Simulizi :Iangalie Tuleane
Sehemu Ya Nne (4)
Kwa mzee Kasoyaga na Tualike ni shangwe tu ndizo zilitawala. Fitina waliyopanga ilifanikiwa, hivyo waliuona mwisho wenye mafanikio huku ukiwa mwanzo wa kuunda mbinu nyingine itakayowahakikishia ushindi.
“Aliyebaki ni mzee Kumwembe.”
“Tunamfanyaje huyu mtu?”
“Akishindwa kukutangaza tunamuondoa duniani, la sivyo kumbambikia kesi ya uhujumu uchumi—kwa matumizi mabaya ya fedha ya umma,” mkakati mpya uliopangwa na mzee Kasoyaga, yote kuhakikisha ushindi unaenda kwa mzee Tualike, ili naye asifanyiwe kitu kibaya kwa kuona kwamba hajamsaidia wakati kipindi cha nyuma alishasaidiwa.
“Hapo sahihi, na ahakikishe hawa wa mtaa, wengi wao awatangaze wale wanaoniunga mkono, akishindwa namfukuza na kumfungulia hiyo kesi,” mzee Tualike naye alichangia hoja.
“Ondoa shaka.”
Mapema tu, mpango mkakati huo ukawasilishwa mezani kwa mzee Kumwembe, Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi, na walinzi wa siri wa mzee Kasoyaga, Morad na Sabaya. Japo lilikuwa jambo la kawaida kwa upande wake, kwani hata kipindi kilichopita alifanyiwa kitu hiki, ila awamu hii kidogo ilimtisha. Na kilichofanya atishike, ni kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi wa kijiji asipotekeleza matakwa yao. Alipata wakati mgumu sana, namna gani atafanikisha, aendeleze ulaji wa pesa ya serikali itokanayo na kodi za wanatuleane. Kichwa kilifikiria mbinu tu, toa hii weka ile lakini hakupata mbinu sahihi yenye kumuwezesha kutoa ushindi kwa mzee Tualike kama wao walivyohitaji. Hadi anarudi nyumbani kwake, hakupata mbadala, zaidi ya kuchosha akili na mwili kwa ujumla kutokana na ufikiriaji.
Hali hiyo iligunduliwa na familia yake, mkewe na mwanaye wakiume, japo alijitahidi kuificha mwishowe ilishindikana kufichika. Kitu kilichomfanya ashindwe ni usonyaji wa kila baada ya dakika. Alikuwa akijiongelesha, jambo lililomshawishi mkewe avunje ukimya amuulize.
“Washaanza tena hao watu wako?”
“Hapana!”
“Ila shida nini?”
“We acha tu,” alijibu mzee Kumwembe akifuta uso wake.
Jibu kuwa “acha tu” moja kwa moja likamtambulisha mkewe kilichomsibu mumewe. Alifahamu kuwa tayari alipewa vitisho kuhusiana na zoezi lililoko mbele yao, jambo lililompa naye mfadhaiko kwa muda. Mfadhaiko huo ulimpa hasira na chuki nzito kwa watoa vitisho wanaofanya familia yake ikose amani.
“Awamu hii, hapana. Siwezi vumilia huu upuuzi. Lazima niwaoneshe kuwa wenye Kijiji ni wanakijiji, kwani wao nani hadi wajifanye waamuzi wa kila kitu hapa kijijini? Kama wanamtumia muwe wangu washinde, basi uchaguzi huu nitahakikisha unakuwa huru na wa haki. Wakihitaji ushindi wa magumashi watumie hao mgambo wao, wanaotii maelezo pasipo kufikiria baada ya hapo wananufaika na nini,” alisema mkewe, mzee Kumwembe kimoyomoyo
Ahadi aliyojiwekea alihitaji iwe ya kweli ili amsaidie mumewe ambaye amekuwa kibaraka kisa tu kulinda ulaji wake huku akisahau kipindi cha nyuma hakutaraji kuwa katika nafasi hiyo. Ama amesahau pia kuwa maisha hutengenezwa na nyanja mbalimbali si kwa fedha za mshahara pekee zitolewazo na serikali, baada ya makusanyo kutoka kwa wananchi.
Naam. Kwa kuanza, aliwasiliana na wakili msomi, Dkt. Emmakulata, atumiwaye na wanaharakati wanaopingana na matendo maovu yatendwayo na serikali. Kama vile utekaji, unyanyasaji, mauaji, vitisho, rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka yasiyo jali utu na hekima. Haya yote wakitendewa wananchi, watoao mamlaka ya hao wanaohusudu mambo hayo.
Akampatia maelezo ya kina, kuanzia matendo ya mihula ya nyuma hadi huo unaoelekea kutimia huku akimuahidi kumtafutia ushahidi wa kipindi wanachoelekea ili iwe rahisi kukabiliana pale Tualike atakapofanikiwa kuingia ofisi kuu. Dhahiri alionekana kuchoshwa na matendo hayo yaliyokomaa hadi kufikia hatua ya kurithishana tawala na tawala. Alithubutu kutovumilia mara nyingine. Alitaka Wanatuleane wasiingie mikononi mwa wanyama washindwao kumthamini anayewapatia ulaji kwa sababu ya ulevi wa madaraka.
“Huu si wakati wa kukaa kimya. Ni wakati wa kupaza sauti, Wanatuleane waamke kukataa utumwa endelevu unaozalishwa kila uchao. Mume wangu kashiriki kwa muda mrefu kuwanyima haki wanatuleane kwa kutangaza matokeo tofauti na maamuzi ya wanakijiji, lakini awamu hii nahitaji iwe mwisho. Mimi, nikiwa kama mwanatuleane, nipo tayari kuanzisha mageuzi ya kijiji chetu kwa manufaa ya kizazi kijacho,” alisema mke wa mzee Kumwembe wakati akiwasiliana na Dkt. Emmakulata.
“Pongezi kwako mama kwa kutambua thamani yako kama mwanatuleane unayehitaji serikali inayojali maslahi ya wanakijiji wake,” Dkt. Emmakulata naye alichangia hoja.
“Nashukuru. Naomba tukamilishe hili kwa pamoja.”
“Usijali, hilo limetimia.”
Maongezi yakaisha!
Mara baada ya maongezi kumalizika, alimfuata mumewe, sebuleni alipokuwa ameketi. Mkononi akiwa kakamatia kilongalonga cha kisasa “smartphone” akiwa kabonyeza programu ya kurekodi sauti. Alipomfikia aliketi karibu naye, na kuanza kumchombeza maswali ya hapa na pale kuhusu alivyoambiwa. Mzee Kumwembe hakuwa na la kuficha, aliamua kufunguka kuanzia mwanzo hadi mwisho, na kumthibitishia zaidi alimpigia simu Mzee Kasoyaga kumtaarifu hatua aliyofikia katika mfumo wa kipaza sauti (Loud speaker). Kitendo kilichomruhusu mkewe aendelee kurekodi mawasiliano yao. Maongezi yalivyomalizika naye akazima ile programu wajadiliane namna ya kujinasua ili jamii impate kiongozi wa halali.
“Usijali maslahi yako tu, angalia na maslahi ya wengine. Huna budi kuungana nami tuwakomeshe, hawapaswi kuvumiliwa hawa watu, umenielewa?”
“Sawa, nakuelewa. Ila sio kwa haraka namna hiyo.”
“Hapana! Wakati ni sasa.”
Majadiliano yao yalichukua muda mrefu kufikia tamati, karibia masaa mawili. Urefu huo wa mazungumzo na yote ni kwa sababu ya mzee Kumwembe kutokuwa mwepesi wa kuelewa kile alichoshauriwa. Baada ya maelezo ya kina kutoka kwa mkewe, akakubali na kuahidi kuachia ngazi katika bodi ya uchaguzi baada ya awamu hiyo kumalizika. Akatoa pendekezo la kuundwa kwa bodi mpya yenye kutetea na kuzithamini hisia na maamuzi ya wanakijiji, na si watawala.
___________
Kila walichopanga kilikuwa sawa, tena tayari kadri ya matakwa yao. Waliingia ndani ya gari ili kuinza safari. Wakiwa bado hawajatoka, ghafla kauli za watu wawili walioketi viti vya nyuma walilalama kuchoka ili tu waahirishe safari ile. Haikukataliwa, kweli safari iliyokuwa tayari ilibidi kupigwa tarehe na kusogezwa mbele.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MJM Zimbwa hakuwa na chembe ya mashaka juu ya kilichojiri kwa kuwa naye miaka ya nyuma alikuwa sehemu ya watendaji hivyo alikuwa na ufahamu wa kilichoendelea na nini kinaweza kutokea mambo yakiwa magumu zaidi alijua. Pia kitendo cha mwanasheria wake kutumika kuwatetea, alifahamu anaweza kuundiwa zengwe ama kumshawishi aitumikie serikali idara yoyote ile, hata ya uwakilishi wa kijiji nje ya kijiji chao kama Balozi ili asiwe sehemu ya uhusika wa harakati za mageuzi.
Ujumbe wa kuhitajika ofisi kuu ili kuonana na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, mzee Kasoyaga ulifika nyumbani kwake naye pasipo hiana alitii wito. Jambo kubwa waliloozungumza, ni kumuomba aitumikie serikali katika nafasi ya Balozi kama alivyohisi, lengo ni kumuondoa kijijini asihusike na harakati za mageuzi ya kijiji, kuuondoa utawala dhalimu. MJM Zimbwa, hakukataa moja kwa moja ombi alilopatiwa, aliomba muda wa kutafakari ndipo atoe jibu sahihi, tena kwa njia ya barua kama alivyoletewa ombi la wito awali. Ila akili yake ilimuongoza kwenda kinyume na ombi aliloambiwa. Kitendo hicho kiliwashitua baadhi ya watu, wale wanaharakati kwa kuona mtu wao anaenda kuwasaliti. Imani kwake ilianza kutoweka, lakini aliirejesha baadaye hasa baada ya kufanya mkutano na watu wa vyombo vya habari, alipodiriki kuweka wazi kila kitu walichoongea alivyotembelea ofisi kuu.
Mkutano huo uliibua matumaini mapya ya upendo kwake, tena maradufu ya awali, huku wale waliompatia ombi wakichukizwa na kuahidi kumfanyia kitu kibaya punde uchaguzi utapomalizika. Kukataa kwa ombi alilopatiwa alijua namna gani atakuwa na maisha magumu baadaye, ya kufuatwa na kuchunguzwa sana, ili jamaa waridhishe mioyo yao.
“Katika mabadiliko nitakayoyafanya nikiingia madarakani, ni pamoja na kinga ya viongozi wa majeshi, kwa ajili ya huyu mtu. Namuondolea kinga kisha nampeleka jela ili harakati zake akafanyie huko,” alisema mzee Tualike, jioni moja akiwa na kundi lake wakipata kahawa.
“Hilo ndilo suluhisho, kwa watu wa namna hii wanaojifanya kuwa na jeuri.”
“Muache, nitamfahamisha kuwa mimi ndiye mwenye mpini,” aliendelea kujigamba mzee Tualike.
Pia kitendo cha Bi. Mwema na wenzake kuwa huru kiliendelea kuongeza hasira na mazingira magumu kwao, walitamani wawafuate muda huohuo na kuwashambulia hadharani ili siku ya uchaguzi na zile za mbeleni iwe rahisi kwao kukamilisha mipango. Iliwabidi wawe wavumilivu, wasubiri siku zijazo pindi wawapo madarakani, maana walishajihakikishia kwa namna yoyote lazima washike dola.
Hatimaye siku ya maandalizi ya uchaguzi iliwadia, siku ambayo mawakala wa wagombea wote walipewa viapo na nyaraka mbalimbali za utambulisho kuwa ndiyo mhusika sahihi anayemuwakilisha Bi. Mwema ama mzee Tualike, au mgombea mwingine yeyote aliyejitokeza. Pindi pilika pilika hizo zikipamba moto, wagombea nao wakihitimisha kampeni zao, gazeti la saa saba mchana litolewalo na kampuni binafsi ya Mangaka Habari, liitwalo “Tuijenge Tuleane” liliuzwa kwa kasi mtaani kutokana na kichwa cha habari kilichopo ukurasa wa mbele kuwavutia wengi. Kilichowavutia zaidi ni jina la mwandishi wa makala hiyo iliyosomeka imeandikwa ukurasa wa nane. “MZEE TUALIKE KUBADILI KATIBA AKIINGIA MADARAKANI” ndivyo kilivyosomeka kichwa hicho, huku jina la mwandishi likizua taharuki kubwa kwa kila mmoja aliyenunua ama aliyepata kuona.
“Inawezekana vipi?” ni swali alilojiuliza kila mmoja, ama watu wakutanapo, wakihoji uhalali wa makala hiyo pamoja na jina la mwandishi.
“Yawezekana ni kampeni tu, wanataka kumchafua.”
“Na huyu aliyeandika katokea wapi ilhali kijiji kizima kinafahamu kuwa alisha...”
“Eeeeh! Nami nashindwa kuelewa. Tutaona mengi sana mwaka huu.”
Hata mzee Tualike na watu wake liliwafikia gazeti hili, vibaraka ndio waliwapenyezea na kuwaonesha kinachoendelea. Hawakuacha kuwa sehemu ya watu walioshikwa na bumbuwazi, huku wakitafakari namna ya kujisafisha na nini cha kufanya. Jina la mwandishi ndilo liliwachanganya zaidi, kiasi kwamba walijisogeza pembeni na kujadiliana imekuaje? Ama kuna mtu katumia mgongo wa hilo jina ili habari yake iuze sana, lakini mwishowe waliamini jinsi hifadhi waliyomtupa ilivyo hawezi baki salama, hivyo kuna mtu kutumia jina la ili afanye mauzo ya kutosha ya gazeti. Mkutano mzima sasa wakajadili yaliyomo kwenye gazeti hilo, kuwa wamediriki kutoa makala hiyo ili wawachafue kwa wananchi, wakati ndio mpango walionao. Iliwalazimu kuwahamasisha wananchi wapotezee huku wakiwaomba wahusika wa gazeti kuomba radhi kwao na kuyazuia magazeti yaliyosalia kusambazwa mitaa mbalimbali kijijini hapo.
Ombi la kuomba radhi lilikataliwa na Mkurugenzi wa kampuni, Prof. Abbas Bob. Aliitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake ili kuwaeleza sababu iliyowafanya kuandika makala hiyo pamoja na matumizi ya mwandishi wa habari aliyekwisha fariki siku nyingi zilizopita, Awetu Mbwela.
Alitoa msimamo wa kampuni, akiwaasa waandishi waliohudhuria mkutanoni kwake kuwa wasisite kuandika habari zenye ukweli kwa kuhofia ujira au kupoteza uhai, bali waangalie maisha ya watu wengine pia.
“Endapo mwandishi ataficha habari zenye manufaa kwa umma atakuwa anasaidia kuchimba kaburi na kuizika jamii yake mwenyewe,” alisema Profesa Abbas.
Alitoa hamasa hiyo kwa kubashiri kituo chao cha utoleaji magazeti kitaenda kufungwa punde, kwa sababu ya makala waliyoandika. “Wanahabari msifiche makucha yenu kuhusu watu waliopo serikalini. Ya nini kuandika mazuri yake tu, ilhali ni muumini mkubwa wa matendo maovu? Lazima tuandike habari zote zinazomhusu, yeye sio Mungu wa kusema kila akitendacho kipo sahihi kwa watu wote. Hili nalizungumza kwa uchungu kwa sababu yaliyotokea ni mambo yanayohuzunisha. Wanatuleane hatuna budi kukemea na kuyazuia. Sisi wanahabari tunapaswa kuwa wa kwanza kufanya hivi kwa kuuhabarisha umma, kijiji chetu kinakoelekea kutokana na utawala uliopo ama huu unaokuja ni kubaya.” Alikunywa maji kisha kuwatazama wanahabari akiwa kimya kwa tafakari.
“Kampuni yetu imeandika makala ile, sio kwa lengo la kumchafua mzee Tualike, mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa serikali ya kijiji chetu, hapana. Tumeandika kwa lengo jema, la kuuambia umma kuwa mipango aliyonayo mgombea huyo aingiapo madarakani si wa heri, akihihitaji ushahidi tutampatia. Tena nyaraka zenye huo mpango uliosainiwa na mwenyewe na wale wanae tunao.
Kingine ninachohitaji kuwaeleza ni kuwa, hakuna kitu chochote kilichoandikwa kwa makosa ndani ya gazeti letu lililotoka mchana wa leo, vyote vilivyoandikwa viko sahihi. Lile jina lililoandikwa kama mwandishi wa ile makala, ni mwandishi halali, ambaye bado yupo ulimw...” alisema Prof. Abbas, ila hakumalizia kauli yake, baada ya kusikia sauti zito toka nyuma ya wanahabari waliokuwa wanakazana kuchukua habari, kwa kuandika kwenye vitabu vyao vya kumbukumbu, kurekodi sauti, kupiga picha za mnato na video, ikitoa katazo la kuendelea kufanya mkutano wake.
Katazo hilo liliwafanya hadi waandishi wa habari waliokuwa wanarekodi wasitishe shughuli waliyokuwa wanaendelea nayo, kisha kugeuka nyuma kumuangalia aliyetoa katazo hilo. Walikuwa mgambo wanne, wawili wakiwa wamekamatia bunduki mkononi na wengine virungu. Mkutano ukaishia hapo, kwani Prof. Abbas aliwekwa chini ya ulinzi kwa kosa la kutoa maneno yenye uchochezi na uvunjifu wa amani. Hivyo akachukuliwa kupelekwa kituoni.
Wakati yeye anapelekwa kituoni, Mkuu anayehusika na mambo ya habari na mawasiliano ndani ya serikali ya kijiji cha Tuleane, aliifungia kampuni ya Mangaka Habari kwa muda usiofahamika kwa kosa la kuandika habari zenye uchochezi pamoja na udhalilishaji kwa mzee Tualike. Pia ilitajwa kuwa, uhusika wa jina la marehemu katika nafasi ya mwandishi wa makala ulikuwa upotoshaji wa hali ya juu.
Siku hiyo ilikatika kwa uenezi na uongelewaji wa hizo habari. Kila mtaa yaliibuka makundi yasiyo na idadi wakifanya mabishano kutafuta uhalali wa habari iliyotokea. Jina la Awetu nalo lilizua balaa. Watu walijiuliza, ilikuwaje jina la Awetu likatumika kama mwandishi wa makala hiyo? Je, bado yupo hai? Na kama bado yupo hai, ilikuwaje hadi akatangazwa amefariki? Yalikuwa maswali ya msingi yaliyohitaji majibu lakini hayakupata majibu katika vijiwe vya wapiga soga.
****
“Nataka nifike nyumbani!...niacheni niende nyumbani, mbona hamnisikii?” ilisikika sauti ya kike, ikiongea na jopo la watu wengi waliovaa makoti meupe, wakiwa wamezunguka kitanda alicholazwa mgonjwa. Chupa ya maji na damu, dripu kwa wakati mmoja zilionekana kushuka kuingia kwenye mishipa ya mwili wake.
“Afya yako bado haijatengemaa, subiri upone ndipo uende,” alisema mtu mmoja kati ya wale waliomzunguka, ambao ni madaktari.
“Lazima nifike nyumbani, kuna zoezi kubwa linatarajiwa kuendelea huko, kabla halijatokea inanipasa kuutaarifu umma wa kijiji changu jambo fulani.
“Sasa si usubiri upone ndipo uende vizuri ili ukakamilishe kabisa hicho unachohitaji kukifanya, isije ukaishia kati.”
“Hapana!...hapana! Lazima niende sasa. Kwanza leo ni tarehe ngapi?”
“Mei 23!”
“Aaah! Mnisaidie kunifikisha nyumbani. Leo nahitaji hicho kitu kiwafikie wanakijiji wa kijiji chetu.”
Baadaye madaktari walisogea pembeni kidogo kujadiliana jambo, kisha kurejea tena pale kitandani.
“Tumekubali hitajio lako, muda gani unahitaji uondoke?”
“Sasa hivi. Pia niwaombe mnihakikishie ulinzi, nisionwe na mtu yeyote hadi sehemu niyopaswa kufika, ambako hata huko mtu yeyote asinitambue zaidi ya nitakayemuhitaji .”
“Ondoa shaka!”
Safari ya kumpeleka anakohitaji yule mgonjwa ilianza robo saa baadaye kwa kutumia gari la madaktari hao walioonekana kujawa na sura za kikarimu. Mwendo ulikuwa wa kawaida, kwa sababu afya ya msichana haikutengemaa, japo mwenyewe muda wote alikuwa anawahimiza waendeshe gari kwa kasi wapate kuwahi waendako. Takribani mwendo wa saa moja na dakika hamsini ndipo walifika sehemu husika. Waliegesha gari mbele ya ofisi ya kampuni ya Mangaka Habari kisha mmoja wa madaktari waliomsindikiza aliteremka baada ya kupatiwa maelezo fulani.
Daktari huyo alielekea mapokezi. Alijitambulisha na kueleza kusudio la ujio wake ofisini hapo kwa mhudumu wa kike aliyemkuta ndani ya ofisi, akiwa katika mavazi nadhifu yamvutiayo kila mmoja amuonaye. Mara baada ya kuambiwa kusudio, mhudumu huyo sekunde chache baadaye alionekana kuwasiliana na mtu fulani kupitia simu ya mezani, ambayo baada ya kukata tu alitoka na kauli iliyomruhusu daktari aende kwa Mkurugenzi wa kampuni.
Haikuchukua muda, daktari kurejea akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa kampuni ya Mangaka Habari, Prof. Abbas hadi eneo la maegesho na kuingia garini. Mshituko, ndicho kitu cha kwanza alichokionesha ndani ya gari mara baada ya kuingia, lakini baadaye alitulizwa na kuomba awe makini amsikilize yule aliyemfanya amshangae. Ambaye ni Awetu Mbwela.
Jopo la madaktari kumi na tano toka hospitali ya Tuleane Medical Center (TMC) kando ya kijiji hicho, waliotembea hifadhi ya wanyama pori ya Tuleane Green Reserve kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, ndio watu wa kwanza kuubaini mwili wa Awetu, akigaagaa na baadaye kutulia kabisa kule alikoachwa. Haraka sana walimsogelea ili kujua kama bado yupo hai ama alishafariki. Mapigo ya moyo yaliyokuwa chini yaliwapa taarifa kuwa alikuwa bado mzima. Walimchukua hadi kwenye hema lao na kuanza kumpatia matibabu.
Taarifa ya kuokotwa kwake ilifika mezani kwa uongozi wa hifadhi siku ya pili yake, walivyofanikisha kurejesha mapigo yake ya moyo, wakiomba kutotoa habari zake ili walinde uhai wake kwani hawakujua mazingira ya kifo cha Awetu yalisababishwa na kitu gani. Yote hiyo ilitokana na uchunguzi waliokwisha kufanya na kubaini amechomwa sindano ya sumu. Mkuu wa hifadhi hakupingana nao, aliridhia ushauri wao, kingine kilichomshawishi akubaliane nao, ni taarifa alizokuwanazo toka awali kuwa msichana huyo alifariki kwa ugonjwa wa kipindupindu. Moja kwa moja akafahamu namna iliyofanyika tofauti na ile iliyotangazwa kwa wananchi.
Kwa usiri mkubwa alitibiwa hadi siku aliyorejewa na fahamu akaomba wamruhusu kurudi kwao. Baada ya mabishano ya muda madaktari walikubali takwa lake, kwa ahadi pale ajisikiapo afya yake kutokuwa vizuri asisite kurudi, kwani wao wapo kwa muda mrefu mahali hapo. Alisafirishwa, hadi sehemu aliyohitaji, ofisi ya kampuni ya Mangaka Habari, akiwa na nia ya kuonana na Mkurugenzi. Hilo lilifanikiwa, kwa usiri kama alivyoletwa, ndivyo alivyotoka ndani ya gari na kuingia ofisini kwa Mkurugenzi akiwa ameambatana naye pasi na fahamika na watu wanaopishana nao. Mavazi aliyokuwa amevalishwa ndiyo yaliyomsaidia asifahamike, yalikuwa makubwa, kiasi kwamba yalizuia eneo kubwa la ngozi yake, kuanzia sura na kichwani ambako alivaa nikabu.
Alivyofika ofisini aliifunua nikabu yake iliyomruhusu sehemu ya uso kuonekana kisha akaketi sofani, macho yakiwa pima kwa Prof. Abbas ambaye alikuwa katika hali ya sintofahamu. Maongezi husika yalichukua nafasi, salamu na habari za hapa na pale juu ya kilichomsibu yalivyopita. Maongezi hayo yaliambatana na vitendo toka kwa Awetu, naye Prof. Abbas kumpa ushirikiano wa kutosha kwa matendo pia kukiafiki kile anachoambiwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Japo tulikuwa na mtafaruku kipindi cha nyuma, sasa hatuna budi kuunganisha nguvu zetu na kuuhabarisha umma wa wanatuleane nini kinachoenda kutokea kijijini kwetu.”
“Sahihi kabisa. Nipo tayari kuungana nawe katika jambo lolote utalohitaji toka kwangu.”
“Nafurahi kusikia hivyo,” alisema Awetu huku akitoa mkoba mdogo alioufunga kiunoni kwa ndani ya dila alilovaa. Aliufungua akatoa taiti chakavu, aliyoipekua pekua na kutoa kadi ndogo itunzayo kumbukumbu, yenye ukubwa wa GB 32 akamkabidhi Prof. Abbas.
“Kuna habari nimeihifadhi humo ambayo nilipata iandika siku kadhaa zilizopita kabla hayajanikuta yaliyonikuta. Hivyo nahitaji habari iandikwe kwenye gazeti lenu litokalo mchana wa leo.”
“Inahusu nini?”
“Iangalie utafahamu.”
Hakuchelea! Prof. Abbas aliiweka kwenye simu yake ya mkononi ya kisasa, ilivyosoma alitafuta mafaili yalipo kwa uchambuzi makini ili asiruke. Alivyolifikia lililoandikwa “document” alilifungua na kukutana na kichwa cha habari kilichosomeka, “Mzee Tualike kubadili katiba akiingia madarakani” kabla hata hajaendelea nayo, kilimsisimua na kumuongezea hamasa ya kuendelea kusoma nini kinachoelezewa.
“Una uhakika juu ya hiki ulichoandika?” Aliuliza Prof. Abbas mara baada ya kumaliza kusoma.
“Pasipo na shaka, naomba itoke ili Wanatuleane iwafikie, kesho waendapo kupiga kura wajue mtu yupi sahihi. Tena nawaomba hiyo habari iwe moja ya habari kubwa ziandikwazo ukurasa wa kwanza, pia jina la mwandishi andikeni langu. Juu ya hayo nakuomba wewe binafsi unisaidie sehemu ya malazi.”
“Kuhusu hayo yote usiwe na shaka nayo. Niko tayari kukusaidia kwa gharama yoyote ile.”
Walivyohitimisha Prof. Abbas aliipeleka ile habari kwa wahariri na kuwaeleza kila kinachohitajika, baada ya hapo aliongozana na Awetu kumpeleka nyumbani kwake anakoishi. Ambako ni nyuma ya jengo hilo la ofisi. Gazeti lilivyotoka, ilikuwa faraja kwa Awetu, kwani kabla hayajaingizwa mtaani alipewa nakala moja aone kile kilichoandikwa. Alifurahi sana, tena sana na kujiona mshindi mbele ya simba mia walio na hamu ya uhitaji wa chakula baada ya kusota na njaa kwa muda mrefu. Pilika pilika za kukamatwa kwa Prof. Abbas nazo alizishuhudia kupitia dirishani akichungulia, kwani jengo hilo lilikuwa la ghorofa moja, chini ofisi, juu makazi ya Prof. Abbas na watumishi wengine wa kampuni hiyo. Kwa kiasi fulani ilimhuzunisha, kumsababishia tatizo hilo, ambalo pasipo yeye lisingemkabili.
“Sababu wameamua kuwasha moto, acha mimi niwawashie zaidi,” alisema Awetu kimoyomoyo, huku akisindikiza kwa macho msafara uliombeba Prof. Abbas.
Alivyofikishwa kituoni, aliandikishwa maelezo. Baada ya hapo, aliamriwa warudi ofisini na nyumbani kwake kwa ajili ya upekuzi. Hakukataa. Walirejea ofisini ambapo hadi muda huo watumishi walikuwa wanaweka nyaraka sawa ili wafunge kutokana na tangazo lililotolewa na Mkuu wa habari na mawasiliano. Mgambo waligawana, baadhi yao ofisini, wengine nyumbani. Wale wa nyumbani walipokelewa na mkewe, wakati huo Awetu hakuwepo, kwani muda mfupi tu Prof. Abbas alivyopelekwa kituoni, timu ya madaktari waliomleta asubuhi walimfuata kurudi naye hifadhini kukamilisha dozi yake ya sindano. Upekuzi ulichukua saa moja kukamilika baada ya hapo alirejeshwa tena kituoni, mgambo wakiondoka na nyaraka mbalimbali za kiofisi kwa ajili ya upekuzi zaidi, kama vile kompyuta na kadi zinazohifadhi nyaraka za aina yoyote, za maandishi, video ama picha, wakati huo akisubiri hatua nyingine inayofuata, ambayo ni kufikishwa mbele ya baraza la kijiji kujibu mashtaka yanayomkabili.
Awetu alivyorudi alihadithiwa kilichotokea, haikumpa mashaka sana, aliona jambo la kawaida kwa sababu hapo awali alishahisi kuwepo uwezekano wa kutokea kilichotokea. Huruma haikumkosa, kwa kuwa chanzo, huku akifikiria namna ya kumuokoa, Prof. Abbas ambaye dhahiri alishafahamu atasoteshwa mahabusu. Njia pekee ya kumsaidia, ni kujitokeza hadharani, ila sio mapema kiasi hicho, alihitaji hadi pale Prof. Abbas atapopandishwa kizimbani ndipo naye ajitokeze wakati huo ashaanza kujieleza.
Uvumi wa kuwepo ama kutowepo nao uliendelea kushika kasi, mithili ya moto wa kifuu lakini hawakuwa na uwezo wa kuthibitisha.
“Kama huyo mtu hayupo duniani, imekuwaje Prof. Abbas akatumia jina lake kuwa mwandishi wa makala?”
“Yumkini apate kuuza gazeti lake. Si unajua magazeti yatokayo mchana mara nyingi hudoda?”
“Sina hakika na usemacho! Kwani huwezi jua, kama ni kweli ama lah, tusubiri atapopandishwa kizimbani ndipo tutajua kwanini kafanya hivyo.”
Kila kona ya mtaa hayakukosekana maongezi ya namna hii, wengi wao wakikosa hitimisho na kuweka subra hadi Prof. Abbas atapoanza kusikiliza mashtaka yake, ndipo wapate muafaka wa majadiliano yao. Masaa yaliyoyoma, hatimaye siku ya uchaguzi iliwadia. Vituo vilifunguliwa mapema sana, saa 12 asubuhi, mamia ya watu walijitokeza kwa wingi kutimiza wajibu wao wa kisheria unavyowataka, kumchagua mtu wampendaye. Kila kituo kiliimarishwa ulinzi na mgambo toka idara mbalimbali zilizopo ndani ya jeshi hilo, kuhakikisha hakuna aina yoyote ya viashiria vya vurugu ama vurugu kujitokeza kituoni hapo. Ndani ya vituo, ambapo wananchi hupigia kura zao walikuwepo wasimamizi na mawakala, wanaowawakilisha wagombea.
Zoezi la upigaji kura lilianza vizuri. Washiriki wengi walipiga kura na kurejea makwao kusubiri muda wa matokeo kutangazwa. Ofisi ya Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi kipindi zoezi likiendelea, kwa ustaarabu pasipo na viashiria vya aina yoyote ya fujo, waliruhusu wagombea kutembelea vituoni kuangalia mwenendo wa upigaji kura.
Wasimamizi na waangalizi pia, nao walikuwa miongoni mwa waliotembelea vituo vyote ili kujua maendeleo ya kila kituo, hali ya usalama na mwenendo wa upigaji kura kama ni wa haki ama una hujuma.
Hadi kufikia saa tatu asubuhi, ushwari ulitawala kila kituo, hakuna lalamiko lolote lililotolewa kulalamikiwa mtu yeyote anayehusika na usimamizi wa upigaji kura. Kila mmoja alifurahia ushwari uliopo, imani ya kuwa uchaguzi huo ni wa huru na haki ilitamalaki kwa kila wakala, hasa wale wa upinzani, huku wale wanaotetea upande wa utawala kwa kiasi fulani walionesha kuchukizwa. Dhahiri! Walionekana kutohitaji utulivu uliopo, kuna jambo walihitaji lifanyike lakini hakukuwa na dalili za kufanyika. Ilifikia hatua fulani walianza kuzurura, kutoka na kuingia kwenye eneo la upigiaji kura, hadi waligeuka kuwa wasumbufu. Uzururaji huo muda wote walionekana kuwasiliana na watu mbalimbali na simu zao za mkononi, mazingira yaliyowaweka wazi kwamba wanaomba maelezo ama kuulizia jambo fulani ambalo liko kinyume na utaratibu na mwenendo wa upigaji kura.
Upande wa wasimamizi wao walikesha kuwasiliana kwa njia ya ujumbe mfupi na watu wao, kuulizia utaratibu wa kufanya, ila mtu waliyemtumia ujumbe alikuwa hajibu. Jambo hilo liliwafanya kupandisha mawasiliano kwa mzee Kasoyaga na Tualike kuulizia.
“Kwani mzee Kumwembe hapatikani?”
“Ndiyo. Tumemtumia jumbe nyingi tu, kuna muda amepigiwa simu hakuna mrejesho.”
“Heee! Anajipenda kweli huyu mzee? Sawa nimekuelewa, nyie ndio wasimamizi. Mnao uhuru wa kufanya jambo lolote pasipo kupewa amri na huyo mtu. Tekelezeni mnavyoweza.”
Presha kubwa iliyoonyeshwa na wananchi kwa uwazi, japo sheria inamtaka mwananchi kufanya usiri wa kura aliyopiga, wao hawakujali hilo, walidiriki kuwa wawazi kuwa nani walimpigia kura, sababu tayari mgombea mmoja wapo hawakumhitaji kabisa, mzee Tualike. Hali hii ilichangia taarifa kuwafikia vibaraka wake, ambao walikesha kuzunguka vijiwe vingi kudadisi waongeacho wananchi kisha kutuma kwa msimamizi mmoja na wazee wenyewe.Taarifa hii iliwasukuma hima wasimamizi kutekeleza walichoambiwa siku zilizopita wakiona mambo magumu. Muda mahususi wa kutekeleza hilo hitajio ulivyowadia, hawakufanya, kwa kuwa hawakuwa na maelezo kamili ni namna gani wanapaswa kufanya, iliwabidi wafanye mawasiliano wakamilishiwe lakini hawakubahatika kufanikisha kwa kumkosa yule aliyepaswa kukamilisha maelezo, mzee Anthony Kumwembe. Jambo lililozua balaa la kuhangaika kwa kila mmoja.
Wakati wanahaha, ilikuwa faraja kwa Bi. Mwema na watu wake, kwani mawakala aliowachagua hawakusita kumtaarifu kila kinachojiri. Furaha yao iliwafanya kuwakebehi wenzao walivyokuwa wanahangaika kama wamepoteza kitu chenye thamani kubwa sana zaidi ya uhai. Walitambua wazi hangaika yao ilikuwa kwa ajili ya nini, ila hawakutilia maanani kwani nao kwa namna yao walikuwa wamejipanga kufanya udhibiti kupitia mtu huyo wamtumiaye wao.
Mapema sana kabla mzee Kumwembe hajaelekea kazini ili kushughulikia zoezi la uchaguzi, mkewe alitoroka akichukua simu zote azitumiazo mumewe. Hali hiyo iliyompa fadhaiko akilini. Kitendo cha kutorokwa na simu zilizochukuliwa ikiwa na maana hakupaswa kufanya mawasiliano na mtu yeyote kwa siku hiyo. Nacho kitendo hicho kilipangwa na Bi. Mwema na watu wake, walipokutana na mke wa mzee Kumwembe kwa mkutano ulioandaliwa na Dkt. Emmakulata.
Mfadhaiko uliongezeka alipokutana na ujumbe ulioandikwa kwenye karatasi ndogo mezani alipokuwa anapata kisabeho. Ulisomeka:
“Tambua wewe ni mtumishi wa serikali, na sio mtumishi wa mtu ndani ya serikali. Utumishi wako ni kuitumikia serikali kwa manufaa ya wananchi na si kwa manufaa ya mtu binafsi. Nakukumbusha, wakati wa kuwatendea haki Wanatuleane ni huu. Furaha ya Wanatuleane iko ulimini mwako, usifanye ukaipoteza furaha hii, itawagharimu wananchi miaka nenda rudi hadi chaguzi nyingine. Naomba nikukumbushe tena, wewe ni mtumishi wa serikali, sio mtumishi wa mtu, nenda katoe maamuzi yaliyoamuliwa na wananchi.”
Hakuwa na jinsi, alienda ofisini pasipo na simu, akili ikiwa na mawazo lukuki yaliyomshinda kuyadhibiti. Simu zilizokuwa zinapigwa na jumbe mkewe ndiye alikuwa anazishuhudia lakini hakutaka kuzijibu, aliishia kuziangalia kisha kutupilia simu pembeni. Miongoni mwa watu waliopiga na kutuma jumbe, baadhi yao aliwafahamu, akiwemo mzee Tualike na Kasoyaga na baadhi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura ambao ni wakereketwa wa mzee Tualike. Piga zao za mara kwa mara ilimpa nafasi nzuri ya kufahamu kusudio, pia nafasi ya kupata ushahidi utakao wasaidia mbeleni wakati matatizo yatakapoanza kuwaandama. Alizihifadhi jumbe na voice note zilizokuwa zinatumwa, sio kwenye simu ya mumewe pekee, hapana! Nyingine alizipiga picha kwa simu yake kwa kushirikiana na Dkt. Emmakulata ambaye naye alifanya vivyo hivyo wakiwa pamoja nyumbani kwake.
Ofisini hakukukalika, alikesha anazunguka mtaani punde alipokamilisha kupiga kura. Kukaa humo aliamini kungempatia wakati mgumu zaidi wa kutembelewa na watu aliopanganao mbinu za kuwaibia kura pale watakapomkosa hewani. Ili asipatwe na usumbufu huo aliamua kuondoka na kwenda kujipumzisha eneo fulani, nje ya kijiji akisubiri muda muafaka wa kusoma matokeo usogee ajisogeze ofisini kwa ajili ya kuyasoma.
Uwingi wa wananchi kutoa taarifa ya wazi kuwa kura yao imeenda kwa Bi. Mwema, nafasi ya uenyekiti wa serikali ya kijiji, huku nafasi za mitaa na matawi nayo zikienda kwa watu ambao ni wapambe wa Bi. Mwema, hakika ziliwachanganya mzee Tualike na Kasoyaga. Moja kwa moja waliona ushindi unaenda kwa mwanamama huyo, kitu ambacho wao hawahitaji, kwa namna yoyote. Upande wa mzee Tualike ilimlazimu aingie madarakani ili alinde mpango wake wa siri, wa kwanza uliovumbuliwa, pamoja na “Mpango wa siri namba mbili” ambao ni hatarishi zaidi, alioupanga kuutekeleza akosapo kuingia madarakani.
Kwa kuwa mipango ilikuwa ya siri, na sasa ilishaanza kufichuliwa, tena na mtu atayeshika madaraka aliamini mara tu baada ya kuapa atashtakiwa na kuhukumiwa kwa haraka ili ashindwe kufanya mpango aliouandaa. Hivyo, kuingia madarakani ndiyo jambo la msingi kwake, nafasi itakayomuweka huru na kuwazuia wote wanaofahamu mipango aliyonayo aingiapo ofisi kuu.
Upande wa serikali nao ulimhitaji mzee Tualike kwa ajili ya urafiki uliopo baina ya wazee hao wawili, kwamba mzee Tualike akiingia, akifanya uchunguzi wa kina na kubaini madudu hawezi kumchukulia hatua mtangulizi wake, tofauti na sera za Bi. Mwema ambazo nyingi zilikinzana na matakwa ya serikali.
Kitendo cha kukosa mawasiliano na mzee Kumwembe kiliwachanganya kiasi kwamba watu walifika kwenye ofisi yake zaidi ya mara tatu pasipo na mafanikio kisha kuendelea kumtafuta kwa njia ya simu, lakini majibu waliyoendelea kuyapata hayakutofautiana na yale ya awali. Walichukizwa na kumchukia mzee Kumwembe pia. Walijiuliza, kwanini kawasaliti?
Baada ya kuona hakuna matumaini ya kumpata huku taarifa za kuendelea kushindwa zikiendelea kushika kasi, ilibidi watafute mbadala wa kuwawezesha wanaongoza kutumia nguvu ya jeshi la mgambo. Hakukawia, mbadala ulioratibiwa ulianza kutekelezwa saa 6:30 mchana huku uvumi wa uwepo wa barua za kugushi za utambulisho wa mawakala zikisambazwa karibia vituo vyote. Hali hiyo ilipelekea wasimamizi kuomba kuzikagua barua kwa makini.
Ukaguzi ulikuwa wa kina; neno kwa neno—barua walizoziona zina kasoro waliziweka pembeni, zile zilizo sawa walirejeshewa wahusika, ila wale ambao zao zilionekana kuwa ni za kugushi waliombwa kutoka nje.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ubishani ulizuka baina ya wasimamizi na mawakala walioombwa kutoka nje, ambapo baadhi ya vituo mawakala wa Bi. Mwema pekee ndio walitolewa. Kwenye vituo vingine walitolewa wote ili kuleta ulinganifu kisha kutoa nafasi kwa wasimamizi kufanya watakayo. Ubishani huo ulisababisha vurugu baina ya mawakala na wasimamizi, ila nguvu ya mgambo iliingilia kati kwa kuwalazimisha wote waliopaswa kutoka nje kutoka. Wapo waliorusha ngumi kwa sababu ya hasira na kuwekwa chini ya ulinzi kisha kupelekwa mahabusu na baada ya muda fulani kurejeshwa tena kituoni kuendelea na zoezi. Muda ambao mawakala walitolewa nje, ni nafasi ya pekee waliyotengeneza wasimamizi, kufanya dhuluma waliyoipanga. Haraka sana, baadhi ya maeneo walibadili sanduku za kura, wengine waliongeza kura kwenye masanduku ya awali. Njia nyingine ambayo walipanga kuitumia ni kuwasainisha mawakala zile fomu za kuandikia matokeo mapema kabla ya matokeo hayajatangazwa ili baadaye wasimamizi waandike namba wanazojisikia kuwapatia wagombea.
Kila mmoja alivyoona ashafanikisha kwa wakati wake ndipo alitoa amri ya kurudishwa ndani mawakala waliotolewa kwa kisingizio kuwa washafanya mawasiliano na watu wa ngazi za juu kuhusu utatuzi wa kayaya hiyo.
Kilichotokea kilisambaa mtaani, ila watu waliishia kulalamika kuwa ulifanyika uonevu kwa muda kisha habari zilisahaulika. Mgambo wa doria waliokuwa wanazunguka kila mtaa walikamata watu waliowakuta wako makundi sehemu yoyote wakijadili kila kinachohusiana na uchaguzi. Wengi wao walikosa suluhu, watumie mbinu gani kukabiliana na dhuluma ya wazi iliyotendeka.
“Waambie wasisaini fomu ya matokeo,” ulikuwa ushauri wa Dkt. Emmakulata walipokutana kujadiliana hatua ya kuchukua kwa kile kilichotokea.
“Sahihi kabisa mama, hakuna mbadala zaidi ya huo uliopatiwa. Huu ni wizi wa wazi kabisa. Hatuwezi kuafikiana nao,” mwingine naye alichangia hoja, Mch. Chilombo.
“Sina budi kukubaliana nanyi. Maamuzi yenu ndiyo maamuzi yangu.”
“Itakuwaje wakikataa kusaini halafu baadaye ukatangazwa mshindi?” aliuliza Mooja.
“Haiwezi kutokea.”
“Ikitokea hivyo itakuwaje?” Mooja aliendelea kuuliza.
Hakujibiwa.
Kama walivyokubaliana, waliwasambazia mawakala wao wote ujumbe wa kukataa kutia saini kwenye karatasi za matokeo yatayopatikana. Hicho ndicho kilichotokea, kweli hawakusaini. Hata kama mgambo waliwalazimisha kwa vitisho vya kila aina, bado hawakutishika. Baada ya mbinyo mkali wa Mgambo baada ya kubaini kuelekea kuharibika kwa jambo, baadhi ya mawakala walikubali kusaini japo kwa shingo upande. Jambo hilo lilikuwa usaliti kwa watu wao waliowaamini. Waliamini kuwa, uhai ni tunu, hutetewa dhidi ya kila baya.
____________
Ilipofika saa 10 jioni, zoezi la kupiga kura lilisitishwa na vituo vilifungwa. Lilifuata zoezi la uhesabuji wa kura zilizopigwa. Kila kituo kilijumulisha na kutangaza. Baada ya hapo matokeo yalipelekwa ofisi ya bodi ya uchaguzi, ambapo matokeo ya nafasi ya uenyekiti wa serikali ya kijiji hujumulishwa na kutangazwa.
Muda huo mzee Kumwembe alikuwepo ofisini ili kukamilisha zoezi hilo kisha kuangalia utaratibu mwingine. Wananchi nao, kwa rika zote, walikusanyika kuwasikiliza ambao hawakufika walikuwa karibu na redio na runinga kufuatilia kila hatua iliyokuwa inaendelea. Ulinzi uliimarishwa, kutoka kwa mgambo wa kila idara, sambamba na magari yao ya kumwaga maji ya kuwasha.
Saa 3 asubuhi siku iliyofuata ndipo zoezi la uhesabuji lilikamilika, lilivyokamilika mzee Kumwembe alikabidhiwa nyaraka za matokeo. Alianza kusoma matokeo ya mitaa katika nafasi ya uenyekiti, namna kila mgombea alivyoshinda, wakati huo wasaidizi wake wakimalizia kuchapa matokeo yote ya ujumla.
Walivyomaliza alipelekewa, hivyo baada ya kumaliza za mitaa, alikamata nyaraka hizo kuendelea na usomaji. Saa tano asubuhi alihitimisha usomaji kwa kumtangaza mzee Tualike kuwa mshindi zaidi ya kura elfu kumi na moja dhidi ya mpinzani wake Bi. Mwema.
Shangwe, vifijo na nderemo vilifuata. Matokeo yalivyotangazwa toka upande wa watu wampendao mzee Tualike, wale wa Bi. Mwema walilipuka kwa mayowe kupinga matokeo yaliyotangazwa. Kwa kuwa walishapata taarifa ya mawakala wasikubali matokeo yatayopatikana, moja kwa moja wakajua fika matokeo yaliyotangazwa ni ya hujuma, hayakuwa na uhalali wowote, hivyo ikawahimiza kufanya fujo. Walianza kutupa mawe, chupa za pombe na sumu kuelekea jengo la ofisi pamoja na ule upande walioko watu wa mzee Tualike. Mabomu yaliyotengenezwa kwa kutumia mafuta ya petroli nayo yalianza kurushwa, vurumai lilizidi ongezeka kila dakika zilivyozidi kusonga mbele, mgambo walioandaliwa kudhibiti ulinzi walionekana kuzidiwa nguvu, hadi vikosi vilivyokuwa vinafanya doria mtaani vikaungana mahali hapo kushirikiana kutuliza vurumai lililopo.
Pindi raia wanatumia zana hizo kukabiliana na mgambo, wao walitumia mabomu ya kila aina ili kutawanya waandamanaji. Virungu navyo vilikuwa sehemu ya silaha zilizotumiwa na mgambo achilia mbali, risasi za moto na baridi, zilizokuwa zinapigwa hewani zingine katika miili ya waandamanaji kuanzia kiunoni kushuka chini. Mazingira hayakutamanika, moshi na milio ya milipuko ilitanda eneo zima. Watu wenye matatizo ya kifua na presha hawakuacha kudondoka, kupoteza fahamu na wengineo uhai kabisa. Kama ni kabumbu, basi timu zilizokutana hapo zilikuwa zenye uhasama mkubwa, na ambazo zilikuwa haziishi kutapiana kwamba kila mmoja ni mbabe wa mwenziye. Ndicho kilichofanyika hapo, wananchi hawakukubali kushindwa kirahisi japo walikuwa na uhaba wa silaha za kushindana. Mgambo waliyobahatika kumkamata, walimpa kichapo hasa, ili iwajengee heshima na kuwapa fundisho tosha kwa wengine ni namna gani wana machungu dhidi yao.
“Piga risasi za moto hao sehemu yoyote ile wasitupotezee muda,” ilisikika sauti ya Kamanda anayeongoza vikosi vya mgambo baada ya kuona wananchi wanazidi kumiminika. Watu walizidi kudondoshwa chini lakini hawakujali, walizidi kuipata nguvu ya ushindi mioyo yao wakasonga mbele.
“Rooja afande!” waliitikia mgambo waliokuwa wanapewa amri huku wakibadili kisanduku cha risasi na kukoki vyema bunduki zao kisha kuchanja mbuga kufuata uelekeo wananchi wanakotokea wakitekeleza amri waliyopewa.
Pasipo kujali, mara baada ya kauli hiyo, risasi za moto zilitumika kwa sana. Baada ya kuona wananchi wameweza kuvumilia kiasi kikubwa cha mabomu kilichotumika, hawakuchagua tena sehemu ya kupiga, walipiga popote walipoona inafaa ili mradi kibarua kisiote nyasi. Juu ya piga nikupige iliyokuwa inaendelea, watu walikamatwa na kupelekwa mahabusu pasipo kuangalia majeraha. Waliwakusanya vivyo hivyo.
Hadi kufikia saa kumi jioni, maandamano yalififia baada ya asilimia kubwa ya watu walioshiriki kuumizwa na kuuawa. Wachache waliosalia walisalimu amri na kuamua kukimbia. Japo nao kwa kiasi fulani nguvu zao hazikwendwa bure, vurugu walizofanya zilipelekea kuchoma moto baadhi ya majengo ya serikali pamoja na ya watumishi wake walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kuhalalisha ushindi.
Siku iliyofuata wote waliokamatwa kwenye maandamano pasipo angalia afya zao zikoje, walifunguliwa mashtaka na kufikishwa mbele ya baraza la kijiji kujibu mashtaka yao. Kesi ilipelekwa haraka sana, siku tatu, zilikamilisha kutolewa hukumu baraza lilivyoridhishwa na maelezo ya toka pande zote. Hukumu ilitoka kwa wote, waliokutwa na hatia, kutumikia kifungo cha miaka miwili jela. Hukumu iliyozua sintofahamu kwa wengi! Tena hakuwekewa rufaa. Ubabe! Afisa Mtendaji wa kijiji ndiye alikuwa muamuzi (Hakimu) wa baraza zote.
Shangwe alilolipata mzee Tualike na kampani yake kwa ujumla halikuelezeka. Alifurahi, tena alifurahi sana, kilichomfurahisha zaidi kuwa huo ndio wakati wa kuwaonesha watu waliokuwa wanampinga anamamlaka kiasi gani. Baada ya siku sita aliapishwa, na mwanasheria mkuu wa kijiji, kisha rasmi alianza kutumikia majukumu ya uenyekiti wa serikali ya kijiji. Kitu cha kwanza kufanya punde baada ya kuapishwa, aliunda baraza la wawakilishi, ambao hutoka kila mtaa pamoja na kumuongezea muda Afisa mtendaji aliyopo. Aliteua watu mbalimbali, toka mitaa tofauti tofauti ila asilimia kubwa ni wale anaoendana nao, ambao wengi wao walimfanyia kampeni. Walikabidhiwa idara zilizopo, huku wale waliokuwa awali, ni wachache tu walibahatika kubaki, waliositishiwa waliahidiwa kupangiwa kazi zingine kipindi kijacho. Karibu kila nafasi aliweka watu wake kuwa waongozaji wakuu kasoro jeshi la mgambo, alishauriwa kumuacha aliyoko kwa muda pindi anafanya mpango wa kumtafuta mwingine.
Taratibu aliwatumikia wanatuleane, kiasi kwamba hadi waliokuwa wanamchukia kipindi cha awali walianza kumpenda. Naye hakusita kuonesha mapendo kwa wananchi kwa kutekelezayale aliyowaahidi pindi anawania nafasi hiyo. Alijenga tabia ya kuwa chaguo pendwa la wananchi, awapo ziarani popote, akutapo halaiki ya watu alisimama, kuwasabahi na kuomba wamueleze shida walizonazo kisha kuendelea na safari. Hata hotuba zake zilijaa maneno yenye hekima na busara za kuwapa matumaini watu wa daraja la chini, waamini wamepata suluhisho la matatizo yao na kijiji kwa ujumla.Wasaidizi wake wakawa msitari wa mbele nao kushughulika, kuunga jitihada zilizoanzishwa na Mwenyekiti wao. Muda mwingine walitumia majukwaa kumuombea, ikibidi aongezewe muda afanye mambo mengi mazuri zaidi.
Siku haikupita pasipo kuzungumziwa kwa namna yoyote, mabaya kwa mema. Waliozungumza mabaya walikuwa ni wale wanaomchukia. Ila walio wengi, wenye nguvu zaidi ya kusikika sana ni wamsifiao. Waliokuwa wanampinga, ambao wakitoa hoja haichukua muda mrefu, walikosa nguvu na kufifia mapema kwa kukosa watu makini na wenye moyo wa uthubutu wa kuunga mkono hoja zitolewazo.
“Huu ni wakati sahihi wa kufanya yale niliyoyapanga,” alisema mzee Tualike pindi akiongea na wanaye asubuhi moja alivyowaita pamoja na watu wake wa karibu, walinzi wa siri waliokuwa wanatumiwa na mzee Kasoyaga, Sabaya na Maroda. Na maafisa wengine wa ngazi za juu wanaoshughulika na mambo ya sheria, ulinzi na usalama.
“Sahihi mkuu!”
“Sasa siwezi kukamilisha ile kitu kama wale wenye ufahamu wataendelea kuwepo uraiani. Nahitaji wote, kuanzia Prof. Abbas, Bi. Mwema, Laumio, Mch. Chilombo, Mooja, Dkt. Emmakulata, MJM Zimbwa na yeyote mwenye kujifanya mwanaharakati wa kupingana na serikali aingie jela ili nipate fursa ya kukamilisha nilichopanga.”
“Kuhusu hilo mzee ondoa shaka, tupe muda ili kufikia lini tuwe tushahitimisha?”Aliuliza Mkuu wa mgambo.
“Anza sasa, haina kusubiri na ndani ya miezi mitatu tu wote niliowataja sihitaji kuwasikia uraiani. Pasipo kumsahau mzee Kumwembe, naye sihitaji uwepo wake.”
“Lishatekelezeka hilo mkuu.”
“Fanyeni haraka tumalize haya mambo, nawaahidi, tukifanikisha tu, mipango yote ya kubadili katiba kwa kunipa nafasi ya kutawala milele, kufungia mitandao ya kijamii, na kuzuia mikutano yote ya wanaharakati wa upinzani, basi nanyi mtakuwa watawala wa milele katika idara zenu.”
“Hilo!...hilo lazima likamilike mkuu, hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kushindana na serikali hapa kijijini,” Afisa mtendaji naye alichangia.
Wote aliowahitaji mzee Tualike wasionekane mtaani kwa kigezo cha kuwa wataharibu mipango aliyopanga walifunguliwa kesi ya uchochezi na uhujumu uchumi siku iliyofuata. Hata ambao walishawahi kuwa na nyazifa za juu ndani ya serikali ya kijiji, hawakuwajali! Walichojali ni kutii maagizo ya mkuu wao. Kesi ziliendeshwa kwa haraka mno, hasa Bi. Mwema na Prof. Abbas ambao walikwishafunguliwa toka awali. Mwendesha mashtaka akiwa Afisa mtendaji wa kijiji, Ndg. Kamilius Mbunda. Mzee apataye kuwa na umri wa miaka sitini na tatu, umbo lake likipambwa kwa urefu, unene kiasi na rangi angavu, nyeusi. Ngozi iliyosinyaa, mvi zilizojaa kichwani na kidevuni, navyo ni sehemu ya mapambo ya mwili wake. Chale zake usoni, pamoja na ndita muda wote, dhihirisho ni mtu aliye na hasira, si vitu vya kusahaulika kumhusu, hata kama mtu akihitaji utambulisho wa kumfahamu afisa mtendaji, huambiwa vitu hivi, ndiyo njia ya urahisi kumfahamu.
Kwa sifa hizo, zilimfanya kuwa mtu wa kuogopeka. Awapo nyuma ya meza kusikiliza mashtaka ya raia wa Tuleane, watu walimhofia. Hata kabla hajatoa sauti yake iliyojaa ngurumo bado walimhofia.
Kwa siku mbalimbali tofauti, upishano wa siku moja, kila mmoja alipandishwa kizimbani. Wananchi walijitokeza kwa wingi ili kujua hatma ya wanaharakati wao, walioitwa wachochezi na wavunjifu wa amani kwa sababu ya kuihimiza serikali kujali maslahi ya wananchi watesekao kwa udhalimu waufanyao.
Upande wa serikali ulivyotoa maelezo, nao walipata fursa ya kujieleza kwa kile wanachotuhumiwa. “Una shahidi wa kuthibitisha maelezo yako?” Aliuliza Ndg. Kamilius, asubuhi moja ambapo Prof. Abbas alipopata nafasi ya kutoa maelezo yake mbele ya baraza, juu ya tuhuma ya kufanya uchochezi na kauli za udhalilishaji dhidi ya mzee Tualike.
“Ndiyo! Ninayo.” alijibu Prof. Abbas. Halaiki kubwa ikimuangalia, jicho lililojaa huruma. Sababu ya uonevu.
“Okay!Tunaghairisha shauri hili hadi siku inayofuata. Mshitakiwa tunaomba uje na shahidi wako.” Faili ikafunikwa. Ikasogezwa pembeni na kuvutwa nyingine.
Taratibu za kumtaarifu, shahidi anayehitajika barazani ilifanyika. Wahusika wa baraza, walijaza fomu, ikasainiwa kisha kupatiwa Prof. Abbas aandike jina la shahidi wake. Alivyokamilisha kuliandika aliwarudishia. Jina aliloliandika liliwastua, wakatazamana na kurudisha jicho la mshangao kwa Prof. Abbas, akawakata kauli.
“Huyo ndiyo shahidi wangu.”
“Inawezekana vipi? Na yuko wapi huyu mtu?”
Hakuwajibu!
Aliishia kuwaangalia, namna walivyokuwa wanafanya tafakuri, iliyowakosesha jibu na utulivu. Hata alivyoambiwa mzee Kamilius, alishangaa. Hakuamini. Na ilimpatia msukumo wa kutoa kilonga longa chake, alibonyeza vitufe kadhaa, kutafuta jina, sekunde chache, akawa ulimwengu wa mawasiliano na mtu wa upande wa pili wa kilonga longa.
“Mzee! Awetu yuko hai.”
“Unasema?” Aliuliza yule aliyeko upande wa pili. Kwa mshituko mkubwa uliomgongesha mkono wake usio kamatia kitu mezani kwa nguvu iliyomshitua mlinzi wake, aliyeketi nje ya chumba cha ofisi yake na kumlazimu kuingia ndani.
“Mkuu, kuna tatizo?” Aliuliza mlinzi alivyoingia ndani. Ila mkono wa kumsukuma arudi atokako ulimwelewesha kutokuwa na tatizo. Akarudi.
“Ukweli ni huo kiongozi. Prof. Abbas kasema huyo ndiye shahidi anayehitaji kuthibitisha maelezo aliyotoa siku ya kesho.”
“Mmmmh!” Alihema mtu huyo kwa shida, ambaye ni mzee Tualike kisha akaendelea na maongezi.....
“Kuna uwezekano wowote wa kusogeza mbele shauri lake? Maana kama kweli Awetu yuko hai, basi mambo yote yataharibika. Nataka huyo mtu ateswe, hadi atueleze wapi Awetu alipo, ili naye tukammalizie huko.”
“Kuhusu hilo hamna shida, mimi ni utekelezaji tu.”
“Sawa, fanya hivyo.”
Akakata simu.
Akili haikutulia kwa mzee Tualike. Kichwa kilijaa moto, moyo ulifubaa kwa chuki, sura ilivaa hasira. Taarifa ilikuwa mbaya. Ikambidi awasiliane na Mkuu wa mgambo, akampatia maelezo ya kufanya, kuhakikisha kusudio linatimia. Hakuishia hapo, aliwasiliana pia, na kina Sabaya na Maroda, nao kuwapatia majukumu, ya kwenda nyumbani kwa Prof. Abbas kufanya upekuzi kama Awetu yuko huko. Wakishindwa wamkamate mkewe, ili iwe njia rahisi ya kumshinikiza ataje Awetu alipo.
Maagizo yote yalitekelezwa. Prof. Abbas alivyorudishwa mahabusu, alipelekwa chumba cha kipekee, chenye giza nene, kilichojaa wadudu warukao na watambaao. Mbu, mende, sisimizi, kunguni, mijusi na tandu. Pasipo kusahau buibui waliojenga karibia eneo lote chumbani humo. Joto lilitamalaki, mwanga hafifu ulioruhusiwa kuingia kupitia kidirisha kidogo kilichojengwa juu kabisa, karibu na paa hakikuwezesha kulipunguza. Hivyo humlazimu mtu yeyote, aingiapo kuvua nguo yake ya juu kujipepea. Ndicho alichofanya Prof. Abbas, ila iliwarahisishia wale wadudu kuutumia mwili wake kama sehemu ya michezo ya watoto.Wenye kuuma na kukesha kuuzunguka, waliitumia nafasi ipasavyo. Kero ilimjaa, kuitoa hakuweza. Akabaki kunung’unika, mwishowe usingizi ulimpitia. Uvumilivu ulivyomjia alikabiliana na wale wadudu. Tafakuri za hapa na pale hazikukosekana wakiulizana kuwa, imekuwaje hadi ahamishwe chumba, tofauti na chumba cha mwanzo alichokuwa anatumia, chumba kilichojumuisha watuhumiwa wengi. Fika alitambua kuwa ni chumba cha mateso kwa sababu ya kutaja jina la Awetu. Kipindi tafakuri hizo zikitawala akilini mwake, maji ya vuguvugu yalimshitua, aliamka! Aliona picha ya video ikimuonesha mkewe akiwa katekwa, akiteswa vikali.
Hiyo ilimpa picha kuwa kuna kitu alihitajika kufanya. Kweli! Video ilivyomalizika, sauti ilisikika. “Tuambie Awetu alipo, kabla hatujaisambaratisha familia yako.” Aliduwaa! Alikosa la kufanya. Machozi yalianza kumtoka, yaliyoambatana na kauli nyingi zenye malalamiko.
“Kama mnataka kuondoa uhai wangu, ondoeni tu. Huyo mwanamke kawakosea nini? Njooni mpambane nami, mwanaume mwenzenu na sio huyo,” alilalamika Prof. Abbas, machozi yalizidi kutiririka shavuni mwake kwa kasi kushuka chini.
“Eeh! Nyie ni Miungu? Watu gani nyie mnaokataa ukweli wenu? Nini maana ya kunipeleka mbele ya baraza kujibu tuhuma zangu kama sasa mnanitendea haya? Niuweni basi mridhike kuficha, mnachotaka kuficha, ila dondoo ishafika kwa wananchi mnachotaka kufanya. Kama hiyo sio nia yenu, imekuaje mnadiriki kutenda haya?” aliendelea kulalamika Prof. Abbas kwa sauti ya juu iliyosikika na watuhumiwa walioko chumba kingine, na raia wapitao karibu na eneo hilo.
Dakika kadhaa baadaye, mlango ulifunguliwa. Sauti za mlio wa watu zikitembea kumfuata aliko, alizisikia. Ila watu walioingia hakuwatambua, giza lililopo liliwaficha. Alijaribu kukaza macho kubashiri hata sehemu waliyosimama, hakufanikiwa. Aliumiza tu misuli yake. Ilibidi awaulize. Huku akitumia mikono kupapasa, awaguse, atambue ni watu wa jinsia gani. Alivyoona kimya, akafahamu, waliongia ni wateswa, kama alivyo yeye, kwa kufichua uovu wa viongozi wao.
“Nina hakika, ninyi ni wenzangu, wateswa kwa kutetea maslahi ya wananchi waliowapa ulaji leo hii.” alisema Prof. Abbas. Ila watu wale walioingia waliendelea kuwa kimya. Akalala tena!
Awamu hii, usingizi haukumfikia, mijeredi ya mpira ilianza tembea mwilini mwake. Alipigwa, mwili uliruhusu majeraha, damu nyingi ilimtoka. Mijeredi ilienda sambamba na kauli, toka kwa watu wale walioingia, ya kumtaka awaeleze Awetu alipo. Maumivu alianza kuugulia, kilio kikawa suluhisho, kutoa machungu yaliyojikusanya moyoni. Hakutamanika! Mwili wote ulitapakaa damu, mithili ya machinjioni. Harufu ya kifo mbele yake aliiona. Juu ya kipigo chote, hakudiriki kufungua mdomo wake kutoa kauli, wapi Awetu anapatikana. Alitoa kauli zingine, zilizomtaka wamuondolee kabisa uhai wake, na si kumuacha aendelee kuwa hai. Alifanya kibri, iliyowarudisha tena wale watu waendelee kumpatia kipigo, lakini bado alisimama kwenye msimamo wake. Hatimaye alipoteza fahamu.
Kupoteza kwa fahamu ilikuwa nafuu kwake. Kwani, wale watu, waliokazana kutoa kipigo, ambao ni Sabaya na Marodawalisitisha na kuamua kuondoka. Maendeleo ya kazi waliyafikisha eneo husika, taarifa zilikohitajika, kwa mzee Tualike. Haikumridhisha, tamanio la kuuondoa uhai wa Prof. Abbas, akilini likashika kasi ili kuficha madudu aliyotenda, na mipango yake endelevu aliyonayo. Himizo akalitoa kwa namna yoyote ili wafahamu kuwa mtu wanayemhitaji anakopatikana, ikishindikana uhai uwe halali yao. Hilo halikuwapa shida. Masaa matatu baadaye walirejea, fahamu zikiwa zishamrejea, walitambua kupitia sauti ya maumivu aliyokuwa anaitoa. Neno huruma kwao lilikosekana. Ukatili ndilo lilikuwa sehemu ya burudani. Hawakuremba, walimtembezea kichapo huku wakitumia chumvi kumtilia majeraha ili kumuongezea maumivu.
“Niueni......niuweni...” alilalamika Prof. Abbas, lakini aliendeleza usiri wa kutotaja wakitakacho watesi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata hakufikishwa barazani kwa sababu ya hali aliyonayo japo alihitajika kuhudhuria. Hata Afisa mtendaji aliyehitajika kuongoza mashtaka hakuhudhuria. Hivyo kesi hazikusikilizwa kwa hiyo siku.
Siku ya pili mambo yalikuwa kama siku ya nyuma, ila mzee Kamilius alifika. Watu waliokusanyika kusikiliza walishangaa siku kupita pasipo shauri la Prof. Abbas kuzungumzwa. Walihojiana wenyewe kumuuliza mtu anayehusika barazani. Walihofia kuitwa kimbelembele, ambavyo vingewaingiza matatizoni siku za usoni. Walibaki na matamanio.
Siku zilipozidi kusogea, Prof. Abbas mwili wake ulizidi kunyauka na kutoa harufu kali akiwa chumbani. Harufu Ilitokana na haja ndogo iliyokuwa ikimtoka pasipo hiari yake usiku kuchwa. Alijisaidia pia kwenye galoni kwa haja kubwa, akiwa ndani ya chumba cha mateso alimokuwa kafichwa. Matibabu hakupatiwa, pia chakula alichopatiwa hakikuwa na ubora.
“Inawezekana vipi, ama kuna namna wamemtendea?”
“Sijawahi kupata kuona hata kusikia sheria hii tangu baraza lianzishwe. Itakuwa kuna kitu wamemfanyia baada ya kusema ana shahidi.”
“Eeeh! Kweli. Tena kwa tetesi nilizonazo, alisema kuwa Awetu ndiye shahidi yake.”
“Kwahiyo unataka kuniambia kuwa Awetu bado ni mzima?”
“Inaweza.”
“Kama ni mzima ilikuwaje Dkt. Makolela amtangaze kafariki kwa ugonjwa wa kipindupindu?”
“Ndugu yangu. Hapa pana namna, ndiyo maana wameizuia kesi ya Profesa ili wamtafute Awetu wamuangamize ndipo kesi irejee. Wambane vizuri.”
“Ooooh! Kweli. Ila, kwanini tusiandamane kushinikiza baraza lisome hilo shauri?”
“Ni ushauri mzuri. Tujaribu kuwahimiza watu wengine, tuone wana mitazamo ipi juu ya hili.”
Wananchi walianza kupanga mikakati. Kila walivyokutana vijiweni walihimizana kuandamana. Kwenye wengi pana mengi, mtazamo huo ulipingwa baadaye. Hata wanaharakati wengine, wakiongozwa na Bi. Mwema, walipoulizwa kuhusu shahidi, walimtaja Awetu. Kitendo cha watu wote kumtaja, Awetu kiliwapa ufahamu walio njia panda ya kufahamu kama binti huyo bado yupo hai. Walitaka kujua kama Awetu anaishi, na kama anaishi, kwanini Dkt. Makolela alimtaja kama mfu katika orodha?
Uwepo wa Awetu sasa ulifahamika kwa asilimia zote. Taarifa ilienea, kila pande na kwa kila rika. Hamu ya kumtafuta ikashika hatamu, mitaa yote walimsaka, kumpata ikiwa yao nia. Pindi wananchi wanahaha kumtafuta, Sabaya na Maroda nao walichanja mbuga kote walikohisi anapatikana. Jitihada za utafutaji zilikuwa za kutosha, lakini matumaini hayakupatikana, hadi siku wanaharakati walivyopanda kizimbani. Mambo yalikuwa magumu. Baraza lilitawaliwa na ukimya, masikio yakawa makini, macho pima yakawa tayari kuangalia, pua kunusa ikawa sehemu yake. Mshitakiwa mmoja baada ya mwingine alipanda, alipoombwa kumleta shahidi, jina Awetu alilitamka pasi na chelae. Ule utulivu uliopatikana, marashi yaliyozoeleka kutumiwa na Awetu yalisikika vyema puani mwa halaiki iliyokusanyika mahali hapo. Harufu, iliwageuza nyuma, kuhakikisha kama marashi hayo yanatoka kwa mtu waliyemzoea kuona anatumia. Mshangao uliojaa furaha haukupingika! Moyo wa ushindi ulijaa, sauti ya ukombozi ilinguruma, haki yenye uhuru ilionekana. Tuleane mpya akilini iliundwa.
Kizimbani Awetu alisimama. Sauti yake ikawa mali kutamkika. Wapo waliotamani kununua kila herufi aliyohitaji kuitamka, sheria zilikataza. Virekoda vilijaa, kamera usipime, vipaza sauti ndiyo zaidi, kunakili aongeacho. Mashtaka ya watu hao, yalipata wasaa mubashara kuonekana, serikali iliidhinisha, ushindi walivyouona upande wao unapatikana.
Alijikoholesha ili matamshi ayatapike pasipo sehemu yoyote kukwamisha. Mzee Kamilius, naye aliketi kidete, nyaraka zilizohifadhiwa kwenye mafaili na vitabu vingi vya kisheria, mezani mbele yake alivipekua kila sekunde, jambo fulani kulitafuta, alipofanikisha, kalamu ya risasi aliiweka kuwa alama. Jicho lililoiva, kwa hasira kali lilitua mwilini mwa Awetu, kumtathmini. Msichana asumbuaye akili za watu wazima waliopungukiwa werevu. Shitaka liligeuka ngonjera, iliyovuta hisia za wengi, namna ubabe walivyooneshana. Sheria tu, zilizuia, ila watu walitamani kupiga yowe, kushangilia, Awetu alivyokuwa anakinzana vikali na mwendesha mashtaka ya serikali pamoja na Afisa mtendaji. Aliwazidi mbinu, hoja zikawa ngangali, ukombozi wa wanaharakati ulinyemelea.
Dalili za nje, serikali kuangushwa kwenye hilo shitaka zilionekana. Jambo ambalo kwao halikuhitajika, ushindi ulipaswa kulazimishwa. Baadaye mzee Kamilius, ilimbidi Awetu kumkana, kutomtambua kama shahidi halali wa washtakiwa, sababu ni mtu aliyepatwa kufahamika ashaaga dunia siku za nyuma zilizokwishapita. Amri akaitoa, Awetu kutooneka. Mgambo waliopo haraka sana amri waliitii, juu juu walimtwaa, kituoni akatuliwa, mashtaka mezani akafunguliwa. Mashitaka ya uchochezi na uvunjifu wa amani kama wengine walivyofunguliwa. Hisia za kuwa mwisho wa maisha yake kufikia, baada ya jaribio la kwanza kufeli, zilimjia. Lakini aliondoa wasi, imani yake ilimthibitishia, alichofanya kinatosha jamii kuipa utambuzi. Viongozi wakuu wa serikali yao ni watu wa namna gani.
Maelezo, yalivyokwisha malizwa kuandikwa, alipelekewa mahabusu, chumba cha mateso, alichopo Prof. Abbas. Hata wale wengine nao, ambao walikuwa na dhamana, baraza lilitengua dhamana zao, wakarudishwa mahabusu, wote katika chumba hichohicho alichopelekwa Awetu. Baada ya hapo, vichapo vikali vilitembea kwa wote.
“Fanyeni muwezavyo, kwa kulinda nafasi zenu, hao watu sihitaji niwaone uraiani kuanzia muda huu. Maana nimeona kila dalili za kuishinda serikali kule barazani,” ilisikika sauti ya upande wa pili wa simu, pindi Mkuu wa mgambo akiwasiliana na mtu huyo.
“Nimekuelewa kiongozi wangu, hawa ni watoto wadogo tu, kuanzia leo utasikia wakiitwa kwa majina mengine.
Nia ya kuzuia midomo yao, ilidhamiriwa kufanyika. Tena awamu hii ni kuwaondoa kabisa ulimwenguni, wapate kuwa huru, kwenye vile wanavyooenda kufanya.
Asubuhi, saa 3:45, moshi mwingi ulitanda angani huku ngurumo zikilikumbatia anga. Ilisikika kama mipasuko ya matairi ama mafuvu yaliyoungua kwenye tanuru la moto. Hatimaye kelele zilifuata na taharuki za watu wakistaajabu. Watu wengi walilia na kuomba msaada ili wapate kuokolewa baada ya moto mkubwa kuzuka na kuteketeza sehemu ya vyumba vya kituo kikuu cha mgambo chaTuleane. Jitihada za ukoaji zilifanyika, baada ya muda kidogo, takribani baada ya dakika tano toka moto ulivyoanza kuwaka Nyaraka ndizo zilikuwa za mwanzo kuokolewa, baada ya hapo walifuatia watuhumiwa, achilia mbali wale waliowekwa chumba cha mateso ambacho moto ulianzia.
Shughuli za uokoaji wa ndani zilifanywa na mgambo pekee, wasamaria wema waliojitokeza kusaidia, wao waliokoa mali zilizoko nje kwa kusogeza mbali kiasi na jengo lilipo ili ziisipate kuteketea. Wakati huo pia, shughuli za uzimaji ziliendelea.
Maji ndiyo yalitumika kwa wingi lakini pampu za kurushia maji zilikosa nguvu. Hivyo maji yalishindwa kuufikia moto. Hata yaliyofikia, yalikuwa kwa uchache sana. Dakika kumi zilitosha kukusanya watu wengi eneo hilo, kama vile kiongozi wa chama cha upinzani akihutubia wananchi. Watu walikuwa wengi, uwingi wao haukuwa na msaada, bali kushangilia.
Ulivyosikika mlio wa kitu kikipasuka, pia walishangilia. Waliamini mgambo walikomolewa kwani hata vielelezo viliungua. Naam! Nyaraka mbalimbali zilizo kwenye maandishi na vifaa vya kutunzia kumbukumbu viliungua. Watuhumiwa baadhi nao moto uliwapitia, ukaunguza sehemu ya viungo vya miili yao.
Wakati mamia ya wakazi wa Tuleane wakihangaika na habari za moto, wenyeviti wa mitaa walikuwa ndani ya jengo maalumu, walitumialo kwa vikao. Iliitwa Ofisi elekezi.
Wakati mezani kwa mzee Tualike kukiwa tayari kumwagwa wino, kwa kutia saini nyaraka ili iwe sheria, wananchi hawakuwa na ufahamu huo. Hakuna yeyote aliyejitolea kufuatilia kwa ukaribu, wengi wao waliohitaji habari, kila walipoingia mtandaoni na kwenye chaneli mbalimbali za runinga, walitaka kufahamu moto uliotokea kituoni umeleta madhara gani. Hawakuwa na habari juu ya kinachoendelea ndani ya ofisi elekezi ambapo miswada ya idara moja, kidete ilimwagwa mezani kuzungumziwa, idara ya habari na mawasiliano; kuhusu kufungwa kwa mitandao ya kijamii. Huo ndio mswada uliokuwa unajadiliwa, waafikipo marekebisho yalifanyika.
Ndani ya jengo hilo lilijumuisha wenyeviti wote, wa pande mbili. Wale wamuungao mkono Bi. Mwema na mzee Tualike. Pamoja na wateuliwa wa bodi ya uchaguzi na Mwenyekiti wa kijiji, kutegemeana na itikadi zao.
Ukinzani ulijaa kwa hoja. Waliozidisha mvutano ni wapinzani ambao walipinga vikali muswada huo--hawakusikika. Wenyeviti wa serikali walikazana kuwa muswada upite. Imani yao iliwahakikishia kutokana na idadi kubwa waliyonayo kulinganisha na wapinzani. Moto wa maneno ulipanda pande zao kuteteana. Katikati ya majadiliano, taarifa ya kuwaka moto kituo kikuu cha mgambo pale Tuleane iliwafikia wenyeviti wote, ikawa fursa kwa upinzani kumuomba muongoza kikao aahirishe kikao ili wakatoe msaada. Hoja ilikataliwa, muswada ulipitishwa kwa lazima kwa kauli ya mzungumzaji mkuu. Wenyeviti wa upinzani hasira iliwapanda, hoja zao kupuuzwa iliwakera. Iliwalazimu kutoka nje.
****
Hakuna aliyehisi kama kituo kuungua ilikuwa njama mahususi, iliyopangwa na wakuu wa vyombo vya dola ili kuteketeza uhai wa wanaharakati pendwa wateteao wananchi. Pia kulikuwa na hisi kuwa waliunguza ofisi ili wapate kupitisha muswada wao pasipo na shida wala malalamiko kutoka kwa wananchi ambao laiti kama kina Bi. Mwema na wenzake wangelikuwa uraiani, wangelihamasisha watu kupinga jambo linaloenda kufanywa na serikali. Hivyo ililazimika, uraiani kuwaondoa, kisha kufanya kitu kitachowahimiza wananchi wakiangalie sana waachane na shughuli zifanyikazo ndani ya ofisi elekezi.
Naam! Mpango ulitimia. Uratibu wa mzee Tualike kwa kushirikiana na wanaye pamoja na Mkuu wa Jeshi la mgambo. Shoti ya umeme ilitegeshwa baada ya dakika kumi, ilijibu kwa mlipuko mkubwa uliosaidiwa na mafuta ya petroli yaliyomwagwa chini, chumbani walimo wanaharakati. Mlipuko ndio uliwashitua wanaharakati, wakiwa wamelala kutokana na uchovu na maumivu makali ya kipigo. Kelele za kuomba msaada walizitoa zilikuwa kali. Katu hawakujaliwa, walianza kuwafuatilia, huku sehemu kubwa ya mwili wakiwa wameungua na baadhi fahamu ziliwatoka. Wananchi nao waliokusanyika nje, baadaye ndipo liliwajia wazo la uwepo wa watu hao, hasa walipoona purukushani za gari ya wagonjwa ikiongezeka, ikichukua majeruhi kupelekwa zahanati.
“Jamani, wale watetezi wetu wako humu ndani?”
“Eeh! Wapo.”
“Watakuwa katika hali gani huko waliko?”
“Sina hakika, ila kuna kitu nahisi.”
“Kipi hicho?”
“Huu moto ni wa kupangwa, umewashwa ili wawaondoe duniani wale watu.”
Wazo kuwa moto uliwashwa kwa ajili ya kusababisha tatizo kwa wanaharakati lilienea. Walipiga kelele kwa ushirikiano kuomba taarifa ya wetetezi. Kelele zao zilizaa shinikizo lililosukuma masaa kadhaa baadaye. Asubuhi ya siku iliyofuata, Mkuu wa kituo alitoa ripoti ya awali kuhusu afya za majeruhi, pia alitaja majina na vitu vingine vilivyoteketea. Majina ya kina Bi. Mwema na wenzake yalikuwa miongoni mwa majina tajwa, tena walio na hali mbaya kwa sababu chumba walichohifadhiwa ndimo moto ulianzia. Malalamiko hayakukosekana, lakini nguvu ilikosekana, kuyasogeza mbele yajadiliwe. Kwani, punde baada ya ripoti hiyo kutolewa, mikutano ya kiharakati ikapigwa marufuku. Mwanaharakati yeyote hakupaswa kufanya mkutano eneo ambalo hakuchaguliwa. Midomo ilifungwa zaidi! Yote ni mipango ya mzee Tualike, katika kuelekea mpango wake mkuu. Wapo wanaharakati waliopinga vikali amri hiyo, hasa wa upinzani. Wao waliendeleza kufanya mikutano ila kila wafanyapo, vyombo vya dola vikawa karibu yao kuwazuia, wakati mwingine kutoa kipigo kabisa.
Naam! Utawala wa Mungu mtu! Endapo walipata fursa ya kufanya kwa kibali, kamera za vyombo vya ulinzi na usalama, hazikubanduka kurekodi tukio moja baada ya jingine litokealo pamoja na hotuba za viongozi wote waongeao. Ili kama katika hotuba zao kuna maneno ya maudhi, kashfa na udhalilishaji kwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, mzee Tualike, achukuliwe hatua. Hayo ndiyo maisha ya Tuleane, chini ya utawala wa mzee Tualike, aliyejinasibu kupenda amani na upendo kwa muda mrefu, kabla hajawa madarakani.
Mambo ya ajabu yalianza kuibuka. Ufukuzaji wa watumishi kazini pasipo kufuata taratibu, ulioambatana na vitisho vikali, wasipomsujudu na kusujudu watu wengine pia waungao mkono haja zake. Upotevu na utekaji wa watu ulishamiri, walio na kimbelembele, kama wasemavyo wahusika walioko madarakani. Watu walipotea, hususani waandishi wa habari, walioandika habari zenye ukweli zinazohusu serikali, ambazo walishindwa kuwajibika ama kutoa ripoti isiyo sahihi kwa umma. Wenye vimbelembele vya kuhoji uhalali wa matukio yatendwayo na serikali, ama wasifu wa mtu, nao walitoweka kama wanyama, vyombo vya ulinzi na usalama vikikaa kimya bila kutoa maendeleo ya upelelezi waufanyao.
Siku nenda rudi, afya za majeruhi ziliendelea kuimarika, walioungua sehemu ndogo za miili walipata nafuu. Lengo la kuwakomesha lilizidi, baraza likaendelea kupanga tarehe kila leo kusikiliza mashtaka yao. Japo walifahamu wahusika wako Zahanati kwa matibabu. Walipanga tarehe kwa awamu mbili. Walipoona washtakiwa hawahudhurii barazani, baraza lilitoa hukumu.
Hukumu ilivyopitishwa, walihamishwa, afya hazikuangaliwa. Gerezani walifikishwa. Matibabu yao yakawa yanatolewa na Zahanati ndogo ya gereza. Sasa kila kitu kilifanywa kwa ajili ya kujitengenezea mazingira mazuri ya mabadiliko ya katiba waliyopanga.
Katika muendelezo wa mafanikio ya mpango wao, Jipendekezo alipelekwa mafunzoni, ndani ya jeshi la mgambo. Mafunzo yalichukua muda wa miezi sita. Baada ya hapo akawa mwajiriwa kamili baada ya majibu yalitolewa siku ya kuhitimu kumpatia upendeleo wa aina yake.
Siku iliyofuata, chuo cha mafunzo ya uafisa waliripoti. Nafasi ya baba ilimbeba Jipendekezo, hata kama hakustahili vigezo vyote. Naye akawa mmoja mwa wafanikiwa.
Mambo yalienda kasi, mafunzo yao yalikuwa ya muda mfupi, wakapewa kamisheni. Kusudio, Jipendekezo kawawa wakuu wa jeshi la mgambo jambo lililokataliwa na wengi, na kuvunja mioyo ya mgambo wenye vyeo vya chini. Manung’uniko yao hayakusikilizwa, na onyo kali lilitolewa. Mwenye kauli mbaya ama atayehisiwa kuunda njama mbaya, cha moto ataoneshwa. Hicho ndicho kilikuwa kitisho cha wakati huo. Vyeo haraka alipandishwa, ukuu aliufikia, ndipo hoja ya mabadiliko ya katiba, ofisi elekezi ilitolewa na mmoja wa wenyeviti wa mitaa anayemuunga mkono mzee Tualike. Wakati huo tayari ilishakata miaka mitatu, mmoja ulibakia muhula wa kwanza kuhitimisha. Viongozi waungao harakati za Bi. Mwema, walibakia wawili, Awetu na Dkt. Emmakulata, wengine walifariki kutokana na ile ajali ya moto wakiwa gerezani. Hata wao nao muda huo walikuwa gerezani wakitumikia kifungo cha maisha.
Pia kipindi hicho, hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, sheria mbalimbali ziliibuliwa ili kuwabana wananchi wasifurukute kwa namna yoyote. Kama vile kuwekewa kodi kiasi kikubwa katika biashara ndogo ndogo, ushuru wa mazao nao kupanda, malipo kufanywa sehemu lukuki, mkulima anapohitaji kusafirisha ama apelekapo kuuza ghalani kote alitozwa kodi. Jambo jingine, ni kupangiwa sehemu za kuuzia mazao. Vyombo vya habari, hasa binafsi, navyo vilibanwa, vilipangiwa habari za kurusha, matukio yahusuyo serikali, matukio ya kuisifu pekee, ndiyo waliamriwa kurusha, yale yenye malalamiko, walizuiliwa vikali na endapo wahusika walikaidi, kituo husika hufungiwa na mwandishi aliyerusha tukio husika kutekwa na kupotezwa uraiani, yote kuuaminisha umma kuwa Mwenyekiti wao, ni mtu mwenye nia njema na kijiji.
Hivyo malalamiko juu ya hoja hii, yalibaki kuwa chini na kuenea tu mtaani. Hakuna chombo chochote kilichojaribu kuandika ama kutangaza kinachoenda kutokea ni kinyume cha sheria. Hata kama viongozi wa upinzani walitoa maoni yao, yaliishia muda huo waongeao baada ya hapo, hakuna sehemu nyingine yaliposikika. Wale walioko upande wa utawala, watoapo, ambayo hujaa utetezi wa hoja, basi muda mchache tu, yalienea kwenye vyombo vyote vya habari vilivyoachwa huru pasipo kufungiwa. Mjadala uliibuka! Ndani ya ofisi elekezi, moto ulifuka, wenyeviti kutetea na kupangua hoja ya uongezaji muda wa utawala kwa kiongozi aliyeko madarakani. Siku mbili ulichukua tamati kuifikia, pasipo na chembe ya uangalifu, uliridhiwa. Japo wapinzani walijitahidi kupinga, hoja zao hazikuthaminiwa, uwingi wa wenyeviti wa utawala dhidi ya wapinzani, ulipelekea kuridhiwa.
Mtaani mambo yakawa ovyo, taarifa ilivyowafikia kuwa muswada umetua mezani kwa mzee Tualike. Hamasa ya kuandamana wakaijenga, utawala dhalimu kuukataa. Uridhiano hoja watoazo wao ulipotea hata za wananchi kuzikana.
“Huu utawala sio kabisa, kama wanahitaji mabadiliko ya katiba, wabadili katiba nzima. Sio kwa kifungu kimojakimoja, tena wakionacho kinawabana.”
“Sahihi! Awamu hii tusirembe, tuwaoneshe nguvu ya umma ilivyo. Kila siku tumekuwa tukipiga kelele waondoe kinga ya viongozi wakubwa wamalizao madaraka ama hata akiwemo madarakani hawataki. Kama wao ni watiifu, na wapenda maendeleo ya wananchi wangefanyia kazi hoja hizi.”
“Yaani acha tu. Ila sasa hivi wananchi tumekuwa werevu, uongo wao tushauzoea. Moto lazima uwake, huo muswada ukipitishwa kuwa sheria.”
Maoni ya wananchi.
Kipindi wananchi wanahimizana kuandamana, mzee Tualike na watu wake, Jipendekezo, Majungu, Sabaya na Maroda kwa usiri mkubwa, walikutana kila siku jioni kuratibu mipango yao ili kuhakikisha wanayadhibiti maandamano yaliyopangwa. Pamoja na kuwatafuta wahamasishaji wa tukio hilo. Walitaka wawazibe midomo kama walivyoanza kwa kina Bi. Mwema na watu wake, ambao walishahukumiwa kifungo cha maisha. Yote kujihakikishia ulinzi wawapo na nguvu ya wananchi, sababu walishakuwa na ufahamu kuwa wananchi wa Tuleane wengi wao ni waoga. Hivyo endapo wataweza kuwatuliza waanzishaji, basi waliosalia hawatakuwa na nguvu ya kuendeleza.
“Mwanangu, sikukosea kukuweka kuwa mkuu wa jeshi letu. Lengo unipatie ulinzi wa kutosha mzee wako. Hiki kitu kilicholetwa kwangu, ni mpango tulioupanga muda mrefu baina yetu kabla hatujaanza harakati za kisiasa, hivyo fanya kweli, kunipatia ulinzi wa kutosha na ulioimarika.”
“Baba! Wala usihofu, kwa asilimia zote. Hilo jambo lazima lihalalishwe. Hamna takataka ya kutushinda, sisi ndiyo washika mpini wa kijiji hiki.”
“Nashukuru sana kama unafahamu hilo, kwani inatulazimu kutimiza tulichopanga ili kujiwekea ulinzi, maana tukitoka tu madarakani usalama wetu unaweza kuwa mdogo. Tumefanya mambo mengi mabaya kwa manufaa yetu na sio wananchi, hivyo hakikisheni wote kwa ujumla hatukosei.”
“Tumekuelewa mzee.”
Mikakati ilikuwa mingi, toa huu weka ule, mwisho wa siku walianza doria za chinichini kumtafuta anayehamasisha. Walizunguka mitaa yote, vijiwe na sehemu mbalimbali za ulabu, ambazo watu wengi hutumia kuhabarishana mambo yaliyo na yatayojiri kijijini kwao baada ya wasikiapo radioni na runingani.
“Jamani, huyu ndugu anaonekana kuwa na machungu mengi na utawala wetu.”
“Tena sana, halafu si alishakuaga mgambo huyu kipindi cha nyuma?”
“Yeah! Na alikuwaga mbabe sana. Kiasi kwamba mtu ukiingia mikononi mwake, hutoki salama.”
“Sasa imekuaje akaacha kazi?”
“Nimesikia kuwa, kipindi cha uchaguzi, matokeo yalivyotangazwa, yeye alikuwa mmoja miongoni mwa mgambo waliokuwa wanatoa kichapo cha nguvu kwa wananchi, kuhalalisha matokeo, kuona hivyo baadhi ya watu walienda kuchoma moto nyumba yake, uliopelekea kuondoa uhai wa mwanaye na mali zake nyingi zilizoko. Alifahamu hilo baada ya kurejea nyumbani, kwenda kuomba msaada kwa viongozi wake, wakamlazimisha aingie kazini, ndipo atatuliwe shida yake.”
“Acha utani ndugu.”
“Huo sio utani kaka. Viongozi wengi hawathamini watu wao wa chini, wajiangalia wao tu. Tena sehemu ambayo huyu jamaa alikuwemo, imezidi. Unaweza kumuomba ruhusa kiongozi una matatizo ya kifamilia, anakukatalia na kukulazimisha ufanye yeye akitakacho kwa manufaa yake, tena kama kapewa amri kutoka kwa mkuu wake, aliyemzidi cheo hapo panakuwa na shida zaidi, mnaweza hata kupigana,” yalikuwa ni maongezi ya wazee fulani, wakipata moja baridi moja ya moto katika baa wakihabarishana habari juu ya mtu aliyeandaa maandamano ya kuukataa utawala uliopo madarakani kupitia kipeperushi kidogo kilichochapwa namna maandamano yatavyofanikiwa kufanyika.
“Hivi anaitwa nani huyo jamaa?” lilikuwa swali toka kwa Maroda, naye alikuwa amejumuika pamoja nao kulainisha koo pasipo na kutambulika kuwa ni mlinzi wa siri wa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, mzee Tualike aliyepo hapo kutafuta habari.
“Jina lake nimelisahau kidogo...” alijibu mzee aliyekuwa anamwaga ubuyu kuhusu mgambo huyo, ila hakumalizia kauli yake, Maroda akamkatisha.
“Maana ana jina gumu kulitamka,” alisema japo hakuwa na ufahamu wowote kuhusiana na huyo mtu.
“Tena sana!”
Ndivyo walifanya. Iliwarahisishia kupata habari wasizozifahamu kuhusu kilichopangwa na wananchi. Walikuwa radhi, kutembelea kijiwe zaidi ya wiki walivyogundua kina habari kemkem zinazohusu mambo ya serikali, hata kama ni ya tawi, ilimradi wapate dondoo. Hivyo zile alizozipata Maroda kuhusu mgambo aliyeacha kazi miaka ya nyuma, baada ya familia yake kuteketezwa na moto aliwataarifu wenziye, kisha walianza fuatilia, mgambo huyo ni nani. Sehemu ya kwanza ni kituo kikuu, ambapo walishapata taarifa kuwa ndipo alikuwa anafanyia kazi. Moja kwa moja, Jipendekezo alijitosa kufuatilia, ili wahojiwa wasibaini kama anatafutwa kwa nia mbaya. Ukuu alionao ulimsaidia. Wala hakudhaniwa kama yake nia ni ovu. Faili zilikesha kuchambuliwa, lake jina lilivyobainika, lakini hakukuwa na matokeo chanya. Faili lake hawakuliona! Hawakuishia hapo, waliendeleza jitihada, masijala zote ila matokeo yalilingana. Jambo lililoibua chukizo moyoni mwa Jipendekezo, kwanini wamekuwa na utunzaji mbaya wa nyaraka zihusuzo askari na watu wengine.
“Hivi sasa anaishi wapi huyo mtu?”
“Hakika hatufahamu afande,” alijibu Mkuu wa kituo.
“Kuna mtu mwenye mawasiliano yake?”
“Hapana, namba zote alizokuwa anatumia sasa hazipatikani.”
“Aliyekuwa rafiki yake?”
“Pasipo kukuongopea afande, mtu tuliyekuwa tunafahamu ni rafiki yake mkubwa, mwisho wa siku tuliona wakigombana, kwa sasa sina hakika kama wana mazoea na ukizingatia mtu mwenyewe amepotea kabisa maeneo haya ya mtaani kwetu.”
“Fanyeni jitihada za kumtafuta, popote atakapoonekana mnipe taarifa.”
“Sawa afande.”
Akaondoka.
Hakukubali kwa urahisi hivyo, baadaye alitoa amri ya kuweka chini ya uangalizi eneo zima la kituo, kwamba mtu yeyote atakayepiga simu abainike anapiga kwenda wapi na anawasiliana na nani. Ili ikitokea mmoja wa mgambo akifanya mawasiliano na yule wanayemhitaji wamchukulie hatua, na ikibidi wamtumie kumpata huyo mtu, Kitenge Malimuka. Hilo halikusumbua watu wa mtandao, walilitekeleza kwa usiri kiasi kwamba, ni mkuu wa kituo pekee ndiye alikuwa anafahamu. Wakati huo Sabaya na Maroda nao waliingia mtaani kumfuatilia. Iliwapatia wakati mgumu kufanikiwa, kwani walikuwa wanamtafuta mtu wasiye na ufahamu wa anuani yake. Kila kukicha, Jipendekezo akawa anapatiwa taarifa za kazi inavyoendelea, naye alimtaarifu mzee wake. Ugumu wa kumpata uliwaongezea hasira na kuwafanya kuweka ahadi nyingi za kuondoa uhai wake, hata kama ni mbele ya halaiki.
Timu ya upelelezi iliundwa kuchunguza, kwanini mafaili ya askari yalipotea. Majibu yalipatikana wiki moja baadaye, kwamba, baada ya uchunguzi, walibaini kuwa yalitupwa jaani na kuteketezwa kwa moto. Jambo hilo lilitokea muda ripoti pendekezi ya uchunguzi hawakuijadili sana. Waliishia kuongeza mikakati ya kufanya doria kwa sana ili wampate mhusika. Awamu hii mgambo wenye vyeo vya chini walihusishwa, baada ya kupewa maelezo kwa kina kuhusu mtu anayehamasisha maandamano. Doria ilitii—mtaa kwa mtaa. Vijiwe vyote na mapori waliyoamini wahalifu hutumia kujificha walifika.
Mgambo walimsaka kwa namna yao, wakimkamata wamfungulie mashtaka. Walinzi wa siri wa mzee Tualike nao walimsaka wajuavyo wao, wakimkamata wamuondoe duniani. Matangazo hayakuisha kutolewa, kuhitajika kwa mtu huyo, kwenye vyombo vya habari yaliyosheheni utoaji wa donge nono kwa atayefanikisha ukamataji wake. Lakini lilikuwa jambo gumu kufanikiwa.
Kila lililoendelea lilitua masikioni mwa Kitenge Malimuka, kupitia redio ndogo aliyonayo bega kwa bega, akiambatana na mke wa aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi, ambaye alifariki miezi kadhaa baadaye, kwa sumu aliyowekewa kwenye maji aliyokuwa anatumia kunywa siku anatangaza matokeo.
Usaliti aliouonesha awali ndiyo ulipelekea afanyiwe hivyo. Kitenge aliungana na mwanamama huyu, aliye na vielelezo vya ushahidi, vyenye kuonyesha kuwa mzee Tualike na serikali iliyopita wametumia njia isiyo halali, kuhalalisha ushindi. Wakati huo walikuwa wameweka maficho katikati ya msitu mkubwa wa kijiji, uliopo karibu na hifadhi ya wanyama pori ya kijiji, Nanenane.
Mikakati iliandaliwa kutokana na hasira walizonazo, za upotevu wa mali na sehemu za familia zao. Maandamano ndiyo mkakati wa pekee, waliokuwa wanauratibu kila leo waamkapo. Wanakijiji wakosoapo mambo yanayowakandamiza muda wote, walikuwa wanacheza na maandishi, kuyaandika katika karatasi mbalimbali na hatimaye kuunda vipeperushi walivyovimwaga usiku wa manane kwenye vijiwe vya ulabu kijijini kisha kurudi tena msituni. Pia, ni muda huo mke wa marehemu mzee Kumwembe, alitumia kuuachia ushahidi hadharani. Zile sauti za maongezi alizozirekodi, alirushia kwenye vifaa mbalimbali vyenye uwezo wa kuhifadhi sauti, jumbe alizichapa kwenye karatasi, hivyo pindi wanamwaga vipeperushi, navyo aliviachia.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waokotaji walikula mambo, yaliyofungua bongo zao, na kuwashawishi wafanye utafiti kama kile wasikiacho na wasomacho kina uhalisia. Sauti ilienea, ilipandisha morali na hamu ya kutekeleza maandamano kwa namna yoyote. Pindi baadhi yao wanasadiki maandamano, wengine walishauri kufungua shauri barazani, hoja iliyopingwa vikali.
“Hakuna baraza la kumhukumu mwenyekiti hapa kijijini.”
“Eeh! Kweli. Wanamuogopa. Wanaogopa kupoteza ulaji.”
Walifanya majadiliano mengi, maamuzi ya kuchukua yalikuwa kizungumkuti, lakini mwishowe walikubaliana kufanya maandamano.
_____________
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment