Search This Blog

Friday, November 18, 2022

YAMENIKUTA SALMA MIE - 1

 






IMEANDIKWA NA : FAKI A FAKI



*********************************************************************************



Simulizi : Yamenikuta Salma Mie
Sehemu Ya Kwanza (1)


 MWANZO



Naitwa Ibrahim Amour. Ni mwenyeji wa Morogoro. Nilisoma morogoro hadi kidato cha sita. Nikafanikiwa kuingia chuo kikuu cha Mlimani jijini Dar es Salaam.

Nilipohitimu elimu ya chuo kikuu na kupata shahada yangu, nilifanikiwa kupata ajira mamlaka ya mapato TRA, nilifanya kazi kwa miezi michache tu nikahamishiwa Tanga.

Baada ya kuishi katika nyumba ya wageni kwa siku chache nilifanikiwa kupata nyumba ya kupangisha maeneo ya Usagara.

Wakati huo nilikuwa sijaoa bado na nilikuwa na mdogo wangu aliyemaliza kidato cha nne aliyekuwa amekaa nyumbani huko kwetu Morogoro. Nikamuita ili nikae naye pale nyumbani kwa sababu nilikuwa peke yangu.

Zacharia akaja Tanga baada ya kumtumia nauli. Nilikuwa pia na mpango wa kumtafutia kazi sehemu yeyote ambayo ningefanikiwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kwa vile bado nilikuwa mgeni katika jiji hilo nikaona nimsubirishe kwanza ili niweze kuzoeana na wenyeji ambapo ingekuwa rahisi kumuombea kazi sehemu yoyote.

Nikiondoka asubuhi kwenda kazini ninamuacha Zacharia nyumbani. Kwa kawaida nikiondoka asubuhi hurudi jioni.

Mara kwa mara Zacharia alikuwa akiniuliza kuhusu ule mpango wa kumtafutia kazi. Na mimi nilimjibu asubiri kwanza.

Baada ya miaka miwili nikafanikiwa kununua gari. Sasa nikawa naenda kazini na kurudi na gari langu. Miezi michache baadaye nikanunua kiwanja jirani tu na pale nilipokuwa naishi.

Wakati naanza kujenga msingi tu, nikapata matatizo kazini. Mimi na maafisa wenzangu watatu tulikamatwa na polisi tukidaiwa kujihusisha na wizi wa mapato ya serikali.

Tulisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi. Wakati uchunguzi unaendelea tulikuwa nje kwa dhamana. Baada ya uchunguzi huo kukamilika tulifikishwa mahakani.

Ilikuwa kesi iliyotuendesha sana. Iliunguruma kwa karibu miezi minane. Katika kipindi hicho nilikonda kwa hofu na wasiwasi wa kufungwa. Kwa bahati njema shahidi muhimu wa kesi ile ambaye angetoa ushahidi ambao ungeniweka mahali pabaya, alifariki dunia kwa maradhi ya sukari.

Hukumu ilipokuja kutolewa mwenzangu mmoja akaenda jela miaka saba. Mwingine alionekana hakuwa na hatia. Mimi nikaachiwa kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha.

Mwenzangu aliyeonekana hakuwa na hatia alirudishwa kazini. Mimi nikafukuzwa kazi kabisa.

Pia nilishukuru. Niliona bora kufukuzwa kazi kuliko kufungwa na ukitoka huko huna kazi.

Hata hivyo mpango wangu wa kuendeleza ujenzi wa nyumba yangu ambao nilikuwa nimeshauanza ukaishia hapo hapo.

Nilikuwa na akiba yangu benki nikaamua kuanzisha mradi wa kuchukua tenda za usambazaji vitu mbalimbali katika mashirika, taasisi na idara za serikali.

Nikafungua ofisi yangu jirani na maktaba. Baada ya kujitangaza katika maofisi mbalimbali nilifanikiwa kupata tenda ndogo ndogo lakini nikitegemea kuwa baadaye ningeweza kupata tenda kubwa kubwa.

Nilikuwa nikisaidiana na Zacharia na nilikuwa nimeajiri msichana mmoja aliyekuwa akibaki ofisini kwa ajili ya kazi ndogo ndogo kama vile kufungua ofisi asubuhi na kuifunga jioni, kupokea simu na kuhifadhi kumbukumbu zetu za kiofisi.

Siku moja nikashuhudia ajali karibu na ofisi yangu.

Msichana mmoja ambaye alikuwa akiendesha baskeli aligongwa na gari ndogo ambayo haikusimama.

Wakati tukio hilo linatokea mimi nilikuwa nikiondoka na gari langu ofisini kwangu. Nikalisimamisha gari karibu na mahali alipoanguka yule msichana na kuzirai.

Kitu kilichonishitua ni kwamba alikuwa akitokwa na damu nyingi iliyokuwa ikisambaa barabarani.

Baskeli yake ilikuwa imeanguka kando yake ikiwa imekunjwa kama iliyokanyagwa na treni.

Gari lililomgonga lilikimbia mara tu baada ya ajali kutokea.

Kutokana na kuona ile damu iliyokuwa ikitoka kwa wingi, nilizima gari nikashuka na kumfuata yule msichana. Sikuwaza hili wala lile, nilimzoa pale chini bila kujali damu iliyokuwa ikimtiririka ambayo ilikuwa ikiingia kwenye nguo zangu.

Nilimpakia kwenye siti ya nyuma ya gari langu, nikajipakia na kumuwahisha hospitali ya Bombo ambapo alipokelewa na kushughulikiwa.

Sikujua kama angepona kutokana na ile damu iliyokuwa ikimtoka kwa wingi, nikapwatwa na wasiwasi.



Wakati nimekaa nje ya chumba cha daktari nikiwaza, daktari alitoka na kuuliza.

“Aliyemleta huyu majeruhi aliyegongwa na gari ni nani?”

Hapo hapo nilishituka nikajua kuwa msichana ameshakufa.

Nilikuwa nimekaa na watu wengine wanne waliokuwa na shida zao. Nikainuka na kumjibu yule daktari.

“Ni mimi”

“Majeruhi amepoteza damu nyingi na anahitaji kuwekewa damu ili kuokoa maisha yake. Na hapa tumeishiwa na damu” akaniambia.

“Sasa tutafanyaje daktari?”

“La kufanya ni kupatikana damu kutoka kwa mtu yeyote, kwani ndugu zake wako wapi?”

“Siwatambui. Kama yangu itafaa niko tayari kumsaidia”

“Haya twende tukakupime kama unaweza kumtolea”



Daktari huyo alinipeleka katika chumba cha maabara. Nilitolewa damu yangu kwa ajili ya kuchukuliwa kipimo.

Niliambiwa kwanza ingechunguzwa ili kuonekana kama ilikuwa salama na kama nina damu ya kutosha kumpatia mtu mwingine.

Nilisubirishwa kwa karibu saa nzima kabla ya kuambiwa kuwa damu yangu ilikuwa salama na nilikuwa na uwezo wa kumtolea yule msichana.

Nilifurahi sana nilipoambiwa hivyo kwani muda wote nilikuwa nikimsikitikia msichana huyo.

Kikubwa kilichokuwa kikinisikitisha ni kwamba sikutaka afe. Baada ya damu yangu kutolewa nilipewa kikombe cha chai ya maziwa ili kiniweke sawa.

Wakati nakunywa chai, damu niliyotoa ilipelekwa katika chumba alichokuwa

yule msichana. Baadaye kidogo polisi wa usalama barabarani wakafika.

Nilikuwa nimeshamaliza kunywa chai na polisi hao walikuwa wameshapewa maelezo na wafanyakazi wa hospitali.

Wakanitaka na mimi niwape maelezo, nikawaeleza jinsi ajali ilivyotokea na jinsi nilivyomchukua huyo msichana na kumleta hapo hospitali.

“Tumeambiwa kuwa alikuwa anahitaji kuwekewa damu na uliamua kumsaidia?” Polisi mmoja akaniuliza.

“Ndiyo nimemtolea damu”

“Sijui kama unamfahamu huyu msichana?”

Nikatikisa kichwa.

“Kwa kweli simfahamu”

“Je ile gari iliyomgonga uliiona?”

“Ndiyo niliiona”

“Unaweza kututajia aina yake na namba yake ya usajili”

“Ni Toyota ya rangi nyeupe. Namba yake ya usajili sikuiona yote. Niliona namba za mwanzo tu”

“Tutajie hizo hizo”

Nikawatajia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Umetusaidia. Kuna mtu aliona namba zinazofuatia. Mtu mwingine alikariri tarakiu zote. Sasa tutakuwa tumepata namba kamili. Ninaamini tutalikamata hili gari muda usio mrefu”

“Mkimpata huyo dereva ni vyema anyang’anywe leseni kabisa. Ni dereva katili sana”

“Tukimpata tutamfikisha mahakamani. Mahakama ndio yenye uamuzi”

“Sawa”’

Baada ya kuzungumza na polisi hao daktari alinifuata na kuniambia kuwa ninaweza kuondoka kwani majeruhi niliyempeleka anaendelea kuwekewa damu.

“Ameshazinduka?” nikamuuliza.

“Hajazinduka bado lakini tunatarajia kuwa atazinduka muda si mrefu. Tunaendelea kumfanyia uchunguzi kuona kama ameumia kwa ndani”

“Sawa. Nitakuja kumuangalia kesho asubbuhi”

“Vizuri”

Wakati natoka hapo hospitali jua lilikuwa limeshakuchwa. Nilimpigia simu Zacharia nikamuuliza.

“Uko wapi?”

“Niko ofisini?”

“Hamjafunga ofisi bado?”

“Ndio tunataka kufunga”

“Basi fungeni, mimi sitafika tena huko. Tutakutana nyumbani”

“Sawa kaka”

Nikajipakia kwenye gari na kurudi nyumbani.

Asubuhi ya siku ya pili yake nilipotoka nyumbani nilikwenda hospitali ya Bombo kumjulia hali yule msichana.

Nilifurahi kumkuta akizungumza na muuguzi aliyekuwa akimhudumia.

“Oh kaka umefika tena?” yule muuguzi aliniuliza akikumbuka kwamba ndiye mimi niliyemleta hospitali yule msichana jana yake.

“Ehe nimefika kumjulia hali mgonjwa wangu” nikamjibu huku nikitabasamu.

“Mgonjwa wako anaendelea vizuri, Jana tumemuwekea damu na jana hiyo hiyo alizinduka”

Wakati nikizungumza na yule muuguzi yule msichana alikuwa akinitazama kwa macho ya shauku na udadisi.

“Salma huyu ndiye yule kaka aliyekuleta hospitali” Muuguzi huyo akamwambia.

Msichana huyo akashituka.

“Ndiye huyu kaka? Nimefurahi kumuona”

Msichana akanitazama kwa macho ya bashasha na kuniammbia.

“Asante kaka, nnakushukuru sana kwa msaada wako. Mungu atakulipa”

“Ni watu wachache sana duniani wenye moyo kama wake, kuacha shughuli yake na kukushughulikia wewe mtu ambaye hakufahamu na zaidi ya hapo akutolee damu iliyoweza kukusaidia hadi leo unajisikia vyema” Yule muuguzi akamwambia.

“Ni moyo wa kibinaadamu kweli kweli. Kwa kweli namshukuru sana. Mimi sina cha kumlipa ila Mungu ndiye atakayemlipa”

“Asante mdogo wangu kwa shukurani zako. Nimekuja kukujulia hali nijue unaendeleaje kwa sababu jana niliondoka ukiwa bado hujitambui”

“Kwa kweli kaka naendelea vizuri, nashukuru Mungu”

“Mimi naitwa Ibrahim Amour, ni mkazi wa Usagara hapa Tanga, sijui wewe mwenzangu unaitwa nani?”

“Naitwa Salma Aboud”

“Unaishi wapi?”

“Ninaishi Chumbageni”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Unaishi na wazazi?”

“Ninaishi na mama yangu, Baba yangu alishafariki”

“Kwa hiyo mama ako anayo taarifa kuwa umepata ajali?’

“Mama hayuko, amekwenda kijijini tangu juzi”

“Basi atakuwa hana habari”

“Atakuwa hajui”

“Alikwambia angerudi lini?”

“Atakuwa huko kwa wiki nzima”

“Si kitu, nitakuachia namba yangu ya simu, ukiwa na tatizo unaweza kunipigia”



Nilimuandikia namba yangu ya simu na kumuachia. Kwa vile yeye hakuwa na simu, sikuwa na haja ya kuomba namba yake.

Baada ya hapo nilitoa shilingi elfu hamsini nikampa.

“Hizi zitakusaidia kwa matumizi madogo madogo ukiwa hapa hospitalini” nikamwambia.

Msichana alipokea pesa hizo na kunishukuru.

“Asante kaka”

Yule muufuzi aliondoka na kutuacha.

“Hivi kaka ile baskeli niliyokuwa naendesha uliiona?”

“Baskeli yako itakuwa imechukuliwa na polisi. Ukitoka hapa unaweza kuifuata kituo cha polisi cha Mabawa”

“Asante kaka”

Baada ya hapo niliagana na yule msichana. Nilimuahidi kumtembelea tena siku itakayofuata.

Wakati natoka nje ya hospitali niliona polisi wa usalama barabarani wakisimamisha gari lao. Nikajua walikuwa wamemtembelea yule msichana.

Nikajipakia kwenye gari langu na kuondoka.



Zilipita siku tatu, sikufika kule hospitali kutokana na kubanwa na majukumu yangu. Siku ya nne yake nikafika kumjulia hali yule msichana.

Lakini nilikuta kitanda kikiwa na mgonjwa mwingine. Kulikuwa na muuguzi aliyekuwa akimpa dawa mgonjwa huyo.

Nikawasalimia wote wawili kisha nikamuuliza yule muuguzi kuhusu yule majeruhi wa ajali ya gari.

“Unamuulizia Salma?” Muuguzi huyo akaniuliza lakini kabla sijamjibu akaniambia.

“Salma alishapewa ruhusa tangu jana”

“Kumbe…!”

Nikaduwaa kidogo kisha nikamuaga muuguzi huyo na kuondoka.

“Kama amepata nafuu ndivyo nilivyokuwa ninamuombea” nikajiambia huku nikijipakia kwenye gari langu.

Nililiwasha moto na kuondoka.

Ikapita wiki nzima. Nilikuwa ninaendesha gari langu nikitokea gereza la Maweni ambako nilikwenda kuchukua hundi ya malipo yangu, simu yangu iliyokuwa kwenye mfuko wa shati langu ilipoita.

Nilitumia mkono wangu wa kushoto kuitoa na kutazama namba iliyokuwa inanipigia. Sikuweza kuitambua. Ilikuwa namba ngeni.

Nikajiuliza haraka haraka ni nani? Sikupata jibu. Nikabonyeza kiwambo cha kupokelea na kuiweka simu karibu na sikio.

“Hello!”

“Hello! Bila shaka nazungumza na Ibrahim Amour?” Sauti laini ya kike ikaniuliza kwenye simu.

Nikajikuta nazungusha akili yangu kujiuliza alikuwa nani.

“Ndiye mimi, nani mwenzangu?” nikamjibu.

“Naitwa Salma Aboud!”

Kusema kweli moyo wangu ulishituka.

Hapo hapo nikamkumbuka msichana aliyekuwa amegongwa na gari wiki moja iliyopita.

“Wewe ndiye yule msichana uliyepata ajali?” nikamuuliza.

“Ndiye mimi. Nilishapewa ruhusa hospitali, samahani kwa kuchelewa kukujulisha. Najua huenda ilikusababishia usumbufu kidogo…”

“Ni kweli, nilifika hospitali nikaambiwa kuwa uliondoka jana yake. Vipi hali yako?”

“Kwa sasa sijambo kidogo”

“Unaendelea vizuri?”

“Nashukuru Mungu, ninaendelea vizuri”

“Nakumbuka uliniambia unaishi Chumbageni, ndipo ulipo hivi sasa?”

“Ndiyo niko nyumbani Chumbageni”

“Ile baskeli yako uliipata?”

“Sijakwenda kituo cha polisi kuifuatilia”

“Natumaini itakuwa bado iko. Siku ukipata nafasi unaweza kwenda kuichukua”

“Sawa kaka. Asante. Kwa mara nyingine nakushukuru sana kwa msaada wako. Ukipata nafasi unaweza kunitembelea nyumbani, mama yangu atafurahi sana atakapokuona. Nilimueleza jinsi ulivyonisaidia”

“Vizuri. Nitatafuta siku ya kuja kukuona”

“Sawa. Asante sana kaka”

“Asante”

Msichana akakata simu.

Nikairudisha simu mfukoni..

“Salma bado ananikumbuka” nikajiambia kimoyomoyo wakati nikikata kona kuelekea benki.

Siku zikaendelea kupita.

Kulikuwa na siku nilikuwa nikiendesha gari langu mitaa ya Chumbageni. Kulikuwa na jamaa niliyekuwa nimemfuata. Sasa wakati narudi ofisini kwangu nikamkumbuka Salma ambaye aliniambia alikuwa anaishi Chumbage. Nikaliegesha gari langu pembeni mwa barabara kisha nikatoa simu yangu na kumpigia.

“Hello Salama!” nikasema mara tu simu ilipopokelewa.

“Kaka Ibrahim. Nimefurahi kuwa leo umenipigia”

“Niko maeneo ya Chumbageni, nataka nikujulie hali?”

“Oh! Uko upande upi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

‘Niko hapa karibu na shule ya chekechea”

Salma akanielekeza nyumba yao ilipo. Haikuwa mbali sana na pale. Nikafika.

Nilishuka kwenye gari. Nilimkuta amesimama mlangoni akinisubiri.

“Oh karibu” alliniambia huku akitabasamu.

Nilikwenda kwenye mlango, Salma akanikaribisha ndani.

Nilipita ndani. Upande wa kushoto wa nyumba hiyo kulikuwa na sebule pana iliyokuwa imepambwa vizuri.

“Karibu ukae” Salma akaniambia. Tabasamu lilikuwa likiendelea kuchanua usoni kwake.

Nikakaa kwenye kochi mojawapo.

“Ngoja nimuite mama, anataka kukuona”

Salma aliingia ndani. Nikabaki nikiyazungusha macho yangu kwenye sebule hiyo.

Punde tu Salama alirudi akiwa amefuatana na mwanamke mmoja. Kwa mimi mwenyewe nisingeweza kuamini kama yule alikuwa ni mama yake kwani alionekana bado msichana. Na walionekana kama mtu na mdogo wake.

“Mama yule kaka aliyenisaidia siku ile kunipeleka hospitali na kunitolea damu ndiye huyu hapa” Salama alimwambia mama yake.

“Baba unajisikiaje hali yako?” Mama huyo akaniuliza kwa furaha.

“Sijambo mama. Shikamoo”

“Marahaba. Habari za siku”

“Ni nzuri, sijui nyinyi hapa”

“Sisi hatujambo. Tunashukuru Mungu”

“Kaka Ibrahim, huyu ndiye mama yangu” salma akaniambia huku akiketi.

“Nimefurahi kumuona”

“Leo umeamua kututembelea…” mwanamke huyo aliendelea kuniambia. Alikuwa bado amesimama na hakuonesha dalili yoyote kuwa angeketi.

Baada ya kuulizana naye hali akatuambia.

“Haya endeleeni kuzungumza, mimi niko huko uani nina kazi kidogo”

“Asante, hata hivyo sitakaa sana. Nimekuja mara moja tu kumjulia hali mgonjwa wangu kisha nitaondoka”





Mama huyo alicheka niliposema ‘mgonjwa wangu’

“Haya nawaacha kidogo”

Akaondoka.

“Nikupatie kinywaji gani kaka?” SALMA akaniuliza.

“Hapana, sihitaji kinywaji chochote”

“Kwanini, tunayo juisi ya parachichi”

“Nitakuja kunywa siku nyingine, usijali”

Tukaendelea kuzungumza kwa karibu nusu saa. Wakati nataka kuondoka nilimuachia Salma shilingi elfu hamsini.

“Hizi zitakusaidia kununua vitu vidogo vidogo” nikamwambia.

“Asante kaka, nashukuru”

Salma alikwenda kumuita mama yake ili niagane naye. Mama huyo alipokuja akanishukuru kwa mara nyingine kwa msaada nilioutoa kwa mwanawe siku alipopata ajali.



Jina langu ni Salama Aboud, nilikuwa mtoto wa tatu wa mzee Aboud ambaye alifariki dunia wakati mimi nikiwa darasa la saba.

Katika kipindi chote hicho nilikuwa nikiishi na mama yangu ambaye alikuwa akinipenda na kunidekeza sana.

Kutokana na utoro wangu wa shule nilishindwa kuendelea na masomo ya sekondari. Niliacha masomo nikiwa kidato cha tatu. Vile mama yangu alikuwa anashindwa kunikemea na kwa vile hakukuwa na mtu mwingine wa kunisema kitu, basi nilifanya vile nilivyotaka mimi.

Kaka zangu walionitangulia mmoja alikuwa amefariki, wawili walikuwa wakikaa Dodoma kwa baba mdogo.

Siku ile niliyopata ajali walikuja Tanga kunijulia hali kisha waliondoka kurudi Dodoma.

Sikujua ni kitu gani kilichofanya nimzowee sana Ibrahim. Pengine ni kutoka na wema alionifanyia siku ile nilipopata ajali. Kwanza nilimchukulia kama msamaria mwema lakini mazoea yetu yalipozidi nilianza kumpenda na nikawa na hisia ya kuishi na mtu kama Ibrahim.

Nilivutiwa sna na staili yake ya maisha na tabia yake. Lakini Ibrahim hakuwa akionesha kutambua mawazo yangu. Jambo hilo lilikuwa likinikera sana. Kusema kweli nilikuwa ninatamani tuwe wapenzi.

Usishangae kwamba nilikuwa nikiwaringia sana wanaume. Walitokea wanaume wawili waliotaka kunioa nikawakataa bila sababu yoyote.

Mama yangu kwa kufuatisha mawazo yangu, naye aliwatolea nje.

Mara kwa mara mama alikuwa akiniuliza.

“Utaolewa lini mwanangu, wenzako wote wameolewa?”

“Hao walioolewa waache waolewe, mimi niache tu”

“Sasa utakaa hivi hivi mpaka lini?”

“Kwani kuna mume aliyekwambia ananitaka nikamkataa?”

“Si walikuja vijana wawili ukawakataa mwanangu”

“Bado unawakumbuka tu”

“Nawakumbuka kwa sababu sioni dalili ya kutokea mume mwingine, naona kama umejitia nuksi”

“Muda wangu wa kuolewa ukifika nitaolewa tu mama”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Haukupita muda mrefu ndipo alipojitokeza Ibrahim.

Ibrahim nilimuonesha dalili zote za mapenzi kwani haikuwa rahisi kwangu mimi mwanamke kumueleza wazi kuwa nimempenda.

Siku moja nikaukata mzizi wa fitina. Nilimtumia meseji nikamwambia.

“Natamani ningekuwa mke wako Ibrahim”

Akarudisha jibu na kuniuliza.

“Kwanini?”

Nikamtumia meseji nyingine ya kumwambia.

“Nimependa tabia zako”

Akanijibu tena kwa kuniambia.

“Kama ungependa tuoane subiri nijiandae”

Kwa sababu nilikuwa nampenda, jibu lake hilo likanifurahisha.

Siku ya pili yake tulikutana katika hoteli moja tukazunguza sana kuhusu mapenzi.

Akaniambia yeye ni muangalifu sana katika kutafuta mchumba lakini katika siku chache tulizokuwa pamoja amegundua kuwa ninafaa kuwa mchumba wake. Ibrahim hakujua alikuwa amenifurahishaje kutokana na kauli yake hiyo.

Dhamiri yetu ikatimia. Baada ya kuzungumzia uchumba kwa wiki kadhaa, hatimaye Ibrahim akaleta barua ya uchumba kwa mama yangu.

Mama yangu aliipokea kwa mikono miwili kwa sababu nilishamueleza jinsi nilivyokuwa ninampenda Ibrahim.

Mama alimfahamisha baba mdogo aliyekuwa Dodoma kuwa kumeletwa barua ya uchumba ya Salma.

Baba mdogo akanipigia simu kuniuliza kama nimempenda huyo mchumba.

“Nimempenda ndio maana nilimuelekeza aje kwetu” nikamjibu.

“Nimesikia kuwa ndiye yule aliyekusaidia ulipopata ajali?”

“Ndiye yeye”

“Imekuwa heri. Huyo ni mchumba mwema. Mimi pia nimemkubali”

Baada ya baba mdogo kuzungumza na mimi alimpigia mama akamwambia kuwa na yeye amekubaliana na huo uchumba.

Mbali ya kumjulisha baba mdogo, mama pia aliwajulisha wajomba, yaani ndugu zake. Wote wakaukubali uchumba huo na jibu likapelekwa kwa Ibrahim kuwa uchumba wake umekuwa makubuli, yaani umekubaliwa.

Sasa ikawa ni mipango ya harusi. Mipango ya harusi yetu ilichukua karibu miezi mitatu. Nataka niseme ukweli kuwa tangu nijuane na Ibrahim mpaka tunakuwa wachumba sikuwahi kutembea naye hata siku moja.

Mimi sikutaka jambo hilo kwa sababu baadhi ya wanaume ukishatemmbea nao hubadili mawazo na kutafuta wachumba wengine.

Ibrahim pia hakuonesha kuwa na uchu wa wasichana. Alipoona dhamiri yangu ilikuwa ni kuoana, hakuwahi hata siku moja kunishawishi tufanye kitu.

Kwa hilo peke yake nilimsifu na kuona alikuwa mwanaume madhubuti aliyeweza kuuzuia moyo wake. Ni wanaume wachache sana wenye tabia kama ya Ibrahim.

Ndoa yetu ilifungwa siku ya ijumaaa saa saba na nusu. Ilifungwa katika msikiti wa Chumbageni baada ya mshuko wa swala ya ijumaa.

Mimi nilikuwa niko nyumbani nikimsubiri mume atoke msikitini. Tangu asubuhi nilikuwa saluni nikipambwa na kuchorwa piko. Nilirudishshwa nyumbani saa sita.

Nilipelekwa saluni nikitokea kwa kungwi ambako nilikaa kwa wiki maja nikifundwa jinsi ya kuishi na mume.

Nakumbuka somo moja muhimu nililolipata kwa kungwi ni kuwa nisimnyime mume wangu anapotaka penzi hata kama niko jikoni napika.

“Acha kazi zako ukamridhishe mumeo” kungwi wangu aliniambia.

Ibrahim aliporudi nyumbani kutoka msikitini alifuatana na watu watatu mmojawapo akiwa sheikh aliyetuozesha.

Ibahim alinipa mkono mke wake. Na hii ni kawaida. Mume akishakuoa akiingia chumbani hukupa mkono.

Sheikh akatuombea dua na kututaka tuishi maisha marefu, tupate watoto wema, tuishi kwa upendo na kuaminiana. Lakini akaongeza sentesi moja mabayo sikuipenda. Alisema.

“Mvumiliane, msameheane, muaminiane lakini kama itatokea mnaachana muachane kwa wema”

Kichwa changu kilikuwa kimefunikwa kwa mtandio unaoonya. Sheikh aliposema hivyo, niliinua uso wangu niliokuwa nimeuinamisha chini. Nikamtupia jicho Ibrahim huku yale maneno, “Kama itatokea mnaachana muachane kwa wema…” yakipita akilini mwangu.

Wakati namtupia jicho Ibrahim nilikuwa kama namuuliza. “Hivi tutakuja kuachana mimi na wewe?”

Moyoni mwangu sikutarajia kwamba hilo lingeweza kutokea kwa vile sheikh alishatuambia tuvumiliane, tusameheane na tuaminiane.

Niliamini kwa falsafa ya kuvumiliana, kusameheana na kuaminiana, suala la kuachana lingekuwa mbali sana na ndoa yetu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Baada ya sheikh kutuombea dua hiyo, sherehe za ndoa yetu zikaendelea hadi usiku wa manane. Lakini mimi na Ibrahim tuliondoka mapema kwenda nyumbani kwake Usagara.

Usiku wa siku ile ndio kwa mara ya kwanza, mimi nilimjua Ibrahim na yeye alinijua mimi kwa maana kwamba ndio tulikutana kwenye sita kwa sita.

Baada ya kitendo hicho cha siku ya kwanza, ndio nilimpenda zaidi Ibrahim na naamini hata yeye alinipenda zaidi.

Ibrahim na mimi tukawa tumefungua ukurasa mpya wa maisha.

Maisha ya siku za mwanzo mwanzo yalikuwa ya upendo sana. Ibrahim akitoka katika shughuli zake hurudi nyumbani. Kadhalika na mimi sikuwa mtu wa kutoka toka wala wa kwenda kwa majirani.

Na hilo ni funzo nililolipata kwa kungwi wangu kuwa nikiwa kwa mume wangu niachane na safari zisizokuwa na msingi na pia niepukane na mashoga na majirani wasio wazuri.



Jirani yangu mmoja wa nyumba tuliyopakana nayo upande wa kushoto alihama nyumba, akaja mpangaji mwingine, mtu mmoja na mke wake.

Huyo mwanaume alikuwa mtu mzima kidogo, alifikia umri wa miaka hamsini wakati mke wake alikuwa bado msichana ila alikuwa amenizidi mimi kidogo kwa umri.

Baada ya kuishi na majirani hao kwa mwezi mmoja nikajikuta nimependa staili yao ya maisha. Kila mmoja wao alikuwa na gari. Mume mtu alikuwa na gari lake na mke naye alikuwa na gari lake.

Aliyekuwa akifanya kazi ni mume, mke alikuwa yuko nyumbani tu wakati wote. Lile gari alikuwa akilitumia kwenda sokoni au kwenda safari zake nyingine.

Mwanaume huyo anapoondoka nyumbani asubuhi hurudi jioni na anaporudi huwa hatoki tena. Vicheko vyao wakati wa usiku vilikuwa vikisikika hadi ndani kwetu.

Taratibu nilijikuta nikizooeana na mke wa huyo jamaa.

Kulikuwa na siku kulikuwa na tatizo la kukatika maji. Msichana huyo akaja nyumbani kwangu asubuhi na kubisha mlango.

Niliposikia mlango unabishwa nilikwenda kuufungua nikamkuta amesimama mbele ya mlango.

“Mmeamkaje jamani?” akanisalimia.

“Hatujambo, sijui wewe” nikamjibu.

“Samahani jirani yangu, nataka kukuuliza huku kwenu maji yanotoka?”

“Hayatoki” nikamjibu na kuongeza.

“Yalikatika tangu jana usiku”

“Basi mwenzako sina habari kuwa maji yamekatika, nafungua bomba nakuta tupu. Mume wangu anataka ajimwagie aende kazini. Hukuweka akiba kidogo ukanigaia”

“Nina tenki la juu, huwa naweka akiba ya maji. Maji yanapokatika sipati taabu”

“Mh mwenzangu umenizindua. Nitamwambia mume wangu naye anunue”

“Sasa lete ndoo uje umchotee”

“Asante jirani, ngoja nikachukue ndoo”

Msichana huyo aliondoka. Nilifunga mlango nikaenda kufungua mlango wa uani na kumsubiri.

Alipotokea nikamuita.

“Njoo kwenye mlango huu”

Msichana huyo akaingia katika mlango huo wa uani. Nilikwenda naye kwenye bomba nikamwambia aweke ndoo yake. Nikamfungulia maji.

Ndoo yake ilipojaa akaniambia.

“Unanipa ndoo hii moja au nije unipe ya pili, kwa maana hii ataoga mume wangu, bado mimi sasa…”

“Na ya kupikia je…?” nikamuuliza.

“Hapo sasa!”

Tukacheka.

“Nakwambia hawa watu wa idara ya maji nao watatupa shida!” akaniambia.

“Njoo uchote shoga yangu usijali, leo kwangu kesho kwako”

“Ngoja nipeleke hii kwanza…”

Msichana huyo alibeba ile ndoo akatoka. Niliingia ndani nikaendelea na shughuli zangu. Punde tu nikamsikia akiniita.

“Jirani nimerudi!”

“Chota tu, nina kazi kidogo” nikamwambia.

“Asante jirani”

Niliendelea na kazi zangu. Baadaye nikamsikia tena.

“Nachota hii ya tatu”

“Chota tu” nikamwambia.

Alipomaliza kuchota aliniambia.

“Haya jirani asante, nakwenza zangu”

“Haya jirani”

Kutoka siku ile ndipo nilipoanza urafiki na jirani yangu huyo. Alikuwa akija nyumbani kwangu kuzungumza na wakati mwingine mimi nilikuwa nakwenda nyumbani kwake. Nikalifahamu jina lake. Alikuwa anaitwa Rita..

Rita akawa rafiki yangu mkubwa, tukafikia hadi kuazimana nguo na vitu vingine na pia tulipeana siri zetu za ndani.

Kutokana na urafiki wetu huo niliweza kugundua kuwa maisha aliyokuwa akiishi Rita na mume wake hayakuwa kama maisha niliyokuwa ninaishi mimi na mume wangu.

Wenzetu walikuwa wanaishi maisha ya hali ya juu na ya kifahari. Rita alikuwa akiniambia kila kitu alichohitaji, mume wake alikuwa akimtimizia. Alihitaji gari akamnunulia. Na wakati ule tunaanza kufahamiana alikuwa akimjengea nyumba maeneo ya Kange.

“Mume wangu si mgumu, ananisililiza na kunijali” Rita aliniambia na kuongeza.

“Kila ninachohitaji ananipatia”

“Basi una raha shoga yangu. Umepata mume mzuri. Wangu mimi ukitaka kitu mpaka kwa mbinde”

“Lakini hata huyu wangu aliponioa alikuwa hivyohivyo, nilifanya kumtengeneza”

Nikashituka.

“Ulimtengenezaje shoga?”

“Nilimuendea kwa mganga nikamlisha madawa mpaka yakamkolea”

“Wacha shoga!. Kumbe kuna madawa yanayoweza kubadili tabia ya mwanaume?”

“Yapo. Si unamuona mume wangu alivyo. Sasa nakwambia hakuwa hivi! Kuninunulia nguo ilikuwa ni mpaka tugombane”

“Wangu mimi hatugombani, ni mgumu tu. Kila siku yeye hana pesa lakini biashara anafanya. Sijui pesa zake zinakwenda wapi!”

“Basi ana mwanamke nje, ndiye anayemla. Mwenzangu wala chuya, mchele waliwa na mwenzio!”

Rita aliponiambia hivyo alinicheka na mimi nikajidai kucheka lakini moyo wangu ulipata fadhaa sana nilipohisi kuwa inaweza kuwa ni kweli mume wangu akawa na msichana wa nje anayekula pesa zake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Siku ile niliwaza sana yale maneno aliyoniambia shoga yangu.

Mume wangu aliporudi jioni nilijaribu kumwambia.

“Mume wangu huninunulii hata pikipiki na mimi”

“Unataka pikipiki ya nini mke wangu?”

“Pikipiki ya nini? Watu wananunuliwa magari, wewe unasema pikipiki ya nini?”

“Kama ni gari si hili tunalo”

“Hilo ni la kwako. Mimi nataka pikipiki”

“Tuombe Mungu, kazi zangu zikienda vizuri nitakununulia”

“Utaninunulia lini?”





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog