Simulizi : Facebook Imeharibu Maisha Yangu
Sehemu Ya Pili
(2)
Resh alipiga kelele ghafla gari
ikayumba huku na huko,dereva akajaribu kwa uwezo wake wote kuirudisha barabarani
"Paaaa!!" mlio mkubwa
ukasikika.
*******************?
Adam
alipokea ujumbe kutoka kwa Reshmail akiwa maeneo ya kijiweni barabara ya lami
kuelekea chuo kikuu cha mtakatifu Augustino,kupitia shule ya wasichana ya
Ngaza.Adam alikuwa pamoja na rafiki yake (Huha) katika pikipiki ya rafiki yao
aliyekuwa amewaazimisha wazungukiezungukie maeneo.
"Huha hebu
endesha twende hapo Nyegezi kona kuna mtu nataka kuonana naye mara
moja"
Adam alimwomba Huha.
"Tayari Halima
ametuma meseji mwambie hatuna mafuta atufate na gari yake
bwana"
Alitania Huha huku akianza kuiondoa pikipiki
taratibu
"Ungejua hata usingesema wewe twende ukajionee maajabu
ya mwaka" alijibu Adamu huku pikipiki ikizidi kushika
kasi.
Ndani ya dakika tano tayari walikuwa Nyegezi kona ambapo
Huha alipaki pembezoni kidogo na barabara iendayo stendi kuu ya Nyegezi jijini
Mwanza,Adam alielekea dukani kununua vocha,na Huha akasogea pembeni kidogo aweze
kuvuta sigara yake.
***
Dereva akiwa mwingi wa
mawazo yake binafsi yasiyomuhusu Reshmail wala Eve na hata kama yangekuwa
yanawahusu ule haukuwa muda muafaka wa kuwaambia.
Macho ya
Reshmail yalikuwa yamekutana na bango kubwa lililoandikwa "KARIBU CHUO KIKUU CHA
MTAKATIFU AUGUSTINO" kwa hamu kubwa aliyokuwa nayo ya kumwona Adam ambaye
alikuwa pia mwanafunzi ndani ya chuo hicho ndio sababu kuu ya kujikuta akipiga
kelele kwa nguvu hali iliyomshtua dereva kutoka katika mawazo mazito na kujikuta
akiyumbisha gari huku na huko hadi ilipokutana na pikipiki iliyokuwa imepakiwa
pembezoni mwa barabara na kuirusha umbali ambao si wa kutisha
sana,
Iligeuka vurumai madereva wa teksi na bodaboda za
pikipiki walikuwa wakali sana hawakutaka kusikia la mtu,wengine hasira za kukosa
abiria tangu waingie kijiweni asubuhi walizihamishia katika tukio
hilo.
Usingekuwa upole wa yule dereva basi mawe waliyobeba
wananchi yangeigeuza ile gari kuwa mkweche. Eveline alitelemka garini kwenda
kumsaidia dereva kujitetea lakini Reshmail uoga ulimtawala akawa amejibana
kwenye viti vya nyuma vya ile gari huku akitetemeka.
"Mh! Adam
hawezi kukosa mwenyeji maeneo haya ngoja nijaribu kumpigia,ah! hii safari
imetawaliwa na mikosi dah!" aliwaza Resh huku akichukua simu yake kutoka katika
kipochi chake.
Lakini kelele zilizokuwa pale aliamini hawezi
kusikilizana vizuri na upande wa pili,taratibu huku akitetemeka alifungua mlango
akashuka na kuanza kutembea kuelekea pahali ambapo kidogo pametulia. Zaidi ya
asilimia 50 ya wananchi wenye hasira eneo lile wakageuza vichwa vyao kuangalia
kazi ya Mungu ilivyotendeka vyema katika mwili wa
Reshmail,
Badala ya kumpigia kelele dereva,miluzi mikali
ikiongozwa na dereva mkongwe wa teksi eneo lile ndugu Sanya Bonda ikahamia kwa
Reshmail,
Resh akajifanya kama hasikii vile "Ilikuwa haki ya
dereva kupotea njia jamani" Bonda alisema kwa sauti ya juu na kugeuza hasira za
watu kuwa vicheko. Resh taratibu akaufikia mti mdogo mbali na eneo la tukio
akabonyeza namba za Adam.
Simu iliita muda mrefu bila
kupokelewa. Alipopiga mara ya pili simu ilipokelewa.
"Helow
Resh subiri nisogee pembeni nakupigia kuna tatizo limenipata" alijibiwa na Adam
katika simu.
"Hata mi....." kabla hajamalizia kauli yake
Reshmail simu ilikatwa akiwa bado anaduwaa kama dakika mbili pembeni yake
alizengea kijana mmoja ambaye Resh hakutaka hata kumwangalia machoni,alijua ni
walewale waliokuwa wakipiga miluzi na kumwita majina
waliyotaka.
Resh taratibu akajisogeza
pemben.
"Vipi dada mbona wanikimbia au mi nanuka halafu we
mrembo haya basi umebarikiwa sana najua unataka kusifiwa" aliongea yule kijana
lakini Resh hakujibu.
Simu yake ya mkononi iliyokuwa katika
mfumo wa kimya(Silence mode) ilikuwa inatoa mwanga kuashiria aidha kuna ujumbe
umeingia au kuna simu inaingia,lakini kwa jinsi alivyoandamwa na yule kaka kwa
maneno hata hakuweza kugundua.
Baada ya dakika kadhaa akaondoka
yule kaka ndipo kuangalia simu akagundua ilikuwa imeita mpaka imekata na hakuwa
mwingine bali ni Adam alikuwa amepiga,harakaharaka akapiga
tena.
Ulikuwa mshangao wa hali ya juu sana Reshmail hakuamini
alipomwona yule kijana aliyekuwa ametokea pale dakika chache zilizopita kuelekea
kwenye zile vurugu ndio anapokea simu.
"Resh mbona nimekupigia
hupokei mamaa" alimshuhudia yule kaka akiongea kwenye simu huku akirejea lile
eneo kukwepa kelele,kama ilivyo kwa mtu aliyenaswa na umeme Reshmail alikuwa
ametulia tuli na simu sikioni huku yule kaka akizidi kulikaribia eneo
lile
?Reshmail mbona huongei!!? aliendelea kuuliza bila kupata
majibu.
"Adam"
Alijitutumua Resh na kutamka
akiwa jirani naye kabisa,bila kujua yule kijana akaangusha simu yake hakuamini
msichana aliyetoka kuongea nae dakika kadhaa ndio Reshmail wa
Arusha.
Vurumai lilisawazishwa haraka sana Adam na
Huha ndio waliokuwa wamiliki wa ile pikipiki iliyogongwa na gari waliyokuwemo
akina Reshmail.
"Jamani huyu hapa ni dada yangu,ndio alikuwa
amenipigia simu tuonane hapa naomba haya mtuachie sisi"
Adam
aliuambia umati ule ambao hasira zao zilikuwa zimeanza kupoa na haraka
walimwelewa wakaacha kumzonga dereva.
Reshmail bila kupoteza
muda akamwongoza Adam wakaingia garini akampa pesa taslimu shilingi laki tatu
kwa ajiri ya matengenezo ya ile pikipiki naye Adam akamkabidhi Huha kisha
akajumuika na Eve pamoja na Reshmail katika gari,huku Reshmail akiwaacha watu
hoi kwa uzuri wake wa asilia ambao hata Adam alikuwa amechachawa nao na
kukubaliana na ukweli kwamba picha zilizotumwa zilikuwa za Resh
kweli.
***
Bi Gaudensia alifika Dar-es-salaam
majira ya saa tatu usiku,bado alikuwa hajaridhika kumaliza siku yake bila
kuongea na mwanae,hivyo punde tu baada ya kuingia chumbani mwake aliamua
kujaribu kupiga namba za simu za Reshmail ambazo zilikuwa hazipatikani siku
nzima.
Furaha aliyoipata ilikuwa haisimuliki,pale simu ilipoita
upande wa pili"Mh! kalala nini huyu?" alijiuliza simu ilivyoita kwa muda mrefu
bila kupokelewa,lakini mara ikapokelewa
"Helow! samahani
Reshmail amelala"
sauti ya kiume ilijibu baada ya kupokea kisha
simu ikakatwa na kuzimwa.
Mama Resh hakuamini kuwa amesikia
sauti ya kiume katika simu ya mwanae alidhani amekosea namba lakini
alipohakikisha zilikuwa zenyewe,wivu mkali ukamshika,akajaribu kupiga mara
nyingi lakini bado hali ilikuwa ileile simu ilikuwa imezimwa usingizi
ulipaa,alitokwa na jasho,hisia mbaya zikamvuruga na kufanya kichwa chake kiume
sana,mama huyu alikuwa amejisahau kabisa kuwa Reshmail ni mwanae wa kumzaa,
alizurura kama mtu anayetafuta kitu ambacho amesahau alipokiweka pale
chumbani,alitamani kupiga kelele lakini aliamini hazitasaidia
kitu.
***
Reshmail akiwa usingizini Adam
pembeni yake,yeye(Resh) alikuwa hoi kwa uchovu wa safari na misukosuko yote
waliyopitia,na alipomaliza kuoga tu na kupata chakula alisinzia,hata simu yake
ilipoita hakuisikia hata kidogo na hata angeisikia asingeweza kunyanyuka
kupokea
"Resh ni kipetito anapiga" Adam alimuuliza Resh
aliyekuwa hoi kitandani.
"Ah! ni rafiki yangu mwambie nimelala"
alijibu kwa taabu akiwa hata hajui anachokiongea.
Naye Adam
bila kugundua kwamba Resh hajui anachokisema na ile namba ni ya mama yake Resh
alipokea na kuzungumza
Kitendo cha Adam kumkuta
Reshmail akiwa bado ni bikra kilimzuzua sana,mapenzi yake kwa Halima yalipungua
sana na kuisha kabisa hatimaye.
Siku tatu mfululizo walizotumia
pale Millenium Hotel zilitosha kuvunjilia mbali penzi la Adam na Halima na
kujenga penzi imara kati ya Adam na Reshmail.
"Mwezi wa pili
uje ujitambulishe nyumbani Adam yaani siwezi kusubiri kwa kweli nakupenda Adam
wewe ni mwanaume wangu wa kwanza na ninakuahidi nitajitunza kwa ajili
yako"
Reshmail alikuwa anamsisitiza Adam siku alipokuwa
amewasindikiza uwanja wa ndege tayari kwa wawili hawa kurejea Arusha
shuleni.
"Mama anapiga! Eve" Resh alimwambia Eve pale simu yake
ilivyoita.
"He! usiniambie huyo ndio mama,sasa mbona ulikubali
niongee nae usiku ule? aliduwaa Adam.
"Eti! uliongea nae? Yesu
wangu!"
alishtuka Resh lakini Eve akamshauri azime simu kwanza
mengineyo watajua mbele kwa mbele naye Resh akatii amri hiyo haraka akaizima
simu bila kupokea Resh kwa kiasi kukuwa alikuwa amemzoea na kumwamini
Eve.
Adam,Resh,na Eve waliagana kama watu waliofahamia na kukaa
pamoja siku nyingi sana,Resh alimkumbatia Resh alimkumbatia Adam kwa muda mrefu
hadi Eve alipowatenganisha na kuambiana
Kwaheri.
***?
Ilikuwa imebaki miezi minne
wafanye mtihani wa kumaliza kidato cha tano,Resh akiwa amekolea katika penzi la
Adam na kusahau kuhusu Mama yake ambaye alikuwa amezuiwa na mwanaye huyo kwenda
pale shuleni kumsalimia kwa madai kwamba yeye(Reshmail) anataka ajikite zaidi
katika masomo.
Reshmail kwa maksudi akabadilisha namba yake ya
simu ili mama yake asiweze kumpata mara kwa mara badala yake muda mwingi akawa
anawasiliana na Adam.
Mwezi wa pili ilikuwa ni likizo ya mwezi
mzima kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita na pia wakati huohuo
wanafunzi wa chuo kikuu cha mtakatifu Augustino huwa katika mapumziko mafupi
baada ya kumaliza muhula(Semister) ya
kwanza.
**********************?
Kwa Reshmail
ulikuwa wakati muafaka wa kumtambulisha Adam kwa wazazi wake jambo ambalo
aliamini lingesaidia kupunguza makali ya mama yake. Tangu akiwa mtoto kamwe
hakuwahi kuwakwaza wazazi wake kwa sababu ya wanaume hata siku moja hivyo
alitegemea hawatampinga.
Ilikuwa siku ya furaha kubwa sana kwa
Bi. Gaudencia na familia yote kwa ujumla kumwona tena Reshmail nyumbani baada ya
miezi mingi tena akiwa mwingi wa furaha. Lakini tofauti na mama yake
alivyofikiria kwamba mwanae huyo anafurahia kurudi katika ulimwengu wao wa
mapenzi haramu yeye(Reshmail) alikuwa anafuraha ya kumtambulisha Adam ndani ya
siku chache.
Kwa kujua wazi kabisa mama yake atachukizwa na
maamuzi yake hayo,Reshmail aliamua kulifikisha hilo mbele ya Mzee. Manyama
ambaye ni baba yake.
"Kwa sababu ni uchumba tu na hakupeleki
popote hamna tatizo hata kidogo,mlete tu mwanangu mlete una maamuzi mazuri sana
sio kama wasichana wengine wanafanya upuuzi kimyakimya mambo yanapokuwa mabaya
ndio wanasema" alijibu mzee.Manyama huku akimshika mwanae huyo
shavuni,
Resh akatabasamu na kumkumbatia baba
yake
"I love you dad(Nakupenda baba)" Resh akamwambia kwa
furaha tele mzazi wake huyo,huku moyoni akijiaminisha kwamba hapatakuwa na
kikwazo tena kwa mama yake kwani baba ndiye kichwa cha
familia.
Baada ya siku tano Adam aliwasili ndani ya kasri la
mbunge huyu.Alikuwa anaogopa na hakuamini kama angepokelewa na kama angepokelewa
alijua yatakuwa mapokezi mabaya sana kwani katika simulizi mbalimbali
anazozisikia kwa watu zilimwonyesha kwamba ni vigumu sana kwa wazazi kumwelewa
mtoto wa kike linapokuja suala la kumtambulisha mwanaume kama mchumba
wake.
"Da Rosemary nina hofu mie" Adam alimwambia dada yake
kipenzi waliyekuwa wameongozana naye
"Acha uoga bro mbona hata
sisi babu yetu alikuwa chifu? kwani chifu na mbunge nani zaidi" alitania
Rosemary kumwondoa hofu kaka yake.
Mapokezi waliyoyapata
kutokea kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo yaliwashangaza mno
waliwakuta watu wa kuwapokea na kwenda nao kwenye gari mbili walizokuja
nazo,waliwafikisha hadi getini ambapo kina dada wawili kwa heshima kabisa
waliwaongoza hadi sehemu maalum iliyoandaliwa kwa ajili yao,japo usoni
waliuficha mshangao wao lakini moyoni uliwajaa tele.
Adam akiwa
ndani ya suti nyeusi wanazotumia wanasheria katika shughuli zao na Rosemary
aliyevaa suti pia walielekezwa wapi walipo wazazi wa Reshmail wakaenda kutoa
salamu zao,ilikuwa ni hafla kubwa sana ndugu,jamaa na marafiki wapatao miamoja
walikuwa wamealikwa na mheshimiwa huyu. Ilikuwa kama harusi kwa asiyejua lakini
ulikuwa utambulisho tu.
Bwana na bibi Manyama walipendeza
kwelikweli na walikuwa na kila haki ya kuitwa wakwe na Adam. Furaha ya Bi.
Gaudencia ilificha chuki aliyokuwa nayo moyoni dhidi ya Adam kwa kumchukua
mwanae ambaye ndio alikuwa anampa raha zote za dunia.
Hadi
hafla inafikia tamati majira ya saa mbili usiku kila mtu alikuwa amepata furaha
kubwa sana,wabunge na madiwani ambao ni marafiki wa karibu wa Manyama walitoa
zawadi nyingi kwa wawili hawa huku babu yake Reshmail akitoa mawaidha yenye
maana kubwa sana katika maisha waliyotarajia kuyaishi Reshmail na Adam siku za
usoni.
Mzee Manyama kwa ombi la mwanae aliwasiliana na wazazi
wa Adam kuwa muda wa mapumziko ya siku tano alizobakiza Adam amalizie katika
familia yake,hapakuwa na kinyongo wala kipingamizi chochote walikubali kwa moyo
mmoja na Adam akaendelea kuishi pale huku dada yake akirejea Mwanza kwa usafiri
wa ndege ambao gharama zote zilikuwa juu ya mheshimiwa
Manyama.
Kila alipowasiliana na wazazi wake Adam hakusita
kuelezea upendo wa kipekee anaoupata kutoka familia ya Reshmail hata wao
walifarijika sana.
***********************
Ilikuwa
jumapili moja tulivu sana baada ya kutoka kanisani familia yote akiwemo pia
Adam,baba yake Reshmail aliongozana na mwanae kwenda mjini kwa lengo kuu la
kuonana na walimu mbalimbali wa masomo ya ziada(Tution) watakaompendeza Reshmail
basi waweze kumfundishia nyumbani.
Huku nyuma alibaki Adam
pamoja na mkwewe (Mama Reshmail) baada ya kupata kifungua kinywa Adam alimwaga
mkwewe kuwa anaenda kuzungukazunguka bustanini
"Tena nilitaka
nikwambie leo unataka uondoke hata bustanini hujawahi kufika,afadhali nenda
mwanangu" alijibu mama Reshmail.
Ulikuwa mpango kabambe
uliosukwa na Bi. Gaudencia,kwa dhumuni kuu la kumwondolea mamlaka Adam ya kuwa
na Reshmail. Kwa kuwatumia vijana kutoka katika ngome ya vigogo,ngome maalum
iliyokuwa inatumiwa na watu wenye pesa zao kwa ajili ya kuwatenda vibaya watu
wanaoonekana kuingilia mambo yao aidha kimapenzi au
kibiashara.
Alipoaga anaenda bustanini Gaudencia alitumia fursa
hiyo kupiga simu kwa wanaume hao wa shoka ambao tayari alikiwa ameelewana nao
bei.
"Ndani ya dakika tano tutakuwa hapo" ndio jibu
lililotolewa upande wa pili
Bila kuongezea lolote Bi.Gaudencia alikata
simu yake na kutoka nje.
"Babu kwa mama Veneranda si unapajua?"
alitoa swali hlo Bi. Gaudencia kwenda kwa mlinzi wao wa
getini.
"Ndio si yule mama anayesuka pale
mbele"
"Hapo hapo haya haraka nenda kaniangalizie kama kuna
foleni kubwa" aliamrisha Bi. Gaude na mlinzi akatii amri hiyo haraka haraka
akaondoka katika lindo lake akaenda kutimiza amri ya bosi wake.
Baada ya
dakika takribani kumi alirejea mlinzi yule
"Yupo mmoja tu
anamaliziwa" alileta taarifa hiyo kwa furaha.
"Haya mi ninatoka
nimemwacha Adam ndani amelala akiamka mwambie nimetoka kidogo" alisema mama
Reshmail huku akiondoka.
"sawa bosi
nitamwambia"
Masaa mawili badae alirejea akiwa amesukwa tayari
nywele zake,ni muda huohuo Reshmail na baba yake walikuwa wametoka mizungukoni,
walimkuta Gaudencia anatokea ndani.
"Babu Adam alivyoamka
ameenda wapi? au bustanini?"Aliuliza Gaudencia na
kuongezea
"Maana nimegonga chumbani kwake kimya, hebu Reshmail
ingia ukamwangalie ndani mwake humo huenda amelala bado" kwa mwendo wa maringo
lakini harakaharaka Reshmail alijongea ndani.
"Babu unasema
Adam hajatoka?" Resh aliuliza baada ya kurejea akiwa na hofu kidogo
usoni.
"Hajatoka na mimi hapa sijatoka tangu mama alipoenda
kusuka na kumwacha Adam amelala" alijieleza mlinzi yule jibu lililopokelewa kwa
furaha na Bi.Gaudencia.
Jambo gumu zaidi kwa ambao hawakujua
janja ya mama huyu ni kwamba simu ya Adam ilikuwa haipatikani hali hiyo ilileta
wasiwasi sana, walisubiri huenda atarudi hadi jioni hali ilikuwa tete ndipo mzee
Manyama alipoamua kupiga simu kituo cha polisi maeneo ya jirani kwa sababu
alikuwa mbunge msako ulianza usiku huohuo.
Siku tatu zilipita
bila taarifa yoyote kutoka katika kituo cha polisi,Reshmail alikuwa amepooza
sana kupita maelezo mara kwa mara alimpigia baba yake simu na kuuliza kulikoni
lakini jibu bado lilikuwa lilelile kuwa hajapatikana.
"Mama
niache tafadhali,tena niache nasema upuuzi wako siutaki tena niache!" alifoka
Reshmail pale mama yake alivyomkuta amekaa sebuleni na kujaribu kumpapasa huku
akimpa pole ya kupotelewa na Adam wake ghafla.
"Mwanangu usiwe
na hasira kiasi hicho polisi watafanikisha upelelezi na watamrejesha Adam akiwa
mzima wa afya" alibembeleza Bi. Gaudencia lakini Reshmail hakujibu kitu
akajiondokea akiwa ameuvuta mdomo wake sana.
Siku ya
tano polisi waliopewa jukumu la kufanya upelelezi huo walirejea na taarifa yao
huku wakiambatana na ushahidi. Zilikuwa nguo aliyokuwa amevaa Adam kwenda
kanisani ikiwa na matundu sita ya risasi na ikiwa imetapakaa damu pote, suruali
ilikuwa na matundu matatu ya risasi.
"Hapana hawezi kuwa Adam
hata kidogo nasema hawezi kuwa yeye" alifoka Manyama huku akiwa wimawima mbele
ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai jiji la Dar-es-salaam Chacha Boniphace
au maarufu kama Chacha B.
"Mheshimiwa lakini huu ni upelelezi
wa awali tunaendelea zaidi na zaidi tutazidi kutoa taarifa kadri tunavyopata
majibu mapya" alijieleza kwa utulivu bila wasiwasi kabisa jambo ambalo kidogo
lilirejesha amani ya Manyama japo hofu tayari ilishaukumba moyo wake kwamba
huenda Adam ameuwawa tena kikatili.
Ilikuwa ni shughuli pevu
kwa Reshmail kuamini kile ambacho alikuwa anaelezwa na baba yake kwamba Adam
anadhaniwa kuuwawa kwa risasi nane kisha mwili wake hauonekani. Bi. Gaudencia
tayari alikuwa anaangua kilio kikubwa hata kabla maelezo hayajaisha ikawa kazi
kwa mumewe kumbembeleza.
"Mke wangu Adam hajafa ila inadhaniwa
pia upelelezi bado unaendelea jamani,ukilia hivyo unakuaribisha msiba mama
watoto sawa" alibembeleza mzee Manyama huku amemkumbatia
mkewe.
"Baba haiwezekani baba haiwezekani nguo za Adam
zipatikane katika hali hiyo halafu mnasema hajafa,jamani Adam wangu
wamemuua"
alipiga mayowe Reshmail ikamlazimu mzee Manyama
kufanya kazi mara mbili jambo ambalo lilimtoa jasho mzee
huyu.
"Reshmail mwanangu,tulia hiyo siyo taarifa rasmi jamani
ni majibu ya awali mbona mnanifanyia hivyo au mnataka nipate presha nife?"
alijieleza Manyama huku akijifuta jasho kwa kutumia shati
lake.
Reshmail mbio mbio akaondoka pale sebuleni akaanza
kuzipanda ngazi kuelekea chumbani kwake huku akilia,mzee Manyama nae huyo nyuma
yake.
"Reshmail mwanangu,njoo malkia wangu,njoo
mwanangu"
aliyazungumza hayo huku akimkimbiza kwa nyuma. Wakati
huo Bi. Gaudencia tayari alikuwa amenyamaza kimya kabisa,akijaribu kupikicha
macho yake.
Reshmail hakusimama hadi chumbani kwake
akajifungia,baba yake alibembeleza mpaka akachoka hakupata jibu zaidi ya kilio
cha kwikwi kutoka ndani.
"Baba Resh twende chumbani mume
wangu,twende utakaa hapa hadi saa ngapi cha msingi tumwombe Mungu asije
akajidhuru mwanetu"
Gaudencia alimnyanyua mumewe wakajikongoja
kuelekea chumbani kwao,Manyama akiwa amelegea kabisa.
Asubuhi ya siku
iliyofuata naibu waziri wa ulinzi na usalama,alifika na msafara wake wa magari
matano kwa mbunge Manyama kuja kutoa pole ya kutokewa tukio hilo lenye utata kwa
mwenzao.
Shughuli ngumu iliyokuwa mbele yao ni jinsi gani
watawaeleza wazazi wake Adam ambao hadi dakika hiyo waliamini Adam yupo salama
na mwenye furaha kwa mchumba wake Reshmail,Manyama alimuomba waziri ashughulikie
hilo suala na bila kupoteza muda alinyanyua simu yake ya mkononi na kutoa
taarifa hiyo kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mwanza pamoja na
mawasiliano anayoweza kumpata baba yake Adam.
Ilikuwa vigumu
sana kwa baba Adam kuelewa anachoelezwa lakini kwa kadri ya uwezo wake na
taaluma yake mkuu huyo alifanikiwa kumwelewesha ambapo baba yake Adam aliondoka
akiwa na matumaini kwamba ipo siku Adam atapatikana.
Nyumba
nzima ya kina Adam ilipooza sana dada yake Adam (Rosemary) alikuwa analia muda
wote kwa uchungu hakuamini kwamba siku ile pale uwanja wa ndege alivyosindikizwa
na familia nzima ya mhe.Manyama ndio ilikuwa mara ya mwisho kumwona kaka yake
kipenzi(Adam).
Uongozi wa polisi uliifikisha taarifa hiyo pale
chuoni ambao pia walipokea kwa simanzi kubwa.
"MAUAJI YA
KUTISHA",
ndivyo mandishi meusi kabisa kwenye magazeti
mbalimbali yalisomeka,hali hiyo ilithibitisha kabisa kuwa Adam hayuko hai
tena.
Picha yake iliyoambatanishwa na habari hizo akiwa na
mtoto wa mbunge iliteka na kuumiza mioyo ya watu wengi hasahasa
vijana.
"Tumempoteza mwanasheria"
ndilo neno
la pamoja walilosema wasomi wa chuo kikuu cha mtakatifu Augustino Mwanza katika
misa ya pamoja kumwombea mema Adam kama yupo hai au kumtakia pumziko jema la
milele kama tayari Mungu ameichukua roho yake,kila uso ulikuwa na simanzi kubwa
ilikuwa kama tamthilia.
Reshmail alikuwa kama zezeta,hamwelewi
mtu yeyote,roho yake ilimwambia kwamba mama yake mzazi anahusika kwa namna moja
au nyingine katika tukio hili lililojaa utata.
Lakini ataanzia
wapi kumweleza baba yake,atajisikiaje mzee Manyama akigundua kwamba mke na mtoto
wake walikuwa katika ndoa haramu ya siri ndani ya nyumba
yake.
"Hapana sitaki kuongeza tatizo juu ya tatizo nitasubiri
liwalo na liwe,kama Mungu alimpanga Adam awe wangu naapa sitaolewa na mwingine
kamwe,lakini kama hakuwa halali yangu basi ataletwa mwanaume duniani kwa ajili
yangu tena"
Alijipa ujasiri wa hali ya juu Reshmail huku
akijipigapiga kifuani.
"Nitarejea shule na nitasoma tena kwa
bidii sana,sitamwaza mwanaume yeyote tena alikuwa Adam na atabaki kuwa Adam hadi
Mungu aamue tena"
aliendelea kujipa
matumaini.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment