Search This Blog

Friday, November 18, 2022

IANGALIE TULEANE - 5

 





    Simulizi :Iangalie Tuleane
    Sehemu Ya Tano (5)




    Taarifa ya uwepo wa watu wanaotembelea kijiji usiku wa manane na kumwaga vipeperushi kwenye vilabu vya pombe iliwafikia Sabaya na Maroda. Hata wale mgambo wafanyao doria. Nao ujumbe uliwafikia. Kilichozungumzwa kiliwafikia na iliwalazimu kutega mtego ili waweze kuwakamata watu hao.

    “Inasemekana kuwa ni mwanaume na mwanamke, ndio wafanyao hivyo vitu,” alisema Maroda akizungumza na Sabaya usiku wa saa nane. Wakati huo walikuwa mafichoni karibu na kilabu kitumiwacho sana na Kitenge . Wakati huo mama muuza wa kilabu hiyo akihitimisha kukusanya chupa, alipomaliza alizima kibatari kilichokuwa kinasaidia kuangaza mahali hapo kisha aliondoka.

    “Huyo mwanamke ni nani tena?” aliuliza Sabaya.

    “Hata sifahamu, ila leo ni mwisho wao,” alisema Maroda, akivuta pande la tofali ili kuketi.



    Haikupita muda mrefu, walisikia sauti za watu wakinong’onezana, umbali mfupi kutokea mahali kilipo kilabu, sauti hizo zilizoambatana na kelele za karatasi, huku sauti ikizidi kusonga mbele kuelekea kilabuni. Walipoifikia, walionekana kusita, migongo wakiwa wameiinamisha, tena wakitembea kwa kunyata wasisikike kama fisi, Sabaya alilazimika kufanya mawasiliano na mtu fulani upande wa pili. Maongezi hayakuwa marefu, alitamka neno moja tu kuwa, “tumewaona” alipojibiwa akakata simu. Alivyoirejesha mfukoni alimpiga mwenziye begani, na kumpatia kauli “haina haja ya kuremba, tufanye kilichotuleta.”Pasi na kawia, waliinama na kutoa silaha walizozihifadhi kwenye begi dogo la mgongoni, bunduki aina ya QBZ, ambayo walikuwa wamezifungua. Haraka, walizifunga, kiwambo kikiwa kimefungwa imara mbele ya mtutu, zilipokamilika walikoki na kupandisha begani, tayari kwa kufanya shambulizi. Kidole cha kupiga kifyatua risasi waliweka sehemu husika, usalama ukiwa wazi kuruhusu mashambulizi. Hesabu waliifanya, wote wapige kwa pamoja“Moja!...mbili...tat...” alihesabu Sabaya, kabla hajamaliza sauti kali ilisikika.

    “Mikono juu...!” ikashitua wote waliosikia.







    Sauti hiyo ilitoka kwa kiongozi wa mgambo aliyeko doria, silaha zao wakiwa wamezikita vyema begani, kidole cha shahada karibu na kifyatua risasi, taratibu wakisonga mbele, kwa wale watu waliowaamrisha kuweka mikono juu. Walitembea hatua kadhaa, baadaye walishuhudia watu waliowapa amri wakibwaga mizigo waliyokamatia mikononi mwao na kutoka mbio. Kabla hawajafika umbali mrefu, risasi walizimimina usawa wa miguu yao, wakaanguka chini.



    Sauti iliyotoka iliwaamrisha watu walioko kilabuni kwa imani kwamba walikuwa ni Kitenge na mke wa marehemu mzee Kumwembe, japo hawakuwa na ufahamu kuwa huyo mwanamke ni nani. Kitendo hicho kilifanya Sabaya na Maroda kuahirisha walichokuwa wanahitaji kufanya. Waliteremsha silaha zao kisha kuangalia sawia kinachoendelea. Moyo wa matumaini uliwajaa; aliyekuwa anawasumbua kapatikana, asilimia zote walimwamini.

    “Mkuu! Mgambo wa doria wamewawahi,” alisema Sabaya akiongea na simu.

    “Kivipi ilhali ninyi ndiyo wa kwanza?”

    “Nahisi walikuja kabla yetu. Hivyo wamewakamata na kuondoka nao. Tena walijaribu kukimbia ila waliwashambulia risasi za mguuni, zilizofanikisha kukatiza mbio zao.”

    “Aaah!... Kwanini hawakuwamaliza kabisa?” ilisikika sauti ya upande wa pili wa simu kwa sauti iliyofura.

    “Ndiyo hivyo mkuu.”

    “Msijali, hakuna kilichoharibika. Tutaenda wamalizia huko kituoni. Ila muna uhakika ndiyo wenyewe?”

    “Ni wenyewe kiongozi, hatuwezi kukuongopea.”



    Walipakizwa ndani ya gari safari ya kuelekea kituoni ilianza. Sababu ya furaha, kufanikisha kuwakamata watu watafutwao na dola kwa muda mrefu, walikosa nia ya kutambua sura zao mahali hapo. Wakashauriana kwenda kufanyia kituoni, kingine kilichochangia ni giza, kwani hata usafiri waliokuwa wanautumia taa zilikuwa hazifanyi kazi. Katika harakati za kuwateremsha, ndipo walibaini, kwamba watu waliowakamata si wahusika, wanaowatafuta.

    “Afande, huyu siye.”

    “Unasemaje?”

    “Huyu si mhusika.”

    “Inawezekana vipi?”

    “Kweli. Waangalie, hawa ni walevi wa mtaani, na asubuhi ya jana, wametolewa mahabusu kwa kosa la uzururaji.”

    “Basi hawa watatusaidia kuwakamata hao, inavyoonekana wanawafahamu.” alisema kiongozi wa mgambo wa doria, huku akihakikisha alichoambiwa kwa kuwatazama kupitia mwanga wa balbu uzalishwao na nguvu ya jua.



    Hakika! Waliokamatwa hawakuwa Kitenge na mke wa marehemu mzee Kumwembe. Walikuwa ni walevi na wazururaji wazuri mtaani hapo, kawaida yao usiku hutembelea vilabu vya pombe ili kuokota zile jumbe zinazomwaga, kisha nao husambaza mtaani. Ni siku moja tu, katika zote walizotembelea kilabuni walifanikiwa kuwaona watu waliokuwa wanaacha hizo jumbe, japo walikuwa wamelewa lakini walishtuka walipowatambua. Hawakujalisha sana, maelezo walivyopatiwa, na ombi la kufanya siri walivyopewa, na kusambaza zaidi jumbe zao ili umma uhabarike. Hilo halikuwa shida, walitekeleza, kwa usiri mkubwa, hadi siku hiyo waliyokamatwa.

    “Usithubutu kuwataja,” waliambizana kimyakimya, pindi wanatenganishwa kuchukuliwa maelezo baada ya hapo walipelekwa Zahanati kupatiwa matibabu.



    Habari kuwa waliokamatwa si wahusika ilifika mezani kwa mzee Tualike, naye kuwataarifu watu wake wa kazi, Sabaya na Maroda. Hawakuremba! Walirejea tena kule maeneo ya klabuni, waliamini wahusika wanaweza kufika. Na kama hawajafika basi walishafika baada ya tukio lililotokea. Hawakukawia kuwasili, lakini hawakufanikiwa kukuta mtu yeyote, zaidi ya vipeperushi, na kuona nyayo zilizoonyesha muda si mrefu kuna watu walipata kuwepo eneo hilo. Walichoamua ni kuviokota vipeperushi kisha kuanza kufuatilia nyayo zilikoelekea, ambazo mwishowe ziliishia kichakani. Kweli kitenge na mke wa marehemu mzee Kumwembe walifika kilabuni hapo, mapema sana, kabla hata vurumai lililotokea. Walifika hapo kipindi mama muuza wa klabu hiyo akihitimisha kukusanya chupa zake na kufunga. Ila walikaa umbali mfupi kutoka pale, hivyo kila kitu kilichokuwa kinaendelea walikishuhudia. Purukushani zilivyomalizika, na walipojihakikishia kuko salama ndipo walijitokeza, wakaacha vipeperushi vyao wakaondoka.

    “Hawa jamaa washashtuka,” alisema Kitenge pindi wakiondoka kuelekea mafichoni kwao.

    “Kwa hiyo tutafanyaje?”

    “Tubadili eneo.”

    “Sasa ni wapi kuna mazingira mazuri zaidi ya hapa?”

    “Tuwe tunabadilisha, leo hapa kesho sehemu nyingine.”

    “Labda hivyo,” waliendelea kupiga soga huku wakichanja mbuga, wakiwa wamejitawala kabisa, pasi na hofu. Kwani hawakusita kuwa sehemu ya mahusiano ya mapenzi, hisia zilivyowapanda zaidi kila mmoja.



    Walichojadiliana ndicho walitenda. Awamu hii ilikuwa zaidi, baada ya kuona unyama waliofanyiwa wale walevi, waliokuwa wanawasaidia kusambaza jumbe zao. Wakati huo wale walevi walishaachiwa, Mgambo walizidisha doria, Sabaya na Maroda nao waliongeza kasi ya utafutaji. Ofisi elekezi nayo mambo yalizidi kupamba moto, hamu ya kuona sheria mpya ya utawala madarakani ikianza tumika, kwa upande wa utawala, huku wapinzani wakimuomba mwenyekiti wa serikali ya kijiji asisaini muswada aliopelekewa. Uraiani nako wananchi waliwaka, morali ya kuandamana ilipamba moto, japo mkuu wa jeshi la mgambo, Jipendekezo alikesha kila siku kupiga katazo. Siku zilikatika, hatimaye ile iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu, Mzee Tualike asaini muswada aliopelekewa iliwadia.



    Makundi mengi yaliundwa asubuhi ya siku hiyo, wakiwa na chombo kiwapatiacho habari, redio. Wengine walikusanyika kwenye vilabu vilivyofunga runinga kutazama mubashara matangazo ya ofisi elekezi, ambayo wenyeviti wa mitaa waliketi sawia kusubiri tamko juu ya muswada walioupendekeza. Wenyeviti wa mtaa upande wa utawala pekee ndiyo walikuwemo, wenyeviti wa upinzani muda huo walishatoka ndani ya ofisi,wakawa wanazurura nje ya jengo kutoa malalamiko yao, hawakuweza kuingia uraiani, walizuiliwa na mgambo waliopo langoni. Kila walivyojaribu kuhimiza wafunguliwe geti waondoke hawakusikilizwa, kiasi kwamba ilifikia hatua ya kutishiwa kufanyiwa shambulizi wakizidi kuwa wakaidi. Kwani amri, ilishatolewa toka majuu kama walivyozoea kusema mgambo wakibananishwa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mnamo saa 3:15 asubuhi ndipo mambo yaliiva zaidi. Vijana wengi wenye vyombo vya usafiri, baiskeli, pikipiki na bajaji walitanda barabarani huku vyombo vyao vikipeperusha jumbe mbalimbali za kushinikiza mzee Tualike na baadhi ya viongozi wake waachie ngazi. Mgambo wa doria nao walikesha kuzunguka mtaa mmoja baada ya mwingine, kuhakikisha watakaojitokeza barabarani kuandamana wanakula nao sahani moja. Matendo hayo yaliambatana na yowe, nyimbo mbalimbali walizoziita za kizalendo katika kufikia hatua waliyoamua. Ilipofika saa tatu na nusu, mmojammoja alijitokeza anakoishi kuelekea eneo la makutano lililopangwa. Wakati huo, muswada uliopelekwa ofisi kuu, ndiyo ulikuwa unarejeshwa ofisi elekezi kufafanuliwa kama tayari ushapitishwa kuwa sheria ama lah! Kitu pekee walichokuwa wanasubiri mamia ya wananchi waliojitokeza kuandamana ni kusikia tamko kuhusu hatma ya muswada huo. Redio walizonazo, ambazo walibeba muda wote kwenda nazo kokote waendako, ndicho walichotegemea kuwaahabarisha, na wachache waliopo kuangalia runinga, ambao wangewataarifu wenzao kwa njia ya simu endapo ile ya radio itakuwa ngumu kusikika.

    “Wanaanza... wanaanza!” walisikika watu wakichanja mbuga kusonga mbele, sikio wakitega kwa ukaribu mkubwa ilipo spika ya radio. Wale waangalio runinga nao walianza kushika vilonga longa vyao kuwataarifu wale walio barabarani.

    “Wiki kadhaa zilizopita, ofisi yetu elekezi, ilijadili muswada pendekezwa kuwa sheria ya ongezeko la muda wa utawala, kutoka miaka minne hadi kutokuwa na ukomo wa kiutawala. Ikiwa na maana, mtu aliyepata wasaa wa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji na mtaa, awe na ruksa ya kugombea mara zote apendazo, mpaka pale mwenyewe kwa ridhaa yake atapoamua kutogombea. Muswada huu, umefikishwa mezani ofisi kuu, kwa mwenyekiti wetu wa serikali ya kijiji, Mzee Tualike, muamuzi wa mwisho wa miswada tunayoijadili. Ifikapo mezani kwake, akiridhia kusaini muswada huu, hugeuka sheria, asiporidhia hutupiliwa mbali. Hivyo basi; muswada uliowasilishwa mezani kwake wiki zilizopita, mwenyekiti wa serikali ya kijiji chetu, ame... !” ilikuwa sauti ya muongozaji wa mijadala ifanyikayo ndani ya jengo hilo, ila kauli yake haikumalizika kusikika kwa wale watu waliokuwa wanamsikiliza kupitia radio na runinga. Mitambo ilikata!

    “Aaaah! Wamekata mitambo, tusisikie.” walipayuka wananchi, hali iliyopelekea kuongeza hamasa ya utekelezaji wao.



    Hawakupoa! Walianza rusha mawe na vitu mbalimbali kuelekea jengo la ofisi kuu, ambalo walishalikaribia. Vitu vilitupwa, vizito kwa vyepesi, milipuko na zana kemkem za kujeruhi, kutokubaliana na kinachoendelea. Mgambo walijibu shambulizi, tena siku hii ulinzi ulikuwa mkali zaidi ya siku zote, sehemu ambazo walibaini waandamanaji watahitaji kuzifikia. Kama vile ofisi kuu, ofisi elekezi, barazani na ofisi za wenyeviti wa mitaa pasi na acha maafisa watendaji wa mitaa na mashina. Mgambo vitengo vyote walijumuika pamoja kulidhibiti hili tukio, wapelelezi, wa gerezani na vitengo vingine pia. Mgambo wa magereza walipungzwa magerezani kwa hiyo siku, kwenda kudumisha ulinzi na kupambana na waandamanaji, hasa kitengo maalumu kifahamikacho sana kwa kutoa adhabu kali mfungwa akoseapo. Maadhibu!

    “Wajinga hawa wanafanya kama kijiji wameanzisha wao. Hatukubali awamu hii, wanakijiji hatujalala, tutapambana hadi tone la mwisho la damu yetu kuhakikisha kijiji chetu kinakuwa na utawala mzuri, ufuatao haki, sheria na kusikiliza maoni pendwa ya wananchi. Kama wameamua kubadili kile kifungu cha katiba, kwanini wasibadili katiba nzima?” walisikika wananchi wakilalamika huku wakizidisha kupiga hatua kusonga mbele, japo baadhi yao walikuwa wanadondoshwa kwa kupigwa risasi za moto. Hawakujali! Waliamua, walithubutu, kwa namna yoyote, mpango ulioratibiwa na serikali hautimii, na kama utatimizwa, wananchi pia wasikilizwe takwa lao la kubadili katiba nzima.



    Wananchi waliteketea, mithili ya ndege aina ya kuku wauguwao kideri hushikwa kwa urahisi. Ndivyo ilivyokuwa kwao, mabomu ya machozi waliyopigwa yaliwapotezea dira, hatimaye wakawa wanakamatwa kirahisi, muda mwingine walifanyiwa hivyo iwe rahisi kushambuliwa kwa risasi. Lakini, usilolijua, sawa na usiku wa kiza. Poteza maboya adui, mpango wako ufanikiwe. Kubali kulipa gharama, uhitajapo mambo mazuri.

    “Afande!...afande! Ni mchezo,” alisema askari mmoja aliyeko kwenye jengo la makao makuu ya mgambo, akiwasiliana na Mkuu wake, Jipendekezo baada ya kuona taarifa fulani runingani. Kwani mitambo ilirejeshwa nusu saa baadaye, wakati huo wananchi hawafahamu kama muswada umepitishwa kuwa sheria au sivyo.

    “Mchezo upi tena?” Aliuliza Jipendekezo.

    “Washa runinga, kuna taarifa inaripotiwa muda huu.”

    “Hapa nilipo naangalia, labda chaneli ipi?”

    “Ya pili ya kijiji,” aliongea mtu huyo kisha simu ikakata. Jipendekezo akafanya alivyoambiwa, alikamata kiungambali akabonyeza kitufe kimoja mara kadhaa, kisha chaneli husika aliyoambiwa aliifikia. Tuli! Alitulia, masikio aliyasimamisha, taarifa ya runingani iliteka yake akili.



    Ufito mwekund ulio na maandishi yaliyosomeka Breaking News ndiyo aliyokutana nayo, na picha ya mwanamke aliye katika mavazi nadhifu, mtangazaji. Akiendeleza kusoma habari.

    “Kiongozi msaidizi wa gereza hilo, anadai kuwa kitendo cha kupunguza askari imewarahisishia wavamizi hao kushambulia askari walioko zamu gerezani hapo, hawakuwa na silaha za msaada za kukabiliana na zile zilizokuwa zinatumiwa na wavamizi.”

    Jipendekezo hakuielewa, ikamlazimu kumpigia simu, mgambo aliyempatia taarifa hiyo, ampe ufafanuzi zaidi nini kilichojiri.

    “Hii taarifa sijaielewa.”

    “Afande! Magereza imevamiwa, kina Bi. Mwema na wenzake wametoroshwa.”

    “Unasema!!”

    “Ukweli ndio huo. Inavyoonekana hawa waanzishaji wa hii kitu, lengo lao ni hiki walichofanya, maandamano ilikuwa ni zuga tu, kutuhadaa ili tuweke nguvu kubwa kwenye maandamano ilhali walikuwa na mipango yao mingine.”





    “Kitenge Malimuka, lazima nibadili jina lako,” alijiapiza Jipendekezo, sura ilibadili muonekano, mistari ya ndita ilianza jidhihirisha kwenye paji la uso wake, mdomo ulifura, mithili ya mtoto mdogo akasirikapo.



    Hamu ya kuendelea kuketi ofisini ilitoweka, aliamua kuondoka kuelekea magereza, kuthibitisha kilichotokea. Kweli! Magereza ilivamiwa, askari kadhaa walinzi walishaaga dunia, wengine walijeruhiwa na sehemu ya milango ambayo wafungwa walihifadhiwa ilivunjwa kwa kutumia mabomu ya kishindo ya asili. Kila aliyepata taarifa hii na kujionea hakuna aliyeamini, imewezekana vipi, lakini kwenye mipango madhubuti, hakuna kinachoshindikana. Hata mzee Tualike alivyopatiwa taarifa hii, ilikuwa ni sawa na kuweka makaa ya moto ndani ya mdomo. Alihangaika wakati huo akifikiria madhara yatakayojitokeza. Hisia mbalimbali kuhusu tukio hilo zilimjaa, sio yeye tu, na viongozi wengine pia, huku njama ikiwa imetawala zaidi ya zingine.

    “Kuna mgambo wametufanyia usaliti, haiwezekani, hawa watu walijuaje kuwa mgambo wengi wameenda kutawanya maandamano?”

    “Ni sahihi, lakini pia, inasadikika kuwa walieneza dhana ya maandamano wakati huo wakiwa na mpango mwingine. Kwa kujua nasi tutatumia nguvu kubwa huko halafu kile walichokusudia wafanikishe kwa urahisi, kama ilivyotokea. Vituo vingi vya ulinzi vimelindwa kwa kutumia rungu, na kama mtu alikuwa na bunduki, aidha ilikuwa tupu ama idadi ndogo ya risasi. Maana kwa ripoti nilizonazo sasa huko mtaani waandamanaji hawaonekani kabisa baada ya taarifa za kuvamiwa magereza zilivyosikika.”

    “Yafaa kuunda timu ya uchunguzi bila kukawia kulichunguza hili. Nina mashaka sana na hawa mgambo wenu waliokuwa zamu. Baadhi yao watakuwa wanafahamu mchezo.”



    Ni maongezi ya baadhi ya vigogo wa serikali ya kijiji walivyokutana kwa dharura, kutafuta ufumbuzi jinsi tukio lilivyotokea. Kama walivyoafikiana, timu ya wapelelezi sita toka vitengo tofauti vya ulinzi na usalama iliundwa, ikiongozwa na mmoja wa viongozi wa juu wa siri wamlindao na watoa ushauri kwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji.



    Guardner! Uchunguzi wao ulianza jioni ya siku hiyo, ambayo walitumia muda mrefu kuyasoma mazingira, mgambo walivyopigwa na vingine vingi vyenye kuwawezesha kufahamu wavamizi waliingiaje na waliweza vipi kufanikisha mashambulizi yao. Siku iliyofuata waliwafuata majeruhi, kuwahoji. Huku imani ikiwaaminisha hao ndio wauza dili, ndiyo maana wameokoka, japo haikuwa hivyo. Walihojiwa kwa siku nne mfululizo, ila afya zao hazikuwa zimetengemaa, zilizidi kuwa mbaya kadri siku zilivyozidi songa mbele, siku ya tano wote waliaga dunia. Timu ya upelelezi ikiwa bado haijakamilisha data kamili toka kwao, lakini hawakujali, walizifuata data za awali walizopewa, mwishowe walimfahamu mmoja wa mgambo waliouza dili kwa wavamizi. Miongoni mwa wale majeruhi walipoteza maisha siku za baadaye. Baada ya kufuatilia mawasiliano yao.



    Kitenge Malimuka, mgambo mstaafu ndiye alikuwa nyuma ya yote, akisaidiana kwa karibu na mke wa marehemu mzee Kumwembe. Mipango ya kumwaga vipeperushi na kuwahitaji wanakijiji siku muswada wa uongezaji muda wa madaraka utakavyosainiwa wafanye maandamano ilikuwa danganyatoto. Sababu kwa wakati huo, alikuwa na machungu sana na serikali yake, kwa kitendo cha kutomjali mara baada ya kupatwa na matatizo ya kuondokewa na familia, alidhamiria kwa namna yoyote kuionyesha serikali yeye ni mtu wa namna gani. Jambo la kwanza walilolipanga ni kuandaa maandamano, nyuma yake wakiwa na mpango wa kuwakomboa wanaharakati waliofungwa kimakosa, hivyo wakawa wanakesha kufanya mawasiliano na mmoja wa marafiki wa Kitenge waliopo magereza sanjari na mzee mmoja kikongwe, ambaye miaka ya nyuma alihukumiwa kifungo cha maisha, baadaye alisamehewa kwa hisani ya mwenyekiti wa serikali ya kijiji kulingana na mamlaka aliyopewa kwenye katiba ya kijiji.



    Wanakijiji wachache walifahamu ukweli wa kinachoenda kutokea. Baada ya kusambaziwa taarifa na wale walevi. Ombi la kujitolea kwa ajili ya kupata maisha mazuri toka kwa serikali yenye kufuata kanuni na taratibu za kijiji kwa siku za baadaye likaafikiwa. Wananchi wengi walikuwa radhi kuyaondoa maisha yao ili kampeni waliyoanza nayo inafika mbali. Siku ya tukio ilivyowadia, mambo yalivyopangwa ndivyo yalivyohitajika kufanywa. Na yalitekelezwa. Kwa ustadi mkubwa pasipo na upande wa dola kufahamu kama watu hao wametumika kuficha jambo fulani. Pindi waandamanaji wanatekeleza ipasavyo jukumu lao, ndipo wakati Kitenge na mke wa marehemu mzee Kumwembe, mwanamama aliyepata kupitia mafunzo ya mgambo kwa mujibu wa sheria, wanafanikiwa kuingia ndani ya uzio wa eneo la magereza. Bunduki za kimapigano ya karibu, na bomu zilizotengenezwa na wao wenyewe kwa kutumia vitu vya kiasili ndizo silaha walizonazo, walizopanga kutumia kuhakikisha tukio lao linakamilika kwa muda uliokusudiwa.



    Hawakubahatisha! Walichofanya kilipangwa. Ramani ya kuingia ndani ya eneo hilo walikuwanayo hasa kwa msaada wa uchoraji walioupata toka kwa rafiki yake Kitenge, na yule mzee aliyetoka gerezani kwa msaada wa mwenyekiti akiwa anatumikia kifungo cha maisha.



    Baada ya mwendo wa takribani robo saa, waliufikia uzio mkubwa, uliojengwa kwa mawe. Ukuta wa gereza. Wakati huo majengo ya makazi na ofisi waliiyaacha umbali fulani, walipita upande mwingine tofauti. Sehemu fulani ya ukuta huo ulikuwa umebomoka na kujengwa kwa mabati, ndipo wao walipotokea. Haraka sana, walitumia bomu moja lenye mlipuko kidogo ili kubomoa sehemu ndogo iliyowawezesha kuingia. Kishindo kilichotoka kwenye mlipuko walioufanya hakikusikika kwa walinzi, waliokuwa wanaranda randa, wakati huo wakiwa wamevalia mavazi ya kininja, yaliyozuia sehemu ya uso na kuacha macho na pua kuonekana. Hadi wanafanikiwa kuingia, hawakuonekana, lakini mbele yao waliwaona askari wawili walio na bunduki aina ya gobole, wakipiga stori, huku wakiwa na machale ya kuangaza angaza huku na kule.

    “Haina kupoteza muda. Tufanye hawa watu tuondoke nao,” alisema Kitenge.

    “Hamna shida, hapa ni mwendo wa kazi,” mke wa marehemu Mzee Kumwembe naye alichangia hoja.



    Kweli! Kazi ilianza. Mmoja akitumia bunduki waliyoibeba na mwingine mabomu na mishale ya sumu, aliyoirusha kwa kupuliza toka kwenye kikopo kidogo vifananavyo na vikopo viwekwavyo grisi. Ilikuwa kimyakimya, kwani bunduki waliyokuwa wanatumia ilikuwa imefungwa kiwambo, kilichozuia sauti kutosikika. Mshituko! Uliwakumba, mgambo walioko ulinzi, namna mmoja baada ya mwingine walivyodondoka chini na kupoteza maisha, wakiangalia wapi watu wafanyao hicho kitu walipo hawakufanikiwa kuwaona. Kwani, kichaka cha maua kiliwaficha.

    “Risasi!”

    “Risasi?”

    “Ndiyo. Na hivi vimishale vidogo ndivyo vinavyowafanya wapoteze maisha.”

    “Inawezekana vipi? Nani anayefanya hivi?” walijadili mgambo wawili waliosalia, baada ya wenzao kupoteza maisha. Waliangaza huku na kule, macho hayakung’amua watendaji. Hiyo iliwasababishia mshangao zaidi, kisha kuchangamsha akili zao, namna gani watajikwamua, wapate msaada.



    King’ora lilikuwa kimbilio lao la kwanza. Walipiga, lakini kabla hakijachanganya wakawahiwa. Risasi zilizoelekezwa mfululizo kwao ziliwafikia. Ziliwapa nafasi Kitenge na mwenziye ili wazidi kusonga mbele, nao ndio walikuwa mgambo wa mwisho, baada ya hapo walikutana na vyumba vya wafungwa huku mmoja wao akiwa mhifadhi funguo wa vyumba. Haraka! Walizichukua. Na sababu walishafahamu ramani, haikuwasumbua, moja kwa moja walipiga hatua hadi vyumba ambavyo Bi. Mwema na wenziye waliwekwa.

    “Tupo kwa ajili ya msaada wenu,” alisema Kitenge baada ya kuwafikia, huku wakifunua sehemu ndogo ya uso wao kujitambulisha ni kina nani.



    Dakika tisa zilitosha kuhitimisha mpango wao, wakaondoka kupitia sehemu waliyotumia awali. Mwendo mdundo! Miguu waliikaza, walipochoka hawakusita kupumzika, baadaye safari iliendelea kama kawaida kuitafuta sehemu waliyoikusudia. Sababu ulikuwa ni mchezo, walivyokamilisha waliwajuza wananchi wasitishe maandamano yao, na ndicho kilichotendeka. Ghafla tu wananchi walitoweka, barabara zote zikawa tupu, mtu haonekani zaidi ya mgambo wenyewe. Walivyokuja kushtuka, tayari walikwishachelewa, kwani walishaufikia msitu watumiao kujistiri mahali pa makazi yao. Bi. Mwema na wenziye hawakuamini, ilibidi waaminishwe na kutolewa hofu kuwa wako mahali salama hata kama wataishi kwa kutanga tanga.

    “Hakuna lengo la kutumaliza? Kwa kuhofia tutatoa hamasa kupitia watu watembeleao magereza kutuona?” Aliuliza Awetu, maana iliwajaa hofu walipomuona Kitenge, waliyemtambua kuwa ni mgambo anayeaminiwa na jeshi la mgambo kwa kutoa adhabu kali.

    “Ondoeni shaka, mimi ni mwenzenu kwa sasa,” Kitenge aliwaaminisha. Tena kwa kuwahadithia ukweli uliomsibu.

    “Serikali yetu inamheshimu mtumishi wake, pindi ikiwa na shida, ila ni vigumu kumjali mtumishi wake akiwa matatizoni,” alimalizia kwa kusema hivyo.



    Maisha yao yalianza upya, mithili ya nyani wenye kawaida ya kuvamia mashamba ya watu hasa yaliyopandwa mahindi. Wanajitokeza kwa muda fulani, baada ya hapo walitumia muda mwingi mafichoni. Kila uchao wakawa na kawaida ya kurekodi video zenye jumbe mbalimbali, kisha kuzituma uraiani, kuwahamasisha wananchi nini kifanyike wauondoe utawala dhalimu, utoao vyeo kwa upendeleo, kwa kutanguliza ukada. Na sio taaluma.

    “Ushawishi huu tunaoutoa, yatupaswa sisi kuwa mstari wa mbele, na sio kuwahimiza wale wafanye halafu sisi tupo tu.”

    “Kwa hiyo unashaurije?”

    “Haina ulazima wa kuendelea kuwa mafichoni, tujitokeze kuanzia siku ya kesho hata kama huko mitaani tunatafutwa kiasi gani, wananchi watatulinda.”

    “Yeah! Ni sahihi.”

    “Basi iwe sahihi ya vitendo.”



    Kesho yake asubuhi na mapema walianza jitokeza mitaani. Waligawanyika, walikuwa wanatembea kwa makundi ili wasiweze kukamatwa wote kwa pamoja. Kuonekana kwao, iliongeza nguvu ya ushawishi kwa wananchi watekeleze walichowaambia. Awali kuomba kura ya maoni ya kutokuwa na imani na kiongozi aliyoko madarakani, pili kufungua shitaka barazani kupinga ushindi na utendaji wa mambo mbalimbali yatendwayo na serikali. Sehemu za ulabu, na nyinginezo zenye mkusanyiko wa watu wengi, ndizo walipenda kutembelea. Hawakujali kutafutwa kwao, waliangalia uhitaji wao, wa kuwafanya wananchi wa Tuleane wanaishi kwa amani toka kwenye manyanyaso ya serikali, kwa kuishi na amani. Shangwe walizokuwa wanapatiwa ziliwaongezea morali na ushawishi zaidi wa kuwashawishi wananchi wengi watoe kilio chao cha uhitaji wa kura ya maoni ya kutoridhishwa na utawala wa Mzee Tualike.



    Shangwe wazipatazo ziliwafikia watafuta, kwamba watafutwa wapo mitaani wanakesha kufanya mikutano ya ushawishi. Hawakuvumilia! Kama ilivyo ada, pande mbili ziliingia kazini, ile inayoongozwa na Sabaya akishirikiana na Maroda pamoja na ile ya kituo kikuu, mgambo maalumu wa doria.

    “Hakikisheni mnawamaliza hata kama wataingia chini ya mgambo wa doria,” alisema mzee Tualike, pindi akiongea na kina Sabaya.



    Baada ya maongezi kufikia tamati, waliagana. Kisha kufunga safari hadi mtaa walioelezwa kuwa Bi. Mwema yuko anahubiri akiambatana na wenziye. Barabarani walipishana na gari iliyobeba mgambo wa doria, nayo ikiwa kasi kuelekea huko, kuwakamata watafutwa wao waliotoroshwa magereza sambamba na watu waliowapatia msaada. Hawakuisha kuweka nadhiri, nini cha kufanya kutokana na usumbufu walioupata kuhusu watu hao. Dhahiri! Walionekana kukerwa na matendo yao, ila hawakuzipa fursa kufikiria upande wa pili manufaa ya watu kama hao, ambao leo hii wamekuwa maadui wakubwa kisa tu kukinzana na matakwa ya utawala, pale waonapo watendaji wake hawako sawa.

    “Watu kama hawa wakikamatwa ni kumaliza kabisa, na sio kuwaacha, si unaona namna wanavyotusumbua?” alisema mgambo, wale wa doria huku gari ikizidi kasi kuutafuta mtaa husika.

    “Wanachukiwa bure tu, ila wana umuhimu mkubwa sana. Kwani si unakumbuka miaka kadhaa ya nyuma, watu wa aina hii ndio walipiga kelele wajengewe nyumba wale watu waliobomolewa makazi kwa sababu ya kumpisha mwekezaji, mtaani ulikozaliwa? Tena hata wazazi wako walikumbwa na adha hii,” Mgambo mwingine alichangia hoja.

    “Eeeh! Ni kweli kaka. Na nahisi serikali haikuwa na mpango kabisa wa kufanya kile kilichofanyika.”

    “Haupaswi kuhisi, amini hivyo. Mpango wao ulikuwa kutolipa, ndiyo maana vyombo vya dola viliwasumbua sana watu waliokuwa wanapiga kelele kuhusu ile kitu.”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pindi mgambo wa doria wanahisi hivyo, Sabaya na Maroda nao walikuwa na hisia zao. Tena stori zilianza toka mwanzo wa safari hadi wanawasili. Neno kubwa lililozungumzwa katika maongezi ni kuuondoa uhai tu, wa watu wanaowafuata, ambao waliwapachika jina la waasi. Mwendo wa dakika kumi na saba, ziliwafikisha, Taarifa walizopatiwa zilikuwa sahihi. Halaiki ya watu waliyoikuta haikuwa ya kawaida, utadhani kulikuwa na kiongozi mkubwa kutoka ngazi ya taifa la nje ambaye katembelea kijiji chao. Mbele ya halaiki hiyo walisimama Bi. Mwema, Awetu, Dkt. Emmakulata, Kitenge na mke wa marehemu Mzee Kumwembe, mmoja wao akiwa amekamata kipaza sauti akihutubia. Walitafuta eneo, wakachukua maficho, zana zao wakaziteremsha haraka. Ufungwaji ukaanza. Lilikuwa zoezi la muda mfupi sana, walichukua dakika mbili tu, kumaliza. Baada ya hapo, kila mmoja hima kona yake alisimama. Mitambo ilikokiwa, pumzi ilibanwa, tayari kwa upigaji.



    Lahaula! Mgambo wa doria wakaharibu. Hamaniko halikujificha katika wajihi wa watu waliokusanyika, lakini hofu, waliiondoa kwa ushujaa.







    _______________



    Hapakuwa na utulivu kabisa siku hiyo.

    “Baba! Baba!” Jipendekezo aliita. Wanguwangu aliiingia ofisini kwa baba yake, ofisi kuu. Jasho jembamba lilimtiririka na kufanya kofia, fimbo na mkanda uvaliwao tumboni kushikwa mkononi. Hadi watu waliokuwa wanamshuhudia walishangaa. Kiongozi mkubwa kuwa hivyo, tena hata ulinzi hakuwa nao, ilikuwa taharuki na jambo la kustaajabisha.



    Alihema kwa nguvu—nje kisha ndani huku koo likikauka utadhani kapuliziwa vumbi la pilipili, mdomo wazi. Macho yalikuwa wazi, nje kama taa za gari moshi gizani.

    “Kulikoni?” alihoji baba yake. Naye alibabaika kwani hakuwahi kuiona sura ya mwanaye ikiwa imejaa hofu kama ya mtu aliyepata taarifa za kuwa roho yake inahitajika kumponya maiti kaburini.

    “Mzee, hali sio shwari. Huko mtaani mambo yamechafuka, ofisi za watu wetu zimevamiwa na zinateketezwa vibaya mno.”

    “Askari hawajaenda kuwazuia?”

    “Wapo, ila nguvu inaonekana kuwa ni ndogo juu ya zana zote walizobeba kuzitumia.”

    “Inawezekanaje? Watu wana mabomu na kila aina ya silaha halafu washindwe?”

    “Nguvu ya umma! Haiwezi kushindana na kitu chochote baba yangu. Hatuna namna, zaidi ya wewe kukuondoa hapa kukupeleka kijiji kingine ukapate hifadhi.”

    “Mwanangu, umeshindwa kunilinda? Hadi unadiriki kuhitaji mzee wako niondoke ndani ya kijiji changu? Wana nini hao wananchi kinachowafanya mushindwe?”

    “Tunawezaje kushambulia wananchi wote? Isitoshe tambua kuna sheria za umoja wa vijiji zinazohusiana na haki za binadamu, ambazo zinawapatia ulinzi. Sasa unaweza vipi kuwatokomeza? Kwa jambo ambalo lipo kisheria ndani ya katiba ya kijiji chetu? Baba! Hiyo njia niliyokushauri ndiyo ifaayo. Nenda. Tukishaweka mambo sawa tutakurejesha.”

    Hadi kuafikiana, muda mrefu walitumia, tena baada ya walinzi wa siri na washauri wa karibu kuingilia kati.

    “Kiongozi, huko nje hali ni mbaya. Wananchi wamechafukwa kiasi kwamba ni moshi tu ndiyo umetawala. Kijiji kizima, na wanashauriana kudhuru ofisini kwako. Hivyo hakuna mbadala, zaidi ya ulioambiwa.”

    “Sasa nitaelekea kijiji gani? Wakati tushagombana?”

    “Tuwaombe tu hawa ambao tuliwaahidi kufanya nao mazungumzo ya muungano wetu.”

    “Eeeeeh! Tufanye hivyo.”



    Sauti za wananchi wenye hasira zinasikika katika wimbo. Zinalichana anga na kuambaa hadi kuwafikia ofisini walipo.

    “Sikia! Nyimbo hizo, sijui hata walikojifunzia kuziimba kwa maana kila mmoja anasikika akiimba kwa ufundi tena kwa sauti.”

    “Mwanangu, wimbo wowote wa harakati za haki haufundishwi bali huja ghafla na watu husonga nao. Ujue itokepo vurumai ndipo akili ya watu kufanya kazi maradufu.”



    Chinja!

    Mchakamchaka

    Chinja!

    Akija mkora!

    Chinja!

    Mkoloni mzawa, kiwavi jeshi tuungane!

    Mkoloni mzawa, akija juu tuungane!

    Mkoloni uchwara, akija kulia tuungane!

    Mkoloni mzawa, akija na bunduki tufumbe macho!

    Chinja. Mchakamchaka—chinja!



    Wimbo unawastaajabisha. Vumbi linatimka na wanatafakari kule watu wale walipata ujasiri wa kufanya hayo mazito bila hata siku ya kuwaona wakifanya mazoezi makali ya viungo.

    “Tuombe hifadhi—kijiji cha pili.”



    Mawasiliano yalichukua nafasi. Upande husika, kijiji cha pili kilichoko kisiwani waliomba hifadhi ya mzee Tualike, huku majadiliano ya amani yakitajwa kuanzishwa. Ombi lao lilijibiwa nusu saa baadaye na jibu walilopatiwa ni kukubaliwa kwa ombi. Walijisikia faraja kisha haraka sana utaratibu wa kumsafirisha mzee ulianza. Walienda kwa njia ya maji, kutumia boti ya serikali. Kasi walifanya, watu wanaosadikika kuja kudhuru ofisi wasiwakute.



    Safari ya utoro, kuikimbia himaya yao iliandaliwa baada ya mazungumzo. Walipofika ndani ya boti ndipo walizungumza kwa dakika kadhaa, takribani nne. Baada ya hapo, mzee Tualike aliruhusu boti kuanza safari.



    Mtaani amani ilitoweka. Zuio la wananchi kwa mgambo kuwakamata Bi. Mwema na wenziye liliamsha hisia kali, vurugu za kutosha, kwani mgambo walitaka kujihakikishia ushindi mbele ya halaiki hiyo, iliyochoshwa na tabia zinazoendelea zifanywazo na serikali.



    Raia walijihakikishia kwa namna yoyote wanawazuia mgambo kufanya ukamataji wanaohitaji kuufanya. Vitendo hivyo viliambatana na yowe hadi ilifikia hatua yakaanza mapigano. Mgambo walikosea awali kujichanganya katikati ya halaiki. Iliwawia ugumu kujitetea kutoka kwenye kichapo walichokuwa wanapatiwa.



    Tafrani! Mgambo walizidi kuongezeka, lakini hakuna badiliko lililotokea zaidi ya wao kupatwa na dalili zote za kushindwa. Japo hao waliojitokeza kusaidia walitumia kila aina ya silaha waliyonayo kuwakomboa wenzao na majengo ya serikali ambayo baadaye yalianza kuchomwa moto, wananchi waliamua kuwazuia lakini walishindwa kwani hofu na uoga, uliokithiri ndani ya mioyo yao kipindi cha nyuma ilipeperuka. Sasa walijidhatiti, nguvu yao kuionesha, kile wanachohitaji wafanikishe. Utawala wa Mzee Tualike kuuondoa.

    “Tumelalamika kwa muda mrefu sana, mkashindwa kutuelewa. Mkatanguliza maslahi yenu mbele, yetu nyuma, sasa wacha tuwaoneshe nani mwenye maamuzi ya nguvu. Tumieni kila aina ya silaha, sisi tutatumia uthubutu wetu tuliouonesha kupambana nanyi.” walisikika wananchi huku wakirusha chupa zilizo na vitambaa vilivyowashwa moto zikiwa na mafuta ya petroli ndani yake. Pasi na acha mawe, uchomaji wa gurudumu barabarani, na uvamiaji wa ofisi, makazi ya watumishi wa serikali kisha kuchoma moto.



    Hakika! Amani ilitoweka, vita baina ya wenyewe kwa wenyewe ilijidhihirisha, kwani mashambulizi yaliyokuwa yanatendeka ndiyo yalileta picha hiyo. Wananchi walipiga tukio na kusonga mbele, kuifuata ofisi kuu ilipo, huku midomo yao haikukauka kuzungumza muda wote, kutoa lawama kwa serikali sanjari na kuimba nyimbo walizozipachika jina la kizalendo. Japo baadhi yao walishaaga dunia kutokana na tukio hilo, ila wao hawakujalisha, walichohitaji ni ukombozi, na waliamini gharama ya ukombozi ni hicho kinachoendelea.

    “Pumzika kwa amani ndugu, tuna hakika wanaokuja watajivunia maisha mazuri kwa gharama uliyoitoa kwa ajili yao,” walisema wananchi kila walipokutana na mwili wa mtu aliyeaga dunia.



    Walitoa kauli kisha kusonga mbele, hadi wanaifikia ofisi kuu, wakaizingira. Wakati huo mgambo nao walikuwepo eneo hilo kuhakikisha ulinzi. Miili yao ilitawaliwa na hasira kali na uchovu uliotokana na kazi nzito waliyofanya ambayo haikuwafanya kuwa washindi mpaka waliamua kurudi nyuma kupanga upya safu zao.



    Jipendekezo alikuwa katikati ya kundi la mgambo hao, waliopangwa kitaalamu kabisa kwa taratibu za kijeshi, akitoa oda mbalimbali, namna ya kuwakabili wananchi walioko mbele yao. Akisaidizana na makamanda wa mitaa, wakuu wa vituo na maafisa wa idara zingine za kijeshi.

    “Mtoeni huyo aamuru kufanyika kwa uchaguzi wa kura ya maoni ya kutokuwa na imani naye. Ikiwezekana aachie ngazi kabisa. Hawa wanaharakati wetu pia wafutiwe mashtaka yao yote yaliyokuwa yanawakabili. Na endapo mtatoa maamuzi ya jambo moja tutalianzisha upya, tunahitaji yote yatekelezwe mara moja,” waliropoka wananchi.

    “Tunawapa muda wa robo saa, msipotekeleza tunalianzisha upya,” waliendelea kusikika.

    Muda walioupanga walianza uhesabu, dakika moja baada ya nyingine, wakati huo upande ulioombwa wakitafakari namna ya kulitatua. Utatuaji wake uliwafanya wakutane viongozi waandamizi wa jeshi la mgambo, wakiongozwa na Jipendekezo pamoja na maafisa waandamizi wa ofisi kuu wakiongozwa na Katibu Mkuu. Bila kusahau viongozi wa ofisi elekezi na wale watu mashuhuri walioko pamoja na mzee Tualike Waratibu wake wa karibu katika harakati za kisiasa walisimama imara.

    “Baba mambo yamezidi kuwa mabaya. Tuleane sasa haitamaniki. Watu wengi wamepoteza maisha. Makazi na ofisi nyingi zimechomwa. Hapa niongeavyo mamia ya wananchi wako nje ya ofisi kuu wakikuhitaji utangeze ridhaa ya upigaji kura ya maoni ya kutokuwa na imani juu yako. Hivyo tupe kauli unaamua nini kuhusu hili?”

    “Ina maana mmeshindwa kuwadhibiti? Fanyeni muwezavyo msishindwe na hao, makanjanja wasio na uelekeo.”

    “Baba! Tutauwa watu wote? Nani utawaongoza?”

    “Wataobaki si watazaliana?”

    “Mzee, acha kuongea pumba, toa kauli.”

    “Subiri nifikirie.”

    “Hakuna cha kufikiria, muda ushakaribia kumalizika. Nini unaamua?”

    “Subiri kwanza, subiri,” alisema mzee Tualike.



    Kitendo cha kukatiwa simu bila muafaka kiliwastajabisha na kuwaacha njia panda.



    Sekunde zilihesabika, jibu lilikosekana. Morali ya wananchi nje nako ilizidi ongezeka.

    “Hakuna jinsi, tuwaache wananchi na maamuzi yao,” alisema Katibu Mkuu. Kauli ilikubaliwa na baadhi ya viongozi waliopo, wengine walipingana naye. Ila mwishowe waliafiki, tena baada ya msukumo wa kitufe kilichorushwa na kuvunja sehemu ya dirisha lililotengenezwa kwa kioo. Shambulio hilo liliambatana na mengine pia, takribani matatu, ndipo wachache wao walijitokeza nje.



    Kimya kilipita ili kuipa nafasi sauti iliyotaraji kutamka maazimio kusikika. Kipaza sauti kilijaribiwa, ngurumo ilitamalaki kabisa, mioyo ilijaa shauku.

    “Kwa namna moja, viongozi wakuu wa serikali, wamefanyia kazi maombi yenu. Yametafakariwa na kujadiliwa, kisha maamuzi kuyapatia. Mwenyekiti wa serikali yetu ya kijiji, mzee Tualike Misifa ameridhia maombi yenu, na ashapanga wiki moja kuanzia sasa kura ya maoni itafanyika. Bi. Mwema na wenzake, waliokuwa wanakabiliwa na vifungo na mashtaka mbalimbali nao wamefutiwa mashitaka.”



    Ghafla! Wananchi walilipuka kwa shangwe. Yalifuata maelezo mengine: kuvunjwa kwa bodi ya uchaguzi, ianzishwe upya kwa kuteua viongozi wengine tofauti na waliopo. Sasa walijiona wathaminiwa, baada ya kulazimisha kwa nguvu kuipata thamani yao iliyokuwa inachezewa.



    Kwa hamu waliisubiri wiki pangwa iwadi, maamuzi sahihi wayaoneshe, kama bado wanaupenda utawala wa mzee Tualike ama lah! Wakati huo ndipo kila mmoja alitoa wazo lake, kwamba, waukatae utawala wa mzee Tualike, apatiwe mtu mwingine, Bi. Mwema.



    Pindi wanaendelea kusubiri siku ya kura ya maoni iwadie, Bi. Mwema akisaidizana na wenzake walikuwa huru mtaani, wakiendelea na jitihada zao za kuifanya jamii iwe erevu katika nyanja mbalimbali. Hawakuacha mikakati endelevu ya kiukombozi, tena walivyopata taarifa kuwa wananchi wanamhitaji awe mwenyekiti wao, aliongeza mikakati na kuweka ukaribu wa kutosha na wananchi.

    ______________



    Wawindaji na wavuvi waliokuwa ufukweni walitaharuki.

    “Nini hicho? Yaonekana kuna jambo linatokea,” alisema mvuvi mmoja. “Itakuwa wanamtorosha mzee Tualike hawa.”

    “Eeeh! Kweli, kweli. Nasikia watu washaandamana huko wanataka kauli ya kuitisha kura ya maoni ya kutokuwa na imani naye. Mambo yamemkalia kooni, sasa kwanini akimbie wakati yeye ni bingwa wa mapambano ya kuteka vijana wa watu?”

    “Watu wa chini ndio huwasaidia watu kama hawa, ila wenyewe hawanaga habari nao zaidi ya dharau.”

    “Kwa sababu katufanyia mambo mengi ya ovyo, sasa ni wakati wa kumuonesha ni namna gani tulivyokuwa na uwezo mkubwa zaidi yake.”

    “Unataka tufanye nini?”

    “Washitue wale jamaa, wazuie safari yake tumteke.”

    “Umenena, tufanye hivyo haraka.”



    Yalikuwa maongezi ya wavuvi na wawindaji walioketi juu ya majabali yaliyoko pembezoni mwa mto, wakibadilishana mawazo baada ya kazi. Walichojadiliana walikitekeleza kwa maana taarifa iliwafikia wenzao, kwa njia ya simu punde walivyowapigia kisha hima walijipanga.



    Safari ilivyoanza waliwataarifu, nao kinyumenyume walifuatia kwa kutumia boti na mitumbwi watumiayo kuvulia. Silaha walizokuwa nazo kwa wavuvi ni mapanga na visu, pinde, mishale na mikuki kwa wawindaji. Imani iliwatawala kwa silaha hizo kuwa watamteka mwenyekiti wa serikali ya kijiji chao.





    .



    Safari ya mzee Tualike ilikuwa na jumla ya watu watatu tu ndani ya boti. Dereva, mzee Tualike na mlinzi wake. Kati ya hao, ni mlinzi pekee alikuwa na silaha, bastola. Ikiwa na kisanduku kimoja pekee cha kuhifadhi risasi. Risasi kumi. Walinzi wengine walisalia kutokana na masharti waliyopatiwa na uongozi wa kijiji walichoomba kuwa mgeni huyo hatakiwi kwenda na walinzi wengi, mmoja tu anatosha, kama atahitaji walinzi wengi, watatumika wale wa kijiji husika.



    Walivyofika umbali wa kilomita kadhaa, toka ofisi kuu, walishuhudia jambo fulani, boti na mitumbwi mingi ilionekana kufunga sehemu ya wao kupita. Hawakujali sana, waliamini wakishazikaribia zitawaachia nafasi ya wao kupita. Baada ya kudhania kuwa ni wavuvi tu, wamefanya hivyo aidha kutoa msaada kwa boti nyingine iliyopata hitilafu, hawakuhisi kama wao ndio wasubiriwa. Hadi wanazikaribia, hazikuonekana kupisha na kuwalazimu kutumia king’ora kuomba njia, lakini hali haikubadilika.



    Hatimaye alipunguza mwendo, hapo ndipo mzee Tualike alipata simu kutoka ofisi kuu ya kuombwa atoe tamko kuhusu maamuzi wanayoyahitaji wananchi. Kabla hajamaliza, boti iliyo na wavuvi itokayo nyuma yao iliwafikia kisha wavuvi kuwavamia. Kuingia tu kwa wavuvi hao, mzee Tualike akakata simu. Hata wale waliokuwa wamefunga sehemu ya kupita nao walijisogeza hadi usawa ule, wakaanza kushirikiana walichopaswa kufanya.



    Mlinzi wa mzee Tualike hakupata nafasi yoyote ya kutumia bastola, alipokonywa. Hakuwa akijua kama wavuvi na wawindaji hao walikuwa na wazo potofu namna ile, hivyo alisita kutumia risasi akidhani walikuwa hawana hatia yoyote. Silaha za jadi ziliwatazama kwa yeyote atayethubutu kufanya jambo lolote pasipo tamko lao. Baadaye waliwafunga vitambaa usoni, kamba mikononi na miguuni na kuwahamishia kwenye boti zao, ile yao wakaisukumizia porini. Wakaondoka.



    Safari iliishia kwenye kambi yao. Kambi ndogo iliyoko umbali mdogo toka usawa wa mto. Vivyo hivyo walivyo, waliteremshwa kisha walianza tembea kwa miguu kuelekea katikati ya mapori, ambako nako kulikuwa na kambi nyingine, kambi kuu.



    Hawakukawia kuwasili, wote watatu walienda kufungwa kwenye miti, wakining’inia kama wezi. Kuanzia muda huo hapo ndipo yakawa makazi yao. Ndoto ya kuingia kijiji jirani ilifutika. Fikra za kuondoka duniani zilitawala akilini mwao. Hawakuamini kama wanaweza kupata msaada.



    Wakati huo mtaani mambo yalizidi kupamba moto, hamu ya kupiga kura ilichukua sehemu kubwa ya akili zao kufikiria. Wakati huo wote bado waliamini kuwa, mwenyekiti wao, mzee Tualike yupo ndani ya kijiji chao, ila taarifa zilizokuwa zinaendelea kuzagaa ziliwashitua na kuwapa hamaniko kubwa lililokosa majibu. Waliposikia kuwa mzee Tualike alishakimbia kijiji siku nyingi zilizopita, walistaajabu.

    “Nasemaje, kwa namna yoyote, hapa tukishamchagua kiongozi mwingine huyu ashitakiwe. Maana katufanyia mengi maovu.”

    “Atashitakiwa vipi wakati katiba ya kijiji chetu hairuhusu?”

    “Kama vifungu vingine vinabadilishwa kwa nini hicho kishindikane? Tutalazimisha tu .”

    Majadiliano ya wananchi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Upande wa serikali ushwari ulipotea mara tu taarifa za kutowasili kiongozi mkuu wa kijiji chao sehemu aliyotakiwa zilipowafikia. Vikao vya dharura havikukosekana, baadaye timu ya wapelelezi wa mgambo, walinzi wa siri na mgambo kadhaa waliingia kwenye majukumu mazito ya kumtafuta. Baadhi yao walisafiri hadi kisiwani, kuhakikisha kama kweli hajawasili ama taarifa walizopatiwa ni za uongo. Uchunguzi ulianza, kwa haraka sana, ili kabla ya uchaguzi wa kura ya maoni apatikane, aweze kutoa kauli yake juu ya mchakato huo. Walizunguka, walikata mapori, na kuufuatilia mto unakopandisha na kule maji yateremkapo. Masaa, siku zilikatika, ilipofika ya tatu toka msako uanze ndipo walifanikiwa kuiona boti iliyotumika kumsafirishia Mzee Tualike, ikiwa imepinduliwa, ishara kuwa boti hiyo ilipinduka pindi wakiendelea na safari. Changa la macho!



    Walishangaa! Hawakuruhusu mshangao uliowapata uharibu kazi yao. Walichofanya ni kutoa taarifa, baada ya hapo walifanya uchunguzi kuhakikisha kama boti hiyo ilipinduka kutokana na mwendo uliokuwa wanaenda nao, au kuna jambo lingine lililo nyuma ya ajali. Pia timu ya mgambo wanamaji nayo iliwasili punde taarifa ilivyowafikia, mtoni wakazama, miili kuitafuta.



    Mbizi za kutosha zilipigwa, kwa wale waliozamia mtoni, lakini hawakupata mafanikio yoyote zaidi ya kukutana na jabali, samaki na wadudu wengine waishio ndani ya maji. Pasipo na kusahau lundo la nguo zilizochanikachanika na viatu pea mbili.



    Masaa mawili baadaye ndipo nje walitoka, wakiwa na hizo nguo na viatu. Wale wa nje nao wakiwa na viashiria fulani vyenye kuthibitisha kitu gani kimetokea. Walivijumuisha pamoja, kisha kuvifanyia tathmini kimoja baada ya kingine. Walivyohitimisha, walipata jibu moja kuwa kipi kilichojiri. Tathmini waliyoifanya iliwabainishia kuwa nguo na viatu walivyovikuta majini sio ambazo zilitumika na mzee Tualike ama mtu yeyote ambaye alikuwepo kwenye safari yake. Hata boti walibaini haikupinduka, hivyo ikawafanya waanze kufikiria kitu gani kilichowapata.

    “Mamba anawezaje kuwamaliza wote pasipo hata kuona viungo vyao? Kama vile mifupa.”

    “Huo uwezekano upo, si wanatumia mashimo yao kufanyia hivyo vitu.”

    “Hapa cha kufanya ni kimoja tu, kutafuta mashimo ya mamba, tuwatoe kisha tuangalie kama viungo vya tunaowatafuta vipo.”

    “Ni sahihi lakini yaweza kuwa tumeshachelewa sana!”

    “Ila mimi ninahisi hawa watu wamebadilisha usafiri, huu waliuacha kisha wakachukua mwingine wa kiraia .”

    “Wangelikuwa washafika kule kisiwani.”

    “Yumkini wameenda sehemu nyingine, si mnafahamu kuna kitu kinaitwa kujiongeza?”

    “Kwa hiyo tunashauriana kipi tufanye?”

    “Watu wazame majini.”



    Wakaafikiana!



    Walewale wa awali waliopiga mbizi mwanzo walizama kwa mara nyingine kutafuta pango waishizo mamba.



    Upungufu wa kasi wa chakula, baada ya kuendelea kuwashikilia mzee Tualike na wenzake, ulipelekea kuingiza wazo jipya kwa wavuvi, kuchoshwa kuendelea kuwa nao. Wazo lililosumbua kwa muda mrefu sana akili zao hadi mioyo iliwasukuma watoe maamuzi mapema kabla huko mbeleni hawajafarakana. Wazo la kuwatoa ndilo lilitamalaki ndani ya mioyo yao, kwani chakula kilizidi pungua kwa kasi zaidi kila uchao--chanzo kikiwa idadi ile ya watu waliowashikilia. Walijadiliana na kuafikiana, wale watu kuwaondoa ndilo jambo sahihi kwao.



    Hawakusita

    Usiku mzobemzobe waliwasomba kisha mtoni wakawatupia. Wakati huo wakiwa wamepoteza fahamu kutokana na adhabu ya kuning’inia juu ya miti waliyowapatia.

    “Acha samaki na wadudu wengine wapate chakula cha ziada,” walisema wavuvi hao mara baada ya kuwarushia mtoni. Wakaondoka zao.



    Sehemu waliyowarushiwa haikuwa sehemu nzuri. Ilikuwa sehemu yenye kina kirefu na iliyoaminiwa kuwa na mamba wengi. Walianza jitihada za kupigania uhai wao, mikono na miguu viliungana maji kuyatawanya, kingo kuitafuta, dhoruba isiwapate. Japo walitawaliwa na uchovu, walijilazimisha, mwishowe walifanikiwa kingo kuifikia. Ahuweni ikawajaa. Mihemo ya nguvu iliwashika, walichofanya hakikuwa rahisi, kiasi kwamba uzima waliuona ukipotea, harufu ya kifo kwa ukaribu waliisikia ikiwanyemelea.



    Pasipo na tambua, usingizi uliwachukua, hoi bin taaban waliyonayo ndiyo chanzo, kuzinduka! Masaa mawili baadaye, tena baada ya masikio kuruhusu sauti za watu walioonekana kutafuta kitu kusikika. Waliamka wakaanza kujikongoja, kuelekea kule sauti walikozisikia hata kama walikosa ufahamu watu wanaowafuata ni wa aina gani. Taratibu walikaza miguu yao, japo njaa na uchovu viliendelea kuwasumbua, hawakuacha kujipa moyo, watu hao wawafikie, msaada wapatiwe. Walitumia zaidi ya robo saa, sehemu husika kuifikia, kisha wakatega chini ya mti, kusikilizia kama watu hao wanaweza kuwa wema kwao, ama ndio wale waliowateka mwanzo. Walizisikiliza karibia dakika nne, ndipo wakatambua sio watu wabaya, ni wema kwao.

    “Ni walinzi wa ofisi kuu,” walijikuta wanatamka wote kwa pamoja baada ya kutambua ni watu gani.



    Kuona hivyo, mioyo yao iliingiwa na furaha, imani ya ukombozi iliwapa nuru, tabasamu likachanua, hawakuvumilia! Moja, mbili, tat... Sauti ya kuomba msaada wakaitoa.

    “Sisi hukuuuuuu! Tupo hapaaaaaaa...”

    Sauti yao ilisikika vyema kwa wale watu walionekana kuhangaika na utafutaji wa jambo fulani. Kweli, walikuwa watu wa ulinzi wa ofisi kuu, walisitisha shughuli, wakatega sikio vyema kusikiliza kwa mara ya pili kuwa ni kina nani waliotoa hiyo kauli.



    Sauti ilivyotolewa kwa mara ya pili, haraka sana wakatambua. Walivuka upande wa pili, ishara ya kuonesha mafanikio ikatolewa kwa kupiga bomu la ishara lenye rangi mchanganyiko angani. Walioko majini nao walipatiwa ishara yao, walivyoiona wakatoka nje. Hawakukawia, wala kujadiliana, waliwabeba na kuondoka nao. Sehemu ya kwanza kupelekwa ni Zahanati, ambako walipata huduma ya kwanza baada ya hapo wakapelekwa ofisi kuu. Siku iliyofuata, walieleza nini kiliwapata, nao kuelezea ya kwao yaliyokuwa yamejiri. Baada ya wananchi kupamba moto.

    “Huo uchaguzi lini?” Aliuliza Mzee Tualike.

    “Kesho kutwa asubuhi. Kila kitu kishaandaliwa, tunasubiri hiyo siku tu.”

    “Mnahisi naweza fanikiwa kupita? Na vipi kuhusu hatma ya sisi wananchi wakinikataa wakamhitaji mtu mwingine?”

    “Ndipo tulipokuwa tunakusubiri, utoe maoni yako.”

    “Mmmh! Nitatoa tamko kesho.”



    Kama alivyoahidi, kesho yake chombo kikuu cha habari cha serikali kilirusha mubashara, hotuba aliyokuwa anaitoa, runingani na radioni. Ambapo sehemu kubwa ya hotuba yake ilijaa maneno ya hamasa, kuwaasa wananchi, nini kifanyike siku ya uchaguzi. Na kuomba hifadhi pia, kwao, wasimchukie, kwani ayafanyayo ndiyo yaliyomo kwenye kitabu cha miiko ya uongozi.

    “Tuwe wavumilivu, wenye imani na subira. Pia tukubali matokeo yoyote yatayopatikana, kwani, wahesabu wanatangaza kile walichokiona kwao kipo sahihi kulingana na jambo lilivyofanyika.” sehemu ndogo ya hotuba ya Mzee Tualike, ilisikika hivyo.

    Wananchi hawakukosa kumsikiliza, ila walio wengi walisikiliza kwa nadra sana. Kutokana na kukosa mapendo naye.

    “Aaah! Hauna ishu wewe.” kauli za wengi walisikika, kila waondokapo kusikiliza hotuba yake.



    Shauku! Ilikata, siku husika ya uchaguzi ilivyowadia. Kwa wingi wananchi walijitokeza, kupiga kura. Walipomaliza walirejea makwao kusubiri muda wa matokeo kutangazwa. Jioni. Mnamo saa 12:45 jioni, mchakato wa uhesabiaji ulifikia tamati, matokeo wazi yakabainishwa, na msimamizi mkuu aliyeteuliwa. Umakini ulienea, matokeo yalivyokuwa yanatangazwa, mwanzo mwisho hadi nukta ya mwisho iliyofunga maandishi, ndipo kelele za watu zilianza kusikika, walivyokuwa wanafanya tathmini ya matokeo.





    Kura ya ushindi iliyopatikana ni kutokuwa na Mwenyekiti. Uamuzi huo ulisababisha shangwe na faraja ndani ya mioyo ya wananchi wengi. Moyo wa matumaini, maisha yenye raha ndotoni yaliwajaa. Tuleane mpya walianza kuiiona. Wadhifa alionao alivuliwa pamoja na safu yake ya viongozi wakuu wa serikali ya kijiji. Uchaguzi mpya ulipangwa, watia nia wakajitokeza. Bi. Mwema alikuwa mmoja wao, tena hakuwa na mpinzani yeyote, alikuwa mgombea pekee. Hivyo uchaguzi ulivyofanyika aliibuka kidedea kwa kura zote zilizopigwa na wananchi. Siku kadhaa baadaye aliapishwa na kuwa mwenyekiti mpya wa serikali ya kijiji cha Tuleane.



    Hakuwa na papara, aliamini viongozi aliowakuta wanamfaa, hivyo hakufanya mabadiliko ovyo hata kama wengi wao ni wa upande wa upinzani. Badiliko kubwa alilolifanya ni kumuondoa Mkuu wa jeshi la mgambo na Afisa mtendaji, viongozi wengine aliwaacha katika nafasi zao.

    “Lengo letu kubwa ni kuijenga Tuleane. Ili tuijenge, yatupasa kuwa na watu wenye imani mbili tofauti pamoja, na si wa imani moja ambao watakuwa wazee wa ndiyo tu hata kama mpango uliopendekezwa ni mbaya kwa kijiji chetu. Wapinzani wana nafasi, ila sio nafasi ya kukosoa kila lifanywalo na serikali, kwenye jema watoe mchango wao pia.” ilikuwa sehemu ya hotuba ya Bi. Mwema kwa mara ya kwanza akiongea na wananchi mara baada ya kuapishwa.



    Tamaa ya kuisadia jamii ya Tuleane iliendelea kuutafuna moyo wake, afanye nini, ndicho kikubwa alichokuwa anakifikiria muda wote. Kikubwa kitachowapa wanakijiji faraja kila wamkumbukapo. Na vizazi vijavyo watambue uwepo wake nini alifanya alipokuwepo madarakani.

    “Kwanza tuzifute sheria zote mpya zilizotungwa, pia na makatazo yote tuyaonayo hayana manufaa kwa wananchi,” alisema mmoja wa washauri wake pindi wakiwa kwenye kikao cha siri, cha kupanga mikakati itayoiweka Tuleane katika ukurasa mpya ukubalikao na wananchi.

    “Pili, tuondoe kinga ya viongozi wakubwa iliyopo,” mshauri mwingine alichangia hoja.

    “Hapo mmenena. Maana nilikuwa na wazo hili, la kuondoa kinga kwetu, ili nimfunge mzee Tualike na wenzake. Kafanya mambo mengi ya kinyama, ambayo hayavumiliki.”



    Kabla wazo la kuondoa kinga kwa viongozi wakuu halijaingia Ofisi elekezi, tayari lilishaanza kuenea, wastaafu liliwafikia wakati huo walikuwa na mipango yao ya kuiharibia serikali, wakiwa wameweka maficho katikati ya msitu na vijana kadhaa wakiwapatia mafunzo mbalimbali ya upambanaji. Adhma yao ikiwa ni moja tu, kuishambulia Tuleane, majengo ya serikali, makazi ya wananchi, utekaji na uuaji pia. Mafunzo yao yalikuwa magumu na makali, vijana ishirini, walioasi mgambo na watano kutoka uraiani ndio waliunda kundi hilo, wakipata msaada wa udhamini kutoka kwa mzee Tualike, Jipendekezo, mzee Kamilius na wastaafu wengine, walioachishwa kazi baada ya Bi. Mwema kuingia madarakani.

    “Huyu mwanamke lazima tumuoneshe, sisi ni kina nani. Na tumpatie utambulisho pia kuwa yeye ni mtoto wa kike hawezi shindana na vidume.”

    “Kali ya kwanza, lazima tufanye shambulizi la kumpa onyo, asifanye hivyo anavyotaka kufanya. Aache sheria zilizopo ziwe vivyo hivyo.”

    “Eeh! Ndio.”

    “Sasa kabla hatujafanya shambulio, tutoe vijana wetu kadhaa, wajifanye wanaharakati wanapingana na maamuzi yanayotaka kuchukuliwa na serikali kwa wastaafu. Serikali ikiwa kaidi ndipo tunafanya kitu.”

    “Ushauri mzuri.”

    “Nani tuwapatie hilo jukumu?”

    “Tuwaache tu Sabaya na Maroda, ila tumuongeze mwingine hapo ambaye ni Maganga. Anaonekana kutufaa sana.”

    “Hakuna tatizo.”



    Naam! Vijana husika walielezwa mpango uliosukwa, nao kuridhia pasipo na hata kuujadili. Siku hiyohiyo waliyoambiwa walianza kazi, kukashfu hoja zinazotakiwa kuchukuliwa na serikali, kwa njia ya kutoa hoja zao radioni, kujirekodi ili tu, viongozi wa serikali wafikiwe. Haikuwa kazi ya siku moja, kila siku, na kadri siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo walivyozidisha kasi, hadi ilifikia hatua ya kujirekodi video matendo gani yatajiri, wabishiwapo.

    “Tuko hapa kuwakilisha wastaafu wakuu wa jeshi la mgambo la Tuleane, na wengine waandamizi wa serikali yetu. Hiki kinachofanywa na serikali ya sasa hatukubaliani nacho, ni jambo la udhalilishaji, ambalo halipaswi kufanywa sehemu yoyote, kwa niaba ya wastaafu, tunaomba serikali iache walichodhamiria kukifanya, endapo watakuwa wakaidi, tutafanya kama hiki kionekanacho katika video hii.” ilikuwa sauti ya Maroda, baada ya hapo ilifuatia picha za video zikionesha watu wakitekwa na kuuliwa, pamoja na mashambulizi ya jengo mbalimbali.



    Liliibuka gumzo, kwa wanakijiji walioshuhudia vipande vifupi vya video walivyokuwa wanaigiza na vipande vya sauti, kuwa nini kitafanyika kuwadhibiti, ukitathmini wanafahamu namna zote serikali watumiazo. Viongozi wa kijeshi nao kila kukicha, wakawa na jitihada za kuondoa presha kwa wananchi, maana ilifikia hatua wengine kuhama mitaa ambayo walisadiki kuwa watashambulia.

    “Wananchi tupo kwa ajili yenu, mliniamini, hivyo ondoeni shaka, hakuna mtu atakayedhurika kuhusiana na matishio yanayoendelea. Walitunyanyasa mwanzo kwa kutetea maslahi yao, sasa wajiandae, nawahakikishia mimi mtoto wa kike kama waniitavyo, naenda kuwaonesha uwezo wangu. Wamefanya dhuluma ya mali za kijiji, wanaenda kuzilipa,” sehemu ya hotuba ya Bi. Mwema akiongea na wanakijiji waliohudhuria mkutanoni kwake, uliojumuisha watu wa muungao mkono na wananchi wasiofungamana na upande wowote.

    “Mhe. Mwenyekiti, kwanini usikae nao meza moja hawa watu muelewane? Maana asilimia kubwa haya mambo yakishatokea sisi raia wa chini ndio watesekaji wakubwa, nyie mnakimbia kijiji na kwenda kupewa maficho kijiji kingine, inakuwaje hapo?” Aliuliza mmoja wa wananchi waliohudhuria, walipopata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa nyanja zote za kimaisha.

    “Wananchi tunahitaji maendeleo, kwa kuwaondoa watu waovu, waliokosa utu na kijiji chetu. Wale Watangulizi wangu ni miongoni mwao, ya nini kuwaonea huruma ilhali mwanzo hawakuwa na huruma na kijiji chetu? Hakuna cha kukaa nao meza moja, wote, lazima waingie gerezani. Kuanzia mzee Tualike, mzee Kasoyaga na mzee Kamilius,” alijibu Bi. Mwema.



    Wastaafu nao walikuwa sehemu ya watazamaji, kwa watu waliokuwa wanafuatilia kupitia runinga. Hawakutaka kupitwa na kila herufi ya neno, walihitaji kusikia kila kitu kilichotamkwa ili wapate wasaa mzuri wa kuamua nini cha kufanya.

    “Katudhalilisha sana huyu mtoto wa kike. Haina haja ya kuchelewa, tumuonesha kuwa sisi tunao uwezo zaidi yake, tuanze sasa.”

    “Tunaanzia wapi?”

    “Alipo!”

    “Sawa mkuu.”



    Vijana waliandaliwa. Zana pia ziliwekwa tayari. Walipokamilika, walisafiri hadi umbali fulani, wakaweka kituo. Bunduki zitumikazo kurusha mabomu umbali mrefu, chini zilikitwa, walizosaidiwa na vikundi vya kiharakati toka vijiji jirani vilivyo na machafuko. Kila kilichohitajika kilikamilika, mabomu na wapigaji waliandaliwa, hesabu ikaanza, kuhesabiwa, kabla haijamalizika ya mwisho, milio ya kufyatuliwa kwa risasi ilisikika.





    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kipindi hesabu ikiwa katikati kumalizika, mlio wa simu unaoashiria ujumbe kuingia, ulisikika masikioni mwa mmoja wa viongozi wanaongoza kikosi cha mgambo walindao viongozi, akiwa hima kudumisha ulinzi kwa Bi. Mwema, kupitia kifaa kidogo kisafirisha sauti kutoka kwenye simu hadi sikioni earphone. Kwa uangalifu aliichomoa, aliifungua kuuangalia ujumbe huo kisha akairejesha mfukoni.

    “095!” Ulisomeka ujumbe huo, alipomaliza kuusoma, aliuinua mkono wake wa kushoto, sehemu ya viganja akasogeza karibu kabisa na mdomo wake, akazungumza jambo.

    “Endeleeni!” Alisema na kurejesha mkono mahali pa awali.



    Wakati huo ni shangwe tu, kwa wale wengine waliokuwa wanashuhudia wenzao walivyokuwa wanahesabiwa tayari kwa kufyatua mabomu, morali ya kazi kukamilisha azma zao, ila ghafla, taharuki ndiyo ilifuatia. Kilichotokea hakikuwa tarajio, milio ya risasi haikutoka kwa washambuliaji wao, kuna watu wengine walionekana kuwazingira wao na kuwafanyia shambulizi. Special Unit.



    Hakuna aliyejua wala kuhisi katika kikundi chao, miongoni mwao ni vibaraka vya mgambo ambao kazi yao kubwa ni kutuma taarifa ya kuwajuza watu kuwa nini kinachoendelea ndani ya kundi hilo.



    Wote walijiona wenye nia moja, kuishambulia serikali, iachane na wastaafu. Ila wao hawakuwa na lengo hilo, kazi yao maalumu ilikuwa kuhakikisha kila siri iliyopo inafika kwa wakuu wao. Mwanadada Havintish na kijana wa kiume, Salidad ndio walikuwa wahusika, vibaraka waliotumwa. Vijana machachari, wanaoaminika, si wagumu kuharibu kazi wapatiwapo.



    Kweli! Walifanya kila mbinu ili kuhakikisha hakuna taarifa inayowapita, na njia pekee waliyotumia ni kujichanganya kila sehemu wenzao washughulikapo hata kama hiyo kazi haiwahusu. Hadi ilifikia hatua ya kupewa jina kimbelembele. Ila kwao ilikuwa poa tu, ilimradi kile walichohitaji kitimie.Wapate taarifa kuhusu kinachoendelea. Kimbelembele hicho, ndicho kilichowavuta hata viongozi wa kundi, na vijana wengine, kwa wingi kujitokeza kumhitaji Havintish waingie kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa kuamini kuwa ni mrahisi. Naye kwa kutumia urembo na siri yake ya kazi, hakuwa mbishi kuwaelewa. Aliwakubali, asilimia kubwa ya waliomtongoza ila si wote alidiriki kufanya nao tendo la ndoa. Baadhi, hasa viongozi ambao walikuwa na siri nyingi kuhusu walichodhamiria. Na wao ndiyo walituma ujumbe kwenye simu ya kiongozi wa walinzi wa siri wa viongozi, pindi wakiwa njiani kuelekea eneo walilopanga kwenda kuweka kambi kwa ajili ya kufanya shambulizi. Iliyoonesha uelekeo, ndipo kiongozi yule akafanya mawasiliano.



    Mawasiliano aliyofanya yalitua kwa kikundi kidogo cha mgambo, kikosi kazi kilivyozoeleka kuitwa ndani ya jeshi, “Special Unit,” Amri walivyoisikia na kabla hesabu haijamalizika tayari, vidole vyao vilikuwa juu ya kifyatua risasi (trigger) kupeleka mashambulizi kwa vijana walioandaliwa kufyatua mabomu.



    Hamaniko! Kila mmoja alitafuta maficho, lakini walichelea, kwani kikosi hicho kiundwacho na mgambo sita, kilisimama kidete kwa shabaha kuzipeleka kwa wahusika waliowahitaji. Walipiga na kusogeza hatua ili kuwafuata kule wanakoelekea, japo wengine ilikuwa ngumu kuwafikia kwa sababu walishakimbia umbali mrefu.



    Baadhi ya majeruhi waliwakamata na kupelekwa kituo kikuu, ambapo walijaziwa fomu kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu kwenye zahanati kisha wakapelekwa. Waliokamatwa wakiwa wazima, wao walipelekwa mahabusu ili kusubiri taratibu zitakazofuatia baada ya hapo. Waliobahatika kukikimbia walikuwa wachache, hasa viongozi na vijana wao wa karibu akiwemo Sabaya, Maroda na Maganga ambaye naye alikuwa timu moja na kina Havintish.



    Vamio walilopatiwa ndilo liliwafanya wakimbie, ukizingatia walikuwa na silaha nzuri za kimapigano ila hawakujipanga kiulinzi kipindi wanaendelea na shughuli zingine. Hivyo iliwarahisishia kikosi kazi kuwashambulia kwa urahisi na kufanikiwa kuteka baadhi ya silaha zao, zilizokuwa tegemeo. Kwa asilimia fulani, walipata mafanikio ya zoezi lao, kukikomboa kijiji kwenye hatari ya kimaslahi iliyoratibiwa na wastaafu, japo hawakufahamu kama wataenda jipanga upya. Tukio lilifanywa kuwa la siri, hawakuhitaji kuwaweka wananchi roho juu, wakose amani ya kuishi wakati ni sehemu waliyopo ni halali kwa makazi yao.



    Tetesi hazikukosa, ila uhakika ulikosekana, hivyo kuendelea kukifanya kile kilichotokea kuwa siri.

    “Vijana wamejitahidi sana, japo hawajafanikiwa kuwakamata viongozi wao.”

    “Yeah! Ni kazi ya kujivunia, wanapaswa kupatiwa pongezi za kutosha.”

    “Wapeni hamasa waongeze bidii, tunawahitaji viongozi kwa udi na uvumba wakiwa hai.”

    “Kuhusu hilo hamna shaka mheshimiwa. Nina imani vijana wetu watafanikisha hilo ndani ya muda mfupi tu.”



    Yalikuwa maongezi baina ya Bi. Mwema na makamanda waandamizi wa kijeshi alipokutana nao ofisini kwake. Kusisitiza nia yake aliyonayo kwa watangulizi kwa manufaa ya kijiji. Na sio kulipiza kisasi, kisa kuwa naye alifanyiwa kipindi cha nyuma, hapana! Lengo ni kuhakikisha wananchi wa Tuleane wanaishi maisha ya amani, yaliyokosa manung’uniko. Alihitaji kujihakikishia aliyoahidi kipindi cha nyuma anayatekeleza pia kuyarekebisha na kuiondoa miongozo ya ovyo iwabanayo wananchi.



    Lazima niwaoneshe nguvu niliyonayo, nawakamata na kufilisi mali zao. Baada ya hapo ndipo niingie kwenye mpango mwingine, aliwaza Bi. Mwema kimoyomoyo.



    Hima! Breki waliifunga kambini kwao, toka eneo la mashambulizi. Hawakuisha kuhema kutokana na umbali mrefu waliokimbia pamoja na uchovu ulioenea karibu katika viungo vyote vya miili yao. Mwishowe walipitiwa na usingizi, walipozinduka, walianza kutathmini kilichowapata. Ila kinaga ubaga kwa sababu ya kukosa uhakika. Haikuwa tathmini nzuri, kingine kilichochangia ni kuingiwa na hofu baadhi yao, kutoliamini tena eneo walilopo kwamba wanaweza kufuatwa endapo walikuwa wanafuatiliwa. Ama kuna mtu alikuwa anatoa siri, basi yawezekana ashatoa kuhusu kambi inakopatikana. Walichoangalia kwa muda huo namna ya kuendelea kulinda uhai wao dhidi ya jeshi la mgambo, lililoanza kuwafuatilia na kutimiza malengo yao. Watu ambao hawakuwepo, hawakuwajadili, waliishia kuwakumbuka kwa kuwafanyia sala ya pamoja kisha waliendelea na taratibu zingine.

    “Kwanza tukikaa kimya huyu mwanamke ataona katuweza. Hivyo usiku wa leo hii, kwa hizi silaha chache tulizonazo tufanye kitu, kumuonesha alichofanya si chochote,” alisema mzee Tualike, akijadiliana na wenzake, wakipiga hatua kuihama kambi yao kwenda kuanzisha nyingine.

    “Wapi Tunaanzia?” Aliuza Sabaya.

    “Sehemu yenye mkusanyiko wa watu wengi usiku wa leo.”

    “Kwa huo muda tutafanikiwa kweli kuipata sehemu ya lengo tulilonalo, maana leo si wikendi.”

    “Hata kama hatutopata sehemu yenye mkusanyiko, lazima kilichopangwa kifanyike.”



    Kweli! Kiza kilipoingia, walitayarika, kila mmoja akiwa katika muonekano wa kipekee, wengine walivaa mavazi ya kike, hasa madela na nikabu juu ili kuzuia sura zao,wengineo walivaa mavazi makubwa ya kiume kama vile makoti yatumikayo zaidi na majambazi, wakiwa na kofia juu. Silaha zao walizoziteua kuzitumia walizihifadhi juu ya miili yao na kuzuiwa na nguo walizovaa. Moja kwa moja walielekea sehemu teule, katika kilabu kikubwa kikusanyacho watu wengi ili kupata burudani za aina mbalimbali. Hawakupata shida, wala haikuwagharimu katika majadiliano wakiwaza namna ya kuingia.

    “Ondoeni hofu, hakuna ulinzi pale, twendeni,” alisema Maroda.

    “Una uhakika na uongeacho?” Mzee Kasoyaga aliuliza.

    “Yeah! Wengine tulikuwa mabingwa wa hayo mambo, kwa hiyo tunafahamu mazingira ya kila kilabu kijijini.”aliendelea kujitapa Maroda.

    “Hawakagui watu waingiao?”

    “Unaanzaje kukagua watu waingio klabuni? Utaratibu huo wa wapi?” Yalikuwa maongezi yao, hatua chache toka lango la kuingilia klabu hiyo ifahamikayo Meswaki.

    “Wa kuchukua picha za video na mnato ajiandae kabisa kuweka wazi kamera.” Mzee Tualike alichangia. Pindi wakianza piga hatua kulifuata lango.



    Wakati huo ulikuwa wa kiza kinene, usiku wa saa nane, ukimya ulitamalaki, mwonekano wa watu kuingia ulikosekana, yaliyoonekana ni watu kutoka kilabuni tu huku langoni wakiwa wamesimama walinzi wawili kuhakikisha usalama. Kuona hivyo, walijiaminisha kuwa hakuna shida wala kizuizi cha wao kuingia.



    Upande wa pili Havintish na Salidad walifanikiwa kuwa miongoni mwa wasalimika. Wao mapema tu, mashambulizi yalivyoanza walichukua maficho na kutoweka moja kwa moja, kwani walishataarifiwa wapi mashambulizi yatatokea. Sababu shughuli yao kubwa walishaifanikisha, hawakuhitaji kurejea tena kwenye hiyo kazi, kwa mujibu wa nafasi walizopata kabidhiwa walirejea kitengoni kwao. Ila wakawa na wajibu wa kupokea taarifa toka kwa Maganga, nini kinaendelea kwenye kambi ya wastaafu. Kisha wao kuisafirisha ngazi za juu.

    Taarifa hizo zilikuwa zinawasilishwa kupitia kamera ndogo ichukuayo picha za video, iliyotegwa mwilini mwa Maganga, katika paji la uso, iliyotengenezwa mfano wa kidoti cheusi Pamoja na kirekoda cha sauti kilichotegwa kifuani.



    Kupitia vifaa hivyo viwili, mambo yote yaliyokuwa yanajadiliwa yalikuwa yanasikika na kuwapa fursa namna gani wajiandae. Mipango ya wastaafu kudhuru kilabu kubwa ya Meswaki, taarifa mezani iliwafikia, haraka mno ilijadiliwa na mikakati madhubuti ilipangwa namna ya kuwadhibiti. Kama ilivyo ada, kikosi kazi kiliandaliwa, huku mikakati mingine nayo ilitekelezwa. Mkakati mmojawapo ulikuwa kuanza kwa shughuli ya ukaguzi wa watu na mizigo mbalimbali iingiayo ndani ya kumbi za starehe, pasipo kusahau vyombo vya usafiri, baada ya muda mambo yakawa sawa kusubiri muda husika uliopangwa tukio kufanyika.



    Mkakati huo ukawa sheria, kuanzia muda huo na kuendelea. Vyombo vya ukaguzi vilimwagwa, serikali ilijitolea, kumbi nyingi tu kufanikisha zoezi hilo, kumbi moja wapo ikiwa ni Meswaki. Masaa yalizidi, saa moja likasalia ili kufikia lile lililopangwa tukio kufanyika, wakati huo watu waliopangwa kwenda kufanya ukamataji mmojammoja alizinduka kutoka usingizini, aliyeonekana kupitiwa zaidi walimwamsha.



    Hatimaye nusu saa ilisalia, wote wakawa tayari washaamka, wakafanya maandalizi ya mwisho hasa kuhifadhi zana zao za kazi ndipo walianza kuondoka kuelekea kilabu ya Meswaki, ambapo tukio lilipangwa kufanyika. Wakiwa katika mwendo, hatua chache, hata kabla hawajamaliza kutoka sehemu waliyokuwa wamepumzika, ghafla walisikia sauti ikiwaomba warejee chumbani walimokuwa awali.



    Walirejea.



    “Aaah! Ndugu zangu poleni kwa usumbufu, ila ndiyo majukumu yetu,” alisema mtu huyo aliyewarejesha na kutulia kwa muda kisha akaendelea.

    “Viongozi wetu wamedhamiria kusitisha zoezi la ninyi kwenda kule kilabuni, wanaamini kuwa watawasumbua tu, hivyo endeleeni kupumzika kwani wale walinzi wa kilabu wamepatiwa vile vifaa vya kukagulia, mtu yeyote mbaya hawezi kupita, na wakifanikiwa kuwabaini watawakamata tu. Hivyo hao waliopanga kwenda kufanya uhalifu hawawezi fanikisha mpango wao, mapema tu watawekwa mikononi mwa sheria.”

    “Hakuna shida kiongozi, kwa hicho walichofanya sidhani kama hao watu watakuwa na taarifa. Leo wanakamatwa mithili ya kuku wauguao kideri,” alisema mmoja wao kati ya wale waliotakiwa kwenda Meswaki klabu kufanya ukamataji wa viongozi wastaafu, waliopanga njama ya kuifanyia mambo mabaya serikali mpaka pale watakapodiriki kukubaliana na matakwa yao ya kuwaacha wawe huru mtaani.



    Hata mgambo waliotangulizwa mapema kabisa kwa ajili ya upelelezi walipatiwa taarifa za kuondoka eneo hilo baada ya kujihakikishia hali ya usalama haitakosekana, nao walitii amri za wakuu wao.



    Kiongozi mstaafu ndani ya Tuleane alionekana mtu aliyeko juu ya sheria. Hakuwa mtu wa kuguswa hata kama atatoa kauli chafu za kudhihaki jamii. Huonekana mara kwa mara pia kutoa matamshi ya maudhi kwa wengine lakini vyombo vya dola hukaa kimya pasipo na kuchukua hatua zozote za kinidhamu. Hata kutoa onyo kwao ni vigumu, huachwa wajitawale watakavyo. Ukizingatia kinga iliyopo ndani ya katiba, muongozo mkuu wa uendeshaji wa kijiji huwabeba. Huwapa kiburi pia cha kuamua jambo lolote watakalo. Vilevile imefikia hatua yakukingiana vifua. Viongozi walioko madarakani huwakingia kifua wastaafu wasiguswe wala kujumuishwa kwenye mashitaka ya kukiingiza kijiji kwenye hasara.

    Toka awali Bi. Mwema hakuwa mfuasi wa itikadi hii, hakuipenda na alipingana vikali. Aliichukia na kudhamiria kufanya marekebisho ya kutosha kuhakikisha raia wote wanakuwa sawa, chini ya sheria na siyo sheria kuwa juu yao. Wastaafu wa serikali alihitaji waishi kama raia wengine waishivyo na wale waliopo ndani ya serikali pia ili kuleta nidhamu, jamii iheshimiane.



    Ukamilisho wa hii dhamira alipanga kuanza kuitekeleza pale wastaafu wakuu wa serikali ya kijiji watakapowekwa hatiani, huku taratibu za chini zikiendelea kufikia tamati kwa muda mfupi. Rekebisho la kwanza alilopanga ni mabadiliko ya muongozo mzima wa kijiji—kuwapa fursa wanakijiji serikali ya aina gani wanaihitaji. Kipaumbele ikiwa ni kuondoa kinga walizowekewa wakuu wote pamoja na adhabu kali kwa wawakilishi wasiotimiza majukumu yao ipasavyo. Japo kwa wakati huo, hicho alichodhamiria kilikuwa kinyume na sheria za uongozaji wa kijiji, yeye hakujali, alichojali ni maslahi kwanza na mamlaka aliyonayo ya kuwa kiongozi mkuu wa kijiji. Alifahamu fika kuwa anayo mamlaka ya kufanya jambo lolote ambalo liko kinyume na sheria ilimradi asipelekee uvunjifu wa amani. Wastaafu lazima waadhibiwe ndilo lilikuwa lengo lake kuu.



    Kwa ujasiri waliojipa walifanikiwa kulifikia lango kuu la kuingilia. Walipangwa mstari mmoja na mmoja wa walinzi waliopo langoni. Haikuwapa tabu kukubali, walijipanga kisha mlinzi huyohuyo alitoa kauli kuwataka wanyooshe mikono yao wakaguliwe ndipo waingie ndani. Walishituka na kuwafanya washangaane.

    “Utaratibu huu umeanza lini?” Aliuliza Sabaya huku akionekana kunyoosha mikono yake tayari kwa kukaguliwa.

    “Umeanza leo. Serikali imeamua hivyo baada ya kuona hatarishi nyingi za kiuhalifu,” alijibu mlinzi, lakini ghafla kelele za watu waliokuwa wanapata burudani ndani wakiita walinzi kuomba msaada ziliwafanya wasitishe zoezi la kuwakagua kina mzee Tualike na wenzake na hatimaye kukimbilia ndani ambako kelele zilikokuwa zinasikika.









    Hii iliwapa nafasi ya wao kuingia kwa urahisi kabisa, bila wasiwasi wowote kisha kujibanza kwenye kona moja. Dakika mbili baadaye mmoja wao alinyanyuka na kurejea hapo baada ya robo saa, akawapatia ishara fulani wenzake.

    “Kuko shwari, tupige kisha tusepe.”

    “Hiyo nzuri, tunashambulia na kuteka baadhi ya watu.”

    “Sahihi!...sahihi!...sahihi!...” walinong’ona.



    Hawakuchelewa, waliinuka na kufanya walichopanga. Jambo la kwanza walipiga risasi kadhaa hewani, zilizopelekea watu kuchanganyikiwa na kutoka kabisa nje ya kile walichokuwa wanaendelea nacho--kila mmoja alianza kujali uhai wake kwa kulala chini na kuanza kutambaa ili akiweza atoroke. Wapo waliofanya hivyo wakafanikiwa, lakini wengi walishtukiwa, wakapigwa risasi zilizoondoa uhai wao. Baadaye walifuatia kumimina risasi kwa yeyote aliyoko mbele yao, na kuteka baadhi ya watu wakaondoka nao. Takribani watu kumi, kisha kufunga lango zote za kuingilia, huku wakiacha bomu kubwa, lililotegwa kulipuka baada ya dakika kumi na tano. Dhamira yao, ilikuwa wanahakikisha jambo walifanyalo lazima liwe kubwa lenye kumtetemesha kila kiongozi wa serikali.



    Dakika tano baadaye, tangu tukio lilivyotokea, mgambo ndio walifanikiwa kupata taarifa kutoka kwa mmoja wa watu waliotoroka.

    “Afande!...afande!... Meswaki hali si shwari, fanyeni hima mkasaidie mamia ya watu walioko mle ndani.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna tukio gani?”

    “Majambazi. Hiyo milio mliyokuwa mnaisikia ni risasi. Watu wengi wameshambuliwa na kupoteza uhai wao, wachache wakisalia majeruhi. Nawaomba mkasaidie wale watu.”

    “Hee! Kumbe hiyo milio tuliyokuwa tunaisikia ilikuwa ni risasi? Pole sana ndugu, wahi nyumbani, ahsante kwa taarifa, tutalishughulikia hili.”



    Haraka waliwataarifu wenzao. Walijiandaa kisha walipanda kwenye usafiri wakaanza safari. Hata wakuu walipopata taarifa, amani ilitoweka ndani ya mioyo yao, wataonekana vipi wakati mwanzo walishashauriwa kukaa meza moja wakapuuzia ushauri wao. Jakamoyo likawapanda, wafanye vipi kuwaokoa ilikuwa mada iliyoenea sehemu kubwa ya akili zao. Hawakuvumilia, wala kuhitaji kufanya kazi wakiwa nyumbani, usiku huo, walikutana, ofisi kuu ya jeshi la mgambo, chumba chenye mitambo maalumu ya mawasiliano ya kijiji kizima na kinachoendesha kamera za usalama zilizoko baadhi ya mitaa. Viongozi wote wakuu walikutana humo, wa kijeshi na serikali kujadili namna ya kutatua tatizo lililoko mbele yao.

    “Nishachafukwa!” Alisema Bi. Mwema kimoyomoyo, kauli iliyofuatiwa na mhemo ulioashiria kuchanganyikiwa.

    “Jamani tufanye jitihada za kutosha kuhakikisha hao watu waliomo ndani wanabaki salama, zaidi ya hapo serikali yangu itachafuka, jamii haitaniamini tena zaidi ya kuniona muuaji wa ndugu zao.”

    “Tumuombe Mungu, ila nina tumaini walioko ndani watabaki kuwa hai, ukiachana na ambao tayari washatangulia mbele za haki,” Kiongozi aongozaye mitambo ya kamera na mawasiliano ya simu za upepo alisema.

    “Ushawasiliana na hao mgambo wanaoenda kuokoa, wakakuambia walipofikia?”

    “Yeah! Nimewasiliana nao dakika chache zilizopita, wakasema wapo maeneo ya Gulioni Pub, ambako ni kama umbali wa mita nane hivi kutoka kilabu ya Meswaki ilipo.”

    “Watafute tena tufahamu wako wapi.”



    Alifanya alivyoambiwa. Alirudi tena mtandaoni kuwafuatilia (kuwatrack) baadaye alibonyeza vitufe kadhaa akawa kwenye mazungumzo na kiongozi wa kundi.

    “Tule!Tule!”

    “Five! Uelekeo, tatu-mbili-moja, siafu jicho nyanya, punde tunaifikia,” alisema kiongozi wa mgambo waliokuwa wanaelekea kuokoa wahanga.

    “Tule! Iko nami muda huu, fanyeni hima kuhakikisha mnawaokoa wote,” alisema kiongozi anayeongoza chumba cha mawasiliano. Akimaanisha viongozi wakuu wa kijiji wako naye ofisini kwake kwa wakati huo kufahamu kinachoendelea.

    “Nawapa uhakika, shaka waondoe, hatuwezi kuwaangusha. Usalama wa watu lazima upat...” alisema kiongozi wa waokoaji.

    Wote waliomo chumbani waliusikia,wajihi zilijaa udhaifu, ukimya ulipita, sauti ya chini ya kuhema nayo ilichukua nafasi, walivyokuja vumbuka toka simanzini, kauli moja waliitoa.

    “Washateketea!”



    Kwa masikitiko makubwa sana, walijikaza na kuendeleza uhitaji wa kufahamu ukweli. Waliunga tena mawasiliano, lakini awamu hii kila walivyojaribu kuwapigia, redio yao ilikuwa haipokelewi. Hawakuishia mara moja, walipiga mara nyingi tu, ila majibu waliyokutana nayo hayakuwa na tofauti na ya awali. Jambo lililowafanya waingiwe na hasira pia hamu ya uhitaji wa kufika eneo la tukio kushuhudia kwa macho yao kilichojiri.



    Waliondoka chumbani kuelekea eneo la hifadhi ya vyombo vya usafiri, walikoegesha usafiri wao, walipanda kisha safari ilianza. Moyoni kila mmoja akiwa na wazo lake kuhusu kilichotokea na hatma ya wananchi watachoamua baada ya mamia ya ndugu zao kupoteza maisha. Mwendo waliotembea barabarani haukuwa wa kawaida, ulikuwa wa kasi mithili ya watu walioko mashindanoni. Hawakuchelewa kuwasili na kuteremka garini kwa haraka mno ili kwenda kushuhudia. Walichokiona waliishia kusikitika, huzuni na simanzi nazo zikizidi kuongezeka na kutawala kwa kiasi kikubwa akili na mioyo yao kwa wakati mmoja. Wafanye nini? Ndiyo kauli ya kwanza kuwatoka mdomoni tangu walivyowasili, huku wananchi waliojitokeza kusaidiana nao kwa ukaribu mkubwa wakawa wanawaangalia na kusubiri kwa hamu kubwa kusikia watachozungumza.



    Hatimaye baadhi yao waliingia kwenye majadiliano, wengine kutoa hamasa ya kufanya uokoaji, kwa sehemu zinazowezekana kuokolewa. Pasi na sahau kuwatafuta mgambo waliokuja kuokoa, lakini hawakuwaona.



    Moshi na mwanga wa moto uliotanda angani uliozalishwa baada ya kuanza kuteketea kwa jengo hilo refu kuliko yote Tuleane. Haukuwa moto wa kawaida, ulikuwa mwingi na mkali. kiasi kwamba watu wengi walishindwa kusogea karibu, waliishia kuangalia tu namna jengo lilivyokuwa linaungua. Ni wachache mno wenye moyo ndio walijitokeza kusaidizana na watu wa uokoaji. Kazi yao kubwa ilikuwa ni kupokea vitu na miili ya watu iliyokuwa inatolewa ndani. Hata walivyoongezeka viongozi wakuu wa kijiji, walivyotoa hamasa ya kuongeza nguvu, si wengi waliojitolea, asilimia kubwa waliogopa kuungua kwani kila baada ya muda fulani vilisikika vitu vikilipuka na kutoa mlipuko uliopelekea kuongeza kasi ya moto kuwaka. Hicho kiliwafanya wengi wao waogope.



    Wachukiao, hawakukosa. Wapendao serikali ipatwe na matatizo kila muda walikuwepo kwa wingi pia na kutamani ili mioyo yao iridhike matatizo lazima yatokee. Hicho ndicho kilichotokea, wale wauchukiao utawala wa Bi. Mwema, ambao wamepandikizwa chuki na wastaafu, hawakuweza kuvumilia bila kuzomea na kutoa maneno mengi ya kashfa ya kuwatuhumu kuwa wahusika wa tukio kwa maana walishaarifiwa tangia awali wakawa wakaidi. Yaliporomoshwa matusi na maneno mengi yasiyo hitajika kutamkika. Ila Bi. Mwema aliwatuliza watu wake na kuwaomba watulie, wafanye kilichowaleta.

    “Achaneni na hao, tufanye hiki kilichotuleta. Tukipambana na hawa tutaonekana akili zetu haziko timamu. Tufanye jitihada za kupambana na hao si hawa,” alisema Bi. Mwema mwisho kabisa katika kuhitimisha majadiliano yao.



    Jitihada za uokoaji ziliendelea na kuhitimishwa saa kumi na moja alfajiri. Uchunguzi wa awali ulifanywa kuanzia muda huo na saa 12 asubuhi ndipo ripoti ya awali ilitolewa. Iliyofanywa na kusomwa na jeshi la mgambo ikielezea idadi ya wafu, majeruhi na watu waliosalimika huku wakitoa miadi ya kueleza chanzo cha tukio kwa siku za baadaye, uchunguzi kamili utapokamilika.

    “Aaaaaaaah! Nani asiyejua kuwa risasi na mlipuko wa bomu lililotegwa na magaidi ndiyo chanzo? Acheni kutuyumbisha nyie watu, muda mrefu sana tulishawaambia kaeni meza moja na hawa watu mkaleta ukaidi, hayo ndiyo matokeo yake. Mnaficha nini?” walisikika wananchi wakilalamika.



    Manung’uniko yalianza. Katikati ya maongezi yao yaliyojaa malalamiko, jipya likaibuka toka moja ya mtandao wa kijamii. Kwani ilisharejeshwa hewani punde, Bi. Mwema alivyoingia madarakani.

    “Kuna nini tena?”

    “Sijajua!”

    “Imekuaje watu wanakusanyika kusanyika makundi?”



    Waliulizana baadhi ya wananchi, walivyoona wenzao wanakusanyika kusanyika katika makundi tofauti tofauti kuangalia jambo fulani. Nao iliwabidi kuchagua kundi moja kujumuika nalo kuangalia hicho kilichowafanya wakusanyane. Waupendao utawala wa Bi Mwema, walivyomaliza kuangalia walitokwa na hamaniko, huku wale wauchukiao walilipuka shangwe.







    Kutoonekana kwa vijana wa kikosi kazi kuliibua taharuki mpya kwa viongozi wakuu wa jeshi na serikali. Ukijumlisha na malalamiko wapatiwayo kutoka kwa wananchi, hali ilizidi kuwa mbaya na mpango wa utatuzi wa haraka hawakuwanao. Iliwabidi waingie kikaoni ndipo wapate muafaka utaokuwa sahihi kwao na kwa wananchi kwa ujumla. Kikao cha dharura kiliitishwa. Mada moto mezani ziliwekwa moja baada ya nyingine.. Wakiwa katikati ya mazungumzo mazito, sauti ya Awetu iliwazuia na kuwataka kusikiliza, akiwa kashikilia kompyuta mpakato mkononi mwake.

    “Hao tunaowatafuta ni hawa hapa,” alisema Awetu akiitua ile kompyuta mezani. Wote walikusanyika kuangalia. Ilikuwa ni picha ya video iliyorekodiwa usiku wa kiza, ila iliweza kuonekana vizuri kwa msaada wa mwanga wa taa zilizokuwa zinawamulika wahusika. Hawakuamini macho yao, walichoona walihisi ni ndoto. Walipikicha macho na kumuomba airejee upya watazame kwa uzuri, Awetu naye pasipo na nongwa, alitekeleza agizo lao. Waliiangalia kwa mara ya pili, hisia ya kuiamini ndipo ilianza kuwaingia.

    “Inawezekanaje?” walijiuliza.



    Picha ya video waliyokuwa wanaiangalia ilikuwa ni ya utekaji uliofanywa na watu walioshambulia kilabu ya Meswaki. Ikionesha toka mwanzo wahalifu walivyoingia kilabuni na kuanza kufanya mashambulizi kwa raia wasio na hatia. Haikuishia hapo, iliendelea kuonyesha namna walivyotega mabomu na kuteka baadhi ya watu, wakaondoka nao. Baada ya hapo kilifuata kiza takribani dakika mbili na sekunde kadhaa, picha zilivyorejea, sura ya mhasibu mkuu wa kijiji na kikosi kazi zilionekana wakiwa wametekwa. Ndipo iliwafanya watokwe na kauli ya inawezakanaje?



    Hamu ya kuendelea na kikao iliishia hapo, hofu ilitamalaki, mabingwa waliokuwa wanawategemea katika matukio ya ukombozi kuwa mikononi mwa wahalifu ambao sasa walishaiva kuwa magaidi, huku watu wa majeshi wakiwaita wahalifu ili kuondoa hofu kwa wananchi.



    Mjadala uliofuata hapo ni namna gani watawaokoa. “Tusichelewe katika hili, ikiwezekana hii video huko mtandaoni ifungiwe kabla haijaanza kuzagaa,” alisema Dkt Emmakulata.

    “Kuhusu kuifungia tushachelewa, maana ishaenea zaidi ya tunavyofikiri. Huko nje mamia ya watu washaiona na asilimia kubwa wanaiunga mkono huku wakiwaomba wahalifu waongeze kasi ya utekaji wa viongozi. Hata wale waliokuwa wanapenda utawala wetu, baada ya kupoteza ndugu zao kwenye lile tukio, washaanza kutuchukia na kuunga mkono hili kundi. Tunawakati mgumu sana.” Awetu alichangia.

    “Tunaamuaje?”

    “Mkuu wa jeshi la mgambo ateue mgambo kadhaa wakafanye uokoaji, hamna namna nyingine zaidi hiyo.”

    “Mkuu! Umelisikia hilo? Mpaka kufikia mchana wa leo tunawahitaji mgambo imara wa kwenda kuwaokoa wale watu.”



    Kikao kikaahirishwa!



    Hakika! Watawala wa muda mrefu wa serikali ya Tuleane sasa waligeuka kuwa magaidi. Kwani hata wawakilishi wa mtaa walioko ndani ya ofisi elekezi hawakuwa na agenda za maendeleo tena zaidi ya kupokea amri mbalimbali kutoka kwa mzee Tualike, nini wafanye kukwamisha jitihada za kimaendeleo zilizokuwa zinaendelea. Yote kuhitaji kulinda wasifu wao waliopata kuwa nao awali. Hawakuhitaji kuwa waathirika wa mipango ya serikali kwa kile walichotenda kipindi cha nyuma, ilhali ndiyo wahusika. Kwa namna yoyote, walijiapiza, kufanya mambo ambayo serikali, wakiyasikia ama kuyaona, yatawayumbisha katika uchukuaji wa maamuzi ya kuyatatua.



    Imani zao ziliwatuma kuwa wao ni waumini wazuri ambao hawakupaswa kuguswa huku wakisahau kile walichotenda miaka ya nyuma kwa maslahi yao binafsi. Walisahau utekaji, unyanyasaji waliofanya kwa raia wasio na hatia kwa sababu tu wamekosoa ama wamehamasisha wananchi wenzao kudai haki zao zilizobainishwa kisheria. Walisahau mauaji, uminyaji na vitu kadha wa kadha vilivyo kisheria, na kujitwalia kuwa kijiji cha Tuleane kipo kisheria kwa halali yao na sio kutawaliwa na watu wengine, watokao upande wa upinzani.



    Upatikanaji wa mgambo wengine wa kwenda kufanya uokoaji ulikuwa mwiba mkali kwa mkuu wa jeshi la mgambo. Mgambo wengine wenye taaluma ya mafunzo kama wale waliotekwa ndani ya jeshi hilo hawakuwepo. Wengi wao walikuwa na ufahamu tu wa awali wa kile kinapaswa kufanyika, ila uhalisia wa ndani zaidi hawakuwa nao.



    Hadi inafikia saa 7:50 mchana, zikisalia dakika kumi viongozi wakuu wakutane tena kwa ajili ya Mkuu wa mgambo kuwasilisha majina ya mgambo watakaoenda kuokoa, hakupata majina.

    “Kijana, unanisaidia vipi kuhusu hii kitu? Watu gani unapendekeza?” Aliuliza Mkuu wa jeshi la mgambo, akimuuliza mlinzi wake.

    “Afande, si wachukue Havintish na Salidad.”

    “Mmmmmh!”

    “Eeh! Chukua hao, wataweza kupambana na hao watu.”



    Kimya kilipita, tafakuri ikachukua nafasi. Ilivyoisha usahihi wa kipi kifanyike ulipatikana.

    “Wapigie simu, wataarifu.”



    Kweli! Mlinzi wake alipiga simu kwa wahusika, na baada ya muda mfupi, Havintish na Salidad waliwasili. Kabla hawajaingia kwenye kikao walikutana na mkuu wa jeshi lao, walipatiwa maelezo nini kilichosibu hadi wapatiwe wito, nao pasi na hiyana, waliridhia. Japo mkuu alikuwa hawaamini kama wana uwezo wa kufanikisha zoezi hilo. Muda wa kikao ulivyowadia, waliingia ukumbini, na punde kilianza. Hata viongozi wengine waliohudhuria, walikosa imani walivyoambiwa kuwa wao ni mgambo pekee waliyopewa dhamana ya kwenda kuwaokoa mateka.

    “Mtaweza kweli?” Aliuliza Bi. Mwema.

    “Ondoa shaka mheshimiwa. Tupo sawa kwa shughuli yoyote, tunakuahidi kukuletea mateka wote walio chini yao,” alijitapa Havintish.

    “Mmmh! Ni sahihi kuhusu hicho mnachotuambia?”

    “Hatukuongopei.”

    “Okay! Tunaweka imani na maombi kwenu, msituangushe. Tunahitaji ushindi.”



    Kuhitimishwa kwa kikao hicho ukawa mwanzo mzuri wa maandalizi kwa kina Havintish na Salidad. Walijiandaa na jioni ya siku hiyo walianza rasmi zoezi la kuelekea mafichoni waliko wastaafu na mateka wanaopaswa kwenda kuwaokoa. Wakati huo bado Maganga alikuwa anaendelea kuwapatia taarifa wapi maficho yalikowekwa. Hakukuwa na usumbufu, kwamba wapi waanzie na kumalizia, taarifa walizokuwa wanapatiwa ziliwasaidia, sambamba na hisia zao pia, kuwa matokeo yote ya uhalifu hayawezi kwenda fanyika sehemu nyingine zaidi ya msitu wahatari uliopo karibu na hifadhi ya wanyama pori Nanenane.



    Taarifa na hisia zilienda sambamba kuwa wanapaswa waufikie msitu huo ndipo watafanikisha wanachopaswa kufanya. Hawakuzembea, walitii na baada ya mwendo wa dakika kadhaa walishaufikia. Walipofika walijigawa, kila mmoja upande wake lakini kwa umbali utaowawezesha kuonana, kisha walizidi kupiga hatua kusonga mbele. Bunduki zilizofungwa kiwambo pamoja na darubini juu ya usawa wa mtutu na kishikio cha mbele vilitulia kuwawezesha kupata dira sahihi walengapo. Muondoko ulikuwa wa kunyata, achilia mbali darubini zilizofungwa kwenye bunduki aina ya Norinco QBZ-97B—walikuwa na darubini zingine walizoning’iniza shingoni, yote hiyo ilifanyika ili kuhakikisha wanafanikisha lengo lao.



    Walivyowasili, ghafla ilianza kutokea hitilafu ya mawasiliano na Maganga. Kila walivyojaribu kumtafuta na kuangalia kwenye kioo cha vifaa vyao palikuwa na chengachenga tu ndiyo walishuhudia, hawakumpata. Hata mawasiliano kwa njia ya simu hawakubahatika kuyapata. Ulikuwa ni mtihani mpya kwao, msitu mkubwa kama huo wapi waanzie ilhali mwanzo wakati wanawasiliana waliambiwa kuwa punde watakapowasili wamtaarifu ili awape uelekeo sahihi. Ilibidi waanze kubahatisha.









    Wakati huo wastaafu na kundi lao, ambalo sasa lilikuwa na wapiganaji wachache hawakuisha vikao vya mara kwa mara, hasa viongozi ili kujadili mustakabali wa mwenendo mzima wa ufanikishaji wa kile walichopanga ili kuidhoofisha serikali. Namna gani wafanye? Suluhisho la kwanza ni kuwateka baadhi ya watendaji wa ofisi nyeti, wa idara mbalimbali, za serikali. Miongoni mwa watu waliopanga kuwafanyia hicho kitu, ni mhasibu, ambaye anaweza kuwapatia dondoo ya mahali pesa zilipo. Hivyo ufahamu kuwa, mhasibu wa serikali ya kijiji, mara nyingi hupatikana ndani ya kilabu ya Meswaki. Wakati wa mapumziko, baada ya muda wa kazi kumalizika, walikuwa nayo, jambo lililo warahisishia kupanga mikakati ya kumteka kwa namna yoyote wakimuona. Wasivyobahatika, wapange siku nyingine. Pia walifahamu, wakishafanya tukio, taarifa itawafikia kikosi kazi cha uokoaji ndani ya jeshi la mgambo, sasa ili nao wawe wahanga, waliwategea mtego.



    Juu ya hilo, kingine walichokesha nacho kujadili ni uvujaji wa mipango wanayoipanga. Inawezekana vipi? Walijiuliza na jibu pekee walilopata ni kuhisi miongoni mwao kuna msaliti anayetoa taarifa.Upande wa pili pia walihisi yawezekana satellite zilizotegwa hifadhi ya wanyama pori, Nanenane ndizo zivujishazo taarifa zao kwa sababu ya ukaribu wa maeneo hayo. Hisia hii ndiyo waliipa nguvu zaidi kuliko ile ya kumhisi mtu, japo hawakuipotezea na waliipa nguvu kwa kiasi fulani ya kuifanyia kazi. Wanahitaji kujikomboa vipi na mitego waliyoihisi? Wakadhamiria kufunga kamera ndogo, kwenye baadhi ya miti kuangalia mwenendo mzima wa sehemu fulani ya msitu waliyoihisi kuwa hatari kwao. Ambazo ziliwasaidia kuangalia mwenendo wa wapiganaji wao pia. Kamera zilifungwa kabla ya siku waliyopanga kwenda kufanya tukio, walipokamilisha ndipo walienda, na kufanikisha tukio lao kwa asilimia zote walizopanga. Mhasibu na kikosi kazi cha mgambo kikawa chini ya yao, muda wote wakawa watu wa kuwapatia kipigo kikali ili wapatiwe siri fulani wanazozifahamu zilizopangwa na watendaji wakuu wa serikali.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kipigo kilikuwa kama dozi kwa mateka, kutwa mara mbili, asubuhi na jioni, lakini hawakudiriki fungua domo zao kutoa japo neno kuhusu maswali waulizwayo. Neno pekee walilotamka ni sijui, na kashfa nyingi zilizowaongezea hasira watekaji.

    “Mkuu! Wale watu wamegoma kabisa.”

    “Kwa hiyo unashaurije?”

    “Tuwaondoe tu duniani. Maana nina hakika tukifanya hivyo, tutakuwa tumewapatia hasara kubwa serikali.”

    “Mmmh! Ni ushauri mzuri, ila... Wamegoma kabisa kuongea?”

    “Ndiyo kiongozi.”

    “Kama ni hivyo, fanyeni mlichofikiri. Inaweza ikawa wakishaona mmoja kadondoka wengine watabadili msimamo.”

    “Sahihi!”

    “Nawaomba hilo tukio lifanyike usiku.”

    “Hakuna shida kiongozi.”



    Maandalizi ya kuwaondoa duniani yalianza. Mioyo ilijaa furaha. Mnamo saa 3:09 usiku, ndipo muda tajwa uliopangwa maangamizi yafanyike. Wote watatu: Sabaya, Maroda na Maganga walifika walipo mateka. Wakiwa njiani, hima pasipo kutarajia, Maganga alikwaa kisiki kilichopelekea aanguke na kuanza kuviringika. Hakuwa na nyota njema! Mviringiko alioupata ulimfanya avivae visiki vingine vidogovidogo, vilivyopelekea kuchubua na kuumiza sehemu mbalimbali za maungo ya mwili wake. Msaada alikuja kuupata baadaye, kutoka kwa wenzake aliongozana nao wakati tayari alikwishaoga maumivu ya kutosha—damu ilimtiririka na baadhi ya meno yake yakiwa yameng’oka. Sehemu kubwa ambayo alikuwa ameumia ni kichwani, alichubuka, kidonda kikubwa kikajijenga na ndicho kilichotoa damui nyingi.



    Iliwalazimu warudi kwa ajili ya kumpatia matibabu. Walipokamilisha, Sabaya na Maroda walirejea kule walikokuwa wanaenda. Anguko lililomkuta Maganga lilimfanya apoteze kamera zilizotegwa mwilini mwake na ndipo muda huo aliopoteza mawasiliano na akina Salidad. Hali yake pia haikuwa nzuri kwani maumivu yalikuwa makali, yaliyochosha sehemu kubwa ya mwili wake. Juu ya hayo, ufahamu wa mambo, haukupotea. Kumbukumbu alikuwa nayo, akijua kilichokuwa kinaendelea na kinachotarajiwa kuendelea. Hivyo kupotea kwa kamera pia kulichangia maumivu. Je, atawafahamishaje wenzake aliowaahidi na namna gani ataendelea kutoa taarifa?

    “Kazi imeharibika,” alisema Maganga kimoyomoyo, akiwa amelala kitandani huku dripu ikiwa imening’inia pembeni yake, iliyojaa maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye mishipa ya mwili.



    Wakati Maganga anaugulia maumivu, Sabaya na Maroda walikuwa njiani wakitembea kwa mwendo wa haraka, baada ya dakika chache waliwasili eneo husika. Hawakutaka kuchelewa, walidhamiria kufanya kilichowapeleka. Waliwachukua mateka wote, wakawapanga msitari mmoja, huku wakiwa wamefungwa vitambaa vyeusi usoni, wasione kiendeleacho. Purukushani za hapa na pale, pindi wakiwahamisha, zilizojaa kelele nyingi, ndizo ziliwaharibia mpango walionao, baada ya kelele hizo kuwafikia Havintish na Salidad walipo, wakitafuta sehemu ya kambi ilipo. Pasi kujadili, kule sauti zilikokuwa zinasikika nao walipiga hatua kwa haraka kuzifuata. Hakika! Waliamini, hao ndiyo watu wanaowafuata. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, walilikaribia eneo la tukio na kujidhirishia walichokiamini. Kupitia mwanga hafifu wa moto za kuni zilizokusanywa sehemu moja kisha kuwashwa, uliwasaidia kubaini na kuona kinachoendelea.

    “Haina kupoteza muda, tufanye shambulizi,” alisema Salidad, taratibu akiiweka vizuri bunduki yake katika nyama ya bega.



    Havintish naye alifanya vivyohivyo, mitutu ilinyanyuliwa, lengo likawekwa kati, pumzi ilibanwa, hesabu ilifuatia: moja, mbili, tat... Kidole cha shahada kikawekwa juu na kufyatua risasi. Sabaya na Maroda waliinua majambia yao tayari kwa kuyafikisha mwilini mwa mateka. Mateka nao walikuwa wanalalama kuomba msamaha, waachiwe huru baada ya kubaini wanaenda kuchinjwa mithili ya kuku wa sikukuu.

    “Hatubembelezi, awali mlijifanya wabishi, huu ndio mwisho wenu. Sabaya anza kazi.” alisema Maroda.

    “Hapana, tufanye wote kwa pamoja itapendeza,” Sabaya alitoa wazo.

    “Haya, twende tuhesabu...moja... Mbili... Tat...”











    Siku zilivyozidi kuyoyoma, mzee Tualike na wenzake matumbo yaliwaka moto, roho mkononi, sura zilijaa matuta ya chuki. Kutokupatikana kwa Sabaya na Maroda katika mawasiliano kila walivyokuwa wanawatafuta kulileta taharuki isiyo na mfano. Fikra za ajabu hazikubanduka ndani ya vichwa vyao, na baada ya muda mrefu waliafikiana kwenda eneo husika wakashuhudie kilichojiri. Njia nzima hawakuisha malalamiko wakiwalaumu akina Sabaya kuwa ndio kisababishi. Kwa uharaka waliokuwa wanatembea, hawakukawia kufika. Hali waliyoikuta iliwafanya kujawa kuondokwa na chuki, furaha ilitwaa nafasi na kutawala ndani ya mitima yao.



    Habari za wapi walipo Sabaya na Maroda walizisahau kwa muda, miili ya watu walioonekana kuwa wafu ilibadili fikra. Kila mmoja alijaa tabasamu. Waliona miili ikiwa imetapakaa chini na kuwafanya wastaajabu maajabu hayo.



    Miili iliyokuwa chini haikuwa ya wafu, bali ni ya watu wazima waliomwagiwa damu na kutengenezewa vidonda na majeraha ya bandia ili tu waonekane wameumia baada ya kukombolewa na akina Salidad ambao ni mhasibu wa serikali ya kijiji cha Tuleane na kikosi kazi cha mgambo. Walikombolewa toka mikononi mwa Sabaya na Maroda. Waliojitayarisha kuondoa uhai wao lakini kabla hawajatekeleza azma yao waliwahiwa na risasi zilizotoka kwenye bunduki mikononi mwa Salidad na Havintish. Baadaye walipanga njama itakayoweza kuwavuta wengine waliosalia hasa viongozi wa kundi.



    Namna gani wafanye? Wakaafikiana wote wajifanye wafu, wakati huo miili ya Sabaya na Maroda ilisogezwa pembeni isionekane. Waliamini, kwa namna yoyote watakavyoona kimya pasipo kupata mrejesho wa kile walichoagiza, lazima watoke waliko waende eneo la tukio. Ndivyo ilivyokuwa!



    Tamaa na uchu viliwaponza. Kitendo cha kuinama kiliwarahisishia wale walioko chini kuinuka, wengine ambao walipaswa kutazamwa jukumu lao lilikuwa kuvuta nguo, waende chini zaidi.

    “Haa! Kumbe wazima,” alisikika mmoja wa wale wazee, ambaye ni mzee Kasoyaga. Baada ya kujikuta anavutwa aende chini huku naye akifanya jitihada za kujiokoa kurudi juu. Wakati huo wengine walikuwa bado hawajafikia usawa wa chini.



    Kusikia hivyo, haraka walirudi juu ili wathibitishe walichosikia, bunduki zilikohoa na kuwathibitishia.

    “Kuanzia sasa mpo chini ya ulinzi,” alisema Havintish, wakati akiiweka sawa bunduki yake katika nyama ya bega.



    Walipoa na kulainika mithili ya kuku aliyonyeshewa. Vipi wajiokoe? Walikwishachelewa kwani tayari walishadhibitiwa.

    “Inawezekana vipi?” kila mmoja wao alijiuliza kimoyomoyo baada ya kutambua watu waliowaweka chini ya ulinzi walikuwa miongoni mwa vijana wao waliokuwa wanafanya nao kazi kipindi cha nyuma.

    “Usishangae sana na usifikirie kuhusu hayo yaliyopita kwa sababu yashapita,” alisema Havintish akimfunga pingu.

    “Binti! Ina maana muda ule ulikuwa unatusoma, sio?” aliuliza mzee Tualike wakati kayatoa macho kama kapoteza hela aliyopaswa kwenda kulipa mkopo.

    “Haikuhusu.”



    Pasipo shida, waliingia mikononi mwa sheria. Hasira na chuki waliyoipoteza ilianza kurudi mahali pake. Ila walivyopepesa macho yao kulia kisha kushoto, walibaini kuwa, watu wao walishapotezwa duniani. Mzobemzobe walisombwa kama mizigo ya viazi kwenda nje ya msitu. Walisubiri usafiri ili wapelekwe kituoni.



    Haikuchukua muda mrefu kabla gari ya ofisi kuu kuwasili, walipanda kisha safari ya kuelekea kijijini ilianza. Jinsi gari lilivyokuwa linaendeshwa, dakika kumi na tatu ziliwawezesha kuingia kwenye lango kuu la kuingilia ndani ya uga wa ofisi hiyo na kuegeshwa sehemu ya maegesho. Haraka kwa kificho, walitolewa ndani ya gari, mzee Tualike, mzee Kasoyaga, mzee Kamilius, Jipendekezo na Majungu walichukuliwa hadi ndani ya chumba cha ofisi ya walinzi wa siri wa Mwenyekiti wa kijiji. Wakati huo viongozi wakuu na waandamizi wa serikali na kijeshi wakiwa ndani ya chumba cha mikutano wakijadiliana hatma ya wahalifu waliokamatwa.



    Furaha waliyokuwa nayo pindi wanajadiliana haikuelezeka. Mioyo ilichanua kwa kupata muafaka waliufikia. Wahalifu wote wapelekwe kituoni, na taarifa itolewe kwenye vyombo vya habari.



    Naam! Walifanya walichojadili. Mkuu wa jeshi la mgambo alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari na habari kuifanya kuenea kwa kasi ili jamii nzima waifahamu.



    Taarifa ilivyopamba moto mtaani hakukukalika, iliwavuta watu na kuwakusanya pamoja kuijadili. Kila walioijadili walikuwa na maoni tofauti tofauti.

    “Sababu washaua ndugu zetu, watuletee mtaani huku nasi tuwaondoe.”

    “Hee! Wafanye hivyo. Hawawezi kutuletea ujinga halafu tuwafumbie macho,” walisikika wananchi wenye hasira kali.



    Siku iliyofuata wahalifu wote waliandikishwa maelezo, baada ya hapo walipelekwa mahabusu kusubiri siku ya kupandishwa kizimbani, mbele ya baraza. Mtaani nako wananchi waliapa kuisubiri siku hiyo kwa hamu kubwa, wajionee hatma ya watu hao.



    Kwa utaratibu wa kisheria na katiba ya kijiji haikuruhusu viongozi wakuu wa kijiji hata kama ni wastaafu kushtakiwa. Mabadiliko yalihitajika, ila kuwaweka wahalifu muda mrefu mahabusu pasipo kuwapeleka bazarani ilikuwa ni kosa pia. Wafanye vipi? Wajadili ofisi elekezi hivyo vifungu vibadilishwe?



    Kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba ilitangazwa. Serikali ilitoa fursa kwa wananchi, wapige kura hiyo.

    “Hili zoezi lifanyike haraka mno, ikiwezekana ndani ya wiki moja tu liwe lishakamilika,” alisema Bi. Mwema akiongea na wanakamati wa zoezi hilo ofisini kwake.

    “Hakuna shida, Mkuu. Tutajitahidi, ikibidi likamilike kabla ya muda uliotupatia.”

    “Itakuwa vyema sana. Na kwa namna yoyote, jibu ninalohitaji ni moja tu, iwe isiwe nahitaji kura ya ushindi.”

    “Tumekuelewa kiongozi.”



    Wakati viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali wanafikiria ushindi wa zoezi walilolianzisha, upande wa mzee Tualike, hasa wawakilishi walioko ndani ya ofisi elekezi, nao hawakusita kukutana kuangalia namna ya kuwasaidia viongozi wao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sheria haiwaruhusu kukaa muda mrefu mahabusu, hivyo tuhakikishe tunasimamia hapa, kuwakomoa hawa watu, lazima tuwalazimishe wapelekwe barazani.”

    “Yeah! Hawana namna ya kutoka, wamekurupuka sana.”

    “Sahihi kabisa, haina haja ya kukaa kimya, nauona ukombozi wa viongozi uko mikononi mwetu.”

    “Ila si nasikia kura ya maoni inapelekwa kwa wananchi?”

    “Ongea ukweli!”

    “Ndiyo hivyo. Wameona wakileta ndani ya ofisi elekezi hawatashinda hicho kitu chao, hivyo wameamua moja kwa moja kupeleka kwa wananchi wafanye maamuzi. Kwa hivi watashinda, sasa tunafanya vipi kurudisha nyuma hizi jitihada?”

    “Ni vikao tu vya kuwashawishi wananchi wasikubaliane.”

    “Hapo umenena.”



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog