IMEANDIKWA NA : SADARI KISESA
*********************************************************************************
Simulizi : Umutwali
Sehemu Ya Kwanza (1)
UTANGULIZI...
“Umutwali katika kabila lenye hasira kali lina maana kuwa ni Baba wa kambo. Baba wa kambo tamaa ya mali na haraka ya kutajirika ndiyo inamfanya kupitia katika mateso na misukosuko, anaona dhuluma ndiyo njia ya kumletea mafanikio kumbe la hasha! anajidanganya. Ajui kama dhuluma ni dhambi na baadae inampa majuto, anazidi kutumbulia macho mali ili afanye janjajanja amtaifishe mama. Baba wa kambo pambana na hali yako pia jua ya kwamba; Siku zote cha mtu hakiliwi na kikiliwa matokeo ni kama ya wanasiasa na wafanyabiashara katika kikaango cha uhujumu uchumi, yaani Baba wa kambo unafanya kila liwezekanalo kwaajili ya kuweka kibindoni mali za mama aliyekuwa mjane ambazo kazitolea jasho. Tabia hiyo yafaa kutafsiriwa kuwa uhaini yenye kukera na isiyopendwa na mwenye nafsi. Waswahili usema; “Bora umfadhili Mbuzi utamnywa mchuzi, na kuliko umfadhili binadamu ukaambulia mashuzi”. Hii husadifu maudhui tanabaishi juu ya unyama wa Baba wa kambo hasa lijapo suala la riziki. Baba wa kambo akampenda mama kwaajili ya kitu alipokomba kile alichokilenga akageuka kuwa Kinyonga, si kwa Baba wa kambo vivyo hivyo kwa Mtanzania na Mwafrika mwenye pumzi na nafsi hai. Msomaji tahadhari na daima ogopa mali zako hazikai mikononi mwa binadamu wa laghai kama Baba wa kambo. Waepuke walowezi maana hao ndiyo watakaothubutu kukuporomosha kutoka juu, kweli tena tamaa ya mali inamfanya mtu akengeuke afanye yasiyofaa katika jamii. Nakusihi sasa jihami na mali zako kama sanamu la askari lililopo katikati ya jiji la Dar es Salaam pale mjini Posta. Lilivyoshika mtutu wa bunduki tayari kujilinda.
SONGA NAYO...
“Kwa utambulisho anaitwa Donald Mtalanze, amezaliwa katika familia yenye wadhifa kiasi na yenye mtoto mmoja tu ambaye ni yeye pekee. Baba yake Donald anafahamika kama Daktari Zungu Mtalanze katika hospitali ya Taifa ya MUHIMBILI, na mama yake anatambulika kama Madam. Leah Zwambanga katika shule ya kulipia “Private School” ijulikanayo kwa jina la ST. MARYS INTERNATIONAL SCHOOL. Donald Mtalanze ni mtoto mpendwa wa Mzee Zungu na Bi. Leah Zwambanga, na ni mwanafunzi bora katika shule yake ya LOYOLA HIGH SCHOOL. Ukweli ni kuwa familia ya Mzee Zungu ikaishi kwa upendo na furaha hakukuwa na mikwaruzo, kila mmoja katika familia ya Mzee Zungu akajiwekea taratibu. Wakajiwekea taratibu ya kuwajibika katika vitengo. Wa kazini wakawahi kazini, wa shuleni ambaye ni Donald akawahi shuleni, akasoma kwa bidii baadae aje kuwa msomi kama wazazi wake. Pia familia hii ya Mzee Zungu Mtalanze wakajiwekea kanuni kama wanafamilia kwamba ifikapo alfajiri yeyote atakayewahi kuamka anapaswa kuamsha na wengine ili wajiandae kwa pamoja kwaajili ya kutekeleza majukumu yanayokabili. Siku hii wazazi wa Donald http://deusdeditmahunda.blogspot.com/wakavunja kanuni wakawahi kuamka lakini cha kushangaza hawakuamsha yeyote, wakajiandaa wakawahi kazini huku wakimuacha mtoto wao akiendelea kuvuta shuka akifaidi usingizi uliokuwa umemteka kitandani. Baadae kidogo Donald akaamka akajinyoosha mwili kwa kufanya mazoezi ya viungo kama kawaida yake ya siku zote, akaingia kisha bafuni kukoga. Alipomaliza kujiandaa akatoka chumbani akaelekea moja kwa moja kwa kulia chakula “Dinning”, alipofika akaonana na dada wa nyumbani “Housegirl” akimalizia kufanya kazi za ndani. Akamuita.
“Dada Angel.”
“Abeeh,” Dada Angel aliitika huku akifuata pahala alipo Donald.
“Vipi..Baba na mama wameelekea kazini tayari?,” Donald aliuliza huku akiendelea kupata kifungua kinywa.
“Ndiyo, wameondoka mapema sana...kwani wewe hawajakuamsha?.”
“Nilikuwa nina usingizi mzito sana hivyo haikuwa rahisi kusikia, kama walikuja kuniamsha au lah,” Donald alijibu huku akijitwika begi mara baada ya kumaliza kunywa kifungua kinywa.
Akuhitaji kuchelewa zaidi, akamuaga Dada Angel hatimaye akatoka nje akakamata barabara ya kituo cha daladala akapande daladala zielekeazo shuleni. Akafika katika kituo cha daladala akasubiri daladala kwa muda pamoja na abiria wengine. Alhamdulillah akukaa kwa muda sana kituoni, punde tu daladala ya Mbezi Buguruni ikawasili akapanda kwa kasumba ya Kondakta ya kutaka kumzuia asipande sababu ya kuona ni mwanafunzi. Akafanikiwa kupanda kibishibishi baada ya purukushani na Kondakta kuisha, akaelekea kuketi kwenye kiti na daladala ilipofika kituo cha Kimara mwisho Donald akamuona mama mmoja mjamzito akipanda kwa tabu kwenye daladala aliyopo.
“Mama, njoo ukae,” Donald alimuita mama yule mjamzito mara baada ya mama yule kuingia garini.
“Ooh!.... Nakuja mwanangu,” Mama yule mjamzito alisema huku akijivutavuta kwa kupishana na abiria wengine akija alipoketi Donald.
“Mwanangu, unaonekana una heshima sana nakuomba kuwa na moyo huohuo wenye huruma,” Mama yule mjamzito aliendelea kusema huku akitabasamu mara baada ya kuketi kwenye kiti alichopishwa na Donald.
“Nashukuru mama,” Donald alishukuru huku akishikilia bomba za juu zilizopo kwenye daladala kuzuia asipepesuke kama kasumba mama ya Mzee Lomolomo wa Mama Ntilie.
Daladala ikawasili kituo cha daladala cha Mabibo Garage yapata saa moja kasoro asubuhi. Donald akashuka garini akaiacha barabara kuu akafuata barabara ya vumbi ambayo inayoelekea katika shule anayosoma. Akiwa njiani kabla ajafika shuleni akamuona mbele yake Fatuma ambaye ni mwanamke mlimbwende, na mwanafunzi nadhifu anayesoma nae shule moja na darasa moja akielekea shule.
“Fatumaaa, Fetty,” Donald aliita huku akikimbia alipo Fatuma.
“Abeeh,” Fatuma aliitika huku akigeuka amtazame anayemuita.
“Oooh! Donald,” Safari hii Fatuma aliongea kwa mshangao huku akisimama akimngojea Donald waongozane mara baada ya kutambua aliyemuita.
“Donald, nawe kumbe huwa unachelewa?,” Fatuma aliendelea kwa kuuliza mara baada ya Donald kufika jirani yake.
“Ni foleni ilizidi barabarani, ndiyo maana nimechelewa leo,” Donald alijitetea mbele ya Fatuma kisha wakaongozana kwa pamoja kuelekea shule.
“Okay...tuwahi masomo sasa yasije yakatupita” alisema Fatuma huku kwa mbali likionekana tabasamu lake likichanua kama Ua kinywani.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakatembea haraka ili kuwahi masomo, lakini kwa kuwa walichelewa wakakuta wanafunzi wote tayari washaingia darasani na kuanza vipindi vya masomo. Basi Donald na Fatuma wakaingia darasani kwa mwendo wa kunyata mithili ya kobe walipoingia darasani, moja kwa moja wakaelekea kuketi kitini ilhali hawajui kwamba kuna mwalimu amekaa kitini amejichanganya na wanafunzi akikagua kazi zake. Wanafunzi wote wakaangua kicheko kwa kitendo kile na punde ikasikika sauti ya mwalimu yule ikizungumza kwa jazba ikiuliza:-
“Huu ndiyo muda, wa wanafunzi kuwasili shule siku hizi...sio?,” Mwalimu aliliuliza darasa zima.
“Hapaana!!,” Baadhi ya wanafunzi wakajibu pamoja kwa kupayuka.
“Sasa ona, hii mitahira inakuja shuleni saa hizi tena kwa kunyata kama shule ya baba yao,” Mwalimu alisema kwa kejeli. Akawatoa mbele Donald na Fatuma wakasimame mbele ya darasa.
“Pigeni magoti.!!,” Mwalimu alikalipia, akafura kwa hasira akabadilika akawa kama Mbogo mara baada ya Donald na Fatuma kuwa mbele ya darasa.
“Mwalimu, tunaomba tusamehe” ilisikika sauti ya Fatuma akiomba radhi wakati wakiwa wamepiga magoti na Donald.
“Sitaki Kenge nyie...Kelviin,” Mwalimu aligoma kutoa msamaha. Akamuita Kelvin ambaye ndiye kiongozi wa darasa lile.
“Naam!!!,” Kelvin akaitika.
“Kimbia kalete fimbo ofisini.”
“Ipo, sehemu gani?,” Kelvin akauliza.
“Ipo chini ya meza yangu,” Mwalimu alijibu huku akitupia jicho la uchu kwa Donald na Fatuma.
Kelvin baada ya kupewa agizo akatoka darasani akaelekea moja kwa moja ofisini. Dakika chache akarejea darasani akiwa kabeba fimbo aina ya Mpera aliyoagizwa. Donald akamtupia jicho Fatuma, Fatuma akaonesha dhahiri kuwa ana hofu ya viboko kwani alikuwa anatetemeka, Kelvin akamkabidhi mwalimu fimbo hatimaye akarudi kitini kuketi.
“Ee waa!!.... Naona fimbo yangu imeshiba vilivyo, na leo nitawatandika hawa Kenge watu hadi iwakatikie mwilini” vilikuwa ni vitisho na mbwembwe za mwalimu mara baada ya kukabidhiwa fimbo na Kelvin.
“Donald Mtalanze, haya njoo hapa nikupe dawa,” Mwalimu aliendelea kuongea huku akimvuta mkono Donald aende akamchape fimbo.
“Lala chini,” Mwalimu akafoka.
Donald akalala baada ya Mwalimu kutoa agizo hilo kwa sauti kali. Akachapwa fimbo za nguvu zilizoshiba hadi Donald akataka kudondosha chozi, hata hivyo kwa kuwa yeye ni mwanaume akajikaza kiume asilie. Alipomaliza kuadhibiwa mwalimu akamuamuru akakae, akakaa.
“Fatuma Binti Kandir, hebu nawe...njoo hapa,” Mwalimu alimuita Fatuma mara baada ya kumaliza kumuadhibu Donald.
“Fatumaaa, si’nakuita,” Mwalimu aliita tena mara baada ya kuona kuwa Fatuma bado kapiga magoti bila ya kuja kuadhibiwa.
Fatuma akanyanyuka kwa ghadhabu akamfuata mwalimu, akakinga mkono achapwe fimbo baada ya adhabu akarejea kitini huku machozi yakimlengalenga. Mwalimu baada ya kutoa adhabu akarejea kwenye jukumu la kufundisha maada ya FASIHI ANDISHI lililopo kwenye somo la Kiswahili, wanafunzi wakatulia! wakawa makini kumsikiliza mwalimu. Alipomaliza kufundisha akaacha kazi kwa wanafunzi akaaga. Masaa machache mbele kengele ya mapumziko ikagongwa, wanafunzi wote wakatoka wakaelekea kantini kupata chochote kitu kwaajili ya kutuliza tumbo. Donald akaelekea kwa mkaanga mihogo akanunua mihogo kadhaa akaenda kununua na juisi hatimaye akatulia chini kwenye mti wa mkorosho akila, dakika kadhaa baada ya kuketi akashtuka kusikia mtu akimshika bega alipogeuka akakutana ana kwa ana na Fatuma ameshikilia sahani ya chipsi na glasi ya juisi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Donald, unaniruhusu niungane nawe?,” Fatuma aliuliza akitabasamu huku amesimama mbele ya Donald akisubiri ruhusa.
“Yes!!!...unaruhusiwa,” Donald alimjibu Fatuma huku akiendelea kula.
“Lakini si mbaya, ukanionjea,” Fatuma alisema ishara ya kutaka kuonjewa chipsi mara baada ya kuketi chini.
“Kula tu, nitachanganya vyakula mwishowe nikavuruga tumbo.”
“Halafu isitoshe, mbona chakula changu ninacho...wee endelea kula tu,” Donald akaongezea kuongea.
“Kila mtu anacho chakula, lakini ladha ni tofauti...nakuomba usijivunge kula hata kidogo tu,” Fatuma akabembeleza Donald apate kula chakula chake. Maneno yake yakamzonga Donald hadi akaamua kuonja chakula ili kumridhisha Fatuma.
“Aagh! kitamu,” Donald alikipa sifa chakula cha Fatuma huku akionyesha kutabasamu. Akaendelea kula chakula chake mara baada ya kuonja chakula cha Fatuma.
Lisaa limoja baada ya kumaliza kula kengele ya kurudi darasani ikagongwa. Wanafunzi wote wakaongozana kurudi darasani kuendelea na vipindi vingine, Donald akaongozana na Fatuma walipofika darasani wakaachana kila mmoja akaenda kuketi Kitini wakisubiri mwalimu aingie afundishe. Wanafunzi wakatulia mara akaingia Madam. Catheline Temba anayefundisha somo la Historia, akafundisha baadhi ya vipengele vinavyotoka kwenye maada ya INFLUENCE OF EXTERNAL FORCES AND THE RISE OF NATIONALISM, alipomaliza kufundisha akaondoka na kuwaachia wanafunzi zoezi la kujadiliana kimakundi. Baada ya siku ndefu kengele ya kurudi nyumbani ikagongwa. Haraka na purukushani wanafunzi wote wanakimbilia kujipanga mstarini “Assembly” kwaajili ya kusikiliza matangazo, wanafunzi wakiwa mstarini wametulia mara Sir. Daniel Kalombo mwalimu wa TAALUMA akapanda kwenye kizingiti kwaajili ya kutoa matangazo.
“Kesho Jumamosi na kesho kutwa Jumapili, wanafunzi wote mtakuwa mapumziko.... Lakini ifikapo Jumatatu wanafunzi wote tambua kuwa itakuwa ni zamu yangu kusimamia katika nyanja ya usafi, kuwahi na nidhamu. Hivyo basi Jumatatu naomba wanafunzi wote mjitahidi kuwa safi, kuwahi na kuwa na nidhamu atakayekiuka nitakula naye sahani moja,” Sir Daniel aliongea kwa msisitizo huku akiyatumbua macho akimaanisha.
Baada ya kumaliza kutangaza mwalimu, wanafunzi wote wakaruhusiwa kwenda nyumbani, baada ya kuruhusiwa Donald akashika barabara kuu ya Mabibo mwisho, akiwa njiani anaendelea kupiga hatua ghafla akasikia sauti ya kike ikimuita.
“Donald” aligeuka Donald taratibu amuone amuitaye. Kugeuka akamuona Fatuma na Amina ambaye ni rafiki wa Fatuma wakijongea kumfuata.
“Mbona hukunishtua?,” Fatuma aliuliza mara baada ya kuwa jirani ya Donald.
“Nilitaka kukushtua, ila sikukuona,” Donald aliongea huku wakiendelea kukaza mwendo wa kusaka Mabibo mwisho.
“Oooh, mimi na rafiki yangu tulikwenda kufagia na kudeki ofisi za walimu,” Amina alidakia mazungumzo huku akikwepesha macho kwa kuangalia chini.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa pamoja wakaongozana kituoni pale Garrage (Chicago) huku wakiendelea na soga wakisubiri daladala za Mbezi, hawakukaa sana daladala ikawasili wote wakapanda. Japo Donald safari hii hakupata pa kukaa akahamua kuongoza nyuma ya daladala kwa ajili ya kusimama, akawaacha Fatuma na Amina kwenye viti vya mbele wakiwa wameketi. Baada ya daladala kujaa kukiwa hakuna wakushuka njiani dereva akaendesha daladala hadi kituo cha Kimara mwisho ndipo Fatuma na Amina wakateremka baada ya kumlipa nauli Kondakta wakaniaga wakaondoka wakamuacha Kondakta akiita abiria. Fatuma na Amina wakajichanganya na watu walioko sokoni mwisho wakapotea machoni pangu, dereva wa daladala lile nililopanda akangoa nanga.
**********
Fatuma ni mtoto wa pekee katika familia ya Mzee Kandir, amezaliwa peke yake kwa wazazi wake. Ni mzaliwa wa kisiwani Zanzibar, mwenye asili ya kiarabu na lafudhi ya kiarabu. Kwasasa anaishi na wazazi katika jiji la Dar es Salaam eneo la Kimara Matangini, walihama kisiwani na kuja bara baada ya Zanzibar kutokea baa la njaa. Amina yeye katika familia yake ni kifungua mimba kati ya watoto watatu wa marehemu Mzee Mapambano, yeye ni mwanamwali wa kitanga na mkoa wa nyumbani wa wazazi ni Tanga. Amina na wadogo zake wanaishi Kimara Mavurunza jijini Dar es Salaam wakilelewa na bibi mzaa baba baada ya wazazi wote wawili kupoteza maisha kwa ajali ya Meli MV BUKOBA ilipozama, pindi walipokuwa safarini kuelekea Bukoba kibiashara kwa ajili ya ulanguzi wa ndizi.
**********
Donald ni mzaliwa wa mkoani Morogoro. Anaishi Kimara Suca eneo la Bwawani jijini Dar es Salaam kwenye nyumba ya familia, iliyonunuliwa na baba yake kutoka kwa Mzee Salim bin Mashudu mjumbe wa nyumba kumi. Ni masaa kadhaa yamekatika tangu haruhusiwe shule kurudi nyumbani, mbilinge mbilinge na foleni akafanikiwa kuwasili nyumbani mawio.
“Ngri, ngrii, ngriii!,” Mlio wa kengele mfululizo ukalia mara baada ya Donald kulifikia geti lao nyumbani.
“Nanii..?” lilikuwa swali alilotupia Dada Angel huku akizidi kuja taratibu kufungua geti.
“Ni mimi dada, nifungulie...,” Donald akajibu.
“Ooh!, naona umechoka.... Karibu,” Dada Angel alisema kwa kuchombeza utani mara baada ya kufungua geti.
“Eeenh...nimechoka kweli dadaangu,” Donald aliongea huku wakiingia ndani na Dada Angel.
“Pole sana,” Dada Angel alitoa pole kwa Donald huku akionyesha nyuso ya huruma na kunipokea begi.
“Ahsante.... Nishapoa.”
Donald akafika sebuleni hakutaka hata kukaa, akampokea Dada Angel begi kisha akaongoza moja kwa moja chumbani kwa ajili ya kubadili nguo. Huku akimuacha Dada Angel akielekea jikoni kupasha na kupakua chakula kwa ajili ya Donald. Baada ya dakika kadhaa Donald akabadili nguo akapandisha na kushusha pumzi kidogo hatimaye akarejea sebuleni akamkuta Dada Angel akitazama runinga huku akiwa tayari ameshamtengea chakula dinning. Wakati Donald akiendelea kula akahamua kutupia swali kwa Dada Angel.
“Dada Angel.... Hivi baba na mama, walisema leo watawahi kurudi?.”
“Hawakusema,” Dada Angel alijibu huku akiirejeza akili pahala pa awali alipokuwa amemakinika katika kipindi cha runinga.
Donald akatumia kama dakika na ushee kula na baada ya kumaliza akaelekea chumbani kwa ajili ya kujipumzisha, akajitupa kitandani baada ya sekunde usingizi ukampitia. Baadae akaja kushtushwa na mikito ya kugongwa kwa mlango.
“Shikamooni” alisalimu Donald mara baada ya kufungua mlango na kukutana na sura za wazazi pale mlangoni.
“Marahaba...hujambo?,” Wazazi kwa pamoja wakaitika na Mama Donald akauliza.
“Sijambo,” Donald alijibu huku akifikicha macho kupunguza kiwingu cha uchovu na usingizi.
“Shuleni imekuaje?,” Baba Donald akauliza.
“Ni safi, na masomo yote nimejifunza vyema,” Donald akajibu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mwanangu, naamini hutotuangusha wazazi wako, soma baba tena jitahidi sana katika masomo. Nawe mwanetu uje upate kazi yako safi kama wazazi wako,” Mama Donald akazungumza.
“Sitowaangusha wazazi wangu, nawaahidi nitajitahidi kwa ari na mali ili nifanye vizuri. Nami siku nije niishi maisha bora hapo baadae.”
“Tumekuelewa mwanetu.... Lakini usijisahau kwamba huu ndio mwaka wako wa mwisho, siku za usoni tu unamaliza kidato cha nne hivyo basi hakikisha unafanya vizuri kwenye mitihani yako ya mwisho,” Baba Donald akasisitiza akimkumbusha Donald.
“Sawa baba...nendeni sasa mkapumzike maana mnaonesha kuchoka.”
Wazazi wa Donald wakaaga wakaondoka wakamuacha Donald akiingia tena chumbani kujipumzisha. Wazazi nao wakaingia chumbani kujipumzisha. Walichoka sana si Donald wala wazazi na kwa kuwa kesho ni Jumamosi wakapata wote wasaa wa kupumzika vizuri.
“Hodiii,” Asubuhi ya Jumamosi ikasikika sauti ikibisha hodi mlangoni mwa Donald.
“Pita, mlango upo wazi,” Donald alimkaribisha mgongaji mara baada ya kuamka na kujiweka poa pale kitandani.
“Umeamkaje?,” Alikuwa ni Baba Donald akimhoji Donald mara baada ya kuingia chumbani.
“Nimeamka salama...sijui nyie?,” Donald alijibu kisha akamtupia swali baba yake.
“Sie wazima, tunamshukuru Mungu tumeamka salama...lakini kwa kuwa leo ni mapumziko mimi na mama yako tulifikiria jambo fulani jana ila tulisahau kukushirikisha,” Hoja ya Baba Donald ikamuacha kwenye mabano Donald asijue ni nini baba yake alikuwa amelenga kumshirikisha. Donald akajiweka makini kumsikiliza baba yake jambo alilotaka amshirikishe.
“Leo tumepanga chakula cha mchana hatutokula hapa ila tutatoka kifamilia kwenda kulia hotelini, Sasa mwanangu wewe ndiye jaji wa mwisho, chagua tukale hoteli gani leo?,” Nafsi ya Donald ikazibuka ikatengeneza bashasha kwani hakutegemea kile alichokisikia kutoka kwa baba yake.
“Baba, nadhani hoteli ya SUN CIRRO itatufaa” alijibu Donald kisha akainuka kitandani akamfuata baba yake aliyekuwa amesimama kwa muda mrefu toka aingie chumbani kwa Donald. Baada ya makubaliano Donald na baba yake wakatoka pamoja chumbani wakaelekea dinning kuweka kinywa sawa kwa kwenda kupata kifungua kinywa kilichoandaliwa na Dada Angel.
“Vipi mama, hajaamka hadi sahivi?,” Donald aliuliza huku wakiendelea kutembea pamoja koridoni na baba yake wakielekea dinning .
“Bado” Baba Donald akajibu. Hatimaye akamuacha Donald aelekee dinning mwenyewe, yeye akarejea chumbani kwa ajili ya kumuamsha Mama Donald. Dakika kadhaa Donald akiwa na Dada Angel wakitazama runinga baada ya kunywa chai. Mara Baba Donald na Mama Donald wakatoka chumbani wakaongozana dinning wakajitengea chai baada ya kufika dinning kisha Baba Donald akatabasamu mwisho akatupia sifa kedekede chai mara baada ya kunywa fundo moja la chai na kipande cha mkate.
“Ouh.... Chai ya leo, tamu.”
“Hamna lolote, unasema chai tamu kwa ajili ya vitafunwa maana navyo vinachangia...na penyewe mkate ndiyo kitafunwa ukipendacho kwa hiyo lazima uone chai tamu,” Ilikuwa ni kauli ya Mama Donald ikiambatana na tabasamu.
“Donald, hii filamu nzuri,” Dada Angel alizungumza mara baada ya kuona Donald amemakinika zaidi kwenye runinga kuliko mazungumzo.
“Kivipi, iwe nzuri?,” Donald akauliza kizushi.
“Kwasababu, love story yake imepangiliwa vizuri,” Dada Angel alijibu huku macho yakimakinika zaidi nae kwenye runinga.
Baada ya dakika kadhaa Baba Donald na Mama Donald wakamaliza kunywa chai, Dada Angel akanyanyuka kwenda kutoa vyombo akaenda kuviosha. Mama Donald na Baba Donald walipomaliza kunywa kifungua kinywa wakahamua kuchukua vitu ili kupoteza muda. Wakaja kujumuika na Donald sebuleni huku Mama Donald akiwa ameshikilia kitabu pendwa cha Mwandishi ERIC JAMES SHIGONGO kinachotambulika kama LAST DAYS OF MY LIFE, Baba Donald nae akiwa ameshikilia gazeti kama kawaida sababu ya ulevi wa magazeti. Basi alichagua gazeti pendwa la MWANANCHI akalifunua akalipitia vichwa vya habari kwanza kabla ya kuanza kusoma kwa undani. Ghafla akapigwa na butwaa pale alipofika kwenye kurasa ya tano akakuta habari iliyomshtua na iliyosomeka hivi;-
“DR. KIMBOKA AMIMINIWA RISASI TANO NUSURA KUUAWA.”
“Yaani, madaktari tunapitia hali ngumu sana...hatuthaminiki hata kidogo,” Mzee Zungu alizungumza moyoni mara baada ya kusoma habari ile kwa kina na kuona uonevu uliofanywa kwa daktari mwenzake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapo wote kwa pamoja wakawa kimya. Ukimya ukatawala kila mtu akawa bize kufanya alichopendezwa kufanya. Mama Donald akaendelea kusoma kitabu, Baba Donald akaendelea kusoma gazeti na Donald nae hakuacha akaweka kipaumbele na kuwa makini kutazama runinga. Mishale ya kijua cha utosi ndipo wakajiandaa pamoja wakaelekea SUN CIRRO HOTEL. Familia nzima wakaenda hotelini kupata chakula cha mchana, wakafika wakatafuta meza ya mkusanyiko wakaketi pamoja, hawakuchukua muda mara mhudumu wa kike akawasili walipo akawachangamkia kistaarabu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment