Search This Blog

Friday, November 18, 2022

YAMENIKUTA SALMA MIE - 5

 





    Simulizi : Yamenikuta Salma Mie
    Sehemu Ya Tano (5)




    Nilifikiri angeniuliza kitu, badala yake nilimuona mwenzangu akiingiza masanduku yake na kuyaweka sebuleni kisha akaketi kwenye sofa. Alikuwa ameshika kitambaa akijipangusa pangusa usoni. Wakati naenda kuketi ili nimuulize yeye ni nani, akaniuliza.

    “John yuko wapi?”

    “John? John ni nani?” nikamuuliza. Sikwenda tena kuketi.

    “Huyu mwanaume anayeishi kwenye nyumba hii” akanijibu kwa sauti tulivu.

    “Humu ndani hakuna mwanaume anayeitwa John, labda umekosea nyumba”

    Msichana akafungua sanduku lake moja akatoa picha moja na kunionyesha.

    “Mtu niliyemuulizia ni huyu, au pia humfahamu?” akaniuliza.

    Nilipoitazama ile picha ilikuwa ni ya Chinga. Moyo wangu ukashituka.

    “Huyu si Chinga?” nikamuuliza yule msichana.

    “Chinga?” yule msichana akaniuliza akiwa amekunja uso wake.

    “Chinga ni nani?”

    “Si ndiye aliye katika picha hii”

    “Mimi najua anaitwa John, jina la Chinga silijui”

    “Basi hayupo.Kwani wewe nani?”

    “Mimi ni mke wake, natoka Nzega. Ndiyo nimefika sasa hivi”

    Moyo wangu ukashituka tena.

    “Kwani Chinga ana mke? Chinga hana mke. Siku zote ulikuwa wapi wewe?” nikamuuliza kwa kutaharuki.

    Yule msichana hakutaka kubishana na mimi.Alitia mkono wake kwenye lile sanduku akatoa hati ya ndoa pamoja na picha kadhaa za harusi. Akanionesha.

    Ile hati ya ndoa ilikuwa na jina la John Boniface ikionyesha kuwa alifunga ndoa na Vicky Leonard wilayani Nzega miaka mitatu iliyopita. Zile picha zilimuonyesha Chinga akifunga ndoa na yule msichana mbele ya Padri.

    Kwa kweli nilishituka, nilishangaa na nilichanganyikiwa si tu kujua Chinga alishaoa wakati alinidanganya kuwa hajaoa, bali pia kuona ndoa aliyofunga ni ya kikristo wakati najua ni muislamu, tena akitumia jina la John badala ya Chinga.

    “Umeamini kuwa mimi ni mke wake?” yule msichana akanieleza huku akizirudisha zile picha ndani ya sanduku.

    Nguvu zilikuwa zimeniishia na nilihisi mwili wangu ukitetemeka kwa ghadhabu, nikajikaza na kumuuliza msichana huyo.

    “Kwani siku zote hizo ulikuwa wapi?”

    “Nimekuambia ninatoka Nzega, mimi na John tulikutana Nzega na tulioana huko huko akanileta hapa Dar. Baada ya miezi michache nikapata ujauzito.Wakati wa ujauzito wangu nilikuwa nikiumwa mara kwa mara na nilidhoofika. Nilipochukuliwa vipimo nikaonekana nimeambukizwa ukimwi….”

    Alipofika hapo moyo ulinishituka kwa mara nyingine tena, sasa kujua kuwa Chinga alikuwa ana ukimwi na alikuwa ameshaniambukiza mimi.

    Msichana alikuwa akiendelea kunieleza.

    “Baada ya kugundulika hospitalini kuwa nina ukimwi nilishauriwa nimpeleke mume wangu naye akapimwe. John akakataa kwenda kupimwa. Akaniambia yeye haumwi kwa hiyo hana sababu ya kupimwa. Akanirudisha Nzega niende nikaugulie kwetu. John alipoondoka Nzega ndiyo hakurudi tena. Huu ni mwaka wa pili”

    Msichana aliendelea kunieleza.

    “Bila shaka alijua nitakufa. Mpaka namba ya simu akaibadilisha ili tusiwasiliane. Lakini nimetumia tiba ya kurefusha maisha, hali yangu ikarudi kuwa ya kawaida ingawa mtoto niliyezaa alikufa. Sasa nimerudi kwa mume wangu”.

    Msichana huyo alimaliza maelezo yake nikajikuta nimeduwaa nikimtazama. Hapo utagundua wazi kuwa nilikuwa

    nimechanganganyikiwa. Kwanza ni kwa kujua kuwa nilikuwa nimeshabambikiwa virusi vya ukimwi. Na pili kujua kuwa Chinga alikuwa na mke wake na kwa mujibu wa ndoa za kikristo asingeweza kuongeza mke wa pili.

    Jambo la tatu lililonichanganya ni kugundua kuwa Chinga hakuwa mwanaume muaminifu. Alikuwa ni laghai na tapeli kwa wanawake. Amedanganya na kufunga ndoa ya kikristo akijifanya ni mkristo wakati ni muislamu. Mbali ya hayo ameonyesha tabia ya ukatili kwa kumtelekeza mke wake mjamzito bila ya kujali mtoto wake aliyomo tumboni.

    Nilikuwa nimejitumbukiza mahali pabaya sana.Nikajifananisha na mtu aliyeruka jivu na kujikuta anakanyaga moto!

    Nilijiuliza kutokana na hali hiyo hatima yangu ingekuwa nini? Nilishatoroka kwa mume wangu kwa tamaa ya kuolewa na Chinga na kumbe Chinga mwenyewe ana mke wake na amesharudi. Sasa itakuwaje?.

    Sikutaka kuendelea kusema na akili yangu. Nilitaka nipate majibu ya haraka kutoka kwa Chinga mwenyewe. Ingawa Chinga hakuwepo Dar lakini simu zilikuwepo, ningeweza kuzungumza naye kwa simu.

    Nikamuacha yule msichana pale sebuleni nikaelekea uani.

    “Wewe dada unakwenda wapi?” yule msichana akaniuliza wakati ninaelekea uani. Sikugeuka wala sikumjibu. Nilikuwa kama nimepagawa.

    “Mbona hujaniambia John yuko wapi, unaenda zako?” akaendelea kuniuliza lakini pia sikumjibu.

    Nilipofika uani, kwa vile simu nilikuwa nayo mkononi, nikampigia Chinga. Madhumuni yangu ya kutoka uani ni kutaka yule msichana asisikie nitazungumza nini na Chinga.

    “Hellow Dear!” Chinga akasema baada ya kupokea simu yangu.

    “Nani Dear wako?” nikamjibu kwa kufoka na kuongeza.

    “Wewe Chinga kumbe ni mwanaume laghai kiasi hicho! Kama ningekujua nisingemuacha mume wangu na kuja kuishi na wewe hapa Dar”

    “Kwanini Dear unaniambia hivi?”

    “Hilo neno Dear sitaki kulisikia. Wewe ni laghai nimeshakugundua! Uliniambia kuwa huna mke kumbe ulishaoa, tena umefunga ndoa ya kanisani.Ulijifanya mkristo na jina ulibadili ukajiita John!”

    “Et! Nini?” Chinga akajifanya anang’aka. Akaongeza.

    “Mimi nilishakuambia usisikilize maneno ya watu.Wanawake wa Dar si wazuri ni wa mbeya na wanafiki. Sasa wameshakudanganya unaanza kufoka. Hao wanataka kututenganisha tu”

    “Una maana wewe hujaoa?” nikamuuliza.

    “Sijaoa. Mke wangu mtarajiwa ni wewe”

    “Hujafunga ndoa kanisani Nzega na msichana anayeitwa Vicky kisha ukamtelekeza kwao na uja uzito ulipoona umemuambukiza ukimwi?”

    Nilikuwa na hakika kwamba Chinga aligwaya baada ya kumwambia hivyo kwani sauti yake ilitoweka kwenye simu kwa sekunde kadhaa kabla ya kusikika tena ikiwa imenywea..

    “Nani amekuambia maneno hayo?” akauliza kwa ukali kidogo.

    “Si suala la kuambiwa, huyo msichana amekuja kutoka Nzega na yupo hapa nyumbani anakusubiri!” nikamwambia kwa mkazo.

    Chinga akabadilika hapo hapo na kuniuliza.

    “Unasema kweli?”

    “Sasa mimi ningemjuaje?”

    “Yukoje msichana mwenyewe?”

    “Ni mfupi wa maji ya kunde. Macho yake ni makubwa”

    “Amekonda au amenenepa?”

    “Amenenepa. Ameniambia anatumia vidonge vya kurefusha maisha”

    “Amekuja na mtoto?”

    “Hana mtoto. Mtoto alikufa. Ameniambia ulimtelekeza Nzega ulipoona ana ukimwi na wewe ulikataa kwenda kupima. Kwanini Chinga umekuwa laghai kiasi hicho?”

    “Sasa sikiliza Salma. Ni kweli huyo msichana nilioana naye lakini nilishamrudisha kwao na nilijua ndiyo tumeshaachana”

    Maneno yake yaliniongezea hasira nikamwaambia.

    “Wewe fala kweli! Maneno gani unaniambia?”

    “Salma usiwe mkali, utaharibu kila kitu. Hebu niambiye yuko wapi huyo msichana?”

    “Nimemuacha sebuleni, mimi nimekuja uani”





    “Ulimwaambia kuwa wewe ni msichana wangu?” Chinga akaniuliza.

    “Sijamwambia isipokuwa yeye ndiye aliyeniambia kuwa wewe ni mume wake, akanionesha hati ya ndoa pamoja na picha zenu za harusi”.

    “Sasa sikiliza ninavyokwambia, usithubutu kumwaambia wewe ni msichana wangu”

    “Unaona jinsi ulivyo laghai, kumbe unataka nimwambie nini?”

    “Unajua Salma inabidi tumdanganye huyo msichana ili asituletee matatizo. Halafu mimi nitajua la kufanya hapo baadaye”

    “Chinga unataka kuniletea matatizo. Sasa tumdanganyeje?”

    “Umwambie wewe ni mtumishi wangu.Usishindane naye. Mimi nitakuja kesho nitarekebisha hilo tatizo”

    Chinga aliponiambia hivyo nikaanza kumlilia.

    “Yaani mimi niwe mtumishi wenu? Chinga tulikubaliana vizuri kuwa tutaoana, nikaondoka kwa mume wangu.Sasa unanigeuka, unataka niwe mtumishi wenu?”

    “Hutokuwa mtumishi kweli, ni kiasi tu cha kumdanganya huyo msichana,vingin

    evyo anaweza kutushitaki kwa kukiuka kiapo cha ndoa yetu”

    “Lakini kwanini ulinidanganya Chinga….kwanini ulinidanganya….sasa hatima yangu itakuwa nini Chinga….?”

    “Usijali Salma.Nina mpango wa kukuhamishia kwenye nyumba yangu ya Masaki ambayo huyo Vicky haijui, usilie”

    “Siwezi kukuamini tena Chinga. Umeniharibia maisha yangu. Kwanza umeshaniambukiza virusi vyako halafu umenitengenisha na mume wangu….”

    Hapohapo mawasiliano yakakatika.Simu ilikuwa imeisha pesa. Nikachukia kwani bado nilikuwa na mengi ya kumueleza Chinga yalioacha dukuduku na hasira ndani ya moyo wangu.

    “Hata akiniambia nini siwezi kumuamini tena” nikajiambia.

    “Maisha yangu yamekwisha. Sasa,sina mume na nitakufa kwa ukimwi alioniambukiza Chinga. Kweli dunia hadaa ulimwengu shujaa na majuto huja kinyume baada ya kwisha kitendo” niliendelea kujiambia kwa hasira.

    Niliondoka pale uani nikarudi ndani.Niliingia chumbani nilimokuwa ninalala na Chinga. Nikahamisha vitu vyangu na kuvitia katika chumba cha wageni kwani chumba hicho sasa atalala mke wa Chinga. Mwenyewe Chinga ameshasema mimi nijitambulishe kama mtumishi.

    Kilikuwa kitendo cha kunishusha hadhi na kunifanya mpumbavu lakini ningefanyaje?.Nilijua kama nitajitia kidomodomo nitafukuzwa humo ndani na sikuwa na pa kwenda. Sikuwa na ndugu wala jamaa ninayemfahamu hapo Dar na nisingeweza kurudi tena kwa Ibrahim.

    Baada ya kuhamisha vitu vyangu pamoja na nguo zangu zilizokuwa kwenye kabati Chinga alinipigia simu. Nikajua wakati simu yangu ilipokatika Chinga alinyamaza akipanga uongo wa kuniambia na sasa alikwisha upata.

    “Usisikitike Salma. Mimi nitakuja kesho, nitarekebisha kila kitu. Nakuomba umpe simu huyo Vicky”

    “Nimpe simu ya nini? kama unataka kuongea naye si umpigie kwenye simu yake!”

    “Sina namba yake.Tafadhali nakuomba mpe simu, kuna kitu nataka kumwambia”

    Nikatoka mle chumbani nilimokuwa nimehamishia vitu vyangu,nikaenda sebuleni na kumpa simu yule msichana.

    “Zungumza na huyo mtu uliyekuwa unamuulizia” nikamwaambia.

    Msichana huyo akapokea ile simu na kuuliza.

    “Wewe ni John?”

    akasikiliza kisha akasema.

    “Mimi ni Vicky. Nimerudi leo kutoka Nzega.Wewe uko wapi?”

    Alipojibiwa alivyojibiwa akauliza.

    “Utakuja lini?”

    Sikujua Chinga alimjibu nini lakini baada ya kujibiwa alisema.

    “Asante sana kwa kunitelekeza. Kumbe wewe John ni mbaya kiasi hicho!”

    Akasikiliza alichoambiwa. Ingawa sikuweza kuyasikia maneno ya Chinga nilijua alikuwa akipewa uongo. Hatimaye akasema.

    “Hapa nyumbani nimekuta msichana uliyempigia simu, ni nani?”

    Moyo wangu ulishituka kidogo.Nikasubiri kusikia yule msichana atasema nini tena baada ya kusikiliza maelezo ya Chinga. Nikamsikia akiuliza.

    “Unasema ni mtumishi wako....? Sasa umeshamueleza kwamba mimi ni mke wako nimesharudi....? Kama umeshamueleza sawa …nimejifungua mtoto lakini si riziki, amekufa…sawa, basi tutaongea mengi hapo kesho utakapo rudi”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Msichana huyo akakata simu. Akaichukua ile namba ya Chinga kutoka kwenye simu yangu na kuisajili kwenye simu yake. Akawa anaiangalia angalia simu yangu kisha akaniuliza.

    “Na hii simu ulinunuliwa na John?”

    Nilijua aliniuliza hivyo kwa sababu ile simu ilimtoa roho kwani ilikuwa ni nzuri na ni ya thamani si kama kimeo alichokuwa nacho yeye. Bila shaka alikuwa akijiambia kama mimi ni mtumishi wa John nisingeweza kumiliki simu kama ile.

    “Nimeinunua mwenyewe” nikamjibu kwa sauti ambayo kama angekuwa mjuzi angedundua kuwa sikufurahishwa na swali lake kwani lilikuwa la umbeya.

    “Uliinunua kiasi gani?”

    “Laki nne”

    Nilipomjibu hivyo aliniangalia usoni kisha akanipa simu yangu. Nilidhani angeniuliza nilipata wapi hizo pesa. Nilikuwa nilishamuwekea jibu lake. Lakini kama aliyejua hakuniuliza kitu.

    Aliponipa simu yangu niliondoka pale sebuleni nikaingia katika kile chumba nilichohamishia vitu vyangu, nikafunga mlango na kujitupa kitandani. Sikuwa na hamu ya kula chakula cha jioni wala kuoga.

    Nikaanza upya kuwaza juu ya mustakabali wa maisha yangu. Nilijiambia kuwa nilikuwa nimecheza pata potea. Nilimtumainia sana Chinga aje awe mume wangu. Nilikuwa nimeyaweka matumaini yangu na akili yangu kwa Chinga. Sasa mambo yamegeuka. Sivyo nilivyokuwa nimetarajia. Maisha ya mimi na Chinga hayapo tena, badala yake nimeambiwa nibaki hapo nyumbani kama mtumishi!

    Nikajilaumu kwa kuchukua maamuzi ya kumkimbia mume wangu na kumuamini Chinga bila kutumia busara. Kwa kweli nilifanya kosa kubwa.

    Lakini si hilo tu. Kulikuwa na tatizo jingine baya zaidi la kuambukizwa virusi vya ukimwi. Kama Chinga ameweza kumuambukiza mke wake,na mimi atakuwa ameshaniambukiza. Kilichobaki kwangu ni kusubiri siku virusi vitakavyoanza kufanya kazi yake.

    Sikuweza kujua wakati huo nitakuwa wapi na sikuweza kujua nitahudumiwa na nani?.Lakini yote niliyataka mwenyewe.

    Nilikuwa nikiishi vizuri na mume wangu,nikapata ushawishi wa kwenda kumfanyia dawa za mapenzi kwa tamaa ya kupata pesa. Dawa zikampofua macho mume wangu, hali ya maisha ikazorota mpaka ikabidi nimkimbie. Na huku nilikokimbilia ninakutana na makubwa zaidi kuliko yale niliyoyakimbia.

    Wakati nikiwa katika lindi hilo la mawazo, nilisikia mlango wa chumba ukigongwa kwa kishindo. Nikajua ni yule msichana. Nikanyanyuka na kwenda kuufungua.

    “Ulikuwa umelala?” akaniuliza.

    “Nimejivyoosha tu, sijalala usingizi” nikamjibu.

    “Mbona hukuniuliza nitakula nini wakati mimi ni mgeni nimekuja, unaingia ndani unalala? Kama ninataka kitu nimtume nani?.Au huyo John hakukueleza kuwa mimi ni mke wake?”

    Maneno ya yule msichana yakanitibua. Lakini nilivuta subira.





    “Sasa maneno mengi ya nini dada? Kwani wewe ulikuwa wataka nini?” nikamuuliza.

    “Nataka chakula”

    “Zungumza na huyo John, mimi sina chakula”

    “Nina pesa yangu, nataka utoke ukaninunulie chipsi”

    Nikaguna. Sikujua kuwa niliguna kwa nguvu mpaka akanisikia.

    “Mbona unaguna? Wewe ni mtumishi wa John kweli au ulikuwa ni mwanamke wake?”akaniuliza.

    “Umenionaje?” na mimi nikamuuliza kijeuri.

    “Sikuelewielewi, mtumishi gani unatumwa unaguna, au mpaka akutume John?”

    “Wewe nipe hiyo pesa yako nikakununulie hizo chipsi, hayo mengine tumsubiri huyo John atakapo kuja”

    Bila shaka majibu yangu yalimtia hofu akanyamaza. Alitoa noti ya shilingi elfu tano akanipa.

    “Kaninunulie chipsi kavu na nusu kuku” akaniambia.

    Nilichukua ile elfu tano yake nikatoka huku nikiwa na mawazo.Niliona kama nitamkatalia anaweza kumshauri Chinga anifukuze na mimi sikuwa na pa kwenda. Nilitaka nibaki pale nyumbani nijue Chinga atachukua uamuzi gani.

    Nilikwenda katika bar moja iliyokuwa jirani ambako palikuwa na jamaa akiuza chipsi.

    Nikanunua sahani moja ya chipsi kavu na nusu kuku.Niliandaliwa na kutiliwa kwenye mfuko mdogo wa plastiki

    Wakati ninarudi nilipitia dukani nikanunua vocha kwa ajili ya simu yangu na kuijaza hapo hapo. Njia mzima nilikuwa nikimlaani Chinga kwa ulaghai wake na huku nikijilaumu mimi mwenyewe kwa kuchukua uamuzi bila kufikiri.

    Nilimkuta Vicky ameketi sebuleni akinisubiri.Alikuwa amevua nguo zake na kuvaa khanga. Alionesha kuwa alikuwa anatoka kuoga.

    “Niwekee kwenye meza” akaniambia kisha akaniuliza.

    “Kuna soda kwenye friji?”

    “Zipo” nikamjibu huku nikielekea kwenye meza. Ndani ya moyo wangu nilimwaambia “Usijifarague dada, mimi ni mke mwenzako.Tunajaribu kukuzuga tu”

    Pengine nilijisemea hivyo ili kujifariji na kujipa moyo kutokana na kule kudhalilishwa na kufanywa kama mtumwa.

    Nilimuwekea ule mfuko wa chipsi kwenye meza kisha nikaenda kumtolea soda na kumuwekea.

    Wakati ninaondoka aliniuliza.

    “Wewe unakula nini?”

    “Kula tu” nikamwaambia.

    Akainuka na kwenda kwenye meza.

    “Njoo tule” akaniambia wakati anaketi.

    Sikumjibu. Nikaondoka na kuingia chumbani. Kabla sijakaa nikasikia akiniita kwa sauti kali. Jina langu alikuwa halijui, aliniita “Wee msichana hebu njoo”

    Nikatoka na kumfuata, uso nikiwa nimeukunja.

    “Wasemaje?” nikamuuliza.

    “Hivi ni vitu gani ulivyoniletea?” akaniuliza huku akinionyesha ule mfuko wa chipsi.

    “Si chipsi na kuku, ama ulitaka nini?”

    “Kuku gani! Sijui ni nyama ya nini?.Nyama hata haikukaushwa, ina damu damu! Wewe unaweza kula nyama kama hii?”

    Aliishika na kunionyesha.

    Nilitafuta neno la kumjibu nikalikosa.Nikabaki kumtazama.

    “Nakuuliza wewe unaweza kula nyama hii?” akaniuliza tena.

    Nilivuta subira. Sikutaka kulumbana naye, nikamwaambia .

    “Bahati mbaya, sikuiona”

    “Hukuiona kwani huna macho au umefanya kusudi,maana tangu nimekuja naona umechukia?”

    Sikumjibu nikaondoka. Nilipoingia chumbani sikutoka tena.

    Usiku kucha sikupata usingizi kwa mawazo. Mawazo yaliponizidi nilijaribu kumpigia Chinga lakini simu yake ikawa haipatikani. Nikaiacha simu na kuendelea kutafuta usingizi.

    Usingizi niliupata kwa tabu. Nilipolala tu nikaota ndoto niko na Rita. Hafla ikanyesha mvua na hapakuwa na mahali pa kujisitiri. Tukawa tunatota. Mvua ikawa kali, maji yakajaa, nito ikawa inafurika. Rita akaniambia.

    “Tukimbie, maji yanakuja!”

    Wakati nainua mguu nikateleza na kuanguka chini, Rita akakimbia peke yake na kuniacha. Maji yakawa yananifuata mimi. Karibu yangu kulikuwa na jiwe kubwa, nikapanda juu ya jiwe hilo. Maji yakazidi kujaa mpaka yakanifikia kule juu. Nikaisikia sauti ya Rita aliyekuwa amesimama juu ya mlima akinicheka.

    Ndoto yangu ilikatishwa na kishindo cha kugongwa kwa mlango. Nikazinduka na kufumbua macho. Kulikuwa kumeshakucha. Nikaondoka kitandani na kuvaa khanga kisha nikafungua mlango.

    Nilimkuta Vicky amesimama mbele ya mlango.

    “Mtumishim gani unalala hadi saa mbili, hii nyumba haijafanyiwa usafi?” akaniuliza kwa kufoka.

    “Dada mbaona unanijia juu, kwani wewe ndiye uliyenileta hapa?. Kwanza mimi sikujui, huwezi kunipa amri zako!” na mimi nikamjibu kwa kufoka vilevile.

    Akanyea “Yaani wewe huwezi kufanyakazi za nyumbani mpaka uamrishwe na John!” akaniuliza lakini sasa sauti yake haikuwa na nguvu.

    “Siyo hivyo, amri zako zimezidi.Mimi mwenyewe ninajua majukumu yangu, nitafanya usafi kwa wakati wangu”

    “Basi dada nenda kalale. Hii nyumba itakuwa chafu mpaka John atakapo kuja”

    “Na ikae, kama usingenikuta mimi ungemuamrisha nani?”

    “Mimi nimeshajua wewe si mtumishi wa John, usingeniletea jeuri namna hii. Na John akija unaondoka hapa nyumbani!”

    “Utajiju…!” na mimi nikamwambia na kuufunga mlango kwa kubwata.

    “Utajiju wewe!” Nikamsikia akinijibu huku akielekea uani.

    Nilikaa kitandani nikawaza kisha nikatoka kwenda msalani. Nilipotoka msalani nikashika fagio kwa hiari yangu na kuanza kufagia.Vicky alikuwa chumbani. Alitoka baadaye na kunikuta nikifagia sebuleni. Alinitupia jicho tu na kuniminyia midomo bila kunisema chochote.

    Alikuwa amevaa nguo za kutokea na mkoba wake ulikuwa kwapani. Alipofika pale sebuleni alitoa simu yake na kuipiga. Simu ilipopokelewa nilimsikia akisema.

    “Kama nilivyokwambia, ndiyo natoka. Hapo jioni utakaporudi utanipitia kwa dada, sawa?”

    Akaisikiliza kisha akaitikia na kukata simu.Aliitia simu yake kwenye mkoba akatoka.

    Alipotoka nilikwenda kumchungulia kwa dirishani nikamuona anaelekea kwenye kituo cha daladala. Nikaendelea kumtazama mpaka alipokata kona.

    Bila shaka walishapigiana simu na Chinga tangu akiwa chumbani. Na alimwaambia kuwa nimemjibu jeuri ndipo akapanga safari ya kwenda kwa dada yake. Nikawaza.

    Niliacha kufagia nikaenda chumbani na kuchukua simu yangu. Na mimi nikampigia Chinga. Nilipiga kwa muda mrefu lakini Chinga hakupokea simu yangu. Jambo hilo lilinihuzunisha sana. Ikabidi nijiulize tena iwapo kweli Chinga bado alikuwa na dhamiri ya kuendelea na mimi.

    Kutokana na dukuduku lililonipata sikutoka tena kuendelea kufanya usafi wa nyumba. Nikajilaza kitandani na kuendelea kuwaza.

    Sikutoka mle chumbani hadi ilipotimu saa sita mchana. Nilikwenda kuchukua soda kwenye friji nikanywa na keki nilizokuwa nimeziweka jikoni kisha nikaenda kuoga.

    Niliporudi nilimpigia simu tena Chinga lakini sasa simu yake ikawa haipatikani.Nilizidi kuumia moyo wangu na kujuta kumkubali Chinga.





    Nilikaaa mle chumbani hadi jioni nikimsubiri Chinga arudi ili nijue moja, lakini hadi inafika saa nne usiku si Chinga wala Vicky aliyetokea.

    Kwa vile sikuwa nimekula mchana kutwa, nilitoka nikaenda kununua chipsi na mishikaki nikala na soda. Nilipomaliza kula nilifunga mlango na kwenda kulala.

    Asubuhi kulipokucha niliona meseji ya Chinga kwenye simu yangu iliyosema. “Usiwe mkali jifanye mjinga kwa akili yako. Nimeshakuambia nitakuhamishia Masaki”

    Kwa sababu maji yalikuwa shingoni na sikuwa na la kufanya, yale maelezo ya Chinga yalinifariji kidogo ingawa nilijua Chinga hakuwa mtu wa kuaminika.

    Nilitoka ukumbini ili niende msalani.Nikashituka nilipomuona Chinga amevaa taulo na Vicky aliyevaa khanga moja tu wakitoka chumbani na kuelekea sebuleni huku wakizungumza na kucheka.

    Wamerudi saa ngapi? Nikajiuliza kwa mshangao.

    Nikahisi bila shaka Chinga alirudi usiku wakati nikiwa nimelala.Akampitia mke wake huko kwa dada yake alikokwenda kisha wakaja pamoja.Kwa vile funguo alikuwa nayo, Chinga hakuwa na haja ya kunigongea mlango.Waliweza kufungua mlango na kuingia ndani bila mimi kujua.

    Kile kitendo cha kuwakuta wamelala pamoja kilinichoma roho, nikajiona kama nimeshatemwa isipokuwa ninadanganywa tu.

    Lakini nikajiambia nifuate vile Chinga alivyoniambia kuwa nijifanye mjinga kwa akili yangu ili nione mwisho utakuwa nini.Nikaenda msalani. Nilipotoka nikaanza kufanya usafi. Nilipofika sebuleni niliwasalimia kisha nikaendelea na usafi.

    Nilipomaliza kazi hiyo Chinga alinituma vitafunio nikaenda kununua. Niliporudi niliandaa chai mezani. Chinga akaniambia tunywe pamoja, tukaenda kunywa na mke wake.Wenyewe walikuwa wanazungumza mimi nilikuwa kimywa.

    Baada ya kunywa chai niliondoa vyombo nikaenda kuviosha. Nilipomaliza Chinga alinipa pesa niende sokoni. Niliporudi sokoni niliingia jikoni. Chinga na Vicky wakatoka. Sijui walikwenda wapi.Walirudi saa saba mchana wakati nilikuwa nimeshamaliza kupika

    Nikataka kwenda kuwaandalia chakula lakini Chinga akaniambia wameshakula huko walikotoka na kwamba chakula nilichopika tutakula jioni.

    Nikashukuru kwani kazi ya utumishi sikuipenda, nikaenda kula peka yangu.

    Tulishinda salama hadi usiku. Baada ya kumaliza kula chakula cha usiku, rafiki zake Chinga walitokea.Chinga akamueleza mke wake kwamba wenzake wamemfuata kwa ajili ya safari ya kwenda Kibaha ambako walikuwa na shughuli zao.

    “Utarudi saa ngapi?” Vicky akamuuliza.

    “Kwenye saa saba au nane hivi”

    “Sawa”

    Chinga na rafiki zake wakatoka.

    Ilipofika saa tano usiku mimi na Vicky tuliingia vyumbani kulala. Kama kawaida yangu nilikaa kitandani kwa muda mrefu bila kupata usingizi kutokana na kusongwa na mawazo.

    Wakati usingizi unaninyemelea nilisikia mlango wa mbele unagongwa kwa kishindo. Nikatega masikio na kusikiliza. Mlango ukaendelea kugongwa.Nikainuka na kukaa kitandani.Niliposikia Vicky anafungua mlango wa chumbani mwao na mimi nilifungua mlango.

    “Ni nani?” nikamuuliza.

    “Ni John amenipigia simu, anasema amepigwa risasi ya bega” Vicky akanijibu.

    Tukiwa tumeshituka tukaenda kufungua mlango.Tulimkuta John ameanguka chini kando ya mlango baada ya kuishiwa na nguvu. Mkono wake wa kulia alikuwa ameshika simu wakati bega lake la mkono wa kushoto lilikuwa linavuja damu ambayo iliunda mchirizi kuanzia alikotokea.

    “Niingizeni ndani haraka!” akatuambia.

    Wakati tunamshika ili tumuingize ndani tukasikia mbwa anabweka. Kutupa macho tuliona polisi wanne mmoja amemshikila mbwa aliyekuwa akiwaongoza kufuatilia ile njia aliyokuwa ameipita Chinga. Nyuma ya polisi hao kulikuwa na gari ya polisi inayowafuata.

    Kutokana na mwanga wa taa iliyokuwa inawaka mbele ya nyumba yetu, polisi hao walituona. Nikamuona Chinga akiachia simu na kutia mkono ndani ya shati lake akatoa bastola aliyompa mke wake.

    “Ficha hii bastola!” akamwaambia.

    Vile Vicky anaipokea tu bastola hiyo, sauti ya mmoja wa polisi hao ikatuamuru.

    “Nyote mikono juu, mko chini ya ulinzi!”

    Polisi hao walikuwa wameshafika karibu na mbwa aliyekuwa akimbwekea Chinga aliyekuwa amelala chini. Polisi wawili miongoni mwao walikuwa wametuelekezea bunduki.

    Vicky alibaki na bastola aliyopewa na Chinga akiwa hajui la kufanya. Mimi niliinua mikono juu huku nikitetemeka. Sikujua nini kilikuwa kimetokea.

    “Nyinyi wanawake ndiyo mnaofuga majambazi!” mmoja wa polisi hao akatuambia.

    “Nani jambazi!” nilithubutu kumuuliza.

    Hapo ndipo tulipoelezwa na polisi hao kwamba Chinga alikuwa jambazi na kwamba yeye na wenzake watatu walikwenda kuvunja duka moja pale Sinza lakini tayari walikuwa wamewekewa mtego na polisi. Wakavamiwa na kuanza kutupiana risasi na polisi. Chinga akapigwa risasi ya bega na kukimbia. Wenzake wawili waliuawa na mmoja alikimbia na gari walilokuwa nalo.

    Lo! Sikujua,kumbe Chinga ni jambazi? Nikawaza.

    Ni kwa sababu tu ya tamaa yangu ya kupenda pesa sasa nimejiingiza katika matatizo yasiyonihusu na nisiyo yajua.

    Wakati tunamshika ili tumuingize ndani tukasikia mbwa anabweka. Kutupa macho tuliona polisi wanne mmoja amemshikila mbwa aliyekuwa akiwaongoza kufuatilia ile njia aliyokuwa ameipita Chinga.Nyuma ya polisi hao kulikuwa na gari ya polisi inayowafuata.

    Kutokana na mwanga wa taa iliyokuwa inawaka mbele ya nyumba yetu,polisi hao walituona. Nikamuona Chinga akiachia simu na kutia mkono ndani ya shati lake akatoa bastola aliyompa mke wake. “Ficha hii bastola!” akamwaambia.

    Polisi hao walikuwa wameshafika karibu na mbwa aliyekuwa akimbwekea Chinga aliyekuwa amelala chini.Polisi wawili miongoni mwao walikuwa wametuelekezea bunduki.

    Vicky alibaki na bastola aliyopewa na Chinga akiwa hajui la kufanya. Mimi niliinua mikono juu huku nikitetemeka. Sikujua nini nilikuwa kimetokea.

    “Nyinyi wanawake ndiyo mnaofuga majambazi!” mmoja wa polisi hao akatuambia.

    “Nani jambazi!” nilithubutu kumuuliza.

    Hapo ndipo tulipoelezwa na polisi hao kwamba Chinga alikuwa jambazi na kwamba yeye na wenzake watatu walikwenda kuvunja duka moja pale Sinza lakini tayari walikuwa wamewekewa mtego na polisi. Wakavamiwa na kuanza kutupiana risasi na polisi. Chinga akapigwa risasi ya bega na kukimbia.Wenzake wawili waliuawa na mmoja alikimbia na gari walilokuwa nalo.

    Lo! Sikujua,kumbe Chinga ni jambazi? Nikawaza.

    Ni kwa sababu tu ya tamaa yangu ya kupenda pesa sasa nimejiingiza katika matatizo yasiyonihusu na nisiyo yajua.

    Baada ya polisi kutupa

    maelezo yaliyoonyesha kuwa Chinga alikuwa ni jambazi na

    alipigwa risasi wakati yeye

    na wenzazke walipojaribu kuwashambulia polisi, Chinga alibebwa juu juu na kupakiwa ndani ya gari ya polisi.

    Vicky aliyekutwa na ille bastola mkononi aliulizwa alikuwa akihusianaje na Chinga, akajibu kuwa alikuwa mume wake.Yeye naye akakamatwa..Mimi nilipoulizwa nilieleza kuwa nilikuwa mtumishi wa ndani. Jibu hilo ndilo lililonisalimisha nikaachwa nibaki na nyumba.Lakini nilitakiwa kufika kituo cha polisi cha Sinza saa mbili asubuhi na nimuulizie Inspekta Amour.





    Polisi hao walipoondoka na Chinga pamoja na Vicky niliingia ndani nikaketi sebuleni na kujiwazia. Kwa kweli nilishukuru kuwa sikuwa mke wa Chinga.

    Kumbe Chinga alikuwa jambazi!. sikuwa nikijua kuwa alikuwa akitudanganya kujidadai alikuwa mfanyabiashara anayesafiri nje ya nchi.Uongo wake ndio ulionifanya nimuache mume wangu na nimfuate yeye hapa Dar.

    Hapo ndipo nilipogundua kuwa vile vitu ambavyo amekuwa akivileta na kuviweka humu ndani ni mali za wizi. Na pia vile anavyotoka usiku nakurudi siku ya pili anakuwa katika shughuli za ujambazi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ingawa nilisalimika kukamatwa lakini kwa upande wangu hilo halikuwa tatizo la pekee. Tatizo ni maisha yangu kuparaganyika. Sasa hata ile chembe ya matumaini ya kupata maisha katika Jiji hilo sikuwa nayo tena kwani mwanaume niliyemtegemea kuwa atanihamishia Masaki ni jambazi na ameshakamatwa.

    Sikujua ni kwanini nilijiingiza katika matatizo makubwa kiasi kile. Hivi ilikuwa ni kwa sababu ya ujinga, tamaa au nini?.

    Inakuwaje anijie mtu ambaye simjui anitongoze kisha nimkubalie kirahisi vile tena si kumkubalia kuvunja amri ya sita tu bali kumuacha mume wangu na kuondoka naye kwa ahadi ya kwenda kunioa. Ulikuwa ujinga wa kiasi gani niliokuwa nao! Nilikuwa nikijiambia mara kadhaa.

    Nikiwa bado nimeketi hapo sebuleni nikiwaza nikasikia gari likisimama huko nje na kisha mlango wa mbele ukagongwa. Nikanyamaza kimya. Mlango ulipoendelea kugongwa nikauliza.

    ''Nani anayegonga?''

    ''Ni sisi polisi tumerudi tena. Fungua mlango'' Sauti ikasikika kutoka nje.

    Moyo ukanipasuka. Nikanyanyuka na kwenda kufungua mlango.

    Walikuwa ni polisi walewale. Walirudi na Vicky. Wakaingia ndani.

    ''Tumekuja kupekua humu ndani.Tunashuku kwamba kunaweza kuwa na vitu vya wizi na wewe utakuwa shahidi wa kila kitu tutakachokikuta'' Polisi mmoja akaniambia.

    Vicky akatakiwa kuwafungulia polisi hao kila chumba ili wakipekue. Kila chumba kikapekuliwa. Lakini hakukuwa na kitu chochote ambacho polisi hao walikikamata. Walipomaliza zoezi hilo waliondoka pamoja na Vicky.

    Asubuhi kulipokucha nilioga nikavaa kisha nikatoka kwenda kituo cha polisi nilikoambiwa nifike saa mbili asubuhi.

    Nilipofika katika kituo hicho nilikwenda kaunta nikajitambulisha na kumuulizia Inspekta Amour kama nilivyoagizwa na wale polisi usiku uliopita.

    Polisi mmoja akanipeleka katika ofisi moja ambapo nilikutanishwa na mmoja wa polisi waliokuja nyumbani usiku. Alikuwa amenisahau kidogo lakini baada ya kujitambulisha kwake akanikumbuka.

    Alichukua karatasi na kuiweka juu ya meza kisha akaniuliza jina langu, nikamjibu.

    ''Una umri gani?'' Ispekta huyo akaendelea kuniuliza

    ''Miaka 27''

    ''Una mume?''

    ''Sina mume'' nikadanganya

    ''Una uhusiano gani na John?''

    ''Sina uhusiano naye isipokuwa aliniajiri kama mtumishi wa ndani''

    ''Ni muda gani sasa tangu umekuwa mtumishi wake?''

    ''Nina muda wa miezi sita hivi''

    ''Je ulikuwa ukijua kuwa alikuwa anafanya kazi gani?''

    ''Kazi yake ninayoijua mimi ni ya biashara''

    ''Biashara gani?''

    ''Alikuwa akisema anasafiri nje ya nchi na kuleta bidhaa''

    ''Uliwahi kuziona bidhaa hizo?''

    ''Niliwahi kuona akileta nyumbani friji, televisheni, majiko na vitu vingine''

    ''Halafu anavipeleka wapi?''

    ''Baadaye analeta gari na kuviondoa.Mimi nilikuwa nikijua anavipeleka kwa wateja wake''

    ''Jana usiku alipotoa bastaola na kumpa mke wake wakati sisi tumetokea, wewe uliona?''

    ''Ndiyo, niliona''

    ''Inaelekea mke wake alikuwa anajua mume wake alikuwa ni jambazi''

    ''Sijui. Sina hakika''

    Wakati wote akiniuliza maswali ispekta huyo alikuwa anaandika majibu yangu kwenye ile karatasi aliyoiweka juu ya meza.

    ''Madhumuni yetu ya kukuita hapa kwanza tulitaka kuandikisha maelezo yako na pili kukueleza kuwa tumegundua kuwa John ni jambazi sugu aliyekuwa anatafutwa na polisi kwa muda mrefu. John amehusika na matukio mengi ya ujambazi hapa Jijini'' Ispekta huyo akaniambia na kuongeza

    ''Katika moja ya matukio ya uporaji aliyoyafanya ni uporaji wa gari aina ya Rav 4 ambayo jana usiku baada ya kumhoji akiwa hospitali ya Muhimbili alikiri kuhusika na uporaji wa gari hiyo na akatuambia alilipeleka kwao Tanga kulificha.Usiku huo huo tuliwasiliana na polisi wenzetu waliopo Tanga walifuatilie gari hilo huko Kisosora alikolificha. Na leo asubuhi wametufahamisha kuwa wamelikamata nyumbani kwa baba yake''

    Nikakumbuka kuwa ni kweli Chinga alipokuja Tanga alikuwa na Rav 4 akadai kuwa ni mali yake. Lakini tulipokuja Dar aliliacha gari hilo tukapanda basi. Kumbe lilikuwa gari la wizi.

    ''Sasa tunasubiri tukamilishe upelelezi wetu ili afikishwe mahakamani yeye na mke wake'' Ispekta huyo akaendelea kuniambia.

    Baada ya hapo aliniruhusu niende zangu. Nikaondoka kituoni hapo mwili ukiwa wangu umetota jasho.

    Wanaume kweli ni walaghai na kama sisi wanawake hatutakuwa waangalifu tutaingizwa katika matatizo siku zote. Kilichoninusuru mimi kukamatwa ni kuonekana ni mtumishi wa John, vinginevyo na mimi ningekuwa nimetiwa ndani.

    Niliporudi nyumbani niliketi sebuleni na kuwaza nifanye nini. Chinga niliyekuwa nikimtegemea hapa Dar ameshakamatwa na sikutarajia kuwa atatoka jela leo. Huenda akafia huko huko. Sasa maisha yangu yatakuwaje?

    Ghafra nikasikia mlango unabishwa. Nikainuka na kwenda kuufungua. Nikamuona mtu mmoja aliyewasili na gari. Akanisalimia kisha akaingia ndani.

    Akasimama sebuleni na kunitambulisha kuwa yeye ndiye mwenye nyumba ile ambayo alikuwa amempangisha Chinga. Akaniambia kuwa amepata habari kuwa Chinga ni jambazi na amekamatwa na polisi. Hivyo alikuja kufunga nyumba yake.

    ''Kwa vile ninamdai kodi ya miaka miwili itabidi nizuie kila kitu kilichomo humu ndani!'' akaniambia

    Kumbe ile nyumba pia Chinga haikuwa yake!

    Baada ya yule mtu kunieleza hayo nilipigwa na butwaa nikawa sina la kumjibu.Alipoona nimeduwaa akaniuliza.

    “Kwani wewe ni nani wake?”

    “Mimi ni mtumishi wake wa ndani” nikamjibu. Jina la utumishi nilikuwa silitaki lakini sasa nililing’ang’ania kwa kujua ndilo litakalo ninasua na matatizo ya Chinga.

    “Sasa utalazimika uondoke. Kama una madai yoyote itabidi uyapeleke polisi.

    “Unaniambia niondoke, niende wapi?” nikamuuliza.

    “Utajua mwenyewe pa kwenda. Hapo umekuja kwa hicho kibarua na kibarua kimeshaota nyasi.Tajiri yako amekamatwa na si wa kutoka leo, sasa utakaa hapa ungoje nini?”

    Sikuwa na la kumjibu, nikabaki kimya nikiwaza.

    “Fungasha kila kitu chako ninataka kufunga nyumba yangu” yule mtu akaniambia sasa kwa kusisitizia.

    “Naomba unisubirishe kidogo niende kwa jirani nikamueleza matatizo yangu”

    “Ukichelewa utakuta nimeshafunga nyumba” akaniambia.

    “Sitachelewa”

    Nilitoka nikaenda nyumba ya tatu kutoka ile yetu ambapo kulikuwa na mashoga zangu wawili waliokuwa wakiishi humo. Mashoga hao Mariamu na Sikuzani tulizoeana hapo hapo mtaani. Mara kwa mara tulikuwa nikitembeleana na kupiga stori.







    SASA ENDELEA

    Nilipofika niliwakuta wamekaa barazani wakizungumza. Nikawaeleza matatizo yaliotokea pale nyumbani kwetu. Nikawambia kwamba licha ya Chinga kukamatwa, mwenye nyumba amenifuata kunitoa akitaka kufunga nyumba yake kwa sababu anamdai Chinga kodi ya miaka miwili na pia hataki mpangaji ambae ni jambazi.

    “Sasa umechukua uamuzi gani?” Mariamu akaniuliza.

    “Nichukue uamuzi gani shoga na mwenye nyumba anataka nyumba yake. Itabidi nitoke na pakwenda sipajui. Sasa nilikuwa naomba nijihifadhi hapa kwenu kwa siku mbili tatu ili nijue nitaenda wapi”

    “Na vile vitu vilivyomo mle ndani utavipeleka wapi?” akaniuliza Sikuzani.

    “Mimi nitachukua vitu vyangu vidogovidogo tu.Vile nilivyovikuta nitaviacha. Mwenye nyumba amesema atavizuia kwa sababu anadai kodi ya miaka miwili”

    Baada ya kunisikiliza kwa makini Mariamu akaniambia.

    “Sasa shoga kama unavyotuona tuko wawili na chumba chetu ni kimoja, kama utaweza kujibana humo humo chumbani kwa siku hizo tatu, karibu”

    “Nitawashukuru mashoga zangu kwa msaada huo kwani mwenzenu nimechanganyikiwa” nikawambia.

    “Wala usichanganyikiwe shoga. Hali hiyo ni ya kawaida Jijini hapa. Kila siku watu wanatimuliwa kwenye nyumba za watu.Wengine hutolewa nyumbo na kuwekewa nje, hawajui pa kuvipeleka. Ni afadhali wewe umesitirika”

    “Basi mashoga zangu ngojeni nikafungashe vyombo vyangu nivilete”

    Nikarudi nyumbani na kuanza kukusanya nguo na vitu vyangu vingine, nikavitia kwenye mabegi mawili. Begi moja lilikuwa langu mwenyewe na jingine nililichukua mle ndani. Nikachukua ndoo tatu za plastiki. Mbili nilizijaza vyombo vya kutumia kama vile sufuria, sahani, mabakuli, vikombe na kadhalika. Ndoo moja nikaitia vitu vilivyokuwemo ndani ya friji.

    Kwanza nikapeleka begi moja kisha nikarudia jingine. Nilipomaliza mabegi, nilibeba zile ndoo. Nilitangulia kubeba ndoo mbili kisha nikairudia ile moja.

    Nilipomaliza nilimwaambia yule mtu aliyekuwa akinisubiria kuwa nimeshaondosha vitu vyangu ingawa vingine nilivyochukua havikuwa vyangu bali nilivichukua nikaanzie maisha huko mbele ya safari.

    Yule mtu akafunga milango ya vyumba vyote.Nikatoka naye, akamalizia kufunga mlango wa mbele kisha akaniaga na kuingia kwenye gari yake. Na mimi nikaondoka kwenda kwa mashoga zangu.

    Mambo ya Dar ni makubwa!.Wale mashoga zangu ni wasichana warembo kweli kweli lakini nilipoingia chumbani mwao kuweka vyombo vyangu niliona hawakuwa na kitanda. Walikuwa wanalala kwenye godoro lililowekwa chini na kufungiwa chandarua. Humo chumbani mwao hamkuwa na chochote zaidi ya kimeza kilichokuwa na vipodozi pamoja na kipande cha kioo kilichovunjika.

    Zaidi ya hapo walikuwa na ndoo karibu nne zilizokuwa na maji na madishi matatu, mawili yakiwa yamejaa vyombo. Nguo zao walikuwa wakiweka kwenye mabegi, kila mmoja alikuwa na begi lake. Kwa kweli kile chumba kilikuwa kama geto.lakini nilishukuru kupata sitara kwani sikuwa na pa kwenda.

    Ingawa niliwaambia mashoga hao kuwa ningekaa hapo kwa siku mbili tatu, ukweli ni kuwa sikujua nitaenda wapi baada ya siku hizo. Hapo ndipo nilipoanza maisha kwa mashoga zangu hao. Habari ya Chinga nikaisahau kabisa. Kama nikudanganywa nimeshadanganyw

    a na kama ni balaa limeshanikuta.Sikuwa na haja ya kufikiria tena yaliyopita.

    Zile siku tatu nilizowaahidi wale mashoga zangu zikapita lakini hakukuwa na aliyeniuliza.

    Maisha yalikuwa tofauti sana. Pale tulikuwa tunaishi kihuni. Wale wasichana tunakuwa pamoja mchana, tunapika kwa kuchangia hela na tunakula pamoja. Ikifika usiku wenzangu wananiachia chumba na tunakutana tena asubuhi.

    Baada ya wiki mbili nikaanza kuishiwa hela ya kuchangia chakula.Wenzangu walinisaidia kwa siku tatu. Siku ya nne wakaniambia watakapo toka usiku nitoke nao.

    Ilipofika usiku wakati wenzangu wakijipara na mimi nikajipara.Tukatoka pamoja. Hawakuwa wakienda mbali.Tulizunguuka mtaa wa pili ambako kulikuwa na baa na gesti humo humo.Tukaingia katika ile baa tukakaa kwenye viti.

    Jinsi wenzangu walivyokuwa wakisalimiana na wahudumu wa baa ile walionekana kuwa ni wenyeji. Mara kwa mara wahudumu hao walikuwa wakiwauliza Mariamu na Sikuzani.

    “Mmetuletea mgeni?” na wao walijibu “Nishoga yetu tunamtembeza tembeza”

    Wakati tumeketi mashoga zangu wakaanza kunisomesha.Wakaniambia hapo baa ndiyo mahali wanapopatia riziki zao kutoka kwa wanaume wanaotaka huduma zao.

    Nilivyowaelewa ni kwamba walikuwa wanajiuza. Hakukuwa na aliyeniambia wamenileta hapa kwa ajili ya gani, ilikuwa ni akili kichwani mwangu kwamba na mimi nijiunge nao.

    Sikutaka kujivunga wala kushangaa kwa sababu kwa upande wangu maji yalikuwa shingoni. Sikuwa na namna ya kuishi katika jiji hilo.Ilibidi niwaige wenzangu ili nipate namna ya kuishi kwani sikutaka kurudi Tanga.

    “Sasa wenzangu mnieleweshe inakuwaje?” nikawauliza huku nikilazimisha kicheko cha uongo ili wasizielewe hisia zangu kwamba jambo hilo sikulipendelea hata kidogo lakini sikuwa na budi.

    Mariamu ndiye aliyechukua jukumu la ualimu akaniambia.

    “Akitokea mteja akitaka kutoka na wewe, mwaambie kwanza akununulie bia unywe kiasi kidogo tu cha kukuondoa aibu na kukufanya uchangamke. Usinywe sana kiasi cha kutojitambua kwani atakwenda kukufanya vitendo visivyo na maana. Umenielewa shoga?

    “Nimekuelewa”

    “Ukifika huko mtakako kwenda patana naye bei kwanza. Sisi tunamuangalia mtu uwezo wake na pupa yake. Kama tumemgundua ana pesa na anakupapatikia unamtoza shilingi elfu hamsini kwenda mbele kwa kulala naye. Kama unamuona ni wa kawaida tu akikupa hata ishirini unakubali”

    “Sasa ninamuambia anipe kabisa au….?”

    “Anaweza kukupa kabisa au asubuhi mkitoka. Kuna wakati wa ambao, wateja hana hata elfu kumi unachukua. Na kuna wateja wengine wanatumia gesti hii hii. Unalala naye hapa hapa”

    Nikawa natingisha tingisha kichwa kuonesha kumkubalia.

    “Kuna wanaume wengine ni wa ‘short time’.Hao kwa usiku mmoja unaweza kuwapata wengi siku za mwisho wa mwezi”

    “Na hao mnawatoza kiasi gani?”

    “Unapatana naye. Akiingia sawasawa unamla hata elfu kumi na tano lakini isiwe chini ya elfu kumi”

    Wakati tunazungumza walitokea wanaume wawili,wakajiunga na sisi. Waliagiza bia na sisi walitununulia bia moja moja. Tukawa tunakunywa huku tunazungumza. Mmoja wa watu hao alionekana kunipenda mimi na mwengine akaelemea kwa Mariamu.

    Sikuwa na shaka kwamba walikuwa wanajua kuwa kukaa kwetu pale baa ilikuwa ni kwa ajili ya kusubiri wanaume. Kwa kweli nilikuwa nikiona aibu kwa sababu licha ya kwamba kazi yenyewe ni ya aibu nilikuwa sina uzoefu nayo.

    Baada ya mazungumzo marefu jamaa hao wakataka tukachukue vyumba pale gesti.Wakati huo tulikuwa tumeshakunywa bi a mbili mbili.

    Niliondoka na mwenzangu Mariam kwenda upande wa gesti.Wakati tunakwenda Mariam aliniambia.

    “Mkiingia chumbani patana naye kabisa. Wanaume wengine hawaaminiki. Kama atataka mlale wote utamwambia akupe shilingi elfu ishirini lakini usimpunguzie chini ya kumi na tano. Na kama ni ‘short time’ ni elfu kumi na tano na isiwe chini ya elfu kumi.Umenielewa?”

    “Nimekuelewa”

    Mtoa vyumba alikuwa mwanaume. Mariam ndiye aliyezungumza naye.

    “Ni vyumba vya ‘short time’ au vya kulala?” jamaa huyo akatuuliza.

    “Hatujajua” Mariam akamjibu

    “Atalipa nani?”

    “Watalipa wao.Tupe hivyo vyumba, mwenzangu atamsubiri mtu wake chumbani. Mimi nitakwenda kuwaita wakija utawauliza. Kama ni ‘short time’ au vya kulala utawatoza kabisa”

    “Sawa”





    Jamaa akatufunguliwa vyumba viwili. Mariam akaniambia niingie kwenye chumba kimoja nimsubiri yule mwanaume aliyenitaka mimi. Nikaingia na kuketi kitandani. Baada ya kama dakika kumi hivi mlango ukafunguliwa.Yule mwanaume akaingia.

    “Ni mpaka asubuhi au ni short time?” nikamuuliza hapo hapo.

    “Ni short time” akanijibu.

    “Umeshalipa chumba?”

    “Nimeshalipa”

    Nikamuona anavua shati

    “Hebu njoo ukae hapa kwanza tuzungumze” nikamwambia.

    Mwanaume huyo aliyeonekana kuwa na pupa akaja kitandani na kuketi na mimi.

    “Utanipa shilingi ngapi?” nikamuuliza.

    “Wewe unataka ngapi?”

    “Elfu ishirini” nikamjibu.

    “Mimi nina kumi” akaniambia.

    “Nitakufanyia kumi na tano”

    “Sikufichi short time huwa tunalipa hiyo kumi, kulala ndiyo ingekuwa kumi na tano” jamaa akaniambia.

    “ Kwanza mimi kulala ni ishirini, short time ndiyo hiyo niliyokuambia”

    Nikamuaona anaendelea kuvua shati.

    “Tukubaliane kwanza”

    “Si umeshakunywa bia zangu mbili, ukichanganya na elfu kumi nitakayokupa ni zaidi ya hizo unazotaka” akaniambia.

    Kwa vile Mariam aliniambia hata elfu kumi naweza kupokea kwa short time, nikamwaambia.

    “Sawa”

    Ilikuwa siku nzuri kwa upande wangu kwani nilipata wanaume watatu wa kuingia na kutoka na mwanaume mmoja wa kulala ambaye alinipa shilingi elfu kumi na tano. Niliondoka hapo gesti saa kumi na mbili asubuhi kurudi nyumbani.

    Mariam alipata mwanaume mmoja wa kuingia na kutoka na mmoja wa kulala. Sikuzani alipata mwanaume mmoja tu wa kulala. Sikujua wenzangu walikuwa wamepata shilingi ngapi lakini waliniuliza mimi nimepata kiasi gani. Nikawaambia kiasi nilichopata.

    Tuliporudi nyumbani tulipiga mswaki na kuoga. Baada ya kuvaa nilitoka. Nilikwenda kwenye bucha ya nyama, nikanunua kilo moja ya nyama. Nikaenda gengeni nikanunua kilo moja ya mchele na vitakataka vingine vya kupikia. Nikapitia dukani ambako nilinunua mikate miwili na siagi, nikarudi nyumbani na kupika chai.

    Chai ilipokuwa tayari nikawakaribisha wenzangu tukanywa kisha tukarudia kulala mpaka saa tano tulipoamka na kuanza kushughulikia kupika.

    Maisha yakawa hivyo. Taratibu na mimi nikaanza kuizoea ile kazi. Kuna siku nilienda kupima HIV nikaambiwa nimepata maambukizo. Kwa vile hilo nilishalijua, sikuwa na wasiwasi. Niliambiwa kinga yangu bado ilikuwa na nguvu hivyo nikatakiwa kila mwezi niende kwenye kile kituo kupima tena ili niweze kushauriwa muda wa kuanza kupata dozi ya kurefusha maisha.

    Hata hivyo nilishauriwa nisiache kutumia kinga (Condom) ili nisiambukize wengine na mimi nisiendelee kuambukizwa.

    Kutokana na kazi yangu ya uchangudoa ilikuwa ni vigumu kufuata ushauri huo kwani nilikutana na wanaume ambao walikuwa hawataki kutumia kinga. Kwa vile mimi mwenyewe tayari nilikuwa muathirika niliwakubalia.

    Zilikuwa zimepita kama wiki tatu tangu nianze kazi ile ya kujiuza ambayo kwa kweli inalipa ingawa ni ya fedheha. Usiku mmoja wakati tumeketi na wenzangu pale bar tukisubiri wateja alikuja mwanaume mmoja akatunywesha sana kisha akaondoka na Sikuzani. Sikujua walikwenda wapi.

    Baadaye alikuja mwanaume mwingine akaendelea kutunywesha mimi na Mariam mpaka mimi nikawa sijielewi.

    Nakumbuka Mariam aliondoka na yule mwanaume akaniacha peke yangu. Lakini baadaye kidogo alikuja mwanaume mwingine akawa ananisemeshasemesha.

    Vile ambavyo nilikuwa nimelewa sana sikumbuki hata mazungumzo tuliyokuwa tumezungumza. Baadaye akaja Mariam na kunichukua. Alinishika mkono na kuniambia.

    “Twende huku”

    Nikamuacha yule jamaa kwenye kiti. Tulikwenda upande ule wa gesti. Mariam akaniambia.

    “Kuna jamaa anataka msichana wa kulala naye na ameshaingia chumbani. Sasa wewe nenda ukalale naye”

    “Yuko chumba gani?” nikamuuliza

    Mariam akanipeleka mpaka kwenye mlango wa chumba hicho.

    “Yumo humu.Yeye amelewa na wewe umelewa. Sasa mtajuana wenyewe lakini usisahau kupatana naye kabisa. Asije akakugeuka asubuhi”

    “Sawa”

    Nikaufungua mlango na kuingia humo chumbani. Nilimkuta huyo jamaa amejilaza kitandani. Alipoona naingia akainuka na kuketi. Na mimi nikaenda kuketi naye pale kitandani.Alikuwa amelewa sana.

    Nilipoketi alinizunguushia mkono kiononi,akaniuliza. “Mrembo hujambo?”

    Nikamjibu “Sijambo, nakuhofia wewe”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilikuwa nataka msichana mrembo kama wewe” akaniambia.

    “Ndiyo mimi nimeshakuja.Unataka short time au kulala kabisa?” nikamuuliza kwa sauti ya kilevi.

    “Kulala kabisa”

    “Utanipa shilingi ngapi?”

    “Sijui wewe unataka shilingi ngapi?”

    “Elfu thelathini”

    “Elfu thelathini zote za nini? wewe msichana mbona una tamaa sana ?”

    “Sasa utanipa ngapi?”

    “Kwa vile ni mzuri sana nitakupa elfu ishirini”

    “sawa”

    Nikalala naye.

    Asubuhi kulipokucha, mimi ndiye niliyeamka kwanza. Nikaenda maliwatoni kisha nikarudi na kuvaa. Wakati ninavaa yule jamaa naye akaamka na kuketi kitandani.







    Nikamfuata pale kitandani ili anipe changu niondoke. Macho yetu yakakutana. Moyo wangu ulishituka nilipomgundua kuwa ni Mashaka mdogo wake mume wangu Ibrahim niliyemkimbia Tanga.

    Na yeye aliponiona alishituka akawa amenitumbulia macho.

    “Wewe si Salma mke wa kaka Ibrahim?” akaniuliza.

    “Kwenda zako!” nikamwambia kwa kutaharuki.

    Nikawa nageuka ili nitoke mle chumbani. Sikutaka tena pesa yake.

    Mashaka akanishika mkono.

    “Yaani umekuja huku Dar ku…”

    “Hebu niache!”

    Niliukutua mkono wake kisha nikamtandika kibao. Nikaenda kwenye mlango nikaufungua na kutoka. Kwa kujua kuwa angeweza kunifuata na kwa aibu niliyoipata, nilitoka mbio.

    Nilipotoka hapo gesti niliendelea kwenda mbio kuvuka barabara bila kujua kuwa kulikuwa na gari inakuja. Hafla nikashitukia nikipigwa kikumbo. Ninachokumbuka ni kuwa gari hilo lilinigonga likaniburuza na kunitumbukiza kwenye mfereji uliokuwa kando ya barabara. Fahamu zikanipotea hapo hapo.

    Sikujielewa tena.

    Nilipokuja kuzinduka ilikuwa ni siku ya pili yake. Nilijikuta nimelazwa kwenye chumba cha hospitali ya Muhimbili. Kitu cha kwanza kunitambulisha kuwa nilikuwa hospitalini ni ile harufu ya dawa niliyoisikia.

    Baada ya kuzinduka, mara moja niligundua hitilafu katika mwili wangu. Jicho langu la upande wa kushoto lilifungwa bendeji wakati jicho la kulia halikuweza kuona sawasawa na lilikuwa linakereketa na kuniuma.

    Hata hivyo nilijikuta na bendeji katika kila sehemu ya mwili wangu. Kwanza sikujua nilikuwa nimefanya nini.Lakini wakati najiuliza ‘kulikoni?’ ndipo kumbukumbu zilipoanza kunijia.

    Nikalikumbuka lile tukio la kumkimbia Mashaka mdogo wake Ibrahim kwenye chumba cha gesti. Nilipotoka nje ya gesti kulikuwa na gari linakuja. Gari hilo lilinigonga wakati ninavuka barabara.

    Hapo ndipo nilipojua sababu ya kuwa pale hospitali. Nikajaribu kujiinua pale kitandani ili nikae lakini nilishindwa. Mkono wangu mmoja ulikuwa umewekewa mpira wa damu na mwili wangu ulikuwa kama uliokufa ganzi.

    Nikapata hisia kwamba mguu wangu mmoja haukuwepo. Nikatumia mkono wangu mmoja kujifunua shuka niliyokuwa nimefunikwa kisha nikainua kichwa na kujiangalia. Nikaona mguu wangu wa kulia ulikuwa umekatwa!

    Nikapiga yowe na kuzirai hapohapo!

    Sikuweza kujua nilipotewa na fahamu kwa muda gani baada ya kuzirai lakini nilipozinduka nilimuona daktari akinipima mapigo ya moyo.

    Kadhalika nyuma ya daktari palikuwa na polisi wa usalama barabarani ambaye alikuwa amesimama akiniangalia.Baada ya daktari kunipima mapigo ya moyo aliniuliza.

    "Unajisikiaje?"

    "Sijisikii vizuri" nikamjibu kwa sauti dhaifu.

    "Ni sehemu gani unasikia maumivu?"

    "Kwenye miguu" nilimjibu lakini ukweli ni kwamba maumivu zaidi niliyoyasikia ni ya uchungu wa moyo wangu.

    "Mguu upi huo, ni huu mzima au uliokatwa?"

    Swali hilo lilinizidishia uchungu. Sikuweza kumjibu. Nikanyamaza kimya.

    "Kama ni huo uliokatwa bado una kidonda. Utaendelea kupata nafuu kadri kidonda kitakavyo kauka" Daktari akaniambia.

    "Kwanini nimekatwa mguu wangu?" nikamuuliza daktari huyo kama vile aliukata kwa makusudi.

    "Ulivunjika vibaya. Kwa kweli usingiweza kuungika hata kidogo"

    Nikahisi machozi yakinitiririka kwenye jicho langu moja.

    "Usisikitike sana. Shukuru kwamba uko hai. Ajali iliyokukuta ilikuwa ni moja ya ajali mbaya sana".

    Nikawa nafuta machozi kwa mkono wangu.

    "Nilitaka kukueleza kuhusu macho yako. Macho yako yameingia vipande vya vioo. Jicho lako moja limeharibika kabisa, haliwezi kuona. Na hilo moja litakuwa linaona kwa tabu kwa wiki zisizo zaidi nne” Daktari huyo akaniambia na kuongeza.

    “Kuna kipande kidogo cha kioo kimeingia kwa pembeni. Sisi hatuna uwezo wa kukitoa. Utawafahamisha ndugu zako watakapo kuja kukuangalia kwamba unahitajika kupelekwa India ili ukafanyiwe oparesheni ya kukutoa kabla hakijaharibu mboni ya jicho lako"

    Hapo nilishituka sana.

    "Kumbe hili jicho lililofungwa limeharibika kabisa na hili jingine mpaka lipelekwe India!"

    "Ndiyo"

    "Hizo pesa za kupelekwa India anatoa nani?" nikamuuliza.

    "Inabidi watoe ndugu zako"

    "Ni kiasi gani?"

    "Kwa pesa zetu unahitajika uwe na milioni nane. Hizo zinahusisha usafiri wako wewe na mtu atakae kupeleka kwenda na kurudi pamoja na gharama ya matibabu"

    "Lakini mimi sina ndugu hapa Dar"

    "Kwani unatokea mkoa gani?"

    "Natokea Tanga"

    "Utawasiliana na ndugu zako waliyoko Tanga"

    Nikaguna.

    "Hata huko Tanga sina ndugu mwenye pesa hizo"

    "Sasa sijui tutafanyaje kwa sababu operesheni yako inahitajika ifanyike ndani ya wiki nne. Wiki nne zikipita jicho lako litaharibika kabisa. Hutaweza kuona tena"

    Maneno hayo ya daktari yalinifanya niangue kilio. Daktari akanibembeleza lakini nikawa simsikilizi tena. Mwisho akaniambia.

    "Kuna askari hapa wa usalama barabarani,anataka kuzungumza na wewe"

    Nikamtazama yule askari. Daktari akamwaambia.

    "Unaweza kuzungumza naye"

    Daktari akaondoka na kutuacha.

    Yule polisi alinisogelea pale kitandani akaniambia.

    "Nyamaza dada yangu ili tuweze kuzungumza"

    Nikajifuta machozi yangu kisha nikamtazama.

    "Unaitwa nani?" akaniuliza.

    Nikamtajia jina langu. Akaandika kwenye jalada alilokuwa amelishika.

    "Una umri gani?" akaniuliza tena

    Nikamjibu.

    "Umwenyeji wa wapi?"

    "Tanga"

    "Unaishi wapi hapa Dar?"

    "Kwa hapa Dar nilikuwa ninaishi Sinza"

    "Umfanyakazi au ni mama wa nyumbani?"

    "Ni mama wa nyumbani"

    "Una mume?"

    "Ndiyo lakini yuko Tanga"

    "Anaitwa nani?"

    Nikamtajia jina la mume wangu Ibrahim.

    "Tangu umeletwa hapa hospitali alishafika kukuangalia?"

    "Bado"

    "Lakini anayo taarifa kwamba umepata ajali?"

    "Hana taarifa"

    "Kwanini?"

    "Hakukuwa na mtu wa kumuarifu. Hapa Dar mimi ni mgeni,nilikuja mara moja tu ndiyo nikapata ajali. Natamani sana niwasiliane naye lakini simu yangu iliibiwa"

    "Namba yake unaikumbuka?"

    "Ndiyo ninaikumbuka"

    Polisi huyo alitoa simu yake na kuniambia.





    "Nitakusaidia uwasiliane naye kwa sababu kuna suala la wewe kupelekwa India. Nitajie namba yake"

    Nikamtajia.

    Polisi huyo akaipiga namba hiyo kisha akaiweka simu sikioni. Baada ya muda kidogo akauliza.

    "Wewe ni Bw Ibrahim?"

    Sikuweza kusikia alichojibiwa. Akaendelea kusema.

    "Sawa. Sasa bwana kuna tuikio limetokea hapa Dar. Mke wako Bi Salma alipata ajali ya gari jana asubuhi na amelazwa hapa katika hospitali ya Muhimbili. Sijui kama unataarifa hizo?"

    Wakati polisi huyo akizungumza hivyo moyo wangu ulikuwa ukinienda mbio. Sijui Ibrahim alimjibu nini lakini nilimsikia yule polisi akimtajia wodi niliyokuwepo kisha akasikiliza kidogo kabla ya kukata simu.

    "Amesemaje?" nikamuuliza yule polisi kwa haraka.

    "Kumbe na yeye yuko hapa hapa Muhimbili.Amesema alikuja wiki moja iliyopita kufanyiwa operesheni ya macho yake.Leo ndiyo amepewa ruhusa. Atakuja hapa hapa kukuona"

    "Kumbe yuko hapa hapa Muhimbili?" nikamuuliza yule polisi.

    "Inaelekea huna mawasiliano na mume wako. Kwani hujui kuwa mume wako yuko hapa?"

    Nikatunga uongo hapohapo.

    "Tatizo ni simu yangu iliibiwa"

    "Basi sasa mtakutana hapa hapa"

    "Amekwambia hivi sasa anaona?"

    "Kwani alikuwa haoni?"

    "Alikuwa haoni kabisa"

    “Natumaini hivi sasa atakuwa anaona kwa sababu amesema anakuja kukuona"

    "Na aje, nataka nionane naye"

    Baada ya kupita nusu saa hivi, mlango wa chumba nilichokuwamo ulifunguliwa..Kwanza aliingia yule daktari aliyekuwa ametoka kisha akaingia mtu mwingine. Nikamkazia jicho langu moja lililokuwa halioni sawasawa na nikagundua alikuwa Ibrahim mume wangu.

    Safari hii alikuwa amevaa miwani ya macho yenye vioo vyeupe

    badala ya ile ya jua. Macho yake niliweza kuyaona. Sasa yalikuwa yanaona. Nikasadiki kuwa Ibrahim alikuwa amepona.

    "Msichana uliyemuulizia ni huyu hapa, je unamfahamu?" daktari huyo aliyeingia akamuuliza Ibrahim.

    Ibrahim alisogea karibu na kitanda na kuniangalia vizuri. Nikamuona akitikisa kichwa.

    "Simfahamu" akamwaambia yule daktari.

    Jibu lake hilo lilinishitua.

    "Mume wangu Ibrahim, mimi ni Salma mke wako nimepata ajali ya gari. Nimekatwa mguu wangu na jicho langu moja limeharibika." nikamwaambia kwa mkazo ili aweze kunitambua.

    "Unasema ulipata ajali?" akaniuliza.

    "Ndiyo mume wangu nilipata ajali" nilimjibu kwa unyonge na kwa nidhamu"

    "Jicho limeharibika na mguu mmoja umekatwa" Ibrahim aliendelea kusema huku akiniangalia kwenye kile kigutu changu kilichokuwa kimefungwa bendeji.

    "Mguu wake ulivunjika vibaya. Kwa kweli mfupa ulisagika kabisa.Tukaona tuuondoe"daktari akamwaambia.

    Hata hivyo Ibrahim hakuonyesha kushituka wala kutaharuki tangu aliponiona. Alikuwa kama anamuangalia mtu asiyemjua kabisa.

    "Pole sana" akaniambia na kuongeza.

    "Nashindwa kukukumbuka. Ni kweli nilikuwa na mke anaitwa Salma lakini alinitoroka miezi mingi iliyopita.Hivisasa sina mke."Ibrahim akasema.

    Maneno yake yakaniacha njia panda.

    "Una maana si yeye?" yule polisi akamuuliza.

    "Si mke wangu.Kwanza ninashangaa akiniita mume wake"

    "Hebu tueleze vizuri. Umesema mke wako alikutoroka miezi mingi iliyopita?"daktari akamuuliza.

    “Nilipopata upofu mke wangu alinitoroka na mwanaume baada ya kunifanyia visa vingi. Nimetoa taarifa polisi na kwa wazazi wake. Wote wanafahamu kuwa sina mke. Sasa nashangaa akijitokea mwanamke akisema ni mke wangu. Si kweli. Mimi simjui."

    Ibrahim alivyomaliza kusema nikamuona anageuka ili aondoke, nikamshika mkono.

    "Mume wangu najua umesema hivyo kwa sababu ya chuki. Naomba unisamehe niliyokukosea, niko chini ya miguu yako Ibrahim" nikamwaambia huku machozi yakinitoka.

    "Sitakusamehe na jina hilo 'mume wangu' ulikome kabisa.Mimi si mume wako.Kama unakumbuka nilikwambia usimcheke kilema, binadamu haishi kuumbwa. Yaliyonipata mimi na wewe yanaweza kukupata. Sasa umeyaona?"

    "Ni kweli mume wangu uliniambia" nilisema huku nikilia kwa sauti.

    "Naomba unisamehe. Ni ibilisi tu aliyenipitia"

    "Kama ni ibilisi amekupitia, sasa mwambie asikuwache hapa hospitali, akuhudumiye na utakapo toka akupeleke nyumbani kwake" Ibrahim akaniambaia kijeuri.

    "Lakini jamani pamoja na makosa mliyofanyiana, kiubinaadamu bwana Ibrahim ulipaswa umsikilize huyu bibi kutokana na matatizo yaliyomtokea. Ukimuacha hapa hospitali, kwa kweli atateseka” Yule daktari akamwambia Ibrahim.

    Ibrahim akawa anamtazama.

    Daktari huyo akaendelea kumueleza.

    Istoshe jicho lake moja limeshaharibika, lile jingine limeingia kipande cha kioo. Oparesheni yake inahitaji zaidi ya shilingi milioni kumi nchini India. Anahitaji msaada. Kama jicho hili litaachwa kwa wiki nne nalo litaharibika. Atakuwa haoni kabisa"

    "Umezungumza suala la msingi dokta" polisi aliyekuwepo hapo akamuunga mkono na kuendelea kueleza.

    "Bwana Ibrahim pamoja na matatizo unayoyazungumza bado una dhima na mke wako. Ulipaswa kwanza kusahau yaliyopita. Msaada wako ni muhimu sana. Baada ya hapo mtakuja kuyazungumza matatizo yenu".

    Nilidhani kwamba Ibrahim angelegea na kuyasikiliza yale maneno aliyokuwa anaambiwa lakini alitikisa kichwa chake kwa hasira.

    "Kutokana na vitendo alivyonitendea huyu bibi, sina dhima naye. Huyo aliyemtorosha huko Tanga akamleta hapa Dar ndiye atakayebeba dhima yake. Amhudumie mpaka apone lakini si mimi Ibrahim. Kwaherini"

    Ibrahim akageuka ili atoke.

    "Ibrahim usiniache!" nikampigia kelele.

    Ibrahim hakusita wala kunisikiliza. Aliendelea kwenda zake

    "Ibrahim....Ibrahim....nisemehe mume wangu!" nikamwambia kwa kelele.

    Ibrahim alifungua mlango akatoka.

    Daktari alitikisa kichwa kusikitika kisha akaniangaliahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Salma unakabiliwa na wakati mgumu sana. Mume wako ameshakukataa, kumbe mlikuwa na matatizo yenu. Sasa sijui itakuwaje!" daktari alisema kisha na yeye akatoka.

    Mimi nilikuwa ninalia. Nililia kwa sababu nilijua kuwa nimeshakuwa mlemavu wa miguu na macho na nisingepata msaada wowote kwingine.

    Yule polisi aliniangalia, mwisho wake nilimuona na yeye akifungua mlango na kutoka. Nikabaki peke yangu.

    Kwa kweli majuto huja kinyume baada ya kwisha kitendo. Sasa nilikuwa ninajuta. Nilijuta kwa kudanganyika. Kwanza nilidanganywa na Rita mpaka nikakubali kwenda kwa mganga aliyenipa dawa zilizoharibu macho ya mume wangu jambo ambalo lilisababisha maisha yetu kuharibika.





    Nilikaa pale hospitali kwa wiki mbili. Sikumuona Sikuzani wala Mariam aliyekuja kunitazama hata siku moja, wakati nilikuwa na hakika kuwa walipata habari kuwa niligongwa na gari na niko Muhimbili.

    Baada ya wiki hizo mbili, kidonda kilichokuwa mguuni kwangu kilikuwa kimepona ingawa hakikuwa kimekauka kabisa. Kadhalika sehemu za mwili wangu nilizoumia nazo zilikuwa zimepona. Hapo hospitali nilipewa magongo mawili ya msaada ili niweze kuendea msalani.

    Daktari aliyekuwa katika wodi yangu alinipa ruhusa lakini aliniambia niende nikatafute msaada wa pesa sehemu yeyote ile ili niweze kupelekwa India kufanyiwa operesheni ya jicho kabla ya wiki nne kumalizika.

    Nilitoka hapo hospitali nikiwa sijui pa kwenda.Vile nilivyofikishwa pale hospitali ndivyo nilivyotoka, sikuwa na kitu chochote zaidi ya mfuko wa plastiki na shilingi elfu tano nilizosaidiwa na daktari kwa ajili ya usafiri.

    SASA ENDELEA

    Sikuwa na pakwenda zaidi ya kupanda daladala na kurudi kule Sinza kwa kina Mariam.

    Nilipofika Sinza, wakazi wa nyumba niliyokuwa ninaishi waliponiona walipatwa na mshangao. Kwanza hawakunitambua mpaka nilipojitambuli

    sha.

    Nikaambiwa kuwa Mariam na Sikuzan hawakuwepo.

    "Wamekwenda wapi?" nikawauliza

    "Wamefungwa" dada mmoja aliyekuwa shoga mkubwa wa kina Mariam akaniambia. Nikashituka.

    "Wamefungwa kwa kosa gani"?nikamuuli

    za.

    "Walikamatwa usiku.Wakashitakiwa kwa kosa la kuendesha biashara ya umalaya"

    "Ilikuwa lini?"

    "Siku ya pili baada ya siku ile uliyopata ajali"

    "Wamefungwa kwa miaka mingapi?"

    "Si miaka, ni miezi sita tu kila mmoja"

    Hapo nikajua sababu ya kutomuona Mariam wala Sikuzan kuja kunitembelea hospitali nilikokuwa nimelazwa.

    "Siku waliyohukumiwa nilikwenda mahakamani.Mariam alinipa funguo ya chumba chao akaniambia kama utatokea nikupe"

    "Shida yangu ilikuwa ni kutoa vitu vyangu ili niviuze nipate nauli ya kunirudisha Tanga. Siwezi tena kuishi Dar" nikamwaambia

    "Sasa ngoja nikupe huo ufunguo"

    Dada huyo aliyekuwa akiitwa Agnes aliingia chumbani mwake akanitolea ufunguo na kunipa.Nikafungua ule mlango na kuingia mle chumbani. Nikafungua dirisha ili niweze kuona vizuri. Agnes naye akaingia.

    Nikaanza kukusanya vitu vyangu. Kulikuwa na mabegi yangu mawili ya nguo.Nikayafungua na kutoa nguo zote zilizokuwemo.Nilichagua nguo chache tu, nikazirudisha kwenye begi moja. Nguo zingine nikamwaambia Agnes ninaziuza.

    "Nitafutie wateja, nataka nipate nauli"

    "Nauli ya shilingi ngapi?"

    "Nataka nipate kama shilingi laki moja hivi kwani huko niendako sijui kukoje. Hivi vyombo vingine pia ninaviuza,sitav

    ichukua"

    Agnes akachukua baadhi ya vyombo na kuchagua nguo alizozipenda, akaniuliza anipe kiasi gani.

    "Nipe utakazo nipa dadaangu"

    "Elfu themanini, sijui kama utaridhika nazo kwa hivyo vitu nilivyochukua"

    "Nipe tu dadaangu"

    Agnes aliponipa pesa hizo, nilimuambia akanitafutie wateja wengine wa kununua vile vitu vilivyobaki.

    "Labda nichukue hizi nguo niende nazo hukohuko.Sasa niambie bei yako"

    "Bei yoyote dadaangu,elfu kumi, kumi na tano, wewe uza tu"

    Agnes akachukua zile nguo na kutoka nazo. Nikabaki mle chumbani kwa karibu masaa mawili. Aliporudi alikuwa hana nguo hata moja. Akanipa shilingi laki moja.

    "Nimekwenda kuziuza kwa majirani" akaniambia.

    "Nakushukuru dadaangu. Hivi vyombo vyangu vilivyobaki nitawaachia mashoga zangu kina Mariam.Wakitoka jela watakuja kuvikuta. Utawaambia nimetoka hospitali na nimerudi Tanga”

    "Sawa mdogo wangu. Nitakuja kuwaambia"

    "Tatizo langu kubwa ni huu mguu wangu uliokatwa na haya macho yangu. Hili jicho langu moja limeharibika kabisa. Hili jingine nimeambiwa limeingia kipande cha kioo huku pembeni, nalo linaweza kuharibika kama sitapelekwa India.Na siku nilizoambiwa zimebaki wiki mbili tu.Sijui nitafanya nini?"

    "Ukifika Tanga utawaeleza ndugu zako. Natumaini watakuchangia"

    Sikumjibu kitu. Niliguna tu kisha nikanyanyuka.

    "Dadaangu ndiyo natoka naenda Ubungo. Gari lolote nitakalo lipata ndilo nitakaloondoka nalo"

    Agnes alinishindikiza hadi kwenye kituo cha daladala.Tukaagana hapo, nikapanda daladala na yeye akarudi.

    Nilipofika Ubungo moyo wangu ulikuwa mzito sana kurudi Tanga. Kwa muda nikawa nimesimama nikitafakari.Nilihisi kurudi Tanga ilikuwa sawa na kujimaliza kabisa.Tatizo langu sasa lilikuwa kupata msaada wa kuokoa jicho langu. Nilikuwa na uhakika kwamba huko Tanga nisingepata ndugu yeyote wa kunisaidia pesa hizo hasa kutokana na visa nilivyovifanya.

    Kama kuna mahali pa kupata msaada, nilijiambia, ni hapa hapa Dar es salaam.

    Nikajiuliza sasa niende wapi kutafuta msaada huo? Niende Ikulu…niende wizara ya afya…au niende kwa mbunge?

    Wakati naendelea kutafakari nikamuona Mzee mmoja mwenye asili ya Kiasia amesimama karibu yangu akizungumza na simu. Alipomaliza kuzungumza nikamfuata.

    “Shikamoo Baba” nilimwamkia.

    “Marahaba” akanijibu.

    Nilimuhisi alikuwa akinidhania kuwa nilikuwa ombaomba niliyetaka kumuomba msaada.

    Nikamuona akijipekua mifukoni.

    “Sihitaji pesa baba, kuna maneno nataka kukwambia. Naomba unisikilize.” nikamwambia.

    Mzee huyo akanishangaa kidogo.

    “Unasemaje?” akaniuliza.

    “Baba kama unavyoniona nina matatizo lakini tatizo kubwa ninalotaka kukueleza ni kuhusu jicho langu hili” nikamwambia na kumuonyesha lile jicho langu linaloona.

    “Mimi nilipata ajali ya gari hivi karibuni iliyosababisha mguu wangu mmoja ukatwe na jicho langu moja kuharibika.

    “Sasa hili jicho langu ambalo linaona lilingia kipande cha kioo kwa pembeni. Madaktari wa Muhimbili wameniambia ni chembe ndogo sana ya kioo. Sasa tatizo liliopo ni kwamba natakiwa kupelekwa India kufanyiwa upasuaji kabla ya wiki mbili. Madakdari wameniambia baada ya wiki mbili kumalizika jicho hili nalo litaharibika kabisa na nitakuwa kipofu”

    Yule mzeebaada ya kunisikiliza kwa makini aliniuliza.

    “Sasa ulikuwa unahitaji nini?”

    “Nilikuwa nahitaji msaada wa kupelekwa India kutibiwa” nikamjibu haraka .

    “Kwani wewe huna ndugu?”

    “Ninao lakini ndugu zangu ni maskini, hawawezi kupata pesa zinazohitajika.”

    “Zinahitajika kiasi gani.”

    “Nimeambiwa zinahitajika shilingi milioni nane”

    “Bado si tatizo kwa sababu zipo taasisi zinazosaidia watu kama nyinyi. Kuna taasisi moja ya misheni ilianzishwa mwaka jana. Ishapeleka watu wengi nchini India kutibiwa maradhi yaliyoshindikana hapa kwetu.”





    “Ofisi zao ziko wapi?” nikamuuliza.

    “Kwani wewe unazo karatasi zako za hospitali zinazoonyesha matatizo ulionayo?”

    “Ninazo, ngoja nikuoneshe”

    “Hapana, usinioneshe mimi. Kama unazo ni vizuri kwani zitarahisisha wewe kupata msaada. Hao watu ofisi zao ziko hapa hapa Ubungo. Subiri nitakupeleka kwa gari langu”

    ***************************

    Sitamsahau mzee yule aliyenipeleka katika taasisi ile ya misheni ambayo iliniwezesha mimi kupelekwa India kuokoa jicho langu.

    Huko huko India nilipata rafiki aliyeninunulia mguu wa bandia ambao ulipachikwa kwenye mguu wangu uliokatwa. Kadhalika akaninunulia jicho la kutengenezwa ambalo lilikuwa halioni lakini liliwekwa katika tundu la jicho langu lililoharibika na kuonekana kama jicho zima. Lakini lilikuwa halipepesi wala kuchezacheza.

    Operesheni yangu ya kuondoa kipande cha kioo kwenye jicho langu ilichukuwa saa tatu. Nikakaa Hosptali kwa siku saba. Siku ya nane nilipewa miwani nikaruhusiwa kuondoka.

    Siku niliporudi nchini nilipokelewa na maafisa wa taasisi iliyonipeleka huko. Wakanipangishia chumba cha kulala katika hoteli kwa siku moja kabla ya kurudi Tanga.

    Kwa kweli niliwashukuru sana. Ingawa sikuwa na mguu mmoja wala jicho moja lakini nilikuwa na afadhali sana. Hivi sasa usichana ulikuwa umenirudia kidogo kwani sikuwa nikitembea kwa magongo na haikuwa rahisi kwa mtu kujua kuwa nilikuwa na mguu wa bandia.

    Kadhalika jicho la bandia nililowekewa lilifanya nisionekane kuwa na upofu.na kwa vile nilitakiwa kuvaa miwani, haikuwa rahisi kwa mtu kunitambua.

    Baada ya kulala hoteli kwa siku moja, siku iliyofuata nilipanda basi kurudi Tanga. Kwa vile baba yangu mzazi alikwishakufa nilifikizia kwa kwa shangazi yangu Makorora.

    Shangazi aliponiona badala ya kufurahi aliangua kilio.

    Nikambembeleza na kumsihi anyamaze. Aliponyamaza akaniambia kuwa aliambiwa na Ibrahimu kuwa nilikuwa nimepofuka jicho na mguu wangu mmoja ulikatwa kutokana na ajali ya gari.

    Nikamwambia shangazi ni kweli mguu wangu mmoja umekatwa na ule niliokuwa nao ni wa bandia.

    Pia nikamwambia jicho langu moja limepofuka na nimewekewa jicho la bandia.

    Nikamueleza kila kitu kilichotokea mpaka Ibrahimu alivyokuja kunikataa hospitali.

    “Mimi simlaumu Ibrahimu. Umeyataka mwenyewe mwanangu. Ulikuwa mzima, sasa umeshapata ulemavu wa kudumu kwa balaa lako”

    “Shoga ndiye aliyeniponza shangazi”.

    “Shoga yako nani?”

    “Yule jirani yangu, anaitwa Rita”

    “Rita alikuja hapa kwangu akasema wewe ulikwenda kwa mganga akakupa dawa zikamuaribu macho ibrahimu” shangazi akaniambia.

    “Rita ni mnafiki tena ni mnafiki mkubwa. Huko kwa mganga si alinipeleka yeye, mbona hakukwambia?”

    “Aniambie ili iweje, wakati alikuja kukusema wewe”

    “Akwambie ule ukweli ulivyokuwa kwamba yeye ndiye aliyenishawishi niende kwa mganga”

    “Sasa ndio ukome kusikiliza maneno ya mashoga “

    “Nimeshakoma”

    “Sasa huyo Ibrahim ameshakuacha?”

    “Hakunipa talaka lakini ni kama ameshaniacha. Siwezi tena kurudi kwake”

    “Haya, sasa kaa hapa utulie. Ulilolitaka umeshalipata”

    “Nitakaa, nitafanyaje shangazi. Hata nikimfuata kumbembeleza, kwa hivi nilivyo sasa hawezi kunitaka tena”

    Lakini baada ya kuwaza sana siku ile ile niliamua kumtumia ujumbe Ibrahim kumjulisha kuwa nimesharudi Tanga na niko kwa shnangazi.

    Nilidhani labda angerudisha moyo na angekuja kunichukua au kunitazama. Badala yake nilitumiwa jibu lililouliza.

    “Nani wewe uliyemtumia sms mume wangu?”

    Moyo ukanipasuka. Nikamuonesha shangazi ile meseji niliyotumiwa.

    “Nilisikia kuwa Ibrahimu ameshaoa mke mwingine. Inawezekana aliyekujibu ni mke wake” Shangazi akaniambia.

    Nikashituka.

    “Hah! Ibrahim ameshaoa mke mwingine?”

    “Kila jambo linakwenda kwa riziki. Riziki inapokwisha hutokea sababu yoyote watu wakaachana. Kama yeye ameshaoa na wewe utakuja kupata mume atakuoa”

    “Mume gani atakayenitaka mimi shangazi?”

    “Hilo si tatizo. Tatizo ni vipi utaendesha maisha yako. Fikiria utafanya nini, utairudishaje heshama yako katika jamii. Kama unahisi si rahisi kupata mume kwa sasa, achana na mawazo ya mume. Angalia mustakabali mwingine. Tafuta kazi ya kukushughulisha uweze kujiingizia kipato”

    “Nitafanya kazi gani shangazi wakati nimeshakuwa mlemavu?”

    “Kazi zipo nyingi za kujiajilri mwenyewe. Hata ukiuza chapati au maandazi ni kazi. Mbona nimeshaona wasichana wengi tu wanaouza chapati, maandazi, vitumbua na wana maisha mazuri tu. Jambo la msingi kwako ni kuamua tu”.

    Nikatikisa kichwa changu kusikitika.

    “Yaani hivi sasa ninajuta shangazi. Nilichezea shilingi chooni”

    “Sasa imeshatumbukia kwenye shimo. Acha kuifikiria kwa maana hutaipta tena. Cha msingi ni kufikiria jnsi utakavyoipata nyingine”

    Ushauri wa shangazi yangu ulikuwa wa maana sana. Hivi sasa ni mwaka mmoja tangu tukio hilo litokee. Nimeanzisha biashara ya kahawa na kashata barazani mwa nyumba ya shangazi. Nimeweka meza na mabechi manne. Ninauza kahawa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa nane kisha ninatoa tena meza saa kumi jioni hadi saa nne usiku.

    Nilianza na wateja wachache wa kahawa lakini baada ya muda mfupi nikawa napata wateja wengi. Kwa siku nilikuwa nikiuza birika saba mpaka nane za kahawa. Kipato chngu cha kila siku nilimshinda hata yule anayefanta kazi ofisini.

    Wateja wangu walinishauri niwawekee bao la kete. Nikanunua bao hilo na kuwawekea. Hivi sasa baraza ya nyumba ya shangazi yangu imekuwa haitoshi. Kuanzia asubuhi watu wanacheza bao. Kadhalika wakati wa jioni na usiku.

    Lakini mbali na wacheza bao kulikuwa na wateja ambao walikuwa ni mashabiki wa timu za mpira wa miguu na vyama vya siasa. Kuna siku watu hujadili mambo ya kisiasa na kuna siku mjadala unakuwa kwenye mpira.

    Jina langu likabadilika, sasa nikaitwa mama kahawa. Ukifika eneo la Makorora ukimwambia mtu yoyote nioneshe kwa mama kahawa atakuleta hadi barazani kwangu. Nimekuwa maarufu.

    Kwa vile nilikuwa nimesha jiunga na kitengo cha matibabu ya HIV au VVU, huko nilikutana na muathirika mwenzangu mwanaume aliyenipenda nakutaka kunioa. Alikuwa ni mtu wa umri mkubwa nikimlinganisha na mimi. Nikaenda kumueleza shangazi yangu. Shangazi akaniuliza.

    “Anafanya kazi gani?”

    Nikamjibu ni mvuvi wa samaki.

    “Kama amekupenda muache akuoe. Utaishi peke yako hadi lini wakati bado umsichana”

    Sikutosheka na jibu la shangazi yangu nilikwenda kumueleza daktari wetu wa kitengo. Akaniambia.

    “Mnaweza kuoana lakini kabla ya ndoa yenu mje kwangu niwafundishe jinsi mtakavyoweza kuishi kwa pamoja.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ya pili yake nikaenda na yule mwanaume kwa daktari. Tukapewa mafundisho mengi ya manufaa katika ndoa yetu. Haukupita hata mwezi mmoja nikaoana na yule mwanaume. Alikuwa anaitwa Kasim.

    Kasim akaniruhusu niendelee na kazi yangu ya kahawa na tukawa tunaishi palepale nyumbani kwa shangazi. Mpaka ninakisimulia kisa hiki tumeshapata mtoto mmoja wa kiume asiye na VVU. Na tumenunua banda la uani palepale Makorora.

    Ingawa miezi mingi imeshapita tangu nilipoachana na Ibrahim, ningali ninaendelea kumkumbuka mara kwa mara na sifikirii kama nitamsahau kabisa kabisa kwa sababu nilikuwa nampenda.

    Mimi salma yamenikuta hayo na mpaka leo ninajutia makosa yangu, je wewe ninayekusimulia kisa hiki umepata fundisho gani kutoka kwangu?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwisho nawahadharisha akina dada wenzangu walio katika ndoa, waache tamaa na kuwasumbua waume zao ambao vipato vyao ni vya chini. Ukijilinganisha na aliye juu utakufuru kama miimi nilivyojilinganisha na Rita aliyenunuliwa gari na mume wake.

    Laiti ningejilinganisha na msichana aliye chini yangu anayechapa lapa asubuhi kwenda kutafuta kibarua cha kubeta buni kwa malipo ya shilingi elfu tano kwa

    siku, ningeshukuru. Na yaliyonitokea yasingenitokea.

    Pia muangalie mashoga wa kushauriana nao. Mashoga wengine si wazuri kama alivyokuwa shoga yangu Rita aliyenipa ushauri uliotaka kuniangamiza.

    Akina dada zangu mridhike na yale maisha mnayoishi na waume zenu, wasije wakatokea akina Chinga wakawalaghai.

    Kisa changu kinaishia hapa. Ningefarijika kupata sms zenu lakini msithubutu kunitumia kwani mume wangu ana wivu ni kiama. Nisije nikalikoroga tena!



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog