Search This Blog

Friday, November 18, 2022

CHUNGA SAANA LAAZIZI WANGU - 2

 





Simulizi : Chunga Saana Laazizi Wangu
Sehemu Ya Pili (2)




Zilipita wiki mbili tangu Tuntu kuonana na yule msichana aliyempamia siku ile maeneo ya sekondari ya jangwani.Hakuwa na mpango wa kuonana naye,kwani aliamini haitokuwa rahisi kuonana kutokana na yeye kutokuwa na muda wa kutosha.Asubuhi alikuwa akipelekwa shuleni na baba yake na muda wa mchana akitoka kazini alimpitia shuleni na kurudi naye nyumbani hivyo hakuwa na muda wa kuzunguka kwenye harakati zake nyingine.

Tuntu alikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu.Alikuwa mchezaji namba tisa katika timu ya shule ya Azania pamoja na timu ya HATARI F.C iliyopo mtaani kwao.Alishiriki ligi mbalimbali za mtaani na kutunukiwa vikombe mbalimbali vya mchezaji bora.Alianza kucheza mpira tangu akiwa darasa la tano katika shule ya msingi Bunge iliyopo maeneo ya Posta Dar es salaam.

Ilikuwa siku ya ijumaa,kulikuwa na mechi ya kirafiki kati ya sekondari ya Azania na Tambaza.Ilipangwa kufanyikia kwenye uwanja wa Tambaza mida ya saa tisa baada ya jua kutuliza makali.Mida ya saa saba na nusu mchana,wanafunzi wa Azania walijongea taratibu kuelekea Tambaza kwaniaba ya kupata muda wa kutosha wa kujiandaa.Walitembea kidogokidogo kutoka shuleni kwao na mida ya saa nane na dakika kama kumi hivi waliingia ndani ya shule ya Tambaza.

Walipokelewa na kiongozi wa michezo wa shule hiyo ambaye aliwapeleka mpaka kwenye chumba kilichoandaliwa maalumu kwa ajili yao kubadilisha mavazi na kupanga mambo mbalimbali.Baada ya kuingia ndani ya chumba hicho,mwalimu wa michezo bwana Jongo alielekea ofisini kuonana na mwalimu wa michezo wa Tambaza aliyejulikana kwa jina la Sir Nzagazaga.Waliongea mambo mbalimbali kisha mwalimu Jongo alirejea kwenye chumba chao huku Sir Nzagazaga akielekea kwenye chumba walichoweka kambi wachezaji wa Tambaza.

Mida ya saa nane na nusu wanafunzi wa shule ya Tambaza na Azania walikuwa wamekwisha uzunguka uwanja mzima huku wakiimba nyimbo mbalimbali za shamlashamla.Wanafunzi wa Azania walikuwa wakipiga ngoma na kuimba nyimbo za amshaamsha huku wanafunzi wa Tambaza wakiwasha moto na kuzunguka nao uwanja mzima wakiimba nyimbo mbalimbali,zote hizo zilikuwa ni amsha amsha tu.

Timu ya Tambaza ilikuwa ya kwanza kuingia uwanjani kutokana na kuwa wenyeji wa mchezo huo.Ilikuwa saa nane na dakika hamsini.Shangwe,vifijo na kelele za furaha zilitawala uwanjani hapo baada ya wachezaji hao kuingia.Muda mfupi baadae timu ya Azania ilijongea kwa mbwembwe uwanjani.Ujio wao ilikuwa kama kutia ubani kwenye maaka ya moto,shangwe zilizidi mara dufu zaidi.Walimu wa shule zote mbili waliopata muda wa kuhudhulia.Walikaa kwenye viti vilivyoandaliwa kwa ajili yao.Taratibu za michozo zilifanyika uwanjani na muda mfupi tu mchezo ulianza,ilikuwa saa tisa na dakika kumi.

Mchezo ulikuwa mkali sana.Wachezaji wa tambaza walikuwa wanamjua sana Tuntu,hivyo walitumia nguvu yao kubwa kumdhibiti.Mchezo uliendelea mpaka dakika ya arubaini na mbili bila ya timu yoyote kupata goli ndani ya kipindi hicho cha kwanza.Katika dakika ya arubaini na tatu,Tuntu aliupata mpira,aliwapiga chenga mabeki wawili na kubaki yeye peke yake.Alikimbia na mpira mpaka karibu na goli kipa,mabeki walikuwa wakimfuta kwa kasi ya ajabu ili kumzuia asipate nafasi ya kuupiga mpira kwani waliujua ufundi wake.Aliupiga mpira kwa kasi ya ajabu kiasi cha goli kipa kubaki akiwa mdomo wazi,kwa bahati mbaya mpira uligonga kwenye mwamba wa juu na kurudi tena kwa wachezaji.Mchezaji namba kumi wa Azania aliupiga tena na golikipa aliupangulia nje ikawa kona kwenye goli la Tambaza.

Tuntu alijilaumu sana kwa kushindwa kufunga,aliyafumba macho yako kwa mikono miwili.Akiwa anafumbua macho yake kuwangalia mashabiki waliokuwa wanamlaumu kwa kulikosa goli,alikutana ana kwa ana na macho ya msichana matata sasa.Mapigo ya moyo yalidunda kidogo kutokana na tabasamu la msichana huyo lisilo la kawaida.

Tuntu alivuta taswira kuikumbuka sura hiyo n a hatimaye kwa haraka aliikumbuka.Alikuwa msichana yule aliyempamia siku ile.Wote walionekana kustuka na mioyo yao kwenda mbio,Tuntu alitabasamu kisha alielekea kuipiga kona.Alikuwa anatumia miguu yote miwili,alipiga kona kwa kutumia mguu wa kushoto.Kabla hajaupiga mpira,alivuta pumzi kwa nguvu kisha alirudi nyuma kidogo kujiandaa kuupiga kiufundi.Mpira ulienda moja kwa moja bila ya kuguswa na mtu na bila kutegemea,ulitumbukia golini.Ndani ya dakika arubaini na nne aliipatia goli la kwanza shule yao ya Azania.Wanafunzi wa Azania waliingia uwanjani kwa furaha na kumnyanyua Tuntu juujuu huku wakilitaja jina lake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mpira uliwekwa kati na kuanza.Muda mfupi kipenga kilipigwa kuashilia muda wa mapumziko ulikuwa umeshawadia.Kwa upande wa Tambaza ilikuwa ni majonzi makubwa huku Azania wakipiga vigoma na kuimba singeli.Kila timu ilikaa sehemu yake kwa ajili ya kutathmin wapi walishindwa na wapi walitakiwa kurekebisha ili kujipatia ushindi.Tuntu mawazo yalimrudisha kwa msicha yule ambaye alikutanisha naye macho. “Amevaa sare za Jangwani sekondari,Tambaza anafuata nini?”Alijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu.

Alipokea maji ya kunywa kwa ajili ya kupunguza kiu.Alikunywa huku akiwa amefumba macho,baada ya kumaliza alifumbua macho yake.Akiwa anaangalia huku na kule aliona wachezaji wa Tambaza wakipepewa na wanafunzi wa kike wa shule yao.Kwa bahati mbaya shule yao ya Azania haikuwa na wasichana hivyo hawakupata nafasi hiyo ya kupepewa na watoto wazuri.Akiwa anaendelea kutazama yaliyokuwa yanafanyika kwenye kundi la wachezaji wa Tambaza,alimuona yule msichana akiwa amesimama karibu ya wale wasichana waliokuwa wanawapepea wachezaji.

Yule msichana alikuwa na hamu ya kukutana na Tuntu.Alishindwa jinsi gani angefika pale alipokuwa Tuntu kwani hakukuwa na msichana hata mmoja hivyo alibaki akiangalia kule alikokuwa Tuntu.Walikutanisha macho tena na yule msichana alitabasamu na kujificha nyuma ya msichana aliyekuwa karibu yake,Tuntu alihisi huenda ndiyo rafiki yake aliyemleta hapo Tambaza.Muda wa mapumziko ulipoiisha timu zote zilirudi uwanjani.Kwa muda wote huo,wanafunzi wa Azania walikuwa wakiimba na kucheza kwa furaha.

Mchezo uliendelea kwa kasi ya ajabu,kila mmoja akihitaji kuutwaa ushindi wa siku hiyo.Tambaza waliongeza mashambulizi ili kusawazisha goli walilopigwa na wapinzani wao.Mnamo dakika ya themanini kipindi cha pili,mchezaji nambari kumi wa Tambaza aliunyakuwa mpira na kukimbia nao kuelekea kwa goli kipa wa Azania.Aliupiga mpira kiufundi zaidi,lakini goli kipa mahari wa Azania Samir Nasri,aliupangualia nje na ikawa ni kona kwenda kwenye goli la Azania.

Kona ilipigwa na Jakson mchezaji namba nane wa Tambaza alipi mpira kwa ustadi Zaidi na mpira ulikuja kwa kasi ya ajabu.Katika gombania ya wachezaji,bahati mbaya mchezaji wa Azania aliushika mpira na ikahesabiwa penalti.Wanafunzi wa Tambaza walifurahia sana kwani hiyo ndio ilikuwa fursa ya kurudisha goli walilofungwa.

Mpiga penalti alikuwa ni Jamse kalengo mchezaji namba sita wa Tambaza.Aliaminika sana kwa upigaji wake mzuri wa penalti.Kila mmoja alikuwa kimya kusubiri nini kitatokea kutokana na penalti hiyo.Azania waliomba dua akose,Tambaza waliomba apate,hivyo mwenye hadhi mbele ya Mungu ndio duwa yake ingekubaliwa.Kipenga kilipigwa na mpigaji alirudi nyuma kidogo ili kujiandaa,goli kipa alikaa vizuri huku akirukaruka kiufundi zaidi.

“Ayaaaaahh….!!! Buuuuuuh…..!!!” Waliosema “Ayaah!” Walikuwa wanafunzi wa Tambaza huku wanafunzi wa Azania wakizomea kwa kusema “Buuuuh!!” kuashiria mpigaji alikosa penalti hiyo.Goli kipa mahiri Samir,aliusoma mguu wa Jamse kisha alitulia ili kusubiria muelekeo wa mpira.Jamse alipopiga,Samir alijirusha na kuudaka mpira kwa urahisi kama kumsukuma mlevi shimoni.

Wanafunzi,wachezaji na walimu wa Tambaza walikata tamaa,muda ulikuwa unayoyoma kwani zilikuwa zimebaki dakika chache zitimie dakika tisini za mchezo.Kwa upande wa Azania ngoma na nyimbo za furaha zilishamiri uwanjani hapo.Mchezo uliendeelea huku Azania wakiimalisha ulinzi golini kwao ili Tambaza wasirudishe goli dakika za mwishoni.Muda ulizidi kusonga mbele na kipenga cha kuashiria mchezo umekwisha kilipulizwa na refalii.Wanazafunzi wa Azania waliwabeba Samir na Tuntu hewani na kuzunguka nao uwanja mzima.

Ilikuwa muda wa saa kumi na moja jioni,yule msichana alihitaji kusalimiana na Tuntu.Alisubiri mpaka shangwe zao ziishe,lakini cha ajabu ziliendelea kwa takribani dakika kumi hivi bila ya kupumzika huku wanafunzi wakiyataja majina ya Tuntu na Samir.Rafiki yake alimtaka waondoke,lakini msichana huyo alikataa.Katika kuendelea kuvuta subira huku akimuangalia Tuntu,walikutanisha macho yao na wote walitabasamu kwa furaha.Kwa kuwa walionana na kutabasamu,Yule binti aliamini kuwa Tuntu hawezi kuondoka bila ya kuonana naye yaani angelimsubiri.

Akiwa hajaamini kilichotokea,alibaki ameduwa kwa kuwaangalia wanafunzi wa Azania wakitoka ndani ya shule ya Tambaza wakiwa wamewabeba mashujaa wao na kuelekea shuleni kwao.Kutokana na muda kuyoyoma,aliamini kwa siku hiyo wasingeweza kuonana hivyo aliamua kuelekea kituoni ili kurudi nyumbani kwao maeneo ya Magomeni mikumi.Aliekea Muhimbili kwa ajili ya kupanda gari la kuelekea Ubungo.

Wanafunzi wa Azania waliwashusha mashujaa wao baada ya kuingia shuleni kwao.Mwalimu Jongo aliongea maneno machache kabla ya wanafunzi kutawanyika. “Nipende kuwapongeza wachezaji wote kwa juhudi zenu,pia wanafunzi wote kwa kuhudhuria kwa wingi na kushangilia kwa nguvu zenu zote.Pia napenda kuwambia kuwa mjiandaye tena wiki ijayo tutakuwa na mchezo wa kirafiki na shule ya Benjamin Mkapa,hivyo inabidi tuwaoneshe adabu pia,mmenielewaa!!”. “Ndioooo..!!” Wanafunzi waliitikia kwa sauti ya pamoja kisha mwalimu aliwaruhusu kurudi nyumbani.

Kwa muda huo Tuntu asingepata lifti kwa baba yake kwani huwa anaondoka nyumbani saa tisa na akichelewa sana huwa ni saa kumi.Siku hiyo baba yake alipita shuleni kumchukua,aliambiwa yupo mpirani hivyo aliondoka nyumbani.Tuntu aliondoka na rafiki zake wawili kuelekea kituoni.Wakiwa wanavuka barabara,Yule msichana alimuona Tuntu,alitamani kushuka lakini haikuwezekana.Alijipa moyo kwa kujisemeza kuwa milima haikutani ila binadamu hukutana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Tuntu alisubiri gari bila ya mafanikio kwani kwa wakati huo abiria walikuwa wengi kiasi cha kukosa nafasi ya kuweka mguu.Nyumbani kwao ilikuwa ni mikocheni kwa Warioba karibu na ofisi za ‘Oxford’. Alichukua bodaboda mpaka magomeni akiamini pale angelipata gari kutokana na mapanda njia ya gari kutokea karume na hizi za kutokea Posta na Kariakoo.Dereva alimpeleka mpaka kituoni ambapo alikaa kidogo na kupata gari la kuelekea Kawe.Alipanda na kuelekea nyumbani kwao ambapo alifika mida ya saa moja usiku kutokana na foleni njiani.

**********

Siku zilisonga mbele.Kila mmoja alikuwa na harakati zake ambazo aliona ni zenye manufaa kwake.Kwa upande wa Tuntu alihitaji kumfahamu zaidi Yule msichana aliyemkumba siku ile.Alijilaumu kwanini hakumuuliza jina lake,na kwanini hakuchukua namba yake ya simu ili kuwasiliana naye.Siku moja mida ya saa kumi na nusu jioni,Tuntu alikuwa anatembea kidogokidogo kutokea shuleni kwao akielekea kituoni maeneo ya “Fire” kwani siku hiyo baba yake alimuacha baada ya kumkuta akifanya mazoezi ya mpira na wenzake kujiandaa na mechi ya kirafiki na sekonda ya Benjanmin.

Akiwa hatua chache mbele baada ya kulivuka geti la sekondari ya Jangwani,alisikia sauti ya msichana ikimwita.”Wee mkaka simamaa!” walikuwa ni wasichana wawili waliovalia sare za Jangwani.Tuntu aligeuka kuwaangalia ndipo alipomfahamu mmoja wa wasichana hao ambaye alikuwa ni yule msichana aleyempamia siku ile.Moyo ulimuenda mbio,alijikaza kiume mpaka walipomfikia.

“Naitwa Salma Jangala na huyu ni rafiki yangu anaitwa Bite nipo naye darasa moja..”Yule msichana alijitambulisha kwa jina hilo na kumtaka Tuntu naye ajitambulishe. “Naitwa Jabil Ramadhan Katuntu,ila jina linalofahamika sana ni Tuntu hivyo ukitaka kunipata shuleni tumia jina hilo. “Tuntu alijitambulisha jina lake kamili.Waliongea mawili matatu kiasi cha Salma kumueleza Tuntu kama alikuwa anasoma kidato cha nne mchepuo wa biashara,hivyo walijikuta wakiwa sawa.

“Naweza kupata namba yako?” Salma alimsemeza Tuntu ambaye alikuwa hatua tatu mbele kuelekea kituoni. “Yaah! usiogope unaweza.”Moyoni Tuntu alifurahia kuombwa namba kwani alihitaji kumuomba lakini alijifanya kama hana shida sana.Salma alichukua karatasi na kuandika namba ya Tuntu.Baada ya kumaliza kuiandika,waliagana.

Usiku mida ya saa tatu,simu ya Tuntu iliita.Ilikuwa ni namba ngeni,alipokea na kuangea na aliyempigia. “Anhaah! niambie Salma vipi hali?” Tuntu aliongea kwa furaha baada ya kumfahamu aliyempigia.Waliongea mambo mengi kiasi cha kuelezana sehemu wanazoishi,vitu wanavyovipenda na wasivyovipenda.Waliongea mpaka mida ya saa nne usiku huku kila mmoja akiwa amemzoea mwenzake ndani ya muda huo kiasi cha kutamani kuongea mpaka asubuhi.

“Naamini kuna mambo mengi ya kuzungumza ila inabidi tulale kwa ajili ya kuamka mapema kesho”.Tuntu alikatikiza maongezi maana Salma alihitaji kukesha. “Aaa bwaanaa..tuongee kidogo..”Salma alisisitiza.Tuntu aliamua kukata simu kwani muda ulikuwa unayoyoma.Salma alimtumia meseji akisema “Umekata simu siku nikikuona nitakupiga”.Baada ya kuisoma,Tuntu alitabasamu kwa furaha kwani ulikuwa ni utani.

Salma alikuwa anayapenda sana masomo ya biashara.Alikuwa na ndoto ya kuwa muhasibu tangu akiwa darasa la sita katika shule ya msingi Madenge iliyopo Temeke.Alipoingia kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Jangwani,yeye na familia yake walihamia Magomeni Mikumi.Salma alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto sita katika familia yao baada ya kutanguliwa na dada yao ambaye alikuwa amekwisha olewa tangu Salma akiwa kidato cha pili.

Dada yao aliishia kidato cha nne katikashule ya sekondari ya Turiania iliyopo magomeni.Alipata daraja la nne ambapo alikaa nyumbani baada ya kukosa pesa ya kumuendeleza.Kitendo cha dada yake kutoendelea kimasomo,kilimsikitisha sana Salma kiasi cha kuahidi kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya kidato cha nne.Alisoma kwa juhudi zake zote na kwa uchungu wa hali ya juu.

Mdogo wake aliyemfuata kwa kuzaliwa alikuwa wa kiume,alikuwa anasoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Msimbazi.Na aliyekuwa anamfuatia alikuwa wa kike naye alikuwa anasoma shule ya sekondari Msimbazi kidato cha kwanza huku aliyemfuatia akiwa darasa la sita katika shule ya msingi Mikumi na mwengine alikuwa darasa la nne huku wa mwisho akiwa darasa la kwanza shule hiyohiyo ya Mikumi.

Kutokana na idadi kubwa ya watoto na wote wakiwa shuleni,ilikuwa ni mzigo mkubwa kwa wazazi wake ambao walikuwa na kazi za kipato kidogo.Baba yake alikuwa fundi selemala,akitengeneza sofa,kabati na viti mbalimbali na kuviuza.Mama yake alikuwa akijishughulisha na uuzaji wa chakula katika shule ya sekondari Turiani,hivyo kipato kilichokuwa kikipatikana kilisaidia matumizi ya nyumbani na shuleni kwa watoto wote.

Salma alikuwa na uwezo mzuri darasani,tangu akiwa darasa la kwanza katika shule ya msingi Madenge hakuwahi kushuka chini ya nafasi ya tatu katika kila somo.Aliendelea kufanya vizuri mpaka alipoingia kidato cha nne hivyo wazazi wake walimtegemea sana kuja kuwakomboa kutokana na juhudi aliyokuwa nayo.

Pamoja na kufanya vizuri darasani,Salma alikuwa anajishughulisha na harakati zingine za nje ya darasani.Alikuwa kiongozi wa nidhamu katika serikali ya wanafunzi,pia alikuwa ni katibu wa klabu ya UN shuleni kwao.Alikuwa anashiriki makongamano mbalimbali yaliyokuwa yanaandaliwa na umoja wa mataifa.Kutokana na kujituma na ufanisi katika utendaji kazi wake,alipandishwa cheo na kuwa katibu wa UN wilaya ya ilala.

Siku moja aliongea na Tuntu mida ya usiku kama ilivyokuwa kawaida yao.Waliulizana hobi zao,ambapo Salma alimueleza kuwa hobi yake ilikuwa ni uongozi ambapo alimueleza nafasi za uongozi anazozishikilia.Kwakuwa Tuntu alielewa kuwa Salma alikuwa kiongozi wa UN wilaya ya ilala,alinuwia moyoni kumfanyia “Surprise” siku moja.Tuntu alimwambi hobi yake ilikuwa ni mpira ila alimficha hobi moja ambayo Tuntu alikuwa anaipenda kuliko hata mpira.Hobi hiyo ndio ilimpatia umaarufu sana shuleni kwao Azania ukiachilia mbali mpira.

UN vijana mkoa wa Dar es salaam waliandaa kongamano la mkoa ambalo ilipangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa michezo tamaduni na vijana mheshimiwa Kabavako Kabambaganya.Wanachama wote wa Klabu ya UN shule zote za Dar es salaam walihudhuria kongamano hilo.Ilikuwa siku ya Jumamosi kuanzia saa tatu asubuhi.Siku hiyo kulikuwa na shamlashamla kutokana na burudani kutoka kwa wanafunzi mbalimbali wa shule tofautitofauti.

Tuntu siku hiyo alihudhuria kwenye sherehe hiyo.Alipanga kumfanyia surprise Salma hivyo hakumuambia kama atahudhuria.Kuna kitu alikuwa amekiandaa maalumu kwa ajili ya Salma.Kitu hicho ndiyo ilikuwa hobi yake kubwa sana.Ili aweze kumuonesha Salma nilizaima apande jukwaani.Alikaa miongoni mwa wanafunzi wengi waliokuwepo ukumbini humi huku akisubiri zamu yake ya kupanda jukwaani ifike na atomize ahadi yake ya kumuonesha Salma hobi hiyo…







“The coming perfomer ii..is..is Tuntu baaabyy!!”Ilikuwa ni sauti ya MC ambaye alikuwa akitangaza kwenye sherehe hiyo.Salma alikuwa kwenye kitengo cha kuwakaribisha wageni rasmi hivyo Tuntu alivyoingia kwenye hema la waburudishaji,hakumuona.

Tuntu alikuwa ni muimbaji mzuri wa “bongo flavor” aina ya R and B akifuata mienendo ya msanii maarufu nchini Tanzania Jux.Alipanda hewani na kuanza kutumbuiza nyimbo yake aliyorekodi ikiwa na jina la “You can do it”.Nyimbo hiyo ilikuwa na lengo la kuwatia moyo wale wote wanaoshindwa kufanya mambo makubwa kwa visingizio kama vile umasikini,ulemavu na uoga.

Mdundo wa nyimbo hiyo uliwavutia wanafunzi na watu wote waliokuwemo ndani ya ukumbi huo kiasi cha wote kusima na kuanza kucheza.Salma alikuwa kwenye hema lililoandaliwa kwa ajili ya wageni rasmi,alishindwa kuvumilia na kuelekea ukumbini kumuangalia Tuntu alivyokuwa anawapagawisha mashabiki.

Alishangaa sana,alijiuliza maswali mengi kiasi cha kukosa majibu.Alijiuliza Tuntu ni mtu wa aina gani mwenye vipaji viwili na vyote anavifanyia haki ipasavyo. “Mh! Kwanini hakuniambia kama ni mwanamuziki mzuri?”Alijiuliza kichwani bila ya kupata jibu.

Alitumia takribani dakika tatu kutumbuiza.Akiwa anamalzia kuimba,alikutana na tabasamu zito kutoka kwa Salma aliyekuwa kasimama mlangoni akishuhudia kulichokuwa kikiendela.Tuntu pia alitabasamu na kuwaaga mashabiki zake kasha alirudi kwenye hema la watumbuizaji.Watu wote walibaki wakishangiria kwa furaha ya ajabu. “Ana nyota kali sana…!”Salma alijisemeza moyoni kisha alimfuata Tuntu kwenye hema la watumbuizaji wa siku hiyo.

Akiwa anakaribia kuufikia mlango wa hema hilo,Tuntu naye alitoka nje akiwa anajipepea ili kupunguza jasho kwani shughuli aliyoifanya haikuwa ndogo. “Pole na pia hongera kwa kazi nzuri uliyoifanya.Kwanini hujaniambia kama muziki ni hobi yako?” Swali hilo lilitoka kinywani mwa Salma ambaye alikuwa akimfuta jasho kwa kitambaa chake. “This is surprise so usishangae.” Tuntu alimjibu. “Nitakupigia baadaye tuongee mengi”Salma alisema huku akielekea kwenye majukumu yake ya kuwapokea wageni waalikwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Salma alijiuliza bila ya kupata jibu juu ya nani alimpa mwaliko wa kuja kutumbuiza siku hiyo.Ukweli ni kwamba Tuntu alialikwa na kiongozi wa Club ya UN mkoa,Alfahad Thabo ambaye alimfahamu siku moja walipokutana kwenye sherehe ya kuzaliwa ya mwanafunzi mmoja wa Benjamin ambapo Tuntu alialikwa kama mtumbuizaji maalumu wa sherehe hiyo.Siku hiyo Tuntu aliimba nyimba maalumu iliyoelezea historia ya msichana huyu tangu kuzaliwa mpaka siku hiyo ya sherehe.

Msichana huyo alimualika Tuntu kuhudhuria sherehe hiyo kwasabubu walisoma wote katika shule ya msingi Bunge.Pia Alfahad alialikwa kutokana na kufahamiana na msichana huyo kutokana walisoma shule moja ya Benjamin ambapo yeye alikuwa kidato cha sita huku msichana huyo akiwa kidato cha nne.Kutokana na kipaji alichokionesha Tuntu siku hiyo,Alfahad alivutiwa naye ndipo alimuomba ahudhurie kwenye kongamano hilo kama mburudishaji,hivyo ndivyo ilivyokuwa mpaka Tuntu kuhudhuria siku hiyo.

********

Mpaka usiku unaingia Salma alikuwa hana salio,aliamua kumbipu Tuntu.Tuntu hakufanya ajizi bali alichukua simu yake na kumpigia.Salma aliuliza maswali mengi sana siku hiyo ya kuhitaji kumjua kwa undani zaidi.Tuntu alimjibu maswali yote ikiwemo historia ya familiya yake,ambapo baba yake alikuwa na asili ya Wanyamwezi wa Tabora huku mama yake akiwa na asili ya Wambondei wa Tanga.

Baba na mama yake Tuntu,walikutana maeneo ya Tanga mjini kwenye mgahawa mmoja ambao alikuwa akipendelea kula hapo akiwa mkoani humo kwenye biashara zake za kuuza nguo kabla ya kuanza biashara aliyokuwa nayo kwa sasa.Bwana Ramadhan Katuntu,baba mzazi wa Tuntu alikuwa kijana shupavu sana.Alijishughulisha na biasha ya nguo za akina mama ambapo alinunua mzigo kutoka Dar es salaam na kuupeleka Tanga.

Siku moja Baada ya kumaliza shughuli zake za kibiashara katika soko la Tangamano aliingia kwenye mgahawa mmoja ambao ulikuwa umejificha kidogo kutokana na kuzungukwa na maduka mbalimbali.Alikaa na kuagiza chakula ambapo aliomba aletewe Ugali samaki.Baada ya muda mfupi,alikuja binti mmoja mwembamba kidogo na mwenye sura ya kuvutia akiwa ameshikilia sahani lililofunikwa vizuri.

Akiwa anaweka chakula mbele ya Bwana Ramadhan ambaye kwa wakati huo alikuwa akitazama vitu mbalimbali kwenye simu yake ya mkononi,bahati mbaya mchuzi ulimmwagikia kwenye paja na kuchafua suruali. “Samahani! Sijakusudia..!”Binti aliomba radhi kwa sauti ya uoga. “Lione! utadhani halina macho,unatembea tembea tuu huangalii mbele..!!” Alifoka mama mmoja aliyekuwa muajili wa binti huyo.

Bwana Ramadhan alimwambia asijali kisha alichukua kitambaa na kujifuta.Walikutanisha macho na binti huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa akijing’atang’ata kwa aibu na uoga. “Usijali endelea na shughuli nyingine.”Bwana Ramadhani alimpa moyo.Alikula chakula kwa haraka zaidi kwa ajili ya kuwahi majukumu mengine kisha alilipia na kuondoka.

Akiwa njiani kuelekea kwenye nyumba ya wageni aliyofikia,kumbukumbu ya tukio la siku hiyo zilikuwa zikipita kwenye fikra zake.”Anaonekana ana adabu sana,kwanini asiwe mke wangu!? Aaah!...Kuoa haitakiwi kukurupuka bwana..maana simjui vizuri…”Alikuwa akijisemeza moyoni.

Uzuri wa binti yule aliyemmwagia mchuzi ulikuwa ukimjia kila mara kiasi cha kusimamisha shughuli ya kutunza kumbukumbu za biashara yake.Alipata wazo moja baada ya kuchakachua fikra mbalimbali zilizomjia kichwani juu ya binti huyo.Alijiridhisha kumtafuta binti huyo kwa niaba ya kumfikishia ujumbe aliouandaa moyoni mwake.

Kesho yake alipomaliza shughuli zake muda ulikuwa umekwenda sana kiasi cha kukosa nafasi ya kwenda kwenye mgahawa aliokwenda jana;badala yake aliagiza chakula kwa mama ntilie aliyekuwa karibu na biashara zake.Bwana Ramadhani alisikitika kwa kukosa muda wa kwenda kumuona binti yule aliyedhamiria kuonana naye siku hiyo,ila alijipa moyo kuwa siku moja ataonana naye.

Kwa upande wa msichana huyo siku hiyo alijisikia vibaya sana kwa kutomuona Bwana Ramadhani kurudi.Alijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu. “Au alikasirika kwa sababu ile…!? Daaah….!mbona alinisamehe..!Mmmh!”Alizidi kuchanganyikiwa zaidi.Alianza kuvutiwa na kijana huyo;alijiuliza lini atamuona tena kwani alimuona jana tu na leo hakujitokeza.Siku hiyo alichelewa kulala kutokana na mawazo kemkem juu ya kijana huyo.

Kesho yake Bwana Ramadhan alimaliza mzigo mapema mida ya saa tano asubuhi.Baada ya kumaliza shughuli zake alielekea kwenye mgahawa alipomuona binti yule alieanza kumchanganya taratibu hisia zake.Alipofika hakumkuta binti yule,bali alimkuta yule mama na msichana mwengine ambaye siku ya mwanzo hakumkuta.

“Umekuja, nilidhani ulikasirika siku ile ndiyo maana jana sijakuona?” Aliuliza mama ntilie ambaye ni muajili wa mabinti aliyekuja kumangalia. “Jana shughuli zilikuwa nyingi,vipi yule msichana yuko wapi?”bwana Ramadhan aliuliza kwa shauku.

“Leo hatokuja kwasababu huwa ana zamu na huyu binti hivyo atakuja keshokutwa.” Bwana Ramadhan alichoka baada ya kupewa jibu hilo,aliagiza chakula na baada ya kumaliza kula aliondoka kuelekea chumbani kwake alikokuwa amepanga.

Alikuwa na huzuni sana ya kumkosa msichana huyo.Alijiuliza ataonana naye lini wakati kesho yake alikuwa na safari ya kurudi Dar es salaam.Alijipa moyo wa kuonana naye awamu nyingine atakapoleta mzigi.Alipofika chumbani mwake hakuwa na hamu ya kukaa humo kwani alihisi kama yuko jela.

Aliamua kutoka na kwenda kuzungukia mitaa mbalimbali kwa lengo la kutuliza akili yake.Akiwa anakatiza kuelekea mtaa wa pili kutoka alipokuwa amepanga,alimuona msichana huyo kwa mbali sana.Alimuangalia kwa umakini wa hali ya juu na kugundua alikuwa ni yeye.Alitamani kumuita,lakini alishindwa kutokana na kutolijua jina la msichana huyo.Alianza kumfuata kwa kasi kidogo na alipokaribia kumfikia,alipunguza mwendo na kumfuata taratibu.

Msichana huyo alikuwa ametokea sokoni kununua baaadhi ya vitu kwa ajili ya maandalizi ya chakula cha usiku.Aligeuka nyuma kidogo na hap bwana Ramadhani alijificha nyuma ya nguzo ya umeme kwa bahati nzuri yule msichana hakumuona.Mapigo ya moyo yalimuenda mbio kama mwizi aliyekamatwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Bwana Ramadhani baada ya kugundua hakuonekana,aliendelea kumfuata mpaka mwisho wa safari ambapo msichana huyo aliingia kwenye nyumba moja iliyokuwa kukuu.Alisogea mpaka karibu na nyumba hiyo na hapo aliisoma namba ya nyumba kisha aliamua kurudi taratibu alikotoka.Kesho yake alirejea Dar es salaam kwa ajili ya kuandaa mzigo mwingine.

Aliporudi kwa mara ya pili Tanga,alifanya chini juu kuonana na binti huyo.Siku aliyopata nafasi ya kuongea naye,ilikuwa mida ya jioni.Alikwenda karibu na mgahawa huo kisha alimsubiri pembeni yake baada ya lijua kuwa ndio muda wa binti huyo kurudi nyumbani kwao.

“Naitwa Sofia Hussein..”Binti alijibu baada kusalimia na bwana Ramadhani aliyejitambulisha na kumtaka naye ajitambulishe.

“Naweza kupata nafasi ya kukusindikiza?”Bwana Ramadhani aliuliza kwa upole.Binti hakujibu Zaidi ya kuinama chini na kuchekacheka kwa mbali.Bwana Ramadhani hakuchezea fursa bali alizidi kumdodosa Zaidi…..







Baada ya maongezi yao marefu,hatimaye alimchumbia.Mwanzoni Sofia alikataa lakini alikuwa akitikisa kibiriti kwani alikuwa amekwisha kufa mbele ya kijana huyo.Zilipita siku kadhaa baada ya kuanzisha uchumba wao. Kadri muda ulivyosonga mbele,taratibu za ndoa zilifanyika mwisho wa siku walioana na kuja kuishi Dar es salaam maeneo ya Mikoroshini Temeke.Hiyo ni historia ya kukutana kwa wazazi wa Tuntu.Historia hiyo Tuntu alimueleza Salma wakiwa wanaongea kwenye simu.

********

“Naweza kukuliza swali lingine la mwisho kama hutajali?”Salma aliuliza kwa uoga kidogo.

“Nimekupa fursa uliza unachojisikia.”Tuntu aliongea kwa upole.

“Hi…hivi…Una…una girlfriend?”.”Ha ha ha ha ha.”Ntuntu alicheka tu bila ya kujibu. “Unamaanisha nini kucheka hivyo inaamana nimeuliza swali la kijinga eeeh..!” Salma aliuliza kwa sauti ya kinyonge kwani alihisi kama amejidhalilisha.

“Hapana hujakosea kuuliza ila tu naona kama mapema vile kuuliza swali hilo,naomba kwanza kama mwezi mmoja hivi upite utaniuliza.”Tuntu alimjibu.

Salma alikubali kishingo upande lakini alihitaji kujua siku hiyohiyo.Alianza kuvutiwa na Tuntu,alivutiwa na mtindo wa mavazi,upole,vipaji pamoja na uzuri aliojaliwa kijana huyo.Aliamini kuwa pamoja na kijana huyo ni sawa na kukaa na muuza marashi.

Waliachana na maongezi hayo na kujikita kwenye masuala ya kitaaluma.Waliulizana ndoto zao za baadaye wangependa kuwa wakina nani.Tuntu alimueleza kuwa alihitaji kuwa Mwalimu ambapo Salma alimueleza kuwa alihitaji kuwa Muhasibu.Waliongea mengi huku wakitaniana kiasi cha kuongeza mazoea na ukaribu wa hali ya juu.

*********

Ukaribu uliongezeka siku hadi siku kiasi cha kila mmoja kupafahumu nyumbani kwa mwenzake.Hisia za mapenzi zilianza kuwatawala taratibu kiasi cha kila mmoja kujua kama alikuwa anapendwa na mwenzake.Mwisho wa siku waliamua kuvunja ukimya na kuelezana kuwa wanapendana.

Siku ya kutamkiana ukweli,Tuntu aliipanga kuwa siku maalumu.Alimuomba nafasi Salma ili wapate muda mzuri wa kuongea. “Naona jumamosi imetulia..”Salma alijibu baada ya kuulizwa siku gani alikuwa huru.

“Na ungependa twende wapi?”Tuntu aliuliza.

“Kigamboni Balakuda beach” Salma alipendekeza.

“Sawa nitakupitia mapema mida ya saa tatu asubuhi” Walikubali.Siku zilisonga mbele na hatimaye jumamosi ilifika.Tuntu alimpitia Salma maeneo ya Magomeni Mapipa.Alimsubiria kituoni na baada ya muda mfupi,Salma aliyokea.

Alikuwa kavalia sketi iliyovuka kidogo magoti,brauzi pamoja na mtantio wa rangi ya pinki. “Umependeza sana.” Tuntu alivunja ukimya baada ya kusalimiana.

“Asante”Salma aliitika huku akimuangalia kwa tabasamu pana.Walielekea kituoni na kuchukua gari za kwenda Posta zinazotokea Ubungo.Baada ya kushuka Posta,walichukua bajaji mbaka Kivukoni na hapo baada ya kushuka walichukua gari za kwenda Mji mwema.Walishuka kituo cha Njia panda ya maweni kasha walielekea ilipo Balakuda bichi.

Eneo la Balakuda lilikuwa zuri sana.Ukiingia kuna sehemu mbili,ya kwanza ni ya juu ambapo kuna ukumbi pamoja na baa na upande wa pili ni wa chini ambapo kuna ufukwe wa bahari.Baada ya kumaliza utaratibu wa kuingia ndani ya ukumbi huo,walielekea sehemu ya chini kwenye ufukwe wa bahari.

Ilikuwa ni mida ya saa tano asubuhi.Waliagiza vinywa pamoja na chipsi mayao na hapo walikaa kwenye viti vilivyoizunguka meza na kuanza kujiburudisha.Wakati wakiwa wanakula,waliendelea na mazungumzo ya hapa na pale yaliyounganisha utani,vichekesho pamoja na mizaha mbalimbali.

Baada ya kumaliza kula,mazungumzo yaliyowakutanisha hapo ilibidi yaanze.Tuntu ndiyo alikuwa muanzilishi wa mchezo kwasababu ndiye aliyeomba nafasi hiyo.Aliguna kidogo kwa ajili ya kuliweka koo lake sawa kasha alianzisha mazungumzo.

“Salma! Naomba unisikilize kwa makini sana” Alimuangalia kidogo kwa sekunde kadhaa kasha aliendelea. “Ikiwezekana fungua masikio ya moyo kuliko haya yanayoonekana.” Wakati huo Salma alikuwa aking’ata vidole vyake na kugeuka huku na kule.Ama kweli mapenzi ni kitu kingine.

“Katika kila mafanikio au kushindwa kwa mwanaume basi mwanamke yupo nyuma yake.Mwanamke anamchango mkubwa sana.Lakini sio kila mwanamke anafaa kuwa nyuma ya mwanaume hususani yule anayetaka kufanikiwa.Ikiwa kama kweli mwanamke anamchongo mkubwa kwa mwanzume basi hata mimi nahitaji mwanamke sahihi ayakayekuwa nyuma yangu.

Nafasi haiji mara mbili.Kwa kulitambua hilo nimeamua kuituia nafasi aliyonipa Mungu ya kunikutanisha na wewe.Kwa akila yangu timamu na moyo wangu mkunjufu,napenda kutamka rasmi kuwa NAKUPENDA SALMA.Sijui wewe unasemaje?”Tuntu aliongea kwa msisitizo.

Wakati wote huo Salma alikuwa kimya.Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka mwilini.Mikono yote ilikuwa ya baridi.Alikaa kimya kwa takribani dakika tano huku akigunaguna tu bila ya kutoa jibu kamili. “Nikuulize?” Salma alifungua kinywa chake.

“Uliza tu nimeshakupa fursa hiyo muda mrefu.”Tuntu akiongea kwa kujiamini.

“Kuna wasichana wengi umekutanana nao,wazuri sana.kipi kimekufanya uje kwa Salma?”

Tuntu alitabasamu kidogo kasha alikohoa kidogo kulisafisha koo. “Kama nilivyosema,sio kila mwanamke anasifa za kuwa mke.Wewe ni mwanamke wa tofauti na wale niliokutana nao.Unanidhamu,una huruma na umekuwa pamoja na mimi kwa muda mrefu hivyo nimetokea kukupenda kutoka moyoni.”Tuntu alimaanisha aliyoyaongea.Alimpenda sana Salma.

Salma alitikisa kichwa kutoka juu kwenda chini mara tatu isha ya kukubaliana na maneno ya Tuntu. “Tuntu siwezi sema kama ninapingamizi.Nipo tayri kuwa na wewe kwa hali yoyote.”Salma alikubali.

“Nakuahidi kwama nitakupenda,nitakulinda na nitakuthamini kadri ya uwezo wangu.”Tuntu alitoa kiapo.

“Nami pia nakupenda,nitakupenda,nitakunyamini na sitokuacha.”Salmi naye alitoa kiapo.Walishikana mikono kuashiria wameungana mkono pia walikutanisha vidole vyao vya mwisho na kupinga.Baada ya hatua kiyo,walielekea karibu na maji baharini na kuanza kucheza kidali.

********

Siku zilizidi kusonga mbele.Mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne ulikaribia.Mpaka kufikia mwezi wa saba,Salma alikuwa bado hajalipia ada ya mtihani wa taifa.Kuchelewa kwake kulipa,kulipelekea deni lake kupanda zaidi kutoka elfu hamsini mpaka elfu themeanini.

Aliamua kumueleza ukweli mpenzi wake Tuntu kwani maji yalikuwa shigoni.Kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo juu ya binti huyo,Tuntu aliampa moyo kuwa atajitahidi kadri ya uwezo wake kulitatua tatizo hilo.

Baada ya siku chache,Tuntu alimtaka Salma waonane.Walionana maeneo ya Kariakoo na hapo Tuntu alimkabidhi Salma kiasi cha shilingi laki moja akalipie deni hilo na kiasi kilicho baki atumie kwenye matumizi mengine.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Asante sana my dear”.Salma aliongea hiku machozi yakimdondoka taratibu kuelekea mashavuni.Tuntu alimfuta machozi na kumpa moyo kuwa asijari ni mambo ya kawaida.

“Nafanya hivi kwasababu nakupenda sana.Nipo tayari kufanya lolote kukufanya uwe na furaha,naomba ufurahi sasa maana nalipenda tabasamu lako.”Tuntu aliongea maneno hayo kutoka moyoni.Walikuwa kariakoo kwenye moja ya migahawa ya kisasa maeneo ya karibu na ofisi za klabu ya Yanga.

“Kunywa sasa juisi yako,sipendi nikuone ukiwa hauna furaha!”Tuntu alimbembeleza Salma ili anywe na waendelee na maongezi ya kawaida.Kwa upande wa Salma hakuamini kilichokuwa kimetokea siku hiyo kwani hakutegea kupatiwa kiasi chote hicho.Alijitahidi kuondokana na mawazo na kuendelea na maongeza ya furaha….

.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog