Search This Blog

Friday, November 18, 2022

MUHANGA WA MAPENZI - 5

 





    Simulizi : Muhanga Wa Mapenzi 
    Sehemu Ya Tano (5)




    ***

    Baada ya mkuu wa polisi kuondoka Rachel alifunga mlango na kusimama nyuma ya mlango na kupumua pumzi ndefu akiwa ameuegemea mlango, kisha alitoka taratibu hadi kitandani ambako palikuwa patupu. Aliamini Athuman akijificha bafuni kwa woga wa kukamatwa.

    Lakini hakumuona ilibidi amwite.

    “Sweet upo wapi?”

    Lakini hakukuwa na jibu alijiuliza Athuman atakwenda wapi au ameruka dirishani bado hakuamini kutokana na dirisha kuwa limefungwa kwa ndani. Alizidi kuita huku akimtoa hofu mpenzi wake.

    “Sweetie hakuna tatizo upo wapi?”

    Athuman alitoka uvunguni akiwa ametokwa na haja ndogo bila kujielewa, Rachel baada ya kumuona Athuman kwenye hali ile aliangua kicheko.

    “Athuman mpenzi wangu ni uoga gani huo?”

    “Rachel we sema tu, ungejua kipigo walichonipiga siku ile ya kwanza kukuta nyumbani kwangu asingesubutu kunicheka badala ya kunionea huruma. Wale watu wanapigia sifa utafikiri wanaua nyoka, basi tu nakupenda lakini kwa kipigo cha siku ile hata kukusogelea nisingekusolegea wacha leo tunalala kitanda kimoja.”

    “Kwa taarifa yako leo nimewatolea uvivu sijui kama watatufuata tena mkuu wa polisi nimempa makavu anashindwa kumlaza mkewe anafuata kuharibu starehe za watu,” Rachel alisema kwa kujiamini.

    “Nimekusikia lakini nilidhani watakupiga.”

    “Waanzie wapi, kwa taarifa yako hakuna mtu wa kutugusa hata tukifanya kosa.”

    “Mmh, sawa lakini baba yako akirudi si ataniua?”

    “Hawezi, nitapambana naye mpaka atua ya mwisho.”

    “Lakini kumbuka yule ni baba yako?”

    ”Athuman hebu tuachana na wajinga wale tule raha zetu,” Rachel alibadili mazungumzo.

    Walizima taa yenye mwanga mkali na kuwasha yenye mwanga hafifu, Rachel alimvutia kifuani Athuman taratibu walilala pamoja.



    ***

    Mzee Mulisa baada ya mkuu wa polisi kukata simu aliwapigia vijana wake kuwauliza nini kimetokea.

    “Eti kuna nini, mbona mkuu wa polisi kanijibu maneno mazito?”

    “Bosi weee acha tu, mwanao mkorofi sana kamtukana mtu mzima kama mtoto mdogo hata maneno ambayo hakutakiwa kuyasema kwa kweli kamdhalilisha sana.”

    “Mmh!” mzee Mulisa aliguna.

    “Kibaya zaidi kamtishia kazi yake na kumwambia kama atamkamata mpenzi wake watafikishana mbali.”

    “Ni kweli kasema hivyo?”

    “Ndiyo mzee.”

    “Amekuoneni?”

    “Hapana, kwa nini mzee tusimfanyie huyo kijana kwani kuna nini kumpoteza katika ramani ya dunia?”

    “Nooo, waacheni wala usimgumse namjua vizuri mwanangu anaweza kuwaweka katika wakati mgumu. Huyu mtoto sasa ameshindikana, sasa fanye hivi ondokeni hapo mara moja kabla hajawaona,” Mzee Mulisa aliwataka vijana aliowatuma waondoke mara moja eneo lile.

    “Kwa nini mzee tuondoke tutaweza kufanya mambo kitaalamu bila yeye kujua,” vijana walitoa ushauri.

    “Hata kama mtafanya kitaalamu kiasi gani lazima atajua ni mkuu wa polisi anaweza kwenda mbele zaidi na kuwafanya muwe kwenye wakati mgumu.”

    “Sawa mzee kwa vile tumeisha lipia tutaondoka kesho asubuhi.”

    “Nimesema ondokeni muda huu sitaki kubishana na mbwa,” mzee Mulisa alifoka. Ilibidi watu aliowatuma waondoke usiku ule ule japokuwa muda ulikuwa umekwenda sana.

    ********

    Rachel alirudi nyumbani kwao siku ya pili majira ya saa tano asubuhi, alipoingia alimkuta mama yake amekaa sebuleni, alipita na kumsalimia kisha alielekea chumbani kwake. Alipopiga hatua mbili mama yake alimwita.

    “Rachel.”

    “Yes mamy.”

    “Unatoka wapi?”

    “Tulikwenda Bagamoyo rafiki zangu tukalala hukohuko kutokana na muda kwenda.”

    “Rachel usinifanye mtoto mdogo, niambie ukweli jana ulikuwa wapi?”

    “Bagamoyo mama.”

    “Ulikuwa unafanya nini?”

    “Nilikuwa kwenye pati na wanafunzi wenzangu,” Rachel alikuwa akidanganya kitoto.

    “Joy alikuwepo?”

    “Hakuwepo.”

    “Pati ile anaijua?”

    “Haijui.”

    “Unajua habari zako nimezipata toka kwa baba yako kuwa ulikuwa na mwanaume Bagamoyo.”

    “Yule ni rafiki yangu ambaye baadaye atakuwa mume wangu,” Rachel alijibu kwa kujiamini.

    “Rachel unajua unazungumza na nini?”

    “Na mama yangu mzazi.”

    “Kwa nini sasa unakosa adabu?”

    “Mama sio kukosa adabu bali kukueleza ukweli ulivyo au ulitaka nikudanganye?”

    “Si unajua baba yako hataki tabia hizo?”

    “Ni kweli kwa vile nimemaliza mtihani nimechagua kuolewa badala ya kuendelea kusoma.”

    “Rachel baba yako atakuua akisikia upuuzi huo,” mama yake alimtaadhalisha.

    “Aniue kwa lipi, la kukataa kusoma na kuolewa si ni yeye alisema mtu akitimiza miaka 18 ana haki ya kujichagulia maisha kwa vile ana umri wa mtu mzima mwenye kutambua mazuri na mabaya?” Rachel alitetea hoja yake.

    “Yote haya niliyajua, baba yako aliyataka kwa kukudekeza kama yai na kutaka maisha ya kizungu, mimi tena simo mtajuana na baba yako,” mama Rachel alijitoa.

    Rachel hakusubiri mama yake azungumze mengine aligeuka na kuelekea chumbani kwake akimuacha mama yake kashika tama.





    Siku zote mzee Mulisa baba yake Rachel alikuwa akitaka mwanaye aishi maisha ya kizungu hata kuvaa nguo za nusu uchi ambazo mama yake alimkanya lakini baba yake alimkataza mkewe kuingilia uhuru wa mtoto wa vile ameisha kuwa mtu mzima. Maneno yale yalimpa kichwa Rachel kufanya mambo yake bila mama yake kumuingilia huku baba yake akichelelea na kumuona mtoto wao yupo sawa.

    Hali ile ilimweka mama Rachel kwenye wakati mguymu wa kumuonya mtoto wao kutokana na kupewa uhuru na baba yake. Siku zote baba Rachel alipokuwa akitoka Rachel alifanya mambo yake bila woga kwa kujua mama yake hawezi kumwambia chochote.

    Mzee Mulisa alikuwa akimpenda sana mwanaye ambaye alikuwa wa pekee kuhakikisha utajiri alionao aishi nusu ya maisha ya peponi.

    ****



    Baada ya wiki mbili mzee Mulisa alirudi toka katika safari zake, bahati mbaya hakumkuta Rachel alikuwa Mikumi na Athuman katika mbuga za wanyama. Vijana wake walimjulisha yupo wapi, kwa hasira baada ya kutua alikodi ndege hadi mbuga ya Mikumi alipofika alikwenda hadi mapokezi na kumuulizia Rachel.

    Alielekezwa yupo mbugani anaangalia wanyama na mpenzi wake, hakuwa na haraka alisubiri kwa muda wa masaa mnne akiwa amefura kama kaumuliwa na amila.

    Majira ya saa kumi na mbili walirudi kutoka mbugani, baada ya kuteremka kwenye gari walishikana kimahaba kielekea hotelini walipopanga kwa mapumziko ya siku mbili.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzee Mulisa aliwaona wakiteremka kwenye gari wakiwa wamekumbatiana, hasira zilimpanda alitamani akamrukie Athuman na kumtafuna mbichi. Walipokaribia mlango wa kuingia hotelini Athuman alikuwa wa kwanza kumwona mzee Mulisa alitaka kutimua mbio lakini alishindwa kujitoa kwenye mikono yaRachel aliyekuwa amemkumbatia kwa nguvu kiunoni akiwa amemlalia kifuani.

    Mzee Mulisa nguvu zilimuishia na kubakia akitumbua macho, kitendo cha Athuman miguu yake kuwa mizito na kushindwa kutembea kilimshtua Rachel na kutaka kujua kulikoni kuwa katika hali ile.

    “Athuman vipi mbona hutembei umechoka nini?” alimuuliza huku akimtazama usoni.

    Athuman alimjibu kwa macho kumuonesha alipokuwa amejaa tele mzee Mulisa kama Malaika mtoa roho. Rachel alishtuka kumuona baba yake kitu ambacho hakukitegemea.

    Alimuachia Athuman na kumkimbia baba yake na kwenda kumrukia.

    “Ooh, Dady siamini hii ni surprise kwangu, umerudi lini Dady?”

    Mzee Mulisa alibakia kimya akikapua macho kama kafumaniwa akifanya mapenzi na mnyama. Hali ile ilimshtua Rachel kutokana na hali aliyoonesha baba yake.

    Wakati huo Athuman haja ndogo na kubwa zilitaka kutoka kwa pamoja kwa kuamini kile kilikuwa kiama chake kama amekutwa live akiwa na mtoto wa tajiri aliyetishia maisha yake. Watu alioongozana nao walimfanya awe kwenye hali ngumu kutokana na kuwa na miili mikubwa ya mazoezi.

    Rachel alijua Athuman yupo kwenye hali gani pia alijua hata baba yake alikuja kule baada ya kusikia yupo na Athuman aliamini kama atakaa kimya atakuwa katika wakati mgumu.

    Alijitoa muhanga kwa baba yake ili kujionesha alichokifanya akikuwa siri au kumvizia baba yake asafiri.

    “Sweetie njoo uonane na baba yangu mzazi.”

    Athuman alibakia bado amesimama kama amebandikwa gundi kwa woga wa kumuogopa mzee Mulisa baba yake Rachel. Mzee Mulisa bila kusema neno alimshika mkono mwanaye na kuelekea kwenye ndege ili waondoke.

    “Baba na rafiki yangu?” Rachel alimuuliza baba yake.

    Baba yake hakumjibu alimshika mkono hadi ndege ilipopakiwa na kumuingiza kisha walinzi wake na ndege kuondolewa kurudi Dar wakiumuacha Athuman peke yake ambaye aliona ajabu baba Rachel kuondoka bila kumfanya chochote.

    Kama kungekuwa na sehemu ya kuruka toka kwenye ndege basi Rachel angeruka kurudi kwa Athuman, kitendo kila kilimuudhi sana na kuanza kulia safari nzima.

    Walipofika walielekea nyumbani mara moja na kutolewa amri Rachel hatakiwi kutoka nje ya nyumbani kwao.

    Athuman alirudi hadi hotelini akiwa hajiamini kuachwa salama bila hata kupigwa kibao aliona maajabu. Siku ile alilala pale na siku ya pili alirudi jijini Dar huku akijiuliza nini hatima ya maisha yake na mapenzi yake na Rachel.

    Wakati huo mpenzi wake Rachel aliwekewa mlinzi kwa kutembea naye sehemu zote ambazo atakazo elekezwa, kitendo kile kilimuudhi sana Rachel na kupanga mpango kabambe wa kukutana na Athuman.

    Mzee Mulisa alipanga mpango wa kumpoteza Athuman bila mtu yeyote kujua kifo chake kiwe cha kawaida, aliwaita vijana wake na kuwaeleza watafute njia ya kumpoteza Athuman bila mtu yeyote kutilia mashaka kifo chake.

    Rachel kama kawaida yake kila siku usiku alitoroka na kwenda kwa Athuman na kula raha zao mpaka usiku wa manane urudi kwao. Mtindo ule uliendelea bila wazazi wake kujua.

    Vijana wa mzee Mulisa walipanga kumchukua Athuman usiku wa manane na kwenda kumuulia pembeni ya bahari ili ionekane kama amekufa maji. Majira ya saa sita usiku wakiwa wapo karibu ya nyumba anayoishi Athuman tayari kuvamia. Waliona teksi ikisimama mbele ya nyumba ya Athuman.

    Walipoangalia vizuri hawakuamini macho yao kumuona mtoto wa bosi wao Rachel akiteremka kwenye teksi ile baada ya kulipa nauli gari iliondoka na yeye kuingia mule ndani, kila mmoja alimtazama mwenzake. Ilibidi mmoja aulize.

    “Jamani yule si mtoto wa bosi?”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    “Ndie yeye.”

    “Sasa jamani hii si picha ya Kihindi, bosi si alituhakikishia amemwekea ulinzi mkali?”

    “Hata mimi nashangaa.”

    “Sasa tutafanyaje kazi? Si unajua akishuhudia tunamteka anaweza kuharibu kila kitu.”

    “Joe hukuwepo Mikumi yule mtoto balaa ni mkorofi sana, kibaya baba yake anampenda sana. Si tulikwenda mbuga ya Mikumi kumfuata mshikaji, kabla ya kuwaona mzee aliapa kummwaga ubongo jamaa lakini alipotokea na binti yake aliishiwa nguvu kwa binti kumtambulisha jamaa kwa mzee.”

    “Patamu hapo, ikawaje?” Jamaa walijikuta wakitaka stori kwanza badala ya kufanya kazi iliyo wapeleka.

    “Mzee alimshika mkono binti yake na kumpeleka kwenye ndege na kuondoka naye.”

    “Na jamaa?”

    “Tulimuacha hukohuko.”

    “Hayo nimeyasikia, sasa ya hapa itakuwaje?”

    “Hapa hakuna ujanja ni kumjulisha mnene tujue tufanye nini si unajua mnene anataka tumalize kazi hii kabla ya kuondoka tuwe tumempoteza huyo kinyago kwenye sura ya dunia.”

    “Na kweli unajua jibu atakalotoa litatuisaidia tufanye nini, si unajua hataki binti yake tumguse.”

    Waliamua kumpigia simu bosi wao mzee Mulisa kumjulisha Rachel ameonekana akiingia kwa Athuman. Mzee Mulisa aliyekuwa usingizini na kuamshwa na simu yake, hakuamini alichosikia kabla ya yote alinyanyuka kitandani kwake na kwenda chumba cha mwanaye ili ajue kuna ukweli gani na aliyoambiwa na vijana wake.

    Mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, alijaribu kugonga kwa nguvu hakukuwa na jibu lolote toka ndani. Alitoka hadi nje na kumuomba mlinzi apande juu na kuingilia dirishani apate uhakika kama kweli Rachel hayumo ndani.

    Mlinzi alirudisha jibu kuwa ndani hakuna mtu, aliufungua mlango kwa ndani kumfanya mzee Mulisa kuweza kuingia chumbani kwa Rachel, naye alizunguka kila kona hakumuona. Alikubaliana na vijana wake huenda kweli Rachel yupo kwa Athuman.

    Alirudi hadi chumbani kwake na kumuasha mkewe ambaye alishangaa kusikia Rachel hayupo.

    “Jamani mbona huyu mtoto ana balaa,” mama Rachel alishangaa.

    “Yaani huyu kijana sijui nimfanye nini?” mzee Mulisa aisema huku akibadili nguo.

    Usiku ule ule waliondoka pamoja kuelekea anapokaa Athuman muda ulikuwa unakimbilia saa tisa za usiku. Waliongozana hadi nyumba aliyokuwa akikaa Athuman. Akiwa na vijana wake wa kazi waligonga mlango.

    Rachel kabla ya kuitika alichungulia na kumuona baba na mama yake wakiwa na mmoja wa vijana ambao walikuja kwa kazi moja ya kumshikisha adabu Athuman. Kwanza alishtuka kwa kusema kwa sauti ya woga.

    “Ha! Baba?”

    “Mungu wangu leo nimekwisha.” Athuman alisema kwa hofu.

    “Usihofu kazi yote niachie mimi, nitapambana nalo mpaka kieleweke,” Rachel alimtoa hofu mpenzi wake.

    “Sasa itakuwaje?”

    “Nawafungulia mlango,” Rachel alisema.

    “Usifungue, wataniulia ndani,” Athuman alijitetea kwa kumuhofia mzee Mulisa.

    “Haguswi mtu leo,” bado Rachel alijiweka mbele.

    Baada ya kusema vile Rachel alifungua mlango na kukutana uso kwa uso, mama yake alishtuka kumuona mwanaye akitoka akiwa amejifunga upande wa kanga.

    “Ha! Rachel?”

    ”Ni mimi mama karibuni,” Rachel alisema bila wasi.

    “Haiwezekani lazima nimmwage ubongo mwanaharamu huyu.”

    Mzee Mulisa alisema huku akitoa bastora mkononi na kutaka kuingia ndani kwa nguvu.

    “Kabla ya kumuua mpenzi wangu niueni kwanza mimi,” Rachel alisimama mbele ya baba yake kumkinga Athuman.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mume wangu punguza hasira kama hasara tumeoshaipata, na siamini kama Rachel atasoma, kwa tukio la leo inaonesha kabisa mtoto wetu kakubuhu zaidi ya hapo ni kunitafutia matatizo makubwa.

    Kwa ushauri wangu kama imefikia hatua ya kutoroka usiku wa manane hatuwezi kumdhibiti tena tumkubaliane na akitakacho,” mama Rachel alimwambia mumewe.

    “Ina maana tumuoze kwa maskini huyu?” Mzee Mulisa alisema kwa hasira.

    “Eeh, ndiyo mwanao kampenda, nina imani nyuma yao kuna matukio mengi ili kuyafunika na kuibariki ndoa yao, tukiyaacha yatatuchafua.”

    Hakukuwa na jinsi mzee Mulisa ilibidi awe mpole kutokana na maelezo ya mke wake, walimchukua Rachel bila kufanya lolote na kurudi naye nyumbani kwao. Siku ya pili Rachel aliwekwa chini na wazazi wake na kukubalia kumtambua Athuman kama mkwe wao na kupanga siku ya kuja kutambuliwa na familia ya mzee Mulisa. Rachel alifurahi baada ya kuona ndoto yake imekuwa kweli.

    ***

    Siku ya pili mzee Mulisa alifika nyumbani kwa Athuman na kumkuta ndio anajiandaa kutoka, hakuwa na wasiwasi tena baada ya kuhakikishiwa usalama wake kwa kuhurusiwa kumuoa Rachel.

    “Karibuni,” Athumani alimkaribisha mzee Mulisa.

    “Asante.”

    “Shikamoo baba.”

    “Marahaba za hapa?”

    ”Nzuri tu, Rachel hajambo?”

    “Naimani hajambo.”

    “Sijui baba mnatumia kinywaji gani?” Athuman alimuuliza mzee Mulisa.

    “Asante tumetoka kunywa sasa hivi.”

    “Ndio baba, naona asubuhi asubuhi.”

    “Kuna kitu kimoja nataka kuzungumza na wewe.”

    “Kitu gani hicho?”

    “Kuhusu Rachel.”

    “Amefanya nini?”

    “Ni hivi kijana unajua nina malengo makubwa sana kwa binti yangu hasa katika elimu, sio kwamba nataka kuingilia mapenzi yenu bali nilikuwa nataka muda kidogo ili niweze kumsomesha kisha hapo ruksa kufunga naye ndoa nami nitaghalamikia kila kitu.”

    “Kwa hilo baba, mimi sina pingamizi,” Athuman hakuwa na kipingamizi.

    “Sasa nilikuwa naomba msaada wako mmoja na tukikubaliana sasa hivi nitakupa kiasi chochote cha pesa ukitakacho cha kuanzia nitakupa milioni 50 ukitaka zaidi nitakupa kwa vile fedha kwangu si tatizo.”

    “Msaada gani huo baba?”

    “Nataka uachane na Rachel kwa wewe kumkataa, ukifanikiwa kulivunja nitakuongezea ishirini zingine zifike milioni 70.“

    Baada ya kusema vile alimtuma kijana mmoja kwenye gari lake na kurudi na pesa hizo, baada ya kupewa mzee Mulisa alimkabidhi Athuman na kumweleza.

    “Nategemea msaada wako.”

    Athuman hakusema kitu, baada ya kuzitoa milioni 50 mzee Mulisa aligeuka na kuondoka akimuacha Athuman amepigwa butwaa





    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Athuman alijawa na mawazo mengi juu ya taarifa zile ambazo hakuzitegemea alijiuliza wazazi wa Rachel walikuwa na maana gani kufanya vile. Alijiuliza kama atakubali kuvunja uchumba na Rachel ambaye alijitoa kwake na kukubali kila kitu kwa wazazi wake ikiwa pamoja na kuwavunjia adabu.

    Alijiuliza tena kuhusiana na pesa alizopewa milioni 50 kwa ajili ya kuvunja uchumba wake na Rachel ili aendelee kusoma. Aliamini kabisa Rachel asingesoma kama angemkataa zaidi ya kufanya jambo zito la kunywa sumu.

    Alijua kabisa kama Rachel atajiua kwa ajili yake uhasama utakuwa mkubwa hata mzee Mulisa kumuua kwa risasi ili kulipa kisasi cha kifo cha mwanaye. Pia kukaidi amri ya mzee Mulisa ingemtia matatani hata kumsababishia kifo.

    Kila alilolifikiria kwake lilikuwa zito aliamini wazo lile bora alifikishe kwa mama Rachel amsikilize na yeye anasemaje.

    ****

    Siku ya pili alikwenda hadi nyumbani kwao Rachel bahari nzuri alimkuta mama peke yake, Rachel alifurahi kumuona kwao alinirukia na kunipiga mabusu mbele ya mama yake bila woga kuonesha jinsi gani mtoto wa kike alivyopagawa kwa Athuman.

    “Karibu baba,” mama Rachel alimkaribisha Athuman kwa heshima zote.

    “Asante, shikamoo mama za hapa?”

    “Nzuri tu baba, Rachel mletee kinywaji mgeni.”

    Rachel aliondoka na kufuata kinywaji bila kumuuliza mgeni ilibidi mama Rachel amuulize mwanaye.

    “Rachel mbona umeondoka bila kumuuliza mgeni anatumia kinywaji gani?”

    “Mama naye mtu na chake, nisipojua mimi nani mwingine atajua.”

    “Haya wapendanao.”

    Rachel alijibu huku akielekea kwenye friza, mama yake alitabasamu na kumgeukia Athuman na kumtania.

    “Baba umemlisha nini mwanangu haoni asikii juu yako?”

    “Nimlishe nini basi nyota zimeoana.”

    “Mmh! Sawa.”

    Baada ya muda Rachel alileta sinia la vinywaji iliyokuwa na glasi tatu, zilizojaa juice.

    “Karibu mpenzi,” alipiga magoti mbele ya Athuman na kumfanya mama yake achekelee moyoni kwa kitendo kile cha heshima aliyopewa Athuman. Kwa mama yake alishangaa hakuwahi kukifanya kile hata kwa baba yake mzazi.

    “Mmh! Mwanangu adabu ya woga hiyo.”

    “Mamaa! Mume lazima aheshimiwe.”

    “Mbona, baba yako hujamfanyia hivi?”

    “Mama kwa Mungu anatambulika mume si baba, ndio maana walisema mwanamke ataachana na wazazi wake na kuambatana na mumewe ambaye ndiye wataungana na kuwa mwili mmoja,” Rachel alishusha mistali ya Biblia.

    “Mmh! Sikuwezi.”

    Baada ya kumgawia kila mmoja kinywaji chake Rachel alikaa pembeni ya Athuman na kuanza kumnywesha juisi.

    “Rachel, tulia basi nizungumze na mgeni.”

    “Sawa mama mkiona hivi basi muharakishe harusi mume mtamu mama.”

    “Haya basi mpe nafasi nizungumze naye kisha nitakuacheni mmalize hamu zenu, mhu baba”

    Athuman kabla ya kuzungumza alishusha pumzi na kuonekana kuna jambo linamtatiza, kitu alichokigundua mama Rachel.

    “Baba kuna kitu najua unataka kuzungumza au cha wawili?”

    “Ni kweli mama.”

    “Athuman ni kitu gani mimi sitakiwi kukijua?” Rachel aliingilia kati mazungumzo yale.

    “Hapana mpenzi kuna kitu nataka kuzungumza na mama kisha nitazungumza na wewe.”

    “Sawa, mimi sifai” Rachel alisema huku akitaka kulia.

    “Hapana Rachel, hebu muache mwenzio azungumze kisha nawe utaelezwa.”

    Rachel aliondoka kwa shingo upande.

    Baada ya kuondoka mama Rachel alimgeukia Athuman na kumuuliza kilichompeleka pale.

    “Mhu, baba ulikuwa unasemaje?”

    Baada ya kuvuta ujasiri alisema kwa sauti ya upole jinsi baba Rachel mzee Mulisa alivyompelekea milioni 50 ili aachane na Rachel.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama, mimi naweza kufanya hivyo, si uamuzi wa kumwambia mimi na wewe basi, lakini mnajua madhara yake?”

    “Mmh! Baba mimi ndio nasikia kwako, unayosema ni kweli?”

    “Kweli kabisa mama.”

    “Na hizo pesa zipo?”

    “Zipo toka jana nilipopewa sijazigusa zimo ndani.”

    “Mmh! Sasa shida yake nini?”

    “Niachane na Rachel.”

    “Mbona mume wangu ana mazito, hajui kama siku utakayo mtamkia Rachel basi ujue na uhai wake siku hiyo ndiyo utagota. Haya ninayo yaona kwa Rachel jinsi alivyochanganyikiwa kwako umwambie mwanangu humtaki si ndio kumpoteza.

    Lakini kwa nini mume wangu ananila kisogo yote haya yamefika hapa kwa ajili yake bado anafanya kitu kujua.

    “Baba nakuomba usimtamkie mwanangu neno hilo hata siku moja nipo radhi kukupa zaidi ya hizo kuhakikisha maisha ya mwanangu yanakuwa ya furaha.”

    “Mama, pia naogopa pindi nitakapo kaidi amri ya mzee maisha yangu yatakuwa hatiani kwani nina imani hapendi mimi kuwa na Rachel. Nakuapia mama kama sio vitisho vya Rachel ningekwisha achana naye lakini amenionesha mapenzi ya kweli na kujitoa muhanga kwa ajili yangu leo hii nimtose, hata kidogo siwezi heri nife kuliko kumpoteza Rachel.”

    “Ni kweli mwanangu siku zote sisi wanawake tuna roho kama ya kuku hatuwezi kuvumilia, uamuzi wetu siku zote ni kujiua kwani huamini ndio njia ya kutatua matatizo.”

    “Basi mama huo ndio mtihani ulio mbele yangu, ningekuwa na tamaa mbona wala nisingekuja kuwaeleza ningechukua hela na kumueleza Rachel mimi na yeye basi angenilazimisha? Lakini naheshimu mapenzi yake kwangu pia uhai wake ni muhimu kuliko milioni 50.”

    “Ni kweli baba, umeonesha jinsi gani ulivyoiva kiakili unamshinda hata baba yenu, milioni 50 zinatafutwa na kupatikana lakini si uhai wa mwanangu.”

    “Sasa mama ulikuwa unanishauri nini?”

    “Mwanangu nimekusikia kazi hiyo niachie mimi, hizo milioni 50 usizirudishe ni asante yako kwa moyo wako wa ujasiri angekuwa mwengine asingefanya haya. Ningempoteza mwanangu hivihivi, narudia nasema asante nenda kwa amani usihofu kitu chochote nakuahidi mimi kama mama yake Rachel lazima utamuoa kwa dini yeyote.”

    Baada ya mazungumzo aliitwa Rachel ili aagane na Athuman, Rachel alitokea akiwa amevimba macho kwa kulia kitu kilichomshtua kila mmoja.

    “Rachel mpenzi nini tena?”

    “Mama ni jinsi gani wazazi wangu msivyo nipenda mnanunua uhai wangu kwa milioni 50, mama kweli kabisa mimi sina thamani kwenu, mnajifanya mnanipenda kumbe waongo...Siamini ...siamini,” Rachel alisema huku akilia kuonesha aliyasikia mazungumzo yale.









    “Mwanangu hata mimi sipo tayari kukupoteza,” mama yake alijitetea.

    “Athuman...Athuman mpenzi, leo ndio nimeamini kweli unanipenda na kujitoa muhanga kwa maisha yangu. Asante sana Athuman Mungu atakulipa hata nikifa nitendelea kukupenda na kuamini kweli wewe ulikuwa na mapenzi ya kweli na mimi.”

    “Rachel nathamini upendo wako nilijiapiza moyo wangu toka nilipojua mapenzi yako kwangu ni ya kweli na kujitoa muhanga kwa ajili yangu. Nakuahidi kwa mara nyingine mbele ya mama, ni kifo pekee ndicho kitakacho tutenganisha si fitina za watu.”

    Rachel alijitupa kifuani kwa Athuman kitu kilichomfanya mama Rachel kuwaacha wamalize hamu zao kwa upana zaidi. Baada ya kuondoka Rachel aliendelea kumshukuru Athuman.

    “Athuman wewe ni mume niliyeshushiwa toka kwa Mungu, hakuna mwanaume mwingine atakaye pata nafasi moyoni mwangu. Kwa ulichokifanya juu yangu mimi nitafanya mara mbili yako. Asante Athuman nimeamini nilipoangukia sikukosea sikugusa chini,” Rachel aliendelea kumshukuru mpenzi wake.

    “Rachel wewe ni mwanamke wa ajabu upendo wako umenifunduisha vitu vingi, upendo wako umenijaza ujasiri na kuweza kukabiliana na chochote kijacho mbele yangu. Wewe ni msichana wa ajabu wenye msimamo na mwenye kutetea hoja zako. Nakupenda sana Rachel.”

    “Asante, hata mimi nakupenda, leo iwe isiwe lazima nije nilale kwako.”

    Baada ya kupozana mioyo Athuman aliaga na kuondoka.

    ***

    Mama Rachel alimsubiri mumewe kwa hamu kubwa ili amweleze sababu ya kutaka kusababisha mauti ya mtoto wao. Muda ulipotimu mumewe alirejea nyumbani kama kawaida ajabu aliikuta hali si ya kawaida. Mkewe hakuwa na furaha kama kawaida Rachel naye alionekana kama mgonjwa macho yalikuwa yamemvimba kwa kulia.

    “Jamani kuna usalama, eti bebiii?” Alimgeukia mwanaye aliyekuwa amejilaza kwenye kochi, Rachel hakumjibu kitu alimuangalia bila kumsemesha wala kumjibu.

    “Eti mke wangu, kuna nini?” Wazo lake lililenga huenda Athuman amemuacha Rachel, moyoni aliamini alichotaka kukifanya kimefanikiwa.

    “Mmh, kawaida tu,” mkewe alijibu bila kuonesha uchangamfu.

    “Lakini hapa kuna kitu si bure macho ya Rachel hayaoneshi dalili nzuri.”

    “Si ndiyo uliyoyataka,” mama Rachel alijibu.

    “Lakini mimi nafikiri kilichotokea ni kitu cha kawaida kinachotakiwa ni kwa Rachel kujikita kwenye elimu, nami nakuahidi mwanangu kukupatia kila utakacho.”

    Mzee Mulisa alizungumza bila kuelewa alichokuwa akikizungumza, Rachel ambaye alikuiwa amejaa jazba alisema kwa hasira.

    “Baba unajifanya unanipenda kumbe muongo mzandiki, unanunua uhai wangu kwa milioni 50?”

    Kauli ile ilimshtua mzee Mulisa kwani hakutegemea Athuman kutoa siri ile kutokana na kumpa kiasi kikubwa cha pesa. Kabla ya kujibu mkewe aliongezea juu.

    “Mume wangu kwa nini umefanya kitendo cha kinyama cha kutaka kuvunja mapenzi ya mwanao, tuliongea nini na umefanya nini? Hivi furaha yako umkute mwanao amekauka au una mpango wa kumla nyama?”

    “Sivyo hivyo mke wangu bado siamini kama yule kijana ni saizi ya mwenetu, ni aibu kumuoza mtoto wetu atatupa nini? Nia yangu ni kuhakikisha mtoto wetu anaachana na yule kijana kisha anarudi shule.”

    “Mimi na wewe tulizungumza nini tulipomkuta Rachel kwa yule kijana, tulikubaliana kwa vile yule kijana hana uwezo mkubwa lakini mtoto wetu kampenda tumwezeshe ili aweze kuishi na mtoto wetu bila matatizo.”

    “Ni kweli mke wangu, lakini bado nafsi yangu haikubali, yule kijana hawezi kumuoa mwanangu.”

    “Haya sasa hutaki mwanao kesha mpenda!”

    “Kwanza habari hizi umezipata wapi?’

    ”Uliyemueleza, japokuwa kijana mdogo ameangalia mbali na kujua madhara ya kuvunja mahusiano yake na Rachel yangekuwa na madhara makubwa kuliko milioni 50 zako.”

    “Mmh!” aliguna na kukosa neno la kusema.

    “Kweli mume wangu una akili za kushikizwa kama umeweza kumpa milioni 50 na kumuahidi milioni 20 zaidi ili ziwe sabini kwa nini usimpe milioni mia moja afanye kazi yenye kuonekana ili aweze kumtunza mwanao? Lakini unatumia pesa nyingi kiasi hicho kutaka kuutoa uhai wa mwanao.”

    “Mama wala baba asisumbuke si ananiona nimekuwa kero kwake, wala asitumie pesa zote hizo kununua uhai wangu. Basi wacha mimi ninywe sumu ya mia mbili ili nimpunguzie mzigo huenda kuwa kwangu humu ndani ni kero kwake,” Rachel aliingia kati mazumgumzo ya wazazi wake.

    “Hapana Rachel nipo tayari kufanya chochote ili uolewe na Athuman, naomba mnisamehe kwa yote niliyotenda. Nimeamini Athuman anakupenda mapenzi ya dhati,” Mzee Mulisa aliomba radhi.

    “Baba siwezi kukusamehe kwa vile ulichofanya ulifanya kwa siri kama Athuman asingekuwa na upendo wa kweli wa kurudisha milioni 50. Kama asingekuwa na mapenzi ya dhati kwangu ningeachwa kama kina la ndege kwenye upepo ukali na kufa kifo kibaya,” Rachel alimwambia baba yake huku akilia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni kweli nimefanya kosa mwanangu nisamehe sana mwanangu na mke wangu, nimekosa jamani, japo mi mkubwa lakini hutenda makosa na kuhitahi msamaha, aliye sahihi ni Mungu pekee.”

    “Mimi nikusamehe kwa lipi nakuona upo sawa kwa kila ulilofanya, kwa vile umeweza kutoa mamilioni ya pesa ili kuhakikisha unaiua furaha yangu. Bado siamini kama wewe mwenyewe ulikubali kisha umenigeuka ..siamini ..siamini,” Rachel alizungumza kwa jazba huku akiendeleza kilio.

    Mzee Mulisa aliona maji yamefuka shingoni na nguo imemvuka pabaya mbele za watu hakuwa na budi kuchutama kwa mara ya kwanza alimpigia magoti mtoto wake kumuomba radhi.

    “Rachel mwanangu nilifanya yote yale si kwa nia mbaya bali kuyaokoa maisha yako, Athuman ni kijana maskini huwezi kuyatengeneza maisha yako.”

    “Aaah! Unajua unanishangaza sana kama ulijua maskini na umeweza kumpa milioni 50 na ishirini ulitaka kumuongezea ili avunje penzi lake kwangu. Huoni huo ni utajiri tosha kwa nini hukutupa hata milioni 500 ili tuweze kuendeleza maisha yetu bila kukusumbua?” Rachel alimuuliza baba yake.







    “Kwa kweli mwanangu sikuwa na wazo hilo, ili kukuonesha nakupenda na vilevile nakuthamini, nakuahidi kukusimamia kwa kila kitu juu ya ndoa yako na Athuman.”

    “Pamoja na kusema yote hayo bado sikuamini, nakuona unanipaka matope kwa mgongo wa chupa,” bado Rachel hakutaka kumuamini wala kumsamehe baba yake kwa kuamini kutoa milioni sabini ni dhahili alikuwa amedhamilia.”

    “Nifanye nini ili mwanangu uamini nitafanya unacho kifikiria?”

    “Chochote utakacho nifanyia siwezi kukuamini na siwezi kukuamini kamwe,” Rachel alimpa wakati mgumu baba yake ambaye kwa mara ya kwanza alijiona kiumbe mdogo asiyejaa mkononi kwa mwanaye.

    “Mama Rachel mke wangu, naomba basi umueleze mwanao ili aniamini kama sitafanya upuuzi kama huu tena.”

    “Mume wangu kwa kweli mpaka sasa sijapata jibu kwa kile ulichokifanya cha kutuzunguka kumbe una ajenda nzito, hivi unajua vizuri jinsi Rachel anavyo mpenda Athuman halafu leo uwaachanishe. Mume wangu kilio ulichotaka kukiiingiza ndani ungekinyamazisha kwa shilingi ngapi kama ulitaka kukiandaa kifo cha mwanao kwa milinini 70?”

    “Mke wangu jamani mimi ndiye kiumbe cha kwanza kufanya makosa ambayo sisitahili kusamehewa? Hata mimi japo kichwa cha familia nahitaji kusamehewa kama viumbe wengine, natubu jamani nimekosa naomba msamaha wenu nipo chini ya miguu yenu.

    Rachel mwanangu nisamehe mama....Mama Rachel mke wangu nisamehe mpenzi, kama hamtanisamehe basi heri ninywe sumu kuliko kuonekana kiumbe nisiye na thamani kwenu kwa kuniona nafaa wakati wa furaha wakati wa matatizo mnanipa kisogo,” Mzee Mulisa naye alichimba mkwala.

    “Mume wangu kwa kweli ulichokifanya kilikuwa sawa na kufanya kipango ya mauaji ya mwanao bila kujua. Nakuapia kama si ujasiri wa Athuman sasa hivi Rachel tungempoteza japo wewe uliamini ndiyo tiba lakini ulikuwa umefanya mauaji ya bila kukusudia. Lakini hatuna budi kukusamehe kwa vile umetambua kosa lako. Rachel msamehe baba yako,” mama Rachel alimweleza mwanaye.

    “Nimemsamehe,” Rachel alisema.

    Rachel alikumbatiana na baba na mama yake wote kukumbatiana kwa kusameheana na kuyasahau yote yaliyopita.

    ***

    Mzee Mulisa alikubali kwa shingo upande lakini moyoni alipanga kumfanyia kitu kibaya Athumani. Aliona kumuoza mwanaye kwa maskini kama yule ilikuwa sawa na kumpa nguruwe. Alimchukia moyoni kwa kuvuruka mipango yake juu ya mwanaye kwanza kamualibia masomo na kuharibu malengo yake ya kumsomesha mwanaye ili awe na digirii ya uchumi aweze kumkabidhi mali zake aziongoze pindi watakapo zeeka.

    Siri ile aliipanga kuifanya baada ya mwaka mmoja wa ndoa ya mwanaye kwa kumuua Athumani kwa siri bila mwanaye kujua wakati huo akijifanya yupo karibu na familia ile na kutoa misaada mingi huku akipanga kushtuka akipewa taarifa ya kifo cha Athumani kwa kulia mpaka kuzirai ili mkewe ajua kile kifo hausiki nacho.

    Pia alipanga kumpiga mwanaye sindano ya siri ya kuzuia kupata ujauzito ili kipindi chote cha mwaka mzima aweze kumrudisha shule ili afikie alichokipanga.

    Siku ya pili alitumwa Rachel kumfuata Athuman ili aonane rasmi na mzee Mulisa kama mkwewe mtalajiwa. Rachel alimfuata Athumani nyumbani alimkuta amejipumzisha. Alipofika alimrukia huku akipiga kelele.

    “Athumani Mungu mkubwa kasikia kilio chetu.”

    “Vipi kuna nini? Naona una furaha usiyo ya kawaida.”

    Rachel alimweleza yote yaliyojili mpaka kutumwa kumfuata.

    “Rachel unamuamini baba yako?” Athumani alimuuliza mpenzi wake.

    “Kwa mkwala niliompiga hawezi kufanya tena ujinga wake twende akakutambue na kupanga mipango ya ndoa.”

    “Mmh! Kama ni hivyo lazima tumshukuru Mungu kwa kazi yake.”

    “Yaani, naona kama vile tayari tumeisha kuwa mke na mume, Yaani sijui itakuwaje baada ya kufunga ndoa.”

    “Tukipata na mtoto!”

    “Yaani mwanangu nitamlea kama yai.”

    Waliondoka pamoja mpaka nyumbani kwao, walipofika mzee Mulisa alimuomba msamaha Athumani mbele ya familia yake kwa yote yaliyotokea huku akiusifu ujasiri wake ambao aliamini ndiyo uliokoa maisha ya mwanaye kipenzi. Siku ile ilipangwa siku ya harusi.

    Maandalizi yalikwenda vizuri ya harusi baada ya Rachel kusisitiza kubadili dini na wazazi wake kumkubalia. Lakini Athuman hakutaka kuwaudhi wazazi wa Rachel ndoa ilifungwa Bomani kwa kila mmoja kubakia na dini yake na baadaye kufanyika sherehe kubwa kwenye ukumbi.

    Kutokana na kuijua thamani ya elimu Athumani baada ya mwezi alimuomba mzee Mulisa amtafutie mkewe shule ili aendeleze elimu yake na kufikia malengo yake. Mzee Mulisa alishtuka kusikia vile na kujiona mpumbavu kutaka kumtendea mabaya mkwewe ambaye kumbe ana mawazo ya kimaendeleo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara moja alimtafutia Rachel shule na kuendelea na kidato cha tano, Athuman aliendelea kuwa karibu mkewe kwa kumpa moyo mpaka alipohitimu elimu ya chuo na kupata shahada ya uchumi. Siku ya mahafari ya mwanaye kupokea cheti cha kupata shahada ya kwanza ya uchumi mzee Mulisa alilia machozi na kukumbuka nia yake mbaya Athumani. Alijikuta akimpenda mkwewe na kutoa sehemu ya mali yake kwa mwanaye na mumewe.

    Sasa hivi wanaendelea na maisha yao huku Rachel akiitafuta shahada ya pili, maisha ya mke na mume yenye upendo yakiendelea. Na kuendeleza miradi walio achiwa na wazazi wao. Walipanga watafute mtoto baada ya shahada ya pili.





    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog