Search This Blog

Friday, November 18, 2022

UMUTWALI - 3

 






Simulizi : Umutwali

Sehemu Ya Tatu (3)





“Donald, umemuona mrembo wa Loyola?,” David aliuliza kisha akazuga kwa kuendelea kufanya usafi pale kantini.



“Mrembo yupi?,” Donald nae aliuliza huku akigeuka upande sio sahihi.



“Kwani hapa Loyola, kuna warembo wangapi...si Fatuma tu au kuna mwingine?.”



“Fatuma!!!...Fatuma yupo wapi?.”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Geuka, upande wa nyuma.”



“Oooh, nishamuona...halafu leo anaonekana ana furaha sana,” Donald alisema mara baada ya kugeuka nyuma na kumuona Fatuma.



“Sijajua...labda kafurahi kukuona,” David akahisi.



“Anifurahie mie, kwa kipi?.”



“Kwasababu, wewe ni mtanashati” aliongea kwa utani David hadi akampelekea Donald kufurahi. Wakiwa wanazidi kupiga soga wakashtukia Fatuma tayari kashajongea walipo.



“Hi,” Fatuma alitoa salamu kwa wote.



“Hi...mzima weye?,” Wote kwa pamoja wakamchangamkia Fatuma kisha wakamuuliza.



“Mi mzima...Sorry, Donald nakuomba pembeni tuongee,” Fatuma alisema huku akielekea pembeni kwa ajili ya mazungumzo ya faragha. Donald akamuacha David akiendelea na usafi akamfuata Fatuma asikilize wito.



“Donald, unajua nilichokuitia?,” Fatuma akauliza.



“Hapana.”



“Nimekuita, ili nithibitishe kweli unanipenda kama ninavyokupenda au lah...mie nakupenda sana na sijawahi kumpenda mwanaume yeyote kama ninavyokupenda wewe. Wewe ndiye mwanaume wa kwanza kwangu niliyekukabidhi moyo wangu na kuniteka akili yangu, nawe kweli kabisa unanipenda au unanitamani tu?,” Fatuma alieleza hisia zake huku machozi ya upendo yakimdondoka taratibu mashavuni.





“Sijakutamani Fatuma, bali nimekupenda sana tena sana...naahidi leo mbele yako kuwa sitokusaliti Fatuma zaidi nitakupenda daima,” Donald alimfariji Fatuma kwa maneno matamu huku akimfuta machozi.



“Nafurahi kusikia hivyo Donald, sasa ngoja nikuache niende darasani kufagia si unajua leo zamu ya wasichana nisije nikalia bure baadae,” Fatuma aliaga na kumchombeza busu Donald kisiri.



“Acha basi nami nikuache, nikaendelee na usafi,” Donald nae aliongea kisha mwishowe akapapasa shavu lililopigwa busu akuamini akahisi kama yupo peponi. Akaondoka na furaha pale baada ya kuona Fatuma nae kaondoka, akarejea tena alipo David.



“Rafiki yangu, kinaendelea nini?” aliuliza David mara baada ya Donald kufika karibu yake.



“Kuhusu nini?.”



“Kuhusu wewe na Fatuma.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Hamna kitu kinachoendelea.”



Usinifiche rafiki yangu, mie nimeona kila kitu kilichoendelea pale mliposimama na Fatuma. Hivyo basi usijaribu na usiendelee kunificha.”



“Mh, kumbe umeona basi hakuna sababu ya kukuficha...bwana rafiki yangu David mie na Fatuma kwasasa tupo kwenye mahusiano ya kimapenzi. Na hivi ninavyokwambia tumepanga mambo mengi ya mimi na yeye,” David mara baada ya kusikia vile akafurahi hatimaye akatulia kidogo kisha akasema kwa sauti ya chini ili washakunaku wasisikie anachotaka kusema.



“Lakini Donald, wewe mwenyewe angalia kipindi tunachokwenda kigumu mno. Kipindi hiki ni cha mitihani ya mwisho, angalieni msije mkafeli mkashindwa kutimiza ndoto, maana familia bora ni ile ya baba na mama kupata elimu, nyumba na hatimaye watoto...kwahiyo basi nakushauri kama rafiki jitahidini kwenye masomo kwa pamoja ili mpate sifa ya kuwa wazazi bora na si bora wazazi,” David akashauri. Na kwa kuwa Donald alimuamini sana rafiki yake basi haikuwa rahisi kumpinga, akamsikiliza na mwisho akaahidi kufanyia kazi ushauri wa rafiki. Donald na David wakiwa bado wanafagia mara kengele ya kwenda mstarini ikalia, haraka wakaacha kufagia upesi wakapeleka fagio stoo kisha wakatimua mbio kuelekea mstarini kumsubiri Sir Daniel aje kuwapa matangazo.



“Nisikilizeni kwa makini, tangazo la leo ni moja tu na linawahusu kidato cha nne. Kidato cha nne mna miezi michache tu ya kuingia kwenye chumba cha mitihani yenu ya mwisho...hivyo basi nipo hapa kwaajili ya kuwakumbusha na kuwaomba kuwa kidato cha nne mjisomee kwa bidii ili hapo baadae mpate nafasi ya kuingia kidato cha tano,” Sir Daniel alitangaza tangazo kisha akawaruhusu wanafunzi wote waingie madarasani.



Wanafunzi wote wakatawanyika na kila mmoja akaongoza kwenye darasa zao, Donald na David wao nao wakaongoza kwenye darasa lao wakaingia mwisho wakaelekea kwenye viti kuketi. Na kwa kuwa walisoma darasa moja na Fatuma pamoja na Amina pia viti vyao ni jirani, hivyo walipofika kwenye viti wakae. Amina akaanza kwa kutoa salamu ile ya sitaki nataka.



“Hello.”



“Hello...wazima?,” Donald na David wote kwa pamoja wakaitika salamu mwisho wakauliza.



“Wazima, hofu kwenu,” Fatuma akajibu.



“Sie tupo poa,” Donald akaongea. Baada ya salamu wote wakanyamaza, Donald akawa anamtazama Fatuma kwa kuibia.



Wakazidi kutazamana kwa wizi hadi pale mmoja alipohisi aibu, Donald akahisi aibu akakaa tuli kwa muda akiangalia chini na bila mwalimu kuingia darasani. Baadhi ya wanafunzi wakahamua kuchukua daftari kwa ajili ya kujikumbusha ya nyuma. Wakajikumbusha mpaka wakati wa mapumziko, wanafunzi wote wakaenda mapumziko kula. Donald akaongozana na Fatuma kantini kwa ajili ya kupata msosi pamoja.



“Donald, tokea nianzishe mahusiano nawe...mbona naona aibu imekutawala?” aliuliza Fatuma mara baada ya kufika kantini na kununua chipsi na mwishowe kumkaribisha Donald wale.



“Hamna kitu kama hicho...aibu haijawahi kunitawala nikuonapo, kwanini umeniuliza hivyo?,” Donald akakataa. Akauliza huku taratibu akila chipsi alizokaribishwa.



“Kwasababu, naona macho yako yananikwepa sana kupita maelezo siku hizi.”



“Hamna...nahisi pengine ni mitihani tu ndiyo inayoniweka katika usawa huo.”



“Mitihani!!!, mitihani imefanyaje?.”



“Naifikiria sana.”



“Kumbe!, basi nilijua unanionea haya...basi kama ni hivyo usifikirie sana ukaja kufa na presha bure.”



“Nitajitahidi yote sitofikiri, mara kumi nitakufikiria wewe tu,” Donald alieleza huku maneno yake yakionyesha kubeba hisia kiasi fulani.



Wakamaliza maongezi walipomaliza kula wakachukuana moja kwa moja hadi darasani walipofika, wakakuta wanafunzi wakiendelea na zoezi lile lile la kujisomea wakaungana nao. Wakajisomea mpaka nyakati za mchana muda wa kurudi nyumbani ulipowasili njiani safari hii wakaongozana wote wanne Donald, Fatuma, David na Amina hadi kwenye kituo cha daladala cha Garage. Hapo ndipo David akawaaga wenzake kisha akavuka barabara kuu kwa ajili ya kwenda kusubiri usafiri wao katika kituo cha upande wa pili, nyuma akiwaacha nao wenzake wakisubiri daladala yao ya Mbezi. Daladala ikawasili wakabahatika kupanda Fatuma na Amina, Donald nae alipotaka kupanda Kondakta akamgomea kisha akasema.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Wanafunzi sasa wanatosha, daladala hii si ya kupakiza wanafunzi kama kumbikumbi,” Kondakta alisema huku akimuamuru dereva aondoe gari.



Hatimaye gari likaondoka, Donald akasalia pale kituoni mwenyewe. Akasonya kisha akajenga chuki kwa Kondakta, akamuona kama Kondakta ana ubaguzi wa kijinsia lakini ndiyo atafanyaje kama kutokea tayari yashatokea ikabidi aketi tu pale kituoni asubiri daladala nyingine. Dakika kadhaa zikapita mara Donald akatupa macho ng'ambo ya pili kwa ajili ya kumuangalia rafiki yake David kama nae kashaondoka, lakini kweli alipoangalia hakubahatika kumuona David kwani alikuwa tayari ameshaondoka. Donald akavuta subira akasubiri usafiri na ndani ya masaa kupita akaona daladala ya Mbezi ikiwasili, akatabasamu kisha akaingia moja kwa moja kwenye daladala hatimaye akaenda kuketi kwenye siti ya nyuma. Muda mfupi tu pale Donald akapitiwa na usingizi.



“Wakushuka Kimara Suca?,” Donald akiwa usingizini akamsikia kwa mbali Kondakta akiuliza mara baada ya daladala kufika kwenye kituo cha Kimara Suca.



“Nishushe..!!,” Donald alikurupuka usingizini kisha akaongea kwa kupayuka.



“Dogo, mbona mzembe?...hivi darasani unakuaga hivyo?. Maana nimeuliza wee kama kuna mtu anashuka Kimara Suca lakini kimya sasa gari linakaribia kupita kituo hicho unasema shusha tena kwa kuropoka kama changudoa aliyechelewa kwenda kujiuza” aligombeza sana Kondakta.



“Bro, mimi ni mwanadamu nilipitiwa na usingizi naomba tusameheane bure,” Donald akajishusha.



“Hebu...shuka yaani nyie Njuka ndivyo mlivyo mnapenda kutusumbua tukiwapiga marufuku kupanda kwenye daladala zetu mnaona tunawaonea kumbe mnajitakia,” Kondakta alizidi kufoka hadi Donald akajihisi aibu mbele ya umati wa abiria wengine.



Donald akashuka kwenye daladala lakini akiwa ameghadhabika na maneno ya Kondakta. Kinyonge akaelekea kwenye ofisi ya Fundi Castle kabla ajaenda nyumbani, akafika ofisini pale kwa Fundi Castle akamkuta Fundi Castle akimalizia kutengeneza gari aina ya NOAH lililokuwepo pale ofisini kwake.



“Donald, vipi mdogo wangu?” alisalimu Fundi Castle.



“Safi tu...shikamoo,” Donald akajibu.



“Marahaba.”



“Fundi, mama kaniagiza nije kukufuata ukamtengenezee gari lake.”



“Lina tatizo gani?.”



“Lina pancha.”



“Sawa, nisubiri nimalizie hili gari halafu twende,” Fundi Castle alisema kisha Donald akatulia akimsubiri, kama dakika kumi na tano hivi fundi akawa ameshamaliza kutengeneza gari lile mwishowe akaingia ofisini kwake kuchukua begi la mgongoni ambalo mara nyingi anawekea vifaa vyake vya kazi. Akatoka.



“Dogo, njoo upande gari tuondoke,” Fundi Castle alisema huku akifungua mlango wa gari ili Donald apande waondoke.



Donald akapanda garini hatimaye Fundi Castle akaondoa gari eneo lile, hawakuchukua muda kufika nyumbani ndani ya nusu saa tu walikuwa washawasili mjengoni. Fundi Castle akapiga honi haraka Dada Angel akaja kufungua geti, gari likaingia ndani Donald na Castle wakashuka garini. Donald akaingia ndani na Dada Angel akamuacha nje Fundi Castle akiziba pancha, akapitiliza akaingia chumbani kubadili nguo pia akamuacha Dada Angel sebuleni akiangalia runinga. Akabadilisha nguo akaenda kwenye droo kuchukua na kuwasha simu, simu ilipowaka tu Donald akazikuta jumbe tatu. Ya kwanza ilikuwa ya Fatuma ikisomeka ifuatavyo;



“Mpenzi, ushafika nyumbani?.”



Ya pili ilikuwa ya David ikasomeka ifuatavyo;http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Mwana, mie nishafika nyumbani. Wewe je, umefika?.”



Ya mwisho ilikuwa ya Amina ikasomeka ifuatavyo;



“Shem, pale tulipokuacha stendi ulipata usafiri mapema?.”



Sababu Donald hakuwa amejiunga kifurushi upesi akakimbia dukani kurusha kifurushi akarusha mwisho akarudi nyumbani. Akaingia chumbani akajiunga na kifurushi kisha akaanza kuchati na Fatuma. Akamtumia jumbe Fatuma iliyosomeka kuwa;



“Nimefika nyumbani tayari, mpenzi,” Donald akajibu kisha akatulia akisubiri Fatuma amchatishe. Akiwa anasubiri akamcheki na David kwa njia ya jumbe.



“Nimefika kitambo kidogo, kwasasa nipo sebuleni nacheki runinga,” Donald alijibu mara baada ya kutoka chumbani na kuja sebuleni kutazama runinga. Akuchelewa akamcheki na Amina kwa njia ya jumbe mara baada ya kuona kashawatumia jumbe Fatuma na David.



“Ukweli ni kuwa, usafiri ulinisumbua sana lakini baadae nikaja kuupata bila mbwembwe wala zengwe,” Donald akajibu. Hakukaa sana mara baada ya kumjibu Amina, Fatuma akawa amesharudisha ujumbe muda ule.



“Okay, siku njema nilitaka nijue tu kama usharudi. Kipenzi,” David kuona Donald anachelewa kurudisha ujumbe akuzubaa akapiga simu.



“Donald, mbona kimya sana...unachati na shem nini?,” David alisikika sauti yake ikiuliza mara baada ya Donald kupokea simu.



“Hamna kitu kama hicho, ni ubize wa hapa na pale tu alidanganya Donald kwa kummezesha mazingaombwe David.



“Mh, basi poa tutazidi kuwasiliana zaidi kesho.”



“Usijali” alikata simu Donald alipomaliza maongezi. Baada ya kukata simu tu! akakuta ujumbe uliotumwa na Amina.





“Shem, acha nikuache nitakucheki siku nyingine,” Donald baada ya kumaliza kuchati na wote ndipo akanyanyuka kitini akaelekea dinning kula, alipokula akatoka nje na nguo za shule kwa ajili ya kuzifua baada ya kufua na kuanika akarudi chumbani kujisomea hayakupita masaa akamsikia Fundi Castle akibisha hodi. Na wakati huo Dada Angel bado amemakinika na runinga hodi ikamfanya aache kuangalia runinga akainuka sofani akaenda kumsikiliza Fundi Castle.



“Dada, mwambie dogo kuwa nishamaliza kuziba pancha gari ya mama yake...aniletee mshiko wangu niondoke,” Fundi Castle alimpa maagizo Dada Angel amletee Donald.



“Sawa” alikubali Dada Angel mara baada ya kupokea maagizo yale. Na papo hapo hakuhitaji kumchelewesha fundi moja kwa moja akaja hadi mlangoni mwa Donald, akabisha hodi.



“Donald, fundi kaniagiza nije kukuambia kuwa yeye kashamaliza kutengeneza gari. Anahitaji malipo yake,” Dada Angel alimuambia Donald mara baada ya kufunguliwa mlango.



“Yupo wapi sasa?.”



“Kasimama nje ya mlango wa sebuleni, anakusubiri.”



“Basi mwambie, nakuja,” Dada Angel alimsikiliza Donald upesi akaenda kurudisha majibu kwa fundi, hatimaye akarudi sebuleni kuzima runinga kisha akaenda kufanya shughuli zake. Donald hakumuweka sana fundi, akatoka chumbani akiwa ameshika pesa ya malipo. Akampatia pesa fundi alizoachiwa na mama yake mara baada ya kufika alipo Fundi Castle.



“Poa dogo, ngoja mimi nikuache,” Fundi Castle aliongea kisha akamuaga Donald na kuondoka.



Wahenga hawakulaghai pale waliposema; Hayawi hayawi, sasa yamekuwa” kweli yakawa. Miezi miwili ikapita wanafunzi wa kidato cha nne wote wakaingia kwenye vyumba vya mitihani, wakafanya mitihani kwa umakini ili baadae waweze kufaulu. Katika mtihani mmoja Donald hakufanya kwa umakini sababu anataka amalize tu mtihani, hiyo siku likatokea tatizo kubwa kwake. Akiwa yupo kwenye chumba cha mtihani akimaliza ngwe ya mwisho akaona msimamizi akimuita baada ya kutoka kuongea na simu punde tu, Donald akajivuta kuinuka kwenda kumsikiliza msimamizi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Kijana, unahitajika ofisini kwa walimu,” Msimamizi alimuambia Donald na haraka Donald akaongoza ofisini. Kufika ofisini akamkuta Madam Odilo, mwalimu anayehusika sana na sekta ya michezo akiongea na simu. Madam Odilo baada ya kuona Donald amewasili akamkabidhi simu upesi aongee na mtu aliyekuwa akiongea nae. Donald akusita akachukua simu moja kwa moja akapeleka sikioni tayari kumsikiliza mtu wa upande wa pili aongee.



“Donald, naomba maliza mitihani yako kisha urudi nyumbani mapema” ilisikika sauti ya Mama Donald upande wa pili ikisema huku akilia, akakata simu.



Ukweli Mama Donald akamuacha Donald njia panda akiwa amesongwa na mawazo asijue anacholia mama yake. Kinyonge Donald akamkabidhi mwalimu simu akaaga akatoka pale ofisini baada ya kumaliza kuongea na simu, akarudi kwenye chumba cha mtihani akamaliza mtihani hatimaye akaharakisha nyumbani. Siku hii ni mbaya kwa Donald maana mawazo yakamsonga hata kuongozana na Fatuma ikashindikana, akajua kuondoka kimya kimya. Baada ya masaa kupita akawa kashawasili nyumbani hakuingia ndani nje tu kukamshangaza kuona umati wa watu umejaa huku nyuso zikichukiza na huzuni pamoja na machozi ya yakibubujika kwa kuomboleza, akashangaa mno maana si kawaida nyumbani kukakusanyika watu wengi vile, wazi akagundua nyumbani kutakuwa na tatizo ila hakujua ni tatizo gani. Donald akazidi kushangaa akijiuliza maswali kumi padogo mara Mama Donald akatoka nje, kutoka akamuona Donald akiwa bado anashangaa shangaa kama mtu aliyetoka mbwinde leo. Mama Donald bila kuchelewa akamvuta mkono Donald waingie ndani bila hata Donald mwenyewe kutarajia. Kufika sebuleni hapo akamueleza kinagaubaga Donald tatizo lililotokea.



“Donald, mwanangu!! pole sana,” Mama Donald aliongea huku akionekana kuwa na majonzi.



“Pole!!!...pole ya nini?,” Donald akauliza kwa kuhamaki.



“Nasikitika sana.”



“Na kipi?...mbona unaniweka kwenye mabano.”



“Nasikitika kuwa...kwa sasa hatunaye tena mzee wetu.”



“Mzee wetu yupi?.”



“Mtalanze.”



“Mtalanze yupi.... Babu?.”



“Hapana.... Mtalanze baba yako.”



“Unasemaje?...siwezi kuamini.”



“Donald pole na uwe mtulivu anachokisema mama ni cha kuamini, mapema leo baba amepata ajali wakati anaenda kazini. Ajali hiyo ndiyo imemfanya apatwe na umauti,” Dada Angel alikazia taarifa iliyomshinda Mama Donald kueleza. Kutokana na kuzidiwa rohoni na uchungu akaishia kulia na kubanwa kooni na kwikwi zisizo na ukomo. Mwili ukaganda kama umepigwa na kani ya umeme, nafsi ikafukuta huzuni na macho yakazidi kufurika mafuriko ya machozi huku kinywa kikilia na kunena maneno machache yasiyoeleweka.



“Umeniacha kwenye wakati mgumu baba!!.”



“Nilikuhitaji na nilikupenda sana. Sasa leo umeondoka.”



“Nani tena wa kunifariji na kunipa ushauri baba,” Mama Donald aliyatoa maneno kwa uchungu huku Dada Angel akisaidia kumbembeleza anyamaze.



“Mama, nyamaza jikaze basii,” Dada Angel alizidi kumnyamazisha Mama Donald.



“Dada, usidhani ni rahisi sio rahisi kabisa...unajua fika ni jinsi gani roho yetu ilivyouma kuondokewa na mtu tumpendae,” Donald alichangia mazungumzo mara baada ya kuduwaa na kulia kwa muda.



“Najua Donald, lakini yawapasa kujivika ukondoo. Na ukiangalia wewe ni mwanaume acha kulia bali umfariji mama, ukilia sana kichwa kitauma...hapa kinachotakiwa si kulia,” Dada Angel alitoa maneno ya kufariji.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Donald akayasikia ikabidi ajikaze kiume ilhali nafsi ilikuwa ikimuuma lakini akazidi kujikaza polepole akazimudu hisia akanyamaza, baadae akateua baadhi ya ndugu wachache akaondoka nao na gari kwenda kufuata mwili wa baba yake mochwari. Donald kidogo akiwa bado kwenye ombwe zito la masikitiko ndani ya gari ghafla akashtuliwa na mtetemo wa simu ikiita iliyokuwa mfukoni mwake, akaitoa akalazimisha tabasamu baada ya kuona jina la Fatuma kwenye kioo cha simu. Akasimamisha gari kidogo kisha akatelemka akajivuta pembezoni palipokuwa hakuna kadamnasi akapokea.



“Halloow!!!, Donald mpenzi mbona leo umeniacha?,” Fatuma akauliza.



“Nisamehe sana mpenzi, leo nimepatwa na tatizo,” Donald akajibu.



“Tatizo gani ulilolipata?, hadi umepelekea kuniacha pekeangu?.”



“Baba yangu.”



“Baba yako?, kafanyaje tena?.”



“Fatuma!!, Baa..ba yangu kafariki.”



“Aisee!!!, pole sana mpenzi...ngoja nijiandae basi nami nije kuhudhuria mazishi. Mazishi lini?.”



“Yatakuwa, kesho saa kumi jioni.”



“Sawa mpenzi, nitakuja basi.”



“Okay, nitakusubiri.”



“Sawa, pole sana.”



“Ahsante,” Donald akakata simu.



Akarejea kupanda gari akawasha gari akaendeleza safari wakafika hospitali wakachukua maiti wakarudi nyumbani. Wasaa huu watu wakapungua na zaidi ni majirani waliopungua wakasalia wanandugu wakazika. Siku mbaya ikapita huzuni ukapungua makali, kesho ikakucha ikawa siku nyengine taratibu za msiba zikaisha zote. Upendo wa Fatuma kwa Donald ukadhihirika katika kipindi kigumu alichopitia Donald. Kwani akamfariji Donald na baada ya msiba ule wote wakaondoka lakini yeye hakuondoka akabaki azidi kumfariji kipenzi chake. Mwaka mmoja ukakatika tangu kifo cha Baba Donald kitokee na matokeo ya kidato cha nne yatoke, matokeo ya Donald na Fatuma yakatoka mazuri. Kwa maana walifaulu wakachaguliwa kwenda kidato cha tano baada ya miezi kadhaa kutokea wasaa ambao matokeo yalitoka, Donald na Fatuma wakapangiwa shule moja wakaanza masomo kwa pamoja wakasoma. Muhula mpya wa masomo ulipowadia wote wakawa na furaha huku wakijua saa yoyote ndoto itatimia, bahati nzuri Mungu akasikia kilio chao wakafanikiwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita wakabahatika kuingia Chuo kikuu. Donald na Fatuma hatua hii wakatengana kila mmoja akabahatika kuchaguliwa Chuo kikuu tofauti cha kwenda kusoma.



**********

Baada ya mwaka mmoja Mama Donald akachoshwa na hali ya kukaa mpweke, akamsaka mwenza ambaye Donald kwa vyovyote angemuita UMUTWALI au Baba mlezi. Donald kama mtoto alivyopokea suala hili hakuwa na kipingamizi juu ya maamuzi ya mama yake akakubali, Mungu akatia mkono wa baraka kwa Mama Donald akamjalia akapata mwenza ambaye alikuwa ni Mwalimu mwenzake anayefundisha nae shule ya “Private” ya BETHEL INTERNATIONAL MISSION SCHOOL aliyetambulika na majina ya Sir au Mr. Stanley Msunga. Mr. Stanley Msunga akabahatika kuishi na Mama Donald katika nyumba moja kama mume na mke, maono ya Donald yakaonesha dhahiri kwamba Mr. Stanley Msunga hakuwa na mapenzi na mama yake bali Mr. Stanley Msunga alikuwa ni mtu wa starehe na aliyelenga uchumaji wa mali kwa mama yake. Japo mwanzoni Mr. Msunga alimpenda Mama Donald lakini kadri siku zinavyosonga na wao kuzoeana mapenzi yakaanza kuota miiba yakabadilika taratibu.





Donald na Fatuma furaha ikatoweka ikaleta huzuni kwao. Yote sababu Donald anakwenda kusoma Mzumbe University na Fatuma anakwenda kusoma University Of Dar-es-salaam, kutengana kwao Donald akahisi kuwa penzi lao litakufa kutwa akanyongea. Kesho ikakamilika safari ya kwenda Morogoro kuanza masomo ikawadia, Donald siku hiyo hakuchangamka alikuwa ni mtu wa mawazo tu yote kwa ajili ya kuwaza penzi. Mama Donald hali ya Donald akaiona akahamua kumfuata alipo pale kwenye sofa sebuleni.



“Mwanangu, mbona unaonekana una huzuni sana...kipi kinachokutatiza?,” Mama Donald akauliza.



“Kwa kweli mama yangu.., dah! sijui nianzaje?,” Donald nae akauliza.



“Nini tena mwanangu?.”



“Mama nilikuficha mno...sijui kama ulijua ni jinsi gani ninavyompenda Fatuma.... Ukweli ni kuwa ninampenda sana Fatuma,” Donald akajibu kwa hisia.



“Eeh, Fatuma mwenyewe anajua?.”



“Anajua.”



“Sasa hiyo huzuni ni yake...yeye ndiye anayekufanya uwe mwenye huzuni?.”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ndio ni yeye..., hivi niendapo kusoma Fatuma hatotumia fursa hii kunisaliti?,” Donald aliuliza huku akijiweka sawa asikie jibu la mama yake.



“Kama kweli mnapendana, hatoweza kukusaliti amini hilo...na kama hofu yako kuwa utachukua muda mrefu masomoni bila kumuona Fatuma tafadhali ondoa hofu maana miaka mitano si mingi sana, vumilia utakuja kumuona tu,” Mama Donald alimfariji Donald, hadi Donald akapelekea kustawisha tabasamu. Huzuni haikuwa upande wa Donald pekee, huzuni ilikuwa hadi upande wa Fatuma. Fatuma nae huzuni ikamgubika akahamua kumpigia Donald mpaka simu ili amueleze anavyojisikia kuwa usiku ameshindwa kupata lepe la usingizi sababu ya mawazo ya kumfikiria yeye.



**********



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog