Search This Blog

Friday, November 18, 2022

UMUTWALI - 4

 






Simulizi : Umutwali

Sehemu Ya Nne (4)





Fatuma siku hiyo akamuaga mama yake akakubaliwa, mwishowe akaondoka kwenda kwa rafiki yake Amina, akafika nyumbani kwa kina Amina akamkuta bibi yake Amina nje akifua nguo.



“Shikamoo,” Fatuma alitoa salamu kwa Bibi Amina.



“Marahaba,” Bibi Amina akaitika salamu.



“Amina nimemkuta?.”



“Umemkuta...kuna nini kwani?.”



“Hamna kitu kibaya, nimekuja kumfuata anisindikize sehemu tu.”



“Haya...rafiki yako yupo hapo sebuleni anamalizia kunywa chai,” Bibi Amina alieleza huku akiendelea kufua nguo. Hatma ya maelezo, Fatuma akaingia ndani akamkuta Amina kweli anamalizia kunywa chai.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Bestie,” Fatuma akaita.



“Karibu my...niambie besti,” Amina alisema kutokea sebuleni alipo.



“Poa my...nimekuja kwako nahitaji unisindikize kwa kina Donald.”



“Kuna nini tena, asubuhi yote hii besti?.”



“Wewe huna taarifa kuwa Donald anaondoka, inabidi aondoke leo kwenda chuo.”



“Sasa nitapata wapi taarifa, kama sio kwako?.”



“Basi ndiyo hivyo, Donald leo anaondoka na anahitaji nimsindikize.”



“Kumbe!!, basi ngoja nikajiandae,” Amina alisema huku akiongoza chumbani kwenda kujiandaa.



Amina akajiandaa upesi kisha akatoka na Fatuma nje, akamuaga bibi yake hatimaye wakaongozana na rafiki kwenda kwa kina Donald walipofika getini. Fatuma akamtafuta Donald kwa njia ya simu.



”Hallow, Donald nishafika,” Fatuma akahabarisha.



“Nakuja,” Donald aliongea kisha akakata simu akatoka kwenda kufungua geti.



“Mpenzi, umeamkaje?,” Fatuma alisabahi mara baada ya Donald kufungua geti.



“Safi tu...kumbe umekuja na Amina?,” Donald akauliza.



“Eeenh, nilimuomba anisindikize.”



“Oooh, haina shida.... Amina, mambo,” Donald aliongea kisha akampa hai Amina mara baada ya kutambua ujio wa Amina.



“Poa,” Amina akajibu. Baada ya kujibu wakakaribishwa ndani na Donald, wakakaribishwa kuketi sofani wakakaa huku wakimsubiri Mama Donald aliyekuwa akijiandaa chumbani.



“Amina, muda mrefu hatujaonana...mwenzangu umebahatika nawe kuchaguliwa chuo gani?,” Donald akauliza. Hatimaye akamuita Dada Angel aje kwa ajili ya kuwahudumia wageni juisi. Dada Angel punde akaleta glasi mbili za juisi kwa wageni kisha akaondoka akawaacha sebuleni kina Donald wakimsububiri Mama Donald.



“Nimechaguliwa, University of Dar es salaam pamoja na Fatuma,” Amina alijibu swali huku akiendelea kupasha koo kwa kupiga fundo la kimiminika. Amina na Fatuma wakaendelea kunywa juisi ghafla Mama Donald akatoka chumbani akiwa kashajiandaa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Mkamwana, umekuja muda mrefu?,” Mama Donald aliuliza mara baada ya kufika jirani walipo kina Fatuma.



“Hapana mama!!, tumekuja muda si mrefu,” Fatuma alijibu huku akimuangalia Donald kwa jicho lenye mahaba mara baada ya kugundua kuwa Donald ndiye aliyemwambia mama juu ya mahusiano yao.



“Halafu mbona sura ya mwenzako ngeni kwangu, ni nduguyo?...kama ndugu yako anaitwa nani?,” Mama Donald akahoji.



“Mama, huyu si ndugu. Ni rafiki yangu anaitwa Amina ambaye tumesoma wote katika shule ya Loyola na darasa moja,” Fatuma akatambulisha.



“Ina maana, nae alisoma na Donald?,” Mama Donald akauliza.



“Ndiyo,” Fatuma akajibu.



“Karibu sana Amina, hapa ndipo nyumbani kwa kina Donald. Hivyo jisikie huru,” Mama Donald akasema. Na wakati huo Mr. Msunga hakuwepo nyumbani, alitoka akaenda katika starehe hivyo hata Donald hakufanikiwa kumuaga bali akafanikiwa kumuaga Dada Angel tu.



“Sasa dada!!. Mie ndio hivyo tena kumekucha, tutaonana Mungu akipenda,” Donald alimuaga Dada Angel.



“Sawa Donald, japo tutakukumbuka,” Dada Angel aliongea huku akimkumbatia Donald kuonyesha ni jinsi gani wanavyopendana na Donald kama dada na kaka.



“Hata hivyo nitarudi, usijali.”



“Haya bwana, safari njema.”



“Shukrani Dada,” Donald na Dada Angel wakaacha kukumbatiana wakaagana, Donald akaingia ndani ya gari na mama yake pamoja na kina Fatuma wakamuacha Dada Angel nyumbani. Mama Donald baada ya kuona vijana washaingia garini akakanyaga mafuta na kuliondoa gari pale, lisaa wakafika Ubungo kituo cha mabasi ya mkoa Mama Donald akaenda kukata tiketi kwa ajili ya Donald kusafiri. Donald akakatiwa tiketi akawa sasa anasubiri usafiri tu aondoke, yapata saa moja basi ndipo likaanza kutia nanga Donald akamuaga haraka mama yake na Amina akamgeukia na kipenzi pia akamuaga.



“Kwa heri Fatuma, nafikiri tutaonana tena.” Donald alimuaga kipenzi chake huku usoni akionekana kujawa na majonzi.



“Lakini Donald...nikiwa mbali nawe, nitakuwa mpweke sana. Hebu, fanya kitu basi, moyo upate kupoa,” Fatuma aliongea huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake.



“Fatuma, basi acha kulia nivumilie miaka mitano tu nitakuwa nisharudi mazima na ndoto zetu zitakuwa zishatimia,” Donald alifariji huku akijitahidi kumfuta machozi kipenzi.



“Nimekuelewa Donald, nitakusubiri” aliahidi Fatuma kisha akamkumbatia Donald kwa nguvu zote kana kwamba akimaanisha Donald abaki.



Wakaagana kwa huzuni mwishowe Donald upesi akadandia basi baada ya kutoka mwilini mwa Fatuma, akaelekea kukaa katika siti ya dirishani kwa ajili ya kuwatazama na kuwapungia mkono wahusika. Donald akiwa bado anaendelea kuaga akaona kupitia dirishani wahusika wake wamesimama nao wakimuaga huku wakiwa kwenye majonzi wakingojea basi liishie, basi lilipoishia hapo ndipo Mama Donald akawaamuru Fatuma na Amina waondoke. Wakakubaliana wakapanda garini wakarudi nyumbani, kufika katika kituo cha Kimara mwisho Fatuma akaomba Mama Donald asimamishe gari washuke.



“Mama, tunaomba tushushe hapo,” Fatuma akaomba.



“Oooh, kumbe mnashuka Kimara mwisho...nishajisahau,” Mama Donald akaongea.



“Tunashuka Kimara mwisho, lakini tunaingia maeneo ya ndani ndani huko,” Amina nae akachangia.



“Maeneo ya ndani ndani!!!, ndani ndani huko wapi?,” Mama Donald aliuliza kisha akasimamisha gari.



“Ni maeneo, ya Matangini,” Fatuma akajibu.



“Aaaanh.”



“Huko ndiko tunakoishi...karibu sana, mama” aliongezea kusema Fatuma kisha akashuka na Amina ndani ya gari. Wakampisha Mama Donald aendelee na safari, Mama Donald akafika nyumbani muda wa kijua cha utosi akamkuta Mr. Stanley Msunga bado hajarudi. Na Dada Angel alikuwa kajipumzisha chumbani, Mama Donald hakutaka kumsumbua Dada Angel ikabidi aelekee moja kwa moja chumbani akabadili nguo akaoge.



**********

Wiki moja ikapita Fatuma na Amina wakafanikiwa kupokelewa na kusajiliwa katika Chuo kikuu cha Dar-es-salaam, pia wakapangiwa “Hostel” moja ya chuo. Siku moja baada ya kuanza kwenda chuo wakiwa mgahawani wakila chakula wakamkumbuka Donald wakamtafuta Donald kwa njia ya simu.



“Hellow...Donald vipi maisha ya chuo. Yapoje?” alihoji Fatuma mara baada ya Donald kupokea simu.



“Maisha yapo poa tu huku, yaani namshukuru Mungu kunileta kwenye chuo hiki cha Mzumbe maana naona mandhari yake ni mazuri mno,” Donald akajibu.



“Nashukuru kusikia hayo...lakini mie huku tangu uondoke nakosa raha kabisa. Nimekuzoea eti.”



“Najua Fatuma...lakini naomba usiwe hivyo vumilia tu kidogo nitarudi,” Donald aliendelea kumfariji Fatuma katika kipindi kigumu anachopitia. Baada ya hapo simu zikakatwa pamoja mara baada ya maongezi kuisha na Fatuma kufika ukomo kutokana na ratiba za masomo kufika .



**********

Mr. Stanley Msunga ndiye Baba Donald wakufikia baada ya Mzee Zungu kuaga dunia. Mr. Msunga siku hiyo akachelewa kurudi nyumbani alirudi usiku akiwa kalewa bwii, akamkuta Mama Donald kashajipumzisha chumbani, akamuamsha kwa fujo kisha akaanzisha zogo.



“Wee!! mwanamke, unalala lala nini mapema yote hii...hebu, amka,” Mr. Stanley Msunga aliongea kwa kebehi huku kinywa chake kikiwa kimechangamka na pombe kali.



“Mume, mbona unakuwa msumbufu niache nilale bwana,” Mama Donald alizungumza kwa sauti ya wastani kidogo.



“Wa kulala, utakuwa wewe bwana...hebu amka huko,” Mr. Stanley Msunga aliongea huku safari hii akimpiga Mama Donald makofi ya haja mgongoni mara baada ya kufunguliwa mlango.



“Yaani wewe mwanaume huna aibu kabisa, umerudi muda mbovu badala ya kuwa mpole ndiyo kwanza unaleta usumbufu,” Mama Donald aliongea huku akilia kwa sauti ya chini sababu ya mkong'oto wa Mr. Msunga.



“Achana na mimi, niwe mpole kwani mgonjwa...halafu ingekuwa mwanamke mwengine angekuwa kashanitengea maji ya kuoga nikaoge, lakini sio wewe....”



“Maji ya kuoga tu, nitakutengea ila nami ninawajibu wangu wa kuongea nawe kama mke,” Mama Donald alizidi kuongea huku akiendelea kuugulia maumivu ya mkong'oto.







“Kwa sasa basi sitaki maongezi nawe, kanitengee maji ya kuoga nioge mie nilale.”



“Sawa, lakini kaa ukijua hivyo vituko vyako ipo siku nitakuchoka.”



“Haijalishi, nitengee maji mie.”



“Na chakula, je?.”



“Chakula chenu, si lazima kula...nishajichokea nahitaji kupumzika. Halafu huyu msukule wako tabia ya kuondoka bila kuniaga sijapenda.”



“Msukuleee!!!, msukule upi?.”



“Si huyo, mwanao.”



“Wee ishia hapo hapo, mwanangu si msukule. Umenisikia?...halafu wewe mwanaume kama kupitiliza kunywa leo umepitiliza, sasa ya nini kujifedhehesha Stanley?.”



“Kama kujifedhehesha si mimi, kwani ni wewe halafu sasa hivi naona unanipanda...sasa kama mimi ni mwanaume sihitaji kupandwa juu,” Mr. Msunga alifoka kisha akaongoza bafuni. Alipotoka kuoga akaelekea kitandani kujitupa kama zigo, mwaka ukapita Fatuma na Donald wakamaliza masomo ya muhula wa kwanza wakaingia muhula wa pili huku wakiendelea kujuliana hali kwa njia ya simu.



**********

Mr. Stanley Msunga vituko akazidisha. Siku moja akamdanganya Mama Donald kwamba kichwa kinamuuma kwa hiyo hatoweza kwenda kazini atabaki nyumbani kujiangaliza ugonjwa. Mama Donald akamuelewa mumewe akachukua maamuzi ya kuondoka pekeake, akaondoka nyuma akamuacha Mr. Msunga na Dada Angel nyumbani. Nafasi ile Mr. Msunga hakuipoteza Mama Donald alipompa kisogo tu akajaribu kumuita Dada Angel. Dada Angel kwa kumheshimu Mr. Msunga upesi akaitika wito, akaenda.



“Angel, kwasasa una kazi gani?,” Mr. Msunga akauliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Kwasasa nishamaliza, nahitaji nikaoge nipumzike,” Dada Angel akajibu.



“Angel, lakini unalijua kwamba wewe ni msichana mlimbwende ambaye uliyeumbika kila idara.”



“Baba, hebu...acha utani wako sasa mimi nina uzuri gani?.”



“Uzuri uliokuwa nao ni wa kiasili hauwezi kuelezewa ukaisha.... Angel, wewe ni mzuri mno na niende mbali sana ya nini?. Mimi leo nimekuita nipatie uroda walau hata kidogo.”



“Baba nini!!!?.... Mimi naogopa kufanya tendo hilo pia namheshimu sana mama.”



“Unamuogopa nani?.... Yule changudoa. Changudoa hapaswi kuogopwa halafu yule kwangu hafui dafu,” Mr. Msunga aliongea kwa kumrubuni Dada Angel. Akajitapa kwa kujipa sifa kede mpaka Dada Angel akalainika akakubali.



Ibilisi akamuingia Dada Angel, akajisahau akaanza kufanya tendo chafu pale sebuleni na Mr. Msunga, wakiwa wanaendelea na starehe bahati mbaya. Siku ile Mama Donald akatoka kazini mapema akawahi kurudi nyumbani. Ghafla kufungua mlango wa sebuleni tu! akatahamaki kumfumania mumewe na Dada Angel wakifanya kushikana shikana miili Romance akabaki bumbuwazi, Dada Angel akawahi kumuona Mama Donald haraka hofu ikamjaa papo hapo akapatwa na butwaa akaanza kutetemeka kwa uwoga.



“Mwanaume usiyekuwa na haya, yaani kukupenda kote kama mume wangu. Nikakupa kila kitu ulichokihitaji leo hii unanifedhehesha kwa kutembea na housegirl!!!,” Mama Donald alilaumu kwa uchungu mno. Hakuamini kilichotokea mbele ya macho yake. Mr. Msunga wakati huo alishaiba hati ya nyumba ya Mama Donald akabadilisha jina la Baba Donald akaweka jina la kwake kwa mwanasheria wake bila hata Mama Donald kujua, hivyo akawa anamjibu Mama Donald anavyotaka.



“Unasema hayo kama nani?...kwanza wewe sasa hivi una mamlaka ya kunizuia ninachotaka kufanya?.”



“Umekutwa na nini?, mbona unaonekana kujiamini.”



“Unataka kutambua kitu gani kinachonifanya nijiamini, sawa utatambua.... Kwasasa najiamini kwa kuwa nyumba sasa ipo chini ya himaya yangu.”



“Wee!!! Stanley, ushakuwa chizi?.”



“Naona wewe ndiye umekuwa chizi. Maana mwenzako ninachosema ni ukweli mtupu.”



“Unajiamini. Kwanini unasema nyumba ipo katika himaya yako?.”



“Sababu hati ya nyumba ninayo mimi na nimebadili jina la mumeo nimeliweka jina la kwangu.... Sasa wewe mnuka haja utaniambia nini.”



Mama Donald baada ya kutaarifiwa kilichojiri kuhusu nyumba. Mwili wake ukaisha nguvu, mapigo ya moyo yakadunda kwa kasi. Ghafla akashindwa kujizuia akadondoka sakafuni puuu! kama furushi, Dada Angel alipoona tukio lile huruma ikamjia akasogea alipodondoka Mama Donald akamshika Mama Donald eneo la moyo. Alipomshika tu akagundua kuwa mapigo ya moyo ya Mama Donald yamesima, hahemi tena.



“Mbwa wee, si unaona sasa ushaua. Donald akija nitamueleza nini wakati huyu ndiye mzazi anayemtegemea,” Dada Angel akang'aka. Akimng'akia Mr. Msunga.



“Wee mwanamke mbona mshamba.... Wewe fikiria nyumba hii ikiwa kwenye mikono yangu huoni raha kuwa tutazidi kutanua na kujimwaya kwa raha zetu,” Mr. Msunga akarubuni.



“Sawa tutajitanua, ila Mama Donald mie ni kama mzazi wangu alinilea tangu utoto wangu hivyo lazima nimpende na nimthamini katika maisha yangu.”



“Sasa ndio uanze kumsahau, tuanze maisha yetu.”



“Siwezi.”



“Kama huwezi tokaa!!, kwasasa mimi ndiye mmiliki.”



“Nitamsahau, kuliko kuondoka kusipofahamika.”



“Hayo ndiyo maneno...sasa huyu maiti ngoja nikamfukie nje ya nyumba ili kupotea ushahidi,” Mr. Msunga alimkatili Dada Angel hadi Dada Angel akahamasika, akamfukia Mama Donald.



**********

Mihula ikaisha, miaka mitano ikakamilika. Mwaka wa mwisho wa kumaliza chuo Donald ukatimia. Akamshukuru Mungu kwa kupata stashahada ya Uchumi katika chuo kikuu cha Mzumbe, Donald alipokamilisha kila kitu akaianza safari ya kurudi nyumbani akakutane na mama yake pamoja na mchumba wake Fatuma. Ambaye ndiye msichana aliyeteka fikra na akili yake, Donald akiwa kwenye basi akajaribu kumtafuta mama yake kwa njia ya simu lakini simu haikupatikana. Akaacha akajaribu kumpigia simu Dada Angel lakini ikawa vivyo hivyo simu ikawa haipatikani, Donald alipoona simu zote hazipatikani akatulia kidogo akitafakari akajiuliza maswali ila hayakuwa na majibu sahihi.



“Mbona simu zao hazipatikani...kulikoni?.”



“Mh!, kutakuwa na tatizo.”



“Lakini kama kungekuwa na tatizo, si wangenihabarisha?.”



“Labda, hakuna tatizo,” Donald akajiwazia.



Yakapita masaa Donald akiwa bado yupo kwenye basi akiendelea kujihoji, ghafla!!! wazo likamjia. Ambalo wazo la kumpigia simu Fatuma, akampigia Fatuma simu. Simu ikaita kwa muda kisha ikapokelewa.



“Hallow, mpenzi” ilisikika sauti ya Fatuma kwenye simu ikiongea kwa huba.



“Hallow...niambie mpenzi,” Donald alimchangamkia Fatuma huku akionyesha tabasamu mwanana angali asijue kinachoendelea nyumbani.



“Safi tu, za wewe.”



“Salama tu.... Umenisusa”



“Hamna sijakukususa kipenzi. Masomo tu ya muhula wa mwisho ndiyo yalinibana sana hadi nikashindwa kukusabahi.”



“Sawa...lakini mambo mengine yanasemaje kipenzi?.”



“Safi kiasi.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Mmmh, sasa mie nipo njiani leo narudi Dar es salaam.”



“Waoooh!!!, nafurahi sana kusikia unarudi maana nimekukumbuka sana.... Sasa hivi umefika wapi?.”



“Kwasasa nipo Chalinze...una nafasi uje kunipokea hapo Ubungo maana nimepiga simu nyumbani ili waje kunipokea wakawa hawapatikani, sijui wanashida gani.”



“Wewe, unahisi kuna shida gani nyumbani?.”



“Sijajua.”



“Usihofu kutakuwa hakuna shida yoyote, labda simu zao zitakuwa zimezimwa tu kwa wakati huu. Mimi nitakufuata,” Fatuma akamtoa hofu kipenzi chake akakata simu haraka, akajiandaa.



Donald alipokwisha ongea na Fatuma akajilaza kidogo kwenye siti ya basi, akajipumzisha kuja kuamka basi likawa lishawasili Ubungo katika kituo cha mabasi. Alipofika akamjulisha kipenzi chake kwa kumchatisha na simu.



“Nimeshafika.”



“Umeshuka eneo lipi?.”



“Nimeshuka ndani, jirani na banda la vitabu linaloitwa Bongo Writer.”



“Sasa mimi nipo nje.... Unaweza kuja mpenzi?.”



“Sawa nakuja,” Donald akamaliza kuchati. Akaweka simu katika mfuko wa suruali akatoka nje. Kufika nje akang'aza macho kila kona akimtafuta tamu yake, walipoonana wakakimbiliana wakakumbatiana kwa upendo wote.



“Mpenzi.... Nina furaha kubwa moyoni ulivyorudi leo,” Fatuma akasema.



“Nami nina furaha pia, mpenzi,” Donald nae akaongezea kusema.



“Shukrani.”



“Lakini kwa sasa, kuna kitu nahitaji kukuambia.”



“Kitu gani hicho Donald, unachotaka kuniambia?.”



“Kwa kuwa nisharudi nahitaji nisichelewe kufanya maandalizi ya ndoa...au wewe unalionaje hilo?.”



“Ni sawa, mimi sina kipingamizi chochote dhidi yako. Nadhani unajua ni jinsi gani ninavyokupenda hivyo kwa suala ulilolisema la ndoa nimefurahi mno,” Fatuma alitabasamu mara baada ya kusikia maneno ya hekima yaliyosemwa na Donald.





Wakasitisha mazungumzo hatimaye wakaelekea kupanda mwendokasi unaoelekea Kimara mwisho, wakiwa ndani ya mwendokasi Donald akasikia simu inaita hakuchelewa akaitoa simu katika mfuko wa suruali akaangalia mtu anayepiga ni nani. Jina akaliona ni la Dada Angel, Dada Angel ndiye aliyepiga. Upesi Donald akapokea simu.



“Dada Angel, kwema huko?,” Donald akadadisi.



“Si sana...niliona missed call yako, kuna tatizo?,” Dada Angel alijibu kimkato. Akaliuliza bila hofu.



“Hapana, nilikupigia ili nikujulishe kwamba leo narudi.”



“Sasa hivi upo wapi!!!?.”



“Nipo Kimara Baruti.”



“Nafurahi, lakini Donald nataka nikuhabarishe kabla hujafika,” Dada Angel aliongea huku kana kwamba akiwa na hofu. Donald akagundua hilo kutokana na Dada Angel kila mara anashusha pumzi ya hofu mfululizo.



“Kuhusu nini?...halafu mbona unasikika ukiwa na hofu, hofu imetokana na nini?.”



“Kweli nina hofu, na hiyo hofu imetokana na kitu kilichotokea hapa nyumbani halafu nimekaa kimya bila kukutaarifu. Kuhofia ukatili nitakaokabiliana nao,” Dada Angel alieleza lakini kwa kuibia ibia huku macho yakitazama katika chumba cha Mr. Msunga ili asibambwe na Mr. Msunga yakawa mengine.



“Kitu gani kimetokea?...niambie.”



“Sijajua nianze, wapi ili unielewe.”



“Hicho kitu kina ukubwa kiasi gani, hadi unafikiria kwa kuanzia kuniambia.”



“Ni kikubwa mno, bora nisikuambie sasa nitakuambia utakapofika nyumbani.”



“Sawa...kama nusu saa hivi nitakuwa nishafika kama si lisaa limoja,” Donald akakata simu.



Wakiwa bado wapo ndani ya mwendokasi, Donald akaonekana kushika tama akifikiria kinagaubaga hicho kitu alichotaka kuelezwa na Dada Angel. Akiwa amezama kwenye fikra mara akahisi kushikwa bega akazinduka fikrani akapinduka amtazame aliyemshika bega, kupinduka akakutana na sura ya Fatuma yenye tabasamu ambaye ndiye mtu aliyemshika bega akitaka kujua Donald amepatwa na nini.



“Mpenzi!!, mbona unaonekana una fikiria sana...kuna kitu kibaya kimetokea?,” Fatuma akauliza.



“Hamna, kitu chochote Fatuma,” Donald hakuwa muwazi. Akamficha Fatuma kinachomtatiza.



“Donald, unanificha. Naomba usinifiche kitu nieleze.”



“Ngoja nikueleze...hapa nimetoka kuongea na Dada Angel lakini maongezi yake anayoongea nahisi kama kuna kitu kibaya kimetendeka anaogopa kunieleza. Ukweli ananiweka kwenye wakati mgumu kichwa chote hakijatulia,” Donald akahisi.



“Kwanini kichwa kisitulie mpenzi. Hebu...tuliza kichwa kiweze kung'amua mambo mengine,” Fatuma alijaribu kumtuliza Donald.



“Sasa nitatulizaje kichwa, wakati jambo lenyewe analotaka kuzungumza linaonekana tu si la heri.”



“Umejuaje, kama si la heri?.”



“Lingekuwa la heri asingekosa kunieleza, hili si la heri ndiyo maana anasua kusema.”



“Sawa, inawezekana kweli lisiwe jambo la heri lakini nawe yakupasa usiwe mtu wa mawazo kuwa mtu ngangari uje kushindana na kila kikwazo,” Fatuma akaeleza.



Masaa kadhaa wakawa washawasili nyumbani, wakafunguliwa geti na Dada Angel. Wakaingia ndani wakionyesha kutabasamu lakini yeye Dada Angel akaonyesha kuwa na huzuni katika sura yake, yote sababu ya mauaji ya Mama Donald yaliyotokea miaka kadhaa huko nyuma.



“Dada Angel, kuna nini kilichotokea?,” Donald aliuliza mara baada ya kugundua huzuni uliomtanda usoni Dada Angel.



“Hamna kitu,” Dada Angel alijibu haraka kana kwamba ni mtu aliyebanwa na haja. Sasa anajibu haraka ili awahi maliwatoni akakidhi hitaji.



“Unadanganya...mbona unaonekana katika uso wako ni mtu mwenye huzuni?.”



“Donald, kwa kuwa ushanitambua bora nikueleze...” alisema Dada Angel huku akibubujikwa na machozi. Akanyamaza akajifuta machozi akazungumza.



“Donald...nyumbani hapa kumetokea tukio kubwa, ambalo limeleta gumzo kwangu na hata kwako.”



“Tukio gani hilo?.”



“Mama, ame...ame,” Dada Angel akamung'unya maneno yasiyoeleweka.



“Mbona unasita, mama amefanyaje?,” Donald alipayuka mara baada ya kuona Dada Angel anajing'ata kusema.



“Mama, amefariki” alijibu Dada Angel huku akiwa na presha kubwa akihofia lile jambo Donald atalipokeaje.



“Amefariki!!!...lini?,” Donald akashangaa, akauliza kwa kustaajabu ya Musa. Hakuamini amini.



“Muda kidogo...alifariki kwa presha.”



“Sasa mbona mama, hakuwahi kuniambia kama ana presha?.”



“Ukweli presha alikuwa hana. Presha hii ni ya ghafla na aliyefanya mama yako apate presha si mwingine bali ni Babaako.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Unamaanisha, ni Mr. Stanley Msunga ndiye aliyesababisha mama yangu kufa?.”



“Eehe.”



“Kilitokea nini, hadi mama akapatwa na presha?.”



“Mr. Msunga alimjibu mama maneno ya mshtuko kuwa eti; hati ya nyumba anayo yeye na amebadilisha hati jina kaliweka jina lake.”



“Kivipi na kwanini hati yetu ya nyumba aweke jina lake?...kwani hii nyumba yeye inamhusu?.”



“Naona hii ni njama ya kutaka kudhulumu.”



“Sasa nishagundua kumbe kweli Mr. Msunga amekuja hapa kwa ajili ya kudhulumu mali.... Sasa mwili wa mama upo wapi?.”



“Mwili wa mama Mr. Msunga kauzika kipindi cha nyuma kisiri. Na hivi tunavyoongea Mr. Msunga yupo huko bustanini akipunga upepo.”



“Ah!, kweli huyu ni binadamu?.... Yaani amemzika mama kama takataka,” Fatuma alichangia mazungumzo huku majonzi yakilanda landa machoni mwake mara baada ya kukaa kimya kwa muda kidogo.



Habari ile ikamuumiza Donald zaidi kilichomuumiza ni kusikia mama yake kuzikwa kama furushi la taka, Donald akakurupuka pale sebuleni alipo keti akaelekea moja kwa moja bustanini alipo Mr. Msunga. Alipofika macho yake yakakutana na macho ya Mr. Msunga jazba ikampanda Donald hasira ikamtawala kichwani mwake, hakutaka kuwa na maongezi na shetani kama Mr. Msunga wala kumsikiliza kwa chochote bali alipomkaribia akamvaa mwilini na kuanza kumpa kichapo cha mwizi. Dada Angel na Fatuma wakiwa wapo pale sebuleni nje wakasikia makelele na purukushani haraka wakatoka nje waamulie kabla ibilisi mbaya hajapamba moto, ile wanafika tu hata hivyo wakawa wamechelewa sababu Mr. Msunga alikuwa kashachomoa kisu kilichopo kiunoni mwake na kumchoma kifuani Donald. Wakamkuta Donald kashakwenda chini anaugulia maumivu, Fatuma upesi akakimbilia alipo Donald akadondoka chini akainua kichwa cha Donald akakipatia hifadhi kwa kukilaza mapajani mwake huku machoni akitoa machozi akimlilia kipenzi chake.



“Donald, naomba usiniache peke'angu katika kipindi hiki ninachokuhitaji,” Fatuma akaongea. Akazidi kumlilia Donald, akiwa bado analia ghafla Dada Angel akachoropoka pale akakimbilia ndani kuongea na simu.



“Hallow...hapo ni kituo cha polisi?,” Dada Angel aliuliza mara baada ya kuhakikisha simu imepokelewa.



“Yes!!!, kuna tatizo?” ilisikika sauti kwenye simu ikijibu na kuuliza. Ile sauti yenye besi na ukakamavu ikathibitisha dhahiri kuwa yule ni polisi.



“Eehe.



“Tatizo gani?.”



“Nyumba namba 112, eneo la Kimara Suca. Mtaa wa Bwawani kumetokea uvamizi na mauaji ya muda kidogo...hadi sasa ninavyoongea mhalifu bado yupo naomba msaada wa kumkamata kabla hajakimbia.”



“Uvamizi na mauaji!!!, shit.... Mauaji yametokea muda gani?.”



“Ni muda.”



“Okay, hakikisha mhalifu asikimbie ndani ya dakika tutakuwa tushawasili,” Polisi yule alitoa ahadi kisha haraka akakata simu.



Dada Angel alipomaliza kuongea na simu akarudi nje huku akiwa makini ili Mr. Msunga asitambue kinachoendelea. Donald akiwa bado amelala hoi mapajani mwa Fatuma ghafla wakaja kuona geti kuu likifunguliwa walipoangalia kwa makini wakaona waliokuja si wengine bali ni mapolisi watatu, wakagundua wale ni polisi sababu ya utambulisho wao adhimu. Walionekana mikononi mwao kushika pingu, virungu na kuvalia vazi lao la kiaskari. Polisi walipoingia ndani na kufika walipo kina Donald, masikio ya Donald yakamsikia polisi mmoja akisalimu na kukunja ndita.



“Habari!!.”



“Salama kiasi chake,” Dada Angel aliitika salamu ya polisi huku akikaza jicho kwa Mr. Msunga.



“Bila shaka, hii ndiyo nyumba iliyotokea mauaji?,” Polisi yule mmoja akazidi kuhoji.



“Hujakosea hii ndiyo nyumba yenyewe, na pia mimi ndiye niliyewapigia simu kuwajulisha kama kuna mauaji yametokea,” Dada Angel alihabarisha mapolisi bila shaka.



“Eehe.... Mlengwa mwenyewe yupo wapi?,” Polisi wa pili akahoji.



“Mtuhumiwa mwenyewe, ni huyo aliyevaa shati la bluu,” Dada Angel akaeleza huku akimuonyesha Mr. Msunga. Polisi baada ya maelekezo wakasogea alipo Mr. Msunga wakamkamata kwa kumfunga pingu mikononi, wakatoa agizo.



“Mgonjwa wenu kachomwa kisu sehemu mbaya, inahitajika apelekwe hospitali upesi akapate matibabu kabla hajaaga dunia,” Polisi wa tatu akahabarisha mara baada ya kumuangalia Donald kwa muda.



Baada ya polisi kutoa maelekezo wakamchukua mhalifu wakaelekea nae kituoni kabla hajafikishwa mahakamani kusomewa hukumu. Dada Angel na Fatuma walipohakikisha Mr. Msunga kaondoka na polisi wakashirikiana wakamuwahisha Donald hospitali akapate huduma, Donald sababu amechomwa kisu pabaya hivyo alipofika hospitalini daktari akampeleka moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji akampatia huduma ya kwanza kisha akamlaza kitandani apumzike. Hatimaye yeye akaende ofisini walipo kina Fatuma awape na wampe mukhtasari.



“Wapendwa, mgonjwa wenu kwani amepatwa na ajali gani?,” Daktari aliuliza mara baada ya kufika ofisini.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Mgonjwa alichomwa kisu na vibaka, nyakati za usiku akiwa ametoka kazini,” Fatuma aliongopa ili kuepusha laumu za Daktari.



“Mh!, kwani mgonjwa wenu anafanya kazi gani?.”



“Mgonjwa wetu anafanya kazi ya ulinzi katika jengo la Benki ya NMB, iliyopo Posta,” Dada Angel alichangia uongo nae mara baada ya kuona Daktari amezidi kudadisi.



“Okay, huyu mgonjwa nyie anawaitaje?.”



“Mimi ni dada yake, na huyu ni mke wa mgonjwa,” Dada Angel akamfahamisha Daktari.





“Kwa sasa wazazi wa mgonjwa wapo wapi?.”



“Wazazi wote wamefariki.”



“Poleni sana!!!.”



“Asante...lakini daktari mgonjwa wetu anaendeleaje?.”



“Mgonjwa anataka afanyiwe upasuaji. Lakini katika upasuaji mgonjwa atapungukiwa damu inahitajika aje aongezwe damu ili awe sawa,” Daktari akataarifu kwa ufasaha.



“Mh, lakini mbona huu utakuwa mtihani. Damu itapatikana vipi!!!, maana sijawahi kuthubutu hata mara moja kutoa damu. Naogopa sana,” Dada Angel aliongea huku akionyesha kuogopa wazi jambo lile la kutoa damu.



“Basi kama Dada Angel anaogopa, kama kuna uwezekano wakutoa damu mimi. Daktari twende ukanipime niweze kumchangia damu kipenzi changu,” Fatuma akadakia mazungumzo yaliyokuwa yanaongelewa baina ya Daktari na Dada Angel.



“Sawa kama umeamua kumchangia mgonjwa damu yote heri, sasa mwenzako asubiri hapa. Mimi na wewe twende maabara nikakupime ili kama damu yako haina kasoro tuweze muongezea mgonjwa,” Daktari alisema huku akinyanyuka kwenye kiti, akavaa koti vyema kisha wakaongozana na Fatuma maabara kwenye vipimo.



Daktari akampima Fatuma damu akagundua damu ya Fatuma haina kasoro, pia akaona damu ya Fatuma inarandana na ya Donald. Hakuwa na budi kuchukuwa damu ya Fatuma kumuongezea Donald, akachukua damu ya Fatuma kisha akarudi nae Fatuma ofisini kule walipomuacha Dada Angel mwenyewe.



“Mmechelewa sana, kulikuwa na tatizo?,” Dada Angel aliuliza mara baada ya kuona Daktari karudi na Fatuma katika ofisi.



“Hakuna tatizo, mambo yanaenda safi tu. Naona,” Fatuma alijibu huku akitabasamu.



“Oooh! kwa hiyo Donald atakuwa vizuri baadae. Kweli hilo ni litakuwa jambo la kumshukuru Mungu,” Dada Angel alisema huku nae akijaribu kuvuta taswira ya tabasamu.



Daktari akakaa kwa muda kidogo ofisini kisha akaelekea katika wodi ya upasuaji kwa ajili ya kuanza upasuaji na kumuongezea damu, alipomaliza shughuli zote akamtazama mgonjwa wake kwa muda hatimaye akatoka wodini akarudi ofisini huku akionyesha kwenye kinywa chake kumejaa furaha tele.



“Daktari una furaha, kuna nini kilichojificha nyuma ya pazia,” Fatuma akazungumza.



“Baada ya upasuaji mgonjwa wenu ataendelea vizuri,” Daktari aliongea mara baada ya kuketi kitini.



“Kwasasa tunaweza kuongea au kuondoka nae?,” Dada Angel akauliza.



“Kwasasa nimempumzisha inabidi mwende nyumbani kesho asubuhi, mrudi,” Daktari akahabarisha.



Dada Angel na Fatuma wakatekeleza agizo la daktari wakaondoka kisha wakarudi nyumbani, kwa kuwa muda ulikwenda Fatuma akafika nyumbani usiku. Ile anafungua mlango tu wa sebuleni akakutana na baba yake akiwa anamsubiri kwa hamu.



”Wewe mpumbavu, umetoka wapi usiku huu?” ilisikika sauti ya Baba Fatuma ikiongea kwa ukali mara baada ya Fatuma kuingia ndani kwa kusua sua.



“Nimetoka kwa Amina,” Fatuma akaongopa.



“Ndiyo usiku.... Naona ushamaliza chuo unaanza umalaya, si ndiyo?.”



“Hapana.”



“Kumbe?.”



“Amina anaumwa, ikabidi nikamsaidie kazi ndogo ndogo,” Fatuma akazidi kudanganya toto.



“Najua kwa hili unanidanganya tu ila siombei mabaya, ipo siku utapata ya kupata ndiyo utakaponieleza vizuri,” Baba Fatuma aliongea kwa hisia kisha akaingia chumbani kujipumsha.



Fatuma akapitiliza bafuni kubafu mwili uliojaa uchafu na uchovu, alipokoga akaenda moja kwa moja kitandani kwa ajili ya kujipumzisha. Asubuhi na mapema akadamka kuamka akajiandaa akaelekea kugonga mlango wa wazazi.



“Hodiii.”



“Ingia,” Mama Fatuma sauti yake ikasikika chumbani ikimkaribisha mwanae. Fatuma akaingia.



“Hadi sasa bado mmelala?” aliuliza Fatuma mara baada ya kuingia chumbani kwa mama yake.



“Mwenyewe si unajua mwanangu, kazi zetu za serikali zinavyochosha hivyo tukipata wasaa kidogo kama hivi yatupasa tutumie vema.”



“Hata hivyo nisamehe sana kwa usumbufu, mwanao nilikuwa sina kingine zaidi ya kukujulia hali na kukuaga.”



“Hata hivyo usijali, maana umenionyesha moja ya upendo na kujiona ni jinsi gani mwanangu unavyonipenda na kunithamini mie mama yako. Asante sana... Unakwenda wapi?.”



“Nakwenda hospitali rafiki yangu anaumwa kweli. Kwani baba yupo?.”



“Kashaondoka zake...kwa hiyo rafiki yako huyo nini zaidi anaumwa?.”



“Alichomwa kisu, kwa hivyo ndiyo kalazwa hospitali.”



“Aisee, augue pole.”



“Hata hivyo Mungu atamsaidia tu.”



“Amen.... Sasa utawahi kurudi?.”



“Nitawahi kurudi.... Kwa sasa ruhusa yako ndiyo muhimu.”



“Haya nenda mwanangu, ila uwahi kurudi kweli si unamjua baba yako alivyokuwa Mbogo,” Mama Fatuma aliongea na Fatuma, kisha wakaagana hatimaye Fatuma akaondoka.



Fatuma akatokomea nyumbani akaelekea hospitalini kuonana na mgonjwa, lakini kabla hajafika hospitali akiwa katika kituo cha daladala akamtafuta Dada Angel kwa njia ya simu. Simu ikaita.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hallow...ushatoka nyumbani?,” Fatuma aliuliza mara baada ya Dada Angel kumpokelea simu.



“Nishatoka. Kwa sasa nishafika hospitali nipo hapa na mgonjwa namnywesha uji...wewe upo wapi?,” Dada Angel akauliza.



“Mimi nipo njiani ndiyo naja huko...eeehee, na kumbukizi ya mama ni lini?.”



“Kumbukizi ni 17/05 Ijumaa.”



“Vizuri, sasa Donald kasharuhusiwa?.”



“Kasharuhusiwa, ila anakusubiri wewe tu ufike twende wote nyumbani,” Dada Angel aliongea kisha akakata simu akaendelea kumnywesha uji Donald. Lisaa likapita Fatuma akawa kashawasili hospitalini.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog