Simulizi : Facebook Imeharibu Maisha Yangu
Sehemu Ya Tatu
(3)
"Bibi yangu aliniambia maneno ya
mdomo huumba halisi,na nina uhakika ninachokiongea kwa mdomo wangu Mungu
ataniumbia"
Aliendelea kuongea huku machozi yakifumba macho
yake na kitambaa alichokuwa anatumia kujifuta kilikuwa kimelowana tayari kwa
wingi wa machozi alikuwa kama yatima vile, Resh alikuwa akifungasha baadhi ya
mizigo yake tayari kwa kurejea shuleni tena,tangu tukio la Adam kupotea hakuna
aliyetegemea hata siku moja Resh atawaza kurudi tena shuleni kwani waziwazi
akili yake ilionekana kuathirika kwa kiasi kikubwa kwa kumpoteza Adam katika
mazingira yasiyoeleweka.
"Baba kesho narejea shule si
unajua tayari shule imefunguliwa?" Reshmail alimkurupua mzazi wake huyo kutoka
alipokaa kwa mshangao
"Umesema nini malkia wangu!" alihoji
Manyama huku akiwa wima
"Narejea shule kesho" kwa msisitizo na
tabasamu alijibu Reshmail.
Mzee Manyama hakuamini kwani alikuwa
akiwaza ni namna gani atamshawishi mwanae aweze tena kurejea shuleni baada ya
matatizo yote yaliyojitokeza kwa mchumba wake Adam ambaye hadi wakati huo bado
mwili wake ulikuwa haujapatikana wala taarifa yoyote zaidi ya nguo zikiwa na
matundu ya risasi na damu.
"asante sana mwanangu nakupenda
sana" mzee Manyama aliongea kwa furaha huku akimkumbatia
mwanae.
Tangu kupotea kwa Adam aliyehisiwa kuwa tayari amekufa
kulipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi huku asilimia kubwa ikiegemea upande
wa imani potofu za kishirikina wakihusisha tukio hilo na utajiri alionao Mh.
Manyama na uchaguzi uliokuwa mbele yake.
****
*******
"Wamemtoa mwanangu kafara ili waongeze
utajiri,nilimwambia Adam aoe msukuma mwenzake ona sasa,watoto wa siku hizi
wabishi wanajifanya wanajua sana na elimu yao
inawadanganya"
mama yake Adam alikuwa analaani vikali mbele ya
mume wake wakiwa ndani ya nyumba yao maeneo ya Igoma kwa
'one-way'
"Usiseme hivyo mama Adam kumbuka sisi ni
wakristu,tumwachie Mungu yeye ndio atajua nini cha
kufanya"
Babaye Adam alimtuliza mkewe huku akimgongagonga
mgongoni kwa kutumia kiganja cha mkono wake wa
kuume.
Mawasiliano baina ya familia hizi mbili ya Adam jijini
Mwanza na ya Reshmail jijini Dar-es-salaam yalikuwa yamekatika licha ya baba
yake Adam (mzee Michael) kutangaza kuwa kutoka moyoni mwake amesamehe yote
yaliyotokea na anaamini ni mipango ya Mungu.
Lakini kinyongo
kilionekana dhahiri kwa matendo,upendo wa zamani haukuwepo tena jambo hilo
lilimfadhaisha sana mzee Manyama kiasi cha kukondeana na kukosa umakini katika
utendaji wake wa kazi jambo lililoishusha sana heshima yake kama mbunge
aliyekuwa anaheshimika sana kuanzia bungeni hadi jimboni
kwake,
Wapinzani walitumia fursa hiyo kumchafua hasahasa na
kweli uchafu huo ukakubalika kwa wananchi kwa ujumla Manyama hakuwa na lake tena
pale,wananchi walimpuuzia sana tofauti na zamani na hata hiyo miaka miwili
iliyobaki wananchi waliiona kama ni mingi sana kuwa na kiongozi wa aina
yake.
Kuliko fedheha yote hiyo Mh. Manyama kwa hiari yake
mwenyewe alipitisha kura ya maoni ya wananchi kuhusu imani waliyonayo kwake kama
mbunge wao.
Asilimia 70 ya waliopiga kura walidai hawana imani
naye huku asilimia kumi na nne tu ndio wakidai bado wana imani naye na kura
zilizobaki zikiharibika,rasmi Manyama akawa ametolewa bungeni na katika uchaguzi
mdogo uliofanyika akachaguliwa mbunge kutoka chama cha upinzani na maisha
yakaendelea huku Mh.Manyama akiendelea na biashara zake
mikoani.
* **
Adam akiwa pale bustanini
alivamiwa ghafla na wanaume wawili wa shoka wakiwa na bunduki,ishara ya kidole
mdomoni ilimfanya atulie tuli kisha wakamwonyesha ishara kwamba awafuate
alifanya kama walivyotaka hadi kwenye gari iliyokuwa imepaki pembeni kidogo ya
nyumba yao Adam alishangazwa sana na ukimya uliokuwepo hakuwepo mlinzi wala mama
mkwe wake.
Safari yao ilikwenda mpaka Iringa gari iliyokuwa na
vioo vyeusi 'tinted' ilimzuia Adam kujua ni wapi alipo,gari ilizimishwa ndani ya
jumba kubwa sana ambapo alipelekwa kwenye chumba kikubwa tu,hofu kubwa
ilimtawala hakujua kwa nini yuko pale,hakupigwa wala kupewa bughudha yoyote,hali
hiyo ilzidi kumshangaza
"au ndio wachuna ngozi" alijiuliza Adam
kwa hofu tele.
Hayo ndio masharti ambayo mama Reshmail alitoa
kwa vijana aliowapa tenda hiyo ya kumtorosha Adam pale nyumbani. Shida yake
haikuwa kumtesa Adam bali kumweka mbali na mwana (Reshmail) ambaye alikuwa
amempagawisha ipasavyo katika mapenzi ya jinsia moja.
Suala la
pesa halikuwa tatizo hata kidogo alichohitaji ni kutimiziwa alichotaka. Mkataba
wa miaka mitano ndio alioingia na watu hawa kukaa na Adam bila kumruhusu kutoka
nje ya jingo.
Bi Gaudencia aliamini kwamba kwa kutokomea Adam
mbele ya uso wa Reshmail ilikuwa fursa nzuri ya kurudisha tena uhusiano wake na
Reshmail ambao ulikuwa unaelekea kufa lakini kinyume chake alikuwa ameibua chuki
kubwa baina yake na mwanae ?heri wote tukose kama ni hivyo? alijiapiza mama
Reshmail baada ya kuona dalili za kumshawishi Reshmail hazipo
tena
Alikuwa ni Reshmail mwingine kabisa mkasa uliomkumba
ulimbadilisha sana na kuitanua akili yake sana,Eveline naye alisikitishwa na
yaliyomkumba shoga yake akajitahhdi sana kuwa karibu naye kumpa moyo huku
akijiepusha sana kufanya vitendo ambavyo vitamkumbusha Resh jinsi alivyoweza
kukutana na Adam.
Ni katika kujiepusha na kumkera rafiki yake
huyo kipenzi Eveline akajikuta amefuta picha za uchi na filamu za ngono katika
kompyuta yake akawa si mtu wa kutoroka shule,hakuwa tena mtu wa wanaume na
hatimaye akawa Eveline wa kuigwa na wanafunzi wenzake jambo hilo liliwaduwaza
sana wanafunzi pale shuleni lakini ndio hivyo Eve alikuwa amekubali mabadiliko
katika maisha yake.
Juhudi zao katika masomo ziliendelea
kuwaweka katika nafasi nzuri ya kufanya vizuri mtihani wao wa mwisho.
Hawakuyazungumzia tena yaliyopita tena walijadili mapya na
yanayowanufaisha
"Eveline wewe ni kama dada yangu nakupenda
sana"
"Nakupenda pia Reshmail umebadili maisha yangu moja kwa
moja nina maisha mazuri sasa" alijibu Eva kwa upole huku akimwangalia Reshmail
aliyekuwa anaishusha chandarua yake aweze kulala. Ni kweli walitokea kupendana
wawili hawa.
"Hivi Resh una mpango bado wa kusomea uhasibu mi
lazima niwe mhasibu"
"Mh! unavyojiaminisha utadhani tumefaulu
tayari" alijibu Resh.
"He! mi najua sisi kufaulu kwetu sio
swali ni jibu,swali ni je tunaenda chuo gani na kusomea nini." alijiaminisha
Eveline.
"ok! nilidhani nitasomea uhasibu lakini kwa heshima ya
Adam nitasomea sheria" alijibu Reshmail kwa furaha.
"Mh! na
upole wako huo na mambo ya kutoa hukumu wapi na wapi? mwenzio naangalia ankara"
alisema Eva.
"Wala hata siendi kuhukumiana naenda kwa heshima
tu" alisisitiza Reshmail.
"Mh! haya mheshimiwa hakimu napenda
kujitetea kama ifuatavyo"
Eve alitania akifuatiwa na kicheko
kikubwa kutoka kwa Reshmail.
Maisha yaliendelea vyema
sana tu japo yalikuwa maisha ya mashaka Adam aliruhusiwa kuongea na kuuliza kila
kitu kasoro swali moja tu "Kwa nini niko hapa?",ndio hakuruhusiwa kuliuliza hata
kwa mbali,watu wote pale hawakuwa na ubaya nae hata
kidogo,hawakumtesa,hakugombezwa wala hakufanya kazi,alipewa huduma zote za
msingi,aliweza kutoka nje na kwenda bustanini lakini nje ya geti
hakuruhusiwa.
Tayari aliyazoea maisha haya lakini kumbukumbu ya
jinsi alivyochukuliwa ndani ya jumba la wakweze bila kupata msaada wowote ule
"Nani atakuwa nyuma ya haya yote mlinzi alikuwa wapi? Mama Resh je?" alijiuliza
sana bila kupata wa kumpa jibu.
"Hivi unaitwa dada nani vile?"
Adam alimuuliza dada mmoja ambaye kila baada ya siku tatu alikuja kufanya usafi
katika chumba chake.
"Naitwa Beatrice Cosmas niite Bite"
alijibu huku anafuta vioo kwa dirisha la chumba cha Adam.
"Una
jina zuri wewe mh!"Alisanifu Adam.
"Asante wewe ni Adam eeh!"
aliongezea yule binti huku akiwa ameacha shughuli yake aliyokuwa
anafanya.
"Ndio mimi ni Adam! samahani nikuulize maswali
machache"
"Uliza tu lakini sitakujibu sasa
hivi"
"Kwa nini?"
"We uliza yote ndo
nitakwambia kwa nini"
"Hivi hapa ni wapi? kwa nani? na kwa nini
nipo hapa?"
"Ndio hayo matatu tu?...sawa nitakujibu kwa sharti
dogo sana yaani"
"Sharti gani hilo mi nipo tayari"alitoa
uhakika Adam bila hata kulijua sharti lenyewe.
"Sikia Adam sina
haja ya kuzunguka zunguka nina mwaka wa pili hapa kitu kinaitwa mwanaume katika
mwili wangu ni kama ndoto sasa ni wewe wa kutii kiu yangu na mimi nitajibu
maswali yako" alijieleza Bite,jambo ambalio lilikuwa zito na la kumshangaza
Adam.
"Mh! au ndo mtego tena kutoka kwa Reshmail? dah! ikiwa
hivyo nitaaibika kweli mimi"Alijiwazia Adam kwa mashaka makubwa kabla ya
kujibu.
"Basi utakuja kunijibu baadaye!" alisema
Adam.
"Haya usiku na wewe jiandae" alijibu na kuaga
Bite.
Hayawi hayawi mara yakawa usiku wa saa tatu,Bite tayari
ndani ya chumba cha Adam ndani ya khanga moja peke yake.
"Haya
nipe nikupe hakuna longolongo hapa" alizungumza Bite.
"Subiri
taratibu basi,sikiliza" alianza kujitetea Adam wakati Bite anajisogeza
kitandani,Adam alikuwa amechelewa tayari joto la Bite lilipenya katika mwili
wake na kumchanganya hadi kujikuta akifanya kinyume na alivyotarajia kwamba
atafanikiwa kutegua mtego wa Bite badala yake alikuwa ameshafanya mapenzi na
Bite.
Kwa Bite ulikuwa ushindi mkubwa sana kwani tangu aletwe
hapo kuwa msaidizi wa kazi za ndani ya vyumba hakuwahi kutoka nje ya jengo
hilo,sio kwamba alikuwa amefungwa hapana kila kitu kilikuwepo ndani kila siku
pia alikuwa ameridhika kuwa hapo.
"Hapa ni Iringa,nimejibu
swali lako la kwanza tuendelee tena nikujibu swali la pili na tatu" alisema Bite
kwa shauku kubwa sana.
"Hapana Bite imetosha kwa leo sijisikii
vizuri,siku nyingine basi sawa!" alidanganya Adam na Bite hakuwa mbishi akambusu
Adam shavuni akajiondokea zake.
Ilimchukua takribani siku tano
Bite kugundua kwamba tayari ameshika ujauzito jambo ambalo halikuruhusiwa katika
jumba hilo na alipewa onyo kali wakati anaingia hapo. Kwa usalama wake na Adam
alifikiria suala la kutoroka lakini haya yote aliyafanya baada ya kuongea na
Adam na kumweleza hali halisi.
Ni katika wasaa huo alimweleza
Adam chanzo ambacho kinaweza kuwa kimemsababishia yeye kuwepo
pale
"Umemchukulia kigogo mpenzi wake,umemendea mtoto wa kizito
au umemkataa kimapenzi mtu maarafu" hizo ndizo zilikuwa baadhi ya sababu
alizoorodheshewa na Bite,lakini kwake yeye aliona hakuna hata moja inayomuhusu
kwani wazazi wote wawili wa Reshmail walimpenda sana hakuwa tayari kuweka hisia
kwamba pengine moyoni wanamchukia.
"Usijali lakini hutakaa
milele humu,huwa unafika
Muda aliyekuweka humu akiridhika
unatoka.
"Nitamlea mtoto,napenda watoto hata kama usipokuwa
mpenzi au mume wangu nitampenda sana na
nitamwita....."
"Christian akiwa mvulana au Christina akiwa
msichana" alidakia Adam ambaye kwa mbali alianza kumtamani Bite
kimapenzi.
* * *
Biashara za baba yake
zilikuwa zinaendelea vizuri na skendo lake lilikuwa linafifia taratibu. Hadi
anamaliza kidato cha sita Reshmail mapenzi kwa wazazi wake yalikuwa palepale na
japo hakutaka kumwongelea Adam jena alikuwa na picha yake waliyopiga pamoja siku
moja kabla ya tukio lile la kushangaza na kuumiza.
Reshmail kwa
ruhusa ya wazazi wa Eveline alienda nae mpaka kwao ambapo walikaa wote kwa siku
tano kisha akarejea tena Arusha.
Urembo wa Reshmail
ulipagawisha kila mwanaume na hata baba yake ilifikia kipindi akakiri kwamba
kweli pale alizaa mtoto mmoja wa kipekee na kweli alikuwa wa kipekee. Mama Resh
bado alikuwa na matamanio lakini kwa sasa alimwogopa sana Reshmail tofauti na
miaka mingi iliyopita.
"Baba na mama wiki ijayo nataka kwenda
Mwanza kwa wazazi wa Adam" Resh alitoa hoja yake wakiwa mezani
wanakula.
"Wapi? Mwanza! hawatakuelewa mwanangu utakuwa kwa
maksudi kabisa unafufua shari iliyopoa tayari"
Kwa busara tele
na upole mzee Manyama alimweleza mwanae ambaye pia aliyapokea kwa nidhamu ya
hali ya juu na kichwa chake kuyakubali kuwa yana maana kubwa ndani
yake.
"Nimekuelewa baba sitaenda tena" alijibu kwa unyenyekevu
sana Reshmail.
Matokeo ya kidato cha sita yalipotoka
hayakuwa ya kushangaza sana kwa upande wake kwani alikuwa amevuna alichokipanda.
Reshmail alikuwa amepata daraja la kwanza na ndivyo alivyotarajia,furaha yake
iliongezeka baada ya kumwona katika orodha Eveline Maige rafiki yake kipenzi
naye akiwa amepata daraja la kwanza huku wakitofautiana pointi
kadhaa.
Akiwa anajiandaa kumpigia simu tayari simu yake
iliwakawaka na kuandika "pacha" jina ambalo alikuwa amemwandika Eve katika simu
yake,badala ya kuongea wote kwa pamoja wakaanza kucheka,walicheka sana hadi simu
ilipokatika. Zilikuwa ni furaha kutoka moyoni,kwa nini wasifurahi wakati ndoto
zao zilikuwa zinatimia?
Tanzania Commission of Universities
(T.C.U) ilipotoa uchaguzi wa kwenda vyuoni Reshmail kama alivyopenda
alichaguliwa chuo kikuu cha mtakatifu Augustine Mwanza kwa masomo ya sheria huku
Eveline Maige akipelekwa Mzumbe chuo kikuu kwenda kuchukua masomo ya uhasibu
shahada ya juu.
"Ndugu hakimu naomba kujitetea!" Eve alimtania
Resh utani wao wa shuleni siku walipokuwa wanaagana.
Walikuwa
wametenganishwa hatimaye lakini mawasiliano yao yalidumu
Kama
alivyojiwekea kiapo chake cha kutopenda hovyohovyo ni hivyohivyo alivyoingia
pale chuoni,hakuringia uzuri wake lakini hakutaka pia usumbufu unaopitiliza
kutoka kwa wanaume yaani kwa kifupi alikuwa na msimamo mkali sana,ni rafiki yake
(Eve) pamoja na wazazi wake ambao wangeweza kubashiri sababu hasa inayomfanya
binti huyu awe hivi na si mtu mwingine pale chuoni.
Maringo
yake yalifichwa na werevu wake darasani,kwani ilikuwa ni warembo wachache sana
wa aina yake waliofanya vizuri kimasomo,jambo hilo lililowavutia waalimu wengi
sana na wanafunzi ambao wanapenda maendeleo kimasomo. Reshmail hakuwa mtu wa
mambo mengi hakunywa pombe wala kwenda kumbi za starehe usiku starehe yake
ilikuwa ni kusoma na michezo.
Mnamo mwezi wa pili michezo ya
FAWASCO ilipoanza michezo hiyo inayohusisha vitivo vyote pale chuoni,kwa maksudi
alichaguliwa kuwa mhamasishaji kwa wasichana wajibu alioufanya vizuri ipasavyo
na kikubwa zaidi akawa pia mdhamini mkubwa sana. Moyo wake wa kujitolea
uliwavutia sana wanadarasa wenzake ambao baadhi walimpenda huku wengine wakidai
ana maringo, msimamo wa Reshmail ulibaki palepale.
Mwaka wa
pili pale chuoni ndio ulikuwa mbaya kwake. Darasa walilolitumia mwaka wa pili
wanafunzi wa kitivo cha sheria,lililojulikana kama Mombasa Raha kwa mbele
lilikuwa na picha kubwa sana ya Adam ambayo ilikuwa pembeni ya ubao wa
kufundishia hiyo ikimaanisha kwamba kila atakapoingia darasani lazima
aione,"ADAM THE GREAT" yaliandikwa maandishi haya chini ya picha kubwa ya
Adam.
Amani,ikatoweka kabisa moyoni mwake kumbukumbu mbaya za
kumpoteza mpenzi wake Adam zikaanza kumrejea kwa kasi sana.Reshmail akaanza
kujihisi yeye ndiye chanzo cha yote hayo,tofauti na waalimu wake hakuna
mwanafunzi aliyemfahamu Adam zaidi ya kujua tu historia ya yaliyomkuta na wengi
kuichukulia kama simulizi tu ya kusadikika. Reshmail alianza kuwa mtoro darasani
na hata alipoingia badala ya kumwangalia na kumsikiliza mwalimu,mawazo yake yote
yalivutwa na picha ya Adam yenye tabasamu pana mara zote aliamini inamuangalia
yeye na kumlaumu kwa kumkatisha masomo yake kwa penzi la
mtandaoni.
"Adam stop blaming me!!(Adam usinilaumu)" alipiga
kelele kwa nguvu Reshmail bila kujitambua.
Mwalimu alimshangaa
na hakuelewa kilikuwa kimemsibu nini "Is she dreaming? (Anaota?)" aliuliza
mwalimu Sijjo aliyekuwa anawafundisha somo la mawasiliano (Communication
skills),darasa zima likacheka kwa fujo sana,lakini Reshmail alikuwa analia huku
akitetemeka sana,kwa ghadhabu akasimama na kutoka nje.
Japo
ulikuwa ni mwezi mmoja tu tangu waanze masomo ya mwaka wa pili
lakini
tabu na mateso aliyokuwa ameyapata yalitosha kumshawishi kuwa
huenda amesoma hapo kwa miaka kumi.Wazazi wake hawakuwa na la kufanya,Eveline
alibaki kumwonea huruma shoga yake huyu alijaribu mara kwa mara kumpigia simu
lakini haikuwa tiba ya tatizo la Reshmail.
Ni kweli Reshmail
asingeweza kujilazimisha kuwa na furaha kwani ni yeye aliyemshawishi Adam awe
nae kimapenzi na ni yeye huyuhuyu alimshawishi Adam aende kwao kwa ajili ya
kujitambulisha na safari hiyo ikawa ya mwisho ya
Adam.
"Nikiwaambia waalimu wangu watanielewaje,na hata
wakinielewa itakuwaje wanafunzi wenzangu wakijua siri hii? watajenga picha gani
tena kuhusu mimi, mh! niepushe na hali hi bwana,kama uliweza kuniondolea mawazo
haya hadi nikamaliza kidato cha sita vyema hebu baba na sasa ondoa tena na hili
jaribu zito mbele yangu na jina lako lisifiwe."
aliweka ombi
fupi Reshmail katika mawazo yake hayo. Lilikuwa ni jambo gumu sana kwa Reshmail
alikonda sana na punde si punde maneno ya wakosaji yakaanza tena "Mh! kumbe ndio
maana anakataa wanaume kumbe anaishi kwa matumaini maskini,dada mrembo kama
huyu" yalisikika maneno hayo katika vijiwe vya wanafunzi pale
chuoni.
Ilikuwa ni kero kubwa kila alipokatiza vidole
vilimwelekea yeye umaarufu wake wa awali kwamba ni mrembo ukaongezeka maradufu
karibia chuo kizima lakini wakati huu ilikuwa ni sifa mbaya kwamba ana virusi
vya UKIMWI hata yeye aliyasikia maneno hayo yalikuwa yakivuma kwa kasi,hakuwa na
uwezo wa kuzuia tetesi hizo
"Wangejua kwamba mi ni bikra na
wanayoyasema yote ni uongo,hata wasingenyanyua midomo yao michafu kuropoka
upuuzi huo,lakini bila Adam watajuaje?" alijiuliza Reshmail akiwa chumbani mwake
katika hosteli ya Ngulelo aliyokuwa amepanga chumba alichoishi peke yake.
Marafiki zake taratibu wakaanza kumtenga wakiamini ameathirika,hilo
halikumuumiza kichwa kwani alilitegemea sana hasa hasa dhana ya unyanyapaa kwa
waathirika iliyokuwa inatawala chuoni
hapo.
***
Bite alifanikiwa kutoroka katika
ngome ile kubwa aliyokuwa amehifadhiwa Adam. Kwa jinsi alivyokuwa amezoeleka
pale haikumchukua muda mrefu kumshawishi mlinzi amfungulie geti atoke kidogo na
ndio ikawa jumla hakwenda mbali sana na mkoa wa Iringa bali aliweka kambi yake
maeneo ya Uyole Mbeya mkoa uliopo jirani na Iringa ambapo kipesa kidogo
alichoondoka nacho pale ndani alifungua kibanda chake sokoni na kupanga nyumba
eneo jirani la Igawilo akianzia maisha ya kulala chini hadi aliponunua
godoro.
Biashara ya kuuza nyanya na mbogamboga ilimkimu sana
maisha yake kwani wazo wala tegemeo lake halikuwa kununua gari,au kujenga nyumba
hapana lengo lake lilikuwa uhai pekee,na shilngi elfu moja alizozipata zilikuwa
zinamtosha kabisa.
Alikuwa mchangamfu na mstaarabu sana,wateja
walivutika kwake kwa kasi kufaidi ukarimu wake katika biashara.Tumbo lake
lilianza kukua taratibu,kina mama sokoni wakaanza kuhisi tayari Bite kapata
mjanja Mbeya amemjaza mimba,lakini miezi yake ya kujifungua ndiyo ilifungua
akili za waliokuwa na maswali na kugundua kwamba ile mimba alikuja nayo pale na
sio kwamba aliipatia pale. Salama bin salmin Bite alijifungua mtoto wa kiume
miezi tisa ilipowadia.
"Mh! baba yake atafurahi tena alimpa
jina pale tu nilipomwambia nimeshika mimba" Bite kwa furaha tele aliwaambia kina
mama wa pale sokoni,akiwemo jirani yake mama wawili,ni hao ndio walikuwa ndugu
zake.
"Hongera Bite,sijui ndio unakuwa mama nani vile" Bite
alihojiwa na mama wawili
"Mwanangu anaitwa Christian" alijibu
Bite huku akibusu kichanga chake hicho ambacho kilikuwa kinarusharusha miguu na
mikono yake huku na huko.
Christian alizaliwa akiwa na afya
tele na hakusumbuliwa na magonjwa wakati wa ukuaji wake mwaka wa kwanza,ilikuwa
furaha kubwa kwa mama
yake.
**************
Miaka ilizidi kukatika
wazo la Bi. Gaudencia kumtoa Adam katika jumba lile lilikuwepo kichwani mwake
kwani udhaifu alioupata Reshmail pamoja na kashfa mbaya anazozipata pale chuoni
zilimsononesha sana lakini ataanzia wapi kuificha aibu yake pale ambapo
Adam,akasababisha uovu wa mama huyu uwekwe hadharani.
Ni jambo
hilo lililomuumiza kichwa mama huyu.
"Reshmail na baba yake
watanielewaje kwa mabaya niliyowafanyia,nimeishusha heshima ya mume wangu
aliyekuwa na heshima kubwa bungeni" alizidi kuwaza
Huku Iringa
maeneo ya Ruaha Adam alikuwa anauanza mwaka wa tatu,akiishi kama nyumbani
kwake,lakini hakuridhika hata kidogo maisha hayo ya
ufungwa.
Miaka mitatu ilikuwa mingi sana "Mama na baba yangu
wanahisi niko wapi? vipi kuhusu mpenzi wangu Reshmail,hapana imetosha nahitaji
kutoka hapa,lakini lazima nijiulize nitatoka vipi hapa katika ngome hii"
alijisisitiza Adam japo ulinzi madhubuti ulioongezwa kutokana na kutoroka kwa
Bite katika mazingira ya kutatanisha pale
ngomeni
***
Mwaka wa pili uliisha hivyohivyo
kimateso makali yaliyojawa na kumbukumbu mbaya na isingekuwa kuhamishwa kwa
darasa la sheria mwaka wa pili kwenda katika maghorofa ya Mwanjonde chuoni hapo
basi Reshmail angefeli vibaya masomo yake kutokana na msongo wa
mawazo.
Akiwa mwaka wa tatu afya yake ilirejea tele kwani
hakuwa akiiona tena picha kubwa ya Adam machoni pake hali hiyo ya afya kurejea
ilizusha msemo mpya tena,tofauti na mwanzo walivyosema ana Ukimwi,sasa walisema
"Akikonda ana virusi,akinenepa ameanza kutumia dozi"
Yote hayo
alituhumiwa Reshmail lakini kamwe hakuwahi kuthubutu kunyanyua mdomo wake kujibu
vijembe hivyo yeye alikuwa mkimya huku akipambana na masomo hadi alipoumaliza
mwaka wake wa nne vyema.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment