IMEANDIKWA NA : HASSAN MBONECHE
*********************************************************************************
Simulizi :Iangalie Tuleane
*********************************************************************************
Simulizi :Iangalie Tuleane
Sehemu Ya Kwanza (1)
Tuleane ni kijiji kidogo. Kinapatikana kusini mwa bara la Afrika—chenye ukubwa upatao kilomita za mraba 9800. Kijiji hiki kimejaa asili. Kimepambwa na vitu mbalimbali vikiwemo mito, milima, mabonde na tambarare zenye kuvutia. Makazi ya watu wa Tuleane si ya kufungamana, pia si ya mtawanyiko wa maili nyingi—ni makazi ya wastani, ya kiwango cha kati.
Haiba na hulka ya Wa-tuleane si ya kumfukuza mgeni kipindi awaonapo, pia si ya kumwogopesha yeyote kwani wamejaliwa upendo baina yao.
Cha kustaajabisha, kila familia hutambulishwa kwa bendera iakisiyo hali ya familia ilivyo—kama ni ya tafrani, utulivu, upendo ama ni ya domo kasuku kwa umbea; yote husemwa na rangi ya bendera ipepeayo. Rangi zilizopo kwenye bendera ndizo hutoa ukweli wa tabia za kila familia.
Familia ya mzee Tualike Misifa ni miongoni mwa familia nyingi zilizomo ndani ya kijiji cha Tuleane. Kama ilivyo, bendera inayotambulisha tabia za ndani na nje ya familia hii ni yenye rangi nyeupe na wekundu kwa kiasi, pembeni mwa bendera, upande wa juu. Rangi nyekundu inatoa sauti kuwa, familia hii ni ya wapenda vurugu kiasi na rangi nyeupe inadokeza uwepo wa faraja na amani ya kutosha katikati ya sikitiko.
Familia ya mzee Tualike inaundwa na watu watano: baba, ambaye ni Tualike, mama aitwaye bi. Mwema Asononekaye na watoto watatu ambao ni Majungu, Jipendekezo na Laumio.
Kila mmoja ndani ya familia hii anayo majukumu yake japo upo wakati fulani hubadilishana nafasi ya utendaji. Hiyo hufanyika ili kujihakikishia ufanisi kwa kila jambo litendwalo.
Mzee Tualike ndiye mwamuzi wa familia__ huratibu mipango yote na kuhakikisha kilichopangwa kinatekelezeka, iwe kwa hiari ama kwa mabavu. Bi. Mwema Asononekaye ni msaidizi katika kiti cha mumewe—hutekeleza majukumu yote ya familia, ikiwemo mapishi, kuteka maji na kufanya usafi wa nyumba ili iwe safi muda wote. Majungu Kiungo Mkabaji ni mhakiki wa mapato na matumizi ya familia. Kila siku iendayo, mara nyingi akiwa katika nafasi hii huhakiki kuwa, kila kilichotumika kilitengwa kulingana na idadi ya watu waliopo. Huyu ni mbana matumizi. Jipendekezo Kiungo Mchezeshaji kazi yake kubwa ni kuhakikisha mafanikio hayakosekani nyumbani. Laumio ni beki, mzuiaji wa michomo langoni, huhakikisha usalama langoni wakati wote. Hivi ndivyo familia ya mzee Tualike Misifa ilivyo, lakini si muda wote kwani inategemea hali ya utendaji sanjari na hali ya uchumi wa familia ulivyo.
Ndani ya kijiji, mzee Tualike ni miongoni mwa wanaharakati wapiga domo, tena anayependwa sana na wananchi. Umahiri wake katika kuhubiri amani na upendo kila awapo katika mkusanyiko wa watu, kama bendera yao inavyoonyesha kuwa na fujo kiasi na amani tele, ulishampaisha kwa sifa na umaarufu. Hata kama yupo nyumbani, Tualike pia ni mhubiri juu ya maisha ya kila siku kwa uzao wake.
Juu ya uanaharakati wake, Tualike ni mwenye nguvu kubwa ,kiasi cha kuweza kuamuru jambo lolote litendeke kijijini hapo na kusitokee mtu wa kuupinga uamuzi wake. Ni mpenda shari wakati fulani. Ni mbabe inapobidi, iwe ndani ya familia hata kwa mambo ya nje ya nyumba yake. Kijiji kizima wanautambua msimamo wake—ni mtu wa njia moja mdomoni na katika matendo. Ni mwabudu wa kauli zake mwenyewe.
“Kokote muendako, onesheni bendera ya familia yetu—familia nyingine zote wapate kutambua,” anasema mzee Tualike Misifa. Hii ni rai yake kila siku kwa wanawe kila wanapoelekea kupata chakula.
“Hakuna shida baba, tunaahidi kufanya hivyo,” ndilo jibu pekee kutoka kwa wanawe, hujibu mara baada ya kumsikia baba yao akiwataka kutenda awazayo kuwa mema.
“Hakikisheni mnamfunga mdomo yeyote thubutuye kutamka jambo lolote baya juu yetu…iwe hapa kijijini na hata kwenye vijiji jirani.”
“Ondoa shaka mzee.”
Naam! Hawasiti kutii. Ni agizo kuzingatia, kumtii mzazi bila kujali mapungufu yake. Ilikuwa halali yao kufanya hivyo ili kumfurahisha. Kila mmoja kwa wakati wake ni mhubiri mzuri wa mambo ya familia yao, popote awapo. Uhubiri wa amani katikati ya nafsi zenye giza hukolezwa kwa viongozi mbalimbali wa kijiji, nao hufanya mahubiri ya aina hiyo ili jamii yao iwe na uelewa wa kutosha.
Wahenga walisema, palipo na moshi hapakosi moto—familia ya Tualike kadri ya muda unapozidi kusonga mbele ndipo dalili za kutokea moto mkubwa huonekana. Mifarakano inaibuka. Inapelekea manyanyaso kwa baadhi ya watu—Bi. Mwema Asononekaye na Laumio ni wahanga wa maamuzi ya Tualike na hulka zake. Wananyanyasika. Hawana sauti hata kama watatoa sauti kueleza hisia zao, wanapuuzwa. Wanabaguliwa kwa sababu wao ni wanawake.
“Sidhani kama ushauri wenu unaweza kuchukua nafasi katika fikra zangu,” anasema mzee Tualike akiwaambia bi. Mwema Asononekaye na Laumio. Ni usiku mmoja walipokuwa wanaomba yafanyike mabadiliko ya vyombo vya kufanyia usafi baada ya kubaini kuwa na hitilafu.
“Lakini tambua nasi tunayo mamlaka, kuamua katika familia hii ni haki yetu,” anapaza sauti Bi. Mwema.
“Sawa. Lakini sio kwangu na si kwa kiwango hicho mnachohitaji. Mimi ndiye mwamuzi, Alfa na Omega—daima nifanyacho sikosei,” mzee Tualike anagongelea msumari kauli yake. Anajiita Mungu mtu.
Mwishowe mama na bintiye wanaamua kutoroka. Wanataka waepukane na manyanyaso. Ni kweli wanayo mamlaka, lakini si ya kumshinda mzee Tualike, hata Majungu na Jipendekezo hawawezi hata kutikisa unywele kwa sauti kutoka kwa wanawake. Hivyo familia inabaki na watu watatu: mzee Tualike, Majungu pamoja na Jipendekezo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Habari ya kutoroka kwao inapata kusambaa kama upepo na kuufikia kila mlango na kila sikio la mzaliwa wa pale kijijini. Mzee Tualike, Majungu na Jipendekezo wanaingiwa fadhaa kwa kusikia habari hiyo. Wanapanga kufanya jambo ili kuzuia kuenea kwa habari hiyo. Watafanya nini kuweza kuzuia habari inayosafiri bure kutoka midomoni mwa wasengenyi na kutua masikioni mwa watu wenye kiu ya kupata habari za fitina? Yawapasa kufanya jambo lenye kushinda siri zote za ulimwengu.
Wanaamua kufunga mikaja na kujipiga vifua kuwa wanaweza. Wanaita waandishi wa habari ili wapate kuwahabarisha juu ya ukweli wa kilichotokea. Bado mashaka yanazunguka ndani ya fikra zao. Hawawezi kunena ukweli, yapo wanayoyaficha. Japo wanasema kwa upole kuelezea ukweli uliopinda, moyoni wanawaka moto, tena moto mkali unaoelekea kutua kwa yeyote aendaye kinyume na kemeo lao—kuwa uvumi huo uachwe mara moja kwani hauna ukweli.
Jumapili, Julai 25, familia ya mzee Tualike Misifa inapata mwaliko wa kuhudhuria kwenye hafla baada ya kuhitimu kwa wanafunzi wa darasa la saba, shule ya msingi ya Maziro, inayomilikiwa na kanisa la kijiji, Angalikana. Lakini hawakufanikiwa kuhudhuria wote, ni Jipendekezo na Majungu pekee ndio wanahudhuria. Hudhuria yao si ya kimyakimya bali imejaa tambo na mbwembwe huku wakipeperusha vyema bendera ya familia yao kama agizo. Watu wengi wanayo matarajio ya kuwaona wote watatu waliobaki katika familia, kikubwa kushinda ukubwa ni kupata kusikia maneno yenye ushahidi juu ya kutoweka kwa bi. Mwema na Laumio. Kuonekana kwa watu wawili pekee kunapunguza shauku ya kujichotea ukweli kutoka kwa vinywa vilivyo na muungano.
Hatimaye sherehe inaanza rasmi, saa 3:30 asubuhi kwa kuzingatia ratiba namna ilivyopangwa. Familia ya mzee Tualike inapata nafasi ya heshima, tena mwisho kabisa, ambapo wanapaswa kutoa hotuba kwa ufupi kisha maswali kuulizwa kutoka kwa wahitimu. Jipendekezo anasimama nyuma ya mimbari kisha kuanza kutoa hotuba kwa niaba ya familia nzima.
“Mnakuja uraiani, hivyo hatutarajii kupata vurugu kutoka kwenu. Njoeni mdumishe amani na upendo ili tuendelee kuwa mfano mzuri kwa vijiji jirani,” anasema Jipendekezo katika sehemu ya mwisho wa hotuba yake.
Hotuba yake fupi tu, baada ya hapo wahitimu wanaanza kuuliza maswali. Wengi wao wanauliza, tena maswali mazuri na Jipendekezo anayajibu kulingana na ufahamu alionao juu ya swali husika.
“Naomba swali la mwisho kutoka kwenu, muda sio rafiki kwangu,” anasema Jipendekezo baada ya kujibu maswali mengi kutoka kwa wahitimu. Jipendekezo ubongo umefubaa, kachoshwa na maswali ya papohapo.
Kimya kidogo kinatamalaki, takribani sekunde arobaini na saba, kisha anajitokeza msichana mwenye ulemavu wa ngozi akiwa na kikaratasi kidogo.
“Awetu Mbwela ndiyo jina langu. Watu wengi huniita mwandishi wa habari, kwa sababu ni kazi niipendayo na niifanyayo katika gazeti letu la kijiji, kwenye ukurasa wa makala uitwayo Kalamu yangu Msanifu wa ukurasa huo ni Hassan Mboneche, mwandishi wa makala iitwayo Tukutane usukumani, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya vyombo vya habari hapa kijijini. Nafarijika sana. Naamini hata wenzangu pia kwa kuhubiriwa maneno mazuri kutoka kwenu wamefarijika. Nikupe pongezi, nikuombe kuyatekeleza kwa vitendo maneno yako. Lakini, pongezi zangu hazitakuwa na thamani kama wangu mhubiri sio muumini wa maneno uliyotamka.
Jipendekezo, familia yenu huku nje inasifika kwa maneno hayo uliyotuhubiria, ila wenyewe mmekosa uumini wa maneno mnayoyahubiri, kiasi kwamba hadi watu wengine waliamua kuitoroka familia yenu na sasa mnatumia nguvu kubwa kukana.
“Mkononi nimekamata kikaratasi kidogo, nilichoachiwa na wale waliokimbia kwenu, ambao nilibahatika kukutana nao usiku walipokuwa wanatoroka. Maneno nitakayoyaongea hapa si ya kubuni kama msemavyo kila wakati ambao wale mnaowanyamazisha husimama na kusema, ni maneno yaliyoandikwa na wao na kuniomba nitumie siku ya leo kuwajuza watu wengi zaidi pia wapate kusikia. Hivyo, kabla sijaendelea, unanipa ridhaa ya kufanya hivyo?” Awetu anauliza na kutulia.
Jipendekezo anahema kwa nguvu na kutoa macho akimtazama Awetu, kijasho chembamba kinamtiririka—kinamsukuma kutoa kitambaa katika mfuko wa nyuma wa suruali ili kulikausha jasho. Anatazama pande zote kwa wasiwasi kisha anajikoholesha kidogo akinuia kusema jambo. Wakati hajazungumza lolote, ghafla simu yake inaaanza kuita. Anasita kuitoa kutoka kwenye mfuko alimoiweka japo mwishowe anafanikiwa. Analiangalia jina la aliyempigia. Anabaini aliyepiga ni baba yake mzazi. Anashituka na kujawa hofu. Kama la kufa na life, hata kama ni la kuvunda tena halina kutia ubani, anaamua kuijibu simu ile. “Sawa baba!” Hilo ndilo neno pekee analolitamka Jipendekezo katika maongezi na babaye. Anakata simu kisha anaitia simuye mfukoni. Anavuta tena pumzi na kuyarejesha macho kwa Awetu, kwa mara nyingine tayari kwa kujipa nafasi ya kuusoma ujumbe aliokabidhiwa kuufikisha.
“Endelea dada yangu,” anasema Jipendekezo huku akioneka katika hali ya kusubiria jambo fulani.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Awetu anashukuru na kukikunjua kijikaratasi alichonacho ili ausome ujumbe ulioandikwa. Anajikoholesha kidogo huku macho yakihama juu ya nyuso za watu walio makini wakimtazama. Analegeza kidogo tai iliyoshingoni mwake ili apate kupumua kwa nafasi..
“Sisi ni miongoni mwa watu wanaounda familia ya mwanaharakati, mzee Tualike Misifa. Tulikuwa na faraja sana katika familia hii hasa kutokana na umahiri wa kuhubiri amani na upendo katika kijiji chetu. Hakika tulifarijika kuwa waumini na mabalozi wa mahubiri popote tuendapo—hali iliyopelekea kuwavutia watu na vijiji vingine. Hatuna budi kutoa shukrani za dhati kwa mzee Tualike, Baba wa familia, aliyejidhatiti ili kijiji chetu kiwe imara kwa mambo haya. Nasi kama wasaidizi wa familia tulioamua kujitoa kwa moyo, hatuna budi kujipongeza.
Pongezi ziende kwa wananchi wa kijiji chetu na wale wavijiji jirani, waliojitoa kufanyia kazi kauli na jumbe mbalimbali tulizokuwa tunazihubiri. Daima mwalimu mzuri ni yule afundishaye jambo alilo na uelewa nalo ili ajitokezapo mtu wa kuhoji juu ya yale anayofundisha aweze kujibu kwa kujiamini. Pia msisahau kauli kwamba. mchungaji mwema ni yule atendaye yale ambayo huyahubiri kwa kondoo wake. Tuleane, tunakipenda sana kijiji chetu. Kwa maana hiyo, hatuna budi kuendelea kuishi kwa mahubiri yetu hadi siku zetu za mwisho.
Tunaipenda familia yetu na shughuli za kiharakati—za kuitaka jamii ya Tuleane itawaliwe kwa amani na upendo,” anasema Awetu na kutulia. Anaigeuza karatasi upande wa pili. anakohoa kidogo ili atake kumalizia kusoma. Kabla hajasema tena, mshereheshaji anataka kumkata hauli.
“Dada samahani, muda umetutupa mkono, tunaomba uishie hapo, utaufikisha ujumbe kwa jamii kwa kutumia njia nyingine. Sasa ni wasaa wa mgeni rasmi kukabidhi zawadi kwa wahitimu kabla muda mchache uliobaki tuhitimishe sherehe yetu.”
Alaaaah! Kwanini asiusome, amalizie! Wananchi wanateta. “Muda hauruhusu. Tunayo mambo mengi ya kuendelea nayo,” anaendelea kusema mshehereshaji.
Hatimaye zogo linazuka kwa kiasi fulani na muda mfupi tu ratiba inaendelea kama kawaida. Jipendekezo anarejea kwenye kiti. Anaketi na Awetu anaketi sehemu yake pia, akijawa na manung’uniko moyoni.
Saa 10:00 jioni sherehe inahitimishwa, watu wanaanza kurejea makwao. Kabla hawajaondoka, Jipendekezo na Majungu wanamtafuta Awetu na kumpata.
“Hongera binti, ujumbe wako ni mzuri. Naamini ipo siku tutakutana kisha unijuze kinagaubaga juu ya ujumbe wao uliokatishwa.
“Ahsante! Naamini pia itakuwa hivyo.”
“Sawa.Tukutakie heri na maisha mema,”anaendelea kusema Jipendekezo kisha wanaondoka.
****
Awetu alirejea nyumbani anakoishi na mlezi wake—shangazi yake ambaye ni kipofu. Akiongozana na wahitimu wenzake na baadhi ya wananchi, alifika nyumbani saa 11:41 jioni. Walimpongeza kwa alichofanya kisha kumbandika majina mengi kulingana na tukio lile. Walimwita shujaa naye alifurahia tunu ya jina jipya lililokuwa maarufu.
Jioni ile alibadili mavazi na kuondoka. Safari yake haikuwa ya kwenda mbali kwani alizipita nyumba tatu tu na kuifikia ile aliyokusudia kuwa kituo cha barizi yake wakati ule wa jua kutua. Ilikuwa mahali penye banda la chumba kimoja.
Alibisha hodi, akafunguliwa. Kabla hajaingia ndani aliangaza macho yake kutazama kila mahali. Ndani ya banda alikutana na watu wawili, walifurahia kufika kwake mahali pale. Kila tabasamu alilooneshwa naye hakusita kuonesha furaha kama jibu kwa mapokezi ya bashasha. Alivuta kigoda akaketi yangali macho yakiwa hayajabanduka kutoka kwa wenyeji wake. “Hongera, tumeona ulichofanya,” alisema mmoja ya watu wale aliowakuta bandani.
“Tuhongere sote. Pamoja na hayo, kwa hiki nilichofanya nahisi wanaweza kututafuta sote watatu. Bila shaka mnafahamu siku za usoni lipo zoezi la uchaguzi wa serikali ya kijiji. Inasemekana mzee wao anahitaji kugombea.”
“Sahihi! Wanaweza kufanya hivyo ili watupokonye huu ujumbe. Lakini kabla hawajatekeleza hilo, tunakuomba uuwasilishe mapema ujumbe huu kwa jamii ili ipate kuwatambua. Nakuomba andika hata gazetini siku ya kesho.”
“Siku ya kesho sina nafasi—hadi kesho kutwa.”
“Kwa hiyo utatusaidia vipi?”
“Tuisubiri hiyo kesho kutwa.”
“Hapana. Huogopi kama wanaweza kufanya jambo lolote ndani ya muda huu hadi kuifikia hiyo siku unayosema?”
“Sidhani! Ninao uhakika, hawatakuwa na uwezo kwa sasa.”
“Sina hakika na kauli yako, ila acha tuone itakavyokuwa.”
Baada ya maongezi ya muda mrefu waliagana. walikubaliana siku ya pili kutoka wakati waliokutana ndipo Awetu auweke gazetini ujumbe aliokuwa anausoma kwenye sherehe. Awetu alirejea nyumbani kwao tayari kwa kuandaa makala kama ambavyo walikubaliana ili wasubiri siku maalumu ya uchapaji. Alifanya hivyo kwa kusudi la moyo wake tena kwa kutumia kompyuta mpakato aliyonayo.
“Huu ndio mwisho wa maigizo yenu,” alisema Awetu baada ya kuandika nukta ya mwisho kukamilisha makala yake.
Wakati huo Jipendekezo na Majungu, baada ya kurejea nyumbani walifikia kwenye kikao cha dharura na baba yao. Mzee Tualike Misifa alikasirishwa na kilichotokea. “Wanakijiji watakuwa na hamu kubwa ya kujua kilichokuwa kinafuata kusomwa. Hivyo basi, kabla hamu yao haijaanza kuwa na uhitaji mkubwa, lazima wahusika watiwe mkononi,” alisema mzee Tualike.
“Tupo tayari kutekeleza chochote mzee wetu.”
“Msifanye mzaha katika hili. Mkifanya masihara dhamira yetu ya kuongoza hiki kijiji itatoweka,” alisema mzee Tualike kwa sauti kali iliyojaa ngurumo na kufanya mate kumrukaruka.
“Sawa, lazima tuwashughulikie,”walijibu wote kwa pamoja.
Utekelezaji wa kile walichokuwa wanazungumza na baba yao ulianza siku hiyohiyo, mara baada ya kuhitimisha kikao cha dharura. Mpango madhubuti uliandaliwa. Usiku wa saa nne Jipendekezo aliambatana na Majungu kwenda hadi kule anakoishi Awetu, wakiwa katika muonekano tofauti na uhalisia wao. Walivaa makoti marefu meusi, yaliyoishia chini ya magoti, buti kubwa nyeusi na glovu pia boshori nyeusi kichwani zilizoshuka hadi kidevuni, zikiwa na tundu nne zilizoonesha macho, pua na mdomo. Dhana za utendaji ambazo ni wembe, kisu, koleo na bisibisi hazikukosekana pamoja na chupa kadhaa zenye sumu ndani yake—wakiwa wamehifadhi katika mifuko ya makoti waliyovaa.
Walifika mahali walipokusudia kuwa na kusimama umbali wa mita mbili kutoka mlangoni—kabla hawajaanza kufanya kile walichodhamiria. Walijadiliana pasipo kujua kuwa watu waliokuwemo ndani walisikia kila neno lao.
“Jipendekezo! Wa muhimu ni wale waliotoroka, huyu atukabidhi ule ujumbe na atueleze ni namna gani alivyokutana nao na wapi wameelekea. Tukimfanyia jambo baya jamii inaweza kutuhisi vibaya.”
“Unataka kupingana na mzee? Tukiachana na huyu lazima ataharibu mambo.”
“Sawa. Ila kuna mtu anaishi naye humu ndani?”
“Ndiyo, lakini hawezi kufanya lolote, ni kipofu.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimekuelewa! Tufanye kilichotuleta,” alisema Majungu kisha wakasogea mlangoni. Walibisha hodi kwa sauti ya chini ili walio nyumba jirani wasisikie.
Mlango ulifunguliwa, mama mwenye umri kati ya miaka arobaini na saba alijitokeza. Mwanga wa kibatari kilichokuwa kikimulika katikati ya giza uliwapa nafasi ya kumtambua mama yule kwa umbo lake—alikuwa ndiye kipofu, asiye na uono wa uhakika kwa waliowasili. “Nani? Watoto wa baba Mchungaji?” aliuliza shangazi yake Awetu, Bi. Mwamini Ndembe.
Jipendekezo akasogeza kopo mdomoni ili apate kuzungumza pasipo kujulikana. “Hapana. Sisi ni watoto wa mzee Radi, aishiye kijiji kilichopo kando ya mlima Naparavi, ukivuka mto Naishelo,” alijibu Jipendekezo kwa kuongopa, sauti ikiwa imebadilika kabisa. Alihofia sauti yake kufahamika kwa wengi kutokana na mahubiri ya kila mara aliyokuwa akiyafanya.
“Naweza kuwasaidia?”
“Ndiyo, tuna shida na Awetu.”
“Usiku huu— shida gani?”
“Ni siri mama, hivyo tunaomba tuongee naye.”
“Nitawaaminije?”
“Tuamini, hatuna nia mbaya. Mjuze kuwa, watoto wa Mzee Radi wamefika, haraka ataelewa.”
“Basi subirini nimwamshe maana kalala,” alisema Bi. Mwamini. Aligeuka na kurudi ndani. Aliurudishia mlango uliotengenezewa kwa mabua ya mtama. Jipendekezo na Majungu walijisogeza pembeni mwa ukuta wa nyumba kusubiri.
“Endapo akikataa tunampotezea kumbukumbu zake---na huyu mama anayeishi naye ili wasitusumbue na kutuharibia mtaani,” alisema Jipendekezo.
“Naam! Hakuna namna itakayotuweka salama zaidi ya hiyo,” Majungu naye alichangia hoja.
Dakika zilikatika, matarajio ya kutoka Awetu ama shangazi yake nayo yaliyeyuka......hakukuwa na dalili zozote zilizowapa ishara kwamba kuna mtu angefika kuwapa taarifa kuhusiana na kile walichoomba ama kumwona wamtakaye wa wakati. Hasira zikawakaa kifuani, jazba ikawaongoza na kufura nafsini—subira ikatoroka na wakataka la muda huo liwe kwa wakati.
“Tuzame ndani,” Majungu alisema wakati akitaka kuuparamia mlango.
“Papara ya panya ndiyo ilimponza kwa paka, taratibu,” alisema Jipendekezo.
Kwakuwa mlango ulikuwa ninyanyue nitue, waliubeba na kuutua kwa taratibu. Waliingia ndani na kuanza kuchunguza chumba kimoja baada ya kingine huku wakijitahidi vishindo vya nyayo zao visipate kuyafikia masikio ya mama kipofu. Walijua fika kuwa, kipofu yule sauti ndiyo ilikuwa jicho lake. wakaitalii nyumba ya vyumba viwili; kimoja kilifunikwa na kanga iliyochakaa na kimoja kilikuwa wazi kama pango la nyikani.
Jicho kwa kitu lakini hakupatikana mtu akiwa ndani kalala ama kangoja kufumaniwa wakati wa ugeni ule wa shari. Hofu! Kila mmoja alistaajabu kuona mahali pa watu palikuwa patupu tena bila hata dalili ya kuwepo kwa dakika chache za kungoja.
Wakachunguza kwa makini kisha kubaini lililowasibu. Hapakuwa na ndumba wala ulozi wa kuwatowesha watu wale kutoka ndani ya nyumba ile zaidi ya kuwa walitoroka kwa kuepa, wakipita kwenye mlango wa nyuma ya nyumba ile kiegama. Macho yakawatoka katikati ya giza na wasijue kile kilichokuwa kinafuata.
Hatimaye wachuuzi wa kifo cha kupangwa nao waliamua kuondoka kupitia mlango huohuo baada ya kujiaminisha kuwa wawatafutao wamepitia hapo na kwenda zao machakani. Walifuata uelekeo wa barabara waliyoiona, ambayo ni nyembamba ikisalimiwa na nyasi ndefu zilizosimama wima pembeni zikiwapangusa miguu yao iliyojaa vumbi.
Kwakuwa giza lilikuwa nene na kuufanya usiku kuogofya, mwanga wa tochi iliyopo kwenye simu ndiyo uliyowasaidia kuiona njia ile kichochoro kisha kuifuata wakielekea kule walidhani watafutwa na watoro waweza kuwa walipita. Ikawa mguu bandika kisha bandua, kwa haraka ya mhalifu asiyejua uelekeo wake. Walitamauka!
“Nyayo! Wamepita muda si muda,” alisema Majungu kisha wakasimama na kuchunguza kwa makini. Nyayo zilikuwepo, tena za watu waliofuatana, mmoja kakanyaga kwa urefu na mwingine kwa kufukia unyayo wa mwingine nusu. Walifuatana kwa kukokotana.
Safari ya ufuatiliaji iliishia kwenye banda lenye chumba kimoja—lile ambalo Awetu alienda mchana wake. Hata zile nyayo walizozifuatilia zilionyesha kuingia humo. Kutokana na hasira na chuki kali waliyonayo dhidi ya watu hao, hawakuhitaji kufanya majadiliano. Baada ya kufika tu, waliusukuma mlango na ndipo waligundua kuwa mlango ulifungwa kwa ndani. Ulikuwa mlango uliotengenezwa kwa bati. Haraka sana walianza ubomoaji uliowachukua dakika kadhaa kumaliza ndipo wakaingia ndani. Ndani hapakuwa na mtu, mbaya zaidi hata kitanda wala vyombo havikuonekana. Walifanya uchunguzi kama ilivyokuwa nyumba ya awali, uliowawezesha kugundua kuwa dirisha lilikuwa limeng’olewa upande wa pembeni ya banda.
“Walikuwepo, lakini wameshaondoka,” alisema Jipendekezo kwa sauti ya mshindwa na mkata tamaa, ikimaanisha kile walichohitaji hawataweza kufanikisha kukipata tena.
“Inakuwaje watoto wa kike watushinde?”
“Washawahi kupitia mafunzo ya mgambo. Hivyo wana mbinu nyingi zaidi yetu, si unafahamu kuwa sisi hatujawahi fika huko zaidi ya wale waliokimbia kule kwetu?”
“Oooooh! Kumbe ndiyo maana wanatushinda,” alisema Majungu, akawa kama amekumbuka jambo fulani.
“Hatuna budi kurudi, ili tukajipange upya kukabiliana nao.”
“Sawa, tufanye hivyo.”
Hatimaye walianza safari ya kurejea nyumbani kwao, tena wakiwa na hasira kisa tu wamezidiwa na watoto wa jinsia ya kike. Waliondoka mle ndani kuianza safari rasmi huku macho yao yakiangaza kwenye mazingira jirani yaliyozunguka banda hilo. Kulikuwa na vichaka kisha msitu. Sehemu kubwa ya eneo la banda lilizungukwa na msitu, uliowakatisha tamaa ya kuingia kuwatafuta, sababu ni msitu mkubwa wasingeweza kubashiri uelekeo. Walipiga hatua na kugeuka nyuma, kutoamini kama wamewakosa wale waliokuwa wanawahitaji. Hatua kadhaa baadaye, Majungu alishituka na kusimama. Jipendekezo pia aliyekuwa na bidii ya kupiga hatua kusonga mbele alisimama.
“Kulikoni ndugu?”
“Nahisi kuna sauti usawa wa lile dirisha.”
“Hayo ni mawenge yako tu, yaweza kuwa ni wanyama.”
“Hapana....sauti ya mtu.”
“Haiwezekani, ama unataka kusema ndani kuna misukule? Si tumejionea hakuna kitu chochote, huyo mtu anatoka wapi?”
“Subiri tuhakikishe,” alisema Majungu huku wakisimama kuhakikisha kile alichokihisi.
Walisimama takribani dakika mbili bila kusikika kitu chochote. ukimya ulitawala. Walivyoona kimya kimezidi ilibidi waendelee na safari.
“Washaondoka!” ilisikika sauti ikonong’ona toka usawa wa chini ya dirisha lile lililobomolewa.
Mwendo wa nusu saa uliwafikisha Jipendekezo na Majungu nyumbani na kumkuta baba yao, mzee Tualike akiwa na mgeni ambaye ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, bwana Tikitia Kasoyaga. Walioonekana kuteta jambo kwa usiri mkubwa. Walipita moja kwa moja hadi chumbani kujipumzisha kwa sababu ya uchovu huku akili yao ikiwakumbuka Awetu na shangaziye na namna ya ufanikishaji wa kuwapata watu hao.
“Tutampatia jibu gani mzee? Maana kwa ninavyomfahamu akimalizana na yule mgeni atakuja kwetu kufahamu maendeleo ya kazi aliyotupatia,” alisema Majungu.
“Usiwe na wasiwasi, changamoto zipo mahali popote pale. Hata hiki tulichokutana nacho ni changamoto pia, haikuwa na ulazima wa ile kazi kumalizika leo.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Taratibu walianza kutafuta usingizi ilhali usiku ulielekea tamati. Uchovu uliwasukuma kufanya hivyo. Wakati huo Mzee Tualike naye alikuwa katika dimbwi la maongezi mazito na yule mgeni aliyeonekana kukubaliana na kila aliloambiwa na mwenyeji wake. Maongezi yao yalikuwa ya muda mrefu, kwani yalianza punde tu baada ya Jipendekezo na Majungu kuondoka kwenda kumtafuta Awetu.
Kubwa walilokuwa wanazungumzia ni kuhusu mzee Tualike kugombea nafasi ya uenyekiti wa kijiji—ulio chini ya mzee Kasoyaga aliyekuwa anaelekea kumaliza muda wake wa utawala. Hivyo mzee Tualike alihitaji msaada kutoka kwake, kiongozi huyo ambaye hata naye kipindi anagombea mzee Tualike alifanya jitihada ya kuwashawishi wanakijiji wampatie ushindi dhidi ya mpinzani wake, Mwl. Kulaga Kinyonga. Akisaidizana na wanafamilia ndipo alifanikiwa kushinda. Juu ya nguvu kubwa ya ushawishi alionao, alihisi haitoweza kumsaidia baada ya kuanza kukumbwa na kashfa mbalimbali. Kashfa hizo aliamini zitamuangusha, na imani ya wananchi kwao ilielekea kutoweka.
Jambo lingine ambalo alihitaji ni Awetu awekwe gerezani, kwani aliamini msichana huyo ataanzisha ligi dhidi yao, kwa kuwa anaufahamu wa ndani kiasi namna familia ilivyo. Aliamini atamchafua na sifa zote alizonazo ndani ya jamii ya Tuleane na ile ya vijiji jirani zitapotea. Kabla yale aliyohisi hayajaanza kutokea, alipanga kudhibiti chanzo, ambacho ni Awetu, ili yeye awe huru kwa kumhifadhi sehemu itayomfanya ashindwe kusikika daima, hadi atapofanikisha kile anachohitaji.
Wanajifanya familia ya watu waliotawaliwa na amani na upendo ndani yao kumbe hamna lolote, ni makafiri wakubwa. Aliwaza mzee Tualike, jioni moja akiwa ameketi barazani mwa nyumba yake akihisi itafikia siku wananchi wataanza kuongea maneno hayo. Hivyo kabla hayajaanza ndipo anahitaji yule anayemhisi atamchafulia kiasi kwamba kukosa ushindi wa nafasi atakayogombea, aondolewe uraiani ili asilete balaa hilo kupitia taaluma aliyonayo.
“Mzee Kasoyaga, kumbuka kuwa familia yangu ndiyo iliyopigana kuhakikisha unakuwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji chetu, sasa kwanini unashindwa kunielewa juu ya vile ninavyohitaji?”
“Nakuelewa sana mzee mwenzangu. Kuhusu hiyo mada yako ya kwanza haina shida, mimi nitatekeleza. Shida iko hiyo ya pili, unahisi wanakijiji watanionaje?”
“Wewe ndiye mwenye mamlaka, hakuna yeyote atayethubutu kufanya jambo lolote pale utakapoamua. Mbona unashindwa na unaogopa kutumia mamlaka yako?”
“Hili la Awetu litakuwa gumu sana na nikuambie tu kuwa sitaweza kufanya, ama unahitaji nipate sifa mbaya mbele ya jamii yangu?”
“Mzee Kasoyaga! Kumbuka jitihada zangu. Na kama utashindwa kufanya kile ninachohitaji, utalazimika kulipa jitihada kwa lazima.”
“Haa! Tunatishiana?”
“Sikutishi, nakueleza ukweli,” alisema mzee Tualike huku akinyanyuka sehemu aliyoketi nakuondoka, hali iliyopelekea mshangao kwa mzee Kasoyaga.
“Mbona unaondoka ilhali hatujafikia muafaka?”
“Sina kingine cha kuongeza, kama umeshindwa kunielewa unaweza kuondoka tu.”
“Sisi sote ni wazee, rudi tuyamalize.”
Hakuwa na budi, mzee Tualike alirejea tena ile sehemu aliyoketi awali kuendeleza maongezi pale walipoishia mwanzo. Mara hii hawakuzozana, mapema tu walifikia muafaka na mzee Kasoyaga kuondoka. Baada ya mzee Kasoyaga kuondoka, mzee Tualike alielekea chumbani kwa wanae, waliokuwa wanabadilisha mitindo ya ulalaji, usingizi ulishafanya kazi yake. Ngurumo za sauti aliyoitoa ndiyo iliwaamsha, kila mmoja akiwa na ulegevu wa viungo. Walijinyoosha kisha kukaa sawa. Ndipo mzee Tualike alianza kuwasabahi na kuwapa pole, kwani uchovu wao aliuona. Haikuchukua muda, maongezi ya kazi waliyoagizwa yalianza. Jipendekezo ndiye alikuwa anahadithia kila kilichojiri.
“Pumbavu!......Wanahizaya nyie---mtashindwa vipi na watoto wa kike?” Aliuliza mzee Tualike.
“Nawahitaji wale watu,” aliendelea kuongea mzee Tualike.
“Hakuna shida baba. Tunakuahidi kukamilisha hilo ndani ya muda mfupi.”
“Jitahidini!” Alisema mzee Tualike, taratibu aligeuka nyuma na kurudi alikotokea.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mapema siku iliyofuata, mzee Kasoyaga, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tuleane alitii ombi la mzee mwenziye, mzee Tualike Misifa, la kumkamata Awetu. Alituma mgambo wa kijiji wapatao wanne wakiwa kwenye mavazi ya kiraia. Ilikuwa ndiyo siku ya kuchapa makala gazetini.
Siku hiyo ofisi ya gazeti la serikali, liitwalo Tuleane yetu ilikuwa wazi. Mgambo walifika eneo hilo. Japo walikuwa na ugeni katika ofisi hizo, hakuna mtu yeyote aliyewashitukia kuwa ni wageni na ni mgambo ambao wako kazini kwa namna walivyokuwa. Kitu kilichowafanya wasitambulike ni namna walivyovaa, hawakuvaa sare za mgambo wala hawakuambatana pamoja. Kila mmoja alipita kona yake ila walikuwa wanawasiliana kwa ishara.
Suala hilo lilikuwa la siri baina ya mzee Tualike, mzee Kasoyaga na mgambo walioagizwa. Hawakuhitaji taarifa za tukio lililokuwa linaenda kutokea ziwe wazi, ingewaharibia na kupoteza moja kwa moja heshima waliyonayo ndani ya jamii yao. Walifuata namna utaratibu ulivyopangwa, ambao ni kujichanganya katika makundi ya watu wapatikanao jirani na ofisi hiyo. Wauza magazeti! Waliokuwa wanakuja kuchukua na wale wauzao eneo la ofisi, macho yakiwa pima katika lango la kuingilia, ili punde wamuonapo Awetu wamvamie na kumuweka chini ya ulinzi.
Ofisi ilifunguliwa rasmi saa 2:00 asubuhi, ila wao walifika mapema, hata kabla ofisi haijafunguliwa. Lengo lao lilikuwa kusoma mazingira na kutengeneza njia ya kuzoeleka kwa watu wapatikanao pale ili wafanyapo kile kilichowaleta wasilete mshangao.
Hatimaye wafanyakazi walianza kuingia ofisini dakika tano baadaye, nao kumlaki kwa macho kila mfanyakazi aingiaye. Hadi kufikia saa 2:58 asubuhi, jumla ya wafanyakazi thelathini na tatu walishaingia ofisini na kubakia dakika mbili ofisi ifungwe kwa muda kwa ajili ya kikao cha wafanyakazi hao ambacho hufanyika kila asubuhi waingiapo kabla hawajaanza kuwajibika.
“Bado watu wawili, nahisi ndio wale wanaoteremka kwenye bajaji,” mgambo mmoja alimnong'oneza mwenzie huku akikielekeza kidole kimoja cha mkono wa kuume eneo la hifadhi la vyombo vya usafiri ambapo bajaji iliegeshwa, walipokuwa wanapishana, huku watu wawili walionekana kushusha miguu kuteremka. Kwa mavazi waliyovaa walitambua wazi kuwa mmoja alikuwa ni wa jinsia ya kike na mwingine wa jinsia ya kiume—wa kike akiwa ni Awetu.
Alfajiri ya saa 11:06, siku ya jumamosi ndiyo walikamilisha walichopanga. Bi. Mwema na Laumio na mwanaye waliafikiana kutoroka. Wawili hao walinuia kuipa uhuru na amani mioyo yao, ambayo muda wote ilijawa nung’uniko. Wakiwa na uchovu uliotawala miili yao kwa kuukosa usingizi, walijitahidi kuruka uzio uliozungushwa nyumbani kwao. Walitumia takribani dakika kumi ndipo waliweza kuwa nje ya uzio na safari ya kwenda kusikojulikana ilianza. Safari yao ya utoro haikuwa ya lelemama, bali ilikuwa ya mashaka, kwani kila hatua moja ilizaa wimbi la hofu nafsini. Walikuwa wakipiga hatua kadhaa kisha waligeuka kuangalia kama kuna mtu nyuma yao aliyediriki kuwafuata.
Punde wasikiapo mlio wa kitu ama sauti za mtu hawakusita kutafuta maficho, baada ya hicho walichosikia kupita nao walijitokeza barabarani kuendelea na safari. Sehemu nyingine waliacha kutumia barabara, waliingia kichakani ili waendelee kwenda kwa amani baada ya kuona usumbufu waupatao barabarani. Haikuwa safari fupi, ni ndefu, tena waendako walikuwa hawafahamu siku na muda wa kufika. Hadi kufikia pambazuko, tayari walikuwa mbali na kijiji chao na kuukaribia mpaka wa kijiji kingine kiitwacho Kalipinde.
Hawakuwa na mizigo zaidi ya nguo walizovaa na vidumu vya maji ambavyo vilikuwa na maji ndani yake. Hivyo iliwarahisishia utembeaji japo uchovu haukuacha kuchukua nafasi mwilini mwao kwa sababu ya umbali waliotembea. Uchovu walioupata ulipelekea kunywa maji waliyobeba, yaliyoonekana kutokidhi haja zao, kwani awamu moja tu waliyokunywa iliwalazimisha kuhitaji zaidi.
Safari ilipozidi kuwa ndefu, wakivuta vilima na mabonde kisha misitu na nyika, hakuna aliyefikiria kumwongelesha mwenzake—kila mmoja alifikiria namna ya kupumzika. Muda mfupi tu baada ya mapumziko, takribani dakika nne hivi, hatua za mtu akitembea zilisikika karibu kabisa na eneo walipo, tena zikielekea kule wao walipo. Ziliwashitua. Hofu ikatanda moyoni mwao, walibabaika na kutafuta mahali pa kujificha kumkwepa yule mtu aliyekuwa anaelekea usawa walipo. Hawakufanikiwa! Yule mtu alitokea walipo, hata kabla hawajakamilisha harakati zao za kuhama eneo.
Msichana mwenye ulemavu wa ngozi apataye kuwa na umri wa miaka kumi na tano ndiye alijitokeza mbele yao—akiwa na ndoo yenye ujazo wa lita kumi katika moja ya mkono wake, akielekea kisimani kuteka maji. Kupita kwake kichakani ilimlazimu kwani alitaka kujibanza kwa ajili ya haja ndogo. Alipowaona watu wawili wasio wa nasaba naye alishituka. Japo aliwafahamu kutokana na umaarufu wa familia yao, katika kijiji watokako—bado hakuamini kuona uwepo wao katika mazingira hayo. Alikuwa msichana aliyebarikiwa ukarimu, unyenyekevu na heshima. Haraka, aliwasogelea walipoketi wakitaka kujibanza.
“Naomba utusaidie maji kwenye hivi vidumu vyetu,” Laumio alisema huku akimsogezea vile vidumu.
Msichana yule, aliyetambulika kwa jina la Awetu Mbwela, alivichukua vidumu na kuondoka. Alifika kisimani na baada ya robo saa alirejea pale alipowaacha Bi. Mwema na mwanaye. Aliwakabidhi kisha kuendelea na safari yake, lakini alitembea hatua kadhaa akasita, akaamua kuwarudia. Aliteremsha ndoo iliyokuwa kichwani, “Mnahitaji msaada wangu kwa mara nyingine kabla sijaondoka?” Awetu aliwauliza.
“Hakika, ni vema kwa hilo! Si vibaya kama utatusaidia kwa awamu nyingine. Nikuombe, hiki ulichokiona kiwe siri kubwa kwako,” Alisema Bi. Mwema.
“Msihofu, itakuwa kama mtakavyo.”
“Na pia tuna huu ujumbe, tunahitaji uwafikie wana Tuleane wote. Hivyo tafuta siku ambayo itajumuisha watu wengi wa Tuleane uwasomee.”
“Kuhusu hilo wala msijali. Nitausoma siku ya mahafali yetu, yatayofanyika wiki ijayo,” alisema Awetu.
“Hakika litakuwa jambo jema, nasi utakuwa umetuweka huru. Na hakikisha huu ujumbe unamaliza kuwasomea, ukiishia njiani, dhamira yetu itakuwa sawa na bure.”
“...ondoeni shaka. Ila,...kwanini nisiwatoe hapa nikawapeleka nyumbani?”
“Hapana. Hatuna nia ya kuwemo ndani ya kijiji hiki kwa sasa. Tunahitaji tuvuke kuelekea kule jirani.”
“Nini kimewapata hadi muwe na hitajio hilo?”
Kimya kilipita kwa sekunde chache ndipo mmoja walijibu swali lake kwa kuanza kumhadithia kilichowasibu.
“Kumbe ndiyo hayo! Sasa kwanini mnaamua kuondoka mapema yote hii? Endeleeni kubaki hapa kijijini, muwaoneshe uwezo wenu, mimi nitawasaidia.”
Bi. Mwema na Laumio walitafakari kwa muda kauli waliyopatiwa, takribani dakika nne ndipo wakatoa majibu ya fikra zao. “Sawa. Tutabaki, ila kaa kwenye ahadi yako kwetu.”
“Hakuna shida, nitatunza nadhiri.”
Makubaliano yalifanyika, namna itakavyokuwa. Bi. Mwema na Laumio watakavyowasili nyumbani kwa kina Awetu ikapangwa. Si kwa muda huo, bali ni usiku. Tena usiku wa kiza, utakaowazuia wasibainike kwa watu watakao kutana nao. Awetu alirejea nyumbani. Usiku, kama walivyokubaliana, aliwafuata na kwenda nao nyumbani kwao, ambapo anaishi na Shangazi yake. Walipatiwa huduma zote walizohitaji kwa muda huo, kama vile chakula na kuoga. Baada ya hapo walipelekwa sehemu ya kulala ambayo haikuwa hapo walipofikia, walipelekwa nyumba nyingine, ambayo ni banda lenye chumba kimoja, lililoko umbali mfupi kutoka pale Awetu anapoishi na shangazi yake.
“Mtakuwa mnaishi humu, hapa ndiyo yalikuwa makazi yetu ya mwanzo kabla hatujahamia tulipokuwa sasa. Hakika yangu, patawafaa, kule kwa mwanzo kubaya kutokana na watu wengi kupazoea.”
“Usipate tabu, sisi tunashukuru kwa msaada wako, ila fanya kama tulivyokuomba.”
“Msiwe na shaka,” alisema Awetu.
Wakaagana.
Awetu alirejea nyumbani kwa ajili ya kulala, mawazo mengi yalimzonga kuhusiana na mzee Tualike na familia yake kwa ujumla. Alianza kuwadadavua, hatua moja baada ya nyingine akashindwa kupata jibu sahihi kuwahusu. Chuki ilianza kujijenga moyoni dhidi yao, chuki kali iliyomsukuma kutekeleza kile alichoombwa kwa wakati.
“Kwisha habari yenu, huu ni wakati wa uwazi, lazima niwatekelezee ombi lao,” alisema Awetu kimoyomoyo, akivuta shuka tayari kwa kulala.
Siku ya mahafali ya kuhitimu elimu ya msingi, Awetu alifanya alivyoahidi—kuusoma ujumbe aliokabidhiwa, lakini hakuumalizia baada ya mshereheshaji kumkatisha akitaka waendelee na ratiba ilivyo. Haikuwa chochote ila ni mbinu mahususi iliyopangwa na mzee Tualike, kumkatisha baada ya kuona msichana huyo anaelekea kumwaga mchele mbele ya kuku wenye uhitaji wa chakula. Kitendo cha kumkatisha kiliongeza chuki, uhitaji wa kuumalizia ule ujumbe kwa namna yoyote na siku si nyingi toka siku hiyo.
“Nitauandika huu ujumbe kwenye makala, kesho kutwa,” alijiahidi Awetu.
Hata alivyoenda kuwaeleza wahusika hawakuchukia, wao walifarijika kwa sababu sehemu ya mwanzo ya ujumbe wao ilishasomwa, ila walimuomba aendelee kuwasaidia kwa kuchapa gazetini kama mwenyewe alivyojiahidi. Hakupingana nao. Japo alikuwa na mashaka kuwa atafuatiliwa, kama wengine wanavyofuatiliwa pindi watoapo maoni yao kuhusu familia hiyo kwa kile kilichotokea.
Ubashiri wake, wa kufuatiliwa ulitimia, kwani usiku wa siku hiyohiyo ya sherehe, Jipendekezo na Majungu waliwasili nyumbani kwao, naye kutambua ujio wao kupitia sauti wakiwa wanajadiliana kabla hawajaanza kubisha hodi.
“Shangazi,.....shangazi, unasikia hizo sauti huko nje?” Awetu alimnong’oneza Shangazi yake.
“Sauti zipi tena?”
“Kuna watu wako hapo nje, wanaonesha hawana nia njema nasi, na nahisi ni watoto wa mzee Tualike.”
“Nawe, watu wema kama wale wanaanzaje kuwa wabaya? Kila kukicha wanahubiri amani, hayo mambo uyasemayo yanatokea wapi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Amini nikuambiacho, na nina hakika ni wao,” aliendelea Awetu, aliinuka kitandani kuchungulia nje kupitia dirishani, usawa waliosimama wale watu, lakini hakufanikiwa kuwatambua tokana na kiza kikali kilichopo. Punde, walianza kusikia sauti ikibisha hodi. Kwa pamoja waliitafakari sauti waliyoisikia, kwa kuvuta kumbukumbu zao nyuma zilizowapa ukumbusho wa jambo.
“Dhahiri, kile ulichozungumza awali kipo sahihi. Hiyo ni sauti ya mtoto wa mzee Tualike, lakini ipo kama imefanyiwa usanii kidogo,” alisema shangazi yake Awetu baada ya kujihakikishia.
“Hakika, yaweza kuwa,” alisema Awetu kisha kupanda kwenye dirisha tena na kubaini kimo na umbile pale gizani vikiwa na uhakika wa hisi zao.
Haraka sana walipanga namna ya kukabiliana nao, ambayo ni kuwatoroka. Hawakufikiria nyingine zaidi ya hiyo. Awetu aliratibu, namna itavyokuwa huku shangazi yake akiwa mtendaji wa kile kilichopangwa. Shangazi alifungua mlango na kuongea na wale wageni, wakati huo Awetu alishatoka ndani kupitia mlango wa nyuma akimsubiria amalize kuongea nao kisha waondoke kabisa. Dhahiri! Haikuchukua muda mrefu, shangazi yake alirejea ndani. Alizima kibatari kisha kutoka nje kupitia mlango wa nyuma, ule alioutumia Awetu. Hawakukawia, mara tu Shangazi yake alivyomfikia aliongozana naye.
Mwendo wa dakika saba, walifika kwenye lile banda ambalo Awetu alienda mchana. Mmoja wao, ambaye ni Awetu alibisha hodi, na kufunguliwa baada ya wale watu wa ndani kuitambua sauti yake. Walikuwa ni Bi. Mwema Asononekaye na Laumio.
“Mnasema kweli?” Bi. Mwema aliuliza.
“Ndiyo. Tena nahisi wanaweza kutufuata kama watagundua.”
“Tufanye vipi kuepukana nao?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tuondoke.”
“Tutaelekea wapi? Ilhali unaona mazingira jirani yalivyo? Tusije liwa na wanyama bure.”
“Bora tuliwe na wanyama, ila siyo kuingia mikononi mwa hawa watu. Hawa ni zaidi ya wanyama.”
Kile walichokubaliana ndicho walifanya. Hawakutumia mlango, walitumia dirisha kutoka kwani waliamini endapo wale watu wakibaini kuwa wameelekea hapo basi watawafuata, hivyo huo muda wa wao kutoka kupitia mlango, inawezekana ukawa muda wa Jipendekezo na Majungu kufika eneo hilo. Walibomoa dirisha lililojengwa kwa miti na mianzi, hawakuchukua muda mrefu kufanikiwa, mmoja baada ya mwingine walipanda na kurukia upande wa pili, ambako ni msituni.
Dakika kadhaa baadaye, Jipendekezo na Majungu walifika, na kuondoka walivyowakosa.Walivyoondoka, wao walirudi tena mle bandani. Wakalala humo kwa staha.
****
Siku iliyofuata ilikuwa rasmi kwa Awetu kutekeleza kile alichoahidi kwa Bi. Mwema na Laumio. Aliamka mapema na kufanya usafi wa mwili, baada ya hapo alipata stafutahi. Ilivyowadia saa 2:50 asubuhi ndipo alianza safari ya kuelekea ofisini, kwa kutumia pikipiki ya matairi matatu—bajaji. Muda mfupi tu walifanikiwa kufika, takribani dakika nane tu ndizo walitumia. Alifanya malipo akiambatana na mwenziye, aliyepanda naye njiani pindi anaenda, kisha taratibu kuanza kuteremka.
“Psiiiiiiiii!” ilikuwa sauti ya mluzi, iliyosikika vyema masikioni mwa Awetu na kumfanya aghairi kwa muda kuendelea na kile alichokuwa anafanya, kisha kuyaangaza macho yake kule sauti ilikosikika.
“Dada teremka basi, nataka niondoke,” dereva alimshitua. Wakati huo yule mwenzie tayari alishateremka.
“Subiri!” Awetu alisema, akimtathmini vizuri yule aliyetoa mluzi kisha kugeuza nyuma kumuangalia nani aliyekuwa anapigiwa. Alipatwa na mshtuko wa ghafla! Kwani wale aliowaona, hazikuwa sura ngeni kwake, aliwatambua.
“Hawa ni mgambo, idara ya ulinzi wa viongozi,” alisema Awetu kimoyomoyo.
“Kaka geuza tuondoke.”
“Nini shida dada yangu?”
“Fanya ninavyokuambia.”
“Kuna wateja wako pale wananisubiri, nikisema niondoke na wewe, wale baadhi yao hawatapata nafasi.”
“Kaka yangu, nami ni mteja kama wao, na ndio wa mwanzo, hivyo una haki kunisikiliza kwanza ndipo usikilize hitajio la wengine,” Awetu aliongea huku mgambo wakisogelea usawa wa bajaji ilipoegeshwa.
“Kaka washa tuondoke, nahisi hao wanaokuja wananihitaji mimi. Halafu sio watu wema.”
Baada ya majadiliano ya kina, dereva alielewa na kufanya alichoambiwa huku wale mgambo wakiwa wameshaikaribia bajaji, umbali wa mita nne. Aliiwasha na kutumia utundu wa hali ya juu kuigeuza nyuma, kufuata uelekeo aliojia mwanzo. Mgambo baada ya kuona hivyo waliongeza kasi ya utembeaji ili wawahi, lakini hawakufanikiwa, tayari dereva alishachanganya mwendo na kuondoka kwa kasi.
Mgambo, ilibidi waikimbize bajaji. Waliacha gumzo nyuma, pale ofisini lakini watu walishindwa kutambua walichofanya, isipokuwa wachache walioshuhudia tukio tangu linaanza.
Jitihada za dereva, za kuwakimbia mgambo hazi kufika mbali, kwani punde baada ya kulivuka lango la kuingilia ofisi za gazeti walikumbana na bajaji nyingine uso kwa uso. Ajali kubwa ilitokea, iliyoondoa uhai wa madereva wote huku Awetu akipoteza fahamu na kuvunjika mkono. Wasamaria wema hawakuisha kujitokeza muda mfupi baadaye na kutoa msaada. Awetu alipelekwa zahanati ya kijiji kwa uchunguzi na matibabu. Taarifa ya ajali ilimfikia mzee Kasoyaga, nusu saa baadaye, baada ya waathirika wa ajali kufikishwa kwenye zahanati ya kijiji, ambayo iko umbali mfupi toka zilipo ofisi za gazeti la serikali ya kijiji. Naye hakukaa naye, alimfikishia swahiba wake, Mzee Tualike, hatimaye wakajikuta wanaingia kwenye majadiliano pasi na kutarajia.
“Tunaamua vipi kuhusu yeye?” aliuliza mzee Kasoyaga.
“Mimi sihitaji awe na uhuru huyo binti, kwani kufanya hivyo kutaendelea kutuharibia.”
“Kwa hiyo unashaurije?”
“Akipata unafuu, fanya kama tulivyopanga.”
“Jamii itatushangaa.”
“Usijali kuhusu hilo, ninachohitaji ni usalama wetu.”
“Basi nitajitahidi mzee mwenzangu.”
“Nitafurahi sana ikiwa hivyo.”
Maongezi yalivyomalizika mzee Tualike aliwaita wanaye na kuwaeleza nini cha kufanya. Kwa hasira walizonazo walihitaji kuhakikisha nia yao inatimia wakati huohuo, ambapo Awetu yuko hospitalini akiugulia maumivu. Walichohitaji kufanya, hawakuhitaji kufanya kwa bahati, walithubutu, na uthubutu wao kuonekana kwa mpango mkakati walioafikiana. Waliokuwa na uhakika hautowaweka wazi kuwa ni wahusika wakisaidizana na watu wa serikalini.
“Mwisho wake ushawadia. Sisi tutamaliza baada ya serikali kutuandalia mazingira rafiki ya kazi,” alijitapa mzee Tualike.
“Mazingira yepi hayo?”
“Kuna mpango ulioandaliwa na serikali, siku zijazo utawekwa wazi. Hapo tutafanya mambo kiulaini, kwani yule tumtafutaye japo ana hali mbaya kwa ajali, atawekwa ndani ya huo mpango.”
“Mpango upi huo?”
“Kuna mazingira ya ugonjwa yanaandaliwa.”
“Unasema?”
“Naam! Ashakuwa kuku wetu, hakuna haja ya kutumia nguvu kupambana.”
****
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mei 10, 2004, Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi wa serikali ya kijiji cha Tuleane, mzee Anthony Kumwembe alitoa tangazo la utaratibu wa uchaguzi, kupitia gazeti, Radio (Tuleane Radio Station-TRS) na runinga ya serikali ya kijiji (TT-Tuleane Television) ambao ulipangwa kufanyika wiki mbili mbele baada ya tangazo kuwekwa hadharani. Alibainisha wazi kuwa, muda wa kampeni ni hizo wiki mbili zilizopangwa kabla ya siku ya uchaguzi, ikiwa pamoja na muda wa uchukuaji fomu kwa watia nia. Hakusita kuwaomba watia nia wajitokeze mapema kuchukua fomu kabla muda husika haujamalizika, ambapo mtia nia atalazimika kulipa faini endapo atazidisha muda.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment