Search This Blog

Friday, November 18, 2022

IANGALIE TULEANE - 2

 






Simulizi :Iangalie Tuleane
Sehemu Ya Pili (2)




Mzee Tualike hakuchelea, punde baada ya tangazo kutoka alifika ofisi ya bodi kuchukua fomu. Kwani alikuwa na nia toka muda ya kufanya hivyo. Aliwasili ofisini hapo kwa majitapo sana, na pale alipopata wasaa wa kuzungumza na wanahabari alizidisha ndambo zake, kwa imani kuwa, hapo kijijini hamna mtu wa kulingana naye kiutendaji. Wala hakulaza, siku hiyohiyo alirejesha fomu alipokamilisha taratibu zote zinazotakiwa.

“Naamini kwa hiki nilichofanya hakuna mwenye uthubutu wa kupingana nami. Sitarajii kupata mpinzani,” mzee Tualike alijitapa mara baada ya kuhojiwa na waandishi wa habari, waliokazana kupiga picha za mnato na video

Pindi mzee Tualike anarejesha fomu kwenye ofisi ya bodi, wazee kadhaa wapatao watatu, walibana sehemu fulani karibu na ofisi hiyo wakiteta jambo lililowapeleka kwenye tafakuri na majadiliano ya kina. Maongezi yao hayakuwa ya juu, waliteta kwa sauti ya chini ili hata wale walio jirani nao wasipate kusikia kile waongeacho. Juu ya kuwa kwenye majadiliano, hawakusita kwa muda fulani kuiba masikio na macho yao kuangaza kule mzee Tualike aliko ili kufahamu kilichokuwa kinaendelea.

“Huyu mzee ana nguvu kubwa, hatuna uwezo wa kushinda naye.”

“Unahisi nani anafaa kukabiliana naye?”

“Kwa hapa kijijini, sidhani kama yupo wa aina hiyo, labda wale wazaliwa wa kijiji hiki lakini maisha yao yapo vijiji jirani.”



Hayo ni baadhi ya maongezi waliyokuwa wanateta. Lengo likiwa mmoja miongoni mwao kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa serikali ya kijiji, lakini walikuwa na hofu, kutokana na nguvu kubwa aliyonayo mzee Tualike. Walimhofia. Baadaye iliwabidi waondoke, kila mmoja kuelekea nyumbani kwake huku wakihaidiana kukutana masaa wawili mbele, ili wapate muafaka wa kile walichokuwa wanajadili.



Naam! Yale masaa waliyokubaliana yaliwadia. Walikutana katika jengo moja, miongoni mwa majengo yatoayo starehe kijijini hapo. Jengo la uuzaji sharabu. Walivuta moja ya meza pembeni mwa jengo na kuitisha vinywaji kadhaa, vilivyotoa harufu ya uvundo, kuashiria ndiyo kwanza vilianza kutumiwa na wao. Pasipo kuchelewa, maongezi yalianza, tena yakisindikizwa na fundo la kinywaji kulainisha koo na kuibadili akili taratibu.

“Mimi nimepata wazo,” mmoja wao alisema, afahamikaye kwa jina la Mchungaji Chilombo.

“Lipi tena? We...we...wewe mzee wa mawazo hewa?” mwenziye alichangia kwa sauti iliyojaa kigugumizi katika matamshi yake. Huyu alikuwa Mooja Mpingo.

“Tumtafute yule mama.”

“Mama yupi?”

“Yule,...”

“Yule yupi nawe?”

“Bi. Mwema!”

“Una maana tumtafute na kumuomba agombee?”

“Ndiyo!...huyu mama ana ushawishi na nguvu kubwa kwa sasa hapa kijijini kwetu. Na ni mtu pekee mwenye uwezo wa kushindana na mzee Tualike.”

“Kama naanza kuyaamini maneno yako. Tujaribu kumtafuta kisha tumshawishi katika hili.”

“Sasa mnahisi tunaweza kumpata wapi?”

“Tukimpata Awetu, uhakika wa kujua aliko ni mkubwa.”



Majadiliano yao yalichukua muda mrefu ili kufikia tamati, wakiwa na maafikiano ya lengo moja la kufanya, kumtafuta Bi. Mwema Asononekaye. Waliahidiana kulifanyia kazi kuanzia siku inayofuata. Kesho yake, walianza mapema sana, ukamilishaji wa lengo lao. Sehemu ya kwanza waliyoanza kumtafuta Bi. Mwema ni nyumbani kwa kina Awetu, ambapo hawakufanikiwa kukutana na mtu yeyote, kwani hawakuwa na taarifa za ajali iliyompata.

Msamaria mwema, ndiyo aliwavumbua akili zao kuhusu hilo. Walistaajabu! Tena mshangao uliowaondolea morali ya kuendelea kufanya kile walichopanga kwa siku hiyo.Ila hawakuruhusu uharibu morali yao kabisa, hivyo muda mfupi tu, walipiga konde na kurejea katika hali waliyonayo awali na kupanga upya mkakati namna watavyoendeleza lengo walilokubaliana nalo. Sababu lengo lilikuwa ni Bi. Mwema, Awetu akiwa kama mfanikishaji wa kumpata yule wanayemhitaji, iliwabidi wamtafute kwanza Awetu awaeleze wapi anapatikana.



Walifunga safari hadi kwenye zahanati ya kijiji, ambayo ilikuwa umbali mrefu kidogo toka nyumbani kwa kina Awetu. Wao hawakujali umbali, walichojali ni utimizaji wa lengo walilopanga. Walihitaji kumuwekea upinzani mkali Mzee Tualike, hata kama aliaminika kuwa na nguvu kubwa kuliko mtu yeyote, ila imani yao iliwaaminisha kuwa yule wanayemtafuta ndiyo mpinzani sahihi. Mwendo wa dakika kadhaa walifika eneo husika, na kuanza kuhesabu wodi moja baada ya nyingine kuelekea ile waliyoambiwa. Ambayo Awetu kalazwa.



Pindi wanazidisha hatua kusonga mbele, ilhali huo sio muda muafaka wa kuwaangalia wagonjwa, chumba cha Mganga Mkuu wa zahanati hiyo, aitwaye Dkt. Makolela Tumkumbe walikusanyika waandishi wa habari kadhaa wakinakili na kurusha mubashara hotuba ya mganga huyo, ambaye aliianza nusu saa iliyopita kupitia runinga na redio ya serikali ya kijiji pasi na sahau vyombo vya habari vya watu binafsi umma wafikiwe na ujumbe anaoutoa.Wao walishuhudia ingia na toka ya waandishi hao, ila hawakujali kufahamu nini walichokuwa wanashughulikia kutokana na mihangaiko waliyoiona, akili yao ilikuwa inamuwazia Awetu pekee.



Hatua chache toka wodi waliyoelezwa, walishuhudia wauguzi wawili wakiwa hima koridoni, paliposakafiwa kwa seruji wakitokea wodi aliyolazwa Awetu, wakisukuma kitanda cha magurudumu manne kikiwa na mwili juu yake—uliofunikwa gubigubi kwa shuka jeupe wakielekea kule Mch. Chilombo na wenzake walitokea. Iliwabidi wasimame, na kusogea pembezoni mwa korido kupisha wale wauguzi. Kwani korido haikuwa na upana kiasi kwamba watu wengi hawawezi pishana, na kuyaongoza macho yao juu ya kile kitanda kuutazama mwili uliofunikwa, ulifunikwa hadi usoni, hivyo iliwapatia wakati mgumu wa utambuzi kama mwili ulioko kitandani ndiyo wa mhusika wanayemfuatilia. Ama mwingine.



Macho yao yalishindwa kung’amua kutokana na mazingira yalivyo hadi walivyopitwa na kuwaachia maswali mengi ya uhitaji wa utambuzi. Waliishia kusindikiza, huku shauku ya safari ikizidi panda ndani ya mioyo, na shauku ya kwenda kuwauliza wale wauguzi ikichipua pia.

“Nahisi yule aliyelazwa pale juu ni Awetu,” alisema Mch. Chilombo.

“Kwanini unahisi hivyo.”

“Kuna vile vidole, vimetokeza chini upande wa kushoto, vya mtu wa ulemavu wa ngozi,” aliendelea kuongea baada ya kuviona vidole vya mtu aliyelazwa juu ya kile kitanda vikielea. Na kuwasukuma wenziye watumbue macho yao kuangaza.







“Aiseee! Yule ni Awetu pale juu. Ina maana ashaaga dunia?” Mooja aliuliza kwa sauti iliyojaa taharuki.

“Tunajuaje wakati wote tupo hapa.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Twendeni kwanza wodini, tusipofanikiwa kumuona ndipo tuwafuatilie wale wauguzi.”

“Kwanini tusiwafuate hawa wauguzi kuwauliza ndipo tuelekee wodini? Maana yule aliyelazwa hata pasipo na hata elimu anamtambua kuwa ni Awetu.”

“Hapana! Twendeni wodini tukapate uhakika kwanza.”



Pasipo na kuchelewa, hatua za kuelekea wodini zilianza, tena za haraka ili wasipofanikiwa kumuona warudi kwa wale wauguzi waliopishana nao koridoni. Hawakukawia kufika na kuingia moja kwa moja wodini baada ya kumpoza kiasi fulani cha pesa mlinzi waliyemkuta mlangoni. Walichokikuta walistaajabu kwani wodi ilikuwa na mgonjwa mmoja na vitanda viwili vilivyo tupu—yule mgonjwa akiwa ni mtu mwingine tofauti na wao waliyemdhamiria.

“Dada, humu ndimo alilazwa Awetu?” Mch. Chilombo aliuliza baada ya kusalimiana.

“Ndiyo!”

“Wapi kaelekea?”

“Ametolewa muda mfupi uliopita na mwenzie aliyekuwa kalazwa hapo jirani yake.”

“Kwa ulivyosikia, ni wapi kapelekwa—na huyo mwenzie yukoje?”

“Sijajua, ila inasadikika kuwa kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu umetokea hapa kijijini, hivyo nao ni miongoni mwa waathirika wa huo ugonjwa.”

“Etiiiii?”

“Ndiyo hivyo kaka yangu. Na huyo mwenzie yupo kama alivyo Awetu, kuanzia rangi na vitu vingine vyote.”

“Yesu wangu!” Mch. Chilombo alihamaki.



Hawakuhitaji kuendelea kuwemo tena wodini, waliondoka, kuwafuata wale wauguzi waliokuwa wanasukuma kitanda japo hawakufahamu wala kumuona huyo mgonjwa wa pili waliyoambiwa wapi amepelekwa. Hawakutembea, walianzisha riadha kuwawahi. Na hatimaye mbio zao ziliishia mbele ya chumba kilichoandikwa “Morgue” mlangoni, upande wa juu, ambapo wale wauguzi walionekana kutoka ndani ya chumba hicho na kile kitanda walichokuwa wanasukuma. Huku juu ya kitanda yakionekana mashuka pekee.



Uvumilivu uliwashinda, waliamua kuuliza ila majibu waliyopatiwa hayakuwa rafiki kuhusiana na swali lao. Hawakuishia mara moja pekee, waliendelea kuuliza zaidi na zaidi tena kwa unyenyekevu lakini majibu hayakubadilika. Walirudi wodini, kule ambapo Awetu alilazwa ili kuulizia uelekeo wa mgonjwa mwingine alikopelekwa kwa mlinzi alindaye wodi hiyo. Mlinzi hakuwa na hiyana, kupitia kiasi kidogo cha pesa alichopewa awali, aliamua kuwafungukia, wapi mgonjwa mwingine kapelekwa. Japo kwa wakati huo akili zao zilikuwa njia panda kuhusu nani Awetu, kati ya yule aliyoingizwa chumba cha kuhifadhia maiti na huyo mgonjwa mwingine.



Hawakuiruhusu akili yao moja kwa moja ikubaliane kuwa yule aliyehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti ndiyo Awetu, hata kama walishamhisi mwanzo. Walihitaji uhakika zaidi, kwa kuona sura na sio vinginevyo. Punde baada ya kuambiwa waliianza safari ya uelekeo ule walioambiwa. Walienda sambamba na korido tofauti na ile waliyotumia awali. Hatua kadhaa mbele waliachana na korido, kisha kuingia mchangani, mchanga tifutifu ulionesha alama za matairi ya gari iliyopita. Walifuata michirizi hiyo hadi sehemu fulani, karibu na banda la kuchoma taka, na kuingia tena koridoni. Waliendelea kukaza miguu yao na kuzidi kusonga mbele kuyafuata maelezo ya mlinzi, Hatua zao ziliwafikisha lango la kuingilia Zahanati hapo, ikawabidi wasimame, mshangao ukijivika usoni kutoamini wakionacho, kwani hawakutaraji kutokeza mahali hapo.



Walivyoangaza chini, hawakukosa kuiona michirizi ya matairi, kwani hapo langoni hapakuwa na kiambaza cha seruji na zege. Pembeni kidogo mwa nguzo zilizotengenezewa lango hilo palipata kuwepo na kikaratasi kidogo kilichokunjwa juu kikiwa na maandishi yaliyosomeka, “Awetu.” Mch. Chilombo ndiye wa kwanza kukiona. Kutokana na hulka ya uharaka iliyotawala moyoni mwake, ya kuangaza huku na kule, alifanya hima kukiokota na kuanza kuusoma ujumbe uliopo ndani. Baadaye aliwasambazia wenzake nao wausome.

“Una maana gani huu ujumbe?”

“Utakuwa umeandikwa na yule tunayemtafuta.”

“Una uhakika? Kina Awetu wapo wengi?”

“Hapana! Tuna Awetu mmoja tu hapa kijijini.”

“Sasa ana maanisha nini?”

“Sijajua, ila hizi ni alama zitumiwazo na watu wa usalama wa kijiji chetu.”

“Inaweza kuwa, watu wanaotumia hizi alama wanahusika katika zoezi lililopo mbele yake.”

“Kwa kiasi kikubwa! Hivyo hatuna budi kufanya jitihada za kufahamu maana ya haya maneno.”

1-2-5 ndiyo ujumbe ulioandikwa katika kile kijikaratasi kilichookotwa, uliowapa wakati mgumu wa kuutambua maana yake. Kila mmoja alijaribu kufikirisha akili yake lakini fikra zao kwa wakati tofauti tofauti ziligonga mwamba.

“Tujaribu kuwatafuta watu wanaohusika na mambo ya ulinzi wanaweza kutusaidia kujua maana,” alisema Mooja.

“Sio watu wote wanaohusika na mambo ya ulinzi wana uelewa na taaluma hii. Hii ni ya siri kwa watu wachache sana.”

“Kwa hiyo tunafanya vipi ili kukamilisha tunachohitaji?”

“Hatuna jinsi, ila......” alisema Mooja na kuonekana kusita, kana kwamba kuna jambo kalikumbuka.

“Nini?”

“Kuna kitu nimekumbuka. Huo ujumbe bado haujamalizika, kuna maneno mengine yalipaswa kuandikwa mbele yake.”

“Yapi hayo? Na umefahamu vipi?”

“Huo ujumbe ulipaswa usomeke, 1-2-5 3 O’clock ahead (One two five three o’clock ahead). Nilishawahi kuwasikia wana usalama wa kijiji chetu wakiongea siku aliyotembelea mhasibu wa kijiji mtaa wa Amani ili kuweka jiwe la msingi katika lile daraja linalounganisha kijiji chetu na kijiji cha Kalipinde.”

“Unahisi walimaanisha nini?”

“Sikujua maana yao, ila nilijaribu kuwafuatilia ili nijue maana ya walichoongea sikung’amua kitu.”

“Tusikate tamaa, tuendelee kupambana hadi mwisho mpaka tufanikishe kufikia azma tuliyojiwekea,” Mch. Chilombo aliwapa hamasa wenzake.



Hatimaye iliwabidi warudi tena maeneo ya jengo la zahanati, kukagua mazingira huku wakifanya uchunguzi kuhusiana na hitaji walilonalo. Katika tembea yao walibahatika kupitia eneo la mapumziko, ambapo wagonjwa na wasaidizi wao hupuzika. Ilikuwa sehemu ya wazi, paa lake liliezekwa kwa bati, ikipambwa kwa viti na mabenchi ya kukalia, mbele yake kulifungwa runinga yenye ukubwa wa nchi ishirini na moja ambayo muda wote ilikuwa inatumika kutoa habari mbalimbali. Haizimwi, labda kutokee tatizo la umeme uliokuwa unazalishwa kwa nguvu za jua ama runinga yenyewe kuwa mbovu ndipo isifanye kazi.



Kwa namna walivyokuwa na uharaka hawakuwa na mawazo yoyote ya kuwahitaji watafute sehemu wapumzike, ila walivyofika eneo la kupumzikia, sauti iliyosikika kutoka kwenye runinga iliwavutia na kuwapa ushawishi wa kuendelea kukisikia kilichozungumzwa. Mvuto walioupata uliwasogeza karibu na kuketi kwenye benchi kusikiliza kilichozungumzwa.



Sura ya Mganga Mkuu, Dkt. Makolela Tumkumbe ilikuwa inarindima kwenye runinga hiyo, ikisoma taarifa kutoka kwenye karatasi kadhaa zilizoenea juu ya meza iliyo mbele yake. Si Mchungaji Chilombo na wenzake pekee ndio waliovutiwa na tukio hilo, bali ni wanakijiji wengi walivutiwa. Kilichokuwa kinafanywa na Dkt. Makolela kilikuwa kinawahusu watu wote wa kijijini hapo. kilichokuwa kinasomwa kiliwashangaza na kuwagawa. Kila mmoja kwa namna yake—aliduwaa kutokana na kijiji hicho kuingia kwenye zoezi zito la kuchagua uongozi wa serikali ongozi kisha taarifa hatarishi kujipenyeza katikati ya wakati huo adhimu.



Taarifa ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ndiyo iliyokuwa inasomwa na Dkt. Makolela, kwa ustadi na ufasaha wa hali ya juu pasipo kumung’unya neno lolote ili asikike sawia na wasikilizaji ama watazamaji. Hotuba ilikuwa ndefu, kwani ilijumuisha chanzo cha mlipuko na waathirika, huku sehemu kubwa ya hotuba hiyo ikitaja mazingira ya zahanati ya kijiji ndiyo eneo athirika zaidi.

“Chanzo bainiwa cha ugonjwa huo ni zahanati yetu, kutokana na mazingira kutokuwa rafiki ambapo huduma za kiafya hupatikana. Hivyo, umepelekea kuathiri hata wagonjwa waliokuwa hapa wakipatiwa matibabu. Madaktari na wasaidizi wao kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kufanya jitihada za kudhibiti tatizo hili kwa wagonjwa hawa, mwishowe baadhi yao wameshaaga dunia huku wengine wakiwa mahututi. Hapa nina orodha ya majina ya wagonjwa waliokumbwa na tatizo hili na kupelekea kuondoa uhai wao pasi na sahau wale walio mahututi.” Alisogeza maji ya chupa, akanywa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Jumla ya wagonjwa walioathiriwa ni kumi na tano, kati yao wagonjwa saba wameshatangulia mbele ya haki, na wanaosalia wanane, hali zao si nzuri. Hivyo naomba nitaje majina yao kwa kuanza na wale walio mahututi kisha kufuatia wale waliotutoka. Majina yao ni; Salima Atunus, Shukran Zebedayo, Maimuna Sowan, Zaitun Chiwila, Kansonso Lauma, James Kadenge, Faria Mkwava na Atu Kalla. Hawa ndio mahututi, wanaoendelea kupatiwa matibabu kwa jitihada zote na wauguzi wetu. Majina ya waliotangulia mbele ya haki ni; Cecy Machea, Zarafi Malingili, Stephen Ndomola, Jangala Mandova, Frida Majasho, Zaudia Jimajima na Awetu Mbwela.”

“Heeeee!” Ulikuwa mshangao, ulioneshwa karibia na watu wote waliokuwa wanafuatilia hotuba hiyo kwa njia mbalimbali: redio na runinga. Mchungaji Chilombo, Mooja na mwenzao aliyefahamika kwa jina la Ayoub Kudabalika nao walikuwa sehemu ya mshangao huo. Mshangao wao ulikuwa wa nguvu, na uliowapunguzia hamu ya kuendelea kuangalia runinga. Waliondoka!



Hata morali ya kumtafuta Bi. Mwema ilitoweka. Wazo la kutoendelea kumtafuta lilishika hatamu akilini kwa kila mmoja, kwa kasi isiyo shikika.

“Tunaamuaje?” Ayoub aliuliza.

“Tupambane wenyewe, mmoja wetu akachukue fomu agombee,” Mchungaji Chilombo alichangia hoja.

“Hapana! Siku bado zipo kabla ya hitimisho la kuchukua fomu, tuvute subira. Yawezekana kilichozungumzwa leo ni zuga, wawapoteze wananchi na habari za uchaguzi ili wajitengenezee mazingira ya ushindi. Hivyo tuvumilie huku tukifanyia kazi ule ujumbe tuliookota,” alisema Mooja.

“Ni vyema pia, lakini unahisi ule ujumbe wapi panafaa kwenda tukaelezwa maana yake?”

“Kwa mstaafu. Twendeni kwa mstaafu, aliyekuwa Mkuu wa mgambo hapa kijijini. Nadhani mnajua kuwa ni mwanaharakati sana yule mzee. Huwa hapendi mambo yanayoendelezwa na serikali ya kijiji chetu.”

“Hapo umenena. Endapo hatutafanikiwa kumpata Bi. Mwema, tumshawishi hata yeye agombee. Nina uhakika ana hasira dhidi ya serikali kwa sasa kutokana na ustaafu wake kugubikwa na mizengwe lukuki. Pia mnakumbuka, muda wake wa ustaafu haukuwadia akaondolewa, kisa tu walikuwa hawaendani na Mwenyekiti wa kijiji chetu.”

“Naam!”



Hata wananchi wengine pia, baada ya kutoka kusikiliza hotuba walijikusanya katika makundi tofauti tofauti kuijadili. Majadiliano yao yalijaa malalamiko ili kuiendea serikali, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Malalamiko yalikuwa mengi, tena yote yalielekea upande mmoja huku wengine kupitia hotuba hiyo walizua fikra tatanishi kuhusiana na Awetu.

“Hii iliyofanywa leo ni zuga kwetu. Hawa watu walikuwa na lengo toka muda, hasa la kuondoa uhai wa Awetu wakakosa mbinu, hivyo wameamua kutumia hii mbinu kutuaminisha wananchi kwamba wao hawahusiki katika kifo chake,” kijana mmoja aliteta na mwenzake wakati wakiondoka katika genge moja la kilevi kusikiliza hotuba hiyo kwa njia ya redio.

“Una uhakika gani? Chunga mdomo wako chalii yangu.”

“Hakuna cha kuchunga, acha wasikie na ndio ukweli. Yule msichana kama kaaga dunia, sababu sio huo ugonjwa, wao ndio wamemuua, maana ana siri nyingi sana yule binti juu ya hiki kijiji chetu.”

“Siri gani nawe acha kuzua mambo.”

“Heeee! Dogo, Awetu ni noma yule msichana, kwani hujui kuwa Babu yake ndiyo kiongozi wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji chetu? Na ashawahi kuniambia kwamba, akishamaliza shule ataanza kuandika makala mbalimbali za kufichua mienendo mibovu ya serikali yetu, pia kuhusu huyu mzee Tualike anayetaka kugombea. Na huyu Mzee ndiye kamwondoa.”



Kila mtaa kwa wakati huo maongezi yalikuwa juu ya hotuba, ila kilichowafanya waijadili kwa kina ni kifo cha Awetu. Wengi wao walihuzunishwa na kuwapa hisia tofauti, huku ile ya serikali kuhusika katika kifo chake kwa lengo la kutunza siri ilishika nafasi kubwa zaidi ya zingine. Imani ya kuwa Awetu kafariki kwa ugonjwa wa kipindupindu uliotangazwa ama ajali aliyoipata kuchangia kifo chake ilikuwa finyu, wananchi wachache ndiyo waliamini, hususani wale wenye mapendo na serikali. Wengi hawakuwa na imani, jambo lililozua chukizo ndani ya mioyo yao kwa uongozi wa serikali ongozi. Baadhi pia walihusisha tukio hilo na mzee Tualike, serikali ilitumika kama kificho cha kumficha asihusishwe nalo kama yule kijana alivyohisi. Hivyo moja kwa moja wale waliohusisha tukio na mzee Tualike, walitokea kuanza kumchukia mzee huyo, na kusambaza chukizo lao kwa watu wengine wafahamu kile walichokiamini wao ukifuatilia mlolongo wa tukio ulivyo.

“Nadhani mnajua kuwa mzee Tualike ana nguvu kubwa sana hata ndani ya serikali yetu, kwa hiyo hata hili lililotokea anaweza toa agizo mtu wa serikali akatenda alichoagiza. Hivyo msishangae haya maneno mnayoambiwa.”

“Inawezekana vipi? Kiongozi wa serikali kuamriwa na raia?”

“Huwezi jua, walisaidiana vipi katika harakati za kimaisha.”



Kadri siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo taarifa ya mzee Tualike kuhusishwa na mauaji ya Awetu ilizidi kuenea. Imani ya kuwa mwanaharakati hodari mwenye kujali umma ilipungua, wakamuona ni muuaji kama wauaji wengine asiye hata na chembe ya vitu anavyohubiri. Watu walimchukia haswa, na walidhihirisha chukizo lao kwa namna nyingi walizokuwa wanazitenda wamuonapo. Sehemu nyingi apitazo hakukosa kuoneshwa vidole ama kuchekwa, kwa cheko lililojaa dharau na kebehi.



Mzee Tualike aliyashuhudia aliyokuwa anafanyiwa, jambo lililopelekea kukutana na wapambe wake kujadiliana hatua ya kuchukua. Kama ilivyo ada, mzee Kasoyaga, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, alikuwa sehemu ya wapambe, tena ndiye mchangiaji mkubwa wa hoja juu ya jambo la kufanya ili kuyakabili machafuko yaliyojitokeza.

“Kama tutaruhusu maneno yaendelee dhidi yangu, akijitokeza mpinzani sitakuwa na ushindi. Mzee Kasoyaga nahitaji jitihada zako, hawa wakome...wakome kunifuatilia.”

“Kuhusu hilo usiwe na shaka, niko nyuma yako. Nitapambana kuhakikisha tuliyopanga yanafikia lengo.”

“Nitafarijika tukifikia huko, kwa sasa nakosa amani kiasi kwamba natumia nguvu kubwa kumshawishi mtu yeyote nikizungumza naye.”

“Pole kwa hilo, lakini kwa leo naongeza kiasi cha upendo na vitendo kwako. Nitahakikisha leo ni mwisho wa uchafuzi wa jina lako, uliokuwa unatendewa na wapinzani wako.”





Jasho jekejeke lilitiririka mashavuni mwa Mchungaji Chilombo na wenzake waliokuwa hainehaine kupandisha vilima wakielekea nyumbani kwa Mkuu wa Mgambo, mstaafu MJM Lucas Zimbwa, aishiye shamba—mbali kidogo kutoka kwenye kijiji chao. Jua lililochomoza kucha zake kwa ukali, pasipo na nafasi ya kupumzia ndilo lililolainisha vinyweleo vyao na kuruhusu jasho kuwatiririka utadhani walitoka kwenye mbio za masafa marefu. Hatua ndefu na za haraka ziliwashughulisha kila sehemu ya mwili. Walitumia muda wa saa moja hadi kuwasili nyumbani kwa Zimbwa wakitawaliwa na uchovu uliotokana na miguu kupoteza nguvu, pamoja na kichwa kupata maumivu kwa mbali sababu ya miale ya jua iliyokuwa inagonga juu ya vichwa.



Walipokelewa na mhusika, tena kwa bashasha ya hali ya juu, mithili ya mtu aliyekosa kupokea wageni watokao mjini miaka mingi. Moja kwa moja aliwakaribisha sebeluni, mlimo pambwa na samani za kiasili kutoka ndani ya kijiji chao kwa kutumia malighafi za kijijini.



Hawakukawia kuanza maongezi, baada ya salamu na utambulisho kupita.“Mzee, tunalo jambo lililotuleta, lakini haliwezi kukosekana la pili endapo utatupatia nafasi zaidi na kama nawe una muda wa kutosha. Nina hakika sitakosea tukijiita wanaharakati, maana ndiyo shughuli tunazojihusisha nazo muda mwingi.......”

“Nawafahamu!” Mzee Zimbwa alimkatisha Mchungaji. Chilombo. Alilegeza koo kwa kukohoa kidogo.



Mchungaji Chilombo hakuishia hapo, aliendeleza maongezi kwa kueleza shida iliyowafikisha pale, ujumbe waliouokota wakihitaji kujua maana na waliamini hapo ndipo sehemu sahihi.

“Mmefahamu vipi haya maandishi?” Mzee Zimbwa alianza na swali punde baada ya kuoneshwa ule ujumbe.

“Kuna sehemu tumeuokota. Tunahisi uliandikwa na Awetu.”

“Hivyo mnachohitaji kutoka kwenye ujumbe huu ni kipi?”

“Kuna maandishi tuyaongezee kisha utupatie maana kamili.”

“Yapi hayo?”

“3 O’clock ahead.”

“Oooh! Ama kweli ninyi ni wanaharakati. Ondoeni shaka, kwa kuwa sote ni wamoja, nitawafafanulia japo ni makosa kwa watu kama nyie kufahamu maneno yatumiwayo na taasisi za siri za ulinzi wa kijiji chetu,” alisema Mzee Zimbwa huku akinyanyuka alipoketi na kutoka. Kwa kutofahamu wapi anaelekea, alipiga hatua kadhaa na kuishia mbele ya kabati dogo lililohifadhiwa nyaraka nyingi zilizoonesha uchakavu.



Aliuongoza mkono hadi kwenye moja ya sanduku lililopo kwenye kabati na kutoka na kitabu kidogo kilichoanza kuchanika na kujaa vumbi, kisha akarejea sehemu ile aliyoketi awali. Alifunua karatasi moja baada ya nyingine. Alipofika katikati, aliwaomba wageni wasogee karibu ili wapate taaluma waliyoifuata.

“Nawapatia maarifa haya kwa sababu sina maelewano mazuri na viongozi wa serikali yetu, kutokana na udhalilishaji walionifanyia.”

“Na ni jambo la kushangaza sana kiongozi. Hivi muda wako wa kustaafu haukufikia?” Mooja aliuliza.

“Acheni tu! Ila wajiandae kuuona ubora wangu. Tena akipita yule mzee Tualike, watauona haswa, maana ndiye mchawi wangu nambari moja.”

“Hata sisi tunahitaji iwe hivyo, na hii mihangaiko yote tuifanyayo ni dhidi yake.”

Dakika mbili baadaye tayari walikuwa jirani na mzee Zimbwa, macho yakiwa kodokodo kwenye kitabu kilichoonesha michoro na namba mbalimbali na maana mbele yake. Ufafanuzi ulianza, neno na namba moja ikifuatia na nyingine hadi kauli ile waliyohitaji kukamilika.

“Haya ni maneno ya wanausalama, ambapo hutumika sana kutoa taarifa fulani ya hatari. Hususani ukiongeza hilo neno la mwisho kunitajia, ‘3 o’clock ahead’ ambapo humaanisha umbali wa mita mia moja. Hivyo ukichukua 125 + 3 o’clock ahead, hapa itakuletea maana nyingine.”

“Hiyo maana ndiyo tunaihitaji.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hakuna shida mtaipata. Tunaanza na 125, hii ina maanisha ni ngome, huku 3 o’clock ahead, ikiwa na maana ya mita mia moja, hivyo ukijumlisha utapata ‘ngome umbali wa mita mia moja. Tukienda kwa neno mojamoja itakuwa hivi; 1= Gari, namba itayofuatia lazima iwe namba ya kiti, hivyo, namba mbili ni namba ya kiti kwenye hiyo gari, vilevile ina maana ya kiongozi, na ile ya mwisho ni uvunguni, ama ina maana ya Mwenyekiti wa baraza la kijiji.”

“Sasa maana kamili ni ipi?”

“Maana yake ni hivi, kuna ujumbe kauacha umbali wa mita mia moja kutoka mlipo uokota huu ujumbe, kauacha kwenye gari ya Mwenyekiti wa baraza la kijiji, ama ujumbe huo upo ndani ya gari hususani basi, siti namba mbili chini ya uvungu.”

“Eti?”

“Hiyo ndiyo maana ya huo ujumbe. Sasa cha kufanya, mjiulize, kutoka pale mlipouokota ujumbe, kuna sehemu yenye hifadhi yoyote ya vyombo vya usafiri kwa huo umbali?”



Kimya cha muda mfupi kilipita, kilichowapeleka kila mmoja kwenye tafakuri ya mazingira ya karibu na walipouokota ujumbe kama kuna kitu walichoambiwa. Haikupita muda mrefu, Mooja alionekana kukumbuka jambo.

“Ndiyo, kuna hifadhi umbali mfupi kutoka pale getini, tena ziko hifadhi mbili, moja ya magari ya serikali na nyingine inahifadhi magari binafsi. Ila tangu ianzishwe hiyo hifadhi ya magari, binafsi ni gari moja tu linalohifadhiwa, ambalo ni Hiace.”

“Nina hakika mtakuwa mmenielewa. Na siri nyingine ninayowapatia, hiyo gari ya huyo kiongozi wa baraza, namba ya usajili wa gari ni 125.”

“Tunashukuru kwa taarifa,” walisema kwa pamoja kisha waliaga na kuondoka.



Baada ya kuondoka walielekea kwenye hifadhi ya magari. Waliifikia ile ya kwanza, ile inayohifadhi magari ya serikali na kukuta mgambo wawili wakiwa na gobore mikononi. Mmoja alijitoa kuwa chambo wa kuwafuata wale mgambo ili kuzungumza nao kuhusiana na shida waliyonayo. Alikuwa ni Mooja. Alitumia ustadi wa matamshi uliowavuta mgambo wote wawili huku wakisindikizwa na sarafu kadhaa za shilingi walizokabidhiwa kwa usiri.

“Fanyeni haraka!” Walisema wale mgambo kwa pamoja huku wakificha kwenye nguo za ndani sarafu walizopewa.



Mooja aliwaita wenzake na kuingia ndani ya hifadhi kuanza kulitafuta gari la Mwenyekiti wa baraza la serikali ya kijiji. Hawakukawia kuungana naye, kisha kujumuika kulitafuta. Walizunguka safu mbili tu, wakaliona likiwa limeegeshwa mwisho kabisa wa safu ya pili. Haraka sana, walilichunguza kila sehemu kwa nje. Hawakuambulia chochote. Hawakufa moyo, waliendelea zaidi na zaidi ila hawakufanikiwa.

“Yawezekana kimo ndani, huku nje tunajisumbua tu.”

“Labda, maana si kila sehemu tushaichunguza. Ama kuna sehemu tuliyoiacha?”

“Sidhani......!” Wanajadiliana.

“Twendeni kwenye hifadhi nyingine. Inaweza ikawa si gari hii,” Mchungaji Chilombo alishauri.



Walipiga hatua hadi kwenye ile hifadhi binafsi. Walimkuta mlinzi aliyeonekana kutoka kulala, mikunjo iliyoenea usoni ilimshitaki. Hawakujali hilo, walishika hamsini zao. Hapo napo walifanya kama kule kwa awali, sarafu kadhaa ziliwasaidia kumshawishi mlinzi wakaingia pasipo zuio. Walifuata maelezo waliyoambiwa. Waliingia ndani ya hiace hadi kiti husika. Waliibaini baada ya kuangaza macho kwenye namba za kiti zilizobandikwa juu, pembeni.



Walivuruga kiti kizima, kila sehemu iliyoonesha uwazi ili wapate walichohisi kinaweza kuwa muhimu katika harakati zao. Walitumia dakika kwa dakika bila mafanikio hadi wakahamia siti jirani nazo kuzipekua lakini matokeo hayakutofautiana. Baadaye ilibidi waondoke, sehemu kubwa ya akili yao ikitawaliwa na mawazo tele ya kitu gani wanachotafuta. Hisia za kuacha walichokuwa wanaendelea nacho, nazo zilianza kutawala, kwa kasi mithili ya moto wa nyika ili wabaki na kitu kimoja tu, kumsimamisha mgombea wa kushindana na Mzee Tualike baada ya yule wanayemhitaji kukosa matumaini ya kumpata. Walishauriana kurudi nyumbani kwa MJM Zimbwa, kwenda kumshawishi agombee nafasi hiyo, ushauri uliokubaliwa na wote kisha kuianza safari.



Walitembea hatua kadhaa toka ilipo hifadhi binafsi, wakaanza kusikia maongezi ya watu fulani yaliyovuta masikio yao kutaka kuyasikiliza.

“Ndugu yangu, hivi unajua Mwenyekiti wa baraza la serikali ameacha kutumia ile gari yake kwa sababu ilimbeba Awetu kipindi amepata ajali pamoja na mwili wa mtu aliyeaga dunia?”

“Hapana. Kwani ana gari mpya siku hizi?”

“Ndiyo. Gari yake ya zamani ile pale hifadhini, wala haijawahi kutembea tena tokea kilivyofanyika hicho kitu. Na walifanya ukatili sana ile siku. Kwani Awetu ambaye ni mzima alibebwa juu ya kichukuzi halafu mwili wa marehemu ukaingizwa ndani.”

“Duh! Uongozi wetu una shida sana. Sasa hayo si matumizi mabaya ya fedha za umma?”

“Tena kufuru!”



Maongezi hayo yalitia tumaini kwao. Walijua wakitafutacho kipo ndani ya gari la Mwenyekiti wa baraza la serikali ya kijiji.Tena walipatwa na mshituko sana baada ya kusikia Awetu alipandishwa juu ya kichukuzi, mshituko uliowafanya kukumbuka jambo.

“Hivi, kuna aliyekagua juu ya kichukuzi?” Mchungaji Chilombo aliuliza.

“Hapana!”

“Twendeni turudi. Yawezekana hicho kitu kipo hapo.”



Mbinu mpya za kuwarudisha ndani zilivumbuliwa. Kwa wepesi, ila awamu hii hawakuhitaji kwenda wote, mtu mmoja miongoni mwao alijiteua, Mchungaji Chilombo. Safari hiyo haikuwa ngumu kuwarubuni wale walinzi, maneno machache tu, yalimpa ruhusa.

“Samahani ndugu zangu, kuna kitu fulani nilisahau.”

“Hakuna shida, nenda tu.”



****



Siku moja baadaye, tangia siku ambayo Mganga Mkuu wa Zahanati ya kijiji asome orodha ya wafu na waathirika mahututi wa ugonjwa wa kipindupindu, wafu walizikwa. Wagonjwa waliendelea kupatiwa matibabu lakini baadhi yao waliaga dunia. Miili ya marehemu haikuagwa wala kupelekwa mtaa mwingine tofauti na ule wa zahanati ili kuepusha maambukizi mapya. Hivyo walizikwa eneo jirani na zahanati.



Shangazi yake na Awetu, ni mmoja ya waliohudhuria mazishi. Alihudhuria baada ya kupata taarifa za kifo cha mtu ampendaye na tegemezi pekee kwake. Muda wote alionekana kulia, tangu mazishi yanaanza hadi yalivyomalizika, na pindi watu wanatawanyika alizimia.



Wasamaria hawakusita kumsaidia. Walimchukua na kumkimbiza kwenye zahanati ambapo alipatiwa matibabu na baada ya muda alirejea katika hali ya kawaida kisha aliruhusiwa kurudi nyumbani. Raha ya maisha aliyokuwa anaishi ilianza kupotea. Ukiwa ulishika nafasi na kuimeza furaha yake yote. Hakuacha kulia. Kila wakati alikuwa mtu wa kujawa simanzi huku akitoa malalamiko kwa kumlaumu Mungu kwa kumchukua ampendaye na jicho lake. Furaha ilikosekana, maisha yakawa machungu, afya ilidhoofika na utendaji wa kazi katika shughuli zake alizokuwa anazimudu kwa kipindi cha nyuma aliachana nazo. Kumsahau Awetu lilikuwa jambo gumu, na halikuwezekana japo Bi. Mwema na Laumio walijitahidi kuwa mstari wa mbele kumpatia faraja kwa muda fulani. Kwani hawakuweza kumpatia muda wote kutokana na kuhisi kutafutwa.



Walifanya siri katika hilo ili wasibainike kama bado wapo kijijini hapo. Waliteua muda wa kumsaidia, mwingine walitafuta sehemu ya kujificha, hususani mchana wasipate kuonekana. Zoezi lilichukua karibu mwezi mmoja, huku afya ya Bi. Mwamini ikizidi dhorota kila kukicha kutokana na msongo wa mawazo uliotawala sehemu kubwa ya akili yake. Kila aina ya jitihada ya kumsaidia ilifanyika kwa kiwango cha juu kurudisha ukawaida lakini zilikosa msaada. Mwezi mmoja na wiki moja tu toka Awetu afariki naye ukawa mwisho wa maisha yake. Mawazo yaliyodhoofisha na kupunguza uzito alionao yalikuwa na nguvu kubwa kuliko jitihada za faraja aliyokuwa anapatiwa.



Maziko yalifanyika siku iliyofuata, alizikwa na wananchi wachache wa kijijini na baadhi ya vijiji jirani waliomfahamu. Lakini Bi. Mwema na Laumio hawakuhudhuria kwa sababu ya hofu ya kutafutwa na hawakuhitaji kuonekana. Kifo chake kilikuwa pigo kwa Bi. Mwema na Laumio, kwani makazi yake ndiyo yaliyokuwa yanawahifadhi kwa kipindi cha usiku. Kuondoka kwake waliamini kutawapatia wakati mgumu wa kutafuta makazi pa kujistiri ili wasibainike. Waliishia kutanga na kuyahamishia makazi yao msituni. Huko waliamini ndipo sehemu sahihi ambayo wangepata kuishi pasipo na shaka.



Shida ilikuja kwenye chakula. Walikosa chanzo sahihi cha kuwawezesha kupata jambo lililowafanya siku mbili za mwanzo walizokimbilia msituni kutokula, walishinda kwa kunywa maji na kuponea matunda pori. Njaa iliwasumbua na kuchosha miili kiasi kwamba hawakuweza kushughulisha akili namna gani watajikwamua. Wazo la kufa njaa halikusita kujipenyeza na kuchukua nafasi kubwa akilini, kwa jinsi njaa ilivyowazidi nguvu. Hasa Laumio, hadi ilifikia hatua ya kushindwa kutamka neno ama kuunyoosha mkono wake.



Baadaye Bi. Mwema ilimbidi aanze kuvamia mashamba ya watu kuiba vitu kadha wa kadha vyenye kufurahisha matumbo. Laumio alivyorejewa na nguvu, naye alijumuika katika utafutaji. Walifanya hivyo takribani muda wa wiki mbili, na kutengeneza akiba ya kutosha ya chakula iliyowasitisha kuendelea kuiba. Walirejea kwenye kazi hiyo wiki kadhaa mbele akiba ilivyomalizika.



Wizi walioendelea nao uliwaibua wanakijiji kutoa malalamiko mengi na kulaani kitendo hicho. Kila wakutanapo wanakijiji wawili hawakuisha kuulizana hali ya mashamba yao, kwa sababu ya kitendo hicho kushamiri kila uchao na kuchwa.

“Huyu anayeiba mbona anataka kutupatia kazi ngumu ambayo hatukuitarajia? Ina maana anataka tukae mashambani hadi usiku?”

“Yaani!....anatupatia mtihani mgumu sana. Nahisi si mtu mmoja anayefanya hivi.”

“Yawezekana, ananichukiza balaa, leo hii ananilazimisha kurudi usiku. Nitamaliza shughuli mapema kisha nitakuwepo kufanya doria kama atajitokeza nipambane.”

“Uamuzi mzuri.”



Yalikuwa maongezi ya wazee wawili walioambatana kuelekea shamba. Walikasirishwa na wizi uliojitokeza shambani mwao. Wakati huo suala la kuikomesha familia ya mzee Tualike lilitoweka kabisa akilini mwao, baada ya yule waliyemtegemea kuwafungulia njia ya kuwasilisha hoja walizonazo juu ya familia watokayo kutokuwepo duniani. Akili iliangalia maisha kwanza, kujua namna watavyoishi wakiwa mbali na wale waliowakimbia. Waliendelea kuamini, endapo watabainika hawatawaacha salama hata kama watapewa nafasi ya kurudi nyumbani. Huku wakiendelea na mipango mingine ya uendelezo taratibu ili pale mambo yatakapokaa sawa watimize yao nia. Hawakuwa na budi kukubali kuishi maisha ya kutangatanga, imani ikiwatuma kuamini kuwa ipo siku watakaa sehemu nzuri na sahihi isiyo na hofu juu ya chochote.



Ilikuwa jioni, mawingu yakiwa yametanda angani ikionesha muda wowote mvua inaweza kunyesha, Bi. Mwema aliambatana na mwanae, Laumio kwa hatua fupifupi wakikatisha shambani kwa ajili ya kuiba mazao ya chakula.

“Mama, leo nataka mihogo, viazi vishanichosha,” alisema Laumio wakizidi kusonga mbele, ndani zaidi ya mashamba.

“Unahisi tutaipatia wapi ilhali unaona mashamba yote tuyapitayo mazao mengi ni yaleyale?”

“Twende hata kwenye lile la mbele, yawezekana tukabahatika kuikuta na hatujawahi kwenda kabisa,” alisema Laumio akilinyoshea kidole shamba.



Walikubaliana. Walitembea hadi kwenye shamba husika. Kabla hawajaliingia, wakaanza kuchunguza kama kuna mhusika ndani, lakini hawakumuona yeyote zaidi ya ndege warukao na wanyama wadogo waliokuwa mawindoni kufukuzia ndege na nyoka. Walijiridhisha kwa mara nyingine, ila matokeo yalikuwa yaleyale ya awali. Hawakuishia hapo, walisubiri karibia dakika nne ndipo waliporidhika kuwa hakuna mtu, waliingia. Hawakuchelea. Walianza kuchukua walivyohitaji kwa uharaka usio wa kawaida ili wasifumaniwe. Waliichangamsha mikono, iweze kuchukua vitu vingi huku vile vilivyoko tayari walivifunga kwenye khanga.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Muda mfupi baadaye mawingu yaliruhusu rasharasha ya mvua iliyozidi kuongezeka kila dakika. Vurugu za mvua ziliwafanya wasisikie hasa kutokana na ngurumo kubwa iliyoambatana na upepo kiasi. Walivuna, walipoona kiasi walichonacho kinatosha waliinua migongo tayari kwa kuondoka.

“Simama kama mlivyo,” sauti kali ilisikika kutoka kwa mzee mrefu aliye na umbo lililoshiba mkononi, akiwa na mshale wenye sumu, umbali mfupi kutoka walipo. Walistaajabu hadi vitu walivyobeba mikononi viliwaponyoka.







Taratibu yule mzee aliwasogelea, sura ikiwa imekakamaa huku ndita zikiwa zimesimama kama matuta ya viazi vitamu usoni. Wakati huo kiza nacho kilianza kuondoa mwanga, hali iliyomsababisha mzee huyo kutoa kurunzi katika moja ya mfuko wake wa suruali aliyoivaa kuwamulika. Miali ya mwanga iliyotua usoni ilifanya waone haya na kujitahidi kuficha nyuso zao lakini walikwishachelewa, kwani mwanga uliomulikwa ulimpa mzee nafasi ya kuwatambua. Alipatwa na mshituko wa ghafla mara baada ya kuwatambua.



Butwaa lililowapata liliumba aibu na mawazo tele baada ya hapo. Picha mbaya ya kudhalilika kijijini nayo iliibuka, waliwaza kuwa watachukuliwaje na wananchi, watu waliokuwa wanadumu kuhubiri amani na upendo halafu wamegeuka wezi, wanaoondoa tegemezi la mwanakijiji aliloliwekeza kwa muda mrefu. Kwa namna moja ama nyingine, imani yao iliwaaminisha huwa huyo mtu aliyewakamata atapobaini kuwa ni wao hatafanya jambo lolote zaidi ya kuwapeleka kijijini akawadhalilishe.

“Mama!...mama...mama!” aliita mzee huyo punde baada ya kuwatambua kuwa ni Bi. Mwema na Laumio. Ila hawakuitika kwa sababu ya aibu.



Alipowafikia alizima kurunzi na kuirejesha alikoitoa, mshale nao aliutupa chini. Alihema kwa nguvu kiasi kisha kuwapa mkono kuwasabahi, lakini walishindwa kuitikia salamu yake kisa tu walishafahamika. Hatimaye walipiga magoti kuomba wasamehewe, wasipelekwe mahali na wasitangazwe kuwa ni wahusika wa hayo yaliyotokea. Msahama wao uliambatana na machozi yaliyotiririka mashavuni kuonesha ni kiasi gani walijutia kile walichofanya.

“Naomba utu...sa...mehe baba yetu, maisha ndi...ndiyo yametufanya tugeuke kuwa na hii hali tuifanyayo,” alisema Bi. Mwema huku akiendelea kulia.

“Mama, acheni kulia. Mimi nimekwisha wasamehe mara baada ya kugundua kuwa ni nyie,” alisema mzee huyo wakati akifanya jitihada za kuwainua pale chini.

“Ahsante sana baba, Mungu akujalie katika mambo yako.”

“Nashukuru sana. Nafahamu mko katika matatizo makubwa sana, ila kama hamtajali nataka niwasaidie.”

“Msaada gani huo unaohitaji kutupatia?”

“Mnataabika sana. Hivyo nimeona si vibaya kama nitawapatia nafasi ya kuishi nyumbani kwangu.”

“Hapana, tuache hukuhuku. Kijijini hatuhitaji kabisa, kama ni msaada tupe msaada wa ridhaa yako ya kuingia shambani. Hapo utakuwa umetusaidia vya kutosha.”

“Najua kitu kipi kinawapa hofu, ila ninawaahidi kuwalinda na kuishi kwenye matakwa yenu mkiwa kijijini.”



Wema uliooneshwa na mwenye shamba uliwapa hamasa na kuondoa fikra hasi akilini, kitendo kilichowafanya watazamane kwa sekunde kadhaa kisha kwa pamoja walijikuta wakimuuliza swali moja. “Kwani wewe ni nani?”

“Ina maana hadi sasa hamjanifahamu? Mimi naitwa...!”

__________



Wakati ajali ya bajaji inatokea, iliyohusisha ile iliyombeba Awetu na nyingine, gari dogo la Mwenyekiti wa baraza la serikali ya kijiji lilikuwa na mtu mmoja, dereva pekee. Lilipita jirani kabisa na eneo la ajali. Kwa ukarimu aliobarikiwa nao dereva alisimamisha gari na kuungana na wasamaria waliojitokeza kusaidia manusura wa ajali.

“Tuwapandishe kwenye lile gari,” alisema dereva akilionesha gari husika, gari aliyoiendesha mwenyewe.



Walifanya hivyo, lakini Awetu alipandishwa juu ya kichukuzi halafu mwili wa marehemu uliingizwa ndani ya gari jambo lililowashangaza baadhi ya watu, lakini hawakuweza kuhoji sababu kwani hayo yalikuwa maamuzi ya dereva. Wakati huo, Awetu alikuwa ameshika flash mkononi, hakutaka kuiachia hadi anapandishwa garini na kuondoka. Hakuna mtu aliyemshuhudia kama ana kitu kashikilia. Walivyofika hospitalini aliibana katika uwazi fulani uliopo juu ya kichukuzi ndipo akateremshwa. Matibabu yalianza punde baada ya kuwasilishwa wodini ili kuyanusuru maisha yake ambayo yalikuwa hatarini kwa sababu baadhi ya viungo vya mwili vilishindwa kufanya kazi.



Madaktari na wauguzi walijitahidi kunusuru maisha yake, kwa kuvishughulikia ipasavyo viungo vyote vilivyoshindwa kufanya kazi pamoja na vile vilivyovunjika. Haikuwa kazi rahisi, ilikuwa kazi ya jasho jingi na kujitolea. Umakini ulitamalaki, hadi mwisho walivyokamilisha ndipo walianza mizaha tena wakiwa nje ya wodi. Pongezi nazo hazikukosekana kwa kazi nzuri yenye weledi waliyoifanya.

“Imani yangu kuanzia sasa wanakijiji wetu watatukubali na kutupa heshima kupitia hii kazi. Hata zahanati yetu nayo itaheshimika, tofauti na awali ilivyokuwa,” alisema daktari aliyeongoza jopo katika matibabu ya Awetu.

“Sahihi kiongozi,” wenzake nao waliunga mkono hoja yake.



Taarifa za ajali zilifika mezani kwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, mzee Kasoyaga, kupitia kwa mgambo aliowatuma, kisha naye kumhabarisha rafikiye mzee Tualike. Walijikuta wanaingia kwenye majadiliano ya muda mfupi wakati wanapeana habari hizo. Hasira kali alizonazo mzee Tualike kwa Awetu, haraka sana alitoa maamuzi juu ya cha kufanya, kwani aliamini tukio hilo lilimrahisishia kazi tofauti na wao walivyofikiri.

“Ninachohitaji huyo binti ni kufungwa mdomo, aidha kwa kumuondoa kabisa duniani ama kukaa sehemu itayomzuia kuonekana uraiani,” alisema mzee Tualike pindi anaongea na mzee Kasoyaga kwa njia ya simu.

“Lakini kwa hiki kilichompata si tusubiri apone ndipo tufanye mambo yetu? Yumkini hili tatizo litamuondoa kabisa duniani.”

“Hapana! Huu ndio wakati sahihi ambao utatufichia uhusika wetu wa kile tutakachomtendea. Tutumie hii nafasi.”

“Kwa namna ipi labda?”

“Tunamuondoa kisha tunatumia tatizo alilonalo kuwa ndilo lililomuondoa.”

“Oooh! Nimekupata. Niachie kazi, muda si mrefu nitakupa mrejesho.”



Simu ilikatwa.



Mara baada ya kukata simu, mzee Kasoyaga aliunga upande mwingine, ambao hakuchukua sekunde nyingi kuwa kwenye maongezi naye. Alikuwa Daktari Mkuu wa Zahanati, Dkt. Makolela Tumkumbe. Maongezi yao yalikuwa mafupi, hata dakika mbili hazikutimia, walihitimisha na simu kukatwa. Kwa mara nyingine alirudi tena kwa mzee Tualike kumpatia mrejesho.

“Andaa vijana wako siku tano toka leo kukamilisha dhamira tuliyonayo.”

“Hilo ondoa shaka, ila ni mpango upi uliouandaa?”

“Nimemshirikisha daktari mkuu wa zahanati yetu kakubali, anamchukia sana yule binti. Hivyo kaniambia atafanya mlipuko wa ugonjwa, ambao utamuingiza Awetu ndani na kumpeleka katika waathirika watakaoondoka duniani. Tutapata nafasi ya kumchukua na kwenda kufanya yetu wakati huo wanakijiji wakiwa na ufahamu kuwa amefariki kwa mlipuko wa ugonjwa.”

“Ugonjwa upi?”

“Hajaniambia ni ugonjwa gani. Ila fahamu hivyo.”

“Nimekuelewa.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/







Kweli, siku tatu baadae, Dkt. Makolela alisambaza bakteria wa ugonjwa wa kipindupindu kwa baadhi ya wagonjwa kupitia dripu za maji, damu na dawa za maji zitumiwazo na wagonjwa. Awetu naye alikuwa miongoni mwa walengwa, tena alikuwa mgonjwa wa kwanza kisha kufuatia mgonjwa mwingine aliyekuwa pembeni yake, ambaye naye ni mlemavu wa ngozi kama yeye.



Matokeo hayakuchukuchua muda kuonekana, jambo lililokuwa la ghafla na kushitukiza lilivyosikika masikioni mwa wanakijiji. Lilishangaza hasa, ila hawakujua kuwa ni tukio lililopangwa kwa makusudi kwa ajili ya mtu fulani, Awetu. Alfajiri ya siku ya pili wagonjwa walioathirika walitolewa kwenye wodi walizokuwa wamelazwa awali na kuhamishiwa wodi nyingine ya muda, iliyotengenezwa kwa turubai. Kazi hiyo ilifanywa na wauguzi wakisaidiana na madaktari wawili ambao waligeuka kuwa waongozaji wa shughuli hiyo.

“Naomba wodi namba mbili asiingie mtu yeyote hadi nitakapotoa maelekezo mengine,” Dkt. Makolela alisema, kuwaambia madaktari waliokuwa wanaongoza zoezi la kuwahamisha wagonjwa walioathirika na ugonjwa wa kipindupindu.

“Hakuna shida bosi, tutatekeleza amri yako,” wale madaktari waliitikia.



Agizo la Dkt. Makolela lilitekelezwa, wagonjwa wote walipelekwa wodi mpya, kasoro waliopo wodi namba mbili, ambayo alikuwemo Awetu. Wakati pilikapilika za kupanga sawa wagonjwa kwenye wodi mpya zikiendelea, watu wawili waliovaa mavazi ya kidaktari na zana za matibabu wakiwa wameshikana walionekana kuingia wodi namba mbili, tena taratibu kabisa pasipo chembe ya shaka. Mavazi waliyovaa, yaliwatambulisha kuwa ni madaktari wenye ujuzi wa kutosha na taaluma hiyo. Miwani ya rangi nyeusi, ile izuiayo miali ya jua ilikaa vizuri usoni, sambamba na vitambaa vilivyozuia pua na mdomo pasipo kusahau koti jeupe lisilo na doa. Mtu yeyote aliyewaona hakuisha kufurahishwa na jinsi walivyoonekana nadhifu kiasi kwamba hawakuweza kutambulika kirahisi kwa watu waliopishana nao.



Umbali mfupi kutoka wodi ilipo alisimama mlinzi mmoja alindaye wodi. Walimfuata na kumsabahi kisha kumuonesha nyaraka zilizoonyesha kuruhusiwa kuingia wodini, kwani chini ya nyaraka ilionekana saini ya Dkt. Makolela. Waliingia moja kwa moja walikwenda hadi kwenye kitanda alicholazwa Awetu, kilichokuwa kati ya vitanda vingine. Vilikuwa vitanda vitatu. Hawakuchelea, walitenda kilichowapeleka. Mmoja wao alichomoa sindano na kunyonya dawa kwenye chupa ndogo na kumchoma katika paja lake la kushoto, mwenyewe akiwa anashuhudia kila kitu, lakini hakuwatambua madaktari hao, walikuwa tofauti na wale waliokuwa wanampatia matibabu siku zote. Sura zao hazikuonekana, kila alivyojaribu kutaka kuwafahamu hakuweza, kwani wale watu walikazana kuficha sura. Uvumilivu ulimshinda baada ya kutofanikiwa, ilibidi awaulize.

“Ninyi ni madaktari wapya?”

“Ndiyo. Kwani kuna tatizo?”

“Hapana, ni wageni kwangu. Mnaweza kuvua miwani niwatambue? Mnaonekana kuwa na sura nzuri sana.”

“Sisi ni madaktari wapya kwa hapa hospitalini, ila ni wazoefu wa taaluma ya udaktari kwa muda mrefu. Tumekuja kuongeza nguvu baada ya kutokea huu mlipuko wa kipindupindu.”

“Oooh! Sasa nimewaelewa...kwa...h...” alisema Awetu, ila alishindwa kumalizia sentensi yake, usingizi ulianza kumchukua uliotokana na ile sindano aliyochomwa.



Pindi hayo yanatokea ni mgonjwa mmoja tu alishuhudia kwa usiri mkubwa kupitia upenyo wa shuka alilojifunika. Mwingine uhai wake ulishapotea muda mwingi uliopita kwani naye alishasambaziwa bakteria. Japo alishuhudia lakini hakutambua kinachoendelea kwani ugonjwa aliokuwa anaumwa ni ugonjwa wa macho, hivyo hakuwa na uwezo wa kuona vizuri. Awetu alitapatapa kidogo pale kitandani, mapovu kidogo nayo yalimtoka kisha alitulia. Alivyotulia walimfunika vizuri, kama mtu aliyekwisha fariki kwa shuka kubwa jeupe na kutoka akiwa juu ya kilekile kitanda alichokuwa amelazwa.



Hawakumpeleka mahali wagonjwa wengine walikopelekwa, uelekeo wao ulikuwa lango kuu la kuingilia ilipo zahanati, ambapo gari dogo lilisimama kuwasubiri. Walivyolifikia walimpandisha nao kuingia ndani kisha iliwashwa na kuondoka. Mwendo haukuwa wa kawaida, dereva alikanyaga mafuta mithili ya gari la majambazi inayofuatiliwa na gari la polisi. Hawakuwa watu wema.

“Uelekeo wetu?” dereva aliuliza.

“Hifadhi ya wanyama pori,” alijibu mmoja wao.



Mwendo wa saa moja waliwasili hifadhi husika. Hifadhi ya wanyama pori ya kijiji iitwayo Nanenane, ambayo iko mpakani na kijiji cha Hatuleani. Waliingia ndani kabisa, sehemu iliyowaficha kuonekana na kutosikika kwa kitu walichodhamiria kufanya. Waliteremka, na kumteremsha Awetu pia ambaye bado alikuwa usingizini na kumlaza chini ya nyasi zilizoenea miba. Walipeana ishara fulani iliyomsukuma mmoja wao kuinama pale chini walipomlaza, huku taratibu akichomoa sindano na kumchoma.



Sekunde chache baadaye Awetu alionekana kufumbua macho, kisha wale waliovalia mavazi ya kidaktari walivua mavazi hayo pamoja na miwani zao. Sura zilizoonekana mbele yake, zilimshitua na kumpa hofu iliyomsukuma kutoa haja ndogo palepale alipokaa. Mwisho wa maisha yake aliushuhudia ukiwa karibu kwa umbali na muda, kwani akili yake ilishamuaminisha baada ya kuwatambua wale walioko mbele yake. Hakuwa na budi, alianza sala, kumuomba Mungu amnusuru dhidi ya watu hao walioonekana kukosa huruma moyoni mwao. Akiwa katikati ya sala alisikia kitu chenye ncha kali kikizamishwa mwilini mwake kwa nguvu, usawa wa mbavu na juu ya matiti. Kitu hicho kilirudia karibia mara mbili na kutoa damu kiasi kidogo katika sehemu zile alizokuwa anachomwa. Ila baadaye alijiona anaishiwa nguvu na kupoteza fahamu kabisa.

“Huo ndio mwisho wa maisha yako, nenda kawasalimie wale wote tuliowatanguliza. Waambie kimbelembele chao ndicho kimewaponza kama wewe kilivyokuponza, bado hao ambao walikupatia ujumbe, siku si nyingi watakufuata. Punde baada ya kuja huko walaumu, kwanini walikukabidhi ujumbe wao,” alisema yule aliyekuwa ameinama, ambaye ndiyo alikuwa anaingiza kitu chenye ncha kali mwilini mwa Awetu. Sindano yenye sumu. Majungu!









Jipendekezo na Majungu ndiyo watu aliowashuhudia mbele yake, wakiwa na sura zilizosheheni hasira iliyojidhihirisha toka moyoni kwamba wanamchukia. Nia yao ilikuwa moja tu, kuuondoa uhai wake kwa namna yoyote bila majadiliano, ili kulinda maslahi ya familia yao yaliyokuwa yanaelekea kuwekwa wazi kwa wanakijiji. Hicho ndicho kilichofanyika, Majungu alimchoma sindano ya sumu iliyopoteza ufahamu na kuvimbisha mwili wake, baada ya hapo wao waliondoka.

“Wanyama watamalizia uhai wako,” walisema kwa pamoja pindi wanaondoka.



Kitu cha kwanza walichofanya ni kumtaarifu baba yao ndipo waliingia kwenye gari na kuondoka. Furaha ilitawala ndani ya mioyo yao, safari nzima hadi wanafika kijijini. Muda mwingine walikuwa wanapiga yowe kushangilia kuonesha furaha waliyonayo. Hata mzee Tualike naye hakuacha kuonesha furaha yake. Huyu ndiyo alikuwa na furaha zaidi ya wanaye, na kilichomfurahisha zaidi ni uhakika wa kukamilisha mipango yake.

“Bado hao watoa ujumbe, wakikataa kurudi, nawaondoa sijali kama ni damu yangu,” alisema mzee Tualike kimoyomoyo.



Sherehe kubwa ikaandaliwa walivyorudi kutokana na furaha yao.

“Acheni tufurahi kwa maana nauona ushindi wangu.”

“Hakuna wa kushindana nawe kiongozi. Wewe ni Mwenyekiti ajaye, hao watakaojitokeza kushindana, wanajisumbua tu.”



Ni sehemu ya maongezi yao wakiwa wanasherehekea kwa sauti iliyojaa ulevi. Tukio hilo lilifikia hadi asubuhi ya siku iliyofuata ndipo lilimalizika, wale walioalikwa wakarejea makwao. Wengi walioalikwa walivyofika makwao, walifikia kulala, lakini ilikuwa tofauti kwa mzee Tualike na wanaye. Wao waliingia kwenye kikao cha dharura ambacho hakikuchukua muda mrefu kufika tamati. Baada ya hapo ndipo walienda kulala. Juu ya mkesha walioufanya, lakini usingizi haukuja, yote kwa sababu ya kiwango kikubwa cha furaha iliyoenea sehemu kubwa ya mioyo yao. Waliishia kutumbua macho pima paani, huku wakiachia kicheko kila baada ya muda fulani wakumbukapo jambo.

“Sisi ni mashujaa wa kweli.” alisema Jipendekezo kimoyomoyo baada ya kukumbuka msemo walioambiwa na baba yao usiku wa jana, kipindi wanaendelea kusherehekea. “wanangu ni mashujaa wa kweli.”

____________



Siku zilizidi kusonga mbele kwa kasi huku akikokesekana mtu wa kushindana na mzee Tualike katika uchaguzi wa uenyekiti wa serikali ya kijiji. Hadi kufikia siku ya mwisho ya kuchukua na kurudisha fomu, hakuna mtu yeyote aliyejitokeza, jambo lililozaa tabasamu kwa mzee Tualike na kampani yake kwa ujumla na wale wanao muunga mkono.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Nilishasema hakuna mtu yeyote wa kushindana nami hapa kijijini, sasa mmeamini? Zimebaki dakika kumi tu milango ifungwe, unahisi nani atajitokeza kwa huo muda uliobakia?” Alitamba mzee Tualike katikati ya kundi la wazee waliokuwa wanapata kahawa katika moja ya vibanda kijijini hapo.

“Mzee, hii nafasi ni yako, ondoa shaka kabisa. Tushangilie ushindi tu...!”

“Oyoooooooo!” Watu wengine, hususani vijana, wanaomshangilia na kumpenda walitanda barabarani kushangilia kuwa mzee Tualike alikosa mpinzani. Shangwe zilizokuwa zimetanda utahisi tayari kashinda, hadi watu wamchukiao walijikuta wakiongeza chuki kwake, lakini hawakuwa na namna ya kubadilisha matokeo.



Saa 9:55 alasiri vijana wengi, wale waliokuwa wapiga shangwe walizingira ofisi ya bodi ya uchaguzi kusubiri tamko la Bodi kuhusu wagombea wa uchaguzi wa uenyekiti wa serikali ya kijiji na idara zake.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog