Search This Blog

Friday, November 18, 2022

KAZI ZA NDANI NCHINI OMAN ZILIVYONIKUTANISHA NA KIFO - 5

 





    Simulizi : Kazi Za Ndani Nchini Oman Zilivyonikutanisha Na Kifo
    Sehemu Ya Tano (5)






    “Jina lako nani?”

    “Nani?”

    “Wewe hapo..”

    “Jina langu....jina langu... jina langu, nimelisahau!!!!”

    “Pole sana binti”

    “Pole ya nini?”

    “Umeokolewa na wanajeshi wa majini waliokuwa katika Nyambizi baharini...Unaijua Nyambizi?

    “Sijui, ni kitu gani?”

    “Nyambizi ni manowari, zinazotembea chini ya maji kama samaki, wanajeshi wa UN kutoka Ujerumani, walikuwa wanasafari na Nyambizi hiyo kwenda Syria, ndio walioyaokoa maisha yako ukiwa katika hatua za mwisho.”



    Yalikuwa ni mazungumzo ya daktari mmoja akiongea na mimi niliyekuwa kitandani.



    Kauli ya mwisho ya daktari huyo ndiyo iliyofungua milango ya kumbukumbu zangu, mtiririko wa kumbukumbu zilianza kujaa kwenye kichwa changu mithili ya simu iliyokuwa imezimwa data kwa muda mrefu na sasa imefunguliwa.

    “Mungu wangu!”nilimaka.

    “Nini?”

    “Nimekumbuka kila kitu...”

    “Kweli?”

    “Kabisa.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haya sema, jina alako unaitwa nani?”

    “Naitwa Agripina”

    “Kwa nini ulitupwa baharini?”

    “Ni stori ndefu, ila nataka kujua hapa niko wapi?”

    “Upo hosptali ya Ahlal bayty mjini Muscut.”

    “Unataka kuniambia nimerudi nchini Oman?”

    “Hujarudi ila umeletwa na wanajeshi wa kulinda amani nchini Syria”

    Nilishindwa kuelewa kama nilitakiwa kufurahia ama kulia, nchi ya Omani kwangu ilikuwa siyo sehemu rafiki, sikutamani kabisa kuendelea kuishi juu ya mgongo wa ardhi ya nchi hiyo.

    Pamoja na kufikiria yote hayo mwisho wa siku nilimshukuru Mungu kwa kuendelea kuonyesha miujiza ya ajabu kabisa kwenye maisha yangu na kunifanya niendelee kuwa hai.

    Nililala pale kitandani kwa masaa mengi hadi badaye aliporudi tena yule daktari niliyekuwa nikizungumza naye.

    “Ulisema jina lako unaitwa Agripina?”

    “Ndiyo” nilijibu kisha nikamwona akiandika kwenye kitabu chake kidogo na kuondoka.

    Akaondoka, kama dakika kumi akarudi tena akiwa ameongozana na watu wengine wawili mwanaume na mwanamke. Wakaja na kukizunguka kitanda changu.

    “Agripina” aliniita.

    “Abee”

    “Unamfahamu huyu dada?” alisema akimsonta binti aliyeingia naye mule ndani.

    Nilipo mtizama vizuri yule binti nikamkumbuka.



    Ni msichana ambaye siku moja alinikuta ndani ya chumba nilichokimbilia kujificha nikiwa nakimbizwa na wanajeshi, baada ya kuzinduka mochwari.



    Katika maficho, nilimkuta mwanaume anayekaribia kukata roho, ambapo muda kidogo akaja huyo msichana, kutokana na mazingira tete aliyonikuta nayo binti huyo wa kiarabu, moja kwa moja akaamini nahusika na kifo cha mtu ambaye inasemekana alikuwa ni kaka yake..



    “Nisha mkumbuka”

    “Basi upo chini ya ulinzi kwa makosa ya mauwaji ya kaka yake, lakini pia kwa makosa mengine ya kutishia kuua na kufanya zinaa ndani ya nchi hii,” alidakiza yule jamaa mwingine aliyeongozana na daktari.

    Alitoa pingu na kunifunga. Angalau safari hii sikuwa na hofu hata kidogo, matukio na mikasa kwenye maisha yangu ilinifanya kuwa na moyo mgumu kama jiwe, kuna wakati kufa, niliona ni kitu cha kawaida. Muda wowote naweza kufariki. Ni kawaida. Nilichokuwa nangoja kwa wakati huo ni siku muda tu mauti.

    “Nafikiri hutakiwi kuendelea kulalia kitanda cha hosptali hii, utatakiwa kupelekwa selo kisha mahakamani, badaye utumikekie adhabu ya makosa yako,” alisema tena yule ofisa, ni kama naye alikwisha nihukumu kabisa bila kuthibitisha.



    Nilichukuliwa na kupelekwa selo, haikuwa selo ile ambayo niliwahi kupelekwa kipindi cha nyuma. Hii ilikuwa ni tofauti. Hii ilikuwa ni selo ambayo haikuwa na tofauti na zile za nchini kwetu. Na nilichokikuta ndani ya selo hizo niliogopa sana.

    Kulikuwa na utitiri wa wasichana wa Kitanzania ambao walikuwa ni mahabusu na wafungwa wenye mashitaka mbalimbali wengine walisha hukumiwa kifo huku wengine wakiongoja hukumu. Wengi wao walikuwa ni wasichana waliokwenda kufanya kazi za ndani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pamoja na hali hiyo ya kutisha, kwa mara ya kwanza nilijihisi siko peke yangu katika ulimwengu, kitendo cha kukutana na Watanzani wenzangu ambao wengi wao walikuwa ni wenyeji wa Zanzibar, Tanga, Singida na Dar es salam ilinipa faraja kubwa. Waswahili husema, kifo cha wengi harusi.

    Mara nyingi tulikaa pamoja na kuzungumza mambo mengi ya nyumbani Tanzania.

    Kila mtu alikuwa na kiu ya kurudi nyumbani lakini hilo lilibaki kuwa ndoto ya mwendawazimu nyuma ya milango ya nondo.

    Siku chache badaye, nilipelekwa mahakamani, sikuwa na imani na mahakama za nchi hiyo, namna kesi zilivyo endeshwa kwakweli zilimnyima mtuhumiwa haki ya kijitetea kwa kiwango kikubwa, na hili ilikuwa hsa kwa watu weusi.

    Hata balozi zetu huko, hazijali watu wake, zimevaa miwani nyeusi na kujifanya haijua wala kuona madhila wanayoyapata ndugu zao. Kuna wakati niliandika barua ubalozini kuomba msaada wa mwanasheria ambaye ataninusuru na kitanzani.

    Hata hivyo, sikupata majibu hadi siku ya hukumu. Ubalozi wa nchi yangu ulitupa kisogo kwa asilimi kubwa. Hatukuthaminiwa kama ambavyo raia wa kigeni wanavyo thamaniwa na balozi zao nchini mwetu.

    Nilihukuwa kifo. Hakimu alisema ilisema, Kwa kuwa nilisha wahi kunyongwa na mahakama za kijeshi kwa kamba, nikarudiwa na fahamu nikiwa mochwari, safari hii nilihukumiwa kuchomwa sindano ya sumu hadi kufa.

    “Haki pekee anayopewa mshtakiwa ni mwili wake kusafirishwa nchini kwao ama kijijini kwao kwa ajili ya mazishi yake.” Alisema, kisha akagonga nyundo mezani.

    Nilishukuru japo kwa hilo kwani niliona angalau sasa ndugu zangu watapata fursa ya kuona maiti yangu na kuzikwa kwenye ardhi ya nchi yangu. Kama nilivyosema, nafsi yangu haikuogopa kufa, ila kilichoniumiza ni kufa nikiwa na mtoto tumboni, hilo liliniliza machozi.





    “Usilie Agripina ndivyo maisha yalivyo, hujafa hujaumbika” mtu mmoja mwenyeji wa Kigoma alinipa moyo.

    “Silii kwa sababu ya hukumu, namlilia mwanangu aliye tumboni”

    “Una mtoto tumboni?”

    “Ndio.”

    “Nafikiri huwezi kutumikia adhabu ya kifo hadi pale utakapokuwa umejifungua mtoto.”

    “Labda ngoja tusubiri,” nilisema kinyonge huku matone ya machozi yakijikusanya kwenye macho yangu.

    Siku, wiki na miezi ikayoyoma, niliendelea kuishi ndani ya gereza kama mfungwa ninayesubiri siku ya kutumikia adhabu yangu ya kifo. Wakati nikingoja siku ya hukumu pia tumbo langu lilizidi kuwa kubwa.

    Siku moja nikafuatwa na askari magereza walikuwa kama sita, mikononi mwao walibeba bunduki. Walinizunguka huku wakionekana kuwa makini na mimi, mmoja miongoni mwao akanisogelea na kunieleza ilibaki wiki moja tu kabla ya kutumikia adhabu yangu ya kifo.

    Nilihisi mate mepesi yakijaa mdomoni, pamoja na kwamba nilikuwa sina hofu dhidi ya kifo lakini kwa mara ya kwanza nikahisi mwili ukinisisimka, hofu ikanisambaa kifuani mwangu, taswira ya tukio la mtu kunyongwa likajitengenza kwenye akili yangu, kwa kweli niliogopa mno.

    Walipoondoka wale askari, wafungwa wenzangu walinifuata na kuniuliza nilikuwa naambiwa nini. Niliwaeleza yote nilioambiwa na wale askari wa kiarabu, simanzi na hofu ilienea katika nyuso za wafungwa hasa Watanzania wenzangu ambao pia walihukumiwa kifo.

    “Ndiyo maana wameanza kuwa makini na wewe, kuanzia leo unaweza usiwe na sisi tena ndani ya selo. Siku za mfungwa kunyongwa zikikaribia huwa anawekwa mbali na watu kwa imani kwamba anaweza kufanya lolote dhidi ya mtu yeyote ili mradi asife peke yake,” alisema mfungwa mmoja miongoni mwa waliokuja kunipa pole.

    Saa kumi na mbili jioni nilijiwa tena na wale askari wenye bunduki, kama alivyonieleza yule mfungwa mwezangu nilihamishwa na kupelekwa katika selo ya peke yangu. Niliingizwa kwenye chumba kimoja kizuri ambacho kilikuwa na kila kitu cha thamani, chumba hicho kilikuwa ndani ya jela hiyo.

    Sikujua mantiki ya kuingizwa kwenye chumba nadhifu ingawa wakati mwingine nilihisi hizo ni itifaki za kumkirimu mtu ambaye hukumu yake ya kifo ipo jirani, hata hivyo wakati mwingine nilipingana na fikra hizo kwa kuwa mwanzoni nilipohukumiwa kifo, sikufanyiwa ikhisani ya mambo haya.

    Niliishi ndani ya chumba kile nadhifu, kila siku nikiletewa vyakula vizuri ambavyo nafikiri vingine sijawahi kuvila hadi leo ninaposimulia mkasa huu. Wiki ile moja ilienda harakaharaka, hatimaye siku ya hukumu ikafika.

    Walikuja askari wenye bunduki na kunitoa nje ya chumba kile, nilifungwa minyororo miguuni, mnyororo huo ukaunganishwa na shingo yangu ukapita hadi mikononi, kisha nikavikwa soksi nyeusi usoni.

    Nilishikwa bega kwa nguvu na askari mmoja miongoni mwa waliokuwa wamenizunguka huku mkono mmoja wa askari yule ukiwa umekamata silaha yake vizuri.

    Akawa ananiongoza na kunipeleka mahali nisikokujua, mapigo yangu ya moyo yakawa yananidunda “duk duk duk” nikaanza kutokwa jasho mwilini, hofu ya kifo ikawa kubwa, hatimaye nikaanza kulia, machozi na kamasi vilinitoka ndani ya ile soksi nyeusi iliyofunika uso wangu. Hata hivyo hakuna aliyejali hilo..

    Nilifikishwa ndani ya chumba kimoja ambacho kilikuwa na baridi kali kisha nikaondolewa ile soksi usoni, nikashangaa nilipojikuta nipo ndani ya mochwari, moyo wangu ukalipuka “paaa” niliogopa.

    Ndugu msomaji hapa ngoja niseme kitu. Hakuna hukumu mbaya ambayo inavuruga saikorojia ya mtu kama hukumu ya kifo, kama wadau wa sheria watapata bahati ya kusoma maandishi haya ni vema wakafanyia marekebisho sheria hii katika taifa letu, kwani sheria hii inamtafuna binadamu kisaikolojia kabla ya kuitumikia.

    Baadhi ya nchi za ulaya na Marekani, sheria ya hukumu ya kifo haipo kidogo na baadhi ya nchi za Afrika, lakini kwa bara la Asia bado sheria hii inaendelea kutesa saikolojia ya binadamu kwa kiwango kibaya sana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kujiona nipo ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti nilianza kuhisi kizunguzungu, maiti nyingi zilikuwa zimetapakaa chini huku zikiwa zimefunikwa kwa mashuka meupe, kulikuwa na harufu kama ya jiki (ile dawa ya kuondoa madoa), nikatambua hiyo ni dawa ambazo maiti zile zimedungwa kwenye miili yao ili pengine zisiharibike.

    Nafsi yangu ikazidi kuzongwa na jinamzi la hofu baada ya kubaini kuwa kumbe na mimi dakika chache nitakuwa maiti kama zile zilizolazwa pale chini kisha nitachomwa sindano yenye dawa ambayo ina harufu ya jiki kisha nitalazwa chini na kufunikwa shuka jeupe nikingoja kuzikwa.

    “Mlazeni juu ya kitanda” alisema daktari huku akivuta sumu kwa kutumia sindano kwenye kichupa kidogo.

    Nilishikwa na askari wawili nikalazwa juu ya kitanda, nikawa nimelala chali, mtoto wangu aliyekuwa tumboni nikamsikia akichezacheza. Machozi yalinitoka.

    “Tutaonana mbinguni kwa baba mwanangu, samahani kwa kutumikia adhabu yangu, Labda pengine ni sahihi tu kufa na mama yako. Kama usipokufa sasa utakufa baadae kwa Ukimwi ambao naamini tayari nimekwisha kuambukiza.”

    Nilinong’ona huku nikisubiri kudungwa sindano yenye sumu hadi kufa. Nilimwona daktari yule akiinyanyua sindano iliyokuwa imejazwa dawa ya Tetrodotoxin ambayo ni sumu maalumu kwa kuulia watu waliohukumiwa kifo, akaibonyeza kidogo ile sindano, matone madogo ya sumu yakaruka angani, kisha akanisogelea pale kitandani nilipolazwa tayari mkononi akiwa amekamata sindano ya SUMU.

    “Nina mimba jamani, msiniue,” nilisema huku nikilia, macho yangu yakimtizama mtu yule kwa huruma.

    “Nina mtoto tumboni baba yangu niache tafadhali, usinichome sindano ya sumu,” niliendela kulalama, hakuna kilicho badilika. Mtu huyo hakuwa na muda na mimi, alionekana alikwisha zoea huruma zile. Kwahiyo jambo lile mbele yake ilikuwa ni kitu cha kawaida. Hakunijali kabisa hata usoni hakuniangalia.

    Alitizama saa yake ya mkononi nikaona ameganda kwenye saa hiyo. Ni kama alikuwa akingoja muda fulani uwadie ndipo afanye kazi yake. Naam! hisia zangu zilikuwa sahihi, baada ya sekunde kadhaa akanigeukia tena na kunikabili:

    “Mfungeni mikanda,” alitoa amri. Askari wenye bunduki wakaanza kufanya kazi hiyo. Pamoja na kwamba nilifumgwa minyororo kwenye mikono na miguu lakini nilifungwa tena mikanda.

    Nikawa siwezi kufurukuta. Daktari yule alinisogelea tena akiwa na sindano mkononi, akanijia usawa wa shingo yangu kisha akaniinamia na kunidunga sindano ile ya sumu kwenye shingo yangu.

    Nilifumba macho wakati tendo hilo linafanyika ingawa niliusikia uchungu wa sindano ile hasa wakati daktari anaibinya sumu ya Tetrodotoxin kuingia ndani ya mishipa ya mwili wangu.

    Sekunde tatu zilitosha kunifanya nianze kuona maluweluwe, nikajiona napatwa na maumivu makali mwili wote, yalikuwa ni maumivu kama vile nababuliwa na moto, nikataka kupiga kelele mdomo nao ukawa mzito, mara povu zito likaanza kunitoka modomoni, damu ikanitoka puani .

    Giza la ajabu likazikumba mboni zangu, muda mfupi badaye sikujua tena kilicho endelea duniani.

    Toba!!

    Nimekufa!!!.





    *********

    “Agripina, we’ Agripina...Agripina amka...Amka upesi!” nilisikia sauti ikiniamsha, sauti hiyo haikuwa ngeni masikioni mwangu, nilifumbua macho kivivu, ingawa niliona kwa mbali lakini sura ya mtu ninaye mfahamu ilijidhihilisha mbele yangu.

    “Mama!”

    “Bee mwanangu.”

    “Nmekufa na mungu ameniingiza peponi!”

    “Hahaha! hapana mwanangu. Upo kijiji cha Makose wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, hujafa”

    “Nipo Makose!i inamaana niko Tanzania?” niliuliza huku macho yangu yakitizama huku na kule ndani ya chumba ambacho pia hakikuwa kigeni machoni mwangu.

    Kabla mama yangu hajanipa jibu mara akaingia mtu ambaye sikumtegemea kumwona. A likuwa ni Mariamu Rashidi huyu ni yule wakala wa wasichana wa kazi wanaokwenda kufanya kazi za ndani nchini ya Oman, alikuja na kuketi karibu yangu.

    “Mambo Agripina, naona mzimu wa kifo uliokukumba Oman umekurejesha Duniani,” alisema kwa masikhara huku akiachia tabasamu pana na kuketi karibu yangu.

    Nikiwa sijakaa sawa nikendelea kushangazwa na utitiri wa ndugu walioingia ndani ya chumba kile nilichokuwa nimelala. Kila ndugu aliyekuja kuniona alionekana kufurahi kwa kuona nikiwa hai.

    “Naombeni tusikilizane jamani,” alisema Mariamu. Ndugu wote waliokuwa mule ndani wakanyamaza.

    “Kila mtu angependa kujua nini kilifanyika hadi Agripina kwa sasa yupo hai ilihali taarifa zilienea kuwa tayari binti huyu kisha chomwa sindano ya sumu na kafa...” aliposema sentesi hiyo watu wote walijenga utulivu zaidi ili kujua nini kilitokea.

    “Kwanza kabisa shukrani na pongezi zote anastahili Mwenyezi Mungu kwakuwa ni yeye ndiye anayejua nini hatma ya maisha ya mja wake. Agripina alikuwa katika hukumu ya kifo na alikwisha ingizwa katika chumba cha kuhifadhia maiti tayari kwa kuchomwa sindano yenye sumu.

    “Kitu ambacho wanajeshi na serikali ya nchi ya Oman hawafahamu hadi sasa ni kwamba mtu anayehusika na kutoa adhabu ya kuwachoma watu sindano ya sumu nilimuhonga Dolla zaidi ya 2000/= ili mradi afanye lolote lile kumwepusha binti huyu na kifo.

    “Siku ya hukumu ya Agripina ilipowadia mipango yote ilikuwa sawa, alichofanya mtu yule ni kumdunga Agripina sindano yenye dawa ya Ketamine benzodiazepine ambayo ilimfanya apatwe na maumivu makali sanjari na kumtoa povu mdomoni lakini ambacho askari waliokuwa hawajui ni kwamba chupa yenye sumu aina ya tetrodotoxin chupa hiyo ilikuwa na dawa ya benzodiazepine ambayo ilikuwa ni dawa ya usingizi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Baada ya Agripina kupoteza fahamu kilichofuata ilikuwa ni kuusafirisha mwili ndani ya jeneza, kama ambavyo mahakama ya nchi ile ilivyokuwa imeahidi, kwa hiyo tulimsafirisha Agripina akiwa kama maiti hadi hapa Tanzania. Hivyo ndivyo ilivyokuwa jamani...” alimaliza kusimulia Mariamu.

    Kila mtu mule ndani maelezo yale yalimsisimua mno. kwa kweli hata mimi nafsi yangu ilikiri kuwa Mungu hashindwi na jambo. Nilipewa pole nyingi na ndugu na jamaa, ilikuwa ni furaha kubwa mno kwa mama yangu, wakati wote alikuwa akibubujikwa na machozi. Kwa upande wangu, jambo lile nililiona ni kama ndoto nzuri inayopita kichwani mwangu.

    Muda mfupi baadaye ilikuwa ni zamu yangu kusimulia mambo yote yaliyo nisibu tangu siku ya kwanza naikanyaga ardhi ya nchi ya Oman, hadi nagota nukta ya mwisho, kila kila mtu alibubujikwa machozi

    Ndugu zangu waliumizwa zaidi kusikia naisha na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, hata hivyo hapakuwa na mwenyekuweza kubadili ukweli wa jambo hilo.

    Maisha yaliendela kama kawaida nikiwa kijijini kwetu Makose. Miezi michache badaye, nilijifungua salama mtoto mzuri wa kiume, ambaye kwa bahati mbaya, alizaliwa akiwa anamambukizi ya virusi vya Ukimwi.

    Wito wangu kwa wasichana wenzangu wa kitanzani hasa wenye ndoto za kwenda kufanya kazi za ndani nchi za nje, ni vema mkawa makini huko mwendako, bila hivyo unaweza kujikuta unatumbukia katika shimo la mauti bila kutegemea.

    Jifunze kusimamia dhamira yako, kazi na mapenzi ni mafuta na maji, lakini pia ningependa mjifunze kupamabana hapa hapa nyumbani, kwani fursa zipo nyingi. Ukipatwa na tatizo hapa, ni rahisi kukabiliana nalo. Waswahili husema, zimwi likujualo halikuli likakwisha.

    Kabla ya kusema kwa heri. Napenda nimshukuru mwandishi wa mkasa huu wa maisha yangu. Kaka yangu, Ally katalambula, ambaye alibadilisha maelezo yangu na kuwa maandishi yaliyonakshiwa na kachumbali za kifasihi na kuchapwa kwa mara ya kwanza katika Gazeti la Risasi toleo la kila Jumatano kutoka Global Publishers.

    Haikuwa kazi rahisi kumsimulia mkasa huu hadi mwisho, kwani mara nyingi maelezo yangu yalikatishwa na kilio na simanzi kila nilipokuwa nikimweleza hadithi hii.



    ***



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ALLY KATALAMBULA:



    Agripina alifariki Dunia January 12 mwaka 2016 huko mjini Tanga kwa maradhi ya UKIMWI. Ameacha mtoto mmoja wa miaka 7 ambaye analelewa kwenye kituo cha watoto yatima cha Umra kilichopo Magomeni jijini Dar es salam.



    Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina leke lihimidiwe. Mungu na ailaze roho ya marehemu Agripina Joseph mahali pema peponi.



    MWISHOOOO


0 comments:

Post a Comment

Blog