Simulizi : Fundo La Umivu
Sehemu Ya Nne (4)
Mambo yalikuwa hivyo. Balaa! Juu ya balaa. Hisia ziliwatesa. Kwa kila mmoja kumpenda mwenziye, ila tatizo likawa ni uzito katika uzungumzaji. Dhihirisho la kupendana kwao, liliendelea chanua. Kwa jumbe na simu wasizoisha kupigiana. Zawadi mbalimbali walizokuwa wanatumiana, na shida nyingi zisizoisha kusaidiana. Ila si upendo wa uhusio mahusiano ya kimapenzi, hapana. Bali ni mahusiano ya urafiki. Siku zilizidi songa mbele. Shauku ya kutamka sasa waanzishe mahusiano ya mapenzi nayo ikawa inazidi panda moyoni mwa Vumilia. Aliandaa mikakati. Kisha kusubiri siku, itayomfaa. Kutupa ndoano yake. Wakati huo, wivu nao ulikuwa sehemu ya mahusiano waliyonayo. Japo ni ya urafiki. Kila mmoja alikuwa na wivu kwa mwenziye, tena wa waziwazi, huku wakionesheana wenyewe, watu wa nje hawakuhitaji wagundue. Kwani mara nyingi, washindwapo kuwasiliana kwa wakati ama kutumika muda mrefu kwa maongezi na mtu mwingine, huchimbua hisia kali za mateso. Zenye kuonesha hajafurahishwa na kitu kilichojiri. Upendo alionesha hali hii sana, pale amkutapo Vumilia hapatikani, wakati kashazoeshwa muda wote simu yake huwa hewani. Kwenye kujieleza, Upendo alikuwa hakubaliani kwa uharaka na maelezo ya Vumilia kwa kitendo hicho. Alikuwa anapingana naye vikali, hadi aeleweshwe zaidi ya mara mbili na kuombwa ombwa radhi ndipo hurudi na kuridhia.
Hata Vumilia naye hakukosa. Pale akutapo Upendo hapatikani ama anatumika kuongea kwa muda mrefu. Naye kuonesha sehemu ya wivu wake. Namna gani aumiavyo.
“Vumi! Tambua nami nina moyo. Naumia, hivyo acha kunihisi vibaya kila wakati,” alisema Upendo, jioni moja baada ya kulalamikiwa anapunguza kujali, kutokana na kuhisiwa kashaanza pata wanaume wengine.
Ni oktoba 27, 2017 Vumilia akiwa kazini. Oparesheni maalumu kuzungukia mipaka ya mkoa wa Dodoma. Shughuli iliyopangwa kuchukua takribani muda wa wiki moja, haja zote wakipata hukohuko, hadi pale muda husika wa kazi utapomalizika. Kazi kubwa ilikuwa kuangalia na kuzichunga barabara za magendo, zisizo rasmi zilizotengenezwa kwa jitihada za wahusika wa ufanyaji wa biashara haramu, zisitumike. Sababu hazipo kihalali. Shughuli ilikuwa pevu, iliyomkosesha uhuru na uchangamfu wa mwili. Muda mwingi alikuwa mchovu, miale ya jua ilichangia. Ilikuwa inamulika kiasi kwamba hadi kichwa kinauma. Wakati wapumzikao, hakuacha kufarijika, kuona katua kero kadhaa ambazo zilimfanya vibaya ila alishindwa kusema kwa sababu ya kutimiza wajibu. Alitumia wasaa huo, kupata mapumziko mazuri zaidi, kwa kuwasiliana na mtu akeshaye kumpatia faraja moyoni mwake. Upendo!
Usiku wa saa 2 ndipo walipata kupumzika. Mara baada ya kutwa kuzunguka vijiji mbalimbali na kupata chakula cha jioni. Alimpigia Upendo. Kama ilivyo kawaida yake. Huyo ndiye alikuwa burudisho la kipekee maishani mwake. Punde alivyopiga, simu haikuchukua sekende nyingi kuanza kuita kisha upande wa pili kupokelewa na kuanza maongezi. Waliongea kwa muda mfupi sana. Simu ikakata. Ila hiyo haikuwa chanzo cha yeye kusitisha mawasiliano. Alipiga mara nyingine. Muda huohuo, isivyo bahati, akakuta inatumika.
Alipatwa na wazo fulani, lakini hakulipa nguvu. Akaamua kupiga mara ya pili, matokeo yakawa kama mwanzo, akapiga mara ya tatu tena, matokeo yakawa yaleyale, yaliyomfanya aanze kujihisi vibaya na kuona kadharauliwa. Katikati ya fikra hizo simu yake ikaanza ita. Alivyoangalia jina la mpigaji kwenye skrini alikutana na jina la Upendo. Pasi na hiyana. Aliipokea. Lakini si kwa furaha ya kufurahia maongezi. Bali kwa uchungu. Wa fundo tele lililojikusanya moyoni.
“Kama hukuitaji kuwasiliana nami si ungeniambia. Si kwa kitendo hicho ulichonifanyia,” alianza kwa kusema hivyo. Taratibu hasira nazo zikishinikiza atoe lake la moyoni.
“Nilijua tu utalalamika.”
“Poa. Acha niendelee kulalamika. Ongea na mtu wako,” alisema Vumilia na kukata simu.
Kitendo hicho kilimpatia umizo. Kukatiwa simu pasipo kutaarifiwa. Kila alivyowazua, aliona dharau tosha. Ya waziwazi ambayo hakuhitaji mtu amdadavulie, maana ya mlolongo wa tendo lilivyojitokeza bayana lilijieleza. Hakika! Ilimuumiza na kusononesha moyo wake kwa kiasi kikubwa. Kiasi kwamba, atafutwapo mara nyingine hukata simu, na pale apokeapo hutoa majibu ya ovyo kwa mwenziye. Alikasirika! Hata alivyoombwa msamaha, hakutambua thamani ya msamaha aombwao. Alikataa katakata kumsamahe, hali iliyopelekea Upendo abwabwaje machozi usiku huo.
“Vumi! Nakuomba msamaha unashindwa nisamehe? Mambo mangapi hunifanyia lakini mimi huwa nakusamehe?”
“Nitakusamehe. Si lazima iwe leo. Siku bado zipo.”
“Unachoshindwa kuniambia sasa ni nini?”
“Nimekuambia nitakusamehe. Kama uhitaji basi. Fanya uamuavyo. Muombe huyo mwingine uliyekuwa unazungumza naye.”
Kauli hizo zilikuwa zimeambatana na kilio toka kwa Upendo. Tena sio cha kujifanyisha ili asamehewe. Hapana! Ni kilio halisia kisababichwasho na maumivu. Kisa kutotambuliwa thamani yake. Hiyo ilikuwa kawaida kwa Vumilia. Mgumu wa kutamka neno msamaha. Na kama atatamka, si kwa maanisho tosha toka moyoni. Huwa kwa kumfurahisha yule mkosa, ila dhihirisho libakilo moyoni ni uchungu na mateso. Sababu kuu impelekeayo kufanya hivyo, ni imani aliyonayo. Watu wengi hufanya maovu kwa mwavuli wa msamaha. Ikiwa na maana atafanya tendo ovu kisha kukimbilia msamaha, kuonesha hajakusudia kufanya. Hicho hakuwa anakubaliana nacho, na ndiyo maana huwa na maamuzi ya aina hiyo. Kutokuwa mwepesi wa kusamehe.
Juu ya hilo huruma hakukosa. Huruma yake hujitokeza, aonapo mtu hutoa chozi, kwa sababu yake. Hujisikia vibaya na mara nyingi hapendi. Hivyo kitendo cha Upendo kuanza kulia, kisa kashindwa kusamehewa naye, kiligusa moyo wake, na kujaza huruma, iliyomsukuma kupiga simu kuanza mbembeleza asitishe kulia. Alitumia maneno yenye ukarimu. Yaliyosheheni nguvu na mshawasha wa kumpatia hamasa asiendelee kuruhusu kutokwa machozi. Ubarikio wa matamshi yenye msisimko, yalipangwa yakapangika, kisha pasipo kusubiri yakafikishwa kwa mhusika. Naam! Yalisaidia. Nguvu ya maneno kushinda nguvu ya kilio, dakika kadhaa baadaye Upendo alitulia.
“Naomba usirudie tena Vumi. Kwani umeuumiza sana moyo wangu. Ila nashukuru kwa kunisamehe. Na kuisikia sauti yako inibembelezayo wakati wa matatizo yetu,” alisema Upendo.
“Siku za nyuma uisikiavyo huwa wakati wa nini?”
“Wakati wa faraja. Na kama matatizoni, ni matatizo yaliyosababishwa na watu wengine.”
“Poa!”
“Okay! Love you, and take care.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ili upate kufanikiwa lazima ukumbane na changamoto za aina mbalimbali. Hakuna mtu wenye historia ya mafanikio pasipo kusimulia dhana hii katika simulizi yake. Kwa nyanja yoyote ya kimaisha. Wawili hawa, makasiriko yalikuwa sehemu ya changamoto katika kufikia hatua ambayo hawakuipanga. Japo mpaka kufikia hapo, bado walikuwa kwenye dhana ya urafiki. Iliyobeba mahusiano ya kimapenzi. Changamoto nyingine ilikuwa ni wivu. Na ndiyo ambayo ilikuwa kubwa zaidi ya nyingine. Wivu ulikuwa mstari wa mbele kwa kila mmoja, si hakika. Kama ulikuwa unadumisha upendo ama walikuwa wanabomoa. Kwani, hazikupita siku nyingi. Wakawa wanakesha kwenye malumbano kila leo. Malumbano yaliyomuacha mmoja umizoni, hasa Upendo. Ila walizidi kusonga kadri siku zilivyokuwa zinazidi kwenda mbele. Walivumiliana, ila kero zilizidi uvumilivu. Kwani haikupita siku, pasipo ingia mtafaruku wa aina yoyote, tena hata kuhusiana na matendo yaliyokwisha pita kipindi cha nyuma. Ule ukaribu uliopata kuwepo nyuma bado ulikuwepo, ila haukuwa na faraja kama ilivyokuwa awali. Kila walivyojitahidi kutafuta waliambulia patupu. Na kuwafanya waanze tafuta mbinu ya kuondoa ubaya uliowateteresha. Imani potofu!
Hasa kwa Vumilia. Kwani toka siku aliyokatiwa simu pasi na taarifa, hakumuamini tena Upendo. Alimuona ni mtu wa wanaume muda wote, huku akitumia mwavuli wa dini kujificha. Hisia zilimtuma, kumuona mwanamke huyo kama wanawake wengine. Japo mwanzo alimuona wa tofauti kutokana na stara aliyonayo. Ila siku za sasa haikuwa hivyo tena. Alimuunganisha katika orodha, ya wanawake wengine wa mtaani, ambao asilimia kubwa hutumia miili yao kuwa kitega uchumi. Imani hii ilimfanya kumropokea maneno machafu. Ya kumtaka awasiliane na wanaume wake na watu wengine, ijapokuwa ndoto ya kuingia ndani ya himaya yake bado ilikuwepo. Na alitaraji siku moja lazima iwe. Si kwa kuingia himayani na kuacha pekee. Bali mazima, kuwa wanafamilia.
Baada ya mtiririko mrefu wa siku za malumbano, Upendo alishindwa kuvumilia. Akawa anamhusisha Mwanjaa amsaidie katika utatuzi. Alikuwa anamhadithia kila kilichojiri leo, na yale ya siku za nyuma, kisha huomba ushauri nini kifanyike na wakati mwingine humpatia majukumu, aongee naye wayamalize, mambo yawe kama yalivyokuwa awali. Asilimia kubwa, msaada uliotoka kwa Mwanjaa ulikuwa ni kumpigia Vumilia kutaka kufahamu undani wa matukio ukoje. Naye alivyohitajika kujielezea, alijieleza kisha kutoa oni amuambie huyo aliyemuagiza. Mambo yalibadilika. Kutoaminiana kulitawala. Na kuathiri mahusiano yao.
****
Tamu chungu ya Zamzam iliendelea. Mipango kabambe ya kusambaratisha mahusiano ya Vumilia na Upendo. Ikashika akili na kunuia. Akasubiri siku tu. Imfaayo kutimiza hilo. Usiku wa ijumaa, 05 novemba 2017, Vumilia akiwa amelala, simu kaweka chini ya kitanda, majira ya saa 5 simu yake iliita. Kutokana na usingizi uliokwishamchukua, hakuweza isikia. Mtu aliyoko pembeni yake, Zamzam ndiye aliisikia. Taratibu aliinuka, aliangalia jina la mpigaji na kubaini ni yule adui yake namba moja kwenye ulingo wa mapenzi, afanye asionwe wa thamani na Vumilia. Upendo! Hakusita, akili ilivyomtuma ndivyo alivyotenda. Aliipokea.
“Hallo!” aliita Zamzam.
Upendo alitulia kwa muda. Takribani sekunde mia moja ndipo akatoa kauli.
“Habari?”
“Salama.”
“Samahani, mwenye simu yuko wapi?”
“Kalala.”
“Sawa. Usiku mwema.”
“Nawe pia. Ama ulikuwa na shida naye ya muhimu nikuamshie?”
“Hapana. Usimsumbue.”
“Haya,” alisema Zamzam. Akakata simu na kuirejesha pale ilipokuwa awali.
Kwa namna yoyote, kitendo hicho aliamini kitamsaidia kuiona thamani yake ndani ya mahusiano. Atajaliwa na kuheshimiwa kama Upendo ajaliwavyo. Pia aliamini nguvu ya mahusiano ya Vumilia na Upendo itapungua ijapokuwa alishaambiwa ni marafiki hapo awali. Lakini baadaye alishindwa iamini kauli hiyo baada ya kuona uchanuzi mkubwa wa mahusiano kila uchao. Asubuhi kulivyopambazuka, punde tu, Vumilia alivyoamka, kitu cha kwanza alikimbilia simuni. Aliingia kwenye orodha ya simu zilizopigwa pasipo kupokelewa, zilizoenda na zile zilizokwisha pokelewa. Mshituko ulimpata. Punde alivyoangalia orodha hiyo na kubaini Upendo kapiga, na simu yake imepokelewa. Aliwazua, kama usiku kaongea na mtu yeyote hakupata kumbukumbu. Wazo la kumshawishi Zamzam ndiye kapokea likachanua, katika kuthibitisha hilo, aliinua macho yake kumuangalia akiwa kitandani kalala, wakagongana macho.
“Umepokea simu ya Upendo?”
“Kwani wewe umeona nini?”
“Nijibu, sio nawe unaniuliza.”
“Ulichokiona ndicho kilichotokea.”
Alipoa ghafla. Sura ya mambo kuzidi kuharibika ikaambaambaa usoni, na fikra za kutafuta suluhu la kumfanya Upendo atulie, asiwe na jazba za kusitisha hali waliyonayo baada ya kusikia sauti ya mwanamke mwenziye. Mnamo saa 2 asubuhi aliunga naye hewani. Aliwasiliana naye kumhoji kilichotokea ila Upendo hakuwa muwazi, kuelezea. Badala yake alimuomba amuulize Zamzam aliyepokea simu nini kimetokea. Hii ilikuwa ishara, iliyomtambulisha msichana huyo kachukia kwa kile kilichotokea. Hivyo hakuwa na budi kuomba msamaha, na kwa sababu aliamini, anakubalika sana, hakuchelea kukubaliwa. Lakini kwa masharti.
“Naomba simu yangu, nikipiga isipokelewe na mtu mwingine zaidi yako.”
“Hamna shida kuhusu hilo.”
“Mmmmh! Sema tu haina shida, kisha kitokee kilichotokea usiku wa jana. Halafu leo baada ya kuniomba msamaha unaanza kuongea ongea maneno yako yasiyoeleweka. Yaani wewe...!” alisema Upendo, kauli iliyoambatana na cheko mwishoni.
Kwa kiasi fulani mambo yalikaa sawa. Alijichunga na kuchunga matakwa aliyoambiwa yasiharibike. Ila tatizo la kutomuamini liliendelea. Na ndilo lilikuwa mwiba mkali. Hatimaye sekunde, saa, siku na majuma yaliyoyoma. Maisha yaliendelea, shughuli nazo ziliendelea kama ilivyo ada, zilizonawirisha miili yao. Mitafaruku iliyoanza ilipelekea kuchanua wigo, wa kuthamini wale aliokuwa nao katika mahusiano. Hasa Sabina. Hivyo kufanya idadi ya wasichana kufikia watatu.
Kwake aliona jambo la kheri. Kuwa na wasichana wengi namna hiyo. Kwani siku zote mwanamke ndiyo huonekana malaya, akiwa na mwanaume zaidi ya mmoja. Ila kwa mwanaume, hujiepusha na aibu hii, na kujihalalisha ustahili wa umiliki huo, kitu ambacho si sahihi. Alirejesha hisia zake taratibu, kwa Sabina, lengo kubadili ladha ya mitindo na ukatikaji wa nyonga. Pia baada ya kuona dalili zilizojaa ukosefu mapema kwa Upendo japo bado hakumtamkia kama anahitaji wawe wanafamilia moja. Mume na mke. Kwa Zamzam aliendelea kuteseka, mwanaume ampendaye kukengeuka. Yeye kuwekwa kapuni na kutafutiwa mtu watayechangia naye. Sababu alikuwa na mapendo ya dhati juu yake, aliendelea kuvumilia. Na kutafuta mbadala utaomhakikishia anakuwa juu ya wote.
Mwishoni mwa mwaka huo 2017, disemba karibu na tarehe za kuelekea msimu wa krismas, Sabina alizuru Dodoma. Baada ya kushawishiwa kwa kina na mapendo sahihi aliyonayo. Si kama alikuwa na uhitaji mkubwa wa kwenda huko, hapana! Bali ni maalumu kwa kufurahisha tu, haja zitapopungua, aondoke na kuwa mwisho wake, kwani Vumilia hakuwa na hisia naye. Kupokelewa! Alipokelewa kwa heshima sana. Alijaliwa namna yeye atakavyo, kwa baadhi ya siku. Ila usiku, nafasi ilibaki kwa mwenye mamlaka ya kupendwa. Upendo. Vumilia, alishindwa kujificha, hali aifanyao kwa Upendo isionwe na wasichana wengine, lakini hakuwa hivyo. Huyu naye alimuonesha namna anavyomthamini na kumpenda Upendo. Ishara tosha, kuwa Sabina, hakuwa wa umuhimu zaidi yake. Kwani naye lilikuwa jambo la kawaida sana kuachwa ndani usiku wa manane kisha hutoka nje kwenda kuzungumza na Upendo kwa njia ya simu.
Hiyo ndiyo nguvu vya upendo. Japo alikuwa rafiki. Aliyo na matamanio ya kuwa mke siku moja. Ili nia itimie, ilimlazimu kuchunga mambo ya wanawake aliopata kuwa nao hawaingilii kati kuanza kugombana na Upendo. Upendo alikuwa lulu kwake. Mtu aliyechukua nafasi kubwa moyoni, ukishawatoa wazazi. Hii yote ni kutokana na mawasiliano ya kila siku kupitia simu. Aliishi naye sabina, takribani siku nne. Ndipo alirejea kwao, jijini Dar es salaam. Lakini alirejea kwa maumivu. Kwani aliyetaraji kuwa sehemu ya faraji kwake kuonesha utofauti. Siku za mwanzoni alivyowasili, alikuwa anamthamini sana. Baada ya kutoa haja zake, mabadiliko yaliibuka. Vitimbi na matendo kemkem yenye udhia. Achilia mbali kuachwa ndani pekee kisha Vumilia kwenda kuongea na simu nje. Kuna siku aliachwa usiku nzima, akaenda kulala kwa Zamzam. Usiku wa mwaka mpya. Kuukaribisha mwaka 2018. Kwa namna moja ama nyingine. Vumilia alicheza na hisia za wadada hawa wawili. Zamzam na Sabina. Aliwafanya watoto wadogo, wasioweza kujitambua. Hivyo kuruhusu kufanya atakacho, huku akisahau kama kuna kitu kiitwacho maumivu, ambacho huwaachia kwa yote awatendeayo.
Sabina alivyorejea jijini Dar es salaam na kitabu chake kilifunikwa na kuhifadhiwa kabatini. Ikiwa na maana huo ndiyo mwisho wake. Hatokuwa na nafasi tena. Labda ya mawasiliano ya siku mojamoja, pale atapotokea kumkumbuka. Mhusika, ambaye ni Sabina, hakubainishwa katika hili. Ila ni matendo tu, ndiyo alibainishiwa. Kwamba haitajiki. Hasahasa ya kutopokelewa simu na kutopigiwa. Kila alivyojaribu, kuhoji kulikoni, hakupatiwa sababu iliyo na tija. Alijaribu kutumia watu, hasa ndugu na marafiki zake wa karibu, pia kutuma zawadi kumshawishi, mambo hayakubadilika. Vumilia alikaza kwenye msimamo wake. Akili ilibaki kwa Upendo na labdalabda, kwa Zamzam ambaye alikuwa karibu naye. Sabina alikuwa chaguo la mwisho kabisa, endapo hawa wawili wa awali wakishapotea himayani ndipo yeye afikiriwe kupatiwa kijiti cha kuongoza jahazi. Tena si kwa uongozaji wa kudumu, wa muda wakati huo akifanya tathmini. Lengo, kumgeuza, binti huyo kuwa mtumwa wa ngono kwake. Ila Sabina hakulifahamu hilo. Hisia na mapendo aliyonayo moyoni, yalimziba na kushindwa kumuonesha uhalisia wa Vumilia kwa kina. Ijapokuwa, alishaanza pata dondoo.
Januari 15, 2018. Usiku wa saa saba, Zamzam aligundua baadhi ya picha kemkem, zilizopigwa pamoja, Vumilia na Sabina. Katika simu ya Vumilia. Akiwa nyumbani kwao, wakati huo Vumilia kalala, hatambui liendelealo. Alifadhaika, mtu ampendaye kukosa kabisa hisia naye. Kiasi kwamba hushindwa kujizuia afanyapo maovu yake. Umizo alilojisikia, karibu moyo uchoropoke, hasira ilimjaa, katika harakati za kutafuta maamuzi.
“Siwezi umia peke yangu,” alisema kimoyomoyo, kisha kuunganisha picha kadhaa na kutuma kwa Upendo, kwa njia ya mtandao wa Whatsapp. Alivyohakikisha mlengwa kafikiwa, alifuta, baadaye akavuta shuka naye kujumuika kulala.
Asubuhi, hata kabla hakujapambazuka vyema. Mlio wa muito wa simu, kuashiria kuna ujumbe umeiingia, ulisikika. Vumilia akiwa tayari kashaamka. Hivyo aliweza usikia. Aliivuta simu na kukamatia vyema kiganjani, aliiendea programu husika ambayo ujumbe umeingia, Whatsapp. Akafungua. Alikutana na ujumbe toka kwa Upendo. Daima siku zote awasilianapo na huyu, huonesha furaha isiyo na kifani. Kwa njia yoyote watumiayo. Ujumbe mfupi ama wapigianapo. Hivyo jumbe ya asubuhi asubuhi hata kabla hakujapambazuka vyema, aliona ni namna gani Upendo anavyomjali. Na kutambua mchango mkubwa kwake. Ndiyo maana kadiriki kumtafuta mapema. Alim-miss! Naye chap, alimjibu. Baada ya hapo waliingia kwenye ulimwengu wa mawasiliano mazito yaliyoteka hisia zao.
“Yule ndiyo wifi yangu?” ilisomeka jumbe toka kwa Upendo. Iliyopelekea mshangao mkubwa kwa Vumilia. Na kujiuliza kulikoni katumiwa jumbe kama hiyo au kakosea.
“Yupi tena? Hiyo si picha ya kupakua toka mtandaoni,” alisema Vumilia, akitolea ufafanuzi kuhusu picha ya mwanamke aliyemuweka umbopande katika mtandao huo wa Whatsapp wanaotumia kuwasiliana. Alitoa maelezo hayo kwa kuhisi Upendo kaona wivu, picha hiyo kuwekwa. Ila alihisi tofauti.
“Mimi sizungumzii hiyo?”
“Picha ipi unaizungumzia?”
Kabla jumbe hii ya mwisho haijaonesha alama ya tiki, kuwa ishafunguka na kusomwa, picha mbili zimuoneshazo Vumilia na Sabina wameambatana katika pozi mbalimbali za kimahaba, zilimfikia Vumilia. Alistaajabu! Papo hapo aliinuka na kumuangalia Zamzam, ambaye alionekana bado kuwa yupo usingizini. Alimuamsha, hata kabla hajakaa sawa alimtupia swali.
“Umetuma picha?”
“Kwa nani?” aliuliza Zamzam, badala ya kujibu. Naye alijifanya kushtushwa na jambo hilo.
“Upendo!”
“Ndiyo nimetuma. Vipi? Si uliniambia kuwa huyo ni rafiki yako? Kuna ubaya gani akimfahamu mpenzi wako. Nimemtumia ili afahamu mwanamke uliye na mahusianao naye.”
Vumilia aliishia kutikisa kichwa. Huku akitoa jicho lililojaa hasira, kuonesha namna alivyokasirishwa na kitendo kilichofanywa. Alitamani kusambaza kipigo. Lakini kwa hali aliyonayo, alianza hisi anaweza mpatia matatizo makubwa. Kwa sababu alikuwa na hasira kwa kiasi kingi mno.
“Naomba kuanzia sasa usikamate simu yangu,” alisema Vumilia, akiwa amefura. Kauli iliyofuatia na mabadiliko. Alibadili nywila alizokuwa anatumia kufungulia. Na kila programu aliiwekea nywila pia, ili mtu asiwe ingia ovyoovyo pasipo ridhaa yake.
Baada ya hapo alimpigia simu Upendo. Lakini hazikupokelewa. Mara zote alizopiga. Hali iliyomfanya ajisikie vibaya mno, na uonaji wa upotevu wa mahusianao waliyonayo. Mambo kuharibika, ndicho kitu pekee kilichotawala akilini kwa wakati huo. Aliona kwa lolote atalofanya, hatoweza samehewa, ila hakulazimika kukata tamaa. Ilibidi apambane kwanza, ashuhudie mwisho utakuwa vipi afuate matokeo yatayojitokeza. Alijitahidi sana kupiga. Simu ziliishia kukata ama kukatwa. Pale zikatwapo hufuatia na ujumbe mfupi, uliosomeka ‘siwezi zungumza’ kauli iliyotonesha jeraha moyoni. Mchana kutwa. Upendo hakupokea katu simu za Vumilia. Ila alipotumiwa ujumbe, baadhi alijibu zingine hakuzijibu. Ila Vumilia alivumilia yote. Kama jina lake linavyojieleza, afanikiwe kupata anachohitaji. Jumbe nyingi zenye kuomba radhi, na zilizojaa bembelezo zilitumwa kama mvua. Muathirika, Upendo! Aliwazike nazo, na kushawishika kuurudisha moyo nyuma, wasamehane waendelee na kawaida ya awali. Lakini hakuna kilichosaidia. Mambo yalizidi kugonga mwamba, kwani Upendo hakuonesha ushirikiano wa aina yoyote.
Dhahiri! Alikasirika. Kilichomkasirisha, si picha alizotumiwa kwa madai yake. Alidai picha zake zinawezwa tumwa mtandaoni pasi na mpangilio. Kauli ambayo kwa Vumilia aliiona haina mashiko ya kumfanya akasirike. Yamkini kwa mhusika mwenyewe ni kweli. Ila upande wa pili. Aliitoa, afiche umizo la utambuzi alilobainishiwa kuwa Vumilia ana mwanamke mwingine. Usiku wa saa saba, ndipo alikuja pokea simu. Na kupata nafasi ya kuzungumza muda mwingi. Ilikuwa ni faraja kwa Vumilia. Nafasi adhimu simu yake kupokelewa. Toka mchana wa siku iliyopita. Fuadi na mwili kwa ujumla vilisisimka. Chungu ikapatikana maongezini.
“Mimi nishakusamehe toka muda mrefu. Ila siwezi kuruhusu mazoea tuliyopata kuwanayo mwanzo. Mazoea tuyapunguze,” alisema Upendo.
“Kwanini?”
“Fahamu hivyo. Kwa sasa haina haja ya kuzoeana kama ilivyokuwa nyuma. Tusitishe mazoea. Kama huitaji basi, ila huo niliokuambia ndiyo msimamo wangu.”
Vumilia hakukubaliana naye. Alimng’ang’ania na kumbembeleza abadili uamuzi alioufikia. Lakini hoja yake haikuthaminika, ilipuuzwa na kutupiwa mbali.
“Hivi huelewi? Ama wewe ni mchawi? Niongee lugha gani unielewe?” aliuliza Upendo, kwa sauti ya ukali, kuonesha hakubaliani na muendelezo wa mjadala.
“Sawa. Usiku mwema. Naomba uniwie radhi kwa kukukwaza kwa mara ya pili,” alisema Vumilia. Sauti ikiwa imejaa unyonge. Uliokaribisha hamu ya kilio. Ila alijikaza, sababu tu, ni mwanaume. Dalili za wazi zilishajiachia, kutoa machozi.
Simu ikakatwa!
Kilichofuata ni fikra, kwa wote. Ila Vumilia alionekana kuzidi. Na kikubwa alichowaza, ni hitajio alilopanga kufika tamati. Japo kuna msemo hunenwa, kwenye faraja lazima upitie vingi vitimbi, kwake msemo huo aliuona hauna maana. Kwani vitimbi alivyofikia, si vya kumpeleka kwenye faraja, bali kwenye zaidi ya umizo. Alikuwa anampenda sana Upendo. Lakini sasa mambo yashabadilika. Hivyo upendo alionao kwa kiasi kikubwa uligeuka kuwa umizo. Kila afiriapo neno mchawi humuongezea maumivu. Hadi ilifikia hatua ya kutoa machozi kudhihirisha namna alivyoumizwa na msemo huo.
“Dah! Leo hii nimekuwa mchawi. Nashukuru sana,” alijisemeza kimoyomoyo. Akiwa kajipumzisha kitandani. Michirizi ya machozi, ilionekana kushu
Furaha yote aliyonayo ilipotea. Ni umizo pekee, ndiyo lilitamalaki na kuchukua nafasi kubwa akilini. Hali iliyochangia, ushukaji wa utendaji wake katika baadhi ya mambo. Aligeuka mgumu wa kufanya karibia vitu vyote. Kufua, kupika hata mazoezi nayo aliyokuwa anafanya kikosini kwao kwa baadhi ya siku aliacha kuhudhuria. Mawasiliano nayo yalisita. Hakumpigia tena Upendo simu. Kwani hakuiona tena thamani yake, kama ashaanza ambiwa maneno ya ovyo. Muda mwingi akawa anashinda mpweke. Akiwa mwenye mawazo tele yaliyouchoma moyo wake. Ni siku mojamoja tu, ambayo kidogo alionekana kukaramka. Hasa awapo na Zamzam. Kwani, hakuhitaji unyonge wake, utambuliwe na wengine. Hata kama ana ukaribu nao kwa sana.
Taratibu chuki nayo ilianza jijenga. Chuki iliyofichika, kwa maneno matamu aliyokesha kutamka. Msichana yeyote sasa alimuona kama sumu. Na hakuupa moyo uruhusu nafasi ya mazoea ya kina kwa msichana mwingine kama ilivyokuwa kwa Upendo. Hata hamu, ya kuketi nao, apige stori, hakuwanayo. Kwani akiketi nao tu, hisia za kuwa yupo na Upendo ziliteka akili yake, na kuona msichana aliyesimama mbele yake hana utofauti na yule aliyemthamini mwishowe kumtamkia maneno yenye udhia. Hakika! Ilimuuma sana.
Baadaye sana, baada ya kuombwa radhi nyingi, na unafuu wa maumivu kupungua. Alirudisha upya moyo wake kwa Upendo. Ila utofauti haukukosekana. Awamu hii mazoea yalipungua, hayakuwa kama yale ya awali. Waliyokesha siku zote kuzungumza usiku kucha. Katika awamu hiyo, ndipo mmoja wa rafiki wa Upendo, Mwanjaa, anayefahamiana na Vumilia alijitokeza kusuluhu, mambo yawe kama yalivyo kawaida. Kipindi cha nyuma.
“Vumi!”
“Naam.”
“Unafahamu kuwa mahusiano ya kweli lazima yaanzie mbali? Yawe na nyingi changamoto na mambo mengine?”
“Nafahamu hilo.”
“Kama unafahamu, ni vyema. Na nashukuru. Hivyo jaribu kusahau yote, murudi mwanzo ili mufikie hatua nyingine. Leo mnaanzia hapa, kesho mnafikia hatua ya kutambulishana kwa ndugu. Nakuomba kaka yangu, msamehe, mambo yapate kuendelea.”
“Mimi sina shida. Niko kawaida, na nishasamehe.”
“Ni vyema. Chunga kauli, usimwambie maneno mabaya, ili mukeshe kuwa na mahusiano mazuri muda wote.”
“Haya ahsante.”
Awamu mpya ilianza. Kwa furaha, msisimko na kila lenye heri katika maisha. Mawasiliano ya usiku wa manane, siku mojamoja nayo yalijirudi, mfarakano ukasahaulika. Ili wapate kufikia hatua iliyo njema zaidi ya ile waliyonayo. Kila mmoja kwa imani yake, aliamini ipo siku watafika sehemu nzuri, iliyojaa baraka, furaha na kila jema lililohalalishwa na Mwenyezi Mungu. Naam! Mambo yalikuwa motomoto. Kama waanza leo, ilhali walishakuwa na mahusiano kwa muda mrefu uliopita. Hali hiyo iliinua hisia zaidi kwa Vumilia, na wazo la kuthubutu kuweka ukweli wazi asiendelee kuteseka na hisia alizonazo. Mahusiano ya kimapenzi!
Mnamo mwezi januari Upendo alibahatika kupata likizo. Baada ya kutumikia majukumu yake ya kazi kwa muda mrefu. Ilikuwa safari ya alfajiri, kwani alisafiri kwa ndege, toka jijini Dar es salaam hadi kwao mjini Katavi. Kwao aliwasili mapema sana. Ila kutokana na uchovu, alifikia kulala, na ilipowadia saa mbili asubuhi aliamka na kumtaarifu Vumilia. Hali fulani ilimvaa Vumilia. Kwamba hakutaarifiwa, kama anasafiri. Na siku aliyoondoka hakupatiwa taarifa yoyote. Wazo likamjaa, anadharauliwa. Ndiyo maana hajafanyiwa hicho kitu. Tena alivyokuja uliza, aliongezewa zaidi hisia zake.
“Vumi! Si nilishakutumia picha ya tiketi kukuonyesha kuwa nina safari?”
“Hapana! Labda pacha mwenzangu,” alisema. Moyo ukiwa umejaa machungu ya vile alivyofanyiwa.
“Mmmmh! Vumi. Ni wewe ndiye nilikutumia. Acha kuniongopea.”
“Kama ni hivyo sawa. Yawezekana nimegeuka kuwa huyo mtu mwingine.”
Hakika! Vumilia aliumizwa na hili. Kisha kujipatia nafasi ya utambuzi, kuwa yupo mtu, anayefananishwa naye, hivyo mambo mengi ya maana hufanyiwa huyo, yeye hana thamani tena. Kuna muda alidiriki kutoa machozi, akiwa pekee, kupunguza machungu yamuumizayo, moyo ubaki na amani. Ila amani ikawa haipatikani kirahisi. Ilikuwa bandu bandua. Likiisha hili lingine hujitokeza. Kabla machungu ya kutoambiwa taarifa za safari hazijaisha, tukio lingine lilijitokeza. Lililompatia maumivu zaidi ya mwanzo. Lililomfanya naye akiweza aweke bayana hisia zake. Isitokee mtu mwinginge akampiku. Jumbe zilizokosewa. Zilizokuwa zinataarifu mambo ya ndoa toka kwa Upendo, kwenda kwa kijana aliyefahamika kwa jina la Palango ndizo zilianzisha upya machungu yake. Jumbe zilimfikia, badala ya kwenda kwa mhusika. Zilimuumiza mno. Alivyoulizia kulikoni? Jibu alilopatiwa, halikuwa rafiki kwake.
Sababu alikuwa na mapendo naye, alivumilia, japo maumivu hayakumuisha. Yote kupalilia hisia zake zisipotee pasipo mhusika kufahamu. Pasi na kificho. Aibu, na hofu. Alimfikishia Upendo ujumbe husika. Nia aliyonayo, ya wawili hao kuwa mwili mmoja katika maisha yao yote ya baadaye, hadi pale mmoja wao atapokumbwa na umauti. Vumilia alitiririka mashairi mazuri sana. Yenye kuleta ushawishi na kuufurahisha moyo wa Upendo, akiamini mambo yatakaa sawa. Halikuwa tukio la kitoto, lilikuwa gumu, kwa kila mmoja kuvutia ngoma upande wake. Kama wadaivyo waswahili. Mwamba ngoma huvutia upande wake.
“Vumi! Ni sawa. Nami nakupenda. Ila tatizo ni dini zetu. Sitaki kukuumiza mbeleni.”
“Dini inahusiana vipi katika mahusiano kwa mtu uliye na mapendo naye?”
“Nafahamu wazazi na ndugu zangu walivyo. Hawatoafikiana nami. Hivyo kabla mambo hayajaharibika huko mbele, ni heri tujiepushe nayo sasa.”
“Mmmmmh!”
“Mbona waguna?”
“Hapana! Kawaida.”
“Vumi! Kawaida ipi? Kwani sikufahamu hadi uniambie hivyo? Naomba usijisikie vibaya. Nielewe. Japo rafiki zangu wengi na Madam cecy mara nyingi tu, washaniambia mimi nawe tuwe wamoja, ila tatizo linakuja hapo nilipokuambia. Unahisi nifanye vipi? Ili hilo unalohitaji lifanikiwe? Isitoshe nilijiwekeaga kiapo, sihitaji kuolewa na mtu anayehusiana na mambo ya ulinzi, ukizingatia nami niko sehemu hiyo.”
“Hamna shida. Kama nimekuelewa, poa, na kama sijakuelewa poa. Acha nibaki na unyonge wangu. Wenye nguvu wafaidi.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa hayo maneno yanatoka wapi?” Aliuliza Upendo lakini hakujibiwa. Vumilia akakata simu.
Jibu halikuwa jema kwake. Alikataliwa, japo alitumiwa mzunguko mkubwa sana wa kulainishwa. Juu ya kulainishwa huko, hakukusaidia kwa upande wake. Alijisikia vibaya, furaha na moyo uliojaa matumaini kwamba anaenda kuingia kwenye mahusiano na msichana huyo ukafutika. Wakati ulibadilika. Maumivu alianza ugulia. Katika kuitafuta njia yenye faraja. Ambayo sasa aliiamini ndiyo sahihi kwake. Ilifikia wakati, awapo nyumbani alikesha kuangusha kilio, cha kimyakimya majirani zake wasisikie, kutoa maumivu na machungu aliyojisikia. Kila akumbukapo wema na yote amtendeayo, hali hiyo haikukosa kumkumba. Kwamba amefanya mengi kwake, naye kufanyiwa, katika hayo mengine yenye ujazo mkubwa wa kimahusiano ya mapenzi. Iweje leo kamtamkia halafu kamtolea nje?
Kila alivyojiuliza, hakupata jibu muafaka. Nini maana ya Upendo. Kuna muda mwingine alihisi kuwa anapimwa imani aliyonayo juu ya hicho alichotamka. Imani hii haikudumu sana moyoni mwake. Hasa kila alipobembeleza kwa siku zilizoendelea jibu lilibaki lilelile alilotamkiwa awali.
“Vumi! Lakini kwanini hukuniambia toka mwanzo? Ni muda gani umepita halafu leo hii unanitamkia maneno haya?”
“Ningelikutamkia hiyo mwanzo ungelinielewa?”
“Inategemea. Hebu angalia sasa tulivyo na mazoea ya kutosha. Halafu unaniambia tuhamishie hatua nyingine. Hiihii tuliyonayo inatosha. Hiyo unayohitaji mimi sitoweza, kwa sababu za awali nilizokuambia.”
“Aaah! Poa. Nami nitajua maamuzi yangu ni yapi.”
Mambo yalibadilika. Upendo alihitaji mahusiano waliyonayo yabaki yalivyo. Vumilia alihitaji yapige hatua mbele. Wawe wachumba! Mfarakano upya ukaibuka. Baina yao, Vumilia akiwa kwenye maumivu makali, yaliyomsukuma kutoa maneno yoyote yaliyojazana hisiani kuhusu Upendo pale wawasilianapo. Alifanya hivyo, kuamini atabaki mtulivu, mawazo umizo yataisha, faraja itateka moyo. Maneno aliyotoa hayakuwa mazuri. Hakika! Si mazuri, kwa mtu ambaye una lengo na matarajio fulani. Ila Vumilia hakujalisha hilo tena. Yeye alitamka tu, lolote litalotokea litokee. Hakutambua, akifanyacho kinajenga umizo upande wa pili. Kwa Upendo.
“Sasa Vumilia mbona nashindwa kukuelewa? Kama unahitaji mimi nawe tuwe wamoja ni maneno gani hayo hunitamkia? Nashindwa hata kuyaamini maneno yako. Ukoje siku hizi?” aliuliza Upendo, siku moja pindi wakiwasiliana na Vumilia kwa njia ya simu. Baada ya kutamkiwa maneno mengi yaliyompatia udhia.
“Kile nilichokuambia kitabaki palepale, na haya ya sasa ni sehemu tu ya hisia zangu, zilizojaa machungu.”
Amani ilikosekana. Hakuna siku ilibahatika kupita pasipo kuingia kwenye mgogoro. Uliosababishwa na hisia za Vumilia zilizomtuma kuhisi mambo yasiyo sahihi wakati mwingine. Mambo yalivyokuwa magumu zaidi, Vumilia hakusita kuwaarika wengine, wapate kuwa sehemu ya msaada kwake. Hasa Mwanjaa. Alimueleza kila kitu. Hali jinsi ilivyo na matarajio ya msaada anaouhitaji. Mwanjaa naye kutekeleza hilo, ijapokuwa jibu halikubadilika naye alivyofikisha ujumbe. Hivyo kufanya umizo kuwa endelevu.
“Hamna namna nyingine, zaidi ya kukata mawasiliano naye ili nisipate kuumia zaidi,” aliwaza Vumilia.
Kweli! Kuanzia siku iliyofuata alifuta namba ya Upendo, na kumtaarifu alilohitaji. Naye afute namba yake. Kauli iliyokataliwa vikali.
“Vumi, siwezi nikafuta namba yako. Nitabaki nayo, kama yangu umefuta si vibaya, na hongera kwa hilo. Ukihitaji nisiwasiliane nawe, badili namba, na nina hakika hata ukibadili nitaipata tu.”
“Mmmmmh! Sawa. Ila nikuombe tu, fanya kama nilivyokuambia. Sihitaji mawasiliano nawe kwa sasa.”
“Kwanini hutaki?”
“Kwa kipi utachonishawishi kwa sasa nikiendelea kuongea nawe? Kama sio kujiongezea maumivu.”
“Kilichokufanya mwanzo uongee na mimi ni nini?”
“Bhana eeh! Usiniulize maswali mengi,” alisema Vumilia na kukata simu.
Japo ni kwa maumivu, lakini Vumilia alitii takwa lake. Alikata mawasiliano kabisa na Upendo. Ijapokuwa Upendo hakuisha kuomba radhi na kumtaka Vumilia warudi kama ilivyokuwa mwanzo. Kwa siku walizokesha kuzungumza maongezi yao yalihusu hii mada pekee. Hakukuwa na nyongeza yoyote, ya kuwafanya wabadilishe. Upendo aliomba radhi, Vumilia alizidi kukataa. Hali iliyochangiwa toka kipindi hicho. Akikosewa husamehe, lakini harejeshi mahusiano jinsi yalivyokuwa kipindi cha nyuma. Vumilia alibaki kwenye huu msimamo wake. Kamwe hakuruhusu mtu kuuharibu kwa ushawishi wa aina yoyote.
Ilibaki kuwa mapisi baina ya hawa wawili. Kwani kila jitihada iliyofanywa na Upendo iligonga mwamba. Vumilia hakuafikiana nayo. Alibaki kwenye msimamo wake. Katika kuelekea safari hiyo ya masahauliano, Vumilia alianzisha muendelezo wa njia nyingine ile iliyokuwa haithamini na kuijali. Zamzam! Na ndiyo mbadala, aliouamini utaenda tuliza moyo wake. Kwa kumsahaulisha yale yote yaliyojiri baina yake na Upendo. Upendo hakuwa na nafasi tena, ilifikia mahali, katika kuonyesha hathaminiwi, akipiga simu haipokelewi ama hukatwa kabisa. Alifanya hivyo kukuza mahusiano aliyonayo kwa sasa yaimarike zaidi. Asimuumize tena binti, aliyejitoa kwa moyo wake mmoja. Akashindwa muelewa kwa hapo nyuma. Mapenzi yaliiva. Yale aliyokuwa anakesha kuyaonesha kwa Upendo akayahamishia huku, mambo yote, hakubakisha hata chembe, ambayo ingeweza rudisha mahusiano.
****
Upendo wa kweli hauji kwa kulazimisha. Hujitokeza kwa msukumo halisia wa kweli wa hisia hupatikanao moyoni. Na huu ndiyo upendo wenye nguvu, amani na faraja ya kweli inayotakikana. Upendo huu hauna migogoro, japo wivu haukosekani. Hufanya nyumba kuwa tulivu, hudumishiwa ubarikio na mambo mengine kemkem yaliyo na heri. Hivyo mahusiano yalivyojirudi, baina ya Vumilia na Zamzam yalisheheni mambo haya. Yalikuwa kama yanaanza. Zamzam alithaminiwa na kujaliwa haswa. Katika kuhakikishiwa hilo, aliandaliwa taratibu za kudumu, zitazowafanya wawe wamoja milele. Wafunge pingu za maisha. Kila mmoja aliuarifu upande wa wazazi wake. Mahusiano waliyonayo na hatua wanayoenda ichukua. Wakakubaliwa.
Wazazi wa Vumilia waliridhia mapema mno, japo kwa wakati huo walikwishatengana. Hali iliyomfurahisha Vumilia na mpenziye. Zamzam. Ambaye alikuwa na hofu ya kukataliwa. Taratibu zingine zilifuata. Kupeleka posa. Mapema tu, baada ya kupata dondoo za huku na kule, Vumilia aliandika barua ya posa, kisha kukabidhiwa mshenga. Apeleke nyumbani kwa kina Zamzam. Kufikia tu, kwa hatua hiyo mahusiano, yalizidi kunoga. Kila mmoja hakuambilika, juu ya mwenziye. Mithili ya wapenzi wapya. Kutokana na uwingi wa shughuli, mshenga alikawiza, kwa siku kadhaa kutopeleka ile barua. Siku nne baadaye ndipo alianza fanya taratibu za kuelekea kwa wazazi wa Zamzam. Mjini Kondoa. Siku hiyo Vumilia alikuwa kazini. Asubuhi, majira ya saa tatu. Akili ikiwazua safari ya mshenga wake itakuaje. Jambo lililomfanya anyongeke kwa muda fulani. Kuhusu namna barua itavyopokelewa na majibu yapatikanayo.
Akiwa katika hali hiyo, ghafla! Alishtushwa na muito wa simu yake, ulioashiria kuna mtu anapiga simu. Haraka sana aliingiza moja ya mkono wake katika mfuko ambao simu ipo, aliitoa na kuangaza jina la mpigaji, alikumbana na jina la baba yake. Mzee Matatizo! Hakuchelea! Alibonyeza kitufe cha kupokelea na kuweka sikioni. Sauti ya mzee wake ikaanza jinasibu na kusikika barabara kwa kuanza na salamu.
“Habari?”
“Salama baba, shikamoo.”
“Marhaba! Vipi ulishaandika hiyo barua?”
“Hapana. Vipi?” Vumilia aliongopa.
“Bhana eeh! Kama hujaandika, nakuomba uachane na hilo wazo. Maana mwenzio nimefikiriaaa, nimeona wanawake wa huko si wazuri, tabia zao mbaya. Bora uje uchukue hukuhuku nyumbani.”
Aliongezwa mshtuko, kikafuatia kimya cha dakika kadhaa ndipo Vumilia aliijibu hoja ya baba yake.
“Huyu msichana niliyemhitaji yuko vizuri. Hana tabia hizo unazozihisi.”
“Baba! Hao wanawake wa mbali hao, mkifanikiwa tu, wanaanza mambo ya ovyo. Mara kuwaondoa waume zao duniani, mara hivi na vingine vingi vya ajabu. Hivyo nakuomba uachane naye.”
“Lakini baba, kuhusu tabia hilo ni jambo binafsi. Kwani hata wasichana wa huko kwetu wapo wenye tabia kama hizo.”
“Usiwe mbishi. Mimi nimejionea kwa Mjomba yangu Mzee Ishara, alifanyiwa hayo mambo, akaokolewa na polisi. Sitaki uangamie mwanangu, chondechonde nakuomba. Hata kama mumeahidiana na kusaidiana mambo mengi na huyo msichana muache,” ilisika sauti ya Mzee Matatizo kwa msisitizo.
“Nitafikiria!” alisema James kisha akakata simu.
Maongezi hayo yalizidisha mawazo na unyonge kwa Vumilia. Kwani yalimfanya afikirie kwa kina kauli za mzee wake na matendo aliyonayo Zamzam, ambaye kwa sasa washashibana. Umakini kwenye kazi ulipotea. Tena ilivyo mbaya alikuwa benki, iliyo nje kidogo na mji wao. Hivyo endapo watu wabaya wangejitokeza kufanya uhalifu, asingemudu mapigano. Pale alipoona mambo yamemzidia, aliwapigia watu wake wa karibu. Hasa jamaa. Mama akiwa mmoja wao na kuwaeleza mkasa mzima. Marafiki hawakukosa. Aliwahadithia, nao kumpatia ushauri kwa mitazamo waliyonayo. Wapo, wachache waliungana na mtazamo wa baba yake, ila walio wengi walimshauri achukue maamuzi yamfaayo mwenyewe sababu huyo mwanamke yeye ndiye anaenda kuishi naye. Mama yake akiwa mmoja wao. Hakika! Njia panda haikumkosa. Maamuzi gani ayafikie, ila sehemu kubwa ya moyo wake ulimhitaji aendelee kuwa naye.
“Lolote litakalojitokeza litokee. Kamwe siwezi mwacha Zamzam. Ni wanawake wachache sana wana tabia kama zake,” alijisemea Vumilia kimoyomoyo.
Alijiapiza kuendelea na imani yake. Japo aliamini kufanya hivyo, kunapelekea sintofahamu na maelewano hafifu na baba yake. Mzee Matatizo. Ila hakujalisha hilo, alichoangalia ni matakwa ya hisia zake yakoje. Kwa ushujaa, hata Zamzam hakudiriki mwambia. Na baadhi ya watu pia walimshauri hivyo, ili asimfanye msichana huyo kujisikia vibaya, na kupoteza furaha yote aliyonayo. Ambayo ingelichangia kutafuta mwanaume mwingine ilhali mapendo ya Vumilia kwake sasa yalikuwa motomoto. Angelimuumiza Vumilia! Kwa ubishi, pasi na mafikirio ya kina, hatimaye barua ilipelekwa. Mshenga alifunga safari toka mjini Dodoma hadi Kondoa, kisha kutekeleza jukumu lake kwa ufasaha. Wazazi wa Zamzam waliipokea, waliijadili na kuahidi kutolea jibu siku za baadaye. Hilo halikuwa shida, mshenga aliridhia, kisha alirejea mjini Dodoma kutoa jibu kwa mhusika.
Vumilia alivyoelezwa, alifurahi. Kufikia tu hatua hiyo aliamini mambo yanaenda vizuri, na lazima Zamzam awe ndani ya himaya yake. Alijipa subira, kama walivyoombwa na wazazi wa Zamzam, kusubiri siku teule itayorejeshwa jibu. Kila hatua iliyofanyika hakusita mtaarifu mama yake. Na baadhi ya ndugu ili nao wafahamu kiendeleacho. Kwani baba walishakosa maelewano kuhusiana na hilo. Siku kadhaa baadaye jibu lilirejeshwa. Kuwa mambo yako vizuri, hivyo afanye maandalizi ya hatua nyingine. Kupeleka mahari na utambulisho wake kwa wazazi na ndugu wa Zamzam. Katika kuelekea hiyo siku, mshawasha hukukatika. Ndugu wa Zamzam walijawa na hamu kwa wingi. Ndugu yao afikie hatua ya heri na iliyobarikiwa. Kila leo hawakusita ulizia, hali iliyoinua fikra ziwe pevu kwa Vumilia namna ya kufanikisha hilo.
Kwa dhati na nia moja. Aliridhia kupingana vikali na mawazo ya baba yake. Zamzam alikuwa chaguo la moyo wake. Kumuacha ni ngumu. Na kwa misingi ipi? Ilhali msichana huyo ana sifa kemkem zenye kuvutia mwanaume yeyote anayehitaji mke. Mipango ya kupeleka mahari ikaanza ratibiwa kila leo. Ilipokamilika, alifunga safari na mshenga wake wakati huo Zamzam alikwishatangulia kwao siku nyingi zilizopita. Safari ilianza mapema sana. Saa 12 asubuhi, na kwa kujiiba, kwani hakuwa na ruhusa ya kusafiri toka kituo chake cha kazi. Hivyo ilichangia muda wote aombe na kufikiria usalama wake utakuwa vipi. Alikesha kuomba, awasili na kurudi salama. Pia, hakuacha kuwazua namna zoezi hilo litavyofanyika. Potezea ya mawazo yake, ilikuwa pale tu, aliposemeshwa na mtu, hasa mshenga ama alivyokuwa anawasiliana na mtu kwa njia ya simu. Hadi walivyowasili mjini Kondoa, walikuwa hivyo. Hakuna kilichobadilika. Walivyowasili kituo cha mabasi, cha mji huo, punde baada ya kuteremka garini walipokelewa na mmoja wa ndugu wa Zamzam. Kisha kuongozana naye hadi sehemu husika ambapo tukio litafanyika. Nyumbani kwa baba wa Zamzam.
Walianza na utambulisho, baada ya kupita salamu kisha maongezi husika yalianza dakika kadhaa baadaye. Ambapo mshenga. Aliyejaa mbwembwe na mingi mikogo alijinasibu kwa uzuri juu ya kile kilichowaleta. Maongezi yalikuwa mazuri. Yalipendeza na kustawisha hali iliyofanya kila mtu awe mwingi wa tabasamu muda wote. Pale palipohitajika Zamzam kuchangia hoja, aliitwa. Alivyothibitisha alirudi alipoketi kisha waliendelea. Ngwe ya kwanza iliishia saa saba mchana. Baada ya hapo walipata chakula kisha kuendelea. Awamu hii ilikuwa nafasi ya kukabidhi mahari, na kukubaliana tarehe adhimu ya kuruhusu sherehe ya ndoa kufanyika. Hivyo, walivyorudi tukioni, chap! Mshenga alianza upya mada kuhusu mahari, michango mingine ya kukirimu na mwezi pendwa wa tukio la ndoa. Ila isivyo bahati, baadhi yalikubaliwa pasi na pingamizi la aina yoyote. Suala la muda wa ndoa ukawa shida. Mmoja wa ndugu, hakuafiki muda pangwa toka kwa kina Vumilia. Hapa waliweka kituo, kujadili kwa kina. Takribani nusu saa, ndipo walifikia muafaka. Vumilia aliridhia, ndoa ipite siku hiyohiyo. Yote kutokana na ufinyu wa muda ambao alipangiwa, kwamba endapo ndoa haitofungwa kwa siku hiyo, basi arejee siku kadhaa mbeleni, hasa wiki ama wiki mbili aje kupitisha tukio hilo. Kitu kilichokuwa kigumu kwake. Hivyo ikamlazimu kuridhia, ndoa ipite. Kisha mambo ya sherehe na mengineyo yatafutiwe siku nyingine.
Alimtaarifu Mama yake, naye aliridhia. Alitafutwa Sheikh na baadhi ya watu wengi kushuhudia baada ya hapo ndoa ilifungwa. Jioni, ya saa kumi na moja walianza safari ya kurudi. Kwa gari za kuungaunga. Hiace! Zilizowachukua muda mwingi hadi wanafanikiwa kuwasili mjini Dodoma. Saa tatu usiku. Kwani zilikuwa zinasimama simama sana na muda mrefu. Walivyoteremka garini, kila mmoja alielekea makwao, baada ya maagano. Vumilia, alivyofika tu nyumbani kwake, alifikia kulala. Kutokana na uchovu wa safari. Hata siku iliyofuata alishindwa kuhudhuria mazoezini asubuhi. Rasmi, sasa alikuwa ndani ya ndoa. Furaha iliyoje ilisheheni moyoni mwake. Zamzam ndiyo usipime. Alikuwa mwenye furaha zaidi yake. Maisha ya pamoja yalianza. Zamzam alivyohamishia vitu vyake nyumbani kwa Vumilia. Maisha ya ndoa. Katika safari ya kutengeneza familia kubwa.
Yote, alifanya pasipo mtaarifu baba yake. Kwa kuwa na utofauti wa maelewano kuhusu jambo hilo. Hakuwa radhi kusikia la mtu kuhusu kutengana na Zamzam kwa muda huo. Kwani alikwishaingia kwa kina moyoni mwake. Taarifa kuhusiana na tukio hilo, baba yake alizisikia toka kwa watu wengine. Ndugu wa karibu, wa Vumilia kwa upande wa mama. Kitendo kilichomzidishia aongeze uhitaji wa kupinga tendo hilo. Kiasi kwamba ilifikia hatua kuhusisha kitendo hicho na imani potofu. Ushirikina!
“Sio bure! Nakwambia sio bure. Huyo mwanamke itakuwa kamroga tu Vumilia. Maana hawezi ng’ang’ania aendelee kuwa naye wakati nishamuambia aje atafute mwanamke huku,” alisema Mzee Matatizo, pindi akiongea na mama mkubwa wa Vumilia.
“Hupaswi kusema hivyo. Kama wamependana utalazimisha vipi waachane? Na hizo tabia unazozisema si huko tu. Hata huku kwetu kuna wanawake wana tabia mbaya. Muache tu, kikubwa mhusie asisahau nyumbani,” alisema mama yake mkubwa na Vumilia.
“Haiwezekani! Hii si kawaida kabisa,” aliendelea kusema Mzee Matatizo.
Mzee Matatizo, hakuwa na imani kabisa, na hakuwa tayari kuona Vumilia akioa msichana wa mbali na mji wao. Mawazo ya watu wengine waliomshauri kuwa amwache afanye alivyoamua aliyaona si sahihi kabisa kwake. Aliamini kile ahisicho kipo sahihi, hata kama kilishatokea miaka mingi iliyopita. Hivyo aliamini mwanaye anapotea, tena anapotezwa na msichana aliyemuoa. Zamzam!
Vumilia naye aliendelea kusikia kila lililoendelea toka kwa baba yake kupitia kwa nduguze, mama yake wa kufikia na mzazi. Pasi na sahau rafiki waliokuwa wanafuatwa na Mzee Matatizo kuwaeleza linaloendelea kufanywa naye. Kila alivyosikia aliishia kupotezea. Kumpoteza Zamzam ilikuwa ngumu. Na kwa namna yoyote hakuwa tayari kufanya hivyo. Kwani akili yake ilimuaminisha huyo ndiyo msichana wa pekee wa maisha yake. Wanaendana! Pindi Mzee Matatizo anaendelea kutoa ushauri kwa jamaa, wasaidizane kumshauri Vumilia asioe msichana wa mbali, jamaa haohao, hugeuka na kumpatia ushauri mwingine Vumilia. Wa kumtaka asiwe msahaulifu. Ushauri ulipokelewa naye kwa mikono miwili.
“Ondoeni shaka. Napakumbuka nyumbani, ndiyo maana mambo yangu nimeanza yafanya huko. Huku sina kitu chochote, nilichojiwekezea,” ilikuwa kauli ya Vumilia kila alipoaswa.
Yote yaliyoendelea katu, hakudiriki mtaarifu Zamzam. Kufanya hivyo ingepunguza nguvu ya upendo. Alibaki nayo moyoni, pale alipoulizwa habari za baba kuhusu matukio yao ya kila uchao, hakuisha mpatia sababu za hapa na pale za kumtuliza asiwe na shaka. Akawa anatumia mgongo wa mama, kumuaminisha kuwa wazazi wote wapo sawa katika mambo yao wanayoendelea nayo. Siku zilizidi katika, na kuendelea kuwa hivyo. Hakuacha! Alizidi songa mbele. Tena kwa kuweka mikakati mingi pamoja itayowafikisha sehemu nzuri kimaisha. Maisha yaliyo bora na si ilimradi maisha.
****
Sintofahamu! Iliibuka kwa Upendo. Kutoamini, kama ashapoteza mawasiliano ya nguvu aliyonayo baina yake na Vumilia. Kila atafakaripo, ilikuwa ngumu kupata suluhisho. Nini afanye? Ili arejeshe hali ya awali na maswali mengi hayakumuisha kila uchao. Japo alifahamu kukataa hitajio la Vumilia kuwa pamoja ndiyo chanzo. Hivyo muda mwingi akawa mtu wa mawazo, sababu ni Vumilia. Na njia ipi ya kutumia arudishe mahusiano yao waliyopata kuwa nayo awali. Rafiki zake, waliokuwa wanafahamu hali waliyonayo, walivyomuona yuko katika hali hiyo, hawakusita kumuuliza. Ila hakutaka kuwaweka bayana, aliwaongopea, hasa Mwanjaa na Madam Cecy.
“Mbona sikuoni ukiongea na Vumilia siku hizi?” aliuliza Madam Cecy siku moja pindi wakiwa wameketi bwenini kwa Upendo wakiteta jambo.
“Yuko bize sana siku hizi. Hivyo kaniambia tupunguze mawasiliano kwa muda,” alijibu Upendo.
Kila alivyoulizwa, hilo ndilo jibu pekee alilowapatia waulizaji. Alikufa na tai shingoni, kutowaeleza sababu halisi. Isipokuwa Mwanjaa, ambaye alikuwa na mawasiliano kila baada ya muda fulani na Vumilia. Hivyo alifahamu sababu na kufanya majaribio ya kuwarudisha pamoja ila ilishindikana. Kwani Vumilia alikataa, katakata! Upendo alikuwa na wakati mgumu. Vumilia ndiyo sababu. Kwani hakuisha kwenye kumbukumbu zake. Si kama hakuwa na matamanio ya kuwasiliana naye, alikuwanayo! Ila anaanzaje? Maana kila afikiriapo hukosa namna ya kuanza kuwasiliana naye, kisa, baadhi ya kauli alizopatiwa na Vumilia juu ya hali ajisikiayo siku za nyuma.
“Upendo! Sina furaha yoyote niongeavyo na wewe. Ni maumivu pekee ndiyo yajaayo moyoni mwangu...yaani!”
“Kwanini unasema hivyo? Kwani mwanzo kipi kilichokuwa kinakupa furaha toka kwangu?”
“Kwa sasa huwezi nishawashi kwa lolote. Fahamu hivyo.”
Ilikuwa ni sehemu ya kumbukumbu kwa Upendo. Kukumbuka kauli za Vumilia alizokwishawahi ambiwaga. Zilizomkatisha tamaa ya uhitaji wa kuwasiliana naye japo alikuwa na mengi matamanio. Siku mojamoja alikata shauri, akawa anampigia, moyo wake ukiwa tayari kwa maandalizi ya kauli zozote atazopatiwa ilimradi aisikie tu sauti yake moyo uridhike. Mambo yalikuwa hivyo. Pale alipo na uhitaji wa kuwasiliana na Vumilia alijitahidi kuwasiliana naye lakini siku nyingine, alipiga kimya kutokana na kauli apatiwazo. Zilizojaa kero upande wake.
Walivyobahatika kuwasiliana, Vumilia hakumtaarifu kuwa tayari kashaoa. Walikuwa wanaongea mambo mengine tu, na kwa muda mfupi sana. Kwani, itokeapo wanazungumza kwa muda mrefu kuna hisia fulani zilikuwa zinajazana moyoni mwa Vumilia, zilizokuwa zinamkumbusha mambo waliyofanya nyuma na namna alivyokatiliwa. Jambo lililomfanya kuzidisha machungu na hasira, imsukumayo kutamka maneno ya ovyo. Nafuu yake, ilikuwa kuongea kwa muda mfupi. La sivyo, hali huchafuka. Vumilia alikuwa na maumivu mazito juu ya Upendo. Kukataliwa hitajio lake ndiyo chanzo. Kuishinda hiyo hali ikawa ngumu, akizungumza naye. Ili aweze kuimudu ni lazima apoteze mawasiliano naye. Ijapokuwa naye kuna baadhi ya siku, mara moja kwa mwezi, ama baada ya wiki mbili, alikuwa anampigia kumtakia hali. Siku zilizidi songa, hali iliendelea kuwa hivyo. Huku Upendo akijidhatiti na mikakati mingi kuhakikisha hapotezi mahusiano aliyopata kuwa nayo na Vumilia awali, na ikibidi azidishe. Yaani, kwa sasa alikuwa rasmi kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na Vumilia. Wapate kufikia ile hatua aliyopata ambiwaga awali akaikana. Wanafamilia! Habari za dini aliziweka kando. Ndugu watamchukulia vipi, pia aliweka pembeni. Alitanguliza hisia kisha kufuatia hayo mengine.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kumbukumbu ya matendo. Nini alichokuwa anafanyiwa, ndicho kilichomfungua sasa kuwa radhi. Ijapokuwa hata kipindi cha nyuma alikuwa radhi, ila hakutanguliza hisia, alitanguliza mapendo ya ndugu watamuonaje, endapo akiwa na mahusiano na muislamu. Hilo sasa aliliona halina maana, katika harakati na hatua za kumtafuta mwenza. Kikubwa ni mapendo. Aliligundua, baada ya pale alipoona kwake ni sehemu sahihi, kwa matakwa ya ndugu na dini kuachwa solembwa. Alitoa mwili kwa nguvu zake zote, mwishowe, akili akiipa utambuzi, kuwa anaenda kuwa mama wa familia wa kijana huyo, mwishowe akaambulia kuachwa. Kwa kisingizio, kuwa hana hadhi ya kuishi na huyo kijana.
Alivyofanya tafakuri ya kina. Baada ya kwenda kwa kijana huyu, baadaye yule, na kote kupata matokeo yaliyolandana. Ndipo alipata utambuzi, Vumilia ndiyo mtu wake sahihi. Ila hakufahamu kama ashachelewa. Na kingine. Vumilia alikuwa na desturi, akishamtongoza mwanamke, akakataliwa, endapo mwanamke atajirudisha siku za kamwe hawezi mkubalia. Mtihani ulioko mbele yake ulikuwa mgumu. Kama yuko radhi kuwa na Vumilia, alipaswa, kuvunja ndoa, na kuipoteza imani hiyo iliyoenea kwa kirefu akilini mwake.
“Vumi! Sasa niko radhi kuwa mama wa familia yako, nawe uwe baba wa familia yangu. Acha kuniambia ambia maneno ya ovyo, yananiumiza,” alisema Upendo kimoyomoyo, jioni moja akiwa amepumzika kambini kwao.
Katika kuhakikisha, mpango huo unatimia, alianza kutekeleza mbinu zake. Za kumfikia Vumilia na kumlainisha ili arudi alivyokuwa awali. Jambo la kwanza aliloanza nalo, aliwashirikisha wenziye. Madam Cecy na Mwanjaa. Aliwaita bwenini kwake, na kuwaeleza kila kitu, kisha kuwaomba msaada, washirikiane katika jukumu hilo. Hawakusita, kumkubalia, ili asiendelee kuwa katika maumivu, ilhali yanatatulika. Mawasiliano na Vumilia yalianza. Kwa pamoja, kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano. Wote walikesha kushambulia, si usiku, si mchana. Ila simu nyingi za usiku zilikuwa hazipokelewi, na baadhi pia za mchana. Hasa Vumilia awapo na mkewe. Zamzam! Jambo lililowafanya wakutane tena washauriane.
“Anaweza kuwa na nini? Maana siku nyingine unaweza mpigia, anapokea na kukutaarifu nitafute baadaye. Baadaye ukimtafuta hapokei kabisa,” alisema Mwanjaa.
“Nami nashindwa kuelewa. Kabadilika sana siku hizi. Vumi, hakuwa hivi. Au sijui ana mwanamke? Ndiyo maana hapokeipokei,” Upendo naye alichangia hoja.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yawezekana! Maana kule whatsapp, nimeona kaweka picha ya mwanamke.”
“Kuhusu picha si tatizo. Inaweza kuwa hata ya ndugu yake. Tujaribu kufuatilia kwa rafiki zake, yumkini tutang’amua jambo.”
“Sahihi! Unawafahamu?”
“Ndiyo. Nawafahamu baadhi ya rafiki zake. Wengine wanaishi hapahapa jijini, wengine huko aliko. Ila hao ambao yuko nao sina mawasiliano nao.”
“Wa hapahapa?”
“Ninao.”
“Anza na hao wa hapa. Kisha tumia hawahawa, kupata namba za marafiki zake wa huko aliko. Ama mtumie mwenywe kupata namba zao. Umwongopee vyovyote vile,” alichangia Madam Cecy.
Kweli! Baada ya kikao hicho cha dharura kuhairisha, alianza wasiliana na rafiki wa Vumilia walioko Dar es salaam. Hasa Lupeto na mwingine aliyefahamika kwa jina la Shauri. Alianza mdodosa, afahamu Vumilia yupo katika hali gani, na mpango gani anaoendelea nao ambaye yeye anaufahamu.
“Siku za hivi sasa nampigia Vumilia hanipokelei simu yangu? Ana tatizo gani?” ndilo swali kubwa alilokuwa anawauliza, ili wao wafunguke yote wanayoyafahamu.
“Yupo, ila ana mambo mengi sana. Maana mke...” alisema Shauri, ila hakuweza malizia kauli yake. Baada ya kukumbuka jambo fulani... “nakuomba usimwambie Upendo kuwa nimeoa,” ilikuwa kauli aliyowahi ambiwa na Vumilia siku kadhaa zilizopita.
“Vipi, mbona kimya?” aliuliza Upendo.
“Aaah! Kuna kitu kimeniponyoka hapa na kuvunjika, ndicho kilichonifanya nishindwe malizia kauli yangu.”
“Mmmmmnh! Haya nimalizie. Umesema kuwa mke...” alisema Upendo kwa kushadadia.
“Tuachane kwanza na hilo. Tutamalizia baadaye, acha nishughulikie hiki nilichovunja, maana si changu.”
“Haya,” Upendo aliitikia na kukata simu.
Japo maongezi hayakumalizika, ila kuna dondoo fulani alizipata. Hakutaka kuziamini moja kwa moja, lakini alikuwa na uhakika nazo kuwa kile alichosikia kipo sahihi. Moyo ulighafirika ghafla, maumivu yalimpanda kooni, hali iliyomfanya asipate hata chembe ya hamu ya kitu chochote. Mpaka akithibitishe. Harakaharaka alimpigia Mwanjaa, ambaye alikuwa na mawasiliano ya kina kwa baadhi ya siku na Vumilia. Alimhadithia alichosikia kisha kumuuliza kama ana taarifa hizo ama lah! Isivyo bahati. Mwanjaa hakuwa na taarifa zozote. Hakuishia hapo. Alipanda hewani, moja kwa moja kwa Vumilia. Lakini nako hakufanikiwa. Kwani simu ya Vumilia iliishia kuita tu pasipo kupokelewa. Hakupiga mara moja tu, alipiga mara nyingi, zote zilikuwa na mrejesho uliofanana.
Kitendo cha kutopata jibu kilizidi kumuumiza. Uchungu ulizidi kujazana na kutamani muda huohuo apae kumfuata Vumilia anakopatikana. Karibu adondoshe chozi, maana hali ilikuwa mbaya kwake. Hisia zilimwendesha, kulisaka pendo, alilolidharau mwanzo kwa ajili ya kufurahisha mioyo ya ndugu. Baadaye sana, ndipo alifanikiwa mpata Vumilia. Usiku, majira ya saa moja. Kidogo, hali ilipoa, sauti yake alivyoisikia. Mada husika chap, ilianza. Punde walivyosabahiana, lakini ilianza kwa manung’uniko kwanini hakupokelewa simu zake. Kwa ustadi wa lugha na uongeaji fasaha aliojaliwa Vumilia, hakupata shida, kujibu tuhuma zote alizoambiwa, alikataa, habari za yeye kuwa na mke na ile ya kwanini hapokei simu, alimwambia wingi wa kazi umesababisha hivyo. Walivyohitimisha akakata simu.
“Kitu kipi kilichokusuma kuuliza. Muulize huyohuyo aliyekuambia, na si kunisumbua,” alisema Vumilia kimoyomoyo, baada ya kukata simu na kuirejesha mfukoni.
Majibu hakuridhika nayo. Moyo ulizidi muuma na ili apoze, alifikiria kuiangalia picha aliyoambiwa. Hivyo aliazima simu kubwa na ya kisasa, smartphone, kwani yeye alikuwa anatumia simu ndogo al-maarufu ‘simu ya tochi’ kwa mtu, kisha kuhifadhi namba ya Vumilia. Baada ya hapo aliruhusu data kuwa hewani ili aweze ishuhudia. Alitumia dakika tatu tu, kukamilisha, na kujionea picha tajwa. Picha ya mwanamke, mrembo mwenye muonekano wa maadili mema, kutokana na mavazi aliyovaa. Kavaa mavazi ya kiheshima. Shungi kubwa kichwani, blauzi ndefu na nzito, pasi na sahau sketi refu na nzito isiyoruhusu ndani kuonekana. Sehemu kubwa ya maungo yatamanishayo yalifichwa na mavazi hayo. Alivuta kumbukumbu kutafakari, wapi sura hiyo ashawahi iona. Ila hakufanikiwa. Ilikuwa sura ngeni machoni mwake, kwani hata Vumilia mwenyewe ni mara ya kwanza kuiweka. Kila alivyojaribu kutafakari kama Vumilia ashawahi weka siku za nyuma, alikumbana na sura yake na ya dada wa Vumilia, mtoto wa mama yake mdogo aitwaye Zulea.
“Yawezekana kweli ni mkewe. Ila kaamua kuniongopea,” alijisemeza, akiwa anazima data kisha kufuta namba aliyoihifadhi na kurudisha simu kwa mhusika.
“Iwe isiwe, nitapambana, hadi nifanikiwe kuwa himayani mwa Vumilia. Niko radhi, kuwa mke wa pili kwake,” aliendelea kujisemeza, kauli iliyopelekea mshangao kwa yule aliyemuazima simu, kumshangaa nini azungumzacho.
Usiku wa siku hiyo ulipita kwa tabu sana. Mawazo yalimsumbua, kwa muda mrefu kiasi kwamba hata lepe la usingizi alilisikia tu kwa jirani. Hisia, zilimtesa. Chanzo Vumilia. Asubuhi kulivyokucha, punde baada ya kusali, mtu wa kwanza kuwasiliana naye ni Zulea. Maana alikuwa na namba zake, alizozipata pindi anatongozwa na Vumilia, hivyo Zulea akawa anatumika kama kiunganishi, kumsaidia kaka yake baadhi ya siku.
“Mambo Zulea?”
“Poa, niambie uliyekataa kuwa wifi yangu.”
“Mmmmh! Acha hizo bhana. Mbona sauti iko hivyo, nini shida?”
“Naumwa. Wiki ya tatu sasa. Nimekuwa mtu wa kitandani tu.”
“Nini kikubwa kinachokusumbua?”
“Mguu!”
“Mmmmh! Pole sana. Naweza kukutembelea?” alisema Upendo, kauli iliyofuatiwa na kicheko. Maanisho la kutania.
“Unaweza, wala hamna shida.”
“Basi kesho naja.”
“Nitafurahi sana. Ila nipo nyumbani, Mtwara, sio kule unakokufahamu.”
“Hamna shaka. Kesho mgeni wako.”
Akakata simu!
Aliamini! Kufanya hivyo, kutampatia mwanga zaidi wa ufahamu na mafanikio ya kusudio lake. Alivyoenda kazini, alifikia kuomba ruhusa na kurudi bwenini kwa ajili ya maandalizi ya safari ya kesho. Kama alivyoahidi. Hapa hakukuwa na matani, alithubutu, na kwa namna yoyote ilikuwa lazima iwe, lengo litimie. Siku iliyofuata, mapema sana. Saa kumi na mbili asubuhi, aliwahi kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, Ubungo. Alifanya utafutaji, uliomchukua dakika nane, kutafuta eneo lililoegeshwa basi ziendazo mikoa ya kusini. Akafanikiwa kuliona, basi nyingi zikiwa zimepakiwa tayari kwa safari. Kwani makondakta waliokesha kuzunguka kuwavaa watu mbalimbali walimpa ishara hiyo. Alilifuata moja wapo, yaendayo mjini Mtwara, Machinga high class, alionana na mhudumu, kisha kuhudumiwa. Hadi kufikia saa 12:30 asubuhi tayari alishakuwa ndani ya basi na safari ilikwishaanza.
Huo ukawa mwanzo mzuri kwake, kwani aliamini itampatia fursa nzuri ya kuonana na kufahamiana na ndugu wengi wa Vumilia. Ule uchungu uliomtawala jana, kwa kiasi kidogo, ulianza potea. Furaha ilimnyemelea kutakasa moyo wake. Saa 7:45 mchana basi iliwasili mjini Mtwara. Aliteremka, akamuita muendasha bodaboda na kumuamuru ampeleke mahali anakohitaji, ambako tayari alikwishapatiwa anuani usiku wa jana. Bodaboda alivyoielewa ile anuani aliyoambiwa, Upendo alipanda safari ikaanza.
“Huko ni elfu moja mia tano tu,” alisema bodaboda, wakiwa katikati ya mwendo kulitafuta eneo husika.
“Hamna shida, twende tu nitalipa,” alisema Upendo, wakati huo dereva bodaboda akizidi pangua na kuingiza gia kwa fujo.
Mwendo wa dakika kumi, alifikishwa sehemu husika. Nkanaledi! Upendo aliteremka na kupokelewa na ndugu wa Zulea, alipolipa pesa ya usafiri waliongozana hadi nyumbani. Kufika tu, alimshukuru Mungu, kuonana na mlengwa pia, alishukuru. Awali ya yote alitambulishwa, baada ya hapo ukawa wasaa mzuri wa mazungumzo baina ya Upendo na Zulea. Alionesha ukarimu na yote mema yanayohitajika, apate teka akili na kujitengenezea nafasi, ili baadaye asipate pingamizi. Alifanya kazi, na kutoa baadhi ya huduma za kumhudumia Zulea na mengine mengi tu yenye kufurahisha.
“Hivi Zulea ulisema kuwa huyu Upendo ni...” aliuliza mama yake Zulea. Ambaye ni mama mdogo wa Vumilia.
“Alitongozwaga na Kaka Vumilia akamkataa sababu ya dini.”
“Mmmh! Ana tabia nzuri sana. Anafaa kuwa mkwe. Sasa si wangeelewana tu waishi pamoja.”
“Yote yamejaribiwa, ila alikataa katakata. Sijui kwa sasa. Lakini si tayari kaka kashaoa, hivyo hana nafasi tena, labda ndoa yao ivunjike siku za karibuni.”
“Ila huyu yupo vizuri. Angelimpata, wangeliendana. Ila sijui huyo aliyonayo sasa yukoje.”
Matendo aliyoonyesha Upendo, yalienda sambamba na akili yake. Apate jina, na utambulisho, utaoweza kumsaidia baadaye. Kwa hapa alifanikiwa. Lakini suala la kufahamu habari za Vumilia kuoa, bado hakuzipatia ufumbuzi. Hakutambua kama ni kweli, ama lah! Kwani hata alivyomuuliza Zulea, aliishia kuzungushwa tu. Zulea alijifanya kutofahamu, ingawa taarifa alikuwanazo. Toka kwa Vumilia na vyanzo vingine. Hatua hiyo, ilimfanya kuanza upya ufikiriaji. Usahihi wa kile alichosikia ni upi. Ruhusa aliyoomba ilikuwa ya siku nne. Ruhusa ya magumashi, isiyotambulika na uongozi wa kambi yake. Hivyo, alipaswa kukaa mjini Mtwara kwa siku tatu. Siku ya nne, siku ya safari ya kurudi. Ilivyowadia siku ya tatu, kuna ugeni mwingine uliwasili, pale nyumbani kwa kina Zulea. Ugeni toka Mangaka, dada wa mama Zulea. Naye alifahamiana naye, baada ya kutambulishwa na kufanya maongezi ya hapa na pale.
Jioni ya siku hii, punde alivyomaliza mapishi alitafuta eneo akaketi, nje kidogo na nyumba ya kina Zulea. Kutafakari mustakabali wa safari yake na matokeo aliyopata ni yapi. Jirani na pale alipoketi, walikaa Mama Zulea na dada yake, wakiteta jambo. Maongezi yaliyosikika vyema kwa Upendo, ila hakuyatilia maanani. Sababu yalikosa umuhimu wa kuyafuatilia.
“Hivi ushasikia kinachoendelea Mangaka kuhusu baba yake Vumilia, Mzee Matatizo?” alisema Dada yake mama Zulea. Kauli iliyopelekea kumshtua Upendo na kumfanya atege sikio hima kusikiliza taarifa hiyo.
“Eeeh! Nina taarifa nayo. Sijui anataka nini yule mzee hadi akazane kumsitisha mwanae asioe huko aliko, au sijui kamtafutia mwanamke?”
“Nami nashindwa muelewa. Maana kaja kwangu mara kibao kuniomba, nimwambie Vumilia asioe huyo mwanamke aliyenayo.”
“Washapendana, yeye leo hii anaingilia. Yaani...acha tu. Ila mwenyewe kaendelea kusimama kwenye msimamo wake. Hataki kabisa kuachana naye.”
“Kikubwa alipaswa kumuambia asisahau nyumbani. Na si hivyo anavyofanya yeye.”
“Nami nilimshauri vivyo hivyo. Kwani wanawake wenye tabia mbaya kokote kule wapo. Hata huku kwetu wamejaa.”
Maongezi hayo yalichimbua upya uchungu wake. Na uthibitisho wa kile kilichokuwa kinamsumbua. Taarifa rasmi, aliinyaka. Vumilia kashaoa. Sababu awali alishajiapiza, kwa namna yoyote atayokutana nayo lazima dhamira yake itimie. Kuvunja ndoa ama kuwa mke wa pili. Atakamilisha vipi? Alilazimika kurudi jijini Dar se salaam kujipanga upya. Siku ya mwisho ya ruhusa yake alifunga safari, kurejea jijini Dar es salaam. Tena alitoka mapema sana ili awahi kufika. Na basi ya kwanza. Awamu hii safari nzima alimfikiria Vumilia. Kwanini kaoa mapema? Fikra zilizokosa majibu hadi alivyowasili jijini. Muda mwingine alikuwa anamlaumu. Kwanini kamuongopea, ile siku aliyouliza habari kuhusu hilo jambo. Ila hakuwa na jinsi, kwani tayari yashatokea. Kikubwa, kukiangalia, kile alichopanga.
Alivyowasili kambini kwao, aliwaita rafikiye. Madam Cecy na Mwanjaa. Kisha kuwapatia mrejesho wa matokeo aliyopata toka kule alikoelekea. Aliwahadithia, kuanzia hatua ya mwanzo, alivyosafiri, alivyopokelewa, alivyoishi na namna alivyoanza kubalika pia. Aliendelea kwa kuwahadithia, habari za kile alichofanya Vumilia. Kuoa, na hali iliyopo baina ya Vumilia na baba yake.
“Sasa kwanini kaoa kimyakimya na kwa haraka hivyo?” aliuliza Madam Cecy.
“Sielewi dada yangu. Safari nzima nimemtafakari, sijampatia picha. Maana nilishamuulizaga, akakataa.”
“Kwa hiyo unaamuaje?” aliuliza Mwanjaa.
“Bado nampenda. Na namhitaji awe mume wangu.”
“Utatumia njia ipi, wakati yupo ndani ya ndoa?”
“Mmmh!...kuna njia mbili nilizofikiria. Ya kwanza, kumtumia huyu anayekinzana naye. Baba yake. Ya pili ni mimi kwenda moja kwa moja, kwa njia ya mawasiliano, na ikibidi kwenda huko anakoishi. Maana kwa sasa niko radhi kwa yote.”
“Kwa yote yapi?”
“Hata kuwa mke wa pili. Maana ule upendo aliokuwa ananipatia kipindi cha nyuma, sijawahi pata kwa mwanaume mwingine toka nipate kujitambua. Alikuwa ananipenda sana. Mimi nikachezea hisia zake. Naamini hata hiyo ndoa ya haraka aliyofunga ni kwa sababu yangu,” alisema Upendo. Kwa sauti iliyojaa unyonge, huku akilengwa lengwa na machozi.
“Jikaze, usilie. Kwa majukumu ya kazi unaamini utaweza kumudu hili tukio?”
“Nitachukua likizo. Ili nifanye kwa uhuru zaidi.”
Majuto yalimtwaa. Kwanini alimkataa Vumilia. Sasa thamani yake alianza iona, kupitia kumbukizi zilizokuwa zinampata kila uchao. Mambo yaligeuka. Wakati huu, Upendo ndiye alikuwa mwingi wa mawazo na maumivu. Aliteseka haswa, na suluhusho pekee, si mwingine bali ni Vumilia. Hakuhitaji mwanaume mwingine zaidi yake, kwa kuwa aliamini, akitoa nafasi kwa mtu mwingine, anaweza fanywa kama alivyofanywa baada ya kutengana naye. Siku hiyohiyo aliyoripoti kazini, alianza fanya mpango wa kuomba likizo, hakutaka kuchelewesha mambo, alihitaji yaende kasi, mithili ya mwanga ama sauti. Aliandika maombi na kupeleka ngazi hitajika, yakajibiwa wiki mbili mbeleni. Hakukuwa na shida. Sababu hitajio lake lilikuwa likizo, alimshukuru Mungu, lilivyofanikiwa, baada ya hapo alifunga safari kuelekea Mangaka. Safari iliyomchukua zaidi ya masaa kumi kuwasili. Alivyowasili, aliomba kupelekwa nyumba ya wageni. Na mmoja wa madereva wa bodaboda, akapelekwa Meswaki. Sehemu pekee, iliyosifika kwa huduma nzuri na ya kuaminika ndani ya Mangaka.
Alifanya huduma, ofisi ya mapokezi, ambapo alikuwepo kijana mmoja mtanashati, aliyefahamika kwa jina la Banzi. Mrefu, mweusi, mwenye umbo lililoshiba wastani na nywele za kipilipili kichwani. Kesho yake hakwenda sehemu yoyote zaidi ya kuzungukia mazingira aliyofikia na kupumzisha mwili wake. Siku ya pili, ndipo alianza majukumu, huku akiwa kapanga muda wa wiki mbili, kuhakikisha anamuweka sawa Mzee Matatizo, baba yake na Vumilia. Kupata habari zinazomhusu, alimpeleleza Banzi. Mhudumu wa Meswaki, naye kumfungukia, pasi na chembe ya shaka, kwanini mwanamke huyo kahitaji habari za Mzee Matatizo. Alivyofanikiwa kupata mawili matatu. Wapi anapatikana kwa muda mwingi, na anapoishi, aliita bodaboda kisha kumuomba ampeleke sehemu hizo mbili. Sehemu ya kwanza, ilikuwa kijiwe, kule anakopatikana muda mwingi, achilia mbali na nyumbani. Ambako ni kwenye kijiwe cha mchezo wa bao. Kijiwe maarufu sana. Kilichopo mkabala na dukani kwa kijana maarufu, anayetoa huduma ya kuchajisha simu na huduma ya pesa ya mitandao ya simu. Jaymoe!
Hapa! Hawakufanikiwa kumkuta. Walijaribu ulizia, lakini hawakupewa jibu sahihi, kama kaja ama hajaja. Hatimaye walifunga safari kwa mara nyingine, hadi mazingira jirani na nyumbani kwake. Hivyo kushuhudia baadhi ya mambo yaliyokuwa yanaendelea kufanywa na wale waliopo. Ila waliyemhitaji hakuwepo. Mpango wake kwa siku hiyo ulienda kombo. Hakuwa na jinsi kukubali kupoteza. Alirejea kule alikofikia, akitawaliwa na mawazo lukuki sana. Itakuaje? Ndicho kikubwa kilichomtatiza. Moja kwa moja alielekea chumbani kwake na kujitupia kitandani. Kupumzisha akili na mwili kwa muda. Ili atapokuwa sawa, apambanue vizuri, mbinu za kuendelea nazo. Al-manusra usingizi umpitie. Ila kumbukumbu ya maongezi, baina ya Mama Zulea na dada yake, aliyefahamika kwa jina la Mama Daduki, ndiye ilimstisha na kumsukuma aamke chap.
“Nasikia siku hizi Mzee Matatizo mwenyewe anakesha kulewa na kurudi nyumbani usiku wa kiza kinene,” alikumbuka Upendo. Hivyo kumuongezea mwanga mwingine. Kuwa Mzee Matatizo anatumia vilevi.
Haraka alinyanyuka pale kitandani. Kuelekea mapokezi, kumuangalia Banzi, ampatie uhakika wa kile alichokumbuka. Alivyomkuta, hakuchelea kuanza maongezi, alimuuliza, naye Banzi kujibu kwa ufahamu wake alionao.
“Sina hakika juu ya jambo la kulewa. Lakini, muda kama huu mara nyingi hushinda kijiwe kimoja hivi cha kahawa. Kwa Mzee Makashata,” alijibu Banzi punde baada ya kuulizwa.
“Naweza pata mtu akanipeleka huko?”
“Kwa huu muda. Wacha mimi nikusaidie, nitaenda kukuitia,” alisema Banzi huku akinyanyuka kwenye kiti alichoketi mule ofisini mwake. Na alifanya hivyo kwa kuwa Upendo alikuwa mgeni, na kiza kilishaingia, hivyo si vizuri kwake kutembea muda huo sehemu asiyoifahamu, ukizingatia ni mtoto wa kike.
Banzi alijitolea kumsaidia. Aliita pikipiki kisha kuelekea nyumbani kwa Mzee Makashata, alirejea hapo dakika saba baadaye, akiwa ameambatana naye yule aliyemfuata.
“Huyu ndiye mhusika anayekuhitaji,” alisema Banzi kumuambia Mzee Matatizo, akimuonesha Upendo kwa moja ya kidole cha mkono wake wa kuume.
Walitafutiwa eneo wakaketi, kwa raha mustarehe, ambalo kidogo litawaweka mbali na bughuza za hapa na pale. Vinywaji navyo vilifuatwa, baada ya muda kidogo, vyenye kilevi, Bia! Pamoja maji yaliyo na baridi kiasi kidogo. Walianza na salamu, kisha kufuatia mada husika. Ambapo Upendo alieleza kwa kina dhamira aliyonayo na maisha ya nyuma pindi wana mahusiano mazuri na Vumilia. Maongezi yao yalisindikizwa na fundo za vinywaji vilivyopo mezani, vilivyofanya kazi ya kulainisha koo na kuipa akili uchangamfu.
“Umesema kwamba wewe ni mwenyeji wa wapi?” aliuliza Mzee Matatizo.
“Katavi baba!”
“Mlikutana wapi na mwanangu?”
“Kwenye mafunzo ya jeshi la kujenga taifa, Mafinga.”
“Oooh! Kwa hiyo mnafahamiana vizuri tu?”
“Ndiyo. Ukiweza mpigie simu kumuuliza.”
Mzee Matatizo alifanya hivyo. Alichomoa simu kwenye moja ya mfuko wake, kisha alibonyeza vitufe kadhaa na kuweka sikioni. Sekunde chache baadaye, ilipokelewa na kuwa kwenye ulimwengu wa maongezi.
“Eeh! Baba.”
“Shikamoo!”
“Marhaba! Unaendeleaje?”
“Namshukuru Mungu.”
“Basi nasi tunashukuru, maana tunaendelea vizuri. Ila tumebahatika kupata ugeni.”
“Ugeni gani?”
“Rafiki yako Upe...” alisema Mzee Matatizo, ila hakumalizia kauli yake simu ikakata. Muda wa maongezi alionao uliisha.
Upande wa pili, Vumilia alitoa mhemo wa nguvu. Uliomshangaza mtu aliyenaye, mkewe. Na kupelekea kutoka na swali.
“Kulikoni mume wangu?”
“Mmmmh! Baba kanipigia. Ameniambia kuwa wametembelewa na rafiki yangu, ambaye ni Upendo.”
“Upendo!” Zamzam alishangaa.
“Ndiyo. Nashindwa hata kuelewa. Na sijui mpango wa huyo binti kwenda huko ni nini?”
“Vumi! Mume wangu, usinifanye mtoto mdogo. Hiyo ni mipango yako. Maana siku za nyuma nimekesha kukuuliza kuhusu kauli ya baba juu ya mahusiano yetu, uliishia kunizungusha. Kama unataka kumchukua huyo mwanamke wako niweke wazi, nami nijue la kufanya,” alisema Zamzam akionekana kuwa mwingi wa hasira.
“Usinihukumu mke wangu. Hata nami sielewi huyo mwanamke ana lengo gani nami.”
“Kapajuaje kwenu? Na mzazi wako kamfahamu vipi kama sio wewe umemuelekeza?” aliuliza Zamzam, machozi yakianza mtiririka.
“Hakika niamini, sijahusika na jambo lolote juu ya ujio wake huko alipo. Naomba unielewe, pia acha kulia. Mimi kwa sasa nakuhitaji wewe ndiyo maana nimekuoa, yeye hana nafasi tena kwangu,” alisema Vumilia, akimvuta Zamzam na kumsogeza karibu na kifua chake, huku akiutumia mkono wake wa kuume kumpigapiga mgongoni atulie.
****
Kwa kiasi fulani Upendo alifanikiwa. Kwani, aliweza mteka Mzee Matatizo, na kukubalika haswa kwake kama mkwe. Na alikuwa ridhaa Upendo kuolewa na mwanaye kwa kuwa wamepata fahamiana tangu muda mrefu. Hakuishia kutambulika kwa Mzee Matatizo pekee, alipelekwa nyumbani kwao pia, familia imfahamu. Mama wa kufikia wa Vumilia na nduguze. Alijenga mazoea, kwa familia nzima, na baadhi ya majirani, kisha kutambulika rasmi kuwa ni mpenzi, mchumba ama mke mtarajiwa wa Vumilia. Kuhusu suala la dini, aliweka bayana kuwa yupo radhi kubadili, Vumilia naye atapokuwa ridhaa kumuoa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuhusu hilo mkwe wangu usiwaze. Ni lazima mwanangu akuoe. Mimi simtambui huyo mwanamke aliyonayo huko. Kwanza mwanamke ana tabia mbaya, na haendani na mila za kwetu,” alisema Mzee Matatizo, jioni moja wakiwa wameweka baraza la kifamilia nyumbani, kujadili hatma ya jambo hilo.
“Nitafurahi sana baba. Hapo ndoto yangu itakuwa timilifu, maana nampenda sana mwanao.”
Hata kule hotelini alikokuwa amefikia alihama. Alipewa chumba kimoja wapo, hapo nyumbani kwa muda wote aliouhitaji. Wiki mbili. Alionyesha nidhamu na unyenyekevu wa hali ya juu kwa wote, hakuangalia umri, awe mkubwa ama mdogo kwake alimheshimu. Alifanya hivyo, kutimiza azma yake na si kitu kingine. Japo kiuhalisia, kweli, ni mtu aliyebarikiwa vitu hivyo kutokana na mafunzo imara ya kidini aliyonayo. Muda wa likizo ulivyofika tamati alirejea jijini Dar es salaam, akiwa mwingi wa matumaini, anaenda kumweka Vumilia himayani. Baada ya mazingira rafiki aliyojitengenezea. Sasa kidogo, moyoni alitawaliwa na furaha, tofauti na awali, iliyowabainisha wamuonao kuwa kabadilika. Kuna kitu kipya kakipata chenye faraja.
“Au kapata mpenzi nini? Maana huyu naye kwa kujifanya bikra, wakati ashaonjesha hayo mambo kipindi cha nyuma hajambo,” walisikika baadhi ya wasichana wenziye wamuonao, pindi Upendo anafurahia furaha tele iliyokithiri moyoni mwake.
Maisha yake yalikuwa kama ndiyo kwanza yanaanza. Kwani siku zote, kuwa na mtu mwenye uhakika baina yenu muna mapendo ya dhati, wote hamuishi faraja. Lakini kwa Upendo ilikuwa tofauti. Juu ya ufahamu, Vumilia kuwa ana mke, yeye alifarijika, kisa, kafahamika kwa wazazi. Huku bado akiamini, Vumilia ana chembechembe za Upendo kwake, hata kama kafanya hilo tukio. Aliamini, msaada tosha toka kwa Mzee Matatizo utaenda timiza takwa lake. Kwa wakati huo, Vumilia, ndiyo mwanaume pekee, aliyehitaji kuwa naye, na si vinginevyo, hivyo ulazima wa kuhakikisha hilo linatimia, alipaswa kuhangaika kwa namna yoyote kulitimiza. Upendo alijipanga kuharibu ndoa ya Vumilia, iliyopita kimyakimya pasi na ndugu kufahamu, ili ajitwalie kijiti, ama awe msaidizi kwa yule aliyemtangulia.
Kila kilichoendelea, nyumbani, Vumilia alipatiwa taarifa na mmoja wa nduguze. Naye kumtaarifu Zamzam, aondokane na sintofahamu, imchukuayo furaha yake, Upendo akiwa chanzo. Kwa kiasi fulani, amani ilitetereka. Kiasi kwamba maelewano yalifikia kuwa hafifu ndani. Mapatano yalikuwa ya chini, hadi mambo ya muhimu kama wanandoa, walikuwa wanapatiana kwa shida. Mara nyingi, Zamzam, alionekana kuwa mpingaji, wa kutekeleza. Kwa kigezo cha Upendo. Hali iliyofanya aanze kuhisiwa vingine, kwamba anatoka nje. Anachepuka! Hakuwa tena, mtu aliye na heshima ya ndoa. Alifanya mambo ajisikiavyo, alianza tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani, kwa baadhi ya siku, huduma nyinginezo pia, alifanya pale aamuapo, na si kwa maelekezo toka kwa Vumilia. Mumewe! Alivyohojiwa juu ya mabadiliko yote aliyonayo, jibu lake, lilikuwa moja tu, anatafuta talaka. Sababu hapendwi na hakubaliki na baba mkwe wake. Hivyo hakuhitaji kuendeleza mahusianao ya ndoa kama mzazi wake, hamtambui. Ilileta ukakasi kwa Vumilia, lakini alivaa ushujaa wa kukabiliana na vyote, ilimradi Zamzam abaki ndani. Hakuwa radhi kuondoka kirahisi, yote kutokana na tabia alizonazo, achilia mbali mambo ya chumbani, yabadilishayo akili.
Japo yalikuwa mambo yenye maumivu, alijipa moyo, ipo siku yatatulia kama sio kumalizika kabisa. Alifanya jitihada za kila aina, kuhakikisha hilo, kutumia muda mwingi, kumshawishi Zamzam, aondokane na imani aliyonayo.
“Unahisi nitakuaje kwa wazazi wako kama hawana hata chembe ya kukubaliana nawe kuwa na mwanamke wa ukanda huu?” aliuliza Zamzam, jioni moja punde walivyopata chakula.
“Lakini tambua si wote. Mama hana shida kuhusu uamuzi niliochukua.”
“Aaaah!...wewe muoe tu huyo uliyeamua kumpeleka kwenu.”
“Amini, nikuambiacho, suala la Upendo kwenda nyumbani si mimi niliyepanga hivyo.”
“Kama hujapanga, kapajuaje?...endelea tu na huyohuyo, nami nitatafuta mwanaume mwingine,” alisema Zamzam, kwa sauti iliyojaa unyonge, kuonyesha namna gani alivyoumizwa na kile kiendeleacho baina yao.
“Lakini juu ya hilo, tambua kuwa, sisi ndiyo tumetongozana, na sio wazazi. Mimi na wewe ndiyo tunajuana, hao hawafahamu hata punje ya taarifa yoyote kutuhusu. Sasa unaanzaje kuwapa nafasi kubwa ya kutuamulia?”
“Bhana eeh! Nishasema. Fanya ujuavyo, lakini uamuzi wangu kwa sasa ni huo.”
“Ina maana hunipendi tena?”
“Utajua mwenyewe.”
Vumilia alikuwa na wakati mgumu. Uliomuondolea amani na furaha ya moyo wake. Kwani, hata raha ya kazi haikuwa kwa kiwango kikubwa tena. Muda mwingi alitawaliwa unyonge na manung’uniko, ambayo, kila alivyoyatafutia uvumbuzi, ayatatue, yalizidi kuongezeka. Matokeo makubwa aliyoyapata katika hali hiyo ni upweke. Hakukuwa na matokeo mengine. Kila aonekanapo alionekana pekee, tena akiwatawaliwa na mawazo tele kichwani. Kumfikiria Zamzam na Upendo. Kuhusu matendo yao.
“Zamzam kabadilika sana siku hizi. Lakini yote ni kwa sababu ya Upendo. Hakuwa hivi mwanzo, sasa kapoteza heshima kwangu na anakesha kunidharau. Ilhali ni mume wake wa halali,” alisema Vumilia kimoyomoyo, jioni moja alivyokuwa anatoka kwenye matembezi yake, akielekea nyumbani.
“Nitavumilia mpaka lini? Kama kaanza kutembea na wanaume wengine huko? Si bora niachane naye. Lakini!...Upendo, si ndiye chanzo?...mmmmh! Upendo ndiyo chanzo, hivyo inabidi nipambane na huyuhuyu, asiniharibie ndoa yangu. Yeye nilishamtongoza akakataa, sasa ya nini arudi kwangu?” aliendelea kujisemeza.
Jioni ya siku hiyo alivyorejea nyumbani, alimvutia waya Mwanjaa, rafiki wa karibu wa Upendo. Simu iliita kwa sekunde chache, kisha kuingia kwenye ulimwengu wa maongezi punde ilivyopokelewa. Alimtolea dukuduku lake, kutohitaji mazoea na Upendo, alivyomalizana naye, alimtumia ujumbe Upendo mwenyewe kusisitiza uthubutu aliochukua. Ujumbe ukajibiwa muda mchache sana baada ya kutuma, ulisomeka ‘ katu sitoacha nilichoanza. Nimedhamiria sasa kuwa mkeo kwa namna yoyote.’ Sasa ulikuwa wakati rasmi kwake, kupambana na Upendo, asitishe takwa lake, ili familia irudi ilivyokuwa awali. Itawaliwe na amani, faraja na neema kemkem.
Njia mbadala ya utekelezaji wa hatua hiyo, alikata kabisa mawasiliano. Zile simu za mara mojamoja alizokuwa anapigiwa na Upendo, sasa, alikuwa hazipokei kabisa. Kila alivyopigiwa naye, alikuwa hapokei kama sio kukata kabisa. Maisha yalienda hivyo, huku kwa mkewe, akijitahidi kuurudisha moyo wake. Ijapokuwa, hakuwa na uhakika wa kile alichokihisi, kuwa mkewe kapata mwanaume mwingine. Pindi yeye, anaimarisha mikakati ya kuboresha familia yake, Upendo naye anatumia, nafasi hiyohiyo, kuidhorotesha, kwa ushirikiano mkubwa toka kwa Mzee Matatizo, baba yake na Vumilia, akisaidizana na Madam Cecy na Mwanjaa. Kila muda alikesha kuwasiliana nao kuwaeleza hali inavyoendelea, kuomba ushauri, kitu gani kifuatacho kitafana katika kuhakikisha anatimiza nia yake. Kwa lolote walilonalo humpatia, kisha huchanganya, ama kulinganisha na vile awazavyo, akiona vina ulandano hutumia, vikitofautiana, huangalia kipi bora chenye manufaa.
“Ndugu zanguni, nisaidie huyu mwanaume aweze kunielewa,” alisema Upendo, usiku mmoja alivyokutana na kina Madam Cecy na Mwanjaa, bwenini anakoishi.
“Kwani bado anaendelea kukataa?” aliuliza Madam Cecy.
“Ndiyo. Tena kwa sasa hapokei hata simu yangu. Nikipiga, anakata, sijui nifanyaje?”
“Mmmmh!...dawa ni moja,” Mwanja alichangia.
“Ipi tena?”
“Kumfuata nyumbani kwake, ama kokote apatikanapo kwa muda huu.”
“Hapo umenena. Ni ushauri mzuri, yanipasa kuutekeleza.”
“Si unafahamu anapoishi?”
“Yeah! Nafahamu, ni Dodoma, sijui ni Dodoma sehemu gani. Ila kwa kumbukumbu niliyonayo ni Dodoma mjini.”
“Haya kazi kwako, kwenda, ama kutokwenda, utajua mwenyewe.”
“Msijali, ni lazima, Vumilia awe ndani ya himaya yangu.”
Alivyomaliza kuzungumza nao, alivuta waya kwa Mzee Matatizo. Alimueleza dhamira yake ya kwenda mjini Dodoma, na Mzee Matatizo kuridhia. Tena kwa uridhiaji uliyomshawishi naye kwenda ndani ya mji huo. Kuangalia mazingira aishiyo mwanaye, lengo likiwa kumsindikiza Upendo, kwani alihisi, hatoeleweka akienda peke yake. Hivyo kuonyesha msisitizo, aliamini naye akienda mambo yatakuwa vyema sana. Katika maandalizi ya sakata hilo, hakumtaarifu mtu yeyote, zaidi ya, mwenyewe kukaanalo moyoni mwake. Hata mtembelewa hakutaarifiwa, alihofu, akitoa taarifa mapema atapewa sababu nyingi za kumtaka asiende. Sababu kubwa, ikiwa sehemu ya kufikia, kwani alifahamu mwanaye anaishi chumba kimoja, alichopangisha mtaani. Alifahamu hilo, kupitia kwa mmoja wa ndugu waliomtembelea siku zilizopita. Pia jambo la kutowataarifu wanafamilia yake, alihofia kumvujishia siri. Alisubiri karibu na siku ya safari, ndipo aliwaambia, tena kwa kuwaongopea, anaenda sehemu nyingine tofauti na ile aliyodhamiria.
Baada ya kufanya maandalizi ya hapa na pale, siku husika iliwadia. Aliamka mapema sana, alifanya usafi wa mwili, alipotayarika, alifanya maagano kwa mara ya mwisho, kisha aliondoka kuelekea kituo cha mabasi kilichopo ndani ya mji huo. Takribani kilomita mbili toka nyumbani kwao. Ambacho kipo mkabala na sheli ya Kinjikitile, mtaa wa Mchangani, kama unaelekea mjini Masasi. Mnamo saa 12:30 asubuhi, tayari alishakuwa ndani ya gari, basi la Tashriff, lifanyalo safari zake, kutoka mjini Tunduru kuelekea jijini Dar es salaam. Safari ilikuwa tamu, kwa huduma nzuri zitolewazo, na wahudumu wa basi hiyo, waliojaa ukarimu na unyenyekevu wa kutosha. Kama vile kugawa vinywaji, na nyinginezo, hasa mtu apatapo tatizo la kiafya. Sehemu yenye kituo cha upumzikaji, basi ilisimama, na kutoa dakika kadhaa za mapumziko, kuwapa nafasi abiria, wanyoshe maungo ya miili yao, zimalizikapo safari huendelea. Wasio wahi kusafiri kwa muda mrefu hawakuacha kuonyesha ushamba wao, kwa kuangaza, jiografia ya vijiji mbalimbali ilivyojijenga. Mzee Matatizo akiwa miongoni mwao. Macho yake hayakubanduka kuangaza dirishani. Tena walivyofika sehemu za mijini, ndiyo alizidisha ushangaaji. Kwa kupeleka macho huku na kule, upande alioko na ule mwingine, kuangalia namna miji ilivyojengwa kwa ustadi. Hasa iliyosheheni majengo marefu, na nyumba za kisasa.
Hakika! Aliosha macho. Kama walivyozoea kuita waswahili. Na kujawa shauku ya kuteremka atembee ili ajionee kwa uzuri. Saa nane baadaye, basi iliwasili kituo cha mabasi Mbagala. Kikusanyacho mabasi mengi yatokayo mikoa ya kusini. Hakuwa na budi, aliteremka. Kwani, hapo ndiyo ulikuwa mwisho wa safari yake. Alijipenyeza katikati ya halaiki ya watu wengi waliokusanyika karibu na mlango, wakinadisha biashara zao za usafiri wa taksi, bodaboda wengine wakisubiri kupokea ndugu zao, achilia mbali wafanyabiashara waliobeba mikate, keki, juisi na kila aina ya biskuti. Alivyofanikiwa kupita katikati ya halaiki hiyo alijisogeza pembeni kidogo na kusimama pembezoni mwa banda moja litumikalo kukatia tiketi. Akiwa na begi dogo la mgongoni lililo na nguo kadhaa. Alitoa kilongalonga, Nokia 110 iliyofungwa mipira mingi kushikilia betri isidondoke. Alibonyeza vitufe kadhaa, kutafuta namba fulani alivyoipata akapiga. Haikumchukua muda mrefu kuingia kwenye mazungumzo, ambayo nayo yalikuwa mafupi tu, kisha alikata simu na kuirejesha mfukoni. Muda mchache baadaye, Upendo alitokeza mbele yake, aliondoa aibu, na kwenda kumvaa kwa nguvu, ishara ya kufurahia kuonana kwao. Walisabahiana, huku wakitembea taratibu kuondoka eneo la kituo hicho cha mabasi.
Walivyotoka nje, Upendo aliita bajaji, na kumuamuru dereva, awapeleke katika moja ya hoteli yenye mazingira mazuri yenye kuridhisha iliyopo karibu. Dereva alitii takwa hilo, alizunguka mitaa miwili na baadaye kupaki bajaji mbele ya hoteli nzuri, iliyojaa raia wengi wa kigeni. Walifanya malipo, wakataremka na kwenda mapokezi kuulizia huduma ambayo Upendo alidhamiria waipate. Chakula! Na mapumziko mafupi kabla hawajaendela na mambo mengine. Waliweka oda, chakula kikawasilishwa dakika nne mbele, na mhudumu mmoja wa kike, mrembo, aliyebarikiwa rangi adhimu duniani, nyeusi, yenye mng’ao wa kuvutia mtu yeyote amuonaye. Wanaume uchwara hawakusita kumeza mate pasipo kutarajia, kutokana na uchu uliowakaba kooni, uliowalazimisha kuzungusha macho kujiiba kumuangalia pindi wapitwapo, kuangalia maumbile yake ya nyuma yalivyojijenga. Hasa makalio (wowowo) yaliyoshindana kutikisika.
Mzee Matatizo, alikuwa muathirika wa maono hayo, punde tu alivyomuona, ijapokuwa umri ulishaanza mtupa mkono. Alichukuliwa muda wake mwingi kumshangaa, hadi alivyoshtushwa na Upendo aliyegundua hilo baadaye.
“Baba! Haya mambo ni ya vijana,” alisema Upendo, huku akipeleka moja ya mkono wake usoni kwa Mzee Matatizo kumzuia asiendelee kutazama.
“Dah! Duniani kuna mengi. Acha nishangae mwanangu. Kule kwetu hakuna kama hawa,” alisema Mzee Matatizo, akivuta kijiko na kuanza kula chakula walicholetewa.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa kumi na moja jioni, ndipo waliondoka hotelini hapo. Kuelekea Ubungo, ambako Upendo alikuwa amepanga chumba kwa ajili ya mambo yake ya hapa na pale, japokuwa muda mwingi alikuwa anapatikana kikosini. Walivyofika Mzee Matatizo alioneshwa mazingira ya nyumba yalivyo, kisha Upendo aliondoka kurudi kikosini. Kwa minajili ya kurejea siku husika ya kuianza safari. Ambayo ni siku ya pili toka hiyo. Kesho kutwa! Alivyowasili kikosini kwao alifanya maandalizi ya safari, pamoja na kupata ruhusa itayomfanya awe huru kwa siku kadhaa, zitazomwezesha kufanya mambo yake pasipo bughuza. Japo alikuwa mtu wa dini, aliyejaa wokovu, ila siku hiyo aliuvua wokovu na kuvaa ulaghai, lengo litimie kwa namna yoyote.
“Hapa lazima nifanikishe, kwani hii ndiyo nafasi ya pekee kwangu, itayokamilisha dhamira niliyonayo,” alijisemeza kimoyomoyo, pindi akikazana kutembelea nyumba za maofisa mbalimbali wanaohusika na kombania aliyopo.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment