jioni”
“Harudi mchana kuja kula?”
“Zamani ndio alikuwa anarudi kula lakini siku hizi akiondoka ndio mpaka jioni. Sijui anakula kwa huyo mke mwenzangu!”
“Yote utayajua huko huko kwa huyo mganga”
“Kama ana mwanamke atanieleza?”
“Atakueleza yote”
“Nataka nijue, uwezekano huo wa kwa na mwanamke upo”
“Sasa basi wewe jiandae, nikikupigia simu kesho asubuhi unakuja, tunakwenda zetu”
“Ni mbali sana”
“Mganga mwenyewe yuko Kisosora”
“Si tutakwenda na gari yako”
“Tutakwenda na gari yangu, usijali. Hapo Kisosora hata lita moja ya petroli haimaliziki”
“Tutatia lita moja”
“Mbona mume wangu ananitilia ya kutosha. Ananiwekea mafuta ya wiki nzima”
“Acha mambo yaende vizuri, na mimi keshokutwa nitakuwa na gari langu. Mwanaume pesa anazo lakini ni mgumu sana. Hataki hata nijue katika akaunti yake ya benki ana shilingi ngapi”
“Tena nakwambia ukimuweka sawa, hata jina la akaunti yake ya benki anaweka la kwako?”
“Acha shoga! Kwani wewe mume wako ameweka jina lako kwenye akaunti yake?”
“Mimi amenifungulia akaunti yangu kabisa, ananiwekea pesa kila mwezi”
“Na mimi itakuwa hivyo hivyo. Nitamwambia anifungulie akanti benki”
Siku ile nilirudi nyumbani kwangu nikiwa na furaha na ndoto za kupata tajiri. Kama mume wangu atanijengea nyumba, ataninunulia gari, atanifungulia akaunti benki, nitajiona kama nimeshakuwa tajiri.
Mume wangu aliporudi nyumbani jioni nilimchangamkia sana kuliko kawaida yangu kwa vile nilishajua mahali ambapo nitakwenda kumnyoosha.
Kwa vile ingekuwa ni mara yangu ya kwanza kwenda kwa waganga, siku ile sikupata usingizi kwa mawazo.
Mawazo yangu yalikwenda mbali nikawa nawaza wakati mume wangu akiwa bwege langu akinitii kwa kila kitu.
Nilijiambia wakati huo maisha yangu yatakuwa mazuri sana. Fedha za mume wangu nitakuwa nakaa nazo mimi.
Asubuhi kulipokucha nilianza kufanya usafi wa nyumbani kwangu. Sikushughulika kubandika chai mapema kwa sababu mume wangu alikuwa akiondoka asubuhi bila kunywa chai. Ananywea huko huko, yeye na mdogo wake.
Muda wao wa kutoka ulipowadia Ibrahim alinifuata uani akaniaga.
“Nimekuachia pesa za sokoni kitandani” akaniambia.
“Hizo ni pesa au visenti. Pesa utakuja kuniachia nitakapokutengeneza” nikamjibu kimoyomoyo.
Alipoondoka na mdogo wake nikaenda bafuni kuoga. Nilipomaliza nilivaa. Nikaenda kuketi sebuleni kwangu kusubiri Rita anipigie simu.
Nilipoona kimya na muda unakwenda nikampigia mimi.
“Shoga habari ya asubuhi?” nikamuuliza alipokea simu.
“Nzuri shoga, mume wangu ndio ameondoka sasa hivi. Nilikuwa nataka kukupigia kukwambia jitayarishe”
“Nimeshajitayarisha shoga”
“Basi njoo, mimi najiandaa”
Nikarudi chumbani kwangu kuchukua baibui langu nikalivaa na kupachika mkoba wangu begani, nikatoka.
Nilifunga mlango wangu wa mbele kwa funguo nikaenda nyumbani kwa jirani yangu.
Aliniacha sebuleni kwa karibu nusu saa kisha naye akatoka na kuniambia.
“Twenzetu”
Tulikwenda nyuma ya nyumba yake akafungua geti na kulitoa gari.
“Wewe jipakie kabisa, mimi nafunga geti” akaniambia na kurudi kwenye geti.
Aliingia ndani akalifunga geti hilo kisha akazunguka kwa mlango wa mbele.
Alifunga mlango na kuja kwenye gari. Wakati huo nilikuwa nimeshajipakia nikiwa kando ya siti ya dereva.
Akafungua mlango na kujipakia.
“Sasa twenzetu” akaniambia huku akiliwasha gari.
Alilirudisha gari kinyume nyume hadi barabarani. Akaligeuza na tukaanza safari yetu.
“Kinachonikera kwa yule mganga ni foleni ya watu, yaani ukifika unakuta msururu wa watu wanaomsubiri” Shoga yangu aliniambia wakati gari likiwa katika mwendo.
“Yeye mwenyewe anakuwa wapi” nikamuuliza.
“Anakuwepo ila wale watu wanafika kabla mwenyewe hajaamka. Wanamsubiri hapo nje mpaka aamke, aoge, anywe chai, unakuta foleni inakuwa ndefu”
“Sasa tutafanyaje shoga, tutawahi kurudi mapema kweli?”
“Tujaribu kubahatisha, tunaweza tusikute foleni ndefu. Kuna siku niliwahi kuja sikukuta mtu yeyote lakini kuna siku nilikuta foleni iliyonikatisha tamaa”
“Ukafanyaje?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ilinibidi nisubiri hivyi hivyo. Mpaka nashughulikiwa ilikuwa imeshafika saa sita’mchana. Lakini nashukuru mambo yangu yalikwenda vizuri”
“Kama tutakuta foleni ndefu utaniacha niendelee kusubiri, hata kama nitaondoka jioni si kitu”
Dakika chache baadaye tukawa tumefika katika eneo hilo la Kisosora. Nyumba ya mganga huyo ilikuwa kibanda kidogo kilichojengwa kwa miti na udongo. Mbele ya kibanda hicho kulikuwa na nyumba kubwa ya matofali iliyokuwa haijakalmilika.
Tuliacha gari mbele ya ile nyumba tukaingia uani. Tulikuta watu ambao hawakuzidi kumi waliokuwa wameketi kwenye baraza ya kibanda hicho.
“Leo hakuna watu wengi, ni wale wachache tu” Rita akaniambia.
“Mbona hawajapanga foleni’ nikamuuliza.
“kila mtu anajijua ni wa ngapi kuingia. Sisi ndio tutakuwa watu wa mwisho. Labda waje wengine nyuma yetu”
Na sisi tukaenda kwnye ile baraza. Tuliwasalimia watu tuliowakuta kisha tukakaa.
Wakati tunakaa, mtu mmoja akatoka ndani ya kile kibanda. Alikuwa ni mteja aliyekwishahudumiwa. Mtu mwingine akaingia.
Baada ya nusu saa mtu huyo naye akatoka akaingia mwingine. Yule aliyeingia hakukaa sana, akatoka na kuingia mwingine.
Kitu kilichonipa moyo ni kuwa foleni ilikuwa ikienda kwa haraka.
Ilikuwa inakaribia kuwa saa nne na nusu, mimi na Rita tulipoingia.
Mganga mwenyewe alikuwa mzee aliyekuwa amejifunga kaniki. Chumba chake hakikuwa na mwanaga wa kutosha kutokana na kuwa na dirisha dogo. Tulipoingia tu nilianza kusikia joto.
“Karibuni” Mganga huyo akatuambia.
Alikuwa amekaa kwenye jamvi lililoenea chumba kizima.
Tukakaa kwenye jamvi mbele yake.
“Shikamoo” Rita akamwamkia na mimi nikamwammkia.
“Marahaba hamjambo”
“Hatujambo. Naona kama umenisahau” Rita akamwambia.
Mganga akamtazama vizuri.
“Kama nakukumbuka”
“Mimi ni Rita. Niliwahi kuja ukanishughulikia matatizo ya mume wangu”
“Ahaa! Nimekukumbuka. Uliniambia unaishi Usagara”
“Haswaa! Ni kweli umenikumbuka”
“Muda mrefu umepita sijakuona ndio maana nimekusahahu kidogo. Habari za siku?’
“Nzuri. Nimekuletea huyu mteja, ni rafiki yangu”
“Ana matatizo gani”
“Atakueleza”
Nikataka kumpima yule mganga kujua uwezo wake.
“Shida yangu nataka unitazamie ramli?” nikamwambia.
“Hapa ramli ndio nyumbani kwake, nipe mkono wako” Mganga akaniambia huku akininyooshea mkono wake.
Nikanyoosha mkono wangu na kumpa. Akaushika na kutazama kiganja changu.
“Huu mstari wa maisha unaonesha kuwa una tatizo na mume wako. Maisha yako hayaendi vizuri’ Mgaga akaniambia kisha akanitazama na kuniuliza.
“Kweli au uongo?”
“Ni kweli” nikamjibu.
“Enhe. Matatizo ya mume wako hayatofautiani sana na matatizo aliyokuwa nayo mume wa mwenzako. Kweli au uongo?”
“Ni kweli”
“Enhe. Mwanamme pesa anapata lakini hazionekani. Ugomvi hawishi nyumbani. Kweli au uongo”
“Ni kweli”
“Yaani ni sawa na kusema kuwa mapenzi hayapo nyumbani. Si kama ilivyokuwa wakati mnaanza sasa maisha. Kweli, uongo”
“Ni kweli”
Sasa mama una wasiwasi, unahisi kama mko wengi. Kweli, uongo’
“Ni kweli”
“Alama za kiganja chako zinanionesha kuwa mumeo ana nyumba ndogo iliyoharibu akili yake”
Hapo hapo nikamtazama Rita kwa mshangao.
“Unasikia maneno hayo. Mimi nilikwambia utaambiwa kila kitu” Rita akaniambia.
“Yaani mume wangu ana mwanamke wa nje?” nikamuuliza mganga huyo kwa taharuki.
“Wewe unadhani ni kitu gani kimeharibu tabia yake?’
“Huyo msichana ndio amemuharibu?”
“Yaani ndio anampenda kuliko wewe”
Nikatingisha kichwa changu kumkubalia.
“Asante kwa kunifahamisha, sasa na mimi nataka kumkomoa. Nataka amuache huyo mwanamke anipende mimi peke yangu, anijali na kunisikiliza, Kila ninachomwambia atii”
“Hata kama utataka akununulie gari atakununulia”
“Nifanyie hiyo kazi, utahitaji shilingi ngapi?’
“Kwa vile umeletwa na mteja wangu wa siku nyingi, nitakufanyia shilingi laki moja”
Nikaguna na kumtazama Rita.
Sikuwa nimechukua shilingi laki moja. Nilikuwa na shilingi elfu hamsini tu kwenye pochi yangu.
“Unajua shoga nilifanya ujinga nilipoondoka nyumbani, nilichukua shilingi elfu hamsini tu”
“Sasa mimi nitakutolee elfu hamsini, tukifika nyumbani unirudishie”
“Sawa shoga, nitakurudishia”
Rita akafungua pochi yake na kutoa shilingi elfu hamsini na mimi nikatoa kiasi kama hicho kutoka kwenye pochi yangu. Tukampa yule mganga.
“Anaitwa nani mumeo?” Mganga akaniuliza baada ya kupokea zile pesa.
“Anaitwa Ibrahim Amour”
Mganga aliuachia mkono wangu akachukua karatasi na kuiandika jina la Ibrahim.
“Na wewe unaitwa nani”
“Mimi naitwa Salma Aboud”
Mganga akaandika jina langu kwenye ile karatasi.
Pembeni mwake palikuwa na tunguri kadhaa. Alichukua tunguri mojawapo akakitia kile kiratasi kwenye mdomo wa ile tunguri kisha akaanza kuitikisa huku akitabana maneno kwa kiluga.
Kila alipotabana alikuwa akilitaja jina la Ibrahim na jina langu.
Baadaye alikitoa kile kiratasi ambacho kilikuwa kimeloa kwa dawa iliyokuwemo ndani ya ile tunguri. Akachukua chetezo kilichokuwa na makaa ya moto akakitia kile kikaratasi, kikaanza kuungua na kutoa moshi.
Akachukua tunguri nyingine akaitabania maneno huku akilitaja jina langu na la Ibrahim kisha akachukua karatasi na kumiminia unga fulani kutoka katika ile tunguri, akakiweka kile kikaratasi mbele yangu.
Akachukua tunguri nyingine nayo akaitabania kisha akamimina unga kama ule wa kwanza kwenye kikaratasi kingine.
Baada ya hapo alikifunga kikaratasi cha kwanza, kikawa kama kipakiti. Halafu alikifunga kikaratasi cha pili.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa sikiliza” Mganga akanimabia.
“Ndiyo nakusikiliza”
Alichukua kile kipakiti cha kwanza akanipa.
“Hiki utamuwekea kwenye maji ya kuoga kwa siku tatu”
“Sijakuelewa, nitamuwekea kwenye maji ya kuoga kivipi?”
“Yaani katika yale maji anayooga kwenye ndoo, tia hii dawa kidogo bila mwenyewe kukuona”
“Sasa sisi hatuogi kwenye ndoo, tunaoga moja kwa moja kwenye bomba”
“Mnatumia bomba la mvua?”
“Ndiyo”
“Sasa itakuwaje, hii dawa ni lazima aioge”
“Hakuna njia nyingine?”
Mganga akatikisa kichwa.
“Ingekuwepo ningekwambia”
“Si kitu, nipe”
“Utafanyaje?” Rita akaniuliza.
“Nitafunga maji kwenye mita kisha nitamtilia maji kwenye ndoo nimwambie maji yamekatika. Atayaoga tu”
“Lakini umeambiwa ni kwa siku tatu”
“Kwa siku tatu itakuwa vigumu, atagundua kuwa maji yanatoka”
Nikamtazama mganga na kumuuliza.
“Kwa siku moja haitatosha”
“Kama ni kwa siku moja itie mara tatu. Yaani chota kidogo tia, halafu chota mara ya pili tia halafu chota mara ya tatu tia. Itakuwa imemalizika yote.
“Ngoja nikwambie nilivyokuelewa. Nikishatia maji kwenye ndoo nichote kidogo hii dawa niitie kwenye maji halafu nichote tena nitie, halafu nichote tena mara ya tatu nitie. Au nimekosea”
“Ni sawa”
“Kwa hiyo nitaimaliza dawa yote?”
“Ndiyo utaimaliza yote”
“Haitaonekana kwenye maji?”
“Hapana, inayayuka na ni nyeupe tu. Hawezi kuiona”
“Sawa”
Mganga akachukua ile pakiti nyingine akanipa.
“Na hii utamuwekea kwenye chakula. Unatia kidogo kwenye mchuzi au wali au hata kwenye chai”
“Nitie wakati napika au wakati tunakula?”
“Wakati wowote, bora uitie tu”
“Sasa tatizo ni kwamba tunakula pamoja”
“Haina madhara hata kama wewe utakula hicho chakula au mtu mwingine atakula”
“Sawa. Nimtilie mara ngapi?”
“Mtilie mara moja kwa siku tatu”
“Wakati gani?”
“Wakati wowote asubuhi au jioni, unaweza kumtilia”
“Sawa”
“Baada ya siku tatu utaona matokeo yake, utakuja kuniambia”
“Atanipenda sana?”
“Na atakupa kila kitu unachokitaka”
“Nitakushukuru sana babu kwa maana yule mwanaume ananitesa sana”
“Mateso yote yatakwisha, utakuwa unamtesa wewe”
“Kila itakavyotokea nitakuja kukuambia”
“Sawa, sasa kazi yenu imekwisha mnaweza kwenda”
Tulipoondoka kwa yule mganga moyo wangu ulikuwa umepata matumaini sana na kufarijika hasa nilivyojua kwamba ninakwenda kumkomesha mume wangu.
“Sasa kazi kwako” Rita akaniambia wakati gari ikiwa kwenye mwendo.
“Nakwenda kumuwekea leo leo, singoji kesho”
“Ndiyo ianze leo”
“Nikifika nayafunga maji, atakapotaka kuoga namtilia maji kwenye ndoo”
Dakika chache baadaye tukafika nyumbani. Rita alilisimamisha gari mbele ya geti. Akashuka na kuniambia nimsubiri.
Alikwenda kufungua mlango akaingia ndani kisha akaja kufungua geti.
Geti lilipokuwa wazi aliingia kwenye gari akaiingiza gari ndani. Tukashuka sote. Alikwenda kufunga geti. Alipomaliza tukaingia ndani ya nyumba yake.
“Shoga asante, acha niende nikatayarishe mambo” nikamuaga shoga yangu kabla ya kutoka kwenda kwangu.
Nilifungua mlango wa nyumba yanngu nikaingia ndani. Wakati nikiwa jikoni nikitafuta mahali pa kuficha vile vipakiti, nikasikia mlango ukigongwa. Nikaviacha vile vipakiti kwenye mkoba wangu, nikaenda kufungua mlango.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikashituka kuona alikuwa mgeni. Alikuwa mdogo wake Ibrahim aliyekuwa akikaa Dar. Alikuwa anaitwa Mashaka lakini mwenyewe alijiita meshack.
Alikuwa ni mdogo wake Ibrahim shangazi kwa mjomba.
“Oh shemeji, karibu sana” nikamkaribisha huku nikipokea begi alilokuwa amelipachika kwenye bega lake.
“Asante, habari ya hapa?”
“Nzuri, za safari”
Baada ya kulipokea begi niliingia nalo ndani.
“Nashukuru ni nzuri, sijui nyinyi hapa”
Meshack aliingia akafunga mlango.
Nikamkaribisha sebuleni lakini begi lake nilikwenda kuliweka kwenye chumba cha wageni.
Nilipotoka Meshack aliniuliza.
“Kaka yuko wapi?”
“Yuko kazini kwake, hapa anarudi jioni sana, si ana taarifa kuwa unakuja?”
“Anayo taarifa na leo asubuhi wakati najiandaa kuja huku nilimpigia simu kumjulisha kuwa ninakuja”
“Ngoja nimpigie nimjulishe kuwa umeshafika”
Nikachukua simu yangu na kumpigia.
“Heloo!” Sauti ya Ibrahim ikasikika kwanye simu.
“Shemeji ameshafika” nikamwambia.
“Shemeji yupi?” akaniuliza.
“Shemeji Mashaka kutoka Dar”
“Oh alinipigia simu asubuhi kunijulisha kuwa anakuja lakini nilisahau kukuambia. Amefika sasa hivi”
“Ndiyo namkaribisha hapa”
“Mwambie ninakuja, tunafunga ofisi”
“Sawa”
Nikakata simu kisha nikamwambia shemeji.
“Anakuja”
Kutokana na ule muda aliofika shemeji nilikisia kuwa hakuwa amekula chakula cha mchana, nikaona angalau nikamtayarishie chai ya maziwa imchangamshe hadi usiku.
“Shemeji naenda jikoni” nikamuaga na kuondoka kwenda jikoni kumtayarishia chai.
Chai ilikuwamo kwenye chupa. Nilichukua slesi tatu za mikate, nilimpakia siagi na kumuandalia kwenye sahani pamoja na kikombe cha chai nikampelekea.
“Karibu shemeji” nikamwambia wakati nikimuwekea sahani.
“Asante shemeji”
Nikakaa kando yake kumzungumzisha huku akiendelea kunywa chai.
Alipomaliza kunywa chai alinishukuru. Nikaenda kuiondoa ile sahani na kuirudisha jikoni. Nikarudi tena pale sebuleni. Tuliendelea kuzungumza hadi mume wangu alipotokea. Niliwaacha wakisalimiana nikaingia chumbani.
Nilijilaza kitandani na kuanza kuwaza jinsi ya kuifanya ile dawa yangu wakati kulikuwa na mgeni ambaye angekula kile chakula. Isitoshe nisingeweza kufunga bomba na kusingizia maji yamekatika wakati kulikuwa na mgeni huyo.
Nilijimbia kama itagundulika kuwa maji yanatoka ispikuwa niliyafunga na kusingizia kuwa maji yamekatika, ningeeleweka vibaya mbele ya mgeni. Ningeonekana kama nimemfungia yeye na kwamba sikuvutiwa na ujio wake.
Nikaona nimpigie simu shoga yangu Rita.
“Tumepata mgeni” nikamwambia Rita alipopokea simu yangu.
“Ni nani?” Rita akaniuliza.
“Ni shemeji yangu, ndugu yake mume wangu. Sasa sijui itakuwaje?”
“Kwani yeye atakuzuia nini?”
“Si ile dawa nilitakiwa niitie kwenye chakula”
“Kama nakumbuka vizuri yule mzee alikwambia hata wewe mwenyewe unaweza kula hicho chakula, kwani si kuna huyo mdogo wake mwingine mnayeishi naye. Si pia atakula hicho chakula?”
“Sasa kama hilo si tatizo, kuna tatizo jingine. Nikiyafunga yale maji, si nitaonekana nimemfungia mgeni? Si unakumbuka tulikubaliana nisingizie kuwa maji yamekatika ili huyu bwana aoge kwenye ndoo?”
“Kwani huyo mgeni atakaa kwa siku ngapi?”
“Sijajua bado”
“Unaweza kusubiri hadi atakapoondoka”
“Naona nachelewa”
“Sasa utafanya nini?”
“Sina la kufanya, itabidi nisubiri hadi atakapoondoka lakini ndio hivyo moyo waumia”
“Subira huvuta heri msichana, acha pupa” Rita akaniambia kwa mzaha. Tukacheka.
“Najua kuwa subira huvuta heri lakini ngoja ngoja nayo huumiza matumbo”
Wakati nasema hivyo mume wangu akafungua mlango ghafla na kuingia ndani. Nikazuga hapo hapo.
“Basi shoga tutaongea baadaye, ngoja nimuhudumie mume wangu ndio amerudi sasa hivi kutoka kazini”
Sikungoja jibu lake nikakata simu.
“Unazungumza na nani?” Ibrahim aliposikia namsema akaniuliza.
“Nazungumza na jirani yangu Rita” nikamwambia huku nikinyanyuka kitandani.
“Umempa chakula mgeni?”
“Nilimpatia chai tu na slesi tatu, hakukuwa na chakula”
“Jioni utapika nini?”
“Mh! Sijajua bado. Ulitaka njipike nini?”
“Labda ukaange chipsi, viazi si vipo?”
“Viazi vipo”
“Kaanga chipsi na mayai”
Baada ya kuzungumza hivyo na Ibrahim nilitoka mle chumbanni nikaingia jikoni na kuanza kumenya viazi. Mpaka inafika saa mbili usiku, chipsi kwa mayai ya kukaanga zikawa tayari. Ndani ya friji kulikuwa na jagi la juisi ya matunda. Nikaenda nalo mezani.
Baada ya kuyayarisha mlo huo nikaenda sebuleni kumuita mume wangu na shemeji zangu.
Tulikula pamoja. Baada ya kula wenzangu waliondoka na kuruidi sebuleni, wakaniacha nikiondoa vyombo.
Muda wa kulala ulipowadia nilimuuliza Ibrahim kama mdogo wake aliyekuja kutoka Dar alikuwa amepata likizo kazini kwake.
“Sijamuuliza kama alipata likizo” Ibrahim akanijibu.
Nikataka nimuulize ataondoka lini lakini niliona swali hilo halikuwa la msingi kumuuliza mume wangu hasa kwa kuzingatia kuwa yule alikuwa ndugu yake.
Asubuhi ya siku iliyofuata nilifurahi Ibrahim alipoondoka na mgeni wake. Walikwenda kunywa chai huko huko.
Walipoondoka tu nikaenda kwa Rita.
Baada ya kusalimiana naye aliniuliza “Vipi?”
“Mpango wangu umekwama” nikamwambia huku nikiketi kwenye kochi.
“Kwa sababu ya huyo mgeni?”
“Na sijui ataondoka lini!”
Rita alipoona nimechukia akanicheka na mimi nikajidai kucheka.
“Huyo mgeni siku zote haji, anangoja nina mipango yangu ndio anakuja. Si balaa hili!”
“Pengine hatakaa sana, ni wasiwasi wako tu”
“Kama hatakaa sana ndivyo ninavyotaka”
Mgeni huyo alikaa kwetu kwa siku nne. Usiku wa siku hiyo ya nne akaniambia kuwa kesho yake ataondoka kurudi Dar kwani alikuja kutujulia hali tu. Nilifurahi sana aliponiambia hivyo.
Asubuhi ya siku iliyofuata Mashaka akaondoka kurudi Dar. Nikaona sasa nitumie ile nafasi kufanya ile dawa yangu. Ilipofika jioni nilijaza maji kwenye ndoo zote na kwenye mabeseni kisha nikaenda kufunga mita ya maji.
Mume wangu alipokuja nikatangulia kumwambia kuwa maji yalikuwa yamekatika.
“Yamekatika saa ngapi?” akaniuliza.
“Hivi jioni”
“Sasa tutaoga nini?”
“Niliwahi kuchota. Nimejaza ndoo zote”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Oh! Umefanya vizuri sana”
Ilipofika usiku yeye alikuwa wa kwanza kwenda kuoga. Aliponiambia nimtayarishie maji, nikaenda kukichukua kipakiti kimoja kati ya vile viwili nilivyopewa na mganga, nikachota ile dawa na kuitia mara tatu kwenye ndoo kama alivyoniagiza yule mganga.
Nilipoona bado ilikuwa ikielea juu ya maji, nilitia mkono wangu nikatibuatibu yale maji, ile dawa ikapotea.
Wakati mume wangu anaoga nilikuwa nikitayarisha chakula mezani, ile dawa nyingine nikaitia kwenye wali upande ule ambao nitamtilia yeye kwenye sahani.
Baada ya kuoga mume wangu alikuja mezani. Mara tu alipoketi kwenye kiti nilimsikia akisema.
“Mbona kichwa kinaniuma halafu macho yanniwasha?”
Akawa anayafikicha fikicha macho yake.
“Hicho kichwa kimekuanza saa ngapi?” nikamuuliza.
“Kimenianza wakati huu huu”
“Basi kula chakula halafu ule dawa”
Hapo hapo nikamuona akitikisa kichwa na kutazama kila upande kwa haraka haraka kabla ya kuniambia.
“Haa! Mke wangu macho yangu yamefunga kiza, sioni kitu!”
“Huoni kitu kwa sababu gani?” nikamuuliza.
“Sijui” akaniambia huku akijitahidi kuyafumba macho yake na kuyafumbua.
“Au ni kwa sababu ya hicho kichwa ulichosema kinakuuma?”
“Kichwa hakiwezi kusababisha macho yasione kabisa. Mimi sioni kabisa”
Wakati akisema Ibrahim alikuwa akiyaangaza macho yake kila upande kutafuta mwanga.
“Mke wangu nimepofuka macho!” akaniambia kwa sauti iliyotia huruma.
Nikaguna. Maelezo hayo yalikuwa yamenishangaza.
“Hebu nitazame nione macho yako” nikamwambia.
Mume wangu akageuza uso wake upande wangu. Macho yake yalikuwa ni mazima lakini yalionesha wazi kuwa hayakuwa yakiona kitu.
“Huoni kabisa?” nikamuuliza.
“Sioni”
“Mbona macho yako ni mazima na yako kama kawaida?”
“Sasa sijui kilichonitokea. Hii hali nimeiona baada ya kumaliza kuoga”
Isijekuwa ni ile dawa niliyomtilia kwenye maji aliyooga ndiyo iliyompofua macho mume wangu? Nikajiuliza kimoyomoyo.
Wakati nikijiuliza hivyo Ibrahim alikuwa akijitahidi kuyafikicha macho yake huku akijaribu kutazama bila mafanikio.
“Sijui ni kitu gani kimenitokea jamani?”
akajisemea peke yake.
“Hebu nisubiri hapo hapo” nikamwambia na kuinuka.
Niliingia chumbani nikiwa nimekishika kile kipakiti cha dawa niliyomtilia kwenye chakula. Nikakitazama vizuri. Hapo hapo niligundua kuwa nilikuwa nimechanganya zile dawa. Ile dawa niliyoambiwa nimtilie kwenye chakula ndiyo niliyomtilia kwenye maji ya kuoga na ile niliyoambiwa nimtilie kwenye maji ya kuoga nilimtilia kwenye chakula.
Sasa nikajiuliza ile dawa ndiyo iliyompofua macho Ibrahim kwa sababau niliitumia kinyume na nilivyoagizwa?
Nikamsikia Ibrahim akiniita.
Nikatoka mle chumbani na kumfuata pale kwenye meza.
Ibrahim alinigundua kuwa nimefika kwa kunipapasa.
“Bado huoni kabisa” nikamuuliza.
“Sioni, naona kiza kitupu. Yuko wapi Zacharia?”
“Nafikiri yuko nje”
“Hebu muite”
Nikatoka nje na kumuita Zacharia mdogo wake. Zacharia alinifuata mezani akijua nimemuitia chakula.
“Huyu hapa” nikamwambia ibrahim.
“Zacharia!” Ibrahim akamuita.
Zacharia mwenyewe alishituka kuitwa na kaka yake kwa sauti kubwa akiwa yuko karibu naye kabisa.
“Ndiyo kaka”
“Nilikuwa nimekwenda kuoga, sasa natoka bafuni nije hapa nikaona kichwa kinaniuma. Mpaka nafika hapa macho yangu yakazima kabisa. Hivi tunavyozungumza sioni kabisa”
“Alah! Huoni kabisa” Zacharia akamuuliza kwa mshangao.
“Sioni. Tangu muda huo nilikuwa namueleza shemeji yako kuwa sioni”
“Ina maana ni macho yenyewe tu hayaoni au kuna sababu?”
“Sijui”
Zacharia akaguna.
“Isije kuwa nina presha, kwa maana kichwa kilianza kuniuma?’
“Labda ni presha” nikaitilia nguvu hoja ya presha.
“Basi twende tukapime. Kama ni presha upate tiba yake”
“Subiri nikavae twende” Ibrahim alisema huku akijitahidi kuinuka kwenye kiti.
Nilimshika mkono nikamuongoza kuelekea chumbani. Tulipokuwa chumbani nilimvua saruni aliyokuwa amejifunga nikampa suruali na shati. Alipovaa nilimwambia achukue pesa za hospitali.
Akafungua kabati na kupapasa kabla ya kuukamata mkoba wake ambao huweka pesa.
“Hebu nitolee shilingi laki moja” akaniambia huku akinipa ule mkoba.
Niliuchukua nikaufungua. Ndani ya mkoba huo mlikuwa na vitita vya noti ambavyo hesabu yake alikuwa akiijua mwenyewe. Pesa hizo ndizo alizokuwa akizizungusha kwenye baishara yake.
Nilihesabu shilingi laki moja nikampa. Hakugundua kuwa ninampa pesa hizo mpaka nilipozigusisha kwenye mkono wake. Akazipokea na kuzitia mfukoni.
Niliurudisha ule mkoba kwenye kabati kisha nikatoka naye.
“Zacharia uko wapi?” akauliza mara tu tulipotoka chumbani.
“Niko hapa” Zacharia aliyekuwa amekaa kwenye meza alimjibu.
“Njoo unishike mkono twende, nafikiri hii itakuwa ni presha” Ibrahim akamwambia kisha akakumbuka kitu.
“Hebu tutolee ufunguo wa gari, nimeusahau” akaniambia.
Nikarudi chumabni na kuchukua funguo ya gari nikampa Zacharia.
“Gari utaendesha wewe” nikamwambia.
“Itabidi”
Zacharia akamshika kaka yake mkono wakatoka.
Nilipobaki peke yangu mle ndani nilikwenda ikata ile sehemu ya chakula niliyoitia ile dawa kwa ajili ya Ibrahim, nikaenda kuimwaga kwenye pipa.
Nilihofia kwamba huenda Ibrahim akirudi kutoka hospitali atataka kula. Nilikuwa sitaki ale ile dawa ambayo ilikuwa ni ya kuoga.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yasije yakatokea mengine, nikajiambia.
Nikataka nimpigie simu Rita nimwambie, lakini niliogopa kutoa ile siri kwamba mume wangu amepofuka macho kwa sababu ya ushirikina wangu.
Lakini nilipanga kwamba kila itakavyokuwa kesho yake niende kwa yule mganga nimueleze hali iliyotokea, pengine angeweza kuwa na ufumbuzi.
Kwa upande mwingine nilijipa moyo kwamba huenda dawa ile aliyooga siyo iliyomfanya mume wangu asione bali ni presha kama mwenyewe alivyokuwa anahisi.
Niliomba Mungu iwe ni presha kweli. Kama itakuwa si presha itakuwa ni ile dawa, nilijiambia.
Ilipita karibu saa nzima, nikampigia simu Zacharia. Zacharia alipopokea simu nikamuuliza.
“Enhe mmefika hospitali?”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment