Simulizi : Yamenikuta Salma Mie
Sehemu Ya Nne (4)
“Nisingekuwa nazo lakini ulipaswa uniambie tu nijue kuwa tunadaiwa”
“Mume wangu nitakuambia madeni mangapi tunayo daiwa? Kila siku ninakwenda kukopa”
“Hizo pesa unazokwenda kukopa mbona sizioni?”
Hapo nikamjia juu
“Huzioni kwani hiki chakula tunachokula humu ndani unafiri nina hawara anayenihonga? Au wewe unanipa pesa yako?”
“Basi mke wangu, haina haja uje juu. Niambie hizo hela unazodaiwa ni shilingi ngapi nikupe”
“Nipe hizo hela zote ulizopewa, mimi mwenyewe ndiyo nitajua nadaiwa kiasi gani na kiasi gani nitabakisha kwa matumizi yetu”
Ibrahim hakutaka makubwa, alitoa zile pesa na kunipa.Nilijua wazi kuwa hakuridhika lakini hakuwa na la kufanya. Nikazichukua zile pesa na kuondoka.
Siku ya pili yake baada ya kunywa chai niliondoka hapo nyumbani bila kumwambia Ibrahim ninakwenda wapi. Nilikwishaamua kutomuaga ninapokwenda mahali kwani sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa mwanaume ambaye sasa amekuwa kama mzigo kwangu.
Saa nne nikawa kwenye kituo cha daladala nikimsubiri yule kijana niliyeahidiana naye. Na yeye alikuwa na ahadi ya kizungu. Alipitisha dakika moja tu kabla ya kuwasili katika kituo hicho cha daladala. Nikajipakia kwenye gari yake tukaondoka.
“Habari za nyumbani?” akaniuliza
“Nzuri. Sijui zako”
“Nashukuru kumekucha salama”
Baada ya hapo ukapita ukimwa wa muda kabla ya kijana huyo kuniuliza.
“Hivi kama mume wako asipopona utafanyaje?”
Lilikuwa swali gumu ambalo sikuwahi kufikiria jibu lake.
“Sijui” nikamjibu.
Nilipomjibu hivyo akanyamaza. Lakini dukuduku likawa limenipata. Nilipomuona yupo kimya nikamuuliza
“Kwanini umeniuliza hivyo? Umehisi kwamba hataweza kuona tena?”
“Nimekuuliza tu kujua mawazo yako lakini usikate tamaa. Endelea kumsilikiza mzee atakavyokuambia” akaniambia.
Tulipofika Kisosora tulikuta wateja kadhaa waliokuwa wakisubiri kuingia kwa mganga. Yule kijana akaniambiahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tuingie tu wewe umeshakuwa mwenyeji”
Tukaingia. Aliniingia kwenye chumba kingine akaniambia nikae kwenye kiti. Nikakaa, yeye akatoka. Baada ya muda kidogo akarudi akiwa na baba yake.
“Shikamoo” nikamwamkia.
“Marahaba. Habari za kwako?” mganga huyo akaniuliza huku akikaa kwenye kitanda kwani hakukuwa na kiti kingine. Yule kijana alibaki akiwa amesimama.
“Mume wako anaendeleje?” mganga akaniuliza.
“Bado hali yake ni ile ile”
“Basi mngeendelea kuwaona madaktari”
“Tumehangaika sana kwa madaktari bila mafanikio. Inawezekana ameshapofuka”
“Kwani mboni zake za macho zimekuwa nyeupe kabisa?”
“Ni nyeusi lakini inawezekana ameshapofuka. Wako watu wenye mboni zao kama kawaida lakini ni kipofu”
“Kwani huyo mwanaume umezaa naye?”
“Hatujapata mtoto”
“Ni miaka mingapi sasa tangu muoane?”
“Inafika miaka mitatu lakini nimeharibu mimba mara mbili”
“Subiani wako ndiye asiyetaka watoto”
“Mimi nina subiani?”
“Ndiyo, ni jini dume. Nilishaliona tangu siku yako ya kwanza ulipokuja kwangu”
“Mimi sijui kama nina jini”
“Si unaota ndoto za kufanya mapenzi na wanaume?”
“Ndiyo, ninaota mara kwa mara”
“Basi ni hilo jini”
“Wakati mwingine ninaota nimezaa kitoto”
“Ndiyo hilo hilo . Usipojishughulikia unaweza usipate mtoto”
“Mume mwenyewe ndiyo yule, huyo mtoto hata nikimpata si atakuja kuteseka bure?”
“Kwani mwanaume ni yeye peke yake?’
“Kwanini?”
“Unaweza kupata mume mwingine mwenye pesa zake”
“Una maana yule niachane naye?”
“Sasa ni akili yako mwenyewe. Kama umeona kuna mwanaume mwenye uwezo wake kipesa anakuhitaji, unaweza kuamua tu lakini inategemea na akili yako mwenyewe. Kama unaona uendelee na mume huyo huyo, mwenye uamuzi ni wewe”
Nikashusha punzi ndefu.
“Babu naona umeniweka njia panda” nikamwaambia yule mzee.
“ Hilo ni suala la kufikiri wewe mwenyewe, mimi ninakushauri tu kwa sababu yupo mtu anatafuta mke wa kuoa na ana pesa. Nimeona anaweza kukufaa”
“Yuko wapi huyo mtu?”
“Yupo. Nenda kafikilie kwanza. Ukiamua kuachana na huyo bwana njoo nitakuonyesha.Yeye yupo tayari kukuoa”
“Atakuwaje tayari kunioa wakati hajaniona?” nikamuuliza.
Mganga akacheka.
“Ameshakuona na amekupenda lakini tatizo ni hilo kwamba una mume”
Hapo nikashangaa kidogo.
“Ameniona wapi?” nikamuuliza yule mganga.
Badala ya kunijibu alicheka kisha akanyanyuka ili atoke mle chumbani.
“Babu mbona huniambii, unatoka?”
Mzee alikuwa ameshafika kwenye mlango akageuka na kuniambia.
“Zungumza na mwenzako, yeye atakuambia”
Aliponiambia hivyo akatoka mle chumbani. Yule kijana akakaa pale alipotoka baba yake.
“Naona baba amekupenda, anataka uwe mkwe wake” kijana huyo akaniambia.
“Anataka niwe mkwe wake kwa nani?” nikamuuliza.
“Mimi nilikuja hapa Tanga kutafuta mke. Kwa kweli siku ile ya kwanza nilipokuona nilikupenda na nikamueleza baba. Akaniambia kuwa una mume wako. Lakini kama nyumbani kwako kuna matatizo twende zetu Dar”
Nikainamisha kichwa changu chini, nusu ilikuwa kwa aibu na nusu kufikilia yale maneno aliyoniambia. Nikawa namtazama kwa kumuiba. Nilimtazama kichwani mpaka miguuni. Kwa kweli alikuwa amevaa nguo za thamani na alionekana mtanashati na mwenye pesa lakini…...
“Mbona uko kimya?” akaniuliza alipoona nimenyamaza.
“Nafikilia hayo maneno uliyoniambia”
“Umeyaonaje?”
“Si wezi kukujibu kwa sasa, acha nikafikirie kwanza”
“Kitakachoendelea kuniweka hapa Tanga kwa sasa itakuwa ni jibu lako”
“Kwani wewe unafanyakazi gani?” nikamuuliza.
“Mimi ni mfanyabiashara”
“Una duka?”
“Sina duka isipokuwa huchukua oda kwa wenye maduka halafu ninakwenda nchi za nje kama vile Dubai au China kununua bidhaa na kuwaletea”
Aliponiambia hivyo niligutuka, nikajiambia kimoyomoyo. “Kumbe huyu kijana ana pesa za maana”
Alichukua kipande cha kioo kilichovunjika ambacho kilikuwa juu ya meza akakiweka mbele ya macho yangu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hebu jitazame mwenyewe ulivyopendeza” akaniambia huku akitabasamu.
Baada ya kujitazama nikalivua.
“Walivulia nini, liache tu”
“Niliache la nini, si niko ndani? Hapo nitakapotoka ndio nitavaa” nikamwambia.
Nikalivua lile juba na kumpa Konda ambaye alilirudisha ndani ya sanduku.
“Sasa ngoja nikutoe nikutambulishe kwa wapangaji wangu. Nina wapangaji wawili humu ndani lakini mwenye mke ni mmoja tu”
Tukatoka ukumbini na Konda. Akawaita ukumbbini wapangaji wake. Aliyekuja alikuwa mpangaji mmojatu na alitokea uani.
“Nimekuita kukutambulisha mke wangu” akamwambia na kuongeza.
“Mke wangu mwenyewe ndiye huyu”
Yule jamaa alinitazama kisha akasema.
“Nimefurahi kumfahamu”
SASA ENDELEA
Nilipoingia ndani nilimkuta mume wangu amekaa sebuleni peke yake. Zacharia hakuwepo.
“Habari ya hapa?’ nikamsalimia.
“Nzuri, mbona umechelewa sana?”
“Nilikwenda huko kwa mama yangu. Kuna mtabibu pale mtaani kwetu amenipa dawa nije nikufanyie”
“Dawa gani?”
“Dawa ya majani. Ameniambia nikufikichie kwenye macho kwa siku tatu”
“Haya tujaribu”
“Ameniambia nikufanyie asubuhi na jioni. Asubuhi imeshapita tusubiri jioni tuanze”
“Unanifikichia vipi?”
Nikamueleza vile nilivyoagizwa na yule mganga.
“Haya utanifikichia tujaribu”
“Amenihakikishia kuwa itakusaidia”
“Lakini haiwashi machoni?”
“Hakuniambia lakini nafikiri haiwashi kama inawasha angeniambia”
Baada ya hapo niliingia jikoni na kuanza kupika. Ile dawa niliitunza mahali pazuri ambapo ingeweza kukaa bila kukauka.
Ilipofika jioni nilichomoa majani matatu ya dawa hiyo nikaenda sebuleni ambako mume wangu alikuwa amekaa nikamwambia alale chini kichalichali ili nimfikichie machoni.
Mume wangu aliondoka kwenye kochi alipokuwa ameketi akasogea mbele kidogo na kukaa chini kisha akajilaza kichalichali.
Nilichutama na majani yangu nikayashika na kuyafikicha kabla ya kumkamulia machoni mwake.
Maji maji yaliyotoka kwenye majani hayo yalipomuingia machoni alifumba macho.
“Usifumbe macho, yafumbue” nikamwambia. “Yafumbue dawa ikuingie vizuri”
Akayafumbua kiuoga.
“Fumbua bwana!”
“Nimeshayafubua”
“Bado, fumbua zaidi”
Macho yake yalikwishakuwa maoga. Alishindwa kuyamfumbua sawa sawa.
Nikamkamulia majani hayo hivyo hivyo. Maji maji machache yalimuingia machoni, mengine yalichirizika kingoni mwa macho na kumwagika chini.
Nilirudia kumkamulia mara tatu.
“Umeshamaliza?” akaniuliza.
“Nadhani imetosha”
Alikuwa anataka kuinuka nikamzuia.
“Ngoja kwanza dawa ikuingie vizuri, una haraka ya nini?”
Akatulia.
Baada ya dakika tatu hivi nikamwambia ainuke. Akainuka na kukaa kwenye kochi.
“Yanawasha?” nikamuuliza.
“Yanawasha kwa mbali”
Nilichukua kitambaa nikamfuta futa yale maji maji yaliyokuwa yamemchirizikia pembeni mwa macho kisha nikaondoka.
Asubuhi nilimfanyia tena, nikarudia tena jioni.
“Vipi, hujaanza kuona ona” nikamuuliza.
“Bado. Naona kiza tu”
“Mganga mwenyewe ameniambia nikufanyie kwa siku tatu”
“Labda mpaka kesho kutwa”
Niliendelea kumfanyia Ibrahim dawa hiyo kwa siku tatu lakini macho ya Ibrahim hayakuona chochote. Siku ya nne yake nikarudi tena kwa yule mganga.
Nilipomueleza nilimuona akikunja uso.
“Bado hajaweza kuona?” akaniuliza.
“Hajaona bado”
Mganga akafikiri kisha akaniambia.
“Njoo kesho nitakupa dawa nyingine”
Nikaondoka. Kwa vile hata zile dawa alizopewa hospitalini hazikuweza kumsaidia, kesho yake nilirudi tena kwa yule mganga. Kwa kweli aliniweka sana. Alipomaliza kuhudumia wateja wake akaniita na kuniambia niende tena kesho kwani hakupata nafasi ya kwenda kunichumia dawa nyingine.
Nikaondoka. Siku iliyofuata Ibrahim alipelekwa hospitali na mdogo wake na mimi nikatoka kwenda kwa mganga.
Nilipofika alinipa dawa ya ungaunga mweusi, akanimbia nichote kidogo niroweke kwenye maji ya vugu vugu kwa dakika moja kisha nimpe mume wangu anawe uso.
“Niroweke kwenye maji ya kiasi gani?” nikamuuliza kwa matumaini.
“Kama nusu lita hivi”
“Anawe uso yote?”
“Ndiyo anawe yote. Unamtilia asubuhi na jioni kidogo kidogo”
“Kwa siku ngapi?”
“Kwa siku tatu”
Baada ya mazungumzo hayo nikaondoka. Nilikuta mume wangu alikuwa amesharudi kutoka hospitali. Alikuwa amepewa dawa nyingine za kutumia kwa siku tatu.
“Na mimi nimekwenda kwa mtaalamu mwingine” nikamwambia.
“Amekwambiaje?”
“Baada ya kumueleza matatizo yako amenipa hii dawa”
“Ni dawa ya aina gani?”
“Ni ya unga unga. Ameniambia nitie kwenye maji ya vugu vugu kisha uoshe uso asubuhi na jioni”
“Kwa sababu tuna shida tutafanya” Mume wangu aliponiambia hivyo niliona huzuni sana.
Tulifanya ile dawa kwa siku tatu bila mafanikio. Zile dawa za hospitali nazo hazikuleta matumaini yoyote.
Kwa vile niliona lile tatizo lilitokea kwa yule mganga nikarudi tena bila kuchoka. Mganga akanibadilishia dawa nyingine. Nazo pia hazikufaa.
Kwa upande wa hospitalini tulimaliza hospitali kadhaa za macho. Mume wangu aliambiwa hawezi kuona tena!
Sasa maisha yetu yalianza kuwa magumu. Mume wangu alikuwa hawezi tena kufanya kazi. Tulikuwa tunakula mtaji. Kusema kweli pesa nyingi zilimalizika kwa uchunguzi na matibabu yake.
Mwisho wake akanimabia anafikiria kuuza ile gari yake ili apate pesa za kuendelea kujitibu. Kulikuwa na watu ambao walikuwa wakimpa moyo kwamba asikate tamaa.
Nikafungua mlango wa gari na kushuka. Nikiwa nje ya gari nilimpungia mkono wa kumuaga na yeye akanipungia.
Nikaondoka zangu. Na yeye akaondka na gari. Nilipitia kwenye bucha ya nyama nikanunua kilo moja ya nyama kisha nikaenda kwenye duka ninalonunulia vitu. Nikanunua kilo mbili za mchele na mahitaji mengine kisha nikarudi nyumbani.
Sebuleni nilimkuta shemeji Zacharia akiangalia Tv. Ibrahim hakuwepo. Nikajua alikuwa chumbani amelala. Sikuingia chumbani kwa kuwa nilijua angeniuliza ninakotoka kwa vile nilichelewa sana.
Nikaingia katika chumba kingine ambacho huweka nguo zangu za kufanyia kazi za nyumbani. Nikabadili nguo nilizokuwa nimevaa kisha nikaingia jikoni na kutayarisha ile nyama. Nyama ilipokuwa jikoni nilichambua mchele. Nilikuwa nimekusudia kupika pilau.
Baada ya masaa mawili pilau ikawa tayari. Nikatenga chakula juu ya meza. Nikamwaambia shemeji akamchukue kaka yake waende wakale. Mimi nilijipakulia kwenye sahani yangu nikaenda kuketi uani peke yangu.
Wakati ninakula kile chakula nilikuwa nikimuwaza Chinga na jinsi nitakavyoweza kuwa naye. Nilijiambia itakuwa ni uzembe kuacha aoe mke mwingine wakati alikuwa ameshanipenda na amekuwa akinipa pesa nyingi.
“Nitaendelea kuishi na hili zezeta hadi lini? Mwisho nitakosa hata nguo ya kuvaa” nikajisemea peke yangu.
SASA ENDELEA
Baada ya kumaliza kula chakula nilirudi ndani. Nilimkuta Ibrahima na mdogo wake na wao wamemaliza kula.
Zacharia aliondoa vile vyombo akaviingiza jikoni kisha akatoka kusafisha meza. Nilijua kuwa alifanya hivyo kwa kuniogopa mimi kwani tayari alikwishaiona hali ilivyo pale nyumbani.
Tangu kaka yake apofuke macho nilikuwa mkali kama simba na sikuwa na adabu kwa kaka mtu wala kwa mdogo mtu.
“Ukimaliza kusafisha meza uje uoshe vyombo” nikamwambia Zacharia.
“Nioshe vyombo?” akaniuliza kwa mshangao. Ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kumwambia hivyo.
“Sasa kumbe ulitaka aoshe nani? Kama hutaki mwaambie kaka yako aje aoshe yeye!” nikamwaambia kwa jeuri na kuongeza.
“Mmenifanya mimi ni kama mtumishi wenu.Chakula nitafute mimi, kupika nipike mimi na vyombo pia nioshe mimi!. Haitawezekana”
Zacharia akanyamaza kimya.
“Zacharia nenda kaoshe” Ibrahim akamwaambia mdogo wake.
Zacharia alipomaliza kusafisha meza aliingia jikoni kuosha vyombo.Mimi nilikwenda kuoga kisha nikabaki chumbani nikijua kuwa Ibrahim asingeingia tena muda ule.
Mchana ukapita. Ilipofika usiku wakati Ibrahim ameingia chumbani kulala, mimi niliketi sebuleni kuangalia Tv peke yangu. Zacharia pia alikuwa ameshaenda kulala.
Lakini lengo langu halikuwa kuangalia Tv. Lengo langu lilikuwa kumpigia simu Chinga tuzungumze. Nikambipu na muda uleule akanipigia.
“Vipi Chinga umeshalala?” nikamuuliza baada ya kupokea simu.
“Hapana, nilikuwa namalizia bia yangu ya pili ndipo nikalale” akaniambia.
“Kumbe unakunywa?”
“Bia zangu hazizidi mbili. Ni za kupatia usingizi tu. Uko wapi?”
“Niko nyumbani”
“Mbona umenipigia, jamaa yuko wapi?”
“Yuko chumbani ameshalala, mimi nipo sebuleni.Nilitaka tuzungumze kidogo”
“kuhusu nini?”
“Kuhusu yale mazungumzo yetu. Ni kwamba mimi nimeshakubali lakini sasa huyu mwanaume nitamuachaje?”
“Si umdai talaka tu”
“Hawezi kuitoa.Mimi ndio tegemeo lake kwa sasa”
“ Hilo si tatizo.Tukutane hapo kesho tuzungumze hilo suala”
“Tukutane wapi?
“Sema wewe”
“Au nikufuate hapo hoteli?”
“Saa ngapi?”
“Usiku itakuwa vizuri”
“Utaweza kutoka usiku?”
“Nitatoka hivyo hivyo. Mchana sitaweza kuja hapo. Kuna macho ya watu wengi”
“Sasa nikufuate na gari au….?”
“Nitakuja na teksi. Wewe niambie upo chumba namba ngapi”
“Nipo chumba namba 15, kipo ghorofa ya kwanza”
“Mimi nitakuja humo chumbani moja kwa moja”
“Sawa lakini utaniambia saa utakayo kuja”
“Nitakuambia kesho”
“Haina tatizo. Sasa utanipigia saa ngapi hapo kesho?”
“Siwezi kukuambia kwa sasa lakini nitakupigia wakati wa mchana kukujulisha. Na huo usiku nitakapo ondoka pia nitakujulisha”
“Sawa nitakusubiri”
“Okey.Usiku mwema”
“Na kwako pia’
Chinga akakata simu. Moyo wangu ukawa umefarijika kwa kuzungumza naye. Nikainuka na kuingia chumbani. Wakati ninapanda kitandani kulala nilidhani kuwa Ibrahim alikuwa usingizini. Niligeuka upande wangu nikajilaza. Mara nikasikia sauti yake akiniita.
Kwanza nilinyamaza. Aliponiita mara ya pili nikamuuliza.
“Unasemaje?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unajua mke wangu hivi sasa tabia yako imebadilika sana …..” akaniambia.
Hapo hapo nikajua alikokuwa anaelekea. Nikamkata kauli.
“Unaanza…unaanza…unaanza! Sitaki maneno. Kama huna maneno ya maana ya kuniambia nitatoka humu chumbani nikuachie chumba chako nikatafute pa kulala”
Ibrahim akanyamaza. Uwanja wa kusema ukawa ni wangu.
“Mwanaume una gubu kama nini. Kila unalofanyiwa huridhiki. Unataka roho yangu au unataka nini?.Hebu niambie!”
“Salma mimi sina gubu isipokuwa tabia yako unayoionesha tangu mimi nipate matatizo ya macho…..”
Sikumngoja amalize maneno yake, nikainuka kwa jazba na kuketi kitandani.
“Sitaki maneno mengi. Kama mimi nimekuwa sina tabia nzuri kukuletea chakula wewe na ndugu yako ule, basi nipe talaka yangu niondoke. Halafu utafute huyo mke mwenye tabia nzuri” nikamwaambia kwa ukali huku nikimnyooshea mkono wa kudai talaka.
“Salma wewe hutaki kuambiwa ukweli. Ukiambiwa ukweli unakuja juu. Mbona juzi na jana wakati nikiwa mzima hukudai talaka?”
“Hukuwa na gubu kama ulivyo hivi sasa. Maneno yamekuwa hayaishi. Balaa gani hili jamani!.Ule muda wa kulala na kupunzisha mwili, ndiyo unaanza maneno. Sasa mimi nitaondoka hapa kwako hata kama hutanipa talaka!”
Nikashuka kwenye kitanda huku nikiendelea kugomba.
“Sitalala tena humu ndani. Nimechoka na kelele zako”
“Sasa unakwenda wapi?” Ibrahim akaniuliza aliposikia ninafungua mlango.
Sikumjibu kitu nikatoka na kwenda sebuleni. Nikajilaza kwenye kochi. Baada ya muda kidogo nilimuona akitoka chumbani huku akiniita.
“Salma! Salma!”
Alikuwa akipapasa kwenye kuta akielekea sebuleni.
Nikamnyamazia kimya. Alipoona kimya akadhani labda nilikuwa nimetoka nje na kwenda zangu. Akapapasa ukuta hadi kwenye chumba anacholala Zacharia. Akamgongea.
“Zacharia! Hebu fungua mlango!” sauti yake ilikuwa imefadhaika.
Zacharia alipofungua mlango nilisikia akimwaambia.
“Shemeji yako ametoka, sijui amekwenda wapi. Hebu toka umuangalie”
“Kwani amekuambia anakwenda wapi?” Zacharia akamuuliza.
“Hakuniambia. Tulisemeshana kidogo akatoka kwa hasira, sijui amekwenda wapi”
Zacharia akatoka na kuja sebuleni, akawasha taa na kuniona nimelala kwenye kochi.
“Shemeji si huyu hapa” akasema.
“Yuko wapi?” Ibrahim akamuuliza kwa pupa.
“Amelala kwenye kochi ”
Ibrahim akapapasa kuta na kuja pale sebuleni.
“Yuko wapi?” akauliza tena.
Wakati wote huo nilikuwa nimenyamaza kimya.
“Shemeji kaka anakuuliza” Zacharia akaniambia.
Mimi nikaendelea kunyamaza.
“Salma!” Ibrahim akaniita.
Sikumjibu.
Ushauri wa Rita haukunifurahisha. Ulikuwa kinyume na mawazo yangu. Mawazo yangu yalikuwa ni kupanga jinsi ya kuachana na Ibrahim ili niolewe na Chinga. Hata hivyo sikutaka kumfichulia Rita undani wangu. Nikamwaambia
“Naenda kumla tu. Si amejileta mwenyewe?”
“Huyo mumeo umemwambia unakwenda wapi?”
“Nimemwambia ninaenda Makorora kwa shangazi amaumwa”
Wakati tunazungumza na mimi nilijisogeza karibu na kioo cha kabati na kuweka sawa nywele zangu pamoja na kuukwatua uso wangu kwa kutumia vipodozi vya Rita.
Ilinichukua karibu nusu saa kujiweka sawa. Nilipohakikisha kuwa nilikuwa nimependeza nikavaa baibui langu kisha nikatoa simu yangu na kumpigia Chinga.
Simu ilipopokelewa nikamuuliza.
“Uko wapi Chinga?”
“Nipo hotelini” Chinga akanijibu kwenye simu kabla ya kuniuliza.
“Utakuja muda gani?”
“Ndio ninakuja”
“Unakuja sasa hivi?”
“Ndiyo ninatoka. Nitakwenda kukodi teksi”
“Sawa, basi ninakusubiri”
“Okey” nikakata simu na kumwambia Rita.
“Natoka. Jamaa ananisubiri hotelini”
Rita akanisindikiza hadi mlango wa mbele, nikatoka. Nilitembea kwa miguu hadi kwenye kituo cha daladala ambako nilisubiri teksi itakayopita niisimamishe. Katika eneo hilo hakukuwa na kituo cha teksi cha karibu.
Nilipoona teksi haitokei na muda unazidi kwenda nikaamua kupanda bodaboda.
SASA ENDELEA
“Nipeleke Chuda” nikamwaambia kijana mwenye pikipiki.
“Chuda sehemu gani?” akaniuliza
“Karibu na hoteli ya Mtendele”
Sikutaka kumwambia anipeleke moja kwa moja katika hoteli hiyo kwani angenishuku vibaya.
“Kaa twende” akaniambia.
Nikajipakia nyuma yake. Pikipiki ikaondoka. Ingawa giza lilikuwa linaingia na isingekuwa rahisi kwa mtu anayenifahamu kunitambua, niliuziba uso wangu kwenye mgongo wa dereva wa bodaboda ili nisijulikane.
Mwendo wa nusu saa ukatufikisha Chuda.
“Simama hapa hapa” nikamwaambia kijana wa bodaboda tulipokuwa tunaikaribia hoteli ya Mtendele.
Kijana akasimamisha pikipiki. Nikashuka na kumlipa pesa zake kisha nikatembea kwa miguu kuelekea upande ilikokuwa hoteli ya Mtendele.
Nilipofika nilijipenyeza kwenye geti bila kusita. Kwenye ukumbi kulikuwa na wateja wachache wakipata vinywaji. Sikuwajali, nikaenda mapokezi na kumkuta msichana mwenzangu niliyemuulizia Chinga.
“Aliacha agizo kwamba akitokea mgeni wake aende chumbani kwake. Yuko chumba namba 15, kipo ghorofa ya kwanza” msichana huyo akaniambia.
Nikapanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza, nikakitafuta chumba namba 15 nikakiona.Nikaenda kubisha mlango. Nilibisha mara moja tu kasha nikasubiri. Baada ya sekunde chache mlango ulifunguliwa. Chinga akatoa kichwa ukumbini.
“Oh! Salma karibu ndani” akaniambia aliponiona.
Alinipisha kwenye mlango, nikaoingia. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza tangu niolewe na Ibrahim kuingia katika chumba cha hoteli na mwanaume.
Kusema kweli baada ya kuingia humo chumbani niligwaya nikajihisi kuwa ni mwenye hatia. Lakini nikajikaza ili nitimize lile nililokuwa ninalitaka. Niliamini kabisa kwamba wakati ule sikuwa mimi kama mimi, kulikuwa na nguvu ya shetani iliyokuwa ikinisukuma ndani ya moyo wangu.
Humo ndani kulikuwa na kitanda kipana cha sita kwa sita. Upande mwingine kulikuwa na kabati la kioo. Katikati ya chumba kulikuwa na meza iliyokuwa na chupa nne za bia, moja ikiwa tupu. Kulikuwa na pakiti la sigara na kibiriti. Kando ya meza palikuwa na sofa moja.
Nikajua kuwa Chinga alikuwa ameketi kwenye sofa hilo akinywa bia. Nikataka kwenda kuketi kitandani lakini nilibadili mawazo nikaenda kuketi kwenye lile sofa. Chinga akafunga mlango. Alipoona nimeketi kwenye sofa yeye akakaa kitandani.
“Habari za nyumbani?” akaniuliza huku akitabasamu.
“Nzuri, za hapa?”
“Hapa kwema. Leo umependeza” akaniambia
Aliponiambia hivyo niliona aibu kwa sababu nilijua alishuku kuwa nilijikwatua kwa ajili yake
“Kawaida tu” nikamwaambia kwa kuvunga kisha nikabadili mazungumzo haraka.
“Ulikuwa unakunywa bia?” nikamuuliza
“Si unajua tena….” akanijibu bila kumaliza sentensi yake. Akanyoosha mkono na kuichukua bilauli iliyokuwa imejaa kilevi akaipiga funda kisha akairudisha juu ya meza
“Nikuagizie bilauli yako unywe kidogo kidogo?” akaniambia.
“Situmii na sina muda. Nimekuja mara moja tu tuzungumze ile habari yetu kisha nirudi”
“Tunahitaji muda wa kutosha Salma. Mbona unaonekana kuwa na haraka hivyo?”
“Si unajua bado niko mikononi kwa mtu. Kuondoka kwenyewe ni kwa kuiba”
“Kwani umemwaambia unakwenda wapi?”
“Kwa shangazi Makorora. Nilidanganya kuwa shangazi anaumwa ili nije huku”
“Hakushituka kuona unaondoka usiku?”
“Ni kwa sababu mchana nilikuwa na kazi ya kufua nguo”
“Sasa Salma tutafanya nini?. Unadhani suala lake litakuwa kikwazo tusiwe pamoja?”
“Litakuwa kikwazo. Wewe si unataka kunioa?”
“Na umesema hataweza kukupa talaka hata kama utaidai?”
“Hataweza kunipa”
“Je ukiifuatilia Bakwata?”
“Bakwata nikawaambie nini?”
“Kwamba huyo mwanaume hana uwezo wa kuishi na wewe, kwa hiyo unataka muachane”
“Bakwata hawatakubali, wataona ninamkataa kwa sababu amepofuka. Wataninasihi niendelee kuwa naye hivyo hivyo”
Chinga akapiga funda jingine la bia. Alipoirudisha birauli aliniambia.
“Hatutakosa njia nyingine. Nakupa muda uendelee kufikiri lakini jaribu kumshinikiza akupe taraka”
“Wewe utakuwa hapa Tanga mpaka lini?”
“Sina muda mrefu. Naweza kuondoka siku yoyote nitakayoamua”
“Basi tuendelee kufikiria njia nyingine. Kwa vile sina nia ya kuendelea kuishi naye, kama hataniacha yeye nitamuacha mimi!”
“Lakini umenipenda?” Chinga akaniuliza ghafla. Macho yake yalionesha kuwa ulevi ulikuwa umeanza kumchukua. Iliwezekana alianza kunywa muda mrefu.
“Kama nisingekupenda nisingekuja huku” nikamjibu.
“Kama ni kweli kunywa bia kidogo”
“Nimekuambia situmii”
“Onja kidogo”
“Nitaonya siku nyingine”
“Basi njoo uketi hapa”
Alimaanisha nikaketi naye kitandani.
“Hapa nilipokaa panatosha”
Chinga akainuka na kunifuata akanishika mkono na kuniinua.
‘Mbona uko hivyo Salma? Hebu twende tukakae pale”
“Chinga utasababisha nichelewe nyumbani” nikajidai kulalamika huku nikimfuata kwenye kitanda. Nikaketi na yeye akaketi.
“Wewe umeshaamua kuwa na mimi, unajali nini kuchelewa? Wewe ni wangu tu au si kweli?”
Nikanyamaza kimya na kubaki kumtazama machoni. Akatabasamu na kunipitishia mkono kiunoni.
“Una macho ya kimahaba kweli!” akaniambia kisha akanibusu midomoni. Kilichofuatia baada ya hapo sitakisema. Ni aibu.
Ilikuwa saa nne ikikaribia kuwa na nusu Chinga aliponirudisha nyumbani. Nilimwaambia asimamishe gari nyumbni kwa jirani yangu Rita ili Ibrahim na mdogo wake wasijue kuwa nimeletwa na gari.
Chinga akanipa shilingi laki moja kabla sijashuka kwenye gari.
“Ahsante” nikamwaambia kabla ya kuagana naye.
Nikashuka kutoka kwenye gari na kutembea kuelekea nyumbani.
Nilikuta mlango wa mbele ukiwa umefungwa. Nikabisha. Zacharia akaja kunifungulia, nikaingia.
“Habari ya saa hizi?” akanisalimia.
“Nzuri” nikamjibu huku nikizuga kwa kuangalia kwenye runinga.
“Unatazama kanda?” nikamuuliza.
Niliona deki imewashwa na kuonesha filamu za kina Kanumba.
“Ndiyo shemeji” Zacharia akanijibu huku akifunga mlango kisha akaniuliza.
“Vipi hali ya shangazi?”
“Bado anaumwa” nikamjibu huku nikiketi kwenye sofa.
Nikajifanya nataka kuangalia ile kanda. Zacharia aliondoka kwenye mlango naye akaja kuketi.
“Kwani ana tatizo gani?” akaniuliza.
“Ni uzee tu. Kila mahali panamuuma. Na presha yake pia iko juu” nikadanganya. Kwa kuwa sikutaka tuendelee na mazungumzo yale nikamuuliza.
“Kaka yako ameshalala?” nikamuuliza Zacharia.
“Ameingia chumbani muda mrefu”
“Mmekula nini?”
“Tumekunywa chai. Nilikwenda kununua mkate”
Nikajidai kumuuliza “Mmenibakishia na mimi?”
“Tumekuachia silesi zako”
“Mmefanya vizuri, njaa inaniuma”
Baada ya hapo tukabaki kimywa tukiangalia ile kanda. Kukaa kwangu pale na kuangalia ile kanda ilikuwa ni kuvunga tu kwani nilijua nilikuwa nimechelewa kurudi na nilikuwa na ile hisi ya kutenda dhambi.
Ghafla Ibrahim akatoka mle chumbani na kumuuliza mdogo wake.
“Shemeji yako hajarudi hadi muda huu?”
Akanyamaza kidogo kabla ya kuniuliza.
“Unamuonaje mgonjwa?”
“Bado anaumwa” nikamdanganya
“Cha mno ni nini hasa” akaendelea kuniuliza
“Mwili wote unamuuma. Pia ana presha”
“Presha gani, ya kushuka au ya kupnada?”
“Presha ya kupanda”
“Sasa amepata tiba?”
“Alipelekwa hospitali, anatumia dawa”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipomjibu hivyo akanyamaza tena kidogo, kisha akaniambia.
“Mimi naenda kulala”
Sikumjibu kitu. Akageuka na kurudi chumbani. Kusema kweli nilikuwa nimemchukia. Nilikuwa nikimuona kama mtu anayenipotezea muda wangu bure.
Wakati alipotoka kule chumbani na kuja kuniuliza, nilidhani angegomba. Nilikuwa nikingoja aseme neno lolote la kunituhumu nimnyambue kisha ningetoka usiku ule ule na kurudi kwa Chinga.
Mkanda ulipokwisha nilikwenda mezani nikanywa chai na silesi walizoniachia kisha nikaingia chumbani.
Asubuhi kulipokucha wakati ninafanya usafi wa nyumba nilienda uani nikampigia simu Chinga kumsalimia.
Akafurahi nilivyompigia simu asubuhi ile.
“Umeshaamka au bado umelala?” nilimuuliza baada ya kukosa maneno ya kuzungumza.
“Bado niko kitandani”
“Kitandani hadi muda huu?”
“Ni harakishe nini, sina pa kwenda”
SASA ENDELEA
“Una raha mwenzetu. Natamani nije tulale sote”
“Sasa nani anakuzuia?”
“Si huyu ‘mnoko’ anayenipotezea muda wangu” nilimaanisha Ibrahim.
“Jana uliporudi alikuambia nini?”
“Hakuniambia kitu, si anajua nilikuwa kwa shangazi”
“Sasa mbona unasema anakuzuia usije huku?”
“Hanizuii lakini si ndiye kikwazo changu. Natamani niliue niondoke”
Chinga akacheka kwenye simu.
“Usimuue utapata hatia, tumia taratibu atakuacha tu. Hakuna ndoa ya lazima”
“Ataniacha lini wakati mimi nataka niondoke hata sasa hivi?”
“Usiwe na haraka hivyo. Mimi nitakusubiri tu”
“Si unataka kurudi Dar”
“Hata kama nitarudi Dar, sitakaa sana nitakuja tena kwa ajili yako”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nataka ukiondoka tuondoke sote. Hata kama sijapewa talaka, huyu mwanaume nitamuacha tu”
“Basi tutazungumza, si utakuja usiku?’
“Leo sitakuja,tufanye kesho ila nitakupigia simu usiku”
“Sawa”
Nilitegemea Chinga angekata simu lakini simu haikukatwa, nikamuuliza.
“Mbona hukati simu?”
“Kata wewe” akaniambia.
“Kata wewe bwana!” na mimi nikamwaambia.
Chinga akacheka kisha akakata simu.
Nilipokuwa narudi ndani nikamuona Ibrahim nyuma ya mlango akipapasa ukuta akielekea upande wa chumbani kwetu. Nikajiuliza ni kitu gani kilichomleta nyuma ya mlango?. Sikupata jibu. Lakini nilishuku kuwa pengine alikuwa akisikiliza nilivyokuwa ninaongea na Chinga.
Nikajiambia kama ametusikia atakuwa ameijua siri yangu wakati mimi sikutaka aujue uhusiano wangu na Chinga.
Ingawa sikuwa na uhakika kwamba alikuwa akitusikiliza au la lakini nilijiambia kama ametusikia nitajua kwani ni lazima ataniuliza.
Na nilingoja aniulize ndipo nimueleze wazi kuwa nilikuwa nimemchoka na nilihitaji kuondoka kwake, hivyo anipe talaka yangu.
Ibrahim akaingia chumbani na mimi nikaingia humo humo ili kama amesikia kitu aniulize. Lakini Ibrahim hakuniuliza chochote.
Ilipofika saa nne nilitoka bila kumuaga nikaenda sokoni.
Niliporudi niliingia jikoni. Nilikuwa nimenunua samaki,mchele na vitu vingine. Pesa ya Chinga ilikuwa inafanyakazi.
Nikaanza kupika. Hadi saa saba mchana wali ukawa tayari. Nikawatengea Ibrahim na mdogo wake kwenye meza na mimi kama kawaida yangu nilijipakulia kiasi changu nikaenda kukaa uani.
Wakati ninakula nilijiuliza, mbona Ibrahim hakuniuliza kitu wala hakuonesha kukasirika?.Huenda hakuyasikia mazungumzo yangu na Chinga. Moyo wangu ukapata faraja kidogo.
Ilipofika mida ya jioni nikamwaambia Ibrahim kuwa ninakwenda kwa Rita kuzungumza. Si kwamba nilikuwa nimebadilika na kuamua kumpa heshima yake ya kumuaga kila ninapotaka kutoka, lahasha. Kumuaga huko kulikuwa ni kuzuga tu kama vile namfanya mjinga. Mbona nikiwa na safari zangu za maana nilikuwa simuagi!
Nilichukua muda mwingi nikiwa kwa jirani yangu Rita tukizungumza hili na lile lakini kubwa tuliloliongelea ni kuhusu uhusiano wangu na Chinga.
Kwa vile msimamo wa Rita ulikuwa nisiachane na Ibrahim kwa kuwa mimi ndiye niliyemsababishia matatizo ya macho, sikumueleza undani wangu kuwa nilitaka niolewe na Chinga kwa sababu angeupinga uamuzi wangu huo.
Katika maongezi yetu tulipanga kukutana kesho yake usiku pale pale hoteli. Baada ya hapo nikamwaambia kuwa nilikuwa nyumbani kwa shoga yangu Rita na kumtaka asalimiane naye.
Nikampa simu Rita, wakasalimiana. Baada ya hapo Rita akanirudishia simu.
Nilikaa kwa Rita hadi saa mbili usiku nikarudi nyumbani kwangu.
Kulikuwa na wali uliobaki mchana, Nikaona tule huo huo. Nikachemsha chai na kuitia kwenye chupa kisha nikaandaa chakula hicho mezani. Kama kawaida yangu nilijitengea chakula changu na kwenda kuketi uani peke yangu.
Nilipomaliza kula na kurudi ndani nilikuta chakula kimebaki kingi. Kumbe Ibrahim hakula, alikunywa chai tupu. Na mimi kwa jeuri yangu sikutaka kumuuliza kwanini hakula chakula kwani nilishagudua tangu niliporudi kutoka kwa Rita, Ibrahim alikuwa amekasirika.
SASA ENDELEA
Alionekana kuwa mnyonge sana.Nilihisi labda alinifikilia nilikuwa natoka kwa mwanaume. Kama alinidhania hivyo alikuwa amejikangaja.
Licha ya kwamba nilitaka kumfanya mpumbavu lakini Ibrahim alikuwa mtu mwenye subira na busara pia, kwani alisubiri hadi usiku wakati tunajiandaa kulala chumbani ndipo aliponitolea undani wake.
Akanieleza kwamba amegundua kuwa nilikuwa na mwanaume mwingine wa nje.
Kwanza nilidhani alikisia kwa vile nilivyokwenda kwa Rita, nikamwaambia atoke aende akamuulize Rita kama nilikuwa kwake ama nilikuwa kwa mwanaume.
Lakini Ibrahim alikuwa timamu, akaniambia.
“Achilia mbali habari ya Rita. Mimi sizungumzii juu ya kwenda kwako kwa Rita. Unaye mwanaume na jana ulikwenda kwake uliponiambia unakwenda kwa shangazi yako.”
Ingawa ukweli wake usingekuwa tishio kwangu kwa sababu tayari nia yangu ilikuwa kuachana naye lakini aliponiambia vile nilishituka na kidogo nilinywea. Hata hivyo nikajihazahaza kwa kutoa kicheko cha uongo nikijifanya namshangaa.
“Wewe sasa huo upofu wako utakutia kichaa, uliniona wapi na huyo mwanaume?” nikamuuliza ili nijue alijuaje kuwa nilikwenda kwa mwanaume.
“Ni kweli nimekuwa kipofu lakini sina kichaa, nipo timamu. Ninachokuambia nina hakika nacho. Wewe una mwanaume ambaye una mpango naye uondoke kwangu, lakini ninakwambia binaadamu haishi kuumbwa na utu ni bora kuliko kitu.
“Yaliyonikuta mimi, na wewe yanaweza kukukuta. Na ni utu wako pekee utakaokupa thamani ya ubinaadamu na siyo kitu. Nilitaka kukuambia hivyo tu.Maneno yangu yameisha”
“Lakini nataka uniambie nani amekuambia kuwa nina mwanaume na nina mipango ya kuondoka kwako.Au unahisi hisi tu?” nikamuuliza. Kusema kweli sauti yangu ilikuwa imenywea kidogo.
“Asubuhi ulikuwa unazungumza na nani kwenye simu pale uani?” Ibrahim akaniuliza.
Moyo ukanipasuka. Sasa nikagundua kuwa Ibrahim aliyasikia mazungumzo yetu na Chinga tulipokuwa tunazungumza kwenye simu wakati wa asubuhi.
Ukweli ni kwamba nilitahayari kwa sababu sikutaka Ibrahim ajue jambo hilo lakini kwa vile alikuwa ameshalijua sikuwa na jinsi.
Nikamjibu kwa kumropokea
“ Kama kazi yako ni kusikiliza watu wanaoongea kwenye simu utasikiliza mengi sana”
Baada ya hapo sikumsema tena. Nikapanda kitandani upande wangu nikalala.
“Mimi nakuonya kama mume wako lakini kama unanidharau endelea na mwenendo wako” Ibrahim akaniambia.
Hapo ndipo aliponipandisha madudu yangu.
“Babu wee usiniletee kelele! Mimi nataka kulala, unanionya kitu gani nisichokijua?” nikamwambia kwa sauti ya dharau.
“Kuelezana kupo. Mimi ni mume wako hata kama umenidharau. Siwezi kuona una mahusiano na mwanaume wa nje nisikuambie” Ibrahim akaniamia kwa sauti tulivu.
“Huyo mwanaume umenifumania naye au ni umbea wako wa kusikiliza simu za watu? Kwani wewe unanipa pesa yako au ninajihudumia mwenyewe? Mume ni pesa siyo maneno matupu. Mimi sijioni kama nina mume, nisingehangaika mchana kutwa kwenda kuombaomba kwa watu. Wenye waume zao huwaoni nini?”
“Sawa bibi, kama leo umefikia kuniambia hivyo ili kunionesha kuwa umepata mwanaume mwenye pesa nakuombea heri. Ibrahim leo ni kipofu lakini narudia kukuambia kuwa binaadamu haishi kuumbwa na utu wa mtu si pesa”
Maneno yake yakazidi kunipandisha.
“Usiniapize mwana wa mwenzio. Binaadamu haishi kuumbwa maana yake nini?” nikamuuliza kwa ukali.
Ibrahim hakujibu kitu. Nikaendelea kumwaambia.
“Sasa kama mimi nimeshakuwa Malaya, nina wanaume je wewe unachukua uamuzi gani?”
“Uamuzi unao wewe mwenyewe” Ibrahim akaniambia kwa sauti iliyonyeea.
“Basi nipe talaka yangu niondoke. Huo ndiyo uamuzi wangu. Kwanza nimeshachoka na maisha ya kuhangaika!”
Ibrahim akanyamaza kwa vile nilikuwa nimemfikisha mahali asipopataka.
“Usijitie kunyamaza, umeyataka mwenyewe. Nipe talaka yangu!” nikaendelea kumwaambia.
Lakini Ibrahim aliendelea kubaki kimya, nikawa ninasema peke yangu. Mwishowe na mimi mikanyamaza.
Asubuhi kulipokucha nikajitia kufura. Sikusafisha nyumba wala sikuchemsha chai. Nilitoka bila kumuaga mtu nikaenda kwa Rita..Nilikunywa chai huko huko kisha nikaingia chumbani mwake nikalala mpaka saa sita. Nilipoamka nikarudi nyumbani.
Sikujua kuwa walichemsha chai asubuhi au walikaa hivyohivyo, sikutaka kujua. Nilifikia sebuleni nikawa naangalia tv.
Kumbe nilipokuwa kwa Rita mmoja wa marafiki wa Ibrahim alikuja nyumbani akampa Ibrahim shilingi elfu kumi. Ibrahim alipogundua kuwa nimerudi, alikuja pale sebuleni akanipa ile elfu kumi aliyopewa.
“Chukua hii elfu kumi uende sokoni. Rafiki yangu Martin alikuja kunijulia hali akanipa” akaniambia.
“Mpe ndugu yako umtume huko sokoni” nikamwaambia kijeuri.
Ibrahim akamuita Zacharia akampa ile pesa.
“Shemeji yako atakuagiza vitu vya kununua” akamwaambia.
“Shemeji yupi!” nikamuuliza kwa kung’aka na kunyanyuka pale nilipokuwa nimekaa.
Huku nikielekea zangu uani nilimwambia.
“Wewe muagize vitu mnavyotaka. Mimi nimuagize nini?”
Nikaenda kukaa uani. Sikujua Ibrahim alizungumza nini na mdogo wake lakini baada ya muda kupita Zacharia alikuja uani na kuniambia amesharudi kutoka sokoni.
“Vitu viko jikoni” akaniambia.
“Mimi sipiki, nenda ukapike mle na kaka yako”
Nilipomwaambia hivyo Zacharia aliondoka. Sikujua walivyozungumza na kaka yake lakini baadaye acharia aliingia jikoni na kupika. Mimi nikaingia chumbani nikalala.
Baada ya muda Ibrahim aliingia chumbani na kuniuliza.
“Unaumwa?”
Sikumjibu kitu.
Akasimama simama karibu ya kitanda kisha akatoka. Nilikaa humo chumbani hadi saa kumi jioni nilipoingia bafuni na kuoga. Nilipotoka bafuni nikajipara na kuvaa viwalo vya gharama kisha nikavaa baibui langu nikatoka. Sebuleni nilimkuta Ibrahim peke yake akiwaza. Sikujua alikuwa akiwaza nini. Nikafungua mlango na kutoka. Wakati naufunga mlango, nilimsikia akiuliza.
“Wewe nani Zacharia?”
Sikumjibu chochote, nikaondoka. Ilikuwa safari ya kuelekea kwa Chinga.
Nilipotoka hapo nyumbani, nilikwenda kukodi pikipiki ya bodaboda ikanipeleka Makorola nyumbani kwa shangazi yangu. Nilijifanya nilikwenda kumsalimia, kumbe nilikuwa na langu jambo.
Vile nilivyomsingizia kuwa anaumwa nilimkuta kweli anaumwa. Akaniambia alikuwa ameshikwa na malaria kwa karibu wiki nzima lakini baada ya kutumia dawa ndiyo ameanza kupata nafuu.
Nilitoa shilingi elfu kumi nikampa shangazi kisha nikajidai kumlalamikia kuhusu gubu la mume wangu na jinsi anavyonishutumu kuwa nina wanaume wa nje.
“Yaani tangu apate ule upofu tabia yake imebadilika. Kila siku tunagombana, akiniona ninatoka anajua ninakwenda kwa mwanaume. Akiniona nimepigiwa simu anaitegea sikio akidhani nimepigiwa na mwanaume” nikamueleza shangazi.
“Mvumilie. Ile hali yake ndiyo inayomfanya anaona kama umemgeuka” Shangazi akaniambia.
“Nimemvumilia sana lakini sasa naona uvumilivu utaisha. Si hilo tu, mume hana pesa anategemea ndugu na jamaa wamsaidie, siku nyingine tunakula mlo mmoja tu halafu ananiletea kero kama hilo”
“Sasa utafanyaje? Kuwa naye hivyo hivyo ndiyo kilimwengu. Maisha yana majaribu mengi”
“Mh! Mimi naona maisha yatanishinda. Usishangae shangazi ukija kusikia nimemuacha yule mwanaume!”
“Usifanye hivyo mwanangu, si vizuri. Dunia yote itakusema wewe. Umekuwa naye katika raha na uwe naye pia katika shida”
“Shangazi mume hana kazi hana bazi, nisitoke nikatafute kazi mahali au biashara, nikae tu pale. Si tutakufa kwa njaa shangazi?”
“Hamtakufa. Kama ni kutafuta kazi au kufanya biashara sidhani kama atakukataza”
Nilivyoona shangazi hakuwa akiliunga mkono wazo langu la kuachana na Ibrahim japo nilimtolea visingizio chungu nzima vya uongo, nikanyanyuka na kumuambia.
“Vikizidi sana nitaondoka. Utakuja sikia
nimeshaondoka”.
Hapo hapo nikamuaga na kuondoka. Nilikwenda saluni nikatengezwa nywele na uso wangu kwa karibu saa moja. Hapo salumi palikuwa panauzwa kashata za kungu. Nilikuwa nazifahamu ingawa sikuwa na ushabiki wa kuzila. Kabla sijaolewa na Ibrahim ndiyo niliwahi kuzitumia sana lakini nilipoolewa nikaziacha.
Kashata hizo zinazochanganywa na unga wa mbegu inayoitwa kungumanga unapozila hukulegeza macho na kukulainisha mwili. Wakati mwingine ukila nyingi zinaweza kukulewesha na kukufanya usitosheke na tendo la ndoa.
Baadhi ya wanawake hupenda kuzila wanapokuwa na ahadi na wanaume zao. Na sana sana ni wale wanawake makahaba.
Nilipoona wasichana wenzangu wanazinunua huku wakizitolea sifa na mimi nikanunua nne na kuzila hapohapo saluni.
“Shoga ukitaka uzipatie mpaka uzinuilie, unazila kwa madhumuni gani” msichana aliyekuwa akinishughulikia aliniambia.
“Unazinuilia vipi?” nikamuuliza
“Unazinuilia vile unavyotaka, kama unataka zikulegeze macho, zikutie kilevi au zikufanye usitosheke na….” hakumaliza sentensi yake akaishia kucheka.
“Usipozinuilia hazifanyi kazi?” nikamuuliza.
“Zinafanya lakini hao makonkodi wenyewe huzinuilia.Vile unavyozinuilia ndivyo zinavyokufanya lakini kwa vle umeshazila basi”
“Nitakuja kuzinunua siku nyingine unifundishe hivyo zinavyonuiliwa” nikamwaambia.
Baada ya kutengezwa nywele zangu sikuondoka haraka hapo saluni, Nilimpigia simu Chinga na kumjulisha kuwa ninakwenda kwake, akaniambia ananisubiri
Ndipo nilipotoka nikakodi tena pikipiki ya bodaboda, ikanipeleka Mtendele Hotel.
Jambo la ajabu lililojitokeza kwa upande wangu ni kuwa safari ile niliingia mle hotelini bila kujali chochote kama vile nilikuwa mwenyeji. Nilimjulisha tu msichana aliyekuwa mapokezi kuwa ninakwenda kumuona Chinga chumba namba kumi na tano. Akaniruhusu.
Na hata nilipoingia chumbani kwa Chinga sikumuona haya kama ninavyomuona siku zote. Nilifikizia kujitupa kitandani. Kichwa changu kilikuwa kizito kama niliyekunywa kilevi. Mwili ulikuwa umenilegea na macho yalikuwa yamenilegea kiasi kwamba nilishindwa kutazamana na Chinga. Nikajua hali hiyo ilitokana na zile kashata nilizokula. Nikajiuliza je kama ningezinuilia ingekuwaje?
Kama kawaida yake nilimkuta Chinga kwenye kochi akinywa bia. Kwa mara ya kwanza siku ile Chinga alifanikiwa kunishawishi ninywe bia. Katika maisha yangu sikuwahi kunywa bia hata siku moja. Siku ile ndiyo niliionja na kuijua ladha yake. Nilikunywa chupa moja tu lakini kwa sababu nilishakula kashata nne za kungu nilionekana kama niliyekunywa chupa nne.
Si kwamba nilikuwa siwezi kusimama au kutembea bali nilikuwa nikiropoka maneno mengi ambayo kwa akili yangu ya kawaida nisingeweza kuyatamka huku nikijifanya nampenda sana Chinga.
Ghafla Chinga alinikata kilevi chote nilichokuwa nacho aliponiambia kuwa anatarajia kuondoka kesho yake kurudi Dar es salaam kwa vile mwenzake anayeshirikiana naye katika biashara zao alimpigia simu na kumueleza kuwa anahitajika Dar.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tutakwenda sote” nikamwaambia Chinga nikiwa nimemkumbatia.
Sikuwahi kumkumbatia Ibrahim namna ile hata siku moja tangu apate upofu.
“Siwezi kukuchukua wakati ni mke wa mtu” Chinga akaniambia.
“Mtu gani…..yule kipofu? Yule tumeshaachana tangu jana usiku” nikamwambia kwa sauti ya kupayuka.
“Mmeachana?” Chinga akaniuliza huku akishangaa
“Tumeachana jana, mimi si mke wake tena”
“Hebu nieleze vizuri, alikwambia anakuacha?”
“Ndiyo ameniambia”
“Ilikuwaje mpaka akakuacha?”
“Ulitokea ugomvi kati yetu. Jana asubuhi tulipokuwa tunazungumza kwenye simu alitusikia akanyamaza hadi usiku alipoanza kunitukana kuwa mimi ni malaya, nina wanaume wa nje. Nikamwaambia kama mimi ni malaya anipe talaka yangu, ndipo akanipa”
“Iko wapi hiyo talaka aliyokupa?”
Aliponiambia hivyo nilishituka kidogo kwa sababu nilihisi Ibrahim akisikia kumeingia ujumbe kwenye simu yangu anaweza kumpa Zacharia amsomee na hivyo kugundua mipango yangu.Lakini nikasema potelea mbali liwalo na liwe. Kuondoka ni lazima niondoke na Chinga.
“Siwezi kujilazimisha kuendelea kuishi na mwanaume ambaye simtaki” nikajiambia kimoyomoyo.
Chinga akaniambia tuingie kwenye basi ambalo lilikuwa karibu na mahali tulipokuwa tumesimama. Tukajipakia kwenye basi hilo la kampuni ya Rahaleo.Tulitafuta siti zetu, tulipoziona tuliweka masanduku yetu kwenye kifaa cha kuwekea mizigo. Tukaketi.
Vile tunaketi tu niliona mtu ambaye sikumtarajia akiingia ndani ya basi hilo, mkono mmoja akiwa ameshika bakora yake na mkono mwingine ameshikwa na kijana ambaye bila shaka ndiye aliyemleta hapo stendi.
Alikuwa Ibrahim!
Moyo wangu ulishituka. Furaha niliyokuwa nayo yote ikanipotea. Nikabaki kumtazama kuona alikuwa anataka kufanya nini.
Nilishajua kuwa alinifuata mimi baada ya kuugundua ule ujumbe niliotumiwa na Chinga ambao ulimtambulisha kuwa nilikuwa nimetoroka kwake na nilikuwa ninasafiri na mwanaume kwenda Dar er salaam kwa basi la Rahaleo.
Mabasi ya Rahaleo yalikuwa yakifanya safari zake Da er salaam na Tanga.
Hata kama Chinga hakuandika kuwa tunakwenda Dar lakini kwa vile alitaja basi la Rahaleo, Ibrahim alishajua kuwa tunakwenda Dar. Bila shaka baada ya Zacharia kumsomea ujumbe huo wa Chinga kwenye simu yangu, Ibrahim alimwaambia aangalie kwenye kabati ambako waliona nilikuwa nimechukua nguo zangu zote muhimu na vitu vyangu vyote.
SASA ENDELEA
Hapo ndipo Ibrahim alipotaharuki na kukurupuka akaamua kunifuata stendi. Sikujua ni kwanini aliletwa na kijana mwingine badala ya Zacharia lakini nilipata jibu kuwa huenda ni kijana wa bodaboda aliyoikodi.
Chinga hakuwa ameshituka. Kwanza alikuwa hamjui Ibrahim. Pengine alipomuona alidhani ni miongoni mwa abiria wa basi hilo, isitoshe alichokuwa anakijua Chinga ni kuwa nilikuwa nimeshaachana naye na nilikuwa nimehamia kwa shangazi yangu.
Sasa sijui itakuwaje? Nikawaza. Hata hivyo nilipata moyo kidogo kwa sababu Ibrahim mwenyewe asingeweza kuniona kwa vile haoni na kijana aliyekuja naye alikuwa hanijui.
Nikatulia kimya kwenye siti huku nikizungumza na Chinga kama vile huyo mtu aliyeingia nilikuwa simjui.
Ibrahim alipoingia ndani ya basi hilo alisimama kando ya mlango akauliza.
“Salma, umo ndani ya basi hili?”
Chinga akashituka wakati Ibrahim alipolitaja jina hilo . Mimi nikanyamaza kimya.
“Anamuuliza nani?” Chinga akaniuliza kwa sauti ya chini.
Nikamjibu “Sijui”.
Ibrahim akauliza tena.
“Jamani namtafuta mke wangu anayeitwa Salma. Kama yumo ndani ya basi hili naomba anijibu”
Chinga akanitazama. Bila shaka alikwisha gundua kuwa yule ni mume wangu na Salma anayemtafuta ni mimi.Lakini aliponitazama hakuniambia kitu, akageuza uso wake kumuangailia Ibrahim.
“Jamani mnaulizwa kuna mtu anayeitwa Salma mke wa huyu bwana?” abiria mmoja akamsaidia Ibrahim kuuliza baada ya kuona watu wako kimya.
Abiria wakawa wanatazamana. Kila mtu akamtazama mwenzake. Kwa bahati wanawake tulikuwa wengi humo ndani ya basi, kwa hiyo hakukuwa na aliyenitilia shaka.
Yule abiria aliyemsaidia Ibrahim kuuliza akamwaambia “Naona hayumo”
“Kwani hili si ndilo basi la Rahaleo au kuna jingine?” Ibrahim akauliza
“Liko jingine lakini limeshaondoka.Labda alikuwa kwenye basi hilo ” Ibrahim akajibiwa.
Hapo nikaona uso wa Ibrahim ukisambaratika na kuonekana kama aliyetaka kulia.Laiti ningekuwa na moyo wa kibinaadamu ningemhurumia na pengine ningebadili mawazo ya kumkimbia.
Lakini ibilisi alikuwa amesha nishika sawasawa. Nilimuona Ibrahim kama shetani aliyekuwa anataka kuzuia mafanikio yangu.
Ibrahim akageuka ili atoke ndani ya basi. Nikaona mistari ya machozi ikitokeza chini ya miwani aliyokuwa amevaa.
Nilimchungulia Ibrahim kwenye dirisha wakati aliposhuka ndani ya basi. Kijana aliyekuwa amemshika mkono alikuwa akienda naye mahali alipoiegesha pikipiki yake.
“Imekuwaje Salma?” Chinga akaniuliza.
“Imekuwaje nini?” nikamuuliza ingawa nilishajua alichokusudia.
“Huwezi kunidanganya, huyu jamaa ndiye mume wako na alikuwa anakuuliza wewe”
Nilibetua mabega “Aka! Si tumekwisha achana. Atakuwaje mume wangu?”
“Sasa kama mmeachana mbona anakufuata?”
“Ni usumbufu tu, labda anataka kunibembeleza nirudi lakini mimi sitarudi tena kwake”
“Na amejuaje kuwa unasafiri?”
Hapo sikuwa na jibu, nikamwaambia.
“Atajua mwenyewe, mimi sijui. Labda ameambiwa na shoga yangu Rita. Rita naye kwa umbeya hawezekani!”
Wakati namuambia hivyo basi lilipigwa moto na kuanza kuunguruma kwa sekunde chache kabla ya kuondoka.
Tulifika Dar er salaama saa sita mchana. Tukiwa katika kituo cha mabasi cha Ubungo, Chinga alikodi taksi iliyotupeleka Sinza.
Nikamuuliza Chinga kwanini tunakwenda Sinza wakati aliniambia nyumba yake iko Masaki.
“Nina nyumba mbili, moja iko Sinza na moja Masaki” Chinga akanijibu.
Tulipofika Sinza niliiona nyumba ya Chinga. Ilikuwa nyumba ya kawaida tu. Chinga akaniambia nyumba yake iliyokuwa Masaki ndiyo ya thamani zaidi.
“Tutaanzia maisha hapa. Nikikuona una upendo wa dhati nitakuhamishia kwenye nyumba yangu ya Masaki” Chinga akaniambia.
“Kwani umenionaje?” nikamuuliza.
“Sijaishi na wewe, siwezi kukujua kwa undani”
“Upendo umo ndani ya moyo wangu. Kama sina upendo na wewe nisingemuacha mume wangu kwa ajili yako”
“Sasa ndiyo uuoneshe na mimi niuthibitishe”
Tulikuwa tumeshaingia ndani ambako tulimkuta kijana ambaye Chinga aliniambia kuwa ni mkazi wa nyumba ya jirani anaye muachia nyumba anaposafiri.
Sebuleni palikuwa na fanicha za thamani. Chinga alinitembeza nyumba nzima akanionesha kila kitu. Chumba chake cha kulala kilikuwa chenye hadhi hasa, siyo kama kile nilichokuwa ninalala na Ibrahim. Kwa jumla nilifurahia kuanza maisha mapya nikiwa na mwanaume tofauti. Sikumfikiria tena Ibrahim wala sikumkumbuka.
Niliishi na Chinga kama mke na mume ingawa hatukulizungumzia tena suala la ndoa. Mimi sikutaka kulizungumza kwa sababu nilijijua kuwa bado nilikuwa mke wa Ibrahim na Chinga hakulizungumza labda kwa sababu alitaka tuishi kwanza ili tupimane tabia.
Wiki moja baada ya kuanza maisha Chinga alininunulia simu nyingine mpya ya bei mbaya. Pia alinifanyia shopping ya karibu nusu milioni. Akaniambia zile nguo nilizotoka nazo Tanga nisizitumie tena kwa sababu haziendani na Jiji la Dar. Viwalo alivyoninunulia vilikuwa ni vya fasheni za kisasa za kisichana. Sikumbuki lile baibui langu nililitupia wapi.
Kila wiki tulikuwa tunatoka mara mbili kwenda kwenye matanuzi. Kumbi zote za starehe za Dar sasa nilikuwa ninazifahamu. Hakukuwa na mahali ambako sikupajua. Chinga alinifundisha ulevi nikawa mlevi wa kupindukia. Friji letu halikukosa kuwa na bia kila siku.
Chinga alinitambulisha kwa marafiki zake mbalimbali waliokuwa wakifanya biashara pamoja. Niliwazingatia marafiki zake wanne Frenk, Steven, Jonathan na Mussa. Mara kwa mara watu hao walikuwa wanakuja nyumbani na kufanya mazungumzo lakini Chinga hakutaka nisikilize mazungumzo yao .
Kuna siku walikuwa wakileta nyumbani vitu vya thamani kama TV na Friji na vitu vingine ambavyo Chinga aliniambia vilitoka bandarini na baada ya siku mbili tatu huvipeleka kwa wateja wao.
Kadiri siku zilivyokwenda Chinga alianzisha tabia mabayo sikuwa nikiipendelea. Kuna siku ambazo hutoka na mimi lakini kuna siku ambazo hutoka peke yake na kurudi usiku wa manane. Siku nyingine anarudi siku ya pili yake tena mchana.
Kila ninapomuuliza hutoa sababu mpya. Kuna siku anazoniambia amelala nje ya Jiji kuitokana na kazi zake za biashara na kuna siku ambazo huniambia amechelewa kurudi nyumbani kwa sababu alikuwa na mikutano na wafanyabiashara wenzake.
Pale ninapoonesha kukasirika kwa kumshuku kuwa ana wasichana wengine, Chinga alikuwa hodari wa kunibembeleza na kujitakasa kwamba hakuwa na msichana yeyote wa nje. Nikawa sina budi nikubaliane naye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilipita miezi minne. Kuna siku Chinga aliniaga kuwa anakwenda Tanga kumsalimia baba yake na kuchukua gari lake. Aliniachia pesa za kutosha na ndani ya nyumba kulikuwa na kila kitu. Nakumbuka aliondoka asubuhi. Ilipofika jioni wakati nimeketi sebuleni nikiangalia tv nikasikia gari likasimama huko nje.
Nilipochungulia kwenye dirisha niliona teksi imesimama mbele ya mlango. Nikaona msichana anashuka. Alionekana kama anatoka safari kwani dereva alimteremshia masanduku mawili.
Teksi ikaondoka.Yule msichana akaja kubisha mlango. Nikanyanyuka na kwenda kumfungulia.
“Hujambo?” akaniuliza.
“Sijambo, karibu”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment